Simulizi : Dimbwi La Damu
Sehemu Ya Tano (5)
Masaa mawili kabla nyumba ya Manjit kulipuliwa kwa moto na majambazi waliotumwa na wafanyabiashara maadui zake, Leah na Victoria waliondoka kwenda kula chakula cha usiku katika mgahawa wa Foodmasters uliokuwa hatua chache tu kutoka nyumbani kwao, cha kushangaza siku hiyo wote wawili hawakutaka kula chakula cha kupikwa nyumbani. Kokote alikokwenda nje ya nyumba Victoria hakukisahau kipande cha noti walichogawana na kaka yake, alikuwa tayari kupoteza vitu vingine vyote lakini si kipande hichoCHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Ghafla wakiwa katika mgahawa huo kabla hata chakula hakijaletwa walishutshwa na mlio ya ving’ora vya magari ya zima moto vikipita kwa kasi kubwa nje ya mgahawa.
Kila mtu alionyesha mshangao mkubwa na kilichofuata baada ya ving’ora hivyo ulikuwa ni moshi mkubwa ulioonekana kuzunguka maeneo ya nyumba yao, Leah alishtuka sana na kukimbia kwenda nje ya mgahawa akiwa amemshika Victoria mkono, nje alimwigiza ndani ya gari na safari ya kurudi nyumbani kwao ilianza haraka!
“Dada kuna nini?”
“Moto, moto unawaka?Sijui ni nyumbani kwetu?”
“Moto? Nyumbani kwetu?”
“Ndiyo!”
“Haiwezekani dada!” Kuna wakati Victoria alimwita Leah mama na wakati mwingine alimwita dada, alishindwa atumie jina gani.
“Acha twende tukaangalie!”Alisema Leah akiliendesha gari lake kwa kasi kubwa, mapigo ya moyo yalikuwa yakienda kwa kasi kubwa, walivyozidi kukaribia dalili zote zilionyesha kuwa ni nyumba yao iliyokuwa ikiungua! Kadri alivyozidi kuelekea nyumbani ndivyo moto na moshi ulivyozidi kuongezeka.
“Ni nyumba yetu!” Leah alisema akimpigapiga Victoria begani.
“Imeungua?”
“Ndiyo inaungua na sijui nini kimetokea mpaka ikashika moto! Kwanini matatizo yamekuwa mengi kiasi hiki kwetu?” Alijiuliza Leah bila kujua la kufanya.
Bila kutegemea machozi yalianza kumtoka kwani vitu vingi vyenye thamani vilikuwa vimeungulia ndani ya nyumba yao, roho ilimuuma sana Leah. Kwa matatizo waliyokuwa nayo katika familia yao alijua tayari walikuwa wamekwisharejea katika umasikini! Leah alikata tamaa!
“Tutafanya nini sisi? Manjit nae ana madeni ya mamilioni ya dola za watu, tutakuwa wageni wa nani sasa?” Alijiuliza Leah huku akilia! Muda wote akiwa amekumbatiana na Victoria wote wakilia.
Ghafla bila kutegemea jambo hilo Victoria alishtukia Leah akichomoka kutoka mikononi mwake na kuanza kukimbia kwenda mbele , kwa jinsi hali ya joto ilivyokuwa mahali waliposimama pamoja na kutokuona Victoria alijua lazima Leah alikimbilia motoni!
Victoria alianza kulia akipiga kelele na kuomba msaada huku nae akijaribu kutembea taratibu kwenda mbele akiita jina Leah kwa sauti ya juu.
“Dada Leah! Dada Leah! Dada Leah! Uko wapi?” Alisema huku akizidi kutembea kwenda mbele zaidi.
Hakusikia sauti ya Leah ikiitika mahali popote na joto lilizidi kuongezeka, moto nao ulizidi kuwaka kuelekea mahali aliposimama, mara ghafla alishtukia akinyakuliwa na mikono mikubwa na mazito ya mwanaume!
“Wewe unafanya nini hapa wakati moto unakuelekea? Utawaka ohooo!”
“Dada yangu ameingia ndani ya moto, dada yangu ameingia ndani ya moto! Tafadhali mtoeni!”Alizidi kulia.
“Ameingiaje?”
“Amekimbilia ndani tu!”
“Kwanini?”
“ Hii ni nyumba yetu!”Alizidi kueleza Victoria huku akilia.
Ilikuwa ni mikono ya mtu wa zimamoto alimchukua victoria na kwenda kumkalisha mbali kabisa ya moto! Ambako Victoria alikaa na kuendelea kulia akijua wazi Leah alikuwa amejiua motoni, alikuwa ameamua kuteketea pamoja na nyumba na vitu vyao.
Nusu saa baadaye watu wengi walifurika eneo la tukio wakishangaa na miongoni mwao alikuwepo Manjit aliyekuwa amerejea nchini Canada kutoka Baghdad muda mfupi kabla!
******************
Manjit aliumia sana moyoni mwake kuona nyumba yao ikiteketea, aliamini mama yake pamoja na Victoria walikuwa ndani ya moto huo! Bila hata kusita aliamua kukimbia kuelekea ndani ya jengo kwa lengo la kwenda kuwaokoa Victoria na mama yake Leah! Mbele kidogo moshi mkali ulijitokeza akawa haoni mbele yake, akashindwa kusonga mbele na kugeuza akikimbia kurudi nje! Alifanikiwa kutoka hadi nje ya jengo ambako alifikia mikononi mwa maaskari wawili wa Zima moto! Walimkatama na kumkimbiza hadi sehemu alipokalishwa Victoria na kuanza kumpepea kwa sababu alionekana kushindwa kuhema vizuri!
“Kifua chake kimejaa moshi hebu mpelekeni hospitali haraka!” Aliamuru mmoja wa maaskari na Manjit alinyanyuliwa haraka na kupakiwa ndani ya gari la wagonjwa kukimbizwa hospitali ambako aliwekewa mashine ya oksijeni na dakika kama ishirini hivi baadaye alirejea katika hali yake ya kawaida na kuanza kulia akiomba aonyeshwe mahali mama yake na Victoria walipokuwa!
“Mama yako bado hajaonekana ila Victoria yupo!”
“Mama yuko wapi? Naomba basi mmlete hata Victoria niongee naye nina uhakika atakuwa anafahamu mahali mama alipo, mali si kitu kwangu ninachotaka ni mama yangu peke yake!” Alisema Manjit huku akizidi kulia, hakuugua mahali popote mwilini kwake.
Hali yake haikuwa mbaya hata kidogo na angeweza hata kuruhusiwa kutoka wodini lakini madaktari hawakufanay hivyo baada ya kupewa taarifa kuwa alitaka kuingia ndani ya nyumba iliyowaka moto ili afe! Walizidi kumweka wodini hadi asubuhi ya siku iliyofuata aliporuhusiwa na kupelekwa chini ya uangalizi wa polisi hadi eneo la tukio na kushuhudia shughuli za uzimaji wa moto zikimalizika! Mtu wa kwanza kumwona mahali pale alikuwa ni Victoria, alimkimbilia na kukumbatiana kwa furaha.
“Anti Vicky mama yupo wapi?” Aliuliza baada tu ya kumbusu kila upande wa shavu lake!
“Alikimbilia kwenye moto! Hivyo atakuwa amekufa!”
“Hapana haiwezekani! Mama hawezi kufa”
“Ni kweli, mimi nilikuwa naye hadi mara ya mwisho, alichomoka mikononi mwangu na kukimbilia motoni, nina imani atakuwa amekufa!”Alisema Victoria akilia na wote walikumbatiana na kuendelea kulia, ilibidi waondolewe hadi hotelini ambako Manjit alipanga vyumba viwili na yeye na Victoria waliishi wakiangalia ni nini cha kufanya baada ya hapo! Kilikuwa ni kipindi kigumu sana kwa Manjit na Victoria, Manjit alishindwa kuelewa ni nani aliyekuwa akimfanyia hujuma hizo! Kilikuwa ni kitendawili alichoshindwa kabisa kukitegua.
Akiwa hotelini alizidi kumtafuta mama yake akiamini bado alikuwa hai, alitangaza hata katika vyombo vingi vya habari na kuahidi zawadi kubwa kwa mtu yeyote ile angefanikisha kupatikana kwa mama yake, lakini kwa masaa mengi hakuna mtu hata mmoja aliyejitokeza kudai kumwona Leah! Manjit alizidi kuchanganyikiwa na hakujua kipi cha kufanya!
Siku ya tatu wakati watu wa idara ya Uokoaji wakiendelea na kazi ya uokoaji walikuta mabaki ya binadamu aliyeungua vibaya katika chumba kilichoonekana kuwa sebule, ingawa ilikuwa si rahisi kufahamu kama mabaki hayo yalikuwa ya mama yake au la, Manjit alilazimika kuamini hivyo na mazishi ya heshima zote yalifanyika, akaamini kuwa huo ndio ulikuwa mwisho wa mama yake! Akabaki na mtu mmoja tu aliyemtegemea nchini Canada, huyo hakuwa mwingine bali Victoria.
Ikiwa ni wiki moja baada ya mazishi ya mama yake, vituo vyake vyote vya mafuta vilikamatwa na shirika la kodi nchini Canada, kwa madai ya kuchunguza kama Manjit alilipa kodi zake sawa sawa, vituo vyote vilitiwa makufuli, wafanyakazi wote wakaondolewa na maaskari waliwekwa kuvilinda! Kifupi hali ilikuwa mbaya mno kwa Manjit! Kwani ni biashara hiyo peke yake aliyoitegemea katika maisha yake. Alishindwa kuelewa angeishije.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Mwezi mmoja baadaye alichukua pesa zake zote zilizokuwa benki na kulipa nusu ya deni la mafuta alilodaiwa na Patrick, akaunti yake ikabaki bila hata senti! Hakuelewa hata kidogo pesa za kumalizia deni hilo angepata wapi, Manjit alitamani kufa lakini alishindwa kuufikiria uamuzi huo kwa sababu ya Victoria! Alishindwa kuelewa angebaki na nani? Huo ndio ulikuwa wasiwasi wake mkubwa, kama Victoria angekufa katika moto hata yeye pia angefuata na wote watatu wangehamia kuzimu alikotangulia baba yake.
***************
Hali haikuwa nzuri pia nchini Iraq, Abdulwakil baba yake Patrick, alikasirishwa sana na kitendo cha mtoto wake kukopesha kiasi kikubwa cha mafuta bila kumshirikisha.
“Ulikuwa mgonjwa baba!”
“Pamoja na hayo yote lakini kwanini ulimkopesha mtu ambaye hana uwezo wa kulipa?”
“Baba, Manjit amekuwa mteja wetu wa muda mrefu na isitoshe alionyesha karatasi zake za zabuni ya kuuza mafuta jeshini! Niliona anafaa nikaamua kumpa mafuta”
“Haiwezekani ni lazima afikishwe mahakamani ili ashinikizwe kulipa pesa hizo!”
“Sawa baba!”
Siku iliyofuata Patrick aliwaita wanasheria wa kampuni yao ofisini na kuwapa majukumu ya kuhakikisha Manjit anakamatwa na kufikishwa mahakamani haraka iwezekanavyo, ili kumshinikiza alipe deni alilodaiwa.
“Sawa mzee, tufanya kazi hiyo lakini ili iwe rahisi zaidi tafadhali muagizie aje hapa Iraq ili kuwa rahisi zaidi kumkamata!”
“Nitafanya hivyo leo na ninafikiri kesho atafika hapa!”
“Itakuwa vizuri sana!”
Jioni ya siku hiyo Patrick alipiga simu Canada na kumwomba Manjit apande ndege kwenda Baghdad siku iliyofuata ili wapate kuliongelea deni lake na ni kwa jinsi gani angeweza kulilipa! Alimtahadharisha kuwa kushindwa kwake kufika Baghdad kungemaanisha kufikishwa mahakamani na kwa mujibu wa mikataba waliyowekeana ni lazima angefungwa, Manjit hakuwa na la kufanya zaidi ya kukubali kwenda Iraq.
“Lakini nitasafiri na anti yangu ambaye ni kipofu, sitaweza kumwacha hapa Canada peke yake watamuua!”
“Hiyo haina tatizo kabisa!”
Siku iliyofuata asubuhi Manjit na Victoria walipanda ndege ya shirika la ndege la Gufl kwenda Baghdad, ndani ya moyo wake Victoria ilikuwa ni kama kuiaga Canada! Hakuamini kama wangerudi tena katika nchi hiyo ingawa hakuelewa ni kwanini moyoni mwake aliwaza hivyo. Walipotua Baghdad, Manjit alichukua teksi iliyowapeleka moja kwa moja hadi ofisini kwa Patrick, haikuwa shida kumwona kwa sababu alishawataarifu walinzi juu ya ujio wao.
“Pole sana Manjit kwa yaliyojitokeza lakini naamini yana mwisho wake!”
“Mungu anajua tu!”
“Habari za Canada?’
“Ndugu yangu ni kama Ulivyosikia!”
“Sasa itakuwaje katika deni lililobaki?”
“Hata mimi sifahamu maana pesa zote nilizokuwa nazo benki ndizo nilizokupa na sielewi nitapata wapi pesa zaidi!”
“Unasemaje?” Aliuliza Patrick kwa hamaki.
“Kwa kweli sijui mahali pa kupata pesa zaidi!”
“Utalipa tu!”
“Patrick sina biashara nyingine yoyote, vituo vyangu vyote vya mafuta vimefungwa!”
“Hayo mimi hayanihusu utalipa tu sababu umejileta mwenyewe hapa Baghdad! Vinginevyo utaozea jela!”
“Patrick!!!!!!!!!!!!!!!!!!!”
“Nini?”
“Tafadhali nivumilie kidogo au nipe kazi yoyote katika kampuni yako ili niweze kulipa deni langu!”
“Haiwezekani hata kidogo ni lazima ulipe pesa!”Alisema Patrick akinyanyua simu yake.
“Hebu waambie hao vijana waingie upesi!”Patrick alisema na dakika kama tatu baadaye mlango ulifunguliwa wakaingia vijana watano wenye nguvu sawasawa na kuwakamata Manjit na Victoria! Wakaanza kuwavuta kuwatoa ofisini kwao Patrick.
“Hebu huyo mama mwacheni, mpelekeni kituo cha polisi huyo tapeli wa kimataifa, niachieni huyo mama hapa!”
“Sawa bosi!”
Victoria huku akilia machozi alirudishwa na Manjit alitolewa hadi nje ambako alipakiwa ndani ya gari na safari ya kwenda kituo cha polisi ilianza haraka iwezekanavyo.
“Mama huyo kijana ni nani yako?”
“Ni mtoto wa dada yangu!”
“Dada yako mbona wewe mweusi yeye mchanganyiko?”
“Ni habari ndefu sana kijana, ila ninaweza kukueleza ukitaka!”
“Nieleze bibi!”
“Niache kwanza nipumzike, itanitia uchungu sana kuyaongelea mambo hayo, naomba unitafutie chakula na mahali pa kulala ili nipumzike na ninachokuomba sana usimfunge mwenzako ana matatizo makubwa mno!”
“Hata mimi namhurumia bibi lakini baba yangu hataki kabisa, anadai deni hili limemuongezea ugonjwa wake!”
“Nipeleke mimi nikaongee naye labda atanielewa!”
“Sidhani!”
“Wewe nipeleke tu! Kwani baba yako anaitwa nani?”
“Anaitwa Abdulwakil
“Ni mwenyeji wa wapi?”
“Tanzania!”
“Tanzania? Alifikaje huku?” Aliuliza Victoria kwa mshangao.
“Ndiyo! Alikuja miaka mingi sana akiwa mtoto”
“Mbona hata mimi pia nilitokea Tanzania?”
“Kweli?”
“Ndiyo!”
“Basi si ajabu mtafahamiana!”
“Inawezekana!”
Victoria anapelekwa kukutana na Nicholaus bila kufahamu! Baad ya kupotezana kwa miaka mingi!
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Tayari Manjit alishaingia mikononi mwa polisi na alikuwa ndani ya gari akipelekwa kituoni, hiyo ilitokea baada ya kumweleza Patrick ukweli kuwa asingeweza kumlipa pesa alizokuwa akimdai,Victoria aliumia sana moyoni mwake wakati Manjit akiondolewa ndani ya ofisi ya Patrick huku akiliita jina lake, alishindwa angemsaidia vipi Manjit mtu pekee aliyekuwa akimtegemea kwa wakati huo.
Walitoka ofisini Patrick akiwa amemshika mkono Victoria na kumuongoza hadi mahali lilipokuwa gari lake la kifahari aina ya Potsche, na kuingia ndani, Patrick alikaa kwenye usukani na Victoria alikaa kushoto kwake, ilikuwa ni safari kwenda nyumbani kwa tajiri Abdulwakil ambako Victoria alikuwa akipelekwa kuongea na tajiri huyo aliyemiliki visima vingi vya mafuta ili ajaribu kumshawishi asimfunge Manjit kwani ndiye alikuwa tegemeo lake maishani.
“Akiniona katika hali hii ya upofu ni lazima atabadili nia yake ya kumfunga Manjit, Mungu yupo pamoja na mimi ninaamini atanihurumia!” Aliwaza Victoria wakati gari likipita kwenye mitaa ya katikati ya jiji la Baghdad kuelekea nyumbani kwa tajiri Abdulwakil kilometa kumi na tano nje ya jiji.
“Hivi baba yangu atakubali kweli? Sina uhakika anachotaka yeye ni pesa na kama hakuna pesa lazima Manjit atafungwa tu!”
“Mwanangu niache nikaongee naye akikataa basi lakini nitakuwa nimejaribu!”
“Sawa mama!”
Gari lilizidi kwenda kwa kasi na dakika kumi na tano baadaye liliacha barabara na kukata kona kuingia kulia likipita chini ya miti mirefu, mbele zaidi kama nusu kilometa lilikata tena kushoto na kuzidi kutokomea ndani! Hatua kama mia mbili mbele Victoria alisikia honi ikipigwa na mlio wa geti likifunguliwa ulisikika, akafahamu walikuwa wamefika mahali walipokuwa wakienda.
“Asalam alekum!”
“Aleikum salam!”
Alisikia maneno hayo kila walivyozidi kusonga mbele hatimaye gari likasimama kabisa na Patrick alifungua mlango na kuzunguka hadi upande wa pili ambako pia alifungua mlango na kumsaidia Victoria kushuka.
“Tumefika!”
“Kumbe sio mbali?”
“Kwa kweli sio mbali sana!”
Patrick akiwa amemshika mkono Victoria waliongozana na kuanza kupandisha ngazi taratibu, aligundua walikuwa wakiingia ndani ya nyumba, kila mahali walikopita salamu zilisikika na milango ilifunguliwa na wakaingia hadi ndani ambako Victoria alisaidiwa kuketi kitini.
“Karibu mama hapa ndio nyumbani kwetu!”
“Ahsante sana mwanangu, kikubwa naomba unisaidie nikutane na baba yako!”
“Basi nisubiri hapa nikaongee naye” Alisema Patrick, alionekana kumwonea huruma sana Victoria lakini hakuwa na uwezo wa kumsaidia kwa sababu mwenye amri alikuwa ni baba yake mzazi.
“Haina matatizo!” Aliitikia Victoria na baadaye akasikia mlio wa viatu ukiondoka mahali alipokaa.
Alisubiri kwa muda mrefu mno bila Patrick kurejea, alishindwa kuelewa ni kitu gani kilichokuwa kikiongelewa huko ndani! Hofu yake kubwa ilikuwa ni tajiri Abdulwakil kukataa kuonana naye alimwomba Mungu wake hilo lisitokee. Mawazo yake yote wakati akisubiri yalikuwa juu ya Manjit ambaye alikuwa polisi, hakujua ni kitu gani wangekuwa wamemtenda! Alizidi kumwomba Mungu amwepushe Manjit na mabaya yote, hakuwa tayari kushuhudia Manjit akipatwa na tatizo kwani maisha bila yeye yasingewezekana, alikuwa tayari kufa pamoja naye.
Baadaye akiwa sebuleni alianza kusikia minong’ono kutoka upande wa pili, ilikuwa ni sauti nzito ya kizee ikifoka! Hakuelewa ni nini kilichokuwa kikiongelewa kwa sababu maongezi yalifanyika katika lugha ya Kiarabu.
Kadri dakika zilivyozidi kwenda ndivyo sauti ya mzee akifoka ilivyozidi kuongezeka na kukikaribia chumba alichokuwa amekaa, hofu kubwa ilimpata moyoni mwake akijua kitu kibaya kilikuwa kikimfuata! Alianza kulia akimwomba Mungu abadilishe mawazo ya wabaya wake.
“Ee Mungu wangu naomba unisai........!” Alisema Victoria lakini kabla hajaimalizia sentensi yake mlango ulifunguliwa na nyayo za watu wengi zilisikika zikiingia, alikaa kimya akisubiri sauti ya Patrick iongee lakini badala yake alisikia sauti nzito ya mzee ikifoka.
“Yuko wapi huyo? Hawa watu wanafikiri sisi tunafanya mchezo na biashara, ikibidi hata huyu mama tutamfunga pamoja na Manjit!” Alifoka mzee huyo, sauti yake pekee ilitosha kumtisha Victoria.
Victoria aliposikia kauli hiyo aliinamisha kichwa chake na kuuficha uso wake katikati ya miguu yake miwili, kwa maneno yaliyosemwa na mzee huyo alijua taabu kubwa ilikuwa inakuja! Aliumia sana moyoni mwake, alifikiri shida zilikuwa zimekwisha katika maisha yake kumbe haikuwa hivyo alitakiwa kupambana na matatizo mengine tena.
“Hebu mleteni hapa!” Aliamrisha mzee huyo na Victoria alibebwa juujuu na kupelekwa moja kwa moja hadi mahali mzee huyo alipokaa.
“Nisamehe sana mzee, naomba unisikilize kwanza ninachotaka kusema!”
“Onyesha uso wako kwanini unaficha sura? Hebu mnyanyueni sura yake niione ingawa ukitaka kumuua nyani usimwangalie usoni!” Alisema tajiri Abdulwakil na vijana kama watatu walimshika Victoria shingoni na kuanza kukinyanyua kichwa chake.
“Khaa! Victoria ni wewe?” Tajiri Abdulwakil alisikika akipiga kelele.
Victoria alishangaa kusikia mtu aliyemhofia akimwita kwa jina, hakuwa maarufu kiasi cha kujulikana kwa tajiri Abdulwakil!
“Wewe ni nani unayeniita jina?”
Tajiri Abdulwakil hakujibu kitu kwa mshtuko alioupata alilegea na kuanguka moja kwa moja sakafuni! Ikawa hekaheka ndani ya chumba, watu wote hawakuelewa ni nini kimempata ikabidi kwa haraka haraka abebwe na kutolewa moja kwa moja hadi nje ambako alipakiwa ndani ya gari na kukimbizwa hospitali! Hakuna mtu aliyeelewa kilichotokea, kilibaki ni kitendawili.
“Au yule bibi ni mchawi nini?” Aliuliza Patrick wakiwa ndani ya gari kuelekea hospitali.
“Kwanini unafikiri hivyo Patrick?”
“Maana amening’ang’ania sana nimlete kwa baba sasa baada tu ya baba kumwona ameanguka na kupoteza fahamu. Kama baba akifa kwa hakika nitamuua huyu bibi kizee! Hawezi kuniulia baba yangu hivi hivi nikamwacha hai” Aliendelea kusema Patrick huku machozi yakimtoka.
Walipofika hospitali walipokelewa na tajiri Abdulwakil akiwa hajitambui alikimbizwa moja kwa moja hadi chumba cha wagonjwa mahututi, iligundulika baadaye kuwa mmoja wa mishipa yake katika ubongo ulipasuka sababu ya mshtuko mkubwa alioupata. Jambo hilo lilimfanya Patrick aamini Victoria alikuwa na majini na alimpiga baba yake na moja ya majini yake.
“Nitamuua! Hakyanani nitamuua! Nikirudi nyumbani tu lazima afe na atafukiwa ardhini hakuna mtu atakayejua”
**************
Kwa sababu ya kuchanganyikiwa na tukio lililotokea Patrick alimsahau Victoria ndani ya nyumba yao na kuondoka mbio kwenda hospitali, alibaki sebuleni akiwa katika dimbwi la mawazo na maswali yasiyokuwa na majibu, alishindwa kuelewa ni nani aliyemwita kwa jina, aliamini hapakuwa na mtu yeyote aliyemfahamu katika nchi ya Iran.
Alivuta kumbukumbu zake kwa muda akijaribu angalau kuikumbuka sauti aliyoisikia lakini hakupata jibu na kilichomchanganya zaidi ni kitendo cha kumsikia Patrick akimtupia lawama juu ya matatizo yaliyompata baba yake! Aliogopa na kuamini lazima Patrick angemfanyia kitu.
Ni wasiwasi huo ndio uliomfanya atoke taratibu sebuleni na kutembea hadi nje akishika ukuta, nyumba nzima ilikuwa kimya iliashiria watu wote hawakuwepo, aliamini wote walimkimbiza tajiri Abdulwakil hospitali.
Nyumba ya tajiri Abdulwakil ililindwa kila upande, ilikuwa si rahisi kutoka wala kuingia ndani ya nyumba hiyo bila kuonekana lakini kwa tukio lililotokea siku hiyo, walinzi wote walikusanyika sehemu moja na kuanza kujadili juu ya kilichompata tajiri wao.
“Sijui kapatwa na nini?”
“Hata mimi sifahamu, nimeona tu akitolewa ndani na kupakiwa ndani ya gari na kwa haraka gari likaanza kuondoka!”
“Labda mama yumo ndani tumuulize?”
“Hata yeye hayupo amekwenda hospitali!”
“Atapona kweli mzee?”
“Kwa hali niliyomwona nayo kwa kweli nina wasiwasi!”
Wakati maongezi hayo yakiendelea Victoria alikuwa akiupapasa ukuta kwa kuuzunguka akitafuta mahali pa kutokea, alikuwa ameamua kutoroka kwenda mahali kusikojulikana, mwili wake ulihisi mabaya! Alijua kama Patrick angerudi kutoka hospitali na kumkuta ni lazima angemdhuru na hata kumuua kabisa, Victoria hakuwa tayari kwa hilo.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Alipapasa kwa dakika ishirini nzima ndipo akafanikiwa kulifikia lango, kubwa lilikuwa limefungwa lakini alipopapasa pembeni alifanikiwa kugusa kitu kama komeo, alipokishika na kujaribu kukifungua na kisha kuvuta alishangaa kuona lango dogo likifunguka! Akamshukuru Mungu na kwa taratibu pamoja na uzee wake alinyata na kutoka nje bila kuonekana na mtu yeyote.
Sababu ya upofu alisimama bila kujua aelekee wapi, aliusikiliza moyo wake kwa muda na akakumbuka maneno aliyoambiwa kanisani miaka mingi akiwa mtoto mdogo kuwa Mkono wa kulia ulikuwa mkono wa Kuume ambao uliaminika kuwa na baraka! Bila hata kujadili mara mbili Victoria alikata kulia akachuchuma na kuanza kutambaa akielekea vichakani bila kujua mahali alikokuwa akielekea.
Kwa saa nzima alitambaa ardhini akipita katikati ya nyasi zilizomuwasha mwili mzima, hakujali kwa sababu alishaamua kujiokoa, machozi yaliendelea kumtoka sababu ya Manjit aliyekuwa polisi! Kwa mara nyingine alikuwa ametenganishwa na mtu aliyempenda na aliyekuwa msaada pekee kwake!Kumbukumbu zake zilimrejesha tena kwa kaka yake Nicholaus.
“Yaani kila mtu anayejitolea kunisaidia anaondolewa kwangu! Wa kwanza alikuwa Nicholaus, akaja Leah, baadaye Manjit lakini hata yeye wameninyang’anya! Nitaishije mimi Victoria? Ni heri kufa kuliko mateso haya!” Aliwaza akizidi kutambaa kwenda mbele zaidi katikati ya vichaka.
Mpaka masaa matatu baadaye alikuwa bado akitambaa porini, alikuwa bado hajaonekana wala kukutana na mtu yeyote! Alimshukuru Mungu kwa hilo mbele zaidi alichoka na kuamua kulala chali ardhini na kuamua kuifungua ncha moja ya nguo aliyojifunga na kutoa kipande cha noti walichogawana na kaka yake, alikuwa bado akikitunza! Hakuwa tayari kukipoteza kwake ilikuwa ni bora apotee yeye lakini si kipande hicho cha noti alichokichukulia kama kaka yake.
“Hivi kweli ipo siku nitakutana na Nicholaus na kuiunganisha noti yetu?” Aliwaza Victoria akiwa amelala chali ardhini, alikuwa amechoka hoi bin taaban na njaa ilimsumbua, si njaa tu kulikuwa na mbu wengi waliomuuma kila sehemu ya mwili wake, ingawa alikuwa kipofu hali ilimuonyesha kuwa tayari usiku ulishaingia.
Hakuwa na matumaini ya kumwona Manjit tena!
*************
Taarifa za tajiri Abdulwakil kuanguka ghafla nyumbani kwake baada ya kumwona mwanamke mzee zilitapakaa kila sehemu ya mji wa Baghdad! Watu wengi walifurika hospitali kushuhudia kilichompata mtu waliyeamini alikuwa tajiri kuliko wote nchini humo.
“Ni jini!”
“Kweli eh?”
“Hakuna kitu kingine! Si ajabu maadui zake walimtuma bibi kizee nyumbani kwake wakiwa wamemvalisha jini chinjachinja!”
“Lakini kweli inawezekana!”
Hayo ndiyo yalikuwa maneno ya kila mtu aliyefika hospitali, hawakuruhusiwa kumwona mgonjwa watu wote waliongea na Patrick na kumpa pole na alivyowasimulia yaliyotokea wote waliamini bibi alitumwa.
“Huyo bibi yuko wapi?” Aliuliza mmoja wa wafanyakazi kwenye visima vilivyomilikiwa na tajiri Abdulwakil.
“Tulimwacha nyumbani!”
“Kwa hiyo atakuwa bado yuko nyumbani kwenu?”
“Naamini hivyo!”
“Jamaniee!” Alipiga kelele mfanyakazi huyo na wafanyakazi zaidi ya mia tatu waliokusanyika walikaa kimya kumsikiliza yeye, alikuwa ni kiongozi wao katika visima vya mafuta.
“Ni lazima huyu bibi tukamuue, hawezi kumuumiza tajiri yetu na ushirikina au mnasemaje?”
“Sawaaaaaaaaa!”Wafanyakazi wote waliitikia.
Kama walioamrishwa waliingia ndani ya magari yaliyokuja nayo kutoka kwenye visima vya mafuta na kwenda moja kwa moja hadi nyumbani kwa tajiri Abdulwakil kwa lengo la kwenda kumkamata Victoria na kumuulia mbali. Walipokelewa na walinzi na walipomuulizia bibi walinzi hawakuwa na jibu kwa sababu hawakutaarifiwa kuwa kulikuwa na mtu aliyebaki ndani ya nyumba!
“Ingieni muangalie!”
Kiongozi wa wafanyakazi hao na wenzake wawili waliingia hadi sebuleni na kuanza kumsaka Victoria bila mafanikio, walinyanyua hadi viti na meza na kumwangalia chini yake lakini bado hakupatikana.
Walitoka nje na kuwataarifu wenzao juu ya kutoonekana kwa mtu waliyekuwa wakimtafuta ndani ya nyumba, waliamua kuacha ili wafanye msako asubuhi iliyofuata, baadaye Patrick alirudi kutoka hospitali na kuungana nao! Yeye ndiye aliwajaza jazba zaidi wafanyakazi wake pale alipowaeleza wazi kuwa mwanamke aliyemsababisha baba yake matatizo alistahili kufa.
Wafanyakazi walilala nje ya nyumba ya akina Patrick na asubuhi ilipowadia, nyumba nzima kwa msaada wa Patrick ilianza kupekuliwa lakini mpaka hatua ya mwisho hawakuweza kumwona ndipo ukatolewa uamuzi watafutwe nje ya ngome.
“Hatakuwa mbali na hapa, si ajabu alifanikiwa kutoka na yupo porini!” Patrick aliwaeleza wafanyakazi wake, alikuwa amedhamiria kumuua Victoria kabisa akiamini alimpiga baba yake na jini! Hakuna mtu kati yao aliyeelewa kwanini Abdulwakil alipoteza fahamu mara tu baada ya kumwona mwanamke huyo na kilichowashangaza zaidi ni kitendo cha Abdulwakil kumtaja mwanamke huyo kwa jina kabla ya kupoteza fahamu.
“Jamani hizi ni nyayo za nani? Lazima kuna kitu kimepita hapa kikijivuta!” Alipiga kelele mmoja wa wafanyakazi waliokuwa wakimsaka Victoria.
Mchana kabla Victoria hajapelekwa nyumbani kwa tajiri Abdulwakil mvua kubwa sana ilinyesha ni hiyo ndiyo iliyofanya nyayo na alama za Victoria akitambaa ardhini zionekane.
“Ni yeye ndiye kapita hapa!”Patrick alisema na kuwaongoza wafanyakazi wake kuzifuata nyayo hizo porini,walitembea karibu masaa mawili wakizifuata nyayo hizo porini, ghafla walimsikia mtu aliyekuwa mbele yao akipiga kelele kwa sauti.
“Huyu hapa! Huyu hapa!” Wafanyakazi wote walikimbia kwenda mbele kila mtu na silaha yake, mwenye rungu, mwenye jiwe, mwenye panga, mwenye nondo tayari kwa kumuua Victoria.
Alikuwa usingizini lakini kelele hizo zilimzindua alishindwa kuelewa ni akina nani waliokuwa wamemzunguka.
Ghafla tajiri Abdulwakil alirejea na fahamu zake tofauti na walivyofikiri madaktari, baada ya kufungua macho yake aliangaza huku na huku chumbani, mwanzoni hakuelewa mahali alikokuwa lakini alipoziona chupa za maji zikining’inia juu ya kitanda chake alijua mahali alipokuwa ni hospitali.
Alimwangalia Patrick chumbani hapo lakini hakumwona badala yake alimwona mkewe akiwa amesimama pembeni mwa kitanda chake uso wake ukiwa umejaa mshangao mkubwa!
“Ma...ma!”Abdulwakil alimwita.
“Pole sana mume wangu!”
“Ahsante!”
“Kilitokea nini?”
“Nili...mwo....na da...da ya...ngu!”
“Dada yako?”
“Nd…i….ooo!”
“Nani?”
“Vict....,hicho ndicho kilinishtua!”
“Unamuongelea Victoria yule pacha wako! Ambaye umekuwa ukinieleza habari zake?”
“Ndiyo!”
“Yuko wapi?”
“Alikuja nyumbani!”
“Unamaanisha ndiye alikuja na yule kijana unayemdai?”
“ Haswa! Yuko wapi?” Tajiri Abdulwakil aliuliza.
Kwa bahati nzuri mama yake Manjit aliyasikia maongezi ya wafanyakazi pamoja na Patrick kabla hawajaondoka hospitali kwenda nyumbani, waliondoka eneo hilo na kwenda kumuua Victoria ambaye kila mtu kati yao aliamini alihusika na matatizo yaliyompata tajiri yao!
Wasiwasi mwingi ulimwingia moyoni mwake akijua ni lazima wakati huo Victoria alikuwa marehemu kama wafanyakazi walifanikiwa kumpata, ilikuwa ni lazima afanye kila alichoweza kuzuia tukio hilo kutokea! Alijua wazi mume wake asingefurahi kusikia Victoria kauawa, kwa jinsi Abdulwakil alivyomuongelea dada yake karibu kila siku alielewa ni kiasi gani alimpenda.
Bila hata kupoteza muda alifungua mkoba wake na kutoa simu yake ya mkononi, akatoka nayo hadi nje ambako alibonyeza namba fulani fulani na kumpigia Patrick, lengo lake likiwa ni kumzuia asifanye kitu chochote kibaya kumdhuru Victoria.
**************CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Jiwe la kwanza lililorushwa na mmoja wa wafanyakazi lilitua moja kwa moja kichwani kwa Victoria likampasua na kumtoa damu nyingi! Ni wakati huo huo simu ya Patrick ilianza kuita! Kwanza alitaka kuidharau lakini alipousikiza vizuri mlio wa simu aligundua ulikuwa ni mlio wa mama yake! Kwani aliseti milio tofauti ya simu za wazazi wake na watu mbalimbali maarufu.
“Patrick! Patrick! Patrick!” Alisikia sauti ya mama yake ikimwita.
“Ndio mama!”
“Uko wapi?”
“Tulikuwa tunamtafuta huyu mchawi porini, tumempata na hivi sasa ninavyoongea na wewe vijana wanamshughulikia kisawasawa, muda si mrefu atakuwa amekufa hawezi kumpiga baba yangu na jini halafu yeye akabaki hai!”
“Mama yangu! Usifanye hivyo Patrick!”
“Kwanini mama?”
“Unamuua shangazi yako Victoria!”
“Shangazi yangu Victoria???” Aliuliza Patrick kwa mshangao mkubwa.
“Tafahdali usimuue! Baba yako amerejewa na fahamu zake na kusema kilichomshtua ni furaha aliyoipata baada ya kumwona dada yake waliyepotezana naye miaka mingi!”
Patrick hakusema kitu tena maneno ya mama yake yalimwingia moyoni, palepale alikata simu na kuanza kukimbia haraka kuelekea mahali alipolala Victoria akipigwa na wafanyakazi wake.
“Jamani msiniue!” Alilia Victoria lakini hakuna mtu aliyejali
“STOOOOOP!” Patrick alipiga kelele alipowafikia wafanyakazi wake , Victoria alilala chini akilia machozi na kuomba asiendelee kupigwa, damu nyingi zilikuwa zikitoka.
“Vipi bosi!” Mmoja wa wafanyakazi alimuuliza Patrick.
“Mbebeni! Mbebeni!”
“Tumpeleke wapi?”
“Hospitali haraka”
Wafanyakazi wote walishangazwa na kauli hiyo lakini kwa sababu alisema bosi wao, hakuna mtu aliyepinga maneno yake, Victoria akanyanyuliwa chini na kuanza kukimbizwa hadi nyumbani ambako alipakiwa ndani ya gari na kwa haraka alikimbizwa hadi hospitali! Madaktari walipomuona katika hali hiyo walikataa kumpokea wakihitaji karatasi ya polisi, lakini baada ya Patrick kuongea nao vizuri na kumpa kitu kidogo daktari wa zamu pesa kidogo, Victoria alipokelewa akiwa katika maumivu makali na kupelekwa chumba cha upasuaji na kushonwa sehemu zote zilizochanika, alipotolewa chumba cha upasuaji alipelekwa chumba cha wagonjwa mahututi ambako alilazwa hali yake ilikuwa mbaya mno! Hakuna mtu aliyekuwa na uhakika kuwa Victoria angepona.
******************
“Baba! Nisamehe baba! Sikujua kama ni shangazi!” Patrick aliongea akiwa amepiga magoti pembeni mwa kitanda cha baba yake ilikuwa siku tatu tu tangu Victoria ashambuliwe kwa mawe kufuatia amri aliyoitoa kwa wafanyakazi..
“Kwanini ulichukua uamuzi wa kuua?”
“Baba ni kwa sababu ninakupenda na sikuwa tayari kuona mtu amekufanyia kitu kibaya wakati mimi nipo!”
“Ndio uue? Sasa akifa je?”
“Mungu atamsaidia baba, nisamehe kwa kitendo nilichokifanya!”
“Nimekusamehe Patrick lakini hakikisha shangazi yako anapata matibabu ya uhakika ili apone, sipo tayari kumpoteza Victoria ni pacha wangu na ninampenda sana, siamini hata kidogo kuwa nimekutana naye tena baada ya miaka mingi! Lolote lifanyike na kwa gharama zozote lakini Victoria apone”
“Sawa baba nitafanya kama unavyoagiza!”
“Na si yeye tu pia hakikisha kijana aliyeko mahabusu anatolewa inawezekana ni mtoto wa dada yangu!”
“Nani Manjit?”
“Ndiyo!”
“Leo hii hii atatoka baba!”
Siku hiyo haikuwezekana kumtoa Manjit mahabusu lakini siku iliyofuata alitolewa na kukaribishwa nyumbani kwa tajiri Abdul Wakil, Patrick alionekana kuwa rafiki zaidi kuliko siku nyingine zote, kitu cha kwanza alichofanya baada ya kutoka mahabusu ni kuuliza mahali Victoria alikokuwa!
“Victoria anaumwa sana!” Patrick alimjibu.
“Anaumwa nini?”
Patrick alikaa kimya kwani hakuwa na jibu la kumpa Manjit kuhusiana na swali lake, alionyesha masikitiko makubwa sana usoni, hali hiyo ilimtia wasiwasi Manjit, hisia zake zikamfanya aanze kufikiria labda Victoria hakuwa hai.
“Umesema anaumwa kitu gani?”
“Alipatwa na ajali!”
“Ajali?”
“Ndiyo!”
“Ajali ya nini?”
“Aligongwa na gari!” Patrick alidanganya
“Kwa hiyo yupo wapi?”
“Hospitali!”
“Nipeleke!”
“Pumzika kwanza!”
“Haiwezekani nipeleke hospitali kwanza!”
Patrick alipoiangalia saa yake ya mkononi ilikuwa saa saba na nusu mchana, aligeuza gari na kuondoka kwa haraka kuelekea hospitalini, ambako yeye na Manjit walikwenda moja kwa moja hadi chumba cha wagonjwa mahututi alikolazwa Victoria, waliruhusiwa na muuguzi na kuingia hadi chumbani kwa mgonjwa, Manjit alilia machozi alipomwona Victoria kitandani, uso wake ulikuwa umevimba kupita kiasi na kichwa kizima kilifunikwa na bandeji.
“Anti Vicky! Anti Vicky! Anti Vicky!” Alianza kumwita akimtingisha lakini Victoria hakuzinduka, muuguzi aliyekuwa karibu alikuja na kumshika Manjit mkono akimzuia kumtingisha.
“Jamani mlimfanya nini mama yangu mdogo?” Aliuliza Manjit huku akilia machozi na Patrick alimshika mkono na kuanza kumtembeza hadi nje ambako alikaa kitini na kuendelea kulia, Patrick alimwekea mkono begani na kuanza kumbembeleza.
“Nisamehe sana!” Patrick alisema.
“Kwa kosa gani?”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Siwezi kukueleza hivi sasa, ila wewe ni ndugu yangu!”
“ Ndiyo binadamu wote ni ndugu lakini nahitaji kufahamu nini mlimfanyia mama yangu mdogo sababu ya kunidai ndio mkaamua kumuua? Sawa tu!”
“Hapana siyo hivyo! Hebu kwanza twende huku!” Patrick alisema akimsaidia Manjit kunyanyuka kitini na kumwongoza hadi katika chumba alicholazwa tajiri Abdulwakili, wote wawili waliingia, hali ya Abdulwakili tayari ilikuwa nzuri alikuwa ameketi kitandani akinyweshwa uji na mke wake, walipoingia mama yake Patrick alishtuka hasa alipomwona Manjit akilia.
“Vipi tena?”
“…nimemleta huyu kijana nimtambulishe kwenu!”
Manjit aliwasabahi wote huku machozi yakiendelea kumtoka! Alionyesha wazi kulikuwa na jambo lililomtatiza, hali hiyo ilishtua wazazi wote wa Patrick.
“Vipi mbona mwenzako analia?”
“Huyu ndiye Manjit!”
“Manjiti???? Ndiye huyu????” Abdul Wakili aliuliza kwa mshangao”
“Usilie mwanangu, madeni yako yote nimeyafuta!” Abdul Wakil alisema akiamini kilichomliza Manjit ni wasiwasi wa kulipa! Alinyanyuka kitandani na kwenda moja kwa moja hadi kwenye kiti alichokalia Manjit na kukaa naye.
“Nashukuru sana kwa kunifuatia deni lakini bado nataka kujua ni nini mmemfanyia mama yangu mdogo wakati alikuwa mzima?”
“Hilo nitakueleza baadae lakini napenda kuongea maneno machache na wewe kwanza!”
“Maneno gani?”
“Ulishawahi kumsikia mtu aliyeitwa Nicholaus?”
“Ndiyo mama mdogo alimtaja mara kwa mara!”
“Basi ni mimi!”
“Ni wewe? Wewe si ni Abdulwakil?”
Tajiri Abdulwakil alianza kumsalimia Manjit historia nzima ya maisha yake, kuanzia Arusha mpaka Baghdad! Alipomweleza kuwa yeye na Victoria walikuwa mapacha Manjit alishangaa sana, alimweleza wazi kuwa miaka yote alikuwa akimtafuta dada yake na alimshukuru sana Manjit kwa kumleta hadi kwake!
“Umefanya jambo kubwa mno na sijui jinsi ya kukushukuru!”
“Kwa hiyo wewe ndiyo Nicholaus?”
“Ndiyo, wewe ulizaliwa wapi Tanzania au Canada?”
“Nilizaliwa Tanzania lakini baadaye tukahamia Canada!”
“Baba yako ndiye Shabir siyo?”
“Ndiyo!”
“Na mama yako ni Leah!”
“Ndiyo!”
“Leah alikuwa yaya katika nyumba yetu mimi na Victoria tukiwa watoto wadogo, wazazi wetu walimchukua akiwa yatima na kuishi nae, hivi sasa wako wapi?”
“Wote ni marehemu! Baba alifariki miaka mingi iliyopita na mama amefariki wiki iliyopita!”
“Masikini waliugua nini?”
“Baba alijinyonga na nilipotoka tu huku kukopa mafuta nilikuta mama yangu akiteketea katika moto! Nyumba yetu iliungua”
“Kweli?”
“Ndiyo!”
“Pole sana mwanangu, tangu sasa niite mjomba si Abdulwakil tena!”
“Sawa lakini ilikuwaje ukabadili jina?”
Swali hilo lilimfanya Abdulwakil asimulie kila kitu kilichotokea maishani mwake ikiwa ni pamoja na namna alivyoupata utajiri wote aliokuwa nao katika biashara ya mafuta, muda wote akisimulia Manjit alibaki mdomo wazi, hakuamini binadamu anaweza kuteseka kiasi hicho kabla ya kufikia mafanikio yake. Baadae wote walinyanyuka na kukumbatiana hapakuwa na uadui tena, kulichokuwa mbele yao kilikuwa ni kuhakikisha Victoria anapona na maisha yanaanza upya.
“Nitafanya sherehe kubwa sana dada yangu akipona, nafikiri nchi ya Iraq hawajawahi kuona sherehe kubwa kama hiyo tangu iwepo juu ya nchi!” Alisema tajiri Abdulwakil huku akitabasamu, kila siku alikwenda wodini kwa Victoria kumwangalia, hali ilimsikitisha sana lakini bado alimwombea dada yake kwa Mungu ili apone na wafurahie tena maisha pamoja baada ya mateso ya muda mrefu! Wiki moja baadae Abdulwakil aliruhusiwa kutoka wodini na kurejea nyumbani ambako aliendelea kupona taratibu, lakini hali ya Victoria bado iliendelea kuwa mbaya.
******************
“Patrick!”
“Naam daktari!”
“Kwa kweli tumejitahidi sana kumsaidia shangazi yako bila mafanikio na sasa tunaelekea kukata tamaa ingawa bado tunayo matumaini kuwa akifikishwa nchini Marekani katika hospitali ya Boston Medical Institute anaweza kupona kwa sababu huko kuna mabingwa wa kufanya operesheni za ubongo kuliko sisi hapa Baghdad, mimi nilisoma katika hospitali hiyo nina imani na madaktari wa hospitali hiyo.
“Kwa hiyo unashauri tumpeleke huko?”
“Kuna njia mbili za kufanya, ya kwanza ni kusafiri hadi huko lakini ya pili ni kuwaleta wataalam hapa kwa gharama zako mwenyewe!”
“Ni hayo tu?”
“Ndiyo!”
“Hakuna shida anachotaka baba ni shangazi kupona hata kama ni kwa gharama gani! Nafikiri hakuna haja ya kusafiri waagize hao madaktari waje wafanyie hapa hapa mimi nitaongea na baba!”
“Basi subiri kwanza!” Daktari alisema na kunyanyua simu, alipiga moja kwa moja hadi hospitali ya Boston Insitute na kuongea na Dr. William Knight, mkuu wa kitengo kilichoitwa NeuroSurgery Department kilichojishughulisha na operesheni za ubongo na mishipa ya fahamu! Na madaktari wawili walikubali kuondoka Marekani kwenda Baghdad kumshughulikia Victoria..
Furaha ya tajiri Nicholaus ama Abdulwakil kama alivyojulikana na wengi katika nchi za Kiarabu kukutana na dada yake Victoria waliyepotezana miaka mingi wakiwa watoto wadogo iliingia dosari baada ya hali ya Victoria kuwa mbaya kufuatia kipigo alichopigwa na wafanyakazi wa kwenye visima vyake vya mafuta kwa amri ya mtoto wake Patrick, wakimhusisha Victoria na uchawi, kuwa alihusika na kuugua ghafla kwa Abdulwakil baada ya kukutana naye.
Abdulwakil hakuwa tayari hata kidogo kuona Victoria anakufa mbele ya macho yake kwani kwa siku nyingi mno alikuwa amemtafuta Victoria bila mafanikio, halikuwa jambo rahisi kwake kukubali mara moja dada yake afe bila juhudi zozote kufanyika!Alikuwa tayari kutumia chochote alichokuwa nacho kuokoa maisha ya Victoria!
“Atapona kweli?”
“Atapona tu wale madaktari ni mabingwa!”
“Kwani tatizo lake kwenye ubongo ni nini hasa?”
“Nafikiri alipigwa na kitu kizito kichwani, fuvu likapasuka kwa ndani na damu ikavuja na sasa damu hiyo inaugandamiza ubongo kwa ndani!”
“Kwa hiyo madaktari hao watafanya nini ili kuokoa maisha yake?”
“Watafanya upasuaji wa kichwa kisha watatoa bonge la damu lililoganda ndani, ni operesheni ngumu kidogo kufanyika lakini kwa madaktari wanaokuja nina hakika wataweza!”
Majira ya saa tatu na nusu usiku wa siku hiyo madaktari kutoka marekani waliwasili katika jiji la Baghdad kwa ndege maalum ya kukodi, iliyokodiwa kwa gharama za Abdulwakil na kwenda moja kwa moja hadi hospitali alikolazwa Victoria, walionana na madaktari na kufanya kikao cha karibu dakika arobaini na tano wakielezwa kuhusu hali halisi ya mgonjwa na kilichokuwa kikimsumbua.
“She was involved in a mob justice act, hit hard by angry civillians! They broke her skull and caused internal bleeding which resulted into a contussion!”(Alipigwa na wananchi wenye hasira wakavunja fuvu lake na kusababisha damu ivuje kwa ndani ambayo iliganda na kuanza kuugandamiza ubongo!)
“Oh! My God did you do a CT-Scan?”(Mungu wangu mlimpiga picha ya CT-Scan kichwani?) Dk. Knight aliuliza, mmoja wa madaktari kutoka Marekani.
“Yes!” (Ndiyo!)
“Can I see it?”(Naweza nikaiona picha hiyo?)
“Ndiyo!” Aliitikia Dk. Khalfa, bingwa wa upasuaji katika hospitali hiyo, madaktari wote walikuwa ofisini kwake wakifanya kikao chao, alinyanyuka na kufungua kabati iliyokuwa nyuma yake na kutoa bahasha kubwa, ndani yake akatoa karatasi nyeupe ndogondogo mbili na kumkabidhi Dk. Knight ambaye alizitupia macho na kuanza kuzikagua.
Madaktari wengine wote walikaa kimya wakisubiri majibu ya Dk. Knight baada ya kuzikagua picha hizo.
“Its gonna be a tough task!”(Itakuwa kazi ngumu!)
“Why?”(Kwanini?)
“The clot is so huge and about to compress the carotid artery! We have to do this operation right now if we’re serious about this patient’s life! Are you ready?”(Bonge la damu lililoganda ni kubwa mno na karibu linaungandamiza mshipa wa damu unaopeleka damu kwenye ubongo, hivyo kama tunataka kuokoa maisha ya huyo mgonjwa ni lazima tuifanye hii operesheni sasa hivi! Mpo tayari?)
“Ready we are!”(Tupo tayari!)
Maandalizi yalifanyika haraka iwezekanavyo, Victoria akakimbizwa chumba cha upasuaji ambako madaktari waliotoka Marekani kwa kushirikiana na madaktari wawili wenyeji walimfanyia Victoria operesheni ya kufanikiwa kulitoa bonge la damu lililoganda chini ya fuvu lake na kuiziba mishipa ya damu iliyopasuka ili kuzuia damu kuendelea kuvuja zaidi.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Ilikuwa operesheni ngumu walifanikiwa kuikamilisha baada ya masaa sita! Kila mtu kati yao alikuwa amechoka lakini walifurahi kuona operesheni imefikia mwisho ingawa hakuna mtu kati yao aliyekuwa na uhakika kuwa Victoria angepona.
Manjit, Patrick, tajiri Abdulwakil na mkewe walikuwa nje ya chumba cha upasuaji wakisubiri operesheni ikamilike, muda wote huo wa masaa sita machozi yaliendelea kumtoka Manjit, hakuwa tayari Victoria afe, ni mtu pekee aliyekuwa amebakiza duniani! Hakuwa na baba, mama, bibi wala shangazi!
Kumpoteza Victoria kungemaanisha yeye kubaki peke yake duniani kitu ambacho hakuwa tayari hata kidogo kupambana nacho, pamoja na wema wote aliofanyiwa na familia ya Abdulwakil, pia msamaha alioombwa bado hakuwa tayari kumsamehe Patrick kwa kitendo chake cha kuamrisha watu wampige kwa mawe Victoria, mara nyingi alimwangalia kwa jicho la chuki! Jambo hilo hata Patrick mwenyewe aliligundua.
Wote watatu walimzunguka Manjit wakijaribu kumbembeleza lakini haikutosha, Patrick aliendelea kulia! Lakini maneno ya tajiri Abdulwakil kuwa maumivu aliyokuwa nayo moyoni mwake kwa matatizo yaliyompata dada yake mpendwa yalimtia nguvu kidogo ingawa bado moyoni mwake alikuwa haamini kama kweli Abdulwakil ndiye Nicholaus aliyeongelewa na Victoria kila mara.
“Pole na kazi daktari!” Abdulwakil alimwambia Dk.Knight baada ya operesheni hiyo, aliongea katika lugha ya Kiingereza.
“Ahsante sana!”
“Kuna matumaini kidogo?”
“Mungu atasaidia ingawa operesheni ilikuwa ngumu!”
Maneno hayo ya daktari hayakumpa Abdulwakil uhakika wa Victoria kupona lakini hakutaka kuonyesha wasiwasi zaidi, aliyaacha mambo yote mikononi mwa Mungu! Baadaye waliiona machela ikipitishwa kutoka chumba cha upasuaji na kupelekwa moja kwa moja chumba cha wagonjwa mahututi ambako Victoria alilazwa, hawakuruhusiwa kumwona mpaka siku iliyofuata asubuhi walipoingia wodini na kukuta bado Victoria hajitambui.
Alibaki katika hali hiyo kwa karibu siku saba, kila siku alipewa madawa makali ya usingizi yaliyomfanya alale kwa masaa yote ishirini na nne, alikula chakula kwa kutumia mrija uliopitishwa puani na pia aliwekewa dripu la maji zilizokimbizana kuingia kwenye mishipa yake! Hali yake haikuwa ya kuleta matumaini kila mtu alikuwa amekata tamaa! Kwa tajiri Abdulwakil ilikuwa huzuni kubwa zaidi pengine kuzidi hata aliyokuwa nayo Manjit.
Abdulwakil alitaka Victoria apone ili wawe pamoja tena naye afaidi maisha kama alivyokuwa akifaidi yeye, mara nyingi alimuuliza Mungu ni kwanini kama aliamua kumkutanisha na dada yake iwe hivyo akiwa katika hali mbaya? Kuna wakati alishindwa kuvumilia machozi yakamtoka.
************
Kwa siku ishirini na saba Victoria aliendelea kulala kitandani bila kujitambua, vipimo vyake vyote vilionyesha hali yake iliendelea vizuri, mapigo yake yalikuwa sawasawa! Hiyo ilimaanisha kilichokuwa kikiendelea ni kupona kwa ubongo wake kazi ambayo hufanyika taratibu sana, sehemu mbalimbali za mwisho wake zilianza kurejewa na fahamu zilizokuwa zimepotea.
Siku ya ishirini na nane alifumbua macho lakini hakuweza kuongea chochote na kwa sababu alikuwa kipofu hakuweza kumwona mtu yeyote chumbani.
Manjit, Abdulwakil na ndugu wote waliokuwepo wodini hawakuruhusiwa kumsemesha kitu chochote kwani kufanya hivyo kungeuingiza ubongo wake katika shughuli na kuufanya uchelewe kupona zaidi, walizuiliwa kumwona kila siku wakawa wanamwona siku mbili tu kwa wiki! Mwezi mmoja baadaye hali yake ilikuwa nzuri aliweza hata kuongea.
“Anti!” Manjit alimwita.
“Wewe nani?”
“Mimi Manjit!”
“Manjit mwanangu au?”
“Ndiyo Anti! Pole sana!”
“Ahsante mwanangu! Walinipiga mno tena bila kosa lolote, lakini hapa tuko wapi?”
“Baghdad!”
“Ahaa! Nimekumbuka tulikuja kwenye matatizo yako ya mafuta?”
“Ndiyo!”
“Si walikukamata? Sasa walikuachia lini na matatizo yamekwisha au la?”
“Yamekwisha!”
“Kwa hiyo tunarudi Canada?”
“Hatutarudi Canada tena!”
“Kwanini?” Aliuliza Victoria lakini badala ya Manjit kujibu swali hilo alikaa kimya na minong’ono ilisikika pembeni, alikuwa akiongea na Abdulwakil aliyekuwemo chumbani akisikiliza maongezi yao.
“Anti!”
“Naam!”
“Hebu ongea kwanza na Abdulwakil!”
“Abdulwakil? Ambaye watu wake walinipiga?”
“Ndiyo lakini msikilize kwanza!”
Victoria alitii sauti ya Manjit na kukaa kimya.
“Kwini!” Victotia alisikia sauti ya mtu akimwita kwa jina ambalo hakuna mtu mwingine yeyote angemwita! Lilikuwa jina ambalo mama yake alimwita alipokuwa mtoto sababu ya muonekano wa sura yake, alishangaa kupita kiasi.
“Wewe ni nani unayeniita jina hilo?”
“Mimi?”
“Ndiyo!”
“Naitwa Nicholaus!”
“Nicholaus? Mbona nimeambiwa unaitwa Abdulwakil”
“Amini maneno yangu mimi ni pacha wako Nicholaus niliyekuacha miaka mingi nyumbani Tanzania!”
“Haiwezekani! Sogea nikupapase usoni, ingawa mimi ni kipofu lakini sura ya Nicholaus bado naikumbuka!”
Abdulwakil hakubisha kitu, alichofanya ni kusogeza uso wake karibu na mahali alipolala Victoria, mkono wa Victoria ukaanza kupita usoni mwake taratibu ukimgusa kwa ulaini.
“Mh! Mbona sio wewe?”
“Ni mimi Nicholaus!”
“Mbona uso wako umejaa makovu kiasi hicho? Nicholaus hakuwa na sura ya aina hiyo”
“Nilipatwa na ajali mbaya sana wakati nakuja hapa kutoka Iran, nimekuwa na shida nyingi katika maisha yangu mpaka kufikia hapa nilipo nitakueleza tukipata nafasi ila maisha yangu yalijaa mateso mengi, kila mara nilikulilia nilitaka sana kukutana na wewe lakini sikujua mahali ulikokuwa! Namshukuru Mungu hatimaye amekuleta, nakupenda sana Victoria miaka yote nimekuwa nikitamani kukuona hatimaye Mungu ametukutanisha! Hakuna deni atakalodaiwa Manjit ila tangu sasa wewe utaishi na mimi hapa Baghdad mpaka mwisho wa maisha yetu na Patrick na Manjit watafanya biashara pamoja sisi sote ni ndugu!” Alisema Abdulwakil na kumbusu Victoria usoni.
“Ilikuwaje ukaitwa Abdulwakil?”
“Maisha!”
“Maisha? Kivipi?”
Nicholaus alilazimika kuanza kueleza yote yaliyompata maishani tangu waachane na dada yake nchini Tanzania, kilichotokea mpaka akabadili dini na kilichotokea mpaka akatajirika kiasi hicho! Muda wote Victoria aliendelea kumsikiliza na Manjit pamoja na Patrick walikuwa kimya maneno yote yakiwaingia vizuri mioyoni mwao. Nicholaus aliongea maneno ambayo hata mke wake hakuwahi kuyafahamu, alilazimika kufanya hivyo kumshawishi Victoria kuamini kuwa yeye ndiye alikuwa Nicholaus.
“Pamoja na maelezo yako yote bado siamini!”
“Kwanini?”
“Mtu yeyote anaweza kusema kama ulivyosema wewe!”
“Nifanye nini ili Victoria uamini!”
“Kuna kitu kimoja tu ambacho ukikifanya nitaamini!”
“Kitu gani?”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Subiri!” Alisema Victoria kisha akaita kwa sauti ya juu ili muuguzi aliyekuwa ofisini aje, sauti yake ilifika hadi katika ofisi ya wauguzi na mara moja muuguzi mmoja alikwenda mbio hadi kitandani.
“Vipi Victoria?”
“Hakuna tatizo!”
“Nikusaidie nini?”
“Nafikiri nilipoletwa hapa nililetwa na nguo zangu!”
“Ndiyo!”
“Ziko wapi?”
“Ziko stoo!”
“Naomba basi uniletee gauni langu!”
“Sawa nakuja sasa hivi!”
Abdulwakil alishindwa kuelewa ni kitu gani alichotaka kufanya Victoria, ilibidi abaki kimya kusubiri! Hakumlaumu Victoria kwa jambo lolote kwani ilikuwa imepita miaka mingi sana bila kuonana na kwa sababu alikuwa kipofu hakuiona sura yake ili kukubali kuwa kweli yeye ndiye alikuwa Nicholaus ukizingatia alishabadilisha jina na alikuwa tajiri kupita kiasi kwa wakati huo. Dakika chache baadaye muuguzi alirejea akiwa na gauni lililojaa damu na kumkabidhi Victoria mkononi.
Victoria alianza kulipapasa gauni lake katika mapindo kama mtu aliyekuwa akisaka chawa! Ghafla alishtuka na kuacha zoezi hilo, akageuza kichwa chake kuelekea mahali sauti ya muuguzi ilikotokea.
“Sista naomba mkasi au wembe!”
“Wa nini?”
“Nataka unichanie hapa!”
“Unataka kuchana nguo?”
“Hapana kuna kitu nataka kukitoa!”
“Subiri nije basi!”
Muuguzi aliondoka aliporejea badala ya kuwa na mkasi alikuwa na wembe wa hospitali na kuanza kufumua sehemu aliyoelekezwa na Victoria, tajiri Abdulwakil bado alikuwa amesimama eneo hilo akishangaa kitu ambacho Victoria alikuwa akifanya! Muuguzi naye alishangaa kukuta sehemu aliyokuwa akifumua kuna kipande cha noti.
“Mbona noti yenyewe kipande?”
“Acha tu mwanangu kazi yake mimi naifahamu!” Alisema Victoria kisha kugeuza kichwa chake kuelekeza mahali ilikotokea sauti ya Abdulwakil.
“Mimi na kaka yangu tuligawana kipande cha noti kama kumbukumbu wakati anaondoka tukiwa tumeahidiana kuviunganisha vipande vya noti tutakapokutana! Nimekitunza kipande hiki miaka mingi ili siku nikikutana na Nicholaus tuviunganishe! KAMA WEWE NI NICHOLAUS TOA KIPANDE CHAKO HUU NDIO UTAKUWA MWISHO WA UBISHI”
“Mh! Ninacho kweli?” Aliwaza Abdulwakil, mara ya mwisho kukiona kipande hicho ilikuwa ni miaka mitano kabla wakati akisoma kitabu cha historia ya Iraq nyumbani kwake, hakuwa na uhakika kama kitabu hicho bado kilikuwepo.
“Bila kipande hicho?”
“Haiwezekani!”
“Basi acha nikajaribu kukitafuta!” Akiwa amekata tamaa kabisa Abdulwakil aliendesha gari hadi nyumbani kwake, alifuatana na mkewe pamoja na Patrick wakimwacha Manjit na Victoria wodini, masaa mawili walipekuwa vitabu vyote vilivyokuwa ndani ya nyumba yao wakikitafuta kipande hicho bila mafanikio lakini dakika za mwisho kabisa Patrick alisikika akipiga kelele kutokea stoo, alikuwa amekiona kipande hicho cha noti na kutoka nacho mbio hadi sebuleni!
Abdulwakil aliruka juu na kushangilia na bila kuchelewa waliondoka hadi hospitali ambako waliwakuta Victoria na Manjit wakiwasubiri, Manjit hakuamini alipoona kipande cha noti nyekundu ya Tanzania kikitolewa na kukabidhiwa kwa Victoria, alikipapasa kipande cha Nicholaus na kupapasa kipande chake kwa taratibu akavinyoosha na kujaribu kuvikutanisha ncha zake, kweli vikashabihiana!
“Manjit hebu weka gundi hapa!”
“Sina gundi hapa anti!”
“Nesi tusaidie gundi!Au plasta kama unayo”
uuguzi bila kuchelewa alikimbia hadi ofisini na kuchukua plasta akaja nayo na kuvigundisha vipande viwili vya noti, vilikuwa vipande vichafu lakini vilipounganishwa vilifanana! Ilikuwa si rahisi kuamini vilikuwa vimeunganisha baada ya kutenganisha kwa miaka zaidi ya ishirini. Victoria alilia kwa furaha baada ya kukutana na kaka yake.
“Nicholaus!”
“Naam!”
“Nibusu usoni tafadhali siamini kama nimekutana na wewe!” Alisema Victoria huku akilia na Nicholaus alifanya hivyo bila kuchelewa.
Ilikuwa ni kama ndoto lakini huo ndio ulikuwa ukweli, Victoria na Nicholaus mapacha waliotengana miaka mingi walikuwa wamekutana na kuunganisha vipande vyao vya noti walivyogawana miaka mingi wakati wa kutengana.
“Victoria!”
“Naam!”
“Mtu akiwa na kipande cha noti anaweza kununua kitu?”
“Hapana!”
“Basi nakupa kipande hiki cha noti kitunze ili siku tukikutana tuunganishe vipande vyetu na kununua kitu chochote!” Victoria aliyakumbuka maneno ya mwisho ya Nicholaus wakati wakiagana miaka mingi mjini Arusha.
“Siamini!” Victoria alisema
“Hata mimi pia!”
Ilikuwa furaha kubwa isiyo na kifani mioyoni mwao hatimaye watu hao wawili kukutana, ulikuwa ni kama muujiza na ilikuwa si rahisi kuamini.
Wiki moja baadaye Victoria alitoka hospitali, sherehe kubwa kuliko zote zilizowahi kufanyika katika nchi ya Iraq ilifanywa watu wote mashuhuri nchini humo walialikwa, Nicholaus alitembea akiwa amemshika mkono dada yake Victoria na kumtambulisha kwa karibu kila mtu aliyekuwepo ukumbini humo! Ilikuwa siku ya furaha kuliko zote zilizowahi kutokea katika maisha ya Nicholaus.
“Inaonekana huu ndiyo mwisho wa machozi yangu!” Victoria alisema akiwa amemkumbatia kaka yake.
“Lakini tumepita katika dimbwi la damu acha tupumzike!” Alimaliza Nicholaus na maisha tangu siku hiyo yalikuwa raha mstarehe!
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
MWISHO
Nashukuru sana kwa kunifuatilia tangu mwanzo wa simulizi hii mpaka mwisho. NAtumaini kuna mengi mmejifunza, kwa yale mazuri, yachukueni ila kwa yale mabaya naomba muyaache.
0 comments:
Post a Comment