Search This Blog

Sunday, July 10, 2022

SAFARI NDEFU KUELEKEA KABURINI - 3

 





    Simulizi : Safari Ndefu Kuelekea Kaburini

    Sehemu Ya Tatu (3)



    Si kila mtu ambaye alikuwa akiufurahia uhusiano kati ya Patricia na Banana. Watu wazima, matajiri ambao walikuwa na fedha zao walionekana kuukasirikia uhusiano huo. Kila tajiri alikuwa akimtaka Patricia, urembo wake ulionekana kustahili kuwa na mwanaume ambaye alikuwa tajiri kama jinsi walivyokuwa wao.

    Kila siku walikuwa wakifanya mishemishe za kumtongoza Patricia lakini msichana huyo alikuwa akionyesha uaminifu mkubwa kwa mchumba wake, Banana. Matajiri wale walijaribu kila siku mpaka kukata tamaa na kuamua kuachana nae.

    Kila mmoja alikuwa akifanya mambo yake huku akiuacha uhusiano ule kuendelea kama kawaida huku wao wakitafuta wasichana wengine warembo wa kutembea nao lakini tajiri Jonathan hakutaka kukubaliana na hilo.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Moyoni mwa Bwana Jonathan bado alikuwa akimpenda sana Patricia na bado alikuwa akimhitaji sana katia maisha yake jambo ambalo lilimfanya kuukasirikia uhusiano ule kuliko mtu yeyote duniani. Moyoni mwake alikuwa akitamani kukaa na msichana huyo ambaye katika kipindi hicho alionekana kuwa msiachana mrembo kuliko wasichana wote ambao walikuwa maarufu duniani.

    Alichokifanya mara baada ya kuona kwamba amekataliwa, akaamua kupanga mipango ya kuwamaliza wapenzi hao kwa kuandaa mpango kabambe. Alichokifanya ni kuwasiliana na watu wake ambao walikuwa wakiishi jijini New York kwa ajili ya kuwaua wapenzi hapo kwa kuwapiga risasi. Mipango ikapangwa na kukamilika, Patricia na Banana wakatakiwa kuuawa ndani ya ukumbi wa Stapple Centre katika siku za ugawaji wa tuzo za BET.

    Vijana wakajipanga vilivyo, walichokifanya siku hiyo ni kufika katika ukumbi huo mapema sana na kuandaa bunduki zao zilizokuwa na lensi vizuri kabisa huku vyombo vya kuzuia milio ya risasi vikiwa mbele ya bunduki hizo. Walichokuwa wakikitaka ni kuwapiga risasi wapenzi hao kwa pamoja na kuwaua kwa pamoja.

    Wakafika katika chuma kimoja ambacho kilikuwa na mavazi mengi, wakachukua mavazi ya wapishi na kisha kujifanya kama wapishi ambao walikuwa wakishughulikia chakula ndani ya ukumbi huo. Walijiona kutakiwa kufanya vitu kwa umakini mkubwa sana bila kugundulika na mtu yeyote ambaye angekua ndani ya ukumbi huo.

    Walipoona kila kitu chao kipo tayari, wakaanza kwenda nyuma ya televisheni kubwa iliyokuwa mahali hapo na kutulia na bunduki zao. Muda ulizidi kwenda zaidi na zaidi mpaka kufika kipindi ambacho watu wakaanza kuingia ndani ya ukumbi huo.

    Wasanii na masupastaa wengi walikuwa wakipita katika zuria moja jekundu na kupiga picha mbalimbali ambazo zilitakiwa kuwekwa kwenye majarida na magazeti ambayo yangetoka siku ifuatayo. Baada ya dakika kadhaa, gari zuri na la kifahari likasimama nje ya ukumbi ule, Patricia na Banana wakaanza kuteremka, wapiga picha mbalimbali wakaanza kuwasogelea na kuwapiga picha.

    Nyuso zao zilikuwa zinaonyesha tabasamu pana, walikuwa wakipunga mikono hewani huku kelele za watu ambao walikuwa wakishangilia zikisikika mahali hapo. Wakaelekea katika zuria lile jekundu na kusimama na kisha picha kuanza kupigwa. Muda wote walikuwa wakionekana kuwa na furaha, hawakufahamu kitu chochote kwamba kwa wakati huo walitakiwa kubakiza dakika chache za kuishi duniani.

    Walipoona zoezi la kupiga picha likiwa limekamilika, moja kwa moja wakaanza kuelekea ndani ya ukumbi ule na kukaa katika viti vya mbele kabisa. Huku ugawaji wa tuzo ukiendelea ukumbini pale. Tuzo ziligawiwa kwa washindi mbalimbali hasa wanamuziki.

    “On my target....(Kwenye usawa wangu)” Mpiga risasi mmoja alisema kwenye chombo chake cha mawasiliano ambacho kilikuwa sikioni. Bunduki yake tayari ilikuwa imemuelekezea Patricia tayari kwa kuachia risasi nne mfululizo kifuani.

    “On my target too...(Kwenye usawa wangu pia)” Mwanaume mwingine alisema na hapo hapo wote kujiandaa kupiga risasi. Bunduki yake pia ilikuwa imemuelekezea Banana kifuani tayari kwa kuachia risasi nne kifuani mwake.

    “Three....twooo....oneee....” Walihesabu kwa pamoja.

    *******

    Umaarufu wa Martin ulikuwa mkubwa kupita kawaida, kila siku alikuwa akiingiza kiasi kikubwa cha fedha, alinunua magari ya kifahari huku asilimia kumi ya kila fedha ambazo alikuwa akiziingiza akizitumia katika kuwasaidia watoto yatima waliokuwa katika vituo mbalimbali. Martin akachaguliwa kuwa balozi wa Maralia na Vyakula, akaanza kuzunguka katika mikoa mbalimbali kwa kutumia ndege.

    Muda wote alipokuwa akisafiri kwa kutumia ndege, alikuwa akilia. Maisha yake ya nyuma ambayo alikuwa ameishi yalionekana kumsumbua sana katika kichwa chake. Mpaka katika kipindi hicho bado alikuwa akiuchukia sana umasikini. Moyoni alikuwa na hamu ya kuwasaidia watu masikini kwani hali ile alikuwa akiijua vilivyo.

    Hakupenda kumuona mtu akiwa katika hali ya umasikini kabisa na hiyo ndio ilikuwa sababu kubwa ya kuwasaidia watoto yatima na watu mbalimbali ambao walikuwa katika uhitaji mkubwa. Mara kwa mara alikuwa akisafiri mikoani kwa ajili ya kuwasaidia watu mbalimbali, alipiga picha na wanavijiji wengi ambao walikuwa wakitegemea maisha yao katika kazi ya ukulima waliyokuwa wakiifanya.

    Maisha ya wanavijiji yalionekana kumuumiza hali ambayo ilimfanya kuwasaidia kwa kuwapa kiasi kikubwa cha fedha katika kila kijiji ambacho alikuwa akitembelea. Msaada wake ukaonekana kuwa mkubwa, magazeti na vyombo vingine vya habari vikazidi kumtangaza sana kiasi ambacho kikamfanya kuitwa bungeni na kushiriki katika kikao kimoja kama mgeni rasmi.

    Hiyo ilikuwa ni heshima kubwa kwake, kwenda bungeni kama mgeni rasmi ilionekana kuwa kama bahati kwake. Bungeni, alikuwa akijisikia ufahari, kuwaona wabunge ambao walikuwa wakichagia mada mbalimbali hasa katika kipindi hicho cha kupanga bajeti ya mwaka ilionekana kumfurahisha moyoni.

    Muda ambao alitakiwa kuongea ukafika, akakaribishwa na kusimama katika sehemu aliyokuwepo na kisha kuweka vizuri kipaza sauti chake. Bunge zima lilikuwa kimya, akaanza kuwaangalia wabunge kwa zamu. Hakuamini kuona kwamba watu waliokuwa na digrii, Elimu kubwa walikuwa wakimsikiliza yeye, mtu ambaye alifeli sana kidato cha nne.

    Macho yake yakaanza kujaa machozi na baaada ya sekunde chache, machozi yakaanza kumtoka. Moyoni alikuwa na mambo mengi ya kuongea, yale ambayo alikuwa akitaka kuyaongea yakaanza kujipanga moyoni mwake.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Namshukuru Mungu kwa kunifikisha mahali hapa siku ya leo na kusimama mbele yenu” Martin alisema na kisha kuendelea. Kila neno ambalo alikuwa akiliongea mahali hapo lilionekana kuwa la msingi sana.

    Aliiongelea hali ambayo walikuwa wakiishi wakulima wengi vijijini, hali ya kimasikini ambayo haikutakiwa kuishi na watu kama wao kutokana na umuhimu mkubwa ambao walikuwa nao hapa nchini. Akaanza kuizungumzia Elimu ya Tanzania na matatizo kadhaa ambayo alikutana nayo kule vijijini, watoto kukosa madarasa, vitabu kutokuwepo madarasani.

    Siku ilionekana kuwa siku ya kukumbuka maishani mwake. Alipomaliza akakaa chini huku wabunge wakimpigia makofi. Hayo ndio yalikuwa maisha yake, mara kwa mara alikuwa akisafiri huku na huko kuwatembelea watu wengi waliokuwa na matatizo mbalimbali. Akaanza kufika katika mahospitali mengi, akaanza kutoa misaada ya fedha za kununulia madawa katika kila hospitali ya kijiji aliyofika.

    Miezi ikakatika na hapo ndipo macho yake yakatua katika magazeti mbalimbali ambayo yakaanza kumtangaza msichana Patricia kuwa kama msichana kutoka nchini Tanzania ambaye alikuwa akivuma kwa uzuri nchini Marekani. Martin hakuonekana kuziamini taarifa zile kiasi ambacho kikamfanya kuyanunua magazeti yale na kisha kwenda nayo nyumbani.

    Akakaa kwenye kochi na kuanza kuyaangalia magazeti yale, picha za Patricia zilikuwa zikionekana vizuri machoni mwake, uzuri ambao alikuwa nao ukaonekana kuongezeka zaidi na zaidi machoni mwake, hakuamini kama Patricia angeweza kuwakimbiza hadi Wamarekani kwa uzuri ule ambao alikuwa nao.

    Hapo ndipo ambapo Martin akaanza kumfuatilia tena Patricia. Kila siku alikuwa akiingia kwenye mtandao wa Patricia na kisha kusoma habari zake. Jina lake lilikuwa likiandikwa sana na kila habari ambayo alikuwa akiiandika Patricia kwenye mtandao ule huku watu wengi wakihoji na kujibiwa kwamba alikuwa rafiki wa karibu.

    Kitendo cha kutajwa tajwa sana na Patricia kwenye mtandao wake ndio ukawafanya Watanzania kutaka kufahamu zaidi kama yule ndiye alikuwa Patricia ambaye alikuwa akimzungumzia au alikuwa mwingine. Kama kawaida akaitwa katika kituo cha televisheni cha Flavour na kisha kuhojiwa. Martin au Mapac Jnr hakutaka kuficha, akawaelezea Watanzania kwamba yule ndiye alikuwa Patricia ambaye aliyabadilisha maisha yake.

    “Mmmh! Sasa kwa nini asimuoe?” Kila mtanzania alikuwa akihoji.

    Watanzania wakaonekana kupata kazi, wakaanza kufuatilia taarifa mbalimbali za Patricia. Kila Patricia alipokuwa akiandikwa kwenye magazeti mbalimbali nchini Marekani, Watanzania walikuwa wakiitoa taarifa ile kwenye magazeti yao.

    Muda wa majonzi ukamfikia Martin hasa katika kipindi ambacho Patricia alipoamua kuingia kwenye uhusiano na Banana. Hizo zilikuwa habari ambazo ziliushtua moyo wa Martin kupita kawaida, akanyong’onyea kupita kawaida. Maisha yake akayaona kuingia doa, ingawa alionywa kipindi cha nyuma kwamba asiingie kwenye mahusiano na Patricia lakini kipindi hicho ndipo alipogundua maumivu halisi ambayo Patricia alikuwa akizungumza masikioni mwake kila siku.

    Martin akaonekana kuwa mpole, mwili wake ukaanza kunyong’onyea, Watanzania wakaonekana kuanza kumchukia Patricia kwa kumuona kwamba alikuwa msaliti katika maisha ya Martin. Martin akaanza kutunga nyimbo mbalimbali ambazo zilikuwa zimejaa huzuni huku akiyaelezea mapenzi kwamba yalikuwa yakimtesa kupita kawaida.

    Nyimbo zake zilikuwa nzuri na zilimvutia kila aliyekuwa akizisikiliza, kwa jinsi ambavyo alikuwa ameimba kwa hisia kali na kwa jinsi Watanzania walivyokuwa wakizisikiliza nyimbo zile, walikuwa wakihuzunika zaidi na kumuonea huruma huku wengine wakianza kutokwa na machozi. Patricia akaonekana kuyabadilisha maisha yake, akajiona kuanza kupata mateso makali moyoni mwake.

    “PATRICIA NA BANANA KUFUNGA NDOA” Yalikuwa maneno ambayo yalisomeka vizuri machoni mwa Martin katika gazeti moja la udaku. Martin akaonekana kushtuka kupita kawaida, habari ile ilimtetemesha sana. Akalinunua lile gazeti na kisha kuelekea nalo nyumbani.

    Kitu cha kwanza alichokifanya ni kumuonyeshea mama yake. Bi Evadia akaanza kuiangalia habari ile. Moyo wa Bi Evadia ukaumia kupita kawaida, hakuamini kama Patricia alikuwa akijiandaa kuolewa na mvulana kutoka nchini Marekani badala ya mtoto wake, Martin.

    “Kwa nini ameamua kufanya hivi?” Bi Evadia aliuliza huku akionekana kuumia.

    “Si kosa lake. Alinionya kabla ila sikutaka kuelewa. Mimi ni rafiki yake tu, huu ni uamuzi mzuri ambao ameupanga japokuwa umetokea kuniumiza kupita kawaida” Martin alimwambia mama yake.

    *********

    Ghafla umeme ukakatika ukumbini, giza likawa kubwa. Kelele zikaanza kusikika ndani ya ukumbi huo kwani kwa miaka themanini tangu kumbi huo ujengwe hakukuwa na siku yoyote ambayo umeme ulikatika ukumbini hata kwa bahati mbaya. Wapigaji risasi kule juu wakashindwa kuelewa kit gani kilikuwa kimetokea. Wakabaki wakiangaliana japokuwa hawakuwa wakionana vizuri.

    Watu wakamulika simu zao, kidogo mwanga ulikuwa ukipatikana wa kuweza kuonana hapa na pale. Walahazikupita sekunde nyingi, ni ndani ya sekunde arobaini na tano umeme ukarudi. Wapigaji wale wakaangalia vizuri katika viti vile, Patricia na Banana hawakuwepo mahali pale jambo ambalo lilionekana kuwashangaza. Waliona kwamba ni lazima kulikuwa na mtu ambaye alikuwa amewashtua juu ya ule mchezo ambao walikuwa wakitaka kuucheza mahali pale.

    Patricia na Banana walikuwa nje ya ukumbi ule, nyuso zao zilikuwa zikionyesha wasiwasi mkubwa. Hawakuonekana kumuamini mtu yeyote, tayari wakajiona kujikomboa kutoka katika mdomo wa kifo. Kila mtu nje ya ukumbi alikuwa akiwashangaa, hawakuelewa ni kitu gani ambacho kiliwafanya watu wale kuonekana kuwa na wasiwasi kwani kwa pale nje wala taa hazikuwa zimezima kama ilivyokuwa ndani. Zilikuwa zikiendelea kuwaka tu.

    Wakalifuata gari lao na kisha kuingia ndani. Patricia akaitoa simu yake na kisha kuanza kuusoma ujumbe ule mfupi ambao alikuwa ametumiwa katika kipindi ambacho alikuwa njiani kuelekea katika ukumbi ule pamoja na mpenzi wake, Banana. Usoni akaonekana kuchoka kupita kawaida, kila alipokuwa akiiangalia namba ya simu ile ambayo ilikuwa imemtumia meseji hakuweza kuitambua, namba

    Wakabaki wakiangaliana tu garini, meseji ile ilivyokuwa imeandikwa na ndicho ambacho kilikuwa kimetokea ukumbini mule. Taa zote zilitakiwa kuzimwa na wao kuondoka ukumbini mule haraka iwezekanavyo kwani kama wasingefanya hivyo basi risasi zingeweza kuingia miilini mwao.

    Kitu ambacho walikigundua kwa wakati huo ni kwamba mtumaji wa meseji ile alikuwa akifahamu kila kitu ambacho kilikuwa kimepangwa juu ya maisha yao. Maswali mengi yakaanza kumiminika vichwani mwao sababu ambayo iliwapelekea watu kutaka kuwamaliza lakini hawakupata jibu lolote lile. Tayari wakajiona kuwa katika hali ya hatari, walijiona kuwa na uhitaji wa kujiwekea ulinzi kila watakapokuwa.

    Safari bado ilikuwa ikiendelea kama kawaida. Vichwani mwao walikuwa na mambo mengi ambayo walikuwa wakiyafikiria kwa wakati huo. Hawakuongea kitu chochote kile, muda wote walikuwa wakionekana kufikiria jambo.

    **********CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kila kitu ambacho kilikuwa kimepangwa kilipangwa na Bwana Jonathan ambaye alikuwa akihitaji watu hao wafe haraka iwezekanavyo. Kila siku kichwa chake kilikuwa kikiuma mpaka pale ambapo alitaka kuwamaliza katika ukumbi ule wakati ambao watakuwa wakitaka kuangalia ugawaji wa tuzo za BET.

    Aliwaandaa vijana wake tayari kwa kutelekeza kile ambacho alikuwa akitaka kifanyike kwa wakati ule. Alitaka watu wale wapigwe risasi na wafe papo hapo. Mpango wake aliuona kufaa sana ila baada ya dakika kadhaa akaona kwamba mpango ule haukuwa na manufaa yoyote yale.

    Kichwani alikuwa akifikiria vitu vingi, kitu cha kwanza alikuwa akiwafikiria wale vijana wake kama wangekamilisha kile alichotaka kifanyike harafu wakamatwe, je wangekuwa na moyo wa kutokumtaja? Kila alipofikiria hilo, wasiwasi ulikuwa ukimshika moyoni mwake.

    Hapo ndipo alipoamua kupanga mpango mwingine. Alichokifanya ni kuwasiliana na vijana wake wengine na kisha kuwaeleza mpango kabambe ambao alikuwa ameufikiria mahali hapo. Alichokuwa akikitaka kwa wakati huo ni kuwaua kwa ajali ya gari, mauaji ambayo yangeonekana kuwa yalitokea kwa bahati mbaya.

    Alichokifanya ni kumpigia simu kijana wake mwingine na kisha kumpa namba ya Patricia ambapo alitakiwa kutumia meseji. Hilo halikuonekana kuwa tatizo, muda ambao meseji ile ilitakiwa itumwe ikatumwa huku njiani akiwa ametegesha gari kubwa tayari kwa kusababisha ajali ambayo ingetokea katika barabara ya St’ Patrick.

    Kila kilichokuwa kimepagwa kilikwenda kama alivyotaka kiwe, ukumbini taa zikazimwa na Patricia pamoja na Banana kutoka nje ya ukumbi na kuchukua gari lao huku wakielekea nyumbani kwao.

    **********

    Ulikuwa ni mlio mkubwa ambao uliskika katika maungano ya barabara ya St’ Patick na Kingstone. Gari dogo aina ya Aston Martin lilikuwa limerushwa mbali huku likiwa limebimbilika zaidi ya mara saba ardhini. Gari lile lilikuwa limebondeka vibaya, sehemu yote ya mbele ilikuwa haionekani kwa jinsi lilivyokuwa limebondeka.

    Damu zilikuwa zinaonekana kutapakaa katika bati la gari lile, hakukuwa na vioo ambavyo vilikuwa vimesalia, vyote vilikuwa vimepasuka. Matairi ya gari lile yalikuwa yamepasuka yote. Kila mtu ambaye alikuwa ameishuhudia ajali ile alionekana kupigwa na mshangao.

    Watu wakaanza kueleke kule ambako gari lile lilipokuwa limebimbilishwa na kuanza kuliangalia, hakukuwa an mtu ambye alidiriki kulisogelea, ajali ile ilionekana kuwa mbaya kuliko ajali zote ambazo ziliwahi kutokea mwaka huo. Wanawake ambao walikuwa wameiona ajali ile walikuwa wakilia kwa woga, walionekana kuogopa kupita kawaida.

    Gari lile kubwa ambalo lilikuwa limeigonga gari ile bado lilikuwa mahali pale pale lakini dereva wake wala hakuonekana, alikuwa amekwishakimbia. Ndani ya dakika nne, gari la mapolisi likafika mahali pale na kisha kuweka kamba za rangi ya njano na kutotaka mtu yeyote kutokusogea sehemu ile. Wala hazikupita dakika nyingi baada ya hapo, gari la wagonjwa likafika mahali hapo.

    Kazi kubwa ikawa ni kuwatoa watu ambao walikuwa ndani ya gari lile. Hakukuwa na dalili zozote kama watu ambao walikuwa ndani ya gari lile walikuwa wamesalimika kutokana na jinsi gari lilivyokuwa.. Mabati yakatanuliwa, picha ya miili ambayo ilikuwa ikionekana machoni mwa mapolisi ilikuwa imewashangaza kupita kawaida, ilikuwa imeharibika vibaya na wala haikuwa rahisi kugundua wale walikuwa wakina nani kwa jinsi damu zilivyokuwa zimetapakaa nyusoni mwao.



    Gari la wagonjwa lilikuwa likiendeshwa kwa mwendo wa kasi kuelekea katika hospitali ya Metopolian iliyokuwa hapo jijini New York. King’ora kilikuwa kikisikika kikilia kitu ambacho kiliyafanya magari mengine kupaki pembeni kulipisha gari hilo la wagonjwa.

    Ni ndani ya dakika mbili gari likafika katika eneo la hospitali hiyo na machela kuletwa na kisha miili ile kuakizwa na machela kuanza kuendeshwa ndani. Kila nesi ambaye alikuwa akiiangalia miili ile, alibaki akishangaa, miili ilionekana kutisha kupita kawaida.

    Safari ile iliishia katika chumba cha wagonjwa mahututi na kisha kuanza kuisafisha. Hakukuwa na mtu ambaye aliyaamini macho yake mara baada ya kugundua kwamba watu wale walikuwa ni Patricia na Banana. Taarifa zikatolewa kwa mapolisi juu ya watu wale ambao walikuwa wamepata ajali na mapolisi kuvielezea vyombo vya habari.

    Kwa haraka haraka taarifa zikaanza kutolewa. Ilikuwa ni taarifa ambayo ilijaa mshtuko sana kwa kila mtu ambaye alikuwa amezisikia habari zile. Kila mtu akataka kufahamu mengi kuhusiana na ajali ile ambayo ilionekana kuwa kama mchezo fulani wa maigizo. Watu wakaanza kujisogeza katika hospitali ile, watu ambao walikuwa wamepata ajali walionekana kuwa watu muhimu kwao.

    Kila mtu ambaye alikuwa akifika katika hospitali ile alionekana kuhuzunika huku hata wengine wakilia kupita kawaida. Tukio la ajali ile lilionekana kuwagusa kupita kawaida, hawakuamini kama wale watu ambao walitakiwa kuoana siku chache zijazo walikuwa wamepata ajali na sasa hivi walikuwa mahututi hospitalini.

    Mzee Thomson akaonekana kuchanganyikiwa, hakuamini kile ambacho alikuwa ameambiwa. Aliuhisi mwili wake ukipigwana ganzi, miguu ikilegea na kukaa kochini huku akiitupa simu yake chini. Alibaki pale kochini katika hali ya mshangao kwa muda wa dakika kadhaa na kisha kuinuka na kuanza kuelekea nje ya nyumba yake.

    Alichokifanya ni kuingia garini na kisha kuondoka kuelekea hospitalini. Kwa jinsi ambavyo alikuwa amechanganyikiwa, alionekana kusahau kama alitakiwa kuendeshwa na dereva wake ambaye alikuwa akiishi nae ndani ya nyumba yake. Alikuwa akiendesha kwa mwendo wa kasi kuelekea hospitalini.

    Alichukua dakika tano akawa amefika katika hospitali hiyo. Waandishi wa habari pamoja na wananchi zaidi ya elfu mbili walikuwa katika eneo la hospitali ile huku wakitaka kusikia ni kitu gani ambacho kilikuwa kinaendelea

    Waandishi wa habari walipomuona Bwana Thomson anatereka kutoka garini mwake wakaanza kumsogelea huku wakimuwekea maiki zao lakini Bwana Thomson hakuongea kitu chochote kile, alionekana kuchanganyikiwa kupita kawaida. Akaanza kupiga hatua kuelekea ndani ya hospitali ile, machoni alionekana akiwa ameumia kupita kawaida, machozi yalikuwa yamejazana machoni mwake.

    Akaingia ndani ya hospitali ile na kisha kuanza kuelekea sehemu ya mapokezi ambako akachukuliwa mpaka nje ya chumba cha wagonjwa mahututi. Wachezaji kadhaa wa timu ya mpira wa kikapu ya Chicago Bulls walikuwa wametulia nje ya chumba kile huku nyuso zao zikiwa kwenye majonzi mazito juu ya rafiki yao kupatwa na ajali ya gari.

    Bwana Thomson akaanza kulia, uwepo wake nje ya chumba kile ulionekana kumuhuzunisha kupita kawaida jambo ambalo lilimfanya kujiona kutokutakiwa kuwa nje ya chumba kile. Akatulia nje ya chumba kile pamoja na wachezaji wale na watu wengine kutoka katika makampuni mbalimbali ya urembo na majarida.

    Walikaa nje ya chumba kile kwa muda wa masaa nane na ndipo miili ile kutolewa na kupelekwa katika chumba kingine kwa ajili ya mapumziko huku oparesheni kadhaa zikiwa zimekwishafanyika. Hawakutakiwa kuwaona wagonjwa wao katika kipindi hicho, bado walihitaji kupata muda wa mapumziko.

    Hawakuwa wakijitambua, walikuwa wamepoteza fahamu tangu pale ambapo ajali ile ilikuwa imetokea. Kila mtu alikuwa akitamani kuwaona wakifumbua macho na kuwaangalia tena, ajali ile ilizidi kuwatia wasiwasi kwa kuona kwamba hali za wagonjwa wale zingeendelea kuwa mbaya zaidi.

    **********CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Martin alikuwa amekaa sebuleni huku akiandika mistari ya wimbo wake mpya aliyoupa jina la ‘Mapenzi yangu’. Kwake, wimbo ule ulionekana kuwa mzuri ambao ungewashika mashabiki wake wengi ambao walikuwa wakipenda kusikiliza nyimbo nyingi kutoka kwake.

    Huku akiendelea kuandika wimbo ule, ghafla simu yake ikaanza kuita. Kwanza akaonekana kukereka, alijilaumu sababu iliyompelekea simu kuiacha wazi bla kuizoma. Mara ya kwanza akaidharau lakini alipoona mpigaji akati, akaamua kuichukua na moja kwa moja kuipeleka sikioni.

    “Upo wapi Mapac?” Sauti ya upande wa pili ilisikika ikiuliza swali.

    “Nipo nyumbani”

    “Unaangalia televisheni?”

    “Hapana. Kuna nini? Wanaonyesha konseti ile niliyoifanya Arusha?” Martin aliuliza huku tabasamu pana likiwa usoni mwake.

    “Kuna ajali. Kuna ajali imetokea”

    “Ajali? Ajali gani na imetokea wapi?”

    “Marekani. Patricia amepata ajali. Fungua CNN” Sauti ya upande wa pili ilisikika.

    Martin hakutaka kuendelea kuongea, alichokifanya huku akionekana kwenye mshtuo mkubwa akaiwasha televisheni na kuanza kuangalia habari ile. Maneno ambayo yalikuwa yameandikwa yakaonekana kumshtua kupita kawaida, hakuyaamini macho yake, hakuamini kama jina la mtu ambaye alikuwa miongoni mwa watu waliopata ajali alikuwa Patricia.

    “Mungu wangu!” Martin alijikuta akijisemea huku akisogea karibu zaidi.

    Bado hakuonekana kuamini kama kile alichokuwa akikiona kilikuwa kweli au si kweli, alishindwa kuamini kama kile kitu kilikuwa kimetokea kilikuwa kwenye ulimwengu halisi au alikuwa ndotoni na baada ya muda angeamka kutoka katika usingizi mzito na kujikuta yupo kitandani mwake.

    Akamuita mama yake ambaye akafika mahali pale na macho yake kuyapeleka katika kioo cha televisheni ile. Yeye mwenyewe hakuonekana kuamini kabisa, akajisogeza karibu kana kwamba kwa mbali hakuwa akiona vizuri.

    “Yesu wangu!” Bi Evadia alisema kwa mshtuo huku akiipeleka mikono usoni mwake na kuziba mdomo wake.

    Tayari Martin alikuwa akitokwa na machozi, alishindwa kuvumilia kabisa. Taarifa ile ya habari ikaonekana kumchanganya kupita kawaida. Alichokifanya ni kuinuka na kuanza kutoka nje. Mama yake akaonekana kumshangaa, hata kabla hajauliza swali lolote, Martin alikuwa amekwishatoka nje.

    Akaanza kuifuata sehemu ya kupakia magari na kisha kufungua mlango wa gari lake aina ya Verosa na kisha kumwambia mlinzi afungue geti na yeye kuondoka. Njiani hakuwa na raha, bado machozi yalikuwa yakimtoka, taarifa ile ya habari kuhusiana na ajali ambayo ilikuwa imetokea ilikuwa imemchanganya.

    Njiani alikuwa akiendesha gari kwa kasi, safari hiyo ilikuwa ni kuelekea Mikocheni B alipokuwa akiishi Bi Beatrice, mama yake Patricia. Kutokana na kasi ambayo alikuwa nayo wala hakuchukua muda mrefu akawa amekwishafika katika nyumba hiyo na mlinzi kufungua geti. Hata kabla ya salamu akaamua kuufuata mlango wa sebuleni na kuingia hata bila hodi.

    Macho yake yakatua machoni mwa Bi Beatrice ambaye alikuwa akiangalia televisheni huku akiwa akisiliza simu iliyokuwa sikioni mwake. Uso wake ulionekana kuwa na huzuni, machozi yalikuwa yakimtoka huku mara kwa mara akiwa anayafuta kwa kitambaa alichokuwa nacho mkononi.

    Alipoona Martin ameingia ndani ya nyumba ile, akaacha kuongea na simu ile na kisha kumfuata Martin na kisha kumkumbatia. Wote walikuwa wakilia, taarifa ile ya habari ikaonekana kuwaumiza.

    “Oooh! Patricia!” Bi Beatrice alisema huku akiwa bado amemkumbatia Martin.

    “Pole mama. Yote ni mambo ya Mungu!” Martin alimwambia.

    Siku hiyo ilikuwa ni kama siku ya msiba, wote walikuwa wakitokwa na machozi, ajali ile ambayo ilikuwa imetokea ilikuwa imewagusa kupita kawaida. Wakaendelea kuangalia taarifa ile ili kujua hali ambayo alikuwa nayo Patricia pamoja na mpenzi wake, Banana.

    Kadri muda ulivyozidi kwenda mbele, hali ya Patricia na Banana hazikuonekana kuwa sawa kabisa. Kila mwandishi ambaye alikuwa akizungumza alikuwa akizungumza kwa majinzi mazito kwani hali za watu wale zilionekana kuwatisha kupita kawaida.

    “Itanipasa kusafiri kuelekea Marekani” Bi Beatrice alimwambia Martin.

    “Nami pia itanibidi kuongozana nawe” Martin alimwambia.

    “Sawa. Ngoja niongee na Thomson ili atume tiketi za watu wawili na afanye mipango ya viza” Bi Beatrice alimwambia Martin ambaye akaonekana kuridhika kwani asingeweza kubaki nchini Tanzania na wakati msichana ambaye alikuwa akimpenda alikuwa amepata ajali mbaya.

    **********

    Wiki moja iliyofuata safari ya kuelekea nchini Marekani ikaanza. Ndani ya ndege kila mmoja akaonekana kuwa na majonzi, taarifa ya ajali ambayo ilikuwa ikisikika katika vyombo vingi vya habari duniani ilizidi kuwaumiza mioyo yao. Martin hakuonekana kuwa na furaha hata mara moja, muda mwingi alikuwa amekiinamisha kichwa chake chini.

    Mawazo yake yalirudi mpaka katika kipindi cha nyuma, kipindi ambacho alikuwa amekutana kwa mara ya kwanza na msichana Patricia katika shule ya Salma Kikwete. Alikumbuka tangu siku ya kwanza alipoanza mahusiano ya kirafiki na msichana yule, katika kipindi kile ambacho alikuwa ameangukia katika mapenzi yake.

    Mawazo yake wala hayakuishia hapo, alikumbuka siku ya kwanza alipomueleza Patricia juu ya moyo wake kwa jinsi ambavyo ulijisikia juu yake. Alikumbuka mambo mengi yaliyopita katika kipindi hicho mpaka siku ile ya kwanza walipofanya mapenzi hotelini bila kuwa na mahusiano ya kimapenzi.

    Martin alibaki akiumia kupita kawaida, moyoni mwake, Patricia ndiye alikuwa msichana ambaye alimpenda kuliko msichana yeyote yule, alimthamini kupita maelezo na ndio maana hata aliposikia kwamba msichana huyo alitaka kufunga harusi na mcheza kikapu Banana, alibaki akiumia.

    Maishani mwake alikuwa radhi kukosa kila kitu lakini si kumkosa Patricia ambaye alimuonyesha mwanga mkubwa sana katika maisha yake. Aliikumbuka barua ile ambayo alimwandikia dakika chache kabla ya kuondoka kuelekea nchini Marekani, aliyakumbuka maumivu makali ambayo aliyapata siku ile. Alilia kupita kawaida, mpaka kipindi hicho bado alikuwa akiendelea kulia.

    Tangu Patricia aondoke kuelekea nchini Marekani, bado Martin hakuwahi kuwa na furaha. Alipata umaarufu mkubwa nchini Tanzania kutokana na muziki ambao alikuwa akiufanya, aliingiza kiasi kikubwa cha fedha na bado alikuwa akiendelea kuingiza kiasi kingi cha fedha lakini bado furaha yake wala haikukamilika hata kidogo.

    Hakujiona kama angetakiwa kufurahi na wakati Patricia hakuwa mikononi mwake, hakujiona kuwa na sababu ya kufurahi na wakati msichana ambaye alikuwa akimpenda sana alikuwa katika mapenzi na mwanaume mwingine. Kwake, kila siku ilionekana kuwa kama jehanamu, maumivu yalikuwa yakiendela kila siku.

    Katika kipindi hiki alikuwa safarini akielekea nchini Marekani kumuona msichana ambaye alikuwa akimpenda kwa moyo wa dhati, Patricia. Ingawa alikuwa na uhakika wa kumuona lakini moyo wake wala haukuwa na furaha hata kidogo. Alikuwa akielekea nchini Marekani huku msichana huyo akiwa mahututi, akiwa amepoteza fahamu zake kabisa.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Martin aizidi kuumia, hakuamini kama siku ambayo angemuona Patricia basi ingekuwa siku ile ambayo asingeweza kuongea nae, angebaki kimya kitandani alipokuwa amelazwa. Wakati mwingine Martin alitamani kile ambacho kilikuwa kinaendelea kingekuwa ndoto na baada ya dakika kadhaa kuamka na kujikuta kitandani huku akiwa amechoka kutokana na tamasha ambalo alikuwa amelifanya Arusha.

    Hiyo wala haikuwa ndoto, hiyo ilikuwa hali halisi ambayo ilikuwa ikiendelea katika ulimwengu halisi. Kila alipokuwa akimwangalia Bi Beatrice ambaye alikuwa pembeni yake, moyo wake ulikuwa ukimuuma sana, mwanamke yule alikuwa amefanana sana na Beatrice ambaye alikuwa akimfuata kwenda kumuangalia nchini Marekani.

    Sala yake bado ilikuwa ikiendelea kimoyo moyo, hakutaka Patricia afariki na wakati wala hakuwa ameongea nae na wala kumshukuru kwa wema wote ambao alikuwa amemfanyia katika kipindi chote. Alihitaji aongee na msichana huyo na kumwambia ukweli kwamba alikuwa akiendelea kumpenda japokuwa alikuwa mahututi kitandani.

    Ndege ilichukua masaa ishirini na mbili na ndipo ikaanza kukanyaga katika uwanja wa kimataifa wa John F Kennedy na kisha abiria wote kuteremka. Kutokana na wakati huo kutokuwa kipindi cha baridi kali, hali ya hewa ikaonekana kuzoeleka miilini mwao.

    Bwana Thomson alikuwa akiwasubii nje. Alipomuona mpenzi wake, Bi Beatrice, akaanza kumfuata na kukumbatiana. Wote wakaanza kulia. Martin alikuwa pembeni huku akiangalia kila kitu ambacho kilikuwa kinaendelea mahali hapo mpaka pale ambapo Bi Beatrice alipoanza kumtambulisha kwa Bwana Thomson.

    Hawakutaka kuendelea kubaki mahali hapo, safari ya kuelekea katika hospitali ya Metopolian kuanza. Njiani kila mmoja alikuwa kimya, bado hali ya Patricia ilikuwa mbaya sana na wala hakuwa amerejewa na fahamu toka alipopata ajali wiki iliyopita. Walipofika katika hospitali ile, kama kawaida yao waandishi wa habari wakaanza kuwazunguka kwa lengo la kuwahoji lakini hawakutaka kuongea kitu chochote kile.

    Wakafika mpaka katika chumba kile alicholazwa binti yao na kisha kumsogelea pale kitandani. Kila mmoja alibaki akimwangalia kwa majonzi. Wote wakajikuta wakianza kulia tena. Martin hakuweza kuvumilia kabisa, msichana ambaye alikuwa akimpenda kwa moyo wake wote kwa wakati huu alikuwa kitandani akipumua kwa msaada wa mashine ya oksijeni huku dripu tatu tofauti zikiwa zinaning’inia.

    Martin akaanza kumsogelea Patricia. Patricia hakuwa akiongea, hakuwa amefumbua macho, yaani kwa kifupi alikuwa akionekana kama mtu ambaye tayari alikuwa amekwishakufa kitandani pale na alikuwa akisubiri kuagwa sura ya mwisho na kuzikwa.

    “Fumbua macho Patricia....fumbua macho uniangalie. Nimekuja huku kwa ajili yako...naomba ufumbue macho uongee nami Patricia....fumbua macho Patricia....” Martin alijikuta akiongea kwa sauti ya chini huku akimwangalia Patricia na huku machozi yakimtoka. Maneno yake yale wala hayakuweza kubadilisha kitu chochote, bado Patricia alibaki kimya, alionekana kama tayari alikwishafariki pale kitandani.

    Siku hiyo ilionekana kuwa siku ya huzuni zaidi kwao wote. Patricia ambaye walikuwa wamekuja kumuona alikuwa kimya kitandani, walitamani muujiza wowote ule utokee na kumuona Patricia akifumbua macho yake na kuwaangalia tena na kisha kuongea nao. Sala zao zilionekana kuwa si chochote kwani waliziona kutokuwa na majibu yoyote yale.

    Wote kwa pamoja walimuona Mungu akiwa amewapa jaribu kubwa ambalo lilikuwa ni zaidi ya uwezo wao wote, wala hawakutaka kukata tamaa, bado walizidi kumuomba Mungu zaidi na zaidi.

    Muda wa kuwaona wagonjwa ulipokwisha walitakiwa kuondoka chumbani hapo na kisha kuelekea katika nyumba ya Bwana Thomson. Kwa kuwa Martin alikuwa mgeni ambaye alitambulishwa kuwa kama mpenzi wa Patricia nchini Marekani, akapewa chumba cha Patricia kwa ajili ya kukitumia katika siku zote ambazo angekuwa nchini Marekani.

    Majonzi kwake bado yalikuwa makubwa, usiku hakulala, alikuwa akizidi kumkumbuka Patricia ambaye alikuwa kimya kitandani. Moyo wake ulizidi kumuomba Mungu afanye muujiza wowote wa kumuamsha Patricia kitandani lakini sala zake hazikuwa na majibu yoyote yale.

    Alimuona Mungu akichelewa kujibu sala zake, alimuona Mungu akiwa haijali furaha yake ambayo ilikosekana kwa kipindi kirefu. Kitu ambacho alikuwa akikihitai katika kipindi hicho ni kumuona Patricia akifumbua macho na kuongea tena.

    Usingizi ulikatika kwake, alishinda akimfikiria Patricia, asubuhi ikaingia huku akiwa hajalala hata dakika moja. Gari likafika katika nyumba hiyo na kuwachukua tena kuwapeleka hospitalini.

    Kama ambavyo walimuacha Patricia na ndivyo ambavyo walimkuta, alikuwa kimya kitandani.

    Mipira ambayo alikuwa amewekewa na madaktari ndio ambayo ilikuwa ikitumika kumpitishia chakula huku mingine akiitumia kama kujisaidia kila alipotaka kujisaidia.

    Patricia alionekana kuwa kama mfu kitandani pale, alionekana kama tayari alikwishakufa ila madaktari hawakutaka kusema ukweli. Kila alipokuwa akimwangalia Patricia, Martin alibaki akitokwa na machozi mfululizo, bado alionekana kuumia kupita kawaida moyoni mwake.

    Chakula hakula, hamu yote ya kula ilikuwa imemtoka, kuna kipindi alihitaji kutokuondoka hospitalini, alitamani aendelee kubaki na Patricia chumbani pale mpaka pale atakapoona mwisho wake ungekuwa nini. Alimpenda sana Patricia, hakutaka kumpoteza katika maisha yake, alimthamini na kumhitaji.

    Alitamani kutumia kila kitu ambacho alikuwa nacho katika maisha yake lakini mwisho wa siku amuone Patricia akiyafumbua macho yake tena na kumwangalia huku akiachia tabasamu pana ambalo mara kwa mara lilikuwa likimchanganya sana shuleni. Kipindi hicho, ilionekana kuwa kama ndoto, tena ndoto mbaya ambayo wala hakutakiwa kuiota katika maisha yake yote.

    "Au ninaota? Lakini kama ni ndoto mbona inatisha halafu ni ya muda mrefu hivi? Mmmh! Inatisha" Martin alijisemea huku akiswa amepiga magoti huku amekiegemea kitanda alicholazwa Patricia na mkono mmoja wa Patricia akiwa ameushika.



    Siku ziliendelea kukatika na hali ya Patricia iliendelea kuwa vile vile. Alikuwa amelala kitandani kama mtu ambaye alikwishakufa. Alipumua kwa kutumia mashine ya oksijeni huku mipira ya kumlisha ikiwa imewekwa mwilini mwake. Kila wakati Martin alipokuwa akimwangalia hakuweza kuamini kama maisha ya baadae ya patricia tangekuwa namna ile.

    Kila siku alikuwa akifika pale hospitalini huku wakati mwingine akitamani kulala katika chumba kile ili mladi tu awe karibu na patricia. Kwake, kuugua kwa Patricia lilikuwa jaribu na pigo kubwa kwake kuliko pigo lolote ambalo alilipata kabla.

    Mwezi wa kwanza ukakatika. Madaktari wakatoa taarifa ambayo ilikuwa imemshtua kila mtu, Banana alikuwa amekufa kitandani. Taarifa ile iliinua vilio kwa wapenzi wote wa mchezo wa kikapu nchini Marekani, hawakuamini kama mchezaji yule ambaye alikuwa ameanza kuvuma angeweza kuwatoka katika siku za karibuni.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mazishi yakafanyika, wachezaji wengi wa mpira wa kikapu wakawa wamehudhuria mazishi hayo ambayo yalikuwa yamemgusa kila mtu. Macho na masikio ya watu yakawa yakisikilizia kuhusu hali ya Patricia ambaye alikuwa kitandani akiendelea kuugua. Kila siku hali yake ilikuwa vile vile.

    Madaktari wakahangaika usiku na mchana, ripoti ya hali yake ikatolewa kwamba kamwe hasingeweza kuinuka kitandani, uti wake wa mgongo ulikuwa umevunjika vunjika jambo ambalo liliufanya mwili kupooza kuanzia shingoni kuja chini. Ile ilikuwa ni taarifa mbaya sana, kupooza kwa mwili wake kulimaanisha kwamba Patricia asingeweza kuinuka kitandani tena wala kukisogeza kiungo chochote cha mwili wake.

    Taarifa ile ilikuwa mbaya zaidi kwa Martin, alibaki akilia chumbani mule huku akimwangalia Patricia ambaye bado aliendelea kuwa kimya. Kila siku alikuwa akitamani Patricia afumbue macho yake tena na aongee nae tena kama jinsi alivyozoea kufanya katika kipindi cha nyuma.

    Mwezi wa pili ukakatika, wa tatu ukakatika na hata wa nne kukatika na ndipo Martin kuamua kurudi nchini Tanzania. Kila mtu ambaye alikuwa amemuona alimuonea huruma, mwili wake ulikuwa umekonda kupita kawaida. Nchini Tanzania hakutaka kufanya kitu kingine chochote zaidi ya kuendelea kuwasiliana na Bwana Thomson na kisha kurudi tena nchini Marekani.

    Japokuwa Patricia alikuwa katika hali mbaya lakini wala hakutaka kuyaondoa mapenzi yake kwa msichana huyo. Bado alikuwa akimpenda kupita kawaida, japokuwa alikuwa katika hali mbaya lakini wala hakutaka kumuacha. Alikumbuka maneno ambayo alimwambia siku za nyuma kwamba angempenda katika hali zote, hayo ndiyo yaliyomfanya kuendelea kumpenda na kumhitaji Patricia.

    Mwaka ukakatika na mwaka wa pili kuingia. Hali ya Patricia iliendelea kuwa vile vile, hakufumbua macho yake wala kinywa chake. Wakati mwingine taarifa zilikuwa zikiendelea kutangazwa kwamba Patricia alikuwa amekwishakufa kitandani jambo ambalo liliwataka watu kuuona mwili wake. Taarifa zile zilikanushwa vikali na Bwana Thomson ambaye bado alikuwa akiendelea kutumia kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya matibabu.

    Miezi sita ikakatika. Mwaka mmoja na miezi sita, Patricia hakuwa amefumbua macho yake. Siku kadhaa zikasogea na ndipo pale Patricia alipoanza kuyafumbua macho yake. Manesi hawakuonekana kuamini, walichokifanya ni kuelekea katika ofisi ya dokta Simpson na kumwambia kuhusu hali ya mgonjwa.

    Dokta Simpson hakutaka kuendelea kubaki ofisini mule, aichokifanya ni kuanza kukimbia kwa kasi kueleka katika chumba kile. Macho ya Patricia yalikuwa yakiangalia juu tu tena sehemu moja, hata pale alipokuwa akimchezeshea mkono karibu na macho yake, mboni nyeusi ya jicho haikucheza kabisa.

    Dokta Simpson akachukua simu yake na kumpigia Bwana Thomson na kumpa taarifa ya maendeleo ya binti yake. Ni ndani ya dakika kumi tu Bwana Thomson akafika hospitalini hapo huku akiwa na Bi Beatrice pamoja na Martin.

    Wote wakaonekana kuwa na furaha, tayari walikuwa wamesubiri kwa takribani mwaka mmoja na miezi sita kusubiri kwa maendeleo ya binti yao pale kitandani. Leo, Patricia alikuwa amefumbua macho yake.

    Ingawa alikuwa ameyafumbua macho yake lakini wala Patricia hakuweza kuyapepesa., bado alikuwa akiangalia sehemu moja tu. Martin alikuwa akitabasamu tu, kitendo cha kuziona mbozi za Patricia kwa mara nyingine kilionekana kumpa furaha na matumaini kwamba kuna siku Patricia angeweza kuongea tena.

    Ilipita miezi miwili mimgine na ndipo Patricia alipoanza kupepesa macho yake. Hiyo ilikuwa ni furaha ya kila mmoja, matumaini ya kuona kwamba Patricia angeweza kuongea kama zamani yalikuwa yameanza kuwarudia tena. Tatizo bado lilikuwepo, kuvunjika vunjika kwa uti wa mgongo na kumfanya kupooza pale kitandani.

    Kila alipokuwa akipepesa macho yake huku na kule na kuyakutanisha na macho ya Martin na wazazi wake, alikuwa akitabasamu lakini wala hakuweza kufanya kitu ingine zaidi ya hicho. Bado hali yake haikuonekana kuwa nzuri hata mara moja.

    Muda mwingi Patricia alikuwa akitokwa namachozi hasa kila wakati ambao alikuwa akimwangalia Martin. Moyoni alionekana kuwa na jambo ambalo lilikuwa likimliza lakini hakukuwa na mtu yeyote ambaye alieleza sababu zilizompelekea Patricia kutokwa na machozi.

    “Nitakupenda siku zote katika maisha yangu” Martin alimwambia Patricia maneno ambayo yalikuwa yakimuongzea tabasamu zaidi pale kitandani alipokuwa amelala huku asilimia kubwa ya mwili wake ukiwa umepooza.

    ********

    Hali ya Patricia haikuendelea zaidi ya hapo. Kitendo chake cha kufumbua macho kilionekana kuwa hatua ya mwisho kabisa katika maisha yake pale kitandani. Alikuwa akiendelea kuwa kimya huku akimwangalia kila mtu ambaye alikuwa akiingia na kutoka ndani ya chumba kile.

    Patricia alionekana kuwa kwenye mateso makali, kitendo cha kutokuongea wala kutokutikisa kiungo chochote mwilini mwake kilionekana kumpa wakati mgumu. Kamwe hakutaka kuwa hivyo, ajali ambayo alikuwa ameipata, ajali ambayo ilipangwa ndio ambayo ilikuwa imebadilisha maisha yake yote.

    Uzuri wake wala haukupungua. Japokuwa mashine ya oksijeni ilikuwa imeziba mdomo na pua yake lakini uzuri wake ulikuwa vile vile. Watu wengi kutoka nje na ndani ya nchi ya Marekani walikuwa wakifika mara kwa mara katika hospitali hiyo na kumtakia afya njema.

    Patricia alikuwa katika wakati mgumu sana, mwili wake ulikuwa umepungua kupita kawaida, kila mtu ambaye alikuwa akimwangalia alikuwa akimuonea huruma. Mwaka wa pili ukakatika, kidogo mafanikio mengine yakaanza kujionysha, mdomo wa Patricia ukaanza kufunguka na kuanza kuongea.

    Hiyo ilionekana kuwa hatua kubwa na muhimu sana katika maisha yake. Aliweza kumuita mtu yeyote japokuwa kwa shida sana. Alikuwa akiongea vizuri kama kawaida japokuwa kwa sauti ya chini sana. Kila mmoja akaanza kumshukuru Mungu kwa ile hatua ambayo Patricia alikuwa ameifikia.

    Patricia aliendelea kubaki hospitalini kwa takribani miezi nane mingine na ndipo hapo akaruhusiwa kutoka hospitalini huku akitakiwa kuwa kwenye uangalizi mkubwa. Kitendo hicho kidogo kilionekana kumpa furaha Martin kwani alikuwa na uhakika wa kumuona Patricia muda wowote ambao angetaka kumuona.

    “Kwa kuwa uti wake wa mgongo umevunjika vunjika, kamwe hautoweza kuungika. Ataendelea kuwa katika hali hii mpaka atakapofariki” Dokta aliwaambia.

    Kwao iliendelea kuwa taaarifa mbaya kuliko taarifa zot ambazo waliwahi kuzisikia katika maisha yao. Walitamani sana kumuona Patricia akisimama na kuanza kutembea kama siku zile za nyuma alivyokuwa akifanya.

    Maisha ya Patricia ya kuwa kitandani yakaanzia katika nyumba ya baba yake, Bwana Thomson. Basi mzee huyo alikuwa akitumia kiasi kikubwa cha fedha kumtibia mtoto wake. Japokuwa Patricia alikuwa kwenye hali mbaya lakini kila siku Bwana Thomson alikuwa akijipa moyo kwamba binti yake huyo angeweza kupona na kuwa mzima kama zamani.

    Muda wote Martin alikuwa katika chumba alicholazwa Patricia nyumbani pale. Yeye ndeiye alikuwa akifanya kazi ya kumlisha kwa kutumia mipira ile na hata kukisafisha chombo chake alichokuwa akikitumia kwa ajili ya haja kubwa na ndogo.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kwa Martin, hakutaka kuupunguza upendo wake, bado alikuwa akiendelea kumpenda Patricia huku akizidi kumpenda kadri siku zilivyozidi kwenda mbele. Patricia kwake alionekana kuwa mwanamke muhimu ambaye wala hakutakiwa kuachwa peke yake kisa alikuwa kwenye hali iliyokuwa na matatizo makubwa.

    Hiyo ndio ilikuwa nafasi kubwa kwake ya kumuonyeshea ni kiasi gani alikuwa akimpenda na kumhitaji katika maisha yake. Kila siku alikuwa akilala katika chumba alichokuwa akilala Patricia, hakujali harufu kali ya aja ambayo alikuwa akiipata kila siku chumbani humo, kitu ambacho alikuwa akikijali ni kuwa karibu na Patricia tu.

    Miezi ikaendelea kukatika, hatimae Patricia akawa na uwezo wa kuongea vizuri. Kila siku Patricia alionekana kuwa mtu wa kulia tu, moyoni aliumia, alikuwa akijutia uamuzi wake ambao ulimfanya kuhamia nchini Marekani.

    Kwake, Martin alionekana kuwa mwanaume pekee ambaye alikuwa na mapenzi ya dhati kwake, upendo mkubwa ambao kila siku Martin alikuwa akimwambia siku za nyuma ulikuwa ukijionyesha katika kipindi hicho cha mateso. Martin hakutaka kuwa na msichana mwingine, msichana ambaye alikuwa akimpenda katika kipindi hicho alikuwa Patricia tu.

    “Nakupenda Martin” Patricia alimwambia Martin kwa sauti ya chini.

    “Nakupenda pia Patricia. Umekuwa mtu muhimu sana kwangu. Nitaendelea kukupenda katika kipindi chote mpaka pale kifo kitakaponitenganisha nawe” Martin alimwambia Patricia na kisha kumbusu shavuni.

    Patricia bado alikuwa akiendelea kuwa katika hali ile ile. Kwa muda wa mwaka wa tatu bado alikuwa kitandani. Martin hakutaka kurudi nchini Tanzania, bado alikuwa akitamani kukaa na Patricia ambaye alikuwa akizidi kumpenda kadri siku zilivyozidi kwenda mbele.

    Bwana Thomson alimchukulia Martin kuwa kama mtoto wake wa kumzaa, moyo ambao alikuwa akiuonyesha kwa mtoto wake ulikuwa ukimfariji kupita kiasi. Katika kipindi cha kula chakula, Martin ndiye alikuwa mtu pekee ambaye alikuwa akimlisha chakula Patricia kwa kutumia mipira ambayo ilikuwa imeunganishwa moja kwa moja mpaka tumboni mwake.

    Kila siku Martin alikuwa mtu wa furaha. Kwa kipindi kirefu cha nyuma alikuwa akitamani sana kuungana na patricia na hatimae kuishi pamoja, kuwa nae katika kipindi hicho kulionekana kumfariji.

    “Hii ni safari yangu ndefu kuelekea kaburini Martin” Patricia alimwambia Martin.

    “Hapana. Hapana Patricia. Hautokufa. Hautokufa Patricia’ Martin alimwambia Patricia.

    Maneno yale yalionekana kumuumiza Martin, machozi yakaanza kumtoka. Hakupenda kabisa Patricia aongee maneno yale ambayo yalionekana kumuumiza kupita kawaida. Kwake, maneno yale yalionekana kuwa kama msumali wa moto ambao uliingia moja kwa moja moyoni mwake.

    Akapiga magoti chini na kisha uso wake kuusogeza karibu na uso wa Patricia na kisha kumbusu. Kila wakati alikuwa akitamani kumbusu Patricia, japokuwa msichana huyo alikuwa amekonda kupita kiasi lakini bado alikuwa akimpenda. Hakukuwa na msichana yeyote katika ulimwengu huu ambaye alikuwa akimpenda kama jinsi ambavyo alikuwa akimpenda Patricia.

    “Hali ya hewa inaonekana kumsumbua mgonjwa. Itatupasa kusafiri kurudi nchini Tanzania pamoja nae” Bi Beatrice alimwambia Martin.

    “Mbona ni uamuzi wa haraka hivyo mama?” Martin aliuliza huku akionekana kushtuka.

    “Ndivyo tulivyoamua pamoja na baba yake. Itatupasa kurudi nchini Tanzania kwani mgonjwa wetu amefikia ukingoni kupata nafuu. Hatoweza kupata nafuu zaidi ya hapo” Bi Beatrice alimwambia Martin.

    Hakukuwa na kitu kilichoendelea zaidi ya harakati za kurudi nchini tanzania kuanza. Martin hakutaka kumficha Patricia, alichokifanya ni kumwambia juu ya kie kitu ambacho kilikuwa kimepangwa na kukubalika na kila mtu.

    “Tunarudi Tanzania. Najua kwamba haukuwa na ndoto ya kurudi Tanzania, haina budi kwa sasa Patricia” Martin alimwambia Patricia.

    “Niko tayari kurudi. Niko tayari kwa kitu chochote kutokea maishani mwangu ila si kukupoteza wewe. Umekuwa mfariji wangu mkubwa Martin” Patricia alimwambia Martin.

    Mipango ya safari ikawa imekamilika, ndege ambayo ilikuwa ikimilikiwa na Bwana thomson ikaandaliwa na kisha safari kuanza huku ndani ya ndege kukiwa na watu wasiozidi saba. Bwana Thomson alikuwa mmoja wapo, hakutaka kubaki Marekani, alitaka kuwasindikiza ili akutane na daktari ambaye angekuwa anafika nyumbani kila siku kwa ajili ya kumuona Patricia.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Je nini kitaendelea?

    Je Huo ndio utakuwa mwisho wa Patricia hasa baada ya kurudi nchini Tanzania?



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog