Search This Blog

Thursday, July 21, 2022

PENZI KABLA YA KIFO - 5

 







    Simulizi : Penzi Kabla Ya Kifo

    Sehemu Ya Tano (5)



    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Kuna nini kinaendelea?” aliuliza Dk. Lazaro mara baada ya kuingia ndani ya chumba kile cha upasuaji.

    “Daktari! Wamemleta huyu mtoto hapa hospitalini kama dakika kadhaa zilizopita,” alijibu nesi mmoja, wenzake wawili walikuwa pembeni.

    “Anaendeleaje?”

    “Amefariki. Nadhani alifariki njiani hata kabla hajafikishwahapa hospitali,” alijibu nesi yule.

    “Hebu subirini.”

    Dk. Lazaro akamsogelea Glory pale alipokuwa, alipomfikia akachukua mashine yakeya kusikilizia mapigo ya moyo na kisha kuipeleka kifuani mwa msichana huyo, moyo ulikuwa umesimama, haukuwa ukidunda hata kidogo.

    Dokta hakutaka kuridhika, alichokifanya ni kuchukua mashine za kushtulia mapigo ya moyo na kujitahidi kuyashtua kwa kadiri alivyoweza lakini haikuweza kusaidia zaidi ya kumthibitishia kwamba Glory alikuwa amefariki dunia.

    “Ooppss!” alishusha pumzi nzito Dk. Lazaro.

    “Tufanye nini dokta,tukamwambie?” aliuliza nesi mmoja huku akionekana kuwa na wasiwasi tele.

    “Huyu si ndiye yule James wa Elizabeth?”

    “Ndiyo!” alijibu nesi mmoja.

    “Sijajua tutamwambia nini! Hebu subiri nijifikirie kwanza,” alisema Dk. Lazaro na kwenda pembeni. Kichwa kikawaka moto.

    ****

    Bado kichwa cha daktari kilichanganyikiwa, hakujua ni kitu gani alichotakiwa kukifanya, kumpa taarifa James kwamba mdogo wake alikuwa amefariki dunia lilionekana kuwa suala gumu kutokana na jinsi kijana huyo alivyokuwa.

    Miezi michache iliyopita alimpoteza mpenzi wake ambaye aliamua kumuacha na kuwa na mwanaume mwingine ambaye alikuwa bilionea, tukio lile lilimhuzunisha sana na kila wakati alionekana kuwa mtu wa mawazo, upweke wake uliandikwa sana magazetini, aliumia mno kiasi kwamba kila mmoja akahisi kwamba James angejinyonga kutokana na msongo wa mawazo.

    Huku akiwa hajachukua hata muda mrefu sana na hata kusahau kama inavyotakiwa akiwa hajasahau, leo hii mdogo wake alikuwa amefariki dunia kutokana na ugonjwa aliokuwa akiumwa kwa muda mrefu wa kupooza mwili.

    Hakufiwa yeye lakini moyo wake ulikuwa kwenye majonzi mazito, kila alipokuwa akiichukua nafasi ya James kwa kujiweka yeye, moyo wake uliumia kupita kawaida. Pale alipokuwa, alitulia, manesi hawakutaka kumfuata na kumuuliza chochote kile, walikuwa wakimwangalia huku wakisubiri ni uamuzi gani ambao angeweza kuuchukua, kama ulikuwa ni wa kumwambia James siku hiyohiyo au la.

    “Nitamwambia,” alisema Dk. Lazaro.

    “Sawa,” alisema nesi mmoja na hivyo kuanza kuufunika mwili wa Glory kwa shuka la kijani.

    Alichokifanya ni kutoka ndani ya chumba kile, alipoufikia mlango na kuufungua tu, tayari James alikuwa amesimama, alimsogelea daktari huku macho yake yakiwa mekundu hali iliyoonyesha kwamba kipindi kifupi kilichopita alikuwa amelia sana.

    “Nini kinaendelea daktari?” aliuliza James.

    “Nifuate ofisini.”CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Amepona?”

    “Naomba unifuate ofisini,” alisema Dk. Lazaro.

    Hakuwa na jinsi, kwa sababu aliambiwa kwamba amfuate daktari huyo, akafanya hivyo. Theodora na Siah hawakutaka kubaki mahali hapo, walichokifanya, nao wakaanza kumfuata daktari yule ambaye safari yake iliishia ndani ya ofisi yake na kuwaambia wakalie viti vilivyokuwa mule ndani.

    Kabla ya kuzungumza kitu chochote kile, akabaki kimya na kumwangalia mmoja baada ya mwingine, moyo wake ulikuwa kwenye maumivu makali lakini katika kipindi hicho alijipa ujasiri, hakutaka kuwaonyeshea kile kilichokuwa kikiendelea moyoni mwake.

    James ndiye ambaye alitia huruma zaidi, kila alipomwangalia kijana huyo, alijisikia kulia, alikuwa mnyonge, mwenye majonzi mengi ambaye alionyesha dhahiri kwamba alikuwa akipitia katika kipindi kigumu mno.

    Dk. Lazaro hakuzungumza kitu, bado aliendelea kuwa kimya, alionekana kama kujifikiria ni kitu gani alitakiwa kuzungumza mahali pale. Akaupiga moyo konde, akatoa kikohozi kidogo na kisha kuanza kuzungumza nao.

    “Nimewaiteni hapa kwa sababu ya kitu kimoja,” alisema Dk. Lazaro.

    “Kitu gani? Amepona?” aliuliza James.

    “Tumejitahidi sana, tumepambana sana kuyaokoa maisha yake,” alisema Dk. Lazaro na kisha kubaki kimya.

    “Dokta...niambie ukweli, amepona?’ aliuliza James huku akimsogelea Dk. Lazaro.

    “Hatukuweza kufanikiwa,” alisema Dk. Lazaro.

    Ilisikika sauti kubwa ya vilio ndani ya ofisi ile, si James peke yake aliyekuwa akilia bali hata watu aliokuwa ameongozana nao, Theodora na Siah walikuwa wakilia kwa sauti kubwa zilizoonyesha ni jinsi gani waliumizwa na kile kilichokuwa kimetokea.

    Manesi wakafika kule ilipokuwa ofisi ile na kuingia ndani, wakawataka watu wale wanyamaze kwani walikuwa hospitalini lakini hilo lilikuwa gumu kutokana na jinsi walivyokuwa wameumizwa mioyoni mwao.

    Kifo cha Glory kilimgusa kila mtu aliyesikia, mtu ambaye walikuwa wakimuonea huruma zaidi alikuwa James. Kila mmoja aliguswa, watu wengi ambao walipewa taarifa juu ya kifo cha Glory wakakusanyika nyumbani kwake na kuanza kuomboleza.

    Kila mmoja aliyeingia mahali hapo, alionekana kuwa mwenye sura yenye huzuni mno. Kwa kila aliyemwangalia James, hata kama hakuwa na huzuni, ghafla alijikuta akilengwa na machozi na kuanza kulia.

    Msibani hapo ni stori kuhusu Elizabeth ndizo zilizokuwa zimetawala. Kila mtu alimpa lawama msichana huyo kwa kusema kwamba yeye ndiye alikuwa chanzo cha kila kitu kwani kitendo cha kumuacaha James hata Glory kilimuathiri kwa kiasi kikubwa.

    “Jipe nguvu James,” alisema rais huku akimpigapiga James mgongoni.

    “Nashukuru mkuu! Nashukuru kwa uwepo wako,” alisema James huku akiyafuta machozi yaliyokuwa yakimbubujika.

    Siku iliyofuata magazeti yaliandika sana kuhusu Glory, binti mdogo aliyeanza kwenye maisha ya kimasikini na hatimaye kupata ajali iliyomfanya kupooza, leo hii msiba wake ulihudhuriwa na viongozi wakubwa wa nchi akiwemo rais mwenyewe.

    Kesho yake, mwili wa marehemu ukasafirishwa na kupelekwa mkoani Dodoma ambapo huko ukazikwa katika Kikiji cha Buigiri, kijiji alichotoka wazazi wake.

    “Nitakukumbuka milele Glory,” alisema James huku akimwaga mchanga katika kaburi la Glory.

    ****

    Wamorocco walichoka, hawakutaka kukubali kuona nchi yao ikidhalilishwa kiasi kile. Hawakutaka kujali sana kwamba Elizabeth alikuwa bilionea au la, walichokitaka kwa wakati huo ni kwamba msichana huyo aondoke nchini mwao tu.

    Mavazi aliyokuwa akiyavaa huku akiacha nywele wazi kuliwakera watu wengi mno, wanawake wakahisi kudhalilishwa kwani hawakutaka wanaume wengine ambao hawakuwa waume zao waone vichwa vyao, hivyo kitendo cha msichana huyo, bilionea huyo kuacha kichwa kikiwa wazi namna hiyo kuliwakasirisha sana.

    Walichokifanya baada ya kuona serikali kuwa na uwezekano wa kumkingia kifua Elizabeth kwa kuwa tu alikuwa bilionea na hata mwanaume wake alikuwa bilionea pia, wakaamua kuandamana mitaani, walibeba mabango makubwa yaliyokuwa yakikemea kitendo chake cha kuacha kichwa wazi na kuvaa mavazi ambayo kwao yalionekana kuwa ya ajabuajabu.

    “Hatumtaki nchini mwetu. Hatuwezi kukaa na malaya huyu. Ni lazima aondoke,” walisema wananchi mbalimbali walioonekana kuwa na hasira mno.

    Maandamano hayo yaliripotiwa kila kona nchini Morocco, kila kona watu waliendelea kulalamika kwamba iwe isiwe ilikuwa ni lazima msichana huyo afukuzwe nchini mwao na kurudishwa nchini Tanzania.

    “Kwa hiyo wanataka niondoke?’ aliuliza Elizabeth.

    “Ndiyo!,” alijibu Rasheed.

    “Wewe hutaki niondoke?” aliuliza Elizabeth.

    “Wala sitaki, na sipendi kusikia.”

    “Kwa hiyo nifanye nini?”

    “Kama vipi baki, hakuna kuondoka, kwani watafanyaje? Watakuua? Hawawezi,” alisema Rasheed.

    Watu hawakutulia, japokuwa Elizabeth hakuonekana kujali lakini vurugu zilizokuwa zikitokea mitaani zilimfanya kuwa kwenye wakati mgumu. Moyo wake ulimchoma mno, hakujua kama kulikuwa na watu waliokuwa na hasira kama wa nchi hiyo, walimaanisha kile walichokisema kwamba iwe isiwe ilikuwa ni lazima mwanamke huyo kuondoka nchini mwao.

    Polisi wa kuzuia vurugu walifika katika barabara kuwazuia waandamanaji kuachana na vurugu hizo lakini hakukuwa na mtu aliyeacha, kila mmoja aliweka wazi kwamba lazima msichana huyo aondoke nchini mwao kwani walichoka kuwa naye.

    Mara baada ya kuona kwamba Rasheed hakutaka kumruhusu mpenzi wake huyo aondoke, hapo ndipo walipoanza kutishia kwamba lazima wachome moto nyumba yake kauli iliyomfanya Rasheed kuogopa kwani alifahamu vilivyo kwamba watu hao hawakuwa na utani hata kidogo mara wanapoamua kufanya jambo kama hilo.

    “Kwa hiyo?”

    “Bora uende tu, haina jinsi.”

    “Kweli?”

    “Ndiyo!”

    “Na umeridhia?”CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Ndiyo! Ila moyo unaniuma,” alisema Rasheed.

    Kilichofanyika, usiku wa siku hiyo msichana huyo akapandishwa ndege tayari kwa kuanza safari ya kurudi nchini Tanzania. Moyo wake uliumia mno, alimpenda sana Rasheed na hakutaka kuwa na mwanaume yeyote zaidi ya huyo.





    Alisononeka, alishindwa kuyazuia machozi yake mara alipoona ndege hiyo ikiiacha ardhi ya Morocco na kurudi nchini Tanzania. Safari haikuwa na furaha hata mara moja, alikuwa mtu wa huzuni sana, kwa kuwa ilikuwa ni ndege ya abiria, pembeni alikuwa amekaa na mwanaume mmoja aliyeonekana kuwa mpole sana.

    “Habari yako,” alimsalimia mwanaume yule.

    “Salama tu. Shikamoo,” alimsalimia.

    “Marahaba! Mbona unalia tena?”

    “Hakuna kitu. Kawaida tu,” alisema Elizabeth, akayafumba macho yake.

    “Unaitwa nani?”

    “Mimi? Haunifahamu?”

    “Hapana! Sikufahamu. Mimi naitwa Rev. Leonard Paul,” alisema mwanaume yule.

    “Rev? Unamaanisha Mwinjilisti?”

    “Ndiyo!”

    “Wa kanisa gani?”

    “Praise And Worship lililopo Kinondoni jijini Dar es Salaam,” alijibu mwanume yule ambaye alikuwa na nguo nyeusi na juu ya kifua eneo la shindoni akiwa na kiplastiki cheupe kilichoonyesha kwamba alikuwa mchungaji wa kanisa fulani.

    “Nafurahi kukufahamu,” alisema Elizabeth, hapohapo akayafumba macho yake tena na kulala.

    Alijaribu kuuvuta usingizi ndani ya ndege lakini haikuwezekana hata kidogo, mawazo yalimsumbua sana, kila wakati alikuwa akimuwaza mwanaume wake aliyekuwa akimpenda kwa mapenzi ya dhati, Rasheed ambaye alimwacha nchini Morocco.

    Moyo wake ulikuwa kwenye majonzi tele, hakuamini kama kweli alifukuzwa nchini huko kwa kuwa tu mavazi yake hayakupendwa na watu hao ambao kwa wanawake mara kwa mara walikuwa wakivaa mavazi ya heshima, walifunika nywele zao na miguu kama misingi ya dini ilivyowataka kufanya.

    Ndege iliendelea kukata mawingu, Mwinjilisti Paul hakuzungumza chochote kile, kwa kuwa aliona binti huyo alihitaji kupumzika, alichokifanya ni kuchukua Biblia yake na kuanza kusoma taratibu.

    Baada ya saa ishirini, wakiwa wamelala na kuchoka ndipo walipoanza kuingia ndani ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta uliokuwa katika Jiji la Nairobi.

    “Tupo wapi?” aliuliza Elizabeth mara baada ya ndege kutua.

    “Nairobi! Pole sana kwa kulala muda mrefu,” alisema Mwinjilisti Paul huku akiachia tabasamu.

    “Ahsante sana! Wewe hukulala?”

    “Nililala sana na kuamka, ila haukuwa umeamka,” alisema Mwinjilisti huyo.

    Ndege haikukaa sana mahali hapo, baada ya saa moja, safari ya kuelekea nchini Tanzania ikaanza. Kuanzia hapo, Elizabeth hakulala tena, kila wakati kichwa chake kilikuwa na mawazo juu ya Rasheed tu, alimpenda mwanaume huyo, alimthamini japokuwa wananchi wa Morocco hawakutaka kumsikia hata mara moja.

    Muinjilist Paul hakutaka kuzungumza naye tena, kila alipomwangalia msichana huyo, alionekana kutokuwa sawa, kulikuwa na mambo mazito yaliyokuwa yakiendelea moyoni mwake.

    Baada ya saa kumi angani, saa tatu usiku wakafika jijini Dar es Salaam ndani ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere ambapo baada ya ndege kusimama, abiria wakaanza kuteremka na kupiga hatua kuelekea katika jengo la uwanja huo kwa ajili ya kuchukua mizigo yao na kuondoka.

    “Kumbe wewe ndiye yule Elizabeth bilionea?” aliuliza Mwinjilisti Paul huku akionekana kushtuka hasa baada ya kumuona msichana huyo akienda katika mlango ulioandikwa VIP kwa juu.

    “Ndiyo!”

    “Mh!”

    “Nini tena?”

    “Tutaongea tukitoka nje.”

    “Kuna nini? Mbona unanitisha?”

    “Tutaongea tu, usijali, kuwa na amani, baki na amani ya Bwana,” alisema Muinjlisti Paul huku uso wake ukiwa na tabasamu pana.

    Elizabeth alichanganyikiwa, hakujua Mwinjilisti Paul alimaanisha nini alivyouliza kama yeye ndiye alikuwa yule bilionea aliyekuwa akizungumziwa sana Afrika kwa kipindi hicho au la. Amani aliyokuwa nayo moyoni mwake ikapotea, hakuhisi kama alitakiwa kuwa na furaha tena, maneno ya Mwinjilisti yule yalimuweka kwenye wakati mgumu.

    Alipofika nje ya uwanja ule hakutaka kuondoka, ilikuwa ni usiku, hakukuwa na mtu aliyegundua kama msichana mrembo aliyesimama sehemu iliyokuwa na mwanga hafifu alikuwa Elizabeth, binti mdogo aliyeogelea fedha kila siku.

    Elizabeth alipomuona Mwinjilist Paul, hapohapo akamfuata na kumuuliza sababu iliyomfanya kusema vile kwani maneno yake alishangaa yakimgusa kitu ambacho hakutegemea.

    “Mwinjilisti...Mwinjilisti...” aliita Elizabeth, Paul akasimama.

    “Samahani!”

    “Bila samahani!”

    “Tunaweza kukaa sehemu tukaongea?”

    “Usiku huu?”

    “Ndiyo!”

    “Hapana! Tufanye siku nyingine, familia yangu ile pale inanisubiri,” alisema Mwinjilisti Paul huku akiwaonyeshea kidole watu watatu, mwanamke mmoja na watoto wawili ambao walisimama huku wakimwangalia.

    “Mwinjilisti...”

    “Elizabeth! Muda wa Bwana utafika tu, ukombozi unakuja! Sijajua nini kinaendelea, Mungu amenionyesha mengi kuhusu wewe, jua ukombozi unakuja,” alisema Mwinjilisti Paul.

    “Amekuonyesha nini?”

    “Maono.”

    “Maono gani?”

    “Kuna mwanamke alikuwa amefungwa minyororo mikononi mwake, pembeni yake kulikuwa na shimo kubwa lililokuwa likiwaka moto mkali, alikuwa akilia huku akiomba msaada, hakukuwa na mtu aliyemsikia japokuwa pembeni yake walipita watu wengi, si kumsikia, bali hata kumuona hawakumuona kabisa:

    “Mwanamke huyu alionekana kuchoka, alikuwa na mavazi yaliyochanika, alionekana kujeruhiwa sana, muda wote alikuwa akilia, aliendelea kuomba msaada lakini bado hakukutokea mtu wa kumsaidia:

    “Nilimuona mwanamke yule, nadhani mimi ndiye mtu pekee niliyemuona, tena baada ya kuonyeshewa na Mungu wa Mbinguni. Nikamsogelea, nikataka kumfungua minyororo ile, nikasikia sauti ikiniambia niache kwanza, muda bado kwani kupitia mwanamke yule, Mungu alikuwa akienda kujinyakulia utukufu,” alisema Mwinjilisti Paul kwa kirefu zaidi.

    “Mungu wangu! Mwanamke gani huyo?”

    “Ulikuwa wewe!”

    “Unasemaje?”

    “Elizabeth, chukua business yangu, Mungu atakaponiambia nikufuate, nitakufuata. Amani ya Bwana ikutangulie,” alisema Munjilisti yule, Elizabeth akaichukua business card ile, hapohapo machozi yakaanza kumbubujika mashavuni mwake, alichokifanya Mwinjilisti yule ni kumfanyia maombezi kidogo na kisha kuelekea kwenye gari lake na familia yake.

    Elizabeth akabaki akiwa amesimama tu, alikuwa akimwangalia Mwinjilisti alivyokuwa akiondoka na kuchukuana na famiia yake na kuanza kutokomea kule kulipokuwa na gari lake, walipolifikia, wakaingia na kuondoka zao.

    Elizabeth hakuwa na nguvu za kuondoka, maneno aliyoambiwa yaliuchoma moyo wake, alivyoambiwa kwamba mwanamke yule aliyefungwa minyororo ambaye alikuwa akihitaji msaada alikuwa yeye, alibaki akiumia moyoni, mbaya zaidi akaanza kuogopa.

    Alisimama katika hali hiyo kwa dakika tano nzima na ndipo alipopata nguvu ya kusonga mbele, akaifuata moja ya teksi iliyokuwa maeneo hayo na kuingia ndani, dereva aliyekuwa nje naye akaingia ndani, kutokana na mwanga hafifu hakuweza kugundua kama mteja huyo aliyeingia alikuwa Elizabeth.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Wapi dada?” aliuliza dereva huyo.

    “Mbezi Beach!”

    “Elfu thelathini!”

    “Wewe twende.”

    Safari ya kuelekea Mbezi Beach ikaanza. Elizabeth bado alikuwa na mawazo tele, wakati huu hakumfikiria Rasheed, mtu aliyekuwa akimfikiria alikuwa Mwinjilisti Paul ambaye alimwambia kuhusu maono aliyokuwa ameonyeshewa.

    Machozi yakaanza kumbubujika tena, alishangaa ni kwa jinsi gani aliumia, alishangaa ni sababu gani iliyomfanya kuwa kwenye maumivu kiasi kile. Hakuzungumza chochote na dereva yule, alikuwa kimya, cha zaidi ambacho alikifanya ni kuchukua simu na kumpigia rafiki yake, Candy.

    “Upo wapi?” ilisikika sauti ya Candy!”

    “Garini! Naelekea nyumbani!”

    “Elizabeth! Umeifanya Tanzania itetemeke kwa kile ulichokifanya,” alisikika Candy.

    “Kipi?”

    “Kumkataa James sekunde chache kabla ya kufunga ndoa.”

    “Kumkataa James?”

    “Ndiyo!”

    “Nani?”

    “Si wewe hapo, si siku ile mlipokuwa mkifunga ndoa ndani ya ndege!”

    “Candy! Mimi kumkataa James?”

    “Ndiyo! Hukumbuki? Wewe Elizabeth! Kwani ulikwenda Morocco kufanya nini?”

    “Nani? Mimi?”

    “Ndiyo!”

    “Mimi nilikwenda Morocco?”

    “Ndiyo!”

    “Hapana!”

    “Sasa umetoka wapi hapo?”

    “Nipo garini, ngoja nimuulize dereva, sijui nimetoka wapi,” alisema Elizabeth na kumuuliza dereva ambaye alimwambia kwamba walikuwa wakitoka uwanja wa ndege na alikuwa akimpeleka nyumbani kwake. Elizabeth akabaki akishangaa.

    *****

    Moyo wa Mwinjilisti Paul ulikuwa mzito, kila alichokuwa akikifanya mahali pale alionekana kutokuwa na nguvu kabisa. Alikuwa garini akirudi na familia yake nyumbani lakini muda mwingi alionekana kuwa na mawazo tele, kitu kilichokuwa kikimfurukuta moyoni mwake ni juu ya maono aliyokuwa ameonyeshewa siku moja kabla ya kurudi nchini Tanzania.

    Alikuwa nchini Marekani kimasomo, hakutakiwa kurudi katika kipindi hicho, ila alipokuwa huko, alisikia sauti ikimwambia ni lazima arudi Tanzania haraka iwezekanavyo. Hakuipuuzia sauti hiyo, aliitii kwa kuwa alijua fika ilitoka kwa Mungu wake, alichokifanya ni kuondoka, kama bahati, ndani ya ndege akakutana na msichana aliyemuona kwenye maono yake, Elizabeth.

    Hapo garini, mawazo yake yalikuwa kwa Elizabeth tu, alijua kulikuwa na kitu kilichokuwa kikiendelea kwa msichana huyo, kitu ambacho piga ua ilikuwa ni lazima akombolewe kutoka kule alipokuwa, sehemu yenye giza, pembeni yake kulikuwa na shimo na tena alifungwa minyororo ambayo hakuwa na nguvu ya kuifungua.

    “Nataka tuombe,” alisema Mwinjilisti Paul, alimwambia mke wake huku gari likiendelea na safari.

    “Kuna nini mume wangu! Unaonekana haupo sawa?” aliuliza mke wake.

    “Mungu anataka kufanya jambo.”

    “Jambo gani?”

    “Wewe tuombe kwanza, kuna nguvu za kuzimu inatakiwa tuzikemee,” alisema Mwinjilisti Paul.

    Alichokifanya mke wake ni kupaki gari pembeni na kisha kushikana mikono kama familia na kuanza kuomba. Walikemea, maombi ya siku hiyo yalionekana kuwa tofauti na siku nyingine, Munjilisti Paul hakuomba kama alivyokuwa akiomba, alikemea kama mtu ambaye mbele yake alikiona kitu fulani, kijasho kilikuwa kikimtoka na hata mikono aliyokuwa ameshikwa na familia yake akaitoa na kuanza kuichezesha.

    Katika maono yale aliyoonyeshewa, alimuona Elizabeth akiendelea kupiga kelele pale alipokuwa, minyororo iliendelea kumfunga, alihitaji msaada lakini hakukuwa na mtu aliyemsaidia.

    Katika lile shimo alilokuwa nalo karibu, kukatoa joka fulani kubwa, lenye vichwa saba na kuanza kutematema mate, lilionekana kuwa na hamu ya kummeza Elizabeth aliyekuwa akilia.

    Ghafla moto kutoka juu ukatokea, moto wenye muonekano wa radi, ukaipiga minyororo ile na kufunguka, Elizabeth akaanguka chini, lile joka likataka kummeza lakini hapohapo moto mwingine ukatokea na kumpiga, ukamuunguza vibaya joka lile ambalo lilitumbukia shimoni.

    Hayo yote alikuwa akiyaona usiku huo, muda huo alipokuwa akikemea kwa ajili ya Elizabeth. Wakati maombi yakiendelea ndicho kikawa kipindi ambacho Elizabeth alianza kurudiwa na kumbukumbu zake, akashangaa kuona rafiki yake akimwambia kuwa alikuwa Morocco, kila kitu alichokuwa akikifanya zamani alikifanya pasipo kujitambua, nguvu za giza zilimfunga.

    “Amen,” alisema Muinjiliti Paul na kufumbua macho yake, amani kubwa moyoni mwake ikaanza kurudi tena.

    “Umeona maono gani?”

    “Kuhusu Elizabeth.”

    “Elizabeth yupi?”

    “Huyu bilionea,” alijibu Mwinjilisti Paul.

    Hapo ndipo alipoanza kumuhadithia kila kitu kilichotokea, tangu alipokuwa nchini Marekani, akakatisha masomo yake kwa kuwa aliisikia sauti ikimwambia ni lazima arudi nyumbani haraka iwezekanavyo.

    Kila kitu kilichotokea kilikuwa ni kazi ya Mungu, akamsifu na kumtukuza Mungu kwani kwa nguvu zake alikuwa ametenda jambo la ajabu. Alichokifanya ni kumwambia mke wake kwamba hawakutakiwa kuelekea nyumbani bali walitakiwa kugeuza gari na kuelekea nyumbani kwa Elizabeth, Mbezi Beach.

    Hakubisha, kwa kuwa mumewe ndiye aliyesema hivyo, akageuza gari na kuchukua Barabara ya Kawawa, wakaanza kuelekea Mbezi Beach, tayari ilikuwa ni usiku wa saa nne. Kadiri walivyokuwa wakisonga mbele, Mwinjilisti Paul aliendelea kuomba.

    *****

    James alikaa kwa wiki kadhaa mkoani Dodoma ndipo alipoamua kurudi nchini Tanzania. Moyo wake bado uliendelea kuwa kwenye maumivu makali, kila alipomkumbuka mdogo wake aliyefariki siku chache zilizopita, moyo wake uliumia mno.

    Alikuwa na mawazo kipindi chote, Siah ndiye aliyekuwa mfariji wake. Msichana huyo alimpenda James kwa kuwa aliamini kwamba endapo angekuwa karibu naye basi hata jina lake lingeweza kuandikwa sana magazetini na hata kutangazwa katika vyombo vingine ya habari, na hivyo ndivyo ilivyokuwa.

    James hakuacha kumkumbuka Elizabeth, bado moyo wake ulikuwa kwenye maumivu makali, hakuamini kile kilichokuwa kimetokea kipindi cha nyuma, kila siku alihisi kwamba labda iliwezekana kuwa ni ndoto.

    Maisha yaliendelea bila Elizabeth, hakuwa na hamu na msichana yeyote yule, kila kitu kilichokuwa kimetokea alikiacha japokuwa moyo wake kila siku uliendelea kuumia kama kawaida.

    Baada ya siku mbili, akaanza kupanga mikakati ya kusherehekea siku yake ya kuzaliwa. Siku hiyo alipanga iwe maalumu kwa kuwatembelea watoto yatima na kuwapa misaada mingi kama kuwatia moyo katika maisha yao.

    Siku hiyo ya Jumapili ilipofika, asubuhiasubuhi waandishi wa habari walikusanyika nyumbani kwake, hakuwa amewapa taarifa kwani aliamini kuwa unapotaka kusaidia, haikutakiwa kujitangaza kwa watu, hakujua ni nani aliwapa taarifa, hakutaka kujali hilo, alichokifanya ni kuendelea na shughuli zake.

    Saa 3:03 asubuhi akatoka ndani na kuelekea nje, walikuwepo waandishi wa habari ambao waliendelea kumsubiri, hakutaka kuwaweka sana, alitoka kwa ajili ya kuzungumza nao mawili matatu kwani aliwaonea huruma kutokana na kazi ngumu waliyokuwa wakiifanya kila siku.

    Alipofika nje, akawakaribisha ndani, waandishi hao wakaingia ndani na moja kwa moja kwenda nao sebuleni.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Hivi nani aliwaambia kuhusu siku ya leo?” aliuliza James huku akiachia tabasamu pana.

    “Tumeambiwa.”

    “Na nani?”

    “Na vyanzo vyetu vya habari,” alijibu mwandihi mmoja.

    “Hahaha! Nyie waandishi kweli siwawezi. Aya subirini nakuja, atakayetaka kinywaji, afungue friji na kuchukua kinywaji akipendacho, ila kumbukeni pombe hakuna,” alisema James huku tabasamu likiwa usoni mwake.

    Huku akiwa amekwishawapa ruhusa waandishi hao na alikuwa akijiandaa kuelekea chumbani kwake, mara simu yake iliyokuwa mezani ikaanza kuita, hapohapo akaifuata na kuichukua. Akakiangalia kioo, mtu aliyekuwa akipiga alikuwa Candy, rafiki mkubwa wa Elizabeth. Moyo wake ukapiga paa!

    Hata kabla hajaipokea, kwanza akabaki akiiangalia, kichwa chake kikaanza kukusanya maswali juu ya simu ile iliyokuwa ikiingia, kwa nini Candy alikuwa akimpigia simu? Haikuwa kawaida hata mara moja, zilipita siku nyingi hakuwahi kupigiwa simu na msichana huyo, kulikuwa na nini? Kila alipojiuliza, akakosa jibu, alichokifanya ni kuipokea.

    “James....” ilisikika sauti ya Candy kwenye simu.

    “Naam!”

    “Njoo kanisani!”

    “Kanisani? Kanisa gani?”

    “Praise And Worship hapa Mwenge!”

    “Kuna nini?”

    “Elizabeth amefika! Njoo James! Elizabeth anakuhitaji,” alisikika Candy.

    “Elizabeth!”

    “Ndiyo!”

    Waandishi wa habari wote walipolisikia jina hilo, wakabaki kimya, wakaanza kumwangalia James ambaye kwa wakati huo alionekana kuchanganyikiwa. Jina la Elizabeth lilikuwa na nguvu kubwa, lilipotajwa tu, kila kitu mule ndani kibadilika.

    “Elizabeth ananihitaji mimi?”

    “Ndiyo! Njoo haraka!”

    James alichanganyikiwa, alipoambiwa kwamba Elizabeth alikuwa kanisani na alimuhitaji alishindwa kuzungumza chochote kile. Kitu cha kwanza kilichokuja kichwani mwake ni kuhusu siku hiyo, alitaka kujua ilikuwa ni siku gani, kama ni siku ya wajinga duniani au la.

    Haikuwa Siku ya Wajinga, alishindwa kuelewa juu ya kile alichokuwa akikizungumza Candy kilikuwa ni kweli au alitaka kumtia roho juu tu, akabaki akiwa ameduwaa.

    “Nimesikia umesema Elizabeth!” alisema mwandishi mmoja huku akishushia na soda.

    “Ndiyo! Candy kanipigia simu.”

    “Kasemaje?”

    “Elizabeth ananihitaji!”

    “Elizabeth! Anakuhitaji wapi? Morocco?”

    “Hapana! Kanisani, yupo Mwenge!”

    “Huyu Candy ana masihara kweli, hajui kama upo na wazee wa udaku hapa halafu tuna njaa ya habari?” aliuliza mwandishi mmoja.

    “Sijui kwa kweli!”

    “Ila nenda! Labda yupo serious!”

    “Acheni hizo, hivi kwa kile kilichotokea, kweli inaweza kuwa hivi? Candy aje kimyakimya hata nyie msijue?”

    “Bro! Wewe twende, kama si kweli kwani utakufa? Hakuna kitu kama hicho,” alisema mwandishi mwingine.

    “Haina noma! Ngoja nijiandae,” alisema James na kwenda chumbani kujiandaa! Waandishi hao hawakuwa na lolote zaidi ya kutaka habari, yaani kama Elizabeth asingekuwepo, wangeandika habari kwamba Candy alimrusha roho James ila kama Elizabeth angekuwepo, walitegemea kuuza sana magazeti yao kwa habari hiyo kwani ingekuwa ni habari ya kipekee.

    “Twendeni,” alisema James na wote kutoka, wakaingia ndani ya gari lake na safari ya kwenda kanisani kuanza.

    *****

    Bado Elizabeth alishangaa, hakujua ni kitu gani kilichokuwa kikiendelea, maneno aliyoambiwa na Candy kwamba alitoka nchini Morocco yalimshangaza sana, hakukubaliana naye hata mara moja kwamba alitoka nchini humo, alichokuwa akikikumbuka ni kwamba alikuwa nchini Tanzania.

    Kitu alichokikumbuka ni kwamba alikuwa ndani ya ndege akiolewa na mwanaume aliyekuwa akimpenda sana, James, ila kitu cha kushangaza ni pale alipokiangalia kidole chake, hakikuwa na pete.

    “Candy!” aliita.

    “Abeee!”

    “Mume wangu yupo wapi?”

    “Nani?”

    “James!”

    “James! Mumeo tangu lini na wakati ulimkataa?”

    “Nilimkataa James?”

    “Ndiyo! Hukumbuki?”

    Bado maneno ya Candy yalimshangaza mno, yalimuweka katika hali ya sintofahamu, hakujua ni kitu gani kilichokuwa kikiendelea katika maisha yake. Akajaribu kuvuta kumbukumbu, mara ya mwisho kabisa kukumbuka lilikuwa ni tukio la kufunga ndoa na James ndani ya ndege.

    Walisimama huku wakiangalia, baada ya hapo mchungaji akaruhusu wavalishane pete, kilichotokea baada ya hapo, hakuwa akikifahamu.

    “Mungu wangu! Nini kilitokea?” alijiuliza lakini akakosa jibu.

    Safari ya kuelekea Mbezi Beach iliendelea kama kawaida, kichwa chake kilikuwa na mawazo tele, hakutaka kutulia, kila alipojaribu kukumbuka kile kilichokuwa kimetokea, akakosa jibu. Walipofika nyumbani, harakaharaka akateremka garini na kumlipa dereva kiasi cha fedha alichokitaka na kuingia ndani.

    Mtu wa kwanza kabisa kukutana naye alikuwa mlinzi, alipomuona, mlinzi akashtuka, alibaki akimwangalia Elizabeth ambaye alionekana kuchanganyikiwa na asijue nini kilitokea kabla ya siku hiyo.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Bosi...” aliita mlinzi huku akionekana kutokuamini.

    “Mikinza, kuna nini?”

    “Wapi?”

    “Humu! Mbona kimya sana?”

    “Hakuna mtu.”

    “Wapo wapi?”

    “Waliondoka.”

    “Kwenda wapi?”

    “Sijui! Ila James alikwenda kwake,” alijibu mlinzi.

    “Kwa nini?”

    “Si kwa sababu ulimkataa!”

    “Nilimkataa? Nani? James?”

    “Ndiyo!”

    “Nilimkataa wapi?”

    “Kwenye ndege ulipotaka kufunga naye ndoa! Baada ya hapo, ukaondoka zako, ndiyo nakuona leo umerudi,” alisema mlinzi yule.

    Elizabeth akazidi kuchanganyikiwa, maneno aliyoambiwa na mlinzi ndiyo yaleyale ambayo aliambiwa na Candy kwenye simu. Hakuwa akijua ni kipindi gani alikuwa amekataa kuolewa na James na wakati ndiye alikuwa mwanaume aliyekuwa akimpenda kuliko wote katika dunia hii.

    Alichokifanya ni kwenda ndani, nyumba ilikuwa kimya, haikuwa kawaida, alizoea kuwasikia wafanyakazi wakiwa ndani lakini usiku huo kulikuwa na ukimya wa hali ya juu. Akaondoka sebuleni na kuelekea chumbani kwa kudhani kwamba James angekuwepo japokuwa aliambiwa hayupo, alipofika huko, hakukuta mtu, alipofungua kabati la nguo, hakukuwa na nguo hata moja ya James.

    Wakati anajiuliza zaidi, mara akasikia mlango wa sebuleni ukifunguliwa, akatoka mbiombio kuelekea huko, alipofika, macho yake yakatua kwa Candy aliyefika nyumbani hapo.

    “Elizabeth....” aliita Candy, hapohapo akamsogelea na kumkumbatia, kila mmoja akaanza kububujikwa na machozi.

    “Candy! Nini kimetokea?” aliuliza Elizabeth huku akilia kama mtoto.

    Walibaki wakiwa wamekumbatiana tu, kila mmoja alibubujikwa na machozi, hawakuamini kama walionana tena. Walikaa katika hali hiyo kwa dakika kadhaa na ndipo walipokaa kochini na kuanza kuzungumza.

    Elizabeth alionekana kutokukumbuka kitu chochote kile, hapo ndipo Candy alipotumia muda huo kumsimulia Elizabeth kile kilichokuwa kimetokea, baada ya kukataa kuolewa mpaka alipoamua kuondoka kuelekea nchini Morocco kuonana na bilionea Rasheed.

    “Mimi nilikwenda kwa Rasheed?” aliuliza Elizabeth huku akionekana kushtuka.

    “Ndiyo! Tena ukawa unakula naye raha visiwani nchini Marekani,” alisema Candy.

    “Haiwezekani, siwezi kufanya hivyo!”

    “Ndivyo ilivyokuwa Elizabeth! Huamini?”

    “Siamini.”

    “Subiri!”

    Alichokifanya Candy ni kuchukua simu yake, akaunganisha  internet na moja kwa moja kuelekea katika Tovuti ya Global Publishers na kuanza kutafuta zile picha zilizomuonyesha akiwa na Rasheed visiwani.

    “Hizi hapa! Ziangalie,” alisema Candy huku akimpatia simu na kuziangalia picha zile.

    “Mungu wangu! Ilikuwaje?’ alijiuliza lakini hakupata jibu.

    Elizabeth akawa anaziangalia picha zile, moyo wake uliumia mno, hakuamini kile alichokuwa akikiona, picha zake alizopiga na Rasheed zilionekana vilivyo katika mtandao. Maumivu aliyoyasikia moyoni mwake yalikuwa makubwa mno, hakuamini, wakati mwingine alihisi zile picha zilipitishwa kwenye kompyuta.

    “Nani ameediti picha hizi?” aliuliza Elizabeth.

    “Hizi si picha za kuediti! Mbona hata wewe mwenyewe ulikuwa ukizungumzia mapenzi yako na Rasheed na tena ulisema hakuna mwanaume unayempenda kama yeye,” alisema Candy.

    “Mimi?”

    “Ndiyo! Wewe!”

    “Hapana! Sikuwahi kusema hivyo,” alisema Elizabeth.

    Ukweli haukubadilika, bado uliendelea kuwa vilevile kwamba picha zile zilizokuwa zikionekana zilikuwa ni za Elizabeth ambazo alipiga na Rasheed katika kipindi walichokuwa nchini Marekani.

    Alibaki akilia tu huku akionekana kutokuamini kile alichokuwa akikiangalia. Baada ya kukaa kwa dakika kadhaa, wakaanza kusikia honi kutoka nje ya nyumba yao, walipochungulia nje wakaona gari likiingia huku mlinzi akionekana kuwa mwenye fuaraha.

    Mlango ulipofunguliwa, Mwinjilisti Paul akateremka na familia yake ambapo wakaongozwa na mlinzi kuufuata mlango wa kuingia sebuleni na kuingia ndani. Elizabeth alipowaona, akaonekana kufurahi kwani ndiye yuleyule Mwinjilisti aliyemwambia wakae sehemu.

    “Mwinjilisti!” aliita Elizabeth.

    “Nimekuja Elizabeth! Bado Mungu ana kazi na wewe.”

    “Ni nini kimetokea?”

    “Ulirogwa.”

    “Na nani?”

    “Na mtu anayeitwa Rasheed.”

    “Aliniroga?”

    “Ndiyo! Alikutupia jini mahaba ili umpende, na kweli ukampenda mpaka kumuacha mchumba wako siku ya harusi,” alisema Mwinjilisti Paul.

    “Mimi nilirogwa?”

    “Ndiyo! Bado Mungu anataka kukukomboa, kuna kingine pia.”

    “Kipi?”

    “Mungu atakupa watoto. Shetani amekuwa akipambana sana katika maisha yako, ulitokea kupendwa sana, alitumia umaarufu wako kujinyakulia watu wengi, Elizabeth, jua kwamba Mungu anahitaji uingie kwenye mikono yake,” alisema Mwinjilisti.

    Hakukuwa na muda wa kupoteza mahali hapo, alichokifanya Mwinjilisti Paul ni kuanza kumfanyia maombezi mahali pale kwa kuamini kwamba bado Shetani alikuwa akimuwinda katika maisha yake.

    Alipoanza kuombewa, hapohapo Elizabeth akaanguka chini na kuanza kutoa sauti za ajabuajabu kwa kuomba asiunguzwe na moto. Aliyekuwa akizungumza hakuwa yeye bali ni majini mahahaba ambaye alitumwa mwilini mwake kwa ajili ya kumpenda Rasheed.

    Mapovu yakaanza kumtoka mdomoni, alizidi kupiga kelele za maumivu ya kuunguzwa na moto ambao watu wengine walipokuwa wakiangalia, hakukuwa na moto wowote ule. Tangu kuanza huduma yake, Mwinjilisti Paul hakuwahi kumuombea mtu aliyekuwa na mapepo mengi mwilini mwake kama ilivyokuwa kwa Elizabeth.

    Alikemea kwa muda wa masaa saba na ndipo mapepo hayo yakamtoka Elizabeth, akawa mtu wa kawaida asiyekuwa na pepo mwilini mwake. Hakuzungumza kitu, kwanza alibaki kimya akimwangalia Mwinjilisti, mwili wake ulikosa nguvu, hakuweza hata kusogeza kiungo cha mwili wake.

    Walikaa mpaka ilipofika saa moja asubuhi ambapo wakambeba na kumpeleka kanisani kwani ilikuwa Jumapili. Walipofika huko, Mwinjilisti Paul akawaita wachungaji na kuwaambia kwamba kulikuwa na maombezi maalumu walitakiwa kuyafanya, wakaelekea kule alipokuwa Elizabeth na kuanza kumfanyia maombezi.

    Walikuja kumaliza saa tatu asubuhi, nguvu zilimrudia Elizabeth, aliuhisi mwili wake kuwa mwepesi mno. Watu ambao walikuwa wakiendelea kufika kanisani hapo walipomuona Elizabeth hawakuamini.

    Wengi walijua labda alikuwa msichana mwingine aliyefanana na Elizabeth ambaye alifika kanisani hapo. Walisogea na kumwangalia vizuri, alikuwa ni yeye, alionekana kuchoka mno, hakuwa na nguvu za kusimama na kutembea.

    “Elizabeth! Imekuwaje tena?’ aliuliza msichana mmoja, alikuwa amesogea kule alipokuwa Elizabeth.

    “Hata mimi sijui! Nashangaa! Halafu inakuwaje Mwinjilisti awe hapa na wakati alikuwa Marekani?” aliuliza msichana mwingine.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Mmmh! Mbona hali inachanganya hivi?”

    Baada ya washirika kuongezeka kanisani, Mwinjilisti akachukua kipaza sauti na kisha kuwataka watu watulie, kadiri muda ulivyokuwa ukizidi kwenda mbele na ndivyo watu walivyozidi kuongezeka kanisani hapio. Hata wale waliokuwa nje waliposikia kwamba Elizabeth alikuwa kanisani hapo, nao wakafika na kusababisha hata washirika kutoweza kuingia kanisani kiurahisi.

    “Mungu ametenda,” alisema Mwinjilisti Paul.

    Hapo ndipo alipoanza kuhadithia kile kilichokuwa kimetokea, tangu siku ya kwanza alipoanza kuonyeshewa maono juu ya msichana Elizabeth mpaka pale alipokutana naye ndani ya ndege. Watu hawakuamini walichokuwa wakikisikia, Mwinjilisti hakutaka kubaki kimya bali aliwaambia watu kuhusu Rasheed, alionyeshewa kila kitu kilichotokea, watu wakaanza kupiga picha huku hata wale waliokuwa na vifaa vya kurekodia wakifanya hivyo.

    Maneno aliyoongea mchungaji yalimshtua kila mtu. Kumbe yale mapenzi makubwa aliyoyaonyesha kwa mwanaume Rasheed, bilionea kutoka nchini Morocco, kumbe alikuwa amerogwa.

    “Kweli dunia ina mambo! Kumbe alirogwa!” alisema jamaa mmoja, alionekana kushangaa haswa.

    *****

    Mbele yao kulikuwa na umati mkubwa wa watu, walikuwa wamejazana nje ya kanisa, kila mtu alitaka kuona ndani, alitaka kuona kile kilichokuwa kikiendelea. Hakukuwa na nafasi ndani ya eneo la kanisa lile kutokana na wingi mkubwa wa watu, walichokifanya ni kuliacha gari mbali kabisa na kanisa lile kisha kuteremka.

    Wakaanza kupiga hatua kuelekea kule lilipokuwa kanisa lile, walitaka kuona kile kilichokuwa kikiendelea. Kutokana na umati mkubwa wa watu waliokuwa kanisani hapo, wakajua kwamba ile simu aliyokuwa amepigiwa James ilikuwa ya kweli.

    Wakasogea kule, wakaanza kupenyapenya kwa watu huku waandishi wale wakilitaja jina la James ambapo watu walipogeuka, kweli macho yao yakatua kwa mwanaume huyo. Wakapata nafasi, wakaingia mpaka kanisa, walichokikuta, kilikuwa kilekile alichoambiwa James kwenye simu.

    Macho ya James yalipotua kwa Elizabeth hakuamini, alibaki akimwangalia tu, alihisi kama alikuwa ndotoni ambapo baada ya sekunde chache angeamka kutoka katika usingizi mzito. Msichana wake yuleyule aliyempenda kwa mapenzi ya dhati, Elizabeth alikuwa mbele ya kanisa lile, alikuwa akilia mno.

    Elizabeth alipomuona James, akaanza kumsogelea kwa lengo la kumkumbatia lakini James alikuwa akimkwepa kwa kurudi nyuma. Hapo, kumbukumbu zake zikaanza kurudi kipindi cha nyuma, pale alipokataliwa na msichana huyo wakati wa harusi, tena sekunde chache hata kabla hajamvisha pete na kuwa mke wake.

    “Naomba unisamehe James,” alisema Elizabeth, alikuwa akimsogelea mwanaume huyo huku akilia, bado James alikuwa akimkwepa kwa kusogea nyuma.

    Hapo ndipo Mwinjilisti Paul alipomuita James, akamshika mkono na mbele ya kanisa akaanza kuhadithia kilekile alichokuwa amekihadithia kwamba kile kilichokuwa kimetokea kwenye ndege kipindi kile, hakikuwa makusudi ya Elizabeth bali zilikuwa nguvu za giza.

    “Kivipi?” aliuliza James.

    “Alirogwa.”

    “Na nani?”

    “Rasheed, mwanaume kutoka Morocco,” alisema Mwinjilisti Paul.

    Kidogo James akapoa, akakubaliana na Mwinjilisti Paul kwani kila kitu kilikuwa wazi na hata Elizabeth alipoulizwa kuhusu mwanaume huyo, alichokikumbuka ni kwamba zamani alikutana naye nchini Morocco alipokwenda kutangaza biashara zake za mavazi, kinyume na hapo, hakukuwa kilichoendelea.

    “Ila niliumia sana,” alisema James.

    “Halikuwa kosa lake, mapepo yanaweza kumuingia yeyote yule,” alisema Mwinjilisti.

    James akamkumbatia Elizabeth, waandishi wa habari wakapiga picha, tayari walipata kitu cha kuandika kwenye magazeti yao. Ilikuwa furaha ya kila mtu, watu pasipo kutegemea, wakaanza kupiga makofi ya shangwe, walimshukuru Mungu kwa kile kilichokuwa kimetokea.

    Kuanzia siku hiyo, wawili hao wakawa pamoja kama walivyokuwa kipindi cha nyuma, huo ndiyo ukawa mwisho wa James na Siah ambaye aliamua kuwa na mwanaume huyo ili mradi tu jina lake liwe kubwa, avume kama alivyovuma Elizabeth.

    Baada ya kurudi nyumbani huku wakiwa pamoja, hapo ndipo Elizabeth akamuulizia Glory, kitu alichoambiwa, kilimliza, kuambiwa kwamba msichana yule alifariki dunia, akahisi moyo wake ukifa ganzi.

    “Unasemaje?” aliuliza Elizabeth, tayari machozi yalianza kumbubujika.

    “Glory alifariki,” alijibu James kwa sauti chini.

    Elizabeth hakutaka kukubali, alichokifanya ni kuomba kupelekwa katika kaburi alilozikwa Glory, akapelekwa mpaka Dodoma tena huku waandishi wa habari wakiwa nyuma yake. Alipofika huko, alilia sana, alipiga magoti kaburini huku akimtaka Glory atoke kaburini japo aje kumuona kwa mara ya mwisho, ila pamoja na kulia kote huko, ukweli ukabaki palepale kwamba Glory alifariki dunia.

    Baada ya mwezimmoja, ile harusi iliyokuwa imeharibika kipindi cha nyuma, ikarudishwa tena. Wageni rasmi walewale, ndege ileile, mchungaji yuleyule, Williams John kutoka Marekani na wanakwaya walewale tena na pete zilezile, ikarudiwa tena na hatimaye Elizabeth kuwa mke halali wa James.

    “Unaweza kumbusu mkeo,” alisema mchungaji Williams huku akiachia tabasamu, wawili hao wakabusiana.

    Maisha yakabadilika, kama jinsi alivyoambiwa na Mwinjilisti Paul, baada ya miezi miwili akahisi kwamba alikuwa mjauzito, na alipokwenda kupima, kweli akakutwa akiwa mjauzito wa watoto mapacha kitu kilichomfanya kuwa na furaha mno.

    Hicho ndicho alichokitaka, furaha yake ilikuwa kubwa, hakuamini kama kweli kipindi hicho alikuwa na mimba, alichokifanya ni kumshukuru Mungu kila siku. Ilikuwa furaha yake, Mwinjilisti Paul ndiye alikuwa baba wake wa kiroho, kila kitu kilichokuwa kikitokea, alikuwa akimtaarifu.

    Baada ya miezi tisa, Elizabeth akajifungua watoto wawili mapacha, jina la mtoto wa kiume alilichagua la Paul kama kumbukumbu ya Mwinjilisti Paul ambaye alimsaidia sana na jina la mtoto wa kike, James akachagua jina la Glory kama kumuenzi mdogo wake aliyefariki kwa ugonjwa wa kupooza.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Nitakupenda milele mke wangu,” alisema James.

    “Nitakupenda pia mume wangu,” alisema mama Glory huku akionekana kuwa kwenye furaha kubwa. Wakabusiana kisha kuwabeba watoto wao mapacha.

    *****

    “Nini kimetokea?”

    “Hatujui, sisi tumesikia kelele kutoka ndani, hatujui nini kinaendelea.”

    “Hebu fungueni mlango!”

    “Umefungwa.”

    “Sasa mbona anapiga kelele?”

    “Nahisi ana maruhani, wewe si unayasikia yanavyosema,” alisema mfanyakazi.

    Wafanyakazi wa Rasheed walishtuka, walianza kusikia kelele kutoka chumbani mwa bosi wao, alikuwa akipiga kelele hovyo kama mtu aliyechanganyikiwa. Wao ambao walikuwa vyumbani mwao, wakatoka na kwenda kusikiliza ni kitu gani kilikuwa kikiendelea, hakukuwa na kingine zaidi ya kusikia kelele tu kutoka kwa bosi wao huyo.

    Waliogopa, hata kuingia ndani ya chumba kile hawakuweza. Walishangaa, halikuwa jambo la kawaida kuwa hivyo, walichokifanya ni kumuita mlinzi ambaye hata naye alipigwa na mshangao.

    Alivyomsikia vizuri Rasheed, alikuwa na mapepo, alikuwa akizungumza mambo yasiyoeleweka. Walichokifanya ni kuwapigia simu ndugu zake ambao walifika nyumbani hapo, wakaanza  kuuvunja mlango na kuingia ndani.

    Walimkuta Rasheed akizunguka huku na kule, alionekana kama kuchanganyikiwa, ili kuonyesha kwamba alikuwa na mapepo makali, tayari alianza kujijeruhi, akaanza kujichanachana na vitu vyenye ncha kali, damu zikatapakaa chumba kizima.

    Wote wakashtuka na kuogopa, hata kumsogelea hawakuweza kabisa, alikuwa akizunguka huku na kule, hakuacha kuzungumza, wakati mwingine mapepo hayo yalijigamba kwamba yalikuwa na nguvu na wakati mwingine yalisema kwamba yalitumwa kumuingia Rasheed, hawakutaka kuondoka kwani yeye ndiye aliyesababisha hayo kumfuta baada ya kule yalipotumwa kuunguzwa moto.

    “Tufanye nini?”

    “Tumpelekeni hospitali.”

    “Mtu mwenye maruhani apelekwe hospitali, nyie wa wapi,” alihoji mlinzi.

    “Kwa hiyo!”

    “Apelekwe kwa mganga.”

    Huo ndiyo uamuzi waliokuwa wamekubaliana, Rasheed hakutakiwa kupelekwa hospitali bali alitakiwa kuchukuliwa na kupelekwa kwa mganga, tena mganga mwenye nguvu ambaye alitikisa Rabat nzima, wakafanya hivyo.

    Wakatoka nyumbani na kuelekea kwa mganga mmoja aliyesifika kwa uganga wa kitabu, huyo alikuwa akiishi pembeni mwa jiji la Rabat, aliitwa mganga Mansoor. Walipofika huko, wakamchukua na kumpeleka chumbani.

    Mganga alipomuona, hata na yeye akanza kupandisha maruhani, alionekana kushangaa kwa nini mtu aliyekuwa na maruhani hayo aliletwa kwake. Hakutaka kumchukua, alichokifanya ni kuwaambia kwamba walitakiwa kuondoka mahali hapo kwani yalikuwa maruhani yenye nguvu na hakuamini kama kungekuwa na mganga angeweza kuyatoa.

    Wakaondoka na kuelekea kwa mganga mwingine, kote huko hawakuweza kupata msaada zaidi ya kuzungushwa tu. Kila mmoja akachanganyikiwa, hawakujua ni kitu gani kilikuwa kikiendelea, hawakukata tamaa, walichokifanya ni kutafuta waganga zaidi, na kila walipokwenda, hawakuweza kupata suluhisho.

    Hali ya Rasheed ilikuwa mbaya mno, kila alipokaa, alikuwa akiongea peke yake, udenda ulimtoka, wakati mwingine alionekana kama zezeta. Wamorocco wakashangaa, hawakujua ni kitu gani kilikuwa kikiendelea mpaka Rasheed kuwa kwenye hali hiyo, tena ghafla sana.

    Walizunguka kwa waganga wengi, hawakufanikiwa, mwisho wa siku wakaamua kumpeleka hospitali ambapo huko wakawaambia kwamba ndugu yao alikuwa amechanganyikiwa, amekuwa chizi, hivyo apelekwe katika hospitali ya vichaa.

    “Haiwezekani!” alisema kaka yake.

    “Ndiyo hivyo Taliqi, hakuna cha kufanya zaidi ya hicho.”

    “Ni lazima tutafute waganga wengine, huyu atakuwa amerogwa,” alisema Taliqi huku akionekana kuwa na hasira.

    Hicho ndicho walichokifanya, wakaanza upya kuzunguka kwa waganga wengi. Baada ya siku chache wakasikia kwamba kulikuwa na mganga aliyekuwa akiishi katika Jiji la Casablanca, hawakutaka kubaki Rabat, walichokifanya ni kwenda huko.

    “Kijana wenu hajarogwa, amerukwa na akili, hana maruwani,” alisema mganga.

    “Mbona anaongea peke yake kama ana maruhani?”

    “Sijajua, ila nikiangalia kwenye kioo changu, hana jini lolote, amerukwa na akili tu,” alisema mganga yule.

    “Hawezi kupona?”

    “Haiwezekani kwa nguvu zetu, huu ugonjwa si wa kurogwa,” alisema mganga.

    “Kwa hiyo atakuwa hivihivi?”

    “Ndiyo! Mpaka kifo chake.”

    Maneno ya mganga yule yakawakatisha tamaa, japokuwa walijipa moyo na kwenda sehemu nyingine lakini ukweli ukabaki kuwa palepale kwamba Rasheed asingeweza kurudi katika hali ya kawaida.

    Watu wakahuzunika mno, bilionea mkubwa nchini Morocco, ghafla alikuwa chizi kwa kipindi kifupi, wakati watu wakihuzunika na ndipo taarifa zikaanza kuzagaa kwamba msichana bilionea kutoka nchini Tanzania alisema kwamba alikuwa amerogwa na Rasheed ili ampende, amuoe na kuishi naye miaka yote.

    Maisha yake yalibadilika baada ya kuombewa, uchawi aliokuwa ametupiwa, ulimtoka na kuelekea asipopafahamu. Hapo ndipo watu walipopata jibu kwamba chazo cha uchizi wa Rasheed ilikuwa ni baada ya kumroga Elizabeth ili ampende, mwisho wa siku madawa yale yakarudi kwake na kumtibua kichwani mwake.

    Watu hawakuwa na cha kufanya, hawakujua ni kwa namna gani wangeweza kumsaidia Rasheed, huku wakionekana kukata tamaa, wakamchukua na kumpeleka katika hospitali ya vichaa ya hapo Rabat. CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Huo ukawa mwisho wake, utajiri wake ukabaki mikononi mwa ndugu zake, hakurudiwa na akili zake, aliendelea kuwa hivyohivyo chizi miaka yake yote. Kutafuta penzi kulimgharimu, kuliyaharibu maisha yake, huku akiwa kijana ambaye bado hakutimiza ndoto zake, kuwa na familia yake, maisha yake yaliharibika kabisa na hakukuwa na dalili kama angeweza kupona tena.

    Waganga walimshindwa, mpaka anafikishwa katika hospitali hiyo, tayari waganga wengi walijaribu kumtibu lakini hakukuwa na aliyefanikiwa mpaka pale walipokata tamaa naye hivyo kupelekwa katika hospitali hiyo.

    Utajiri wake uliokwenda kwa ndugu, ukagaiwagaiwa, ndugu wakagawana mali, fedha zake zikagaiwa, mwisho wa siku Rasheed yule aliyekuwa bilionea, akabaki akiwa hana kitu mikononi mwake, akabaki akiwa mtupu ila kilichosaidia, ni kwa sababu hakuwa na akili, hivyo hata kuumia hakuwahi kuumia zaidi ya kukaa hospitali huku kila wakati akiongea peke yake, tena miguuni alifungwa minyororo kama vichaa wengine waliokuwa wamechanganyikiwa zaidi.



    MWISHO.!!!

0 comments:

Post a Comment

Blog