Search This Blog

Sunday, July 10, 2022

SAFARI NDEFU KUELEKEA KABURINI - 1

 





    IMEANDIKWA NA : NYEMO CHILONGANI



    *********************************************************************************



    Simulizi : Safari Ndefu Kuelekea Kaburini

    Sehemu Ya Kwanza (1)





    Muda ulikuwa ukizidi kwenda mbele huku dereva wa gari ndogo aina ya Prado akiwa amesimama nje ya gari hilo huku akimsubiri msichana mrembo, Patricia Thomson aweze kutoka ndani ya nyumba yao na hivyo kuanza safari ya kuelekea shuleni alipokuwa akisoma kidato tatu, Salma Kikwete Secondary School iliyokuwa Kijitonyama. Muda ulikuwa ukizidi kwenda lakini bado Patricia alikuwa ndani akiendelea kujiremba, bado alikuwa akiendelea kujipaka mafuta ya gharama pamoja na kujipulizia manukato ya bei kubwa.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Muda mwingi dereva wa gari lile, Sam alikuwa akipiga honi kama hatua moja ya kumfanya Patricia ndani alipokuwa afanye haraka lakini hiyo wala haikuweza kusaidia. Bado Patricia alikuwa akiendelea kujiremba kana kwamba honi zile ambazo zilikuwa zikiendelea kupigwa hakuwa akizisikia masikioni mwake.

    “Mbona unamchelewesha mwenzio?” Bi Beatrice alimuuliza Patricia mara alipoufungua mlango wa chumba cha binti yake.

    “Nakuja mama. Kuna kitu namalizia” Patricia alimwambia mama yake huku akiendelea kujiremba.

    Zilipita dakika thelathini na ndipo Patricia alipomaliza kujiremba na hivyo kutoka ndani ya chumba kile. Kitu cha kwanza alichokifanya ni kumfuata mama yake sebuleni alipokuwa na kisha kumbusu na kumuaga. Bi Beatrice alibaki akimwangalia Patricia huku uso wake ukiwa na tabasamu pana, uzuri wa binti yake ulionekana kumvutia hata yeye mwenyewe.

    Patricia akaingia garini bila ya kumsalimia Sam ambaye alionekana kukasirika. Akajifunga mkanda na kutulia kimya mpaka pale Sam alipoingia garini na kasha kuwasha gari na kuliondoa mahali hapo. Ukimya mkubwa ulikuwa umetawala garini, Patricia hakutaka kuongea kitu chochote kile kwani aliamini kwa kile alichokuwa amekifanya cha kuchelewa kutoka ndani ya chumba chake kilikuwa kimemkasirisha Sam.

    “Naomba unisamehe kaka Sam” Patricia alimwambia Sam ambaye alionekana kuwa bize na usukani.

    Patricia akaonekana kuumia, ni kweli alijua kwamba alikuwa amefanya kosa na ndio maana kwa wakati huo alikuwa radhi kuomba msamaha lakini ukimya wa Sam ukaonekana kumuumiza, hakupenda kumuomba msamaha mtu halafu asijibu kitu chochote kile, alipenda kusikia Sam akiongea neno lolote lililomaanisha kumsamehe kwa kile alichokifanya cha kumchelewesha.

    “Naomba unisamehe kaka Sam” Patricia alimwambia kwa mara nyingine tena.

    “Nimekwishakuzoea Pat” Sam alimwambia Patricia.

    “Hapana. Usiseme hivyo kaka. Nakuahidi sitokuchelewesha tena” Patricia alimwambia Sam.

    “Sawa. Hakuna tatizo. Nimekusamehe” Sam alimwambia Patricia huku tayari wakiwa wamekwishafika Magomeni Morocco. Kidogo Patricia akaonekana kuwa na furaha moyoni mwake, kitendo cha Sam kumsamehe kilionekana kumfariji, amani ikaanza kumjaa moyoni mwake.

    Patricia Thomson alikuwa msichana mrembo ambaye alikuwa na mchanganyiko wa rangi huku baba yake akiwa mzungu kutoka nchini Marekani na mama yake akiwa Mtanzania mweusi kutoka mkoani Kilimanjaro. Wazazi wake walikutana miaka kadhaa iliyopita mkoani Arusha na hivyo kukutana kimwili nay eye kuzaliwa miaka kumi na saba iliyopita.

    Baada ya Patricia kuzaliwa, Bwana Thomson hakuendelea kukaa nchini Tanzania, akaamua kurudi nchini Marekani kuendelea na kazi zake katika jiji la Washington. Kutokana na ubize mwingi ambao alikuwa nao katika kazi zake wala hakupata nafasi ya kurudi nchini Tanzania, aliendelea kuishi kwa miaka mingi zaidi huku ni mara chache sana akiwasiliana na mzazi mwenzake, Bi Beatrice kwa ajili ya kujua hali ya binti yake.

    Katika kipindi kirefu cha maisha yake, Patricia alikuwa amelelewa na mama yake, Bi Beatrice. Alimfahamu vilivyo baba yake kutokana na picha kadhaa ambazo alikuwa nazo na hata mzee huyu wakati mwingine kuja nchini Tanzania katika kipindi ambacho alikuwa na miaka kumi na nne.

    Mara kwa mara alikuwa akiwasiliana na baba yake ambaye alikuwa akimtaka sana kuelekea nchini Marekani kuishi nae lakini Beatrice alikuwa akikataa katakata. Kamwe hakutaka kuelekea nchini Marekani, alitamani kuendelea kubaki nchini Tanzania pamoja na mama yake ambaye alikuwa amemzoea kuliko mtu yeyote yule.

    Ni kweli kuna wakati alikuwa akitamani sana kukaa pamoja na baba yake lakini kila alipokuwa akimfikiria sana mama yake, wala hakutaka kuishi mbali nae, bado alijiona kuwa na uhitaji mwingi wa kuendelea kukaa pamoja na mama yake. Mzee Thomson hakuishia hapo, bado alikuwa akimhitaji binti yake aende akaishi nae nchini Marekani pamoja na kuwaonyeshea wazazi wake msichana ambaye alizaa pamoja na mwanamke wa Kiafrika. Beatrice haku wa na jinsi, kitu alichokifanya ni kumuahidi baba yake kwamba ni lazima angekwenda kuishi nchini Marekani mara tu atakapomaliza kidato cha nne.

    Ahadi hiyo alikuwa amempa baba yake mwaka jana katika kipindi ambacho alikuwa kidato cha pili na hiyo ilimaanisha kwamba ulikuwa umebakia mwaka mmoja tu hata kabla hajaenda nchini Marekani kuanza maisha mapya pamoja na baba yake, Bwana Thomson.

    Bwana Thomson hakutaka binti yake, Patricia aishi maisha ya tabu jambo ambalo lilimfanya kila mwezi kutuma zaidi ya dola elfu tatu, zaidi ya milioni nne na nusu kwa ajili ya matumizi ya binti yake pamoja na Bi Beatrice. Patricia alikuwa na uhuru wa kuishi maisha ya kifahari ambayo alikuwa akijisikia kuishi lakini wala hakupenda kuishi maisha hayo hata kidogo.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kutokana na kusoma shule za gharama ya juu kuanzia darasa la kwanza mpaka darasa la saba, Patricia hakutaka tena kusoma katika shule za aina hiyo jambo lililomfanya kidato cha kwanza kuanza katika shule ya Sekondari ya Salma Kikwete iliyokuwa Kijitonyama

    Aliishi maisha ya kifahari, na sasa alijiona kuwa na nafasi ya kutamani kuishi pamoja na watu ambao walikuwa wametoka katika familia za chini. Hiyo ndio ilikuwa sababu kubwa iliyomfanya kuanza kusoma katika shule hiyo ya mchanganyiko na kukutana na wanafunzi ambao walikuwa wakiishi maisha ya chini kabisa.

    Patricia hakupenda kabisa kupelekwa na gari shuleni lakini mama yake hakutaka kukubaliana na suala hilo, kwake, Patricia alikuwa kila kitu, hakutaka apate shida ya aina yoyote ile na wala hakupenda binti yake atumie mwendo mkubwa ardhini na wakati alikuwa na uwezo wa kuzuia jambo hilo.

    Msichana huyu, Patricia ndiye ambaye alikuwa akiongoza kwa uzuri shuleni hapo. Alikuwa akionekana msichana wa tofauti, mchanganyiko wa rangi ambao alikuwa nao ulimfanya kuvutia zaidi. Kila mwanafunzi alitamani kuwa pamoja na Patricia ambaye alikuwa amefanana sana na mwanamuziki wa kike, Alicia Keys kwa kila kitu kana kwamba walikuwa mapacha.

    Patricia hakuwa msichana wa majivuno, alikuwa akiishi maisha ya kawaida shuleni, alichangamana na kila mwanafunzi ambaye alikuwa akihitaji urafiki pamoja nae. Japokuwa wavulana wengi walikuwa wakitamani kumtongoza Patricia lakini walionekana kutokuwa na nguvu za kufanya jambo kama hilo kutokana na ukaribu mkubwa ambao alikuwa nao Patricia kwao.

    Patricia akawa akipendwa sana na kila mwanafunzi shuleni hapo isipokuwa baadhi ya wasichana ambao walikuwa wakijiona kuwa bora zaidi yake. Patricia hakutaka kujali kitu chochote kile, kwake, heshima na kuwathamini watu wengine ndio aliliona jukumu lake alilokuwa nalo.

    Uwezo wake darasani wala haukuwa mkubwa sana japokuwa alikuwa akifahamu mambo mengi kutokana na kununuliwa vitabu vingi vya kujisomea. Kile ambacho hakuwa akikifahamu, alikuwa akifundishwa na wanafunzi wengine na hata vile ambavyo alikuwa akivifahamu basi alikuwa akiwafundisha wanafunzi wengine.

    “Ni msichana mzuri sana. Hapana, acha mimi nijaribu kuwa nae” Martin aliwaambia wanafunzi wenzake.

    “Acha utani bwana. Hebu muangalie Patricia halafu jiangalie wewe. Mnaendana?” Juma alimuuliza Martini.

    Martin akayapeleka macho yake mwilini mwake, miguuni alikuwa na kandambili huku miguu yake ikiwa michafu kutokana na kucheza mpira pekupeku katika kipindi cha mapumziko. Akayaamisha macho yake na kuyapeleka katika shati lake, shati lilikuwa limechakaa, chafu huku likiwa limechanika makwapani. Kila alipokuwa akijiangalia, kulikuwa na utofauti mkubwa sana na Patricia.

    “Mmhh!” Aliguna.

    “Vipi tena?” Ashrafu aliuliza.

    “Mmesema kweli. Manake kila nikijiangalia sipati jibu kama mimi ni mwanadamu au mnyama aliyeachwa porini” Martin aliwaambia na wote kuanza kucheka.

    Martin ndiye alikuwa kijana ambaye alikuwa akivutiwa sana na Patricia kuliko mvulana yeyote shuleni hapo. Kila siku alikuwa akipenda kumwangalia Patricia, moyo wake ukatokea kumpenda sana msichana huyo kiasi ambacho kama ilipita siku pasipo kumuona basi alikuwa akipata shida sana usiku.

    Alitamani kumfuata Patricia na kumwambia ukweli kwamba alikuwa akimpenda sana lakini hakujua ni wapi alitakiwa kuanzia. Maisha yake yalikuwa ya kimasikini sana, ingawa alikuwa akikaa mbali na shuleni hapo lakini kila siku alikuwa akienda shuleni hapo kwa miguu. Si kwamba hakuwa akipenda kupanda daladala, alikuwa akitamani lakini umasiki ulikuwa umeitawala familia yao.

    Hakujua mwendelezo wa maisha yake ya mbele ungekuwaje hapo baadae. Njia za kutoka kimaisha zikawa zimekwisha akilini mwake jambo lililomfanya kuanza kufikiria kufanya muziki. Kila siku shuleni alikuwa akiandika mistari ya muziki aina ya RnB huku akiwaimbia wanafunzi wenzake.

    Baada ya miezi miwili kupita, shule nzima ikajua kwamba mwanafunzi masikini asiyekuwa na mvuto wowote ule, Martin alikuwa mwanamuziki chipukizi ambaye hakuwa na mbele wala nyuma. Walimu walijaribu kumuita ofisini na kumshauri kwamba ingekuwa vizuri kama angetilia maanani masomo lakini Martin hakuonekana kujali, kitu alichokuwa akikitaka ni kuwa mwanamuziki mkubwa wa muziki tu.

    “Kila ninapomsikiliza R Kelly, ananitia mzuka sana” Martin aliwaambia wanafunzi wenzake.

    “Unataka kuwa kama yeye?”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Unaulizia chumvi baharini. Ndio, ninataka kuwa kama yeye” Martin alijibu.

    Hizo ndizo zilikuwa ndoto zake za kila siku, aliupenda sana muziki kwani aliamini kwamba huo ndio ungekuwa njia ambayo ingemfanya kutoka kimaisha na kuwa mwanamuziki mkubwa ambaye angekuja kuwa na fedha nyingi hapo baadae.

    Ingawa alikuwa akiendelea na juhudi zake za kutunga nyimbo mbalimbali lakini bado ndoto yake ya kuwa na msichana Patricia ilikuwa kichwani mwake, alikuwa akimhitaji sana msichana huyo kiasi ambacho usiku kwake ulikuwa ukionekana kuwa wa shida sana. Alitamani kumfuata na kumwambia kile ambacho alikuwa akijisikia moyoni mwake juu yake lakini alionekana kuogopa.

    Kwanza kila alipokuwa akiiangalia hali yake, hakuamini kama msichana Patricia angekubali na kuwa nae. Alijidharau sana na kutokuamini kama alistahili kuwa na msichana huyo. Kwake, kuwa na msichana Patricia ilionekana kuwa kama ndoto ya mchana wa saa saba.

    Kila alipokuwa akifikiria utofauti mkubwa ambao ulikuwepo kati yake na Patricia, wala hakutamani kuwa pamoja nae, aliona ni bora kuendelea kutunga muziki ili kama kungekuwa na siku angekuja kupata fedha, kurekodi na kuwa maarufu basi isingekuwa jambo gumu kumpata Patricia. Kwake aliona fedha kuwa kila kitu katika maisha yake, kutokuwa na fedha kulionekana kuwa tatizo kubwa ambalo lilikuwa likimkosesha kufanya jambo lolote la maana.

    “Ngoja niachane nae na nijiingize moja kwa moja kwenye muziki. Naamini kuna siku utanitoa tu, na hapo ndipo nitakapokuja kumwambia Patricia ukweli kwamba sinywi, sili wala silali kwa ajili yake. ....mwisho wa siku nakuja kumuoa. Hahahahaha...Sijui itatokea au ndio ndoto za mchana. Ila poa. Mziki kwanza halafu mapenzi baadae” Martin alijisemea katika kipindi ambacho Patricia alikuwa akipita mbele yake pamoja na wanafunzi wengine wa kike.



    Bado kichwa cha Martin kilikuwa kikimfikiria sana Patricia japokuwa alijiahidi kumsahau msichana huyo huku akiendelea na shughuli zake za kuandika nyimbo mbalimbali. Bado Patricia hakutaka kutoka kichwani mwake, kadri siku zilivyokuwa zikizidi kwenda mbele na ndivyo ambavyo alikuwa akizidi kumfikiria zaidi na zaidi.

    Kila siku Patricia alionekana kuwa mrembo machoni mwake, alipendeza na kumvutia kuliko msichana yeyote yule. Jina lake likawa kubwa shuleni kutokana na nyimbo mbalimbali ambazo alikuwa akiziimba. Wasichana wakaonekana kuzipenda nyimbo zake ambazo zote zilikuwa zikizungumzia mapenzi.

    Martin hakukata tamaa, marafiki zake ambao walikuwa wakizisikiliza nyimbo zile walikuwa wakimpa moyo kwamba kuna siku ambayo angekuja kuwa maarufu na hivyo kupata fedha nyingi, hakutakiwa kuacha kutunga nyimbo.

    Japokuwa wasichana wengi shuleni walikuwa wakizifurahia nyimbo zake lakini kwake yeye bila Patricia kuzisikia nyimbo hizo hakujisikia raha. Alijiona kwamba angefurahi zaidi kama tu nae Patricia angekuja na kumsifia kama wasichana wengine walivyofanya.

    Kitu alichokifanya ni kuanza kuutafuta ukaribu wake na Patricia. Alijijua fika kwamba alikuwa kijana masikini ambaye wala hakustahili hata kupiga stori na Patricia lakini akaamua kujipa moyo kwamba Patricia asingeweza kumdharau au kumdhihaki.

    Martin akapanga siku maalumu ambayo angeweza kumfuata Patricia na kumtongoza na kisha kuwa wapenzi. Ingawa ulionekana kuwa uamuzi wa haraka lakini kwake ndio aliuona kumfaa zaidi. Hakutakiwa kuanza urafiki na kisha baadae ndio amtongoze, kwake alihofia mazoea.

    Aliona endapo angeanza mazoea na Patricia na kisha baadae kuja kumtongoza basi ingekuwa ni vigumu sana kwa msichana huyo kumkubalia. Uamuzi ambao alikuwa ameupanga ndio ambao aliuona kuwa sahihi na wala haukuhitaji hata ushauri kutoka kwa mtu yeyote.

    Kila kitu alikuwa amekipanga lakini tatizo likatokea. Angeanza vipi kuongea na Patricia na wakati hakuwahi kuongea nae hata siku moja? Angeeleweka vipi na msichana huyo ambaye alikuwa akionekana kuwa mtu wa watu asiyekuwa na ubaguzi wowote ule.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kila kitu ambacho alikuwa akijifikiria mahali hapo au kujiuliza alikosa jibu kabisa. Alichoamua ni kuanza kumtafuta Patricia na kisha mambo mengine kufuata baadae kabisa. Hakujua ni kwa jinsi gani angempata Patricia na kisha kuanza kumwambia kile ambacho alikuwa amekikusudia.

    Alipoona anakisumbua sana kichwa chake, jibu la haraka haraka likaja kichwani mwake kwamba basi angemfuata huko huko darasani alipokuwa. Wala hakutaka kuchelewa, alichokifanya ni kuinuka na kuanza kuelekea katika darasa ambalo alikuwa akisoma Patricia. Alipofika umbali wa hatua kumi kabla ya kuufikia mlango wa kuingilia katika darasa lile, akayapeleka macho yake katika mwili wake.

    Miguuni bado alikuwa na kandambili huku suruali yake ikiwa imepauka sana, shati halikuwa na mvuto wowote ule, lilikuwa limechakaa sana. Ghafla, akasita, hakutaka kwenda akiwa namna hiyo. Alichokifanya ni kukimbia kuelekea bombani ambako akanawa miguu, kichwa na kisha kuanza kuelekea kule ulipokuwa mlango wa kuingilia darasa alilokuwa akisoma Patricia.

    “Martin....” Alisikia akiitwa. Alipogeuza macho yake, alikuwa rafiki yake, Onesmo.

    “Vipi?” Aliuliza.

    “Mbona unaonekana una haraka hivyo?” Onesmo aliuliza.

    “Kuna sehemu nakwenda”

    “Wapi tena?”

    “Darasa lile”

    “Kufanya nini?”

    “Nakwenda kuchukua kitabu cha Biologia”

    “Du! Kwa mara ya kwanza nasikia ukisema hivyo. Poa. Lakini mbona nywele ziko timtim hivyo?” Onesmo alimuuliza huku akionekana kumshangaa.

    Martin akaonekana kushtuka, akakumbuka kwamba alikuwa ametoka kunawa na hivyo hata kichwa alikuwa amekiloanisha na maji. Akazishika nywele zake, ni kweli akahisi kwamba zlikuwa timtim. Safari ya kuelekea katika lile darasa ikaishia hapo. Moja kwa moja akaelekea darasani kwao ambako akatangaza kwamba alikuwa akihitaji kitana na kupewa, akaanza kuzichana nywele zake kwa haraka haraka na kisha kuendelea na safari yake.

    Alipofika nje ya mlango ule, akaanza kujiangalia tena. Moyo wake ukatokea kuuchukia sana umasikini ambao alikuwa nao. Alichokifanya, akapiga konde moyo wake na kuingia ndani. Darasa zima likanyamaza hasa mara baada ya macho yao kutua usoni mwa Martin. Sauti za shangwe zikaanza kusikika darasani hapo.

    “Tupe wimbo mmoja” Mvulana mmoja alimwambia.

    Martin hakusema kitu chochote kile, akabaki akiwaangalia wanafunzi huku akionekana kuwapuuza. Akaanza kuyapeleka macho yake huku na kule, yakamuona Patricia akiwa kimya akisoma kitabu. Martin akaonekana kushtuka, hakujua kama Patricia hakuwa amemuona katika kipindi kile alichoingia au la. Iweje darasa zima limuangalie na huku yeye akiwa amuangalii huku akionekana kutokuwa na hisia zozote kama kuna mtu ameingia darasani mwao? Kwa mbali akaanza kunywea.

    “Nakupendaaaaaa wewe ndiye malaika wa moyo wangu. Nakupenda kila siku mpenzi nitakuwa nawe katika maisha yangu yote. Wewe ndiye faraja langu, wewe ndiye furaha yangu mpenzi” Martin alianza kuimba na kunyamaza.

    Patricia bado alikuwa amenyamaza huku akiwa amekiinamia kitabu chake, Martin akaonekana kuanza kushangaa, japokuwa darasa zima lilikuwa likipiga kelele za shangwe lakini yeye wala hakuwa na habari na kelele hizo kwani mtu muhimu ambaye alitakiwa kuyasikia maneno yale alionekana kutokuwa na habari yoyote ile.

    Moyo wa Martin ukazidi kunyong’onyea, akajiona kukosa nguvu. Kwa hatua za taratibu akaanza kupiga hatua kuelekea nje jambo ambalo wanafunzi wote wakaonekaa kushangaa. Akaanza kutembea kwa mwendo wa haraka haraka huku macho yake yakimwangalia Patricia kupitia madirishani huku akizidi kupiga hatua.

    Akaingia darasani kwao na kutulia. Moyo wake ulikuwa umeumia kupita kawaida, kufanya kitu bila mlengwa kuwekea umakini wowote ule ulionekana kumuumiza. Martin alikaa katika hali ya unyonge kwa dakika kadhaa na ndipo mwalimu wa somo la historia kuingia darasani.

    Bado Martin alikuwa akionekana mnyonge, muda wote mwalimu alipokuwa akifundisha wala hakuonekana kutilia umakini somo lile. Moyo wake ulikuwa na hamu ya kutamani kumfukuza mwalimu ili arudi tena katika darasa lile. Mwalimu alichukua dakika arobaini ambazo zilionekana kuwa kama mwaka kwa Martin na kisha kutoka.

    Martin hakutaka kupoteza muda, hapo hapo akaanza kutoka darasani na kisha kuelekea katika darasa lile. Kama kawaida yao, wanafunzi wakaanza kupiga kelele za shangwe lakini kipindi hiki wala Martin hakutaka kuimba kitu chochote zaidi ya kumfuata rafiki yake, Saidi na kuanza kuongea nae.

    Alikaa darasani mule kwa kipindi kirefu huku muda wote macho yake yakimwangalia Patricia ambaye alikuwa bize akisoma kitabu cha Kingeleza. Muda nao ulizidi kuyoyoma mpaka kufikia kipindi ambacho kengele ya kwenda nyumbani ilipopigwa. Wanafunzi wakaanza kutoka huku macho ya Martin yakizidi kumwangalia Patricia ambaye alikuwa akijiandaa kuondoka.

    Patricia akasimama na kuanza kupiga hatua kuufuata mlango wa darasa lile. Martin hakutaka kubaki, nae akainuka na kuanza kumfuata Patricia. Alichokifanya ni kumuita kwani aliona kama angefika nje ingekuwa ngumu sana kwake kuongea na msichana huyo kutokana na macho ya watu kuwa wengi.

    “Mambo vipi?” Martin alimsalimia Patricia.

    “Safi” Patricia alijibuhuku akitoa tabasamu ambalo lilimfanya Martin kusahau kila kitu alichokuwa akitaka kuongea.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “OK! Tutaonana kesho” Martin alisema na kisha kuondoka bila kungoja Patricia angeongea nini.

    Patricia alibaki akimshangaa Martin, hakumuelewa mvulana yule alikuwa akitaka kuongea kitu kwake au alikuwa amekuja kumsalimia tu kama wavulana wengine, alichokifanya Patricia ni kupuuzia tu.

    Martin akaingia darasani mwao na kisha kuanza kuufuata mfuko wake wa Rambo ambao ulikuwa na madaftari yake na kisha kuubeba. Moyoni mwake akaanza kujuta kwa nini hakumwambia Patricia kile ambacho alikuwa akitaka kumwambia na wakati alikuwa amepanga kila kitu kabla. Moyo wake ukajuta zaidi na zaidi kwani hakuamini kama kuna siku angepeta bahati yoyote ya kuongea na msichana yule.

    “Mmmmh! Mbona moyo wangu unamuogopa msichana yule. Yaani mpaka nasahau kile ambacho nilitaka kumwambia. Kweli nitafanikiwa mimi au ndio nitakuwa napoteza muda wangu! Lakini hata haya mavazi nayo yanachangia mimi kumuogopa, yaani naonekana kama nimetoka kulima. Umasikini huu...huu umasikini....nitauchukia milele” Martin alijisemea huku akiwa amesogea dirishani akimwangalia Patricia akiingia ndani ya gari lile aina ya Prado akiondoka nyumbani kwao.

    ******

    Maisha yalikuwa yakiendelea kama kawaida. Moyo wa Martin bado ulikuwa ukiendelea kumuuma kupita kawaida. Alitamani sana kumwambia Patricia ukweli halisi wamoyo wake jinsi ulivyokuwa ukijihisi kwa wakati huo ila tatizo kubwa lilikuwa hofu.

    Martin alikuwa akimuogopa sana Patricia, kila alipokuwa akikutana nae alikuwa akikosa kabisa uhuru wa kumueleza kile ambacho kila siku alipokuwa akikaa kitandani alikuwa akitamani sana kumwambia. Muda ulizidi kwenda mbele, siku zikakatika na hata miezii nayo ilikwenda kwa kasi lakini bado Martin hakuwa wazi kumwambia Patricia kile ambacho kilikuwa kikimsibu moyoni mwake.

    Umaarufu wake shuleni bado ulikuwa ukizidi kuongezeka lakini aliuona kuwa si kitu kama tu msichana Patricia asingeweza kukubaliana nao. Kitu alichokuwa akikihitaji kwa wakati huo ni kuwa pamoja na Patricia tu.

    Bado juhudi zake za kuendelea kutunga nyimbo mbalimbali zilikuwa zikiendelea kama kawaida, hakutaka tena kusoma, kwake elimu ilionekana kuwa si kitu, muziki ndio ulikuwa ukishika kasi moyoni mwake. Aliwatazama wasanii wengi ambao hawakwenda shule lakini walikuwa na umaarufu mkubwa pamoja na fedha za kutosha ambazo walikuwa wakizitumia kufungulia biashara mbalimbali na kisha kuwaajiri watu ambao walikuwa na elimu zao.

    Hakuwa tayari kukiona kipaji chake cha kuimba muziki kikipotea, alikuwa akihitaji sana kuendelea kuimba na mwisho wa siku kuwa msanii mkubwa na kumchukua Patricia kwani aliamini endapo angepata umaarufu na fedha, kamwe Patricia asingeweza kumkataa.

    “Sasa nitamueleza lini?” Martin alikuwa akijiuliza katika kipidni ambacho alikuwa akiwangalia Patricia akipita na marafiki zake.

    “Ngoja nijitahidi kuutoa woga wangu leo” Martin alijisemea.

    Moyo wake ukaonekana kuchoka, kila siku kuuacha ukiumia kwa sababu ya mtu ambaye alikuwa na uwezo wa kumwambia kile ambacho alikuwa akikusudia kumwambia kulionekana kumpa tabu. Siku hii ya Jumatatu alikuwa ameamua kumwambia Patricia ukweli halisi wa moyo wake.

    Alichokifanya siku hiyo ni kuondoka nyumbani mapema sana. Ingawa kila siku alikuwa akivaa kandambili lakini siku hiyo akaamua kuazima vitau kwa rafiki yake, Jumanne. Japokuwa havikuwa viatu vya sare ya shule lakini akaamua kwenda navyo hivyo hivyo tu. Hakujali kama walimu wangemfukuza au kumwambia kitu gani, alichokuwa akikijali ni kumfuata Patricia na kumwambia ukweli juu ya mapenzi mazito ambayo alikuwa nayo juu yake.

    Alifika shuleni na moja kwa moja kuanza kuelekea darasani. Alitulia huku akisubiri kengele ya mapumziko kugongwa. Hakukuwa na somo lolote siku hiyo ambalo lilimuingia kichwani, muda wote alikuwa akimfikiria Patricia. Siku hiyo, masaa yalionekana kwenda taratibu sana tofauti na siku nyingine, alitamani kumwambia mwalimu kwamba atoke darasani ili aende kuongea na Patricia.

    Muda ambao alikuwa akiutamani ufike ukawadia, kengele ya mapumziko ikagongwa na kwa haraka haraka kutoka darasani. Ingawa alikuwa na presha kubwa ya kutaka kumuona Patricia lakini alipomtia machoni nguvu zote zikamtoka. Mapigo ya moyo yakaanza kudunda kwa kasi mara mbili zaidi ya ugongaji wake wa kawaida.

    Akaupiga moyo konde, akatoka dirishani alipokuwa akichungulia na kuingia ndani ya darasa lile. Kutokana na kutokuwa na wanafunzi wengi darasani, akaanza kumfuata Patricia pale alipokuwa amekaa.

    “Mambo” Martin alimsalimia Patricia ambaye akayainua macho yake na kumwangalia Martin usoni.

    Martin akaonekana kushtuka, siku hiyo Patricia alionekana kuwa mzuri zaidi ya siku nyingine. Nywele zake ndefu ambazo alikuwa amezifunga kwa nyuma zilioekana kumfanya kupendeza zaidi siku hiyo. Woga ambao alikuwa nao Martin ukazidi kuongezeka mpaka kufikia hatua iliyomfaya kujuta kwa nini alikuwa amekuja mahali hapo.

    “Poa. Karibu Martin” Patricia alimkaribisha.

    Martin akaonekana kutokuamini, japokuwa alikuwa maarufu shuleni hapo lakinihakuwa akijua kwamba hata Patricia alikuwa akimfahamu. Moyo wake ukatabasamu lakini huku macho yake yakionyesha hofu kubwa. Akavuta kiti na kutulia.

    Kila kitu ambacho alikuwa amekipanga kumwambia Patricia kikaonekana kupotea kichwani mwake jambo lililomfanya kubaki kimya huku akijifikiria ni kitu gani alitakiwa kuongea kwa wakati huo. Mwanzo alipanga kumtongoza Patricia moja kwa moja mara tu apatapo nafasi ya kuongea nae lakini muda huo hali ilionekana kuwa tofauti kabisa.

    Kadri muda ulivyozidi kwenda mbele na ndivyo ambavyo alikuwa akizidi kujawa na hofu moyoni mwake. Maneno yote ambayo alipanga kuyaongea yakampotea kichwani, hakujua aanzie wapi, aendelee na yapi na kumalizia na maneno gani.

    “Mbona kimya? Unafikiria wimbo wa kuniimbia?” Patricia alimuuliza.

    “Hapana. Unajua kuna kitu nafikiria sana” Martin alijibu.

    “Kitu gani?”

    “Unajua ni kwa kipindi kirefu sana nilikuwa nafikiria juu ya jambo moja”

    “Jambo gani?”

    “Masomo. Yaani natamani sana kusoma ili nami nifaulu kama wenzangu ila ninashindwa kabisa” Martin alisema huku akijua kwamba alikuwa amekwenda nje ya lengo lililompeleka mahali pale.

    “Sasa unashindwa nini kusoma?”

    “Muziki”

    “Umefanyaje?”

    “Umenikaa kichwani. Yaani kila wakati nafikiria kuandika nyimbo kuliko kusoma”

    “Vizuri. Kila mtu anafanya kile ambacho moyo wake unatamani kufanya. Inaelekea malengo yako makubwa yapo kwenye muziki na si kusoma. Kama yapo kwenye muziki, fanya muziki ila kama yapo kwenye masomo, soma tu” Patricia alimwambia Martin.

    “Mmmh! Nitaweza kweli?”

    “Kwa nini usiweze? Hayo ni maamuzi tu. Ukiamua utaweza” Patricia alimwambia Martin.

    Martin akabaki kimya kwa muda, akaanza kujifikiria ni maneno gani yangefuata baada ya hapo. Huku akiendelea kujifikiri, mara kengele ikasikika ikigongwa. Kidogo akaanza kuuona unafuu wa kuaga mahali hapo kwani tayari alikuwa amekwishaishiwa na maneno, mbaya zaidi hata hakujua aanzie wapi.

    “Tutaonana baadae” Martin alimwambia Patricia.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Haitowezekana. Nitaondoka mara nitakapofuatwa. Labda kesho”

    “Sawa” Martin alimwambia Patricia na kuondoka mahali hapo.

    Siku hiyo ndio ilikuwa siku ya furaha kuliko siku zote ambazo alikuwa amekaa shuleni hapo. Kitendo cha kuongea na Patricia kilionekana kumfurahisha kupita kawaida. Alitamani kuruka ruka kwa furaha, kwake, kuongea na Patricia japo kwa muda mchache kulionekana kumfurahisha sana.

    “Afadhali....... Afadhali.....” Martin alijisemea.

    “Ila ninavyoona kumtongoza haraka haraka sitofanikiwa kwani siku zote haraka haraka inaonekana haina baraka kabisa. Mmmh! Lakini si hata ngoja ngoja utakuta mwana si wako. Hawa wahenga wanachanganya sana, sijui hapa nimuamini mhenga gani, yaani wanatunga maneno huku wenyewe wakitofautiana. Ila poa, acha nimvutie kasi, siku nikichomoka, nachomoka na zote” Martin alijisemea huku muda wote tabasamu pana likionekana usoni mwake.



    Kitu ambacho Martin alikuwa akikitamani sana kutoka kwa Patricia kilikuwa ni mazoea tu. Alihitaji kuanza kumzoea binti yule mpaka pale ambapo angeamua kumtongoza na kumsikilizia angesema nini. Ingawa katika kipindi cha nyuma alikuwa na mpango wa kumtongoza haraka iwezekanavyo lakini hali ikaonekana kubadilika, Patricia hakuonekana kuendewa pupa, mtu ilibidi ujipange ili ufanikishe kile ambacho ulikuwa ukikihitaji.

    Kuanzia siku ile ambayo alikuwa ameongea nae, ilikuwa ni siku ya mwisho kuongea nae mpaka pale ambapo shule ikafungwa kwa likizo ya mwezi wa sita. Katika kile kipindi, Patricia alikuwa bize sana jambo ambalo lilimfanya Martin kutokuwa na muda wa kuongea nae kabisa. Hali ilionekana kuwa ngumu kwa Martin, kila siku alikuwa akionekana kuwa na mawazo kupita kawaida.

    Mwezi mzima walikuwa wamekaa nyumbani na hata pale shule ilipofunguliwa, bado mawazo yake yalikuwa juu ya msichana Patricia. Mishemishe yake ikaanza tena, hakutaka kushindwa tena, alimpenda na kumhitaji Patricia kuliko msichana yeyote yule.

    Akaanza kujipanga tena namna ya kumpata Patricia na kuanza nae mahusiano, Siku zilikwenda mbela lakini wala hakupata nafasi ya kuongea na Patricia. Marfiki zake Patricia walikuwa karibu nae siku zote kiasi ambcho hali ikaonekana kuwa ngumu sana kwa Patricia kupata muda kuongea na Martin.

    Kila siku Martin alikuwa akiumia kupita kawaida, alikuwa akizidi sana kumhitaji Patricia lakini mazingira ambayo yalikuwepo yalimfanya kuwa katika hali ngumu kumpata. Siku zikakatika, wiki zikakatika lakini bado hali ilikuwa ile ile, Patrica hakukaa nae chini na kuongea kama kipindi kile cha nyuma.

    Hapo ndipo Martin alipoamua kujitoa mhanga. Hakuwa radhi kujiona akiendelea kuteseka na wakati msichana ambaye alikuwa akimhitaji angeweza kumfuata na kumuomba kuongea nae. Siku hiyo ambayo alipanga kuongea nae ikawadia, kama kawaida, akaazima viatu na kuelekea shuleni. Muda ulikuwa ule ule, muda wa mapumziko ndio kwake ulionekana kufaa sana.

    Kila wakatika alikuwa akiulizia muda kwa marafiki zake, walimu ambao walikuwa wakiingia darasani wala hakuwaelewa hata kidogo. Kichwa chake kilikuwa kikimfikiria Patricia tu. Muda wa mapumziko ukawadia na hatimae mwalimu kutoka nje. Martin hakutaka kuchelewa, kwa haraka sana akatoka nje ya darasa lile na kuelekea katika darasa alilokuwa akisoma Patricia.

    Kila siku ambazo alikuwa akimwangalia Patricia alionekana kuwa na uzuri zaidi. Siku ile ambayo ilikuwa mara ya mwisho kuongea, uzuri ule ambao alikuwa nao siku ile haukuwa sawa na uzuri ambao alikuwa nao siku ya leo. Huku akionekana kujiamini, akaanza kupiga hatua kumfuata Patricia katika kiti kile alichokuwa amekaa na yeye kuvuta kiti cha pembeni na kukaa pamoja nae.

    Hata kabla hajaongea kitu chochote, akaanza kumwangalia Patricia usoni. Patricia alikuwa bize akisoma kitabu cha hadithi kilichoandikwa na mwandishi ambaye alikuwa akivuma sana kipindi hicho, Nyemo Chilongani kilichoitwa ‘ULINIUA GLORIA’.

    Patricia akayainua macho yake na kukutana na macho ya Martin, uso wa Martin ulikuwa ukionyesha tabasamu ambalo lilimfanya hata Patricia nae kutabasamu. Martin akaonekana kuchanganyikiwa, kuliona tabasamu la Patricia kwa mara ya pili kulionekana kumchanganya sana. Akashusha pumzi nzito.

    “Ilishindikana kabisa” Martin alimwambia Patricia.

    “Ilishindikana nini?”

    “Kusoma. Nilifeli sana ila kwa sasa sitotaka kufeli” Martin alimwambia Patricia.

    “Sawa. Uamuzi ni wako tu. Umechukua hatua gani kuzuia usifeli tena?” Patricia alimuuliza.

    “Nitahitaji msaada wako Patricia” Martin alimwambia

    “Msaada gani?”

    “Wa kunifundisha. Nahitaji unifundishe masomo mbalimbali” Martin alimwambia Patricia.

    “Sawa. Nitajitahidi”

    “Nitashukuru sana”

    “Ila na mimi nina ombi kwako”

    “Ombi gani?”

    “Nataka unifundishe muziki”

    Martin hakujibu kitu chochote. Kwanza akaanza kutabasamu, moyoni alitamani asimame na kushangilia, ombi ambalo alikuwa ameliomba Patricia lilikuwa moja ya ombi ambalo lingemfanya kuwa karibu na msichana huyo na hatimae kufanikisha kile ambacho alikuwa amekipanga.

    “Mbona upo kimya?” Patricia aliuliza.

    “Najaribu kufikiria kama nitakuwa na muda wa kufanya hivyo” Martin alimwambia.

    “Kama hauna muda, usijali, acha tu” Patricia alimwambia Martin.

    “Hapana. Muda ninao. Nitakufundisha tu” Martin alimwambia Patricia.

    Siku hiyo ndio ilikuwa siku ambayo urafiki wao ukafunguliwa rasmi. Martin hakutaka kuacha kuwasiliana na Patricia, kila siku alikuwa pamoja nae wakipiga sstori na kufurahi pamoja. Martin hakutaka kumpa nafasi Patricia kuwa na marafiki zake wengine, akaendelea kuwa bize nae na hatimae wawili hao wakawa marafiki wakubwa.

    Muonekano wa Martin ukaanza kubadilika, hakuwa Martin yle ambaye alikuwa akivaa kandambili, siku hizi akawa akivaa viatu huku akiwa na sare mpya zilizokuwa zikimvutia kila aliyekuwa akimwangalia.

    Patricia alikuwa akinukia kila kulipokuwa na uwepo wake,manukato mazuri na ya gharama ambayo alikuwa akinunuliwa na Patricia yalikuwa yakimfanya kuonekana mvulana mtanashati na anayevutia. Nywele zake hazikuwa tim tim kama kipindi cha nyuma, Martin huyu alikuwa amebadilika kwa asilimia mia moja.

    Akili yake akaituliza katika kusoma huku Patricia akianza kumfundisha masomo mbalimbali. Ingawa alikuwa akijifunza sana na kuanza kupiga hatua katika masomo yake lakini bado moyo wake ulikuwa ukimhitaji Patricia. Kuwa na uhusiano wa kimapezi ndio kitu ambacho alikuwa akikihitaji sana, kama urafiki ungeendelea namna ile hakika asingekuwa mtu huru kabisa, yaani asingeweza kuzungumzia mapenzi kila atakapokuwa nae.

    Siku zikaendelea kwenda mbele, wanafunzi wote wakaufahamu uhusiano ambao ulikuwepo kati ya watu hao, mabadiliko ya Martin hayakuonekana kuwashtua kwani walijua Patricia ndiye alikuwa mtu aliyeyaleta mabadiliko yale. Kila mwanafunzi alikuwa akijua kwamba watu hao walikuwa na uhusiano wa kimapenzi kwani ilikuwa ni vigumu sana kujua kwamba watu hao walikuwa marafiki wa kawaida kwa namna ambavyo walikuwa wakijiweka kila siku.

    “Bado ninahitaji awe msichana wangu” Hayo yalikuwa maneno ambayo mara kwa mara Martin alikuwa akiyaongea.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Siku ziliendelea kukatika huku urafiki ule ukizidi kuchanua. Martin alikuwa akimtembelea Patricia nyumbani kwao huku akitambulishwa kama rafiki mkubwa ambaye alikuwa akisoma nae shuleni. Martin akajisikia huru, tayari alijiona kuwa mpenzi wa Patricia japokuwa bado hakuwa ameambiwa hivyo na msichana yule.

    Martin akaamua kuanza kujipanga tayari kwa kumwambia Patricia ukweli wa moyo wake, kamwe hasingeweza kuvumilia na wakati moyo wake ulikuwa ukizidi kujisikia kiu ya kufanya kile ambacho alikuwa akihitaji kukifanya. Siku hiyo aliamua kukaa sana na Patricia chumbani kwake na hapo hapo ndipo alipoamua kulitoa duku duku lile ambalo lilikuwa moyoni mwake.

    “Nafahamu hata kabla haujaniambia hivyo” Patricia alimwambia Martin na kuendelea.

    “Sihitaji kujiingiza kwenye mapenzi Martin” Patricia alimwambia Martin maneno ambayo yalionekana kumvunja nguvu.

    “Kwa nini Patricia? Kwa nini hautaki kuingia kwenye mahusiano ya mapenzi pamoja nami?” Martin aliuliza kwa sauti ndogo iliyojaa huruma.

    “Unafahamu kwamba ninakupenda?” Patricia alimuuliza Martin.

    “Nafahamu”

    “Basi fahamu kwamba sitaki uumie” Patricia alimwambia Martin ambaye alionekana kuchanganywa na maneno yale.

    “Hautaki niumie? Kivipi?” Martin aliuliza kwa mshangao.

    “Wewe jua hivyo tu. Sitaki kukuumiza” Patricia alimwambia.

    Patricia hakutaka kukaa sana chumbani humo, akatoka na kuanza kuongea na Bi Maria, mama yake Martin. Martin alibaki chumbani huku akionekana kuchoka kupita kawaida, maneno ambayo aliyaongea Patricia yalionekana kumuondoa nguvu zote. Mawazo yake katika kipindi hicho yakajipa uhakika kamba msichana huyo tayari alikuwa katika uhusiano na mtu mwingine na ndio maana hakutaka kuwa nae kwa kuwa aliamini angemuumiza tu.

    Akainuka kitandani pale na moja kwa moja kueleka nje ya chumba kile. Kila alipokuwa akimwangalia Patricia alikuwa akichka zaidi, uzuri wa Patricia ambao alikuwa akiuona wala haikufaa kabisa kuwa rafiki yake. Patricia akaamua kuaga mahali hapo na kisha kuingia ndani ya gari pamoja na Martin.

    Martin alikuwa ametulia katika kiti pembeni ya Patricia, muda wote alikuwa akimwangalia huku akionekana kumchunguza kutokana na uzuri wake ambao alikuwa nao, bado moyo wake atika kipindi hicho ulikuwa na hamu kubwa ya kuendelea kumwambia Patricia umuhimu wa msichana huyo katika maisha yake.

    “Nakupenda Patricia. Nakupenda sana” Martin alimwambia Patricia.

    “Nafahamu. Nakupenda pia Martin ila kuingia kwenye uhusiano pamoja nae ni kitu kisichowezekana kabisa” Patricia alimwambia Martin.

    “Lakini kwa nini Patricia?”

    “Nimekwishakwambia kwamba sitaki kukuona ukiumia Martin. Ninakupenda sana tena sana tofauti na unavyofikiria. Sitaki kukuona ukiumia Martin” Patricia alimwambia Martin.

    “Hautaki kuniona nikiumia! Kivipi? Una mvulana au? Hata kama una mvulana, niambie tu ili nijue sababu kuliko kuniweka kwenye hali kama hii” Martin alimwambia Patricia.

    “Sina mvulana na wala sihitaji kuwa na mvulana. Na kama nitahitaji kuwana mvulana basi naamini wewe ndiye utakuwa mvulana wangu” Patricia alimwambia Martin.

    “Lakini mbona hautaki kuniambia?”

    “Muda bado. Muda ukifika nitakwambia. Tusome kwanza” Patricia alimwambia Martin.

    Bado maneno yale yalionekana kumchanganya Martin, ilikuwaje msichana akatae kuwa nae kwa kuwa alihofia kumuumiza. Kwake, alikuwa amejitoa asilimia mia moja kuumia kwa ajili ya Martin hata kama kitu gani kitatokea huko mbele lakini ili mladi tu awe nae katika uhusiano wa kimapenzi.

    “Labda kama una sababu nyingine”

    “Wala hakuna. Sababu ni hiyo hiyo. SITAKI KUKUUMIZA” Patricia alimwambia Martin ambaye alionekana kuwa mpole.



    Je nini kitaendelea?

    Je Patricia ataendelea na msimamo wake?

    Je ni maumivu ya aina gani ambayo yanamfanya Patricia kutotaka kuingia katika mahusiano na Martin?

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    ITAENDELEA





0 comments:

Post a Comment

Blog