IMEANDIKWA NA : NYEMO CHILONGANI
*********************************************************************************
Simulizi : A Living Dream ( Ndoto Inayoishi )
Sehemu Ya Kwanza (1)
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Watu walikuwa wamejazana ndani ya Uwanja wa Mpira Jamhuri uliokuwa mkoani Dodoma kwa ajili ya kusikiliza mahubiri kutoka kwa Mchungaji aliyekuwa akivuma kwa upako aliopewa wa kuponyesha magonjwa mbalimbali, Mchungaji Emmanuel Kihampa.
Kila mtu aliyekuwa ndani ya uwanja huo alikuwa akisikiliza kila kilichokuwa kikiendelea uwanjani hapo, vilio vya chinichini vilikuwa vikisikika kutoka kwa watu waliokusanyika ndani ya uwanja huo kutokana na maneno ya mchungaji huyo kumgusa kila mtu.
Hiyo ilikuwa ni mara ya pili mwaka huo kwa mchungaji huyo kuhubiri ndani ya uwanja huo mkubwa wa mpira wa Jamhuri huku watu wakiwa wamejazana. Kila neno alilokuwa akiongea, watu walipiga kelele kuonyesha kwamba walikuwa wakikielewa kile kilichokuwa kikizungumzwa uwanjani hapo.
Mahubiri yaliendelea zaidi, japokuwa wingu kubwa lilikuwa limetanda angani lakini hakuwa na mtu aliyekuwa na wasiwasi, na hata mvua kubwa ilipoanza kunyesha, hakukuwa na mtu aliyeondoka mahali hapo, kila mmoja alikuwa akimsikiliza mchungaji huo ambaye aliendelea kuhubiri mpaka kulivua koti kubwa la suti alilokuwa amelivaa.
“Mvua ni baraka, acha iendelee kunyesha. Tunapokuwa mashambani, tunamuomba Mungu atupe mvua, tunaporudi nyumbani tunawaambia wafanyakazi watuandalie maji ya kuoga, tunapotaka kufua nguo zetu, huwa tunatumia maji ili ziwe safi. Maji ni baraka, leo tukinyeshewa mvua hapa si kwamba tutakufa, tutaendelea kuishi,” mchungaji alisema na kuendelea:
“Si mvua tu, Neno la Mungu ni Neno lenye nguvu, hata ukishuka moto mahali hapa, bado tutaendelea kulisikia Neno lake yule Aliye juu, Muumba Mbingu na Nchi,” alisema mchungaji Emmanuel.
Watu wote waliokuwa mahali hapo wakapiga makofi na kelele zilizojaa shangwe, maneno aliyoyaongea yakawafanya watu kuendelea kubaki mahali hapo zaidi. Hakukuwa na mtu aliyekimbia kisa mvua, hakukuwa na mtu aliyeogopa kulowa.
Dakika ziliendelea kukatika huku mchungaji akiendelea kuhubiri. Usikivu kutoka kwa watu wengine ulikuwa mkubwa mahali hapo, hakukuwa na mtu aliyetaka kufanya kitu kingine chochote kile zaidi ya kuendelea kumsikiliza mchungaji huyo.
Ilipofika saa moja kamili, mchungaji akaacha kuhubiri, akawaita watu waliokuwa wakitaka kufanyiwa maombezi, wakaja mbele na kuendelea na maombezi hayo.
Hayo ndiyo yalikuwa maisha ya Mchungaji Emmanuel Emmanuel, kila siku maisha yake yalikuwa ya kumtegemea Mungu. Alihubiri katika sehemu mbalimbali nchini Tanzania huku katika kila mkoa aliokwenda, alitangulizana na mke wake aliyekuwa akimpenda, Luciana Paul.
Siku hiyo ya mwisho ya mkutano huo uliopewa jina la ‘Delivarance’ mchungaji Emmanuel alihubiri kwa nguvu zote huku akiwafanyia maombezi watu mbalimbali waliokusanyika mahali hapo.
“Amen,” alimalizia mchungaji Emmanuel mara baada ya kuufunga mkutano huo kwa maombi na watu kuondoka mahali hapo na yeye kurudi hotelini huku akiongozana na mkewe, Luciana ambaye alikuwa mjauzito.
“Tunarudi Dar usiku huuhuu,” alisema mchungaji Emmanuel, alikuwa akiongea na mke wake.
“Tuondoke usiku huuhuu?” aliuliza Luciana huku akiwa na mshangao.
“Ndiyo. Kesho nataka niwepo kanisani, kuna huduma kubwa ninataka kuifanya asubuhi,” alisema Emmanuel.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Luciana hakuwa na kipingamizi, kwa sababu walikuwa wamekwishafanya mkutano huo kwa muda wa siku saba, siku hiyohiyo mchungaji alitaka kuondoka na kurudi Jijini Dar es Salaam.
Wakaanza kujiandaa, japokuwa muda ulikuwa umekwenda sana kwa safari ya kurudi Dar es Salaam lakini Emmanuel hakutaka kubaki mkoani Dodoma, aling’ang’ania kurudi Dar es Salaam kwa ajili ya kujiandaa na ibada ya kesho, siku ya Jumapili.
Kila kitu kilipokamilika, safari ya kurudi Dar es Salaam ikaanza kwa kutumia usafiri wao binafsi. Katika safari nzima, wote walikuwa wakicheka kwa furaha, kitendo cha kuwa wote kila wakati kiliwapa furaha mno.
Emmanuel alikuwa akiendesha kwa mwendo wa kasi kwani kitu alichokuwa akikitaka, mpaka ikifika saa sita usiku awe ameingia ndani ya Jiji la Dar es Salaam. Kwa sababu hakukuwa na magari mengi barabarani, Emmanuel hakupata tatizo lolote lile, taa zilikuwa ‘full’ huku umakini wake ukiwa mbele barabarani.
“Nakupenda kipenzi,” alisema Luciana huku akilishika tumbo lake kubwa, alionekana kujifungua muda wowote ule.
“Unaongea na mimi?” aliuliza Emmanuel.
“Hapana. Naongea na kababy kangu,” alisema Luciana huku akitoka tabasamu, mkono wake ulikuwa tumboni, kila alipoliangalia tumbo lake, tabasamu liliendelea kuwepo usoni mwake.
Safari iliendelea kama kawaida. Walipofika maeneo ya Kijiji cha Buigiri, simu ya Emmanuel ikaanza kuita. Kwa sababu alikuwa akiendesha gari, hakutaka kuipokea simu hiyo, alichokifanya ni kumwambia mke wake, Luciana kuichukua simu hiyo kumsikiliza mpigaji.
Luciana akaichukua simu hiyo, akaanza kukiangalia kioo cha simu ile kwa muda fulani, akapigwa na mshtuko mkubwa. Namba aliyokuwa akiiona katika kioo hicho haikuwa ya kawaida hata kidogo, ilikuwa ni namba ngeni kabisa katika ulimwengu wa mitandao ya simu Tanzania.
Kichwani mwake alikuwa na ‘code number’ za mitandao mingi duniani lakini kila alipoiangalia namba ile, alishindwa kuielewa ilikuwa ni ‘code number’ ya nchi gani.
“Nani?” aliuliza Emmanuel.
“Sijui, namba yake ngeni. Mmmh! Namba hii kama nilikwishawahi kuiona mahali, ni namba kutoka katika ulimwengu wa giza, nimekuwa nikitumiwa meseji kwamba ninapoona namba hii inaingia simuni sitakiwa kuipokea simu hiyo” alisema Luciana huku akiiangalia namba iliyokuwa ikiingia katika simu yake. Ilikuwa +255901009999
“Unasemaje?”
“Ni namba ya kuzimu.”
“Katuma nani?” aliuliza Mchungaji Emmanuel.
“Sijui...Mungu wangu.....!” alisema Luciana huku akiwa katka hali ya mshtuko.
Ghafla, mapigo yake ya moyo yakaanza kudunda, mwili wake ukaanza kutetemeka huku kijasho chembamba kikianza kumtoka. Hofu ikamjaa moyoni, kabla hajaamua nini cha kufanya, mbele yake akaanza kuona giza huku akianza kupiga kelele.
Mchungaji Emmanuel akashtuka, akamgeukia mke wake na kuanza kumwangalia. Akataka kufunga breki na kulipaki gari pembeni, breki ikawa inakataa kana kwamba chini ya kifaa cha breki kulikuwa na jiwe.
Ghafla katika hali ya kushangaza, gari likaanza kuhama njia na kuingia porini. Mchungaji akashindwa kulidhibiti gari lile, liliendelea kwenda zaidi tena kwa mwendo wa kasi. Lilipofika umbali mrefu kidogo, gari hilo likagonga mti mkubwa, na kwasababu hawakuwa wamefunga mikanda, wakatolewa kupitia kioo cha mbele na kujigonga katika miti kadhaa iliyokuwepo porini humo.
Hazikusikika kelele zozote zile, walipotua chini, hakukuwa na mtu aliyejua kilichoendelea, miili yao ilitulia chini kama mizigo ya mahindi, kwa jinsi walivyoonekana, ilionekana dhahiri kwamba walikuwa wamekufa.
****
Saa 12:00 alfajiri, wanakijiji watatu wakatokea katika sehemu ambayo gari la Mchungaji Emmanuel lilipokuwa limepita. Alama za matairi zilikuwa zikionekana kuonyesha kwamba gari hilo lilielekea porini.
Kati ya wanakijiji hao watatu, hakukuwa na mtu aliyefikiria kwamba inawezekana kulikuwa na ajali iliyotokea, kila mmoja alijua labda kulikuwa na watu ambao waliingia porini huko kwa ajili ya kutafuta asali, moja ya vitu walivyokuwa wakipenda kuvifanya kila siku nyakati za asubuhi.
Hawakutaka kutilia umakini sana lakini michimbiko ya matairi ya gari ikazidi kuwatia hofu kwani endapo kama gari hilo lilikuwa la watu waliokuwa wakipakua asali, lisingeweza kuchimba namna hiyo, lingepita kistaarabu kuelekea porini huko.
Wanakijiji hao wakaendelea kupiga hatua mbele, kadri walivyokuwa wakisogea na ndivyo ambavyo hali ikaanza kuonekana ya tofauti, wasiwasi ukaanza kuwashika kwa kuona kwamba inawezekana walivyokuwa wakifikiria kwamba alama za matairi yale ilikuwa ni ya gari la wapakuaji asali ikawa si sahihi bali lilikuwa gari lililokosea njia.
Wakaanza kuona vipande vya vioo chini kwenye majani, mpaka kufikia hatua hiyo tayari walikuwa na uhakika kwamba gari ambalo liliingia njia hiyo lilipata ajali na hivyo kuingia porini.
Wanakijiji wale wakazidi kusogea zaidi, walipofika umbali fulani, kwa mbali macho yao yakagonga katika garri moja dogo lililokuwa limebondeka kwa mbele mara baada ya kuugonga mti mkubwa ulioanguka chini.
Wakaanza kulisogelea gari lile, walipolifikia, wakachungulia ndani, hakukuwa na mtu ila kioo cha mbele kilikuwa kimevunjika kwa kuacha matundu mawili makubwa hali iliyoonyesha kwamba watu waliokuwa ndani ya gari hilo walikuwa wamepitishwa kupitia katika matundu hayo ya dirisha na kurushwa nje.
Wakaweka vizuri majembe yao na kuanza kusogea mbele zaidi. Hakukuwa na mtu aliyeongea kitu, kila mmoja alikuwa kimya na kufuatilia kile kilichokuwa kimetokea porini hapo. Hatua hamsini mbele, macho yao yakatua katika miili ya watu wawili...
walioonekana kama wamekufa, mmoja alikuwa mwanaume na mwingine mwanamke aliyeonekana kuwa mjauzito.
“Mungu wangu!” alisema mwanaume mmoja kwa mshtuko huku akisogea karibu zaidi.
Mara baada ya kuifikia miili ile, kitu cha kwanza walichokifanya ni kusikiliza kama mapigo ya mioyo yao ilikuwa ikidunda.
Miili ya majeruhi wale ilikuwa imeharibika vibaya kiasi kwamba haikuwa rahisi kumtambua hata mmoja wao kutokana na damu zilizokuwa zimetapaa miilini mwao. Nguo zote za juu walizokuwa wamezivaa, zilichanika na kuwaacha wazi.
“Wazima,” alisema mwanakijiji mwingine huku akiliweka jembe lake chini.
“Wanapumua?” aliuliza mwanakijiji mwingine.
“Kwa mbali. Tuwapelekeni hospitali,” alishauri mwanakijiji mwingine.
Hakukuwa na kitu kingine cha kufanya, kwa haraka sana pasipo kupoteza muda wakawabeba mchungaji Emmanuel na mke wake, Luciana na kuanza kuondoka nao mahali hapo kuelekea hospitalini.
“Wapi sasa?”
“Twendeni Mpwapwa.”
Hiyo ndiyo ilikuwa hospitali ambao katika kipindi hicho ilikuwa na uafadhali wa kutoa huduma bora kwa wagonjwa wake. Wakawachukua majeruhi na kuanza kuelekea nao barabarani, walipofika huko, wakasimamisha baiskeli za wanakijiji waliokuwa wakipita ambao walibeba kuni na kuwaomba lifti.
“Kwa hiyo kuni zangu niziweke wapi?” aliuliza jamaa aliyeombwa lifti.
“Popote tu, kwanza tuwasaidie hawa,” alisema mmoja wa wanakijiji mmoja.
Kwa haraka, huku majetuhi wakionekana kuwa katika wakati mbaya kutokana na majeraha makubwa waliyokuwa nayo, wakawabeba katika baiskeli hizo na safari ya kuelekea Mpwapwa kuanza.
Kila mmoja alikuwa akijiuliza juu ya ajali ile mbaya iliyotokea, kwa muonekano tu, hakukuwa na mtu aliyejua ni kwa namna gani gari lile lilipata ajali na kuelekea porini kutokana na sehemu ile kutokuwa na utelezi au shimo lolote lile.
Walichukua dakika thelathini kutoka hapo Buigiri, wakafika katika Hospitali ya Mpwapwa. Kila mgonjwa ambaye alikuwa hospitalini hapo alipigwa na mshangao, majeruhi ambao waliletwa ndani ya hospitali ile walikuwa katika hali mbaya.
Damu zilikuwa zikiwatoka mfululizo huku miili yao ikiwa imewalegea kupita kawaida. Hawakuwa wakijitambua kabisa, kwa jinsi walivyokuwa wakionekana, hakukuwa na matumaini yoyote ya majeruhi yeyote kuamka.
“Hapa si pa kukaa, itabidi wapelekwe Dodoma General Hospital,” alisema dokta mmoja wa kike huku akionekana kuwa mwenye hofu tele.
“Kwa hiyo haitowezekana kutibiwa hapa?” aliuliza jamaa mmoja.
“Haiwezekani. Nyie mmewatoa wapi?”
“Tumewatoa porini dokta wakiwa kwenye hali mbaya.”
“Ilikuwaje?”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Ajali. Gari lao liliacha njia na kuelekea porini,” alijibu mwanakijiji.
“Toeni taarifa polisi kwanza wakati sisi tunafanya jitihada za usafiri,” alisema dokta yule aliyejitambulisha kwa jina la Seche.
Wanakijiji wale wakaondoka na kuelekea katika Kituo cha Polisi cha Mpwapwa kwa ajili ya kutoa taarifa juu ya ajali ile mbaya ambao ilitokea katika usikuwa wa siku hiyo.
Huku nyuma, Dokta Seche na madaktari wengine wakaanza kufanya mishemishe zao kwa ajili ya maandalizi ya kuwapelekea majeruhi hao katika Hospitali ya Dodoma General kwa ajili ya kupatiwa matibabu zaidi ambayo kwa muonekano tu, Hospitali ile ya Halmashauri haikuwa na dawa za kutosha.
Mara baada ya majeruhi kuoshwa vidonda, gari la wagonjwa likaletwa mahali hapo na miili ile kupakizwa na safari ya kuelekea Dodoma Mjini kuanza.
Njiani, bado mchungaji Emmanuel na mkewe, Luciana hawakuwa wamerejewa na fahamu, walikuwa kimya huku muonekano wao ukionyesha kwamba tayari watu hao walikuwa wamekufa jambo ambalo kwa madaktari ambao walikuwa nao ndani ya gari lile walionekana kushikwa na wasiwasi.
“Mmmh!” Sijui kama watapona,” alisema dokta mmoja huku akionekana kukata tamaa.
“Kama wakipona, wakachinje mbuzi au waokoke kabisa,” alisema dokta mwingine, katika kipindi chote hicho, hali ya mchungaji Emmanuel na mkewe, Luciana hazikuwa za matumaini kabisa, walionekana kama wafu.
****
Mara baada ya kupewa taarifa juu ya tukio lililotokea, polisi wakafika katika eneo la tukio ambapo wakaanza kuangalia kila kitu kilichowahusu kukiangalia huku wapiga picha maalumu kutoka katika kituo hicho wakiendelea kupiga picha.
Ajali ile bado iliwashangaza, hakukuwa na mtu aliyekuwa akifahamu sababu hasa iliyowafanya watu wale kupata ajali katika sehemu isiyokuwa na kona kali, utelezi au shimo.
Polisi wakaingia mpaka porini na kulifuata gari lile, kitu cha kwanza walichokifanya mara baada ya kulifikia ni kufungua milango na kuanza kuangalia ndani. Hakukuwa na vitu vingi zaidi ya Biblia mbili na mkoba wa Luciana huku simu mbili zikiwa chini.
Walichokifanya polisi wale ni kuzichukua simu zile kwa mikono yao iliyovalia ‘gloves’ na kuangalia, hasa namba zilizoingia na kutoka.
“Kuna namba gani?” aliuliza polisi mmoja.
“Kuna namba nyingi, zimepigwa toka jana,” alijibu polisi yule aliyeshika simu zile.
“Na hiyo simu nyingine?”
“Subiri,” alisema polisi yule na kisha kuanza kuiangalia simu ya mchungaji Emmanuel.
Hakukuwa na namba nyingi zilizoingia usiku uliopita ila namba ya mwisho ambayo waliitazama iliwashtua, ilikuwa ni namba ambayo ilikaa kiutata na hata ‘code’ zake zilikuwa tofauti kabisa.
“Mmmh!” aliguna polisi yule.
“Kuna nini?”
“Hii namba.”
“Imefanya nini?”
“Iangalie jinsi ilivyo,” alisema polisi yule na kumpa mwenzake.
Akaanza kuiangalia, polisi wengine waliokuwa pambeni nao wakajivuta, kila mmoja akaanza kuiangalia namba ile. Wote wakashangaa, namba ilikuwa ngeni na hakukuwa na mtu yeyote aliyekuwa akifahamu ilikuwa ni ya nchi gani.
“Ninaifahamu namba hii,” alisema polisi mmoja, tayari uso wake ulijawa na hofu.
“Ni namba ya nani?”
“Kuna ndugu yangu alikwishawahi kupigiwa, alipoipokea tu, alipigwa na kitu kama shoti ya umeme, alifariki palepale,” alisema polisi yule.
“Unasemaje?” polisi mmoja aliyeonekana kuwa kiongozi wao aliuliza huku akipigwa na mshtuko.
“Hii namba ni ya hatari,” alisema polisi huyo.
Kila mmoja akaingiwa na HOFU.
****
Namba za simu na vitambulisho kadhaa vikawafanya polisi wale kugundua kwamba watu waliokuwa wamepata ajali walikuwa mke na mume huku mwanaume yule akiwa mchungaji Emmanuel.
Taarifa za ajali zile zikaanza kusambazwa katika kila kona hapo Dodoma Mjini kwamba mchungaji yule aliyekuwa na mkutano kwa wiki nzima ambao aliufanya katika Uwanja wa Jamhuri alikuwa amepata ajali na mkewe na kuharibika vibaya.
Taarifa zile zikawafikia wachungaji ambao wakafika hospitalini hapo kwa lengo la kumuona lakini hawakuruhusiwa kwa sababu majeruhi hao walikuwa katika chumba cha wagonjwa mahututi.
Washirika wengine kutoka katika makanisa mbalimbali mkoani hapo wakafika hospitalini kwa lengo la kuwajulia hali lakini nao hawakupewa nafasi ya kuwaona majeruhi hao.
Taarifa ziliendelea kusambazwa kama upepo, washirika wengi wa makanisa mbalimbali waliendelea kufika kanisani hapo kuwajulia hali lakini bado hali ile iliendelea kuwa vilevile, hakukuwa na mtu aliyeruhusiwa.
Hapo ndipo washirika hao walipoanza kufanya maombi kila walipokuwa wakifika hospitalini hapo. Mioyo yao ilijua kwamba vitu vyote hivyo vilikuwa mipango ya shetani ambaye hakutaka kuona kazi ya Mungu ikiendelea huku watu wakizidi kuokolewa.
Taarifa zile zikafika mpaka katika kanisa lake Jijini Dar es Salaam, baadhi ya washirika wakasafiri na kuelekea Dodoma kumuona mchungaji Emmanuel na mke wake, Luciana.
Hali zao hazikuwa nzuri kabisa, nyuso zao zilikuwa zimeharibika mno. Kwa Lucciana, hali ilikuwa mbaya zaidi kwa sababu alikuwa mjauzito.
Matibabu yakaanza lakini baada ya wiki kukatika huku watu hao wakiwa hawajarudiwa na fahamu, hapo ndipo uamuzi ukachukuliwa kwamba watu hao walitakiwa kusafirishwa na kuelekea Dar es Salaam katika Hospitali ya Muhimbili kwa ajili ya matibabu zaidi.
“Hapa tumeshindwa, matibabu yao yanahitaji wataalamu zaidi,” alisema Dokta Chungua
Hakukuwa na cha kupoteza, kwa sababu kila kitu kilikuwa tayari, usafiri ukaandaliwa na baada ya saa moja safari ya kuelekea Dar es Salaam ikaanza huku ndani ya gari hilo kukiwa na washirika wao watatu ambao walikuja kuwajulia hali.
Bado njiani waliendelea kumuomba Mungu ili afanye muujiza na watu wake warudiwe na fahamu ili waendelee na kazi ya kumhubiri siku zote.
Walichukua masaa sita mpaka kufika Jijini Dar es Salaam. Kwa sababu taarifa zilikuwa zimekwishatoleawa, kwa harakaharaka mara baada ya gari kusimama, machela zikaletwa na wagonjwa kupakizwa na majeruhi kuanza kupelekwa ndani ya jengo la Hospitali hiyo idara ya wagonjwa mahututi.
Washirika wa kanisa la Praise And Worship ambao walifika hospitalini hapo kazi yako kubwa ilikuwa ni kuomba tu. Bado walikuwa wakiamini kwamba Mungu angeweza kufanya muujiza na hivyo majetruhi wale kupona na kuwa wazima kabisa.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Mungu atatenda,” alisema muumini mmoja.
“Nina wasiwasi moyoni mwangu,” alisema muumini mwingine.
“Kwa nini uwe na wasiwasi? Humuamini Mungu?” aliuliza muumini huyo.
“Namuamini sana, lakini wakati mwingine yatupasa kuangalia kile kinachoendelea,” alijibu muumini huyo mwenye mashaka.
Bado majeruhi hao hawakuwa wakijitambua, toka walipopata ajali mpaka kufikia muda huo, bado walikuwa kimya vitandani mwao, hakukuwa na dalili za watu hao kuzinduka.
****
Hali ya hewa ilikuwa ni ya joto sana, jua lilikuwa kali lililowafanya wakazi wengi wa Bagamoyo kupata tabu kana kwamba jua hilo lilikuwa limeshushwa chini kidogo.
Adhana ilikwishaanza kuadhiniwa kama kuwakumbusha Waislamu kwamba walikuwa wakihitajika misikitini kwa ajili ya swala. Wakati wa jua hilo kali, hasa katika mikoa ya Pwani, kila mtu alikuwa ndani huku wale waliokuwa na kazi za kufanya wakiwa makazini.
Katika kipindi hicho, msichana mdogo mwenye miaka kumi na sita, Luciana, alikuwa akilia kwa uchungu alipokuwa akimuaga mvulana ambaye aliyekuwa akimpenda kwa dhati, Patrick aliyekuwa akihamia Dar es Salaam na familia yake.
Luciana, alimpenda Patrick kwa moyo wote, alikuwa akimthamini kwa sababu muda mwingi sana walikuwa pamoja, kuanzia shuleni, nyumbani na hata kanisani.
Ukaribu wao huo ukawasababishia kitu kingine kabisa, MAPENZI.
Wawili hao, Patrick na Luciana wakaanza kupenda, ukaribu wao uliendelea kuongezeka kikafika kipindi wazazi wao waliulizana kama ule ulikuwa ni urafiki kama walivyojua au kulikuwa na kitu kingine kilichokuwa kikiendelea nyuma ya pazia.
Maswali yao hayakuwa na majibu. Wawili hao, japokuwa hawakuwa wakubwa lakini walifanya mambo yao kwa kujificha sana. Kila siku ilikuwa ni lazima waonane sehemu, hasa chini ya mbuyu uliokuwa mbali kidogo na nyumbani kwao, huko, walikuwa wakikutana na kupiga stori za mapenzi.
Japokuwa kulikuwa na maneno mengi kuhusiana na mbuyu huo kwamba ilikuwa ni sehemu ambao wachawi walikuwa wakipenda kukutania na hata wakati mwingine majini kuonekana mahali hapo lakini hawakutaka kujali.
Walikuwa wakipendana mno, walitamani muda wote wawe pamoja. Hakuwa na sehemu nyingine ambayo kwao ilionekana kuwa salama zaidi ya hapo chini ya mbuyu. Walipokuwa hapo, hakukuwa na mtu aliyekuwa akiwaona kutokana na giza nene lililokuwepo mahali hapo, hiyo iliwapelekea kufanya mambo mengi ikiwepo kufanya mapenzi.
“Nakupenda Luciana,” alisema Patrick aliyekuwa kidato cha pili.
“Nakupenda pia Patrick,” aliitikia Luciana.
“Ila nitakapoondoka, nataka ulitunze penzi letu, utakuwa tayari?” alisema Patrick.
“Nitakuwa tayari mpenzi.”
“Naomba tuweke alama.”
“Alama gani?”
“Atakayemsaliti mwenzake, asipate furaha kwenye mahusiano, na mwisho wa mwaka afe,” alisema Patrick huku akionekana kujiamini.
“Hakuna tatizo.”
Walichokifanya, japokuwa ilikuwa ni usiku mno, Patrick akachukua wembe aliokuwa nao mfukoni na kisha kujikata, damu zilipotoka, akampa Luciana ailambe, vivyo hivyo kwa Luciana, naye akajikata na wembe, akampa Patrick ailambe damu yake.
“Hii ni ahadi yetu chini ya mbuyu huu,” alisema Patrick.
“Hakika sitokusaliti.”
“Una uhakika Luciana?”
“Asilimia zote, labda wewe.”
“Kwangu? Hapana, siwezi hata nikitishiwa kifo,” alisema Patrick.
Sawa. Acha mbuyu uwe shahidi yetu”
Hawakutaka kuendelea kubaki mahali hapo, kwa sababu walikuwa wamekwishamaliza kila kitu, wakaondoka mahali hapo na kila mmoja kurudi kwao. Walionekana kuwa na furaha lakini jambo la Patrick kutaka kuhamia Dar es Salaam lilimuumiza mno Luciana.
“Nitakupenda siku zote Patrick,” alisema Luciana huku akitabasamu, hawakujua madhara ya kuwekeana yamini chini ya mbuyu ule uliosemekana kutumika kama kituo cha kukutania wachawi na makazi ya majini.
***
Hicho ndicho kilikuwa kipindi chenye maumivu kuliko vipindi vyote katika maisha yake. Luciana alibaki akimwangalia Patrick kwa mtazamo uliojaa maumivu makubwa. Macho yake yalikuwa mekundu mno na baada ya muda mfupi, machozi yalikuwa yamekwishaanza kujikusanya na kuanza kububujika mashavuni mwake.
Alimpenda sana Patrick kuliko mvulana yeyote, alimzoea kiasi kwamba katika kipindi hicho alichokuwa akimuaga kwamba alikuwa akihamia Dar es Salaam na familia yake, kilimuumiza kupita kawaida.
Machozi yalimbubujika zaidi na zaidi, kila alipokuwa akimwangalia Patrick, alitamani kumfuata, amkumbatie tena, ambusu kwa mara nyingine ili moyo wake uridhike zaidi. Hakukuwa na nafasi ya kufanya hivyo tena, kama kumkumbatia na kumbusu, tayari alikuwa amekwishavifanya na katika kipindi hicho alitakiwa kumuacha mvulana huyo aondoke zake.
Japokuwa alikuwa binti mdogo lakini moyo wake ulikuwa kwenye hisia kubwa za mapenzi, Patrick alimfundisha kupenda na kuthamini na ndiyo maana katika kipindi hicho, moyo wake uliendelea kuhisi maumivu kama moyo uliochomwa na kitu cha moto kilichokuwa na ncha kali.
“Usinisaliti mpenzi,” alisema Luciana kwa sauti ya chini ambayo alijua kwa asilimia miamoja Patrick alikuwa akimsikia.
“Nakuomba usinisaliti, mbuyu acha uwe shahidi yetu,” alisema Luciana huku akiendelea kusimama kituoni pale akiliangalia gari lile lilivyokuwa likiondoka mahali hapo.
Luciana hakutaka kuondoka mpaka pale alipohakikisha gari lile limepotea machoni mwake. Huku akionekana mnyonge, akaanza kupiga hatua kurudi nyumbani. Mawazo yake bado yalikuwa kwa Patrick, mvulana huyo aliuteka moyo wake kupita kawaida na alikuwa tayari kufanya lolote lile ili aendelee kuwa wake peke yake.
Usiku hakulala, mawazo juu ya Partick yalimtesa. Kuna kipindi alikuwa akiamka usiku wa manane, anakaa kitandani na kuanza kumfikiria mvulana huyo, alikuwa akijikuta kukaa katika hali hiyo mpaka alfajiri.
Hayo ndiyo yalikuwa maisha yake ya kila siku. Hakuwa na simu, njia pekee ambayo ilikuwa ni rahisi kwake kuwasiliana na Patrick ilikuwa ni kuandikiana barua tu, kilichomsikitisha zaidi, hata anwani ya Patrick hakuwa nayo.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Maisha ya majonzi yenye maumivu yakamuingia, akaanza kupigana nayo kila siku lakini hali ile haikumtoka. Kila siku ilikuwa ni lazima kuelekea chini ya mbuyu ule na kukaa mahali hapo, Luciana alionekana kuwa chizi, mapenzi yalimchanganya kupita kawaida.
Siku zikaendelea kukatika, hakukuwa na mawasiliano yoyote na Partick japokuwa hakutaka kumsahau mvulana huyo. Shuleni hakusoma vizuri, muda mwingi alipenda kuutumia kwa kulichora jina la Patrick tu.
“Hivi kwa nini ninateseka hivi? Hivi kwa nini Patrick haurudi kuja kuniona?” alijiuliza Luciana, maswali yote hayo, yalikosa majibu.
Mwaka huo ukakatika, hakukuwa na mawasiliano yoyote yale na Patrick, mwaka wa pili ukaingia huku akiingia kidato cha tatu, bado hakukuwa na mawasiliano yoyote yale na Patrick jambo lililompelekea kuwa na msongo wa mawazo.
Mwaka wa tatu ulipoingia, mzee James, baba yake Patrick akafika Mjini Bagamoyo, hiyo ilikuwa moja ya safari yake ya kutembelea mashamba yake kadhaa. Kwa sababu alikuwa na urafiki na mzee Paul, akaamua kumfuata huku akiwa na mzigo wa Luciana, barua iliyoandikwa kwa mkono wa Patrick.
Luciana alipomuona mzee James, moyo wake ukamshtuka na kuanza kudunda kwa kasi ya ajabu. Kitendo cha kumuona mzee huyo, alifarijika na kuona kama alimuona mvulana wake aliyekuwa akimpenda kwa moyo mmoja, Patrick.
Mara baada ya maongezi na mzee Paul na mkewe, akaamua kumpa Luciana barua ambayo aliandikiwa na Patrick. Kwa harakaharaka bila kupoteza muda akaelekea chumbani, akajifungia, akajilaza kitandani na kuanza kuisoma, muda wote alionekana kuwa na furaha.
Mpenzi, Luciana.
Umekuwa mtu muhimu sana katika maisha yangu, uwepo wako ulinifanya kujiona mtu wa thamani mwenye kuhitajika kipindi chote cha maisha yangu. Kwa siku zote tulizokuwa pamoja, ulinifundisha kupenda na kumthamini mtu kwa mapenzi ya kweli.
Kila ninapofumba macho, ninaiona taswira yako, ninaziona siku zote ambazo tumekuwa tukizitumia kukaa chini ya mbuyu, lakini mara ninapofumbua macho yake, najikuta nipo chumbani kwangu, peke yangu huku upweke ukiwa umetawala chumba kizima.
Ninazikumbuka lipsi zako laini, macho yako ya goroli mithiri ya msichana aliyekula kungu, ninakikumbuka kiuno chako chembamba ambacho nilipenda sana kukishika na kukuvutia kwangu, naikumbuka miguuyako na hipsi zako za pundamilia, sura yako ya kitoto na kila kitu ulichokuwa nacho mwilini.
Kuishi mbali na wewe, hakika yamekuwa maisha magumu yenye mateso yaliyonitesa katika kipindi chote hiki. Kila ninapoamka na kujikuta nipo Dar es Salaam, ninaumia, ninatamani niwe karibu yako tena lakini haiwezi kuwa hivyo, kila nikitaka kuja huko, baba ananizuia kwa kunitaka nisome kwanza.
Luciana, wewe ni Cleopatra wangu, wewe ni malaika wangu wa pekee ambaye kila siku ninatamani nipae pamoja nawe. Ulinifanya niwe na furaha katika siku zote nilizokaa nawe hapo Bagamoyo. Nakuomba usinisaliti, kumbuka kila kitu tulichofanya na ahadi tulizowekeana chini ya shahidi yetu, mbuyu.
Huku ninajilinda, sitaki kuwa na msichana yeyote yule, ninakupenda na kukuhitaji wewe tu. Sihitaji msichana mwingine kwani wewe unanitosha, na milele utaendelea kunitosha mpaka pale nitakapokuoa na kuwa mke wangu wa ndoa.
Luciana, ninakupenda mpenzi, ninatamani nije kukuona lakini ninashindwa, wazazi wananibania, ila usijali, kuna siku nitakuja na kuwa pamoja nawe. Nakuahidi kuja huko mwaka huu...hii ni ahadi, nakuahidi kukuona kwa mara nyingine mwaka huu, tunza maneno yangu.
Nakupenda Luciana.
Mpaka kufikia hapo, mashavu ya Luciana yaliloanishwa na machozi, kile alichokuwa amekisoma, kiliyafanya mawazo yake kurudi nyuma kabisa na kukumbuka kila kitu alichofanya na Patrick. Akajikuta akimpenda zaidi Patrick, moyoni alijisikia kuwa na mzigo mzito wa kumpenda Patrick.
“Nakupenda Patrick, nakuahidi kutokukusaliti,” alijisemea Luciana huku akiibusu barua ile.
****
Hayo ndiyo yalikuwa maisha yao. Mara kwa mara walikuwa wakiwasiliana kwa barua kwani hakukuwa na njia nyingine yoyote ya kuweza kuzungumza, maandishi ndiyo yalikuwa mawasiliano yao makuu.
Kwa sababu mzee James hakuwa akisafiri mara kwa mara kuelekea Bagamoyo, Patrick na Luciana wakaanza kuwatumia madereva wa magari katika kusafirisha barua zao kutoka kwa mtu mmoja mpaka mwingine.
Bado mapenzi yaliendelea kuchipua mioyoni mwao na kila siku walikuwa wakijaliana sana. Simu zilikuwepo lakini kwa sababu katika kipindi hicho wanafunzi wengi hawakuwa na simu, wazazi wao hawakutaka kuwapa simu.
Luciana alitamani sana kwenda Dar es Salaam kuonana na Patrick ili amueleze ukweli alivyokuwa amemkumbuka lakini pia naye Patrick alitamani kufanya hivyo, maisha bila Luciana yalionekana kuwa si kitu.
Hakukuwa na njia nyingine, hawakuwa zaidi ya hiyo waliyokuwa wakiitumia. Kila siku mchana ilikuwa ni lazima Luciana aelekee stendi na kuonana na dereva aliyekuwa akiendesha ‘coaster’ iliyoandikwa Yesu Ni Jibu na kisha kumuuliza kama alipewa barua kutoka kwa Patrick.
“Hakunipa barua yoyote ile,” alisema dereva huyo.
“Jamani, mbona ananifanyia hivi? Ngoja, kesho nakuja na barua umpelekee,” alisema Luciana.
Hakukuwa na njia nyingine ya kufanya, ili waweze kuwasiliana ilikuwa ni lazima wamtumie dereva huyo katika kuwasafirishia barua zao kwa gharama ndogo kabisa, tena barua ingetumia dakika chache mpaka kuingia Dar es Salaam au Bagamoyo.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kila alipokuwa akikosa barua kutoka kwa Patrick, Luciana alijisikia mnyonge mno kwani hilo halikuwa jambo alilokuwa akilitaka, kila alipokuwa akimuuliza dereva kuhusiana na barua kutoka kwa Patrick, alitaka kupewa jibu kwamba ipo, asubiri na kuichukua.
“Mwambie nimemkumbuka sana,” Luciana alisema huku akimkabidhi barua dereva yule, hiyo ilikuwa ikienda kwa Patrick, ndani alikuwa akiipulizia pafyumu, na hata karatasi aliyotumia kuandikia ilikuwa ni zile karatasi zilizokuwa na mauamaua ili kumuoneshea Patrick kwamba alikuwa akimpenda.
Sefania ambaye alikuwa dereva wa gari hilo hakuwa na hiyana, kila alipopewa barua ili aisafirishe kuelekea kwa mtu fulani, wala hakuwa akikataa, kile alichokuwa akikiangalia kilikuwa fedha tu.
Mwaka wa kwanza ukakatika, hawakuonana, mwaka wa pili pia ukaingia lakini bado hawakuwa wameonana.
Hakukuwa na mtu aliyekata tamaa, maisha yao ya kuwasiliana kwa kutumia barua bado yalikuwa yakiendelea kama kawaida. Katika kipindi hiki, Luciana alikuwa kidato cha nne huku Patrick akiwa kidato cha tano katika shule ya Tabora Boys iliyokuwa Tabora.
Luciana alikuwa kwenye maumivu makali hasa pale alipofaulu na kufanikiwa kujiunga na Shule ya Sekondari ya Jangwani. Kwake, mtu ambaye alimfanya kutamani sana kuelekea Jijini Dar es Salaam alikuwa Patrick tu.
Leo hii, alikuwa amepata nafasi ya kwenda Dar es Salaam lakini mtu aliyekuwa akimfanya kuelekea ndani ya jiji hilo hakuwepo Dar es Salaam.
Hata alipofika ndani ya jiji hilo na kwenda kukaa kwa shangazi yake, bi Anna bado Luciana alikuwa na majonzi makubwa, kilikuwa kimepita kipindi cha miaka miwili na nusu hakuwa ameonana na mvulana aliyekuwa akimpenda kwa moyo wake wote.
“Mapenzi. Ninampenda sana Patrick, kwa nini haji Dar es Salaam?” alijiuliza Luciana.
Mvulana aliyekuwa akimpenda alikuwa akimaliza mwaka wake wa mwisho kidato cha sita. Luciana aliona muda kwenda taratibu sana kwani alichokuwa akikitaka ni kumuona Patrick anakuja na kuungana naye, wayafurahie mapenzi kama walivyokuwa Mjini Bagamoyo.
Siku ya kwanza Luciana kuelekea shuleni hapo Jangwani, moyo wake ulifurahi kupita kiasi. Hiyo ilikuwa ni miongoni mwa shule alizokuwa akizipenda sana katika kipindi hicho.
Pembezoni mwa shule ya Jangwani, kulikuwa na Shule ya wavulana ya Azania. Kila siku ilikuwa ni lazima wakati wa kutoka wanafunzi wa Jangwani wawasubiri wavulana wa Azania kwa ajili ya kuondoka nao kitu kilichowafanya wanafunzi wengi baina ya shule hizo kuangukia kwenye mapenzi.
Japokuwa zilikuwa shule mbili tofauti lakini ukaribu wao ukawafanya kuonekana shule moja. Kila siku ilikuwa ni lazima waonane na hata wakati Azania walikuwa wakicheza mechi na shule yoyote ile,
“Yule kaka anajua kucheza mpira,” alisema Luciana, walikuwa wakiangalia mechi kati ya Shule ya Sekondari ya Azania na Makongo.
“Unamzungumzia yupi?”
“Yule aliyevaa jezi namba tisa,” alijibu Luciana.
“Mvulana yule anaitwa Emmanuel anacheza mpira mzuri kuliko wanafunzi wote hapo Azania. Umempenda?” aliuliza msichana huyo aliyekaa na Luciana.
“Hapana, sijampenda.”
“Kama umempenda sema bwana, si unajua hapa ni lazima uwe fasta,” alisema msichana huyo.
“Hapana. Kwani hana mpenzi?”
“Mmmh! Alikuwa naye, ila sijui kama wanaendelea pamoja.”
“Alikuwa na msichana gani?”
“Hadija.”
“Sawa.”
“Unamtaka?”
“Mbona unaning’ang’ania Joah? Simtaki,” alisema Luciana huku akiachia tabasamu.
Joah hakutaka kuendelea, akanyamaza kimya huku wakiendelea kutazama mechi iliyokuwa ikiendelea. Katika kipindi chote hicho cha mpira, Emmanuel alionekana kuwa nyota wa mchezo, alicheza mpira mkubwa uliowafanya wasichana kutoka Jangwani kumshangilia kwa sauti kubwa akiwepo Luciana.
Siku hiyo ikapita, baada ya kushuhudia ushindi mkubwa wa magoli matatu, wakaamua kuendelea na masomo kama kawaida.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kwa Luciana, tayari kukaonekana kuwa na tatizo, kila alipokuwa akikaa, moyo wake ulikuwa ukimfikiria mvulana ambaye alimfurahisha kwa kusakata kabumbu la maana, Emmanuel Emmanuel.
Sura ya mvulana huyo haikumtoka kichwani, kila alipokuwa akijitahidi kumtoa kwa lengo la kumuingiza mpenzi wake, Patrick, mvulana huyo alikataa kutoka kabisa. Siku hiyo, Luciana hakulala kwa raha, kila wakati alikuwa akimfikiria Emmanuel jambo lililompa wakati mgumu.
“Jamani, ni nini hiki?” alijiuliza Luciana huku kichwa chake kikiendelea kumfikiria mvulana huyo.
Mateso makubwa yalimtesa usiku wa siku hiyo, kila wakati alikuwa akimfikiria mvulana huyo aliyeonekana kuanza kuchukua nafasi kubwa moyoni mwake. Luciana hakutaka kabisa hali hiyo iendelee kutokea, alichokifanya ni kusimama, akalifuata kabati na kutoa albamu iliyokuwa na picha kadhaa za Patrick na kuanza kuziangalia huku lengo lake likiwa ni kumsahau Emmanuel.
Hiyo wala haikusaidi, bado Emmanuel aliendelea kukaa moyoni mwake jambo lililompa wakati mgumu sana Luciana.
“Patrick rudi uuokoe moyo wangu,” alisema Luciana, kadri muda ulivyozidi kwenda na ndivyo alivyokuwa akimuona Emmanuel akichukua nafasi kubwa moyoni mwake.
***
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment