Simulizi : Safari Ndefu Kuelekea Kaburini
Sehemu Ya Nne (4)
Taarifa zilikuwa zimekwishatolewa kwamba Martin alikuwa akirudi nchini Tanzania baada ya kukaa nchini Marekani kwa muda wa mwaka mmoja na nusu. Katika kipindi hiki hakuwa akirudi peke yake kama kipindi kingine, kwa sasa alikuwa akirudi na msichana ambaye alikuwa akimpenda, msichana ambaye alikuwa ameyabadilisha maisha yake, Patricia.
Watu wakakusanyika katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere kwa ajili ya kuwapokea watu hao. Mabango mbalimbali ambayo yalikuwa yakimtakia Patricia afya njema yalikuwa yakionekana kushikwa na watu wengi ambao walikuwa wamekusanyika uwanjani hapo.
Saa saba na robo mchana ndege ikaanza kuingia uwanjani hapo. Watu wakaanza kujisogeza huku waandishi wa habari wakizishika kamera zao vizuri. Ndege iliposimama, Bwana Thomson pamoja na mpenzi wake, Bi Beatrice wakaanza kuteremka. Baadae, kitanda kilichombeba Patricia kikaanza kuteremshwa huku Martin akiwa pembeni. Watu wakashindwa kujizuia, machozi yalikuwa yakiwatoka huku vilio vikianza kusikika uwanjani hapo
Hali aliyokuwa nayo Patricia ilionekana kumgusa kila mtu, watu walionekana kuumizwa kupita kawaida. Martin alikuwa pembeni, alionekana kuwa mnyonge na hata lile tabasamu ambalo alikuwa akilitoa halikuwa lile tabasamu ambalo lilizoeleka kuonekana usoni mwake.
Moja kwa moja waandishi wa habari wakaanza kumsogelea na kuanza kumuhoji baadhi ya maswali. Kila kitu ambacho alikuwa akikiongea mahali hapo bado alikuwa akisisitiza upendo wake mkubwa ambao alikuwa nao juu ya Patricia.
“Ninampenda. Ninamuhitaji sana” Martin aliwaambia.
Kitu alichokifanya Bi Beatrice ni kuwashukuru watu wote elfu mbili ambao walikuwa wamejitolea muda wao kufika uwanjani pale kwa ajili ya kuwapokea na kisha safari ya kuelekea nyumbani kuanza.
Muda wote Martin alikuwa pembeni ya Patricia, hakutaka kukaa mbali nae hata mara moja. Kwake, bado Patricia alionekana kuwa msichana ambaye alihitaji uangalifu mkubwa kutoka kwake.
“Najua nitakufa Martin” Patricia alimwambia Martin huku akionekana kukata tamaa.
“Haiwezekani. Hautokufa”
“Unanifariji tu Martin. Nitakufa tu. Yaani ni afadhali nife Martin kuliko kuendelea kuteseka kitandani namna hii” Patricia aimwambia Martin ambaye alibaki kimya.
Tayari machozi yakaanza kumtoka Martin. Kukata tamaa kwa Patricia kulionekana kumuumiza kupita kawaida. Alijua kwamba Patricia alikuwa katika hali mbaya lakini bado hakutaka kumpoteza.
*********CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Tajiri mkubwa, Bwana Jonathan alionekana kuridhika na ile ajali ambayo ilikuwa imetokea, mipango yake ambayo alikuwa ameipanga akaiona ikiwa imekwenda kama vile alivyopanga kabla. Moyo wake ukawa unasherehekea, kitendo cha Patricia na Banana kulazwa hospitalini kilionekana kumfurahisha.
Moyo wake ulikuwa ukimpenda na kumtaka sana Patricia, kitendo cha kumkatalia mara kwa mara ndicho kilimfanya kuamua kuipanga ajali ile mbaya. Kila alipokuwa akiona Patricia na Banana wapo hospitalini alikuwa akijisikia faraja kupita kiasi moyoni mwake.
Siku ziliendelea kukatika huku nae akijifanya kufika hospitalini pale kwa ajili ya kuwaangaia wagonjwa wake. Kila alipokuwa akifika hospitalini hapo alikuwa akifurahia kupita kawaida, tayari aliona kwamba alikuwa amewaweza kwa kipindi hicho.
Kadri siku zilivyozidi kwenda mbele na ndivyo hali za wagonjwa wale zilivyozidi kuwa mbaya kiasi ambacho moyo wake ukaanza kuingiwa na wasiwasi zaidi. Ni kweli alitaka wawili wawe wapatwe na ajali ile ambayo alikuwa ameipanga lakini moyo wake haukutaka watu wale wakae hospitalini kwa kipindi kirefu.
Kadri hali ilivyozidi kwenda mbele na ndivyo ambavyo hali ya Patricia na Banana zilivyozidi kuwa mbaya. Bwana Jonathan akaanza kujutia kile ambacho alikuwa amekifanya, mara kwa mara alipokuwa akilala alikuwa akipata ndoto na mawazo ya ajabu ajabu.
Moyo wake ukaanza kujawa na majuto. Kila siku alikuwa akijikalia kitandani mwake akilia. Kadri picha ya Patricia na Banana zilivyokuwa zikimjia kichwani kwa jinsi walivyokuwa kule hospitalini alikuwa akiumia zaidi. Usiku hakulala vizuri, utajiri mkubwa ambao alikuwa nao ukaonekana kutokuwa na furaha kabisa.
Hali ilizidi kuwa mbaya kwake hasa pale ambapo Banana alipofariki. Akaanza kuihisi damu ya Banana ikimlilia kila usiku alipokuwa akilala. Ndoto mbaya za kutisha na kusisimua zilikuwa zikimuandama kila siku. Amani akakosa moyoni mwake, akawa mtu wa mawazo kupita kawaida.
Alitamani kutubu juu ya kile kitu ambacho alikuwa amekifanya, hakujua dunia ingemchukulia vipi na watu wangemuonaje. Kutubu ndicho kitu ambacho alikuwa akitaka kukifanya kwa kuamini kwamba angeweza kuwa na amani moyoni mwake kama ilivyokuwa zamani.
Kila siku alikuwa akipiga magoti na kutubu mbele ya Mungu wake lakini hali ile haikuweza kumtoka, damu ya Banana ilikuwa ikimlilia kila siku. Mipango yake mingi ya biashara ikaonekana kuanza kwenda hovyo, muda mwingine Bwana Jonathan alionekana kuwa kama mtu ambaye alichanganyikiwa.
Kila siku alikuwa akiongea peke yake, akili yake ikaonekana kuanza kuharibika kutokana na mawazo mabaya pamoja na mambo ya ajabu ajabu ambayo yalikuwa yakimjia kichwani mwake. Walinzi wake walionekana kumshangaa sana, hali ambayo alikuwa nayo katika kipindi hicho ilionekana kuwa tofauti kabisa na zamani.
Tayari mkewe, Bi Leticia alikuwa amekwishaanza kuyaona mabadiliko ya mume wake jambo ambalo likapelekea kuanza kufanya mawasiliano na watu wa Saikolojia na kumpeleka mumewe katika ofisi za watu hao. Huko ndipo ambapo akili ya Bwana Jonathan ikaanza kushughulikiwa kwa kuambiwa mambo mengi kama kuifanya akili hiyo irudi kama zamani.
Kila siku Bwana Jonathan alikuwa akipelekwa kwa watu hao lakini bado hali haikuweza kubadilika kabisa. Kila siku alikuwa akiona mauza uza hasa nyakati za kulala, sauti za ajabu ajabu zilikuwa zikisikika masikioni mwake huku wakati mwingine picha ya Patricia akiwa kitandani ikimjia pamoja na kuona jeneza lililoandikwa jina la Banana pembezoni mwa chumba chake.
Kazi zote ambazo alikuwa akizifanya akamuachia mtoto wake, Robert. Kadri muda ulivyozidi kwenda mbele na ndivyo ambavyo Bwana Jinathan alivyozidi kuchanganyikiwa mpaka kufikia hatua kubwa zaidi ya kuanza kutupa vitu huku na kule.
Kila mtu ambaye alikuwa akisikia juu ya hali aliyokuwa nayo Bwana Jonathan alikuwa akishangaa, hakukuwa na mtu ambaye aliamini kama tajiri yule alikuwa amechanganyikiwa kiasi cha kupelekwa katika hospitali ya vichaa iliyokuwa hapo jijini New York.
Hakukuwa na mtu ambaye aliujua ukweli zaidi yake yeye pamoja na wale watu ambao alikuwa ameshirikiana nao. Bwana Jonathan akawa amechanganyikiwa kwa asilimia mia moja. Mauza uza ambayo yalikuwa yakionekana kwake hayakuwa yakipungua, mara kwa mara alikuwa akipiga kelele huku akiliita jina la Banana kitu ambacho kilionekana kuwashangaza manesi na madaktari.
Kila siku mkewe, Bi Leticia alikuwa akimtembelea katika hospitali ile. Kwa wakati huo na ile hali ambayo alikuwa nayo, Bwana Jonathan hakuwa akimtambua mtu yeyote yule. Kila alipokuwa akimuona mke wake na mtoto wake, aliwaona watu wageni ambao walikuwa wamekuja kumtembelea.
Mara kwa mara alikuwa akilitaja jina la Patricia na Banana, hakukuwa na mtu aliyeelewa sababu ambayo ilimpelekea Bwana Jonathan kuyatamka majina hayo ya watu ambao walikuwa wamepata ajali kipindi cha miezi sita iliyopita.
Mwaka wa kwanza ukapita, wa pili ukapita na wa tatu kuingia. Bwana Jonathan alikuwa katika hali ile ile ambayo ilikuwa ikiwashangaza watu wote. Wapo ambao waliamini kwamba mzee huyo alikuwa amerogwa na watu ambao hawakupenda kumuona akiendelea kuvuna kiasi kikubwa cha fedha.
Mara kwa mara waandishi wa habari walikuwa wakielekea kwa mganga Mutinho ambaye alikuwa na asili ya Brazil aliyekuwa akiishi pale nchini Marekani na kuanza kumuuliza chanzo cha ugonjwa wa Bwana Jonathan.
Mganga Mutinho ndiye alikuwa mganga mashuhuri nchini Marekani ambaye alikuwa akitumia uchawi wa nyumbani kwao Brazil na kuwaponya watu, kuwapa watu utajiri, mafanikio na hata umaarufu mkubwa duniani. Watu wengi ambao walikuwa wakihitaji kufanikiwa katika maisha yao walikuwa wakimfuata Mutihno ambaye alikuwa akiwapa dawa na baada ya siku saba kupata kile ambacho walikuwa wakikihitaji.
Mgana Mutihno alikuwa na jina kubwa nchini Marekani, umaarufu wake ndio uliwafanya Wabrazil wengi kuanza kuruhusiwa nchini Marekani kwa kuonekana kwamba wangeweza kuwa kama Mutinho ambaye alionekana kuwa msaada mkubwa kwa watu ambao walikuwa wakitafuta mafanikio na umaarufu nchini Marekani.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kila alipokuwa akiulizwa na waandishi wa habari juu ya hali ya Bwana Jonathan, Mutinho hakutoa jibu lolote zaidi ya kutaka mtu huyo kupelekwa kanisani na kufanyiwa maombezi.
Jibu lile likaonekana kumshangaza kila mtu. Mganga yule ambaye kila siku alikuwa akiupinga Ukristo kwa nguvu zote leo ndio alikuwa akitaka mtu huyo apelekwe kanisani kufanyiwa maombezi. Kila mtu alionekana kushtushwa na ushauri ule wa mganga Mutinho.
Mganga Mutinho hakuishia hapo, akaanza kuwaambia waandishi mambo mengi ambayo yangemfanya yeye kushindwa kabisa kumtibia Bwana Jonathan kwa kuwaambia kwamba ugonjwa ule haukuwa na wakurogwa au mchezo mchafu ambao matajiri hasa wa Marekani walikuwa wakipenda kutumia bali ulikuwa ni ugonjwa ambao wala haukutakiwa kutolewa na nguvu za majini kwa sababu yasingeweza kabisa.
Bi Leticia alipoambiwa kuhusu kumpeleka mumewe kwenye kanisa lolote nchini Marekani, akaonekana kupinga. Katika maisha yake alikuwa kama mumewe, alikuwa akiuchukia Ukristo kupita kawaida. Hakuupenda Ukristo, kila siku katika maisha yake alitamani dini hiyo ipotee kabisa na dunia nzima kuwa wapagani kama jinsi alivyokuwa yeye na familia yake.
Toka siku ambayo Bi Leticia alipopewa ushauri kuhusu kumpeleka mumewe kufanyiwa maombezi na ndio siku ambayo ugonjwa ule wa mumewe ukazidi kuongezeka na kuwa mbaya zaidi. Kila mtu ambaye alikuwa akipita mbele yake, Bwana Jonathan alikuwa akichukua viti, chupa na vitu vingine na kuanza kumrushia.
Madaktari wakaona hali kuwa mbaya zaidi, walichoamua kukifanya kwa wakati huo ni kumfunga minyororo Bwana Jonathan huku tiba ambayo wala haikuonekana kuwa na mafanikio ikiendelea kutolewa mwilini mwake.
“Impossible (Haiwezekani)” Bi Leticia aliwaambia waandishi wa habari ambao walimpelekea ushauri wa mganga Mutinho.
Huo ndio msimamo ambao alikuwa ameuweka katika maisha yake. Aliapa kutokuingia kanisani kabisa, kutokana na kuuchukia Ukristo basi hata kanisa alilichukia kabisa. Kila siku alipokuwa akiambiwa kuhusiana na ushauri ule wa kumpeleka mumewe kufanyiwa maombezi kanisani bado aliendelea kupinga.
Ilikuwa ni afadhali umchome hata kisu lakini si kumwambia kuingia kanisa. Kila mtu alionekana kumshangaa Bi Leticia. Kama mwanamke huyo alimuamini sana mganga Mutinho kama Wamarekani wengi walivyomuamini, sasa kwa nini hakuwa akiamini kama ushauri wake ule ungeweza kufaa?
Kadri alivyozidi kukataa na ndivyo hali ya mumewe ilivyozidi kuwa mbaya zaidi na zaidi. Katika kipindi hiki Bwana Jonathan akaanza kujidhuru yeye mwenyewe. Akaanza kujipiga piga huku akijing’ata ng’ata kila wakati hali ambayo ilimfanya muda wote kutokwa damu.
Hali ile ilitisha, kila siku ilikuwa ikimliza Bi Leticia lakini kamwe hakutaka kuufuata ushauri wa kukubali kumpeleka mumewe kanisani kufanyiwa maombezi, bado aliendelea kukataa.
Maisha yakaanza nchini Tanzania, bado Patricia alikuwa mtu wa kulala kitandani huku mipira ya chakula ikiwa imepitishwa kama kawaida yake. Hali yake bado ilikuwa ikionekana mbaya pale kitandani. Wazazi wake walikuwa ni watu wa kuhuzunika kila wakati, mioyo yao ilikuwa ikimshukuru Martin ambaye kamwe hakutaka kutoka nje ya nyumba ile, kila siku alikuwa ndani akikaa pamoja na Patricia huku akimhudumia kwa kila kitu.
Watanzania wengi wakaonekana kuguswa na hali ambayo alikuwa nayo Patricia jambo ambalo likawafanya kumiminika ndani ya nyumba ile kwa lengo la kumuona msichana huyo ambaye alikuwa katika matatizo makubwa. Kila mtu ambaye alikuwa akimwangalia Patricia alikuwa akilia, hakukuwa na mtu ambaye aliamini kwamba duniani kulikuwa na mtu ambaye alikuwa na matatzo makubwa kama aliyokuwa nayo Patricia.
Wachungaji mbalimbali walikuwa wakienda kumwangalia Patricia na kumfanyia maombi huku nao hata mashehe kutoka sehemu mbalimbali wakimiminika nyumbani pale na kumuombea dua. Kila mmoja alikuwa akiamini kitu kimoja kwamba kungetokea siku ambayo Mungu angefanya miujiza na hatiamae Patricia kupona na kuwa mzima kabisa.
Martin alikuwa akionekana kuwa na huzuni muda wote, maisha yake yalikuwa yamebadilika kwa asilimia mia moja. Furaha haikupatikana tena moyoni mwake, alikuwa mtu wa majonzi kila siku. Mtu ambaye kila siku alikuwa akitamani kumuona tena alikuwa amekwishamuona ila tatizo lilikuwa ni hali ambayo alikuwa amemkuta nayo.
Bwana Thomson alikaa kwa muda wa mwezi mmoja huku akiwa amekwishamuandaa daktari ambaye kila siku alikuwa akitakiwa kufika mahali hapo kwa ajili ya kumhudumia Patricia huku akiwa amekwishalipia gharama za mwaka mzima. Ingawa daktari alikuwa akimhudumia Patricia lakini kamwe Martin hakutaka kuondoka chumbani humo, bado alikuwa akitamani kuwa na Patricia katika kipindi chote.
Watu ambao walikuwa wamesoma nao katika kipindi cha nyuma katika shule ya Sekondari ya Salma Kikwete wakaanza kufika nyumbani hapo. Hali ambayo walimkuta nayo Patricia, wasichana wakashindwa kujizuia, walikuwa wakilia kama watu waliofiwa.
“Patricia. Unanikumbuka?” Msichana mmoja alimuuliza Patricia.
“Nakukumbuka. Rosemary” Patricia alijibu huku kwa mbali akiachia tabasamu.
“Pole sana Patricia. Sikutarajia kukuona ukiwa katika hali hii. Hali yako imenigusa sana” Rosemary alimwambia Patricia.
“Usijali Rosemary. Naendelea vizuri. Kila kitu ni mipango ya Mungu” Patricia alimwambia Rosemary.
Martin alikuwa amesimama pembeni ya Patricia, muda wote mkono wake ulikuwa umekishika kiganja cha Patricia, hakutaka kumuachia, aliona kama Patricia angeondoka endapo tu asingekuwa amemshika.
Muziki ambao alikuwa akiufanya, hakuufanya tena japokuwa jina lake bado lilikuwa kubwa huku watu wengi wakitamani kumuona tena akiingia studio na kurekodi wimbo wowote na hata kupanda jukwaani kwa mara nyingine baada ya miaka miwili kupita bila kufanya hayo.
Ingawa muziki ulikuwa ni kipaji chake ambacho alikuwa amezaliwa nacho lakini kwa wakati huo hakutaka kabisa kujiingiza katika muziki. Kwanza alikuwa akitaka kupata muda zaidi wa kukaa na Patricia, msichana ambaye alikuwa akimpenda sana kwa kipind hicho.
“Lakini haya matatizo hadi lini? Binti yangu atapata nafuu lini?” Bi Beatrice alimuuliza Martin.
“Madaktari walisema kwamba huu ndio mwisho wa maendeleo yake. Inaniuma sana mama, inaniuma sana kumuona Patricia akiwa katika hali hii” Martin alimwambia Bi Beatrice.
Kila siku walikuwa ni watu wa kutiana moyo kutokana na hali ile ambayo alikuwa nayo Patricia. Miezi sita ikakatika lakini bado Patricia alikuwa katika hali ile ile kama alivyokuwa zamani. Martin aliumia kupita kawaida.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Kuna kitu nataka kukwambia Patricia. Ila naomba ukubaliane nami ili nifurahi” Marin alimwambia Patricia
“Kitu gani?”
“Ninakupenda sana”
“Hilo nafahamu. Hicho ndio kitu chenyewe ulichotaka kuniambia?” Patricia alimuuliza.
“Hapana. Kuna kitu kimoja cha muhimu sana” Martin alimwambia Patricia.
“Niambie Martin”
Martin akabaki kimya kwa muda, akaanza kumwangalia Patricia, machozi yakaanza kumtoka. Kulia ndio ilikuwa ni sehemu ya maisha yake katika kipindi hicho cha shida, mara kwa mara alikuwa akilia hasa katika kipindi ambacho alikuwa akimwangalia Patricia.
“Nataka........” Martin alisema na kukaa kimya.
“Unataka nini?” Patricia aliuliza.
“Nataka kukuoa. Nataka uwe mke wangu wa ndoa” Martin alimwambia Patricia huku akimshika mkono japokuwa alijua fika kwamba Patricia hakuhisi chochote kama alishikwa mkono kutokana na kupooza.
“Kunioa?” Patricia aliuliza kwa mshtuko.
“Ndio”
“Hapana Martin. Hapana Martin” Patricia alisema huku nae akianza kutokwa na machozi.
“Kwa nini?”
“Sijiwezi kitandani Martin. Siko kama siku ya kwanza tulipofanya mapenzi hotelini. Nipo hapa kama gogo tu. Itakuwaje unioe? Sitoweza hata kukuzalia watoto, na hata kama tukifanya mapenzi, sitohisi chochote Martin. Nimekuwa gogo katika jamii ya watu, sistahili kuolewa wala kuwa na mpenzi Martin” Patricia alimwambia Martin.
“Hata kama Patricia. Ninahitaji kukuoa. Ninahitaji kufanya kile kitu ambacho nilikuahidi kama tu ungekuwa mpenzi wangu” Martin alimwambia Patricia.
“Hapana Martin”
“Kwa nini Patricia? Nataka kukuoa tu, sitohitaji kufanya mapenzi na wewe na wala sitohitaji mtoto kwako. Ninachokihitaji ni kukuoa tu” Martin alimwambia Patricia.
“Mart....”
“Usinikatalie Patricia. Nimefanya mambo mengi kwako. Wewe ndiye ambaye umenifundisha kupenda katika maisha yangu. Ninakupenda Patricia, ninahitaji kuwa nawe, ninahitaji kukuoa na uwe mke wangu wa ndoa” Martin alisema huku machozi yakianza kumtoka.
Patricia hakuongea kitu chocchote kile, alibaki kimya huku akimwangalia Martin. Kwa jinsi Martin alivyokuwa akionekana, alionekana kuwa na uhitaji wa kuwa na Patricia. Hakutaka kusikia kitu chochote kile, kitu ambacho alikuwa akikitaka ni kuwa na Patricia tu.
“Nimekubali” Patricia alimwambia Martin ambaye alitamani kuruka ruka kwa furaha.
*******
Hali ya Bwana Jonathan haikuwa na unafuu hata kidogo, kila siku alikuwa akiendelea kuwa vile vile. Minyororo ilikuwa imeifunga mikono yake na miguu yake huku katika kipindi hiki hata mdomo wake ukiwa umewekewa gundi ya karatasi kwa ajili ya kumzuia kutokujing’ata.
Taarifa kwamba Bwana Jonathan alikuwa kichaa zilikuwa zikiendelea kuwashtka watu mbalimbali duniani, hawakujua ni kitu gani kilikuwa kimetokea mpaka kuwa katika hali hiyo, hawakujua kama mawazo ndio yalikuwa chanzo au kulikuwa na kitu kingine.
Viongozi mbalimbali wa nchi walikuwa wakikusanyika katika hospitali hiyo kwa ajili ya kumuona. Hawakuruhusiwa kuingia mpaka kule alipokuwa kwani kama wangefika huko basi ni lazima wangezua tatizo jingine zaidi.
Siku ziliendelea kukatika, Bi Leticia hakukubali kabisa mume wake apelekwe kanisani kufanyiwa maombezi. Kadri siku zilivyozidi kwenda mbele na ndivyo ambavyo hali yake ilivyozoso kuwa mbaya zaidi. Mwisho wa siku, Bi Leticia akakubali japo kishingo upande.
Siku ya Jumapili ikawadia, Bi Leticia pamoja na wafanyaazi wake wakaanza kuelekea katika hospitali hiyo ambako wakambeba Bwana Jonathan na kuanza kuondoka nae mahali hapo. Njiani ilikuwa ni matatizo, Bwana Jonathana alikuwa akipiga kelele huku wakati mwingine akivipiga vioo vya gari.
Wanaume watatu ambao walikuwa na nguvu za kutosha walikuwa wamemshika vilivyo Bwana Jonathan kama kumzuia asiweze kuleta madhara yoyote ndani ya gari lile.Safari nzima Bi Leticia alikuwa amekasirika, ndita zilikuwa zimekujamana usoni mwake, kitendo cha kusaliti amari na kukubali kumpeleka mume wake kwenda kanisani kilionekana kumuumiza na kujiona kama kuusaliti uamuzi wake ambao alijiwekea wa kutokukanyaga kanisani.
Kanisa la Pentekoste ambalo lilikuwa likiongozwa na mchungaji Henry White ndilo kanisa ambalo Bwana Jonathan alikuwa njiani akipelekwa. Kanisa hilo ndio lilikuwa kanisa kubwa jijini New York, watu wengi walikuwa wakipenda kwenda katika kanisani lile kwa kuwa miujiza mbalimbali ilikuwa ikifanyika kila Jumapili.
Viziwi walikuwa wakifanyiwa maombezi, wakaanza kusikia, bubu walikuwa wakifanyiwa maombezi na kuanza kuongea tena huku viwete nao wakifanyiwa na maombezi na kutembea tena. Idadi ya washirika elfu ishirini ambao walikuwa wakipatikana kanisani humo walionekana kuongezeka kadri siku zilivyozidi kwenda mbele.
Mchungaji White, kazi yake kubwa kanisani ilikuwa ni kuwafanyia watu maombezi, alimuamini Mungu wake ambaye alikuwa akimwamini katika maisha yake yote, alijua fika kwamba Mungu wake hakushindwa na kitu chochote kile.
Kufanya miujiza ndio ilikuwa sehemu ya maisha yake. Mungu alikuwa akimtumia kuponya watu wengi waliokuwa na matatizo mbalimbali na kuwafungua watu ambao walikuwa wamefungwa katika vifungo vya giza vilivyojaa mateso makali.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Wachawi walikuwa wakitupa vitu vyao na kuokoka, watu ambao walikuwa wakishuhudia miujiza mbalimbali walikuwa wakiyakabidhi maisha yao kwa Yesu jambo ambalo liliwafanya watu wengi waliokuwa wakichukia Ukristo kufanya kila mipango kutoka kulichoma kanisa lile moto kama makanisa ya Nigeria lakini ulinzi mkubwa ulionekana kuimarishwa katika kanisa hilo.
Saa 3.30 asubuhi, gari aina ya McLloyd 23 lilikuwa likipaki katika eneo la kanisa hilo. Ibada bado ilikuwa ikiendelea kama kawaida kanisani hapo. Kitendo cha kuingia ndani ya eneo la kanisa lile, Bwana Jonathan alikuwa akianza kupiga kelele, hali ya ukichaa ambayo alikuwa nayo ikaonekana kuzidi kuongezeka zaidi na zaidi.
“Let me out of here (Niacheni niondoke mahali hapa)” Mdomo wa Jonathan ulisema.
Watu ambao walikua nje ya kanisa lie wakaanza kulisogelea gari lile ambapo mlango ukafunguliwa na Bwana Jonathan kutolewa. Akashikwa pande zote na kuanza kuingizwa ndani ya kanisa lile.
Sauti ya Bwana Jonathan bado ilikuwa ikisikika, katika kipindi kile, si yeye ambaye alikuwa akipiga kelele bali zile roho ambazo zilikuwa ndani yake ndizo ambazo zilikuwa zikipiga kelele. Mchungaji White alipomuona, akaachia tabasamu pana huku akinywa maji yaliyokuwa pale madhabahuni.
“God told me about this man (Mungu aliniambia kuhusu mtu huyu)” Mchungaji White alisema huku akiachia tabasamu pana jingine.
Bwana Jonathan bado alikuwa akileta vurumai katika mikono ya watu ambao walikuwa wamemshika, alionekana kama kutaka kukimbia mahali hapo na kutoka nje. Ingawa Bi Leticia alikuwa hatamani kuingia kanisani lakini muda ule akaanza kujihisi mtu wa tofauti moyoni mwake.
Akaanza kuhisi hali ya amani moyoni mwake, hali ambayo hakuwahi kuipata kabla ya hapo. Moyo wake ukaonekana kujawa na furaha japokuwa hakujua furaha ile ilikuwa imetokea sehemu gani. Kipindi cha nyuma alijiona kuwa kama alikuwa amebeba mzigo mkubwa moyoni mwake, kwa kipindi kile akajiona kama ameutua mzigo ule.
Tabasamu pana likaanza kuonekana usoni mwake. Hakujua ni hali gani ambayo ilimpelekea kutabasamu, ila alijihisi kufanya hivyo moyoni kwa kuwa alikuwa akijisikia huru kupita kawaida.
Mchungaji White akaanza kumsogelea Bwana Jonathan ambaye bado alikuwa akiendelea kupiga kelele huku akiendelea kuleta vurumai kitendo ambacho kwa kiasi fulani kilitaka kuharibu ibada nzima. Alipomfikia Bwana Jonathan, akamuwekea mkono kichwani.
“Who are you? (Wewe ni nani?)” Mchungaji White alimuuliza.
“Jethro. I am Jethro. We are one thousand in here (.Jethro. Mimi ni Jethro. Tupo elfu moja hapa)” Sauti ambayo ilikuwa ni tofauti na sauti ya Bwana Jonathan ilisikika kinywani mwa mzee huyo.
“Ok! Do you know this place? (Unaifahamu sehemu hii?)” Mchungaji White aliuliza.
“The Church. This is the church (Kanisani. Hili ni kanisa){
“So you have to keep quite. In the name of Jesus Christ (Kwa hiyo unatakiwa kubaki kimya. Kwa jina la Yesu Kristo)” Mchungaji White alimwambia.
Hapo hapo mchungaji White akawaambia wale watu ambao walikuwa wamemshika Bwana Jonathan kumuachia. Kuanzia hapo hakukuwa na vurumai zozote zilizoendelea zaidi ya utulivu mkubwa uliowekwa na Bwana Jonathan. Mchungaji White akaendelea kuhubiri huku Bwana Jonathan akiendelea kubaki kimya huku akiwa amesimama kanisani pale.
Alipomaliza kuhubiri, maombezi yakafanya na kanisa zima na kisha kuanza kumfuata Bwana Jonathan ambaye alikuwa katikautulivu mkubwa. Alipomfikia, akaupeleka mkono wake kichwani kwa Bwana Jonathan.
“Let him free...in the name of Jesus Christ (Mwacheni huru....kwa jina la Yesu Kristo)” Mchungaji White aliamuru.
Bwana Jonathana akaanguka chini, akaanza kutupa miguu yake huku na kule, kelele zikaanza kusikika tena kutoka kinywani mwake huku zikilalamika kwamba kulikuwa na moto ambao ulikuwa ukiwaunguza mahali pale. Washirika wengine hawakubaki kimya, walikuwa wakizidi kuomba.
“Let Jesus finish His work (Mwacheni Yesu amalize kazi yake)” Mchungaji White aliliambia kanisa huku yeye akiifuata madhabau ambapo akamimina maji katika grasi yake na kunywa huku tabasamu pana likiwa usoni mwake.
Bwana Jonathan bado alikuwa akiendelea kupiga kelele mahali pale, baada ya dakika tano, akabaki kimya. Watu ambao walikuwa wamemleta mahali pale wakaambiwa wambebe na kumuweka kwenye kiti kwa ajili ya kupumzika hata kabla mambo mengine hayajaendelea.
Bi Leticia alibaki akilia, hakuamini kile ambacho alikuwa amekiona kwa macho yake. Kitu ambacho mganga mkubwa Moodinho alikuwa ameshindwa kukifanya, kanisani pale kiliweza kufanyika, mumewe alikuwa mzima kama siku za nyuma. Huku akionekana kuwa na furaha, akaanza kumfuata mchungaji White, machozi ya furaha yalikuwa yakimtoka.
“Thank you (Asante)
“Glory to God. I am not the one who healed him. Jesus is the one who healed him and let him free (Utukufu kwa Mungu. Mimi siye ambaye nimemponya. Yesu ndiye ambaye amemponya na kumuweka huru)” Mchungaji White alimwambia Bi Leticia ambaye alikuwa akilia na kuomboleza.
Watu hawakuamini kile ambacho walikuwa wamekisikia katika vyombo mbalimbali vya habari juu ya msanii Martin kuamua kufunga ndoa na msichana ambaye alikuwa amelala kitandani kwa muda wa miaka mitatu. Watu wakaanza kufuatilia kwa ukaribu zaidi kwa taarifa zile ambazo wala hazikuonekana kuaminika masikioni mwao.
Mpaka pale ambapo Martin alipohojiwa na kukubaliana na tetesi zile ndipo ambapo watu wakaamini kwamba taarifa zile zilikuwa na ukweli na wala hazikuwa tetesi zozote zile.
Watu wengi walikuwa wakimshangaa Martin ambaye alikuwa ameamua uamuzi mkubwa ambao kamwe usingeweza kufanya namtu yeyote yule kama asingekuwa na mapenzi ya dhati. Watu wakaanza kumuona Martin kama mtu ambaye alikuwa amekosea kufanya uamuzi huo kwa sababu tu kulikuwa na wanawake wengi wazuri na wazima ambao walikuwa wakitamani kuwa nae.
Kwa wasichana hao wengine wote, Martin alikuwa hajawaona, kwake, msichana ambaye alikuwa amepooza kitandani ndiye ambaye alikuwa ameonekana machoni mwake.
Taarifa zile zikaanza kusambawa kwa kasi, watu wengi wakawataarifu marafiki zao katika mitandao ya kijamii kama facebook, Twitter na mitandao mingine. Kila mtu ambaye aliisikia taarifa ile alionekana kushangaa na kushtuka.
“Mapac huyu huyu ndiye anataka kumuoa Patricia?” Jamaa mmoja aliwauliza wenzake huku akionekana kushangaa.
“Ndio”
“Yaani pamoja na kumsaliti kote kule kwa kutaka kuolewa na mcheza kikapu?”
“Kwani alisalitiwa! Hapana. Wakati msichana yule alipokuwa akiondoka nchini Tanzania hakuwa na uhusiano wa kimapenzi na Mapac, walikuwa ni marafiki tu” Jamaa mwingine alijibu.
“Lakini si walifanya”
“Kufanya sio ishu. Unajua msichana yule alikuwa amelelewa kiulaya ulaya tu, kwa hiyo kufanya ni jambo la kawaida kwake”
“Acha kunitania wewe”
“Kweli. Unamjua Angelina Jolie?”
“Amefanya nini sasa?”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Mbona yeye alikuwa akifanya mapenzi na marafiki zake wa kawaida kila alipojisikia kufanya mapenzi. Sisi Waafrika ndio tunachukulia jambo hili kubwa, ila huko mbele au kwa watoto waliokulia maisha ya kiulaya ulaya, mbona kawaida tuuu”
Kila mtu mitaani alikuwa akiongea lake, uamuzi ambao alikuwa ameufanya Martin ulionekana kuwashangaza kupita kawaida. Hakukuwa na kitu walichokisubiria zaidi ya kuisubiria siku ile ambayo ilipangwa, baada ya wiki mbili ifike ili kuishuhudia harusi hiyo ambayo ilitarajika kufanyika katika kanisa la Praise And Worship huku watu wengi wakijiahidi kuihudhuria kanisani hapo.
“Siku tano zimebaki kabla ya harusi”
***********
Siku ambayo ilikuwa ikisubiriwa na watu wengi ikafika. Watu wakaanza kujisogeza katika kanisa la Praise And Worship lililokuwa Mwenge kwa ajili ya kushuhudia harusi ya msanii wa muziki ambaye alikuwa ameachana na muziki kwa kipindi kirefu, Martin ambaye alikuwa akijulikana kwa jina la kisanii la Mapac ambaye alikuwa akifunga ndoa siku hiyo na msichana Patricia, msichana ambaye alikuwa hajiwezi kitandani kwa muda wa miaka mitatu mpaka kipindi hicho.
Wasanii wengi wa muziki, viongozi mbalimbali wa siasa pamoja na viongozi wengine wa dini walikuwa wamekusanyika kanisani hapo kwa ajili ya kuiona harusi hiyo ambayo ilionekana kushika hisia za watu nchini Tanzania.
Kanisa lilikuwa limejaza watu wengi kiasi ambacho mpaka wengine wakatakiwa kubaki nje kutokana na watu zaidi ya elfu mbili kuwa ndani ya kanisa hilo kubwa. Kwaya mbalimbali zikaanza kuimba kama kuvutia muda ili maharusi hao waweze kuingia kanisani hapo ifikapo saa tano kamili asubuhi siku hiyo ya Jumamosi.
Kila wakati watu walikuwa wakiangalia saa zao, waliuona muda ukienda sana lakini wala maharudi hawakuweza kufika kanisani hapo. Dakika zilikatika zaidi na zaidi, magari ya maharusi yakaanza kuingia ndani ya eneo la kanisa lile.
Waandishi wa habari wakaanza kupiga picha. Picha zilipigwa kwa mfululizo na kwa haraka sana. Kila mwandishi wa habari kwa wakati huo alikuwa akifikiria kuhusiana na magazeti ambayo wangeyatoa siku inayofuata na siku nyingine pia.
Kikundi cha matarumbeta bado kilikuwa kikiendelea kupiga matarumbeta mahali hapo mpaka pale bwana harusi, Martin alipoteremka kutoka garini. Suti nzuri nyenye rangi nyeusi, shati jeupe na tai nyekundu vilionekana kumpendezesha kupita kawaida. Akaanza kupiga hatua kadhaa, alipofika mlangoni akasimama kumsubiria bibi harusi.
Kitanda alichokuwa amelazwa Patricia kikaanza kusukumwa na wapambe wa bibi harusi mpaka pale ambapo alisimama Martin. Uso wa Martin ukajawa na tabasamu pana kila alipokuwa akimwangalia patricia aliyekuwa pale kitandani.
Shela kubwa ambalo lilionekana kuwa la thamani lilikuwa limempendezesha Patricia. Uzuri wake siku hiyo ulionekana kuvutia zaidi huku vijipambo vingi vikiwa vinaung’arisha uso wake.
Bibi Beatrice pamoja na mpenzi wake, Bwana Thomson walikuwa miongoni mwa watu ambao walitembea karibu na kitanda alicholazwa Patricia. Kitanda kikaanza kusukumwa kuelekea mbele ya kanisa, watu walikuwa wakipiga vigelegele huku kwaya nazo zikiendelea kuimba.
Machozi yakaanza kumtoka Martin. Ni kweli alitamani sana kumuoa Patricia, katika maisha yake hiyo ndio ilikuwa ndoto yake ya kila siku. Siku hiyo ndio ilikuwa siku ile ambayo alikuwa akiisubiria katika kipindi chake chota. Alikuwa akimuoa Patricia lakini tatizo lilikuwa ni kwa jinsi Patricia alivyokuwa.
Kwa wakati huo wala hakuonekana kujali, kitu ambacho alikuwa akikijali kwa wakati huo ni kumuoa patrici a tu na kisha kumuita mke wake. Huku wakiwa wanasogea mbele ya kanisa kwa mwendo wa taratibu, mawazo ya Martin yakaanza kujirudisha nyuma kama mkanda wa filamu.
Akaanza kukumbuka kipindi kile ambacho walikuwa shuleni. Katika kipindi ambacho alikuwa akifanya kila jitihada za kuongea na patricia, msichana ambaye alikuwa mrembo kuliko wasichana wote shuleni pale. Alikumbuka mpaka katika siku ya kwanza ambayo aliongea na Patricia huku akionekana kusahau maneno mengi ambayo alipanga kumwambia mara tu atakapoongea nae.
Mawazo yake hayakuishia hapo, alikumbuka vilivyo alivyokuwa akisaidiwa mambo mbalimbali na Patricia, alipokuwa akisaidiwa nguo, fedha na vitu vingine vingi. Kwa wakati huo alikumbuka kila kitu, alikumbuka mpaka pale alipomtamkia neno ‘Nakupenda’ kwa mara ya kwanza, mpaka pale ambapo Patricia alipokataa kuwa mpenzi wake.
Akaendelea kukumbuka zaidi, akakumbuka mpaka siku ambayo alifanya nae mapenzi hotelini na kuutoa usichana wake. Alikumbuka mpaka siku ambayo Patricia alikuwa akisafiri kuelekea nchini Marekani huku akiwa amemuachia barua ambayo ilimuumiza kupita kiasi. Alikikumbuka kiasi cha fedha cha shilingi milioni kumi na tano ambacho aliachiwa na msichana huyo kwa ajili ya kuanza maisha yake.
Kwa wakati huo bado alikuwa akiendelea kukumbuka mambo mengi. Alikumbuka mpaka miezi ambayo msichana yule, patricia alipokuwa akimtumia kiasi kikubwa cha fedha katika akaunti yake. Katika kila kitu ambacho alikuwa akikikumbuka kwa wakati huo, alijiona kuwa na kila sababu ya kumuoa Patricia.
Walipofika mbele ya kanisa, mchungaji akaanza kuhubiri maneno machache kuhusiana na ndoa na kisha pete kuletwa mikononi mwake. Mchungaji Mshana akazichukua pete zile na kisha kumtaka Martin achukue kipaza sauti.
“Martin Mruma. Umekubali kumuoa Patricia Thomson awe mke wako katika shida naraha, hzuni na fura, maumivu na faraja, ugonjwa na afya?” Mchungaji Mshana alimuulliza Martin.
“Ndio nimekubali” Martin alijibu huku akiachia tabasamu pana.
Mchungaji Msahana akarudia swali lile mara tatu, bado jibu la Martin lilikuwa lile lile, ‘Mdio nimekubali’. Mchungaji akataka kipaza sauti kiwekwe karibu na mdomo wa patricia na kisha kumuuliza maswali yale yale.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Ndio nimekubali” Patricia alijibu kila alipoulizwa.
Kanisa zima likaanza kupiga makofi ya shangwe. Martin akakabidhiwa pete na kisha kumvarisha patricia na kumbusu. Kwa niaba ya Patricia, mama yake, Bi Beatrice akapewa pete na kumvarisha martin, kanisa zima likaanza kupiga makofi.
Kutokana na furaha kubwa ambayo alikuwa nayo, Martin akashindwa kujizuia, machozi yakaanza kumtoka, akamsogelea Patricia na kumbusu shavuni. Siku hiyo ikaonekana kuwa siku ya furaha kuliko siku zote katika maisha yake, kitendo cha kufunga ndoa na Patricia kilimpa furaha moyoni.
“Nakupenda mke wangu” Martin alimwambia patrica.
“Nakupenda pia” Patricia alijibu na kisha kumbusu tena.
Harusi hiyo haikuwa na sherehe yoyote ile, harusi ilipookwisha, maharusi wakaelekea nyumbani kupumzika. Martin hakutaka kutoka karibu na Patricia, muda wote alikuwa karibu yake akimfariji.
Miezi iliendelea kukatika, hali ya Patricia wala haikubadilika, bado alikuwa vile vile. Martin hakutaka kumuacha Patricia, kila siku alikuwa pamoja nae akimfariji katika ile hali ambayo alikuwa akipitia kwa wakati huo. Yeye ndiye ambaye alikuwa akimfariji kama mumewe.
Martin wala hakufikiria kuhusu utajiri mkubwa ambao alikuwa akiumiliki Patricia, kitu ambacho alikuwa akikifikiria kwa kiipindi hicho ni mapenzi mazito ambayo alikuwa nayo kwa Patricia tu.
“Nitakufa mume wangu” Patricia alimwambia Martin.
“Hautokufa mpenzi mpenzi. Usiongee maneno hayo, unaniumiza” Martin alimwambia Patricia.
“Nitakufa tu Martin. Ila sijui kwa nini nimekuwa na safari hii ndefu kuelekea kaburini. Imekuwa ni safari ngumu na nzito kuipitia, imekuwa ni safari iliyokuwa na maumivu makali sana” Patricia alimwambia Martin ambaye akaanza kulia kwa sauti hali ambayo iliwafanya Bi Beatrice na Bwana Thomson kuja chumbani mule.
“Kuna nini tena?”
“Patricia mama”
“Amefanya nini?”
“Anaonekana kukata tamaa, yaani anaonekana kutotaka kuamini kwamba amepona. Ananiambia maneno yanayoonekana kunitisha, maneno yanayoonekana kunikatisha tamaa moyoni” Martin alimwambia Bi Beatrice ambaye akaanza kumsogelea Patricia pale kitandani.
“Utapona binti yangu. Naomba usimtishe mume wako” Bi beatrice alimwambia Patricia.
“Sikumtisha mama. Nilikuwa nikimwambia ukweli”
“Sasa huo ukweli wako ndio uliokuwa ukimtisha na kumkatisha tamaa.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Je nini kitaendelea?
Je Patricia atapona na mwili kutengemaa?
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment