Search This Blog

Sunday, July 10, 2022

USILIE NADIA - 1

 





    IMEANDIKWA NA : GEORGE IRON MOSENYA



    *********************************************************************************



    Simulizi : Usilie Nadia

    Sehemu Ya Kwanza (1)



    Mwendo wa kutoka nyumba ya kulala wageni tuliyolal usiku uliopita haukuwa mkubwa sana hadi kuifikia staendi kuu ya mjini Musoma ambayo ujenzi wake ulikuwa unaendelea bado licha ya kwamba ilikuwa imeanza kutumika. Mara yangu ya mwisho kuingia katika mji huo ambao ni makao makuu ya mkoa wa Mara kituo cha mabasi bado kilikuwa kipo katikati ya mji.

    TULIPOFIKA kituo cha mabasi tuliangaza huku na kule huku tukikwepa usumbufu wa ‘wapiga debe’ wa kutuchagulia gari la kupanda huku wakitoa sifa kedekede kuhusu gari wanalolipigia debe.

    “Tupande Zacharia Coach” alininong’oneza binti yule huku akinielekeza mahali zilipo ofisi zao. Tukajongea huku kila mmoja akiwa ametundika begi lake mgongoni. Nilimsaidia kubeba kifurushi kimojawapo.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Baada ya kupata tikiti zetu mbili ambazo zilituruhusu kuketi pamoja katika basi lenye hadhi ya V.IP, tulijongea upesi garini japo muda wa kuondoka ulikuwa haujafika. Lakini hatukuwa na jambo lolote la kutufanya tukae nje.

    “Naomba nikae dirishani kaka” aliniomba, nikamruhusu nami nikaketi mkono wake wa kushoto, hapa sasa niliweza kumchunguza kidogo kwa macho ya kuibia ibia nywele zake jinsi zilivyokuwa zimenyonyoka, huenda ni kwa sababu ya kukosa matunzo. Uso wake ulikuwa umechujuka na ile rangi yake ya asili ilikuwa imetoweka. Alikuwa na mabaka mabaka yasiyokuwa rasmi na ambayo nilikuwa sijajua sababu yake.

    Nikiwa katika kumchunguza mara alinigeukia huku macho yake yakiwa yanalengwa lengwa na machozi. Midomo ikimtetemeka, bila shaka alikuwa anataka kusema kitu, ama la kuna kumbukumbu ilimjia. Ni hicho ambacho nilikuwa nataka kutoka kwake.

    Upesi nikafungua begi langu, nikatoa kijitabu changu kidogo na kalamu kisha niitegesha na simu yangu upande wa kunakili sauti. (sound recording).

    Badala ya kusema neno alitazama nje pale dirishani, nami nikachungulia na kukutana na wauzaji wa bidhaa ndogo ndogo, sikujua hii inamaaanisha nini.

    Binti yule akageuza kichwa na kunitazama sasa alianza kuzungumza



    AKAANZIA HAPA. Nami nikamrekodi huku kiuandishi nikinukuu mazingira na muonekano wake ili nisipoteze uhalisia.



    “Mara ya kwanza kabisa nilikutana naye hapa, alikuwa anauza maji na soda za kopo pamoja na biskuti. Sikuwa na mpango wa kununua chochote lakini ucheshi wake ukanifanya ninunue soda ya kopo, huwa sipendi kula nikiwa safarini. Sipendi kabisa. Sijui nini kilinivuta kwake, nikanunua. Akatabasamu baada ya kuona amefanikiwa kunishawishi, wakati anataka kunipatia chenchi yangu mara gari likaanza kuondoka, nilikuwa nimempatia shilingi elfu mbili tu na alitakiwa kunirudishia shilingi elfu moja. Nikamsikia anapiga mayowe ya kuzuia basi lisiende anipatie pesa yangu, nilitamani kupiga kelele kumwambia abaki na ile pesa lakini sikubarikiwa uwezo wa kupiga kelele. Nilikuwa siti ya dirishani kama leo hii hapa, nikachungulia anapotokea ili kama nikifanikiwa kumuona nimpungie mkono na kumuashiria kuwa sihitaji pesa ile. Na kweli sikuwa na haja na pesa ndogo kama ile, nilikuwa na nyingine nyingi. Lakini mara macho yangu yakashuhudia kitu kibaya sana kijana yule alijibamiza katika basi jingine akapiga mweleka chini, maji na juisi zake zikatapakaa huku na huko. Hapo sasa niliweza kupiga kelele huku nikiwa nimetaharuki. Yule kijana alikuwa amepata ajali.



    Safari yangu ikaharibika, nikawa namlilia mwanaume nisiyemjua hata jina na ilikuwa mara ya kwanza kuonana naye. Nililia sana bila kukoma, hakuna aliyeweza kunibembeleza maana ni moyo wangu ulikuwa unalia. Walionitazama nje hawakujua lolote.

    Laiti kama ningejua lijalo, nisingethubutu kununua maji yake mwanahizaya mkubwa yule, nisingethubutu kusema naye na nisingedanganyika na ucheshi wake hata kidogo. Yaani nikamlilia nikiwa hat simjui lakini yeye akaja kuniliza huku akiwa ananijua kila kitu nje na ndani. Akiwa anaijua historia yangu, ile siku analifukuza gari ili anipe chenchi yangu kisha akagongwa na gari akaibadilisha na kuja kunifukuza mimi ili anipige. Desmund! Desmund!! Hakufanikiwa kulipata gari alilokuwa akilifukuzia ili anipe chenchi yangu lakini alifanikiwa kunipata Desmund akanipiga, tazama alichonifanya (Hapa akajifunua kidogo blauzi yake upande wa bega…kidonda!! Sijui niite jeraha…nikachukua kamera yangu nikampiga picha.)…..kisha akaendelea tena “Desmund kweli aaargh!.....akanikanyagia chini bila huruma hata kidogo. Siku alipogongwa na gari nilitoa kelele kidogo lakini siku hii nilitoa kelele kubwa, hakukithamini kilio changu Desmund. Akanitemea mate kisha akaniita Malaya ninamtia kichefuchefu. Akaenda ndani ya nyumba, akaufunga mlango. Nikalala nje kwa mara ya kwanza. Mvua kali ilinyesha yote ikatua katika mwili wangu. Asubuhi alipoamka aaargh Desmund….hivi hakutosheka kunilaza nje ya nyumba yangu. Hakuridhika kwa mimi kunyeshewa mvua, akaniamkia asubuhi na kipigo, eti namdhalilisha na sikupaswa kuwa katika historia ya maisha yake!! Yaani mimi…mimi niliyeibadili historia mbaya ya maisha yake leo hii anasema sikustahili kuwa katika maisha yake…yaani kwa mambo yote niliyomfaanyia mimi…akaniita mbwa ninayefaa kuishi na kula jalalani.” Hapa akashindwa kuendelea alikuwa anatetemeka sana, uso wake ukawa mwekundu sana, mikono ikawa inatetemeka na kisha akawa anatokwa jasho. Bila shaka alikuwa na hasira iliyopitiliza. Upesi upesi nikahifadhi kamera yangu, ‘kinasa sauti’ na daftari langu vyote pamoja na kalamu nikahifadhi katika begi.

    “Usilie Nadia jamani!!” nikamchukua kichwa chake, nikakilaza katika bega langu. Machozi yake yakawa yanatua katika shati langu. Alipokuwa amenilalia niliweza kuyahisi mapigo yake ya moyo. Yalikuwa yanaenda kasi sana. Na midomo ikizidi kumcheza cheza, nikajipapasa na kutoka na leso, nikamfuta machozi yake huku nikikumbuka kuwa binti huyu ana kilio moyoni haya machozi ya nje kwake si tatizo. Nikajikaza sana nisionyeshe udhaifu nami nikatokwa machozi.

    Maswali na majibu yalishaanza kurindima katika kichwa changu.



    MOJA. Kumbe jamaa anayehusika na hali niliyomkuta nayo anaitwa Desmund!!

    MBILI. Kumbe alikutana naye stendi akiwa masikini wa kutupwa. Nini kikajiri sasa?

    TATU. Baadaye wakaunda mahusiano? Waliunda vipi sasa mahusiano wakati walionana na kuachana pale stendi?.

    NNE. Jamaa aliwahi kumpiga? Kisa nini sasa. Tena akamwita mbwa!!!

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    BAADAYE binti akanyamaza, sikutaka kuwa na papara za kumuuliza maswali katika mfumo wa ‘Swali na jibu la papo hapo’ nilihitaji zaidi maelezo ili nikiandika kitabu kiwe na mashiko ndani yake. Na ili kitabu kiwe hivyo basi ni vyema msimuliaji aamue mwenyewe kusema bila kuulizwa. Ama la mwandishi atumie mbinu zake ili msimuliaji ajibu bila kujua kama ameulizwa.

    “Hii barabara yenu imenyooka sana….” Nilimgusia ili asikumbuke machungu ya alichokuwa anasimulia awali juu ya jinsi alivyokutana na Desmund.

    Alinijibu huku akiwa amechangamka, lakini sikujua kama swali langu linaweza kuleta athari kwake!!

    “Ndio ni nzuri lakini zamani sasa dah! Palikuwa na mashimo mashimo, sikudhani kuwahi kutegemea nitakuja kupita barabara kama hii. Mwaka ule ninakuja huku palikuwa hapapitiki, mimi nilidhani kuwa nilipoondoka kuwa sitarudi tena huku hata rafiki zangu niliosafiri nao kipindi kile walinambia ‘Nadia hutaweza wewe mtoto mayai’ …nilicheka tu huku nikilazimisha kuwa nitaweza. Ilikuwa haki yao kusema kuwa sitaweza, mimi mzee wangu amenidekeza, sio mimi pekee hata dada na kaka zangu wote walidekezwa sana yaani, sijui hata pale nyumbani nilikuwa nakosa nini. Shuleni napelekwa na gari na kurudishwa hivyo hivyo, nilipoingia chuo na kuchaguliwa kusomea Mwanza, sikuwahi kupanda basi kila likizo ni ndege kila likizo ndege tu. Si kwamba sikuyafurahia maisha yale la! Ila kwa kiasi fulani yaliwafanya rafiki zangu wanione mimi mzembe na ndo maana hata rafiki yetu alipofiwa na baba yake huko Mugumu Serengeti nami niliposema kuwa naenda kumsindikiza walinambia kuwa ‘Nadia huko hakuna ndege wala uwanja wa ndege’ baki tu. Sikukubaliana nao kirahisi, ule ulikuwa msiba. Nikalazimisha nikaenda, huko Dar es salaam, baba na mama hawajui lolote. Nd’o nikaujua uchungu wa kupanda basi tena barabara mbovu. Kutoka Mwanza hadi Musoma hapakuwa na tatizo lakini kutoka Musoma kuelekea Serengeti, nilifika nikiwa mgonjwa lakini sikutaka kudeka ule ulikuwa msiba nilikunywa dawa za kutuliza maumivu kisha nikalala, nilikuwa msichana pekee mwenye asili ya kiarabu katika msiba ule.

    Maisha ya kule yalinishinda lakini nilivumilia, ukarimu wa watu niliowakuta kule ulinipa faraja nikayasahau machungu. Siku tuliyoondoka ndo niliapa kuwa sitakanyaga kule tena kwa namna yoyote. Rafiki zangu walinitania kuwa naweza kupata mchumba kutoka huko itakuwaje niliwajibu kuwa ni heri nisolewe kabisa. Lakini cha ajabu sasa ambacho hadi leo ninakishangaa nilipofika Mwanza nilirudi peke yangu tena kule Musoma, kwa lengo ambalo hadi wakati huu sijui shetani gani alilileta kwangu, nikarudi Musoma kwa ajili ya Desmund.

    Desmund kijana aliyeniuzia maji kisha akapata ajali. Nilishuka pale Musoma na kuanza kuulizia huku na kule, lilikuwa limepita juma moja tu tangu ajali ile itokee, hivyo taarifa zilikuwa zimezagaa. Nikafanikiwa kumwona tena.



    Alhamdulilah!! Alivunjika miguu yote miwili, na mwajiri wake alikuwa hayupo tayari kumuhudumia, na tayari alikuwa ametafuta kijana mwingine kwa kazi ileile. Alikuwa amedhoofu sana, na matusi kutoka kwa madaktari kuwa watamfukuza pale hospitali kwa sababu hakuna ndugu anayefanya malipo yoyote. Sikungoja zaidi, nilifanya malipo kama yalivyohitajika, bado alikuwa akinishangaa kuwa mimi ni nani. Huduma ikaboreshwa, nilikesha pale wodini nikizungumza na naye na ni siku hiyo aliponiambia jina lake. Desmund!!



    Nilikesha nikiumwa na mbu mimi, nikajitoa kwa moyo wote japo ajali sikuipanga mimi, lakini yeye aliponipiga na na mpini wa jembe akanivunja mguu aliniacha nikilia peke yangu barabarani, yaani kweli Desmund mimi kukuuliza tu yule mwanamke ni nani ukanipiga hadharani aah. Wema wote niliouonyesha kwake, uvumilivu wote nilioufanya kweli akaishia kunikana hadharani kwamba nilikuwaga demu wake tu lakini tumeachana tayari. Watu nisiowafahamu wakaniokota na kunipeleka hospitali nikiwa sina hili wala lile Desmund hakuja kunisalimia, hakuja kulipa bili nilizokuwa nadaiwa. Kale kasimu kangu nikaamua kukauza ili nipate tiba kwa mguu wangu uliokwisha teguka. Nilisaidiwa kurudi nyumbani baada ya kupata nafuu huku nikitumia mpini wa jembe kujikongoja…yaani Nadia mimi nikafikia kumkufuru Mungu sasa. Ndani ya chumba changu kitanda changu ninacholalia na Desmund wangu..nikakuta chupi na sidiria ..havikuwa vya kwangu. Kwa hiyo kumbe Desmund….De…De…” akashindwa kusimulia kilio kikaanza tena wakati huu safari ilikuwa inaendelea. Upesi nikahifadhi vifaa vyangu. Nikamchukua na kumlaza katika mapaja yangu, nikausikia mwili wake wa moto ukizidi kuchemka.

    “Usilie Nadia…yamepita hayo mpendwa wangu…USILIE NADIA….USILIE” nilimsihi kwa upole na sauti ya chini…….

    Wakati huo kichwani yakifuata maswali kadhaa na majibu.



    MOJA. Kumbe Nadia alikuwa mtoto wa familia bora? Sasa kulikoni mbona kachakaa kiasi kile.

    MBILI. Kumbe Desmund alikosa wa kumuhudumia akatunzwa na Nadia, sasa mbona akamvunja mguu? Nadia alikuwa na kasoro gani kwani.

    TATU. Halafu Desmund akaleta msichana nyumbani kwake? Hivi ilikuwa maksudi? Mpuuzi sana huyu. Halafu kumbe nd’o chanzo cha kumpiga kisa kuulizwa yule msichana ni nani? Au huyu alikuwa mwingine?

    NNE. Hivi Nadia na kuchakaa kote huku kumbe ana elimu ya chuo kikuu tena chuo chenyewe kikuu kwelikweli!!! Sasa mbona hafanyi kazi!!

    TANO. Familia yake ilikuwa wapi huyu bwege anamnyanyasa hivi? Na ni mkoa upi huo waliishi??







    Mwandishi wa habari wa kujitegemea na pia simulizi za kweli zinazotokea duniani. Mwandishi wa vitabu vya chokoraa, Hatia, Kizuizi, Nisamehe Tanga na kile kitabu chake matata cha Albino wa kimasai, yupo na mwanadada Nadia katika kuiandika simulizi nyingine. Wapo ndani ya basi, kuna safari wanafanya. Safari hii inaanzisha safari nyingine ya Mwandishi kuandika juu ya maisha ya Nadia. Maisha yaliyomchakaza na kumnyong’onyesha, maisha yanayomfanya awe mtu wa kulia tu!....mwandishi anatumia mbinu ya kumwacha Nadia ajieleze bila kuulizwa, mbinu hii inamsaidia kujua mengi kwani ‘MTU MWENYE HASIRA HUSEMA MENGI KULIKO YULE ASIYEKUWA NAZO’

    Kuna maswali hayajapata jibu na kuna mengine yamepata ufumbuzi.

    Mwandishi amefahamu kuwa Nadia anamlilia Desmund, huyo Desmund aliwahi kuwanaye kimapenzi……mapenzi yaliyozua utata, utata uliomchanganya na kupoteza uelekeo wa Nadia. Sasa yupo na mwandishi wanasafiri. Mwandishi hajui lolote, Nadia ndiye anasimulia.

    Katika fasihi andishi usimuliaji huu unaitwa mfumo Rejea ambatano na mfumo MOJA KWA MOJA.



    Baada ya kumlaza mapajani kwangu huku akilia kwa uchungu mkuu, nami nikifanya jitihada za kuyafuta machozi yake. Hatimaye Nadia alitulia. Nilipomtazama alikuwa amepitiwa na usingizi, nikamfunika na upande wa kanga yake. Kisha nikaiweka mikono yangu vyema aweze kuegemea vizuri.

    Ukimya uliotanda ukanifanya nami nianze kusukwa sukwa na usingizi, nilijitahidi kuukabiri lakini sikuweza. Nikajiegesha vyema katika kiti, nikasinzia pia.



    SAUTI nzito ya mpiga debe ndo ilitukurupua.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/---

    “Oyooo mwisho wa gari hapa!!”



    Nadia naye alisikia sanjari na mimi, tukatazamana na kutabasamu kama kwamba tuliambiana kufanya hivyo. Nadia akajinyoosha huku akipekecha macho yake, mimi nikajishughulisha katika kuweka sawa mabegi yetu. Tukatoka ndani ya gari tukiwa abiria wa mwisho kabisa. Tukaikanyaga stendi ya Buzuluga jijini Mwanza, safari yetu fupi kutoka Musoma kwenda Mwanza ikawa imekamilika.



    Nadia alilalamika njaa inamuuma. Nilitazama huku na kule nikauona mgahawa ng’ambo ya pili ya barabara. Nikamshika kiganja cha mkono wake, tukavuka barabara kama hatuzisikii kelele za madereva taksi waliokuwa wakitupigia kelele ili tukodi mojawapo ya teksi kwa ajili ya safari yetu.

    Hakika tulikuwa na haja na teksi lakini matumbo yalikuwa matupu, tulihitaji chochote kitu hasahasa cha moto.

    Tulisfutahi kimya kimya bila mazungumzo baina yetu. Kila mmoja alionekana kuwa na uchovu wake.

    Baada ya hapo nd’o tulihitaji taksi, ikatuchukua hadi G & G Hotels, ni huku nilipendekeza. Teksi ilipotoweka, Nadia aliniuliza swali.

    “Umeifahamu vipi hii hoteli kaka.”



    Kwanza nilimtazama huku nikitafakari nini cha kujibu.

    “Hi ndo hoteli yangu mara kwa mara nikitembelea jiji hili.” Nilimjibu, kisha nikaongezea kidadisi, “Kwani kuna tatizo?”

    Hakujibu kitu nami sikuuliza tena, nilitambua kwa nini hakujibu, bila shaka ni uwepo wa watu kadhaa mahali tulipokuwa, nikajisogeza mapokezi nikafanya malipo ya vyumba viwili tofauti vyenye hadhi ya ‘Deluxe’ kisha nikamfanyia ishara Nadia akanifuata. Nikamwongoza hadi katika chumba ambacho angelala siku ile.

    Alipokiona chumba alishusha pumzi kwa nguvu, nikakifungua akaingia, hapa akafika na kusimama katikati ya chumba akiwa anatazama dirishani. Upesi nikachukua vifaa vyangu. Bila shaka Nadia alitaka kujibu lile swali dogo nililomuuliza na kutarajia majibu ya kawaida.



    “Kila moyo huwa na shukrani, lakini mwanadamu hana shukrani. Naamini kabisa mwanadamu hana shukrani, Afadhali Punda aliyejiweka wazi na shukrani yake ya mateke kuliko mwanadamu. yaani angekuwa mlemavu Yule. Huduma mbovu za kule Musoma wakadai anatakiwa akatwe mguu. Nikamdanganya mzee wangu kuwa nimepoteza Laptop ya rafiki yangu yenye thamani ya milioni nyingi. Mzee wangu mimi na upendo wote anaonionyesha lakini bado nikamdanganya eti kisa Desmund. Tukakodisha usafiri akaletwa Bugando, naikumbuka siku aliyofika kwa mara ya kwanza tulifikia hoteli hii, laiti ningeyajua ambayo yangekuja kutokea nisingepoteza pesa zangu wala nisingemlaghai baba, Desmund bila ndugu yeyote mimi nikawa kila kitu. Alifikia hatua ya kuniita Mungu wake, akanililia siku ambayo aliweza kusimama kwa mara ya kwanza, nikamshika mkono akiwa anafanya mazoezi ya kuimarisha miguu, nikaacha kuingia darasani hadi alipopona.



    Nilipomrudisha Musoma kwao ndo hapo niliposikitika zaidi, kile chumba alichokuwa akiishi Desmund tulimkuta mtu mwingine, alipoulizia samani zake akapewa mkeka na sufuria ndogo mbili. Nilishangaa lakini yale nd’o yalikuwa maisha yake halisi.



    Sitaisahau siku ambayo tulilala wote ili nimtazame afya yake, sikutaka awe mbali nami. Moyoni nilianza kukumbwa na pepo mchafu, pepo wa maajabu aliyesema eti siwezi kukaa mbali na Desmund. Nikalala naye katika hoteli ya Grand Villa huko Musoma. Ni usiku huo ambapo nilianza rasmi mahusiano na Desmund, vishawishi vya kimwili, tamaa ya muda mfupi nikajikuta kwa hiari yangu nafanya mapenzi na Desmund. Siwezi kusema alinilaghai la! Hata yeye hakutegemea kama jambo hilo litatokea, hakika siwezi kujuta maana ni upendo wa dhati ulinituma.



    Desmund akatumia neno hilo ‘nakupenda’ nililomtamkia kuanza kunisulubu. Alijua nampenda sana hilo alilijua hadi siku ya mwisho na ataendelea kulijua. Nikampangia chumba kikubwa na kumnunulia baadhi ya vifaa vya ndani, hii nyumba ikaja kuwa chungu kwangu kile kitanda, lile godoro na mashuka niliyonunua mimi ikafikia kipindi akawa jasiri kuingiza wasichana pale ndani. Alimuingiza hadi yule msichana ambaye alisababisha anitegue mguu kwa mpini wa jembe.

    Desmund alikuwa mshamba wakati naanza naye mahusiano, hakuna chakula cha kifahari alichokitambua zaidi ya Chipsi kuku. Nikamwonyesha dunia ilivyo, hakujua hata mkanda wa ndege unafungwa vipi? Nikampandisha ndege….hakujua nini maana ya ‘body exercise’ yote haya nikamwonyesha mimi, akatanua kifua na kuvaa vizuri hatimaye akapendeza.



    Kweli yule Desmund ambaye hata hakuwa akijua nini maana ya ‘Piza na Baga’ ikafikia kipindi akanipiga mateke akisema mimi ni mshamba sana, nimekalia kukuza matiti tu kila kukicha, sijui kuoga. Na mbaya zaidi akafikia hatua ya kusema eti ninanuka sana hawezi kuishi na mimi anajilazimisha. Nilitamani sana kuondoka lakini ningeenda wapi mimi ningekimbilia kwa nani? Kila mtu anayeitwa ndugu yangu alikuwa amenitenga.” Safari hii Nadia hakulia bali alifanya tabasamu hafifu…lakini alikuwa amechukia. Nikaaga na kuelekea chumbani kwangu. Majibu yake ya sasa yakiwa yanaongeza giza mbele yangu. Sikupata jibu kabisa alikuwa ana maanisha nini.

    Nikavuta subira nikaenda chumbani kwangu. Nikaoga na kubadili nguo kisha nikarejea chumbani kwa Nadia.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Nilimkuta akiwa analia, nilipoufungua mlango akazidi kulia, japo kwa sauti ya chini. Luninga ilikuwa ikipiga kelele na hakuonekana kama alikuwa anaitazama.

    Nikaketi pembeni yake mara akasimama ghafla.

    “Hivi wanaume mnataka mfanyiwe nini hasa, mnataka mliliwe vipi ndipo mjue kuwa mnapendwa eeh….hivi mnataka roho zetu eeeh nakuuliza ..nakuuliza wewe na wewe ni mwanaume ujue nasema na wewe …” Hapa akanikamata ukosi wa shati langu kwa ghadhabu, akaanza kunitikisa, sikujishughulisha kuitoa mikono yake nilitaka aseme kitu akiwa na hasira. Kweli akaendelea.



    “Yaani wakaona kuninyoa nywele zangu haitoishi, wakanifanyta mtumishi wao wa ndani nayo pia haikutosha. Kweli Desmund akawaangalia dada zake wananimwagia maji mimi, maji machafu…Desmund ulishindwa kuwakaripia waache kunionea.

    Mama yake naye niliyedhani kuwa anaweza kunionea huruma akapigilia nyundo ya mwisho katika kidonda change. Eti hakuna ndoa wala ndoano mpaka….yaani mpaka nifanyiwe tohara. Nilishtuka nikataka kukimbia lakini nani angenipokea kama ningekimbia kila mtu alikuwa ananiona mimi adui. Mbaya zaidi baba na mama yangu hawakutaka kunisikia na kubwa zaidi walijikusanya na kurejea Doha Saudi Arabia. Nikabaki Tanzania nikiwa peke yangu. Licha ya upweke ule mwanaume na mwanadamu pekee niliyetegemea atasimama upande wangu kila siku akaniacha nikakamatwa kwa nguvu. Naikumbuka siku hiyo nililia lakini hawakuniachia, wakanifikisha mahali ambapo ni kama machinjioni, looh!! Kuna makabila yana roho mbaya namna hii, kumbe kabila la Desmund lina mambo haya.

    Wakanifanyia ukeketaji, Desmund akiwa mkimya kabisa, lakini kumbe haya yote yalifanyika ili mimi nikate tamaa ya kuolewa na Desmund, walijua kuwa nitakataa lakini mimi nikakubali kumbe Desmund hakunipenda alikuwa na mchumba aliyechaguliwa na mama yake. Lakini mchumba wa kupewa na mama mimi sina tatizo, mbona sasa akaanza kulewa, mbona sasa akaanza kuwabadili wasichana hovyo, au kwa sababu …au kwa sababu nilikuwa sizaiiii….eeeh au kwa sababu sikumzalia mtoto mimiii……Desmund hivi sio wewe uliyenisindikiza kutoa mimba mara tatuw tofauti. Si wewe Desmund uliyesema kondomu huwa zinakuwasha na hauzipendi hata kidogo. Nikakusihi tuwe makini ukanikaripia nikakusikiliza usemayo mume wangu. Kama mimba tulienda kutoa wote mbona nilipopata tatizo la kizazi ukanitenga, ukanitupia katika midomo ya mawifi zangu. Nikatukanwa nikasemwa kikabila chenu, wakanitukana kikabila chenu wewe naye ukasema nao kikabila chenu ili nisiweze kuwasikia. Kumbe nawe ulinitenga Desmund…..Desmund….

    Wakanilaza jikoni huku wewe ukilala chumbani kwa raha zako, ukaridhika kuniona nasulubika, asubuhi ukaondoka bila kunisalimia..na ukatoweka kwa siku ishirini.

    Desmund nilikunong’oneza kuwa siyajui maisha ya kijijini, nawe ukasema hutaniacha pekee kamwe, lakini ukatoweka, nikawa mtumwa rasmi, nikaosha vyombo nikafua hadi nguo za mawifi. Nikakamua ng’ombe maziwa, mara nikaambiwa niwe naenda kuwapeleka malishoni.

    Ni lini mimi nimejua kuchunga ng’ombe…lini nimejifunza kitu hiki. Nilikwambia Desmund kuwa maisha niliyotoka mimi ni ya kudekezwa sana, sawa sikatai kuchunga ng’ombe lakini walau basi ningefundishwa taratibu.

    Nikaenda malishoni, ng’ombe wakapandwa mori zao mmoja akanitupa mbali kwa pembe zake, nikavunjika kiuno. Desmund ukanipa pole kwa njia ya simu…..kweli kiuno kimevunjiaka ukatumia simu …Desmund….simu!!!!! aaaargh Des…De…..Desmu…..Desmuuu…….” hapa uvumilivu ukashindikana akaangua kilio, hiki cha sasa kilikuwa kilio kitakatifu, akajirusharusha kitandani, akaruka huku na kule. Hapa nikashtuka kuwa anaweza kujizuru, nikamkamata mabega yake nikamgandamiza kitandani. Akashindwa kufurukuta lakini hakika alikuwa amechachamaa sana.

    Niliendelea kumgandamiza huku nikimchukia Desmund.



    MOJA. Yaani mkeo anavunjika kiuno hufiki kumwona unapiga simu.

    MBILI: Mwanamke aliyeweka masomo kando akakupigania unashindwa kumpigania mbele ya ndugu zako.

    TATU: Yani kumbe Desmund mpuuzi bado anaendekeza mila za kizamani za tohara.



    “MASKINI NADIA ……USILIE NADIA……jikaze jikaze ndo wanadamu hawa…..jikaze usilie…” nilimsihi……..







    Niliendelea kumsihi Nadia asiendelee kulia kilio kikuu namna ile. Laiti kama angechomoka katika mikono yangu bila shaka angefanya kitu kimoja kibaya sana, ndio! Nilihisi ni kibaya lakini sikujua ni kitu gani angeweza kuongozwa na hasira zake kukifanya.

    Hatimaye alitulia akabaki kulia kwa kwikwi tu binti yule aliyekeketwa katika safari yake ya kutafuta ndoa. Ndoa ya hayawani!!



    “Unajua Nadia, sometime you have to let it go…ukiwa mtu wa….” Kabla sijamaliza akiwa amelala chali aliyaingilia maongezi yangu. Wakati huu sikupata nafasi ya kukishika kifaa changu cha kuinasa sauti yake. Hivyo nikaweka umakini kumsikia anachotaka kusema. Huenda katika kauli yangu fupi kuna kitu alikumbuka.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Desmund! Alikuwa na lafudhi mbaya kweli, hakujua hata ‘give me some water’ ina maanisha nipe maji ya kunywa, sikupenda kuonekana nipo juu yake kwa kila kitu, nikamwanzishia kozi ya kujifunza kiingereza. Wanafunzi wenzake walimcheka alivyoshindwa kujitambulisha iwapo yeye ni ‘boy’ ama ‘girl’ nikasimama kidete kumshauri juu ya hilo nikampa moyo asonge mbele. Akanielewa akazidi kujituma, mwishowe akaanza kukijua kiingereza. Wakati huo sijui hata kama atakuja kukitumia kila kiingereza vibaya kwa kuniambia ‘you bitch pack your things and leave! My house!!’….sasa niende wapi na kwa kosa lipi sijui, halafu ilke nyumba kodi yote nilikuwa nimelipa mimi lakini akadai ni nyumba yake nichukue kilicho changu niondoke. Hakuishia hapo akaniuliza swali ambalo lilinifanya nimuone mpuuzi na mwendawazimu, eti ‘don’t you understand English?’ ..sasa mimi nimemchukua akiwa hakijui hata hicho kiingereza lakini leo hii ananiuliza eti iwapo sijui kiingereza was he crazy!!!” hapa Nadia kwa mara ya kwanza tangu tuanze safari alifanya kicheko kidogo, kasha akaendelea “wanaume huwa mnakuwa wapumbavu sana mkishashika pesa kidogo halafu mkagundua kuwa mnapendwa mnavimba sana vichwa. Basi Desmund akawa ana kiburi kilichopitiliza, eti hapo kisa tu nilimwambia yeye ni kila kitu kwangu. Desmund akayatumia madhaifu yale kunifanya apendavyo.

    Unajua kaka…katika haya maisha hakika tunatenda maovu mengi sana, mengine yanasameheka lakini kwa akili ya kibinadamu mengine yanakuwa magumu sana kusamehe, ujue kucheza na akili ya mwanadamu mwenzako ni kitu kibaya sana maana hujui ataathirika kiasi gani akijua kuwa unamchota akili. Fikiri kuhusu Desmund yaani na miaka yake thelathini na mbili, alikuwa ananidekeza sana. Nitake nini Desmund asinifanyie, mara apike uji mara anibembe mgongoni. Nikinuna kidogo ananibembeleza na kila alivyonikumbusha kuwa ananipenda sana mwanaume alitoa machozi, alilia haswaa. Chozi lake nililiona la thamani sana lakini nikagundua baadaye kuwa anacheza na hisia zangu, niliumia alivyokuwa analia lakini yeye alikuwa akinitukana kuwa niache kujilizaliza. Niache kujiliza wakati nimeumizwa kabisa, Desmund hakuliona chozi hili akawasaidia wale wanawake kunitawanya miguu yangu kisha wembe mkali ukanifyeka, nikakeketwa Nadia mie. Nikakeketwa ili niolewe.



    Wakati mwingine najilaumu mimi mwenyewe halafu nahisi ni laana hii inaniandama kakangu, hii itakuwa laana tu. Ujue mama alilia sana siku ambayo baba alikuwa ananifukuza nyumbani, wadogo zangu walilia sana kaka, wote wakanisihi kwa kiarabu kuwa nibadili maamuzi yangu. Tayari alikuwa amechaguliwa mchumba wa kiarabu kutokea Jedah kwa ajili yangu nikimaliza chuo. Mchumba ambaye alinivumulia tangu nikiwa mdogo hadi nikiwa chuo kikuu, huyo nikaona hana maana nikakabidhi maisha yangu kwa Desmund. Mama alisema maneno mengi huku akigalagala chini, alilia sana, na kwa mara ya kwanza katika maisha yangu mzee wangu Ramadhani licha ya ukorofi wake uliokithiri na usiomithirika alitokwa na chozi katika jicho moja. Nikaondoka na sikutaka kuangalia nyuma. Nikaenda kwa Desmund ambaye alikuwa kila kitu kwangu. Nikaamini kuwa nipo katika njia sahihi kabisa, wala sikujilaumu!!



    Elimu ilinipotosha hakika, bila elimu sidhani kama ningeyajua mambo ya kujichagulia mume wa kunioa, mimi nilifunguliwa na elimu nikajichagulia Desmund labda kweli elimu ni ufunguo wa maisha lakini kwangu mimi el;imu ilinifungua na kasha ikanifunga katika utumwa wa mapenzi.

    Mdogo wangu alinipigia simu kwa mara ya mwisho akanieleza taarifa mbaya sana ambayo nd’o naiita laana maishani. Hakika ilikuwa laana, mdogo wangu alikuwa analia na akaniambia waziwazi kuwa familia nzima inanichukia tena inanichukia sana. Hakunipa nafasi ya kuongea neon lolote aliendelea kuzungumza akinirushia lawama kuwa nimemuua mama, hapa nikahisi kuzizima kabisa, Kassim akaniambia kuwa mama alikufa akinilaumu kwa kila neno, na neno lake la mwisho alisema ‘Nikifa mnitupe baharini ama mnichome moto simtaki Nadia kaburini kwangu, sitaki kuisikia sauti yake, kama ataweza aiombe bahari initapike kama ataweza ayaombe majivu yaungane tena aweze kuniona. Msinizike aje kulowanisha kaburi langu na machozi yake yaliyolaaniwa, sitaki kelele za kilio chake zinisumbue katika usingizi wangu wa milele. Mwambieni namchukia kupita watoto wangu wote kwa yote aliyonifanyia na kunifedhehesha!!!’. Maneno yale yalikuwa makali sana, kisha simu ikakatwa. Nilipojaribu kupiga haikuwezekana.

    Simu ilipigwa kutoka katika vibanda vya simu Jeddah Saudi Arabia.

    Huo ukawa mwisho wa kuwasiliana na ndugu zangu, ndugu pekee alibaki kuwa Desmund, na nilimweleza yote haya kuwa mama yangu amekufa akinilaani, nikamsihi Desmund awe mkweli kwangu ili mama yangu popote alipo atambue kuwa huyu alikuwa mwanaume sahihi, najua roho ya mama inanizomea kwa wakati huu kwa sababu nimeaibika tayari. Nilimvumilia Desmund ili mama asijue kama tuna matatizo katika familia lakini haikuwa hivyo kwa upande wangu, kwa maana hiyo Desmund aliona sawa tu nilivyochukiwa na familia, aliona sawa tu mama yangu mpenzi alipokufa akinilaani, yaani kwa ufupi kila lililo baya Desmund aliona sawa tu….aliona Nadia alizaliwa ili ateseke…Desmund u mwanaume gani sasa wewe…eeh Desmund..” kilio kikamzidi…akajilaza tena, nikampiga piga begani bila kusema naye lolote. Huku nikidhani kuwa amenyamaza na hatazungumza tena kumbe alikuwa akijifuta machozi kisha akaendelea, sasa alikuwa anakaripia. Ni kama mbele yake alikuwapo huyo wa kuitwa Desmund….hapa nilikumbuka kurekodi.



    “Mbona alifanya hivyo Desmund!! Naamini alifanya yeye japo sina uthibitisho lakini Desmund alinitafutia sababu maksudi, kivipi mwanamke ambaye nimeamua kupoteza kila kitu kwa ajili yake ashindwe kunisikiliza na kujifanya anamuamini sana Frank, Frank si amekutana naye akiwa ameng’ara tayari, wanajifanya wanajua sana wanaongea kiingereza cha kipumbavu, kiingereza nilichoongea darasa la pili wao wanakuja kukiongea mbele yangu na kujifanya wananificha wanachozungumza. Yaani rafiki yako anakueleza kuwa mkeo ni Malaya nawe unatabasamu unasema ndio ndio….Desmund hivi ulirogwa. Walikuroga Desmund!!! Umuulize basi niliufanya wapi, si ni huyu nilikwambia anavyonitazama sipendi maana anaonyesha matamanio, mwanzoni ukanielewa leo hii anakuletea ujinga kwamba mimi nilikuwa Malaya SAUT (Saint Augustine University Of Tanzania) na wewe unaamini Desmund, ama hakika walikuroga wewe si bure nasema, sio wewe ulifanya mapenzi na mimi mara ya kwanza nikikueleza kuwa sijawahi kushirikiana na mwanaume tangu nizaliwe, sio wewe nilikueleza kuwa nilikuwa nangojewa na bweana wa kiarabu anioe huku nikiwa na bikira yangu, huo umalaya niliufanyia mdomoni we fala!! Nakuuliza niliufanyia mdomoni mimi, au niliufanyaje sasa hadi ukanikuta na bikira yangu. Desmund kumbe u mpumbavu kiasi kile, mimi nikawa mpuuzi nikafanya sherehe kubwa kukutambulisha kwa rafiki zangu kama mchumba wangu. Marafiki wakakutukana kabisa kwa kunong’ona kuwa wewe si saizi yangu, wakakucheka na kimwili chako kilichokondeana, hivi ningekuwa wa kuitwa Malaya wewe nawe ulikuwa mwanaume wa kushiriki nami mapenzi…..au kwa kuwa nilikusifu kuwa unaniridhisha kila siku Desmund. Sikukusifu bure, sikufanya maigizo yoyote mimi, lakini aaah Desmund ukaja kusema mimi ni mzigo tu kitandani tena Malaya wa kutupwa wewe na huyo rafiki yako Frank mnanitukana, kumbuka nilikuokota mimi nilikuokota Deeees niliku…..okotaaa….leo hii unanitupa kwa kishindo, nilikuokota wewe nikiwa nikiwa peke yangu, kwa uamuzi wangu nikatumia pesa zangu mimi mwenyewe!!! lakini unashirikiana na rafiki zako kunitupa Desmund….Desmu…..Desmuuu kweliiii wanifanyia hivi kweli mimi yaani….aaargh!!!” hii haikuzuilika sasa, vifaa vikawekwa kando nikachukua jukumu la kumbembeleza, alilia kwa sauti kuu sauti ilishtua sana, kuna mengi moyo wa huyu dada ulibeba hakika.

    Mimi nikazidi kuumizwa na hii simulizi na kwa mara ya kwanza nikatamani kumwona huyo Desmund ili nimfikishe katika vyombo vya dola kwa unyama huu, japo simulizi ilikuwa nusunusu bado. Japo kwa matukio hayo tu ningeweza kumfikisha pabaya, walau kwa kalamu na karatasi ningemfanya dunia aione chungu na mahali pasipokuwa salama kabisa.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    KUMBE!!!!!



    MOJA: Mama yake Nadia alimlaani vikali kiasi kile!!! Je ni laana inaishi??



    MBILI: Familia ilimtamkia kuwa inamchukia, na wamekaa kimya moja kwa moja ama??



    TATU: Desmund na FRANK!! Jina jipya tena huyu naye anamuitaje mke wa mtu Malaya???



    NNE: Desmund na kiingereza….hapa niliweka nukuu ili niwe nacheka mwenyewe…hajui ‘boy na girl’ zina maana gani. Huenda elimu ndogo nayo ilichangia.



    TANO: Desmund akamkuta msichana ana bikra halafu analeta dharau…bikra zilivyokuwa hadimu!!!



    SITA: Hivi wapo wapi hawa akina Desmund mpumbavu na Frank mshenzi?? Swali hili nililihitaji jibu lake sana.



    “NADIA…..USILIE NADIA……nipo kwa ajili yamko” niliyasema maneno yale kimoyomoyo huku nikiogopa asiweze kunisikia maana bila shaka alikuwa akiwachukia wanaume wote na mimi nikiwemo…..







    ******



    Kama ni kulia hakika Nadia alikuwa Amelia haswa, na kama ni majuto hapakuwa na shaka alikuwa amejutia mengi sana ambayo aliyafanya kisha kutumbukia katika mdomo mbaya wa Desmund. Bado nilikuwa katika fumbo gumu sana la kuweza kujua nini kilijiri hadi binti huyu yakamsibu mazito kiasi kile. Alikuwa amekonda na hakuonekana kujali kuhusu hilo. Hakika alikuwa katika majuto makuu.

    Sikutaka kusema neno lolote la ziada maana nilihofia kumtibua na kuanza kusimulia mkasa mwingine mpya ambao ungekiamsha kilio chake upya tena.

    Lakini ni neno gani nilipaswa kusema na lipi sikupaswa kusema. Maana kama neno dogo la kiingereza nililosema lilimtibua Nadia na kujikuta akinieleza mambo mengine mengi. Ni neno gani lilikuwa sahihi kwa wakati ule. Nilifumba macho yangu na kumkabidhi Mungu wakati ule ili aniongoze vyema katika matamshi yangu. Ni kweli nilihitaji kuandika kitabu cha kusisimua kutoka katika simulizi ya kweli ya Nadia lakini bado sikupenda kumwona binti yule wa kiarabu akilia kilio cha uchungu, sikupenda Nadia alivyokuwa anajuta mbele yangu. Niliumia sana hakika. Lakini nilijionya kuwa kama nikiendel,ea na huruma ile nitajikuta siifanyi kazi yangu.

    “Nadia mama….” Nilimuita, akageuka kunitazama.

    Ebana eeee!!! Jicho jekunduuu!! Msichana alikuwa Amelia sana, kuwa jekundu pekee hakukutosha. Lilikuwa limevimba haswa.

    “Abee!” aliitika, nikawahi kukwepesha macho maana nilihisi muda wowote naweza kutokwa machozi pia.

    “Nenda ukaoge dadangu….nenda ukaoge….”

    Alinitazama kiasi kwamba nikahisia ameijiwa na kumbukumbu nyingine, jambo ambalo sikuwa tayari kuliona likitokea.

    “Kuna maji ya moto…” aliniuliza kwa sauti ya chini ambayo ilikuwa inakwaruza.



    Upesi nikairukia simu nikapiga mapokezi na kuomba huduma hiyo.

    Acha hoteli za kitalii ziitwe hivyo hivyo. Hazikupita dakika nyingi simu ikaita, nikapewa maelekezo kuwa tayari mambo yamesetiwa kitaalamu ni mimi tgu kama nataka kuoga.

    Laiti kama ningekuwa na mahusiano na Nadia, siku hiyo ningemsaidia kumwogesha. Hakika alikuwa amechoka sana, alikuwa amechoka Nadia. Alistahili kusaidiwa lakini mimi nilibakia kuwa mwandishi tu. Alipoingia bafuni name nikaenda chumbani kwangu. Nikajimwagia maji.

    Baada ya muda tulikuwa tunatelemsha ngazi kuelekea katika mgahawa mpana wa hoteli ya G & G. tukatafuta mahali tulivu tukajiweka hapo.

    Mara muhudumu akafika tukiwa tunapitia karatasi ya orodha ya vyakula.

    “Tutakuita” nilimweleza akajiondokea huku akiwa anaendelea kutabasamu kama ilivyo kawaida ya wahudumu.

    “Hivi hawa Capuccino (soma: kapuchino) yao itakuwa murua.” Nilimuuliza Nadia ambaye alikuwa mwenyeji wa jiji la Mwanza.

    Cappuccino ni kinywaji mchanganyiko wa kahawa na maziwa na madikodiko mengine, mara nyingi kinapatikana katika hoteli za wazito.



    Kwa mara nyingine Nadia akatabasamu, kisha kwa mara ya kwanza kabisa Nadia akacheka, Nadia alicheka vyema na kwa mara ya kwanza nikafanikiwa kutambua kuwa kabla ya matatizo Nadia alikuwa mrembo haswaa. Kubwa zaidi alikuwa na mwanya katikati ya meno yake ya mbele.

    Ebwanaa eee! Kilichofuata hapo ni kingine. Alianza kwa furaha….

    “Ina maana unanicheka Nadia au haitamkwi hivyo jamani, hivi ni kapuchino ama kapusino…mi sijuagi hata” nilimweleza huku nikiwa katika kufurahia tabasamu lake.

    “Hamna inaitwa hivyo hivyo ila umenikumbusha dada yake Desmund, mwenzangu!! mara yake ya kwanza kuiona hiyo Kapuchino sasa, kwanza alikuwa haijui, hata Desmund mwenyewe alikuwa haijui lakini eti siku hiyo akajifanya anaijua sana akamwambia dada yake aitamke, he! Akasema kafufinyo wacha tucheke hadi nikapaliwa, maskini wifi yangu akawa amekodoa macho tu. Sie tunacheka na Desmund wangu.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mambo yanabadilika kweli jamani, wifi yangu Janeth yaani alikuja huku mjini miguu imepasuka wewe sijui nd’o wanaita magwambala, imepasuka haswaa, yaani dah! Mimi hata sikujali, alikuwa hajui kutamka maneno mengine ya Kiswahili lakini yote mi nasema Mungu atanilipia, kweli Janeth mimi nilimpatia nguo zangu, sikuona aibu kumfunza mambo mengi ya mjini hatimaye nikamtafutia kazi akaanza kujitegemea kwa mshahara wake mkubwa tu. Mshahara ambao kwa darasa lake la pili aliloishia angelipwa kwa mwaka mzima ama miwili. Janeth hakuyakumbuka haya, Janeth akasimama kidete kabisa anamweleza kaka yake eti mimi ni mchawi nimemwendea kwa mganga nimemwekea dawa, Janeth jamani yaani nilipokosa kanga ya kujifunika huko kijijini kwao nikachukua kanga yake akanikwapua na kudai nitaiwekea chawa kanga yake. Janeth ambaye alikuja mjini akiwa ananuka mbuzi na ng’ombe nikampulizia marashi nikamkumbatia bila kujali harufu yake, na yeye akasimama kunipinga, Janeth kweli nikaugua Malaria akashangilia eti madawa ya mganga yamenirudia, mwandishi yaani mimi sijui lolote kuhusu waganga , sijawahi kwenda Mungu aliye hai ananiona, sasa nilimkosea nini mimi Janeth., na Desmund akanyanyua kinywa chake akadai dada yake huwa hasemi uongo hata kidogo. Amakweli mfadhili mbuzi akikukera umle nyama si mwanadamu, si mwanadamu nasema.



    Mwandishi yaani kumbe kumtunza kote huko huyo Janeth wala hakuwa dada yake na Desmund, eti kumbe ndiye yule mke ambaye alichaguliwa na mama yake, kwa hiyo Desmund kumbe hakunipenda tangu zamani yule. Alinitumia tu, sitaki kukumbuka pesa zangu alizotumia lakini kwa nini ameivuruga akili yangu kwa kiasi kile. Desmund na Janeth ni wanadamu wa aina gani sasa hawa, eeh!! Wanadamu gani msiojali kuwa Nadia hana ndugu mwingine katika dunia hii mnaitwaa Roho yake mnaitwangatwanga. Si mngechukua pesa zangu zote, si mnenidhulumu hata viungo vyangu iwapo vinafaa mkaniachia moyo na roho yenye amani, mbona mkanitenda vile.

    Yaani Desmund kweli ukamwachia huyo mwanamke wako duka langu kubwa la nguo kisha ukanipeleka mimi huko kwenu mimi nikawe mvuvi wa samaki, Desmund ukanikabidhi katika kundi la wanaume eti nijifunze uvuvi. Desmund saa nane usiku mtoto wa kike ukaniacha ziwa Viktoria, desmund si heri ungenipiga risasi mimi Nadia nife mara moja kuliko kuniua taratibu. Nikayavumilia hayo yote hukujali, ukanikomaza mikono Desmund kwa kushika nyavu na kuwavua samaki. Wewe na hawara yako mnatesa na mali zangu unaniambia ni dada yako, shenzi kabisa Desmund, shenzi nasema. Na laiti ningejua mapema Desmund wallah ningekufanyia kitu kibaya ujue, Desmund nilikustahi sana we mwanaume. Ujue sitakiwi kulaumiwa mimi sitakiwi kabisa kulaumiwa basi tu lakini yaani basi….

    Unanikabidhi kwa wavuvi kisha wananitaka kimapenzi ukaniita mimi Malaya eti ni mimi nawataka. Hivi Desmund nani alikudanganya kuwa wewe na hao ndugu zako kuwa mlikuwa na mvuto wa kupagawisha msichana?? Basi tu nilikupenda mimi Nadia, haukuwa na hadhi walau ya kunisimamisha na kuanza kunitongoza hakika.



    Lakini nafasi niliyokupa ukaamua uitumie vyema, eti huyo unayemuita dada yako, na mama yako ambaye sipendi kutukana lakini ni mama mjinga kupita wote duniani mnaniweka kikao na kunishutumu kuwa ninafanya umala katika mtumbwi. Hivi mlikuwa na akili ninyi viumbe mlikuwa na akili Desmund.

    Nakuomba nirejee kuuza dukani kwa sababu upepo wa bahari unaniumiza kifua unanieleza kuwq mahesabu yatanichanganya hapo dukani labda Janeth akipata muda anielekeze, Desmund ulikuwa umelewa siku hiyo ama? Yaani Janeth aliyekuja na miguu imepasuika mjini wewe na yeye kwa pamoja hamjui kapuchino wakati huo mnatumia pesa yangu, leo hii unaniambia eti sijui mahesabu yatanichanganya. Hakika ulipitiwa na dharau ya hali ya juu. Na kama hiyo haitoshi ndugu mwandishi Desmund, mama yake na huyo Janeth siku moja wa…….”

    Kabla hajamaliza muhudumu alikuwa amefika, tukamuagizia kapuchino mbili. Moja ya kwangu na nyingine ya Nadia.

    Nadia akasitisha mazungumzo yake, akainama kwa muda. Mimi nikjapiga funda moja la kapuchino kisha nikamsihi Nadia naye apate kapuchino kabla haijapoa.

    Akainua uso wake nikampatia kitambaa akajifuta machozi kabla hayajatiririka.



    Kisha akapiga funda moja kubwa.

    “Si nilikwambia yaani hawa jamaa kapuchino yao wanatumia maziwa freshi kabisha sijui wanayatolea kwa akina Desmund maana wana mang’ombe mengi hao duh halafu yana afya kama nini…..” hapa alisema huku akitabasamu.

    Nilimtazama kidogo nikamjibu kwa tabasamu pia kisha nikainama.

    Nikajiwekea maswali na majibu mapya.



    MOJA; Yaani Desmund na Janeth kumbe ni wapenzi wakahudumiwa na NADIA jijini Mwanza….UNYAMA NA USHAMBA MKUBWA….



    MBILI: NADIA binti wa kiarabu akapelekwa kuvua samaki…HATARI hii lazima kulikuwa na kitu hapa.



    TATU: NADIA alipogundua Janeth ni mke mwenza nini kilitokea???



    NNE: Mbona NADIA anadai hatakiwi kulaumiwa???



    TANO: DESMUND, MAMA YAKE NA JANETH wapo wapi??



    Nikapiga funda jingine kubwa la kinywaji kile cha moto huku nikikiri kuwa hakika kapuchino yao ilikuwa maridadi kuliko baadhi ya maeneo jijini Dar es salaam.

    Nikamtazama Nadia naye alikuwa amejikita katika kukifurahia kinywaji kile.

    Kimya kikatanda….

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog