Simulizi : Nisamehe Mpenzi
Sehemu Ya Pili (2)
Moyo wa Richard ulikuwa katika hofu kubwa mno, hakutaka kuamini kama kweli alikuwa amemsaliti Evelyne tena katika mazingira ambayo hakuyategemea.
“Nadhani biashara yetu imeishia hapa,” alisema Richard alipoamka asubuhi na kumkuta Monalisa akiwa tayari ameshajiandaa na kwa wakati huo alikuwa ameketi kitandani huku akiiperuzi simu yake.
“Itaisha vipi wakati mimi na wewe tayari ni wapenzi?” aliuliza Monalisa huku akijibebisha.
“Monalisa unajua unanichanganya kwani haya ndiyo yalikuwa makubaliano yetu?”
“Mimi sijui ila fahamu kuwa sisi tumeshakuwa wapenzi.”
“Acha utani Monalisa.”CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Tangu lini nimeanza utani na wewe?”
“Monalisa lakini si unajua kuwa mimi nina mpenzi wangu na ninampenda sana.”
“Hilo silijui kama kweli ulikuwa unampenzi na unampenda kwanini umekubali kumsaliti, kwanini umekubali kunikubaliana ombi langu.”
“Unasemaje?”
“Tayari umeshakuwa mpenzi wangu,” alijibu Monalisa huku akitabasamu.
Richard alikurupuka pale kitandani kisha akaanza kuitafuta simu yake, hakuiona ilibidi amuulize Monalisa.
“Simu yangu iko wapi?”
“Ninayo.”
“Naiomba.”
“Siwezi kukupa,” alijibu Monalisa kisha akaamka pale kitandani akatoka nje huku akiwa anakimbia, Richard alishindwa kumfuata Monalisa kwani kwa wakati huo alikuwa uchi wa mnyama, alibaki pale kitandani huku akilalamika, alijilaumu mno kwa kufanya kosa la kumsaliti mpenzi wake ambaye aliamini kwa vyovyote alikuwa anaenda kumpoteza katika maisha yake huku sababu kubwa ikiwa ni Monalisa msichana ambaye tayari alionekana kuwa sumu ya penzi hilo.
Muda ambao Evelyne alikuwa akimpigia simu Richard ndiyo muda huohuo ambao Monalisa alikuwa na simu ya Richard. Hakutaka kuipokea simu baada ya kuona mpigaji alikuwa ni Evelyne, alipokuwa hostel kuna muda alitamani kuipokea lakini alisita kufanya hivyo, hakutaka kuwa na haraka ya kumpa maumivu Evelyne katika moyo wake mwisho aliamua kuizima kabisa.
Alichokuwa akikifikiria katika kichwa chake kwa wakati huo ni jinsi gani angeweza kumuumiza Evelyne, alifahamu fika alikuwa akimpenda sana Richard na hakutaka kusikia kitu chochote kuhusu mpenzi wake huyo.
“This will be the end of your love for Richard,” (Huu ndiyo utakuwa mwisho wako wa kumpenda Richard,) alijisemea Monalisa maneno aliyoyasindikiza na tusi zito.
Aliichukua simu yake kisha akaiwasha, kitu cha kwanza aliingia katika sehemu ya kuhifadhi picha na video, alianza kutabasamu baada ya kuziona picha alizokuwa amejipiga akiwa pamoja na Richard kitandani, wakati huo Richard alikuwa amelala, hakuishia hapo pia aliamua kuingia katika sehemu ya video na hapo aliweza kuitazama video aliyoirekodi kipindi alipokuwa amelala na Richard, wote walikuwa uchi wa mnyama.
Aliamini kwa asilimia kubwa ni lazima video ile pamoja na zile picha alizopiga na Richard kitandani ni lazima zingeweza kuyasambaratisha mapenzi ya wawili hao.
“Your dangerous,” (Wewe ni hatari.)
“I told you that I can’t never fail,” (Nilikuambia kuwa kamwe siwezi kushindwa.)
“So what you are going to do?” (Kwahiyo nini unakwenda kukifanya?)
“I must make sure I destroyed this love,” (Lazima nihakikishe naliangamiza penzi hili.)
“About those photos and videos Richard has he seen?” (kuhusu hizo picha na video Richard ameziona?)
“Everything I did in secret so they did not know anything,” (Kila kitu nilikifanya kwa siri hivyo hajui lolote.)
Yalikuwa ni mazungumzo kati ya Monalisa na Adela, wakati huo Monalisa alikuwa akimuonyesha picha na video aliyojirekodi kipindi alipokuwa amelala na Richard. Adela alishikwa na butwaa baada ya kuziona picha hizo pamoja na video iliyokuwa ikimuonyesha Monalisa akiwa juu ya kifua cha Richard.
“Itabidi uzifiche maana italeta picha mbaya endapo kila mtu akaziona,” alisema Adela huku akionekana kuogopa.
“Siogopi lolote ila ninachokitaka kuona nilichokipanga kinatimia,” alisema Monalisa.
“Unamaanisha nini?” aliuliza Adela.
“Nitamtumia hizi picha pamoja na hii video WhatsApp.”
“Nani?”.
“Evelyne.”
“Ataumia sana.”
“Nataka aumie zaidi yangu, nimeteseka sana katika kumpata Richard na huu ndiyo utakuwa mwanzo wa moyo wake kupokea maumivu ya kimapenzi,” alisema Monalisa huku akionekana kutokujali lolote.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Alidhamiria kufanya kila aliwezalo ilimradi afanikiwe kuliangamiza penzi hilo ambalo hakupendezewa nalo hata kidogo, alitamani yeye ndiye awe mpenzi wa Richard hivyo kwake kufanya lolote kwa ajili ya penzi hilo bila kujali maumivu ambayo angeweza kuyasababisha kwa Evelyne.
Hakutaka kupoteza muda alichoamua kukifanya usiku wa siku hiyo aliamua kuwasha data kweye simu yake kisha akaingia WhatsApp, alianza kuitafuta namba ya Evelyne ambayo alikuwa ameisevu kwa jina la “Vomiting” (Matapishi.) alipoliona jina hilo alilibonyeza kisha akaingia moja kwa moja katika uwanja wa kuandika ujumbe na kutuma chohote na kama alivyokuwa amepanga alianza kumtumia zile picha pamoja na video ambayo ilikuwa ikimuonyesha yeye akiwa kitandani pamoja na Richard.
Hakuishia hapo baada ya kumaliza kumtumia aliamua kuandika maneno machache ambayo pia alimtumia Evelyne, maneno hayo yalisomeka kwa herufi kubwa “YOUR HUSBAND.” (MUME WAKO.)
****
Richard alikuwa chumbani kwake huku akionekana kutokuwa sawa kabisa, hakutaka kuamini kwa kile kilichokuwa kimetokea siku hiyo alipokuwa hotelini.
Kichwani kwake mawazo ya Monalisa ndiyo yalikuwa yamemtawala, alikumbuka kila kitu kilichokuwa kimetokea lakini hakutaka kuamini hata kidogo, kuna muda alihisi labda alikuwa katika ndoto lakini haikuwa hivyo, alizidi kuchanganyikiwa baada ya kukumbuka kuwa simu yake aliichukua msichana huyo na kukimbia nayo.
Muda mwingine alimkumbuka mpenzi wake Evelyne, aliamini kwa vyovyote ni lazima alikuwa akimtafuta na kwa muda huo simu yake alikuwa nayo Monalisa.
“Mungu wangu sijui Monalisa akipokea atamuambia nini?” alijiuliza swali hili katika mawazo yake.
Hakufahamu ni nini alichokuwa amedhamiria kukifanya Monalisa, alibaki katika hali ya sintofahamu huku asijue nini alitakiwa kukifanya kwa wakati huo.
Wakati akiendelea kuwaza mambo yote hayo lilimjia wazo kichwani, lilikuwa ni wazo la kumtafuta Evelyne kwa njia yoyote ili aweze kuzungumza naye, alipokumbuka umbali uliyokuwepo kati ya Mikocheni na Kigamboni alighairi kuchukua maamuzi hayo.
Alikumbuka kuwa Evelyne alikuwa akijulikana na Mama yake na alikuwa akipenda kuwasiliana naye mara kwa mara, hakutaka siku hiyo iweze kupita bila ya kuzungumza naye. Alichoamua kukifanya ni kwenda kumuomba Mama yake simu kisha akampigia, simu ya Evelyne ilikuwa ikiita bila ya kupokelewa.
“Mbona hapokei simu ni nini kimemkuta?” alijiuliza Richard baada ya kumpigia simu Evelyne zaidi ya mara tatu bila kupokelewa.
Hakutaka kukata tamaa, aliendelea kupiga huku akitegemea kuna muda Evelyne angeweza kuipokea simu hiyo lakini tukio hilo halikuweza kutokea.
****
“Punguza wasiwasi Richard yuko salama.”
“Nitapunguzaje na wakati hapokei simu yangu.”
“Labda yupo mbali na simu yake.”
“Sio rahisi.”
“Sasa unahisi atakuwa wapi?”
“Embu ngoja nijaribu kumpigia tena,” alisema Evelyne kisha akaamua kuipiga simu ya Richard kwa mara nyingine tena, safari hii simu ilikuwa haipatikani, akahisi labda mtandao ulikuwa unasumbua hivyo akarudia kupiga tena huku akijaribu kuzunguka huku na kule mule chumbani lakini majibu yalikuwa ni yaleyale.
“Hapatikani,” alisema kwa sauti ya unyonge.
“Hapatikani?” aliuliza Happy kwa mshangao.
“Ndiyo,” alijibu Evelyne kisha akakaa chini, nguvu zilikuwa zimeanza kumuishia kwa wakati huo.
“Mbona alikuwa anapatikana lakini?”
“Mimi sijui ni nini kilichomkuta Richard wangu jamani.”
“Embu ngoja nijaribu na mimi kumpigia,” alisema Happy kisha akaichukua simu yake halafu akampigia Richard, hakukuwa na jibu lingine alilojibiwa kwa wakati huo zaidi ya kuisikia sauti ya msichana ikimuambia “ Mtumiaji wa simu unayempigia kwa sasa hapatikani, tafadhili jaribu tena baadae.
Evelyne aliendelea kuwa ni mwenye wasiwasi mkubwa baada kuona Richard hapatikani, tukio hilo lilizidi kumnyima furaha kabisa katika moyo wake, alikosa amani muda wote alikuwa akimfikiria Richard.
“Kwanini nakufikiria muda wote Richard utakuwa umepatwa na nini?” alijiuliza kwa sauti mpaka Happy akamsikia.
“Usiwaze hayo kama Richard angekuwa amepatwa na tatizo ni lazima ungepata taarifa.”
“Nani angeniambia?”CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Mama yake,” alijibu Happy kisha akamfanya Evelyne apunguze wasiwasi kidogo, alianza kuyaamini maneno ya rafiki yake baada ya kukumbuka alikuwa akifahamiana na Mama yake Richard, alimuheshimu sana Mama mkwe wake mtarajiwa na hii ndiyo sababu iliyomfanya ashindwe kumpigia simu.
Usiku wa siku hiyo Evelyne alishindwa kulala kabisa, hakutaka kuamini kama siku hiyo alikuwa analala bila kuzungumza wala kuchati na Richard. Japo aliambiwa na Happy apunguze wasiwasi lakini hakutaka kukubaliana na jambo hilo. Wakati Happy alipokuwa amelala usingizi yeye aliamka kisha akaanza kumpigia simu Richard lakini bado alikuwa hapatikani.
Baada ya kuona ameshindwa kupata usingizi kabisa aliamua kuwasha data simu yake kisha akaingia WhatsApp kwa lengo la kujibu jumbe za watu waliyokuwa wamemtumia kwa siku hiyo, alianza kuzipitia moja baada ya nyingine.
Hakutaka kuamini macho yake baada ya kuona ujumbe kutoka kwa Monalisa, haraka aliufungua na ni hapo ambapo alishikwa na bumbuwazi baada ya kukutana na picha pamoja na video iliyokuwa ikimuonyesha Richard na Monalisa wakiwa kitandani. “YOUR HUSBAND” (MUME WAKO.) aliyasoma maneno haya mara mbilimbili, hakutaka kuamini hata kidogo kile alichokuwa akikiona kwa wakati huo.
Kitendo cha kuziona picha za mpenzi wake akiwa amelala kitandani na Monalisa hakika zilimuumiza mno moyo wake, alihisi kupata maumivu makali asiyoyatarajia kwa wakati huo.
Kila kitu alichokuwa akikiona katika picha hizo kilimfanya abaki katika wakati wa maumivu mno. Machozi yalianza kumbubujika mashavuni mwake, akajaribu kuyafuta lakini huo haukuwa ndiyo mwisho wa kuyamaliza, yalizidi kumbubujika mfululizo bila kukoma.
Hakukuwa na kitu kingine kilichokuwa kikimuumiza moyo wake zaidi ya usaliti, alisalitiwa na mpenzi wake ambaye alikuwa akimpenda sana. Alikumbuka mambo mengi waliyowahi kuyafanya na Richard katika mapenzi yao lakini mambo yote hayo yalibaki kuwa hayana mashiko yoyote.
Muda huo ambao alikuwa katika maumivu ghafla! simu yake ikawa inaita, alipaitazama mpigaji wa simu hiyo aliliona jina la Mama Richard, hakutaka kupokea, aliamini Richard ndiye aliyekuwa akimpigia. Hakutaka kuzungumza naye lolote hivyo aliamua kuiacha simu iendelee kuita mpaka pale ilipokata. Aliendelea kulia huku akiwa ameukumbatia mto pale kitandani.
****
Monalisa alikuwa katika furaha isiyokuwa na kifani, muda wote alikuwa ni mtu wa kucheka peke yake baada ya kufanikiwa kumtumia picha Evelyne. Aliamini picha hizo lazima zingeweza kuliua penzi kati ya Richard na Evelyne na hiyo ndiyo sababu iliyomfanya azidi kubaki akiwa ni mtu mwenye furaha muda wote.
Aliamini hakuwa na sababu ya kuendelea kulia au kuumia tena kwani mwanaume aliyekuwa akimuhitaji tayari alikuwa ni wake, hilo lilizidi kumfurahisha mno.
“Amekujibu lolote mpaka sasa baada ya kumtumia hizo picha?” aliuliza Adela.
“Hapana bado hajanijibu ila amezipokea tayari,” alijibu Monalisa huku akitabasamu.
“Hivi umejiamini nini mpaka ukaamua kuzipiga hizo picha?”
“Nampenda sana Richard, nimeshindwa kujizuia kwa kweli imenibidi nifanye hivyo,” alijibu Monalisa.
Monalisa aliendelea kuushikilia msimamo wake wa kumpenda Richard, muda mwingine aliamini kwa tukio alilokuwa amelifanya la kumtumia picha za utupu Evelyne ni lazima zingeweza kuwagombanisha wawili hao na huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa kulifaidi penzi la Richard kwa uhuru. Alichokuwa anakihitaji ni kuwa na Richard bila kujali maumivu ambayo alikuwa anaenda kuwapa wawili hao waliyokuwa wanapendana kwa dhati.
Adela ndiye alikuwa msichana pekee ambaye alifahamu kila kitu kilichokuwa kikiendelea kuhusiana na picha ambazo alikuwa amezipiga Monalisa na Richard.
Monalisa aliamua kumuonyesha Adela picha hizo huku akiwaficha Penina na Mary, hakutaka wafahamu lolote zaidi ya uhusiano wake na Richard tu.
“Kwanini nisiwaambie?” aliuliza Adela huku akionekana kushangazwa mno.
“Sitaki uwaambie lolote kuhusiana na hizi picha nilizozipiga,”alijibu Monalisa huku akimtazama kwa macho ya msisitizo Adela.
“Kuna kitu gani kinachoendelea kati yenu?”
“Hakuna.”
“Sasa kwanini hutaki niwaambie?”
“Nimeamua tu kwani picha ni zangu au za kwao?”
“Una uhakika hakuna tatizo?”
“Ndiyo hakuna,” alijibu Monalisa.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Waliendelea kuzungumza wakati huo Penina na Mary hawakuwepo hostel, mpaka kufikia muda huo Adela hakujua ni nini kilichokuwa kikiendelea mpaka Monalisa aamue kuwaficha Penina na Mary na wakati wote walikuwa ni marafiki na kila jambo ambalo alikuwa akilifanya ilikuwa ni lazima awaambie, hilo lilizidi kumchanganya kichwa chake.
****
Siku iliyofuata ndiyo ilikuwa ile siku ambayo Evelyne alishindwa kuendelea kubaki darasani baada ya kumuona Richard akiwa ameingia, alishindwa kuyavumilia maumivu ambayo moyo wake tayari ulikuwa umshayapata, alimchukia mno Richard na hakutaka kuendelea kumtazama katika mboni za macho yake.
Alichoamua kukifanya ni kuondoka kabisa eneo hilo la chuo huku akiamini kwa kufanya hivyo angeweza kuyapooza maumivu na machungu ambayo moyo wake ulikuwa ukipitia.
Rafiki yake Happy hakuwa anafahamu lolote lile lililokuwa limetokea, alibaki katika wakati mgumu baada ya Evelyne kushindwa kumuelezea ni nini kilichokuwa kimetokea na kwa wakati huo aliamua kuondoka zake.
Alitamani sana kufahamu ni nini kilichokuwa kimetokea na mtu pekee ambaye aliamini angeweza kumueleza ukweli wa mambo yote hayo alikuwa ni Richard lakini na yeye alishindwa kumueleza ukweli, alibaki akiwa haelewi ni nini kilichokuwa kimetokea baada ya kumuona mpenzi wake akiwa ameondoka.
“Unasema amerudi nyumbani?” aliuliza Richard huku akionekana kuwa mwenye wasiwasi.
“Ndiyo,” alijibu Happy.
“Kigamboni au?” aliuliza Richard.
“Richard inamaana hujui Evelyne anapoishi?” aliuliza Happy huku akionekana kumshangaa Richard kwa wakati huo.
“Hapana, nafahamu ila nimechanganyikiwa,” alijibu Richard.
“Halafu mbona jana ulikuwa unapigiwa simu hupatikani?” aliuliza Happy.
Richard alianza kukumbuka tukio la Monalisa kuichukua simu yake, alishindwa kutoa jibu la haraka, alibaki mithili ya mtu ambaye alikuwa akitafakari jambo na mwisho lilimjia jibu la kudanganya.
“Nimeibiwa,” alijibu.
Happy alianza kuingiwa na wasiwasi baada ya kumuona Richard akionekana kuficha ukweli wa jambo ambalo alihitaji kulifahamu, aliamini Richard alikuwa akifahamu kila kitu kilichokuwa kikiendelea lakini alishindwa kujua alitakiwa aanzie wapi kumuhoji ili aweze kumwambia.
“Una uhakika na unayonieleza?”
“Ndiyo nina uhakika,” alijibu Richard huku kijasho chembamba kikianza kumtoka mwilini.
Richard alishindwa kuzungumza ukweli kwasababu mpaka kufikia wakati huo hakujua ni nini kilichokuwa kimetokea, kuna muda alianza kuhisi labda Monalisa aliamua kumueleza ukweli Evelyne wa kile kilichokuwa kimetokea kati yao na hiyo ndiyo ilikuwa sababu iliyomfanya mpaka abadilike. Lilipomtoka wazo hilo liliingiwa wazo lingine hivyo alishindwa kabisa kuelewa ni nini ambacho alitakiwa kuzungumza.
“Unajua Richard sikuelewi unachokizungumza?”
“Hunielewi nini?”
“Mimi nahisi utakuwa unafahamu kila kitu kwasababu haiwezekani Evelyne halafu abadilike bila sababu.”
“Kama ningekuwa ninafahamu ukweli ningekueleza sasa kwanini nikufiche na kwanini nikufiche?”
“Namfahamu sana Evelyne mimi naamini kuna kitu kati yenu kimetokea.”
“Kitu gani?”
“Sikifahamu,” alijibu Happy.
Wazo lililomjia Richard kwa wakati huo ilikuwa ni kwenda Kigamboni nyumbani alipokuwa akiishi Evelyne na Happy, hakutaka kuendelea kubaki katika mabishano na Happy, alitamani kufahamu ni nini kilichokuwa kimemtokea mpenzi wake bila kujua kuwa kumbe yeye ndiye alikuwa sababu ya mambo yote hayo kutokea.
“Let’s go.” (Twende zetu.)
“Where?” (Wapi?)
“I say let’s go.” (Nasema twende.)
“Where?” (Wapi?)CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Kigamboni.”
“Okay, but let me then I take a bag to class,” (Sawa ila ngoja basi nikachukue begi darasani.”
“Hurry up,’ (Fanya haraka,) alisema Richard kisha Happy akafanya kama alivyoomba, aliporudi safari ya kwenda kigamboni ikaanzia hapo. Richard hakutaka kwenda na gari lake ili kuepuka usumbufu ambao wangeweza kukutana nao kivukoni, waliamua kupanda bajaji ambayo iliweza kuwafikisha mpaka kivukoni.
Mpaka kufikia muda huo Richard alitamani sana kumuona mpenzi wake ili aweze kuzungumza naye, moyoni aliamini katika mapenzi ya dhati ambayo aliahidi kamwe yasingeweza kufa.
Alimpenda sana Evelyne na aliamini hakukuwa na msichana mwingine ambaye angeweza kuiziba nafasi hiyo katika moyo wake, wakati ambao alikuwa akiendelea kuyawaza hayo nyuma ya pazia hakujua kuwa kumbe alikuwa amepigwa picha za utupu na Monalisa ambazo zilitumwa kwa Evelyne na picha hizo ndizo ambazo zilimfanya abadilike kiasi cha kuondoka kabisa eneo la chuo.
Walipokuwa wamepanda kwenye panton Richard alitamani liongeze mwendo ili aweze kufika haraka nyumbani alipokuwa akiishi Evelyne, alitamani kumuona mpenzi wake na kuzungumza naye kwa wakati huo. Alipokuwa ameketi alipaona kuwa kama kuna misumari iliyomchoma hivyo hakutaka kuendelea kuketi sehemu hiyo, alisimama na kuanza kuzunguka huku na kule kama mtu aliyeanza kuchanganyikiwa, kitendo hicho kiliwafanya baadhi ya watu waliyokuwemo kwenye panton hiyo waanze kumshangaa Richard.
Kichwani alikuwa akimuwaza Evelyne tu, hakutaka kuzungumza lolote na Happy, kimoyomoyo alikuwa akiomba wawahi kufika haraka ili aweze kuzungumza na mpenzi wake huyo.
Baada ya kupita dakika kadhaa waliweza kuvuka salama kisha wakaianza safari ya kuelekea nyumbani alipokuwa akiishi Evelyne pamoja na Happy, palikuwa na umbali kidogo hivyo waliamua kutumia usafiri wa bajaji ambao uliweza kuwafikisha kwa haraka sana.
Baada ya bajaji hiyo kuwafikisha walishuka kisha Richard akamlipa dereva wa bajaji kiasi cha pesa alichokuwa anawadai, alipomalizana na dereva huyo walitembea kidogo mpaka kufika katika chumba ambacho alikuwa anaishi Evelyne pamoja na Happy.
Walipoingia ndani ya chumba hicho walimkuta Evelyne akiwa amejilaza kitandani huku akiwa analia, alionekana kutochukua muda mrefu tangu alipoweza kuingia katika chumba hicho. Alipohisi kuna watu wameingia ndani aliamka na kuwatazama.
Hakutaka kuamini macho yake baada ya kumuona Richard akiwa ndani ya chumba hicho, hasira zilizidi kumpanda, alihisi kumuona adui mkubwa wa maisha yake ambaye alimchukia sana.
Alichokuwa anakihitaji Richard kwa wakati huo ni kupewa nafasi ya kuzungumza na Evelyne ili aweze kujua ni nini kilichokuwa kimetokea mpaka akaamua kuondoka chuoni lakini nafasi hiyo ilikuwa ngumu mno kupatikana. Evelyne hakuwa tayari kuzungumza naye lolote.
“Happy naomba umtoe huyu ibilisi nje, sitaki kumuona katika macho yangu,” alisema Evelyne huku akiendelea kulia.
“Kuna nini kimetokea Eve mbona sikuelewi?” aliuliza Happy huku akizidi kuchanganywa na maneno ya rafiki yake, hakuelewa ni nini kilichokuwa kimetokea mpaka kikamfanya Evelyne abadilike kiasi kile.
“Nimesema sitaki kumuona Richard katika macho yangu, naomba utoke Richard, sikutaki kukuona,” alisema Evelyne kisha akaanza kumfukuza Richard.
“Lakini Richard si mpenzi wako?” aliuliza Happy.
“Alikuwa mpenzi wangu lakini sio sasa naomba umtoe,” alijibu Evelyne kwa sauti ya kilio iliyo sanjari na maumivu pamoja na hasira.
Richard hakutaka kuamini kile alichokuwa akikisikia kutoka kwa mpenzi wake huyo, aliamini hakukuwa na tatizo lolote lile hivyo bado alizidi kuomba kupewa nafasi ya kuzungumza naye.
“Mpenzi wangu naomba unipe nafasi ya kuzungumza na wewe, niambie nini kimetokea mbona unanichukia bila sababu?” aliuliza Richard huku akimtazama Evelyne ambaye alikuwa akilia kwa wakati huo, hakutaka kuendelea kuyashuhudia machozi ya mpenzi wake yakiendelea kumbubujika mfululizo, alichoamua kukifanya akakitoa kitambaa mfukoni mwake kisha akahitaji kumfuta machozi lakini kabla hajamsogelea kwa lengo la kumfuta machozi alishtukia akipigwa kibao na Evelyne.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Naomba utoke Richard sitaki kuzungumza lolote na wewe,” alisema Evelyne kisha akamfukuza Richard, wakati huo alikuwa akilia.
Richard alishindwa kabisa kuamua nini la kufanya kwasababu kila alilokuwa anahitaji litokee kwa muda huo lilishindikana, alimbembeleza sana mpenzi wake huyo ili aweze kumuambia ni nini ambacho kilikuwa kimetokea lakini hakuwa tayari kuzungumza lolote.
Hakutaka kuondoka kirahisi wakati alipokuwa akifukuzwa lakini mwisho ilibidi Happy amuombe aondoke eneo hilo kwani ilikuwa ni kawaida ya Evelyne kutozungumza lolote kipindi ambapo alikuwa katika hasira. Alimuahidi kipindi ambapo hasira za Evelyne zitakapokuwa zimeisha ndipo angeweza kupata muda wa kuzungumza naye.
****
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment