Search This Blog

Thursday, July 21, 2022

MTU WA UFUKWENI (THE BEACH MAN) - 2

 







    Simulizi : Mtu Wa Ufukweni (The Beach Man)

    Sehemu Ya Pili (2)



    Miaka ilizidi kukatika na umri uliongezeka. Ilikuwa tayari miaka kumi imepita ikimaanisha kuwa tayari Ramson alikuwa ameshamaliza kidato cha sita. Majibu ya kujiunga na Chuo Kikuu hayakumpa nafasi hiyo, hivyo kumfanya aendelee na shughuli za shamba. Mengi yamepita magumu na ya kuumiza dhidi yake kijijini hapo. CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Hakukuwa na nafuu yoyote kuhusiana na shutuma juu yake kuwa yeye ni mwizi wa nazi za watu, pamoja na mifugo kama vile kuku, mbuzi na ng’ombe. Vitu hivyo sio kwamba vilisingiziwa kuibiwa tu, bali ni kweli kabisa vilichukuliwa lakini lilikuwepo genge la wizi lililofanya kazi hiyo. Kwa sababu ya tabia ya uvivu Wanakijiji wa Taabu ya nini hawakutaka kupata tabu ya kuchunguza. Hivyo shutuma zote zilitupwa kwa Ramson. Ramson akawa Gumzo mitaani, mashambani, mpaka kwenye visima vya maji. Kama kulikuwa na habari kila wakati basi habari zote zilimhusu Ramson.

    Ramson alikuwa kila siku akiomba Mungu siku zote ili ukweli ujulikane na kumtakasa mbele ya wanakijiji hao waliomchukia. Kijiji kilimchukia sio Ramson tu bali hata Mzee Kihedu na mkewe kwa shutuma kuwa alikuwa anafuga jambazi nyumbani kwake. Vijana walijitenga na Ramson naye pia alijitahidi kujilinda kila wakati akiogopa kudhuriwa. Genge la akina Alen lilizidi kufanya uhalifu kwani lilikuwa tayari na kinga; Kinga yao kubwa haikuwa hirizi ya kichawi bali Ramson alikuwepo kuzipokea shutuma zote!

    “Mambo haya yatakuwa kwangu mpaka lini babu?” Aliuliza Ramson siku moja wakiwa wamekaa mezani na babu yake wakipata chai ya asubuhi. “Wewe vumilia tu mjukuu wangu, Mungu hamfichi mnafiki siku moja kila kitu kitakuwa wazi!” Alijibu babu yake. “Ni sawa babu hayo unayoyasema lakini mambo haya yamedumu kwa muda mrefu sana na kila siku maadui wanaongezeka juu yangu.

    Sijui nifanyeje ili Genge hili linalofanya uhalifu hapa kijijini likamatwe na kutiwa mbaroni? Askari wetu hapa kijijini nao wamekaa tu kama raia, sina shaka kuwa inawezekana kuwa wanashirikiana na hawa wahalifu.. Kwakweli haki haiwezi kupatikana mapema juu yangu kwa mzigo huu wa lawama niliotwishwa bila kujulikana nitautua lini! CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Unajua babu kila wakati ninafikiri kujiunga na jeshi la Polisi ili siku moja nije kukisafisha kijiji chetu maana kimechafuka kwa uovu! Lakini ni ajabu kuwa maovu hayo yote amebebeshwa mtu mmoja tu!”Alisema Ramson kwa upole wenye Uchungu mkubwa. “Iko siku kila kitu kitakuwa shwari mjukuu wangu, tuendelee kumwomba Mungu atatusaidia.” Hayo ndiyo maneno pekee babu yake Ramson aliyokuwa akimwambia Mjukuu wake kila wakati.



    * * *

    Ilikuwa ni mapema sana asubuhi kuliposikika zogo na kelele kutoka kona moja ya kijijihiki cha Taabu ya nini. Kelele zilizidi kuongezeka na watu walikuwa kama vile wako kwenye maandamano. Sauti hizi zilisikiwa vema na Ramson na babu pamoja na bibi wakati wakijiandaa kwenda shambani. kila baada ya muda kidogo kelele hizi ziliongezeka na kusogelea makaazi yao.

    “Kuna nini leo mbona kuna maandamano?” Aliuliza bibi Namkunda baada ya kuchungulia dirishani na kuona watu wengi vijana kwa wazee, mbeleyao akiwepo mwenyekiti wa kijiji. “Ngoja nitoke nione kuna nini asubuhi yote hii, alisema hivi huku akifungua mlango na kutoka nje. nyuma yake alifuatiwa na Ramson! “Hatumtaki Ramson ahame kijiji hiki!!.. Ramson hahitajiki katika kijiji cha Tabu yanini! atatufilisi.

    Ramson ni mwizi hatumtaki ama sivyo tutamwangamiza!!!”Hizo ni nyimbo zilizokuwa zikiimbwa na wanakijiji waliokuwa tayari wameizingira nyumba ya Mzee Kihedu. Umati wa watu ulijazana nje ya nyumba hiyo huku wakipiga kelele na Mwenyekiti akiwa kasimama mbele ya watu hao kwa hasira. “Jamani kuna nini tena asubuhi yote hii?” Aliuliza Mzee Kihedu kwa hamaki kidogo!!

    “Mzee Kihedu miguu yote hii unayoiona imekanyaga hapa ni kwa sababu tumefikia mwisho kukaa na mjukuu wako katika kijiji hiki. Wizi wake akaufanyie huko mbali lakini kijijini hapa aondoke.” Alisema Mwenyekiti kwa ghadhabu sana huku akiitikiwa na watu wote waliofika hapo. “Kwani Ramson kafanya nini tena? Unajua ndugu mwenyekiti habari zote zinazoongelewa si vizuri zichukuliwe juu juu bila ya kufanyiwa uchunguzi! Inawezekana Ukweli ukajulikana.” Alisema Mzee Kihedu kwa utaratibu kama ilivyo kawaida yake.

    “Mzee Ninakuheshimu sana! sidhani kuwa kuja kwangu hapa na watu wote hawa unaweza kutushawishi kwa Propaganda zako ili tumwache kijana wako aendelee kuwatia hasara wanakijiji wangu. Mimi mwenyewe ameshaniibia mbuzi wangu wawili. Nasema inatosha Ramson aondoke huo ndio uamuzi pekee wa kijiji!”

    Alipomaliza kuzungumza aliwaamrisha watu wake watawanyike. “Nafikiri umenielewa, aondoke mapema sana maana sitegemei kuwa baada ya amri hii ataendelea kuwepo kesho kijijini hapa.” Alisema Mwenyekiti wakati watu wakitawanyika huku kila mmoja akisema lake kuhusu Ramson. Hali ilikuwa tete sana kwa familia hii kutokana na amri hiyo mbaya iliyotolewa dhidi ya Ramson.

    Kila mmoja alichanganyikiwa na kukosa pa kuanzia ili kulitatua swala hili. Wazo la kuhama halikuwepo kwenye akili zao kwa maana hakukuwa na sehemu nyingine ambayo Ramson anaijua ya kuishi. Alipopajua tangu utoto wake ni hapo kijijini. Kijiji cha Tabu yanini ndipo mahali Mzee Kihedu alipozaliwa na familia yake aliikusudia ikae hapo na kuangalia mali zake, mali alizozitafuta kwa muda mrefu sana.

    Hakuwa na mrithi zaidi ya Ramson vile vile hakuwa na ndugu wa karibu zaidi ya Ramson. Hali hii ilikuwa na utata wa aina yake. Alihisi kuwachukia watu wa kijiji hiki na mwenyekiti wao.“Ninashindwa nifanyeje kwa sasa lakini babu usiwe na wasiwasi, mambo yote yatakuwa shwari tu.” Alisema Ramson akiwa kasimama kwenye pembe ya nyumba, babu yake akiwa amekaa kwenye kiti akiwa kajiinamia. “Unafikiri tufanyeje mjukuu wangu kuhusu jambo hili? Mazao ndio hayo bado madogo mavuno bado mpaka labda baada ya miezi miwili.

    Juzi ndio tumeuza ng’ombe wetu wanne wa kienyeji ili tununue Ng’ombe wa Kisasa.Tulifurahi sote kuwa sasa tutapata maziwa kwa wingi ya kuuza. Hapa nilipo sina akiba ya hela nyingi za kusema kuwa uende kupangisha nyumba mjini na kufanyia biashara. Unafikiri tufanyeje?” Aliuliza Babu akiwa anatafakari kwa undani cha kufanya. “Babu yangu na bibi naomba msihuzunike juu ya hili. Nitakwenda mjini na kuangalia ninini cha kufanya halafu nitajitahidi kuja ili nitoe taarifa kuwa niko wapi.

    Najua Mungu amenipangia maisha mazuri sana mbali na kijiji hiki cha Tabu yanini. Maisha ni popote babu. Kuna msemo usemao kuwa ‘’Mwanamme hana kwao’’. Sijajua kuwa ni msemo wa busara sana, lakini haya ya leo yanaufanya usemi huo kuwa na maana kwangu.

    “Hapana Ramson ninawaza baadaye niende ofisini kwa mwenyekiti ili niongee naye aitishe kikao cha kamati ya kijiji tuyazungumzie mambo haya. Sipendi uondoke na kukaa mbali na mimi tumekuwa wazee sasa mimi na bibi yako wewe ndio Mwangalizi wetu na mrithi wa mali hizi.” Alisema Mzee Kihedu kwa hamaki!Sawa kabisa unavyosema, mpiganie mjukuu wako. Uhalifu wafanye watoto wao wamsingizie mjukuu wangu? Kwanini lakini mambo haya mabaya hayachunguzwi ninani wanaohusika badala yake watu wanafuata majungu tu?” Alisema bibi Namkunda kwa kufoka.

    “Bibi achana nao! Babu naomba sana usiende kulizungumzia jambo hili ofisini kwa mwenyekiti. Utaonekana kama unanitengenezea mazingira ya kuwepo kijijini hapa kama mjukuu wako na si kama mtu mwema. Acha nikajaribu maisha sehemu nyingine.” Ramson Aliingia ndani na kuchukuwa baadhi ya nguo zake na kuziingiza ndani ya begi lake. Baadaye alichukuwa akiba yake ndogo ya hela kama laki moja na ishirini aliyoipata kwa kuuza magunia mawili ya karanga.

    Pesa hii alikusudia aifanyie bustani za mbogamboga kando ya kisima kilichopo shambani kwao. Lakini baada ya kutokea matatizo hayo akazifutika mifukoni zikamsaidie mbele ya safari. Kisha baada ya kufungasha vitu vya muhimu na kuweka kwenye begi lake dogo alimuaga babu yake na bibi yake kuwa anaondoka. Bibi yake alimpatia kiasi cha Shilingi elfu ishirini na babu yake alimpa kama Shilingi laki mbili na kumtaka aende lakini atakapopata nafasi awe anarudi kuchukuwa fedha ya matumizi au mtaji pale mambo yatakapokaa vizuri.

    Walimwombea heri na kumtakia baraka nyingi. Machozi yaliwatoka kwa huzuni pale walipokuwa wakiagana kwa kukumbatiana. “Msijali sitakuwa mbali na hapa. nitakuwa hapo mjini Tanga na sitaacha kuwatembelea na kuwajulia hali zenu.” Alisema Ramson kisha akabeba begi lake na kuanza safari kwa mwendo wa haraka!

    * * *

    Ilikuwa ni maisha ya Geto ambayo hakuyaweza, wala hakupata kwa haraka jambo la kufanya hapo mjini. Alipotoka kijijini kwao hakusumbuka kumpata rafiki. Tayari alikuwa na rafiki yake aitwaye Richard Rafiki huyu walisoma naye Kidato cha tano na cha sita katika shule ya Tanga Technical Secondary School. Richard alikuwa akiishi Makorora.

    Baada tu ya kufika mjini mtu wa kwanza kumtafuta alikuwa ni Richard. Urafiki wao walipokuwa Shuleni ulifanyika kama undugu, kwani walisaidiana kwa mengi. Walisoma pamoja na pia waliazimana vitabu na kusaidiana katika matatizo madogo madogo. Waliishi vizuri sana katika chumba cha Richard, wakashirikishana mawazo kuhusu maswala ya maendeleo. Kwa bahati mbaya wote hawakuwa wamepata nafasi ya kuchaguliwa kwenda Chuo kikuu. Hatua waliyoifikiria ambayo ingewawezesha kupata kazi ilikuwa ni kuandika barua katika mashirika mbalimbali na makampuni. CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Njia hii ilikuwa ni ndefu sana japo kila mahali walipewa matumaini aidha kwa kuitwa kwenye majaribio, pengine waliahidiwa kuwa nafasi zikipatikana za kazi watajulishwa. Miezi mitatu ilipopita bila mafanikio yoyote Ramson alipata maamuzi mapya. “Ndugu yangu mimi nimechoka kabisa kusubiri hapa kwa muda wote huo. Unajua tukiwa tunasubiri kitu fulani huku tukiwa tunakitu kingine tulichoshika kuna unafuu, kuliko kuangalia hicho kimoja?” Alisema Ramson siku moja wakiwa wanatoka katika ofisi moja ambapo majibu ya kuomba kazi hayakuwa mazuri. “Mawazo yako ni ya kweli kabisa japo sasa tukiangalia kwa haraka tushike kipi kwa wakati huu? Pesa ndiyo hiyo imeisha kwa upande wako na wangu. Na mimi nimechoka kwenda kumwomba baba mkubwa ambaye kabla hajakusaidia anatanguliza masimango kwanza.” Alisema Richard kwa namna ya kukata tamaa.

    “Mimi naona twende mwahako kuna bonge ya ufukwe! Nilikwenda pale wakati tulipokuwa shuleni, nikatamani sana siku moja kama nikifanikiwa nipatengeneze Beach ambayo watu wangelipia huduma ya kuogelea. Nilizingatia yale wanayofanya watu wa Mombasa. Siku moja nilikwenda huko na babu yangu Alipomtembelea rafiki yake. Nilitembezwa na marafiki niliowakuta pale mpaka kwenye fukwe mbalimbali.

    Kila ufukwe kulikuwa na biashara zilizokuwa zinaendeshwa na vijana. Wanachofanya vijana wale ni kutengeneza vibanda vidogo vidogo na kujinunulia mipira ya ndani ya matairi ya gari; kisha baada ya hapo huweka maji safi na sabuni kwenye vibanda vile. Wakishafanya hivyo labda huongeza na viti kadhaa vya Plastiki na kuvipanga vizuri. Tuko pamoja mpaka hapo?” Aliuliza Ramson kwa utani.

    “Tuko pamoja ninaisikiliza vizuri hadithi yako ya Mombasa endelea mtu wangu, ehee wakishaweka viti ndio wanapataje hela baada ya hapo?” Aliuliza Richard. Yaani nakwambia wale watu wanatengeneza hela sijapata kuona.” Watu wanapokuja kuogelea ufukweni hapo wanawakaribisha kwenye viti wakae, kisha huwashawishi kama wanataka kuogelea wawape mipira ya kujifunzia kuogelea. Na wengi kipindi cha joto hupendelea kuogelea kama tu watahakikishiwa usalama wa vitu vyao yakiwepo mavazi.” Kisha baada ya kuogelea huelekezwa yalipo maji safi na sabuni. Mtu mmoja anaweza kulipishwa pesa ya kukaa kwenye kiti, kuogelea na baadaye kujisafisha na maji safi. Jumla ya bei ya huduma hizo zote ni hela nzuri, ambapo wakitokea kama watu kumi na tano ni kiasi kinachokuwezesha kutumia kwa wiki moja.

    Mimi naona tukibuni mradi huo Mwahako utakuwa ni mzuri zaidi ya kuajiriwa.” Alihitimisha Ramsoni kutoa somo kwa Rafiki yake. “Ni ndoto nzuri sana rafiki yangu! Ndoto ya matumaini mema ya mafanikio kwa njia hiyo. Lakini kwangu ni ndoto tu kama ndoto nyingine tena za mchana kweupe! Ndoto za namna hii huitwa ndoto za mchana! Alisema hayo Richard Kwa dhihaka kisha akasafisha koo lake na kuendelea.. “Huwezi wewe kufananisha Tanga na Mombasa kwenye maswala ya Beach! Fukwe za wenzetu zina viwango na watalii wengi hupenda kuzitembelea kwa jinsi zinavyovutia.

    Uwekezaji wa wakenya kwenye Beach zao ni wa faida kubwa kwa sababu unaingiza fedha nyingi za kigeni kwa kupitia watalii. Usione watu weusi wengi wanakuja katika fukwe hizo kwa kufurika. Ni kwa sababu kuna watalii. Wengine hujipatia ajira humo na marafiki, ambao baadaye huwapa nafasi za kuwatembelea katika nchi za kwao. Wengine pia hupata bahati ya wachumba wa kizungu wakike au wakiume. Yote haya hufanyika katika fukwe hizo.

    Hii ndiyo sababu wengi huvutwa kwenda kule ufukweni. Labda wale wanaoenda bila makusudio hayo huenda tu kustarehe kwa sababu fukwe zenyewe ziko viwango umenipata rafiki yangu? Hayo ni machache ya mengi niliyoyataja kuhusu fukwe za wenzetu. Ndio maana nikakuambia kuwa mawazo yako ya kuweka biashara kwenye ufukwe wa Mwahako hapa Tanga ni ndoto nzuri sana lakini ni ndoto ya mchana!”

    Alisema Richard na kupuuza wazo la rafiki yake.“Nimekusikia rafiki yangu ila nia yangu ni kwenda kufanya kazi hiyo kwa sababu nijuavyo mimi ni kwamba hata Mbuyu ulianza kama mchicha. ukubwa na umaarufu wa Fukwe za wenzetu haukutokea tu bila kutengenezwa.

    Na si ajabu lilikuwa wazo la mtu mmoja ambalo baadaye limekuwa kama cheche ya kuambukiza moto kwa maeneo mengi ya Fukwe zilizozunguuka ukanda wote wa Pwani ya Mombasa na popote pengine duniani. Wazo langu ni cheche ndogo sana labda kama tu njiti ya kiberiti mbele ya msitu uliofunga giza.

    Lakini mara baada ya muda fulani kila kitu kinaweza kikatazamika kivingine. Hayo ndiyo maoni yangu kuhusu maendeleo. Maendeleo hayatokei kwa miujiza ya Mwenyezi Mungu bali maendeleo hutengenezwa na watuwenyewe.TukiangaliaHistoria ya mambo makubwa yanayoonekana yakimaendeleo duniani leo yanatokana na wazo. Ndege zinazoruka angani leo zinatokana na wazo la mtu mmoja tu. Maendeleo mengi sana yaliyopo leo kwa wingi na uajabu wake, havikuteremshwa kwa miujiza kutoka juu bali yalianzia katika wazo, kisha watu wakahusika kuvitengeneza. Hata leo mipango hii ninayoipanga ya kuweka Beach maeneo haya ya Mwahako hapa Tanga, hii ni cheche ndogo itakayosababisha moto mkubwa sana wa kimaendeleo katika fukwe zetu hizi.

    Nina Imani siku moja kutatapakaa Mahoteli makubwa sana kandokando ya Fukwe hizi. Watalii watakuja kwa wingi na kusababisha fedha nyingi za kigeni kuingia katika nchi yetu. Hayo ndiyo maoni yangu rafiki yangu na sasa ninajiandaa kwenda kuweka Beach maeneo ya Mwahako, kama wazo langu linavyonituma.” Alisema Ramson kwa uhakika juu ya azimio lake hilo. Sawa rafiki?”

    “Mimi ninafikiri wazo lako ni sahihi sana ila mtaji unahitajika tena mkubwa sana. Huwezi kuwashawishi watalii waje kwenye Beach yako isiyo na vitu vya kukidhi haja yao. Ninaamini hata watu tu wa hapa hapa Tanga hawawezi kushawishika kuacha fukwe nyingine na kukufuata Mwahako kama hawataona kitu cha tofauti na cha kuvutia.

    Labda nikutakie mafanikio katika zoezi lako lakini angalia kwa makini na kuzingatia maneno yangu, mtaji ni lazima uwepo katika mkakati wako.” Alisema Richard kisha akakohoa halafu akaendelea..”Ninajaribu tena kukushauri kuwa unaweza kuvuta uvumilivu tukahangaikia maswala ya kazi fedha itakayopatikana ikusaidie katika njozi yako hiyo. Kufanya jambo hili kwa sasa ni kama kupoteza muda wako tu ambao baadaye utakuja kuujutia,na na pengine kuchukia wazo lako hilo ambalo ni la thamani kama ukisubiri lifanyike kwa wakati wake.”

    Richard alisema hayo huku akisimama na kusogelea Televisheni. Aliiwasha na kutafuta chanel kwa Rimote huku akirudi taratibu kwenye kiti alichokuwa amekalia. “Nafikiri umenielewa kama mimi nilivyokuelewa na wazo lako.” Alisema huku akijiweka sawa kwenye kiti chake. “Nimekuelewa rafiki yangu ila kazi kupata hapa ni ngumu sana. CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Angalia mwenyewe tangu tulivyoanza kutafuta miezi mitatu imeshapita hakuna jibu lolote. Nina wazo la kuwepo maeneo yale ya Mwahako kusudi nijishughulishe na kazi mbalimbali, hata ikibidi za uvuvi huku nikiwekeza katika kutengeneza ufukwe wangu taratibu. Waswahili wanasema, “pole pole ndio mwendo.”..“Kama nitavuta muda ili nipate kazi na baadae ndio nifanyie kazi wazo hili hakuna kitakachofanyika. Heri wazo hili lifanyiwe kazi likiwa bado la moto likipoa hapa halifanyiki tena. Unajuaje huenda kuna mtu anawaza pia kufanya hivyo katika eneo lile lile? Vichwa vina mengi hivi ndugu yangu.

    Mimi kesho ninataka kuhamia mahali pale ili nitengeneze sehemu ya kukaa, huku nikiangalia uwezekano wa nini cha kufanya.” Alisema hivyo kuonyesha msimamo kwa maamuzi yake. “Unataka kuniambia umeamua kujitengenezea mahali pa kukaa pale Ufukweni sivyo?”Aliuliza kwa hamaki Richard!

    “Ndio rafiki yangu huo ndio msimamo wangu juu ya hilo.” Alijibu Ramson. “Kwa hiyo unataka uwe The Beach Man sio?” Aliuliza tena swali la kichokozi.“Ndio kuanzia sasa niite The Beach Man, maana nitakwenda kuishi ufukweni, nitafanya kazi ufukweni na nitakuwa mtu wa ufukweni kwa ujumla. Hayo ndiyo mawazo yangu na ninayaingiza kazini kuanzia sasa ili yawe ndio sehemu ya maisha yangu.” Alisema Ramson huku akijiandaa kuweka sawa vitu vyake.

    Siku hii ilikuwa ni ya maandalizi ya kufua nguo na kujitayarisha kwa safari ya kwenda kwenye makao mapya. Moyo wake ulikuwa na shauku kubwa ya kuanza maisha katika eneo lenye changamoto ya kipekee. Amejifunza kuwa mtu wa vitendo sio maneno peke yake. Tendo moja huongea zaidi ya maneno elfu moja. Amejikita kuwa mtendaji zaidi ya kusema tu.



    Yalikuwa ni mazingira ya kutisha kutokana na ukimya uliozingira eneo hilo. Ni sauti ya ndege tu pamoja na wadudu waishio kando ya bahari kwenye miti ya mikoko. Vichaka vilikuwa ni vingi ila ufukwe ulikuwa ni mzuri sana. Kulikuwa na nafasi ya kuweka vibanda na kutayarisha mandhari nzuri sana ya kupendeza.

    Kando ya miti mikubwa pembeni ya mwishilizio wa maji ya bahari alijenga kijumba chake kwa kikata miti imara na kuikita, hatimaye kuizungushia fito. Alikuwa na kamba za kutosha katika kufunga fito hizo, kisha alienda kijijini Mwahako na kununua makuti, kisha aliezeka kibanda chake chenye vyumba viwili.

    Baada ya kukamilisha zoezi lake hilo lililochukua wiki nzima, alikaa ili ajipange jinsi ya kuanza mikakati yake.Siku moja akiwa nje ya kibanda chake alijiwa na mgeni. Mgeni huyo alikuwa ni Ringo. Ringo aliwahi kuishi katika kijiji cha Tabu yanini, lakini aliondoka kijijini hapo zamani kidogo. “Ohooo!! karibu Mr. Ringo.” alisema Ramson akimkaribisha jamaa huyo, aliyekuwa ameduwaa kwa mshangao baada ya kuona kijumba maeneo hayo.

    “Asante! Ehee umenijuaje jina langu? mimi sikukumbuki.” Alisema Ringo huku akimtazama kwa mshangao Ramsoni. “Mimi ni mjukuu wa Mzee Kihedu anayeishi katika kijiji cha Tabu ya nini. Ninakujua kwa sababu ulikuwa unaishi pale kijijini, japo uliondoka zamani kidogo. Pia nilisona darasa moja na mdogo wako Bwizo.” alihitimisha maelezo Ramson. “Ni sawa ninakukumbuka sasa. ila ulikuwa hutaki kujichanganya na vijana wenzio ulikuwa ukiambatana na babu yako muda wote. nakukumbuka japo kweli ni siku nyingi sana.” Alisema Ringo. “Nashukuru kwa kunikumbuka karibu kiti Mr. Ringo.” Alimsogezea kigogo na yeye akarudi kuketi kwenye gogo kubwa la mnazi. “Asante haya na huku umekuja kufanya nini?” Aliuliza Ringo huku akijikalisha kwenye kigoda hicho.

    “Ni hadithi ndefu sana kaka.” Alimhadithia habari yote hatua kwa hatua. “Ndio hivyo baadaye nimeamua kujijengea kibanda hapa, ili nianzishe maisha yangu peke yangu.“Mmmmh! pole sana dogo. Ninayajua matatizo ya pale kijijini. Watu ni wavivu sana na pia hawataki kujisumbua kwa lolote. Nashangaa kwa hatua hiyo iliyofikia kwamba pamoja na wizi unaoendelea pale bado hawataki kujishuhulisha kutafuta wahalifu, badala yakewameridhika tu kuwa wewe ndiye mwizi wao!

    Kwanini wasichunguze basi kuwa katika wizi huo unaoufanya unashirikiana na nani? Maana haiwezekani wizi ukafanyika kijiji kizima, kila wakati na mhusika akawa ni mtu mmoja tu!Alisema Ringo kwa masikitiko. Kaka hii naijua ni njama za baadhi ya watu ambazo zimefanywa dhidi yangu. Njama hizi zimefanyika ili kuficha ukweli wa nani wanahusika kwenye uhalifu unaofanyika. Vijana wengi kijijini ni wavuta bangi, wanakaa tu maskani bila shughuli yoyote.

    Hii inatokana na Uvivu! Watu hawana kazi ya kufanya wanasubiri nazi tu! Nazi zenyewe ziko wapi, wakati tayari minazi imeshazeeka?” Unafikiri watu watafanya nini wakati hawana kazi za kuwapatia kipato? Alisema Ramson kwa uchungu kidogo! “Hiyo ni kweli dogo ninakubaliana na wewe kwa uchunguzi ulioufanya. Tangu mwanzo yule kijana Alen alikuwa ni mkorofi na mwizi mkubwa. Alikuwa anashirikiana na baadhi ya vijana palekijijini kuiba mazao ya watu. Nafikiri kama bado yupo kijijini pale hilo ndio kundi hatari kwa wanakijiji. Nashangaa wanakutwisha mzigo ambao sio wa kwako.

    Lakini kuna sababu gani ya kuja kuishi huku Ufukweni tena porini peke yako? Huoni kuwa ni hatari sana?” Aliuliza kwa mshangao Ringo. “Bwana kaka nina mpango wa pekee sana mahali hapa. Mtazamo wangu kwa haraka ukiusikia unaweza kuuchukulia kama ndoto fulani, lakini nataka niifanye ndoto hiyo kuwa kweli.” Alisema kwa hisia kali Ramson.“Ehee! ndoto gani hiyo dogo?”Alidakia na kuuliza Ringo.“Hapa nataka nipatengeneze baadaye pawe Ufukwe Utakaotembelewa hata na watalii kutoka ulaya.

    “Kwa hatua ya kwanza kabisa nataka nitengeneze vibanda vingi vizuri na kununua mipira ya ndani ya magari na kuijaza upepo kwa ajili ya kuwafundishia watu kuogelea.” Ramsoni alieleza mpango wake wote kuhusu makusudi yake. “Ninakuelewa dogo na wala hilo sio ndoto ni jambo linalowezekana, mbona kwa wengine yamewezekana itashindikana kwako kwanini?

    Mimi ninakupongeza na pia ninakuunga mkono mia kwa kwa mia, niko tayari pia tushirikiane ukitaka.” Alisema Ringo akimtia moyo Ramson juu ya wazo lake.“Mimi sina neno ndugu yangu, hilo ndilo ninalolihitaji angalau niwe na mtu tutakayepeana mawazo kwa kila jambo katika mikakati hii.” Alisema Ramson kwa shauku kubwa. “Mimi nilikuja mjini toka kijijini kwa nia ya kutafuta kazi. Alianza kujieleza Ringo… kisha akakohoa na baadaye akaendelea…”Nimetafuta kazi na baadaye nikapata hizi za kujenga. Nimekuwa saidia fundi kwa kipindi kirefu mpaka sasa kidogo ninajua kujenga lakini kazi kwa kweli hakuna. Nimekaa muda wa mwezi mmoja lakini bado sijapata kazi. Kutokana na kukosa kazi kwa kipindi chote hicho imeamua kujishughulisha na uvuvi.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Hiyo ndiyo kazi yangu, wakati mwingine ninanunua samaki na kwenda kuwatembeza kijijini.” Alitoa maelezo marefu Ringo, mwishowe wakakubaliana washirikiane katika kazi ya uvuvi na ujenzi wa ufukwe huo. Kaka huku ndio kufanya kazi kwa malengo. Sio unafanya kazi fedha inayopatikana unaitumia tu na kesho unarudi tena kazini kuanza moja.” Alisema Ringo akimaanisha kuwa hela yao itakuwa ikitengenezea kitu kitakachosababisha mafanikio makubwa sana katika maisha yao.

    “Ni kweli kabisa. nafikiri huu utakuwa ni mradi utakaowavutia watu wengi kuiga na baadaye mabadiliko yatatokea katika Fukwe zetu zote katika pwani hii.” Ramson aliongea hivyo na baadaye alinyanyuka na kumtaka Ringo waende kutafuta chakula kwani giza linaingia.



    * * *

    Kelele nyingi zilisikika alfajiri na mapema katika mtaa mmoja wa kijiji cha Tabu ya nini! Kelele hizo zilivuma kila mahali kwani zilikuwa kelele zilizochanganyika na mayowe. Watu wenye masikio ya udadisi waliyatega ili kusikiliza kuwa kelele hizo ni za nini? mara haikuchukuwa muda bila kusikia sauti ya Weziiiii!! Hili lilimfanya hata mtu angekuwa mvivu namna gani kuamka kitandani na kwenda kushuhudia mwizi ninani.

    Kila mtaa walisikia sauti hizo nao wakaitikiana na kujikusanya ili kuwaandama wezi hao ili kuwaadabisha. Wingi wa watu wenye hasira ulisaidia kukamatwa kwa vjana watatu waliojulikana vema kijijini hapo. Inasadikika walikuwa wameiba mbuzi wawili wa Mzee Amana, majirani wa mzee huyo ndio walioshtuka walipowaona wakiwatoa kwenye banda lake.

    Kelele za mwizi ziliwashtua wezi hao na kuanza kukimbia. Lakini mara tu baada ya kusikia sauti hizo wanakijiji walitoka kwa wingi wakiwa na dhana za kila aina. Mwisho wa yote Vijana hao walikamatwa karibu na kisima cha maji wakitaka kukimbilia nje ya kijiji hicho. Hasira za wananchi zilikuwa kali sana ila baada ya kuona kuwa vijana hao ni watoto wa Viongozi wa kijiji, walisita kuwapiga zaidi na kutaka kuwapeleka moja kwa moja kwenye ofisi ya kijiji.

    Karibu kijiji chote kilikusanyika Kituoni hapo, ili kushuhudia watu waliokuwa wakiwasumbua na kuwakosesha usingizi kila siku. Katika mkusanyiko huu hata Mzee Kihedu na mkewe Bi Namkunda walikuwepo. Vijana wale waliokuwa wamefungwa kamba walikuwa wamekalishwa katikati ya umati mkubwa wanakijiji, kila mmoja akiwashangaa! “Sio mtoto wa Mtendaji yule!” Aliuliza mwanamke mmoja kwa hamaki baada ya kumwona Alen, akiwa amejiinamia huku damu zikiwa zinamtoka katika majeraha machache usoni mwake.

    “Na yule pale umemwona?” Aliuliza mwenzake akinyoosha kidole kwa Rama aliyekuwa amefunika uso kwa shati lake. “Mmh! yule si amejifunika? Jamani wafunueni tuwaone wanaotuhangaisha katika kijiji hiki.” Alisema mama mmoja wa makamo, Askari wakawasogelea vijana wawili waliokuwa wamejifunika na kuyaondoa mashati waliyokuwa wamejifunika. “Aaaa! kumbe ni Watoto wa Viongozi wetu wote?” Abuu alikuwa ni mtoto wa Katibu wa kijiji, Rama alikuwa ni mtoto wa Mwenyekiti ambapo Alen alikuwa ni mtoto wa Mtendaji wa Kata. Walitumwa vijana wawili kwenda kumwita Mwenyekiti. Wanakijiji walitaka kusikia uamuzi wa kiongozi wao juu ya wezi wale, mmoja wapo akiwa ni mtoto wake mwenyewe. Kwakweli ilikuwa ni aibu sana kwa viongozi wa kijiji hiki; ilikumbukwa kuwa Kijana Ramson alifukuzwa kijijini hapo akidaiwa kuwa ni mwizi, lakini leo ukweli umebainika.

    Hali ilikuwa ni tete sana. Uamuzi haukuweza kujulikana mapema utakuwaje. Wajumbe waliotumwa kwa mwenyekiti walirudi na ujumbe kuwa Mwenyekiti anasema vijana hao wawekwe mahabusu. Askari waliwasweka ndani na kuwaacha wananchi kutawanyika.

    Kila mmoja aliguna kivyake wengine waliridhika kwa hatua hiyo. Lakini wengine walilalamika, walitaka Viongozi hao wajitokeze mbele ya wananchi ili wasikie maamuzi yao juu ya watoto wao. Hii inatokana na maamuzi yaliyochukuliwa dhidi ya Ramson, walitamani kuona kuwa hatua iliyochukuliwa kwa Ramson inachukuliwa pia kwa watoto wa Viongozi hao wa kijiji. Hata hivyo malalamiko yao hayakuweza kubadilisha maamuzi ya wakubwa wao.



    * * *

    Baada ya miezi mitatu tayari ufukwe wa Mwahako ulikuwa unaonyesha sura fulani. Sura waliyoihitaji itokee kusudi kuwapatia wateja wazuri watakaokuja kuogelea na kujipatia baadhi ya bidhaa ufukweni hapo. Asubuhi vijana hawa Ramson na Ringo walikuwa wakinunua samaki na kwenda kuuza kijijini. na baada ya kazi hiyo walirudi Ufukweni hapo ili kuendelea kujenga vibanda. Vibanda walivyokuwa wakijenga kwa ajili ya kazi vilifikia kumi.

    Vilikuwa ni vizuri na vyenye kukidhi haja ya wateja watakaokuja kutaka huduma ya kuogelea. vibanda hivi vilikuwa ni bafu kwa ajili ya kuondoa maji ya chumvi kwa waogeleaji. Sambamba na vibanda hivi waliweka vihema vya kuweka vimvuli kisha walitengeneza vimeza vya kuwekea vinywaji. Mahali hapo palifaa sana kupumzikia hata kama watu wengine hawakutaka kuogelea, watakaa mahali pale na kununua vinywaji.Ramson na Ringo walilazimika kuweka vinywaji ili kuwavutia wateja zaidi.

    Kwa ujumla palipendeza sana mahali hapa. Watu waliokuja waliongeza matangazo kwa kuwasifia rafiki zao juu ya ufukwe huo. Muda mwingine wa Mapumziko Ramson alikuwa akitengeneza cheni za Vikobe vya baharini na pia alibuni jinsi ya kutengeneza Frem za kuhifadhia Picha kwa vikobe hivyo ilipendeza sana.

    Mapambo mbalimbali waliweza kuyabuni yeye na Rafiki yake yakiwepo hereni zinazotokana na vifuu vya nazi na vidude mbalimbali vya baharini. Bidhaa hizi zote ziliuzwa kwa bei nzuri ya faida kubwa, maana wengi walianza kuja na kuvutiwa na kununua. Taratibu walianza kuacha biashara ya samaki, badala yake walijikita kwenye biashara ya mapambo. Wakawa wanasimamia watu wanaokuja kuongelea na kuchukuwa picha za Arusi katika eneo hilo.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Waliingiza fedha za kukidhi mahitaji yao ya muhimu. Maisha ya Ramson na Ringo yalikuwa ni mazuri sana. Walishaanza kutoka katika hali ya kuishi kwa kubahatisha. Walikuwa wanaweka vinywaji baridi na walivitunza kwa kujaza mabarafu kwenye vyombo maalum. Zaidi ya hapo waliuza mavazi ya aina mbalimbali ya kuogelea, na mapambo mbalimbali ya asili ya pwani.

    Hii iliwavutia wateja wengi sana na mara kwa mara Ringo alikwenda mjini kufungasha bidhaa za kuuza Ufukweni hapo. Miaka miwili ilipita tangu walipoanzisha ufukwe huo. Biashara ilishamiri sana na ufukwe huo ulijulikana na watu wengi. Kwa namna hiyo iliwalazimu Ramson na rafiki yake kufikiri namna ya kuweka sehemu ya kupaki magari. watu wengi walikuja na magari yao ila sehemu ya kuyaweka haikuwa inatosheleza.



    * * *

    Ilikuwa ni siku mpya, siku iliyopokelewa na mawingu machache angani, yaliyokuwa yakipita kwa haraka kuashiria kuwa anga lilikuwa na upepo mwingi. Asubuhi hii ilikuwa ya maandalizi na heka heka kwa Ramson. Leo hii alipanga kumtembelea Babu yake kijijini. vitu alivyonunua jana aliviweka vizuri kwenye mifuko na maboksi kusudi avipakie kwenye Taksi tayari kwa kwenda Kituo cha mabasi yaendayo kijijini kwao.

    Ilikuwa ni kitambo kirefu kama cha wiki mbili zote babu yake hajamtafuta kwa simu, Hata yeye alipojaribu kumpigia simu yake ilikuwa haipatikani. Kutokana na sababu hiyo aliamua kwenda kuwaona. Asubuhi na mapema alipanda magari ya abiria maarufu kama dala dala yaliyomfikisha stendi ya magari yaendayo kijijini Taabu yanini.

    Alipofika alibahatisha kupata Gari la kwanza kabisa liendalo kijijini kwao. Saa tano kamili gari lilikuwa limefika kijijini hapo. Marafiki zake wawili Walikuja kumpokea na kumbebea mizigo yake. Mmoja alibeba maboks mawili na mfuko mmoja wa Rambo kisha akatangulia na kumwacha Ramson akiongea na Jafa.“Una habari gani mtu wangu?” Alisema Jafa kwa sauti ya kimbea. “Kuhusu nini?” Aliuliza Ramson.“Wezi halisi si wamekamatwa juzi? Nakwambia watu wengi waliingia aibu na majuto sana kwa kukufukuza kijijini kwa kufuata majungu tu.” Alisema Jafa kwa kunong’ona kidogo.

    “Enhee wezi ni akina nani?” Aliuliza Ramson kwa shauku ya kutaka kujua. “Huwezi kuamini mwanangu kuwa Watoto wa wakubwa wa kijiji hiki ndio wanaowasumbua watu. Alen Mtoto wa Mtendaji wa Kata, Abuu mtoto wa Katibu wa kijiji na Rama Mtoto wa Mwenyekiti wa kijiji. wote walikamatwa na kukusanywa kwenye ofisi ya kijiji mbele ya wanakijiji wote.” Alisema Jafa kwa kunong’ona kimbea.

    “Kwakweli hizo taarifa zinatia uchungu sana.” Alisema Ramson...na kutulia kidogo kisha akauliza.. “Wamechukuliwa hatua gani sasa?” “Wachukuliwe hatua gani? Kwa kuzuga tu waliwekwa mahabusu kwa masaa machache, kisha baada ya Tukio hilo hawajaonekana tena ni zaidi ya wiki mbili sasa. Watakuwa wamewapeleka mafichoni ili hali ikitulia wardishwe kinyemela.” Alisema Jafa kwa masikitiko kidogo. “Okay Jafa! Poleni sana, mimi nimekuja kumwona babu na bibi yangu kisha nirudi zangu mjini.”Alisema Ramson kwa utulivu.

    “Nilijua una habari juu ya bibi yako kuwa anaumwa.” Alisema Jafa. “Sina habari mtu wangu! Bibi Namkunda anaumwa? Basi ngoja niende haraka tutaonana baadaye.” Ramson aliachana na Rafiki yake na kuchapusha mwendo kuelekea nyumbani kwa Babu yake. Alikutana na Beka akiwa tayari amefikisha mzigo anarudi. “Asante Beka wote wapo nyumbani?” Alisema Aliuliza Ramson.“Ndiyo wapo tena naona kuna matibabu yanaendelea kwa ajili ya bibi.” Alisema Beka.

    “Sawa ngoja niwahi.” Alitoa hela mfukoni na kuchambua kidogo kisha akampa noti moja. “Asante Bro.” Alishukuru Beka, lakini Ramson hakuwa na muda wa kuitikia kutokana na shauku ya kumwona Bibi yake ambaye inasemekana kuwa ni mgonjwa sana. Hali ya bibi kweli haikuwa nzuri baada ya kuingia ndani alimkuta bibi akiwa kalala chini hajitambui. Pembeni alikuwepo babu pamoja na mganga wa kienyeji akimwagua.

    Hali ya hewa pale ndani ilikuwa imechafuliwa na madawa ya kienyeji. Madawa yaliyokuwa yanatolewa kwenye tunguli na baadhi ya vifaa vya kiganga. “Karibu sana Ramson Mjukuu wangu.” Alisema babu Kihedu kwa sauti ya unyonge. “Asante babu bibi anaumwa nini?” Aliuliza kwa hamaki. “Bibi yako katupiwa jini kali sana. Mtaalamu hapa ameona kila kitu na maadui zetu kanitajia mmoja baada ya mwingine. Tulia apate tiba halafu tutaongea mengi baadaye.” Babu alisema hivyo kwa masikitiko makubwa.

    “Sawa babu pamoja na hayo uliwahi kumpeleka kwenye vipimo vya Hospitali?” Aliuliza kwa sauti ya msisitizo. “Kwa kweli Ramson Bado sijampeleka huko. Nilianza kwanza kutafuta tiba asili na ndipo nilipopata kila kitu kuhusu maadui zetu. kwa hiyo naona haina haja kuhangaika na Hospitali; huyu mtaalamu atamaliza matatizo yote haya.” Alisema babu Kihedu akimwangalia yule mganga aliyekuwa katika shughuli ya kutoa madawa kwenye mikoba yake.

    “Hivi babu tangu bibi aumwe amechukuwa muda gani?” Aliuliza Ramson. “Wiki mbili alijibu babu kwa mkato.”“Sawa na huyu mganga ulimwita mara tu baada ya kumgundua bibi kuwa anaumwa?” Aliuliza Ramson. “Ndiyo Mjukuu wangu, mganga huyu nilimwita mapema sana na amehangaika sana pamoja na sisi na mpaka sasa anasema matatizo yote ameyagundua hivyo atampatia dawa mara moja za kumponya bibi yako.” Unajua Ramson Mawasiliano yamekuwa magumu sana.

    Ile simu yangu imeharibika ndio maana hatukuwa tukiwasiliana. Hivi umeletwa tu na Mwenyezi Mungu.” Alisema Mzee Kihedu. “Hakuna shida babu lakini kuanzia sasa Naomba mganga aache kwanza tiba zake twende kwenye vipimo vya Hospitali sawa?” Alisema Ramson kwa mamlaka. “Wewe kijana una wazimu? huna adabu ee!” Aling’aka mganga wa kienyeji kwa sauti kubwa.

    “Ramson acha tu huyu mganga amfanyie bibi yako dawa halafu tutajaribu kufuatilia mambo mengine kesho au kesho kutwa.” Babu alisema kwa udhaifu akiwa hana uhakika kama bora ni lipi kati ya dawa za Mganga na Hospitali.“Babu mimi nimesema huyu mganga akae kando kwanza bibi akaangaliwe kwenye vipimo vya kitaalamu. CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kama hakutaonekana ugonjwa tutajua kuwa karogwa kweli baadaye mganga ataendelea na kazi yake. Mimi naenda kuita Daktari babu sawa? Ramson alitoka na kutaka kuelekea Hospital, lakini kwa bahati Jafa alikuwa akipita nje ya nyumba yao akamwita na kumwagiza aende kumwita Daktari wa Dispensari ya hapo kijijini. Kisha yeye akarudi ndani.

    “Nimeagizia mtu aende. Daktari atakuja hapa muda si mrefu.” Alisema Ramson. Alikuwa kama anasema peke yake, babu yake aliduwaa Wakati mganga wa Kienyeji akiwa anamwangalia kwa Jicho la shari! Baada ya muda Daktari alikuja na kuanza kumpima Bibi Namkunda vipimo mbalimbali. “Hee! mbona mmemwacha mgojwa kwa muda wote huu bila kumpeleka Hospitali, Mzee Kihedu vipi?” Aliuliza daktari kwa hamaki kidogo.

    Bibi ana tatizo la Shinikizo la Damu kitaalamu wanaita:“Low Blood Pleasure!” Alisema Daktari kisha akatulia na kumwangalia Mzee Kihedu kwa makini. halafu akaendelea… “Hii ni Presha ya kushuka na Sukari iko juu sana. Pia anaonekana kuwa na upungufu wa damu mwilini. Tatizo lenu wazee wetu mnafikiri kuwa kila ugonjwa unaponywa na waganga wa kienyeji tu. Mnakosea.

    Kwa sasa nitamtundikia Drip la Glucose kwa ajili ya kumwongezea nguvu kidogo kisha tutapiga Redio call Hospitali ya mkoa watuletee gari ya wagonjwa ili bibi awahishwe kwenye matibabu ya uhakika.”Alisema Daktari baada ya kukamilisha kazi yake. “Kijana inaelekea Adabu zako ni ndogo sana!” Alifoka Mganga wa kienyeji na kumwangalia kwa macho makali ya kutisha..Kisha akaendelea..“Wewe hujui dunia unavamia tu mambo, hasa baada ya kusomea mambo ya kizungu unataka kuleta dharau zako hapa. Tangu enzi za mababu watu walitegemea madawa ya miti shamba.

    Wewe leo unataka kuleta dharau zako za kijinga hapa alaa!” Daktari baada ya kusikia maneno hayo makali ya mganga hakumjibu bali alimgeukia mzee Kihedu na Ramson na kuwaambia wamsubiri akaite gari ya wagonjwa. “Sawa Daktari tunakusubiri.” Alisema Ramson na babu yake alitikisa kichwa kwa kukubaliana.

    “Mimi sasa naondoka!” Alisema Mganga baada ya muda kidogo kupita tangu Daktari aondoke. “Naona nimekuja kutukanwa tu na watoto wadogo hapa.” alifungasha zana zake na kuzitumbukiza kwenye mfuko. Kisha akanyanyuka kwa hasira. “Kwaheri bwana Kihedu. Ukinihitaji mimi sina kipingamizi.” Alisema huku akitoka mlangoni. “Sawa karibu sana.”

    Ramson na babu yake waliitikia kwa pamoja na mganga yule aliondoka kwa hasira kubwa. Ramson alimwangalia babu yake na kutoa tabasamu hafifu huku akimtazama bibi yake aliyekuwa hajitambui pale kitandani. Huzuni ilimshika sana Ramson alikumbuka mambo mengi sana.Alijikaza sana kusudi asidondoshe machozi kwa sababu aliona hali ya bibi yake ilivyokuwa.



    * * *

    Hali ya Bi Namkunda ilishakuwa mbaya sana baada ya kuonekana kuwa alikuwa na kansa ya ini. Lawama nyingi alitupiwa Mzee kihedu kwa kumchelewesha kumpeleka Hospitali na badala yake kujihusisha na waganga wa kienyeji. “Kwakweli sikufikiri kuwa itakuwa ni ugonjwa wa aina hiyo. Vipi lakini mke wangu atapona lakini?” Aliuliza Mzee kihedu kwa masikitiko makubwa sana.“Tunajitahidi kwa kadri ya uwezo wetu na dua zenu tunazihitaji sana pia.” Alisema Daktari kisha akapotelea ofisini kwake kuendelea na majukumu.

    Muda si mrefu akapita akiwa na baadhi ya vifaa akiwa ameongozana na madaktari watatu wakielekea kwenye chumba alicholazwa Bibi Namkunda. Wakiwa wamekaa kwenye viti nje ya Chumba hicho walikuwa wametekewa kabisa wasijue la kufanya. Hawakubanduka mahali hapo kwa muda mrefu sana kwani pia hawakupewa nafasi ya kuingia katika chumba hicho cha wagonjwa mahututi. Mchana wa siku hiyo iliwabidi waende kutafuta chakula kwenye Hoteli iliyopo karibu na Hospitali hiyo.

    Njaa iliwafanya wasivumilie japo kuwa walikuwa na huzuni juu ya ugonjwa wa Mpendwa wao. Waliporudi walikutana na Muuguzi wa kike akiwa amesimama nje ya Word ile. Muuguzi huyu inaelekea alikuwa akiwasubiri wao, ndipo alipowapa ujumbe kuwa wanahitajiwa kwa Daktari Mkuu wa Hospitali hiyo. Haraka sana walichapusha mwendo kuelekea ofisini kwa Mganga mkuu huyo.

    Waliingia na kukaribishwa viti, taarifa waliyopewa ilikuwa ya huzuni sana kwao. “Ninasikitika kuwaambia kuwa mgonjwa wetu ametutoka!” Alisema Daktari huyo kwa sauti ya Upole na ya busara kubwa. “Heee!! mke wangu namkunda! kafanyaje?!” Alisema kwa hamaki sana Mzee Kihedu na kulegea mwili. Haraka sana Ramson pamoja na kwamba alichanganyikiwa alisaidiana na Daktari kumweka babu yake sawa pale alipoangukia.

    Daktari alipiga simu na kuita wasaidizi wake, nao walikuja na kumbeba Mzee Kihedu na kumpeleka chumba cha matibabu. Drip la Glucose lilimsaidia baada ya muda wa masaa mawili aliamka, baadaye aliungana na Ramson kwa mipango ya kuihifadhi maiti na kutoa taarifa kwa jamaa na marafiki juu ya msiba ule.

    Huu kwao ulikuwa ni msiba mkubwa sana, kwani aliyeondoka alikuwa ni kiungo muhimu sana wa familia yao. Familia yao ilikuwa ya watu watatu tu! Bibi kuondoka lilikuwa ni pigo kubwa sana katika familia hiyo. Ramson alilia na kubeba uchungu mkubwa sana moyoni mwake. Babu yake naye alikuwa hajiwezi aligumia tu kila saa bila kutoa maneno ya kueleweka.

    Mpaka mazishi yanafanyika baada ya kusafirishwa kwa mwili wa Marehemu kwenda kijijini, Mzee Kihedu hakuwa na nguvu kabisa. Ramson ndiye aliyekuwa msimamizi wa kila kitu akisaidiana na wanakijiji na jamaa zake waupande wa bibi wakiwemo wajomba na ndugu zao. Ushirikiano wa wanakijiji ulikuwa ni mkubwa sana baada ya kukaa matanga kwa siku tatu walitawanyika. Lakini ndugu na marafiki waliendelea kuja kutoa pole kwa babu Kihedu.



    * * *

    “Babu inabidi nikuache mara moja niende kuangalia mradi wangu. Unajua jamaa niliyemwacha mpaka sasa haelewi kuwa nimepotelea wapi. Wiki mbili hizi tangu Tumefiwa kwake pia zitakuwa ni kitendawili, maana nilimwaga kuwa nitakaa kwa muda wa siku mbili tu.”Ramson alimwaga babu yake. “Mjukuu wangu Ramson mimi sina neno na wewe. Ila kumbuka kuwa mimi sasa niko peke yangu, wewe ndiye mwenzangu. Usikae sana huko ukikaa kidogo njoo uangalie mashamba yako na mifugo na mimi Babu yako unasikia?” Alisema Mzee Kihedu huku akitokwa na machozi mengi. CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Babu usilie tuko pamoja! Nitakuwa karibu na wewe mara kwa mara. Isitoshe wafanyakazi wetu wa shamba na wa mifugo wataendelea kuwa msaada kwako wakati nikisimamia kazi yangu kule mjini.Usijali babu kwaheri Rafiki yangu.” Ramsoni alimwaga babu yake kwa kumpigapiga begani kisha akabeba begi lake na kuondoka. Nje ya nyumba alikutana na Mfanya kazi wao anayesimamia mifugo yao.

    “Mimi ninaondoka tafadhali mwangalieni mzee na kumchukulia kwa upole sawa?” Alisema Ramson akitoa maagizo kwa jamaa huyo. “Sawa bwana kaka tutafanya hivyo Mzee wetu hana neno na sisi tunampenda. tutaendelea kufanya vizuri katika nyanja zote.” Alisema jamaa huyo aitwaye Habibu.

    “Sawa naenda lakini nitarudi muda sio mrefu kuangalia maendeleo yake.” Alisema Ramson na kuondoka kuelekea katika kituo cha magari kijijini hapo. Alipanda gari baada ya kufika hapo na gari hilo halikuchukuwa muda mrefu liliondoka kuelekea mjini Tanga. mawazo aliyokuwa nayo yalimfanya apitiwe na usingizi hadi aliposhtuliwa na kondakta kuwa Tayari wamefika mjini.



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog