Search This Blog

Sunday, July 10, 2022

SIPENDI UJINGA MIMI - 1

 







    IMEANDIKWA NA : NEA MAKALA



    *********************************************************************************





    Simulizi : Sipendi Ujinga Mimi

    Sehemu Ya Kwanza (1)

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Ni asubuhi tulivu, yenye mawingu mepesi, iliyopambwa na sauti za watu na vyombo mbalimbali vya moto. Wakina mama wengi wanaonekana vibarazani mwao wakipika chapati, maandazi, bagia, mihongo na vitafunwa vingine vya kila aina. Wengine wakiwa katika vibanda vyao vya biashara wakiandaa chai na supu kwa wateja wao.



    Ni wanawake wachache tuu kati ya wengi waishio Buguruni na vingunguti wanaonekana wakiwa nadhifu katika mavazi ya kiofisi. Wanaume pia hawakuwa nyuma kuacha vitanda vyao na kuwahi makazini, huku idadi ya vijana wengi wenye nguvu ya kufanya kazi wakiwa bado vitandani mwao wakiilaumu serikali kwa kutowapa ajira.



    “Jamani hii nyumba mnanitafuta ubaya walah! Maji nichote mimi nyie mtumie bila haya,” alikuwa mama Juma ambaye alilama baada ya kukuta maji yake yametumika bila ridhaa yake.

    “Kabla sijafanya lolote aliyetumia maji yangu naomba ajitokeze”

    “Eenh! Bibi wewe, kelele za nini asubuhi yote hii, watu tumelala na waume zetu watukera,” alisema mama Salehe ambaye aliamua kutoka chumbani kwake baada ya kuona mama Juma anazidi kulalama.

    “Mama Salehe naomba tueshimiane”

    “Nyoo! Niache kumueshimu mume wangu anayenifanya nijihisi kuwa mimi mwanamke, nikueshimu kinyago kama wewe inahuuu……,”

    Mama Juma akamuangalia mama Salehe kwa jicho kali, kisha akachukua ndoo iliyokuwa tupu na kuingia chumbani kwake bila kusema kitu.

    “Haloooo! Kumbe mikwala ya soda, kutikiswa na kutoa gesi ukishaachwa wazi kidogo Kushinehii,” mama Salehe alizungumza kwa kumkejeli mama Juma.



    Mama Juma na mama Salehe wanaishi katika nyumba moja kubwa yenye wapangaji 6 huku wao wawili tuu ndio wanaishi na waume zao, Wapangaji wengine walikuwa bado wanaishi kisela tuu hawajaoa na wengine hawajaolewa. Mzee kobelo anasifika kwa kuwa na busara nyingi mtaani ila wapangaji wake tuu hasa wakike walijizoelea umaarufu wa kuwa watu wa mdomo, wasiopitwa na jambo hata dogo.

    “Sasa aliyetumia maji yangu atajua mwenyewe na chooni leo sifanyi usafi kutabaki hivyohivyo,” akasema mama Juma mara baada ya kutoka ndani.

    “Wee mama usituzingue! Zamu zetu tumedeki vizuri tuu ukawa unaona raha kupeleka msambwanda wako kujisaidia leo imefika zamu yako visababu vingi,” Conso akajibu.

    “Halafu mama Juma sijui unatatizo gani, kila inapofika zamu yako uachi vituko, mara fagio limeibiwa, mara sabuni hamna, leo unasema maji wamechukua, mwanamke mzima tena unaitwa mama huoni haya,” Upendo nae akadakia.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Alafu nyie vishankupe acheni kufatilia mambo yasiyowahusu, ndio maana hamuolewi kazi kutumika na kuachika,” Mama Juma alijibu.

    “Mama Juma koma tena ukomae, wewe uliyeolewa umepata faida gani,” Conso akaendelea kujibishana na mama Juma. Ugomvi ule ukawafanya watu wote kuamka na kujazana uwani.

    Swala la kugombana katika nyumba ile ya mzee Kobelo lilikuwa la kawaida hata majirani walishazoea hiyo hali, hakuna siku iliyopita kwa amani. Japo lilikuwa jambo la kawaida ila kwa upande mwingine ilikua kero kubwa sana hasa kwa wapangaji wasiopenda fujo.

    “Jamani fujo za nini asubuhi yote hii, si muongee kistaarabu yaishe,” Fadhili akaingilia kati baada ya kutoka chumbani kwake akielekea msalani na kukuta mzozo huo.

    “Wewe nawe pita hayakuhusu, usije kusutwa bure mtoto wa kiume,” mama Juma akatupa dongo kwa Fadhili, Jamaa alivyoona vile akaamua awaache aendelee na shughuli zake.

    “Yaani paka akiondoka kidogo panya unajifanya kutawala, mbona ulinikimbia kama wewe mwanamke kweli, sasa hivi eti unajidai kuwasemesha wasichana wa watu, mtu mzima ovyo,” akasema mama Salehe.

    “Huhuhuhu! Mpee huyooo!” Upendo na Conso wakasapoti kinafiki.

    “Mimi ndiye niliyetumia maji yako nikayafulia na nguo hizo apo kwenye kamba zishakauka,” akasema mama Salehe.

    “Oooh! Kama mie sikubali,” Conso akaongea.

    “Yaani mama Juma, ukimuacha mama Salehe leo yaani wewe ni bonge la jinga, kama mie nalipiza maana sipendagi ujinga mimi,” Upendo akadakia.



    Maneno yale yakampa kichwa mama Juma akaenda kuanua nguo za mama salehe na kuzitupa kwenye karo la maji machafu, Mama Salehe akatweta kwa hasira akamuangalia mama Juma asimmalize, akajikuta anatoka nje, akainua sufuria la Supu na kulimwanga kisha akarudi ndani akamuangalia mama Juma na kumwambia,

    “Sipendi ujinga mimi…….”

    Maneno yale yakampa kichwa mama Juma akaenda kuanua nguo za mama salehe na kuzitupa kwenye karo la maji machafu, Mama Salehe akatweta kwa hasira akamuangalia mama Juma asimmalize, akajikuta anatoka nje, akainua sufuria la Supu na kulimwanga kisha akarudi ndani akamuangalia mama Juma na kumwambia,

    “Sipendi ujinga mimi…….”



    Watu wote wakashangaa kwa kitendo kile cha mama Salehe kumwaga biashara ya mwenzie, mama Juma uvumilivu ukamshinda akajikuta akimvaa mama Salehe kama mbogo, bila kutegemea wakajikuta chini wakioneshana ubabe, mama salehe akamgeuza mama Juma na kuanza kumshambulia kwa makofi ya uso. Kama unavyojua tena uswahilini watu wakipigana hamna wakuamulia hadi mmoja ashike adabu na kumueshimu mwenzie, ndivyo ilivyokuwa kwa wamama hao, majirani wenye simu zao zenye uwezo wa kuingia kwenye mitandao ya kijamii wakawa wanafanya kazi ya kupiga picha na kurekodi video kisha kuzituma mtandaoni,

    “Jamani waamulieni, watauana hao,” alikuwa mzee mmoja wa makamo aliyekuwa akipita njia na kukuta ugomvi huo.

    “Hamna wa kuwaamua waache wafundishane adabu,” jirani mwingine aliyetambulika kwa jina la Mwanahawa akadakia.

    Yule mzee akaangalia ule umati uliokuwa ukishangilia ugomvi ule, akatikisa kichwa hasa baada ya kuona kuna watoto wadogo pale ambao hata shule hawajaanza wakiangalia mama zao wakidhalilishana hadharani. Mzee akasogea karibu zaidi na alipo mama Salehe na mama Juma,

    “Wanangu embu acheni kuabishana”

    “Wee mzee mwanga nini, acha kuaribu starehe yetu”

    “Ndio kwanza ondoka hapa kabla ugomvi haujageuka kwako”

    “Kabisa ondoka, nenda kawange”



    Yalikuwa maneno ya kumkashifu mzee yule ambaye alikuwa na nia ya kuamulia ugomvi ule, mzee hakusikiliza maneno yao akamshika mama Salehe ambaye alimzidi nguvu kwa kiasi kikubwa mama Juma, Mama Salehe alichukia mno na kumuangalia yule mzee kwa hasira,

    “Wee mzee umeona majini yako yameshindwa kufanya kazi umeamua uje mwenyewe”

    “Hapana mwanangu, si jambo jema kupigana hadharani”

    “Nyoo! Uwe na mtoto kama mimi ulinge kwanza niachie na ondoka hapa kabla sijakufanyizia na wewe, Sura imekukomaa kama gaga”. Mama Salehe aliendelea kumshambulia mzee yule kwa maneno machafu,



    “Naomba muache hiki mnachokifanya saa hii,” alisema mzee yule.

    Mama Juma akamuacha mama Salehe na kuingia zake ndani, lakini kabla hajafika anapoenda mama Salehe akamuwahi na kumvuta nje,

    “Umenianza na mie ndio nitamaliza”

    “Sio kwamba nimekuogopa mama Salehe nimemueshimu yule mzee tuu la sivyo ungelitaja jina langu la utoto na lazima nitakuonesha tuu”

    “Hehehe! Halooooo!, sema mama mdomo mali yako wee,” walikuwa Upendo na Conso wakishabikia ugomvi ule.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kabla mama Juma hajajibu kitu, baba Salehe akatoka na kumshika mkono mkewe,

    “Hivi wewe mwanamke kwanini unapenda kuniabisha, huu ugomvi wako utaacha lini,” Baba salehe alifoka lakini kabla hajajibu yule mzee akasogea tena akamtazama baba Salehe kisha akamwambia,

    “Mrekebishe mkeo, nimemvumilia sana leo”

    “Eenh! Wewe kikongwe vipi, kiuno akate mwingine kuchoka uchoke wewe inahuu……puuuu!” akatema mate kuashiria mzee anamtia kichefuchefu.

    “Wooyooo! Hapo tuu mama Salehe ndio unatufurahisha wazee wengine bhana asubuhi yote hii wanaleta nuksi,” majirani wakadakia na wote wakaanza kucheka.

    Mzee akawatazama wote kwa makini zaidi, kisha akaondoka bila kusema neno,

    “Kwendraaaaa! Siku nyingine uangalie ugomvi wa kuamua, utaumbuka zee zima hovyooo!”

    Mama Salehe akamuandama mzee wa watu huku akibetua midomo yake, Japo baba Salehe alikuepo lakini hakuweza kusema kitu mbele ya mkewe. Baba salehe ambaye siku zote anapelekwa pelekwa na mkewe, wengi wakasema sio bure lazima mwanamke yule wa kidigo atakuwa amemficha kwenye chupa.



    Saa zikaenda kwa kasi na mambo yakawa shwari na kila mmoja akasahau kile kilichotokea asubuhi, japo katika vijiwe haikuwa rahisi kwa jambo ilo kusahaulika, kila mmoja akalielezea tukio lile kwa mtazamo wake. Gumzo kubwa lilikuwa kwa yule mzee aliyejaribu kusuluhisha ugomvi wapo waliosema amefanyiwa vibaya na mama Salehe na wapo waliomuunga mkono mama Salehe kwa kumuaibisha mzee yule.



    Jioni ya Siku hiyo hali ya hewa ikabadirika, wingu zito likatanda na upepo mkali ukautikisa mtaa wa Faru, wakina mama wakaanza kuhaha kutafuta watoto zao na kuwafungia ndani maana hali ya hewa iliogopesha mno. Mtaa wa Faru ni mmoja kati ya mitaa 4 iliyopo kata ya Mnyamani, mtaa huu unakasumba yakukutwa na mafuriko hasa mvua zikinyesha ivyo mabadiriko yale yaliwaogopesha wengi. Wapo waliojitahidi kurekebisha mabati yao, huku wengine wakishangilia mvua ije ili wapate nafasi ya kutapisha vyoo vyao. Ilikuwa ni saa 11.30 jioni lakini wingu lilitanda na kusababisha giza zito kama la saa 1.



    “Nyesha wee heshima iwepo chumbani, msio na waume mtajiju,” alikuwa mama Salehe ambaye alifurahi mno kwa mabadiriko yale akatamani mvua inyeshe.

    “Mvua hii leo itaniumbua, chumba changu kinavuja na mzee kobelo kila siku namlalamikia anirekebishie hataki,” akasema Conso.

    “Pole shosti nitakuazima beseni uweke kitandani mwako,” Upendo akamjibu Conso.

    “Mhmh! Leo shosti unistili mwenzio mvua ikinyesha ntakuja kulala kwako”

    “Wee! Ilo mwenzangu gumu hapa nilipo nishampigia kituu anakuja, wewe tafuta pengine”

    “Jamani! Basi tutajibana wote humo humo”

    “Shindwaa wee!”



    Wakati wakiendelea kuongea, upepo ukawa mkali ukaitikisa ile nyumba, na ghafla wakasikia sauti ya mtu akilia, walipoisikiza kwa makini wakagundua ni sauti ya mama Salehe ambaye aliwaacha muda mfupi uliopita na kuingia ndani.

    “Salehe mwanangu umekutwa na nini, mbona ulikua mzima tuu, jamani njoeni mumuone salehe wangu mie”

    Conso na Upendo ikabidi wakimbie kwa haraka kwenda chumbani kwa mama Salehe,

    “Kuna nini tena?”

    “Mtazameni salehe wangu mboni hatikisiki wala haongei, sijui kimemkuta nini mwanangu,” mama Salehe akaongea huku akilia asijue la kufanya.

    “Basi nyamaza mpigie simu baba yake aje tumuwaishe hospitali”

    “Mbona mwanangu hakuwa na dalili yoyote ya kuumwa alikuwa mzima tuu, sasa nini kimemkuta jamani,” mama Salehe aliendelea kulalama huku akilia.



    Bila kupoteza muda Upendo na Conso wakasaidiana na mama Salehe kumpeleka mtoto yule hospitali, Walifika na moja kwa moja Salehe akapelekwa chumba cha daktari, lakini daktari alivyomuona tu, akawaambia kuwa tayari Salehe alikwishafariki muda mrefu tuu. Mama Salehe alilia kama mtoto mdogo, Conso na Upendo wakajitahidi kumbembeleza lakini hawakufanikiwa. Manesi wakamshika mama Salehe na kumtoa kwenye chumba cha daktari hili kupisha uchunguzi zaidi wa kilichomuua Salehe.

    Baba Salehe akafika hospitali baada ya kupokea taarifa ya mtoto wake kuugua ghafla na kupelekwa hospitali, lakini akashindwa kuyazuia machozi yake hasa baada ya kumuona mkewe analia, akatazama pembeni akawakuta wapangaji wenzake pia wanalia, akaishiwa nguvu akajikuta anakaa chini na machozi yakimtoka,CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    “Ooh! Salehe mwanangu nini kimekuua katika umri mdogo hivi,” wakati akiendelea kujiuliza maswali yasiyo na majibu muuguzi akaja na kumtaka mzazi wa marehemu kwenda kupokea majibu ya vipimo. Baba Salehe akanyanyuka na kueleka alipoelekezwa, daktari akampokea vizuri na kumtaka akae,

    “Bila shaka wewe ni mzazi wa Salehe”

    “Ndiyo daktari”

    “Tumefanya vipimo vyote ili kugundua nini kilichosababisha kifo cha mwanao lakini hatukuona tatizo lolote”

    “Una maana gani daktari kusema hivyo wakati mwanangu amefariki”

    “Ukweli nina muda mrefu katika kazi hii ya udaktari lakini mazingira ya kifo cha mwanao nashindwa kuyaelewa, ila kwa sasa nenda tuu ukafanye taratibu zingine”

    Kauli ile ikamshtua zaidi baba Salehe, akutaka kusikia lolote akakimbia moja kwa moja hadi chumba cha kuhifadhia maiti, baada ya maelezo mafupi akaruhusiwa kuingia na akaoneshwa maiti ya mwanae, asee chozi lilimtoka mtoto wa kiume, mwanae aliyekuwa na rangi ya maji ya kunde leo amebadirika na kuwa wa mweusi kama mkaa. Baba Salehe alilia mno ila wauhudumu wakamtuliza na kumsii aende kufanya mpango wa mazishi tena kesho mapema sana.



    Kama wahenga wanenavyo penye wengi kuna mengi, kila mtu akaelezea kifo cha Salehe kwa namna aliyofikiri yeye,



    “Jamani hiki kifo cha Salehe sio bure lazima kuna mkono wa mtu”

    “Kweli kabisa, mimi nahisi mama Juma kamfanyia mwenzio ubaya”

    “Mhmh! Mimi nahisi yule babu wa asubuhi kaamua kumkomesha mama Salehe”

    “Alafu kweli! Inawezekana yule babu anajuana na mama Juma, si unaona alivyokuja kuwaamua mama Juma hakusema kitu akaondoka tuu”

    “Hapo umenena shosti, kwa hiyo yule babu na mama Juma njama moja”

    “Kabisa yaani”

    “Mhmh! Mwenzangu kama ndiyo hivyo mama Salehe asikubali alipize naye”

    Yalikuwa maneno ya majirani waliofika msibani wakiongea juu ya kifo kile cha ghafla cha Salehe. Nasra ni mdogo wa mama Salehe, wamezaliwa tumbo moja, wakati maongezi hayo yakiendelea akashindwa kuvumilia akatoka na kwenda alipo dada yake. Akamuelezea kila alichosikia ghafla hali ya mama Salehe ikabadirika, akahisi baridi kali japo jasho likawa linamtoka,

    “Ma….ma…. Ju……ma…….” Akawa anashindwa kumalizia sentensi yake, akahisi kukabwa kohoni, akaanguka chini na kuendelea kusema,

    Baada ya ugomvi mzito wa asubuhi ile, Mama Juma aliamua kwenda kwa dada yake anayeishi Kimara Suka, siku nzima aliamua aimalizie huko ili kuepusha shali. Wakati akijiandaa kurudi kwake ghafla hali yake ikabadirika,

    “Dada mbona sijielewi, najisikia vibaya sana,” alisema mama Juma.

    “Mhmh! Unajisikiaje kwani?”

    “Mapigo ya moyo yanaenda mbio mno, pia kichwa kinauma sana”

    “Mama Salehe kwani bado unayafikiria yaliyotokea asubuhi, utajiumiza kwa ujinga wako”

    “sio ivyo dada ila naumwa sana”

    “Basi pumzika nitamjulisha mumeo kuwa hautorudi leo”

    “Sawa dada,”

    Dada yake mama Juma akapiga simu ya shemeji yake lakini iliita tuu pasi na kujibiwa, alipiga tena na tena lakini haikujibiwa.

    “Naona baba Juma yuko bize sana leo maana hata simu hapokei”

    “Mhmh! Yule naye kazi zake utaziweza, mtumie ujumbe mfupi ataelewa”

    “Sawa ngoja nifanye hivyo”



    ***************



    Baada ya mama Salehe kuanguka na kupoteza fahamu, watu walitahayaruki na kila mmoja akasema lake, huzuni na uchungu mwingi ulimkumba Nasra akajikuta akiropoka kwa sauti ya juu iliyoambata na kilio,

    “Ooh! Mama Juma umemuua Salehe sasa hivi unaamia kwa mama yake,”

    Majirani wakajitahidi kumsii asitamke maneno hayo, maana huo sio wakati wake. Taarifa za kuanguka kwa mama Salehe na kupoteza fahamu zikamfikia Baba Salehe ambaye alikuwa kama amechanganyikiwa kutokana na kifo cha ghafla cha mtoto wake, busara ikafanyika mzee Kobelo ambaye ni baba mwenyenyumba akisaidiwa na Fadhili pamoja na baba Juma wakaenda kule alipoanguka mama Salehe,

    “Mtoeni nje haraka,” alisema baba Juma

    “sasa mbona atikisiki”

    “nyie mleteni huku anahitaji hewa ya kutosha,” alisema Mzee Kobelo baada ya kuona wanasita kufanya maamuzi.



    Mama Salehe akatolewa nje, watu wakaombwa waendelee na shughuli nyingine, wakamuacha kwa muda ili apate hewa nzuri. Wakati yakiendelea hayo Baba Juma akatoa simu yake ya mkononi na kukuta missed call nyingi, ikabidi asogee pembeni hili aangalie nani waliompigia, akakuta wengi hila akashtuka kuona shemeji yake alimpigia mara nyingi. Hofu ikaanza kumshika ukizingatia mkewe yupo huko, akaingia kwenye ujumbe mfupi na kukuta taarifa ya ugonjwa wa ghafla wa mkewe. Nguvu zilimuisha na hofu ikamzidi, akaaunganisha ugomvi wa asubuhi, kifo cha Salehe na kupoteza fahamu kwa mama Salehe, ikabidi asogee pembeni na kumpigia simu shemeji yake.

    “Hallo!”

    “Hallo shem habari yako?”

    “Habari yangu nzuri ila mkeo anashida”

    “Hiyo hali imemuanza muda gani”

    “Jioni hii, wakati anajiandaa kurudi huko”

    “Sawa shemeji ila huku nyumbani kuna matatizo”

    “Matatizo gani shemeji?”CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Salehe amefariki”

    “Mungu wangu! Shemeji wasema kweli?”

    “Ndiyo Shem, ila tafadhali usimwambie lolote mama Juma hadi hali yake itakapo kuwa sawa”

    “Usijali na poleni sana”

    Baba Juma akakata simu na kukaa chii huku akiendelea kutafakari juu ya matukio yale asipate jibu la kuridhisha.



    *************************



    “Yaani huyu mama Juma sio mtu kabisa”

    “Mwenzangu kweli mambo usiyoyajua ni sawa na usiku wa giza”

    “Nadhani huko aliko atakuwa anafuraha maana alichotaka kimetimia”

    “Kwani nyie mnajua mama Juma ameenda wapi?”

    “Aende wapi Zaidi ya kwa yule babu mchawi”

    “Mhmh! Ila mie aliniambia anaenda kimara kwa dada yake”

    “Kakuzuga huyo! Angekuwa kwa dada yake angesharudi”

    “Sijui baba Juma atajisikiaje akisikia mkewe mchawi tena muuaji”

    “Atakuwa anajua tuu, kwanza muda umemuona alivyokuwa na wasiwasi muda wote anaangalia simu”

    “Mimi nahisi kamzuia mkewe asirudi leo, maana pangechimbika bila jembe”



    Yalikuwa maongezi ya kinamama ambao walikuwa jikoni wakiandaa chakula kwa ajili ya watu waliokuja kuungana na baba na mama Salehe katika kuomboleza. Kama kawaida ya maisha ya uswahilini fikra za wengi zimefungwa kwenye Imani za kishirikina kwa kiasi kikubwa watu waliamini yote yanayotokea ni kazi ya mama Juma na yule babu.



    Siku ikapita na siku mpya ikaaingia, baada ya dua wanaume wakaanza safari ya kwenda maloloni kumpumzisha Salehe. Wakati wanaume wakiwa wameshaenda kuzika mama Juma naye alishaelezwa juu ya msiba wa Salehe hivyo akawa anawahi nyumbani kushirikiana na wenzake. Maskini mama Juma hakuwa anatambua tuhuma zilizozagaa juu yake, alipofika tuu nyumbani watu wote wakasimama na kumuangalia kwa hasira mno, mama Juma akasalimia lakini hamna aliyemuitikia, akapuuzia na kwenda moja kwa moja alipo mama Salehe lakini kabla hajafika akashikwa mkono na kuvutwa pembeni, akamtazama mtu aliyemvuta akashangaa sana.

    “Conso nini shida mbona umenivuta pembeni?”

    “Mama Juma sehemu hii si salama kwako”

    “Unamaanisha nini?”

    “Kwani uelewi au unanizuga?”

    “Embu niache nikamuone mama Salehe”

    Mama Juma akaanza kupiga hatua fupi kuelekea alipo mama Salehe, lakini Upendo akatokea na kumshika mkono kasha akaenda naye alipo Conso,

    “Nyie mna nini leo mbona siwaelewi?”

    “Mama Juma yaliyotokea yanatosha hatutaki matatizo Zaidi tafadhali ni bora ukaondoka kwa sasa,” akasema Upendo.

    “Jamani mbona mnaniacha njia panda nisielewe wapi pa kuelekea, niambeni nini kinaendelea”

    “Japo hatuna uhakika ila kila aliye hapa msibani anajua wewe ndiye uliyemuua Salehe na kama haitoshi mama Salehe pia alipoteza fahamu na hali yake bado sio nzuri sana na yote kwa sababu yako,” Conso akaamua amuanike kila kinachoendelea mama Juma.

    “Nyiee! Kuna vitu vya kutaniana ila sio hili jamani”

    “Hatukutanii ila ukweli ndio huo”

    “Sasa mie nahusika vipi na haya majanga”

    “Mhmhm! Mwenzangu sie hatusemi sana ila ndio ivyo wewe hukushangaa kwa nini watu hawakuitikia salamu yako”

    Mama Juma akajikuta anaishiwa nguvu na kukaa chini ukweli kwamba hajawahi kuamini ushirikina hata maswala ya waganga yeye aliyasikia tuu kwa majirani, roho ilimuuma sana akabaki Analia asijue nini la kufanya.

    “Hapana siwezi yafumbia macho haya lazima niende kwa mama Salehe, mie siyo muuaji na wala hata uchawi siujui”, akasema mama Juma na kuinuka pale alipokaa.

    Mama Salehe akawa mtu wa kulia kila anapomkumbuka mwanae, akamlaani sana mama Juma kwa kuwa aliamini kwa asilimia zote yeye ndiye aliyesababisha kifo cha mwanaye. Wakati akiendelea kulalamika na kuhuzunika mara watu wote walio pamoja na mama Salehe wakasimama, mama Salehe naye kilio kikakata, akajikuta ananyanyuka bila kuelewa nguvu alitoa wapi akamvaa mama Juma kama gari bovu, kwa kuwa mama Juma hakulitegemea hilo akajikuta naye akianguka chini kama gunia,



    “Mama Salehe japo mimi nawe hatuna maelewano lakini kamwe siwezi kuua mtu na wala huo uchawi au ushirikina unaoufikiria wewe mimi sina”

    “Mwanaharamu mkubwa wewe! Unajifanya mwanakondoo kumbe ndani nyoka mla watu, umeona kugombana name haitoshi ukaamua ukamle nyama Salehe wangu,” Mama Salehe aliongea kwa jazba sana.

    Ndugu na majirani waliopo hapo wakaona hatari iliyokuepo wakajitahidi kuwatenganisha huku wakimtaka mama Juma aondoke eneo lile.

    “Siwezi kuondoka katika hali hii, nani mwenye ushahidi wa kuonesha kuwa mimi ndiye niliyemuua Salehe?” mama Juma akahoji.

    “tutokee hapa na siasa zako nani asiyejua kuwa wewe ni mwanga na yule babu yako akajifanya kutaka kusuluhisha kumbe njama yenu moja tuu msyuuuuu!,” akasema mama Ashura ambaye ni rafiki wa karibu sana wa mama Salehe.

    “Kweli aondoke kabla hatujampiga mawe”

    “Ndiyo ondoka na uchawi wako hapa”

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Majirani wakaja juu kama moto wa kifuu kutaka mama Juma aondoke na asirudi tena pale. Wakati hayo yakiendelea walioenda kuzika wakawa wanarejea, baba Juma akastaajabu kukuta mkewe akiwa katika hali ile aidha baba Salehe pia akawa aamini kile anachokisikia. Kama ilivyo kawaida katika maisha ya binadamu linapokuja swala la maamuzi basi wengi huwa wanashinda hata kama wanachokipigania si chema. Baba Salehe akajikuta akimfata mama Juma na kuanza kumshambulia kwa makofi, baba Juma naye uvumilivu ukamshinda akashikana na mwanaume mwenzie, ugomvi ukaama toka kwa wanawake ukawa kwa wanaume.

    Wengi walihuzunishwa na tukio lile la kupigana msibani, wapo waliokubaliana na hiyo hali kwa kumuona mama Juma ni mwanamke hatari asiyefaa kuishi na watu, wazee wenye busara na hekima wakaamulia ule ugomvi na kuita kikao cha dhalura.



    “Japo si sawa kuyaongea haya ila siku zote ulimi ni kiungo kidogo lakini kinaweza sababisha madhara makubwa kama tunayoyashuhudia sasa, binafsi nimehuzunishwa na kifo cha Salehe lakini siwezi kusadiki hata kidogo kuwa kifo chake kilitokana na Imani za kishirikina,” alisema mzee Kobelo.

    “Wewe mzee nawe mwanga nini, daktari kathibitisha kabisa kuwa kifo cha mwanangu hakikuwa cha kawaida, alafu wewe unaongea pumba gani hapa, huyu mwanamke lazima atakuwa amemuua mwanangu,” akajibu mama Salehe.

    “Jamani kwanini tunaikosoa kazi ya mungu, baada ya kumuombea Salehe aione pepo tunakaa tukirumbana, hakika hii sawa,” alisema mzee kamanga mabaye ni m/kiti wa kitongoji hiko.

    “Mimi hapa naona mnanichanganya tuu, siwezi kuwaelewa,” mama Salehe akanyanyuka na kuondoka kwa hasira.



    “Baba Salehe, wewe ni mwanaume na kichwa cha familia jambo ulilolifanya muda ule si jema ivyo sisi kama wazee wa mtaa huu, tunakusihi usisikize maneno ya watu amini kuwa Salehe amekufa kwa mpango wa Mungu na jitahidi kumuongoza vyema mkeo” alisema Mzee Kamanga.

    “Sawa mzee wangu nimekuelewa na samahani sana kwa kilichotokea zilikuwa ni hasira tuu”

    “Baba Juma na mkeo msiwe na wasiwasi endeleeni na maisha yenu kama kawaida na ongezeni umakini Zaidi kwa kila mlichokifanya maana sio wote wanaopenda maendeleo yenu”

    Kikao kikafungwa na kila mmoja akaendelea na shughuli zake, ndugu, jamaa na marafiki wakabaki kumalizia tanga ndugu, kasha siku iliyofatia kila mmoja akarudi kwake kuendelea na shughuli za kila siku.



    BAADA YA MWEZI MMOJA



    “Hivi mama Salehe ndio umeamua kusahau kila kitu kuhusu mwanao, mie roho inaniuma sana hasa kumuona aliyesababisha bado anaendelea kuishi kwa furaha,” alisema mama Ashura.

    “Sio kama napenda shoga yangu ila sijui hata nifanyaje maana hata mimi naumia mno”

    “Mie kuna mtaalamu namjua, nataka nikupeleke akakufanyie mambo nawewe ulipize”

    “Mhmh! Mama Ashura unamaanisha kwenda kwa mganga?”

    “Ndiyo shoga yangu, tena huyo mganga ni kiboko hamna ashindwalo chini ya jua”

    “Hapana! Japo nimeumia na kifo cha mwanangu ila mungu atanilipia tuu”

    “Usiwe mjinga ujue hata Salehe huko mbele za haki alipo anaumia kwanini mama yake hutaki kumlipizia kisasi”

    “Mhmh! Tuyaache hayo bhana”

    “Mhmh sawa ukitaka msaada wangu mie nipo muda wowote”

    “Nashukuru sana, ukweli umekuwa kama ndugu yangu umenisaidia katika mengi mno”

    “Usijali sisi ni ndugu sasa”

    Wakaendelea kupiga soga hadi kiza kilipoanza kuingia mama Ashura akarejea kwake na kumuacha mama Salehe.



    Ni usiku mnene, mama Salehe akahisi kubanwa na haja ndogo, akatoka chumbani kwake na kuelekea chooni lakini kabla hajafika anasikia sauti anayoifahamu ikimuomba msaada,

    “Mama nakufa nisaidie! Mama……. Mama njoo unichukue….nateseka mwenzio”.

    Sauti hiyo inamshtua mno mama Salehe anaamua kuifata kule inapotokea, alipokaribia hakuamini macho yake kumuona salehe akiwa amezungukwa na watu asiyowafamu, akaumia sana akajikuta akitokwa na machozi.

    “Mwacheni mwanangu, msimtese kwani amewakosea nini?”

    Wale watu wakamwangalia mama Salehe na kucheka kwa nguvu, wakaanza kuimba na kuongea maneno yasiyoeleweka huku wakimsogelea mama Salehe.

    “Mkamateni tumchinje, zamu yake imewadia, hahahahahahaha!” ilikuwa sauti kubwa na yenye mitetemo ikiwaamrisha wale watu wamkamate. Mama Salehe alivyoona hayo ikabidi aanze kutimua mbio, akakimbia mno bila kuangalia wapi anaelekea, kadri alivyozidi kukimbia ndivyo upepo mkali mfano wa kimbunga ukawa unamfata. Mama Salehe aliongeza nguvu na kukimbia kuliko kawaida lakini akafika sehemu ambayo hakuwa na namna yeyote ya kujiokoa, akapiga magoti kusubiri kile watakachomfanya. Wale watu wenye kuogofya kwa kuwatazama, wakamsogelea na kucheka kwa nguvu sana kasha mmoja akanyanyua mkono na kumpiga kofi la usoni, mama Salehe akahisi kizunguzungu, akahisi mwili unashikwa ganzi na kuishiwa nguvu kasha akaanguka chini huku akisema,

    “Msiniue niacheni, mwachieni pia Salehe wangu”



    “Msiniue niacheni, mwachieni pia Salehe wangu”

    Kisha akaamka kutoka ndotoni, Baba Salehe naye akashtushwa na kelele alizopiga mkewe,

    “Vipi unanini wewe”

    “Baba Salehe mwanetu watamuua tukamuokoe”

    “Mhmh! Yaani bado unafikra potofu juu ya kifo cha Salehe, mke wangu embu jaribu kusahau hayo”

    “Siwezi kabisa! Salehe ananiita huku akiomba msaada kama haitoshi wanataka kuniua na mimi”

    “Mama Salehe hiyo ni ndoto tuu, na usiifikirie sana”

    “Sikubali na sitojali kama utaungana namimi au la, ila lazima nitamuonesha mama Juma kuwa hata mimi nayaweza”CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Unafikiria kufanya nini?”

    “Kwenda kwa mtaalamu”

    “Mama Salehe! Mimi sikubaliani na wewe, waganga wengi ni waongo na wagombanishi tuu”



    Mama Salehe akamwangalia mumewe, kisha akavuta shuka na kuendelea kulala bila kusema kitu, akayakumbuka maneno ya shoga yake mama Ashura, akaomba usiku upite tuu hili akamueleze aliyaota na ikiwezekana afunge safari ya kwenda kwa huyo mtaalamu.



    ****************



    “Vipi shoga yangu mbona asubuhi yote hii?” aliuliza mama Ashura.

    “Mwenzangu yamenikuta na siwezi kuvumilia tena”

    “Yapi tena hayo”

    “Mimi nataka unipeleke kwa mtaalamu wako”

    “Hahaha! Mara hii shosti, wewe jana tuu si ulikuwa una itikadi za kilokole”

    “Mama Ashura kwa nilichoshuhudia usiku wa jana siwezi nikakaa hivi hivi”

    Mama Salehe akamuelezea rafiki yake kila kitu kuhusiana na ndoto yake, mama Ashura akamuhurumia sana na kumtaka akajiandae ili waweze kuelekea kwa mtaalamu,

    “Sasa shosti ndiyo tunaenda vipi kuhusu mumeo utamuagaje au naye anajua kuhusu hili?”

    “Niliongea naye usiku nikamwambia kila kitu lakini hakuniunga mkono, ila mimi siwezi kufumbia macho hili swala, haiwezekani mtoto wangu afe, halafu aliyemuua anaishi kwa furaha na biashara zake zinazidi kushamiri”

    “Alafu nasikia wanajenga huko mbezi,” mama Ashura akachochea.

    “Kafara hilo la mwanangu wao wanafanikiwa tuu ila lazima nimuoneshe joto ya jiwe, asipoulamba mchanga basi ata uchizi hautomkosa”.

    Wakaagana na mama Salehe akarejea kwake kujiandaa kwa ajili ya safari ya kwa mganga.



    Baada ya muda mfupi wakawa tayari ndani ya daladala inayoenda mbagara alafu wakifika hapo ndiyo wapande gari linaolekea Rufiji. Magari ya mbagala yanasifika sana kwa kujaza abiria hadi mlangoni, hali haikuwa tofauti katika gari alilopanda mama Salehe na rafiki yake kipenzi mama Ashura.

    “Oyaah! Kinamama sogeeni nyuma na wenzenu waende”

    “Tusogee wapi! Kwani wewe huoni kama tumefika mwisho na hamna nafasi nyingine”

    “Aah! Bimkubwa unanibania riziki yangu, utajitanuaje hivyo kama upo leba bana miguu wenzio wapate nafasi”.

    “Eenh! Wewe konda huna wakubwa kwenu, maneno gani hayo ya kuongea”

    “Wewe mama kausha mimi naongea na mwenzio”

    Konda akawa analumbana na mama Salehe ambaye alikuwa mpole sana siku hiyo, kitu kilichomfanya mama Ashura aingilie kati kumtetea shoga yake.

    “Mama Ashura achana naye ajielewi na wala sisogei”

    “Wewe mama mwanga nini! Ntakushusha ujue, siwezi kukosa pesa kwa sababu yako”

    “Eenh! Kijana naona unataka kunipanda kichwani sasa kama wewe unajiamini niguse uone”

    “Oyah suka simamisha gari, kwanza nimfundishe adabu mtu”

    “Aah! Mnatuchelewesha bwana kama hamuendi tushuke tupande gari linguine”

    “Hapa hamna kushuka ila huyu mama lazima ashuke yeye,” aliongea konda huku akimfata mama Salehe aliyesimama nyuma kabisa.



    Wakati hayo yakiendelea askari wa usalama barabarani akawa anasogea maeneo yale, baada ya kusikia kelele za mzozo, mama Salehe alivyoona askari amekaribia akampiga kofi kondakta, huku abiria pamoja na askari wakishuhudia.

    “Sio kila mwanamke unayemuona unajua wa kumchezea, mimi ni sawa na mama yako, kijana mdogo kutamani watu wazima, mfyuuuu”

    “Huhuhu! Mpe huyo kazoea kushika shika wanawake,” mama Ashura akaendeleza mchezo na konda akabaki kuduwaa asielewe kinachoendelea.

    “Sasa wewe si umezoea huu mchezo wa kudharirisha wanawake leo tutafika mbele ya sheria”

    Minong’ono ikaanza ndani ya gari kila mmoja akaongea lake wapo waliomsapoti mama Salehe na wapo baadhi waliokuwa katikati wasijue waungane na konda au mama Salehe.

    “Abiria wote shukeni mpande gari nyingine,” ilikuwa sauti ya askari wa barabarani aliyefika muda kidogo na kushuhudia mama Salehe akimuwakia konda.

    “Bora askari ulivyokuja yaani huyu hawezi kunidhalilisha alafu mimi nikamuachia hivi hivi,”

    “Nimeyasikia yote mama yangu, dereva unakosa la kusimamisha gari katika kituo kisicho rasmi, hivyo unatakiwa kulipa faini ya shilingi elfu thelasini (30,000) pesa za kitanzania, na kuhusu kesi ya huyu mama maelezo mtayatoa kituoni”.

    Konda aliishiwa nguvu kabisa, akamtazama mama Salehe asimmalize, ikabidi alipe faini aliyotajiwa papo kwa papo alafu abaki na swala la mama Salehe.

    “Sasa afande mie siwezi kwenda kituoni naomba tuyamalize hapahapa,” konda akasema

    “Hapana afande hiyo sio sawa lazima twende kituoni, yaani utawezaje kunishikashika mie mke wa mtu tena kwenye gari kila mtu anashuhudia asee wewe”

    “Duuh! Wewe mama umetumwa au?”

    “Afande si unashuhudia alivyo kiburi mimi naona tutaelewana kituoni,” mama Salehe akaongea.

    “Embu malizeni haya mambo kiutu uzima, mfidie muendelee na shuguli zenu”

    “Afande swala la kumlipa fidia litakuwa gumu twende popote pale,” konda akajibu.

    “Dereva na nyie wakina mama pandeni kwenye gari tutayamaliza kituoni”

    “acha ujinga wewe, kituoni sehemu nyingine, mlipe uyo mama unajua hata nusu hesabu hatujafikisha,” dereva akawaka.

    Konda akaingiza mkono mfukoni akatoa elfu kumi na kumpa mama Salehe, lakini hakuipokea akamkazia jicho,

    “Wewe mtoto kuwa na adabu, kosa ulilolifanya unafikiri linafutika kwa hiyo elfu kumi yako”

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Konda akaingia tena mfukoni na kumuongeza mama Salehe jumla ikawa elfu ishirini, Mama Ashura akamwambia aipokee waondoke muda unazidi kwenda, mama Salehe akaipokea wakamshukuru yule afande na wakamtazama konda kasha wakasema,

    “Usirudie siku nyingine, hatupendi ujinga sisi mfyuuuuu!”

    Safari ikaendelea na baada ya saa 4 wakawa wamefika nyumbani kwa mganga mashuhuri mzee Bang’ala, wakakaribishwa na kukaa kwenye mkeka uliopo maeneo hayo, tayari kwa kusubilia huduma.

    “Subilini kidogo babu kuna mtu amuhudumia”

    “Sawa”





    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog