Search This Blog

Sunday, July 10, 2022

SIKUJUA UNGENISALITI MPENZI - 2

 





    Simulizi : Sikujua Ungenisaliti Mpenzi

    Sehemu Ya Pili (2)



    Ni mwanamke wa aina gani? Si kwamba ni vigumu mambo haya kufanyika, lakini kuwe na uhusiano mwema basi baina ya watu hawa wawili! Lakini ndiyo kwanza wanafahamiana, tena hapo hapo hospitalini! Lakini kubwa zaidi, ni kwamba, tayari Bruno anaonekana kuwa na tofuati na mjomba wake Vanessa, tofauti ambayo bado Vanessa hajaijua!

    Anawezaje?

    Bruno akamwangalia kwa jicho la kuhitaji huruma yake, ambaye naye alijibu kwa jicho la kupokea huruma hiyo. Kama ndoto ya mchana, tabasamu changa likachanua usoni mwa Bruno, Vanessa akajibu!

    Kama ungefanikiwa kuwaona, usingekuwa na mashaka kwamba wale walikuwa wapenzi. Haikuwa hivyo! Walikuwa marafiki tu, tena wasio na umri mrefu. Hata mwezi hawana. Tena wana ugomvi uliosababishwa na mjomba wake Vanessa.

    “Bruno...” hatimaye Vanessa akaita.

    “Vanessa!” Bruno akaitikia kivivu akionesha kudeka kidogo.

    “Kwanini una mawazo sana?”

    “Matatizo Vanessa, matatizo.”

    “Lakini siku zote, matatizo huwa hayakimbiwi Bruno, ni kuyakabili tu. Kwanini unakuwa mwoga wa kukabiliana na matatizo?”

    “Siyo woga!”

    “Bali nini?”

    “Lazima uwe na hofu na jambo ambalo hujui mwisho wake Vanessa.”

    “Najua Bruno, lakini si kwa kiwango ambacho wewe unayachukulia matatizo yako.”

    “Kwanini unasema hivyo?”

    “Mambo mengi sana, unayachukulia kwa ukubwa. Kama unakumbuka, siku ya kwanza kukutana na wewe nilikuambia najua unadhani huna thamani tena kutokana na tatizo lako.

    “Unajiona huwezi kuwa na marafiki tena, huwezi kupata mtu wa kukujali, huwezi kukubalika, huwezi kupendwa. Huwezi kuwa na sauti na kadhalika lakini nataka kukuambia kwamba unawaza tofauti sana, kila kitu kinawezekana na unaweza kuondoa fikra hizo kichwani mwako ukawa Bruno mpya kabisa...” sauti ya Vanessa ilikuwa tulivu, ambayo aliitoa kwa mpangilio unaofaa.

    “Ahsante sana Vanessa kwa kunipa moyo, kuanzia sasa naanza kuwaza upya.”

    “Nimefurahi sana kusikia hivyo. Ok! Vipi hali yako sasa?”

    “Dokta amepita round, ameniruhusu!”

    “Hongera, nyumbani ni wapi?”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Sina.”

    “Huna mahali pa kukaa?”

    “Ndiyo Vanessa.”

    “Kwanini?”

    “Sina nyumba hapa Dar.”

    “Ndugu?”

    “Sina!”

    “Anyway, mambo mengine tutazungumza baadaye, lakini kwasasa hebu tumalize kwanza hili suala la makazi. Naomba nikusaidie kwa mara nyingine Bruno.”

    “Nitashukuru sana.”

    “Nitakutafutia sehemu ya kuishi kwa muda, ukipata huduma zote, halafu baadaye nitajua cha kufanya.”

    “Sawa.”

    “Nimefurahi sana Bruno, sasa amka upate mtori kwanza, halafu nitakuacha kwa muda ukiendelea kukamilisha taratibu za discharge ili nikaandae mazingira then nije nikuchukue.”

    “Sawa.”

    Bruno akainuka na kukaa kitako. Vanessa akamimina mtori na kuanza kumnywesha. Taratibu Bruno akawa anakunywa mpaka akashiba kabisa! Akamenya machungwa mawili na kumpa, akala na kumaliza.

    “Good! Ukiwa na bidii ya kula hivi, uta-recover mapema zaidi.”

    “Usijali Vanessa, kwenye kula wala usiwe na wasiwasi, mimi ni mkali sana kwenye eneo hilo!”

    Wakacheka pamoja!

    “Acha basi mi’ niondoke, ndani ya saa moja nitakuwa nimesharudi, halafu tutaondoka.”

    “Sawa.”

    Vanessa akatoka wodini na kwenda alipoegesha gari lake, akaingia na kuwasha. Safari yake iliishia Manzese Tip Top, alipotafuta hoteli nzuri na kupanga.

    “Hiki chumba ni kwa ajili ya ndugu yangu, mgonjwa. Nahitaji apate huduma zote akiwa hapa, nitakuwa nakuja kumwangalia kila siku, lakini ningependa kama angekuwa anapewa uangalizi wa karibu zaidi,” Vanessa akamwambia dada aliyekuwa mapokezi.

    “Kama vipi yaani!”

    “Huduma muhimu, chakula, kufuliwa nguo n.k.”

    “Hilo halina tabu, kama utanitoa itakuwa poa!”

    “Kuhusu hilo, weka shaka pembeni, utafurahi. Sasa vipi ukiwa haupo?”

    “Nitaacha maagizo kwa nitakayemuacha, naye nitamkatia chake mapema, kwahiyo atakuwa anafanya kama mimi, kifupi usiwe na shaka, atakuwa salama!”

    “Nimefurahi sana kusikia hivyo, acha nikamchukue!”

    “Ok!”

    Vanessa akaondoka zake.

    ***

    Vanessa alimkuta Bruno akiwa ameshakamilisha taratibu zote na alikuwa akimsubiri yeye! Bruno akampokea kwa tabasamu changa, lakini Vanessa akajibu kwa tabasamu lililochanua. Akamshika mkono, kisha Bruno kwa msaada wa gongo, akaanza kupiga hatua fupi fupi kuelekea gari lilipoegeshwa.

    Vanessa alikuwa ameshika gongo moja na kumuachia Bruno moja, wakatembea taratibu sana. Watu waliowaona, waliweza kugundua upendo wa ndani kwa ndani walionao wawili hawa! Taratibu wanakwenda mpaka kwenye gari!

    Vanessa akampandisha na kuyaweka magongo yake siti ya nyuma, akawasha gari na kulitoa getini taratibu. Alipofika barabarani, akakata kushoto akiifuata barabara inayokwenda kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.

    Kwenye mataa ya Barabara ya Kawawa, akakata kushoto kuelekea Magomeni, alipofika kwenye mataa ya Usalama, akapinda kushoto, kuishika Barabara ya Morogoro hadi Tip Top, ambapo aliingia kushoto kwenye kituo kidogo cha daladala, akaifuata Barabara ya Kione.

    Hapo akakatiza mitaa miwili mitatu na kuegesha gari lake nje ya hoteli. Akamsaidia Bruno kushuka na kutembea naye pole pole hadi Mapokezi.

    “Huyu ndiyo yule mgeni wangu.”

    “Ok! Karibuni sana. Ni ghorofa ya nne, chumba namba 502. Ngoja nikusaidie tumpelekea mgonjwa!” Yule dada wa Mapokezi akajibu akitabasamu.

    Akatoka na kusimama kushoto mwa Bruno, Vanessa akasimama kulia, kisha wakakutanisha mikono yao, Bruno akakaa katikati, wakapandisha ngazi hadi ghorofa ya nne!

    Wakaingia chumbani na kumkalisha kitandani, yule dada wa Mapokezi akarudi zake ofisini kwake, chumbani wakabaki Bruno na Vanessa. Vanessa akiwa amechoka kabisa, Bruno akiwa ametulia kitandani akimwangalia Vanessa.

    “Lakini kwanini unafanya yote haya Vanessa?” Bruno akauliza kwa utulivu sana.

    Lilikuwa swali muafaka kwa Vanessa lakini gumu kujibika! Ni kweli alikuwa na sababu ya kufanya yote yale kwa Bruno. Mwanzoni hakujua, lakini tayari ameshajua, kwamba anafanya yote kwa sababu ndani yake kulikuwa na mzigo mzito wa mapenzi!

    Hilo alilijua!

    Ndiyo ukweli wenyewe!

    Lakini atasemaje?

    Akabaki anamwangalia bila kujibu neno, ingawa kwa mbali, macho yake yalikuwa yanatoa majibu. Majibu mazito. Kwamba anampenda, lakini domozege!

    Hisia za moyo wake zilishamhakikishia kwa asilimia mia moja kwamba, anampenda sana mwanaume huyu. Mwanaume huyu ambaye yupo mbele yake akisubiri jibu la swali alilomwuliza; kwanini anamfanyia wema wote ule?CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Alitakiwa kutoa jibu moja jepesi sana....kwamba anafanya yote yale kwasababu ndani yake kuna mapenzi ya dhati, lakini Vanessa hawezi na amejikuta akishindwa kabisa kutoa jibu la swali hilo lililomchanganya kidogo.

    Bado Bruno ameyatuliza macho yake usoni mwa Vanessa na alichokuwa anasubiri ni jibu tu!

    “Niambie basi,” Bruno akaomba.

    “Kwanini umeniuliza hivyo Bruno?”

    “Sina nia mbaya, nataka kujua tu!”

    “Kila kitu kina sababu Bruno, najua hata wewe una sababu za kuuliza hilo, hebu niambie ni nini?”

    “Umenifanyia mambo makubwa sana, umekuwa muungwana mno kwangu, lazima nihisi huenda kuna sababu.”

    “Kama ipi Bruno?”

    “Sijui.”

    “Bruno.”

    “Nakusikia Vanessa.”

    “Hakuna sababu kubwa sana, lakini lazima utambue kwamba wewe ni binadamu mwenzangu, moyo una nyama Bruno...hivyo nilivyokuona upo katika mateso, sikupenda, nikaona ni vyema kukusaida. Sidhani kama kuna sababu kubwa zaidi ya hiyo...” Vanessa akasema akionekana wazi kabisa kuacha sababu nyingine ya msingi zaidi nyuma ya maneno yale.





    “Kama ndivyo nashukuru, lakini nina swali nataka kukuuliza.”

    “Uliza tu.”

    “Uliona tafrani kidogo kati yangu na mjomba wako?”

    “Ndiyo!”

    “Unahisi kuna nini kati yetu?”

    “Sijui!”

    “Alipata kukuambia chochote?”

    “Hapana.”

    “Najua hawezi kukuambia!”

    “Kwanini?”

    “Tuachane na hayo, lakini hujachukia au kukwazwa na jinsi ambavyo hatuna maelewano, ingawa hujajua ni nini?”

    “Hapana, siwezi kuumizwa na kitu ambacho sikijui, ingawa najua kipo. Unaweza kuniambia?”

    “Ndiyo!”

    “Ni nini?”

    “Si leo. Tunahitaji muda zaidi!”

    “Hapana, tafadhali naomba uniambie leo.”

    “Nitafurahi sana kama utaheshimu hili, naahidi kukuambia, lakini si leo. Muda ukifika nitakujulisha, shaka ondoa.”

    “Hapana, nataka uniambie leo.”

    “Leo haitawezekana.”

    “Kwanini isiwezekane?”

    “Nina sababu zangu, lakini naomba uwe mvumilivu, muda ukifika nitakuambia.”

    “Naona sasa hatutaelewana, kwanini wewe unakuwa msiri sana? Hutaki nijue mambo yako, kuna nini?”

    “Kwa hili, nipo tayari kwa lolote Vanessa, lakini sitakuambia.”

    “Lakini una nini?”

    Bruno hakujibu kitu!

    Machozi yakaanza kumtoka machoni!

    ***

    Wakati anashuka kwenye basi katika Kituo Kikuu cha Mabasi ya Mikoani jijini Tanga, akitokea Arusha, mvua kubwa ilikuwa ikinyesha. Mbaya zaidi simu ya mpenzi wake Tunu ilikuwa haipatikani. Mara ya mwisho aliwasiliana naye akiwa Hale, akimuahidi kwenda kumpokea stendi.

    Aliposhuka aliangaza macho huku na huko lakini hakumuona. Akajaribu kumpigia kwa mara nyingine tena, lakini bado jibu lilibaki kuwa lile lile, haipatikani! Akachanganyikiwa kidogo. Alikuwa na haki ya kuchangangikiwa, maana ilikuwa usiku, halafu sehemu aliyokuwa akiishi Tunu mwanzo Mabawa alikuwa amehama na alipohamia hakupafahamu.

    Ilikuwa saa 4:25 hivi za usiku, mvua ikianza kupungua kidogo na kuwa manyunyu, akachepuka kidogo na kuifuata taxi iliyokuwa mbele yake na kuingia akijikinga na mvua.

    “Wapi kaka?” Dreva taxi akamwuliza.

    “Sikumbuki vizuri eneo, lakini ni Chuda, kuna Gesti moja nzuri sana niliwahi kulala pale. Ndipo ninapotaka kwenda,” Bruno akajibu akiwa na mashaka kidogo.

    “Chuda?”

    “Ndiyo.”

    “Naijua sehemu unayosema, kuna eneo moja lina Gesti nyingi sana, lakini nzuri zaidi ni Flowers Hotel.”

    “Hiyo hiyo.”

    “Ok! Twen’zetu!”

    Dereva akaingiza gia na kuondoa gari taratibu. Dakika mbili tu, ikiwa ndiyo kwanza wanazunguka kutoka eneo la kituo cha mabasi, simu ya Bruno ikaita, alipotazama namba kwenye kioo, ilikuwa ngeni. Akaamua kupokea.

    “Nani mwenzangu?” Ndiyo neno la kwanza Bruno kuongea.

    “Tunu!”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Tunu?”

    “Ndiyo Tunu, samahani mpenzi, simu yangu imeisha charge ghafla, upo wapi?”

    “Ndiyo natoka stendi, nipo kwenye taxi naelekea Gesti.”

    “Sikia, mwambie huyo dereva wako akulete Nguvumali, akifika Denare Hotel, asimame hapo ni jirani na nyumbani nilipohamia, unijulishe.”

    “Sawa, nakuja sasa hivi.”

    Bruno akamgeukia dereva wake na kumpa maelekezo aliyopewa, dereva akageuza gari na kuondoka. Muda mfupi baadaye walikuwa nje ya Hoteli ya Denare. Bruno akashuka na kumlipa dereva, akaingia mle hotelini. Alipotulia akatoa simu yake na kumpigia Tunu.

    “Umeshafika hapo?”

    “Siyo kufika tu nimeshashuka, nimeingia humu hotelini.”

    “Nakuja mpenzi wangu.”

    Bruno akaagiza kinywaji akiwa na shauku kubwa ya kukutana na mpenzi wake Tunu. Hakuchelewa, akafika haraka na kuondoka naye hadi kwenye makazi yake mapya. Alipofika tu na kukaa kwenye kochi, Bruno akaonekana kuwa na mawazo sana. Tunu akagundua tofauti hiyo na kumuuliza...

    “Vipi baby, mbona kama una mawazo?”

    “Ni kweli, bado nafikiria sana kama ni kweli hunisaliti mpenzi wangu nikiwa sipo. Hivi huna mpenzi yeyote kweli baby?!”

    “Bruno acha wivu dear, utakufa kwa presha.”

    “Kweli?”

    “Mmmmh!” Tunu akaitikia kimahaba na kumsogelea Bruno aliyekuwa hoi kwenye kochi.

    Akambusu na kuamsha hisia zake zilizokuwa zimejificha. Kilichofuata ilikuwa ni kuanza kufungua vishikizo vya shati na kumuamuru avue nguo zote. Bruno akatii. Akampa taulo na kumwongoza bafuni. Akamwogesha!

    ***

    “TUNU NOOOO...” Bruno akasema kwa sauti kuu akizidi kulia.

    Vanessa akashindwa kuelewa Bruno alikuwa na tatizo gani, ni mara ya pili sasa anataja jina la Tunu na kila anapomwuliza, anakuwa hana jibu la maana. Tunu akazidi kumchanganya.

    Vanessa akayatuliza macho yake usoni mwa Bruno akiwa na simanzi tele moyoni, ni mwanaume ambaye moyo wake ulikubali kumuhifadhi katikati ya kiota cha huba. Kuona machozi yake ilikuwa ni kidonda kibichi kabisa. Hakutaka kukiona kikiendelea kutoa maji!

    Alitamani sana kipone!

    Akamwangalia Bruno kwa macho yanayozungumza, tena kwa uwazi sana. Kwamba alikuwa akiteswa na matatizo aliyokuwa nayo. Kwamba alikuwa akiumia sana na jinsi ambavyo hataki kuwa mkweli juu ya huyo Tunu ambaye alikuwa akimtaja kila siku. Vanessa aliumia sana.

    “Lakini Bruno una nini?”

    “Acha tu!”

    “Kwanini?”

    “Vanessa kama ni kweli unatamani niishi kwa furaha naomba tuache kuzungumza juu ya hili!”

    “Napenda sana uishi kwa furaha Bruno, ndiyo maana nafanya yote haya kwa ajili yako. Tafadhali naomba uniambie tatizo ni nini, unajua hakuna kitu kibaya kama kukaa na kitu kichwani na kukitolea maamuzi peke yako, unaweza kufanya maamuzi mabaya sana, kwahiyo ni vyema ukaniambia ili tushirikiane pamoja, tafadhali Bruno naomba uniambie!”

    “Vanessa, Tunu ni mwanamke mbaya sana. Ni adui namba moja katika maisha yangu.”

    “Kivipi?”

    “Na namba mbili ni Bryson!”

    “Bryson?”

    “Ndiyo!”

    “Mjomba’ngu?”

    “Off course!”

    “Ok! Niambie basi wamekufanyia nini?”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Umeshawahi kusikia jina la Tunu?”

    “Hapana.”

    “Basi kwa leo tuishie hapa na naomba sana iwe hivyo kweli, nakuahidi kuzungumza na wewe siku nyingine!”

    “Kweli?”

    “Niamini.”

    “Poa.”

    Mazungumzo yakahama, wakaanza kuongelea mambo mengine kabisa. Jioni, Vanessa akaaga na kwenda zake nyumbani. Akamwacha Bruno mwenyewe hotelini.

    ***

    Ni saa 4:45 za usiku, macho yake kwa mbali yalianza kuwa mazito, lakini hakutaka kulala. Kichwani aliendelea kusumbuliwa na kijana Bruno. Ni mara nyingi sana alijiuliza sababu za kumpenda Bruno, lakini hakuzijua.

    Alikuwa mwanaume asiyejiweza, hana fedha na anayemtegemea kwa kila kitu. Kubwa zaidi alikuwa mlemavu!

    Haina maana kwamba mlemavu hana haki ya kupendwa, lakini huyu hakuwa mlemavu kabla. Amepata kilema baada ya ajali, tena akiwa amemkuta hospitalini amelazwa, alijihoji mwenyewe kwa muda mrefu sana, lakini jibu alilolipata ni kwamba alikuwa akimpenda sana Bruno.

    “Lakini nitaanzaje kumwambia?” Anawaza Vanessa akikosa majibu.

    “Anyway, labda naweza, lakini vipi kuhusu huyo Tunu? Kwanza ni nani na ilikuwaje wakawa hawana maelewano mazuri na Anko? Hapo napata na maswali ambayo hayana majibu ya kuridhisha, lakini naamini kama nikiendelea kuwa karibu na Bruno ataniambia ukweli...” anawaza Vanessa.

    Akiwa bado yupo kwenye lindi la mawazo, simu yake inaita. Anaichukua na kutazama kwenye kioo, jina linalotokea ni la mpenzi wake Emma. Anasita kupokea na kuitupa simu pembeni. Simu inaendelea kuita mpaka inakatika!

    Baada ya muda inaanza kuita kwa mara nyingine tena. Vanessa anaiangalia kwa muda na kuachana nayo. Iliendelea kuita zaidi ya mara tano, hakupokea. Ilipokatika, akaizima kabisa na kuiweka kwenye chaji, akazima taa na kujilazimisha kulala.

    Kiasi cha nusu saa mbele, akasikia geti likigongwa na honi kwa fujo, akajua kwa vyovyote vile atakuwa ni Emma. Hakujigusa. Lakini baada ya muda mfupi akasikia muungurumo wa gari likiingia ndani, kumbe msichana wake wa kazi alikwenda kumfungulia. Baada ya muda, Emma alikuwa chumbani kwake akiwa amefura!

    “Umeshamtoa huyo mwanaume wako?” Emma akauliza akionekana kuwa mkali sana.

    “Mwanaume gani?”





    Emma hakuongea kitu, akamzaba kibao cha nguvu kilichotua vyema usoni mwa Vanessa.

    “Lakini kwanini unanipiga? Kwanini unaninyanyasa? Kwanini unanitesa kiasi hicho? Kwani nimekukosea nini hadi unipe adhabu kubwa kiasi hicho? Kwani mimi ni ngoma? Mbona unaninyima raha?” Vanessa alisema akilia.

    “Huo umalaya wako hautakusaidia kitu we’ mwanamke. Haya kwanini ulikuwa hupokei simu yangu?”

    Vanessa hakujibu!

    Emma akafungua mkanda wake kiunoni na kuanza kumchapa nao Vanessa, Emma hakuwa na huruma kabisa. Alimpiga mpaka aliporidhika akaacha na kuvaa mkanda wake.

    “Nitakuua wewe mwanamke, unaleta tabia zako za kimalaya hapa? Nitakuja kukuua siku moja, mimi siyo wa kuchezewa...” Emma akasema na kubamiza mlango kwa nguvu.

    Kitambo kidogo, mlio wa gari ukasikika nje, alikuwa anaondoka zake.

    Vipigo vya Emma vimekuwa vikimnyima raha kabisa Vanessa, pamoja na mapenzi yake yote, lakini alijikuta akianza kumchukia. Emma hakuwa na mapenzi ya kweli, siku zote alimfanya Vanessa ngoma, jambo ambalo lilimuumiza sana.

    “No, muda wa kuachana naye umefika. Kuanzia sasa simtaki tena Emma na kinachofuata ni kuhakikisha Bruno anakuwa hapa. Lazima iwe hivyo, lazima...” akawaza Vanessa moyoni mwake huku akilia kwa uchungu.

    Akavuta shuka na kujifunika, akisaka usingizi. Alikuwa mchovu sana, mchovu wa vitu viwili; pilika-pilika na mapenzi!

    ***

    Kila alipogeuza macho yake na kutazama meza ya jirani yake, jicho la mwanamke yule mrembo liliendelea kumkodolea. Jicho lenye uzuri wote wa kike. Lililopambwa kwa wanja na kila aina ya vikorombwezo! Jicho lililochongwa nyusi vyema na kulifanya lizidi kuvutia!

    Mbali na yote, lilikuwa legevu kama linataka kuanguka. Bruno hakuzoea macho ya aina hiyo, Mwanza hakuna macho ya aina hiyo. Pamoja na kuwa mzaliwa wa Mwanza, lakini alitembelea sehemu nyingi kikazi, ila jicho lile hakukutana nalo.

    Si Mwanza, Moshi, Arusha, Dodoma, Mombasa, Shinyanga, Iringa, Mbeya na mikoa mingine yote, hakukutana na jicho lile. Leo hii anakutana nalo Tanga! Moyo ukamzizima! Akashawishika kuzidi kuliangalia, lakini alifanya hivyo kwa kuibia!

    Hakutaka kuonekana wakuja, akalitizama kwa kujificha kwa mtindo wa siri yake. Akiwa ameyarudisha macho yake kwa marafiki zake, akamwona Mhudumu anakuja mpaka alipokuwa amekaa. Akamkabidhi karatasi na kumwonesha yule msichana aliyekuwa akimwangalia kwa jicho lake tamu!

    “Nimepewa na yule dada pale,” yule Mhudumu akasema akisonza kidole kwa yule dada.

    Kile ki – memo hakikuwa na maneno mengi. Kiliandikwa hivi; Karibu sana Tanga. Kama hutajali, ningependa niwe mwenyeji wako. Namba zangu ni 0841 17074512. Tunu.

    Moyo wake ukapasuka, akageuza macho yake na kumtazama yule msichana. Akampokea kwa tabasamu pana. Tabasamu mwanana. Tunu alikuwa tunu kweli, tabasamu lake likamwongezea uzuri wake.

    Tunu toto la Kitanga!

    Bruno hoi!CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    ***

    Kuachana na Emma ndiyo wazo alilolala nalo Vanessa, pia wazo hilo hilo aliamka nalo kichwani mwake. Hakutamani kabisa kuwa na Emma, mwanaume mkorofi, anayempiga kila siku, anayemnyanyasa, anayemuonea! Hakuwa na thamani tena katika maisha yake.

    Aliapa kumuacha!

    “Lazima niachane naye, lazima,” akatamka kwa sauti ya chini akionekana kuwa na uchovu mwingi wa usingizi.



    Mara moja, akachukua simu yake iliyokuwa mezani, kisha akabonyeza jina la Bruno haraka. Alitamani sana kuzungumza naye, akiamini angekuwa msaada mkubwa wa mawazo tele aliyokuwa nayo kichwani mwake. Muda si mrefu, sauti ya upande wa pili ilisikika; alikuwa ni Bruno akiongea kwa sauti ya taratibu.

    “...umeamkaje Bruno?”

    “Salama, vipi wewe?”

    “Sijambo kabisa.”

    “Yeah, ndiyo nimeamka muda huu, nikafikiria naweza kufanya kitu gani kama cha kwanza kwa leo, nikaona bora nikupigie wewe, nikusalimie, hili ndiyo jambo nililoamua kulifanya la kwanza kwa leo.”

    “Nashukuru sana Vanessa, naweza kukuuliza jambo?”

    “Yeah!”

    “Kwanini umenichagua mimi kuwa wa kwanza kuanza ratiba zako za leo?”

    “Tupo karibu Bruno, sisi ni marafiki wakubwa sasa, marafiki wa karibu sana Bruno.”

    “Hakuna kingine?”

    “Kipi? Au wewe unacho?”

    “Sidhani, lakini kama ndivyo, nashukuru sana maana naona nitakuwa nina nafasi kubwa sana kwako.”

    “Ni kweli kabisa, ipo nafasi kubwa sana moyoni mwangu kwa ajili yako. Ipo.”

    “Ahsante sana.”

    “Basi nikutakie, asubuhi njema, baadaye nitakuja kukuangalia.”

    “Nashukuru sana, ahsante sana Vanessa, nawe nakutakia kila la kheri katika siku yako ya leo. Mungu awe taa yako!”

    “Nashukuru kwa baraka zako.”

    “Ok!”

    Wakakata simu zao.

    Vanessa akavuta pumzi ndefu sana kisha akazishusha taratibu kabisa, akatabasamu. Taratibu akamvuta Bruno kichwani mwake, akamwangalia akiwa amesimama mbele yake; naam! Alikuwa mwanaume thabiti kwake. Anayejiheshimu, mwenye mapenzi ya dhati, mwenye upendo wa ndani, mvumilivu na kila sifa njema, akammiminia Bruno.

    Akatabasamu tena.

    “Yeah! Yule ndiyo mwanaume, mwenye kauli njema na kujua kubembeleza, najua nikimsogeza kwangu, nitakuwa na amani. Ninazo fedha, lakini sina amani. Nahitaji amani ya moyo wangu. Naamini ipo kwake, nitajitahidi sana niipate,” anawaza Vanessa akiwa amesimama na kanga moja kifuani.

    Anatoka nje na kusaidiana usafi na msichana wake wa kazi.

    ***

    Alishasahau kabisa kwamba mkononi mwake ameshika glasi yenye kinywaji, aliulegeza mkono wake, macho yake yakiwa bado yanamwangalia yule msichana aliyemtumia kikaratasi chenye ujumbe. Akarudia kusoma kwa mara ya pili, halafu akarudisha macho yake tena kwa yule msichana.

    Akakaribishwa na tabasamu mwanana kabisa. Naye akajibu. Wakatazamana wakitabasamu. Punde kile kinywaji ndani ya glasi, kikaanza kumwagika!

    “Oyaaa vipi mkubwa, unanichafua!” Alikuwa ni rafiki yake aliyekaa meza ya jirani.

    “Oh! I’m sorry kaka, sikukuona.”

    “Usijali, lakini kuwa mwangalifu.”

    “Poa.”

    Kazi ikaendelea kuwa ile ile, lakini muda kidogo, akiwa kama amegutuka hivi, akaiandika ile namba ya simu kwenye simu yake, kisha akaihifadhi. Alichokifanya ni kwenda kwenye sehemu ya kuandka ujumbe mfupi, kisha akaandika ujumbe na kutuma kwenda katika ile namba.

    Ulisomeka hivi; “Ahsante Tunu, nimefurahishwa sana na ukarimu wako.”

    “Nami pia, nimevutiwa sana na wewe. Naomba usitafsiri vibaya, nimevutiwa na wewe....” Tunu akamtumia.

    “Ahsante kwa hilo, unaishi maeneo gani kwa hapa Tanga?”

    “Mabawa.”

    “Ni mbali sana kutoka hapa?”

    “Hapana...sijui mwenzangu unaitwa nani?”

    “Bruno.”

    “Najua ni mgeni, unatokea wapi?”

    “Kiukweli hapa Tanga siyo mgeni sana, kwani ni mara ya sita sasa nakuja hapa.”

    “Ni mfanyabiashara?”

    “Hapana ni mfanyakazi wa mfanyabiashara!”

    “Sawa, karibu sana Bruno, kama nilivyokuambia, nimependa sana kampani yako...kama hutajali ningependa ulale kwangu kwa kipindi chote utakachokuwa hapa.”

    “Nilale kwako?”

    “Ndiyo...nina nyumba kubwa Bruno, hata chumba cha wageni pia ninacho, nadhani kitakufaa.”

    “Nitashukuru....acha niongee kwanza na wenzangu, halafu nitakujulisha.”

    “Sawa.”

    Bia zikaendelea kunyweka, huku Bruno akichati na Tunu, baadaye Tunu akahamia kwenye meza ya akina Bruno kabisa, wakaendelea kukata maji kama kawaida. Muda wa kuondoka, Bruno akaomba kwenda kulala na Tunu. Hakuna aliyemzuia, kila mtu alikuwa amelewa.

    “Sasa Tunu, twende zetu,” Bruno akamwambia Tunu ambaye aliitikia kwa kutingisha kichwa huku akijitahidi kuamka kwa kuyumba kidogo.

    Wakashikana mikono na kwenda kwenye taxi. Wakaingia na kuketi wote siti ya nyuma. Mabusu ukawa ndiyo wimbo mzuri kwako kwa usiku huo.



    ***CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Waliingia kwenye chumba kimoja kizuri chenye mpangilio wa kuridhisha. Kilikuwa chumba kimoja chenye kila kitu ndani, choo na bafu vilikuwa ndani. Ile kuingia tu, Tunu akavua nguo zote harakaharaka, akamsogelea Bruno na kuanza kumvua.

    “Vipi?” Bruno akauliza, pombe ikianza kumtoka.

    “Nataka twende bafuni.”

    “Si ulisema kuna chumba changu?”

    “Acha ujinga, utaniaibisha mwanaume. Hebu vua nguo twende bafuni, tuoge tuje tulale.”

    Bruno akawa mpole, akapelekwa bafuni na kuogeshwa kwa maji ya karafuu. Starehe zote alizisikia. Neno moja tu, lilimponyoka; “Hivi Tunu hujaolewa?”

    “Bado, kwani unataka kunioa?”

    “Nitakuwa muongo, nilitaka tu kujua.”

    “Sijaolewa.”

    “Huna bwana anayekuja hapa?” Swali hili aliuliza akionekana kuwa na mashaka kidogo.

    “Sina, kwanini una mashaka sana? Unadhani mimi ni mwanamke mpumbavu wa kiwango gani nikulete kwenye nyumba ambayo ina mmiliki wake? Bruno jiamini,” Tunu akasema, akimbusu midomoni mwake, kisha akamsukuma kitandani.

    Akazima taa.

    ***

    Alitulia kitandani kwa muda, akijitahidi kujisahaulisha kumbukumbu za nyuma, lakini ilishindikana. Hakutaka kuendelea kumkumbuka Tunu, kikubwa kwake kwa wakati ule ilikuwa ni kupona kwanza, halafu kisasi kingefuata baadaye.

    Ilikuwa lazima afanye kitu kwa ajili ya Tunu, kumuacha hivi hivi haikuwa ndoto yake hakika. Lazima amkomeshe. Lazima.

    “Ndiyo, nitamkomesha, nitaanza na Tunu, halafu nitamaliza na Bryson, lakini wote lazima niwaachie maumivu kama ambavyo wao wameniachia mimi maumivu. Siwezi kukaa kimya wakati naumia, nimeteswa, nimenyanyaswa! Siwezi na kweli siwezi na sitaruhusu hilo kabisa,” anazidi kuwaza Bruno.

    Anaamka kwa kujikongoja kidogo, kisha anaingia bafuni kujiswafi. Anarudi na kuvaa nguo zake, anachukua gazeti la Championi lililokuwa mezani na kuanza kuperuzi. Alikuwa anapenda sana kusoma hadithi.

    Macho yake yametulia kwenye hadithi ya The Devil’s Smile (Tabasamu la Shetani) iliyotungwa na mtunzi mashuhuri katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati Eric Shigongo, ambaye anasifika sana kwa vitabu vyake vya President Loves My Wife (Rais Anampenda Mke Wangu) na The Last Days of My Life (Siku za Mwisho wa Uhai Wangu), akasoma akiwa ametulia, mstari kwa mstari. Utulivu huo ukamfanya asisikie mlango uliokuwa ukigongwa!

    Baadaye mgongaji akazidisha kasi, akagonga kwa kasi zaidi...

    Akashtuka sana!

    “Nani?” Akauliza.

    “Jane, vipi umelala?”

    “Hapana, ingia.”

    Akaingia.

    “Vipi?”

    “Salama, za asubuhi?”

    “Njema. Mbona umechelewa kuitika?”

    “Bwana, sikusikia, akili yangu yote ipo kwa Shigongo, napenda sana hadithi zake!”

    “Ok! Kumbe wewe ni mpenzi sana wa hadithi?”

    “Sana!”

    “...sasa vipi, nikuletee nini?”

    “Hata sijui dada’ngu, unaweza kunichagulia?”

    “Sema chochote utakacho.”

    “Kwani mna nini na nini?”

    “Kama kawaida, supu zote, maziwa, chai rangi na mtori.”

    “Nadhani leo ninywe mtori, utaniwekea na chapati mbili, mchana ugali samaki.”

    “Sawa.”

    Jane akaondoka, huyu ni dada maalum ambaye alikuwa akimhudumia kwa kila kitu pale Hotelini na malipo yote hufanywa na Vanessa. Pamoja na kwamba alikuwa mgojwa, lakini sasa afya yake ikaanza kuimarika.

    Akazidi kuvutia!

    ***

    Anatazama maji yanavyopiga kwa kasi baharini, yupo katika Ufukwe wa Coco, akipunga upepo. Vanessa aliamua kwenda ufukweni kwasababu mbili; alihitaji kumpumzisha akili yake, lakini pia alitamani sana kupata jibu la uhakika kuwa anampenda nani kati ya wanaume wawili. Emma na Bruno!

    Alihitaji kupata jibu moja yakinifu ambalo lina maana, hakutamani kupata maumivu ya moyo, ufukweni ni sehemu ambayo akili yake huhiyari kutulia na kuchanganua mambo vyema, kwahiyo aliamini kwa vyovyote vile angepata jibu la moja kwa moja.

    Akiwa katika tafakari, mkononi mwake akiwa na boksi la juice, mara simu yake ikaita. Mara moja akatazama kwenye kioo cha simu, akakutana na jina la Emma. Moyo wake ukashtuka sana.

    Ni Emma!

    Emma mpigaji!

    Anayeugeuza mwili wake ngoma kila siku. Ni kweli alikuwa anampenda sana, lakini yeye hajali wala kuthamini penzi lake, kazi yake imekuwa kumshushia kipigo kila siku, jambo linalomuumiza sana.

    Akaiangalia ile simu ikiita mpaka ikakatika! Ikaanza kuita tena, baadaye ikakatika. Ikaita kwa mara ya tatu; akaamua kupokea.

    “Unasemaje Emma?” Vanessa akasema kwa hasira mara tu alipopokea simu.

    “Acha hasira mpenzi.”

    “Emma, naona mwisho wetu sasa umefika.”

    “Najua sweetie, najua...na ndiyo maana nimekupigia simu...” Emma alikuwa akizungumza kwa sauti ya taratibu sana, akionesha upole wa hali ya juu.

    Haikuwa kawaida yake kabisa. Emma si mtu wa kumbembeleza Vanessa, siku zote alikuwa wa kutukana na kumpiga. Leo anazungumza taratibu?

    Anabembeleza?CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Amestaarabika?

    Maajabu haya!

    “Hivi ni Emma mwenyewe nazungumza naye au kuna mtu ameiba simu yake?” Vanessa alisema akijitahidi kuisikiliza vyema sauti ya Emma.

    “Najua ni vigumu kuamini, umeshazoea kelele zangu, si kawaida yangu kuzungumza hivi, lakini leo nimejua thamani na maana ya mapenzi, nimegundua kwamba nilikuwa nakutesa sana mpenzi wangu, sipendi iwe hivi na ndiyo maana nimekupigia...nahitaji kuonana na wewe mpenzi!”

    “Leo una nini?”

    “Kwanini?”

    “Mbona siku nyingine ukinihitaji umekuwa ukija moja kwa moja nyumbani, leo mbona unaomba ruhusa, una nini Emma?”

    “Nimezaliwa katika ulimwengu mpya wa mapenzi, ndiyo maana kila kitu kimebadilika, nakupenda Vanessa...” Emma akazungumza kwa sauti ya taratibu sana, iliyojaa ustaarabu.

    Vanessa akachangayikiwa sana, yalikuwa maneno makali sana yaliyomchoma, alikuwa katika wakati mgumu wa kuaga penzi la Emma, lakini inakuwaje leo hii anampigia na kumwambia anamhitaji, anampenda na anataka kuwa mpenzi mpya kwake?

    Alisisimka mwili!

    Moyo wake ukaenda mbio, kisha akakata simu na kuizima kabisa! Akaketi chini akijilazimisha kuwa katika hali ya kawaida. Hakuweza. Mvua ya machozi ikaanza kumiminika machoni mwake.

    Ufukweni pale, hapakuwa mahala pazuri tena kwake, akainuka pale chini, kisha akapiga hatua za kivivu kwenda alipoegesha gari lake. Akaingia na kuwasha, akaondoka kwa kasi.

    ***

    Hakuangalia sehemu yoyote baada ya kuegesha gari lake nyumbani kwake. Vanessa akapiga hatua za taratibu akiufuata mlango wa kuingilia ndani. Hakusikia hata sauti ya msichana wake wa kazi akimsalimia pale sebuleni.

    Mguu wa kwanza, mguu wa pili hadi chumbani. Hamad! Anakutana na Emma, akiwa ametulia kitandani. Alikuwa na dalili zote kwamba alikuwa akimsubiri yeye tena kwa mazungumzo muhimu.

    “Usishtuke mama, pole na mihangaiko yako. Karibu ndani mpenzi...kama nilivyokuambia kwenye simu, nahitaji kuzungumza na wewe, nataka sana kuzungumzia penzi letu, nahisi linayumba sasa!” Emma akasema akisimama taratibu na kumvuta Vanessa ndani.

    Akaingia akionesha woga. Akambusu na kumkalisha kitandani. Mazungumzo yakaanza, Emma mtulivu kuliko kawaida. Walikuwa kama wapenzi waliokutana kwa mara ya kwanza. Wakaingia bafuni na kuoga pamoja. Wakarudi chumbani na kujitupa kitandani.

    Moyo wa Vanessa ukaingiwa na ubaridi, akishindwa kuwa na msimamo nani awe wake. Kwa unyonge akanyoosha mkoko wake na kushika bed switch akazima. Akiwa analala sawasawa, simu ya Vanessa ikaita.

    Kwakuwa Emma alikuwa karibu nayo, akaichukua na kumpa Vanessa.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog