Simulizi : Mpenzi Wangu Sarafina
Sehemu Ya Tano (5)
Richard alihisi mwili wake ukitetemeka, alihisi kabisa kijasho chembamba kikimtoka. Hakuamini kile alichoambiwa na Ibrahim, alimwangalia kijana huyo, alimwambia kweli kwamba alikuwa na mtoto wake na alitakiwa kuondoka naye na kwenda kumuona.
Richard hakutaka kupoteza muda, hapohapo akawasha gari na kuondoka mahali hapo, ilikuwa ghafla sana kiasi kwamba mpaka polisi wenyewe walishangaa. Alitamani kumpigia simu mke wake na kumwambia kilichokuwa kimetokea lakini wakati mwingine alisita kwa kuona kwamba inawezekana kijana huyo alikuwa akimdanganya.
Hakukuwa na siku ambayo aliendesha gari kwa tahadhali kama siku hiyo, hakutaka kupata tatizo lolote, hiyo ilikuwa nafasi yake ya kumuona mtoto wake, pacha ambaye kila siku alimnyima furaha, pacha ambaye kila siku alimfanya kulia kwa maumivu makali.
Safari ikaishia Magomeni nje ya nyumba moja ya kawaida ambayo kwa kuonekana ilikuwa imejengwa kwa ajili ya kupangishwa tu. Haraka sana akazima gari na kuteremka, alionekana kuwa na haraka hata zaidi ya Ibrahim aliyekuwa amemuita.
Akatangulia ndani, hakujua aingie chumba gani, alijifanya kuwa na haraka kupita kawaida, mwenyeji alikuwa nje, tayari yeye alikuwa ndani, akajikuta amesimama tu ukumbini.
“Yupo wapi?” alimuuliza Ibrahim.
“Subiri kwanza! Hebu njoo ndani,” alisema Ibrahim na kumchukua mwanaume huyo kumpeleka chumbani kwake.
Richard alipoingia tu, akahisi hali ya tofauti, chumba kilikuwa na harufu nzito, kilikuwa shaghalabaghala, kwa jinsi kilivyoonekana ilikuwa ni rahisi kusema kwamba mtu aliyekuwa akiishi humo alikuwa masikini ambaye aliishi chini ya dola moja kwa siku.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Richard akahisi machozi yakianza kujaa machoni mwake na ndani ya sekunde chache yakaanza kutiririka. Moyo wake uliumia, hakuamini kama mtoto wake alikuwa akiishi ndani ya chumba hicho kilichoonekana kutokuwa na hadhi ya kukaliwa na mtu yeyote yule.
“Mtoto wangu yupo wapi?’ aliuliza Richard, mwanaume alikuwa akitiririkwa machozi tu.
Kwanza kabla ya kumwambia mahali alipokuwa mtoto wake, akaanza kumwambia kila kitu kilichokuwa kimetokea siku hiyo, tangu nesi mmoja alipompeleka mtoto wake nyuma ya ofisi ile kulipokuwa na pipa, alipomuona mwanaume akija kwa ajili ya kumchukua na yeye kumuwahi.
“Nashukuru sana! Mtoto wangu yupo wapi?” aliuliza Richard, hakutaka kusikia ilikuwaje mpaka mtoto wake alichukuliwa, alichokihitaji ni kujua mahali alipokuwa.
Ibrahim akatoka ndani ya chumba kile, akamfuata mama Issa ambaye akampa mtoto na kurudi naye chumbani. Richard alikuwa kwenye presha kubwa, mlango ulipofunguliwa, haraka sana akasimama na kuanza kumsogelea Ibrahim.
Alipomfikia, macho yake yakatua kwa mtoto wake, alikuwa amefanana na mtoto aliyekuwa nyumbani kwake, ilikuwa kazi nyepesi kugundua kwamba watoto hao walikuwa mapacha.
Machozi yake yakaongezeka, akamchukua mtoto huyo na kumkumbatia, moyo wake ukawa na furaha, furaha ambayo hakuwahi kuipata tangu siku alipozaliwa ndani ya dunia hii.
Alishindwa kuongea kitu chochote kile, kila alipotaka kuongea, alilia kwa kilio cha kwikwi, ilikuwa ni zaidi ya furaha, wakati mwingine kile kilichokuwa kikiendelea alihisi kwamba alikuwa katika njozi moja ya kusisimua ambapo baada ya dakika kadhaa angeamka na kujikuta akiwa kitandani.
Hakubaki ndani ya chumba hicho, akajikuta akitoka na kuanza kuondoka chumbani humo, alipofika nje, akaingia ndani ya gari lake na kuondoka pasipo kuzungumza lolote na Ibrahim ambaye alibaki akishangaa, ilikuwaje mtu amsaidie kwa kiasi hicho halafu aondoke pasipo hata kumshukuru.
“Tenda wema nenda zako,” alisema Richard, akakaa kitandani, kitu alichokikumbuka kichwani mwake ni msichana Malaika tu.
Hakutaka kuendelea kubaki chumbani humo, haraka sana akasimama na kuondoka, alikuwa na haraka, mpenzi wake ndiye alikuwa kila kitu maishani mwake. Hakuchukua muda mrefu akafika katika hospitali hiyo ambapo akaelekea katika wodi aliyolazwa mpenzi wake.
Hali haikubadilika, madaktari walikata tamaa, kila siku walipokuwa wakimwangalia msichana huyo walijua kabisa kwamba alikuwa akienda kufariki dunia kitandani hapo.
“Dokta! Nini kinaendelea?” aliuliza Ibrahim.
Siku hiyo daktari alibadilika, alionekana kuwa tofauti kabisa na kila alipomwangalia Malaika aliona kifo kikiwa mbele yake. Yeye na madaktari wengine walifanya kazi yao, walimpima Malaika na kugundua kwamba ule ugonjwa wa sickle cell aliokuwa akiumwa, ghafla ulibadilika na kuwa ‘terminal cancer’ ikiwa na maana kwamba ilikuwa ni kansa ambayo ni lazima imuue kitandani.
“Naomba nikwambie kitu kimoja,” alisema daktari huku akimwangalia Ibrahim.
“Kitu gani?” aliuliza Ibrahim.
Daktari huyo alimwambia kwamba mbali na ugonjwa wa sickle cell aliokuwa akiumwa mpenzi wake pia waligundua kwamba damu yake ilianza kushambuliwa na kansa na ndiyo sababu iliyomfanya kuteseka zaidi kitandani.
Hawakujua kansa hiyo ilianzaje, ilikuwa ghafla sana na mbaya zaidi ilivyokuwa imeanza kukomaa, haikuanza kikawaida, ilianza huku ikiwa na nguvu kubwa ya kuyapoteza maisha yake.
“Ni habari mbaya. Mwenzio amepata ugonjwa wa kansa ya damu, mbaya zaidi imekuwa terminal cancer,” alisema daktari huyo.
“Hiyo terminal ndiyo kitu gani hicho?”
“Ni kansa ambayo ni lazima afe, hawezi kupona kamwe. Mpenzi wako amebakiza miezi mitatu tu ya kuishi, baada ya hapo, atakufa, hatoweza kuishi tena,” alisema daktari huku akimwangalia Ibrahim.
“Unasemaje?”
“Mwenzio atakufa ndani ya miezi mitatu tu. Kansa hii imeharibu mfumo mzima wa damu mwilini mwake,” alisema daktari huyo.
“Yaani unamaanisha kwamba mbali na sickle cell pia ameanza kuumwa kansa?” aliuliza Ibrahim.
“Ndiyo! Tulishindwa kufahamu kabla juu ya kansa hiyo, ilijificha na ninahisi ni tatizo ambalo linawatokea watu wengi tu. Ila ukweli ni kwamba mwenzio ana terminal cancer, ni mbaya sana, huwa ikija inakuja na muda wa kuishi, wengine hupewa miaka miwili, wengine mitatu, wengine mwaka na wengine hata mwezi. Kwa hii aliyokuwa nayo mwenzio imebakiza miezi mitatu tu ya kuishi,” alisema daktari huyo.
“Miezi mitatu?”
“Ndiyo!”
“Dokta! Hebu niambie ukweli kwanza, sijasikia! Umesema Malaika amebakiza miezi mitatu?” aliuliza Ibrahim.
“Ndiyo!”
“Ya kuishi?”
“Ndiyo!”
Akasikia kitu kikali kikiuchoma moyo wake, hakuamini kile alichokisikia, akajikuta akisimama na kuanza kuelekea kule alipokuwa Malaika, alikuwa akitembea huku akipepesuka, alihisi kabisa mwili wake ukianza kuishiwa nguvu, alipofika huko, akasimama pembeni ya kitanda chake, moyo wake ulikuwa na maumivu makali, alimwangalia mpenzi wake pale kitandani alipokuwa, hakuamini kama alikuwa njiani kumpoteza mpenzi wake huyo ambaye kwake alikuwa kila kitu.
“Terminal cancer…hawezi kuishi zaidi ya miezi mitatu lazima atakufa,” aliisikia sauti ya daktari moyoni mwake.
Malaika alikuwa kimya, aliyafumba macho yake lakini baada ya kuhisi kwamba kulikuwa na mtu amesimama mbele yake, akayafumbua macho na kumwangalia mtu huyo, akatoa tabasamu pana kwani mtu aliyekuwa amesimama alikuwa Ibrahim, mwanaume aliyekuwa muhimu sana katika maisha yake.
“Ibrahim! Mungu atatenda maajabu!” alisema Malaika huku akimwangalia Ibrahim ambaye alikuwa kimya tu.
“Najua unahuzunika! Nimeambiwa kwamba nimepatwa na kansa na nitakufa ndani ya miezi mitatu. Ibrahim, huu ndiyo muujiza ambao nimekuwa nikikwambia, hii kansa ndiyo muujiza ambao Mungu aliniotesha kwamba nitakutana nao,” alisema malaika huku akimwangalia Ibrahim.
“Unaumwa kansa Malaika! Si sickle cell tena! Kwa nini Mungu anafanya yote haya?” aliuliza Ibrahim.
“Kwa sababu anataka kuniponya!”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Kukuponya! Kukuponyaje?” aliuliza Ibrahim.
“Sijajua lakini nahisi hii ndiyo nafasi ya Mungu kujionyesha kwamba Yeye ni Mungu asiyeshindwa,” alisema Malaika kitandani pale ambapo alikuwa amekonda kupita kawaida.
Maneno yake yalikuwa hayohayo, alikuwa akijitia imani kila siku kwamba Mungu angekwenda kumponya. Aliendelea kubaki hospitalini hapo na baada ya wiki moja madaktari wakamwambia Ibrahim kwamba kiasi cha fedha alichokuwa akidaiwa kilikuwa kikubwa, asingeweza kulipia lakini wakamtaka kumchukua Malaika na kurudi naye nyumbani ili akamtibu hukohuko nyumbani.
Hakuwa na jinsi, akamchukua Malaika wake na kurudi naye nyumbani kwake ambapo akaanza kumpa matibabu hukohuko, akaanza kumnunulia dawa na kumuhudumia kwa kila kitu kama alivyokuwa akiambiwa.
Mwili wa Malaika ukazidi kukongoroka, akabaki mifupa mitupu, kansa ya damu ikaanza kumtesa, mwili ukapauka na wakati mwingine akaanza kutoka damu puani na masikioni, ngozi yake ikashindwa kupambana na ugonjwa huo, ikaanza kusinyaa, ikaanza kutoa vipele vilivyokuwa vikimuwasha usiku na mchana, alipoanza kuvikuna, vikatumbuka na kuanza kutengeneza vidonda mwilini mwake, vidonda vilivyokuwa vikimuuma na kumfanya kupiga kelele usiku.
“Ibrahim mpenzi! Ninakufa…” alisema Malaika huku akilia kitandani pale.
“Malaika! Kumbuka uliniambiaje! Kumbuka maneno uliyosema kwamba Mungu atakuponya. Mpenzi utapona, utapona, hautokufa! Nakwambia hautokufa,” alisema Ibrahim huku akimwangalia mpenzi wake huyo pale kitandani.
Kila siku ikawa mateso juu ya mateso, vidonda vile vilivyosababishwa na vipele viliendelea kumuuma zaidi, akawa mtu wa kulia, vikatoa damu na mwisho wa siku hali kubadilika na kutoa usaha kitu kilichosababisha harufu kali ndani ya chumba hicho.
“Mmh! Kuna panya ameoza au kuna maiti humu ndani?’ alisikika akiuliza mwanamke mmoja ndani ya nyumba hiyo.
Mwili wa Malaika ukazidi kutoa harufu kali ambayo iliwafanya wapangaji wengi kuanza kulalamika ndani ya nyumba hiyo kwamba iweje wakae na maiti ndani iliyokuwa imeoza na kunuka, wengi wakamtaka Ibrahim kwenda kumzika Malaika kwani tayari alikuwa amekufa na ndiyo maana mwili wake ulikuwa ukitoa harufu mbaya kama kitu kilichooza.
Kwa Ibrahim, ni kama pua zake ziliziba, chumba kizima kilikuwa na harufu mbaya lakini hakusikia hata kidogo. Kila siku alikaa chumbani humo, mpenzi wake alionekana kukata tamaa, mwili wake ulizidi kuisha na vidonda vilimtesa kupita kawaida.
Hakuondoka chumbani, hakumkimbia, kila siku alipambana naye pamoja, alimtia nguvu na kumwambia kwamba kuna siku angepokea uponyaji na Mungu aliyaandaa maisha mazuri kwa ajili yake.
Malaika alilia na kulia, hakuwa na nguvu, kila alipomwangalia Ibrahim, aliyaona kabisa mapenzi ya mwanaume huyo, jinsi alivyompenda kiasi kwamba hakuwa tayari kumkimbia kwa kuwa tu alikuwa akitoa harufu mbaya.
Imani yake iliyoanza kuyumba kipindi cha nyuma ikaanza kurudi tena, alimwamini Mungu kwamba kuna siku angeweza kusimama tena, kutembea na kufanya mambo mengine kama kipindi cha nyuma.
Hakujua sababu ya Mungu kumpitisha katika maisha hayo, yalikuwa ni maisha yaliyoumiza mno, maisha ambayo yalimfanya kila siku kuona muda wowote ule angekufa kama alivyokufa mama yake. Hakuona kama angepokea tumaini lolote lile, alijua kabisa kwamba hizo ndizo zilikuwa siku za mwisho za uhai wake.
“Ibrahim mpenzi!” aliita Malaika huku akimwangalia mwanaume huyo.
“Ndiyo mpenzi!”
“Unaamini pamoja na mimi kwamba nitapona?” aliuliza Malaika huku akimwangalia Ibrahim, kwa kukiangalia kitanda harakaharaka, tena katika kipindi ambacho Malaika alikuwa amejifunika shuka, ilikuwa vigumu kuamini kama kitandani hapo kulikuwa na mtu kwa jinsi alivyokonda na kubaki mifupa mitupu.
“Ninaamini kwamba Mungu atakuponya! Huwezi kufa Malaika,” alisema Ibrahim huku machozi yakimtoka, alikosa tumaini, hakujua ni kwa jinsi gani angeweza kumsaidia msichana huyo maishani mwake.
“Hata mimi naamini nitapona. SITOKUFA BALI NITAISHI,” alisema Malaika kwa imani kubwa kutoka moyoni mwake, kama Mungu alikuwa akitenda miujiza kwa kuwa tu watu waliamini, aliamini kwamba hata yeye pia angeweza kumfanyia muujiza huo.
Kila siku wapangaji walikuwa watu wa kulalamika, walimlalamikia mwenye nyumba kwamba Malaika hakutakiwa kuishi ndani ya nyumba hiyo kwani kwa jinsi alivyokuwa akinuka, ilikuwa ni balaa tupu.
Mwenye nyumba hakutaka kuwasikiliza, aliyajua maisha ya msichana huyo, jinsi alivyokuwa akiteseka lakini zaidi alijua maisha ya Ibrahim, alikuwa akimpenda Malaika kiasi kwamba hakutaka kusikia lolote lile kutoka kwa mtu yeyote.
Kila siku ndani ya nyumba kulikuwa na kelele kiasi kwamba baadhi ya wapangaji wakatishia kuhama nyumba hiyo kwani mateso yalizidi, harufu kali iliendelea kuzitesa pua zao kila siku.
Mwenye nyumba hakuwa radhi kuona akipoteza wapangaji kwa ajili ya mpangaji mmoja tu, hivyo alichokifanya ni kumfuata Ibrahim na kuzungumza naye.
Alimwambia hali halisi, jinsi wapangaji wenzake walivyokuwa wakilalamika kimyakimya kwamba mpenzi wake alizidi kutoa harufu kiasi kwamba hata kama utapika pilau, harufu ya pilau haisikiki zaidi ya harufu mbaya ya mwili wa Malaika.
“Mzee! Sina pesa yoyote ile, tutaishi wapi?’ aliuliza Ibrahim huku akimwangalia baba mwenye nyumba.
“Popote pale lakini si hapa. Ibrahim, si kwamba mimi ndiye nawafukuza, ninalazimishwa, ninafanya hivi huku nikiumia sana, hasa hali aliyokuwa nayo mwenzio, hakika inaniumiza sana,” alisema mzee huyo huku akimwangalia Malaika, kwa jinsi alivyokuwa kitandani pale, ilionekana kama angeishi mpaka siku inayofuata basi alitakiwa kumshukuru sana Mungu.
“Mzee! Nipo kwenye wakati mgumu sana. Unaweza kutupa hata mwezi mmoja?” aliuliza Ibrahim.
“Mwezi mmoja? Kwa jinsi hawa watu walivyokuwa na kelele, hata wakijua nimewapa siku mbili, maneno mengi,” alisema mzee huyo.
Aliumia lakini hakuwa na jinsi, alimwangalia mpenzi wake, Ibrahim akashindwa kuvumilia, akaanza kulia kwa sauti, aliumia moyoni mwake, hakuamini kama kweli alikuwa akipitia maisha hayo, mpenzi wake aliteseka, mpenzi wake alikuwa hoi, mpenzi wake alikaribia kufa, mpenzi wake huyo alikuwa na siku chache za kuishi dunia.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Siku iliyofuata, akaamua kuondoka nyumbani hapo, hakujua ni mahali gani alitakiwa kwenda, aliuchukua mkeka tu, mpenzi wake, Malaika hakuweza kutembea, alimbeba mgongoni, alipotoka ndani tu, watu wote waliokuwa nje wakaziba pua zao kwani harufu iliyokuwa ikisikika ilinuka mno.
Nzi wakaanza kumfuata Malaika aliyekuwa mgongoni, kila mtu alikuwa akishangaa, wengine wakahisi kwamba Ibrahim alikuwa amebeba maiti ambayo ilianza kuharibika, wengine wakaelekea msikitini na kuleta jeneza kwani walihisi kwamba ile iliyokuwa imebebwa ilikuwa maiti.
“Tukaizike! Utatembeaje na maiti?” aliuliza jamaa mmoja, alikuwa mtu mwema, hakujua kama mtu aliyebebwa alikuwa mzima kabisa.
“Mpenzi wangu yupo hai. Mungu atamponya!”
“Yupo hai huyu?”
“Ndiyo! Mungu atampa mwili mpya, kama binadamu tunakuwa na spea taili, kwamba kama taili hili likiharibika linawekwa jingine, unafikiri Mungu katuumba bila kutuwekea spea nyingine? Mwili huu ukichoka, Mungu anautoa na kuweka mwingine. Mpenzi wangu atapona tu,” alisema Ibrahim kwa ujasiri na imani kubwa.
Akaondoka na kuelekea Tandale. Njia nzima alipokuwa akipita watu waliziba pua zao, Malaika alikuwa akinuka sana, vidonda viliendelea kumuuma na muda mwingi pale mgongoni alipokuwa amebebwa alikuwa akilia kama mtoto mdogo.
Hawakujua ni mahali gani walitakiwa kwenda kuishi, alichokifanya Ibrahim ni kwenda Tandale katika Mto wa Ng’ombe, pembezoni mwa mto huo na kujenga kibanda fulani kidogo ambacho hakikuonekana kuwa na nguvu, alichomeka miti na kukizungushia magunia, akaingia ndani na kuanza kuishi na Malaika.
Yalikuwa ni maisha yaliyoumiza sana, hakuwa na kiasi kikubwa cha fedha, hichohicho kidogo alichokuwa nacho ndicho ambacho alikitumia kununua chakula na dawa ambazo kila siku ilikuwa ni lazima Malaika apakwe katika vidonda vyake.
“Malaika! Hapa ndiyo kwetu! Tutaishi mpaka hapo Mungu atakapoona imetosha,” alisema Ibrahim huku akimwangalia Malaika aliyeitikia tu. Huku wakiwa wanazungumza ghafla Malaika akaanza kusikia baridi kali.
Akaanza kupiga kelele kwa maumivu makali, alimwambia Ibrahim kwamba alikuwa akisikia maumivu makali ambayo hakuwahi kuyasikia kabla. Ibrahim akamsogelea, akamshika kichwa, joto la mwili wake lilibadilika na kuwa la juu kabisa.
Palepale chini akaanza kurusha miguu na mikono yake huku na kule kama mtu aliyekuwa akikaribia kukata roho. Ibrahim alichanganyikiwa, alimuita Malaika kwa sauti kubwa, hakutaka kuona msichana huyo akifa, hakutaka kuona msichana huyo akimuacha peke yake.
“Usiniache mpenzi! Naomba usiniache! Usife mpenzi! Ninakupenda naomba usife. Mungu naomba usimchukue Malaika wangu, chukua chochote kile lakini niachie Malaika wangu,” alisema Ibrahim huku akijaribu kuzuia kilichotaka kutokea.
Hapohapo, ghafla sana Malaika akatulia, joto la mwili likazidi kupanda, mwili ukanyooka na kutulia tuli.
“Malaikaaaaaaaaa…..” aliita Ibrahim kwa sauti kubwa huku akijaribu kumuamsha mpenzi wake lakini hakuamka, hata macho yake yalifumba.
***
Richard alikuwa njiani akielekea nyumbani kwake, hakuamini kilichokuwa kimetokea, mtoto wake mpendwa alikuwa mapajani mwake. Hakutaka kumpigia simu mke wake na kumwambia kilichokuwa kimetokea, alitaka kumsapraizi kwani aliamini kwamba kile kingekuwa kitu ambacho kingempa furaha maisha yake yote.
Aliendesha gari kwa umakini mkubwa na baada ya dakika kadhaa akafika nyumbani kwake ambapo mlinzi akafungua geti na kuteremka. Akaanza kuelekea ndani, akamkuta mke wake akiwa sebuleni akimnyonyesha mtoto.
Akasimama, akamwangalia huku akitoa tabasamu. Bianca akashtuka, hakujua ni kitu gani kilikuwa kikiendelea, akamsogelea mume wake ambaye alimuonyeshea mtoto yule. Kitendo cha Bianca kutua macho yake kwa mtoto yule, moyo wake ukapiga paaa kwani alifanana na mtoto aliyekuwa akimnyonyesha.
“Is this my baby?” (huyu ni mtoto wangu?) aliuliza Bianca huku akiwa haamini.
“He is the one,” (ndiye yeye)
“Where did you get him?” (umempata wapi?) aliuliza Bianca huku akimchukua.
Hakuamini macho yake, machozi ya furaha yaliyochanganyikana na uchungu yakaanza kujikusanya machoni mwake na kuanza kulia. Alijisikia hali ya tofauti kabisa, hakuamini kile kilichotokea, alijua kwamba asingeweza kumuona tena mtoto wake, alikata tamaa na kumwachia Mungu kumbe upande wa pili bado Mungu alikuwa akiendelea kufanya kazi yake.
Kila mmoja alikuwa na furaha tele, Bianca akashindwa kuvumilia, akawapigia simu marafiki zake na kuwaambia kwamba alimpata mtoto wake, ni kwamba Mungu alikuwa upande wake na alimpigiania.
Wote walifurahi, furaha ikarudi ndani ya nyuma. Richard hakukumbuka chochote kuhusu Ibrahim, kwake maisha yalikuwa yakiendelea kama kawaida. Siku moja baada ya kukaa ofisini na kuanza kuyakumbuka maisha yake ya nyuma ndipo akakumbuka namna alivyompata mtoto wake.
Moyo wake ukauma, hakuamini kama yeye ndiye aliyefanya ujinga ule, kuondoka chumbani kwa Ibrahim pasipo hata kumshukuru na wakati yeye ndiye aliyemsaidia kumpata mtoto huyo, ndiye alikuwa kijana aliyemuiba mtoto kule nesi alipomficha, kwa maana hiyo alikuwa na uwezo wa kumfanya chochote mtoto yule.
Moyo wake ukamuhukumu, hakuwa amefanya utu, alisikia maumivu mazito moyoni mwake, aliumia kupita kawaida na kujiona akiwa mkosaji mkubwa ndani ya dunia hii.
Hapohapo akachukua simu yake na kumpigia mke wake, alipopokea, akaanza kumwambia jinsi alivyompata mtoto, hakumficha, alimwambia ukweli kwamba alishindwa kumshukuru kijana yule, hivyo akaondoka zake huku akiwa na mtoto.
“Hukumshukuru?” aliuliza Bianca huku akishangaa.
“Mke wangu! Nilizidiwa na furaha, nilitaka kuzungumza, nikashindwa, kiukweli nilifanya kosa kubwa sana,” alisema Richard huku simu ikiwa sikioni mwake.
Bianca akamwambia kwamba ilikuwa ni lazima waelekee huko kwa ajili ya kumshukuru kijana huyo kwani kwa kile alichokuwa amekifanya kilikuwa ni kitu kikubwa ambacho hata kama wangempa milioni mia moja bado kusingelingana na kile alichokuwa amekifanya.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Richard hakutaka kubaki ofisini, akatoka, akachukua gari lake na kumpitia mke wake ambapo moja kwa moja wakaanza safari ya kuelekea huko. Njiani, walizungumza sana, Richard aliendelea kuhuzunika moyoni mwake, hakuamini kama aliweza kufanya jambo kama lile, alitakiwa kuonyesha shukrani, alitakiwa kumuonyeshea kijana yule dalili zote za kumshukuru kwa kile alichokuwa amekifanya.
Hawakuchukua muda mwingi wakafika Magomeni ambapo moja kwa moja wakapaki gari na kuelekea ndani ya nyumba ile. Hakukuwa na mtu ila kwa kuwa Richard alikuwa akikifahamu chumba, akaelekea na kuugonga mlango ule ambapo baada ya sekunde chache, mlango ukafunguliwa na mwanamke mmoja mweupe aliyejichubua kufungua mlango.
“Kuna mtu namuulizia,” alisema Ricard mara baada ya salamu.
“Nani?”
“Anaishi katika chumba hiki,” alisema Richard.
“Humu haishi mwanaume. Nimepanga mimi tu,” alijibu msichana huyo.
Richard alishangaa, alihisi kwamba alikosea chumba, akaangalia vyumba vyote na kuvihesabu, kilikuwa chumba kilekile. Wakati wakiwa wamesimama hapo baba mwenye nyuma akatokea na mwanamke yule kumwambia kile kilichokuwa kimetokea.
“Hebu njooni huku,” alisema baba mwenye nyumba ambapo akawapeleka nje ya nyumba ile na kuanza kuzungumza nao.
Alijua aliokuwa akiwaulizia, aliwaambia kwamba mtu huyo hakuwepo nyumbani hapo, hakuishia hapo, aliwahadithia kila kitu kilichokuwa kimetokea, kwamba Ibrahim alikuwa akiishi na msichana mmoja ndani ya chumba kile, msichana mgonjwa aliyekuwa hoi, mwili kuharibika na kutoa harufu chafu.
Ilikuwa simulizi ya kusisimua ambapo Richard na mkewe wakabaki wakitokwa na machozi, hawakuamini kile walichokuwa wakikisikia kwamba mtu aliyekuwa akiwasaidia alikuwa na mpenzi aliyekuwa kwenye hali mbaya, na mbaya zaidi hakuwa na pesa, aliteseka, maisha yaliwapiga mno.
Moyo wa Richard ukazidi kuumia zaidi, alijiona kufanya kosa kubwa, alikuwa na uwezo mkubwa wa kumsaidia msichana huyo na hata kama alibakiza miezi mitatu ya kuishi, aliona kabisa kwamba angejitahidi sana kumuhudumia kama shukrani yake kwa Ibrahim mpaka siku ambayo angefariki dunia.
“Baada ya kuhama walihamia wapi?’ aliuliza Richard huku machozi yakitiririka mashavuni mwake.
“Waliondoka! Taarifa za chini nilisikia wakiishi Tandale, kando ya Mto wa Ng’ombe, Ibrahim alijenga kibanda hapo lakini….” Alisema baba mwenye nyumba na kunyamaza.
“Lakini nini?”
“Yule mpenzi wake alifariki dunia katika maumivu makali sana,” alisema baba mwenye nyumba, yeye mwenyewe akashindwa kuvumilia, machozi yakaanza kumlenga.
“Alifariki dunia?”
“Ndiyo! Ilikuwa juzi ndiyo nilipata taarifa hiyo na watu kwenda kumzika katika makaburi ya Kwa Ally Maua,” alisema baba mwenye nyumba. Bianca akashindwa kuvumilia, akaelekea ndani ya gari na kuanza kulia kama mtoto kana kwamba msichana aliyekufa alikuwa mdogo wake wa damu.
Watu wote duniani macho na masikio yao yalikuwa nchini Marekani kulipokuwa na uchaguzi mkuu mwaka huo ambapo kwa kipindi hicho kampeni zilikuwa zikifanyika kila kona.
Wagombea wengi walisimama majukwaani kwa ajili ya kuwaambia wananchi kile ambacho wangekifanya endapo tu wangepewa nafasi ya kuchukua nchi hiyo. Wamarekani walichoka, wengi walikasirika baada ya kuona wanajeshi wakiondolewa katika familia zao na kupelekwa katika nchi za Kiarabu kwa ajili ya kulinda amani za nchi hiyo.
Wamarekani wengi wakatamani Kendrich August kutoka katika Chama cha Democratic awe rais wa nchi hiyo kwani sera kubwa ya chama hicho ilikuwa ni kutaka kuwazuia wanajeshi kuondoka nchini mwao na kuelekea katika nchi za Kiarabu ambapo huko kila siku walikuwa wakiuawa.
Mioyo ya Wamarekani ikawa na maumivu makali, hawakutaka kuona ndugu zao wakielekea katika nchi hizo kitu ambacho kiliwafanya kuamua kwa moyo mmoja, tena kwa kuungana kuhakikisha chama hicho kinaingia madarakani na Kendrich anakuwa rais wa nchi hiyo.
Kila kona watu walikuwa wakizungumzia uchaguzi huo, ulikuwa uchaguzi ulioshika vichwa vingi vya habari, mashirika ya habari dunia yalikuwa yakiendelea kuripoti kila kitu kilichokuwa kikiendelea nchini humo hasa kwa upande wa Kendrich ambaye kwa kipindi hicho alikuwa mtu wa watu, aliyependwa na watu wa rika zote kuanzia watoto mpaka watu wazima.
Katika kila jimbo alilokwenda nchini humo alipokelewa kwa shangwe, watu walimpenda, picha zake zilisambazwa kila kona, wengine wakashindwa kuvumilia, kila alipokuwa akifika katika jimbo moja, huduma zote siku hiyo zilikuwa hazifanyi kazi, kila kitu kilifungwa mpaka pale ambapo alimaliza kufanya kampeni na kuondoka jimboni humo.
“This is the man of Almighty God,” (huyu ni mtu wa Mungu mwenye nguvu) alisema jamaa mmoja.
“Sure he is,” (kweli kabisa)
Alizunguka katika majimbo mbalimbali, kila alipokwenda kuliwekwa ulinzi mkubwa, hakukuwa na mtu aliyemsogelea kwani mbali na kupendwa huko lakini bado kulikuwa na watu waliokuwa wakimchukia, hasa Warusi ambao waliweka wazi kwamba hawakutaka kuona Kendrich akiingia madarakani, mtu waliyekuwa wakimtaka alikuwa Paul Poulsen kutoka katika Chama cha Republic.
Kwa sababu alikuwa mgombea mwenye nguvu, hata waandishi wa habari wengi walikusanyika katika mikutano yake. Kendrich alipokuwa akisimama, alizungumza kama mtu aliyekuwa akijiamini ambaye alikuwa na uhakika wa kushinda uchaguzi huo.
Siku zikakatika mpaka siku ya mwisho wa kampeni ambazo zilitakiwa kufanyika katika Jimbo la Ohio lililokuwa hapohapo nchini Marekani. Siku hiyo, kila kitu kilichokuwa kikiendelea jimboni humo kilisimamishwa, kila mmoja alitaka kumsikiliza Kendrich kwani mbali na kuwa mgombea lakini pia alikuwa mtu wao, alizaliwa, alikulia na kusomea ndani ya jimbo hilo.
Siku hiyo ilikuwa kizaazaa, ofisi nyingi zikafungwa, hakutakiwa mtu yeyote kufanya kazi. Sehemu ambayo Kendrich alitakiwa kufanya kampeni kuliandaliwa na kuwekewa ulinzi mkubwa kuhakikisha kila kitu kinakwenda sawa, kampeni ziishe na hatimaye nchi kuingia katika uchaguzi mwingine na kuona ni nani angepewa kijiti cha kuiongoza nchi hiyo kwa miaka minne.
Ratiba ambayo ilipangwa ilionyesha kwamba Kendrich alitakiwa kusimama kuanzia saa 10:30 jioni lakini mpaka inafika saa 7:00, uwanjani hapo walikuwa wamejazana na wengi wao walikuwa na fulana zilizokuwa na picha yake.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Waandishi wa habari walikuwa kila kona wakiripoti kila kitu kilichokuwa kikiendelea mahali hapo. Kila mmoja alitaka kujua ni mambo gani ambayo Kendrich angeyazungumza siku hiyo, kampeni yake tu ya kusema kwamba wanajeshi wasingekwenda tena Uarabuni ndiyo iliyowafurahisha zaidi Wamarekani wengi.
Ilipofika saa 9:45 gari magari yakaanza kuingia mahali hapo, watu wakaanza kushangilia kana kwamba tayari mtu huyo alikuwa ametangazwa kuwa rais wa nchi hiyo. Waandishi wa habari wakajisogeza na kuanza kuupiga picha msafara uliokuwa ukija na mtu huyo.
“Take the pictures,” (piga picha) ilisikika sauti ya msichana mmoja, alikuwa na koti lililoandikwa CNN kwa nyuma, msichana huyu aliitwa Amanda Penn, msichana mrembo aliyefanya kazi hiyo kwa miaka miwili.
Alikuwa na mwandishi mwenzake mahali hapo, kazi yake kubwa ilikuwa ni kuwahoji watu na kuwaambia watazamaji kila kitu kilichokuwa kikiendelea huku mwenzake akipiga picha matukio yaliyokuwa yakiendelea mahali hapo.
Baada ya dakika kadhaa, msafara ule ukasimama na Kendrich kuteremka kitu kilichowafanya watu wengi kupiga makofi ya shangwe. Mwanaume huyo akawapungia mikono watu, tabasamu pana lilikuwa likionekana usoni mwake lakini wakati akipiga hatua kuelekea sehemu zilizokuwa na viti, ghafla watu wakashtuka kuona mwanaume huyo akianguka chini, damu zikatapakaa kifuani mwake, risasi iliyopigwa ikapenya kifuani mwake.
Watu hawakuamini kile walichokiona, kila mmoja akashtuka, haraka sana polisi waliokuwa mahali hapo wakaangalia huku na kule, wakabahatika kuona dirisha likiwa wazi katika ghorofa moja ambalo halikuwa mbali kutoka mahali hapo, wakagundua kwamba mtu aliyepiga risasi alikuwa ndani ya chumba kile, hivyo wakaanza kwenda kule.
Kila mmoja alishangaa, Kendrich alikuwa chini, alikuwa akihangaika kuiokoa roho yake, waandishi wa habari waliendelea kupiga picha kila kitu, wanaume wawili wakamnyanyua, wakamuingiza ndani ya gari na kuanza kuondoka naye.
Amanda hakutaka kubaki mahali hapo, ilikuwa ni lazima kufuatilia kila kitu kilichokuwa kikiendelea. Akaingia ndani ya gari na mwandishi mwenzake na kuanza kuelekea katika Hospitali ya Ohio Health Dublin Methodist.
Tukio hilo lilikuwa kubwa, lilimgusa kila mtu, wengi waliongea yao, wengine wakahisi kabisa kwamba kila kitu kilichokuwa kimepengwa, kilipangwa na Warusi ambao waliahidi kwamba ni lazima wafanye jambo kuhakikisha mwanaume huyo haingii ikulu.
Hawakuchukua muda mwingi, wakafika mahali hapo. Kendrich alikuwa amekwishafikishwa, aliteremshwa, akawekwa juu ya machela na kuanza kuingizwa ndani. Hata kabla watu wengine hawajaingia ndani, Amanda akasimama, akaliona gari moja la wagonjwa likiingia mahali hapo, alitaka kuondoka kuelekea ndani ila moyo wake ukaa mzito kufanya hivyo, akajikuta akianza kulisogelea gari lile.
“Amanda, let’s get inside,” (Amanda, twende ndani) alisema mwandishi mwenzake aliyeitwa Henry.
“No! Just wait,” (hapana! Subiri kwanza)
Mlango wa gari lile ukafunguliwa, machela ikashushwa kutoka ndani ya gari lile, alipoangalia juu ya machela ile, macho yake yakatua kwa mgonjwa aliyekuwa hoi, alikonda mno, alionekana kama mfu pale alipokuwa, dripu ilikuwa juu yake na mwili wake ulikuwa na vidonda vingi.
“What the hell with her?” (nini kimempata?) alijikuta akiuliza Amanda huku akimwangalia mgonjwa huo. Alishangaa, ni kweli aliwahi kukutana na wagonjwa wengi lakini wa siku hiyo alionekana kuwa tofauti na wengine.
“She is very sick,” (anaumwa sana) alijibu daktari mmoja.
“What?” (nini)
“Sickle Cell and Leukemia.”
“Ooh! My God!” (Ooh Mungu wangu!) alisema huku akishangaa.
Wakati akiuliza maswali hayo, mlango wa mbele ukafunguliwa na wanaume wawili kuteremka, mmoja alivalia suti na mwingine alikuwa katika mavazi ya kawaida. Kichwa chake kikamwambia kwamba watu hao ndiyo walikuwa ndugu wa mgonjwa huo.
Hakuamini kama mtu aliyekuwa akiumwa kansa ya damu na sickle cell angekuwa katika hali aliyokuwa nayo mgonjwa yule, alishangaa, alitaka kujua mengi kwani aliona kabisa kulikuwa na kitu zaidi ya hicho kilichokuwa kikiendelea.
Hakutaka kusimama, kwa kuwa alikuwa na kiu kubwa akaanza kuwafuatilia watu hao, alitaka kujua ni kitu gani kilichokuwa kimetokea. Machela ikasukumwa mpaka katika chumba cha upasuaji, akabaki nje na wanaume wale.
Alitamani kufahamu kilichokuwa kimetokea, alisahau kabisa kuhusu Kendrich, upepo ulibadilika na alichotaka kujua zaidi kilikuwa ni kuhusu mgonjwa yule.
Alitaka kuzungumza na wanaume wale lakini kila mmoja akaonekana kuwa na mawazo tele, hakujua ni kwa jinsi gani alitakiwa kuzungumza nao, alibaki kimya kwa muda lakini baada ya dakika tano kupita, akamsogelea mmoja.
“I’m a journalist from CNN! My name is Amanda,” (mimi ni mwandishi wa habari kutoka CNN, naitwa Amanda) alijitambulisha.
“Ok! I’m glad to know you. My name is Richard and this is Ibrahim. We are from Africa, Tanzania,” (sawa. Nashukuru kukufahamu. Mimi naitwa Richard, huyu ni mwenzangu anaitwa Ibrahim, tumetoka Afrika, nchini Tanzania,” alijibu mwanaume huyo huku akionekana kuwa bize.
****
Ibrahim alibaki akimwangalia Malaika aliyekuwa chini pembezoni mwa mto wa Ng’ombe, aliendelea kumuita mpenzi wake huyo lakini hakuyafumbua macho yake. Moyo wake ulimwambia kwamba tayari alifariki dunia na kamwe asingeweza kuamka tena.
Alikuwa akilia, machozi yakaanza kutiririka mashavuni mwake na kitu pekee ambacho kilimwambia kwamba binti huyo hakuwa amekufa yalikuwa ni mapigo ya moyo ambayo yalikuwa yakidunda kwa mbali mno.
Wakati akiendelea kumuita Malaika, mawingu mazito yakaanza kutanda angani na ndani ya dakika mbili tu, mvua kubwa ikaanza kunyesha. Alishangaa, si yeye tu bali hata watu wengine walishangaa, hawakuamini kama Dar es Salaam kungekuwa na mvua ya ghafla kiasi hicho, tena ilikuwa mvua kubwa ambayo iliufanya mto ule kuanza kujaa maji.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Haraka sana akachomoka mahali hapo, ilikuwa ni lazima atafute msaada. Akaanza kwenda katika nyumba moja baada ya nyingine kuomba msaada lakini hakukuwa na mtu aliyemsikiliza kwani muonekano wake tu ulionyesha kwamba alikuwa kibaka, na mbaya zaidi hata machozi yaliyokuwa yakimtoka hayakuonekana kwani yalifichwa na maji yaliyokuwa yamemlowanisha.
Hakurudi nyuma, alikuwa akienda nyumba moja mpaka nyingine kuomba msaada. Mvua iliendelea kuwa kubwa, wenye vyoo vyao, wakavifungulia na kuanza kutoa maji machafu. Mto ule uliendelea kujaa, ulifurika maji mpaka katika kibanda kile alicholala Malaika na kusombwa na maji.
Yote hayo yaliyokuwa yakiendelea, Ibrahim hakuyaona, aliendelea kuomba msaada kutoka nyumba moja na nyingine, alitaka kusaidiwa hata dawa kwani hali aliyokuwa nayo Malaika haikuwa ya kawaida tu.
Alikosa msaada kitu kilichomfanya kuanza kurudi kule katika kile kibanda alichomuacha mpenzi wake. Alipofika, kitu cha ajabu kabisa kibanda hakikuwepo, si hicho tu bali hata Malaika hakuwepo. Alichanganyikiwa, akaanza kuangalia huku na kule, akaanza kuita, hakujua mpenzi wake alikuwa amekwenda wapi.
Kwa kuwa maji yalikuwa yakielekea upande wa kushoto, akaingia katika mto ule na kuanza kuogelea kwani aliamini kwamba maji hayo ndiyo yaliyomchukua Malaika.
Hali ilikuwa mbaya, maji yalikuwa machafu lakini yote hayo Ibrahim hakutaka kujali, alichokuwa akikihitaji kilikuwa ni mpenzi wake tu. Wakati mwingine alipishana na haja kubwa kutoka katika vyoo mbalimbali, hakujali, alikutana na uchafu wa kila aina lakini kwake kila kitu kilionekana si kitu.
Aliogelea kwa umbali kama wa mita hamsini ndipo akafanikiwa kumuona msichana huyo akielea juu ya maji ya mto ule huku mvua ikizidi kuendelea kunyesha kwa kasi.
Akapiga mbizi zaidi, baada ya dakika mbili, akamfikiria Malaika, haraka sana akamshika mkono na kuanza kumvuta pembeni. Malaika aliyafumbua macho yake, alikuwa akiangalia huku na kule lakini alishindwa kujitingisha na hata alipokuwa akivutwa, alimwangalia tu mpenzi wake.
Akamtoa majini na kumlaza kwenye tope jingi, pale alipokuwa hakukuwa mbali kutoka kwenye makaburi ya msikiti wa Kwa Ali Maua. Akamwangalia mpenzi wake, alikuwa akimwangalia lakini kitu cha ajabu kabisa kilichomshangaza, msichana huyo alikuwa akitabasamu tu kana kwamba alikuwa akilifurahia lile lililokuwa likiendelea.
“Mbona unatabasamu?” aliuliza Ibrahim kwa sauti ya chini.
Msichana huyo akamjibu lakini sauti yake haikutoka kama inavyotakiwa, ilikuwa ni ya chini mno kiasi kwamba Ibrahim akasogeza sikio lake kumsikiliza msichana huyo.
“Mungu ameleta mvua,” alijibu Malaika huku akiendelea kuonyesha tabasamu pana.
“Sijakuelewa!”
“Mwili ulichemka, Mungu ameupoza kwa kuleta mvua. Ibrahim, nakwambia kwamba Mungu ana makusudi na maisha yangu, hatoweza kuichukua roho yangu kwa sababu tu nina imani kwamba ataniponya,” alisema Malaika huku akimwangalia mpenzi wake.
Maneno aliyoongea yalikuwa ni ya kijasiri sana, alishangaa ni kwa jinsi gani mpenzi wake alikuwa na imani kubwa kiasi hicho. Alikuwa kwenye hali mbaya mno lakini badala ya kuona kwamba muda wowote ule angekufa, ndiyo kwanza alikuwa akimwambia kuwa kila kitu kilichokuwa kikiendelea kilikuwa ni makusudi ya Mungu.
Hawakuwa na pa kulala, hapohapo makaburini ndipo palikuwa makazi yao, waliendelea kukaa mahali hapo, watu walipokuwa wakifika na kuzika, walikuwa wakiwaona, hakukuwa na mtu aliyejali kwani kwa muonekano wao walionekana kama machokoraa waliokuwa wakiishi tu pale makaburini.
Vidonda viliendelea kumsumbua Malaika, alikuwa kwenye mateso makali na wakati mwingine alikuwa akilia kwa uchungu mkubwa. Aliamini kwamba Mungu angekwenda kumponya lakini wakati mwingine alimuona Mungu akichelewa kumjibu maombi yake na kumponya kama alivyokuwa akiamini.
Makaburini hapo, mateso mengine makubwa yalikuwa ni wadudu wadogo wakiwemo mbu na sisimizi. Waliwasumbua na wakati mwingine walitamani hata kuwa na dawa za kuwapulizia lakini hilo lilishindikana.
Siku ya kwanza ikakatika, siku ya pili nayo ikakatika, maisha yalikuwa magumu makaburini hapo, hawakuogopa, watu walishindwa kuwasaidia kwani wakati mwingine walihisi kwamba watu hao walikuwa vichaa.
“Maisha haya mpaka lini?” aliuliza Ibrahim huku akimwangalia mpenzi wake.
“Mungu atafanya!”
“Kweli tutatoka hapa tulipo?”
“Nina uhakika tutatoka tu! Nikipona, naamini Mungu atatufungulia mlango tena,” alisema Malaika huku akimwangalia mpenzi wake, siku zote uso wake ulikuwa na tabasamu pana.
Kila mmoja alibaki akihuzunika, Richard hakuamini kile alichoambiwa na baba mwenye nyumba kwamba yule kijana aliyekuwa amemsaidia kumpata mtoto wake alihama nyumbani hapo na mchumba wake mgonjwa ambaye alikufa na kuzikwa makaburini.
Hakutaka kubaki mahali hapo, alihitaji kuliona hata kaburi la mpenzi huyo ili moyo wake ulidhike, na upande mwingine akahisi kwamba endapo kama angefika makaburini hapo na kuliona kaburi hilo basi ingekuwa rahisi hata kuambiwa na majirani kwamba mtu aliyezikwa mahali hapo ndugu zake walikuwa mahali gani.
Wakaingia ndani ya gari na kuanza kuelekea huko. Njiani, kila mmoja alikuwa na huzuni tele, kwa Bianca alikuwa akilia tu, hakujua ni kwa sababu gani hali hiyo ilimgusa mno moyoni mwake.
Hawakuchukua muda mrefu sana wakafika hapo kwa Ali Maua, wakaulizia mahali makaburi yalipokuwa, walipoonyeshewa wakaanza kuelekea huko huku kila mmoja akitaka kuliona kaburi hilo.
Walipofika huko, wakaanza kuangalia huku na kule, hakukuwa na mtu yeyote yule lakini walipoangalia kwa mbali kabisa, macho yao yakatua kwa msichana aliyekuwa amelala kwenye majani pembeni kidogo mwa kaburi moja lililokuwa na msalaba kwa juu.
Wakaanza kumsogelea mtu huyo, kitu cha kwanza walichokutana nacho ni harufu mbaya, walihisi kwamba inawezekana mvua iliyonyesha juzi ilisababisha baadhi ya maiti kufukuliwa na hivyo harufu kuenea eneo lote. Wakamsogelea msichana huyo, walipomfikia, alionekana msichana ambaye hakuwa akijiweza kabisa.
“Habari yako dada,” alisalimia Richard huku akimwangalia Malaika.
Msichana huyo hakujibu kitu, alibaki akiwaangalia huku tabasamu pana likiwa usoni mwake. Walibaki wakimshangaa, wakahisi kwamba inawezekana msichana huyo alikuwa kichaa, mchafu na ndiyo maana alikuwa akitoa harufu mbaya mahali hapo.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Wakati wakiwa wanamshangaa, wakamsikia mwanaume mmoja akiongea kwa sauti kwamba walitakiwa kuondoka haraka mahali hapo. Wakayageuza macho yao na kumwangalia mwanaume huyo, alikuwa Ibrahim aliyekuwa akija huku akikimbia.
Alipofika, macho yake yakatua kwa mwanaume aliyekuwa akimfahamu, ndiye yuleyule aliyemsaidia kumpatia mtoto wake. Wakabaki wakiangaliana kwa mshangao, Richard akashindwa kuvumilia, akamsogelea Ibrahim na kumkumbatia.
Furaha aliyokuwa nayo ikasababisha machozi kuanza kumtiririka, alihisi kitu cha tofauti moyoni mwake na kila alipomwangalia mwanaume huyo, aliisikia sauti ikimwambia kwamba alitakiwa kufanya jambo kwa ajili ya watu hao.
“Huyu ndiye mpenzi wangu,” alisema Ibrahim huku akimuonyeshea Malaika aliyekuwa chini hoi.
Malaika alikuwa anatia huruma, Bianca akashindwa kuvumilia, kama kawaida yake akaondoka na kuelekea ndani ya gari na kuanza kulia huko. Hakuamini kama kulikuwa na watu waliokuwa wakipata mateso namna hiyo, muonekano wa Malaika tu ulionyesha kwamba hakubakiza siku nyingi za kuendelea kuishi.
Ili kurudisha fadhila, Richard akamwambia Ibrahim kwamba angempatia matibabu Malaika kuhakikisha kwamba anapokea anapona na kuwa kama zamani.
“Ila madaktari wamesema kwamba atakufa ndani ya miezi mitatu,” alisema Ibrahim huku akilia.
“Hata kama. Tutamsaidia mpaka hapo tutakapoona amekufa, vinginevyo, tutaendelea kumsaidia,” alisema Richard.
Hakutaka kupoteza muda, wakamchukua Malaika na kuondoka naye. Sehemu ya kwanza kabisa kwenda ilikuwa ni katika Hospitali ya St. Marie iliyokuwa Kijitonyama ambapo baada ya muda akahamishwa na kupelekwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Huko, madaktari walikuwa wakihangaika kuhakikisha msichana huyo anarudiwa katika hali yake ya kawaida, walihangaika kwa siku mbili na walipoona kwamba imeshindikana ndipo wakampa taarifa Richard ambaye tayari naye alianza kufanya mawasiliano na Hospitali ya Ohio Health Dublin Methodist iliyokuwa huko nchini Marekani ambapo walimwambia kwamba kusingekuwa na tatizo lolote kwa mgonjwa huyo kupelekwa huko.
“Ni lazima tuelekee Marekani!” Richard alimwambia Ibrahim.
“Marekani! Kufanya nini?” aliuliza Ibrahim.
“Kwenda kumtibu mpenzi wako! Hatuwezi kumuweka nchini Tanzania tu, anaweza kufa kwani kwa jinsi anavyoonekana, kama tusipofanya jambo, tutampoteza,” alisema Richard.
Hakukuwa na la kufanya zaidi ya kukubaliana kumpeleka msichana huyo nchini humo. Baada ya siku nne kila kitu kilipokamilika, wakaanza safari ya kwenda nchini humo.
Njiani, Ibrahim alikuwa akilia, furaha ilimzidi kabisa na kujikuta akiangusha machozi ndani ya ndege. Mpenzi wake, Malaika aliendelea kumwambia kwamba Mungu alikuwa akifanya muujiza taratibu na ipo siku angesimama na kutembea tena.
“Ibrahim! Nilikwambia kwamba nina imani kwamba nitapona. Kuna siku nitawasimulia watoto wangu juu ya mateso makubwa niliyopata lakini pia nitawasimulia jinsi Mungu alivyonipambania baada ya kuwa na imani moyoni mwangu. Nitaambia matendo makuu aliyonifanyia Bwana,” alisema Malaika huku tabasamu pana likionekana usoni mwake kama kawaida.
****
Ilipofika majira ya saa 9:30 alasiri ndege ya Shirika la Ndege la American Airlines ikaanza kutua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Rickenbacker uliokuwa jijini Ohio. Kila mmoja alikuwa amefunga mkanda wake, Ibrahim pale alipokuwa amekaa macho yake yalikuwa yakimwangalia mpenzi wake aliyekuwa kitandani.
Moyo wake ulirudiwa na tumaini jipya kwamba inawezekana baada ya kumpeleka Malaika nchini Marekani kwa ajili ya kupatiwa matibabu angeweza kupona tena. Pale kitandani alipokuwa, msichana huyo alikuwa kwenye tabasamu pana, bado moyo wake uliendelea kuamini kwamba huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa uponyaji wake japokuwa alikuwa amekonda kupita kawaida.
Baada ya ndege kusimama, kitanda alicholalia kikasukumwa mpaka nje ambapo hapo wakakuta gari la wagonjwa na baadhi ya madaktari wa Hospitali ya Ohio Health Dublin Methodist na kuanza safari ya kuelekea katika hospitali hiyo.
Walipokuwa njiani, muda mwingi Ibrahim alikuwa akimwangalia Malaika, uso wake ulikuwa na furaha tele, japokuwa madaktari walisema kuwa msichana huyo alibakiza miezi mitatu ya kuishi lakini bado yeye mwenye alikuwa na imani kwamba msichana huyo angeweza kuvuka siku zaidi na kuendelea kuishi.
Hakujua ni kwa jinsi gani alitakiwa kumshukuru Richard kwa msaada mkubwa aliokuwa ameufanya kwani aliamini kwamba bila mwanaume huyo maisha ya mpenzi wake ingewezekana kabisa yangeishia katika Makaburi ya Kwa Ali Maua.
Hawakuchukua muda mrefu wakafika katika hospitali hiyo ambapo machela ikateremshwa na wao kuteremka. Hapo ndipo walipokutana na msichana mrembo, aliyekuwa ameshika karatasi kadhaa mkononi mwake huku uso wake ukiwa na miwani.
Msichana huyo akawasogelea na kuwauliza maswali kadhaa. Ibrahim hakujua aliuliza nini lakini kwenye kusikiliza vizuri akasikia Richard akilitaja jina lake, kilichomfanya kujua kwamba yule ni mwandishi wa habari ni mtu aliyeshika kamera ambaye alikuwa ameongozana na msichana huyo.
Hawakutaka kubaki hapo nje, wakaunganisha mpaka ndani. Huko, wakakaa na kuzungumza mambo mengi mno. Hicho ndicho kipindi ambacho Ibrahim akaanza kumuhadithia Richard historia ya maisha yake mpaka alipokutana na msichana Malaika na kuanza kuishi pamoja.
“Ni historia inayogusa sana! Kwa hiyo hujui huyu binti alitoka wapi?” aliuliza Richard.
“Sijui chochote kile. Mimi nilimkuta kitaani, nikawa namega kisela,” alisema Ibrahim na wote kuanza kucheka.
Msichana Amanda alikuwa pembeni, kichwa chake bado kilikuwa na maswali mengi kuhusu msichana Malaika, hakujua alikuwa nani na alitoka nchi gani lakini kwa jinsi alivyokuwa amekonda, moyo wake ulimuuma mno.
Hakuwa na habari kuhusu mgombea urais, Kendrich, mawazo yake yalikuwa kwa msichana huyo, alitaka kufahamu mengi na aliamini kwamba kama angejua historia ya maisha yake, angeitolea kitabu ili kiweze kuuzwa duniani kote.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Matibabu yakaanza nchini Marekani, Richard ndiye aliyegharamia kila kitu. Hakuamini kama kulikuwa na mtu aliyekuwa akiumwa kama ilivyokuwa kwa Malaika. Alijisikia kumsaidia kwa sababu mpenzi wa msichana huyo alimsaidia kumletea furaha kubwa maishani mwake.
Kila siku hapo hospitalini walikuwa wakionana na Amanda ambaye aliwaambia wazi kwamba alitaka kufahamu mambo mengi kuhusu msichana huyo kwamba kwa nini aliugua ugonjwa huo, na kama alikuwa akiumwa magonjwa hayo, kwa nini mpaka siku hiyo hakuwa amekufa.
Majibu ya madaktari ndiyo yaliyomtisha zaidi na kumuonea huruma zaidi Malaika. Alikuwa binti mdogo mno, aliyetakiwa kuishi zaidi, kitendo cha ripoti kuonyesha kwamba alibakiza miezi mitatu ya kuishi ilionekana kama Mungu alikuwa akimuonea.
Kila siku Ibrahim alisimama pembeni ya Malaika na kuzungumza naye, aliendelea kumwambia namna alivyokuwa akimpenda, jinsi alivyopambana naye mpaka kufikia kipindi hicho.
Malaika hakuwa na cha kusema, kila alipokuwa akimwangalia Ibrahim, kwake alionekana kuwa mwanaume wa ajabu, alipambana usiku na mchana hata kama alikuwa kwenye matatizo makubwa kiasi gani.
Alimpenda kwa moyo wake wote, akaona kabisa kwamba huyo ndiye alikuwa mwanaume aliyeumbwa kwa ajili yake. Palepale kitandani akamwambia wazi kwamba alimpenda kwa moyo wa dhati na angempa moyo wake mpaka siku ambayo angeingia kaburini.
Madaktari waliendelea kufanya kazi yao, kila mmoja aliamini kwamba Malaika angekufa kitandani hapo. Amanda alikuwa akifuatilia, kila siku alifika hospitalini hapo na kuzungumza na Malaika huku Richard akiwa pembeni kwa ajili ya kutafsiri kila kitu alichokuwa akikiongea.
“Anataka tutengeneze kitabu?” aliuliza Malaika.
“Ndiyo! Amesema historia yako inaweza kuwagusa watu wengi sana,” alisema Richard.
“Mmh!”
“Malaika! Naomba ukubaliane naye! Hujui kwa nini Mungu amekuleta huku. Kama unaamini kwamba kuna siku utapona, naomba uamini kwamba Mungu amekuleta huku kwa ajili ya kuonana na Amanda,” alisema Richard.
Walizungumza sana, Malaika hakuwa na jinsi, akakubaliana na Richard kwamba mwandishi atafutwe kwa ajili ya kuandika kitabu cha maisha yake ambacho kwa Amanda aliamini kwamba kingeuza sana.
Alichokifanya Richard ni kumpigia simu mwandishi huyo ambaye baada ya saa moja akafika hospitalini hapo akiwa na mwanaume mmoja mtu mzima ambaye alikuwa na begi dogo mgongoni, alifika hapo kwa ajili ya kuzungumza na Malaika na hivyo kuandaa kitabu ambacho waliamini kuwa kingeuzwa sehemu kubwa duniani.
“Lakini madaktari wanasema kwamba nina miezi michache ya kuishi,” alisema Malaika.
“Sawa. Wao wanasema hivyo! Wewe unasemaje?” aliuliza Richard.
“Nina miaka zaidi ya hamsini!”
“Basi amini Mungu kwamba utaishi miaka hiyo yote!” alisema Richard.
Huo ndiyo ukawa mwanzo wa msichana huyo kuanza kutoa historia ya maisha yake. Wakati akiwa anasimulia, kila mtu alikuwa kimya pembeni ya kitanda chache. Malaika alisimulia huku akiwa ameyafumba macho yake.
Simulizi yake ilimuhuzunisha kila mtu, Richard ambaye alikuwa akitafsiri wakati mwingine alinyamaza na kulia, hata Amanda na mwandishi aliyekuwa mahali hapo walipokuwa wakisikiliza historia ya msichana huyo kila mmoja alikuwa akilia.
Alipitia maisha ya mateso mno, hakuwahi kupata furaha hata siku moja, hakuwahi kumuona baba yake, alizungumza hatua kwa hatua, jinsi alivyokuwa akiteseka mitaani, alivyokuwa akiomba kwa ajili ya mama yake aliyekuwa na kansa ya titi, jinsi alivyobakwa mpaka siku ambayo alirudi nyumbani na kumkuta mama yake akiwa amefariki dunia.
“Umesema mama yako aliitwa Sarafina?” aliuliza Richard huku akimwangalia Malaika.
“Ndiyo!”
“Na baba yako aliitwa David?”
“Ndiyo!”
“Ndiye ambaye aliwatelekeza?”
“Ndiyo!”
“Mama yako ni mtu wa wapi?”
“Msukuma! Ila sijawahi kufika Mwanza!”
“Kwa sababu gani?”
“Alisema bibi na babu walimfukuza kwa kuwa alikuwa na mimba,” alisema Malaika na kuendelea kulia kama kawaida.
Richard akasimama, kila akaanza kumwangalia, hawakujua ni kitu gani kilikuwa kikiendelea mpaka kusimama na kuelekea pembeni ya chumba hicho na kuanza kulia.
Alionekana kuumia, wote wakajiuliza maswali juu ya mwanaume huyo kulia kwa kuhuzunika sana. Hawakujua sababu ilikuwa nini, hawakujua kama aliguswa kwa kiasi gani mpaka kulia namna hiyo.
Ibrahim akamsogelea na kuanza kumfariji kwa kumpigapiga mgongoni. Richard hakufarijika, kwa harakaharaka kama mtu angetokea ndani ya chumba hicho, ni lazima angefikiria kwamba mgonjwa alikuwa Richard badala ya Malaika aliyekuwa kitandani.
“Bro! Nini tena?” aliuliza Ibrahim huku akiwa amemsogelea Richard.
“Namfahamu mama yake!”
“Unamfahamu mama yake?”
“Ndiyo!”
“Huyo Sarafina?”
“Ndiyo!”
“Imekuwaje bro! Mbona unanichanganya?” aliulizia Ibrahim.
Richard hakujibu kitu, akamrudia Malaika pale alipokuwa na kuanza kumwambia kwamba alikuwa akimfahamu sana mama yake. Hakutaka kumweleza juu kwa juu bali alichokifanya ni kumuhadithia historia ya maisha yake kuanza siku ya kwanza walipokutana.
Hakutaka kumficha, alimwambia ukweli kwamba mama yake alimkataa kwa sababu alionekana masikini na mwisho wa siku kuchukuliwa na mwanaume aliyeitwa kwa jina la David aliyekuwa akitembea na wanawake na kuwaacha.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Unawajua wazazi wangu?” aliuliza Malaika huku akionekana kutokuamini.
“Nawajua wote. Baada ya kuondoka Mwanza sikuweza kuonana na Sarafina. Nilimpenda sana mama yako, alikuwa kila kitu kwangu. Sikujua kama kuna siku nitakuja kumsaidia mtoto wake...” alisema Richard na kuendelea kulia.
Moyo wake ulimchoma lakini kwa upande mwingine alifurahi mno, alimpenda sana Sarafina hata kitendo cha kumsaidia mtoto wake kwake kilikuwa ni faraja kubwa moyoni mwake. Akamshika mkono Malaika na kuanza kusali naye pale kitandani.
Malaika hakuweza kumalizia historia yake siku hiyo, kila siku Amanda na mwandishi yule walikuwa wakija hospitalini hapo na kuzungumza na msichana huyo. Historia yao iliwaumiza na kuwaumiza kiasi kwamba kila siku walipokuwa wakienda huko walijua kabisa kwamba siku hiyo ilikuwa ni ya kulia hivyo walibeba vitambaa vyao vya kufutia machozi.
Wakati akiendelea kusimulia hatua kwa hatua, huku nyuma matibabu yalikuwa yakiendelea. Mwezi wa pili ukakatika, hali yake ikaanza kurudi upya, vidonda vikapona na mwili wake kuanza kuwa katika hali ya kawaida ambayo hata yeye mwenyewe alikuwa akishangaa.
“Sura yako inakuja! Umefanana sana na mama yako! Ulipokuwa mwembamba, sikuwa nikikufananisha, sura ya mama yako imekurudia,” alisema Richard huku akiachia tabasamu pana.
Walichokifanya madaktari ni kumpima tena Malaika na kitu cha ajabu kabisa kilichowashangaza ni kwamba Malaika hakuonekana kuwa na ugonjwa wowote ule. Walishangaa, ilikuwaje msichana huyo asiwe na ugonjwa wowote na wakati kipindi alichokuwa amefika alionekana kuwa na magonjwa mawili, kansa ya damu na sickle cell iliyokuwa imemsumbua kwa kipindi kirefu?
Walichokifanya ni kumwambia Richard kwamba walishangazwa na matokeo waliyokuwa wameyapata kwa msichana Malaika kwamba hakuwa na ugonjwa wowote ule, damu yake ilikuwa safi na hata sickle cell hakuwa nayo.
“Haiwezekani!” alisema daktari huku akirudia mara kwa mara kusoma ripoti ya majibu ya mgonjwa Malaika.
“Inabidi uamini.”
“Lakini alikuwa mgonjwa mno.”
“Ndiyo! Ila Mungu amemponya. Nisikilize daktari! Ukimuomba Mungu mkate, naye atakupa mkate, ukimuomba jiwe, naye atakupa jiwe, hata ukimuomba uponyaji, atakuponya tu! Hivyo ndivyo Mungu anavyofanya kazi yake, wala haingiliwi na mtu yeyote yule,” alisema Richard huku akitoa tabasamu pana.
Kila mtu aliyepata taarifa kwamba Malaika alikuwa amepona hakuamini, wengi wakaelekea katika chumba alichokuwa kwa ajili ya kumwangalia, walitaka kujionea kwa macho yao lakini la zaidi ni kwamba walitaka kuona ripoti ile.
Richard akamfuata Malaika na kumwambia kila kitu kilichokuwa kimetokea kwamba Mungu alikuwa ametenda muujiza na hakukuwa na ugonjwa wowote ule mwilini mwake.
“Mungu huwa hadanganyi! Anaposema kwamba anataka kufanya muujiza, anafanya. Mkumbushe yule mwandishi mwambie aandike kuhusu hili,” alisema Malaika.
“Aandike nini?”
“Kwamba imani yangu ndiyo iliyoniponya. Niliteseka, nililia sana, niliumia moyoni mwangu lakini kila siku niliamini kwamba Mungu angeniponya. Leo hii ameniponya, ninasimama, ninatembea na kurukaruka. Nimpe nini Mungu wangu?” alisema Malaika, maneno hayo yalimchoma mpaka yeye mwenyewe na kuanza kulia hapohapo.
Huo ulikuwa muujiza, mpaka wanaondoka nchini Marekani bado madaktari walikuwa wakimshangaa msichana huyo. Alikuwa amepona magonjwa mawili, aliondoka hospitalini huku akiwa mzima wa afya, yaani aliwaacha hata wale ambao walikuwa wakililia uponyaji kitandani hapo.
Walipofika Tanzania, kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kumtafuta David. Richard alimfahamu mwanaume huyo, alioa hivyo kitu cha kwanza kilichofanyika kilikuwa ni kumtafuta mwanaume huyo na kumwambia kwamba japokuwa alimkataa mpenzi wake lakini mtoto wake alikuwa hai.
Kutokana na jina alilokuwa nalo David jijini Dar es salaam, hawakupata tabu kupajua alipokuwa akiishi ambapo alikuwepo mke wake aliyekuwa akiishi na mwanaume mwingine aliyekuwa amemuona.
Wakataka kuzungumza naye, hilo halikuwa tatizo, wakakutana na kuzungumza mambo mengi huku Malaika akiwa pembeni. Kitendo cha kulitaja jina la David, Gloria akaanza kulia, moyo wake ulimuuma, alikumbuka jinsi alivyokuwa akimpenda marehemu mume wake.
“Aliniambia kuhusu Sarafina. Kuna siku tulikutana na mwanamke huyo akiwa amebeba mtoto,” alisema Gloria.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Sasa yule mtoto ndiye huyu!”
“Ooh Mungu wangu! Ndiye huyu?”
“Ndiyo! Anaitwa Malaika!”
“Amefanana kweli na marehemu mume wangu,” alisema Gloria na kumkumbatia Malaika.
Gloria hakuishia hapo, akawaambia kwamba kabla ya mumewe kufariki alikuwa ameandika barua kwa ajili ya Sarafina kwani hakujua kama alikuwa amefariki dunia na katika barua hiyo alijuta, alihuzunika, alilia kutokana na yale yote aliyomfanyia Sarafina.
“Iko wapi?”
“Ngoja nikailete!” alisema Gloria, akaelekea chumbani, aliporudia akawa na barua hiyo huku akiwa na picha kadhaa za David na kumpa Malaika ambaye akazichukua na kuanza kuziangalia, kwa jinsi alivyokuwa amefanana na David, yeye mwenyewe akaanza kulia.
“Nitakukumbuka baba! Nimekusamehe na ninaamini hata kama mama angekuwa hai angekusamehe,” alisema Malaika huku akiendelea kulia.
Barua ndiyo iliyozidi kumuonyeshea ni jinsi gani baba yake alijutia kile alichokuwa amekifanya, aliumia sana, hawakutaka kubaki mahali hapo, wakaondoka mpaka katika Makaburi ya Kinondoni kwa ajili ya kuliona kaburi la David.
Moyo wa Malaika ukawa na amani tena, akajisikia faraja moyoni wake japokuwa hakuwa ameonana na baba yake macho kwa macho. Wakaondoka na kuelekea nyumbani ambapo maisha yakaendelea huku picha za baba yake zikiwa katika chumba alichokuwa akiishi katika nyumba ya Richard.
Baada ya miezi miwili, Amanda akawapigia simu na kuwaambia kwamba kitabu cha Malaika kilikuwa kimekamilika na kitu kilichokuwa kikisubiriwa ni kuchapishwa na kisha kuanza kuuzwa kama kuwahamasisha wagonjwa kwamba kitu pekee walichotakiwa kufanya ni kuamini kwamba hata kama wangeumwa nini, mwisho wa siku kama wangeamini wangeweza kupona tena.
Kwa sababu walihitaji kitabu hicho kimfikie kila mtu, kikachapishwa kwa lugha nne, Kiingereza, Kifaransa, Kireno na Kiswahili na kiliandaliwa tayari kwa ajili ya kuuzwa duniani kote.
Kitabu kikachapishwa na Malaika kupelekwa nchini Marekani ambapo akavisaini vitabu vyote na kuanza kuuzwa. Yalikuwa ni mafanikio makubwa, kwa jinsi promosheni ya kitabu hicho ilivyofanyika, kila mtu akatamani kukisoma na hivyo kitabu hicho kuingiza dola milioni tano kwa wiki ya kwanza tu, pesa ambazo kwa thamani ya shilingi ya Kitanzania ilikuwa ni sawa na shilingi bilioni kumi.
Yalikuwa ni mafanikio makubwa, kilikuwa kitabu cha kwanza kuingiza kiasi kikubwa cha fedha kwa wiki ya kwanza tu. Watu walikinunua sana na kila aliyekuwa akikisoma, alilia kutokana na historia hiyo kumgusa kila mtu.
Yule Malaika mtoto wa mitaani, maisha yake yakabadilika, akaingiza mabilioni ya shilingi kwani ndani ya mwaka wa kwanza tu, kitabu hicho kiliingiza zaidi ya dola bilioni mbili, zaidi ya shilingi trilioni nne kwa pesa za Kitanzania.
Maisha yalibadilika, akafungua biashara zake huku zikisimamiwa na Richard aliyekuwa mzoefu katika biashara, hakutaka kuachana na Ibrahim, kwake, mwanaume huyo alikuwa kila kitu. Wakaamua kuishi pamoja katika jumba lao kubwa walilolinunua huko Mikocheni B, moja ya jumba kubwa lililokuwa na vyumba zaidi ya kumi na tano.
Malaika yule akawa bilionea na kilichokuwa kimempa pesa nyingi ni historia ya maisha yake ambaye baadaye aliiweka kwenye kitabu. Watu wengi walitaka kufahamu, msichana aliyekonda mno, aliyekaa kwenye kava la kitabu, aliyekuwa akiumwa kansa ya damu na sickle cell aliponyaje? Ili watu kujua hayo yote, ilikuwa ni lazima kununua kitabu na kusoma kitu kilichompa pesa nyingi msichana huyo ambaye aliamua kutoa asilimia kumi ya mauzo ya kitabu hicho kwa kuwasaidia watoto wa Kiafrika waliokuwa wakisumbuliwa na magonjwa mbalimbali duniani.
“Malaika! Mungu aliyaandaa maisha haya tangu ulipokuwa katika tumbo la mama yako. Alikuwekea kitu kimoja, ili uweze kuyafikia ilitakiwa kuamini. Namkumbuka mchungaji aliposema kwamba kama kweli unataka kufanikiwa ni lazima Mungu akupitishe katika tanuru la moto, kwenye hilo tanuru la moto kuna wengine watakata tamaa, wengine watapambana, na watu watakaovuka basi ndiyo watakutana na mafanikio ambayo Mungu aliwaahidi tangu wakiwa tumboni kwa mama zao,” alisema Richard huku akimwangalia Malaika.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Nilizaliwa kuamini, nimekuwa nikiamini kwa kipindi chote cha maisha yangu. Nilijua kwamba kuna siku haya yaliyotokea yangetokea na hakika Mungu amefanya,” alisema Malaika na kumkumbatia Ibrahim ambapo ilipofika Jumamosi ya tarehe 03/07/2017 wawili hao wakafunga ndoa katika Kanisa la Living God lililokuwa jijini Dar es Salaam.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment