Simulizi : Siku Za Mwisho Za Uhai Wangu
Sehemu Ya Tano (5)
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kesi ya Beatrice na Angelina ilikuwa na mashabiki wengi sana mjini Mwanza, siku hiyo mamia ya watu walifurika katika mahakama ya wilaya ya Mwanza ili kujua hatima ya ndugu yao na rafiki yao, Beatrice ingekuwa nini.
"Haya upande wa utetezi una vielelezo kuthibitisha kweli nyie ni warithi halali wa mali za marehemu Mike?"
"Ndiyo Mheshimiwa na ninawasilisha mbele ya mahakama hii tukufu hati halali ya urithi iliyoandikwa na marehemu siku chache kabla ya kifo chake na ninaomba mahakama hii tukufu isiitambue hati iliyotolewa awali na upande wa mdai kwani hati hiyo ni batili na ya kughushi."
Wakili Magesa alisonga mbele na kumkabidhi hakimu hati ile. Baada ya kuipokea hati ile hakimu alionyesha mshangao wa wazi.
"Naomba niletewe haki iliyotolewa awali na upande wa mdai," hakimu aliagiza.
Zilipoletwa, hakimu aliziangalia na palepale akagonga meza kuashiria kuwa mahakama ilikuwa inapumzika kwa muda. "Mahakama itapumzika kwa muda wa dakika tano, ninaomba nionane na mawakili wa pande zote mbili chemba," hakimu alinyanyuka na kuondoka kuelekea ndani akifuatiwa na mawakili wa mdai na mdaiwa.
Mahakama ilikuwa kimya, Angelina alianza kuona mambo yakimwendea kombo. Mwelekeo wa ile kesi hakuutazamia hata kidogo, katu hakutegemea kuwa Beatrice angeweza kuleta uthibitisho wa kurithishwa mali za Mike. Jasho likamtoka.
Dakika tano baadaye mawakili wote wawili walirejea na punde hakimu naye aliingia na akatoa hukumu yake.
"Mrithi halali wa mali za marehemu Mike Martin ni Beatrice Rugakingira, kama lolote litatokea kwamba Beatrice anashindwa kuziendesha mali za marehemu basi, dada wa marehemu, Violeth Martin, ndiye ataziendeleza," hakimu alitoa hukumu na huo ukawa mwisho wa kesi na watu wote wakatoka nje ya mahakama.
Nje ya mahakama ilikuwa furaha tupu, watu wakimpa mkono wa hongera Beatrice, Violeth na mzee Martin! Angelina akiwa amevimbiana alimfuata Beatrice mbele ya mzee Martin na ndugu wengine bila hata ya salamu na kuanza kumtukana.
"We malaya unajiona bingwa sio? Mali hii itakutokea puani, nakwenda Dar es Salaam lakini yatakayokukuta nyuma utajuta!"
"Lakini wee mwanamke mbona unashupalia kiasi hiki mali ya kaka yangu?" Violeth aliuliza.
"Na wewe funga do..." kabla hajamaliza Angelina alikamatwa na polisi kurudishwa tena mahakamani ambako alitakiwa kujibu shitaka la kugushi hati. Hakuwa na la kujitetea, hivyo alihukumiwa kifungo cha miaka miwili jela.
"Nitarudi tu kutoka jela na mapambano bado yanaendelea!" Angelina alisema wakati anapandishwa kwenye karandinga kupelekwa gereza la Butimba.
***
Baada ya kesi hiyo kwisha Beatrice alimwandikia Chancellor Edmund kumtaarifu juu ya kifo cha mumewe! Haukupita muda mrefu Chancellor Edmund alikuja nchini kuhani na kuzuru kaburi la rafiki yake mpendwa, Mike.
Kutokana na uzoefu wa kufanya biashara wakati wa uhai wa mume wake, Beatrice hakupata matatizo kuendesha biashara yao. Biashara iliendelea vizuri na katika muda wa miaka mitatu tayari mali iliongezeka mara tatu, kwani aliendesha kampuni ya ujenzi kwa ubia na raia wawili wa Uingereza aliotafutiwa na Chancellor Edmund, hisa zake katika kampuni hiyo zilikuwa asilimia sabini.
Beatrice alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa Chama cha Walio katika Mapambano dhidi ya UKIMWI. Alituma pesa nyingi kusaidia kituo hicho na siku zote hakuyasahau maneno ya mumewe kuwa awakumbuke yatima wa UKIMWI na hatawatupa wengine walioteseka na ugonjwa huo, na hivyo ndivyo siku zote alivyofanya. Alifanya yote hayo huku akitambua kuwa huo ndio ungekuwa mwisho wake.
***
Kutokana na utajiri aliokuwa nao Beatrice, vijana wengi hawakuacha kumtaka kimapenzi lakini siku zote jibu lake lilikuwa moja tena la wazi: "Nina virusi vya UKIMWI."
Hata hivyo, pamoja na kuwaeleza hayo bado wanaume waliendelea kumbembeleza wakidai kifo ni kifo.
Siku zote Beatrice aliyafuata maneno ya mume wake: "Tufe peke yetu, Beatrice, usimuue mtu mwingine ni dhambi."
Hakutaka kufanya jambo tofauti na alivyoagizwa na mume wake.
KUMBUKUMBU ZANGU ZIKO WAPI ?
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Sista, hivi mimi naitwa nani?"
"Wewe, unaitwa Beatrice."
"Beatrice? Beatrice nani?"
"Beatrice Rugakingira."
"Na hapa kwenu nilifika vipi na nilikuwa naishi wapi kabla ya kuja hapa?"
"Wewe, ulikuwa ukiishi hapahapa Mwanza."
"Mwanza? Ndiyo wapi?"
"Hujui Mwanza?"
"Sijui! Lakini nilikuwa nafanya shughuli gani kabla?"
Beatrice hakuwa na kumbukumbu yoyote juu ya maisha yake ya nyuma! Hakuwa na kumbukumbu hata juu ya utajiri wote aliokuwa nao! Alikuwa akiishi katika jumba la masista nje tu ya hospitali ya Bugando!
Alikuwa na jeraha kubwa la panga kichwani lililodaiwa kuukaka ubongo wake kiasi cha kumsababishia ugonjwa wa kupoteza kabisa kumbukumbu zake, yaani Amnesia. Wakati Beatrice anapelekwa hospitali ya Bugando miezi sita kabla ya kuhamishiwa kwa masista hakuna mtu aliyetegemea kuwa angepona kwa jinsi mwili wake ulivyokuwa umesambatarishwa kwa mapanga!
***
Ilikuwa ni siku ya Ijumaa, mawingu mazito yalitanda angani na dalili zote za mvua zilionekana. Siku hiyo Beatrice alikuwa na furaha mno kwani ilikuwa ndiyo siku aliyosaini mkataba wa ujenzi wa barabara ya Mwanza hadi Biharamulo kwa niaba ya kampuni yake ya ujenzi iliyoitwa Beatrice & Mike Construction Limited na kukabidhiwa hundi ya dola za Kimarekani milioni hamsini.
Siku hiyo wifi yake, Violeth, hakuwepo nyumbani, alikuwa amekwenda Nyakato kumwona mama yake aliyekuwa na homa ya malaria.
Beatrice alimteremsha sekretari wake, Linda, nyumbani kwao, hatua chache kutoka nyumbani kwake na kunyoosha moja kwa moja hadi ndani ya ngome ya nyumbani kwake ambako aliegesha gari lake.
Saa nzima baadaye alipomaliza kuoga alichukua kinanda chake na kuanza kuimba mapambio huku akijirekodi kwenye redio yake kubwa iliyokuwa sebuleni. Siku zote alifurahia sana kumwimbia Bwana, ilionekana kuwa siku ya furaha kwake, kidonda cha kufiwa na mume wake kilishapona.
Majira ya saa nne hivi usiku, huku mvua kubwa ilikuwa ikinyesha, Beatrice alisikia mlio wa risasi nje ya nyumba yake. Hofu kubwa ilimjaa akaacha kupiga kinanda na kukimbilia chumbani.
Akiwa huko, aliusikia mlango wa mbele ya nyumba yake ukivunjwa na baadaye akasikia vishindo vya watu wakitembea kuelekea chumbani kwake ambako pia waliuvunja mlango na kuingia ndani.
Beatrice alijificha ndani ya kabati kubwa la nguo huku akiendelea kumwomba Mungu aepushe balaa lililokuwa likija mbele yake, alijua kilichokuwa mbele yake ni tabu.
"Baba ikiwezekana kikombe hiki kinipishe lakini mapenzi yako yatimizwe!" Alisema Beatrice akiyakumbuka maneno ya Mwokozi Yesu Kristo, matumaini yake yote alishahamishia kwa Mungu.
"Yuko wapi?"
"Hata mimi sijui."
"Au kapitia dirishani nini?"
"Haiwezekani nondo zote hizi? Ingekuwa ni Uswahilini angeweza!"
Majambazi yalimsaka huku na kule chumbani bila kumwona, Beatrice alikuwa ndani ya kabati akihema polepole kwa kuhofia kugundulika.
"Yuko wapi?" Yaliendelea kuulizana.
"Labda humo ndani ya kabati."
Beatrice alijikuta mkojo ukimtoka kwa hofu!
"Yaani leo ndio mwisho wangu kweli?" Beatrice alijiuliza.
Ndipo kwa bahati mbaya kwa Beatrice na nzuri kwa majambazi, mmoja wao alifungua mlango wa kabati la nguo, alimkuta Beatrice akitetemeka kwa hofu, akamvuta na kumtoa nje.
"Njoo huku wewe kunguni, watu tumeshakula pesa nusu halafu unataka kuleta kiwingu?" Jambazi mmoja alisema.
Beatrice alipowaangalia watu wale aliogopa sana, walivaa vitamba vyeusi usoni na kuacha matundu ya macho peke yake. Walikuwa na sauti nzito zilizokwaruza.
"Jamani msiniue semeni chochote mnachotaka nitawapa!" Alisema Beatrice akilia, alijua watu hao walitumwa na alijua walitumwa na mtu mmoja tu: Angelina.
"Hatutaki pesa yako ila tunakuuliza swali moja. Je, unamfahamu Angelina?" Swali hilo lilifanya mawazo yake kuwa kweli.
"Ndiyo namfahamu! Kwani anahusiana nini na suala hili?"
"Tutakayokufanyia yote ni vema ukamuulize yeye, sisi hatuna kosa lolote ni watekelezaji tu!"
"Lakini jamani nawaomba msiniue! Hebu nisikilizeni kwanza."
"Hapana ni lazima ufe."
Mmoja kati ya majambazi yale lilimwangalia Beatrice kwa huruma na kujikuta likisema maneno ambayo wenzake hawakuyategemea.
"Jamani kwa nini tumuue mwanamke mzuri kama huyu?" Aliwauliza wenzake.
Ghafla jambazi mmoja lilitoka nyuma likiwa na panga, liliwapita wenzake wote na kwenda mpaka mahali alipokaa Beatrice na kuanza kumkatakata na panga bila huruma!
Beatrice alilia akilibembeleza lile jambazi lisiendelee kumtendea unyama lakini jambazi wala halikusikia, liliendelea kufanya hivyo mpaka Beatrice akapoteza fahamu!
"Twendeni bwana! Mnachelewesha kazi wakati pesa zinatusubiri," aliyaambia majambazi mengine na majambazi yote yakatoka nje na kuondoka zao yakijua kazi ya kumuua Beatrice imekamilika. Kilichofuatia kilikuwa kwenda kuchukua mabaki yao.
Asubuhi ya siku ya Jumamosi Linda aliamka mapema na kujiandaa kwa ajili ya kwenda kazini. Kama ilivyokuwa kawaida yake. Alitembea kwa miguu kutoka nyumbani kwake kuelekea nyumbani kwa Beatrice ambako siku zote alipewa lifti na bosi wake hadi kazini.
Tayari jua lilishatoka, ilikuwa ni siku isiyo na mawingu kabisa. Mwanga ulitawala kila mahali, dalili kuwa mvua isingenyesha.
Kabla hajaingia ndani alishangaa kuona damu nyingi sakafuni ambayo ilionekana kutiririka kutoka ndani. Mlango wa nyumba ya Beatrice ulikuwa wazi! Moyo wake ukaruka, akajua ni lazima kuna tatizo lililokuwa limempata Beatrice.
Aliingia hadi sebuleni ambako alikuta damu imetapakaa kila mahali! Hakumwona Beatrice mahali pale na kuamua kwenda chumbani ambako pia hakumkuta! Ndipo alipoamua kurudi sebuleni akiita jina la Beatrice bila kuitikiwa.
"Beatrice! Beatrice! Uko wapi?" Linda aliuliza lakini bado nyumba nzima ilikuwa kimya, akaanza kuita jina la Violeth lakini bado kuliendelea kuwa kimya! Alirudi sebuleni na kuanza kuangaza kila mahali bila kumwona Beatrice wala Violeth. Ndipo alipoamua kuufuata mchirizi wa damu iliyoganda ulioelekea nyuma ya kochi kubwa lililokuwa hapo sebuleni, kule nyuma ya kochi hakuamini alichokiona na kujikuta akipiga kelele kwa sauti ya juu.
"Beatrice what has happened to you!" (Beatrice kimekupata nini?).
Beatrice alikuwa pale amelala chini mwili ukiwa umetapakaa damu! Alikuwa amekatwakatwa mwili mzima, damu ilikuwa haimtoki tena ila mabonge ya damu yalikuwa yameganda pembeni ya mwili wake. Linda alimwangukia na kuanza kumtingisha lakini hakushtuka, alionekana tayari amekwishakufa! Alilia kwa sauti ya juu.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Linda aliikimbilia simu iliyokuwa hapo sebuleni na kuinyanyua ili apige polisi kuwataarifu juu ya kilichotokea. Alishangaa kukuta simu haina mawasiliano yoyote, na alipochunguza vizuri kwa juu aligundua kuwa waya ulikuwa umekatwa.
Hakutaka kupoteza muda, alitoka mbio kuelekea nyumbani kwao ambako aliwasimulia wazazi wake kilichotokea na akapiga simu polisi.
"Ni nyumba namba 150, kitalu namba FFF/555 karibu na Hoteli ya Kamazimas, njooni haraka nafikiri amekufa."
"Kimetokea nini?"
"Mtu kakatwakatwa na mapanga."
"Hiyo nyumba unayoisema sio ya Beatrice?"
"Ndio yenyewe na ni yeye aliyekatwakatwa."
"Mama yangu! Tunakuja sasa hivi!"
Linda alibaki pale akipiga kelele kuita majirani wengine zaidi, kilio chake kilisikika na watu wengi walikusanyika. Kila mmoja wao alikiri kusikia milio ya risasi jana yake lakini hawakuelewa ni nani aliyevamiwa sababu baadaye hali ilikuwa shwari tu.
"Risasi tulizisikia lakini baadaye ikawa kimya hivyo hatukujali sana!"
Dakika kumi baadaye gari la polisi lilifika na kuuchukua mwili wa Beatrice kwenda hospitali ya Bugando kwa uchunguzi. Kila aliyeuona mwili huo ulivyokatwakatwa alijua alikuwa mfu tayari, lakini madaktari walipompima waligundua moyo ulikuwa bado unapiga kwa mbali.
Hali ya Beatrice ilikuwa mbaya kiasi kwamba hata madaktari walikuwa na wasiwasi. Hata hivyo, madaktari waliamua kujaribu kuyanusuru maisha yake.
Bila kuchelewa, zilichukuliwa chupa tano za damu kutoka benki ya damu na Beatrice alishonwa majeraha yake yote huku akiongezwa damu kwa kasi ili kufidia damu iliyopotea.
"Nafikiri atapona ila...!" Mmoja wa madaktari alisema.
"Ila nini?"
"Atakuwa na majeraha sana, hawa watu waliomvamia wanaonekana ni makatili sana, sasa pua yake waliiondoa ya nini?"
"Atahitaji ushauri nasaha ili aweze kuishi vinginevyo hataishi," daktari mwingine aliongezea wakati operesheni ikiendelea.
Habari za kuvamiwa na kukatwakatwa kwa Beatrice zilitapakaa kila mahali. Zilipowafikia wazazi wake huko Bukoba ilibidi wasafiri hadi Mwanza.
Violeth alilia na kuzimia kwa uchungu! Kila mtu alimwomba Mungu muujiza utokee ili Beatrice apone. Ibada na misa vilifanyika katika vituo mbalimbali vya kulelea watoto yatima, ambavyo Beatrice alivifadhili, ili kumwombea apone.
***
Beatrice alilala kitandani kwa mwezi mzima bila kujitambua. Manesi walimsafisha vidonda vyake bila yeye kusikia maumivu ingawa vidonda vyake vilikuwa vikubwa mno. Alikuwa ni kama mfu ingawa alikuwa bado akipumua, mapigo yake ya moyo na shinikizo yalikuwa sawa.
Ndugu na marafiki walishapoteza matumaini, walikaa kusubiri siku ambayo Beatrice angekata roho na kuzikwa!
Siku ya tatu ya mwezi wa pili tangu Beatrice apatwe na mkasa huo, alifumbua macho, kila mtu hakuamini kumwona Beatrice akiangalia tena.
"Linda lete faili la Invoice zote za Rwanda haraka!" Beatrice alisema baada ya kuzinduka akidhani alikuwa ofisini.
Mzee Rugakingira aliyekuwa jirani alimshika na kumtuliza kitandani alipotaka kunyanyuka ili akae.
"...Wewe mtoto tulia Mungu amekusaidia," alimwambia mwanaye. Watu wote waliokuwepo pembeni mwa kitanda walipiga magoti na kusali wakimshukuru Mungu, kwani hakuna aliyetegemea kuwa Beatrice angeweza kufumbua macho tena. Kila mtu alishakata tamaa.
Pamoja na Beatrice kuamka hakuwa na kumbukumbu yoyote juu ya yaliyompata, wala hakukumbuka alikuwa nani! Hakuwakumbuka hata baba na mama yake, sekretari wake, Linda na hata Violeth wifi yake, watu waliokuwa karibu naye sana katika maisha.
Jambo hili liliwashangaza wote ikabidi wamuombe mzee Rugakingira amuulize daktari.
"Mzee, kilichompata Beatrice ni mshtuko mkubwa wa ubongo kutokana na majeraha makubwa aliyoyapata kichwani ambayo yalisababisha vituo vya kumbukumbu kutikisika na kufuta kumbukumbu zote! Hivyo, tunategemea Beatrice atakuwa katika hali hii kwa muda mrefu lakini ipo siku kumbukumbu zake zote zitarejea."
"Kweli?"
"Ndiyo baba, ingawa itachukua muda kidogo! Cha kushukuru Beatrice yuko hai tena."
Kila siku mamia ya watu waliompenda Beatrice walimiminika kwenda kumwona hospitali ya Bugando, wengine walimpelekea chakula, kadi na vinywaji. Kwa sababu ya chanzo cha tatizo la Beatrice, ilibidi chakula na vinywaji vyote alivyoletewa vipimwe kabla hajapewa ili kuhakikisha usalama wake.
***
Ilikuwa ni asubuhi na mapema siku ya Jumatatu zikiwa ni siku kumi na tano tu tangu Beatrice arejewe na fahamu zake. Wauguzi walikuwa wakisafisha wodi, ghafla mmoja wao aliona kikaratasi kidogo chini ya kitanda cha Beatrice.
Alijikuta akitamani kukiokota ili akisome. Kiliandikwa kwa wino mwekundu, maandishi yaliyokuwa katika kikaratasi hicho yalimtisha sana na kumfanya awaite wauguzi wenzake waje mbio karibu na kitanda cha Beatrice.
"Vipi?"
"Jamani huu ujumbe ni nani ameuweka hapa chini ya kitanda cha Beatrice?"
"Sijui kwani unasemaje ujumbe wenyewe?"
"Aisee unatisha!"
"Kwani unasemaje?"
Wote walisogeleana na kuanza kuisoma kwa pamoja kila mmoja wao akitetemeka na kushindwa kuelewa uliandikwa na kuletwa wodini na nani?
“Pamoja na kuwa umepona sijakata tamaa ni lazima ufe tu. Nimedhamiria kukuua na ni lazima utakufa hata kama ungefanya kitu gani kujilinda.
Ni mimi adui yako.”
Yalikuwa maneno machache lakini ya kuogofya. Wauguzi walikipeleka kikaratasi hicho ofisini kwa muuguzi mkuu na tangu siku hiyo watu wa ajabuajabu walianza kuonekana kumtembelea Beatrice katika muda wa kuwaona wagonjwa. Madaktari na masista walipokaa na ndugu wa Beatrice waliamua kwa kauli moja kumhamisha Beatrice wodini kumpeleka mahali kulikokuwa na usalama zaidi.
Usiku wa manane siku iliyofuata, chini ya ulinzi mkali, masista walimbeba Beatrice kumpeleka kwenye nyumba yao ya utawa ambako walimpa chumba maalumu alikoendelea kulala na kupata matibabu yake.
Ni yeye tu aliyeishi katika nyumba hiyo asiye mtawa, hakuna mtu aliyejua Beatrice alikuwa wapi, hata ndugu na marafiki pia hawakuelewa jambo hilo.
Kwa pesa za Beatrice, nyumbani kwa masista, palilindwa usiku na mchana.
"Lakini kwa nini wanataka kumuua msichana huyu?"
"Hata mimi nashindwa kuelewa!"
"Yaani pamoja na kumjeruhi na pia kuiharibu sura yake kiasi hiki bado wanataka kumuua tu?"
"Lakini kwa hapa kwetu kidogo kuna usalama kulinganisha na ulinzi ambao ndugu zake wameweka hapa nje!"
Yalikuwa ni maongezi kati ya sista Florentina na Agnes waliokuwa watawa viongozi wa nyumba hiyo, kila mmoja alionekana kumuonea huruma sana Beatrice.
Mpaka miezi sita baadaye Beatrice alikuwa bado akiishi katika nyumba ya masista. Hali yake haikuwa mbaya, kilichomsumbua ni kidonda kilichokuwa puani kwake, hicho kiligoma kabisa kupona lakini pamoja na hayo yote Beatrice alikuwa na uwezo wa kufanya hata kazi ndogondogo.
Kila siku asubuhi alifanya kazi ya kumwagilia bustani ya maua ya jumba la masista, alipazoea sana mahali hapo na kuona ndipo palikuwa nyumbani kwao! Hakukumbuka kitu kingine chochote katika maisha yake, hakuelewa alikotoka na hakukumbuka hata alikuwa nani.
Kwa jinsi alivyovalishwa na masista, ilikuwa si rahisi kumtofautisha nao kwani alifungwa kilemba cheupe kichwani na kuvalishwa gauni kubwa jeupe na miwani mikubwa iliyofanana na miwani ya macho ingawa haikuwa hivyo.
Yote hayo yalifanyika ili kufanya isijulikane kuwa Beatrice alikuwa ndani ya nyumba ya masista. Ilikuwa ni siri kubwa hata wageni waliotembelea jumba hilo hawakuelewa kuwa Beatrice alikuwa pale.
Lilikuwa ni jambo la ajabu sana binadamu kupoteza kumbukumbu zake lakini huo ndio ulikuwa ukweli. Beatrice hakuwa na kumbukumbu yoyote ile juu ya yaliyotokea maishani mwake.
Mapanga aliyokatwakatwa kichwani yaliziharibu kumbukumbu zake zote kichwani. Kumbukumbu zake zote za nyuma zilipotea, kila alipoangalia mwili wake uliojaa makovu alishindwa kuelewa ni kitu gani hasa kilifanya awe hivyo.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Aligundua wazi hakuwa kawaida lakini hakuelewa tofauti hiyo ilitokana na nini. Kila siku masista walijaribu kuzipima kumbukumbu zake ili kuona kama angeweza kukumbuka lakini mabadiliko hayakuwepo.
"Mimi naitwa sista Floretina, wewe mwenzangu jina lako nani?" Hilo ndilo lilikuwa swali la mtego ambalo masista walimuuliza Beatrice kila siku asubuhi kuona kama kumbukumu zake zilikuwa zimerudi.
"Mimi? Jina languuuuuu! Sijui nani vile?" Hakuwa na kumbukumbu ya jina lake, si hilo tu bali hata utajiri aliokuwa nao! Alimtia huruma kila mtu aliyemwona, sura yake ilibadilika mno.
Beatrice hakuwa mzuri kama alivyokuwa awali, uso wake ulijaa makovu makubwa na hakuwa na masikio wala pua! Vyote vilikatwa na majambazi waliomvamia nyumbani kwake.
Vidonda vyote mwilini mwake vilipona kasoro kidonda kimoja kilichokuwa puani, hicho ndicho kilimpa mateso kila siku! Nacho pia hakuweza kuelewa kilitokana na nini.
"Sista hivi kwa nini kidonda changu hakiponi? Na nilikuwaje? Mbona mimi sikumbuki kuanguka?" Mara kwa mara Beatrice alimsumbua sista Florentina kwa swali hilo.
"Kilitokea tu na kitapona hivi karibuni, usiwe na wasiwasi! Niambie kwanza jina lako nani?"
"Jina langu?"
"Ndiyo!"
"Mmmmmh! Naitw.aa.aaa...B!" Alisema huku akijikuna kichwani, kichwa chake kilionekana kuwa tupu kabisa, ilikuwa ni kama kompyuta mbovu inayowaka na kuzimika yenyewe!
***
Taarifa kuwa Beatrice hakufa baada ya uvamizi wa majambazi aliowatuma zilimtia hasira kali sana Angelina na kulazimika kupanga mauaji mengine. Alilazimika kuwatafuta vijana wake wa kazi na kuwaahidi pesa nyingi zaidi ili wamuue akiwa wodini!
Kwa miezi miwili majaribio kadhaa ya kumuua yalifanyika bila mafanikio, na hatimaye taarifa za mpango huo zilivuja baada ya mmoja wa majambazi aliyemwonea huruma Beatrice kutoa taarifa hizo kwa uongozi wa hospitali. Siku chache baada ya kipande cha karatasi kiliokotwa chini ya kitanda cha Beatrice kilichoandikwa maneno ya kutisha kumuua.
Ndipo masista walipoamua kumhamisha Beatrice kwa siri kutoka wodini kumpeleka katika jumba lao lililokuwa jirani tu na hospitali.
Lilikuwa ni jengo la masista wa Roho Mtakatifu wa Bwana, ambao hawakutakiwa kutoka nje wala kuonana na watu maishani mwao. Walikuwa ni wana maombi na sala kila siku, waliiombea dunia ipate msamaha kwa Mungu!
Usiku na mchana waliishi ndani ya vyumba wakisali. Ni masista wawili tu walioruhusiwa kutoka nje ya jengo hilo, hao walikuwa viongozi wao, sista Florentina na sista Agnes.
Majambazi walimtafuta kwa muda mrefu bila kujua mahali alikofichwa. Hakuna hata mmoja kati yao aliyehisi Beatrice angeweza kuwa ndani ya jengo la masista.
Walifanya kila aina ya upelelezi ili waweze kujua alipo bila mafanikio yoyote. Waliamini wazazi wake walimtorosha na kumpeleka Bukoba lakini upelelezi wao mjini Bukoba na mkoa mzima wa Kagera haukuonyesha hivyo! Walizidi kuchanganyikiwa.
"Nitamuua tu ni lazima afe! Hata kama watamficha wapi?" hayo ndiyo yalikuwa maneno ya Angelina kila siku.
Upande mmoja wa Angelina ulikuwa ni wa ukatili, na huu aliutumia kwa siri kubwa. Upande wake wa pili baada ya kutoka gerezani, aliutumia kujifanya mwanamke msamaria mwema na muungwana, aliyekuwa tayari kuutumia utajiri wake wote kusaidia wenye shida.
Kila mwaka alitumia kiasi kikubwa sana cha fedha kusaidia watu wenye matatizo. Hilo lilimpa heshima kubwa sana katika jamii kiasi kwamba ilikuwa si rahisi kwa mtu yeyote kuamini kuwa Angelina alikuwa muuaji.
Alikuwa miongoni mwa watu waliolisaidia sana jumba la masista kwa chakula na mambo mengine mengi. Alitenga kiasi kikubwa cha pesa kuwasaidia masista wa Roho Mtakatifu na walimheshimu kutokana na msaada wake, bila kuelewa alikuwa ni mtu mnyama kuliko Hltler. Laiti wangejua wasingeipokea misaada yake.
***
Jiji la Dar es Salaam lilikuwa na joto kali sana siku hiyo. Ilikuwa ni siku ya Jumapili jioni, watu walikuwa katika hekaheka za mwisho wa wiki.
Angelina alikuwa nyumbani kwake akiwa amepumzika, kichwa chake kilijaa mawazo alifikiria ni kwa njia gani angeweza kumuua Beatrice. Ilikuwa ni lazima Beatrice afe kwa sababu kuu mbili.
Ya kwanza ikiwa ni kulipiza kisasi baada ya kushindwa kudhulumu mali zilizoachwa na marehemu kaka yake, ya pili ilikuwa ni kuficha siri ya majambazi aliowatuma kwenda kumuua!
Alijua wazi kama Beatrice angepona na kurejewa na fahamu zake vizuri angetoboa siri na kumtia Angelina matatani, kitu ambacho hakutaka kabisa kitokee kwa sababu aliheshimiwa mno na jamii.
Akiwa katika mawazo hayo ghafla simu yake iliita.
"Hallow!" Ilikuwa ni sauti ya sista Florentina akiongea kutoka Mwanza.
"Tumsifu Yesu Kristu sista?" Angelina alimsalimia sista kama alivyozoea siku zote.
"Milele amina!" Sista alijibu salamu hiyo.
"Ndiyo…ndiyo...sista unasemaje leo? Kuna matatizo yoyote?"
"Hakuna matatizo yoyote ila kuna jambo nataka kukueleza, kifupi tunahitaji ushauri wako."
"Jambo gani sista?"
"Kuna msichana ambaye alivamiwa na majambazi kama miezi saba iliyopita na kulazwa hospitali ya Bugando, majambazi walimkatakata vibaya mno na kumtoa hata baadhi ya viungo vyake lakini kwa uwezo wa Mungu amepona!
“Cha kushangaza hao majambazi bado wanataka kumuua na wameshamtumia kikaratasi cha kutishia kufanya hivyo, tulichofanya ni kumtorosha na kuja kumficha hapa kwenye jumba letu."
"Mnaye?" Aiuliza Angelina kwa mshangao.
"Ndiyo tunaye."
"Kweli?"
"Kwa nini nikudanganye?"
Angelina hakuyaamini masikio yake kuwa aliyoyasikia yalikuwa sahihi lakini sista Florentina alizidi kusisitiza jambo hilo na kumwomba Angelina afanye kila awezalo kuwasaidia masista kumhamisha msichana huyo kwa siri kumpeleka Dar es Salaam.
"Nitakupigia kesho sista juu ya mpango nitakaokuwa nimeuandaa! Usiwe na wasiwasi nitawasaidia tu," alisema Angelina na kukata simu.
Bila kuchelewa alinyanyua simu haraka na kuwapigia vijana wake waliokuwa Mwanza kutekeleza mpango wa mauaji, aliwataarifu juu ya mahali alikofichwa Beatrice.
"Yuko kwenye jumba la masista."
"Lipi?"
"La masista wa Roho Mtakatifu."
"Wale wasioonana na watu?"
"Ndiyo!"
"Tutaingiaje huko ndani?"
"Hiyo mimi sio kazi yangu, ninachojua ni kupatikana kwa Beatrice na sitaki mmuulie hapo Mwanza, nataka atekwe na muondoke naye hadi Nairobi ambako nitakuwa nimeshamtaarifu mfanyabiashara mwenzangu aitwaye Njoroge. Huyo atawasaidia kila kitu!
Mtamuua, na hakuna hata mtu mmoja atakayefahamu na wala mfupa wake hautaonekana.
"Sawa mama, basi tupe muda tupange na wenzangu jinsi ya kufanya."
"Muda gani niwape?"
"Saa mbili"
"Oke, nitapiga baada ya muda huo lakini nataka utekaji ufanyike leo hiihii."
Dakika mbili baadaye Angelina alikuwa kwenye simu akiongea na William Njoroge, mfanyabiashara maarufu mjini Nairobi na kumweleza mpango wote aliokuwa nao. Alihakikishiwa kila aina ya msaada na kufurahi sana. Aliwapigia tena vijana wake mjini Mwanza akitaka kujua ni wapi walikuwa wamefikia.
"Mama usiwe na wasiwasi kazi itafanyika! Tayari tumeshapanga mkakati wa kazi, hivi sasa mafundi wanashona mavazi kama ya masista."
"Ya nini?"
"Tutavaa tufanane nao, kisha tutakwenda kwenye jumba lao kama wageni, tukishaingia ndani ya jengo lao risasi zitaanza kulia na tutawaamuru masista wote walale chini, ni hapo ndipo tutakapomteka Beatrice na kuondoka naye.”
"Mtafanya usiku, sio?"
"Hapana, hii inafanyika saa tisa mchana! Tukifanya usiku watatushtukia!"
"Sawa lakini msije mkaua sista yeyote, hiyo ni dhambi kubwa sana."
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Masista walikuwa wameketi sebuleni ndani ya jengo lao baada ya chakula cha mchana. Ilikuwa tayari imetimu saa 8:30 mchana, Beatrice alikuwa miongoni mwao na akicheka pamoja nao! Alifanana kabisa na masista kwa kila kitu, kumbukumbu zilikuwa bado ni tatizo kwake, bado hakuelewa kitu chochote kuhusu maisha yake.
Masista walimsikitikia na kumwonea huruma, walijua alikuwa msichana tajiri kiasi gani ambaye kwa hakika wakati huo alitakiwa awe kwenye shughuli zake za biashara akiendesha makampuni yake. Alikuwa ni mwanamke tajiri pengine kuliko mwanamke mwingine yeyote katika Afrika Mashariki.
"Hivi tutafanya kitu gani ili huyu binti arejewe na kumbukumbu zake? Maana sasa karibu miezi minane tangu apatwe na matatizo yake."
"Daktari alisema ipo siku kumbukumbu zake zitarejea ingawa inaweza kuchukua muda mrefu kidogo."
Waliendelea kuongea mambo mengi pamoja na baadaye ilipotimu saa 9:00 alasiri waliingia katika chumba cha maombi na kuanza kusali.
Dakika mbili tu tangu waanze sala hizo, gari aina ya Range Rover jeusi liliegesha mbele ya jengo la masista, liliendeshwa na kijana mweusi mrefu aliyevaa suti ya rangi ya kijivu.
Katika kiti cha nyuma cha gari hilo, walikaa watu watatu wakiwa wamejifunika nyuso zao kwa vitambaa vyeupe, kichwani walikuwa na vilemba vyeupe na walivalia magauni makubwa ya rangi hiyohiyo.
Maaskari waliolinda jengo la masista walilizunguka gari hilo na kuanza kumhoji dereva maswali mbalimbali ya kiusalama.
"Vipi mzee?"
"Hakuna tatizo nimewaleta hawa masista."
"Masista gani?"
"Masista wa Mtakatifu Marietha kutoka Nakuru Kenya, wapo safarini kuelekea Rwanda na wamependa kupita hapa kuwasalimia masista wenzao!"
"Hakuna tatizo," alijibu askari mwenye bunduki mkononi, na hilo ndilo kosa pekee kubwa alilofanya. Alitakiwa kumuuliza kwanza sista Florentina juu ya ujio wa wageni hao lakini hakufanya hivyo badala yake alifungua lango na gari likaingia moja kwa moja hadi uani mwa jengo la masista.
Sista Florentina na wenzake wakati huo walikuwa katikati ya maombi.
"Wako wapi masista?" Dereva alimuuliza mlinzi.
"Wako kwenye maombi."
"Masista wanauliza chumba gani ili waungane nao?"
"Wapo kwenye hicho chumba kilichoandikwa 26D."
"Sawa, basi wewe unaweza kuendelea na shughuli zako sisi tutawasubiri."
"Sawa!" Alijibu mlinzi na kutoka hadi nje ambako yeye na wenzake waliendelea na kazi ya kuhakikisha kuna usalama kwenye jumba la masista.
Alipoondoka tu majambazi wakiwa ndani ya mavazi ya kitawa walishuka garini na kwenda moja kwa moja hadi kwenye chumba walichoelekezwa. Ndani ya mavazi yao kila mmoja alikuwa na bunduki aina ya SMG tayari kwa kazi.
Waliusukuma mlango na kuingia hadi ndani na kukuta masista wamesujudu wakisali.
"Wote mko chini ya ulinzi, atakayefanya fujo au kupiga kelele atauawa ingawa tumekatazwa kuwaua!" Alisema mmoja wa majambazi kwa sauti ya tahadhari lakini masista hawakuonyesha kushtuka wala kukatisha maombi yao.
Waliendelea kusali mpaka wakamaliza sala yao. Walikuwa masista zaidi ya ishirini, na wote wakawa chini ya mtutu wa bunduki. Walifungwa kamba na kujazwa matambara mdomoni kisha majambazi wakamchagua Beatrice peke yake na kuanza kumvuta kutoka naye nje akiwa amefunikwa mdomo kwa kiganja ili asipige kelele.
Walimtambua kwa alama walizopewa hasa kidonda kilichokuwa puani. Nje walimpakia kwenye gari na taratibu walianza kuondoka na kuwaacha masista wakiwa wamefungwa kamba ndani ya chumba cha maombi.
Walinzi walifungua lango na majambazi waliwapungia mkono na kuondoka kwa kasi. Hakuna mlinzi hata mmoja aliyeelewa kilichotokea.
Walikuja kugundua saa nne baadaye, mpishi alipoivisha chakula cha usiku na kwenda vyumbani kwa masista kuwapa taarifa.
Alishangaa kutomkuta hata sista mmoja chumbani lakini alipoingia katika chumba cha maombi aliwakuta masista wote wamelala chini wakiwa wamefungwa kamba na kujazwa matambara mdomoni.
Alipiga kelele akiwaita walinzi na walipokuja waliamini waliowakaribisha hawakuwa masista bali majambazi. Hawakutaka kupoteza muda waliwafungua masista kamba na haraka waliwakimbiza hospitali ya Bugando ambako walipewa matibabu.
Taarifa zilitolewa polisi lakini zilichelewa kwani wakati huo tayari majambazi walikuwa wakivuka mpaka kuingia Esbania nchini Kenya.
Beatrice alikuwa amefungiwa nyuma ya gari na majambazi walikaa viti vya mbele. Nia yao ilikuwa ni kufika Nairobi siku hiyohiyo na kukamilisha mauaji hayo.
Walipotoka mpakani gari liliendeshwa kwa mwendo wa kasi ya kilometa 250 kwa saa! Ulikuwa ni mwendo wa kasi mno ukizingatia usiku ulishaingia lakini dereva hakujali na wote walifurahia kuikamilisha kazi hiyo kwani walijua malipo yao yalikuwa makubwa mno wakirejea Dar es Salaam baada ya kumuua Beatrice.
Hilo ndilo jambo pekee lililokuwa limebaki.
Kilometa kama tano hivi baada ya kuiacha Esbania, ghafla bila kutegemea dereva aliliona lori kubwa likiwa limeegeshwa katikati ya barabara. Lilikuwa mita kama 50 kutoka mahali gari lao lilipokuwa!
Kwa kasi waliyokuwa nayo, dereva alijua wazi hiyo ilikuwa ni ajali. Alijaribu kukanyaga breki ili lisimame lakini haikuwezekana. Lilijivuta na kwenda moja kwa moja na kuligonga lori kwa nyuma, sehemu ya mbele ya gari lao ilijikunja na kurudi ndani ikiwakandamiza majambazi wote na kuwaua palepale!
Kumfungia Beatrice ndani ya gari kulisaidia sana kuokoa maisha yake! Hakuuumia wala kuchubuka mahali popote zaidi ya mtikisiko mkubwa uliompata. Alifungua mlango kwa haraka na kutoka nje na kuanza kukimbia kuelekea porini ambako alitafuta mahali pazuri chini ya mti na kulala.
Kulipokucha asubuhi alitembea na kuelekea hadi kijijini ambako alikuta watu wakiongelea sana ajali iliyotokea.
"Ajali gani hiyo?" Alijiuliza Beatrice, tayari alishapoteza kumbukumbu juu ya yaliyotokea. Huo ulikuwa utaratibu wa ubongo wake tangu akatwekatwe mapanga, haukutunza kumbukumbu kwa muda mrefu.
Siku hiyohiyo alitembea kwa miguu kurudi hadi mpakani Esbania ambako aliendelea kuishi akirandaranda mitaani. Alionekana kama mwendawazimu na hakuna mtu aliyefahamu ni wapi alikotokea.
Baadhi ya watu walihisi alikuwa ni mkimbizi wa Rwanda aliyenusurika katika vita vya kikabila na kukimbilia nchini Kenya. Walifikiria hivyo sababu ya majeraha aliyokuwa nayo usoni! Hata hivyo, walipokisikia Kiswahili chake waliyafuta mawazo hayo na kugundua alikuwa Mtanzania.
Kwa muda mrefu aliendelea kuishi hapo mpakani kama mwendawazimu. Ndugu zake pamoja na masista walishamtafuta kwa muda mrefu bila mafanikio. Hatimaye wakaamua kupitisha kuwa Beatrice alikuwa marehemu, wakakaa matanga ya siku tatu wakimlilia mtoto wao.
Kupotea kwa Beatrice kulikuwa ni pigo kubwa pia kwa familia ya marehemu mume wake, Mike! Alikuwa tegemeo lao kwa vitu vingi hasa uendeshaji wa miradi iliyoachwa na marehemu mtoto wao.
Miezi mitatu baadaye, siku moja akiwa Esbania akitoka msituni kukusanya kuni kwa ajili ya kubadilishana na chakula hotelini -- kazi aliyokuwa anaifanya ili aweze kuishi kwa sababu hakuwa na pesa -- ghafla aliliona lori kubwa lenye tela likiwa limeegeshwa kandokando ya barabara ya kuelekea Nairobi. Alipolisoma ubavuni aligundua lilikuwa limeandikwa maandishi makubwa ya MIKE TRANSPORTERS LTD!
‘Mmh! Hili jina mbona kama nalifahamu? Hiki ni kitu ninachokifahamu kabisa, ni nini hiki?’ Alijiuliza Beatrice na kuutupa mzigo wake wa kuni na kuanza kukimbia kwenda kwenye mlango wa dereva wa gari hilo.
"Aaah! Mama!" alipiga kelele dereva wa gari hilo na kuruka hadi chini ambako alimkumbatia Beatrice na kuanguka naye hadi chini. Badala ya kufurahi, Beatrice alionyesha mshangao! Hakumkumbuka kijana huyo.
"Malik! Malik! Malik! Njoo umwone Beatrice huyo hapa bado yuko hai!" Dereva alipiga kelele akimwita utingo wake.
"Ndiy...ndiy...ndiyo! Nimekumbuka jina langu naitwa Beatrice! Ndiyo Beatrice Rugakingira, lakini mbona simwelewi anachokisema mtu huyu!" Aliwaza Beatrice.
Kitendo cha kumkumbatia kiliwafanya watu wengi washtuke na kwenda hadi eneo alilosimama Beatrice, dereva pamoja na utingo wake na kutaka kujua kilichotokea.
Walieleza kila kitu na watu wote walishangaa! Beatrice aliyasikia maneno yote na kumbukumbu zake zilianza kurejea polepole, hatua kwa hatua.
"Sasa mtafanya nini?" Aliuliza mama mmoja miongoni mwa watu waliokusanyika.
"Hatuna la kufanya zaidi ya kumrudisha nyumbani, itabidi tuondoke naye kwa sababu hata sisi tunakwenda Mwanza. Watu watashangaa sana kumwona Beatrice akiwa hai tena," alisema dereva.
Siku hiyohiyo walimpakia Beatrice ndani ya gari lao na kuondoka naye. Iliwachukua saa nne kuingia mjini Mwanza!
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Njiani walijaribu kumuuliza Beatrice mambo mengi juu ya mahali alikokuwa lakini hakutoa ushirikiano mzuri ambapo waligundua kwamba hakuwa na kumbukumbu vizuri na hata hakukumbuka kuwa ni yeye aliyewapa ajira. Hawakutaka kwenda moja kwa moja nyumbani kwake, badala yake walinyoosha kuelekea ofisini kwake mtaa wa Nkrumah.
Kwenye makutano ya Barabara ya Kenyatta na Posta walikata kulia na kuingia Barabara ya Posta kuelekea Barabara ya Nyerere.
Ghafla alishtuka na kukaza macho yake na kuangalia pembeni.
‘Mh! Hapa napafahamu mara nyingi nilikuja hapa kuongea na rafiki zangu,’ aliendelea kuwaza Beatrice alipoliona jengo la Hoteli ya Mwanza.
“Hapa ni Mwanza, aisee hivi kumbe nipo Mwanza?!” Beatrice alimwambia dereva.
Baadaye waliingia Barabara ya Nkrumah, mbele kidogo Beatrice alipiga kelele akimwomba dereva asimamishe gari.
"Hallo! Hallo! Hebu simama! Kuna kitu nimekiona hapo!"
Dereva alielewa, alisimamisha gari na Beatrice akafungua mlango na kushuka kwa haraka na kuanguka chini! Alikuwa ameona jengo lililoandikwa MIKE TRANSPOTERS LTD, ilikuwa ni kampuni yake mwenyewe.
"Nilishawahi kuingia katika jengo hili mara nyingi," alisema Beatrice baada ya kunyanyuka chini. Tayari watu walishajaa na hawakuamini kuwa msichana waliyemwona alikuwa Beatrice. Wengi walijua alishakufa, walimwonea huruma kwa jinsi alivyokuwa amebadilika sura yake.
"Masikini Beatrice ndio amekuwa hivi?" Alisema dada mmoja na Beatrice aliyasikia maneno hayo.
Dereva na utingo walimshika Beatrice mkono na kuanza kuvuka naye barabara kwenda kwenye ofisi ya MIKE TRANSPORTERS LTD huku kundi kubwa la watu likiwafuata nyuma! Alipoingia tu ndani, macho yake yalitua usoni kwa Linda.
"Ah! Jamani Linda!" Alipiga kelele Beatrice baada ya kumwona sektretari wake wa siku nyingi.
"Ah! bosi karibu sana!"
“Hivi mimi ni bosi? Bosi wa nani?” Aliwaza Beatrice na ghafla kumbukumbu zote zilimrejea akaanza kulia na kupiga kelele akitaka kukimbia kwenda nje.
"Haooooo! Haooooo! Wananiua! Hao wanataka kunikatakata, hao, wametumwa na wifi yangu Angelina, jamani majambazi hao nisaidieni!"
Kumbukumbu za tukio la usiku alipokatwakatwa kwa mapanga zilimiminika kama filamu kichwani mwake. Beatrice alianguka chini na kuzimia, ikabidi yaletwe maji amwagiwe na baadaye daktari alipigiwa simu na kufika katika muda wa dakika kumi na kukuta Beatrice ameshazinduka.
"Amezinduka?"
"Ndiyo!" alijibu Linda.
"Basi mwacheni apumzike."
"Sawa."
Aliachwa kwa saa nzima lakini muda wote huo alilia na kutetemeka kwa hofu. Picha iliyokuwa ikija kichwani mwake ilimtisha sana! Kutajwa kwa Angelina kuwa ndiye aliyewatuma majambazi kuja kumkatakata mapanga, kuliwafanya wakazi wa mji wa Mwanza kutoa taarifa polisi na maaskari wa upelelezi walikuja haraka hadi ofisini kwa Beatrice.
"Beatrice!" Daktari alimwita.
"Bee!"
"Hawa ni maaskari, wanataka uwaeleze ukweli juu ya jambo lililotokea."
"Sawa nitawaeleza."
Watu wote walikaa kimya kumsikiliza Beatrice akieleza kilichotokea mpaka kukatwakatwa mapanga kiasi hicho. Maaskari walikuwa wakichukua maelezo na waandishi wa habari pia walikuwepo wakirekodi kila kitu alichokisema.
Kilikuwa ni kitu cha kushangaza sana kwa mtu aliyeaminika kuwa mfu kuonekana tena! Watu wengi hasa wanawake walisikika wakilia nje ya ofisi sababu ya kumhurumia Beatrice.
"Jana nilikuwa nyumbani baada ya kutoka kanisani," alianza Beatrice akifikiri labda tukio hilo lilitokea siku moja kabla wakati ilishapita miezi mingi tangu tukio hilo litokee.
Alieleza kila kitu kilichotokea, jinsi majambazi walivyoingia na walivyomweleza kuwa walitumwa na Angelina ili wamuue.
"Niliwauliza wamepewa shilingi ngapi ili niwape zaidi lakini walikataa na kuanza kunikatakata kwa mapanga bila huruma mpaka nikapoteza fahamu kabisa!" alimaliza Beatrice na kuanza kulia.
Baada ya maongezi askari waliondoka hadi kituoni wakiwa na hasira kali dhidi ya Angelina na siku hiyohiyo mawasiliano yalifanyika kati ya Mwanza na Dar es Salaam.
Angelina alikamatwa na kupewa mateso makali kupita kiasi, alishindwa kuvumilia na kuwataja majambazi wote alioshirikiana nao kufanya unyama huo ambapo nao walitiwa mbaroni siku hiyohiyo jijini Dar es Salaam.
Walipofikishwa mahakamani ushahidi wa kutosha ulikuwepo na hawakuwa na jinsi ya kuruka, wote pamoja na Angelina mwenyewe walikiri kosa na kuhukumiwa kunyongwa.
***
Miezi mitatu baada ya hukumu ya Angelina na wenzake, hali ya Beatrice iliendelea vizuri, kumbukumbu zake zilikuwa sawa na aliendelea na kazi zake kama kawaida. Kilichomsikitisha kilikuwa ni sura yake!
Kwani kila alipojianglia katika kioo, roho ilimuuma sana, muda mwingi alilia kila alipoiangalia picha yake ya zamani aliyoibandika ofisini mwake na kuona tofauti iliyokuwepo kabla na baada ya kuvamiwa na majambazi.
Alipatwa na simanzi kubwa sana moyoni mwake, kwani vitu vingi vilimuumiza. Hakuweza tena kujiangalia kwenye kioo! Alikiogopa na alikiona ni adui yake, kila alikopita watu walimshangaa na kuonyeshana kwa vidole na alikuwa gumzo la kitu mtu mjini Mwanza na Tanzania nzima kwa ujumla.
Kasoro pekee iliyokuwepo katika mwili wake ni kidonda cha puani, hicho hakikukubali kabisa kupona! Kilizidi kuchimba kwenda ndani zaidi, hatimaye alijikuta amerudishwa tena hospitali na kulazwa. Alipewa matibabu kwa muda mrefu lakini kidonda hakikupona na hali yake ilizidi kudhoofika.
Hatimaye Beatrice alikufa kwa mateso makali lakini kabla ya kifo chake aligawa mali zake kama ifuatavyo: Asilimia 25 alitoa kwa wazazi wa Mike, asilimia 10 kwa sektretari wake Linda, asilimia 15 kwa wifi yake Violeth na asilimia 50 kwa watoto yatima wa UKIMWI na pia aliacha ujumbe kwa vijana wote duniani akisema kilichomponza yeye ni mapenzi na kutofikiria maisha ya baadaye.
“Nilimpenda Mike lakini sikutakiwa hata kidogo kumlazimisha alipokataa kunioa! Sikutakiwa kumlazimisha kwa sababu alishagundua kuwa ana virusi na mimi sikuwa navyo na simlaumu Mike kwa kitu chochote kilichotokea maishani mwangu.
Nawaonea huruma sana watu waliobaki duniani, wakubwa kwa wadogo, kwani ugonjwa huu si wa kuchezea. Ni vyema watu wakachukua hatua madhubuti kubadilika, dunia nzima ni lazima iungane katika vita hivi.
Kama hapatakuwa na ushirikiano hakuna atakayebaki hai si Mwingereza, Mmarekani, Muasia, Mwafrika au mtu yeyote yule. Ni lazima watu wote duniani waelewe kuwa wapo ndani ya mtumbwi mmoja unaopita katika bahari iliyochafuka!
Kama ukizama hakuna atakayedai yupo salama...” ilisema sehemu ya barua hiyo na Beatrice akawa amepumzika kwa amani!
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
MWISHO.
Nawashukuru wasomaji wote ambao mmekuwa mkiifuatilia simulizi hii toka pale ilipoanza. Ninashukuru kwa maoni yenu, ushauri wenu na hata kuniambia pale nilipokuwa ninakosea, kwa staili moja au nyingine, mmekuwa mkinikomaza zaidi ili nije kuwa mwandishi mzuri zaidi ya nilivyo kwa sasa.
0 comments:
Post a Comment