Simulizi : Siku Za Mwisho Za Uhai Wangu
Sehemu Ya Nne (4)
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Mike alikuwa hoi kitandani, nyumbani kwake, akiamini kabisa kuwa angekufa baada ya siku si nyingi. Alikuwa katikati ya mateso makali na mawazo mengi na alimhurumia sana mke wake kwa sababu mateso aliyokuwa akiyapata hata mkewe pia yalikuwa yakimsubiri.
Ndani ya nafsi yake alijilaumu ni kwa nini alikubali kuacha matumizi ya kondomu kama walivyokuwa wamepanga.
"Mke wangu, UKIMWI si mchezo. Nakuhurumia sana nisingependa mateso haya yakupate lakini hakuna la kufanya, itabidi tu uyapitie haya yote. Mimi najua nitakufa lakini mali yote nitakuachia wewe na ninaagiza kuwa uitumie pesa hiyo kujali afya yako na kuwatunza wagonjwa wengine wa UKIMWI na hata yatima."
"Usiwe na wasiwasi, utapona tu Mike," Beatrice alimpa moyo.
"Mke wangu hali yangu si nzuri, naomba uende mjini haraka iwezekanavyo ukamwite Rwezaura nije nikuandikie hati ya urithi usije ukasumbuliwa baada ya mimi kuondoka."
"Mike lakini unajuaje kama unakufa? Tumwachie Mungu mume wangu!"
"Mimi najua tu Beatrice, ninaomba ufanye hivyo."
Beatrice alizidi kusimama pale bila kujua la kufanya, jambo lililomkera Mike ambaye aliangaza macho yake huku na kule na kumwona dada yake mdogo Violeth aliyeishi naye nyumbani.
"Violeth!" Mike aliita akiwa kakasirika. Violeth alikuja mbio chumbani.
"Nenda kwa Rwezaura upesi mwambie aje na mihuri yake yote nina kitu nataka kuandika sawa?”
Violeth aliitikia na kutoka hadi nje ambako aliondoka na gari la Mike, dakika kumi baadaye alirejea na wakili Rwezaura. Hali ya Mike ilikuwa dhaifu mno. Wakili aliandika hati ya urithi kuwa baada ya kifo cha Mike mali yote irithiwe na Beatrice na Beatrice akifa mali yote irithiwe na Violeth au watoto yatima.
Wakili aliondoka na nakala moja ya hati ya urithi kama kumbukumbu na nakala halisi alibaki nayo Beatrice.
"Mke wangu, najua nikifa wanaume wengi watakufuata na kutaka kukuoa sababu ya mali. Naomba usikubali, si kwamba sitaki mali yangu itumiwe na mtu mwingine, ila sitaki uue mtu mwingine tena; acha tufe wenyewe!" Mike alimwambia mkewe baada ya wakili kuondoka.
Baadaye Mike alimwomba Beatrice amsaidie kuandika barua kwa Chancellor Edmund kumjulisha juu ya hali mbaya aliyokuwa nayo kwani hapakuwa na mawasiliano yoyote kati yao. Beatrice hakutaka kufanya mzaha tena kwani hali ilishamtisha.
"Iweke hiyo barua kwenye bahasha kesho ukaitume Uingereza, pia hiyo hati iweke kwenye bahasha uitunze vizuri maana familia zetu za Kiafrika zina matatizo. Mara nyingi wake wa marehemu hunyanyaswa sana baada ya waume zao kufa!"
Beatrice alifanya kama alivyoambiwa, bahasha iliyokuwa na hati aliiweka katikati ya Biblia na kuifungia ndani ya kabati.
***
Mlango uligongwa, Beatrice akaufungua, alikuwa daktari Kalegeya kutoka kitengo cha kupambana na UKIMWI, pamoja na sista Fortunata aliyekuwa mhamasishaji wa mapambano dhidi ya UKIMWI kutoka Kanisa Katoliki jimbo la Mwanza.
"Ah! Karibuni sana dokta."
"Ahsante, tumekuja kumwona Mike maana siku nyingi sana zimepita bila kumtia machoni, anaendeleaje?"
"Yupo ndani, anaendelea hivyohivyo, tafadhali ingieni tu muongee naye."
Daktari Kalegeya na sista Fortunata waliingia ndani.
"Karibuni sana," Mike alimkabisha Dkt. Kalegeya.
Baada ya maongezi marefu na kupeana pole, daktari Kalegeya alikuwa na jambo.
“Kesho ni Siku ya UKIMWI Duniani, tungependa sana tuwakaribishe mshirikiane nasi katika kuadhimisha siku hiyo.”
"Zitafanyika wapi?" Mike aliuliza.
"Uwanja wa mpira wa Nyamagana."
"Nitapenda sana kuwepo...nina jambo la kuwaeleza vijana ambao bado wanauona UKIMWI kama kitu kidogo, ninataka wapate nafasi ya kuona labda itasaidia kidogo kuibadilisha jamii."
***
Maelfu ya watu walifurika katika Uwanja wa Nyamagana Barabara ya Posta mjini Mwanza, wakisikiliza hotuba za viongozi mbalimbali akiwemo Mkuu wa Mkoa juu ya ugonjwa wa UKIMWI.
Kila mtu alionekana kuwa na huzuni, yalikuwa ni maadhimisho mengine ambayo hufanyika katika viwanja hivyo. Kila kilichoongelewa kilionekana kuwagusa kwa uzito wote waliokuwepo uwanjani.
"Hivi sasa ni wakati wa kumkaribisha Mike Martin, kijana mwathirika wa UKIMWI ambaye ameamua kuongea nanyi siku ya leo ili mpate kuuona mfano hai wa mtu anayekufa kwa UKIMWI.
"Karibu Mike!" Mshereheshaji alimkaribisha.
Mike alinyanyuka kwa msaada wa mkewe na kusimama wima huku akiyumba, ilibidi Beatrice amshikilie vizuri. Uwanja wote ulikuwa kimya kabisa. Watu walipomwona jinsi alivyokuwa amekonda walisikitishwa sana.
"Jamani mnanionaaaa!" Mike alisema kwa sauti, umati wote wa watu ukaitikia.
"Ndiyoooooo!"
"Basi mimi ni mfano halisi wa mtu aneyekufa kwa UKIMWI, ndugu zangu! Leo hii nimeamua kujitokeza hadharani ili muelewe ugonjwa huu unatesa kiasi gani, mpate kubadilisha tabia zenu.”
Alisita kidogo, baadaye aliendelea: "Ndugu zangu ugonjwa huu ni mbaya nikisema mbaya, naomba nieleweke una mateso mengi mno na nisingependa mateso haya yampate mtu mwingine yoyote!
Ningependa mimi ndiye niwe mtu wa mwisho kufa kwa ugonjwa huu. Ndio maana nimesimama mbele yenu kuwaelezeni ninayoyasema.
Nimesikia vijana wengi wakisema UKIMWI ni kama mafua, UKIMWI ni kama malaria, UKIMWI ni kama taifodi lakini maneno hayo mnayasema kabla hamjaupata ugonjwa huu na kuyashuhudia mateso yake.
Ukishaupata utaomba atokee mtu autoe mwilini mwako lakini haitawezekana tena. Ni hapo ndipo utakapoanza kujuta na kuteseka."
Aliendelea, "Kama UKIMWI ungekuwa unaondolewa mwilini kwa pesa mimi ningepona, kwani nilibahatika kupata pesa nikiwa katika umri mdogo sana lakini pesa zangu zimeshindwa kunisaidia! Nimeshakwenda Kenya na Zaire nikatumia mamilioni ya fedha kwa dawa za Kemron na MMI bila mafanikio.
“Nimekwishakwenda Marekani kubadilisha damu mara mbili bila mafanikio, leo hii ninakufa pamoja na fedha nilizo nazo, naziacha pesa zangu!
"UKIMWI si jambo la kufanyia mzaha ndugu zangu..." Wakati Mike akitoa hotuba hii karibu nusu ya watu uwanjani hapo walikuwa wakilia.
"Msilie, chukueni tahadhari kabla mambo hayajawafika..." Alipofika hapo ghafla Mike alianguka chini na kugeuza macho, akaanza kutupa mikono.
Beatrice alianza kulia akimtingisha.
ANGELINA MOSHA 1962-1999 (2)
Mzee Martin, baba yake Mike, alizaliwa katika familia ya Mtemi Mchenya wa huko Dutwa, Bariadi. Alizaliwa akiitwa Longa na alikuwa mtoto wa mwisho katika familia yao iliyokuwa na watoto wengine saba waliotangulia. Ndugu zake wengine wote hawakujaliwa kwenda shule, walibaki nyumbani kumsaidia baba yao kazi na utawala wa ufugaji wa ng'ombe.
Longa akiwa na umri wa miaka mitano, baada ya kiongozi wa kikoloni DC William kumwona na kumpenda, alimwomba Mtemi Mchenya kumruhusu amchukue na kwenda kuishi naye Ikulu ili awe akicheza na mtoto wake aliyeitwa Smith mwenye umri sawa na Longa.
Kwa sababu aliombwa na DC, Mtemi Mchenya hakuwa na pingamizi, alikubali mtoto wake achukuliwe, Longa akawa amejiunga na familia ya DC Smith, Shinyanga mjini. Muda mfupi baadaye alibatizwa na kuitwa Martin Longa Mchenya.
Martin na Smith, kwa pamoja walifundishwa na mwalimu Mwingereza na katika muda mfupi Martin alijikuta akibadilika na kuwa kama Mwingereza. Ilikuwa sio rahisi kuamini alizaliwa katika familia ya Mtemi Mchenya, mara chache sana alikwenda nyumbani kwao Bariadi. Muda mwingi wa maisha yake alikuwa uzunguni, Shinyanga.
Martin akiwa na umri wa miaka kumi na mitano, DC William alitakiwa arudi nyumbani kwao Uingereza, kwa jinsi familia nzima ya DC huyo ilivyokuwa imemzoea Martin, ilishindwa kumuacha Tanganyika.
DC alimfuata Mtemi Longa kuomba ruhusa ili waondoke naye, lakini Mtemi alikataa na kusema mtoto wake asingeweza kuishi mbali na wazazi wake kiasi hicho. Alitaka Martin arudishwe nyumbani mara moja.
Hata hivyo, baadaye Martin alikwenda Bariadi kumbembeleza baba yake ambaye hatimaye alikubali na kutoa ruhusa mtoto wake aondoke na familia ya DC William kwenda Uingereza.
Martin hakurudi nchini mpaka mwaka 1961, ambapo alikuta utaratibu wa Utemi umefutwa lakini kwa elimu aliyokuwa nayo alipata kazi ya Ualimu katika shule ya msingi Mwika, huko Marangu, Kilimanjaro.
Ni shuleni hapo ndipo alipokutana na msichana wa Kichaga aliyeitwa Veridiana Mosha, yeye pia alikuwa mwalimu katika shule hiyo, na kujenga naye urafiki wa kimapenzi.
Matokeo ya urafiki wao yalisababisha ujauzito lakini mimba hiyo ikiwa na miezi sita mwalimu Martin aliomba uhamisho kwenda Mwanza ambako miaka mitatu baadaye alimwoa Cecilia Ndaki, mwanamke wa Kisukuma na miaka mitano baadaye mama huyo akawa mjamzito na kuzaa mtoto wao wa kwanza wa kiume ambaye walimwita jina la Mike!
Mike alikuwa ni mtoto mzuri mno, kila mtu alimpenda. Mama yake kila alipopanda basi na kusimama abiria walimgombania kumbeba mtoto huyo.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kitendo cha Martin kuhama Moshi kwenda Mwanza na kuoa, kilimuudhi sana Veridiana na kumfanya aamue kukata mawasiliano kabisa na Martin. Alijifungua mtoto wa kike aliyemwita Angelina, aliendelea kumtunza peke yake bila msaada wa baba mtoto wake.
Akiwa na umri wa miaka kumi, Angelina alionekana wazi kuwa mtoto mtukutu kupita kiasi na utukutu huo uliendelea. Akiwa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari Ashira alimpiga mwalimu wake kwa jiwe jichoni na kulipasua kabisa jicho lake na kulifanya ling'olewe. Mwalimu akawa chongo.
Kwa kosa hilo Angelina alishitakiwa na kufungwa mwaka mmoja na nusu gereza la watoto lililoko Upanga jijini Dar es Salaam! Alipomaliza kifungo, hakuendelea tena na masomo ya sekondari kwani jina lake lilishafutwa katika shule aliyokuwa akisoma.
Mama yake alimtafutia nafasi katika shule ya sekondari ya Kibosho ambako hata huko hakumaliza kidato cha pili akatoroka na kurudi tena mjini Dar es Salaam ambako alijiunga na watoto wa mitaani. Akawa analala kwenye mabaraza ya maduka ya Wahindi. Baadaye alijiingiza katika biashara ya ukahaba, akiwa na umri wa miaka kumi na sita tu.
Akiwa katika biashara hiyo alikutana na mtalii wa Kiitaliano aliyeitwa Mariano Covre ambaye alimpenda na kuamua kumtoroshea Milano, huko Italia.
Wakiwa huko walifanya biashara ya madawa ya kulevya kutoka Pakstani na kuyaingiza nchini humo ambapo walijipatia mamilioni ya dola za Kimarekani na kutajirika!
Maisha yao yalibadilika na kuwa ya kifahari. Siku zote waliishi hotelini na kila mumewe alipotaka wanunue angalau nyumba Angelina alikataa.
Mumewe alipotaka pesa walizopata waziweke angalau benki pia Angelina alikataa! Hivyo, mamilioni yote ya dola waliyoyapata yalirundikwa ndani ya chumba chao kwenye sanduku kubwa! Lengo la Angelina lilikuwa ni kumdhulumu mwanaume huyo pesa zote.
Hivyo ndivyo ilivyokuja kuwa, kwani miaka ishirini baadaye Angelina alimuua Mariano Corve kwa kumnywesha madawa ya kulevya aina ya Morphine! Alikufa akiwa usingizini na Angelina akatoroka na pesa zote kuja Dar es Salaam ambako alianzisha kiwanda cha kutengeneza vyombo vya Plastiki alichokiita Longa Plastics Ltd.
Hii ni kwa kulienzi jina la baba yake ambaye hakuwahi kumwona hata mara moja! Hakuna mtu aliyeijua siri ya utajiri wa Angelina na iliaminika ndiye alikuwa mwanamke wa kwanza kumiliki kiwanda nchini Tanzania.
Akiwa katika shughuli zake za biashara, Angelina alianza kusikia habari za mfanyabiashara Mike Martin Longa wa Mwanza. Jina hilo lilimfanya ahisi kuwa kijana huyo angekuwa ni mtoto wa baba yake! Hakuwahi hata siku moja kusafiri kwenda Mwanza kuwaona Mike wala baba yake Martin.
Aliendelea na maisha yake, alimjengea mama yake nyumba ya kifahari huko Marangu na maisha yao yaliendelea vizuri.
***
Baada ya Mike kuanguka mbele ya watu waliofurika uwanjani wakisikiliza hotuba yake, Beatrice alimwangukia palepale na kuanza kumkumbatia huku akilia.
"Mike please dont die, please live for me Mike, I love you so much. Please don't go, don't leave me!" (Mike tafadhali usife, tafadhali ishi kwa ajili yangu, nakupenda mno Mike, usiende usiniache Mike).
Mkutano ulivunjika palepale na harakaharaka Mike alibebwa na kuingizwa ndani ya gari la WAMAU lililokuwa uwanjani na kukimbizwa moja kwa moja hadi hospitali ya Rufaa ya Bugando. Alipofikishwa aliingizwa katika chumba cha daktari ambaye baada ya kumpima palepale aliwatangazia waliomleta kuwa Mike hakuwa duniani tena.
Alikuwa amefariki dunia baada ya mateso ya muda mrefu!
Beatrice alianza kulia, haikuwa rahisi kwake kuamini kuwa ule ndio ulikuwa mwisho wa mume wake. Palepale taswira ilimrudisha toka siku ya kwanza kabisa walivyokutana shuleni Nsumba. Aliikumbuka barua ya kwanza ambayo alimwandikia Mike kumtaka urafiki.
"Hapana, daktari umekosea, huu hauwezi kuwa mwisho wa Mike, tafadhali rudia tena kupima!" Beatrice alisema kwa sauti, baadaye alianguka chini na kupoteza fahamu. Alipozinduka baadaye alikuwa wodini akiwa na dripu mkononi.
"Masikini Mike mume wangu umekufa kweli? Kwa nini umeniacha peke yangu darling?" Beatrice aliendelea kulia huku ndugu na jamaa wakimfariji.
Baadaye usiku, kama majira ya saa nne hivi, hali ya Beatrice ilipoonekana kuwa nzuri aliruhusiwa kwenda nyumbani. Watu wengi walikusanyika wakiomboleza kifo cha mume wake.
Mama yake marehemu Mike alianguka chini na kupoteza fahamu mara tu baada ya kumtia machoni Beatrice na palepale alichukuliwa na kupelekwa hospitali ya Mkoa ya Sekou Toure kwa matibabu zaidi.
Ilikuwa siku ya huzuni mno. Nguzo ya familia ilikuwa imeondoka! Mama yake aliona giza nene mbele, hakujua maisha yangeendeleaje baada ya hapo maana waliishi kwa kumtegemea mtoto wao.
Kufuatia kifo cha Mike, kijana aliyekuwa kipenzi cha watu, mji wa Mwanza ulikuwa kimya, kitendo cha kufa akitoa hotuba juu ya UKIMWI kilimfanya Mike aonekane shujaa kupita kiasi. Maneno ya hotuba aliyotoa siku hiyo uwanja wa Nyamagana juu ya UKIMWI ndio yalitumika kukitangaza kifo chake redioni, ambapo WAMAU ndio waliolipa gharama zote za matangazo ya kifo chake.
****
Ilikuwa ni jioni, Angelina alikuwa nyumbani kwake akisikiliza redio, ghafla akasikia tangazo la kifo lililotanguliwa na hotuba juu ya UKIMWI.
"Alikuwa mpiganaji hodari dhidi ya gonjwa hatari la UKIMWI, hakuificha hali yake, alitaka watu wote wajue kuwa UKIMWI ni hatari!
“Mike Martin Longa, mfanyabiashara maarufu mjini Mwanza aliyekuwa akiteseka kwa UKIMWI amefariki dunia leo wakati akihutubia uwanjani Nyamagana... Maziko yatafanyika mara baada ya kufika kwa ndugu wa marehemu. Shujaa ameondoka."
Taarifa ile ilimshtua sana Angelina, akaamua kumpigia simu mama yake kule Moshi. Mama Angelina alidai kuzisikia pia taarifa zile za redioni. Wote walikuwa na imani kuwa aliyefariki alikuwa ni Mike mtoto wa mzee Martin.
"Hivyo mama mimi kesho nitakwenda huko Mwanza nikahakikishe kama kweli aliyefariki ni kaka yangu."
"Huyo baba yako mwenyewe hamjawahi kukutana hata siku moja atakufahamu kweli?" Mama Angelina alimuuliza mwanaye.
"Nitajitambulisha kwake," alijibu.
***
Watu walikuwa wengi mno msibani, wengi walilia na kuomboleza, wengine walizimia, kwaya mbalimbali zilikuwepo msibani hapo kuwafariji wafiwa.
Mpaka saa sita mchana Beatrice alikuwa amekwishazimia mara saba. Kila alipozinduka aliendelea kulia huku akiwa na picha ya marehemu mumewe mkononi. Watu walijaribu kumpa kila aina ya faraja lakini haikuwezekana.
Hadi majira ya saa saba mchana watu bado walikuwa wakivutana kuhusu kwenda makaburini kuzika. Tangu Mike afariki na mama yake kuzimia na kupelekwa hospitalini mvutano ulitokea kama Mike azikwe au hadi mama yake atoke hospitalini.
Wakati haya yakiendelea, ghafla helikopta moja ilitokea na kutua mbele ya nyumba. Iliposimama ardhini mwanamke mmoja aliteremka akiwa amevaa nguo nyeusi zilizoashiria kuwa alikuwa akihudhuria mazishi, akifuatiwa na kijana mmoja nyuma yake.
"Dada ni hapa."
"Asante sana, wewe chukua hii shilingi elfu tano uchukue teksi urudi uwanja wa ndege sawa?" Angelina alimwambia yule kijana aliyemchukua uwanja wa ndege wa Mwanza ili ampeleke kwenye mazishi ya Mike. Alikuwa rubani wa ndege za Wazungu wa kampuni ya madini ya Tanzania Mines.
Baada ya kuachana na kijana huyo huku watu wote wakimshangaa, Angelina alitembea taratibu hadi karibu kabisa na kundi kubwa la vijana waliokusanyika wakionekana wenye huzuni.
"Habari zenu jamani na poleni kwa matatizo."
"Nzuri shikamoo," walijibu karibu wote kwa pamoja.
"Marahaba, ninaweza kuonyeshwa mahali alipokaa mzee Martin?"
Kijana mmoja alijitokeza na kumpeleka hadi ndani ambako alimkuta mzee Martin pamoja na wazee wengine wamekaa wakiongea.
"Shikamooni wazee, poleni sana kwa matatizo yaliyowapata."
"Asante sana mwanetu ni mambo ya dunia."
"Ninaitwa Angelina, ninaomba niongee na mzee Martin kama yupo hapa kati yetu," Angelina alisema.
Mzee Martin aligeuka na kumwangalia mwanamke huyo lakini hakumtambua. Hilo halikuwa tatizo kwake, alinyanyuka wakaondoka kwenda kukaa kando.
"Mzee, mimi naitwa Angelina Martin. Nafikiri utakuwa unamkumbuka mama yangu mzazi anaitwa Veridiana Mosha uliyemwacha akiwa mjamzito huko Kilimanjaro! Mimi ndiye mtoto niliyezaliwa kutokana na ujauzito huo."
"Kwa hiyo wewe ndiye mwanangu?"
"Ndiyo baba."
"Aah, karibu mwanangu, tupo katikati ya msiba wa kaka yako Mike, alifariki dunia jana bahati mbaya hamkuwahi kuonana."
"Pole sana baba, nilisikia taarifa hizo redioni jana ndiyo maana nimekuja nihudhurie mazishi ya ndugu yangu."
"Ulitoka lini Moshi?"
"Nimetoka Dar es Salaam leo hii kwa helikopta ya kukodi."
"Helikopta ya kukodi?"
"Ndiyo baba."
Baada ya salamu hizo mzee Martin alimwongoza Angelina hadi chumba walichokuwa wanawake ambako pia alikaa Beatrice na Violeth, dada yake Mike.
"Samahani jamani huyu ni dada yake marehemu anaitwa Angelina, kafika sasa hivi kutoka Dar es Salaam naomba mkae naye tuomboleze pamoja," Mzee Martin alisema.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Beatrice alinyanyua uso wake kumwangalia Angelina. Hakukumbuka kama aliwahi kuona sura kama ile maishani mwake. Angelina hakuwa amefanana kabisa na marehemu mume wake.
Siku iliyofuata baada ya mama yake Mike kuruhusiwa kutoka hospitalini na ndugu wote kufika, mipango ya mazishi ilikamilika, heshima za mwisho zikatolewa, baadaye mwili wa marehemu Mike ulibebwa mpaka kanisani eneo la Buzuruga kwa ajili ya ibada.
Ilikuwa ni siku ya huzuni mno kwa Beatrice, alitembea akiwa ameshikwa na watu kila upande, akiwemo dada yake Maggie, wifi yake Violeth, mama yake mzazi na marafiki wengine wa familia.
Baada ya ibada ya Kikatoliki, mwili wa marehemu ulibebwa hadi makaburini karibu tu na kanisa ambako uliingizwa kaburini na kufukiwa. Baadaye zege ilimwagwa juu yake! Beatrice hakuamini kama ule ndio ulikuwa mwisho wa Mike, mume wake.
Siku zote alizoea kupita eneo hilo akienda kwa shangazi yake aliyeishi jirani na makaburi hayo lakini hata siku moja hakuwahi kufikiria kuwa pale ndio mume wake angelala mauti!
***
Baada ya maziko kila mtu alianza kuondoka kurejea nyumbani. Akiwa hatua kama ishirini kutoka kwenye kaburi, Beatrice aligueka kuangalia nyuma. Ukweli ulikuwa dhihiri kuwa mume wake aliyempenda sana alikuwa amemwacha peke yake duniani, hakuelewa maisha yangekuwaje bila Mike.
Ilikuwa ni sawa na mshumaa bila sehemu ya kuusimamisha, ni lazima angeanguka.
Kitendo cha kuondoka na kumwacha mume wake makaburini alikiona kama usaliti na ghafla alijichomoka kutoka mikononi mwa watu waliomshikilia na kuanza kukimbia akirudi makaburini! Alipolifikia kaburi la mume wake alilala juu yake huku akilia.
"Tafadhali Mike rudi, tafadhali Mike rudi siwezi kuishi bila wewe."
Akinamama waliokuwa naye, akiwemo mama yake mzazi, walifika kaburini wakikimbia na kuanza kumbembeleza anyanyuke ili waondoke lakini alikataa katakata na kuendelea kugalagala kwenye kaburi la mumewe akiliita jina lake!
Baada ya kuombwa na kubembelezwa sana hatimaye Beatrice alikubali na kunyanyuka wakaanza kuondoka kurudi nyumbani ambako bado aliendelea na kilio chake!
Siku hiyo hakupata usingizi hata kidogo, kwani sura ya mumewe iliendelea kumjia kichwani mwake, alishindwa kuelewa nini kingefuata baada ya pale maishani mwake bila Mike.
Ni kweli kulikuwa na mali nyingi zilizoachwa lakini kwake hazikuwa na maana bila mume wake.
***
Mzee Rugakingira na mkewe walikuwa ni miongoni mwa watu waliohudhuria msiba huo, moyoni mwake mzee Rugakingira alijiuliza maswali mengi kama kweli Beatrice na marehemu walipima UKIMWI au walidanganya!
Katika siku zote za ugonjwa wa Mike mzee Rugakingira alipokuja Mwanza kuwajulia hali hakuwahi kuliuliza swali hilo ingawa dalili za ugonjwa wa Mike zilifanana kabisa na za wagonjwa wa UKIMWI.
"Kama kweli walipima kuna mmoja wao alikuwa si mwaminifu katika ndoa! Lakini ni nani? Je, ni Beatrice au ni Mike?" Kwa jinsi mzee Rukakingira alivyowafahamu vizuri watoto wake hapakuwa na mtu mwenye tabia ya umalaya kati yao. Alishindwa kuelewa ugonjwa huo uliingiaje katika familia yao.
Mzee Rugakingira alikuwa ni mzazi mwenye busara, pamoja na kuelewa wazi kilichomuua Mike lakini alizidi kumfariji na kumtia moyo ili asimame imara katika wakati huo mgumu. Alijua muda si mrefu pia mwanaye, Beatrice, angekufa kwa ugonjwa huohuo na hilo lilimuumiza sana moyoni mwake. Hakuwa na njia yoyote ya kulikwepa zaidi ya kuukubali ukweli uliokuwepo!
Kilichomshangaza zaidi Beatrice ni Angelina, aliyedaiwa kuwa ni dada wa marehemu mumewe. Angelina hakuonekana kuwa na majonzi hata kidogo na zaidi ya yote hayo, jicho alilomwangalia halikuwa la kawaida! Lilikuwa jicho la chuki.
***
Siku tatu baada ya maziko ya Mike wazazi wa pande zote mbili, ndugu na marafiki wa karibu na familia ya mzee Martin walikuwa wamekaa barazani baada ya maombi ya usiku kabla ya kwenda kulala. Angelina alionekana mwenye mawazo mengi.
"Baba!" Angelina alimwita mzee Martin huku wote wakisikiliza.
"Naam mwanangu."
"Mimi kesho nitaondoka kurudi Dar es Salaam lakini kuna kitu nilitaka tukiongelee kabla sijaondoka!"
"Kitu gani mwanangu?"
"Ni juu ya mali za marehemu..."
Watu wote walipigwa na butwaa hawakutegemea jambo kama hilo ikiwa ni siku tatu tu tangu Mike afariki.
"Mali za marehemu?" Mzee Martin aliuliza, naye pia kwa mshangao.
"Ndiyo! Huyu mwanamke nilichoambiwa ni kwamba hakuzaa na marehemu kaka yangu hata kitoto kimoja, hivyo ni vyema aondoke kurudi kwao na hizo mali tubaki nazo sisi, hana haki ya kupata kitu chochote hapa!"
"Mwanangu unauliza swali gani hilo tena katikati ya majonzi kiasi hiki?"
"Nina haki ya kuuliza kwani aliyefariki ni kaka yangu kabisa."
Watu wote walionekeana kuchukizwa vibaya na jambo hilo.
"Wewe unauliza kama nani katika familia hii maana mimi ndiyo kwanza nimekuoa na sijui hata huyo marehemu kama unamfahamu kwa sura," Violeth aliuliza kwa hasira.
"Mimi dada wa marehemu Mike."
"Kutoka wapi? Eti baba huyu naye nani?" Violeth alijifanya kuuliza.
"Ni nduguyo, nilimzaa huko Moshi miaka mingi iliyopita!"
"Muda wote huo alikuwa wapi mpaka aje leo kuulizia mali ya Mike baada ya kifo chake?" Violeth aliendelea kuuliza akionyesha hasira ya waziwazi, Beatrice alijifunika kwa kanga usoni na kuendelea kulia.
"Nimekwishasema ninayo haki ya kuuliza kama dada na si vinginevyo!" Angelina alijibu kwa ukali.
"Jamani yaani mimi bado namlilia mume wangu leo siku ya tatu tu nyie mnaanza mzozo wa mali? Niacheni nisahau jamani na mali zote nitawaachia kwangu kilichokuwa cha muhimu ni Mike wala si mali, baba naomba mnielewe!" Beatrice alianza kulia tena.
Mzozo huo uliwaudhi sana mzee Rukakingira na mkewe, wakanyanyuka na kutoka nje ambako mzee Martin aliwafuata.
"Mzazi mwenzangu vipi tena hali hii?" mzee Rugakingira aliuliza.
"Bwana hata mimi nashangaa huyu mtoto ndiyo ni mtoto wangu kweli, nilikuwa sijamtia machoni kwa miaka karibu thelathini, ndio kwanza kaja hapa kwangu juzi, leo hii anaulizia mambo yasiyomhusu hata mimi nimeshtuka sana ndugu zangu!"
"Kama ndivyo mlivyopanga basi acha sisi tuondoke na mtoto wetu," mama yake Beatrice alisema.
"Mkifanya hivyo mtakuwa mnafanya makosa makubwa sana na mtatuhukumu kwa kosa lisilo letu, tafadhali hebu mvute subira kidogo nijaribu kulishughulikia suala hili," Mzee Martin alisema.
Baadaye aliingia ndani na kuwakuta watu wote wakilia lakini Angelina alikuwa akisoma gazeti, kitu kilichoashiria kweli alikuwa na roho ya kinyama!
"Binti yangu nakuomba tuongee kidogo nje,” mzee Martin aliingia na kumwambia Angelina ambaye akawa mzito kutoka nje. Hivyo mzee Martin akabidi ayaseme aliyokuwa nayo moyoni palepale.
“Uliyoyafanya yamenifedhehesha sana. Unaona hali uliyoisababisha hapa nyumbani? Sababu mimi nina masikitiko makubwa ya kufiwa na mwanangu, badala ya kuhuzunika wewe unafikiria mali. Nakuomba uondoke hapa kwangu mara moja na nisikuone tena maishani mwangu, sina haja ya kuwa na mtoto kama wewe!"
"Sawa lakini ukweli utabaki palepale kuwa huyu mwanamke ni lazima arudi kwao na mali zibaki kwetu, kwanza ndiye aliyemwambukiza Mike ugonjwa wa UKIMWI," maneno yale yalimhuzunisha kila mtu hata Beatrice mwenyewe alipoyasikia aliangua kilio upya!
"Sawa naondoka lakini nitarudi mpaka nihakikishe mwanamke huyu hapati kitu!" Alisonya, akapanda helikopta na kuondoka zake.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
BEATRICE RUGAKINGIRA 1962-2002 (3)
MPAKA miezi mitatu baadaye Beatrice alikuwa bado hajapona kidonda cha kuondokewa na mume wake moyoni. Kila siku alilia hasa alipopita makaburini akienda kanisani! Alipoliona kaburi la Mike alilia mfululizo na kuna wakati alishinda kaburini kwa mume wake akiimba na kusali! Alifanya hayo yote kumuombea mume wake mpendwa.
Jumatatu ya kwanza ya mwezi wa nne tangu mume wake afariki alipokea wito wa kuitwa mahakama ya wilaya ya Mwanza. Alipoisoma barua ile ilikuwa ni ya kuitwa kwenye kesi ya mirathi!
Aliyeileta kwake alikuwa balozi, mdai alikuwa Angelina Martin Longa, aliyetajwa kama dada wa marehemu na mdaiwa alikuwa Beatrice Rugakingira mke wa marehemu.
Taarifa hiyo ilimshtua karibu kila mtu na mzee Martin alizidi kuchanganyikiwa. Kila alipojiuliza Angelina alikuwa akitafuta nini hasa kutoka katika familia yake, alikosa jibu. Alimchukia kupita kiasi.
Mahakamani Angelina aliwakilishwa na wakili wake Johnson Rutashobya, kutoka Dar es Salaam na Beatrice alisimama mwenyewe kizimbani kwa sababu alikuwa hajajiandaa vya kutosha.
Cha kushangaza na kilichowafanya Beatrice na ndugu wengine waamini kuwa Angelina alikuwa ametembeza pesa, kesi hiyo ilianza kusikilizwa siku hiyohiyo! Jambo ambalo kisheria lilikuwa nje ya utaratibu.
Angelina alikabidhi hati ya urithi aliyodai iliandikwa na marehemu Mike kabla ya kifo chake kuwa mali zote za marehemu azirithi yeye! Nakala ya hati ile Beatrice alipoipata alishangaa na kukuta kweli ilikuwa na saini ya marehemu mumewe.
Alishindwa kuelewa iliandikwa lini mpaka ikamfikia Angelina wakati marehemu Mike alifia mikononi mwake?" Beatrice alimwaga machozi mahakamani.
"Ndiyo, Mheshimiwa, ninayo nakala aliyoandika marehemu mume wangu ikiwa imesainiwa na wakili wetu."
"Basi unaombwa uiwasilishe mahakamani kama utetezi wako, saa tatu asubuhi wiki mbili zijazo, kesi hii inaahirishwa mpaka tarehe hiyo," hakimu alitangaza.
Angelina aliondoka mahakamani kwa gari la kifahari aina ya Nissan Patrol bila hata kusalimiana na mzee Martin! Watu wote walishangaa na kugundua kweli alichotaka ni dhuluma.
"Achana naye huyo mwehu, mama umesema unayo nakala siyo?"
"Ndiyo baba."
"Basi kaitayarishe tutapambana naye yeye si anajifanya ana pesa?"
****
Kumbukumbu alizokuwa nazo Beatrice ni kwamba hati ya urithi aliitunza ndani ya Biblia, hivyo alipofika nyumbani alikwenda moja kwa moja hadi chumbani, na kufungua kabati akaitoa Biblia na kuanza kuangalia katikati ya karatasi zake.
Ingawa hakuwa na uhakika sana lakini alipoiona bahasha aliiweka Biblia pembeni na kuanza kuifungua. Alichokikuta humo kilimfanya atokwe na machozi! Haikuwa hati ya urithi bali barua ambayo Mike alimwandikia Chancellor Edmund kumbe wakati wa kuzitunza alizichanganya!
Hati ya urithi aliiweka ndani ya bahasha ya Chancellor Edmund na kuituma Uingereza na barua yake ndiyo akaiweka ndani ya bahasha ya hati na kuitunza katikati ya Biblia akifikiri katunza hati ya mirathi!
Beatrice aliishiwa nguvu na akahisi kukata tamaa, alijua tayari jambazi Angelina lilikwishamdhulumu mali zote alizoachiwa na mumewe! Alishindwa kuelewa maisha angeyaandesha vipi wakati akisubiri kifo chake.
Akiwa katikati ya mawazo hayo alikumbuka kuwa mwanasheria wao alichukua nakala moja ya hati hiyo! Bila kupoteza muda alitoka akiwa na furaha ya ajabu kuelekea barabara ya Posta ilipokuwa ofisi ya Rwezaura and Co. Advocates.
Aliegesha gari na kuingia ndani moja kwa moja lakini alishangaa kukuta ndani ya ofisi aliyoijua kama ya wakili wao kuna nguo nyingi za kike zimetundikwa.
"Dada habari yako?"
"Nzuri, karibu uchague nguo dada kuna magauni mapya kabisa yameingiza juzi tu kutoka Uingereza!" Dada aliyekuwa akiuza nguo dukani mle alijibu.
"Samahani naomba nikuulize."
"Uliza tu dada yangu."
"Ofisi iliyokuwa hapa ilihamishiwa wapi?"
"Ah, wale mawakili?"
"Ndiyo."
"Walifunga ofisi yao wakaenda masomoni Uingereza, tena wameondoka mwezi mmoja tu uliopita."
Beatrice alihisi kuchanganyikiwa, akaanza kulia mbele ya msichana aliyemkuta ndani ya duka hilo.
"Vipi mbona unalia dada?"
Beatrice hakujibu kitu bali aliondoka bila kuaga, baada ya kutoka dukani hakwenda nyumbani kwake ila alinyoosha moja kwa moja kwenda Nyakato kwa wazazi wa marehemu Mike.
Kwa kasi ya ajabu, Beatrice aliendesha gari hadi Nyakato kwa mzee Martin, akaliegesha, akateremka na kuingia ndani.
"Vipi mwanangu mbona unahema kasi kiasi hiki kimetokea nini?" Mzee Martin aliuliza.
"Baba ni matatizo makubwa sana inavyoonyesha huyu mwanamke ni lazima atatudhulumu mali zote."
"Kwa nini unasema hivyo?"
"Kwa sababu nimeikosa ile hati aliyoandika marehemu kuturithisha mali mimi na Violeth."
Mzee Martin alikaa kimya habari ile ilikuwa nzito kwake.
"Unasema nini mwanangu?" Aliuliza kwa huzuni.
"Ile hati baba nimeikosa!" Beatrice alijibu.
"Imeibiwa au ndio ile aliyoiwasilisha yule mwendawazimu kule mahakamani?"
"Hapana baba, ukweli ni kuwa nilizichanganya," baada ya kusema hayo Beatrice aliinama na kuanza kulia.
Mama yake Mike aliyekuwa jikoni alisikia sauti ya Beatrice akilia. Alitoka mbio kukimbilia sebuleni.
"Vipi tena jamani?" Aliuliza.
"Kuna tatizo kidogo, lakini si kubwa sana," mzee Martin alimpoza mkewe sababu alikuwa ni mgonjwa wa BP!
"Tatizo gani hilo? Hebu niambie upesi maana wengine roho zetu zina mushkeli."
"Mtoto kapoteza ile hati ya mirathi aliyoandikiwa na marehemu mwanao."
"Ni kweli Beatrice?"
Beatrice alieleza jinsi alivyozichanganya barua na hati.
"Sasa tutafanya nini?" Mama aliuliza.
"Cha muhimu nafikiri Beatrice aende nyumbani ajaribu kutafuta angalau namba ya simu itakayowezesha kuwasiliana na Chancellor Edmund, tumwombe atutumie ile hati. Nina imani ni lazima atakuwa bado ameitunza," mzee Martin alisema.
Ghafla mzee Martin alikumbuka kitu.
"Nakumbuka Violeth aliwahi kuniambia kuwa nakala ya hati mliipeleka kwa wakili au siyo mama?"
"Ndiyo baba lakini bahati mbaya wakili hayupo, amekwenda Uingereza kimasomo, ilipokuwa ofisi yao siku hizi kuna duka."
"Basi kajitahidi sana kutafuta namba ya simu au njia yoyote ya mawasiliano ili tuwasiliane na Chancellor Edmund."
"Nitajitahidi kuitafuta namba nikifika nyumbani kasoro pekee ni kuwa baada ya marehemu mume wangu kufariki vitu vingi nilivichoma moto kwa sababu viliendelea kunikumbusha maisha yetu ya nyuma! Lakini nitajitahidi kutafuta..."
***
Mpaka siku moja kabla ya kesi, Beatrice alikuwa bado hajaipata hati ya mirathi aliyoandikiwa na mumewe! Walishauriana na mzee Martin kuwa watafute wakili awawakilishe mahakamani na kuomba wapewe muda zaidi wa kuitafuta hati hiyo muhimu katika kesi yao kwani ilionekna bila hati hiyo haikuwa rahisi kushinda kesi.
Siku ya kesi Beatrice na Angela waliwakilishwa mahakamani na mawakili wao. Wakili wa Beatrice aliiomba mahakama itoe muda wa miezi miwili zaidi ili upande wa utetezi uandae vizuri ushahidi wake.
Hakimu hakukataa ombi hilo alikubaliana nalo na badala ya miezi miwili alitoa miezi mitatu lakini alisisitiza umuhimu wa kupelekwa vielelezo hivyo kwani kulikuwa na uwezekano wa mahakama siku hiyo kutoa hukumu.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Miezi mitatu iliyotolewa na mahakama ilipita, Beatrice alikuwa bado hajafanikiwa kupata anwani wala namba ya simu ya Chancellor Edmund, walipokwenda mahakamani wakili wake aliiomba mahakama iongeze tena muda wa wiki moja ili akamilishe utetezi wake.
Walipotoka mahakamani Beatrice na wakili wake walipata muda wa kukaa na kuongea.
"Nafikiri kitu pekee unachoweza kufanya kwa hivi sasa Beatrice ili kuziokoa mali zote ulizoachiwa na mumeo ni kwenda huko Uingereza na kumtafuta huyo Chancellor nani vile?"
"Edmund."
"Yes, kisheria bila kuipata hiyo hati utapoteza kila kitu."
Beatrice alikaa kimya akimsikiliza wakili wake akitoa maelezo.
"Nina hakika katika muda wa wiki moja utampata na akishakupa hiyo hati rudi hapa mara moja!" Wakili wa Beatrice aliendelea kushauri, baada ya kufikiri kwa dakika tano Beatrice aliibuka na jibu.
"Hamna tatizo, nafikiri itanibidi nijiandae tu na safari. Lakini inawezekana kupata viza hapa Mwanza ya kuniruhusu kuingia Uingereza kweli? Tuliposafiri na marehemu mume wangu kwenda Marekani tulichukua viza Dar es Salaam sasa sijui kama na hapa Mwanza huduma hiyo ipo?"
"Hapa, hakuna, itabidi usafiri hadi Dar es Salaam au Nairobi ambako kuna balozi za Uingereza huko utafanya maombi ya viza, ukishapata viza utakata tiketi na kuondoka, wala usiwe na wasiwasi, ni kitu rahisi tu."
"Sio kazi ngumu kupata viza kweli?" Beatrice aliuliza kwa wasiwasi.
"Sio kazi ngumu kama una vitu vyote vinavyohitajika. Je, pasipoti unayo?"
"Ninayo!"
"Basi hakuna tatizo," wakili alimtoa hofu.
***
Siku mbili baadaye alikuwa safarini kwenda Nyakato kumuaga mzee Martin na familia nzima. Alitegemea kusafiri siku iliyofuata hadi Nairobi ambako angepata viza na kupanda ndege kwenda Uingereza kumsaka Chancellor Edmund.
Kama kawaida, Beatrice aliendesha gari lake kwa kasi kubwa sana. Alipofika maeneo ya sokoni Nyakato karibu na Msikiti, kabla hajakata kona ya mkono wa kushoto kuelekea mtaa wa Mecco ambako ndipo yalipo makazi ya wazazi wa marehemu mumewe, aliona basi la kiwanda cha nguo cha Mwatex likiwa limeegeshwa pembeni mwa barabara, tairi lake la kulia likiwa limefunguliwa. Lilionekana kuwa na pancha.
“Haya magari ya Mwatex bwana! Tangu marehemu aache kazi kila siku yamekuwa mabovu, sijui kwa nini?” Beatrice alishangaa.
Akiwa katika mawazo hayo alimwona mtu mmoja aliyeonekana kama utingo wa basi akimwonyesha ishara ya kusimamisha.
“Haya mashirika ya umma bwana. Sijui watakuwa wanataka spana! Ah! Bwana mimi sisimami mwisho nitamkuta mzee Martin amekwenda kanisani bure!” Beatrice alijisemea moyoni wakati akilipita basi lile na kuendelea na safari yake.
Mtu yule hakusita, alizidi kupunga mkono wake juu huku akikimbia kulifuata gari la Beatrice. Mbele kidogo Beatrice alipoangalia kwenye kioo cha pembeni alimwona yule kijana akiendelea kulifuata gari lake kwa nyuma. Mwisho aliamua kusimama na kuanza kurudi kinyumenyume, alipomfikia kijana yule alisimamisha gari.
"Shikamoo mama!" yule kijana alimwamkia Beatrice huku akihema kwa taabu, kifua kilimbana kwa sababu ya kukimbia.
"Marahaba, hujambo? Vipi gari limeharibika nini? Si basi la Mwatex hilo au siyo?" Beatrice aliuliza.
"Ndiyo mama, tuna pancha kidogo."
"Haya nieleze niwasaidie nini?"
"Hapana mama, wenzangu wamepeleka tairi mjini kuzibwa, ila mimi nina barua yako ambayo nilipewa na Ofisa Usafirishaji miezi minne iliyopita, lakini kwa bahati mbaya nikaisahau kwenye kisanduku cha huduma ya kwanza ndani ya basi. Naomba unisamehe sana mama, naomba tafadhali mama usimwambie bosi atanifukuza kazi."
"Barua yenyewe iko wapi?" Beatrice aliuliza.
"Ngoja niilete mama!" yule kijana aliondoka mbio kuelekea kwenye basi na dakika moja tu baadaye alirejea akiwa na bahasha mkononi na kumkabidhi Beatrice na kupiga magoti.
"Mama naomba sana usimwambie bosi wangu juu ya jambo hili!"
Beatrice aliipokea barua ile na alishangaa kuona juu yake kuna stempu za Uingereza, moyo wake ukadunda kwa kasi na akatokwa na kijasho cha shauku.
Kwa kasi ya umeme, Beatrice aliifungua bahasha ile na kutoa barua iliyokuwa ndani. Juu kabisa ya barua aliona jina Edmund! Moyo wake ukaingia hamu ya kutaka kujua kilichoandikwa ndani ya barua ile. Beatrice hakumkumbuka tena kijana aliyepiga magoti chini na kuendelea kuisoma barua hiyo.
Dear Mike,
At the moment the weather here in the United Kingdom is very cool, people are as busy as bees. How is Tanzania at the moment? And how is your beautiful wife, Beatrice, your dad and mom as well?
Your letter landed in a month ago, I couldn't respond immediately because I wasn't in the UK at the time. I was in Philadelphia on my study tour. Now I', back, that is why you have my letter in your hands!
I was tremendously puzzled when I found a WILL in your letter. That really troubled my mind, and to be frank what I have in my mind right now is that you're not fine Mike! It shows me that you are very sick! I wish I was there to give you my support or could come to Tanzania and help you out of the agony you're facing! But I can't come to Tanzania because I have a very tight programme.
However, I have sent you two British Airways tickets for both of you so that you may come to the UK. As soon as you receive the tickets please come and meet the best doctors in the world. I will be right here waiting for you and ready to pay all the medical costs!
I have also sent back the original copy of your WILL and retained its copy. I did so because there is a long distance between the UK and Tanzania. For that reason, I saw you had the need to stay with the original copy in case anything happens!
I'm looking foward to seeing you in a week!
Thanks.
It is me,
Chancellor Edmund
Get well soon!
Mpendwa Mike,
Kwa sasa hivi hali ya hewa Uingereza ni tulivu ingawa watu wanafanya kazi kwa nguvu kama ilivyo kawaida yao. Vipi Tanzania? Je, mkeo mzuri, Beatrice, hajambo na baba na mama yako nao hawajambo?
Barua yako ilifika hapa mwezi mmoja uliopita lakini sikuweza kuijibu haraka kwa sababu sikuwa Uingereza wakati huo. Nilikuwa Philadelphia huko Marekani katika ziara zangu za kimasomo. Hivi sasa nimerudi ndio maana unayo barua yangu mikononi mwako.
Nilishtushwa sana kukuta hati ya mirathi katika barua yako, suala hilo limenivuruga sana akili na kusema ukweli ninachoamini hivi sasa ni kuwa una matatizo na afya yako si nzuri!
Ningependa sana niwe huko kukupa moyo na kukusaidia kukutoa katika masaibu uliyonayo lakini inaonekana kama siwezi kufanya hivyo kwa sababu hivi ssa nimebanwa na mambo mengi sana hapa Uingereza.
Ila nilichofanya ni kukutumia tiketi mbili za ndege ili wewe na mkeo muweze kusafiri kuja hapa Uingereza kutibiwa na daktari bora kuliko wote duniani na niko tayari kuwalipia gharama zote! Nawategemea hapa katika muda wa wiki moja!
Pia narudisha nakala halisi ya hati ya mirathi uliyonitumia kwa sababu Uingereza na Tanzania ni mbali sana, hivyo ni vyema ukawa nayo HATI halisi ili ikusaidie litakapotokea tatizo lolote.
Mungu akusaidie upone upesi, nategemea kukuona wewe na mkeo katika muda wa wiki moja.
Asante.
Ni mimi Chancellor Edmund.
Ugua pole!
Beatrice alisikitika sana kugundua kuwa kumbe Chancellor Edmund alikuwa hajui kuwa Mike alikwishafariki dunia! Alijisikia vibaya ni kwa nini hakukumbuka kumwarifu.
Pamoja na huzuni hiyo lakini alipoigeuza barua kwa nyuma na kuitia machoni hati aliyokuwa asafiri kuifuata Uingereza alipiga kigelegele cha furaha na kushangilia, akamshtua yule kijana aliyekuwa amepiga magoti ardhini ambaye wakati wote Beatrice alipokuwa akisoma barua alikuwa amezama katika mawazo, akawa kama amezinduka usingizini.
Naye akataka kumsemesha Beatrice ili amhakikishie usalama wake.
"Sasa mama..." yule kijana alianza.
"Hee kijana kumbe upo? Nakushukuru sana na Mungu akubariki," Beatrice alisema akiwa katika hali ya furaha kupita kiasi.
Hakuamini kama muujiza ule ulikuwa umetokea! Shukurani aliyompa yule kijana aliona haitoshi akachukua mkoba wake na kuufungua, akatoa shilingi elfu hamsini na kumkabidhi yule kijana. Kijana yule hakujua ni kwa nini barua ile ilimfurahisha Beatrice kiasi kile lakini alishindwa kuuliza.
"Unaitwa nani, kijana?"
"Mimi?" Yule kijana aliuliza kisha akajibu, “ninaitwa Hollywood..”
"Umenisaidia sana, kijana, matatizo haya yakiisha, njoo ofisini kwangu nitakupa kazi."
"Matatizo gani mama?"
"Siwezi kukuambia sasa hivi."
"Ofisini ni palepale zilipokuwa ofisi za mzee au sio?"
"Ndiyo, njoo baada ya wiki mbili sawa?"
"Sawa mama."
Waliagana.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/*
Bila kuchelewa Beatrice alitia gari moto na kuendelea na safari yake moyoni akiwa amejawa na furaha, alihisi ushindi mkubwa mno dhidi ya Angelina.
"Nimeipata hii haki, yule jambazi sasa amekwisha. He! He! He!" Beatrice alisema na kucheka kicheko cha ushindi.
Alipofika nyumbani kwa mzee Martin aliwasimulia jinsi Mungu alivyo wa ajabu, walisikitika kugundua kuwa Chancellor Edmund hakuwa na taarifa juu ya kifo cha rafiki yake.
"Bwana ashukuriwe sana, mwanangu ulitaka kudhulumiwa kila kitu na Angelina," mzee Martin alisema huku akimshika mkono Beatrice.
Alipotoka pale Beatrice aliipeleka hati ile kwa wakili wake, hata yeye hakuamini muujiza ulioileta hati ile.
"Sasa ushindi ni wako mama na mimi nitahakikisha yule shangingi anakwenda gerezani kwa kosa la kughushi," Revocatus Magesa, wakili wa kujitegemea kutoka Magesa and Co Advocates, alisema.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment