Search This Blog

Thursday, July 21, 2022

HUWEZI KUUA MAITI - 4







    Simulizi : Huwezi Kuua Maiti

    Sehemu Ya Nne (4)



    Usiku huo kwa bibi Nyanjige hakutaka uwe usiku wa bure, alitaka kuutumia kwa kazi katika zungukazunguka yake bila kutiliwa mashaka alifanikiwa kufika mahali yalipofichwa mabomu na silaha nyingine za kijeshi, alianza kusomba mabomu taratibu na kuyatega sehemu mbalimbali za kambi bila kugundulika, aliyaseti yote yalipuke baada ya masaa mawili.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Hii ndiyo kiboko yao lazima niwamalize hawa watu, nataka siku moja niingie katika kitabu cha orodha ya watu maarufu duniani na huu ni wakati wa mimi kuondoka niwaachie kasheshe yao” Alisema bibi Nyanjige huku akitabasamu.

    Aliondoka kama anakwenda kukojoa na kutokomea porini akijua baada ya masaa mawili kambi lingegeuka tanuru la moto na mamia ya wanajeshi wangegeuka mkaa au matofali ya kuchoma.



    Masaa mawili kama alivyopanga akiwa katikati ya pori aliona moto mkubwa ukiwaka nyuma yake! Akajua tayari kazi yake imekamilika. **************

    Maaskari walizinduliwa na milipuko ya mabomu na kuanza kukimbia huku na kule wakijaribu kuokoa maisha yao! Haikuwa rahisi hata kidogo kwani wengi walilipuliwa na kuwaka kwa moto! Mahema yaliwaka kwa moto na wengi wa wapiganaji walikufa ndani ya mahema yao!



    Mpaka hali inatulia masaa matatu baadaye tayari wanajeshi 150 walikuwa chini wakiwa maiti! Kamanda alinusurika na alizidi kusikitika na kushindwa kuelewa ni kitu gani kilikuwa kikiendelea alianza kuhisi kulikuwa na vibaraka wa bibi Nyanjige kati yao, hakufikiri hata kidogo kuwa bibi Nyanjige ndiye aliyeifanya kazi hiyo kama kikulacho ki nguoni mwako. ***********



    Kulipokucha asubuhi bibi Nyanjige alikuwa katika kijiji cha Kiambali mkoani Tanga, kijiji hiki kilikaliwa na watu wa jamii ya Kimasai peke yao! Kwa magwanda aliyokuwa nayo alijua ni lazima angewatia wasiwasi na wangetaka kumwona sura yake jambo ambalo kwa hakika lingesumbua.



    Hakutaka kujitokeza mchana alichofanya ni kujificha kichakani mchaka kutwa, usiku ulipoingia aliyavua magwanda yake na kuanza kutembea taratibu kuingia kijijini.



    Mtu wa kwanza kukutana naye alikuwa mlevi akitoka kilabuni, mtu huyo alishtuka sana kuona mwanamke yu uchi.

    “We iko nani?”

    “Mimi?” “Ndiyo!”

    “Bibi Nyanj….!” Alitaka kutaja jina lake lakini alipokumbuka kuwa alikuwa akitafutwa na tayari jina lake lilikuwa maarufu midomoni mwa Watanzania alisita kulimalizia.



    “Uuuuuuuuuuwiiiiiiii, saidia, jamani saidia! Mchawi! Mchawi huyu hapa!” Alipiga kelele mzee huyo, alikuwa ndiye mwenye nyumba zilizokuwa jirani na eneo hilo aliendelea kupiga kelele kwa muda mrefu hatimaye watu wengi walijitokeza wakiwa na silaha zao mikononi, wengine mapanga, mikuki na mawe..



    Wananchi wa kijiji hicho walichukia wachawi hivyo walianza kumshambulia bibi Nyanjige kwa mawe na marungu na wengine walimrushia hata mikuki yao, alianguka chini huku akilia.



    “Jamani mie siyo mchawi!” Alisema lakini hakuna aliyemsikiliza watu walizidi kumshambulia kila mtu akiamini bibi Nyanjige alikuwa mwanga!



    Jeshi lilishituliwa sana na vifo vya wanajeshi wake msituni viongozi hawakuelewa ni nani aliyezitungua ndege zao kiasi hicho ingawa waliamini mtambo uliotumika kuzitungua ulikuwa wao.

    Walioshindwa kuelewa bibi Nyanjige aliwezaje kuwashawishi wapiganaji wao mpaka wakafikia uamuzi wa kulisaliti jeshi lao! Siku zote waliamini wapiganaji wao walikuwa waaminifu kupita kiasi.



    Hakuna mtu hata mmoja aliyehisi bibi Nyanjige ndiye alifanya ukatili huo baada ya kuingia katika jeshi lao bila kugundulika.

    Msako mwingine mkali zaidi uliitishwa wanajeshi zaidi ya elfu sita walitumwa kwenda kuuvamia tena msitu kumsaka bibi Nyanjige, bado waliamini alikuwemo msituni! Ni maaskari katika msako wa mara ya pili walioigundua maiti ya askari waliyehisi alizitungua ndege zao ukiwa ndani ya kichaka!



    Kilichopelekea maiti hiyo igundulike ni harufu kali iliyosikika wakati wakipita pembeni mwa kichaka, walipoingia ndani walikuta maiti ya mpiganaji mwenzao ikiwa imelala bila magwanda zaidi ya chupi! Gauni chafu lilikuwa pembeni.



    Walipoliangalia gauni hilo waliligundua kwa haraka kuwa lilikuwa la bibi Nyanjige! Wote walielewa kilichotokea waligundua ni bibi Nyanjige aliyezitungua ndege zao na ni yeye aliyetega mabomu na kuwaangamiza maaskari wenzao! Hasira zilizidi kuwapanda wanajeshi na kila mtu alipania kumpata bibi huyo.

    “Lazima apatikane!”



    Gauni la bibi Nyanjige lilipopelekwa makao makuu ya jeshi, wakubwa walishindwa kuelewa ni uwezo gani aliokuwa nao bibi huyo kizee hadi asumbue jeshi kiasi hicho!
“Alikuwa na nguvu gani mpaka kumuua askari wetu kisha kumvua nguo, nafikiri magwanda yake ya askari aliyavaa mwenyewe ndio akaanza kutungua ndege zetu?” Aliuliza mkuu wa majeshi!



    “Nafikiri ni hivyo sijui hivi sasa atakuwa wapi?” Msaidizi wake Brigedia Mwita alijibu

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Hakuna sehemu yoyote anayoweza kuwa amekimbilia zaidi ya humohumo porini! Hivyo hakikisheni pori lote linazingirwa ili asipate mahali pa kutokea! Na mkimpata naomba maiti yake iletwe hapa makao makuu, tunahitaji kuikausha ili iwekwe makumbusho kwa ajili ya historia ya nchi yetu kwani mpaka sasa siamini kama kuna bibi kizee anayeweza kufanya maajabu kiasi hiki……!” Mkuu wa majeshi alimwambia msaidizi wake na kabla hajamaliza simu yake ililia.



    “Hallow, nani anaongea?” Aliuliza.

    “Ni mimi Brigedia Bukuku!” Alijibu Brigedia aliyekuwa akiongoza msako msituni.

    “Ndiyo Brigedia mnaendeleaje?”

    “Tunaendelea vizuri nilitaka tu kukutaarifu kuwa tayari ule mtambo wa kutungulia ndege tumeupata ulikuwa umefichwa kichakani kabisa!”

    “Vizuri, endeleeni na kazi mpaka mmkamate huyo bibi kizee, yupo hapohapo porini!”

    “Sawa afande!”

    *

    *



    Habari za msako wa bibi Nyanjige zilishaenea kila mahali mjini na vijijini, hapakuwa na mtu asiyefahamu juu ya bibi huyo! Hata katika kijiji cha wamasai cha Kiambali ambako bibi Nyanjige aliendelea kusambuliwa kwa mawe akidhaniwa mchawi, kijana mmoja aliikumbuka sura yake na kupiga kelele akiwaomba wenzake wasitishe zoezi la kumpiga.



    “Nimemkumbuka huyu bibi!” Alisema kijana huyo kwa kimasai.

    “Ni nani?”

    “Ni bibi Nyanjige!”

    “Mama yangu nimekwisha!”Bibi Nyanjige alijisemea moyoni akiwa amelala chini damu nyingi zikimtoka katika majeraha aliyoyapata sababu ya kipigo kibaya alichopewa na wananchi wenye hasira, alijua kutambuliwa kulimaanisha kifo!



    Alijua tayari alishaingia mkononi mwa wanajeshi na kwa zawadi iliyokuwa imetolewa na serikali hapakuwa na njia ya kuwshawishi wamasai wamwachie.

    “Bibi Nyanjige ndiye nani?”

    “Si anayetafutwa kwa mauaji!”

    “Una hakika ndiye huyu?”

    “Ni yeye!” Kijana huyo aliendelea kusisitiza.



    “Sasa tufanye kitu gani?”

    “Mimi naomba tuchague morani watatu ili twende kupeleka taarifa hizi makao makuu ya jeshi waje wamchukue!” Alisema kijana huyo na maneno hayo yalimfikia bibi Nyanjige moja kwa moja, aliomba wazee wa Kimasai wamkatalie kijana huyo lakini haikuwa hivyo, wazee wote walikubaliana na jambo hilo.



    Usiku huohuo kwa kutumia baiskeli morani watatu waliondoka kuendesha baiskeli zao hadi mjini Korogwe ambako waliziacha kwa marafiki na kupanda mabasi kuelekea Dar es Salaam.

    Waliingia jijini saa moja asubuhi na kufika makao makuu ya jeshi saa mbili na nusu ambako baada ya kujieleza kuwa walikuwa na taarifa za mahali bibi Nyanjige alikokuwa walipokelewa vizuri na kuonana na mkuu wa jeshi kama walivyoomba.



    “Yule bibi tunaye!” Ndivyo walivyosema baada ya salamu zao kwa mkuu wa majeshi msaidizi aliyewapokea kabla hawajaenda kuonana na mkuu wa majeshi mwenyewe!

    “Bibi gani?” Aliuliza mkuu wa majeshi msaidizi.

    “Bibi Nyanjige!”

    “Nyanjige?” Aliendelea kuuliza kwa mshangao.



    “Ndiyo!”

    “Mnae nyinyi? Mmempataje wakati kahangaisha jeshi kiasi kikubwa?”

    “Kweli tunaye kama huamini tupatie vijana wako twende nao hadi kijijini kwetu lakini zawadi itakuwa yetu sisi!” Alisema mmoja wa Morani.



    “Hilo si tatizo ili mradi tu awepo kwa sababu mkitusumbua hatutafurahi!”

    “Wewe tupe tu vijana na gari twende nao!”

    “Si vijana bali mimi mwenyewe nitaondoka nanyi!”

    “Tena wewe ndiyo vizuri zaidi!”

    “Haya hebu nisubirini kwanza nije!” Alisema mkuu huyo wa majeshi na kutoka nje ya ofisi na kwenda moja kwa moja kwa mkuu wa majeshi na kumweleza habari za vijana wa kimasai walioingia ofisini kwake.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mkuu wa majeshi hakuiamini habari hiyo aliuona kama uongo fulani na kuomba awaone vijana wa kimasai walioleta taarifa, mkuu wa majeshi msaidizi alitoka kwenda kuwachukua na kuwapeleka ofisi ya bosi wake.



    Mkuu wa majeshi alipowauliza vijana hao maswali majibu yao yaliendeela kuwa yaleyale na walijibu kwa uhakika zaidi, jambo lililowafanya wakuu wa majeshi waamini kila kitu!Hapakuwa na ubishi wala kusita tena bali mkuu wa majeshi alimwamuru msaidizi wake pamoja na wanajeshi wengine waongozane na vijana wa kimasai kwenda kijijini kuona kama kweli bibi waliyedai kuwa nae alikuwa bibi Nyanjige!



    Magari matatu yakiwa na askari wapatao sitini yaliondoka makao makuu ya jeshi kwenda kijiji cha Kiambali, kwa sababu walimfahamu bibi Nyanjige na maajabu yake waliondoka na silaha za kutosha, kila mwanajeshi akiwa na bunduki yake na pia mabomu.

    “Kama ni yeye basi mkamlete akiwa hai!”

    “Sawa mkuu!”

    *

    *



    Kutoka jijini Dar es Salaam hadi kijiji cha Kiambali kupitia Kibaha, Chalinze ulikuwa ni mwendo wa masaa manne waliingia kijijini hapo majira ya saa nane mchana! Wote walishangazwa na hali waliyoikuta, ng’ombe waliokuwa wakikimbia huku na kule mikia ikiwa imenyooka, walionekana kama wamepatwa na kichaa mamia ya watu walikuwa wamelala ardhini wakivuja damu na wengine walikuwa wakichomwa kwa pembe za ng’ombe ardhini, wengi walikuwa wamekufa.



    Dereva aliegesha gari lake na wanajeshi walianza kushuka taratibu kutoka garini bunduki zao zikiwa tayari kufanya kazi, ghafla walishitukia kundi kubwa la ng’ombe kama mia mbili likija kwa kasi kuelekea mahali walipokuwa wamesimama,wanajeshi wote walihisi hatari.



    “Jamani hawa ng’ombe hawana kichaa kweli?” Maaskari waliulizana na kuwageukia vijana wa kimasai.

    “Nyie vijana vipi hawa ng’ombe wenu?”

    “Hata sisi hatuelewi kabisa tuliacha hali ni shwari kabisa hapa kijijini sijui kimetokea nini!”



    Wakati wakiongea hayo tayari ng’ombe walishafika na kuanza kuwashambulia wanajeshi kwa pembe zao kali, walijaribu kupiga risasi lakini haikusaidia ng’ombe walizidi kuja mbio, baadhi ya wanajeshi walirusha hata mabomu yalipolipuka yaliua ng’ombe wachache!Makundi mengine makubwa zaidi ya ng’ombe yalizidi kujitokeza na kuwashambulia wanajeshi! Kifupi hali ilitisha.



    Wakati yote hayo yakitokea mkuu wa majeshi alikuwa bado hajateremka garini, hali aliyoishuhudia ilimtisha, badala ya kushuka alijikuta akifunga mlango wa gari zaidi! Hakuna kilichokuwepo zaidi ya kujiokoa na alilazimika kumwamuru dereva aliondoe gari kuokoa maisha yao.



    Ni wao tu wawili waliokoka hata vijana wa kimasai pia walikufa katika mashambulizi hayo ya ng’ombe! Lilikuwa ni tukio la ajabu katika historia ya Tanzania.



    Dereva aliliendesha gari kwa kasi huku akipiga honi iliyowatisha ng’ombe waliokimbia kulifuata gari, njiani alizipita maiti nyingi za watu zikiwa zimelala chini na wengine wengi walikimbia huku na kule kuokota maisha yao.



    Mkuu wa majeshi na dereva wake walifanikiwa kutoka kijijini ndani ya gari wakiwa salama salimini lakini wenzao wote waliokuwa nao walikufa, jambo hilo liliwasikitisha sana, mpaka wakati huo hawakufanikiwa kuelewa kama kweli bibi Nyanjige alikuwa katika kijiji hicho au la! Kilikuwa kitendawili.



    “Inawezekana kweli yupo na ameitumia elimu yake ya viumbe niliyosikia kuwa anayo kuwatia ng’ombe vichaa ili wafanye mauaji bibi mimi anatisha jamani!” Alisema mkuu wa majeshi msaidizi.

    “Nafikiri inawezekana sasa kitafanyika kitu gani ili bibi huyu akamatwe maana anazidi kuua watu!”



    “Hata mimi nashindwa kuelewa, acha kwanza tupeleke taarifa hii kwa wakubwa, nafikiri kutakuwa na kitu cha kuamua!” Alijibu mkuu wa majeshi msaidizi huku mwili wake ukitetemeka kwa hofu mpaka wakati huo alikuwa haamini kama kweli alikuwa amenusurika katika janga hilo la kushambuliwa na ng’ombe.



    “Hivi kumbe ng’ombe ni hatari eh?”

    “Mimi ndio nimegundua leo kuwa ng’ombe wanaweza kuua kikatili! Tunakula nyama yao kila siku kumbe ni viumbe hatari”

    *

    *



    Bibi Nyanjige hakuwa tayari kuingia mikononi mwa wanajeshi kwani kitendo hicho kwake kilimaanisha kifo! Alikuwa tayari kufa kwa kupigwa na wananchi wenye hasira lakini si kuingia mikononi mwa wanajeshi ambao alijua alishawatia hasira kali kupita kiasi.



    Pamoja na mawazo hayo alishindwa afanye nini ili ajiokoe kwani alizungukwa na idadi kubwa ya wamasai wenye silaha za jadi kama mikuki, pinde na mishale! Alikuwa amepoteza damu nyingi sana lakini bado alihisi kuwa na nguvu mwilini mwake ambazo zingemwezesha kukumbia lakini alisita kuchukua uamuzi huo akiogopa kushambuliwa kwa mikuki na mishale.



    Jua lilizidi kumchoma akiwa amelala ardhini, muda wote alifikiria namna ya kujinasua mikononi mwa kifo lakini alikosa njia! Mara nyingi alishawhi kunusurika vifo katika mazingira magumu lakini siku hiyo alishindwa kuelewa ni kitu gani angefanya kujiokoa!



    Majira ya saa saba ikiwa ni saa moja tu kabla magari ya wanajeshi hajawasili kijijini, wazo lilimwijia bibi Nyanjige kichwani mwake, wazo la kutumia mifugo kama ng’ombe iliyokuwa mingi kijijini hapo kujiokoa! Aliielewa lugha ya ng’ombe na alijua ni maneno gani huwatia ng’ombe vichaa na hasira.



    Baada ya fikra hizo alikunja mdomo wake na kutoa muungurumo kama wa ng’ombe ambao kwa mbele uliishia na maneno “uwooou” watu wote waliokuwa wamekusanyika eneo hilo kumshangaa bibi Nyanjige walicheka walipomwona akifanya kitendo hicho! Alirudia kufanya hivyo mara nyingi na kadri alivyozidi kutoa muungurumo huo ndivyo watu walivyozidi kucheka! Hawakuelewa ni nini alichokuwa akifanya.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Ghafla bila kutegemea wamasai walishtukia ng’ombe wengi wakija mbio kuelekea eneo hilo huku mikia yote ikiwa imesimama wima nyuma yao! Dalili kuwa ng’ombe walikuwa wamepatwa na kichaa.

    Kijiji cha Kiambali kilikuwa cha wafugaji wa Kimasai tupu na kilikuwa na ng’ombe wasiopungua 10,000 ukiondoa ndama 5,000! Ng’ombe wote waliruka kutoka mazizini mwao na kukimbilia kuelekea mahali sauti ya bibi Nyanjige ilikokuwa ikitokea, nao walikimbia huku wakitoa mlio huohuo ambao hatimaye ulisambaa kijiji kizima!



    Mlio huo ulikuwa ni matusi makubwa kwa ng’ombe wote kijijini humo, uliwatia hasira mbaya sana ng’ombe wote na kukimbia kwenda mlio ulikotokea ili kupambana! Wanakijiji hawakuelewa lolote kwa sababu wao hawakuelewa lugha ya ng’ombe pamoja na kuwa waliishi nao, ilihitaji elimu kubwa sana kuelewa kilichokuwa kikitokea.



    Ng’ombe walipofika eneo la tukio bibi Nyanjige alitoa tena mlio mwingine na ng’ombe wote walianza kuwashambulia wamasai waliokuwa eneo hilo kwa kutumia pembe zao zenye ncha, wamasai wengi walikufa mbele ya macho ya bibi Nyanjige!

    “Nimesurika tena!” Alisema bibi Nyanjige wakati akinyanyuka kutoka ardhini ni yeye peke yake ndiye hakushambuliwa na ng’ombe siku hiyo kila ng’ombe walipomsogelea alitoa mlio ulioishia na “ssssssssss!” na ng’ombe wote walimwacha na kuwashambulia wamasai.



    Baada ya kunyanyuka bibi Nyanjige alitembea kuelekea msituni huku akichechemea! Mwili wake wote ulimuuma na ulijaa majeraha sababu ya kipigo alichopata! Mbele kidogo kama kilometa moja alijikutaka akitokeza barabarani alikuwa akisikia kizunguzungu sababu ya kupoteza damu nyingi na alihisi asingeweza kuendelea zaidi na muda mfupi baadaye alianguka chini.



    Ghafla alisikia muungurumo wa gari likija kwa mbali na alipojaribu kunyanyua kichwa chake kuangalia ulikokuwa ukitokea muungurumo huo alishindwa na kuendelea kulala chini! Giza lilikuwa limeyafunika macho yake

    “ Ni kitu gani kile pale!” Dereva alimuuliza msaidizi wa mkuu wa majeshi baada ya kuona kitu kama mwili wa binadamu umelala chini!



    “Au ni mmoja wa watu waliojeruhiwa na ng’ombe?”

    “Hapana watu wa kijijini watakuwa hawajafika huku!”



    “Sasa ni nani? Halafu naona yupo uchi wa mnyama! Hebu chukua bunduki yako tukamwangalie!”Mkuu wa majeshi alisema na wote wawili walichukua bunduki zao na kuanza kusogea mahali ulipolala mwili ule!



    Walishangaa kukuta ni mwili wa bibi kizee! Dereva aliusukuma kwa mguu wake wa kulia ukalala chali, hawakuamini macho yao walipokuta alikuwa ni bibi Nyanjige!

    Bunduki zote mbili zilimlenga bibi Nyanjige ardhini na hasira ilizidi kuwapanda mkuu wa majeshi na dereva wake, mioyo yao iliwaambia wammiminie idadi kubwa ya risasi ikilinganishwa na unyama alioufanya bibi kizee huyo lakini walishindwa kufanya hivyo baada ya kufikiria agizo walilopewa na mkuu wa majeshi.



    “Ikiwezekana mmlete akiwa hai ili akaushwe na kuwekwa jumba la makumbusho...!” Kauli hiyo ya mkuu wao ilikuja vichwani mwao.

    “Nyie mbwa hebu nipigeni hizo risasi zenu ili mimi nife nipumzike! Au hamjui kutumia bunduki nini? Nyie wapumbavu sana yaani bibi kama mimi nimewasumbua kiasi hicho?” Bibi Nyanjige alisema maneno ya kutia hasira ili kuwalazimisha wampige risasi! Alitamani kufa kwa risasi kuliko kuingia mikononi mwa wanajeshi.



    “Para tat lita-pa! Pa! Pa!”Risasi zilisikika zikilia

    “Mkuu umefanya nini sasa? Umesahau maneno tuliyoelezwa kuwa tumepeleke akiwa hai?”Dereva aliuliza.

    “Hasira imenipanda sana!” Alisema msaidizi wa mkuu wa majeshi baada ya kumimina risasi.



    “Sijafa bado nipigeni za kichwa!” Alisema bibi Nyanjige huku akicheka kwa dharau.

    Mkuu wa majeshi alijiandaa tena kumimina risasi lakini dereva wake alimuwahi na kumnyang’anya bunduki yake!



    “Ha! Ha! Ha! Mmeshindwa kuniua sasa subirini mimi niwamalize!” Alisema bibi Nyanjige.



    Tukio la bibi Nyanjige kutoroka kwa mara nyingine liliwashangaza viongozi wote wa jeshi na kuwafanya washindwe kuelewa bibi huyo alikuwa wa aina gani kwani alifanya mambo makubwa yasiyolingana na umri wake kabisa! Vichwa viliwagonga wakuu wa jeshi! Ilikuwa ni mara ya tatu bibi Nyanjige kutoroka mikononi mwao. Jambo hilo liliwakera sana.



    Maiti zote zilizokufa kwa kuumwa na nyuki zilitolewa ndani ya chumba na kufanya idadi ya watu waliokufa katika harakati za kumsaka bibi Nyanjige kuwa zaidi ya elfu sita! Jambo hilo lilimtia hasira kila mtu katika jeshi, ilikuwa ni aibu kwa jeshi kubwa kama hilo kushindwa kumkamata kibibi kama bibi Nyanjige!

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kufuatia tukio hilo Mkuu wa majeshi hakuwa na jambo jingine la kufanya zaidi ya kujiuzuru wadhifa wake mara moja na aliteuliwa mwingine palepale! Hiyo ilifanya wakuu wa majeshi waliojiuzuru sababu ya bibi huyo kufikia wawili!



    “Hii ni aibu tena aibu kubwa sana kwa jeshi lenye watu makini kama mimi, naahidi nitamtia mbaroni tu! Subirini!’ Alisema mkuu mpya wa majeshi baada ya kuapishwa na wanajeshi wote walimpigia makofi!



    Siku iliyofuata msako mkubwa ulitangazwa nchi nzima kumsaka bibi kizee aliyeshindikana kutiwa mbaroni! Mikoa yote ilitaarifiwa na ni mchana wa siku hiyo hiyo taarifa zilifika makao makuu ya jeshi kutoka mbugani Mikumi kuwa gari alilotoroka nalo bibi Nyanjige lilikutwa limetelekezwa karibu na lango la kuingilia kwenye Mbuga ya Mikumi! Taarifa hiyo ilimaanisha wazi bibi Nyanjige alikuwa amekimbilia ndani ya Mbuga ya Mikumi.



    “Askari wote waliopo katika kikosi cha jeshi la 201 KJ mkoani Morogoro waondoke haraka iwezekanavyo kwenda mbugani Mikumi na waliopo Kilosa pia wapelekwe huko huko Mikumi, jeshi jingine nitaliongoza mimi kutoka hapa Dar es Salaam nina uhakika kufikia kesho huyu bibi atakuwa amekwishatiwa mbaroni!”Alisema mkuu wa majeshi baada ya kupokea taarifa hiyo.

    Amri hiyo ya mkuu wa jeshi ilitekelezwa kwa haraka, wanajeshi wa kambi ya Morogoro na wa Kilosa waliondoka katika magari na kupelekwa hadi mbugani na mamia ya wanajeshi walisafirishwa kwa magari ya jeshi kutoka Dar es Salaam na Dodoma hadi katika mbuga hiyo hiyo kwa lengo la kumsaka bibi Nyanjige.



    Kwa idadi hiyo ya askari wengi walikuwa na uhakika bibi Nyanjige angekamatwa.

    Helkopta zisizo na idadi zilipita angani zikimsaka bibi huyo machachari, ulikuwa ni msako mkali kuliko msako mwingine wowote uliowahi kufanyika katika historia ya Tanzania! Hata msako wa porini Kongo haukuwa mkali kiasi hicho! Wanajeshi wote walikuwa na hasira kali ya kutaka kumtia bibi Nyanjige mikononi mwao na kumuua kikatili, waliamini alikuwa ameliaibisha jeshi.



    ************** Kwa siku tatu mfululizo kulikuwa na hekaheka ya aina yake mbugani, kila kichaka kilichoonekana mbele ya wanajeshi kilifyekwa na kusabararishwa ili mradi ulikuwa ni msako wa bibi Nyanjige lakini bado hakuonekana mahali popote, wanajeshi hawakukata tamaa sababu walijua kwa uhakika alikuwa ndani ya pori hilo.



    “Mpaka tumpate haiwezekani hata kidogo jeshi kubwa kama hili lishindwe kumkamata bibi kizee wa aina hii tu!”

    “Ingawa historia yake inashangaza ni lazima atiwe mbaroni, safari hii hatumpeleki akiwa hai tena, tutamuuua huku huku porini tu!”



    “Kweli sababu tukimfisha watataka kumkausha ili wamhifadhi, ninajua atawatoroka na kutufanya sisi kuacha familia zetu kuja kumtafuta huku porini, hii haiwezekani hata kidogo ni lazima tumuue!”Wanajeshi waliendelea kuongea huku wakiendeleza msako wao porini, kwa kutwa nzima walipita kila mahali porini wakimtafuta bibi lakini hawakufanikiwa kumpata wala kuona dalili yoyote ya kuonyesha mahali alikokuwa. Ikawa usiku ikawa asubuhi siku ya kwanza ikapita!



    Siku ya pili kama ilivyokuwa imepangwa na mkuu wa majeshi aliyekuwa pamoja na wapiganaji wake msako uliendelea, wanajeshi walikuwa wamechoka lakini waliendelea na msako wao bila kukata tamaa, azimio lao likiwa ni hakuna kurudi nyumbani bila bibi Nyanjige, pamoja na kukatakata miti na hata kuchoma hifadhi kwa moto bado hawakufanikiwa kumwona bibi Nyanjige, walishindwa kuelewa mahali alipokuwa!



    Wanajeshi wasiopungua elfu tatu walimtafuta bibi Nyanjige mbugani kwa siku zote tatu bila mafanikio hatimaye walianza kupoteza matumaini kabisa lakini siku ya nne asubuhi waliibukia sehemu iliyokuwa wazi na iliyolundikwa udongo mwingi kama tripu za mchanga zilizomwagwa tayari kwa ujenzi.

    “Mh!”Mmoja wa maaskari aliguna

    “Vipi afande?”



    “Nashangaa ni nani amerundika mchanga huu hapa?”

    “Labda watu wa hifadhi walitaka kujenga hoteli!”

    “Hoteli?”

    “Ndiyo!”

    “Hoteli eneo hili alale nani?”

    “Watalii!”

    “Hapana, sitegemei hata siku moja kama kunaweza kuwa na mtalii wa kulala katikati ya pori kiasi hiki!”



    “Aisee hebu angalieni pale!” Alisema mmoja wa wanajeshi akiwaonyesha shimo kubwa lililokuwa mbele yao.

    “Shimo?”

    “Ndiyo!”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Sijui la nini?”

    “Hebu twende tukalione!” Waliongozana wakitembea kuelekea mahali lilipokuwa shimo hilo, wote walibaki midomo wazi kukuta shimo refu likielekea ardhini na mwisho wake haukuonekana, lilikuwa shimo lenye uwezo wa kupitisha mtu mzima na pembeni yake kulionekana alama za miguu.



    “Mh jamani hii si miguu ya mtu?”

    ‘Ndiyo tena kwa jinsi miguu hii ilivyo midogo lazima ni ya mwanamke!”

    “Inawezekana kabisa!”

    “Lakini nani alichimba shimo hili?”

    “Hata mimi sijui labda ni wachimbaji wa madini walitaka kuufanya huu mgodi!”

    “Hakuna mtu mwenye akili timamu anaweza kuja porini kwenye wanyama wakali kiasi hiki kuanzisha mgodi labda kama anataka kuliwa na simba!”

    Wanajeshi karibu mia mbili walikusanyika eneo hilo na kuendelea kulishangaa shimo lililokuwa mbele yao halikuwa la kawaida hata kidogo, kifupi lilitisha na walijua ni lazima ndani yake kulikuwa na kitu, wanajeshi wengine walihisi bibi nyanjige alikuwa ndani yake.



    “Mimi nafikiri hii miguu ni ya huyu bibi Nyanjige hakuna mwingine, hebu nifungeni kamba mimi niingie hadi ndani nikachanguze ila nikitingisha kamba basi mjue nina matatizo mnivute haraka!”Alisema mwanajeshi huyo na kamba ililetwa haraka na akafungwa kiunoni na kuanza kushushwa taratibu kuingia shimoni! Kamba ilikwenda hadi ikafika mwisho bila mwanajeshi huyo kufika chini, shimo lilionekana kuwa refu na lilikuwa na kiza kinene alitumia tochi kuona ndani, ilibidi wamvute haraka na kumtoa hadi nje.



    “Vipi afande?”

    “Jamani huko ndani ni kiza kitupu na shimo bado linaendelea sijui ni kitu gani kimechimba shimo refu kiasi hiki!”

    “Huko ndani hujaona dalili yoyote ya bibi Nyanjige?”

    “Hapana ila kuna alama za mtu alikuwa akikanyaga ukutani akishuka shimoni!”

    “Umeona alama za miguu?”

    “Ndiyo tena na mikono!”

    “Sasa?”



    “Sijakata tamaa unganishe kamba nne ili iwe ndefu zaidi niingie tena, ninafikiri bibi yupo humuhumu shimoni!”Alisema askari huyo huku akitabasamu, alionekana jasiri kupita kiasi

    “Au tudumbukize bomu ndani ili ateketee?” Aliuliza mkuu wa majeshi na wanajeshi waligawanyika makundi mawili juu ya suala hilo wengine wakisema ni sawa lakini wengine walikataa na kufanya afande aliyejitolewa atumbukizwe tena.



    Palepaple kamba iliunganishwa na kuwa ndefu, afande huyo aliyeitwa Alphonce kwa mara nyingine alitumbukizwa shimoni, safari hi alifika hadi chini akimulika kwa tochi yake lakini alipotua tu chini alishangaa kusikia akikabwa na kitu kama mzizi mkubwa shingoni.



    Pumzi ilianza kupungua baadaye na baadaye alishindwa kabisa kuhema, macho yakamtoka, kabla hajakata roho alisikia sauti ya mwanamke akicheka kwa sauti ya juu.

    Baada ya kuliacha gari kwenye lango la kuingilia mbugani bibi Nyanjige alikimbia huku akichechemea hadi katikati ya mbuga ambako alikuta kundi kubwa la pundamilia, alipiga mluzi mrefu na wa ajabu Pundamilia wote walisogea karibu yake na kumzunguka!Lengo lake lilikuwa ni kufika katikati ya pori kwenye wanyama wengi ili ajichimbie huko na kuunda jeshi jingine kali la wanyama na kupambana na jeshi la serikali kama wangejaribu kumsaka tena. Alimshukuru Mungu kwa elimu ya viumbe aliyokuwa nayo bila elimu hiyo alijua asingekuwa hai.



    “Jeshi nitakalounda safari hii litaushangaza ulimwengu huu! Nataka niache historia nyuma yangu nataka dunia inielewe na nikifa watu wote waseme bibi nyanjige aliishi na kuusumbua ulimwengu nataka nirudishe heshima ya mwanamke iliyopotea siku nyingi!”Aliwaza bibi Nyanjige akiwa katikati ya kundi kubwa la pundamilia walioketi chini na kuwazunguka, heshima kutoka kwa wanyama ilikuwa ni ileile aliyopata msituni Kongo.



    Mahali alipokuwa palimhakikishia usalama lakini bado alikuwa na wasiwasi wa kusakwa! Gari aliloliacha kwenye lango la kuingilia mbugani lilitosha kabisa kuonyesha mahali alikokuwa na hivyo kuendelea kusakwa.

    “Kama ni hivyo inabidi nisogee mbele zaidi na haraka iwezekanavyo hawa washenzi lazima watakuja, hilo nalijua wazi!”



    Alinyanyuka haraka na kumchagua pundamilia mmoja mwenye nguvu kati ya Pundamilia waliomzunguka na kupanda juu yake kama vile watu wapandavyo farasi, huo ndio ulikuwa usafiri wake hata wakati akiwa katika msitu huko kongo!

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Alimshika mkia na Pundamilia na kuanza kuukunja! Kitendo hicho kilimfanya Pundamilia aondoke kwa mwendo wa kasi ya ajabu,bibi alizidi kuukunja mkia wakipita katikati ya mbuga na kupishana na wanyama wengi wakali lakini hapakuwa na wasiwasi wowote sababu wanyama wote walimtii, mbele zaidi alitokeza katika sehemu ya wazi na aliuachia mkia wa Pundamilia akasimama.



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog