IMEANDIKWA NA : HALFANI SUDY
*********************************************************************************
Sehemu Ya Kwanza (1)
Ilikuwa mara yangu ya kwanza kufika jijini Mbeya. Jiji nililokuwa nalisikia tu hapo kabla na kuliona katika ramani ya Tanzania. Uhamisho wa kikazi wa baba yangu toka Dodoma kwenda Mbeya ndiyo uliotufanya twende Mbeya familia nzima.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Mimi na baba yangu tulitangulia kwenda Mbeya, wakati mama pamoja na mdogo wangu wa kike, Christina walipanga kuungana nasi baada ya wiki moja.
Kwa majina naitwa James Natai, lakini marafiki zangu wengi wa huko Dodoma walizoea kuniita Jimmy. Mtoto wa kwanza katika familia ya Mzee Natai. Katika familia yetu tulikuwa tumezaliwa wawili tu, mimi na mdogo wangu Christina. Baba yangu alikuwa ni muajiriwa wa shirika la umeme Tanesco katika mkoa wa Dodoma. Huku mama yangu akiwa ni mwalimu wa shule ya Msingi Uhuru.
Kitabia mimi huwa napenda sana kusafiri, na safari ya kuelekea Mbeya niliifurahia sana. Nakumbuka tulipanda basi ya Sai baba. Baba alikaa katika siti ya watu wawili, lakini hatukukaa pamoja. Huku mimi
nikikaa siti ya tatu nyuma toka pale alipokuwa amekaa baba. Siti hiyo ya tatu, kwa bahati mbaya au nzuri ilinikutanisha na mtoto wa kike mrembo sana. Nilikaa kwenye ile siti na kutulia.
Nakumbuka hatukusalimia kabisa na yule msichana, alionesha alikuwa na majivuni sana. Alikuwa amevaa jeans nzuri sana ya bluu na kitop cheupe chenye michirizi meusi chini ya kwapa kuelekea kiunoni, huku masikioni akiwa ameweka earphone zenye rangi ya bluu sawa na ile suruali yake ya jeans, alikuwa makini akisikiliza mziki. Nami nilikaa na kufungua zipu ya pembeni ya begi langu, nikatoa kitabu cha riwaya ya Farida. Nilianza kusoma taratibu.
Safari ya kutoka Dodoma kwenda Mbeya kwa kawaida ni ndefu sana. Takribani saa kumi na mbili. Cha ajabu katika saa zote hizo hatukuongea lolote na yule msichana. Tulikuwa kimya. Yeye akisikiliza muziki, mimi nikisoma riwaya. Tulifika jijini Mbeya saa moja jioni. Jiji lilitukaribisha kwa baridi kali sana. Yule msichana nakumbuka alishuka katika stendi ya mabasi ya Meta, pale katika hospitali kubwa ya wazazi.
Wakati mimi na baba tulishuka stendi kuu, Uhindini. Hatukuwa na pakufikia, kumbuka tulikuwa wageni katika Jiji hilo la kijani. Jiji lililozungukwa na milima mingi sana. Jiji lenye rutuba nzuri kwa kilimo, Jiji
lenye idadi kubwa sana ya watu, Jiji lenye kustahili kuitwa Jiji. Tulipanga vyumba katika nyumba ya kulala wageni palepale Uhindini. Wakati tunaingia katika nyumba ile ya kulala wageni, nilibahatika kusoma bango kubwa la jeusi lenye maandishi meupe makubwa, bango lenye jina la nyumba ile ya kulala wageni. 'SOWETO GUEST HOUSE' Baba alipanga chumba chake, nami alinipangia chumba changu. Tulilala katika nyumba ya kulala wageni siku ile.
*****CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Wiki tatu baadae nilikuwa nimeshalizoea Jiji la Mbeya japo kwa uchache. Baba alikuwa ameshaanza kazi katika shirika la umeme Tanesco, Mbeya. Nami nikiwa naendelea na kidato cha tano, katika shule ya Sekondari Sangu. Mama na mdogo wangu Christina au Tina kama tulivyozoea kumuita, walikuwa wameshakuja Mbeya nao.
Ndugu yangu Tina alikuwa anasoma kidato cha pili katika shule ya Sekondari Meta. Sasa hatukuwa tunakaa katika nyumba ya kulala wageni tena. Tulikuwa tumeshapanga nyumba nzuri na ya kisasa, katika mtaa wa Forest. Maendeleo yangu kitaaluma shuleni yalikuwa mazuri sana. Nilikuwa nafanya vizuri sana darasani. Kama ilivyo katika shule ya awali kule Dodoma.
Wiki mbili baadae nilipata rafiki, rafiki wa kiume, rafiki mpole na mwenye busara sana. Rafiki wa kweli. Alikuwa anaitwa Richard Chali. Richard alikuwa rafiki mwema sana kwangu. Tuliyependana na kuelewana sana. Tulikuwa tunashirikiana katika masomo na mambo mengine yote pale shuleni. Ilikuwa utakapomuona Richard Chali basi mimi niko pembeni yake, au utakaponiona mimi basi Richard Chali yuko pembeni yangu. Baadhi ya wanafunzi wengine walikuwa wanatuita sisi mapacha, kwa jinsi tulivyoshibana na kuelewana. Ulikuwa upendo wa dhati ulioanza bila sababu maalum.
Ilitokea tu mimi na Richard Chali kuelewana. Mwanzoni nilidhani labda ukaribu wa viti vyetu darasani ndio uliosababisha tuelewane na Richard Chali, lakini baadae nikagundua hapana ukaribu wa madawati haikuwa sababu, mbona Victor Anyimike na Mgeni Francis nao nilikuwa nakaa nao karibu sana kimpangilio wa meza lakini hawakutokea kuwa marafiki zangu kama ilivyokuwa kwa Richard Chali.
Ukweli ni kwamba urafiki wangu na Richard Chali ulitokea tu....
Maisha ya jijini Mbeya yalikuwa mazuri kwa ujumla. Pengine kuliko hata yalivyokuwa kule mkoani Dodoma. Kitaaluma shule ya Sekondari Sangu ilikuwa tofauti sana na shule ya Jamhuri nikiyosoma Dodoma. Sangu walikuwa makini sana kuhakikisha wanafunzi
wanafaulu vizuri katika mitihani yao ya shule na Taifa. Kwanza walikuwa na program wakiyoiita 'Crash program' hii ilikuwa kwa vidato vyenye mtihani wa Taifa, vidato kama cha pili, kidato cha nne na kidato cha sita. Walikuwa wanarudi jioni kusoma baada ya vipindi vya kawaida. Pia walimu walikuwa mahiri sana katika masomo wayafundishayo, na mwisho mkuu wa shule alihakikisha wanafunzi wanakuwa na nidhamu siku zote. Siku zilisonga mbele. Na maisha yaliendelea vizuri katika shule hiyo. Ikapita miezi, ikaja wiki na hatimaye ikaja siku. Siku ya jumatatu. Jumatatu Iliyonifanya nichukue kalamu yangu na kuandika Simulizi hii ya kusikitisha sana. Simulizi ya huzuni. Simulizi inayonifanya nitamke maneno haya huku nikitoa machozi.... Simulizi inayonifanya nilie huku nikisema kamwe SITOISAHAU MBEYA!
Ilikuwa jumatatu tulivu. Sawa na jumatatu zingine zilizotangulia. Jumatatu hiyo jioni tulikuwa na 'debate', kati yetu wanafunzi wa kidato cha tano na wanafunzi wa kidato cha nne. 'Debate' ilikuwa inafanyika katika Ukumbi mkubwa wa shule yetu.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Ilivyotimu saa kumi kamili jioni ukumbi mzima ulikuwa umejaa wanafunzi kushuhudia mashindano hayo ya 'debate'. Ingawa 'debate' iliwahusu wanafunzi wa kidato cha nne na wanafunzi wa kidato cha tano. Lakini hadi wanafunzi wa vidato vingine walikuja
kushuhudia. Kwa upande wetu, wanafunzi wa kidato cha tano imani ya ushindi ilikuwa kwetu, kwangu mimi na kwa rafiki yangu kipenzi, Richard Chali. Sisi tulikuwa mahiri katika kutoa hoja, mahiri katika kupinga hoja, mahiri katika kuuliza na kujibu maswali. La zaidi tulikuwa mahiri sana wa kuongea lugha ya kiingereza.
Ulikuwa mpambano mkali sana wa 'debate'. Ilitupasa tutumie akili zetu za ziada ili kuweza kushinda mpambano ule. Wanafunzi wa kidato cha nne walikuwa wamejipanga vizuri sana, huku wakishangiliwa na wanafunzi wenzao wote wa O-level. Pamoja na vifijo, nderemo na kelele zao. Mimi niliamini tutashinda tu katika 'debate' ile. Maana nasi tulikuwa tumejipanga vizuri sana, huku tukipewa sapoti kubwa na wanafunzi wa kidato cha sita.
'Debate' ilianza, kijana mmoja wa kidato cha nne aitwaye Mnubi Francis ndiye aliyeanza kuongea katika debate ile. Alikuwa kijana mahiri na mwenye akili sana. Nakumbuka Richard Chali alikuwa wa kwanza kuongea kwa upande wetu. Richard Chali alikuwa katika ubora nzuri sana siku ile, alitoa hoja nzuri sana muda wake ulipofika. Watu wengi walichangia. 'Debate' ilikuwa kama ngoma droo. Ilikuwa inasubiriwa hitimisho tu, labda ndio lingetoa mshindi.
Mimi ndiye nilichaguliwa kwenda kutoa hitimisho kwa upande wa wanafunzi wa kidato cha tano. Nakumbuka mada ilikuwa 'Education is better than money' Sisi tulikuwa tunaikubali hiyo mada, wakati wanafunzi wa kidato cha nne walikuwa wanaipinga.
Wakati nimesimama pale mbele, baada tu ya salamu macho yangu yaliangalia nyuma ya ukumbi ule, ndipo macho yangu yalipoona kitu cha ajabu sana! Mdomo wangu ulishindwa kuongea. Miguu ilikuwa inatetemeka, nilishindwa kabisa kutamka maneno. Ukumbi mzima ulibaki kimya, wakishangaa nimepatwa na nini, maana niliacha kuongea ghafla. Wanafunzi wa kidato cha tano walibaki midomo wazi. Roho zikiwadunda kwa kasi. Walikuwa wanategemea mimi ndiye ningepeleka ushindi darasani kwangu katika mashindano yale ya 'debate'. Sasa shujaa wao nilikuwa nimepatwa na kigugumizi.
Wanafunzi wa kidato cha nne walikuwa wanashangilia sana, walikuwa wanatamani nishindwe kuongea vilevile ili ushindi uende upande wao kiurahisi. Mimi niliendelea kuganda vilevile, ilikuwa ni kama kuna mtu kashika rimoti ya runinga, na kubonyaza kitufe kilichoandikwa 'pause'.
Ndipo nilipomwona akitabasamu!
Kule nyuma kulikuwa na msichana. Msichana mrembo sana. Msichana yuleyule tuliyekaa katika siti moja wakati nakuja Mbeya kutokea Dodoma. Msichana ambaye alinichunia katika gari la Sai baba, hakutaka hata kunisalimia, hakutaka hata kuniangalia, alikuwa 'bize' na 'earphone' zake, sijui akisikiliza muziki ama aliegesha tu zile earphone masikioni. Majibu anayo yeye. Msichana ambaye alinionesha kama ana kiburi ama pengine alikuwa na nyodo. Msichana ambaye sikuwahi kumjua hata jina lake. Nitamjua vipi wakati hatukuongea lolote ndani ya basi? Cha ajabu, cha kushangaza, cha kustaajabisha kumbe tulikuwa tunasoma shule moja, sikuwahi kumuona hata siku moja shuleni. Leo ndio siku ya kwanza kumuona pale shuleni, na ni siku ya pili kumuona hapa duniani, na sasa alikuwa ananitabasamulia!CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Nami nilitabasamu kidogo, nikajitahidi kuongea, sasa sauti ilitoka!
Nilihitimisha ile mada ingawa sio kwa ufanisi mkubwa kama nilivyokuwa siku zote. Nilivyomaliza kuongea moja kwa moja nilienda kule nyuma, alipokuwa yule msichana, cha ajabu alisimama na kunikimbilia. Alinikumbatia kwa furaha sana. Nilijisikia aibu sana, lakini yeye hakujari hata chembe. Macho ya watu wote ukumbi mzima yalikuwa yanatuangalia sisi. Nilijari, hakujari. Tulivyomaliza kukumbatiana tulikaa kwenye viti. Tuliongea mambo mengi sana, ilikuwa ni kama marafiki tuliopoteana kwa muda mrefu sana. Hakuna
aliyekuwa anajua kwamba tulikuwa ni maadui wa kwenye gari ambao sasa tulikuwa marafiki ukumbini. Marafiki wa kweli. Huo ndio ulikuwa mwanzo wa urafiki wangu na yule msichana niliyekuwa namuona alikuwa na majivuno sana na kiburi hapo kabla. Msichana niliyekuja kumtambua kuwa alikuwa anaitwa Evelyne, Evelyne Gando.
Kwa kuwa Evelyne alikuwa rafiki yangu, moja kwa moja alikuwa rafiki wa rafiki yangu pia, Richard Chali. Sasa kampani yetu ikaongezeka, ikawa kampani ya watu watatu, ninaweza kusema kampani yetu ilikuwa ndio kampani nzuri zaidi pale shuleni Sangu Sekondari. Tulisaidiana kwa kila kitu. Wanafunzi wengine hawakuupenda urafiki wetu, wapo waliosema tunaringa eti kwa kuwa tulikuwa tunajiona tuna akili sana pale shuleni, wengine walisema tunajivuna kwakuwa ni wazuri na mambo mengine mengi. Lakini maneno ya watu hayakuaathiri kabisa urafiki wetu, maneno ya watu ni maneno tu. Yalipitia sikio la kushoto yakapitiliza hadi sikio la kulia. Yakapeperukia kuleeeeee.
*****
Nakumbuka ilikuwa mwezi wa tatu baada ya kukutana na Evelyne Gando, nakuwa rafiki yangu. Ndipo ndoto na mawazo ya ajabu yakaanza kunitawala kichwani
mwangu. Ndoto na mawazo yaliyokuwa yananiambia kwamba nilikuwa nampenda Evelyne Gando. Naam, ndotoni usiku nilioteshwa hivyo, na mawazo mchana yalinipeleka hukohuko.
Nilijitahidi kupingana na mawazo yangu. Lakini ilikuwa kama nafanya kazi ya kutwanga maji kwenye kinu. Yaani ilikuwa hivi, nikiwa nyumbani sebuleni nikiangalia runinga, watu wakibusiana tu kwenye runinga, mimi mawazo yangu yanaenda kwa Evelyne Gando moja kwa moja. Nikitembea barabarani nikiwaona mwanamke na mwanaume wameshikana mikono tu, mawazo yangu moja kwa moja yalinipeleka kwa Evelyne Gando.
Ndio..nilianza kumpenda Evelyne kimawazo mchana na ndotoni usiku.
Ndoto zangu zote zikabadilika, toka katika vitu nilivyokuwa naviota hapo zamani, sasa zilihamia kwa Evelyne, Evelyne Gando. Shuleni nako nilibadilika. nikaanza kumuonea aibu Evelyne Gando. Yalikuwa mabadiliko yaliyowashangaza sana marafiki zangu, Evelyne Gando na Richard Chali.
Sikuwa naweza kuthubutu kabisa kuangaliana na Evelyne Gando uso kwa uso. Aibu zile wanazokuwa nazo wanawake pindi watongozwapo zikanivamia mimi, tena kwa kasi kubwa sana!
Kutoka mawazoni, kupitia ndotoni, hatimaye ikaja duniani, katika dunia halisi. Ikawa kweli. Nilianza kumpenda kweli Evelyne Gando, na upendo wangu kwake ulizidi kila mshale wa sekunde katika saa ulivyokuwa unasogea. Nilikuwa nampenda sana Evelyne, lakini nilikuwa nampenda kimoyomoyo, hakuna aliyekuwa anajua zaidi ya mimi na moyo wangu. Nikaanza kufikiria namna sahihi ya kuwasilisha hisia zangu za mapenzi kwa Evelyne.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Ilikuwa kazi ngumu kuliko kazi yoyote ile unayoijua wewe hapa duniani. Ngoja nikupe taarifa, hadi naingia kidato cha tano sikuwahi kumtongoza mwanamke yeyote yule hapa duniani. Mimi ni aina ya wale wanaume waitwao domo zege. Nilikuwa mwoga balaa. Pamoja na uwoga wangu lakini sikuwa na jinsi, ilinipasa kumueleza ukweli Evelyne Gando kuwa nilikuwa nampenda. Hisia zangu zilikuwa zinaniambia hivyo, ilikuwa ni ngumu kukaa na hisia hizo moyoni mwangu, hisia zilizokuwa zinaleta humwehumwe kubwa katika moyo wangu, ili kulitoa humwehumwe hilo, ilikuwa ni lazima nimueleze Evelyne kuwa nilikuwa nampenda. Tatizo sasa lilikuwa nitaanzaje?
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment