IMEANDIKWA NA : ALLY MBETU
*********************************************************************************
Sehemu Ya Kwanza (1)
SI KILA CHOZI LIDONDOKALO, hudondoka kwa huruma au maumivu, mengine nyuma yake yamebeba siri nzito. Siku zote siraha ya mnafiki huwa machozi, unaweza kuona anakuonea huruma kumbe kikulacho kinguoni mwako, anakutafuna taratibu ukishtuka amekumaliza. Deusi aliamini wote waliomlilia siku ya hukumu yake hasa mkewe na rafiki yake kipenzi walikuwa na uchungu wa kweli, lakini kumbe ilikuwa siri nyuma ya machozi. Ukitaka kujua yote naomba twende pamoja katika hadithi hii tamu. TWENDE SASA….
Gari aina ya Toyota Land cruser GX lilionekana likitembea taratibu mbele ya lango kuu la gereza la Segerea. Askari magereza wa zamu alilifuatilia lile gari huku moyoni akiamini kazi anayofanya na mshahara anaopata kununua gari lile ingebaki ndoto ya mchana.
Aliliona gari lile likisimama na kutulia kwa muda bila kufunguliwa mlango, kutokana na uzuri wake aliendelea kulitazama kwa matanio huku akijisemea moyoni’ Wenye fedha wanafaidi.” Baada ya dakika kumi mlango wa gari ulifunguliwa na kuteremka mwanamke mmoja aliyeonekana mjamzito, maisha yake mazuri, akiwa na kitoto kidogo cha kike cha miaka mitatu. Baada ya kutoka nje ya gari, yule mama alichuchumaa kuzungumza na kile kitoto. Baada ya muda yule mwanamke aliingia kwenye gari na kuondoka akimuacha mtoto amesimama peke yake. Alikuwa na boksi la biskuti ameshikilia sambamba na bahasha iliyofungwa kwa uzi mkononi. Kitendo kile kiliacha maswali mengi kwa askari , mbona kitoto kidogo kimeachwa pale. Wazo la haraka lilimjia huenda amekwenda sehemu mara moja atarudi kumchukua mwanaye. Lakini muda uliendelea kukatika bila kuonekana, na kitoto kile kiliendelea kusimama palepale kilipoachwa bila kujitikisa. Wakati huo wingu zito lilitanda na mvua ilianza kunyesha kitoto kile kikiwa pale pale huku kikiangua kilio cha kutaka msaada. Askari magereza alitoka kwenye lindo lake na kukifuata ili kukiondoa kwenye mvua. Alikibeba mpaka kwenye kibanda chake na kukiketisha kwenye benchi, ilibidi aingie kazi ya ziada kukimbembeleza kutokana na kumlilia mama yake. Jicho la askari lilitua kwenye bahasha aliyofungiwa mkononi yenye maandishi makubwa, MKUU WA GEREZA. Alishtuka na kujawa na mawazo mengi juu ya barua ile, alijiuliza kwa nini haikupelekwa moja kwa moja kwa mhusika au kulikuwa na ajenda gani kuachiwa mtoto mdogo barua ya mkuu wa gereza. Wasiwasi wake mkubwa alifikiria labda yule ni mtoto wa pembeni wa mkuu wa gereza hivyo aliletwa pale ili kumsusia. Hakutaka kumpeleka moja kwa moja kwa mkuu wa gereza, kuhofia kuleta mtafaruku ndani ya ndoa yake. Alimuita askari mwenzake aliyekuwa akipita. “John hebu njoo.” “Okote umeamua kuingia lindo na mwanao?” “Kaka wee acha, kuna gari moja la kifahari limesimama mbele ya lango kuu na kumuacha mtoto huyu.” “Halafu waliomuacha walikueleza nini?” “ Lilisimama kule, nilijua labda wamemwacha watamrudia, lakini mpaka mvua inateremka sikuona gari wala mtu. Ilibidi nikamchukue na kumuhifadhi hapa, kilichonichanganya na kutaka msaada wako ni barua aliyokuwa amefungwa mkononi , imeandikwa mkuu wa gereza.” “Eti?” “Imeandikwa mkuu wa gereza,” Okote alirudia kusema. “Sasa mkuu wa gereza na mtoto huyu wanahusiana nini?” “Kuna kitu kimenitisha.” “Kipi hicho?” “Huenda mkuu alimpa mimba mwanamke, leo ameamua kumletea mtoto hapa.” “Mmh! Inawezekana, kwani si yupo ofisini kwake?” “Sijui, nilikuwa naomba msaada niangalizie kama yupo tumpeleke mtoto na barua” “Gari lake sijaliona kupita atakuwa yupo.” “Basi naomba unipelekee na kumpa maelezo haya.” Alikubali kumpeleka, alimbeba na kuelekea naye kwenye ofisi ya mkuu wa gereza, mlango ulikuwa umefungwa, mlinzi wake alimuuliza. “Vipi John mbona na mtoto ofisini?” “Nina shida na mkuu.” “Shida gani?” “Sefu, shida ya mkuu nikueleze wewe?” “Ok, ingia.” John aliingia hadi mapokezi, sekretari naye alishtuka kumuona John amembeba mtoto. “John, vipi mtoto anaumwa mbona hivyo?” “Hapana nina shida na mkuu.” “Sasa hivi amesema hataki kuonana na mtu ana kazi nyingi.” “Najua lakini kuna mzigo wake.” “Huyo mtoto?” “Ndiyo na barua,” alimkabidhi barua ambayo aliisoma na kukutana na jina la Mkuu wa gereza. “Umemtoa wapi?” “Kuna mwanamke kamtelekeza hapo nje na kuondoka.” “Mmh, isiwe nyumba ndogo?” Suzy alisema kwa sauti ya chini. “Hata mimi ndiyo wasiwasi wangu.” “Hebu ngoja nimpigie simu nimsikie anasemaje, unajua John hii kashfa.” “Tena inabidi tusijichanganye tutakimbia kazi.” Suzy alimpigia bosi wake simu. “Halo Afande kuna ugeni wako mzito.” “Nani?” “Kuna mtoto katelekezwa nje ya gereza mkononi ana barua yako.” “Barua yangu! Inasemaje?’
”Hatujaisoma afande ila kuna jina la mkuu wa gereza.” “Mmh! Hebu mlete ofisini haraka.” John alimbeba mtoto na kuingia naye ofisi kwa mkuu wake, baada ya kupiga saruti alimtua mtoto . Mkuu wa gereza alimuangalia yule mtoto lakini hakugundua kitu chochote katika uso wa mtoto. “Nipe hiyo barua,” John alimkabidhi na kusubiri maelekezo. Mkuu wa Gereza Mzee Sikamtu aliifungua ile barua na kuisoma kwa muda kisha alishusha pumzi na kusema: “John.” “Naam afande.” “Nenda gerezani kaniletee mfungwa Deusi Ndonga njoo naye mara moja,” alisema huku akiweka barua juu ya meza. Baada ya maelekezo John alipiga saruti na kugeuka kisha aliondoka kwa mwendo wa ukakamavu.
********
Ndani ya gereza Deusi Ndonga alikuwa amejiegemeza kwenye ukuta huku maumivu ya moyo wake yalikuwa makubwa zaidi ya yale ya kufungwa gerezani miaka saba. Lakini kitendo cha usaliti wa mkewe Mwaka mmoja toka aingie gerezani kwa kosa la kukamatwa na dawa za kulevya ambazo aliamini kabisa ule ulikuwa mtego alitegewa na bosi wake. Kila dakika aliiona kama njozi ya mchana isiyo na ukweli wa kumuona mkewe akiwa mjamzito, mimba ambayo haikuwa yake. Akiwa katikati ya mawazo jina lake liliitwa. Alinyanyuka na kusogea mlangoni. “Deus unaitwa na mkuu wa gereza.” Deusi alitoka chumba cha gereza na kufuatana askari aliyetumwa na mkuu wa gereza. Akiwa nyuma yake, alijawa na mawazo na kujiuliza mkuu wa gereza anamuitia nini. Na kwa nini amuite ofisini kwake. Alipofika nje ya ofisi John alimweleza Deusi asubiri na yeye kuingia ofisini kwa mkuu wa gereza. Baada ya muda alitoka na kumweleza aingie, alipoingia moyo wake ulishtuka kumuona mtoto pale ofisini. Lakini hakutaka kuhoji kitu kwa vile
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
aliitikia wito si kuuliza swali. “Deusi,” mkuu wa gereza alimuita baada ya kuketi kwenye kiti. “Naam mkuu.”
”Unamfahamu huyu?” alimuuliza huku akinyoosha mkono kwa mtoto mdogo aliyekuwa ameketi kwenye kochi. “Ndiyo mkuu.” “Unamfahamu vipi?” “Ni mwanangu,” Deusi alijibu kwa utulivu. “Shika barua hii usome,” aliipokea na kuanza kusoma taratibu. Alitembeza macho taratibu kusoma herufi moja baada ya nyingine, kila alichosoma kilikuwa sawa na kuupasua moyo wake kwa kisu butu bila ganzi. Mkuu wa gereza alimfuatilia Deusi alipokuwa akisoma barua huku akishuhudia michirizi ya machozi ikiteremka kwenye mashavu yake. Mishipa ya kichwa ilimsimama na macho kuzidi kuwa mekundu ikifuatiwa na kamasi nyepesi, baada ya kuimaliza kuisoma barua alimwangalia mwanaye aliyekuwa amekaa kwenye kochi akishangaa picha ya mkuu wa nchi iliyokuwa ofisini huku akiendelea kutafuna biskuti zake. Baada ya kumwangalia mwanaye aliyemuonea huruma huku moyo wake ukiongezeka maumivu mara dufu. Katika maisha yake kitendo cha yeye kufungwa gerezani hakikumuumiza moyo wake kwa kuamini ile ni mitihani ya maisha, mwanadamu anatakiwa kupambana nayo. Lakini pigo zito la kwanza lilikuwa kumuona mkewe akiwa na ujauzito usio wake, akiwa bado katika maumivu ya mkewe kukosa uaminifu mwaka mmoja baada ya kifungo chake. Pigo zito zaidi ya bomu la kilo 1000 lililousambalatisha moyo wake lilikuwa kwenye ile barua. Barua ilikuwa imeandikwa hivi: Dear zilipendwa, mume wangu wa zamani, najua kidonda cha kuona mwanaume mwenzako kunijaza tumbo bado hakijapona, lakini sina jinsi, siku zote punda unaweza kumlazimisha kumpeleka mtoni, lakini huwezi kumlazimisha kunywa maji. Hii ilikuwa sawa na tamaa ya wazazi wangu kunilazimisha niolewe na wewe, mwanaume asiye chaguo langu. Walijua kabisa chaguo la moyo wangu ni Kinape. Kuolewa nawe ilikuwa sawa na punda kumlazimisha kuingia mtoni lakini ilikuwa vigumu kuendelea kuwa na wewe kwa vile si chaguo langu. Baada ya kufungwa kwako ilikuwa ni nafasi yetu ya kujinafasi kufanya mapenzi kwa uhuru mkubwa. Kwa muda mrefu tulikuwa tukifanya kwa wizi, najua itakuuma sana na kuupasua moyo wako kwa kisu butu bila ganzi. Lakini ukweli unabaki palepale nilikuwa sikupendi na sitakupenda milele. Kama Kinape angekuja mapema hata huu uchafu wako usingeingia tumboni mwangu, nilipanga kukinyongea mbali. Lakini moyo wa huruma ulinijia wa kuidhuru damu yangu ilinishika. Nimeamua kukuletea mtoto wako ili ukae naye gerezani. Siwezi kumtunza mtoto wa mwanaume nisiye mpenda, siwezi kuchanganya mtoto wa njiwa na bundi. Mimi kuolewa na Kinape sawa na mshare umerudi porini haukupotea, sasa hivi mimi ni mke mtarajiwawa Kinape. Nakutakia maisha marefu yenye furaha na mwanao gerezani. Ni mimi dear zilipendwa Kilole. Mkuu wa gereza alimshuhudia Deusi akiwa naye kimwili lakini kiakili alikuwa mbali sana, alimuita. “Deusi...Deusi.” “Haiwezekani... haiwezekani, kwa nini lakini, kwa nini mke wangu unanitendea unyama kama huu. Nimekukosea nini? Kwa nini unamtesa mtoto asiye na hatia, kwa nini unanisaliti na rafiki yangu. Eee Mungu kosa langu nini, haya huyu mtoto mdogo nitamweka wapi, anajua nimefungwa anakuja kuniterekezea mtoto. ” Deusi alishindwa kujizuia aliangua kilio cha sauti ya chini. “Deusi pole,” Afande John alimtuliza. “John,” Mkuu wa gereza alimuita. “Naam afande.” “Nipe nafasi nizungumze machache na Deusi.” Baada ya John kutoka, alitulia kwa muda akimwangalia Deusi aliyekuwa akitoa kamasi kwa mkono na kufuta kwenye shati lake. Alinyanyuka na kwenda kwenye friji ndogo ya ofisini na kutoa chupa kubwa ya maji yaliyokuwa nusu na kummiminia kwenye glasi kisha alimpa Deusi. “Pole sana Deusi, naomba unywe maji haya kwanza.” Deusi aliipokea glasi na kuyanywa maji yote kwa mkupuo kisha aliiweka glasi juu ya meza. “Deusi.” “Naam mkuu.” “Kwanza pole sana.” “Sijapoa mkuu.” “Kuna siri gani kati yako na mkeo?”
“Kwa kweli sijui hata kitu kimoja, ni mwezi wa pili sasa, mke wangu ameujeruhi moyo wangu kwa kukosa uaminifu wa kubeba ujauzito usio kuwa wangu.”
“Mkeo ulimuoa kwa mapenzi yake au kwa kulazimishwa?” “Kwa kweli mke wangu nilichaguliwa na wazazi wangu nilipokwenda kijijini kuwatembelea. Mwanzo wa ndoa yetu alionesha mapenzi ya dhati kumbe nilikuwa nafuga nyoka, amekua sasa amenimeza. ” “Na Kinape ni nani?”
“Kinape alikuwa zaidi ya rafiki, tumesoma na kucheza pamoja kabla ya mimi kuendelea na masomo mpaka kupata kazi katika kitengo cha kuzuia dawa za kulevya.” “Na alifikaje kwako?”
“Ni historia ndefu”
******
Miaka minane iliyopita Deusi King’ole baada ya kuanza kazi kama mkuu wa kitengo cha kuzuia madawa ya kulevya. Miaka mitatu katika kazi yake alipata likizo iliyomfanya aende kijijini kwa wazazi wake. Katika watu wa karibu baada ya wazazi wake, walikuwa wazazi wa Kinape ambaye toka wakiwa shule ya msingi waliitwa pacha kutokana na ukaribu wao. Deus baada ya kufika kijijini na kupokewa na ndugu na jamaa ambao walimshangaa kumuona amerudi katika gari la kifahari, wengi walizoea kuliona gari kama lile kwa mbunge wao tu, alipokwenda kujijini kuwatembelea wapiga kura wake. Ilikuwa ni furaha hasa kwa wazazi wake ambao waliamini kazi ya kumsomesha mtoto wao ilikuwa imezaa matunda. Kitu kikubwa alichowaahidi wazazi wake kuhakikisha anayabadili maisha ya familia yake ikiwa pamoja na kuwajengea nyumba ya kisasa na kuwachimbia kisima cha maji. Baada ya kutulia alitaka kujua habari za rafiki yake Kinape.
“Jamani Kinape yupo?”
“Mmh! Nina siku sijamtia machoni,” mama Deusi alijibu.
“Nasikia sijui alikwenda mjini kutafuta kazi,” mdogo wake alisema.
“Sasa wewe mjini huko hukumuona?” Mzee King’ole aliuliza. “Baba mji ni mkubwa, mnaweza kukaa miaka kumi bila kuonana na mtu pengine mnakaa kitongoji kimoja.”
“Labda siku hizi, siku za nyuma watu tulikuwa tunajuana hata wageni walipoingia tuliwatambua.”
“Ni wakati huo baba, sasa hivi mji umepanuka.”
“Basi atakuwa hukohuko mjini.”
“Na yeye atarudi na gari?” Mdogo wake aliuliza.
“Siwezi kujua,” Deus alijibu kwa mkato.
“Lakini mzee Solomoni na mkewe si wapo?” Deus aliuliza.
“Wapo, waende wapi,” mzee King’ole alijibu.
“Basi ngoja nikawaone kabla ya kujipumzisha.”
“Haya baba,” mama Deus alijibu. Deus alinyanyuka ili aelekee kwa mzee Solomoni. “Kaka twende wote,” mdogo wake wa kike aliyekuwa anasoma kidato cha kwanza aliomba kuongozana na kaka yake.
“Hakuna tatizo,” alijibu huku akimshika mkono. Walikwenda hadi kwa mzee Solomoni, alimkuta mama Kinape akisuka ukiri. “Hodi hapa.”
“Karibu,” alijibu huku akiacha kusuka na kumtazama mgeni aliyekuwa amesimama mbele yake. “Shikamoo mama.” “Marahaba, karibu.”
“Asante.”
“Ndiyo baba,” ilionesha mama Kinape kamsahau Deus. “Mama unamjua huyu?” Salome mdogo wa Deus alimuuliza mama Kinape.
“Hata,” alijibu huku akijitahidi kumkazia macho.
“Si kaka Deusi huyu.”
“Deusi wa mjini?”
“Ndiyo.”
“Jamani, mwanangu mwenyewe nimemsahau, karibu baba tusameheane, macho ya uzee haya.”
“Kawaida, mama za hapa?”
“Hebu ngoja kwanza, Salome kamletee kiti kaka yako.” Salome alikwenda ndani na kurudi na kiti cha kukunja, alikiweka pembeni ya mama Kinape.
“Wee, Salome kiweke mbele nimuone vizuri,” Salome alifanya kama alivyo agizwa. Baada ya kukaa alianza kuzungumza: “Ndiyo, mama za siku?”
“Mmh! Hivyo hivyo tu baba, kila kukicha afadhari ya jana.”
“Ni kweli sasa hivi nasikia hata mvua zimegoma.”
“Kama unavyoona.”
“Baba yupo wapi?”
“Ametoka kidogo, ila achelewi, unavyomtaja pengine yupo njiani anarudi.”
“Na ndugu yangu?”
“Kinape?”
“Eeeh.”
“Mmh! Kakimbilia mjini.”
“Kufanya nini?”
“Mwanangu kwani wewe mjini unafanya nini?”
“Mimi nafanya kazi serikalini kutokana na elimu yangu.”
“Kwa kweli hatujui mjini anafanya kazi gani.”
“Anakaa wapi ili nikifika nimtafute?”
“Hatujajua ila yeye kasema atalala popote hata sokoni.”
“Mmh! Haya.”
“Vipi umeoa?”
“Bado.”
“Unasubiri nini?”
“Nilikuwa najipanga.”
“Deus wazazi wenu lini tutacheza na wajukuu?”
“Nina imani sasa hivi nitafuta machozi yenu.”
“Fanya hivyo, usiwe kama mwenzako kila siku kesi za watoto wa watu.”
“Sasa mama, wacha nikapumzike ndiyo nimefika nahitaji kupumzika.” “Hakuna tatizo, tuachie basi hata fedha ya unga.” Deus aliingiza mkono mfukoni na kutoa noti moja ya shilingi elfu kumi na kumkabidhi. Kabla hajaipokea alitokea mzee Solomoni na kusema: “Mheshimiwa nami usinisahau.”
“Aah, baba.” Deus alisema huku akimgeukia mzee Solomoni, Mzee Solomoni alishtuka kumuona Deus.
“Ha! Ni wewe Deus?”
“Ni mimi baba.”
“Umefika lini?”
“Leo.”
“Na lile gari la mbunge lililopaki kwenu?”
“Si gari la mbunge ni gari langu mwenyewe.”
“Ha! Ina maama na wewe siku hizi mbunge?”
“Hapana kuwa na gari kama lile halimaanishi mbunge, mtu yoyote anaweza kumiliki.”
“Kwa hiyo ni la kwako?”
“Ndiyo baba.”
“Hata hali yako inajionesha.”
“Kidogo kidogo.”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Una habari gani?” Mzee Solomoni alisema huku akimtazama kwa makini Deus. “Nilikuja kuwajulia hali mara moja, ila nimesikitika kumkosa rafiki yangu kipenzi Kinape.”
“Yule rafiki yako mpumbavu, tena hana akili, amekimbia kilimo, ona jinsi tulivyochoka wazazi wake yeye anakimbilia mjini. Kibaya anapokwenda hana ndugu wala sehemu ya kufikia,” mzee Solomoni alisema kwa hasira.
“Lakini baba si kulalamika, ni kumuombea ili milango ya riziki ifunguke na kupata shughuli yoyote ya kumpatia kipato.”
“Kweli kabisa usemayo, kila siku baba yenu analalamika hajui kama ni laana kwa mtoto,” mama Kinape aliunga mkono.
“Wazazi wangu nakuahidini kitu kimoja, kwa vile mmesema yupo mjini nitamtafuta kila kona ili kuhakikisha nampata.”
“Litakuwa jambo la zuri.” Deus aliagana na wazazi wa Kinape ili arudi nyumbani, mzee Solomoni alikumbusha.
“Mwanangu na mimi mbona umenisahau?” Deus aliingiza mkono mfukoni na kutoa noti nyingine ya elfu kumi na kumkabidhi. “Asante sana mwanangu Mungu akizidishie.”
“Asante wazazi wangu, atuzidishie wote.” Deusi aliwaaga na kurudi nyumbani, njiani wakati wa kurudi walikutana na binti mmoja aliyekuwa amebeba chupa ya mafuta ya kula. “Shikamoo,” yule binti alimsabahi Deus.
“Marahaba.”
“Salome, mambo?”
“Poa, umemuona kaka yangu anayeishi mjini?”
“Kumbe ndiye huyu, shikamoo.”
“Jamani Kilole, mbona unataka kumchosha kaka yangu, shikamoo mara ngapi?”
“Jamani ya kwanza ya kutomjua, ya pili ya kumfahamu, kuna ubaya?”
“Hakuna ubaya, marahaba,” Deus aliitikia huku akitabasamu. “Karibu kwetu kaka.”
“Asante.”
“Haya nawahi nyumbani, Salome baadaye.”
“Haya.” Waliagana na Kilole kila mmoja aliendelea na safari yake, wakiwa wanarudi nyumbani Deus alijikuta akivutiwa na mchangamfu wa Kilole.
“Salome, Kilome mtoto wa nani?”
“Wa mzee Sikwera.”
“Mmh! Mbona huyu msichana simfahamu?”
“Kwani ulikuwa unapenda kutembea kijijini, mbona alikuwepo.” “Kumbe, rafiki yako?”
“Kiasi, vipi umemependa?”
“Basi tu kanivutia kwa uchangafu wake.”
“Hata mimi nampenda.”
“Ameolewa?”
“Mtu yupo kwao, atakuwa ameolewa vipi?”
“Kwa hiyo hajaolewa?”
“Hajaolewa.”
“Kama hajaolewa atakuwa na rafiki wa kiume?”
“Kaka swali hilo gumu.” Salome alificha siri ya Kilole kutokana na siku za nyuma kuwa na urafiki wa kimapenzi na Kinape rafiki kipenzi cha kaka yake. Kwa vile Kinape alikuwa na miezi sita toka aende mjini. Hakukuwa na haja ya kumzibia riziki kama kweli kaka yake anampenda.
“Basi tuachane na hayo,” Deus alibadili mada. “Vipi umempenda, kama umempenda nitafurahi siku moja akiwa wifi yangu.” “Ni haraka sana, kila kitu kizuri kinataka subira.” Kutokana na mazungumzo kupamba moto walijikuta wakifika kwao bila kujua, Deus hakutaka tena mazungumzo aliingia chumbani kwake na kujilaza. Kabla ya kulala mawazo yote yalikuwa kwa Kilole. Aliamini kabisa kama hana mtu basi nafasi ile aitumie vyema mpaka anarudi mjini awe amepata jibu la uhakika. wake kuhamishwa na wazazi wake kwa ajili ya tofauti ya dini. Deus alikuwa na Alikumbuka moyoni mwake kuna chumba hakina mpangaji baada ya mpangaji mpenzi wake anayefanya kazi katika shirika la vifaa vya Electonic kama Series Officer. Uhusiano wao ulianza taratibu, mpaka ulipofikia hatua ya kutambulishwa Deus kwa wazazi wa mpenzi wake Halima. Tatizo lilikuwa dini Halima muislamu na Deus mkiristo, wazazi wa Halima hawakuwa na pingamizi kama Deus atabadili dini kumfuata Halima.
Deus hakuwa tayari wazazi wake walisema kama ni hivyo hakuna ndoa. Deus alibembeleza wafunge ndoa ya serikali, pia hiyo waliikataa. Hakuwa na jinsi zaidi ya kukubali kubwaga manyanga kutokana na kushindwa masharti. Miezi sita ilikatika huku ukaribu wake na Halima ukipungua na mwisho kabisa ulivunjika. Wazo la kutafuta mpenzi mwingine aliliweka kando na kujikita katika kuyatengeneza maisha yake na ya wazazi wake kijijini. Baada ya kukaa kwa muda alijikuta turufu yake ya upendo anaitupa kwa Kilole, baada ya kuwaza sana usingizi ulimpitia. ********** Alishtuka jioni, baada ya kuoga na kupata chakula alikaa na mama yake, katika mazungumzo alimgusia mama yake msichana aliyekutana naye wakati akitoka kwa mzee Solomoni. “Mama wakati narudi toka kwa mzee Solomoni, nimekutana na msichana mtoto wa m.. mmm..ze..ee.ee, eti Salome yule msichana tuliyekutana naye ni mtoto wa mzee nani?” Alimuuliza mdogo wake aliyekuwa amekaa mbali kidogo. “Mmh! Kaka bado unaye, kweli kakugusa.” “Salome hebu tuambie mtoto wa nani?” Mama yao alikuja juu. “Mama si Kilole?” “Kilole huyu mtoto wa mzee Sikwera?” “Ndiye huyo huyo.” “Eeh, amefanya nini?” Mama Deus alishusha sauti na kuzungumza kwa sauti ya chini na mwanaye. “Unamuonaje?” “Kivipi?” “Hata sijui, nimempenda alivyo pia ni mchangafu akiwa ndani nyumba haizubai.” “Kwa hiyo unataka awe mkeo?” “Mama mbona kila kitu kinajieleza.” “Kwa kweli ni mmoja wa wasichana wenye heshima hapa kijijini, mengine siwezi kujua lakini ametulia.” “Mmh! Sawa.” “Vipi? Tufanye mpango?” “Kwa sasa ni maandalizi kama atakuwa tayari, basi tujipange kwa harusi baada ya miezi mitatu tufunge ndoa, vipi kuhusu elimu?” “Mi sijui labda umuulize Salome.” “Eti Salome, shoga amesoma mpaka darasa la ngapi?” “Kidato cha nne.” “Kinatosha ataendelezwa kwa vile elimu haina mwisho.” “Basi kazi hii nitaifanya na baba yako leo usiku tutakwenda kwa wazazi wa Kilole.” ******** Usiku ulipoingia wazazi wa Deus walikwenda kwa wazazi wa Kilole kupeleka ujumbe wa Deus. Walipokelewa vizuri, bila kupoteza muda waliwaeleza kilichowapeleka. “Utani huo mzee mwenzangu, Deus aache wanawake wote mjini aje atafute kijijini?” Baba Kilole alisema baada ya kusikia ombi la mzee mwenzake. “Najua utasema hivyo, kila kitu ni uamuzi wa mtu.” “Wala hatujamshinikiza, sijui kamuona leo,” mama Deus aliongezea. “Jamani kampenda au kamtamani?” “Mzee mwenzangu mpaka kuja hapa tumelijadili jambo hili kwa kina.” “Mmh! Haya, umesikia mke wangu?” Baba Kilole alimuuliza mkewe. “Mimi nafikiri hili ni jambo jema, sifikiri tunatakiwa kuhoji sana,” mama Kilole alijibu. “Mke wangu kuuliza si vibaya japo sisi wenyewe tunajua.” “Ni kweli, lakini mpaka kufunga safari basi hawakuja kufanya utani.” “Wazee wenzetu tumekusikieni tupeni muda tuzungumze naye, majibu mtayapata kesho.” “Hakuna tatizo, jambo lolote zuri linahitaji subira.” “Na kama akikubali harusi mnatazamia iwe lini?” “Amesema baada ya jibu zuri kuna miezi mitatu ya maandalizi.” “Kama ni hivyo itatusaidia nasi kujipanga.” Waliagana na kurudi nyumbani, Deus alikuwa na shauku ya kujua wazazi wake wamerudi na jibu gani. Lakini baba yake alimtuliza kwa kumweleza ujumbe umefika jibu watalipata kesho yake. ******* Baada ya kuondoka wazazi wa Deus, mama Kilole alimwita mwanaye aliyekuwa ndio kwanza ametoka kuoga. “Kilole mwanangu.” “Abee mama.” “Unajijua wewe sasa hivi umeisha vunja ungo?” “Najua mama.” “Unajua huu ni mwaka wa ngapi?” “Mmh! Wa tano sasa.” “Kwa hiyo nina imani upo tayari kwa ndoa.” “Mmh! Nitaweza?” “Kilole kila siku ulikuwa unatoroka usiku kwenda kulala kwa Kinape, bado unajiona mtoto?” “Nani anataka kunioa? Kinape! Vipi amerudi?” Kilole aliuliza kwa mshtuko. “Siyo Kinape.” “Nani?” “Mtoto wa mzee King’ole.” “Yupi?” “Deus” “Yule anayekaa mjini?” “Huyo huyo, nasikia mlionana leo.” “Mmh!” Kilole aliguna. “Mbona unaguna?”
”Lakini mama si unajua kila kitu.” “Kuhusu Kinape?” “Ndiyo.” “Wee mtoto hebu acha ujinga, Kinape atakusaidia nini?” “Mama, siwezi kuvunja ahadi yangu na Kinape, ameniahidi anakwenda mjini kutafuta maisha na akirudi anakuja kunichukua.” “Mwanangu haya si ya kuyasema kwa baba yako, ile ilikuwa siri yetu. Baba yako akijua atatuua.” “Mama mimi siwezi kuolewa na mume nisiyempenda.” “Haya maneno yaishie hapa, chonde mwanangu usiangushe, nakuomba ukubali.” “Mama kama nitaolewa nitakuwa sikuolewa kwa hiyari yangu.” “Najua mwanangu, ila nakuomba unifichie aibu hii.” “Mama Kinape nitamueleza nini? Kumbuka nilimuahidi, kuendelea kumsubiri mpaka atakapo rudi na ahadi ni deni.” “Mwanangu, sivyo vyote vinavyo ahidiwa hutimia, kumbuka Deus ni mtu mwenye uwezo mkubwa kimaisha, huoni itatusaidia hata sisi wazazi wako? Hebu ona Mariamu mumewe ana uwezo mdogo, lakini wazazi wake wanaishi maisha mazuri. Deusi amejenga nasikia mshahara wake mkubwa ana gari zaidi ya matatu tofauti na hili alilokuja nalo kama la mbunge, tena ni mtu tunayemfahamu.” “Mama nakubali kwa shingo upande, bado nampenda Kinape,” Kilole alisema huku akibubujikwa na machozi. “Najua mwanangu, lakini inaonesha Deus naye mtu mzuri, si unaona familia yetu, hebu tutoe kwenye dimbwi la umaskini nafasi hii asije pata mwingine tukaijutia.” mama yake alisema huku akiwa amemkumbatia na kumpigapiga mgongoni taratibu. “Sawa mama, sina jinsi lazima nikubali.” “Asante mwanangu.” Mama Kilole aliagana na mwanaye aliyeingia chumbani kwake kulala, alishukuru Mungu mwanaye kukubali kuolewa na Deus. Alipoingia ndani alikutana na mumewe akimsubiri. “Vipi imekuwaje?” “Hakuna tatizo.” “Amekubali?” “Ndiyo.” “Lakini kuna kitu nina wasiwasi nacho,” kauli ile ilimshtua mama Kilole. “Kitu gani?” “Kuhusu uhusiano wa Kilole na Kinape.” “Uhusiano upi?” Mama Kilole alijifanya hajui kitu.
”Wewe ndiye ulitakiwa kunifafanulia na sio kuniuliza.” “Mume wangu, ungeweka wazi ili nielewe unalenga nini.” “Ukaribu waliokuwa nao.” “Ni wa kawaida, Kinape si alikuwa kama mtoto wa familia.” “Mbona nilisikia wana uhusiano wa kimapenzi, sio tumuoze aje atutie aibu.” “Kwa kweli hilo mwenzangu nilikuwa silijui, mbona hukunieleza mapema ili nilifanyie kazi.” “Nikueleze nini wakati siku zote siri za watoto wa kike wanajua mama zao.” “Mume wangu kumbukeni mmekuwa mkitutia lawama wazazi wa kike, kuna mzazi anayetaka mtoto wake wa kike aharibike?” “Mbona mama yako ndiye aliyekuwa akinipa wepesi wa kuzungumza na wewe?” “Kwa vile alijua una nia nzuri, lakini kama ungetaka kunichezea na kuniacha asingekubali.” “Tuachane na hayo, kwa hiyo amekubali?” “Amekubali.” “Na una uhakika bado msichana?” “Mume wangu hilo swali siwezi kulijibu labda umuulize mwenyewe.” “Si swali la baba kumuuliza mtoto wa kike bali mama yake.” “Basi nitamuuliza, kama hana itakuwaje?” “Tujiandae na aibu au kupimwa kukutwa na wadudu.” “Mungu apishe mbali.” “Basi tulale ili kesho tuwape jibu lao.”
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Lakini upande wa pili wa Kilole alikosa usingizi kuwaza usaliti wake kwa Kinape mwanaume aliyemuingiza katika katika dunia ya wapendanao. Katika maisha yake aliamini Kinape ndiye mwanaume pekee katika moyo, alijiuliza atamwambia nini akimkuta ameolewa. Akiwa amejilaza chali kalalia mikono kwa nyuma, alijikuta kwenye mtihani mzito wa kuingia katika maisha ya ndoa ya mwanaume asiyekuwepo moyoni mwake. Lakini alikumbuka shoga yake Mariamu mtoto za mzee Sadiki jinsi alivyo ibadili familia yake kimaisha baada ya kuolewa na mwanaume mwenye uwezo aliyekuwa akiishi mjini. Aliufananisha uwezo wa mume wa Mariamu haukuwa mkubwa kama wa Deusi mtoto wa mzee King’ole. Deus alikuwa akimzidi mara mia mume wa Mariamu. Mume wa mariamu pamoja na kuwa amejenga nyumba hakuwa na gari, Deus alikuwa na jumba la kifahari na magari ya kutembelea zaidi ya matatu. Japo moyoni bado alikuwa amemjaza Kinape alijikuta akijisemea moyoni: “Liwalo na liwe.” Alivuta shuka na kujilaza, lakini bado usingizi ulimkimbia na kujikuta akikumbuka ahadi aliyopeana na Kinape. “Kinape nakupenda sana, nakuomba usiniache kumbuka wewe ndiye unayeijua thamani ya usichana wangu, wewe ndiye uliyenionjesha tamu ya dunia. Nakupenda kulicho kitu chochote chini ya jua.” Kilole alikumbuka siku aliyomlilia Kinape baada ya kuzijua raha za dunia. “Kilole naheshimu zawadi uliyonipa, nakuhakikishia wewe pekee ndiye utakaye kuwa mke wangu. Nakuomba usinisaliti.” “Sitakusaliti, nakupenda sana Kinape.” Kilole alipoyakumbuka yale alijikuta akitokwa na machozi kwa kuamini kilichopo mbele yake ni maamuzi mazito kama kumeza mfupa.
********
Siku ya pili familia ya mzee Sikwera ilirudisha majibu kukubali Kilole kuolewa na Deus, taarifa ilipoifikia familia ya mzee King’ole walimfikishia Deus ambaye moyo wake ulijaa furaha baada ya ombi lake la kumuoa Kilole kufanikiwa. Alipata muda wa kuonana na mchumba wake kabla ya kuelekea mjini. Iliandaliwa siku maalumu ambayo ilikuwa kufahamiana na kukubaliana kuunganisha ukoo mbili. Sherehe ndogo ilifanyika nyumbani kwa mzee Sikwera baba yake Kilole. Deus na Kilole waliwekwa sehemu maalumu kwa ajili ya kufahamia kwa karibu. Wakiwa kimya kila mtu akitafakari lake Deus alikuwa wa kwanza kuvunja ukimya. “Kilole,” Deus alianza kwa kumuita jina lake. “Abee,” alijibu huku ameangalia chini. “Naomba unitazame basi.” “Sema tu ninakusikia,” Kilole alijibu huku akiwa ametawaliwa na aibu. Deus alitumia nafasi ile kumchunguza Kilole kwa karibu na kugundua vitu vingi sana, haiba na umbile lililojengeka kike hasa. Moyoni aliona muda aliopanga wa miezi mitatu ni mrefu sana. Mvuto wa Kilole ulikuwa mkubwa baada ya kumsogelea kwa karibu. “Asante sana.” “Asante ya nini?” “Ya kukubali ombi langu.” “Mmh,” Kilole aliguna tu. “Kilole nakuahidi kukupenda kwa moyo wangu wote.” “Asante, nami pia nitakuwa mke mwema.” “Pia nakuahidi kukuendeleza kimasomo.” “Nitashukuru kwa vile kiu yangu ya kutafuta elimu haijaisha.” “Nitakuacha kwa muda kwa vile nawahi kazini, ila kila kitu nimewaachia wazazi. Baada ya miezi mitatu tutakuwa mke na mume.” “Hakuna tatizo nitakusubiri.” “Nashukuru kusikia hivyo.” Baada ya mazungumzo na sherehe iliyochukua saa sita familia mbili ziliagana, Deus aliamini kila kitu duniani hupangwa na Mungu, hakuamini kama kijijini kutakuwa na wanawake wazuri kushinda mjini. Aliapa kumlinda Kilole kwa nguvu zake zote. Upande wa pili Kilole bado mzimu wa Kinape ulimsumbua, ulijikuta akilaumu muda mrefu uliopangwa wa harusi. Wasiwasi wake mkubwa ulikuwa kwa Kinape kutokea kijijini kabla ya ndoa ya kuharibu kila kitu. Moyoni aliomba kila alichokijua ili Kinape asionekane kabla ya ndoa yake ili akikutana naye apate cha kudanganya.
BAADA YA MIEZI MITATU
Muda ulipotimu Deus alirudi mjini huku akiacha maandalizi ya harusi yake yakianza taratibu ikiwemo kuwekwa ndani kwa ajili ya mafunzo kabla ya ndoa. Deus baada ya kufika mjini aliendelea na shuhuli zake huku watu wake wa karibu akiwapa majukumu ya kufanikisha harusi yake. Muda ulipotimu Deus alimuoa rasmi Kilole na kuwa mke wake wa kufa na kuzikana. Ndoa yao ilijaa kila aina ya furaha huku Kilole ajilaumu kwa uamuzi wake wa kutaka kuikataa ndoa yake na Deus kwa ajili ya Kinape. Maisha aliyoishi kwa Deus hakuyawaza kuishi siku moja. Kwake aliamini maisha yale ni ya ndotoni kumbe yapo kweli.
KINAPE MJINI
Kinape naye baada ya kuingia mjini akiwa na shauku ya kupata maisha mazuri, lakini haikuwa kama alivyodhani. Maisha yalikuwa magumu sana kiasi cha kujiuliza maisha mazuri watu wanayapata vipi. Alijikuta akifanya kazi ngumu mshahara mdogo uliomtosha kula siku moja tu na siku ya pili alipoamka alianza upya. Alijikuta akiingia katika makundi ya wahuni ili aweze kuihimili kasi ya ugumu wa maisha kwa kulala nje ya soko kuu. Kila siku asubuhi walipo amka na kugombea kushusha mazao yaliyoingia sokoni, wazo la kuendelea kuishi mjini aliliona alifai kutokana na mateso ya kukamatwa na askari kila kukicha. Siku aliyopanga kesho yake arudi kijijini ndiyo usiku uliyokuwa mbaya kwake baada ya msako wa wazurulaji kukamatwa na kufunguliwa mashitaka. Kinape alikosa dhamana na kujikuta akihukumiwa miezi mitatu jela. Maisha aliyoishi gerezani yalimfanya kuuchukia mji. Siku alipotoka hakuwa na hamu ya kukaa mjini alirudi moja kwa moja kijijini kwao, hakutaka kuingia mchana kuhofia kuonekana na watu jinsi alivyo konda na mwili kuwa na upele na ukurutu. Aliingia kwao usiku hakuna aliyemuona. Alipofika wazazi wake walishtuka kumuona mtoto wao amedhoofu mwili. Walitaka kujua nini kimemsibu aliwaeleza: “Wazazi wangu nimekoma, kweli kiburi si maungwana jiji limeninyoosha.” Aliwaeleza yote yaliyomsibu mpaka kuingia gerezani. Wazazi wake hawakuwa na neno zaidi ya kumpokea. “Pole mwenetu hayo ndiyo maisha, tumshukuru Mungu umerudi salama, basi tusaidiane kwenye kilimo.” Kinape baada ya kurudi nyumbani kwao hakutaka kuonekana na mtu, aliishi maisha ya kujificha mpaka atakapopona upele na ukurutu. Hakuwa na hamu tena ya kusikia neno mjini, aliapa kwenda mjini kwa kazi maalumu na si kwenda kubahatisha. Kutokana na hali yake ya kukonda na ukurutu hakutaka kuonana hata na mpenzi Kilole. Alipanga hali yake itakapo imalika afya yake ndipo angeweza kujitokeza hadharani, pamoja na kuwa ndani taarifa za kuolewa kwa Kilole zilimshtua sana. Ili kupata ukweli alimuuliza mdogo wake wa kike. “Eti Eliza Kilole ameolewa kweli?” “Ndiyo kaka.” “Nasikia na rafiki yangu Deus.” “Ndiyo kaka.” “Siamini mpaka niende kwa mama Kilole anieleze ukweli, itakuwaje amuoze Kilolo akiujua ni mchumba wangu.” Kinape alijikuta akitoka ndani japo hali yake ilikuwa haijatengemaa vizuri na kwenda moja kwa moja nyumbani kwao Kilelo kupata ukweli wa kuolewa mpenzi wake ambaye ndiye aliyepanga kuwa mkewe. Njiani alijawa na mawazo juu ya usaliti wa Kilole aliyemuhakikisha kumsubiri mpaka atakaporudi. Alipofika nyumbani kwao Kilole alimkuta mama Kilole akianika mpunga, alipomuona alishtuka kwa mambo mawili. Kwanza kumuona Kinape aliyepotea miezi zaidi ya saba iliyopita, pili hali yake iliyodhoofika. Badala ya kumkaribisha alimshangaa. “Shikamoo mama,” Kinape alianza kumsalimia baada ya kugundua mama Kilole alikuwa akimshangaa. “Kinape!” Badala ya kuitikia alizidi kumshangaa. “Naam mama.” “Ni wewe?” “Ndiyo mama.” “Ulikuwa unaumwa?” “Hapana.” “Nini kimekusibu mwanangu?” “Ni habari ndefu mama.” “Hebu karibu ndani,” aliacha kazi zake na kumkaribisha ndani. Baada ya kuingia ndani alimkaribisha kwenye kigoda. “Karibu.” “Asante mama.” “Haya niambie nini kimekufanya uwe hivi wakati unasema ulikuwa huumwi?” Kinape alimueleza yote yaliyomkuta na kumfanya aishie gerezani badala ya kupata kazi. “Ooh, pole sana mwanangu.” “Asante mama.” “Inaonekana ulipoondoka hukuaga, baba yako kila siku alikuwa akilalamika, safari kubwa kama hizo unatakiwa kupata baraka za wazazi.” “Mama tuachane na hayo, kuna kitu kimoja muhimu ndicho kilichonileta hapa.” “Kipi hicho?” “Kuhusu Kilole.” “Kilole kafanya nini?” “Nasikia ameolewa?” “Ndiyo.” “Nani aliyetoa idhini ya kuolewa?” “Kwa nini unaliza swali kama hilo?” “Mama si unafahamu Kilole ni mchumba wangu?” “Najua.” “Sasa kwa nini mmemuoza kwa Deus?” “Uchumba wako na Kilole tulikuwa tunajua sisi lakini baba yake alikuwa hajui lolote, na penzi lenu lilikuwa la wizi halikuwa wazi.” “Hata hivyo lakini si mnajua mimi na mwanao tulikuwa na marengo gani katika maisha yetu?” “Nimekueleza idhini ya kuolewa kaitoa baba yake siyo mimi.” “Kwa nini hukumwambia amechumbiwa?” “Ningeanzia wapi wakati hatukujua upo wapi, ulikuja kutuaga kuwa unasafiri?” “Sikufanya hivyo, kutokana na dharula iliyojitokeza kwa hilo naomba mnisamehe.” “Sasa kama hivyo hatujui ulikuwa wapi tungeweza vipi kukusubiri mtu tusiyejua upo wapi na utarudi lini. Kuolewa ni bahati tusingeipoteza bahati ile ambayo msichana yoyote kijijini asingekubali kuipoteza” “Sawa, lakini kumbukeni wewe na mwanao mmenifanyia ukatiri mkubwa.” “Utatulaumu bure makosa umeyafanya mwenyewe.” Kinape aliaga na kuondoka huku moyo ukiwa na majonzi ya kuolewa mpenzi wake Kilole mwanamke ambaye aliamini ndiye aliyemuonesha raha ya mapenzi. Lakini hakuwa na jinsi kwa kujua siku zote mwenye kisu kikali ndiye hula nyama.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
MIAKA MIWILI BAADAYE Maisha mjini yaliendelea vizuri kwa Kilole kuzidi kupendeza baada ya kupata mtoto wa kike kwenye ndoa yake. Kijijini kwao nako hakukusahau kwa kupeleka misaada ikiwemo kubadili paa la nyasi na kuweka bati. Mabadiliko yale yalifanya mama Kilole aamini kama mwanaye angeolewa na Kinape angempoteza. Maisha ya Kinape aliyajua mwenyewe kazi yake kubwa kijijini ilikuwa kulima shamba la wazazi wake na mashamba ya watu na kulipwa fedha kidogo. Ugumu wa maisha ulimfanya akate tamaa ya maisha na kuamua kuwa mvuta bangi na mlevi wa pombe za kienyeji. Matumizi yale yalimchakaza na kuoneka amechoka kama alirudishwa gerezani, wazazi wake walisikitika kwa hatua aliyofikia. Hata jina lake alilibadili na kujiita Marehemu mtalajiwa kwa vile aliamini kuwa maisha mazuri ni sawa na ngamia kupita katika tundu la sindano yeye ni wa kusubiri kufa. Kama ilivyokuwa kawaida ya Deus kila baada ya miezi sita alikwenda kijijini kuwatembelea wazazi wake, taarifa za kuwepo rafiki yake Kinape zilimfikia. Baada ya kufika kijijini alikwenda moja kwa moja nyumbani kwao na Kinape ili aonane naye, alipofika alimkuta mama Kinape aliyempokea kwa furaha na bashasha. “Karibu mwanangu.” “Asante mama, za hapa?” “Nzuri kiasi.” “Shikamoo.” “Marabaha.” “Unasema kiasi kivipi?” “Ukimuona Kinape utamtambua?” “Kivipi?” “Kinape anajiita Marehemu mtalajiwa.” “Kwa nini?”
