Search This Blog

Sunday, July 10, 2022

USINILILIE MIMI KAWASIMULIE WANAO - 1

 





    IMEANDIKWA NA : GEORGE IRON MOSENYA



    *********************************************************************************



    Simulizi : Usinililie Mimi Kawasimulie Wanao

    Sehemu Ya Kwanza (1)



    Nani ambaye hakulijua jina langu shule ya sekondari Ruvu? Nani hakunijua hata nilipokuwa shule ya msingi Jitegemee? Jibu ni hapana, kila mtu aliyependa michezo na yule asiyependa michezo wote walinifahamu.

    Hakika nilikuwa nacheza mpira wa miguu katika kiwango cha juu sana. Mpira huu ulinipeleka mikoa mbalimbali, na kwa mara ya kwanza ukanifikisha jijini Dar es salaam. Nilikuja kimichezo lakini nikatamani tena na tena kurejea katika jiji hilo siku moja. Nilitamani kuziona starehe wanazohadithia rafiki zangu waliokuwa wakiishi huko, nilitamani kila kitu kuhusu Dar es salaam. Nikaongeza bidii katika kusoma na hatimaye nikamaliza kidato cha sita na kufanikiwa kutimiza ndoto yangu ya muda mrefu.

    Nikachaguliwa kujiunga na chuo kikuu cha Dar es salaam. Nilikuwa mgeni wa kila kitu jijini, lakini na wenyewe walikuwa wageni katika kipaji changu cha kucheza soka na ziada nilikuwa nina uwezo mkubwa darasani. Nikapata marafiki, wanaume kwa wanawake, matajiri kwa maskini, wanaochukua mkopo na wasiokuwa na mkopo.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Katika hao marafiki hatimaye nikampata na mpenzi!!

    Hamisa!!

    Kwa kumpata Hamisa najua nilimuumiza sana Dorice, Hanifa na Getrude. Wote hawa walikuwa wakinihitaji kimapenzi waziwazi, nisiwataje akina Neema, Josephine na wengineo ambao macho yao yalionyesha waziwazi kuwa walikuwa wakinihitaji kimapenzi waziwazi lakini hawakunitamkia wazi. Lakini sikujali sana kuhusu kumuumiza huko maana moyo wangu haukutua kabisa kwao licha ya urembo wao na mali walizokuwanazo. Hamisa akawa chaguo la mwanasoka mimi!!

    “Tuone mtafika wapi, hata mwaka huu hamuumalizi nyie” haya nd’o maneno yaliyowatoka waliouchukia uhusiano wetu.

    Katika mkasa huu sitaki kumshutumu mtu yeyote kwa sababu sina uhakika hata kidogo ni kwa nini haya yananitokea. Mkasa huu naueleza nikiwa sina hata uwezo wa kupiga mpira ukaenda mbali kwa hatua nne, sina uwezo wa kukimbia, uso umebonyea na kuzama ndani kabisa, nguo zangu sikumbuki hata rangi zake maana ninazovaa sijui hata zimetoka wapi. Na ninayasimulia haya nikiwa sina hata uwezo wa kutembea mwenyewe.

    Ni kama mfu tu ambaye kwa bahati ya mtende bado napumua…….



    ****



    TULIZA AKILI YAKO SASA NAANZA KUSIMULIA!!!

    KUMBUKA USINILILIE MIMI BALI KAWASIMULIE WATOTO WAKO!!!



    Ndio kwanza nilikuwa na miezi minne chuoni na kila kitu kilionekana kwenda sawa. Afya yangu ilikuwa imara kabisa na nilinawiri zaidi kutokana na penzi thabiti kutoka kwa Hamisa. Kwa jina naitwa Gerlad Masembo, walizoea kuniita GM ninapokuwa uwanjani huku wengine wakienda mbali zaidi na kuniita ‘Christiano Ronaldo’ hasahasa akina dada. Walisema kuwa nilikuwa na mvuto kama mchezaji yule. Sikujali sana, lakini naitwa Gerlad mjukuu wa Masembo.

    Siku hiyo nilivaa suti yangu nadhifu kabisa, zawadi kutoka kwa Hamisa binti wa kiislamu ambaye hakujali udini kati yangu mimi na yeye alichosema ni kimoja tu ‘Mioyo ikiongea udini hukaa kimya kwa aibu’. Kauli ile ikanipa nguvu sana na penzi likanoga. Tuliandamana na Hamisa hadi mgahawani, maeneo ya Mlimani city. Ilikuwa kawaida ya Hamisa siku nikiwa nakabiliwa na mechi za kimashindano alikuwa akiandamana nami kila kona hii ilinitia nguvu na kunifanya nicheze kwa kujituma zaidi. Hamisa hakuwa mpenzi wa mpira hapo awali lakini mahusiano kati yangu na yeye yalibadilisha kila kitu. Hamisa akawa mfuasi wa kile nilichokuwa nakifanya. Akaupenda mpira wa miguu. “G mpenzi wangu, najua leo utafunga magoli matatu. Moja la kwangu, moja la kwako na la tatu kwa ajili ya mahusiano yetu si ndiyo mpenzi wangu eeh!!” Hamisa alinieleza kwa sauti ya chini huku akipepesa macho yake kunisaili. Nikatabasamu bila kusema chochote na hiyo ilikuwa kawaida yangu hasahasa nikiwa nakabiliwa na mechi ngumu.

    “Na hiyo suti yako ilivyokupendeza watabaki kukushangaa tu, na ukiingia uwanjani usisahau kuvaa ile niliyokununulia sawa, yaani ukivaa ile lazima ufunge…” Hamisa akanieleza nikafahamu anazungumzia nguo ya ndani aliyoninunulia maalumu kwa ajili ya mchezo ule. Nikacheka kwa sauti ya juu kidogo na yeye akacheka. Nikajisikia fahari kuwa na mpenzi anayenijali namna ile. “Nd’o maana mama alinishauri sana kuoa mwalimu….” Nilijiwazia huku nikimtazama Hamisa, ambaye alikuwa anachukua shahada ya ualimu chuoni DUCE.

    BAADA ya stafutahi ile ya nguvu, tulielekea uwanja wa uhuru jirani na chuo cha DUCE, hapo nikamuaga Hamisa na kujiunga na wachezaji wenzangu. Nasikitika kukumbuka kuwa ile ilikuwa furaha yetu ya mwisho kabisa kutoka mioyoni. Na labda ile ilikuwa siku iliyobadili kila kitu katika maisha yetu. Sio maisha ya mapenzi tu… namaanisha KILA KITU.

    MAJIRA ya saa tisa na nusu timu ziliingia uwanjani kwa ajili ya kupasha viungo moto. Nilifahamu vyema ni mahali gani Hamisa wangu ameketi nilijaribu kuangaza labda nitamuona lakini uwanja ulikuwa umefurika sana jambo ambalo sikulitegemea hata kidogo. Ilikuwa ni mechi ya kimataifa kwa ngazi ya vyuo, chguo chetu kilikuwa kinakabiliana na chuo cha Zambia. Wanafunzi watano kutoka chuo cha Zambia walikuwa wachezaji wa timu ya taifa, hivyo sisi kuwafunga ingekuwa gumzo kuu. Na nilitamani kumfunga yule kipa wao ambaye alikuwa pia anadakia timu yao ya taifa. Baada ya kupasha viungo moto tukarejea vyumbani kwa dakika kadhaa, kocha akatupa mawaidha ya mwisho na kututia munkari. Kwa kila alivyoongea nilijua kuwa ni mimi niliyekuwa nategemewa!! Nikajiandaa kumfurahisha Hamisa na timu nzima kwa ujumla lakini kubwa zaidi kuwapa furaha mashabiki.

    Mpira ulianza kwa kasi sana, timu zote zilicheza kwa kasi kubwa huku Zambia wakionekana kutulia zaidi. Katika maisha yangu nilicheza mpira mara kwa mara na nikiwa na umri wa miaka ishirini na nne sikuwahi kufikiria kuwa nakaribia kuachana na soka. Lakini dakika ya kumi na sita ya mchezo kila ndoto yangu ilifutika. Ilikuwa kama utani, niliupiga mpira shuti dogo tu, nikaanguka bila kutarajia!! Nilijaribu kuinuka lakini mwili ukawa mzito sana, nikajaribu tena na tena, mchezaji wa Zambia akajaribu kunipa mkono ili niweze kuinuka lakini haikuwezekana, mguu ulikuwa unauma sana.

    Madaktari wa timu wakafika eneo nililokuwepo, wakaniwekea barafu ya baridi, nikapata unafuu kisha nikatoka nje nikiwa nachechemea huku nikiwa nimewashika mabega yao. Walijaribu kunichua huku wakinipulizia madawa. Uwanja mzima ulikuwa kimya, siku hiyo nd’o nilitambua waziwazi ni kiasi gani nilikuwa nategemewa.

    “Sitaweza kuendelea….maumivu ni makali sana dokta.” Nililazimika kumweleza kauli ambayo hata wachezaji wenzangu uwanjani wasingependa kuisikia. Lakini ilibidi iwe hivyo. Kocha mkuu alionyesha wasiwasi waziwazi, baada ya daktari kumweleza.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mwishowe kibao kikanyooshwa juu, Gerlad Masembo hawezi kuendelea na nafasi yake inachukuliwa na mchezaji mwingine. Uwanja mzima watu wakashika vichwa nikiwatazama kwa jicho langu. Jicho likazunguka na mwishowe nikamuona Hamisa. Alikuwa analia!! Chozi likanidondoka na mimi.

    ****

    Halikuwa tatizo dogo kama nilivyodhani na kila mtu alivyodhania kuwa ni misuli tu ilikuwa imenibana. Nilichua kwa kila dawa, nikajifunga ile mipira ya kukaza misuli lakini wapi hali ilikuwa tete. Kwa siku nne mfululizo sikuweza kutembea mwenyewe bila msaada wa marafiki. Hasahasa wachezaji wenzangu. Maumivu ya mguu taratibu yakahamia mgongoni. Nikawaeleza rafiki zangu kama utani vile, wakasema yawezekana ni kutokana na kulala sana kitandani. Wakaanza kuuchua mgongo wangu pia. Baada ya siku nane nikalalamika kuwa maumivu yalikuwa yanaongezeka badala ya kupungua. Zikachukuliwa hatua, nikapelekwa hospitali ya taifa Muhimbili. Daktari akachukua vipimo vyote kwa utulivu. Mwishowe likatolewa jibu lililomfanya Hamisa apoteze fahamu. Niliambiwa kuwa nilikuwa nina kansa iliyokuwa inashambulia uti wangu wa mgongo. Daktari akaongezea zaidi kuwa hata mguu wangu ulikuwa ukitafunwa na wadudu wabaya na walikuwa wametafuna sehemu kubwa!!

    Ndugu msomaji, sijawahi kulia kwa kipindi kirefu kama ilivyonitokea siku hiyo. Nilikuwa nauelewa vizuri ugonjwa wa kansa, mbaya zaidi naambiwa ilikuwa inakula uti wa mgongo. Yaani kuanguka uwanjani kidogo vile naambiwa nina kansa. Daktari alivyoelezwa kuwa nilikuwa nacheza mpira na sijawahi kupata walau mushkeri wowote uwanjani alikataa kata kata na kudai kwa namna nilivyoshambuliwa nilitakiwa kuwa kitandani miezi minne hadi mitano iliyopita. Ajabu haikuwa hivyo!! Kansa gani hii ya maajabu. Nililia sana, Hamisa yeye aliendelea kuwa kimya akiwa amepoteza fahamu.



    JIFUNZE…. Dakika moja ni kubwa sana katika maisha yako, dakika moja unaweza kuwa unacheka lakini dakika inayofuata kikafuata kilio cha milele. Kilio kisichopoozeka na ambacho kinaweza kukuachia jeraha la milele huku likitoneshwa kila kukicha. Ishi kwa tahadhari kubwa!! Iheshimu LEO yako na ujipange kwa KESHO yako kila wakati.





    Mwanzoni watu waliokuwa wanakuja kunitembelea walikuwa wengi sana. Kila mgonjwa aliyelazwa katika wodi niliyolazwa mimi alijua kabnisa kitanda kile amelazwa mwanafunzi wa chuo kikuu. Vyakula vililetwa kwa wingi, nikawa nawagawia wagonjwa wenzangu karibia wodi nzima. Hospitali pabaya sana, pasikie tu ukiwa unapita kwa nje na kuliona jengo liking’ara kwa rangi murua lakini usiombwe kulazwa ndani yake. Kila ndani ya siku nne nilishuhudia mgonjwa mmoja ama wawili wakikata roho mbele yangu. Hali hii ilinitesa sana. Maneno ya mgonjwa mmoja aliyekata roho usiku mmoja baada ya kusema nami kwa kirefu yaliishi nami kwa kipindi kirefu.

    “Gerlad. Nikikutazama wewe najiona mimi ndani yako, wakati naanza kuugua huu mguu, nilikuwa natembelewa na watu wengi sana, yaani hadi nikawa nanenepa wakati mguu huu upo katika hatihati ya kukatwa. Lakini taratibu wakaanza kupungua, wakabaki kunijulia hali katika simu tu. Akabaki mke wangu. Hata nisimuite mke wangu labda niseme hawara tu yah! Tumuite hawara ama Malaya ukitaka kumuita hivyo (akakunja sura akafumba macho yake kisha akameza funda la mate)…. Huyo hawara siku za awali alikuwa anaonyesha mapenzi motomoto, mama yangu hakuwa akimjua walau kwa sura sembuse jina. Nilimuamini sana, nikampatia kadi yangu ya benki ili awe anatoa pesa na kuja kulipia huduma hapa hospitali, kumbe alikuwa anafanya mambo yake ya ziada yaani pesa yangu ya benki akaitumia kuwanunua madalali wakatafuta mnunuzi akauza nyumba yangu, akauza gari yangu Malaya yule. Nikashangaa ghafla mara leo aje mara leo asitokee, madaktari wakaanza kulalamika kuwa nimelimbikiza madeni, nikimpigia simu mara apokee mara asipokee. Hatimaye akapotea moja kwa moja, taarifa niliyoletewa na mdogo wangu nd’o itakayoniua leo ama kesho nasema. Eti yule Malaya ameolewa na mwanaume mwingine, ameitoa mimba aliyokuwa nayo, yaani ameua kiumbe changu katika tumbo lake, ili aolewe. Huo ukawa mwanzo wa kupata kiharusi, kitaniua hicho. Oooh! Samahani nimesema mengi sana G, ila kikubwa ninachotaka kukueleza ni kwamba usiwaamini na kuwapa maisha yako wanadamu maana si leo wala kesho wanageuka hao. Tena wanageuka vibaya!! No no no simaanishi uwachukie hawa wanaokuletea chakula na kushinda nawe hapa. Lakini ishi kama vile hawatakuja kesho…..” mgonjwa yule ambaye sikukumbuka kumuuliza jina lake alikomea pale kisha akalala, sikutaka kumbughudhi kwa sababu nilijua anao uchungu mkubwa sana. Nikajiahidi asubuhi nitazungumza naye.

    Asubuhi mwili wake ukahamishiwa mochwari!!

    Alikuwa maiti!



    Ile ndoto yake ni kama alikuwa akiniotea kweli mimi. Umati ukaanza kupungua taratibu, Hamisa kila siku alikuwa anakuja kunisalimia, alishinda nami na alilia nami sana. Mapenzi aliyonionyesha sikuyafananisha na ya yule Malaya niliyesimuliwa na hayati nisiyetambua jina lake. Marafiki wakaanza kulalamika kuwa mitihani ya kila mwezi inawabana, mazoezi ya darasani yanawafanya washindwe kufika hospitali. Mtu ambaye alinipa kauli ya kishujaa hadi nikaduwaa alikuwa ni mchezaji ambaye yeye alikuwa anacheza namba kumi mimi nikicheza namba tisa, na mara kwa mara tulipangwa wote katika mechi. “Gerlad Masembo, umekuwa shujaa wetu na kubwa zaidi umekuwa mfano mkubwa kwangu, nitafeli masomo yangu lakini sio kukosa muda wa kukusabahi swahiba wangu, wachezaji wakicheza pacha uwanjani,,,, wanajiandaa kuwa pacha hata katika maisha halisi. Wewe ni pacha wangu!!!” alizungumza kwa hisia, nadhani aligundua hofu yangu juu ya kutengwa hivyo akaamua kuniaminisha kuwa yu upande wangu. Kwa jina aliitwa Joshua Masilingi!! Kwa heshima kuu nilimpatia jezi yangu ambayo niliivaa katika mechi yangu ya mwisho kabisa dhidi ya Zambia kabla sijagundulika kuwa nina kansa. Alinishukuru huku akitokwa machozi!!



    ***



    KAMA utani vile nikashauriwa kusimamisha masomo yangu hayo ya mwaka wa kwanza ili nijikite zaidi katika matibabu, barua ikaandikwa nikaweka sahihi yangu. Mkataba wa kuhudumiwa na chuo ukawa umeishia pale!!! Nikaingia katika maisha mapya! Mkopo na akiba ya ziada iliyokuwa katika akaunti yangu ikafutika, tukahamia katika akaunti ya Hamisa na marafiki wengine. Jitihada zikagonga mwamba. Hali yangu ikazidi kuwa tete. Gerlad Masembo ‘Christiano Ronaldo’ nikaanza kuoza mgongo kwa sababu ya kulala sana. Nilitabasamu na kutikisa kichwa kushoto na kulia siku niliyoamua kuzungumza na Hamisa. “Najua utafikia wakati utaniacha…. Najitahidi kuizoea hiyo hali lakini siwezi. Sijui nitaanza vipi kuishi bila wewe, unadhani ni mwanamke gani wa kuweza kufua kinyesi cha mtu mzima… jitazame Hamisa ulivyokonda eeh! Angalia ulivyopauka. Ona sasa hadi nywele hauendi saluni kisa G. marafiki najua wanakushauri mengi sana, unakuja wakati ambao G atabaki mpweke tena, nguvu za maadui zitalishinda lile pendo imara lililonawiri kwa kipindi kifupi sana. Kama ni kulia nimelia sana, lakini kinakuja kipindi ambacho moyo wangu utavuja damu na nadhani huo utakuwa wakati muafaka wa kumwomba yule Mungu ninayemcha kila leo kuichukua Roho hii upesi kuliko wewe kupotea machoni pangu” Hamisa alijiziba mdomo wake asiweze kuangua kilio kwa nguvu, machozi yalimbubujika na hakufanya jitihada za kuyazuia. Hamisa aliinama kisha akapiga goti na kuanza kusema nami huku akijikaza asitokwe na kilio kikubwa.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Gerlad, mbona umenipa tusi kubwa kiasi hicho mpenzi wangu. Mbona umenihukumu kiasi hicho, umekubali kusikiliza maneno ya watu Gerlad, ni miezi sita nipo nawe, nimewahi kusema unanuka Gerlad? Umewahi kutapika nami nikapika kwa kichefuchefu, ama kuniona hata naziba pua. Nimewahi kulalamika naumwa mbu nikashindwa kulala na wewe, Gerlad … Gerlad naumia Gerlad naumia sana. Niseme nini sasa ujue kuwa nakupenda na nimejitoa kwa kila kitu kwa ajili yako, ama unataka nianze kukueleza kuwa nimefeli masomo matatu natakiwa kuyafanyia mtihani tena, Gerlad nina kiumbe chako tumboni… sina cha kunitenganisha nawe kamwe!!!” Hamisa alimalizia kauli nzito iliyonitoa katika majonzi na kunileta katika mshtuko mkubwa sana. “Whaat!! Hamisa una mimba…. Una mimba… una..” nilitaka kusema neno lakini sikujua ni neno gani.

    “Mimba ya miezi minne…. Niliipata ulipopata nafuu siku ile.” Alinikumbusha siku ambayo aliipata mimba. Nikashusha pumzi kwa nguvu sana huku nikijiuliza huyu ni mwanamke jasiri kiasi gani ambaye hakutaka kunichanganya akadumu na siri hiyo kwa kipindi hicho. Nilistaajabu hakika.

    “Tutazungumza akili zetu zikiwa zimetulia tuli. Naomba tupumzike kwa sasa, nenda shule na uniache mimi katika makazi yangu, mpigie simu mama mwambie mimi nipo salama.” Nilimpa maelekezo Hamisa ambaye alikuwa akijulikana kwa mama yangu mzazi na baba japo si sana. Hadi wakati huo mama hakuwa akitambua kuwa hali yangu ni mbaya kiasi kile na sikutaka ajue maana alikuwa ana matatizo ya presha ya kushuka. Kaka yangu mkubwa chaulevi hakuwa akijua kabisa kama nipo kitandani, na mdogo wangu wa kike alikuwa anatambua kuwa naumwa na ndo kwanza alikuwa kidato cha kwanza.



    ****



    SIKU MBILI BAADAYE!!



    ASUBUHI TULIVU kabisa manesi wakiwa wamekuja kunigeuza upande mwingine maana sikuwa na uwezo wa kugeuka, walipoondoka tu nilipata ugeni. Wageni hawa walikuwa wageni kweli machoni kwangu. Mwanaume na mwanamke, mwanaume sikuwa nimewahi kumwona sehemu yoyote lakini huyu mwanamke akili yangu ikajiaminisha kuwa haikuwa mara ya kwanza kumuona. Lakini nilimuona wapi sasa…. Nesi akawaelekeza wakajisogeza kiustaarabu kabisa kuja katika kitanda changu. Nilijenga tabasamu dogo kwa ajili ya kuwakaribisha.

    “Shkamooni!!” niliwasalimia kwa pamoja nao wakaitikia hivyohivyo kwa pamoja. Kama kawaida wakanipa pole nilizozizoea. Wakaniuliza naendeleaje na mwisho mwanaume akayatawala maongezi huku mama akiwa kimya! “Umesema unaitwa Gerlad, na ninaona rozali hapo na biblia ni vya kwako mwanetu.”

    “Ndio baba, vyangu nimemkabidhi Mungu ugonjwa huu wa kustaajabisha.”

    “Ok! Kumbe ni mkristu eeh..”

    “Haswaa mkristu safi niliye majaribuni” nikajibu kiujasiri, wakati huo akili yangu ikinishawishi kuwa kwa unadhifu wao wale wawili basi watakuwa ni viongozi wa dini. Lakini huyu mwanamke mbona kama nimewahi kumuona?? Nilitamani sana kuuliza lakini nikavuta subira.

    “Ahaa!! Kwa majina sisi tunaitwa bwana na bibi Mustapha… yaani mtu na mkewe..”

    “Nafurahi kuwafahamu….” Nilijibu kama ilivo kawaida.

    “Bwana Gerlad, hatutaki kuzungumza kwa hasira ama shari yoyote mbele yako, maaa sisi ni wazazi na tunaumizwa sana na hali uliyonayo na hatupendi kuona ukiendelea kuteseka. Kwa huruma yetu hii hatutafanya tulichotaka kukifanya kwako, tumekusamehe kwa kumpa mwanetu ujauzito huku ukijua wazi kuwa dini zenu hazifanani. Tunavyozungumza na wewe Hamisa yupo hospitali kwa ajili ya kuutoa huo uchafu wako mapema kabla haujatuletea kero mbeleni. Ukituona tena hapa ujue kuwa Hamisa amepata matatizo wakati wa kutoa mimba hivyo adhabu yetu itakuwa palepale, lakini usipotuona tena basi kwa namna yoyote ile usije ukathubutu kutafuta mbinu za kumwona Hamisa. Tumekuheshimu kwa sababu ya majanga haya yaliyokukuta lakini vinginevyo…….. ubaki salama na ugua pole!!” alimaliza yule mzee kisha akasimama wima akatoa noti kadhaa mfukoni na kuziacha pale kitandani, mkewe akamfuata nyuma wakatoweka. Niliangaza macho huku na kule nikatamani kama ningekuwa na uwezo wa kusimama wima niwafuate lakini sikuweza kusimama. Machozi yakanitoka na kuilaani hali niliyokuwanayo. Punde aliingia Joshua Masilingi, alikuwa amevaa ile jezi niliyompatia. Alipoingia nikaanza kuangua kilio kwa nguvu!!

    Ikawa kazi kwake kunibembeleza……… Joshua alikuwa wa kipekee!! Alizifua nguo zangu bila kinyaa. Alikula nami na alinibeba kunipeleka chooni, Joshua aliniogesha. Eeh! Mungu mlaze mahali pema peponi, wema wake ulimponza Joshua!!!



    JIFUNZE!!! Thamani ya mwanadamu huonekana wakati ule akiwa na mchango katika jamii. Aidha kiuchumi, kimawazo na hata kimichezo. Lakini kile kilichokufanya uwe na thamani kikitoweka nawe unasahaulika mara moja. Wanadamu tuliumbwa na kasumba moja mbaya kabisa, tunathamini kilichopo mbele yetu na kukipuuzia kilicho nyuma yetu. Kwa sababu tu tunaamini uwepo wa macho mbele yetu unamaanisha tutazame vya mbele tu.. tunasahau kuwa tulipewa pia uwezo wa KUGEUKA NYUMA.

    GEUKA sasa umtazame aliye nyuma yako, mtazame masikini, ombaomba, yatima, mjane, na yeyote aliyenyoosha mkono rudi nyuma ukamnyanyue, na Mungu atakubariki!!





    JOSHUA alinibembeleza sana asijue ni kitu gani nilikuwa nalilia. Alijaribu sana kunipooza lakini ilikuwa ngumu sana kukiri kuwa tukio kama lile lilikuwa limetokea. Wazazi wa msichana aliyenipenda nami nikampenda kunifuata na kunieleza maneno makali kiasi kile , hakika lilikuwa pigo kubwa sana upande wangu. Baada ya kutulia nilimsimulia Joshua japo kwa ufupi juu ya kilichokuwa kinaniliza. Japokuwa alijaribu kukwepesha macho yake lakini niliweza kumuona kuwa alikuwa analia. Jambo hilo liliniumiza zaidi na kuendelea kuamini kuwa tukio lililotokea halikuwa la kibinadamu kabisa.

    “Gerlad, huu sio wakati wa kulia. Hilo jambo limetokea tayari, najua kuwa unahisi dunia imekutenga lakini mimi nipo kwa ajili yako, nilisema nitakuwepo na nipo tayari kupoteza kila kitu lakini sio kujitenga mbali nawe.” Joshua alisema nami huku akinifuta machozi kwa kutumia kitambaa alichokuwanacho mkononi. Upendo wa Joshua haukuhitaji ushuhuda wowote kuhakikisha kuwa ni upendo wa dhati ama la! Alinitia moyo, nikaimarika sana na kujiona kuwa licha ya kuwa naozea kitandani bado nilikuwa na thamani kubwa mbele ya watu wengine. Nikapiga moyo konde na kujiona mshindi, lakini huo ushindi uliendelea kuishi Joshua akiwa pembeni yangu, alipotoweka nikakabiliwa na upinzani mkubwa dhidi ya jeraha la moyo lililoanza kunishambulia, nikaanza kujihisi kumkosa Hamisa pembeni yangu, nikailazimisha akili yangu iamini kuwa naweza kuishi bila yeye lakini moyo ukasema nami. Moyo ukanisihi nisiwe mnafiki sikuweza kuishi bila Hamisa. Machozi yakanitoka tena, nikajifunika shuka gubigubi, na manesi wakafika kwa ajili ya kunigeuza ubavu mwingine .CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Usiku huu nao ukapita!! Majira ya saa nane usiku nilijikuta naanza upya zoezi la kuusaka usingizi na kupambana na mawazo yaliyokuwa yakiushambulia ubongo wangu, nikakitazama kifua changu kilichokuwa kimepasuka pande mbili enzi hizo kutokana na mazoezi makali, sasa zilikuwa ni idadi ya mbavu zilizoweza kuhesabika, nilijisikitikia. Nikazitazama mbingu na kumuuliza Mungu swali.

    “Ni kitu gani labda nilikosea baba!! Ni njia gani isiyokuwa sahihi nilipita baba yangu, mbona kila mara niliyainua macho yangu na kukuomba wewe… sijawahi kumtumikia mungu mwingine zaidi yako, sijawahi hata kukusahau licha ya umaarufu na kipaji nilichokuwa nacho…. Ni wapi baba nieleze nirekebishe” Sikupata jibu usiku ule, japo niliamini Mungu wetu halali wala hachokli kutusikiliza, majibu yake niliyapata asubuhi. Uongozi wa hospitali uliamua kuwa hakuna tiba zaidi ninayoweza kuipata katika kitanda kile na kwa madaktari wale. Nikatakiwa aidha kusafirishwa hadi India ama la nirejeshwe nyumbani nikalale huko. Nikalale hadi mauti yangu!!!

    Neno hilo liliniumiza sana lakini haikuwa ndoto, nilipatiwa juma moja tu la kuwa katika kitanda kile na baada ya pale sikutakikana tena. Na hata huduma zilishia pale, walibakia wauguzi tu wa kunigeuza na kunibadilishia mashuka, pia akabaki Joshua aliyeniogesha na kufua nguo zangu.

    “Kwanini ulikufa Joshua eeh! Kwanini uliondoka wakati hata sijafahamu kwenu, sijamfahamu baba wala mama yako, niwape shukrani tu kwa ajili ya kukuzaa kijana ujuaye vyema somo la utu na ubinadamu kwa ujumla…..”



    *****



    JOSHUA alihaha huku na kule, hakuhudhuria tena darasani, aliamua kuwa mzazi wangu!! Najua alipitia magumu mengi tu japo hakutaka kunieleza. “Nimezungumza na mama…… amesema anajiandaa kuja huku Dar es salaam. Anadai kuwa ameuza kiwanja chako alichokurithisha babu yako, na pia kuna mahali amekopa kiasi cha pesa aweze kufika huku…” Joshua alinieleza zikiwa zimebakia siku tatu tu niweze kuondolewa uhalali wa kuwa katika kitanda kile. Nilimjengea picha mama yangu!!

    Tatizo ambalo chuo changu wameshindwa kulitatua, hospitali nayo ikashindwa kunivumilia, wazazi wa Hamisa na wao wakaliona kubwa… leo hii anaenda kubebeshwa mama yangu mzazi. Mama aliyeuza mifugo yote niweze kusoma, mama mwenye ugonjwa wa shinikizo la damu la kushuka. Atafanya nini na hili tatizo kama sio kujiua kwa shinikizo hilo, nilitamani sana kumweleza Joshua amzuie mama asije Dar lakini ningepelekwa wapi iwapo asingekuja?? Kwa shingo upande nikamshukuru Mungu kwa mtihani ule na kwa imani thabiti nikamwomba anionyeshe njia!!!



    ****



    GHARAMA zilikuwa juu sana, Joshua hakuwa na pesa na hata mama hakuwa akijiweza na sikuwa na ndugu jijini Dar. Hospitali haikutuelewa kwa namna yoyote ile. Joshua akaonekana kukata tamaa, mama akawa mtu wa kulia tu na kuomboleza. Kilio cha mama kikanijengea picha moja tu mbele yangu, picha ya kaburi!! Mama alikuwa akijiandaa kunizika na hata kilio chake kilimaanisha vile. Kutambua kuwa nipo katika siku za mwisho za uhai wangu nikatamani jambo moja tu ambalo litahitimisha safari yangu fupi ya furaha na ndefu ya maumivu makali kupindukia. Nikatamani Hamisa aseme nami walau neno moja tu ili niwe huru katika moyo wangu.

    Nikaamua kupigania kitu kimoja ambacho walau kilionekana kuwa kinawezekana, nikamueleza Joshua juu ya hisia zangu za nafsi na ni kwa namna gani nahitaji kuonana na Hamisa walau kwa dakika chache tu. Sikutaka kumueleza wazi kuwa najihisia kuwa nakaribia kuiaga dunia maana Joshua angeanza kulia. Nilimuelekeza nyumbani kwao Hamisa pia nikamweleza juu ya ‘hosteli’ aliyokuwa akiishi. Joshua akatoweka huku akinihakikishia kuwa lazima atarejea na Hamisa hapo hospitali. Ulikuwa kama muujiza, masaa mawili baadaye nikapata ugeni wa ghafla pale hospitali. Alikuwa ni Hamisa!! Hakuwa na tabasamu hata kidogo na sura yake ilikuwa imepauka, badala ya kujisikitikia mimi nikajikuta namsikitikia yeye. Akili yangu ikakumbuka kauli ya Hamisa mara ya mwisho, alinieleza kuwa yu mjamzito. Nikalitazama tumbo lake, lilikuwa wazi kabisa kwamba yu mjamzito.

    “Kama ni kufa basi tutakufa wote G…. kama ni mateso naamini tutayapata wote. Na ninajisikia fahari kuteseka namna hii kwa ajili yako. Wasichana wa chuo waliokutaka kimapenzi wamenicheka sana kwa hali hii lakini nd’o kwanza nimezidi kupata nguvu!!....” kabla hajaendelea kuzungumza zaidi nilimkatisha kwa swali fupi sana.

    “Mbona upo hivyo….”

    “Siishi nyumbani G, wazazi walipanga nikatoe hii mimba. Nikaamua kutorokea huko Kimanzichana kwao rafiki yangu mmoja. Na nimetokea huko kuja hapa….”

    “Inamaana sio Joshua aliyekufuata??” “Mungu weee! Joshua ameenda nyumbani???” aliuliza huku akionyesha wasiwasi wa hali ya juu. Nikamweleza juu ya hali yangu ilivyobadilika na nikahitaji kuonana naye hivyo nikamuagiza Joshua amtafute. Bila kuaga Hamisa aliondoka mbiombio, nikatamani kugeuka upesi nimuite lakini nd’o nilikuwa sijiwezi hata kugeuka.

    Nikabaki kusononeka huku nikijiuliza ni kitu gani kinatokea?? Hamisa hakurudi na hata Joshua hakutokea tena!! Hadi ulipofika ule wakati wa kuumiza zaidi, wakati wa mama kurudishiwa kile alichokileta duniani kwa uchungu, alichokihifadhi tumboni miezi tisa kwa mateso makali. Mama aliyekuwa na mategemeo tele kuwa baada ya kufanikiwa kuifikia elimu ya chuo kikuu basi nilikuwa nakaribia kuwa mkombozi wake, ndoto zake zikafutika ukarejea tena ule uchungu wa miaka mingiiliyopita, uchungu wa kuzalishwa na wakunga wenye elimu ndogo kabisa juu ya uzazi.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Hospitali ikamkabidhi mama yangu mwili huu uliokuwa unazidi kuoza. Akameza mate kwa uchungu, akaikaza kanga yake chakavu iliyokuwa na picha ya mgombea udiwani kijijini kwetu, nikamtazama miguu yake ilivyopauka, macho yakapanda hadi katika mikono yake yenye misuli mingi kutokana na kufanya kazi za suluba, mwisho nikagonganisha macho na mama aliyekuwa anatetemeka. Machozi yakamtoka akakimbilia pale kitandani na kuniokumbatia sote tukatokwa na kilio kikubwa…. Mama alilaani umaskini, akawalaani wanbadamu kwa roho zao za kutu. Akalaani kizazi cha yeyote yule aliyetumia nguvu za giza kunipa mateso yale. Akalaani karibia kila kitu.. mwisho akalilaani tumbo lake kwa kunizaa mimi niteseke kiasi hicho. “Ni bora usingekuja duniani Gerlad, ni bora usingekuja kunipa ushuhuda mbaya kama huu. Unateseka mwanangu, unateseka Gerlad weee!! Unaumia mwanangu, si haya maumivu nihamishiwe mimi mama yako, sina elimu umri nilioishi unatosha kabisa, nife mimi Gerlad usome mwanangu, nife mimi Gerlad unizike mwanangu….. “ Mama hakuweza kuendelea kuzungumza madaktari na manesi waliwahi kumtoa pale kitandani kwa sababu alikuwa akisumbua wagonjwa wengine katika wodi ile na wodi ya jirani.

    Wanafunzi wa chuo kikuu niliokuwa nimeanza nao mwaka wa kwanza, walikuwa wamemaliza hatimaye ‘SEMISTA’ ya kwanza.. na mimi nikaimaliza SEMISTA ya kwanza ya mateso kitandani!!

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    __________ JIFUNZE: CHOZI la mama ni la gharama kuliko kitu chochote duniani, likidondoka chini akiwa amefurahi amini ni furaha toka moyoni. Akilidondosha kwa sababu umemuudhi/umemkosea, fanya upesi kumwomba msamaha maana litakugharimu ukilidharau. Mwanamke anaonekana kuwa mtu dhaifu katika muonekano wa nje.. lakini OLE WAKO WEWE UNAYEMDHARAU MAMA kutokana na muonekano wake..….. hawakukosea waliposema mama ni Mungu wa dunia hii, anatuzaa na kutulea… jihadhari asije akakulaani!! Mama wa mwenzako ni MAMA YAKO!! _________

    TOA MAONI YAKO!!!



    ITAENDELEA……

0 comments:

Post a Comment

Blog