Simulizi : Lidake Tena Chozi Langu
Sehemu Ya Pili (2)
Kitendo cha kuuona mkono wa mwanadamu mwenye ulemavu kama mimi katika gari kukanitia hofu na kunifanya nitetemeke.
Nguvu zilizokuwa zimeanza kupotea zilirejea kwa kasi nikatambua kuwa kuendelea kuwa pale zaidi nilikuwa nahalalisha kifo changu kwa kukatwa na mapanga huku nikiwa najioona.
Nilijiuliza juu ya yale maumivu yanayopatikana pale mtu unapochomwa na mwiba kisha nikayakadiria maumivu ambayo yanapatikana kwa kukatwa mkono ama kiungo chochote kile. Hakika sikuhitaji mtu wa kunijibu swali lile. Hisia zangu ziliniambia kuwa ni maumivu makali sana!!!
Kufikia hapo nikajisemea kuwa hata katika vitabu vya Mungu wanasema kuwa jisaidie naye atakusaidia.
Nikajivuta kwa taabu hadi nikaweza kupaona nje hapo nikaishia kuona hali kama ya jangwa hapakuwa na kiumbe yeyote yule. Nikarejea ndani kisha upesi nikaanza kuzifungua zile kamba ngumu zilizokazwa katika miguu yangu.
Zilikuwa ngumu sana na vile nilikuwa ninaoigopa basi kila muda nilishindwa kujua ni namna gani ya kuzifungua. Nilibinua huku ikashindikana nikajaribu huku sikuweza. Mikono ilikuwa haina utulivu kabisa, lakini hatimaye nikalipata fundo sahihi nikafanikiwa kuupata mzunguko ule. Nilijifungua upesi sana huku nikitambua wazi kuwa wale watu wakinikuta katika jaribio lile basi nitakuwa katika wakati mgumu sana, huenda wataniwekea tena zile soksi chafu mdomoni ama wanaweza kuamua kuniua nitajuaje!!!
Nilipowaza juu ya kuuliwa nikajisikia kutetemeka sana amakweli hakuna mtu mwenye urafiki na kifo!! Kila nikigusa kamba mikono ilikuwa inateleza kutokana na kutetemeka nikajaribu sana kuizuia akili yake isiishi katika hofu, hatimaye hofu ikapungua kiasi na umakini ukarejea.
Hatimaye nikafanikiwa kuzifungua na kubaki huru!!
Upesi nikaruka na kutua chini, na hapo nikatambua kuwa kila pande palikuwa na hali za kufanana, hakuna sehemu ambayo palikuwa na watu.
Nilifanya patapotea na kuamua kukimbilia upande nilioamini kwangu mimi kuwa ni upande salama kabisa.
Nilikimbia sana hadi nilipoanza kukutana na mti mmoja mmoja na vichaka kadhaa.
Baada ya kukimbia sana hatimaye kwa mbali nikaona kundi la watu. Nikataka kukimbilia katika kichaka ili niweze kujificha lakini macho yangu yakavutiwa kutazama watu waliokuwa katika lile kundi.
Nilisimama kama nisiyekuwa na haja ya kujificha tena, katika lile kundi kuna kitu nilikiona.
Awali sikuwa na uhakika sana lakini kadri walivyosogea nilizidia kuamini kuwa sikuwa naidanganya nafsi yangu.
Wazo langu la kujificha likaishia palepale.
Nilikuwa natazamana na baadhi ya watu ambao tulikuwa tuna tatizo moja. Sote tukiwa ni walemavu wa ngozi yaani Albino.
Walikuwa wakitembea kwa kujiburuza sana bila shaka walikuwa wametoka umbali mrefu ama walikuwa na njaa sana.
Ningeanza vipi kujificha sasa? Sawa ningeweza kujificha na kisha kufanikiwa kutoroka na kuwa huru!! Lakini ni usaliti wa hali ya juu ambao ningekuwa nimeufanya, yaani kuwatoroka wenzangu ambao walikuwa wanaenda kuuwawa!! Kuuwawa kwa kukatwa na mapanga!!!
Lile kundi liliponikaribia nilimuona mtu mmoja mweusi akinikimbilia kwa kasi kana kwamba hapo awali nilikuwa nakimbia na yeye anajaribu kunikimbiza!! Wakati nilikuwa nimesimama wima nikimsubiri anifikie!!
Kadri alivyonikaribia nilitambua wazi kuwa laiti kama nikiamua kumkaba bwana yule kiubavu tulikuwa tunawezana kabisa.
Lakini sikuhitaji kufanya vile kwa wakati huo kwani ningehatarisha maisha ya wenzangu japokuwa tayari yalikuwa katika hatari.
Yule mtu mweusi mfupi alinifikia nakujaribu kunikaba kwa nguvu, sikujibu pigo lolote. Mwenzake akafika na kunifunga kamba katika mikono yangu!!
Na wakati huo lile kundi lilikuwa limefika pale nilipokuwa.
Kwa harakaharaka nikatambua kuwa jumla palikuwa na walemavu wa ngozi sita na mimi nikiwa wa saba.
Jicho langu lilikutana na sura ambayo haikuwa ngeni kabisa machoni kwangu. Nikajiuliza huyu msichana nimewahi kumuona wapi.
Akili yangu haikuwa na hiyana ikanipatia jibu!!
Ilikuwa ni sura ya msichana niliyoiona katika picha ile ndani ya kile chumba nilicholala na kale katoto kachangamfu!!!
Tulitazama na hapo nikagundua kuwa alikuwa amevimba sana uso na macho yake yalikuwa mekundu!!
Niliposhusha macho yangu chini nikaona damu ikiwa imegandamana katika eneo lake la mguuni kutokea pajani.
Maskini!! Sijui na yeye walimdanganya kuwa anakuja kuwa mwalimu wa kwanza katika shule yao mwenye ulemavu wa ngozi kama walivyonidanganya mimi!!!
Nilijiuliza huku safari ikiendelea!!!
Tukiwa tunaendelea na safari katika eneo lile lililokuwa na mchanga tele mara nilisikia sauti ya kitoto ikilia.
Awali sikuwa nimeona mtoto mdogo katika msafara ule, nikageuka na kutazama ni wapi sauti ilikuwa inatoka.
Nilipogeuka nikamuona yule binti ambaye nilifanikiwa kumuona kwenye picha kabla ya kukutana naye pale akibembeleza mtoto.
Kwa jinsi ya muonekano wake sikudhani kama angeweza kuwa na mtoto kama yule. Hakufanania kuwa mama kabisa.
“Mnyonyeshe mara moja!!!” yule jamaa mfupi mweusi aliamrisha, nikamuona yule binti akitangaza sura ya masikitiko.
Sikuona ambaye alijali kuhusu hilo.
Yule mtu mweusi alipoona amri yake haifanyiwi kazi alifyatuka na kisha akamtishia kumnasa kofi, kisha akamuamrisha tena amnyonyeshe.
“Sasa jamani mimi nitamnyonyeshaje? Maziwa nitayatoa wapi ya kumpa!!” yule binti alilalamika sana huku sauti yake ikionyesha wazi kukata tamaa. Na kweli hakuwa na maziwa kwa mtazamo tu wa kifua chake kidogo ambacho bado kichanga!!
“Ahaa unataka kujua maziwa yanapopatikana eeh!!” yule jamaa mweusi alimweleza kisha akamfikia na kuichana nguo yake na kukiacha kifua chake wazi.
Matiti yote yakawa nje, unyanyasaji wa namna gani hu jama!! Mbele ya wanaume unamwacha msichana akiwa kifua wazi!!
Ilisikitisha sana, ulikuwa udhalilishaji wa hali ya juu.
Nisingeweza kuvumilia zaidi msikilizaji..
Nikiwa nimefungwa kamba vilevile, nilitoka kwa kasi kisha nikampiga teke kali yule mtu mfupi akatokwa na yowe la hofu. Nikataka kumkimbilia tena lakini wale wenzake wakaniwahi.
“Wauaji wakubwa nyie, mmetukamata bila sababu, mnampango wa kutuua, sawa tumekuwa watulivu mtufanye mnachotaka mnaanza kutudhalilisha. Angekuwa dada yako ungekubali kuona anavuliwa nguo hivi, ungekubali kuona analazimishwa kunyonyesha wakati huenda hata hajawahi kuzaa na hana maziwa katika kifua chake, nasema hivi sisi ni wakosefu huenda kilio chetu hakitawaletea athari zozote lakini nasema ole!! Ole wenu mnaokisikia kilio cha huyu mtoto mdogo na kujifanya hamkisikii, Mungu aliye hai atawapa adhabu kali sana, mtalia na kusaga meno huku mtoto huyu akiwatazama kwa huruma kwa sababu yeye si shetani kama nyie!! Sijui kama nitakuwepo kushuhudia lakini ole wenu!!!” nilitokwa na maneno yale makali kwenda kwa bwana aliyeonekana kuwa mkuu wa msafara. Niliyasema yale kwa uchungu sana!!!
Hakunijibu kitu chochote akatokwa na tabasamu!!
Nilitambua wazi kuwa lile halikuwa tabasamu kutoka moyoni alidanganya tu kuwa ametabasamu hapakuwa na tabasamu pale!!!
Yale maneno lazima yalimuingia!!
Yule bwana akachukua shuka la kimasai alilokuwa amejifunika akamfunika nalo yule binti kumsitiri na uchi ule!!
Msafara ukaendelea huku nikijisikia vibaya sana kuwa mateka katika nchi huru!!
Nilipokuwa karibu kabisaa na yule binti nilimuuliza jina lake akanijibu kuwa jina lake ni Grace!! Nikamuuliza na yule mtoto ni wa nani akaniambia kuwa hajui lakini anahisi kuwa mama yake ni aidha ameuwawa tayari ama ni mama mweusi ambaye amezaa albino basi wamemuibia mtoto wake.
Grace akanigusia pia kuwa hao watu wamembaka mara mbili kila mmoja. Hakuwa amewahi kujihusisha na mapenzi hivyo wamemuumiza sana!!
Niliumia ndugu unayenisikiliza ama utakayeyasoma haya, yaani wanasema sisi sio wanadamu wa kawaida na hapohapo wanathubutu kumbaka mtu asiyekuwa wa kawaida. Hakika moyo wangu uliuma mno.
Hatimaye tukalifikia lile gari na hapo hapakuwa na kuingia ndani ya gari badala yake tulikutana na sura nyingine ngeni.
Baada ya kufika pale, wale watu wakatuzunguka na kuanza kutukaguakagua, mara walalamike kikabila mara wacheke.
Sisi tulikuwa kimya bila kujua jambo lolote.
Na hatimaye likafika gari jingine tena. Ilikuwa yapata saa kumi na moja jioni. Lilikuwa gari ambalo lilikuwa katika namna moja ya fuso tukaamuriwa kuingia mle ndani.
Tukaingia na kuwakuta watu wengine watatu!! Kuna sehemu kadha wa kadha zilikuwa zimefunikwa sikujua hata ni kwa nini.
Tuliingia kisha gari likafungwa lile, na baada ya masaa kadhaa taa zikawashwa mle ndani na zile sehemu zilizokuwa zimefunikwa zikafunuliwa ni hapo ambapo kamwe sitapasahau.
Niliwahi kukutana na mambo ya kutisha niliwahi kuota ndoto kali za kutisha lakini kujikuta katika gari nikiwa nimefungwa mikono na kisha macho yangu yanakutana na mashoka, visu na mapanga huku akili ikitambua wazi kuwa vinatakiwa kuukata mwili wangu!!! Ni jambo ambalo akili yangu haitaweza kulisahau kamwe!!
Najua unajiuliza inakuwaje hadi sasa nipo hai, hili swali hata mimi najiuliza sana lakini nasema huenda nilipona ili nije kuwa shuhuda.
Nikusimulie kilichotutokea mimi pamoja na albino wenzangu.
Kisha nikusihi ulidake tena chozi langu!!!
JIFUNZE!!
WANADAMU tuliumbwa na kuletwa duniani tukiwa katika usawa mmoja kabisa, usawa wa kuitawala dunia huku tukikumbukuka kumtumikia Muumba wetu na kumuheshimu!!
Kushindwa kumtumikia muumba muweza wa yote na kisha kujipangia wewe sheria zako kwa ajili ya kumgandamiza mwanadamu mwenzako ni kosa mbele ya haki za Mungu!!!
Ishi kwa usawa na wenzako, Mungu anakuona!!!!
******************************************
WALE watu tuliowakuta mle ndani walikuwa hawajatusemesha kitu chochote kile. Baada ya mwanga ule wakajifunika vitambaa vyeusi usoni!!!
Kisha wakaenda mahali vilipokuwa vile visu na kuanza kuchagua na kufanya kama wanavijaribisha makali yake kama ni thabiti ama la!!
Niliwaona wenzake wakiwa wanalia.
Grace yule binti aliyebakwa alinisogelea na kuninong’oneza huku sauti yake ikiwa imejaa uoga mkubwa.
“Kaka tuokoe!!”
Kauli yake hii ilinifanya nijisikie fadhaa sana, ningeweza vipi kuwaokoa kutoka katika janga lile ambalo lilionekana wazi kuwa haliepukiki. Na hadi kufikia kusema nami aliamini fika kuwa naweza kuwasaidia.
“Unaweza kaka tuokoe!!!” alininong’oneza tena.
“Sina la kufanya dada Grace natamani sana iwe hivyo!!” nilimjibu kwa sauti ya chini lakini hakuridhishwa na jibu langu akabadili kauli.
“Tusikubali hili jambo litokee kirahisi… tupambane tu!!” alinisihi kisha akaniambia iwapo naogopa basi yeye ataanza. Nikamwambia kuwa siogopi tatizo ni kwamba sijui nitaanzia wapi. Sikumbuki kama Grace aliniaga lakini ghafla alijirusha na kukwapua kisu kikubwa na sekunde iliyofuata alianguka chini na mmoja kati ya wale wanaume na kilichofuata ulikuwa mtafutano wa hali ya juu mle ndani.
Damu iliruka juu sana huku kelele kubwa ikitoka na kuzima mara moja.
Wale wanaume wawili walibaki kuwa wamepigwa butwaa!!!
Grace akasimama akiwa amelowana damu na vile taa ilikuwa inawaka mle ndani alitisha kumtazama.
“Mwanaume yeyote na anisogelee sasa!!!” alitisha huku akiwa anawatazama wale wanaume wawili ambao hawakuwa eneo lenye vile visu.
Na sekunde nyingine alinitazama na ni kama ishara alikuwa ananipa. Ishara ile ikanifungua akili, nikaingilia kati lile pambano. Ni kweli ulikuwa ni muda mrefu hatukuwa tumepata chakula zaidi ya maji lakini nguvu ya ukombopzi hailetwi na chakula.
Nikamuwahi bwana mmoja akiwa amejifunika bado kitambaa chake usoni.
Alipoanguka chini mara Grace akafika na kumchana na kisu katika paja lake.
“Ladha ya kisu tamu eeh!!” akamuuliza yule bwana hakujibu kitu alikuwa analia kama mtoto.
Wakati tumewakabili hawa wale wenzetu waliobaki wakamkaba yule mmoja.
Baada ya kuwadhibiti ipasavyo kilichobaki ikawa ni namna gani tunatoka mle ndani.
Yule aliyechomwa bisu na Grace hakuwa na dalili zozote za uhai!!
Grace allipohangaika na kukosa kabisa namna ya kutoka katika gari lile akatuita kwa ujumla na kufanya kama ametukumbatia na sisi tukajikumbatia.
Kale katoto kadogo kakiwa kamelala Grace alianza kuzungumza. Alizungumza kwa uchungu sana akijielezea ni kwa namna gani amefika hapo alipo.
“Nimeonelea ni vyema tuzungumze sisi kwa sisi, japokuwa hatujua kama tutatoka humu tukiwa hai ama la basi ni vyema kuzungumza. Maana mazungumzo pia ni tiba naamini kila mmoja analo la kusema kwa upesi nitaanza mimi. Labda tukizungumza Mungu aliyetuumba atakisikia kilio chetu na kututoa humu ndani tukiwa wazima kabisa, ni jambo gani analoshindwa Mungu kwani? Halipo” aliendelea kuzungumza.
Alielezea juu ya familia yake yeye akiwa ni dada mkubwa, wadogo zake wote hawana ulemavu wa ngozi ni yeye tu na anapambana kumsaidia mama yake ambaye ni mlemavu wa mguu na umri umemuacha!!
Alipambana hadi kufanikiwa kumaliza kidato cha nne akaanzisha darasa lake kwa ajili ya kufundisha watoto wadogo kusoma na kuandika, alifanya yale kutoka na misukumo miwili kwanza kusaka kipato kwa ajili ya kuilisha familia yake na pili kutokana na upendo mkubwa alionao kwa watoto wadogo.
Hapakuwa na kipato kikubwa na baadhi ya wazazi walikuwa wanagoma kuwapeleka watoto wao katika darasa lake kutokana na ngozi aliyokuwanayo walikuwa wakiamini kuwa yeye si mwanadamu wa kawaida na ni hatari kwa watoto wao. Tatizo ni kwamba watoto walikuwa wakimpenda sana.
Moyo wake huu wa kujitolea akajikuta akiwaruhusu watoto wengine kuingia darasani bila kulipia ada ndogo kabisa aliyokuwa ameipanga.
Kutokana na watoto kumpenda wakajikuta wakimuelewa sana na hatimaye wazazi wakasahau imani zao na kuwapeleka watoto wao katika darasa la Grace.
Ni hapo ndipo wadhamini wakajitokeza na kutaka kumsaidia Grace ili aweze kuwa na shule yake kabisa kwa ajili ya watoto wadogo.
Mama yake alifurahi sana kutokana na nafasi hiyo iliyomuangukia mwanaye.
“Niliisubiri sana hiyo siku ya siku ifike ili niweze kubadili maisha ya familia yangu na kijiji changu kwa ujumla. Na kweli hiyo siku ikafika…. Ndiyo siku ambayo nilitekwa bila kujua iwapo nilikuwa nimetekwa!!! Sijui iwapo nitarudi nyumbani salama, na iwapo sitarudi najua tu lazima mama yangu atakufa kwa sababu ya presha atakufa tu mama yangu!!!” alinyamaza Grace na alikuwa akilia. Tukajikuta tumesahau kabisa kuwa tupo katika wakati mgumu na hatuwezi kutoka nje.
Alipomaliza kuzungumza akaingia kijana mwingine ambaye kwa kumtazama angeweza kuwa na umri wa miaka kumi na saba ama kumi na sita. Huyu alikuwa hajazungumza hata kidogo alikuwa ni mvulana.
“Namchukia sana mama yangu mdogo…..” alianza kusema kisha akajifuta machozi na kuendelea, “na alaaniwe kwa yote mabaya aliyonifanyia hadi kufikia hatua hii hapa nilipo. Nilimuona kwa macho yangu akipokea pesa kisha kunikabidhi kwa watu wabaya. Mama yangu mdogo, yaani anatoka marehemu mama yangu kisha yeye ndiye anayeachiwa titi anyonye lakini hakujali ukaribu ule. Aliniuza mama yangu mdogo ili nife kifo cha kikatili. Na hata kabla hajaniuza ni sawasawa tu alikuwa amenifanya kuishi maisha mabaya sana nahisi hata marehemu mama yangu angekuwepo angekataa katakata kumsamehe.
Mama yangu mzazi alimsomesha mama yangu mdogo hadi kidato cha nne, na baada ya hapo akaugua. Nakumbuka siku anayotuaga aliniita mimi akamuita na mama yangu mdogo… sijayasahau kamwe maneno ya mama alimwambia mama mdogo ‘Jovina mdogo wangu sihitaji kuongea makuu mengi sana, hali yangu si njema hata wewe unaniona hili sio la kusimuliwa. Mama yetu alipofariki alinikabidhi nikupiganie nimekupigania hadi hapo ulipofikia, sasa najiona hali yangu ni mbaya naomba na mimi nikuachie huyu mtoto wangu. Najua hata wewe utazaa siku moja tafadhali umtunze kama mwanao wa kumzaa, umtunze kama mimi nilivyokutunza wewe. Nitatabasamu nikiona mwanangu anafurahi na kunisahau kabisa akiwa katika mikono yako salama. Naamini hautaniangusha’ …… hayo yalikuwa maneno ya yule mama ambaye kamwe sitayasahau. Lakini hata mwaka haukupita mama mdogo akaanza kunifanyia visa, kila ninalofanya kwake linaonekana baya. Mara ghafla akanibadilikia na kuanza kunipenda huku akinisihi kuwa eti mzimu wa mama yangu umemtokea na kumpa onyo kali akaniomba msamaha. Maisha yakabadilika sana, lakini baaya ya wiki tatu tu…. Akaniambia kuwa anahitaji nimsindikize mahali. Haikuwa kawaida hata kidogo lakini kwa sababu alikuwa ameniomba msamaha tayari niliona kuwa si vibaya nikiongozana naye pasipo na kinyongo. Ilikuwa yapata saa moja za usiku. Tukaondoka na kufika katika nyumba ambazo hayakuwa makazi ya watu wengi. Nikamuuliza mama mdogo tunaenda huko kufanya nini, akaniambia kuna marafiki zake huko anaenda kuwapelekea mzigo wao wampatie pesa zake. Sikujua kabisa ule mzigo nilikuwa mimi.
Nilipofika nikamuona anakabidhiwa pesa zake na kisha kutoweka!!
Nilipiga kelele kumuita lakini hakuniitikia. Na wale watu wakanikamata kwa nguvu sana.
Nikawa nimetekwa rasmi hadi hivi ninavyozungumza nanyi!!! Ikitokea natoka hapa salama Mungu atanisamehe kwa sababu nina hasira kali sana nitamfanya mama mdogo jambo lolote baya na kama kufa ni heri tufe wote!! Mtanisamehe siwezi kuudanganya moyo wangu eti naweza kumsamehe yule mwanamke katili.
Nitamuua!!!” alimaliza kuzungumza kijana yule.
Grace akadakia.
“Kabla ya huyo mama mdogo hivi ni kwanini tusianze na hawa wanaojifanya wao ni Israel waliotumwa kutoa roho zetu??”
Aligeuka na kuwatazama wanaume wale waliokuwa wakivuja damu pale chini!!
Akiwa hajapata jibu lolote lile mara kutoka nje ikasikika sauti ikiita.
“Prospa eeh!! Oya Prospaa bado tu!!”
Grace akatufanyia ishara za sote kuiziba midomo yetu!!
Nilikuwa natetemeka na sikujua hata ni kitu gani kitafuata!!!
Kutoroka lilikuwa jambo gumu sana!!!
JIFUNZE!
HAKUNA kitu kizuri katika maisha kama roho ya KUTHUBUTU…. Ukiwa mtu wa kutolea mambo maamuzi bila ya kuthubutu kila siku utabaki kuyaona maisha ni magumu sana.
Ni heri yule aliyethubu na kushindwa amejiongezea ujuzi katika maisha yake kuliko ambaye aliamua kushindwa tu bila kuthubutu!!!
Hata hivyo sio kila kitu uthubutu kukifanya thubutu katika mambo ya msingi!!!
******************************
Yule mtu aliendelea kuita kutokea nje lakini hakuna jibu lolote lililotolewa kutoka mle ndani.
Yule mtu kule nje naye akakoma kuita baada ya muda tukasikia sauti zikinong’ona kule nje. Kisha kimya kikatanda, na mara ghafla milango ilifunguliwa na wanaume watatu wakavamia mle ndani.
Grace akajitosa tena kukabiliana nao lakini safari hii balaa likawa upande wetu, Grace akakutana na panga kali, akatega mikono yake ili kujikinga na kujikuta ameyashika yale makali.
Najisikia vibaya sana kwa sababu kumbukumbu ile kamwe haitaki kutoka katika kichwa changu. Ushike moyo wako ewe mtanzania na ulidake chozi la albino!!!
Nakumbuka jinsi mtu yule aliyekuwa ameshikilia lile panga alivyolivuta kwa nguvu sana na kusababisha mikono ya Grace ikachanika vibaya sana na kabla hajaweza kujitetea kwa macho yangu nikamuona yule mtu mtanzania mwenzetu akilinyanyua panga lake kali na alipolishusha Grace alianguka chini na kamwe hakuweza kusimama tena. Hawakumuacha alivyo, waliendelea kumkata wakaitoa kabisa mikono yake.
Grace alitapatapa pale chini na kuna muda niligonganisha naye macho ni kama alikuwa akihitaji nifanye kitu lakini sikuwahi kukijua kamwe.
Nilitamani kufanya lolote ili kumuokoa lakini miguu haikuwa na nguvu kabisa. Fahamu ni kama zilikuwa zinaniruka na kurejea kila baada ya sekunde kadhaa. Niliuona mwili wa Grace ambao ndani ya muda mchache uliopita ulikuwa wima sasa ulikuwa umeanguka chini sikuwai kuiskia sauti ya Grace tena. Binti yule mrembo na jasiri. Ahadi zote alizokuwa amefanya kwa kijiji na familia yake zikawa zimeishia pale pale.
“Yeyote atakayethubutu kuleta fujo zozote zile hatutamuonya badala yake tutamfyeka mara moja.” Alikaripia yule bwana huku panga likiwa bado linavuja damu!!!
Damu ya mwanadamu!
Hakuna hata mmoja kati yetu ambaye alikuwa anazungumza kila mmoja alikuwa amejikunyata kivyake!!
Grace akafutika katika ramani ya duniani kwa hujuma za watu wachache wapuuzi!!
Tukiwa bado eneo lile mara simu iliita kutoka mifukoni mwa yule bwana. Akazungumza kwa dakika chache kisha akamaliza na kuwaeleza wenzake kuwa kinahitajika kitovu cha mtoto.
Nilisisimka sana nikageuka kumtazama yule mtoto hakuwa akilia alikuwa ametulia tuli ni kama aliyekuwa akifuatilia kila tukio lililokuwa linaendelea!!! Niliamini alikuwa akitazama vyema ili siku ya kiama awashtaki kwa Mungu aliyetuumba!!
Yule bwana akapiga hatua ili amchukue yule mtoto nikaona hapana ngoja nijaribu kufanya lolote kwa ajili ya yule mtoto, nikamshika yule mtoto na kumkumbatia kwa nguvu, ndugu msikilizaji sikuwa tayari kuona unyama ule mbele yangu sikutaka kushuhudia kitovu cha mtoto yule asiyekuwa na hatia kikitolewa.
“Unakiita kifo kijana!!” alinieleza baada ya kufika pale na kukuta nimemkumbatia mtoto kwa nguvu sana.
Hakurudia tena kuongea ananipiga kwa kutumia ubapa wa panga lake.
Niliyapata maumivu makali lakini sikumuachia yule mtoto nikaendelea kumngángánia walinipiga sana hatimaye nikasalimu amri nikamuachia wakamchukua.
Naam kwa macho yangu yote mawili nikamshuhudia yule mtoto mdogo asiyekuwa na hatia akipewa hukumu kubwa sana.
Nilijiuliza sana ikiwa wale wanaume walikuwa wameumbwa na Mungu huyu ambaye aliniumba mimi na wewe unayesikiliza na kusoma simulizi hii. Kama kweli ni Mungu aliwaumba basi alikuwa ananipa mtihani mkubwa sana wa kuyashuhudia yale lakini kwa akili yangu nilihisi wale ni mali ya shetani laiti kama wangekuwa wa Mungu wala wasingeweza kumfanya vile mtoto asiyekuwa na hatia.
Yaani wakamkata kata huku wakisaidizana!!
Mwili wangu uliingiwa na ubaridi sana nikashindwa hata kulia nikajihisi kupararaizi. Moyo wangu nao ulikufa ganzi, nilimwomba Mungu anichukue upesi ili niweze kuyakwepa mambo mawili kwa pamoja. Kwanza nikiepuke kifo kile cha mateso ama nikwepe kabisa kushuhudia tena mwenzangu akikatwakatwa mapanga.
Ajabu macho yaliendelea kuwa na nguvu za kuona. Sijui ilikuwaje labda ni Mungu alipanga iwe vile.
Baada ya kumalizana na yule mtoto wale watu sasa kwa hasira walinifuata mimi na kitu cha mwisho nilichokiona ni jinsi walivyokuwa wakinyanyua mapanga yao juu na kisha kuyashusha kwa nguvu sana.
Kiza kikatanda!!
Sikujua kilichoendelea tena.
****
Nilikuja kurejewa na fahamu tena nikajikuta nipo katika kitanda cha kamba, nilitaka kujigeuza na hapo nikatambua kuwa nilikuwa napatwa na maumivu makali sana.
Nikajitazama ni kitu gani kilikuwa kinanitokea hadi naumia vile!!
Ndugu msikilizaji moyo wangu ulipiga kwa nguvu sana yaani ulipiga kwa nguvu mno!!
Nikajaribu kuyafumba macho yangu na kuyafumbua tena huenda nitaona kitu tofauti lakini yaliendelea kuona kitu kilekile.
Mkono wangu ulikuwa haupo!!
Mkono wangu ulikuwa umekatwa mpenzi msikilizaji!!
Nilianza kulia kwa sauti ya juu, nililia sana na hapo wakatokea wazee wawili na mwanamke mmoja.
Wakaanza kusemezana kikabila.
Sikusubiri wazungumze nami neno lolote nikaanza kuwaambia kwa uchungu.
“Kwanini mmeniacha hai, ni kwanini nasema mmeniacha hai kwanini hamkuniua. Mmeuchukua mkono wangu kwa nini hamjauchukua uhai wangu, niueni niueni sasa hivi mashetani wangu…” walikuwa kimya tu na mimi nikanyamaza na kuzitazama nyuso zao zilizokuwa katika mshangao. Hawakufanania na wauaji hawa, hawakufanana hata kidogo.
Sasa ni akina nani hawa!!!
Nilijiuliza bila kupata majibu. Na baada ya mimi kunyamaza mzee mmoja alinisogelea kidogo huku akionyesha ishara za kunituliza.
“Tulia mjukuu wane… tulia mjukuu…” alinisihi na mimi nikatulia nimsikilize atakalosema.
“Hatuui sisi.. sisi wazuri tu… wazuri kabisa mjukuu wangu. Wazuri sana tulia mjukuu wangu..” alinisihi yule mzee.
Amakweli sauti ya mwema itabaki kuwa ya wema tu. Inajulikana moja kwa moja!!
Nafsi yangu ikahisi kuwa nipo sehemu salama kabisa.
“Mletee amanche anywe…” alizungumza akichanganya na kikabila ambacho sikukielewa!!
Baada ya muda nikaletewa maji ya kunywa kutoka katika kibuyu.
Nikayagida kwa fujo na hapo nikatambua kuwa nilikuwa nina njaa.
“Njaa inaniuma sana” nikamwambia yule mzee. Na yeye akawaambia wenzake na baada ya muda nikaletewa chakula. Nikala kwa fupo nikitumia mkono wangu wa kulia maana ule wa kushoto haukuwepo tena eneo lake.
Ulikuwa umekatwa na bila shaka kwenda kuuzwa!!!
Baada ya kula chakula niliwauliza wale wazee mkono wangu ulikuwa umeenda wapi. Wakanieleza kwa shida shida kwa sababu hawakuwa vizuri sana katika Kiswahili.
Walinieleza kuwa waliniokota nikiwa nimepoteza fahamu huko porini walipokuwa wameenda kuwinda, mkono wangu mmoja ulikuwa umekatwa na nilikuwa navuja damu sana. Wakanifunga kovu langu na ile ilikuwa siku ya pili ndo nikarejewa na fahamu.
Waliniambia kuwa waliwahi kunihifadhi kwani walitambua ni kitu gani kilikuwa kimenitokea, walikuwa wakizisikia imani potofu za watu wanaokata viungo vya albino.
Kwa maelezo yao na uzoefu wao walidai kuwa kuna uwezekano mkubwa baada ya kukatwa mkono wangu mmoja nilirukwa na akili na kutimua mbio kabla ya kupoteza fahamu.
“Na wenzangu wapo wapi?” niliwauliza. Wakanijibu kuwa hawajamuona mtu mwingine zaidi yangu.
Nikawasihi kuwa nilikuwa na wenzangu wengi tu.
Habari hizo wakazifikisha kwa mwenyekiti wa kijiji, siku mbili baadaye nikaongozana nao kuelekea sehemu ambayo niliwaeleza kuwa tulikuwa pale. Tulizunguka huku na kule hatimaye tukafika lile eneo ambalo ndipo kwa mara ya mwisho mkono wangu ulikuwa bado haujakatwa sasa narejea pale nikiwa sina tena ule mkono.
Wanakijiji kadhaa tulioandamana nao walianza kupekua huku na huku wakidai kuwa watu wale huwa hawasafiri na miili iliyopoteza uhai tayari. Kikubwa huwa wanachukua viungo na kuondoka navyo.
Saa saba mchana jua likiwa limewaka haswa tukamsikia mbwa akibweka kwa fujo. Awali tulimpuuzia lakini baadaye tukafuata kilio cha mbwa yule wananchi wakiwa na majembe na makoleo walianza kufukua eneo lile.
Mungu wangu!! Nikashuhudia tena magumu mengine, miili ya wale wenzangu ilikuwa imefukiwa kama mizoga tu ya wanyama wengine, yote ilikuwa imeondolewa viungo kadhaa macho na mikono na sehemu za siri.
Nikauona mwili wa kile kitoto kidogo.
Sikuweza kutazama tena nikaanguka na kiza kikatanda!!!
JIFUNZE!!
MWANADAMU huwa hazaliwi na kisasi, wanadamu wote huzaliwa nafsi zao zikiwa safi kabisa KISASI husababishwa na matukio kama haya unayoyasoma katika simulizi hii. Unadhani mtu ameshuhudia yote haya atashindwa vipi kuwa na kisasi!!
Usimlaumu mwenye kisasi jitahidi kwanza uijue simulizi ya maisha yake!!!
ITAENDELEA...
0 comments:
Post a Comment