Search This Blog

Thursday, July 21, 2022

HUWEZI KUUA MAITI - 1





    IMEANDIKWA NA : ERIC SHIGONGO



    *********************************************************************************



    Simulizi : Huwezi Kuua Maiti

    Sehemu Ya Kwanza (1)

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Ingawa ilikuwa mchana hali katika msitu wa Kungoni nchini Kongo ilikuwa ya kiza nene! Mawingu yalitanda angani. Ni asubuhi ya siku hiyo tu ilinyesha mvua kubwa tena ya mawe na kusababisha baridi kubwa! Wanyama wengi walijikunyata sababu ya kulowa.



    Milio ya ndege na wanyama mbalimbali ilisikika kila pembe ya msitu huo uliokuwa kilometa kama 520 kutoka Jiji la Kinshansa, ulikuwa ni msitu wenye tembo wengi kuliko msitu mingine yote barani Afrika na uliwavutia watalii wengi lakini waliogopa kuutembelea sababu tembo wa msitu huo waliua watalii.



    Kila mtu aliamini hakuna mtu aliyeishi katika msitu huo jambo ambalo halikuwa sahihi hata kidogo, kwani mtu mmoja tena bibi kizee mwenye umri wa miaka 80 aliishi katika msitu huo kwa miaka mingi.

    Alikuwa ameishi katika msitu huo kwa muda wa miaka isiyopungua thelathini akifanya utafiti wa maisha ya tembo na wanyama wengine kama ndege, Nzige na Mbungo! Alipofika Kongo kwa mara ya kwanza alikuwa na umri wa miaka 30, aliingia nchini humo akitokea Tanzania.



    Kinshansa chini ya Patrice Lumumba ilimpokea mwanamke huyo kama mtafiti wa wanyama bila kudadisi sana kilichomfanya aondoke Tanzania na kumpa kibali cha kwenda kuishi msituni Kungoni.



    Ni bibi huyo pekee aliyeishi katika msitu huo akizungukwa na wanyama wengi wao wakiwa ni tembo! Aliishi na wanyama hao kwa miaka thelathini mpaka wanyama wote wakamwona ni kama mnyama mwenzao, aliijua lugha za tembo, nzige, mbung’o na ndege mbalimbali! na kuwasiliana nao kama binadamu.



    Kulipokuwa na hatari aliitambua kwa kuwasikiliza tembo, nzige, mbung’o na ndege! Alipohitaji kitu chochote porini alitoa mlio fulani mdomoni mwake na Tembo wote walikuja na aliwaagiza kufanya kitu chochote alichotaka! Kifupi wanyama wote walimwona kama malkia wao!



    Kila sehemu aliyokwenda alizungukwa na tembo wakimlinda, ilikuwa si rahisi kwa wanyama wengine wa porini kama simba, chui, kumdhuru sababu ya ulinzi aliopewa na tembo alioishi nao kwa miaka mingi na aliwafahamu tembo kwa majina. Kila mtu aliyesikia habari za bibi huyo alishangaa na Wazungu wengi walikwenda msituni ili kumwona lakini hawakurudi salama, wengi walikufa kabla ya kumfikia. ****



    Bibi huyu aliitwa Nyanjige Ndaki, hakuwa Mkongo bali Mtanzania tena kutoka Mkoani Mwanza, alikuwa msomi wa chuo kiku cha Edniburgh, nchini Uingereza alikopelekwa na gavana kama zawadi kwa mama yake aliyekuwa mpishi wa Gavanna huyo kwa kipindi kirefu!



    Gavana alipotaka kuondoka chini alimchukua bibi Nyanjige wakati huo akiwa na umri wa miaka mitano tu ili akamsomeshe nchini Uingereza. Aliishi Uingereza kwa miaka karibu ishirini na tano bila kurudi Tanzania na aliporejea nchini mwaka 1967 alikuwa tayari ana digrii mbili za elimu ya viumbe badala ya kufanya kazi aliushangaza ulimwengu alipofanya mauaji ya watu 150 kwa mpigo na hakuna aliyeelewa sababu ya mauaji hayo!



    Tangu siku ya kwanza aliyoingia Kongo na kupewa kibali cha kuishi porini Kungoni hakurudi tena mjini kwa kuogopa kukamatwa, siku zote aliishi na wanyama porini, akila matunda kama wanyama, wakati mwingine aliua swala na kula nyama! Hayo ndiyo yakawa maisha yake siku zote, hakutaka kabisa kukutana na binadamu yeyote.



    Patrick Lumumba alipokufa serikali ya Kongo chini ya Mabutu Seseko ilimsahau kabisa bibi huyo, hakuna mtu aliyetaka kujua habari zake. Serikali ya Tanzania nayo baada ya kumtafuta kwa muda mrefu bila mafanikio iliamua kuachana na swala hilo ikiamini bibi Nyanjige alikufa! Ingawa msako wa chini chini uliendelea kwa usaidizi wa nchi nyingine kama Marekani, Ufaransa, Ujerumani ambazo pia Raia wake walikufa katika tukio la mauaji hayo.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Ilikuwa si rahisi kumwona bibi Nyanjige kwa ulinzi mkali uliokuwepo nyumbani kwake porini, nyumba yake ilizungukwa na Tembo wasiopungua kumi, waliomlinda usiku na mchana! Wazungu wengi waliojaribu kumfikia ili kupata picha yake waliuawa kwa kunyangwa na Tembo!



    Mzungu mmoja aliyekwenda porini kwa helkopta alifanikiwa kuipata picha ya bibi Nyanjige akiwa katikati ya tembo!

    Ni picha hiyo iliyoleta matatizo kwani ilipochapishwa katika magazeti na majarida mbalimbali nchini Uingereza na Marekani serikali ya Tanzania ilishtuka na kuamini kuwa mtu aliyekuwa akitafutwa alikuwa porini nchini Kongo.



    Bila kuchelewa ilituma wanajeshi wapatao ishirini waliopewa msaada na askari wengine kumi wa Kongo! Walifika hadi msituni lakini hawakufanikiwa kumkamata bibi Nyanjige na pia hawakufanikiwa kurudi salama nyumbani! Wote walikufa kifo hichohicho cha kukanyagwa na Tembo!



    Mpaka mwezi moja baada ya askari hao kuondoka hapakuwa na mawasiliano yoyote kutoka msituni, simu zao za upepo ziliendelea kuita bila majibu! Hilo lilionyesha wazi watu hao hawakuwa hai!



    Ilibidi serikali za Tanzania na Kongo kwa kushirikiana ziandae jeshi kubwa lenye askari wasiopungua elfu tano waondoke kwenda msituni kumsaka bibi Nyanjige!

    Maaskari wote 5000 walilizunguka pori wakiwa na silaha kali mikononi mwao na ndege za kivita zilipita angani!



    Askari ndani ya ndege hizo walipoangalia chini ka kutumia viona mbali waliziona maiti za askari wenzao zikiwa ardhini na tembo wengi wakiwa wamezunguka kibanda kidogo kilichoonekana kuwa kama nyumba.



    Ghafla mamia kwa maelfu ya ndege walionekana angani, hawakujulikana walikotokea! Wengi walitua kwenye vioo vya mbele vya ndege hizo na kuwafanya marubani washindwe kuendesha ndege zao vizuri kwa sababu hawakuona mbele.

    “Tufanya nini sasa?”



    “Turudi tukatue kwanza, vinginevyo hawa ndege watasababisha tuangushe ndege ni wengi mno na sielewi wametoka wapi!”

    “Sawa geuza basi!”



    Wakati wanageuza ndege nyingine ilishafika karibu yao ikipita katikati ya makundi ya ndege, zote mbili ziligongana na kuwaka moto zikiwa angani! Askari waliokuwa wakitembea kwa miguu walishangaa kuona ndege zikigongana.



    “Tusongeni mbele! Mpaka tumtie nguvuni huyu bibi, kazi hii tumepewa na serikali zetu ni lazima tumkamate na kumfikisha Tanzania akiwa hai, ajali hii imeniongeza hasira zetu unanipata lakini, ovaaa!”

    “Ndiyo ninakupata mkuu! Hata sisi tumeishuhudia ajali hiyo na tunazidi kusonga mbele ila kuna kitu cha ajabu kidogo kimetokea hapa!”



    “Kitu gani?”

    “Kundi kubwa sana la mbung’o na nzige wamejitokeza na wanatuuma sana! Maaskari wengi wameshindwa kabisa kuendelea wa safari na wameanguka chini! Hivi ninavyoongea wanashambuliwa na mbung’o hata mimi mwenyewe mwili wangu wote umezingirwa na mbung’o pamoja na nzige wanakula magwanda yangu!”
“Kweli?” Aliuliza Meja Jenerali Job Lupilya aliyekuwa mkuu wa operesheni hiyo, hakupata jibu kutoka upande wa pili!



    Alizidi kuita kwa muda mrefu bila kutikiwa, hali ilimtisha na kumwamuru mmoja wa wapiganaji wake awashe kifaru cha vita na wakaondoka kuelekea upande wa pili kulikokuwa na kikosi alichowasiliana nacho!



    Iliwachukua kitu kama dakika ishirini kufika eneo hilo, hawakuamini walichokiona walipofika, miili ya zaidi ya maaskari mia moja ililala chini ikiwa imeliwa nyama zote na Nzige pamoja na Mbung’o! Ilikuwa ni mifupa tupu iliyolala chini ambayo wazungu huiita Skeleton! Nzige na Mbung’o wengi wasio na idadi walitapakaa kila mahali wakiendelea kula miili ya maaskari waliokufa.



    “Hivi hawa ni Nzige gani yaani wamewaua askari wetu wote?” Aliuliza mwanajeshi mmoja na kabla hajafanya lolote walishangaa kuona kundi kubwa la Nzige kama wingu au kundi la nyuki wakihama kutoka sehemu moja hadi nyingine likiwafuata!

    “Ina maana wanatufuata sisi?”

    “Inavyoonekana!”



    “Hebu ngoja!” Alisema mkuu wa kikosi na kutoa baruti na akawalipulia, nzige wengi walikufa lakini dakika moja tu baadaye kundi jingine la Nzige na Mbung’o lilitokea upande wa pili na kuanza kuwashambulia! Yalikuwa ni maumivu makali mno, magwanda yao ya jeshi yalitafunwa na kujikuta wakiwa uchi katika muda wa sekunde chache ndipo minofu yao ilipoanza kuliwa kwa kasi ya ajabu.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Ghafla Meja Jenerali Lupilya akiwa amekata tamaa kabisa alisikika kitu kama mluzi ukipigwa pembeni yake

    “Pswiiiiiiiiiiii!” Kufuatia mluzi huo Nzige wote wakasimamishwa zoezi lao la kula minofu yake! Mluzi mwingine tena ulifuata lakini katika mtindo tofauti kidogo! Kufuatia mluzi huo Nzige wote waliruka na kuondoka zao.



    Meja jenerali Lupilya alipogeuza uso wake na kuangalia pembeni alikiona kibibi kizee kikitembea taratibu kuelekea mahali alipolala, Tembo wengi walikizunguka na mmoja wao alipomfikia alizungushia mkonga wake shingoni mwa Meja jenerali, alimnyanya na kuanza kumzungusha hewani, Lupilya alipiga kelele na kulia.



    “Wiiiiii!” Bibi alitoa mlio mdomoni kwake na Tembo akamweka chini Lupilya, alikuwa akitoka jasho mwili mzima na mkojo ulimpenya! Tembo wote walikaa chini na kulaza vichwa vyao ardhini kama ishara ya kuonyesha heshima kubwa kwa bibi Nyanjige.



    “I’m the queen of the forest who are you?”(Mimi ni malkia wa msitu wewe ni nani?)

    “I’m ...ma...jor gene...ral Lupi...lya fro..m Tan..zania!”(Mimi ni Me...ja jene....rali Lupil....ya natoka Ta....nzania)

    “Tanzania? From what tribe are you?”(Tanzania? Wewe ni kabila gani?)

    “Su…ku..ma!” Alijibu Lupilya huku akilia na kutetemeka! Hakuamini kulikuwa na binadamu aliyekuwa na uamuzi mkubwa kiasi hicho mbele ya wanyama wa mwituni!



    “Ule Nsukuma getegete?”(Wewe ni Msukuma kabisa?) Bibi Nyanjige alimuuliza meja kwa kabila ya Kisukuma, Lupilya alibaki mdomo wazi akishangaa.

    “Ngh’ana gete mama! Nu bebe gashi uli wa Kukaya?”(Kweli kabisa bibi kumbe na wewe ni mtu na nyumbani!) Alijibu Lupilya huku akiendelea kulia machozi, mwili wake wote ulimuuma sababu ya kuliwa na Nzige, alipomwangalia mwenzake alikuwa kimya nyama zote hazikuwepo mwilini!Alibaki mifupa.



    “Mnataka nini hasa nyinyi?” Bibi aliuliza kwa kiswahili.

    “Nduhu mhayo mama! Nilekejage natalashogeja kabili!(Hakuna neno bibi nisamehe sitarudia tena) Meja Lupilya aliendelea kuongea kwa Kisukuma.

    “Ongea kiswahili mpumbavu wewe! Unafikiri Kisukuma kitakusaidia HAPA?”

    “Nisamehe bibi na mimi nilitumwa tu!” Lupilya alibadilisha lugha.



    “Sasa wewe nakuachia nenda kawaeleze ndugu zako kuwa hapa ni moto wa kuotea mbali! Mimi ndiye malkia wa msitu huu! Jeshi langu si mchezo nitawamaliza! Ondokaaaa upesi!” Aliongea kwa ukali bibi Nyanjige na Lupilya ulinyanyuka na kukimbia kuelekea porini akiwa uchi wa mnyama kila alikopita alikuta miili ya watu ikiwa imelala chini bila nyama! Na Nzige walikuwa kila mahali lakini hawakumgusa amri aliyoitoa bibi ilionekana kusambazwa kila mahali.



    “Mh! Huyu bibi si mchezo ni heri upambane na dunia nzima lakini si yeye!” Alisema meja Lupilya Baada ya kutembea kwa nusu saa hivi aliikuta helkopta imeegeshwa watu wengi walikuwa pembeni yake wakiwa mifupa mitupu, aliwaruka na kuingia ndani ya helkopta, mifupa mingine ya watu wawili ilikuwemo ndani ya helkopta hiyo.



    “Hii acha niondoke nayo ili wakaelewe vizuri nitakachokuwa nawaeleza, maana ninajua itakuwa si rahisi kuamini yaliyotokea! Huyu bibi si mchezo jamani!” Alisema meja jenerali Lupilya akiwasha ndege ili aondoke.



    Kwa muda wa miezi kama mitatu ya mwisho kabla Nyanjige hajaondoka Uingereza alikoishi kwa miaka 30 kurudi nyumbani Tanzania, alipoteza kabisa mawasiliano na mama yake na alishindwa kuelewa ni kitu gani kilimpata mpaka akawa kimya kiasi hicho kwani kwa kawaida alipokea barua moja kila mwezi kutoka kwa mama yake lakini kwa miezi mitatu mfululizo yote hakupata taarifa yoyote juu ya hali ya mama yake.



    Ni jambo hilo ndilo lilifanya Nyanjige aamue kuondoka Uingereza mapema kabla ya muda aliopanga, lilimtia wasiwasi mwingi sana moyoni mwake na kumpa kumbukumbu nyingi sana juu ya mama yake na alitaka kuwa naye wakati huo.



    Katika miaka yote 30 ambayo Nyanjige aliishi nchini Uingereza akisoma na hatimaye kufanya kazi ni mara mbili tu aliwahi kuonana na mama yake na mara ya mwisho ilikuwa miaka kumi kabla ya kufikiria kurudi Tanzania.



    “I have got to go home! Tanzania is my country!Tanzania is my home! My people are in Tanzania not here in the UK! I have to go and serve my own people rather than serving Britains(Ni lazima nirudi nyumbani, Tanzania ndiyo Taifa langu, Tanzania ndiyo nyumbani kwetu, Tanzania ndiyo asili yangu, watu wangu wako huko ni lazima niende kuwatumikia wao kuliko kuendelea kuwatumikia waingereza) Alisema Nyanjige akiwa mwenye mawazo mengi.



    Alikuwa mwanamke mzuri sana lakini katika miaka yote aliyoishi Uingereza hakujaliwa kupata mtoto wala mchumba wa kumuoa! Si kwamba sura yake ilikuwa mbaya mno la hasha! Bali hakuwa na bahati ya kuolewa na hiyo ilitokana na shughuli nyingi alizokuwa nazo! Nyanjige alitamani sana kuwa na mtoto lakini haikuwa hivyo.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kabla ya kuondoka nchini Uingereza alimnunulia mama yake zawadi nyingi za nguo za Kiingereza, alitaka mama yake apendeze na kuwa tishio mtaani kwao na ikiwezekana hata mkoa mzima wa Mwanza na vitongoji vyake wamfahamu!



    Siku ya kuondoka London ndiyo ilikuwa siku ya furaha zaidi katika maisha yake, alipanda ndege ya shirika la ndege la Alliance Airlines iliyoondoka London kuja Dar es Salaam kupitia Paris, Uturuki, Misri, Ethiopia, Nairobi na hatimaye kuingia Dar es Salaam. Safari hiyo ilimchukua masaa zaidi ya ishirini na nne, wakati anaingia Dar es Salaam saa nne ya asubuhi alikuwa amechoka kupita kiasi lakini hakutaka kulala Dar es salaam kabisa na kuamua kuunganisha siku hiyo hiyo kuelekea Mwanza ambako aliwasili saa 10 jioni.



    Alikuwa na hamu kubwa ya kuonana na mama yake hivyo alikodisha teksi kutoka uwanja wa ndege ambao upo kama kilometa nane kutoka Mwanza mjini hadi kijijini kwao Usagara kilometa kama sabini kutoka Mwanza mjini, ambako mama yake aliishi baada ya kustaafu kazi ya upishi nyumbani kwa gavana.



    Iliwachukua zaidi ya masaa mawili kufika kijijini Usagara, sababu ya ubovu wa barabara uliokuwepo mjini Mwanza. Alishangazwa na hali aliyoikuta nyumbani kwa mama yake, nyumba ya mama ilikuwa imebomoka na kuanguka upande mmoja, nyasi ziliota hadi mlangoni mwa nyumba hiyo iliyojengwa kwa udongo! Mlango ulikuwa wazi na ilikuwa rahisi sana kufikiri watu walioishi katika nyumba hiyo walihama miezi michache kabla.



    Hali hiyo iliufanya moyo wa Nyanjige upige kwa nguvu na kasi ya ajabu alihisi kuna tatizo lilitokea ambalo hakuwa na habari nalo! Hakutaka kuteremsha mizigo yake ndani ya gari na kuamua kuusukuma mlango na kuingia hadi ndani ya nyumba ya mama yake ambako alianza kuita jina la mama yake lakini hakuitikiwa hatimaye aliamua kusukuma mlango wa chumbani na kukuta umefungwa kwa komeo kutoka ndani, alijua kwa hakika ndani kulikuwa na mtu!



    “Mama! Mama! Mama!”Aliendelea kuita lakini hali ndani ya nyumba ilikuwa kimya! Baada ya kuita sana hatimaye ilibidi amwite dereva ajaribu kumsaidia kuuvunja mlango wa chumbani ili waigie na kuangalia! Alipokuja dereva walifanikiwa kuuvunja mlango na kuingia hadi ndani! Ingawa giza lilikuwa halijaingia chumba hicho kilikuwa kiza tupu na ilikuwa si rahisi kuona kitu chochote kilichokuwemo ndani.



    “Dereva una tochi?’

    “Tochi dada sina ila nina kiberiti!”

    “Basi nisaidie hicho hicho kiberiti nataka kuangalia humu ndani!”

    “Kwani kuna nini dada?”

    “Mama yangu aliishi hapa lakini dalili zilizopo zinanitisha sijui kahama?Sijui yupo wapi? Naomba hicho kiberiti nijaribu kuangalia vizuri humu chumbani!”



    Dereva aliingiza mkono wake mfukoni na kutoa kiberiti na kumkabidhi Nyanjige, alipokiwasha tu kwa mwanga mdogo uliokuwepo aliweza kukiona kitanda cha mama yake na kukisogelea, juu kulitandikwa shuka jeupe lakini hapakuonekana kuwa na kitu chochote chini ya shuka hilo cha kufanya afikirie mama yake alikuwa kitandani amelala!



    Alikibeza kitanda na kuendelea kukagua sehemu mbalimbali za chumba huku akiwasha njiti nyingine ya kiberiti kila moja ilipozimika.

    Alizunguka chumba kizima bila kuona kitu, akahamia chumba kilichokuwa kimebomoka upande huko nako pia hakuona kitu chochote! Nyanjige alizidi kuchanganyikiwa, ghafla wakati akirudi kwenye chumba cha mama yake aliona kitu kama karatasi chini ya kitanda aliinama na kuiokota, akaikunjua vizuri na kuanza kuisoma.



    “Ng’wanone Nyanjige, nene nalisatu no! Ubusatu wenubu ndibona bukunibulaga! Bale bizile banhu bunisola bahayaga angu ndi nogi nakabulagaga bana babo! Aho banisola Bunitwala Kwibanza Lya sungusungu, bunitula mpaga nudeda getegete, Nushoka kukaya nalagula giti kanegene! I hali yane ya bubi no natumanaga nulu ukunisanga nali mhola! Aliyu mhayo untale ukonisanga nachile ng’wanone nalibona atiho nu munho wakunijeka leka nikundikile shuka ulagasanga maguhwa gani habulili wenubu! Nacha ng’wanone wikate mhola.



    Nini.

    Noko!

    Barua hiyo iliandikwa kwa kisukuma lakini ilimaanisha maneno yafuatayo:

    “Mwanangu Nyanjige, mimi naumwa sana na ugonjwa huu naona utaniua! Walikuja hapa watu wakanichukua hadi kwenye kikao cha sungusungu wakidai eti mimi ni mchawi, wakanipiga mpaka nikaja hapa nyumbani natambaa kama mtoto! Hali yangu ni mbaya mno mwanangu sijui kama utanikuta hai ukirudi lakini kikubwa najua utanikuta nimekufa na ninaona hakuna mtu wa kunizika hivyo najifunika shuka utaikuta mifupa yangu chini ya shuka hili hapa hapa kitandani, nakufa mwanangu naomba ubaki salama!

    Mimi,

    Mamayo!



    Nyanjige alimaliza barua hiyo mwili wake ukiwa umekufa ganzi alitembea taratibu kuelekea kitandani na alipofunua shuka ilikuwa ni mifupa ya mama yake ikiwa chini ya shuka! Alishindwa kuvumilia akanguka chini na kuzirai! Dereva kuona hivyo alimbeba na kumtoa hadi nje na kuchukua maji yaliyokuwemo kwenye galoni ndani ya gari lake na kummwagia usoni na mwilini! Haikuchukua muda mrefu akazinduka na kuanza kulia machozi. Pamoja na kilio hicho hakuna hata jirani mmoja aliyejitokeza kuja kumsaidia au kuuliza ni kitu gani kilitokea Nyanjige na dereva walishangaa.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Baada ya kitu kama masaa mawili hivi bila kuona jirani akitokeza Nyanjige aliamua kwenda nyumba ya jirani kuulizia lakini alipofika watu wote walikimbilia ndani na kufunga milango ya nyumba zao na wengine kuongea naye kupitia dirishani.



    “Nyanjige nitwa kwambilija, aliyo ikaya ying’we ituligije konguno na bulogi (Nyanjige tungekusaidia lakini familia yenu imetengwa na kijiji sababu ya uchawi)

    “Hata kama mmenitenga ndiyo mnaweza mkamwacha mtu akafa mpaka kuwa mifupa? Huu ni unyama ni lazima niwaonyeshe nimechukia kiasi gani!



    Isitoshe mama yangu hakuwa mchawi au mlimwita mchawi kwa sababu ya macho kuwa mekundu?Mmesahau kuwa alikuwa mpishi wa gavana?”

    “Kwa kweli sio sisi ni serikali ya kijiji iliyoamua hivyo, hata sisi tumesikitika mno!” Alisema mama mmoja kupitia dirishani.



    Nyanjige akiwa amepandisha hasira kupita kiasi alirudi nyumbani kwao huku akilia, hakuwa na la kufanya kwani hakufahamu ndugu hata mmoja nchini Tanzania wazazi wake walitokea Kongo miaka mingi walipofika Mwanza walichukua majina ya Kisukuma na kujifunza kabila hiyo wakaonekana Wasukuma wakati walikuwa Wabembe kutoka Zaire.



    Ndugu pekee aliyekuwa nae pale alikuwa ni dereva aliyemleta kutoka mjini huyo ndiye aliyemtegemea kumpa kila aina ya msaada!

    “Siki...li...za ka...ka mimi nime..pa..twa na ma..tati..zo nafi..kiri ume..ona, hivi una...weza kunisaidia vipi?’

    “Kwa tatizo gani?”

    “Nataka kuzika mifupa ya mama yangu!”

    “Hilo tu lisikumbue dada yangu nitakusaidia mimi ni binadamu kama wewe!”



    “Nisaidie nitakulipa kiasi chochote cha pesa!”

    Dereva alirudi nyuma na kufungua buti la gari na kutoa jembe na koleo ambavyo alitembea navyo wakati wa mvua kumsaidia kila anapozama katika tope! Baada ya kuvichukua alivua shati lake na kukunja suruali.



    “Ni wapi tuchimbe kaburi dada?”

    “Chimba tu hapa hapa mbele!” Alijibu Nyanjige akilia machozi kwa uchungu, moyo wake uliuma sana na hasira ilimkaba kooni aliamini asilimia mia kuwa mama yake hakuwa mchawi ila aliponzwa na macho mekundu sababu ya moshi wa miaka mingi nyumbani kwa gavana.

    “Haiwezekani ni lazima nilipe kisasi kwa wananchi wa kijiji hiki hawawezi kumuua mama yangu mpendwa kinyama namna hii wanastahili adhabu tena adhabu ya kuchukua maisha yao!” Aliwaza Nyanjige huku akiendelea kulia machozi na dereva akiendelea kuchimba kaburi.



    Masaa mawili baadaye shimo lilikuwa tayari na dereva alimpa Nyanjige taarifa hiyo na wote wawili wakaingia hadi ndani ambako Nyanjige alibeba mwili wa mama yake uliokuwa mifupa tupu katika mikono yake na kuanza kutembea hadi nje! Baadhi ya mifupa ilikatika na kudondoka chini akalazimika kurudi kuiokota ndipo shimo likafunikwa!



    Yalikuwa mazishi ya watu wawili tu!Katika maisha yake yote Nyanjige hakuwahi kuumia moyo kama siku hiyo, walipomaliza mazishi hayo tayari ilikuwa saa sita ya usiku na dereva aliomba ruhusa ya kuondoka lakini Nyanjige alikataa na kuahidi angemlipa pesa za siku zote ambazo angekaa naye.



    Kwa usiku mzima Nyanjige alilia akimlilia mama yake, moyo wake ulijaa kisasi alitaka kulipa kisasi kwa unyama aliofanyiwa mama yake! Asubuhi siku iliyofuata waliondoka hadi mjini Mwanza kwenye maduka ya madawa ya mifugo ambako Nyanjige alinunua sumu ya kuulia wadudu aina ya DDT bila dereva kugundua kilichonunuliwa na wote wawili walirejea tena hadi kijijini Usagara!



    Jioni Nyanjige alizunguka kijijini bila kuongea na mtu yeyote akijaribu kutafuta ni wapi kilipokuwa kisima ambacho wanakijiji walitumia kwa maji ya kunywa, alipogundua mahali kilipokuwa alirudi nyumbani na usiku wa siku hiyo dereva akiwa usingizini alitoka na kutembea hadi kwenye kisima akaimiminina sumu yote kwenye maji.



    Usiku huohuo alitoroka na dereva wake kuelekea Kigoma kupitia kibondo, Kasulu hadi Kigoma mjini ambako alimlipa dereva kiasi cha shilingi laki tano na kuagana nae! Ni siku hiyo hiyo aliyoingia Kigoma ndiyo siku aliyovuka na boti hadi mji wa Kalemi nchini Kongo ambako alipanda basi lililompeleka moja kwa moja hadi Kinshasa ambako alijitambulisha kama mtafiti wa wanyama na kuruhusiwa kuishi porini.



    Alijua aliyoyaacha nyuma yake yalikuwa makubwa na kweli watu mia moja na hamsini walikunywa maji ya kisimani asubuhi ya siku aliyomwaga sumu walikufa! Uchunguzi ulipofanyika sumu aina ya DDT iligundulika katika maji na kila mwanakijiji alikua na uhakika sumu hiyo ilimwaga katika kisima na Nyanjige na kutoroka ni hapo ndipo msako kumsaka ulipoanza.



    Askari aliyenusirika msituni Kungoni:

    “Jamani huko hali ni mbaya kupita kiasi, jeshi lote mlilonipa limemalizika kuna mbung’o na Nzige wa hatari sijapata kuona, wanakula miili ya watu kama mchezo! Watu wote mlionipa wameliwa na kubaki mifupa tupu! Njooni muone mfano wake huku kwenye helkopta!” Alisema Meja Jenerali Lupilya na kuwachukua wakuu wa majeshi hadi kwenye helkopta aliyowasili nayo! Kila mtu alishika mdomo kwa mshangao jinsi wanajeshi wawili walivyoliwa nyama za mwili wao.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Waliofanya hivi ni mbung’o na nzige?”

    “Ndiyo na vijana wote niliokwenda nao wapo kama unavyoiona hii mifupa!”

    “Du! Na wewe umeokoka vipi?” Mkuu wa majeshi aliuliza.

    “Huyo bibi kanihurumia tu kwa sababu niliongea Kisukuma!”

    “Anaongea Kisukuma?”

    “Ndiyo tena vizuri tu! Ila jeshi lake si mchezo ni la wanyama na wadudu tupu na wote wanamtii anaishi peke yake msituni, mlishawahi kuona binadamu anazuia Nzige kula kitu?”



    “Hapana!”

    “Basi mie nimeona kwa macho yangu nzige walikuwa wanile lakini bibi huyo alipofanya “Psyiiiiii” nzige wote wakatulia!”

    Siku hiyo hiyo kikao kilikaa na kuamriwa kuwa jeshi jingine lenye askari 10,000/= lipelekwe haraka msituni kwa mapigano mengine makali zaidi ili kuhakikisha bibi Nyanjige anakamatwa na kurejeshwa nchini Tanzania kwa mashtaka ya mauaji ya halaiki ya watu na Lupilya alitakiwa tena kuliongoza jeshi hilo.



    Wakuu wa majeshi walishangaa kumwona Meja Jenerali Lupilya akivua magwanda yake pamoja na silaha akakabidhi kwa mkuu wa majeshi akawa ameacha jeshi! Kujiuzuru kwa Lupilya kuliwafanya wengi waamini jeshi la bibi Nyanjige hakuwa mchezo.



    “Jamani mimi naona ni heri muombe msaada umoja wa Mataifa nina hakika nyie wote mnaokwenda hamtarudi hapa Tanzania!” Alishauri Lupilya lakini hakuna mtu aliyesikiliza, siku hiyo hiyo alifukuzwa kambini na mkuu wa majeshi aliamua kuongoza kikosi hicho kwenda Kongo kupitia Kigoma kushuhudia mwenyewe! Alisomea mambo ya jeshi nchini Cuba na Israel hivyo alikuwa na uhakika wa kupata ushindi dhidi ya jeshi la wadudu na wanyama wa bibi Nyanjige.





    ...Msituni:

    Tembo zaidi ya elfu tano walikusanyika kumzunguka bibi Nyanjige! Mbung’o pamoja na Nzige wasio na idadi walizunguka angani na kufanya eneo hilo liwe na kivuli ingawa ilikuwa ni hali ya jua kali! Ulikuwa ni kama mkutano wa hadhara wa wanyama na wadudu na bibi Nyanjige alikuwa akiwasiliana na wadudu na wanyama wote katika lugha zao akiwatahadharisha juu ya uvamizi mwingine na kuwaomba wakae tayari.



    Wanyama na wadudu waliomchukulia bibi Nyanjige kama Malkia wao waliahidi kutoruhusu mtu yeyote amdhuru labda wote wawe wamemalizika! Lugha ya wadudu na wanyama aliojifunza ilimsaidia sana kuwasilina sana kuwasiliana na wanajeshi wake.Baada tu ya mkutano huo Tembo, Nzige na Mbung’o wote walisambaa na kuanza ulinzi msituni. ****************



    Meli zipatazo ishirini kubwa zikiwa zimebeba askari pamoja na vifaa mbalimbali vya kivita zilikuwa safarini kuelekea Kongo! Ndege zaidi ya hamsini ziliruka moja baada ya nyingine kutoka uwanja wa ndege wa Kigoma kwenda Kongo, helkopta zilizojazwa madawa ya kuua wadudu zilikuwa hewani zikielekea msituni kwa lengo la kuwaua Nzige na mbung’o wote kabla ya kumkamata bibi Nyanjige!



    Kulikuwa na kila dalili kuwa isingechukua masaa hata mawili kabla msitu huo haujafutwa katika uso wa dunia Tembo wote wakiwa wameteketezwa kwa makombora!



    Askari wote walifurahia vita hiyo na walikuwa na uhakika wa kumkamata bibi Nyanjige na kumrudisha Tanzania akiwa maiti au hai! Vifo vya wenzao zaidi ya 5000 viliwatia hasira kali sana na walitaka kulipiza kisasi!



    ..Asubuhi ya siku hiyo msitu ulikuwa kimya kabisa, ni ndege tu waliopiga kelele wanyama wengine walikuwa kimya! Tembo wengi walikusanyika katikati ya msitu wakiwa wameiweka nyumba ya bibi Nyanjige katikati kuhakikisha usalama wake.



    Ndege aina ya Tai ambao idadi yao ilikuwa si rahisi kuifahamu walionekana wakiruka angani, walikuwa tayari kwa hatari yoyote ambayo ingetokea na walikuwa na ufahamu kuwa wakati wowote msitu ungeweza kuvamiwa tena.



    Kwa amri waliyopewa na bibi Nyanjige kama wangevamiwa Tembo na nzige wangeendelea na vita vya nchi kavu na ndege aina ya Tai, Kunguru na mwewe wangeendelea na vita vya angani wakipambana na na ndege zilizotegemewa kuuvamia msitu. Hali ya vita ilinukia kila mahali,kilichokuwa kikisubiriwa wakati huo ni kuwasili kwa maadui.



    Masaa machache baadaye miungurumo wa ndege za kivita ilisikika angani upande wa mashariki, bibi Nyanjige aliponyanyua uso wake kuangalia angani aliziona ndege kumi zikipita na alipozisoma kwenye mabawa yake aliliona neno TAN na zilikuwa na nembo ya Twiga nyuma yake alijua ndege hizo zilikuwa ni za jeshi la Tanzania.



    Bila kuchelewa alipiga mluzi kwa sauti ya juu ili kuashiria kuwa sasa mambo yalikuwa tayari na palepale makundi yote ya ndege waliokuwa wakizunguka angani walizizingira ndege zote tatu na kuziweka katikati kisha wakaanza kutoboa vioo vya ndege hizo kwa mbele na kuingia hadi ndani ambako walianza kuwashambulia marubani kabla hawajafanya jambo lolote.



    Ndege walifanya hivyo kwa ndege ya kivita moja baada ya nyingine hatimaye ndege zote kumi zilianguka chini na kulipuka! Mamia ya ndege pia walilipuliwa na moto.

    *

    *

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Bibi Nyanjige aliyekuwa bado yu katikati ya kundi kubwa la tembo alishuhudia mashambulizi ya ndege wake na kuhisi ushindi! Lakini ghafla alishtuka alipoona helkopta tano zikiruka kutoka upande mwingine wa msitu na vitu kama mipira ya maji ilichungulia kutoka ndani ya helkopta hizo, alijua tayari vita nyingine ilikuwa imefika.



    ITAENDELEA



0 comments:

Post a Comment

Blog