Search This Blog

Thursday, July 21, 2022

MY REPENTANCE (KUTUBU KWANGU) - 5

 







    Simulizi : My Repentance (Kutubu Kwangu)

    Sehemu Ya Tano (5)

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    ILIPOISHIA:

    Alipoondoka tu, simu yangu ilianza kuita. Nilipotazama namba ya mpigaji, alikuwa ni Evans, moyo ukanilipuka tena huku nikiandaa majibu ya kumpa.

    “Nimemuona mumeo akiondoka kwenda kazini, nakuja hapohapo nyumbani tuzungumze,” alisema Evans kisha simu ikakatwa bila kunipa hata nafasi ya kuzungumza chochote.

    SASA ENDELEA...

    Kweli muda mfupi baadaye, nilisikia mlango ukigongwa, nikamuambia msichana mmoja kati ya wale wawili tuliokuwa tunaendelea kuishi nao pale nyumbani wakinisaidia kazi ndogondogo ikiwa ni pamoja na kumlea mtoto, aende kufungua.

    Alikuwa ni Evans, tukasalimiana kisha akakaa kwenye moja kati ya masofa ya kisasa yaliyokuwa kwenye sebule yetu, akijifanya naye amekuja kumsalimia mtoto ili wale wasichana wasielewe chochote kilichokuwa kinaendelea. Sikutaka hata kumtazama usoni, nikamuuliza kilichomleta.

    “Huna haja ya kunichukia kiasi hicho, mimi na wewe tunaunganishwa na kitu kikubwa sana,” alisema Evans kwa sauti ya chini huku akigeuka huku na kule kuhakikisha hakuna aliyekuwa anatusikiliza.

    Aliposema kauli hiyo, moyo wangu ulilipuka mno na mapigo ya moyo yakaanza kunienda mbio. Bila hata kuuliza, nilijua kwamba tayari Evans ameshajua kwamba yule mtoto ni damu yake.

    “Kitu gani kinachotuunganisha?” nilijifanya kuhoji kwa ukali ili nipate uhakika kama kweli nilichokuwa nakifikiria ni kweli.

    “Siwezi kukisema, wewe mwenyewe unakijua,” alisema huku akiachia tabasamu hafifu. Kijasho chembamba kilianza kunitoka kwani kama ni wimbo, sasa ulikuwa umefika kwenye korasi.

    Kama Evans ameweza kugundua kwamba yule mtoto ni wake bila mimi kumwambia chochote, tafsiri yake ni kwamba lazima walikuwepo watu wengine ambao nao waliligundua hilo lakini wakawa wanashindwa tu kusema.

    “Umejipanga kumwambia ukweli mumeo? Mwambie tu ili muachane uje kwangu tumlee mtoto wetu,” alisema Evans, kauli yake ikawa mithili ya mkuki mkali kwenye moyo wangu.

    “Sikia nikwambie kitu, kama hicho ndicho kilichokuleta naomba uondoke haraka. Sielewi unazungumzia kitu gani.”

    “Unanielewa sana, nashukuru sana kwa kuniletea zawadi kubwa kwenye hii dunia, fanyia kazi nilichokwambia mi nitaendelea kukusubiri,” alisema Evans na kuinuka, akasogea kwenye sofa nililokuwa nimekalaza kachanga kangu, akakaangalia na kutasamu kwa furaha kisha akatoka na kuondoka.

    “Mungu wangu, sasa itakuwaje?” nilijisemea baada ya Evans kuondoka, nikashusha pumzi ndefu na kuendelea kutafakari kwa kina juu ya nini cha kufanya. Yaani nilikuwa nimeingia kwenye matatizo makubwa mno ambayo hata sikuwa najua mwisho wake utakuwa ni nini.

    Naijutia sana nafsi yangu kwa kumsaliti mume wangu kwani bila kufanya yote hayo, si ajabu mpaka leo ningekuwa naishi naye kwa raha mustarehe na kupeana mahaba ya dhati kwani kiukweli Ibra wangu alikuwa anajua sana kupenda ukiacha kasoro ndogondogo alizokuwa nazo.

    Baadaye mume wangu alirudi kazini na kunikuta sipo kwenye hali ya kawaida, nikamdanganya kwamba bado tumbo lilikuwa linauma, akanipa pole sana na kuendelea kunidekeza kama kawaida yake huku pia akitumia muda mwingi kumuangalia mtoto.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Yaani furaha uliyoileta kwenye maisha yangu, haielezeki mke wangu, nakupenda na nitaendelea kukupenda siku zote za maisha yangu.”

    “Ahsante mume wangu, nakupenda pia,” nilisema huku nikikwepesha macho yangu kwani kama angeendelea kunitazama usoni, huenda angegundua kuwa kuna jambo linaloutesa sana moyo wangu.

    “Nimekuandalia zawadi nzuri ambayo naamini utaipenda,” alisema mume wangu na kuendelea kunieleza kuwa ameagiza gari jipya kutoka Japan kwa ajili yangu kama zawadi kwa kumzalia mtoto mzuri. Maskini Ibra wangu, hakuwa anajua kwamba nimemfanyia ushetani mkubwa kiasi hicho.

    Narudia tena kusema kwamba naijutia sana nafsi yangu kwa nilichokifanya, Ibra hakuwa mwanaume wa kustahili maumivu makali kiasi hicho. Nilimshukuru sana na akanihakikishia kwamba wiki chache baadaye, litawasili bandarini kwa hiyo nisiwe na wasiwasi.

    Siku hiyo ilipita, maisha yakaendelea huku mapenzi ya mume wangu yakiwa yameongezeka kuliko mwanzo. Kila siku alipokuwa akirudi kutoka kazini ilikuwa ni lazima atuletee zawadi mimi na mwanangu. Siku aambazo alikuwa haendi kazini, tulikuwa tukishinda naye nyumbani au wakati mwingine anatutoa ‘out’ mimi na kachanga kangu.

    Wiki kadhaa baadaye, kweli gari liliwasili bandarini, akasimamia kila kitu na kufanikiwa kulitoa. Lilikuwani gari zuri mno, Toyota IST lenye rangi ya bluu iliyokolea sana, akanikabidhi funguo na kadi ya gari iliyokuwa imeandikwa jina langu. Kiukweli nilifurahi sana ndani ya moyo wangu.

    Nikawa naendelea kujilaumu kwa kumkosea mume wangu, narudia tena kusema hakustahili kufanyiwa mabaya. Kwa kuwa bado mtoto alikuwa mdogo, sikutaka kujifunza kuendesha wala kulitumia gari hilo, tukalipaki tu uani nikisubiri mtoto achangamke ili na mimi nianze kujifunza kuendesha.

    Siku zilizidi kusonga mbele, Evans akawa haji kabisa pale nyumbani zaidi ya kuendelea kunisumbua kwenye simu akinishawishi eti niachane na mume wangu tukaishi naye na kumlea mtoto pamoja, jambo ambalo nilijiapiza kuwa siwezi kulifanya.

    Alipoona nashikilia msimamo, alianza tena kutumia vitisho kama kawaida yake, akaniambia zile picha za kipindi kile alizonipiga nikiwa mtupu, bado alikuwa nazo hivyo nikiendelea kumkatalia, atamuonesha mume wangu na kumpa ukweli kwamba nimembambikia mtoto. Matatizo yakawa yameanza upya kabisa.



    Miongoni mwa vipindi ambavyo akili yangu ilikuwa njia panda, ilikuwa ni kipindi hicho baada ya kujifungua. Dhamira ilikuwa ikinisuta mno, ilifikia kipindi nikawa nahisi kama dunia nzima inajua nilichokifanya.

    Usaliti inafahamika kwamba ni mbaya na hakuna mtu anayeweza kuuvumilia katika uhusiano lakini kwangu mimi ilikuwa imezidi kwani mbali na kusaliti, nilikuwa nimepata ujauzito nje ya ndoa na hatimaye kujifungua mtoto ambaye mume wangu alikuwa akiamini kwa asilimia mia moja kwamba ni wake.

    Evans naye alikuwa anazidi kupalia makaa ya moto kwenye mtima wangu, kitendo cha kuanza kunishinikiza eti niachane na mume wangu ili mimi na yeye tuishi pamoja na kumlea mtoto, ulikuwa ni mtihani mgumu mno.

    Mbaya zaidi alikuwa akinitolea vitisho kwamba kama sitakubaliana na anachokitaka, ni bora tukose wote kwani atamwambia ukweli mume wangu na kumpa ushahidi wote. Nilijikuta nikiwa kwenye wakati mgumu mno. Kila nilipokuwa namtazama mwanangu, roho ya ibilisi ilikuwa inanijia.

    Nikiri hadharani kwamba kuna wakati nilikuwa natamani mwanangu hata afe ili kumaliza janga kubwa lililokuwa mbele yangu. Japokuwa mwenyewe hakuwa akijua, mimi mama yake nakiri kwamba nilikuwa namuwazia mabaya sana alipokuwa mdogo. Nimeamua kukiri mwenyewe kwa hiyo sina sababu ya kuendelea kuficha jambo lolote, Mungu anisamehe.

    Basi siku zilizidi kusonga mbele, maisha yakizidi kuwa mtihani mkubwa kwangu. Mume wangu hakuwa akijua chochote, aliendelea kunionesha mahaba mazito mimi pamoja na mwanangu. Nilitamani sana angekuwa mwanaye halisi kwani mapenzi aliyokuwa anayapata, yalikuwa makubwa mno.

    Evans naye aliendelea kunisumbua, baada ya kukaa na kutafakari kwa muda mrefu, niliamua kumtafuta Evans ili mimi na yeye tukae na kufikia muafaka, sikutaka anivurugie ndoa yangu na njia niliyoona kuwa inafaa, ilikuwa ni kujifanya mjinga.

    Nakumbuka siku hiyo mimi ndiye niliyempigia simu, nikamwambia nahitaji kuonana naye, akacheka sana kwa dharau kisha akaniuliza kama nimeshaanza kuona umuhimu wake au nimekubali alichokuwa anakisema.

    Nilichomjibu ni kwamba nahitaji kukutana naye ana kwa ana ili tuzungumze. Tukakubaliana kwamba yeye hataweza kuja nyumbani bali tukutane kwenye mgahawa mmoja wa Kijapan uliokuwa jirani na pale tulipokuwa tunaishi, Mikocheni.

    Siku hiyo nilimuacha mwanangu kwa wifi yangu ambaye kwa kipindi chote tangu nijifungue nilikuwa nikiishi naye akinisaidia malezi ya mtoto. Nikamdanganya kwamba naenda saluni abaki na mtoto.

    Nikaenda mpaka kwenye mgahawa huo ambapo nilimkuta Evans akinisubiri kwa hamu, kama kawaida yake tayari alikuwa ameshapata ‘mbili tatu’ kichwani japo ulikuwa ni muda wa kazi. Tukakaa kwenye meza iliyokuwa pembeni kabisa ili isiwe rahisi kwa mtu yeyote anayetufahamu kutuona.

    “Mi ninachotaka ni penzi lako tu, nataka niendelee kufaidi mapenzi yako, hilo tu.”

    “Lakini mimi ni mke wa mtu Evans, tena mke wa rafiki yako kipenzi.”

    “Mimi ndiyo mumeo, kama yeye ni mwanaume kweli mbona ameshindwa kukupa ujauzito? Mimi ndiyo kidume na inabidi uniheshimu kwa sababu nimekuzalisha,” alisema Evans kwa mbwembwe za hali ya juu.

    Tukaendelea kulumbana kwa muda mrefu, yeye akisema hiki mimi nasema kile. Mwisho niliamua kujifanya mjinga, nikamuuliza nimpe kitu gani ili akubali kuniacha niendelee na maisha yangu ya ndoa bila mume wangu kugundua chochote.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Nimeshakwambia sihitaji chochote zaidi ya mapenzi yako, kama ukiwa tayari kuniridhisha muda wowote ninaokuhitaji wala mumeo hatafahamu mpaka mtoto atakapokuja kuwa mkubwa,” alisema Evans.

    Ili kumaliza mjadala, nilimjibu kwamba anipe muda wa kwenda kufikiria alichokuwa anakitaka. Ilikuwa ni lazima nifanye hivyo kwani hali ilishakuwa mbaya, kwa akili zake, ni kweli Evans angeweza kwenda kumwambia ukweli mume wangu.

    Nilipomjibu hivyo alichekelea sana, akaniambia kuwa hayo ndiyo maneno aliyokuwa anasubiri kuyasikia kutoka kwangu. Tuliagana, nikaondoka kurudi nyumbani huku nikiwa hata sijui nifanye nini.

    Akili nyingine zilinituma kufunika kombe mwanaharamu apite, yaani nikubali kuendelea kuwa na uhusiano wa siri na Evans ili tu maisha yangu yaendelee, bado nilikuwa nampenda mume wangu na sikuwa tayari kumpoteza, hiyo ndiyo njia pekee niliyoona inafaa.

    Hata hivyo, upande mwingine nilikataa kuwa mtumwa wa mapenzi, yaani nimridhishe Evans huku moyo wangu ukiteketea? Lakini nilipopima huku na kule, niliendelea kubaki njia panda.

    Wiki nzima ilipita bila kumjibu chochote Evans, huku maisha na mume wangu yakiendelea, kila siku nikijitahidi kuficha hisia chungu zilizokuwa ndani ya mtima wangu.

    Baadaye niliamua liwalo na liwe, nikamwambia Evans kuwa nimekubali ombi lake lakini asubiri mpaka nimalize kunyonyesha ndiyo mapenzi ya siri yaendelee. Nilijua kwa kumwambia hivyo nitakuwa nimemkwepa kijanja kwani isingekuwa rahisi kwake kunisubiri kwa miaka miwili yote mpaka mwanangu aache kunyonya.

    Kumbe mwenzangu alikuwa mjanja zaidi yangu, akakubali na kuahidi kuwa atanisubiri wala nisiwe na wasiwasi wowote. Kidogo nikaona mzigo mzito niliokuwa nimeubeba umepungua uzito. Laiti kama ningejua mawazo ya Evans, ni bora ningeendelea kushikilia msimamo wangu. Nilikuwa nimekubali kujiingiza mwenyewe kwenye mdomo wa mamba.



    Siku zilizidi kusonga mbele huku mwanangu akizidi kuwa na afya njema na mapenzi kati yangu na mume wangu yakizidi kunoga. Mwenyewe alizidi kutuonesha mahaba mazito mimi na mwanangu, akawa anatuletea zawadi nyingi nzuri ambazo ama kwa hakika zilikuwa sawa na mwiba mkali kwenye mtima wangu.

    Kadiri alivyokuwa anazidi kutuonesha mahaba mazito ndivyo nafsi yangu ilivyokuwa inazidi kunisuta, nilijilaumu sana kwa kosa kubwa nililomfanyia. Mtoto alipofikisha umri wa miezi mitatu, hali yake ya kiafya ilianza kubadilika.

    Ule uchangamfu aliokuwa nao ukaanza kupungua, muda mrefu akawa analialia hasa nyakati za usiku na kuchemka sana homa. Awali nilidhani ni maradhi ya kawaida ya watoto lakini kadiri siku zilivyokuwa zinazidi kusonga mbele, ndivyo mimi na mume wangu tulivyoanza kuingiwa na wasiwasi mkubwa kuhusu afya ya mtoto.

    Awali tulikuwa tukimpeleka kwenye hospitali binafsi iliyokuwa jirani na pale tulipokuwa tunaishi ambapo walipompima kwa mara ya kwanza, walisema ni homa ya kawaida kwa mtoto, wakampa dawa lakini haikusaidia chochote.

    Siku chache baadaye tulirudi tena hospitalini hapo, akafanyiwa vipimo tena, majibu yakatoka eti anasumbuliwa na malaria, akaandikiwa dozi ambayo nayo haikusaidia chochote.

    “Inabidi tumpeleke kwenye hospitali kubwa, inawezekana hawa vipimo vyao havioneshi kwa usahihi kinachomsumbua,” alisema mume wangu, wazo ambalo nililikubali.

    Kesho yake mume wangu hakwenda kabisa kazini kwani ndiyo siku tuliyokubaliana kumrudisha mtoto Hospitali ya Aga Khan ambako ndiko nilikojifungulia. Hali ya mwanangu ilikuwa imebadilika kabisa, jambo lililosababisha huzuni kubwa kwenye familia yetu.

    Hakuna aliyekuwa anakula chakula kinashuka wala kulala usingizi, usiku kucha tulikuwa tukikesha kuhangaika na mtoto. Kweli tulifunga safari mpaka Hospitali ya Aga Khan ambako mwanangu alipokelewa na kuanza kufanyiwa vipimo vyote ili kubaini kilichokuwa kinamsumbua.

    Japokuwa vipimo vyote vilikuwa vikigharimu fedha nyingi, hilo halikuwa tatizo kwa mume wangu kwani alikuwa anajimudu kiuchumi. Baada ya kuchukuliwa vipimo vyote, tulienda kukaa kwenye chumba maalum kusubiri majibu.

    Baada ya kusubiri kwa muda mrefu, daktari mmoja aliyekuwa na asili ya Kihindi ambaye ndiye aliyekuwa akisimamia vipimo vya mwanangu, alikuja kutuchukua mimi na mume wangu, tukaongozana mpaka kwenye ofisi yake ambapo juu ya meza yake kulikuwa na kibao kilichoonesha kuwa kumbe anaitwa Dokta Prakesh.

    Daktari huyo alisema vipimo vya mtoto vimeshatoka lakini ili kuwa na uhakika wa majibu hayo, ilikuwa ni lazima mimi na mume wangu tupimwe pia ili kuwa na majibu ya kuaminika. Kengele ya hatari ikalia ndani ya kichwa changu, sikuelewa daktari huyo amegundua nini mpaka atake mimi na mume wangu pia tupime kipimo kiitwacho FBP (Full Blood Picture).

    Nikajua mwisho wa uongo wangu juu ya baba halisi wa mtoto huyo ulikuwa umekaribia. Nilichokihisi ni kwamba huenda daktari amebaini kwamba mwanangu ana ugonjwa ambao amerithi kutoka kwa wazazi wake na alichokuwa anataka kukifanya ni kuthibitisha tu, mapigo ya moyo yakaanza kunienda mbio.

    Nilitamani kukataa lakini sikuwa na ujanja kwani huenda ningetoa picha mbaya mbele ya mume wangu, nikakubali ambapo tulipelekwa maabara tulikochukuliwa damu kwa ajili ya vipimo, tukarudi tena kwenye kila chumba cha awali kusubiria majibu.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Nilikosa amani mno ndani ya nafsi yangu, nikajua ule usemi wa wahenga kwamba mbio za sakafuni huishia ukingoni, zilikuwa zimetimia. Baada ya takribani dakika 40, yule daktari alitufuata tena na tukaongozana naye mpaka ofisini kwake.

    Tulipoingia, alianza kwa kutuhoji maswali mbalimbali kila mmoja kuhusu historia ya familia yake. Alianza na mume wangu ambapo alimuuliza kama katika ukoo wao, kuna historia ya maradhi ya kuambukizwa.

    Mume wangu alifikiria kwa muda lakini mwisho alikataa kwamba hakukuwa na magonjwa yoyote ya kurithi. Mume wangu alikuwa sahihi kwa sababu tangu nianze kuwafahamu ndugu zake, hakuna hata mmoja aliyekuwa na matatizo yoyote ya kiafya.

    Aliponigeukia mimi, alianza kuniuliza maswali kama yaleyale, akaniuliza historia ya ukoo wetu nami sikutaka kuficha chochote kwani hata kama ningedanganya, vipimo vya damu yangu vingeonesha au pengine tayari vilishaonesha hivyo kwani majibu alikuwa nayo mkononi.

    Kiukweli katika ukoo wetu, kulikuwa na ugonjwa uliokuwa unawasumbua sana ndugu zetu wa karibu wa sickle cell. Hata katika familia yetu ya baba mmoja na mama mmoja, mdogo wetu wa mwisho alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa huo, achilia mbali ndugu zetu wengine wa upande wa baba na upande wa mama.

    Baada ya kumpa maelezo hayo, nilimuona akikuna kichwa chake, akasema kuna hali isiyo yakawaida ilikuwa imetokea kwa mtoto wetu. Akaanza kutufafanulia kwamba ili mtu awe na ugonjwa wa sickle cell, lazima arithi chembe moja ya ugonjwa huo kutoka kwa baba na nyingine kutoka kwa mama.

    Akaeleza kwamba ili mzazi amrithishe mtoto ugonjwa, siyo lazima na yeye awe mgonjwa kwani wapo watu wengi wenye seli moja ya ugonjwa huo ambao hawaumwi kabisa na ili mtu augue, ni lazima awe na seli mbili.

    “Sasa vipimo vinaonesha kwamba wewe mama umemrithisha mtoto seli moja lakini vipimo vya baba havioneshi kama ana seli hata moja za ugonjwa huu, jambo ambalo siyo la kawaida,” alisema daktari huyo kwa Kiswahili chenye lafudhi ya Kihindi, mapigo ya moyo yakawa yananienda mbio kuliko kawaida kwani nilichokihisi ndicho kilichokuwa kinaenda kutokea. Lazima mume wangu angeujua ukweli ambao nilijitahidi kuuficha kwa kipindi kirefu.



    “Daktari, kama sijakuelewa hivi! Hebu naomba njoo tuzungumze peke yetu pembeni,” alisema mume wangu, kijasho chembamba kikawa kinanitoka mtoto wa kike. Nilitamani dunia ipasuke ili nizame ndani na kuikwepa aibu kubwa iliyokuwa inaelekea kunipata.

    Kweli daktari na mume wangu walisogea pembeni na kwenda kuzungumza, hata sijui walizungumza nini lakini naona tayari mume wangu alishaingiwa na wasiwasi kwamba huenda mtoto hakuwa wake lakini alitaka kupata uhakika zaidi.

    Walitumia zaidi ya dakika thelathini kuzungumza, mume wangu akimuuliza maswali mengi daktari, naye akimfafanulia kwa kina. Nikajua nimekwisha. Baadaye walirejea pale waliponiacha lakini mume wangu hakuonesha uchangamfu kama awali, alionesha kuwa na mwazo mengi sana ndani ya kichwa chake.

    Sikutaka hata kumtazama usoni, ukimya mkubwa ukatawala kati yetu. Daktari yule na wenzake waliendelea kumhudumia mtoto wetu na kutokana na hali mbaya aliyokuwa nayo, walimuandikia mwanangu kwamba alazwe ili apate matibabu ya uhakika. Akapelekwa wodini ambapo alitundikiwa dripu na kuchomwa sindano nyingi pamoja na dawa za kunywa.

    Siku ya kwanza ilipita bado tukiwa hospitalini, mume wangu akiendelea kuwa na mawazo mengi sana. Sikutaka hata kumuuliza chochote kwani na mimi sikuwa na jibu la kumpa endapo angeniuliza swali lolote.

    Tulikuwa tukilala wodini na mtoto wetu huku kila mmoja akiwa kimya kabisa, sikujua mume wangu alikuwa anawaza nini kwenye kichwa chake. Siku ya tatu, ilibidi aende kwanza nyumbani kujiandaa kwa ajili ya kwenda kazini, akanibebea na nguo za kubadilisha pamoja na za mtoto, akatuletea hospitalini kisha yeye akaniaga kwamba anaenda kazini lakini atarejea baada ya muda mfupi.

    Nikabaki na mwanangu ambaye baada ya kupatiwa matibabu ya uhakika pale Aga Khan, angalau hali yake ilianza kutengemaa, akawa halii tena kama ilivyokuwa awali na hata tabasamu lake la kitoto likaanza kuchanua upya kwenye uso wake.

    Mchana mume wangu alikuja tena hospitalini kuungana na mimi lakini kilichonishangaza, alikuwa akinukia harufu ya pombe japokuwa nje kulikuwa na jua kali. Nikajua tayari ‘kimenuka’ kwani dalili ya kwanza kuonesha kwamba mume wangu hayuko sawa kiakili, ilikuwa ni kunywa sana pombe.

    Moyoni niliingiwa na hofu kubwa sana kwani ni bora kama angeniuliza chochote ili nipate nafasi hata ya kumdanganya lakini mwenzangu alikuwa kimya kabisa. Nilitamani kutubu na kumwambia ukweli lakini thubutuu! Ningeanzia wapi? Nikaamua kukubali kuendelea kuteketea ndani ya moyo wangu.

    Kwa kuwa alikuwa amekunywa pombe, kidogo alianza kunionesha uchangamfu, tukawa tunazungumza mambo mbalimbali na baadaye mtoto alipolala, aliniambia anataka anitoe tukazunguke kidogo mjini kupunguza uchovu wa akili kwani tangu tufike hospitalini hapo, sikuwa nimetoka hata mara moja.

    “Japokuwa nilikuwa nafurahia sana kutolewa ‘out’ na mume wangu, siku hiyo nilikuwa na hofu kubwa ndani ya moyo wangu kiasi kwamba hata sikutaka kutoka na mume wangu. Bado sikuwa najua anafikiria nini ndani ya kichwa chake. Nilishindwa kuelewa kama ameshaujua ukweli au bado, nilibaki gizani.

    Hata hivyo, nilishindwa kumkatalia, nikakubali kwa shingo upande ambapo tulitoka mpaka nje ya hospitali hiyo huku jukumu la kumuangalia mtoto kama ataamka tukiwa tumeamuachia nesi aliyekuwa akituhudumia kuanzia siku ya kwanza.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Tulienda mpaka kwenye mgahawa mmoja maarufu sana katikati ya Jiji la Dar es Salaam, King Steers ambapo tulienda kula piza na vinywaji, huku muda wote mume wangu akijaribu kunipigisha stori za kunifurahisha. Ilikuwa ni kawaida ya mume wangu kwamba kama amekunywa pombe kidogo, anakuwa mzungumzaji sana.

    Baadaye tulirudi hospitalini tukiwa tumebeba vyakula vingine kwa ajili ya mtoto na sisi wenyewe usiku kwani hatukuwa na ratiba ya kutoka tena. Tuliporudi, mume wangu alijilaza kwenye kitanda kingine kilichokuwa ndani ya wodi hiyo na akapitiwa na usingizi kutokana na kunywa pombe.

    Nilibaki nimekaa pembeni yake, majuto makubwa yakiendelea kuutesa moyo wangu, nilitamani siku zirudi nyuma ili nirekebishe makosa yangu lakini hilo halikuwezekana.

    Njia pekee niliyoona inaweza kunisaidia, nilipanga kwamba tukiruhusiwa kutoka hospitalini nitajitahidi kumpa mume wangu mahaba mazito ili kumfurahisha na kumfanya kama alikuwa ananihisi mabaya, basi aanze tena kuniamini.

    Kwa bahati nzuri, kesho yake asubuhi tuliruhusiwa kurudi nyumbani kwani mtoto alikuwa na ahueni kubwa, mume wangu akalipa kila kitu na kutoka mpaka nje, safari ya kuelekea nyumbani ikaanza.

    Tulirudi nyumbani na kwa kuwa bado ilikuwa ni mapema, mume wangu alijiandaa kwa ajili ya kwenda kazini. Sikutaka kumruhusu kwani tayari nilishakuwa na mipango yangu kichwani, na mimi nikaenda kuoga baada ya kuwa nimemlaza mtoto vizuri kisha nikarudi chumbani nikiwa na khanga moja tu.

    Kwa kuwa nilikuwa najua namna ya kumteka hisia mume wangu, nilianza kumfanyia vituko vya hapa na pale na kwa kuwa tangu tuende hospitali siku nne zilikuwa zimepita bila kukutana naye faragha, haikuwa kazi ngumu kumuingiza mchezoni.

    Mtoto wa kike nikajiweka sawa huku moyoni nikijiapiza kuwa nitampa mume wangu mahaba ya nguvu ili kumfanya arejeshe tena imani na mimi na kusahau matatizo ya mtoto.

    Kipyenga kilipopulizwa tu kuashiria kuanza kwa mechi ya kirafiki, isiyo na refa wala mwamuzi, mtoto wa kike nilianza kwa spidi 120, nikitumia mpaka mbinu za ziada kumpagawisha mume wangu. Nilifanikiwa kwa kiasi kikubwa kumchanganya kabisa akili zake, akawa anagugumia kama dume la njiwa.



    Siku hiyo kazi ilikuwa moja tu, nikajituma mtoto wa kike mpaka mume wangu akafurahi. Hakwenda tena kazini, tulishinda ndani kutwa nzima. Mbinu yangu ikawa imefanikiwa.

    Sikuishia hapo, kwa karibu wiki nzima nilikuwa na kazi moja tu ya kumfurahisha mume wangu. Akawa akitoka kazini tu basi tunashinda ndani na kufanya yetu. Sikutaka kitu chochote kiingie tena katikati yetu, hata mtoto hakuwa tena na umuhimu kwa kipindi hicho.

    Niliamini kwa mahaba ya dhati niliyompa mume wangu, hawezi tena kuendelea kunihisi vibaya, nikawa nimefanikiwa kurejesha amani na furaha kwenye ndoa yangu. Mume wangu akawa haendi tena kunywa pombe, hali iliyonifanya niamini akili yake imeshatulia. Hali ya mtoto nayo iliendelea vizuri, akawa amepona kabisa matatizo yake.

    Katika kipindi ambacho nilikuwa naamini kila kitu kimeisha, siku moja nilishtuka mno baada ya mume wangu kuniambia jambo ambalo sikuwahi kuwaza kama anaweza kufikiria hivyo.

    “Nataka twende tukampime mtoto DNA,” aliniambia mume wangu, kauli iliyonifanya moyo wangu ulipuke mno.

    Nilishindwa cha kumjibu, nikabaki nimezubaa nikiwa kama siamini. Mume wangu hakuwa na hata chembe ya masihara, alichokisema alimaanisha na kwa msisitizo akaniambia nikajiandae mimi pamoja na mtoto. Sikuwa na cha kufanya, nikajua hatimaye ukweli unaenda kufahamika.

    Kweli nilienda kujiandaa huku mwili ukiwa hauna nguvu kabisa, sikujua nitauficha wapi uso wangu. Ule msemo kwamba mwanamke mpumbavu huvunja nyumba yake kwa mikono yake ulikuwa ukienda kutimia kwangu, ujinga wangu ulikuwa unaelekea kunigharimu.

    Baada ya kumaliza kujiandaa, nilimuandaa na mwanangu kisha tukatoka mpaka kwenye maegesho ya magari. Tukaingia kwenye gari lile ambalo mume wangu alikuwa ameninunulia, yeye akakaa nyuma ya usukani, mtoto nikawa nimembeba mimi kisha safari ikaanza.

    Tulienda mpaka Posta kwenye ofisi za mkemia mkuu ambapo ndiyo mahali pekee kipimo cha DNA kilikuwa kikifanyika kwa kipindi hicho. Tukaingia mpaka ndani ambapo mume wangu ilionesha ameshazungumza na wale watu wa pale kwani walipomuona, walimchangamkia na kutukaribisha.

    Wakamchukua mwanangu sampuli za mate, nywele na kucha kisha mume wangu naye akachukuliwa vitu hivyo. Nikawasikia wakizungumza kwamba kipimo hicho kitaalamu kilikuwa kinaitwa partenity test ambacho kilikuwa maalum kwa ajili ya kutambua uhalali wa mzazi wa kiume wa mtoto.

    Nilikuwa na hali mbaya sana lakini sikuwa na jinsi, kama ni maji tayari yalishamwagika na hakukuwa na namna yoyote ya kuubadili ukweli. Sikuwa najua mume wangu atafanya nini baada ya kuujua ukweli kwamba yule mtoto hakuwa wake.

    Nilijisikia kuwa na hatia kubwa mno ndani ya moyo wangu. Kwa bahati nzuri, kumbe majibu ya DNA huwa hayatoki siku hiyohiyo, wakatuambia kuwa yatakuwa tayari baada ya siku nne au tano. Nilimshukuru sana Mungu wangu kwani nilijua ndani ya siku hizo nitakuwa nimeshapata majibu ya nini cha kufanya.

    Tulirudi nyumbani na mume wangu huku nikiwa kimya kabisa. Siwezi kumlaumu sana mume wangu na ndiyo maana kuanzia mwanzo nilisema kwamba mimi ndiyo nilikuwa chanzo cha yote na huu ushuhuda wangu nataka uwe fundisho kwa wanawake wenzangu kutorudia kufanya ujinga kama nilioufanya mimi.

    Tulipofika nyumbani, niliendela kuwaza na kuwazua nikiwa sijui mume wangu atachukua hatua gani atakapoujua ukweli. Japokuwa alikuwa ananipenda sana, sikuwa na uhakika kama anaweza kunisamehe kwa nilichomfanyia.

    Usaliti pekee lilikuwa kosa kubwa lakini mbali na kumsaliti, nilikuwa nimemfanyia kosa lingine kubwa zaidi kwa kumbambikia mtoto ambaye si damu yake. Kila nilipokuwa nikimtazama mwanangu, nilikuwa nikimuonea sana huruma kwani yeye hakuwa na kosa lolote.

    Uamuzi nilioona unafaa, kabla majibu ya DNA hayajatoka, niliamua kuondoka kwa mume wangu na kurejea nyumbani kwa wazazi wangu kwani wahenga wanasema ng’ombe akivunjika mguu hukimbilia zizini. Nilimdanganya mume wangu kwamba mama yangu alikuwa anaumwa hivyo alitaka niende kumuuguza.

    Sababu hiyo ilikuwa nyepesi sana kwa mume wangu kuniamini, akaniambia suala la kwenda kukaa nyumbani wakati nikiwa na mtoto mdogo alikuwa haliafiki na akasema kama ni suala la kumuuguza, naweza kuwa naenda asubuhi na kushinda huko mpaka jioni ndiyo nirudi kwangu.

    Japokuwa nilimkubalia lakini kichwani nilikuwa na wazo langu tofauti kabisa, sikutaka kusubiri mpaka mume wangu aje kuujua ukweli nikiwa bado nakaa naye. Nilisubiri alipoondoka kwenda kazini ambapo nilichukua baadhi ya nguo zangu na za mwanangu, nikaondoka na kurudi nyumbani kwetu, Morocco jijini Dar es Salaam.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kwa kuwa hapakuwa mbali, nilikodi Bajaj tu iliyotubeba mimi na mwanangu. Nilipofika nyumbani, mama alifurahi kuniona, akajua nimeenda kumsalimia kama kawaida yangu kumbe tayari nilikuwa nimeshaharibu kwa mume wangu.

    Nilishindwa hata nianzie wapi kumueleza mama, nikaamua kujipa muda kwanza mpaka akili itulie. Nilikaa nyumbani pale tukipiga stori za hapa na pale, muda ukawa unayoyoma hatimaye jioni ikafika.

    “Vipi mwenzetu leo unalala hapahapa nini? Naona muda unakwenda lakini hauna dalili za kurudi kwako,” mama aliniuliza, nikakosa cha kumjibu zaidi ya kumwambia tu kuwa nitalala palepale nyumbani.

    “Ulimuaga mumeo?” mama aliniuliza swali lingine lakini kabla sijajibu, simu yangu ikaanza kuita mfululizo, nilipotazama namba ya mpigaji alikuwa ni mume wangu, moyo wangu ukanilipuka kwa nguvu.



    “Uko wapi mpaka muda huu?”

    “Niko nyumbani.”

    “Utarudi saa ngapi huoni muda umeenda sana?”

    “Sirudi, si nilikwambia mama anaumwa?”

    “Lakini hayo hayakuwa makubaliano yetu.”

    Mume wangu alionyesha kukasirishwa sana na nilichokuwa nimekifanya, lakini sikuwa na njia nyingine. Hata kabla hatujamaliza kuzungumza alikata simu, jambo ambalo siyo kawaida yake. Ikabidi nimpigie lakini hakupokea simu, ikaita mpaka ikawa inakaribia kukata ndipo alipopokea. Nikaanza kumuelewesha kwamba hali niliyomkuta nayo mama haikuwa nzuri hivyo nisingeweza kurudi.

    Japokuwa nilikuwa nikimdanganya nilijitahidi kupangilia maneno mpaka akanielewa. Usilolijua ni sawa na usiku wa giza laiti kama angejua sababu iliyonifanya kuondoka nyumbani kwangu wala asingekubali niendelee kumdanganya.

    Nikiri wazi kwamba japokuwa nilikuwa nampenda sana mume wangu, sikuwa tayari kuendelea kukaa naye kwani kuna bomu kubwa ambalo lilikuwa likikaribia kulipuka. Siku chache baadae majibu ya DNA yangetoka na kumfanya ajue ukweli ambao sikuwa na uhakika angeupokeaje. Nilikuwa nimefanya dhambi kubwa sana ambayo hakuna mwanaume angeweza kuivumilia. Wanaume wenyewe watakuwa mashahidi kwamba hata iweje huwezi kuendelea kuishi na mwanamke ambaye mbali na kukusaliti amefikia hatua ya kuzaa nje ya ndoa.

    Baada ya kumaliza kumdanganya mama aliniita chumbani kwake na kunikalisha chini. Nahisi alinisikia wakati nikizungumza na mume wangu na kumfanya awe na maswali mengi yaliyokosa majibu.

    “Mwanangu hebu niambie ukweli,wewe na mume wako mpo sawa kweli?”

    “Tupo sawa mama,”nilijaribu kumdanganyana mama lakini kwa sababu alikuwa akinijua vizuri alishtuka haraka kwamba namdanganya. Akazidi kunibana kwa maswali na kunitaka nimwambieu kweli. Nilishusha pumzi ndefu na kumtazama mama, uso wake ulionesha kutokuwa na masihara hata kidogo.Nikabaki kimya kwa sekunde kadhaa nikitafakari kama nimwambie ukweli ama nimdanganye. Kwa kuwa mama yangu alikuwa ni rafiki yangu mkubwa tangu nikiwa mdogo niliamua kumweleza tuu kweli.

    Nilimweleza kila kitu kuanzia matatizo aliyokuwa nayo mume wangu mpaka jinsi nilivyoshawishika na kujikuta nikiangukia dhambini na rafiki yake. Maelezoyangu yalimfanya mama abaki amepigwa na bumbuwazi kubwa, akanitolea macho akiwa kama haamini.

    “Umekosea sana mwanangu, ulichofanya ni uuaji mkubwa,” mama alisema na kuendelea kunishangaa. Akaniambia licha ya umri wake mkubwa, angekuwa yeye katika nafasi yangu wala asingethubutu kufanya kama nilichokifanya mimi. Aliendelea kunisema kwa muda mrefu mwisho akaniuliza kama mume wangu alikuwa anajua? Nikamjibu kwamba hakuwa akijua ila siku chache baadae angeufahamu ukweli wote.

    “Kivipi?” Mama aliniuliza huku akionesha kuwa na shauku kubwa ya kutaka kusikia nitamjibu nini. Ilibidi nimueleze kuwa mume wangu tayari alishaanza kuwa na wasiwasi hasa kutokana na maradhi aliyokuwa nayo mwanangu.

    Sikumficha kitu kwani yeye ndiye mtu pekee ambaye angeweza kuwa msaada wangu kwa kipindi hicho. Japokuwa alinisema sana lakini mama ni mama kwani ilifika kipindi akawa ananionea huruma na kuanza kunishauri nini cha kufanya.

    Aliniambia kwamba inatakiwa nimwambie mume wangu ukweli hata kabla hayo majibu ya DNA hayajatoka ili kama ni kuchukua hatua, ajue mwenyewe nini cha kufanya. Alichoniambia mama kilikuwa kitu kigumu sana kwangu. Nimwambie mume wangu kwamba nilikuwa namsaliti na rafiki yake mpaka nikazaa nje ya ndoa yangu? Thubutuu, ningeanzaje?

    Hata hivyo,mama aliendelea kunisisitiza kuwa ni lazima nifanye hivyo kwani ndiyo njia pekee ambayo angalau ingesaidia kwa wakati huo. Alipoona nakuwa mgumu wa kuelewa alichokuwa ananiambia, aliamua kuchukua jukumu hilo yeye mwenyewe.

    Kwa kuwa alikuwa na namba ya simu ya mume wangu, aliamua kumpigia yeye mwenyewe na kumwambia kuwa asubuhi na mapema aje nyumbani ana mazungumzo naye.



    Moyo wangu ulilipuka mno, nikawa hata sielewi nini kitatokea. Usiku huo ulikuwa mrefu sana kwangu, kila nilipokuwa namtazama mwanangu ambaye hakuwa akijua chochote, nilimuonea huruma sana. Yeye hakuwa na makosa yoyote isipokuwa mimi mama yake.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Usiku mzima sikupata usingizi hata kidogo, kesho yake asubuhi kweli mume wangu aliwahi kuja mpaka pale nyumbani kwetu. Alipofika, mama aliniambia mimi ndiyo niende kumpokea na kumpeleka sebuleni kisha yeye atajua nini cha kufanya.

    Kumbe tayari alikuwa ameshawapigia simu na washenga wetu ambao nao muda mfupi baadaye walikuja, mume wangu akawa anashangaa kwani bado hakuwa akijua chochote. Baada ya watu wote kufika, mama alimuita baba ambaye muda wote alikuwa bado chumbani.

    Nadhani mama alishamwambia kila kitu kwani yeye ndiyo alipaswa kuwa msemaji mkuu kwenye kikao hicho cha dharura. Kila macho yangu na ya baba yalipokuwa yakigongana, nlikuwa naziona hasira alizokuwa nazo dhidi yangu. Nilichokifanya kilikuwa kimewatia aibu sana kwani mwisho wa siku ilionekana kwamba wao ndiyo hawakunilea katika maadili.

    Baba alivunja ukimya kwa kuanza kuzungumza lengo la kuitisha kikao hicho cha dharura.



    Alianza kwa kueleza masikitiko yake kwamba mimi binti yao waliyenioza kwa Ibra, nilikuwa nimewasababishia aibu kubwa kiasi kwamba hawakuwa wakijua wazifiche wapi nyuso zao. Nilipomtazama mume wangu, nilimuona bado akiwa na shauku kubwa ya kutaka kujua kilichotokea kwani bado alikuwa gizani.

    Baba alishindwa kwenda moja kwa moja kwenye pointi, akawa anaendelea kueleza masikitiko yao wao kama wazazi juu ya kilichotokea, akanitupia lawama nyingi sana na kumpa pole Ibra kwani nilichokifanya kwake, ilikuwa sawa na ushetani wa hali ya juu.

    “Mkeo alikuwa akiisaliti ndoa yenu kwa kutembea na rafiki yako, mimi simjui lakini naskia mnafanya naye kazi, anaitwa nani sijui... Evans. Matokeo yake, walinogewa na mchezo huo na kusababisha mkeo abebe ujauzito ambao siyo wako.

    “Najua ulifurahi sana mkeo kupata ujauzito, hata siku alipojifungua, nakumbuka jinsi ulivyokuwa na furaha. Mimi ni mwanaume kama wewe, sioni sababu ya kukufanya uamini jambo ambalo siyo kweli.

    “Najaribu kujiweka kwenye nafasi yako na ndiyo maana nimeamua niwaite wote na kueleza ukweli huu, najua utaumia sana lakini mwisho yatapita na utakuwa na uchaguzi wa ama kuendelea na mkeo ukiwa unaujua ukweli au kuachana naye.

    “Sisi wazazi wake tutakuwa tayari kupokea uamuzi wowote ambao utauchukua, hilo ndiyo jambo kubwa lililonifanya niwaite hapa leo,” alisema baba na kushusha pumzi ndefu.

    Sikuweza hata kumtazama mume wangu, muda wote nilikuwa nimejiinamia, huku nikijisikia aibu ya hali ya juu. Hakuna siku ambayo niliijutia nafsi yangu kama siku hiyo, kamwe sitakuja kusahau kwenye maisha yangu.

    Kwa macho ya kuibia nilimtazama mume wangu, alikuwa amepigwa na butwaa kubwa akiwa ni kama haamini kile alichokisikia kutoka kwa baba. Japokuwa ilikuwa ni asubuhi, nilimuona akitokwa na kijasho chembamba, macho yake yakabadilika na kuwa mekundu mno. Ama kwa hakika alitia huruma sana.

    Ilibidi wale washenga waanze kumwambia maneno ya kumtuliza kwani kwa hali aliyokuwa nayo, ama kwa hakika angeweza kufanya jambo lolote muda ule. Badala ya kumtuliza, maneno aliyokuwa akiambiwa na washenga wetu kwamba apige moyo konde na kuuvaa ujasiri wa kiuanaume, yalimfanya aanze kutokwa na machozi ya uchungu.

    Hakuishia hapo, alianza kuangua kilio kwa sauti huku akiniuliza alikuwa amenikosea jambo gani hadi kusababisha nimfanyie ukatili mkubwa kiasi hicho. Sikuwa na jibu zaidi ya mimi pia kuanza kulia. Japokuwa baba ni jasiri sana, nilimuona naye akitoa kitambaa chake mfukoni na kuanza kujifuta machozi.

    Hali kadhalika, wale washenga nao niliwaona kila mmoja akifuta machozi ingawa hakuna aliyependa kuonekana kwamba analia. Mama ambaye alikuwa chumba cha pili, akisikiliza kila kilichokuwa kikiendelea, naye nilimsikia akilia kwa uchungu. Ilikuwa siku mbaya sana, ungeweza kudhani pale nyumbani kwetu kuna msiba.

    Mume wangu alishindwa hata kuaga kwa jinsi alivyokuwa analia kwa uchungu, akainuka kwa kusaidiwa na wale washenga ambao walimtoa mpaka nje kwenye gari lake, wakamsihi sana kwamba asiendeshe gari akiwa kwenye hali hiyo bali ajipe muda wa kupumzika kidogo lakini hakuwasikiliza.

    Tulisikia gari lake likiondoka kwa kasi kubwa kutoka pale alipokuwa amelipaki, mita chache kutoka nyumbani kwetu. Mimi niliendelea kulia kwa uchungu, sikuweza kuendelea kukaa pale sebuleni, nikakimbilia chumbani alipokuwepo mama pamoja na mwanangu, tukawa tunalia kwa uchungu mithili ya watu waliopokea taarifa za msiba.

    Wale washenga nao walishindwa kuendelea kukaa pale nyumbani, waliagana kuondoka huku waakimuachia maagizo baba kwamba kama atawahitaji muda wowote, watakuwa tayari kufika pale nyumbani.

    Baba alipoingia ndani, alipitiliza moja kwa moja mpaka chumbani kwake, tukamsikia akibamiza mlango kwa nguvu, kuonesha ni kwa kiasi gani alikuwa amekasirishwa na upumbavu niliousababisha.

    Waliosema mchuma janga hula na wa kwao hawakuwa wamekosea. Nilikuwa nimelichuma janga kubwa ambalo sasa halikumuathiri mume wangu na mimi pekee bali watu wote waliokuwa wakitupenda.

    Kwa jinsi baba alivyokuwa na hasira, nilijua kwamba nikiendelea kukaa pale nyumbani, anaweza kunidhuru vibaya kutokana na aibu niliyokuwa nimewasababishia.

    Kimbilio langu pekee alibaki kuwa mama yangu ambapo tulipanga naye njama kwamba mimi na mwanangu tuondoke nyumbani hapo bila baba kujua chochote na kwenda kwa mama yangu mpogo aliyekuwa akiishi Mkuranga mkoani Pwani.

    Nilipanga kwenda kukaa huko mpaka mambo yatakapotulia kwani kwa jinsi mume wangu alivyolipokea jambo hilo, uwezekano wa mimi na yeye kuendelea kuishi pamoja ulikuwa mdogo.

    Siku hiyohiyo, nilijiandaa mimi na mwanangu na kwa kuwa bado nilikuwa na kiwango kikubwa cha pesa nilizotoka nazo kwa mume wangu, ambazo siku za nyuma alikuwa akinipa kwa ajili ya matumizi yangu binafsi ila mimi nikawa naweka akiba, sikupata shida.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Niliondoka kimyakimya mpaka kwenye kituo cha daladala cha Morocco na kumuacha mama akiendelea kulia huku baba naye akiwa amejifungia chumbani kwake, nahisi naye alikuwa analia. Nilijisikia kuwa na hatia kubwa ndani ya mtima wangu kuwatoa machozi wazazi wangu, mume wangu pamoja na washenga.

    Nilipanda magari yanayoelekea Mbagala ambapo nilipofika, nilishuka na kuanza kutafuta magari ya kuelekea Mkuranga huku nikiwa na mwanangu mgongoni. Maisha yalikuwa yamebadilika kwa kasi kubwa mno.



    Nilisubiri usafiri kwa muda, baadaye likaja gari ambalo mimi pamoja na abiria wengine tuliokuwa tukisubiri usafiri tulipanda na kuanza safari ya kuelekea Mkuranga. Kiukweli kila nilipokuwa namtazama mwanangu mdogo, nilikuwa nashindwa kuyazuia machozi yasiulowanishe uso wangu.

    Hatimaye niliwasili Mkuranga ambapo nilipokelewa vizuri na mama yangu mdogo, Mrs. Mpogo ambaye tayari alikuwa ameshawasiliana na mama na kuelezwa kila kitu kilichokuwa kimenitokea. Kiukweli mama mdogo alinipokea vizuri sana, akawa ananifariji na kunisihi nijipe muda wa kukaa na kutafakari mustakabali wa maisha yangu.

    Alinihakikishia kwamba kwa muda wote nitakaokuwa naishi naye, nitakuwa huru na salama. Akaniambia kuwa pia nisiwe na wasiwasi na mwanangu kwa sababu atalelewa vizuri kama alivyokuwa akilelewa kipindi nikiwa kwa baba yake.

    Namshukuru sana mama yangu mdogo na namuombea kwa Mungu ampe maisha marefu kwani alifanikiwa kunituliza kwa kiasi kikubwa sana. Pia alinipa ushauri kwamba kama nahisi kukaa tu nyumbani kutanizidishia mawazo, yupo tayari kunipeleka kwenye saluni yake iliyokuwa hapo Mkuranga ili nikawe nafanya kazi.

    Kiuchumi mama yangu mdogo alikuwa vizuri kwani ukiachilia mbali kazi ya ualimu aliyokuwa akiifanya, yeye na mumewe aliyekuwa akifanya biashara kwa jumla, walikuwa na vitega uchumi vingi yakiwemo maduka ya jumla, saluni ya kike na ya kiume pamoja na mashamba. Kimsingi walikuwa wakiishi maisha mazuri.

    Nilikubali kwenda kufanya kazi lakini nikamuomba kwanza nikae nyumbani ili akili yangu itulie na nipate muda wa kuwa jirani na mwanangu.

    Ili kukwepa usumbufu kutoka kwa watu wa Dar es Salaam, siku hiyohiyo nilienda kununua laini mpya ya simu, nikatoa ile ya siku zote na kuweka hiyo mpya ambayo sikutaka mtu yeyote aifahamu zaidi ya mama yangu peke yake.

    Nikawa nimeyaanza maisha mapya nikiwa ugenini, mbali kabisa na mume wangu. Hata hivyo, japokuwa nilikuwa mbali, bado moyo wangu uliendelea kunisuta, kila nilipokuwa nikimkumbuka mume wangu na mahaba ya dhati aliyokuwa ananionesha, nilikuwa nashindwa kuyazuia machozi yasiulowanishe uso wangu.

    Hata kama alikuwa na udhaifu kipindi fulani, kamwe Ibra wangu hakustahili adhabu kali kama hiyo. Kila nilipokuwa nakumbuka siku ya mwisho alipokuja nyumbani kwetu na kuambiwa ukweli na baba yangu na jinsi alivyoangua kilio, nilikuwa nikijisikia uchungu mkali ndani ya moyo wangu.

    Nilipozidi kumfikiria mwanangu na maradhi yaliyokuwa yanamsumbua ambayo kwa mujibu wa daktari aliyarithi kutoka kwangu na Evans, nilikuwa nazidi kumuonea huruma.

    Kwa kifupi ni kwamba maisha yangu yalikuwa yamepoteza kabisa mwelekeo, sikuwa najua nini itakuwa hatima yangu na ya mwanangu. Baada ya siku kadhaa baadaye, nilimpigia simu na mama kutaka kujua kilichokuwa kinaendelea.

    “Mumeo amekuja na majibu ya DNA hapa nyumbani ambayo yanathibitisha kwamba ni kweli mtoto siyo wake,” mama aliniambia, mapigo ya moyo wangu yakanilipuka mno, nikiwa bado sijui nimwambia nini mama, alipigilia msumari wa mwisho.

    “Ameleta na talaka yako, amesema utakapopata nafasi atakukutanisha na mwanasheria wake ili mgawane mali mlizochuma pamoja,” mama alihitimisha. Nilishindwa kuendelea kumsikiliza, nilikata simu na kuanza kuangua kilio kama nimepokea taarifa za msiba.

    Ilikuwa ni habari mbaya sana kwangu, japokuwa nilikuwa nimemkosea sana mume wangu, niliamini anaweza kunisamehe na kunipa nafasi ya pili lakini kumbe nilikuwa najidanganya. Ibra alishaamua kuachana na mimi na hakukuwa na kitu chochote cha kumrudisha nyuma. Ama kwa hakika nililia sana siku hiyo, mama yangu mdogo alijitahidi kunibembeleza lakini haikusaidia chochote.

    Baadaye mwanangu mdogo ambaye hakuwa akielewa chochote, alipoona nalia sana na yeye alianza kulia, nyumba nzima ikakumbwa na simanzi ya hali ya juu. Nilipotulia, nilichukua ile laini yangu ya simu ya zamani, nikaiweka kwenye simu na kumpigia Ibra wangu, nilitaka japo nizungumze naye kwani niliamini baada ya kunisikia nilivyokuwa nalia, angeweza kunionea huruma.

    Nilipojaribu kuipiga namba hiyo, haikuwa ikipatikana hewani. Niliijaribu zaidi ya mara kumi lakini bado majibu yalikuwa yaleyale, haikuwa ikipatikana hewani. Hata nilipotuma meseji, hazikuwa zikienda kuonesha kwamba tayari namba hiyo ilikuwa imefungwa.

    Waliosema sikitiko la mahaba lashinda msiba hawakukosea. Kwa wiki nzima iliyofuata, hali ilikuwa ileile, Ibra hakuwa akipatikana kabisa hewani, nikawa naendelea kuomboleza kila siku, chakula hakikupita kooni wala usingizi haukupatikana.

    Macho yangu yalibadilika rangi na kuwa mekundu mno, ama kweli yalikuwa yamenikuta. Hali hiyo ilisababisha nianze kuumwaumwa hovyo, mara kichwa, mara mapigo ya moyo yawe yananienda mbio mfululizo, mara tumbo la kuhara, yaani ilikuwa taabu tupu. Kama hiyo haitoshi, nilianza pia kuwa natapika mara kwa mara, hasa asubuhi.

    Ilibidi mama mdogo anichukue na kunipeleka hospitalini kwani hali ilishakuwa mbaya. Nikaenda kuchukuliwa vipimo vyote kuangalia ni nini kilichokuwa kinanisumbua. Akilini nilikuwa najua kwamba siwezi kuwana ugonjwa wowote bali mshtuko wa kuachwa na Ibra na yote yaliyotokea ndiyo uliosababisha niwe kwenye hali hiyo.

    Hata hivyo, mawazo yangu hayakuwa sahihi kwani baada ya kuchukuliwa vipimo vyote, mambo mawili makubwa yalibainika. Daktari akatuita mimi na mama yangu mdogo kwenye chumba chake na kuanza kutusomea majibu.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Jambo la kwanza ambalo daktari aliniambia, ni kwamba nilikuwa na tatizo la shinikizo la damu (presha). Akaniambia kwamba mapigo yangu ya moyo yalikuwa yamehama kabisa kutoka kwenye hali ya kawaida ambapo alituambia kuwa kitaalamu ni 120/80 mmHg.

    Akaniambia kwamba mapigo yangu yalikuwa yamefikia 149/94 mmHg, hali ambayo kama sitapatiwa matibabu ya haraka na ya dharura, moyo wangu ungeweza hata kusimama ghafla na kusababisha nipoteze maisha.

    Yote tisa, kumi aliniambia kwamba vipimo vya haja ndogo vilionesha kwamba pia nilikuwa na ujauzito mwingine.



    “Niniii?” nilisema kwa mshtuko mkubwa huku nikisimama kwenye kiti nilichokuwa nimekaa, nikiwa ni kama siamini nilichokuwa nimekisikia kutoka kwa daktari. Nilihisi ni jambo ambalo haliwezekani, yaani niwe nimenasa tena ujauzito?

    “Haiwezekani,” nilisema huku nikizungukazunguka ndani ya chumba cha daktari. Akili yangu ilichanganyikiwa kabisa kwa sababu bado mwanangu alikuwa mdogo, hivyo suala la kupata ujauzito niliona kama ni kitu kisichowezekana.

    Daktari alinikalisha chini na kuanza kunihoji kwa undani. Kiukweli ndani ya kipindi hicho, sikuwa nimekutana kimwili na mwanaume yeyote zaidi ya mume wangu ambaye naye nilifanya naye mapenzi kabla matatizo hayajatokea na kusababisha tutengane.

    Daktari akanifafanulia kwamba kwa kawaida, kipindi ambacho mwanamke ametoka kujifungua au kipindi ambacho ananyonyesha, huwa ni rahisi sana kunasa ujauzito mwingine na ndiyo maana akina mama wanaonyonyesha huwa wanashauriwa kutumia njia za uzazi wa mpango.

    Akazidi kunieleza kwamba kwa kuwa tayari nilishakuwa nimepata ujauzito, ilitakiwa nichague jambo moja, kutoa ujauzito huo ili niendelee kumlea mwanangu au nimkatishe kunyonya mwanangu kwa sababu kama angeendelea kunyonya, angepata madhara ya kiafya.

    “Naomba nikafikirie kwanza,” nilimwambia daktari huku nikiinuka kutoka kwenye kiti nilichokuwa nimekaa, nikatoka ofisini kwake na kuelekea kule nilikomuacha mama mdogo na mwanangu, kichwa changu kikiwa kimevurugika kabisa.

    “Vipi mwenzetu?” mama mdogo aliniuliza lakini sikumjibu chochote, nikakaa pembeni na kujiinamia. Ni kweli ujauzito niliokuwa nao ulikuwa ni wa mume wangu na nilikuwa na uhakika wa asilimia mia moja kwamba ni wake lakini ningeanzaje kumueleza?

    Hata kama ningemueleza, nani angeniamini nilichokisema? Tayari historia ilikuwa ikinihukumu na kuonekana msaliti, malaya, mwanamke nisiyejiheshimu na sifa mbaya kibao, kiasi kwamba isingekuwa rahisi mtu yeyote kuniamini.

    Nilifikiria sana suala la kutoa ujauzito lakini kila nilipokumbuka kilichonitokea mara ya kwanza nilipojaribu kutoa ujauzito wa Evans, nilijikuta nikilifuta wazo hilo kichwani.

    Sababu nyingine iliyofanya nisifikirie kutoa ujauzito, ni kwamba nilikuwa nampenda sana Ibra wangu japokuwa mwenyewe alishaamua kuniacha kutokana na ukatili niliomfanyia. Niliona kwamba jambo pekee litakalonifanya niendelee kumkumbuka maishani mwangu mpaka siku nafunika uso wangu, ilikuwa ni kumzalia mtoto.

    Sababu nyingine iliyofanya nisifikirie kutoa ujauzito huo, ni kwamba nilikuwa nampenda sana Ibra wangu japokuwa mwenyewe alishaamua kuniacha kutokana na ukatili niliomfanyia. Niliona kwamba jambo pekee litakalonifanya niendelee kumkumbuka maishani mwangu mpaka siku nafunika uso wangu, ilikuwa ni kumzalia mtoto.

    Niliendelea kujiinamia pale nilipokuwa nimekaa huku nikijisikia maumivu makali sana ndani ya moyo wangu. Waliosema kwamba mwanamke mjinga huvunja ndoa yake kwa mikono yake mwenyewe, hawakukosea, ujinga wangu ndiyo uliokuwa umenifikisha mahali hapo.

    “Mwenzetu vipi mbona hunipi majibu uliyopewa na daktari?” mama mdogo aliniuliza swali ambalo lilinizindua kutoka kwenye dimbwi la mawazo machungu. Nikainua uso wangu na kumtazama.

    Mama mdogo alishtuka mno aliponitazama usoni hasa baada ya kugundua kuwa kumbe muda wote huo niliokuwa nimejiinamia nilikuwa nalia. Alishindwa kuendelea kunihoji, akanyamaza kimya, na mimi nikaendelea kujiinamia.

    Nilifikiria mambo mengi sana, mwisho nikaamua kupiga moyo konde na kuamua kwamba liwalo na liwe, sitautoa ujauzito huo. Nikainua uso wangu na kutoa kitambaa kwenye mkoba wangu, nikajifuta machozi na kamasi zilizokuwa zinanitoka kwa wingi.

    Kwa kuwa sasa angalau nilikuwa na ahueni, niliamua kumueleza ukweli mama mdogo juu ya majibu niliyopewa na daktari.

    “Una mimba? Mungu wangu,” alisema huku na yeye akionesha kupatwa na mshtuko mkubwa sana ndani ya moyo wake, akabaki ananitazama huku akiwa ameishiwa maneno.

    “Kwa hiyo utafanyaje?” aliniuliza huku akianza kumbembeleza mwanangu ambaye alianza kulia. Japokuwa tayari nilikuwa nimefikia muafaka kwamba siwezi kukubali kuutoa ujauzito huo, nilimdanganya mama mdogo kwamba sikuwa nimeamua nini cha kufanya.

    Niliinuka na kuelekea ofisini kwa daktari huku nikimuacha mama akiendelea kumbembeleza mwanangu, nikaingia kwenye ofisi ya daktari na kumueleza kwamba nilikuwa nimeamua kumwachisha mwanangu ziwa ili nilee ujauzito huo.

    Yule daktari naye alionesha kunishangaa kwani alitegemea nitamwambia naomba kuutoa ujauzito huo ili niendelee kumlea mwanangu kwani kiumri bado alikuwa mdogo, ukichanganya na maradhi yaliyokuwa yanamsumbua, alikuwa akihitaji sana uangalizi wa karibu.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Una uhakika na uamuzi uliouchukua?” aliniuliza yule daktari huku akishusha miwani yake na kunitazama vizuri usoni. Nilimwambia kwamba nina uhakika, akashusha pumzi ndefu na kuanza kunipa mbinu za kitaalamu za namna ya kumuachisha mwanangu ziwa bila kumsababishia matatizo yoyote ya kiafya na vyakula ambavyo alitakiwa kupewa kila siku.

    Baada ya somo hilo lililochukua dakika kadhaa, nilimshukuru daktari na kutoka, nikamuacha anaendelea kunitazama huku akionesha kunionea huruma kwa hali niliyokuwa nayo. Japokuwa sikuwa nimemwambia ukweli wa maisha yangu, muda mfupi tu niliozungumza naye, alishagundua kwamba nina matatizo makubwa sana.

    Nilitoka mpaka pale nilipokuwa nimemuacha mama mdogo, nikamsaidia kumbeba mwanangu kisha tukaondoka hospitalini hapo kurejea nyumbani. Njiani nilimuomba mama mdogo asimwambie mtu yeyote kuhusu ujauzito wangu, akaniahidi kuwa itakuwa siri yetu.

    Kama ilivyokuwa kwa daktari, naye alionesha kunionea sana huruma kwa yaliyokuwa yananitokea kwani kiumri bado nilikuwa mdogo kukabiliana na mambo makubwa na mazito kiasi hicho.

    Akaniambia nisichukue uamuzi wowote wa haraka bali nikae na kutulia kisha chochote nitakachoamua, yeye atakuwa upande wangu. Akawa anaendelea kunibembeleza na kuniambia kwamba matatizo ni sehemu ya maisha ya binadamu hivyo sitakiwi kukata tamaa bali kukubaliana na hali halisi iliyokuwepo kisha kutafuta njia nzuri ya kujikomboa.

    Tulipofika nyumbani, mimi nilienda kujifungia chumbani kwangu, nikamuacha mwanangu kwenye mikono ya mama yangu mdogo ambaye kwa wakati huo ndiye aliyekuwa na jukumu la kumlea. Nikiwa chumbani, niliendelea kulia kwa uchungu kutokana na jinsi maisha yangu yalivyoharibika ghafla na kunifanya nipoteze kabisa mwelekeo.

    Nilijaribu tena kumpigia simu mume wangu lakini bado majibu yalikuwa yaleyale, hakuwa akipatikana hewani.

    “Nitaulea huu ujauzito peke yangu,” nilisema huku nikifuta machozi. Siku hiyohiyo nilianza maandalizi ya kumwachisha mwanangu ziwa kwani kwa mujibu wa daktari, ilikuwa hatari kuendelea kumnyonyesha mtoto wakati nikiwa na ujauzito mwingine. Namshukuru sana mama yangu mdogo kwani alinisaidia sana, siku tatu baadaye nikawa nimefanikiwa kumkatisha ziwa mwanangu.



    Japokuwa nilikuwa namuonea sana huruma kwa jinsi alivyokuwa anahangaika kukosa ziwa la mama, sikuwa na namna. Nikiri wazi kwamba japokuwa ni dhambi kwa mama kumchukia mtoto aliyemzaa kutoka kwenye tumbo lake, mimi nilitokea kumchukia sana mwanangu.

    Japokuwa muda mwingine nilikuwa najikosoa mwenyewe kwamba mtoto hakuwa na hatia yoyote, lakini ukweli ulibaki palepale kwamba nilimchukia sana mtoto huyo pamoja na baba yake, Evans kwani niliamini bila uwepo wake, ningekuwa naishi kwa mume wangu, nikifaidi mapenzi ya dhati aliyokuwa ananionesha tangu aliponioa.

    Kuna wakati nilikuwa natamani hata Mungu ayakatishe maisha yake lakini niligundua kuwa hilo halikuwa suluhisho. Japokuwa nilikuwa naendelea kuwasiliana na mama, kamwe sikumwambia kwamba nimepata ujauzito na kwamba nimeshamuachisha mwanangu ziwa.

    Mwezi mmoja baadaye, tayari tumbo lilishaanza kuchomoza kuonesha kwamba nilikuwa mjamzito. Asubuhi moja, nikiwa bado nimelala, niliamshwa na mama mdogo akinipa taarifa kwamba mama alikuwa amekuja kuniona.

    “Mama amekuja?” nilihoji huku nikiwa na wasiwasi mkubwa ndani ya moyo wangu. Sikutaka ajue kwamba nimebeba ujauzito mwingine.

    Niliamka nikiwa na wasiwasi mkubwa, nikasimama pembeni ya kioo na kujitazama, nikaona tumbo langu limeshaanza kuchomoza kiasi kwamba mama akinitazama tu, lazima atagundua kwamba sikuwa sawa.

    Kwa wanawake wenzangu watakuwa wanajua kwamba ukishajifungua mara ya kwanza halafu ukapata mimba nyingine katika kipindi kifupi, tumbo huwa kubwa haraka kuliko unavyotegemea.

    Nilichukua khanga na kujifunga tumboni ili kubana tumbo, nikavaa gauni kubwa kisha nikatoka na kwenda mpaka sebuleni nilikomkuta mama amekaa kwenye sofa akiendelea kuzungumza na mama mdogo huku akiwa amembeba mwanangu.

    “Mbona mtoto amebadilika hivi? Halafu kwa nini analialia sana?” mama alinidaka juujuu na kuniuliza swali hilo kabla hata hatujasalimiana, ilibidi mama mdogo amtulize kwanza na kumwambia atamuelekeza mwenyewe vizuri. Nilishusha pumzi na kukaa pembeni ya mama, machozi yakinilengalenga.

    Nikamuona mama mdogo akinitazama kwa macho yaliyobeba ujumbe, akitaka kujua kama nilikuwa tayari mama aambiwe ukweli juu ya ujauzito wangu, nami nikatingisha kichwa kidogo kuashiria kwamba sikuwa na jinsi zaidi ya kumueleza mama ukweli.

    Mama mdogo alishusha pumzi na kumgeukia mama, akamsema kwanza kwamba kitendo alichokifanya cha kunidaka juujuu na kuanza kunifokea hakikuwa kizuri, hasa ukizingatia kwamba hatukuwa tumeonana kwa kipindi kirefu na kilichoniondoa mpaka nikawa hapo ilikuwa ni matatizo makubwa ya ndoa yangu.

    Mama alikiri kosa lake lakini akasema ameshtushwa na hali aliyonayo mtoto, hasa ukizingatia kwamba ana matatizo makubwa ya kiafya ambayo mimi mwenyewe nilikuwa nayajua.

    Baada ya kuwekana sawa, mama mdogo alianza kumueleza mama kuanzia siku ya kwanza nilipofika na maisha niliyokuwa naishi, akamzungusha wee mwisho akagonga kwenye pointi ya msingi.

    “Whaaat?” (niniii) mama aliniuliza swali kwa Kiingereza, tangu nipate akili sikuwahi kumsikia akiniuliza kwa lugha ya kigeni zaidi ya siku hiyo, kweli alichanganyikiwa sana. Maskini mama yangu! Alisimama na kutaka kumdondosha mwanangu kwa mshtuko, mama mdogo akamuwahi na kumpokea mtoto, akamtaka akae chini na kutulia kwa sababu huo haukuwa muda wa kulaumiana au wa kupaniki.

    Mama alikaa huku mikono yake ikiwa bado kichwani, akashusha pumzi ndefu na kunigeukia, akiwa ni kama haamini alichokuwa anakisikia.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Yaani umekuja huku badala ya kutulia umeendeleza umalaya wako?” kwa mara nyingine mama alizungumza kitu ambacho sikuwahi kukisikia kikitoka kwenye kinywa chake hata mara moja, kuniita malaya!

    Sikuweza kumjibu chochote, nikajiinamia chini na kuanza kulia kwa kwikwi, mama mdogo akawa na kazi ya ziada ya kumuelekeza kwamba tangu nifike Mkuranga, sikuwa na mwanaume yeyote na kwamba ile mimba ilikuwa ni ya mume wangu. Mama akaonekana kukataa katakata, vilevile nilivyokuwa nimetegemea kuanzia mwanzo kwamba hakuna anayeweza kuniamini.

    Historia ilikuwa ikinihukumu, hakuna mtu ambaye angeamini kwa urahisi kwamba ujauzito huo ulikuwa ni wa mume wangu kutokana na mazingira yenyewe na jinsi historia yangu ilivyokuwa.

    Licha ya mama mdogo kuendelea kumuelewesha, bado aliendelea kukataa, ikabidi mama mdogo aende kumtolea vyeti vyangu vya daktari ambayo vilikuwa vikionesha umri wa ujauzito wangu.





    MWISHO



0 comments:

Post a Comment

Blog