”Amekwisha kata tamaa ya maisha.” “Kwa nini?” “Maisha ya kijijini yamekuwa magumu kwake hata huko mjini alikokutegemea anapaogopa kama kuzimu.” “Yupo wapi?” “Akitoka asubuhi kurudi jioni.” “Mmh, sasa sijajua hiyo jioni itakuwa saa ngapi? Maana nategemea kuondoka saa kumi na mbili jioni.” “Baba wala usisumbuke kumsubiri, hiyo jioni bahati lakini muda wake kabisa ni saa mbili usiku akiwa amelewa.” “Sasa mama, nataka kufufua matumaini yaliyopotea ya Kinape.” “Yapi tena hayo baba?” “Nitamchukua, nina imani kwa muda mfupi atakuwa tegemeo la familia.” “Tutashukuru, kwani tumekwisha kata tamaa na kumuachia Mungu.” “Basi mama mwambie jumapili nitamfuata au kama nitakuwa na kazi nyingi nitamtuma mtu amfuate.” “Sijui baba nikushukuru vipi.” “Wala hakuna cha kunishukuru, Kinape ni ndugu yangu wa damu siwezi kukubali kumuona akiadhirika wakati ndugu yake nina uwezo wa kumsaidia.” “Nitashukuru baba,” mama Kinape alisema huku akitaka kupigia magoti, Deus alimuwahi asifanye vile. Waliagana huku akimsisitiza asisahau kumweleza Kinape siku hiyo asitoke, jioni ilipofika Deus alirudi mjini bila kuonana na rafiki yake kipenzi. **** Kinape aliporudi alikuta salamu kwa mama yake. “Kinape, Deus alikuja.” “Shida yake nini?” “Swali gani hilo mwanangu, Deus si rafiki yako?” “Deus si rafiki yangu ni adui yangu namba moja.” “Kwa nini unasema hivyo?” “Atamuoaje Kilole akijua ni mchumba wangu.” “Kinape, maisha yako yanakushinda ungeweza vipi kukaa na mwanamke?” “Hii haikuwa juu yenu.” “Basi kwa taarifa yako huyo adui yako ndiye anayetaka kuyabadili maisha yako kwa kukurudisha mjini.” “Kufanya nini?” “Deus ni mtu mkubwa sana, siku hizi ana gari kama la mbunge, kweli duniani hakuna mtu mwembamba. Deus kanenepa huyo na kitambi juu, kaacha maagizo kuwa jumapili atakufuata uende mjini.” “Ni umaskini ndiyo utakaonifanya niende kwake, lakini niliapa sitamsamehe mpaka nakufa.” “Lakini unamlaumu bure, nina imani alikuwa hajui, kama angejua sidhani angekubali kumuoa Kilole.” “Kwa nini hakuuliza kabla ya kuoa?” “Ni wazi alifichwa.” “Kama ni hivyo familia ya kina Kilole kimenitendea unyama.” “Kwa hiyo mwanangu nakuomba usiipoteze nafasi hii, nina imani ndoto zako huenda zikatimia.” “Sawa mama nitajiandaa na safari.” “Basi acha kunywa mipombe yako ili kidogo mwili upendeze kwa siku mbili” “Nitafanya hivyo mama.” ******* Siku ya jumapili Kinape alijiandaa na safari ya kwenda mjini kwa ajili ya safari. Saa nne asubuhi gari aina ya Toyota land cruser Vx ilisimama mbele ya nyumba ya mzee Solomoni baba yake Kinape. Kinape alikuwa wa kwanza kutoka nje ili aonane na rafiki yake kipenzi Deusi. Baada ya mlango kufunguliwa, kwanza kuteremka alikuwa Salome mdogo wake Deus, alipomuona tu alipaza sauti: “Kaka Kinape mwenyewe huyo hapo,” alisema huku akigeuza shingo kumuangalia mtu aliyefuatana naye. Alikuwa kijana mmoja mtanashati alisogea hadi alipokuwa amesimama Kinape. “Habari ndugu?” “Nzuri tu, karibu.” “Nina imani wewe ndiye Kinape?” “Hujakosea ndiyo mimi.”
”Vipi wazazi wamo ndani?” “Yupo mama, baba ametoka kidogo.” “Naomba nionane naye.” “Karibu kwenye kigoda nimwite,” Kinape alimkaribisha mgeni kwenye kigoda kisha aliingia ndani kumwita mama yake. Baada ya muda mama Kinape alitoka alipomuona mgeni alimkaribisha. “Karibu baba.” “Asante, shikamoo mama. “ “Marahaba, karibu.” “Asante, mama mimi si mkaaji nimetumwa hapa na brother Deus nimfuate Kinape.” “Hakuna tatizo baba, ndugu yenu mwenyewe huyo hapo.” “Nashukuru nilipofika tu Salome kanionesha, kwa hiyo nilikuwa naomba ruhusa niwahi kuondoka.” “Hakuna tatizo hata yeye mwenyewe amekwisha jiandaa” “Basi tunaweza kwenda.” Kabla ya kuondoka mama Kinape alimwita ndani mwanaye na kumpa maneno ya mwisho. “Kinape mwanangu najua wazi ulikuwa na urafiki wa karibu na Kilole, nakuomba chondechonde achana naye, fuata kilichokupeleka. Kumbuka kosa lako moja linaweza kuwa majuto ya milele. Muogope Kilole kama ukoma muone ni shemeji yako.” “Sawa mama nimekuelewa.” Kinape na Dereva aliyetumwaamfuate aliongozana hadi kwenye gari na kuondoka pamoja. ****** Dereva aliyemfuata Kinape alimjulisha Deus kuwa wamekaribia nyumbani, Deus alimjulisha tayari yupo nyumbani kwa ajili ya kumsubiri mgeni. Sauti ya gari ilimfanya Deus asogee mlangoni kusubiri kumpokea rafiki yake kipenzi waliopotezana muda mrefu. Gari liliposimama dereva alimfungulia mlango Kinape ambaye aliteremka kwenye gari, Deus alipomuona akipaza sauti huku akitoka mbio kwenda kumpokea rafiki yake kwa kumwita jina alilolizoea. “Keiii Piii.” “Dewuuuu.” Wote walikutana na kukumbatiana kwa furaha. “Ooh, karibu sana rafiki yangu.” “Asante nimekaribia” Walishikana mikono na kuiingia ndani pamoja, wakati wanaingia Kilole alikuwa anatoka kwenye friji kuchukua juisi ya mtoto. Macho yake yalipatwa na mshtuko baada ya kumuona Kinape ndani ya nyumba yake mwanaume aliyemkimbia na hakutaka hata siku moja aonane naye na kujibu maswali ambayo aliaminbi kwake ni magumu. Kinape hakushtuka sana kwa vile alijua Kilole yupo wapi na ni mke wa mtu, Kilole glasi ya juisi ilimponyoka na kuanguka chini. “Mke wangu vipi mbona hivyo?” “Ha..ha..pana.” “Kinape, karibu sana hapa ndipo ninapoishi.” “Asante kupafahamu.” “Nina imani nilikueleza tutakuwa na ugeni, naomba basi apatiwe huduma zote muhimu kisha aoneshwe chumba chake,” Deusi alimwambia mkewe. “Ha..ha..kuna ta..ta..tizo.” Kilole alisahau kuokota glasi iliyoangukia juu ya zuria, aligeuka na kuelekea chumba cha mgeni kuangalia kama matayarisho ya mwisho kabla ya kumkaribisha chumba mgeni. Alijikuta akikosa raha kwa kitendo cha mumewe kumwingiza ndani ya nyumba yake mwanaume ambaye lazima atataka majibu ya usaliti wa ahadi yao. Alijikuta akimlaumu mumewe kwa kitendo cha kutomjulisha ni mgeni gani anayekuja. Kwa upande wa Kinape alibakia na siri moyoni hakutaka kumueleza rafiki yake uhusiano wake na Kilole. Pia alikumbuka wosia wa mama yake juu ya kuwa karibu na mke wa mtu japo alikuwa mpenzi wake. ******* Baada ya Kinape kuoga na kubadili nguo Deus alimtambulisha rasmi rafiki yake kwa mkewe Kilole. “Mke wangu, huyu ni rafiki yangu kipenzi Kinape nina imani si mgeni kwako.” “Ni kweli, lakini sikuwa na mazoea naye,” Kilole alimjibu mumewe akiwa ameangalia chini. “Kinape huyu ndiye mke wangu Kilole ambaye ni shemeji yako.” “Nashukuru kumfahamu shemeji.” “Mke wangu, Kinape atakuwepo hapa kwa muda mpaka nitakapomtafutia kazi na yeye kuanza maisha yake.” “Hakuna tatizo, karibu shemeji,” Kilole alimkaribisha Kinape kwa sauti ya chini. Baada ya utambulisho ule, Deus na Kinape walizungumza mengi wakikumbushia mambo ya miaka mingi. Deus alikuwa na furaha tofauti na Kinape aliyejifikiria atatazamana vipi na Kilole mwanamke aliyemsaliti. Usiku ulipoingia waliagana kuonana kesho asubuhi. Chumbani aliyelala usingizi uzuri alikuwa Deus peke yake lakini Kinape na Kilole kila mmoja aliwaza lake. Kilole aliamini kabisa kuolewa na Deus kumeweza kuyabadili maisha yake, alijiuliza kama Kinape ameletwa na mumewe ili amsaidie, angeweza vipi kumtimizia mahitaji yake muhimu. Aliamini Kinape pamoja na kuahidiana kuoana angempotezea muda tu na si kumtengenezea maisha yake. Alijikuta akiondoa hofu moyoni na kuwa tayari kukabiliana na maswali atakayo ulizwa na Kinape. Naye Kinape alijikuta akiumia kwa usaliti wa mpenzi wake wa kuolewa na mtu mwingine. Kilichomuuma sana kilikuwa kuolewa na mtu wa karibu na kibaya zaidi kukaa nyumba moja huku wote wakilishwa na mtu mmoja. Siku ya pili Deus baada ya kujiandaa kwenda kazini alimfuata rafiki yake Kinape chumbani kwake kumuaga. “Best mimi nawahi kazini tutaonana jioni.” “Hakuna tatizo.” “Kila kitu nimemuachia maagizo shemeji yako, nakuomba uwe huru au siyo Keiiii Piii,” Deus alikumbushia enzi zao. ‘Hakuna tatizo Dewuuuu.” Walicheka pamoja na kuagana Deus alitoka chumbani kwa Kinape na kumpitia mkewe aliyembusu kisha walisindikizana hadi kwenye gari. “Bai Bebi.” “Bai honey safari njema, kazi njema.” “Asante mke wangu.” Deus aliondoka na kumwacha mkewe akimsindikiza kwa macho mpaka alipopotea ndipo alipogeuka kurudi ndani. Alirudi taratibu huku akiwa na mawazo mengi juu ya kuwepo Kinape pale, hakutaka hata siku moja katika maisha yake baada ya kuolewa na mtu mwingine kwa kuvunja ahadi yao asikae karibu na Kinape.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kilole hata alipokwenda kijijini baada ya ndoa hakutaka kuonana na Kinape, aliingia kimya kimya mpaka anaondoka Kinape hakujua. Alijiuliza akimtaka mumewe amuondoe Kinape na kumtafutia sehemu nyingine atamuelewa. Jambo lingine alilojifikiria lilikuwa kama hilo litashindikana basi atatafuta mbinu nyingine kuhakikisha anauvunja urafiki wa Deus na Kinape. Baada ya kuingia ndani alifanya usafi wote muhimu, akiwa jikoni akiandaa kifungua kinywa, Kinape aliamka na kwenda hadi sebuleni. Sebule ilikuwa tupu ila runinga ilikuwa wazi, alikaa kwenye sofa viti ambavyo toka azaliwe hakuwahi kukalia. Taratibu alitembeza macho kuangalia uzuri wa nyumba ambayo ilikuwa na kila kitu, akiwa bado anashangaa alisikia sauti ya vyombo. Aliamini Kilole anaosha vyombo, alinyanyuka na kuelekea jikoni. Alimkuta akikaanga mayai huku amempa mgongo, alimsogelea taratibu bila kumshtua alipomkaribia alimsalimia. “Za asubuhi shemeji,” sauti ile ilimshtua sana Kilole na kumfanya ashike mkono kifuani. “Kilole usishtuke maji yamekwisha mwagika jione huru,” Kinape alimtoa hofu. “Sio hivyo Kinape ni wazazi si mimi,” Kilole alijitetea. “Najua, ndiyo maana nikasema jisikie huru, tupo sehemu ya watu tusije kosa mwana na maji ya moto.” “Nisamehe Kinape bado nakupenda nipo hapa kwa shinikizo, lakini mimi nilikuwa radhi kukusubiri mpaka atakaporudi,” Kilole alijikuta akiomba msamaha huku akibubujikwa machozi ya aibu. “Si kweli Kilole, kwa nini hukuwaeleza ukweli, ina maana mama yako hajui uhusiano wetu. Au ndiyo sababu ya pesa?” “Mama alikuwa anajua lakini alimuogopa baba ambaye hakuujua uhusiano wetu.” “Kilole muongo, baba yake alitufuma mara ngapi asijue?” “Kama alikuona alijua ni mzowezi si muoaji.” “Si kweli kwa nini hukumwambia kuwa mimi ndiye mumeo mtarajiwa au kwa vile sina kitu. Kumbuka Kilole mateso yote niliyoyapata mjini ni kwa ajili yako, nimefungwa kwa ajili yako kutafuta maisha mazuri ili tuje tuishi maisha mazuri. Lakini mwisho wa siku umeamua kunisaliti.” “Niamini Kinape si mimi ni wazazi wangu.” “Kwa nini hukukataa?” “Nilik...,” Kilole alinyamaza baada ya kusikia sauti ya gari, kweli alikuwa mumewe amerudi mara moja. Aliingia ndani haraka na kukutana na Kinape anatoka jikoni, alishtuka kumuona Kinape akitokwa na machozi. Hakumuuliza kitu alikwenda moja kwa moja jikoni, alishtuka kumkuta mkewe anafuta machozi alishtuka sana na kuhoji. “Vipi mbona mnalia, kuna usalama?” Kilole alishtushwa na swali la mume wake na kujilaumu kusahau kufuta machozi. “Mke wangu kuna nini mbona wote mnalia?” Kilole alikosa jibu la kumjibu mumewe alibakia ameinama huku akijiuliza mumewe kama atajua kuwa alikuwa na mahusiano na Kinape ndoa yake itakuwa hatiani. Alitamani kuomba radhi na kumweleza ukweli juu ya uhusiano wake na Kinape na kumhakikishia hawezi tena kuwa na uhusiano naye. Deus bado alikuwa yupo kwenye kizungumkuti asijue nini kimetokea muda mfupi baada ya kuondoka kwenda kazini na kumuacha Kinape amelala na mkewe akirudi ndani. Lakini amerudi na kukuta mabadiliko na mkewe kushindwa kumjibu. “Mke wangu kuna habari za msiba?” “Hapana.” “Sasa kuna nini?” Kilole aliendelea kukosa jibu kwa mumewe, Deus alimwacha mkewe jikoni na kumfuata Kinape aliyekuwa amesimama sebuleni akifuatilia jibu la Kilole ambalo alijua linaweza kuharibu ndoto yake kwa mara ya pili. “Kinape.” “Naam.” “Kuna nini mbona mnaniacha njia panda kuna kitu gani kimetokea muda mfupi baada ya kuondoka?” “Ni jambo la kijijini.” “Jambo gani lililowatoeni machozi?” “Ni kweli, sikutegemea shemeji kuniuliza swali kama lile.” “Swali gani?” Kilole mapigo ya moyo yalimwenda mbio miguu ilianza kumwisha nguvu kwa kuamini kosa moja la Kinape litayagharimu maisha yake yote. Alitamani kumuomba Kinape asiseme ukweli ambao ungemgharimu maisha yake. Alipotaka kumuomba Kinape anyamaze ili akayazungumze na mumewe ndani mdomo ulikuwa mizito alibakia akimuomba Mungu amuepushe na balaa lile. “Shemeji aliniulizia habari za rafiki yake kijijini.” “Sasa habari za rafiki yake na machozi yenu yanahusiana vipi?” Swali lile lilizidi kumuweka katika hali mbaya Kilole kwa kujiuliza yeye alimuuliza swali gani kuhusu rafiki yake lililosababisha watokwe na machozi. “Aliniulizia shoga yake aliyesoma naye ambaye alikuwa rafiki yangu wa kike, mwezi jana tumemzika baada ya kufa kwa uzazi. Kwa kweli kwangu ilikuwa sawa na kutonesha kidonda kilichoanza kupona, nilipomweleza habari zile shemeji alianza kulia kitu kilichonikumbusha maumivu ya moyo ya kumpoteza kipenzi changu aliyekufa na kiumbe changu tumboni.” “Ooh! Poleni sana, sikujua rafiki yangu kama ulipata msiba mzito kiasi hicho, Mungu atakulipia hiyo yote ni mitihani ya maisha.” Deus alimvutia kifuani rafiki yake na kumpigapiga taratibu huku akiendelea kumfariji. “Pole sana rafiki yangu Mungu atakulipia mara mbili.” “Asante.” Alimwacha Kinape na kwenda kumkumbatia mkewe aliyekuwa bado akitokwa na machozi ya hofu. “Pole mke wangu kwa kuondokewa na rafiki yako kipenzi.” “Asante mume wangu.” “Nakuombeni msahau yaliyopita kwani kuendelea kuumia ni kuingilia kazi ya Mungu na kuona kama mmeonewa lakini kumbe hiyo ni njia yetu sote tatizo kutangulia.” “Tumekuelewa, kwangu ulikuwa mshtuko ambao sikuutegemea,” Kilole alijikuta akipata nguvu za kuongeza uongo baada ya Kinape kumuokoa kwenye swali lililokuwa kama kaa la moto mdomoni mwake. “Basi jamani mimi si mkaaji nimerudia flash disic yangu niliisahau juu ya droo ya kitanda.” Deus alielekea chumbani na kumuacha mkewe akiwa bado amesimama, Kilole naye aliamua kumfuata mumewe chumbani. Alipofika alimkumbatia kwa nyuma na kusema kwa sauti ya chini. “Samahani sweet.” “Samahani ya nini tena mpenzi?” “Kwa hali uliyonikuta nayo, sikupenda upatwe na mshtuko kama ule.” “Aah, kumbe hilo mbona la kawaida, si ujajua nakupenda kiasi gani, sipendi kukuona kwenye matatizo, heri niteseke mimi si wewe kipenzi changu.” “Najua, ndiyo maana nikakuomba samahani mpenzi wangu, hata mimi sitaki nikuone unaumia kwa ajili yangu.” “Nashukuru kwa kulifahamu hilo.” “Basi mpenzi nisikucheleweshe, mke mwema ni yule anayemhimiza mumewe katika kazi zake na si yule anayemuacha akiharibikiwa.” “Asante sana mke wangu, lazima nimshukuru Mungu kunipa mke mwema.” Baada ya kuchukua Flash disc Deus alimuaga tena mkewe na kuwahi ofisini. ******** Baada ya kuondoka Kilole alishindwa amshukuru vipi Kinape kwa kumuokoa kwa mumewe kwa kuamini kama angejibu yeye lazima angejichanganya. Wakiwa wanapata kifungua kinywa, Kilole alimshukuru Kinape. “Kinape sikuwezi wewe kiboko sikutegemea ungejibu vile.” “Hiyo mbona kazi ndogo hata kama angenifumania natoka chumbani kwako bado ningeweza kujitetea na yeye angekubali kwa kukiamini nitakacho mweleza.” “Basi nilikuwa na wasiwasi na kujua talaka ipo usoni mwangu.” “Kama nilivyokueleza maji yameisha mwagika hayawezi kuzoleka.” “Usiseme hivyo Kinape, sipendi uumie kiasi hicho.” “Nimeishaumia kinachotakiwa kutuliza maumivu.” “Nitakusaidia kuhakikisha maisha yako yanakuwa mazuri.” “Sawa, lakini naomba tuishi kama mtu na shemeji yake tuondoe mazoea ya karibu yatakayo muondoa wasiwasi mumeo.” “Nashukuru Kinape kuwa muelewa, nakuhakikishia kuyasahau mateso yote ya kijijini na kuyaanza maisha mapya.” MWAKA MMOJA BAADAYE Maisha ya Kinape yalibadilika kutokana na kazi aliyokuwa akifanya, hata hali ya mwili ilikuwa ya mvuto kutokana na maisha aliyokuwa akiishi. Kilole alijikuta akivutiwa na Kinape kila alipopita au alipokuwa amekaa alimwangalia sana. Tofauti ya Deus na Kinape ilikuwa katika mavazi, Deus siku zote alivaa nguo za heshima muda wote tofauti na Kinape alivaa nguo zinazokwenda na wakati kama jeans tisheti na raba za bei mbaya kutokana na pesa aliyokuwa akipata. Kinape alijipenda kwa kujipulizia manukato ya bei mbaya kifuani alikuwa na mkufu mkubwa wa dhahabu. Kila mwanamke alitaka awe wake, lakini alichagua msichana mmoja ambaye aliamini ndiye anayefaa kuwa mkewe baada ya kila kitu kwenda vizuri. Hakuisahau familia yake kitu ambacho siku zote alisisitizwa na rafiki yake ahakikishe kipato anachokipata aikumbuke familia yake kijijini pamoja na kufanya marekebisha ya makazi ya wazazi wake. Kinape alikuwa makini sana katika maisha yake hakutaka mchezo kabisa. Mvuto wake machoni kwa wanawake ulikuwa mateso mazito kwa Kilole na kujikuta akimuona Kinape kama mwanaume pekee mwenye mvuto na uwezo wa kitandani tofauti na Deus, ambaye hakuwa mtundu sana kitandani zaidi ya upendo wa dhati. Kilole alijiuliza atawezaje kumsogeza karibu Kinape ambaye tayari ameisha jitangaza kuwa ana rafiki wa kike ambaye wakati wowote atatambulishwa kwao. Kila alipokuwa Kinape peke yake alitamani kuzungumza naye ili kumweleza jinsi gani anavyoteseka juu yake. Japo hakutaka kuachana na mumewe lakini shida yake wawe karibu ili kukumbushia mapenzi yao ya zamani ambayo aliamini hakuna mwanaume mwingine wenye kumpa raha kama Kinape.
Wakati huo Deus mambo yake yalizidi kuwa mazuri kutokana na kuingiza kipato kikubwa kutokana na takrima ya kazi yake. Aliweza kumpa siri nyingi rafiki yake kipenzi jinsi anavyoweza kupata pesa nyingi nje ya kipato chake cha kawaida. Deus alijikuta akimuamini sana Kinape kwa kumweleza mambo mengi kuhusu uwezo wake wa kipesa na madaraka yake kazini. “Kinape nipo kwenye kitengo cha hatari sana ukiwa mnoko huchelewi kufa, hivyo inabidi uume na kupuliza. Kitengo cha kudhibiti madawa ya kulevya ni kitengo hatari sana vigogo ndiyo wahusika wakuu kama utakamata mizigo yao huchelewi kuhamishwa au kutengenezewa zengwe litakalo kulaza pabaya hata kukumaliza kabisa.” “Kwa hiyo vigogo hawakamatwi?” Kinape alimuuliza Deus. “Utaanzia wapi, nyuma yako kuna wakubwa wanakula kupitia mgongo huo huo, sasa wewe jitie kiherehere.” “Kwa hiyo matumizi ya dawa ya kulevya kwisha ni vigumu?” “Ni vigumu lazima tuseme ukweli.” “Sasa kitengo hicho kazi yake nini?” “Kudhibiti dawa za kulevya.” “Lakini mbona wengine mnawakamata?” “Hao ukiona hivyo hawana mikono ya wakubwa.” “Kwa hiyo unapata posho nene toka
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
kwa hao vigogo?” “Kweli rafiki yangu, nisingeweza kuwa vitu hivi kwa muda mfupi.” “Alafu unafahamika sana na watu wazito, huwezi kuamini siku ile uliponituma niende kwenye kampuni ile nilipokelewa kama mfalme. Nje niliacha watu wakisota kuomba kazi hata jioni baada ya kazi nilipewa gari la kunirudisha nyumbani, wote pale wanajua Paroko ni ndugu yangu wa damu.” “Hao ndio watu tunaokula nao mjini, waswahili wanasema sema na watu uvae viatu.” ******* Wakati Deus akiuweka wazi uwezo wake wa pesa na njia zinazoingilia, Kilole alikuwa katika wakati mgumu kuhakikisha Kinape kabla ya kuhama mule ndani basi awe ameisha mrudisha katika himaya yake. Siku moja Deus alisafiri kikazi na kuwaacha ndani ya nyumba mkewe, Kinape na mfanyakazi wa ndani. Kilole aliamini ile ni nafasi pekee ya kumsogeza Kinape karibu, Lakini siku hiyo jioni ilikuwa chungu kwa Kilole baada ya Kinape kuja na mpenzi wake nyumbani kumtambulisha. Roho ilimuuma kwa kuamini Kinape amefanya vile ili kumlingishia yeye, alipofika na rafiki yake wa kike Kinape alimtambulisha kwa Kilole. “Shemu huyu ndiye ubavu wangu kama nilivyowataarifu, nilipanga leo awakute wote, lakini kwa vile Swahibu amesafiri nimeonelea si vibaya hata wewe kuwa muwakilishi hata siku akija asionekane mgeni.” “Karibu sana mgeni,” alimkaribisha kinafiki lakini moyoni alikuwa na donge zito. “Asante nimekaribia,” mgeni alijibu huku akijilaza kwenye kifua cha Kinape kama katumwa. “Shemu usione Kinape natakata sababu ya mtoto huyu, kwao wamemlea akalelewa, sifa ziende kwa wazazi wake.” “Mmmh! Kama hivyo hongera.” Siku ile walishinda pale na jioni alimsindikiza nyumbani kwao, aliporudi alimkuta Kilole hayupo katika hali ya kawaida kitu kilichomshtua Kinape. “Vipi shemu mbona upo hivyo, maana naona ghafla umekosa raha au unamkumbuka mzee mbona ni leo tu?” “Kwanza Kinape jina hilo unaloniita silipendi sema hujui tu.” “Jina gani?” “La shemeji.” “Aah, sasa wewe ni nani kama siyo shemeji yangu.” “Niite mpenzi au jina langu.” “Eti?” Kinape alishtuka. “Umesikia sana napenda uniite mpenzi mahawala hawaachani.” “Lakini kwangu wanaachana.” “Kinape kumbuka bado nakupenda.” “Hata mimi nakupenda,” Kinape alimjibu Kilole. “Sasa kwa nini unanionesha mwanamke wako mbele yangu?” “Jamani kuna ubaya gani nami kuwa na wangu mbona mimi sijakuzuia kunionesha kuwa ni mke wa Deus?” “Kinape sikia, kama nilivyokueleza kuwa mimi nilikubali kuolewa kwa shinikizo, lakini nakuhakikishia bado nakupenda na upendo wangu hautakufa milele.” “Sawa, sikatai lakini sasa hivi nitaendelea kukuheshimu kama shemeji yangu na si mpenzi wangu.” “Hilo najua endelea kuniheshimu kama shemeji yako, lakini Deus akiwa mbali utabaki kuwa mpenzi wangu. Nitahakikisha kutokana na uwezo wa mume wangu kukuwezesha kipesa kisha nitaachana naye ili tuishi pamoja.” “Kilole hilo halitawezekana hata siku moja,” Kinape alimjibu huku akimkazia macho. “Litawezekana, kwa vile wewe ndiye mwanaume aliye moyoni mwangu, hakuna mwingine zaidi yako.” “Kilole siwezi kumtendea unyama rafiki yangu kwa ajili ya tamaa zako za mwili, pia siwezi kukorofishana na rafiki yangu kwa ajili yako, sitaki nionekane mwizi wa fadhira kukosa nuksani kwa ajili ya starehe za muda.” “Kama hutaki tumfanye hivyo basi tufanye penzi la siri.” “Kilole hakuna siri katika mapenzi.”
“Lipo kama wenyewe tukiitunza siri hiyo.” “Haitawezekana, Kilole mshukuru Mungu kwa kukupa mume wenye uwezo pia mwenye mapenzi ya dhati na wewe. Kwa nini unataka kuichezea shilingi kwenye tundu la choo?” “Kumbuka wewe ndiye uliyenionjesha tamu ya dunia.” “Ni kweli, lakini kisicho riziki hakiliki, haukuwa riziki yangu ndiyo maana ameolewa na mwingine.” “Kama ulijua hivyo mbona ulinilaumu?” “Nilikulaumu kwa haki kwa vile ulivunja ahadi yetu, lakini uliponieleza umeozwa kwa shinikizo la wazazi wako nilikuelewa.” “Kinape nimekubali, basi naomba kwa leo tu ili nipoze machungu ya moyo wangu, usiponipa nitateseka na nitakuwa radhi kuachika na kurudi nyumbani.” “Kilole kwa nini hukusema mapema mpaka umesikia nina mwanamke ndiyo yazuke haya?” “Nilikuwa natafuta nafasi ili nikueleze, kumtambulisha mpenzio ilikuwa kama kuniwahi kuzieleza hisia zangu.” “Nimekuelewa, lakini nakuomba chonde heshimu ndoa yako, kumbuka bomu unalotaka kulitega litatusambaratisha na kijiji tutashindwa kurudi.” “Kinape nakuhakikishia hata Deus akijua hawezi kufanya lolote kwa vile nina siri zake nyingi chafu.” “Lakini kipi unachokikosa kwa mumeo?” “Mapenzi yako, ilinionjesha sasa hivi siyapati.” “Kilole bora lawama kuliko fedheha, nakuhakikishia siwezi kushea mapenzi na rafiki yangu na ukizidi kunilazimisha nitahama hapa. Kuanzia leo nione kama mbingu na ardhi,” Kinape alisema kwa kujiamini bila mzaha. “Wapii? Kinape nakuhakikishia lazima utakuwa mpenzi wangu.” “Labda kwa nguvu za giza.” “Walaa, situmii mizizi wala hirizi wenye hila ni wanawake bwana.” “Tutaona, na sasa naomba unione kama kituo cha polisi kwa muuza unga, Kilole nimeteseka sana kutafuta maisha, mwanga unaonekana unataka kunipeleka wapi, nitawaeleza nini wazazi wangu.” “Wee, maliza yote lakini mwisho wa siku utabakia kuwa mpenzi wangu, kumbuka wewe ndiye uliyenirubuni na kupoteza sifa za usichana wangu, leo hii eti nikuone kama kituo cha polisi na mvuta bangi. Kwa taarifa yako mimi nakuona kama jalala na siku zote ndilo kimbilio la mimi nzi.” “Haya tutaona.” “Si upo, ipo siku utakubaliana na mimi ninachokisema, haiwezekani nitunze mimi wengine wafaidi utamu. Kumbuka Kinape nimekuwa na wewe katika mazingira magumu na uliniahidi ipo siku nitafaidi raha. Leo hii umepata unanikataa.” “Sijakukataa, sasa hivi wewe ni mke wa mtu kuwa muelewa.” “Kwa hili siwezi kukuelewa mpaka naingia kaburini nakuapia ukinikataa nitajiua.” “Umefika mbali, lakini mbona una maisha mazuri mumeo anakuhudumia kila kitu kwa nini unataka kulipiga teke fuko la pesa.” “Kama unataka suruhu tufanye penzi la siri, nakuhakikishia kumheshimu mume wangu wala sitamdharau.” “Kilole najua hutanielewa nakuomba umkemee shetani wa uzinzi.” “Kinape uniniambia hivyo? Leo hii unajua kukutamani ni kuwa na shetani wa uzinzi kama ungejua hivyo usingenihalibia usichana wangu kumbuka nilikueleza mpaka utakaponioa au zawadi kwa mwanaume yeyote atakayenioa. Lakini ulinidanganya kuwa utanioa mbona hukunioa?” Kilole alizugumza huku akilia kwa hasira. “Kilole naomba unisikilize tena unisikilize kwa makini, kabla ya kuja mama yangu alilijua hili na kunieleza nisiwe na wewe karibu hivi akisikia nimefukuzwa na Deus kwa sababu yako nitakuwa mgeni wa nani. Kumbuka sasa hivi wazazi wangu wanaishi maisha ya raha kwa ajili ya Deus huoni kujiingiza katika mapenzi na wewe itakuwa sawa kukata tawi nililokalia?” “Kinape usiwe mwingi wa nahau, Deus hajui lolote kuhusu uhusiano wetu kwa hiyo itatupa nafasi ya kufanya mambo yetu kwa siri bila kujua.” “Kilole narudia tena sitafanya na wala sitegemei kufanya tuheshimiane na kuanzia leo humu ndani nahama nitakuja akiwepo Deus tu.” “Na akikuuliza kwa nini umehama utamjibu nini?” “Nitajua nitakacho mjibu lakini hakitahusiana na wewe.” “Kinape naomba uje unizike, ukiondoka jiandae kusikia msiba wangu.” “Kwa hilo sitakutenga nitahudhuria mazishi yako.” “Yaani upo tayari nife unaniona?” “Kwa hili nipo radhi ufe, nina imani hata bila kuwa na mimi bado utaendelea kufurahia maisha. Kusema utajiua kwa ajili yangu ni uongo mkubwa, kama ungekuwa na mapenzi na mimi usingeolewa.” “Nikueleze mara ngapi nililazimishwa lakini mapenzi yangu yote kwako.” “Nimekuelewa, basi endelea na mumeo.” “Upo tayari nife?” “Kwa hili nipo tayari, sipo tayari kujigeuza nyoka mdogo nimekuwa nammeza mfugaji kwa ajili ya tamaa zako za mwili.” “Kinape nimekuelewa, ila nakuomba kitu kimoja endelea kuniita shemeji na mimi nitakuheshimu kama rafiki ya mume wangu. Nakuahidi sitakutamkia tena maneno ya mapenzi. Nakuomba unisamehe kwa yote yaliyojitokeza, nina imani ukiondoka lazima siri itavuja naweza kukosa Bara na Pwani. “Kinape nisamehe sana, ni mapenzi mazito kwako, lakini nakuhakikishia nitarudia tena nisamehe sana,” Kilole alisema kwa sauti iliyoambatana na kilio. “Nimekusamehe Kilole, tuiheshimu safina hii tunayosafiri pamoja, lolote baya tukilitenda itakuwa sawa na kuitoboa kwenye kina kirefu tutazama wote.” “Nimekuelewa Kinape, nakuomba unisamehe sana.” “Nimekusamehe, asante kwa kunielewa.” Walikubaliana kuendelea na taratibu zilizokuwepo za kuheshimiana kama mtu na shemeji yake na si wapenzi. Kilole baada ya kugonga mwamba alikuwa na mpango mzito moyoni mwake wa kikakikisha anampata Kinape bila mwenyewe kujua. Wakiwa katikati ya mazungumzo simu ya Kinape iliita, alipoangalia aliona ni ya mpenzi wake. “Haloo sweet.” “Haloo darling.” “Niambie mpenzi wangu.” “Vipi upo tayari?” “Ooh, sorry nilikuwa na mazungumzo na shemeji kidogo yamechukua muda ngoja nijimwagie maji.” “Fanya haraka nakuja sasa hivi.” Baada ya kusema vile alielekea chumbani kwake kubadili nguo akaoge ili atoke na mpenzi wake. Usiku wa siku ile walipanga kwenda kwenye kumbi za starehe, Kinape toka awe na mpenzi wake mpya amekuwa akionjeshwa raha za duniani ambazo hakuwahi kuziota. Alipokuwa akielekea chumbani kwake, Kilole alimsindikiza kwa macho huku moyoni akisema “nitakomesha jeuri yake.” Akiwa bado yupo katika hali ya uvivu kutokana na maneno ya Kinape yaliyomkata maini. Alishtushwa na sauti ya Happy mpenzi wa Kinape akiwa katika vazi la kutokea jioni. “Aah, dada kumbe upo sebuleni, ina maana husikii hodi yangu?” “Aah! Kumbe ni wewe nilikuwa mbali kimawazo.” “Dada, shemeji kuondoka asubuhi tu umekuwa hivyo, je, akimaliza wiki?” “Wee acha mdogo wangu, nawe utaolewa utayaona.” “Ahaa! Umeishafika?” Kinape alisema akiwa anatoka bafuni. “Niliona unachelewa nikaamua nikufuate, si unajua mtu chake.” “Na kweli mdogo wangu,” Kilole alijibu huku roho ikimuuma. “Hongera umependeza,” Kinape alimsifia Happy. “Nawe nataka upendeze kama mimi, vaa nguo nilizokununulia.” “Hakuna tatizo dear nipe nusu dakika.” “Aah, wapi nakuja huko huko.” Waliongozana wote hadi chumbani huku Happy akiwa amemkumbatia Kinape. Kilole alijua Kinape amefanya vile kumuumiza roho, lakini aliapa kumshikisha adabu huku akipanga mpango kabambe wa kusambaratisha penzi lile. Baada ya muda walitoka wakiwa wameongozana katika mtembeo wa mapenzi mazito. Kilole aliwasindikiza kwa macho huku roho ikizidi kumuuma jinsi walivyopendana. Alijua maisha yale hakuna sehemu ya kuyapata zaidi ya kuwa na Kinape. Toka aolewe na Deus hakuwahi kwenda sehemu za starehe zaidi ya kwenda kwenye dhifa ya kiserikali. Lakini mashoga zake walimweleza raha wanazozipata wanapokwenda kwenye kumbi za starehe hata kwenye vikundi vya taarabu. Moyoni alijisemea: Leo mjanja lakini ipo siku utanijua mimi na yeye nani zaidi.”
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kilole akiwa na mpango mzito moyoni mwake ambao aliujua yeye na Mungu wake, ili kuufanikisha alionesha ukaribu na mpenzi wa Kinape kitu kilichomziba macho Kinape kwa kuamini Kilole amekubaliana na alichomueleza *****
Maisha yaliendelea kama kawaida kwa Kilole naye kumtembea mchumba wa Kinape kuonesha ukaribu. Hali ile iliongeza mapenzi kwa Kinape kuona hali ipo shwari bila kujua kuna bomu zito limepangwa dhidi yake ya kulisambaratisha penzi lake. Wakati huo Kinape alikuwa katika hatua za mwisho kumpeleka happy kijijini kutambulishwa kwa wazazi wake. Kilole alipanga kutekeleza mpango kabla ya Kinape hajampeleka Happy kijijini, aliamini kama atachelewa itakuwa vigumu kuutekeleza mpango wake. Matumaini ya kutekeleza mpango wake yalikuwa makubwa baada ya kupewa na taarifa na mumewe ana safari ya kikazi nje ya nchi kwa siku tano. Siku ilipofika ya mumewe kusafiri ilikuwa tofauti na siku zote, Kilole alionesha kumhitaji mumewe kuliko kipindi chochote kilichopita.
“Mke wangu siku tano si nyingi,” Deus alimtuliza mkewe aliyekuwa akilia.
“Kwako si nyingi lakini kwangu naona kama miaka mitano,” Kilole alidondosha machozi ya uongo.
“Najua basi nitajitahidi safari nyingine tusafiri pamoja.”
“Itakuwa afadhari.”
“Kinape kuwa karibu na shemeji yako hata ukiwa mbali na nyumbani mpigie simu ili asipate upweke.” Deus alimweleza rafiki yake.
“Deus si mpo kwenye Facebook twitter instagram usiku tumieni kuliwazana ili usijione mpo mbali mbali,” Kinape alitoa wazo ili ajiweke mbali na Kilole.
“Na kweli mke wangu, kila baada ya kazi nitakuwa pamoja na wewe katika kuchati.”
“Lakini si sawa na wewe kuwa pembeni ya ubavu wangu,” Kilole alilia wivu wa uongo.
“Basi mke wangu niombee niende salama nirudi salama, si unajua kazi zetu.”
“Na ukirudi utimize ahadi ya kuninunulia gari langu,” Kilole alisema kwa sauti ya kideka.
“Kila kitu kipo tayari, subiri nikufanyie Surprise.”
“Waawoo mpenzi wangu.” Kinape alijikuta akifurahi furaha ya kweli baada ya kuona ndoto yake ya siku moja kuendesha gari lake mwenyewe inatimia. Alimkumbatia mumewe na kumtakia safari njema.
“Dear usafiri salama na urudi salama, ukiwa mbali kumbuka umeniacha kama kinda la ndege linalomsubiri mama yake aliyekwenda kutafuta chakula.”
“Hilo nalijua, nataka mpenzi wangu na mwanangu muishi maisha nusu ya peponi.” “Asante mume wangu.
” Kilole aliagana na mumewe na kurudi nyumbani na Kinape katika gari moja, wakiwa njiani Kinape alimchokoza.
“Ona ulitaka kupoteza bahati yako bure, haya ndiyo mapenzi unayotakiwa kuyapigania.”
“Kinape yale yalikwishapita achana nayo.
” Walirudi wote mpaka nyumbani, walipofika Kinape hakukaa aliaga na kwenda kuonana na mpenzi wake kitu ambacho Kilole hakupenda kukisikia.
*****
Kilole akiwa peke yake aliamini mpango alioupanga Kinape hawezi kuruka, alichukua simu yake na mkononi na kutafuta jina la mtu, kisha alipiga na kuiweka sikioni kusikiliza. Baada ya kuita kwa muda ilipokelewa upande wa pili.
“Haloo Sisiter.”
“Haloo Jimmy.”
“Ndiyo Sister lete stori, naona leo umenikumbuka.”
“Mambo mengi mtu wangu, upo pande zipi?”
“Ndiyo nafika kijiweni, ulikuwa unasemaje? Najua wito wako lazima nidake vumba nene.”
“Unaweza kuja nyumbani mara moja?”
“Hakuna tatizo.” “Basi njoo mara moja.”
“Okay, nakuja.”
Kilole alikata simu na kutabasamu mwenyewe huku akijisemea moyoni: “Kinape hana ujanja japo mjini aliwahi lakini mimi ndiye mwisho wa matatizo lazima arudi mikononi mwangu na uchumba wake ubakie hadithi.”
Kengele ya mlangoni ilimuondoa kwenye mawazo na kumfanya ananyuke kwenda kufungua.
“Ooh! Jimmy, karibu.”
“Asante Sister.”
Baada ya Jimmy kuingia alikaa kwenye kochi la watu watatu, Kilole alikaa kwenye kochi la mtu mmoja. Kwa vile Jimmy alikuwa mbali na Kilole, alimuomba asogee kochi la karibu.
“Jimmy, njoo ukae kwenye kochi hili.”
Jimmy alinyanyuka na kwenda kukaa karibu yake, Jimmy alionekana mtu mwenye wasiwasi sana.
“Jimmy mbona hivyo?”
“Mmh! Jinsi tulivyokaa mumeo akitokea inaweza kuwa msala.” “Kwani hajui kama wewe mpiga picha?”
“Anajua, lakini naona kama tumekaa karibu sana.”
“Wasiwasi wako kwanza mume wangu kasafiri.”
“Na mdogo wake?”
“Ametoka na hawezi kurudi sasa hivi.”
“Haya sister nipe dili basi.”
“Kuna kazi nitakupa uifanye, ukiifanya vizuri nitakupa pesa nzuri sana ambayo hukuwahi kuipata toka ulipoanza kazi ya kupiga picha.” “Kazi gani hiyo dada?”
“Ya kupiga picha.”
“ Mmh! Ni kazi ipi, mbona kama naona kama si ya kawaida?”
“Ni kweli, hii itakuwa siri yako na malipo yatakuwa mazuri.”
“Kazi hiyo itakuwa lini?”
“Ikiwezekana leo hii.”
“Poa basi ikiwa tayari nishtue.”
“Jimmy, naomba usifanye kazi yoyote kuanzia sasa hivi, nitakulipa pesa ya usumbufu na kazi ikikamilika nitakupa fedha nzuri sana.”
“Hakuna tatizo sister, nakuamini dada yangu wa ukweli.” “Nisubiri,” Kilole alinyanyuka na kwenda chumbani, baada ya muda alirudi na elfu 50 na kumpa Jimmy.
“Hii ya usumbufu, ya kazi bado.”
“Asante Sister.” Jimmy alipokea na kutoka akimwacha Kilole akifurahia mpango wake, alichukua simu yake na kumpigia Kinape. Baada ya simu kuita kwa muda Kinape upande wa pili aliipokea.
“Haloo Shemu.”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Kinape upo wapi?”
“Nipo na mke mwenzio hapa.”
“Waawoo! Nimeipenda hiyo,”
. “Kweli?” Kinape alimuuliza.
“Kweli, inafurahisha, mmeonesha jinsi gani mnavyo pendana.” “Ndiyo shemeji yangu, una lipi tena?”
“Nimesahau kukujulisha kuwa leo ni siku yangu ya kuzaliwa.” “Wawooo, mbona hukuniambia mapema nikuandalie zawadi?” “Nilipitiwa lakini jioni kutakuwa na sherehe fupi ya kifamilia.” “Hakuna tatizo nitakutafutia zawadi nzuriii shemeji yangu.” “Nitashukuru, uje na Happy.”
“Hakuna tatizo.”
Baada ya kuzungumza na Kinape, alimpigia simu mtengeneza keki ili amuandalie keki ya birthday, ambaye aliwahi kumtengenezea mwanaye alipotimiza mwaka mmoja.
“Sakina ninaweza kupata keki ya birthday?”
“Lini shoga?”
“Leo hii jioni.”
“Jamani! Mbona haraka, ya nani?”
“Yangu mwenyewe.”
“Jamani shoga! Mbona hukunialika?”
“Kwani mimi? Shemeji yako ndiye kasema akirudi jioni akute keki, mwenyewe nilikwisha sahau kama leo siku yangu ya kuzaliwa,” Kilole aliunda uongo unaofanana na kweli. “Kwa hiyo jina lako ni lilelile?”
“Lipi hilo?”
“La Kilole?”
“Hilohilo mpenzi.”
“Basi hakuna tatizo nipe saa mbili kila kitu kitakuwa tayari.” “Nitashukuru.” Baada ya kuachana na mtengeneza keki, alikumbuka kitu muhimu kilichotakiwa kiwepo pale ili kufanikisha mpango wake. Alimpigia simu mpiga picha, simu iliita kwa muda kisha ilipokelewa upande wa pili.
“Oya, sister mambo tayari?”
“No, kuna kitu nataka kukutuma kabla ya kazi yetu.”
“Kitu gani hicho?”
“Eti kete ya unga shilingi ngapi?”
“Unga upi?”
“Kokeni, sijui heloin.”
“Una maanisha madawa ya kulevya?”
“Ndiyo.”
“Mmh! Ya nini?”
“Jimmy, utajua baadaye.”
“Sijajua bei yake, lakini sidhani kama inazidi elfu tano kwa kete.” “Basi njoo uchukue fedha ukaninunulie kete mbili.”
“Sister unajidunga nini?”
“Jimmy, kazi itakushinda.”
“Basi Sister nakuja.”
Baada ya muda mfupi alifika na kupewa elfu ishirini akanunue kete mbili za unga. Alitoka na kumwacha Kilole akiendelea na maandalizi ya mipango yake ambayo ilikuwa siri yake na Mungu wake.
Alimtuma mlinzi kununua vinywaji ambavyo alivijaza kwenye friza, kila kitu kilikwenda kama kilivyopangwa. Kilole baada ya kuridhika na mipango yake kwenda vizuri alijiandaa kuisubiri keki ili akamilishe zoezi lake.
Baada ya saa mbili kama alivyoahidia alijulishwa kuwa keki tayari, kwa vile hakutaka kutoka alimuomba mpelekewe. Sakina alimletea keki baada ya nusu saa, wakati huo mpiga picha alikuwa amefika na kumpa kete mbili za unga.
“Asante Jimmy, kwa kazi hii nitakupa posho elfu kumi, ila kuna kazi nyingine unatakiwa kuifanya.”
“Ipi hiyo?”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Nitakupa namba hii nikikubip ipige, akipokea mwambie anatakiwa kwao haraka sana kuna matatizo.”
“Sawa.”
“Hakikisha unakaa mkao wa kazi usicheze mbali nakutegemea wewe ndiye steling wa picha.”
“Hakuna tatizo sister.”
“Jimmy ukiifanya kazi kwa ufanisi nitakupa laki mbili.”
“Utani huo sister!”
“Sina utani kwa jambo nitakalo kuahidi.”
“Sawa, wacha nikuache uendelee na mambo mengine.”
Jimmy aliondoka na kumuacha Kilole akitengeneza nyumba kwa ajili ya sherehe ya kutengeneza ya birhtday yake. Sebule aliipamba na kupambika ikawa katika muonekana wa kupendeza.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment