Simulizi : Usilie Nadia
Sehemu Ya Pili (2)
Nilimtazama kidogo nikamjibu kwa tabasamu pia kisha nikainama.
Nikajiwekea maswali na majibu mapya.
MOJA; Yaani Desmund na Janeth kumbe ni wapenzi wakahudumiwa na NADIA jijini Mwanza….UNYAMA NA USHAMBA MKUBWA….
MBILI: NADIA binti wa kiarabu akapelekwa kuvua samaki…HATARI hii lazima kulikuwa na kitu hapa.
TATU: NADIA alipogundua Janeth ni mke mwenza nini kilitokea???
NNE: Mbona NADIA anadai hatakiwi kulaumiwa???
TANO: DESMUND, MAMA YAKE NA JANETH wapo wapi??
Nikapiga funda jingine kubwa la kinywaji kile cha moto huku nikikiri kuwa hakika kapuchino yao ilikuwa maridadi kuliko baadhi ya maeneo jijini Dar es salaam.
Nikamtazama Nadia naye alikuwa amejikita katika kunywa kile kinywaji.
BAADA ya cappuccino kutuburudisha vyema na kutupunguzia baridi kwa kiasi fulani, tuliamua kuunganisha na chakula kabisa.
Nadia akaagiza mchemsho wa kuku, mimi nikaagiza ugali na samaki aina ya sato wa kuchoma. Hiki chakula kilikuwa ni kama kaugonjwa kwangu.
Kila mmoja akajikita katika kusosoa kivyake chakula kile. Hakuna alitemsemesha mwenzake, Nadia alikuwa na staha haswaa katika kula, hakuwa akitafuna huku akiacha kinywa wazi. Alijua kuishika uma vyema na nzuri zaidi hakusema sema wakati anakula. Makosa ambayo wasichana wengi hujikuta wakifanya bila kujua kama ni makosa.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Baada ya dakika hamsini tulikuwa tunanawa mikono. Hapakuwa na jipya jingine tukaelekea nje ya hoteli ile kulitazama kidogo jiji la Mwanza. Ilikuwa ni saa tatu usiku, na jiji la Mwanza lilikuwa bado katika heka heka za hapa na pale. Kila tulichokiona na kikafaa kuzungumzwa tulifanya hivyo. Hadi tulipokifikia kijiwe kimoja cha kahawa, Nadia aliomba tuketi kidogo.
Sikumpinga maana maana kidogo alionyesha kuchakaa uso waker ghafla, bila shaka alikuwa amevamiwa na wazo la ghafla.
Nikaiandaa simu yangu katika sehemu ya kurekodia.
“Duniani kuna mengi sana, na huwezi kuijua kesho yako iwapo leo tru kuimaliza hujui itamalizika vipi. Na katika kitu kinachosababisha tusiijue kesho yetu ni wanadamu wabaya wasiokuwa na huruma kwa wenzao. Nimewahi kuumia sana katika maisha yangu, nimeumia sana baada ya kusikia mama yangu amekufa kwa ajili yangu eti kisa tu mwanaume ambaye nilimpenda kwa dhati nikitarajia atakuja kuyafuta maumivu yangu. Lakini siku nyingine ambayo niliumia sana ni pale ambapo niligundua kuwa sijaipoteza familia yangu tu bali hata wale marafiki ambao nilikuwa nawategemea nao walikuwa kinyume na mimi. Sikutarajia kabisa ingekuwa rahisi kiasi hicho mimi kujikuta katika mji huu nikiwa mpweke, yaani wakati mwingine najilaumu mimi mwenyewe kwa tabia yangu ya kutochangamana na wanafunzi wengine kwa ukaribu zaidi ya marafiki zangu wanne tu. Sikujua kuwa siku moja nitawahitaji na hawatakuwa tayari kunisikiliza kabisa.” Alisita kisha akatazama huku na kule akapepesa macho kisha akaendelea.
“Yaani Desmund alikuwa mjanja hakika katika hili, yaani akanitoa Musoma na kunitupa jijini Mwanza kisha akaniacha huku akiwa ameharibu kila kitu. Desmund alikuwa amecheza karata sahihi kabisa, yaani akanitelekeza Mwanza bila msaada wowote, usiku nikalala nje kisha asubuhi nikaenda kuwatafuta marafiki zangu ni huku nilipokutana na kituko cha mwaka…..yaani kweli rafiki zangu niliosoma nao miaka mitatu chuoni wakaaminishwa kuwa mimini mshirikina, nina majini ambayo ni hatari sana katika mwili wangu? Marafiki wakanikataa eti mume wangu amewaonya wasije kumlaumu wakinikaribisha, niliwalilia na kuwasisitiza kuwa sijui hata hayo majini yanafanana vipi nikawaomba wanipe nafasi ya kunisikiliza lakini hilo halikuwezekana, kila mmoja alidai kuwa anaogopa majini na yanaweza kuhamia kwao.
Nikajikuta nikiwa yatima kamili jijini Mwanza, mbaya zaidi baba yangu alinifanyia komesho alipoamua kuteketeza vyeti vyangu vyote kuanzia awali hadi chuo kikuu.
Nikawa naonekana kituko rasmi, Desmund akawaambia rafiki zangu kuwa majini yalinipanda nikachoma vyeti vyangu.
Ama kwa hakika Desmund aliniweza.
Jijini Mwanza ningeishi vipi sasa iwapo hakuna mtu ambaye alihitaji kunisikia? Ningekimbilia wapi mimi Nadia.
Nikisema kuwa ipo siku nililia ni ile siku yangu ya kwanza kugawa penzi ili nipate pesa ya kujikimu, eneo lenyewe ni lile pale mbele, siku ya kwanza sikupata mtu wa kuninunua ni hapa nilipokutana na Jadida, msichana ambaye sikuwahi kuona tabasamu wala cheko lake isipokuwa siku moja tu, siku ambayo sitaisahau kamwe. Jadida akanichukua usiku ule na kunipeleka katika chumba ambacho alikuwa anaishi yeye na machangudoa wengine. Jadida aliniuliza maswali mawili matatu, nikamueleza kijuu juu kuhusu uwepo wangu eneo lile nikalalamika kuwa ni njaa na sina ndugu yeyote wa kunifadhili. Akanitazama vizuri, nikayaogopa macho yake ambayo yalitangaza chuki waziwazi. Kisha akachukua mkate na juisi akanipatia. Nilipomaliza kula akanipatia maji kidogo nikaoga.
Siku iliyofuata akanipamba kidogo na kisha usiku akawa kiongozi wangu nikijipanga katika barabara kwa ajili ya kusubiri wateja, mteja wangu wa kwanza alikuwa mswahili tu. Sikuamini kama yalew yote yanatokea kwa sababu tu nilimkabidhi moyo wqangu Desmund. Usiku ukamalizika nikiwa nimepata watejawanne. Jadida akawa meneja wangu rasmi.
Kama yeye ambavyo alikuwa hatabasamu basi name sikuwahi kuifurahia siku hata moja ya biashara hiyo. Yaani Desmund hakujishughulisha kunitafuta? Desmund huyu huyu ambaye alikuwa na kitambi kutokana na pesa zangu leo hii amenitupa bila msaada wowote, akaniacha niwe changudoa, akanishutumu kuwa nina majini. Siku ambayo niliamua rasmi kuachana na uchangudoa ulikuwa usiku wa saa nne ambapo nilichukuliwa na mwanaume ambaye alikuwa na asili ya kihindi lakini alionekana kuwa mswahili sana. Huyu alilazimisha niende naye gesti jambo ambalo dada Jadida alinikataza kabisa nisikubali, lakini kutokana na pesa aliyoitoa basi Jadida akaniruhusu niende naye tu. Hii ilikuwa baada ya kuhahakikishiwa usalama wangu.
Sikujua kama yangeweza kutokea mambo ya ajabu kama yale yaliyotokea siku ile.
Tulifika vizuri chumbani, nilijiweka sawa kumridhisha kisha biashara iishie hapo, kweli nilifanya yote aliyoyataka, sikuwa nimewahi kulala na mteja gesti huyu alikuwa wa kwanza akataka nimfanyie kila jambo ambalo huwa namfanyia mwanaume ambaye ni mpenzi wangu mimi nikatii yote haya, kila alivyorudia maneno hayo kuwa yeye ni mume wangu kwa siku hiyo basi alinikumbusha sana kuhusu Desmund wangu, nilitamani sana dunia inimeze lakini cha ajabu nilikuwa sijisikii kabisa hata dalili ya kupata wazo la kujiua.
Baada ya kumfanyia kila kitu kinachoitwa mapenzi lilifuata jambo ambalo lilinifanya kwa mara ya kwanza nimchukie Desmund kabisa na kutotamani kumuona tena maishani. Yule mwanaume akanilazimisha kufanya mapezni kinyume na maumbile, nilibishana naye sana nikagoma kabisa nikidhani atanielewa kama alivyoonyesha usoni kuwa ni mpole. Haikuwa hivyo, mara akaiendea suruali yake. Yule bwana alikuwa na bunduki, kwa mara ya kwanza nikatazamana na bunduki!!! Hakika niliishiwa nguvu. Akaniambia nichague moja tu, kufanya atakavyo ama kuniua palepale. Mwandishi kifo ni kitu kingine na hakika hakizoeleki yaani sikuwa tayari kufa.
Akanivamia pale na kuniambia nikifanya kipingamizi chochote tu ananisambaza ubongo wangu….yaani niliumia, nililia mtangazaji nililia na kumlaani Desmund kwa kila neno nililoweza kusema, sijui kama dua zangu zilifika kwake sijui kabisa kama Mungu alikuwa anatega sikiona kunisikiliza walau kidogo tu! Nililalamika sana siku hiyo.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Nadhani nilipoteza fahamu, maana asubuhi nilijikuta peke yangu, maumivu makali nikashindwa kukaa vizuri, nikaanza kulia upya. Mara mlango ukagongwa. Ilikuwa imetimu saa nne asubuhi.
Muda wa kukabidhi chumba, nilipogeuka kutazama mashuka nikakutana na matone ya damu. Nikamuomba yule dada dakika mbili nivae akaniruhusu huku akisisitiza kuwa ziwe dakika mbili kweli. Nilihaha nisijuie nini cha kufanya, mwisho nikaamua kujikabidhi tu kwa muhudumu nikamueleza kuwa nimeingia katika siku zangu ghafla na nimechafua mashuka.
Hakutaka kunielewa mwisho nikaamriwa kuyafua mashuka yale, nikafanya walivyotaka. Huku maumivu makali yakitambaa katika mwili wangu. Jina la Desmund likichemka katika kichwa changu. Nikamlaani tena asubuhi ile, nikamwombea mabalaa yote yamwandame, hadi ninavyozungumza nawe nitaendelea kulalamika kuwa Mungu hakutega sikio kunisikiliza, angenisikiliza kweli yasingenikuta haya. Sijui hata ni wapi mimi Nadia niliwahi kumkosea Mungu wangu!!! Niliondoka nikiwa nachechemea hadi nikafika nyumbani kwa Jadida. Aliponiona klwa mbali tu alijua kuna tatizo akanikimbilia kwa kasi.
“Nadia..amekufanyaje yule mteja..nimekutafuta sana..” aliniuliza huku akiwa amenikamata mabega. Badala ya kumjibu nilianza kulia, nililia sana akanituliza mwisho nikamwambia kilichojiri.
“Ame….amekufanyaje…yaani…” alishindwa kuzungumza akaanza kutetemeka na kwa mara ya kwanza nikaliona chozi la Jadida….
Afadhali alilia tukalia wote nikahisi yupo mtu aliyeutambua uchungu wangu…..si Desmund aliyeniharibia maisha yangu. Katika zungumza yangu na Jadida nilijikuta kwa hasira nikimweleza mambo mengi sana kuhusu mimi, nilimweleza huku ninalia. Na ni katika siku hii nilipoweza kutambua Jadida alikuwa msichana wa aina gani yaani alikuwa zaidi ya changudoa. Na kubwa zaidi alikuwa akinifaa kabisa, alinibadili kiuelekeo akanibadili kifikra akayafuta machozi yangu na kisha akanionyesha njia ambayo sikujua kama ni mbaya ama ni nzuri hadi nilipoamua kuifuata…..” Akasita kidogo kisha akaendelea….
“Waliosema wema hawagandi alikuwa na maana yake, wema huyeyuka upesi. Jadida ambaye alikuwa mwanga wangu naye akapotea katika namna ya ajabu, hivi yawezekana mimi nilikuwa na bahati kuwa walinifanya vile kisha wakaniacha hai. Jadida…aaah Jadida yaani wakakufanyisha mapenzi kinyume na maumbile kisha wakakuua, hivi uliwaamini kwa nini watu wale, kwanini uliwaamini Jadida. Kumbe Jadida nawe hukuwa nma ndugu, serikali ikakufukia kama mzoga tu…ni mkimi pekee niliyesikitika wengine walisema alikufa akifanya uchangudoa….Jadida ambona uliondoka mapema sasa eeh!!” hapa hakuweza tena kuongea, alikuwa ameuma meno yake kwa hasira sana. Na machozi yalikuwa yanamtiririka.
Upesi nikaita taksi, ikatupakia na kuturudisha hotelini.
Nikiwa natazama mbele nilikuwa nawaza na kuwazua. Mkasa huu ulikuwa mtata kweli, ulikuwa mkasa unaozua maswali mengi na majibu machache.
MOJA: NADIA alifanya uchangudoa kumbe DES alimtimua? Alitoa wapi ujasiri huo.
MBILI: Akalawitiwa akifanya uchangudoa….akaacha uchangudoa halafu??
TATU: JADIDA alimwongoza katika njia ipi sasa?
NNE: DES ana akili kweli yaani anamzushia mtu kuwa ana majini?? Vipi dua za Nadia zitamkumba Desmund??
*******
Tulipofika hotelini sikuhitaji Nadia aseme neno lolote la ziada maana hakika alikuwa amechoka, alikuwa Amelia haswa. Na alikuwa na hasira.
Mawazo aliyokuwa nayo hakika yalikuwa yakimtafuna ndani kwa ndani. Nilijisikia vibaya kama vile alikuwa dada yangu wa kuzaliwa tumbo moja.
Niliamini kuwa hata Nadia atakuwa amechoka na atakuwa anahitaji kupumzika lakini sikuwa sahihi hata kidogo.
Tulipofika chumbani Nadia aliendelea kuzungumza, sasa kwa hasira zaidi tofauti na wakati ule tulipokuwa nje.
“Japo nilihisi nimetengwa na kila kitu na dunia ikiwa imenitukana kila aina ya tusi, naweza kukiri kuwa Jadida alikuwa mwanamke ambaye alikuwa zaidi ya ndugu kwangu. Alinisimamia hadi dakika ya mwisho, hakika niliujua umuhimu wake kiukweli lakini niliutambua vyema baada ya kuhakikishiwa kuwa Jadida hatarudi tena alikuwa amekufa. Moja kwa moja!!
Nilibaki katika kile chumba alichokuwa akiishi na wale machangudoa wengine.
Baada ya majuma mawili nikaanza kuombwa pesa ya matumizi, ama la nitajua jinsi nitakavyokula mimi mwenyewe.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Mwandishi ujue tangu nilipoingiliwa kinyume na maumbile sikutaka kabisa kujiingiza katika katika uchangudoa. Hata Jadida alisema nisijiingize tena, yeye atajiuza name nitakula na kulala bila mashaka, sasa hayupo tena watu wabaya walikuwa wamemuua, ni hapa nilipoanza kujiona mkiwa tena na kisha kujiuliza hivi nilizaliwa kwa ajili ya kuteseka, nikamlilia Mungu na kuona kwa hakika sikutakiwa kuendelea kuadhibiwa baada ya yote niliyopitia. Hata kama ilikuwa adhabu basi ilikuwa imetosha. Lakini Mungu hapangiwi, nilibaki kunung’unika tu huku nikiendelea kuteseka. Baada ya kunivumilia siku kadhaa hatimaye likafuata suala la kulipa kodi ya pango, hapa sikuonewa huruma yoyote, nilitakiwa kuchangia pango.
Ningetoa wapi pesa na Jadi hakuwepo!! Nikaumiza akili yangu sana kisha nikamkumbuka Ramadhani ama Ramso…” akasita kidogo, kisha akanitazama kwa uchungu mkuu.
“Mwandishi yaani ni basi tu sina mtoto, ni basi tu nasema sikuweza kuzaa lakini kama ningekuwa na kizazi nisingeweza kumwita mtoto wangu jina hilo hata kidogo, yaani nisingeweza kumwita Rama nasema. Yaani basi tu hatukupewa uwezo wa kujua lijalo nasema jambo hili kwa mara nyingine lakini laiti tungewezeshwa kujua huenda ningeliepuka.
Na bado haya yote yalitokea kwa sababu tu Jadi hakuwepo maana Rama alikuwa amenitongoza siku nyingi sana lakini sikuwahi kumkubalia, naweza kukiri kuwa ule urembo wangu ulikuwa umeanza kuchepua tena baada ya matunzo mazuri kutoka kwa Jadida na ilikuwa lazima wanaume waanze kunitamani, kweli Rama akaanza kunitongoza mara kwa mara lakini Jadi aliyesimama kama dada yangu alinikemea kabisa, lakini sasa Jadida amekufa. Natakiwa kulipa kodi nikajikuta sina kimbilio zaidi ya Rama. Nikamtafuta mwenyewe na kumweleza kuwa nina shida na shilingi elfu tatu, alkanitazama kisha akakumbushia lile lengo lake la awali kuhusu kunitaka kimapenzi. Nilijua lazima tu atataka kitu hicho, nikajikuta katika maamuzi ya aina mbili tu nikose mahali pa kulala nikalale stendi wahuni wanibake bila kunipa hata senti tano ama nikubali kufanya mapenzi na Rama anipe hiyo pesa nikalipie pango niendelee kulala sehemu ambayo walau kidogo ina usalama.
Tukakubaliana na Rama kuwa nitaenda kuchukua nyumbani kwake, na sio nyumba bali ni chumba kikubwa. Majira ya saa tisa sitasahau ilikuwa saa tisa na robo maana saa kilikuwa kitu cha kwanza kuangalia baada ya kuingia katika chumba chake. Niliketi katika stuli iliyokuwa wazi, Rama akaniuliza natumia kinywaji gani nikaagiza maji, nililetewa nikayanywa huku nikijisikia aibu kuu, aibu kwa sababu nilikuwa pale kwa ajili ya kudhalilishwa. Nadia mimi niliyeitunza bikira yangu hadi chuo kikuu leo hii nauza ngono. Nauza nipate pesa ya kulipia chumba.
Niliumia sana kwa kweli, lakini wakati naumia katika nafsi Rama alikuwa akiniita majina ya kimahaba ambayo hayakuwa na maana kwangu, huwezi kuniita mpenzi mtu kama mimi ambaye nilijiona kama uchafu tu.
Alipotaka kunivutia kitandani nilimsihi kitu kimoja kuwa nilikuwa nina njaa kali, hakika sikuwa namdanganya yaani baada ya kuwa nimekula muhogo mmoja asubuhi hiyo sikuwa nimepata kitu chochote tena. Kweli Rama alitoka nje na kisha akaingia na sahani ya wali nikauvamia na kwa fujo, kisha nikashushia na maji. Sasa hapa niliweza kumridhisha Rama. Tukapanda kitandani anifanye anachotaka.
Akafanya kweli huku nikimzuga kuwa ninafurahia tendo lile. Lakini sikuwa pale hata kidogo.
Rama akamaliza, nikadhani nimemaliza kulipa deni lakini mara kutokea chini ya kitanda wakatokea wanaume wengine watatu ambao naweza kuwaita wababe.
Nikamuuliza Rama kulikoni akaanza kuniambia jambo ambalo sikutarajia hata kidogo mwanaume anaweza kufanya hivyo.
Rama akadai kuwa nilijifanya mjanja sana kumkatalia kimapenzi mapema, sasa nitamkoma yeye sio wa kuzungushwa hovyo. Nilijaribu kujitetea huku nikimtupia lawama dada Jadida lakini haikusaidia, wale wanaume wakaanza kuniingilia kwa zamu, nikiwa nimezibwa na kanga yangu mdomoni. Ramso ameketi akivuta sigara huku akicheka, mwandishi sio siri niliumia mno, nilijitahidi kuwahimili lakini walinizidi kwa nguvu, nikajikuta sasa nazizima!! Nikaanza kuona maluweluwe tupu!!
Na bado niliwasikia wanaendelea kuniingilia……
Kabla sijapoteza fahamu kuna mabo niliyasikia wakisemezana na sikujua yana maana gani maana ni kama nilikuwa nasikia kiarabu na kihindi ikiwa lugha wanayotumia. Masikio yalisikia kama kengere kali sana zikipigwa. Kisha kimya kikatanda…..kimya kikuu.
Nilikuja kushtuka usiku sana nikiwa kando kando ya maji ya ziwa viktoria. Nilijaribu kusimama lakini nilianguka tena, nikajaribu kupiga kelele lakini sauti haikuweza kutoka, nikaanza kujikongoja huku nikiwa nimepatwa na hali fulani iliyonikumbusha jambo fulani, nilijaribu kupingana na hali hiyo lakini ukweli ulikuwa huu huu ninaokueleza sasa. Rama akishirikiana na washirika wake walikuwa wamenifanyisha mapenzi kinyume na maumbile. Nilizidi kutambaa gizani, mara mbwa wakaanza kubweka. Walibweka hasa kisha wakanifikia nilipokuwa, mbwa mmoja akanisukuma chini na kuanza kunikwangua na makucha yake. Nilijaribu kujitetea lakini haikuwezekana, mara akaongezeka mbwa mwingine huyu alinivamia moja kwa moja na kuning’ata mkono wangu hapa (akajifunua mkono na kunionyesha kovu). Nililia kwa nguvu mara akafika mmiliki wa hizo mbwa, huyu alikuwa ni mlinzi. Akawafukuza wale mbwa. Akanimulika na tochi huku akiniuliza mimi ni nani, wakati huo sikuwa na nguo mwili, mbwa walizigawana.
Labda hata hili lilikuwa tatizo lililonifanya nizidi kuuchukia usiku ule mgumu kupindukia.
Yule mlinzi kijana alizima tochi yangu, akanisogelea na kujifanya anataka kunisaidia, lakini na yeye akanifanya vibaya. Alinibaka upesiupesi kisha akajiondokea, nilidhani ameondoka kweli lakini haikuwa hivyo alikuwa ameenda kuwashirikisha na walinzi wengine wenye tamaa.
Wawili wakanikuta nikiwa bado pale, mmoja aliomba sana niachwe kama nilivyo lakini bahati mbaya hakuwa mbabe kuliko wenzake. Mwenye nguvu akashinda nikabakwa tena. Kwa mara nyingine nikapoteza fahamu.
Nilikuja kushtuka alfajiri, bado sikuwa na nguo. Lakini kabla sijajua nini cha kufanya mara akina mama wanaowahi katika biashara zao asubuhi walinikuta nikiwa pale bila hili wala lile. Wakanipa msaada wa kanga wakiamini mimi ni changudoa niliyepata ajali kazini.
Labda walikuwa sawa….lakini siamini kama nilizaliwa kuwa changudoa.
Fadhaa ile ikanifanya nijikute katika maamuzi ya aina yake, maamuzi ya kurejea Musoma kudai changu….ni lazima nipewe changu…..ama la! Desmund anieleze kwanini aliamua kunitenda vile.
Sikuwa na la kupoteza kwa sasa, nikajikuta napoteza rasmi tabasamu langu, bila shaka roho ya Jadida ilinivamia…..niaamua kurejea Musoma kulisaka jibu la matatizo hayo. Maana haiwezekani yaani nimelawitiwa kisa Desmund, nikabakwa tena na teana kisa yeye, halafu anaendelea kuyafurahia maisha wakati mimi nadhalilishwa hapana Hapana mwandishi, mnyonge mnyongeni lakini haki yake……” Nadia hakuweza kumalizia, akaingia katika kilio cha kwikwi.
“Usilie nadia, nipo kwa ajili yako kama nilivyokwambia sawa!!” nilimweleza kwa sauti ya chini. Kisha nikamvuta na kumkumbatia. Hapa sasa akaanza kulia kwa sauti ya juu kabisa.
Kwa sababu hakuwa akiniona, nami uvumilivu ukanishinda nikajikuta natokwa na chozi hadharani kwa mara ya kwanza tangu nianze kuifuatilia simulizi hii ya Nadia.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
******
Usiku ulipita nikiwa chumbani kwangu nikijiuliza, wanaume tumelaaniwa ama? Nilikosa jibu kwa sababu na mimi ni mwanaume kama ni kweli tumelaaniwa basi hata mimi nimelaaniwa pia.
Nikakosa kundi la kumweka Desmund, nikakosa kundi la kuwaweka wale wanaume waliombaka Nadia akiwa katika hali mbaya kabisa kiafya, nikakosa pia kundi la kumweka Ramadhan Ramso yule mwanaume aliyempa adhabu Nadia ya kufanya mapenzi hadi kupoteza fahamu eti kisa tu alimkatalia ombi lake la kuwa naye katika mahusiano. Kisha baadaye akamkubalia.
“Sasa jamaa yeye ni nani hadi anataka kila anapotongoza akubaliwe?” nilijiuliza. Bado nikakosa jibu, lakini mwisho kwa shingo upande nikakiri kuwa tupo katika kundi moja lakini tabia zilitutenganisha!!!
Hilo lilikuwa wazo langu la mwisho. Nikasinzia!!
****
Nilisikia kama midundo ya ngoma za kizaire, midundo ambayo haikuwa katika mojawapo ya simu zangu. Halafu mbaya zaidi haikuwa katika mpangilio maalum.
Nikajigeuza, kuzikwepa zile kelele, lakini mara zikageuka!! Hazikuwa ngoma za kizaire, bali ulikuwa ni mlango wangu unagongwa!!
Nikasimama wima, nikapekecha macho yangu na kujifunga taulo kiunoni nikajongea mlangoni nikaufungua malango.
Hah! Alikuwa ni Nadia, alikuwa amebadili nguo tayari. Alikuwa ameng’ara na bila shaka alikuwa ametoka kuoga.
“Nchi itauzwa wewe!! Unalala hadi dakika hii, saa tatu sasa.” Alisema huku akionyesha uchangamfu wa hali ya juu. Nikastaajabu, nilikuwa nimelala sana. Nikatabasamu kisha nikainama na kukiri kuwa nilichoka sana usiku uliopita.
Nadia akaaniambia yu chumbani kwake, nikaiufunga mlango nikaoga name nikabadili nguo. Kisha nikamchukua kwa ajili ya kwenda kupata kifungua kinywa!!
Wakati tunakabidhi funguo mapokezi. Yule muhudumu akatuuliza iwapo tulihitaji kufanyiwa usafi ama la!
Mimi nikamwambia sikuwa nahitaji usafi Nadia yeye akamtazama kwa muda bilakusema lolote.
Nikamvuta mkono kando na kumuuliza.
“Nadia,mbona haujamjibu sasa. We unadhani atachukuliaje hapo…sikia Nadia usiruhusu kila mtu ajue matatizo yako sawa.” Nilimkemea. Bado hakunijibu kitu, nikajua tayari kuna jambo limemtokea katika akili yake kama kumbukumbu.
Nikamrudisha chumbani ili asije kusema lolote mbele ya hadhira, na pia kwa upande wangu ilikuwa nafasi nyingine ya kupata majibu ya maswali yangu ama kujua zaidi kuhusu Nadia.
Nikamwingiza chumbani kwangu. Nikategesha vifaa vyangu.
“Mwandishi, sio kwamba nina dharau la! Sio kwamba nilikosa cha kumjibu yule dada hapana! Lakini niliifikiria dunia isiyokuwa na huruma. Dunia mbaya! Dunia inayotunza watu wabaya.
Hivi kweli unaweza kuwa mwanadamu mwenye moyo na damu inayozunguka ukaamua tu kila mara kutumia matatizo ya mtu mwingine kujinufaisha? Halafu mwisho unaheshimika mbele ya hadhira kama mtu mwema?
Sawa nilijipeleka mwenyewe, na nilihitaji sana kuipata nauli ya kwenda Musoma. Sikuwa na raha ndo maana nikaenda pale. Ningekuwa na raha wala nisingeweza kuingia katika kazi hiyo.
Wakati mwingine ni heri ufe katika tatizo moja kuliko kuteseka katika matatizo mbalimbali ambayo kila moja lina uzito mkubwa kuliko lile lililopita.
Duniani kuna matusi na kuna wakutukanwa, ujue mabaamedi tunadharauliwa sana, yaani mwanmaume anakushika makalio anakutukania mama yako lakini ole wako umjibu na achukie!! Eti mmiliki wa baa anadai ni utovu wa nidhamu kumjibu hovyo mteja. Lakini nisingeweza kudhalilisha utu wangu. Nisingeweza hata kidogo kujiuza tena kwa wanaume ninaowachukia.
Mtu unafanikiwa kumtoroka mteja na vishawishi vyake halafu bosi nunayemuheshimu anadiriki kukufanyia ubaya!!
Sikujua kama yule bosi ninayemuheshimu angeweza kunitenda vile, mimi nilijiuona nina msimamo sana na wateja walilifahamu hilo, wewe nitukane nishike matako utakavyo lakini hunipati ng’o, hiyo ndo ilikuwa kauli mbiu yangu.
Nitakufungulia chupa, ukitapika nitadeki ukivunja chupa nitaokota lakini usitegemee nitakunyenyekea katika mwili wangu.
Nilikuwa nimejiwekea kiapo kuwa sitashiriki na wanaume tena, nia yangu kuu ilikuwa kufanikiwa kufikisha nauli ya kwenda Musoma kumkabili Desmund ambaye kuna maswali kadhaa nilitakiwa kupata majibu kutoka kwake. Maana Jadida alivyoenda mara ya kwanza hakupata majibu sahihi, na hata kabla hajajipanga kwenda mara ya pili akabakwa na kuuwawa.
Kutokana na msimamo wangu bosi wangu akanipandisha cheo, nikatokea kuwa baamedi, nikawekwa kaunta. Huku napo nilikuwa makini sana na pia mwepesi katika kuhudumia wateja. Bosi alikuwa akivutiwa na utendaji wangu wa kazi haswaa.
Siku moja bosi alitoa udhuru kuwa anaumwa, na ilikuwa lazima kukabidhi mahesabu jioni, nisingeruhusiwa kulala na pesa ya bosi.
Bosi akapigiwa simu, akampa maelekezo bwana mmoja anipeleke nyumbani kwake kukabidhi zile pesa.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Mimi sikuwa na shaka hata kidogo, nikaamini kuwa bosi alikuwa mgonjwa. Majira ya saa nne huyo bwana akanipeleka nyumbani kwa huyo bosi.
Nilipofika tu sebuleni nilitambua kuwa bosi alikuwa anaishi na familia yake. Picha ukutani zilimwonyesha akiwa na familia, lakini sikusikia hata kelele mle ndani. Bosi akajikongoja kutoka chumbani akiwa na bukta, akaketi huku akijinyoosha viungo nikatoa heshima yangu na kisha kuweka daftari na pesa mezani, tukaanza kupiga mahesabu. Lakini tofauti na siku nyingine bosi wangu alikuwa hana umakini kabisa, nikakiri kuwa bosi alikuwa anaumwa.
Lakini haikuwa hivyo, bosi hakuwa mgonjwa bali ulikuwa mtego tu. Mara akaniomba nimwongoze chumbani kwake akalale kwani kizunguzungu kilikuwa kimemzidia, mimi kama mwanadamu nikafanya alivyoniomba. Nikamshika mkono mmoja na bega nikamkongoja hadi katika chumba chake.
Tulipofika nikadhani atajilaza kitandani lakini badal;a yake akafunga mlango.
“Nadia, ni kweli naumwa…..lakini naumwa ugonjwa wa mapenzi.” Bosi alizungumza huku akionyesha uimara. Nikaduwaa maana sikutegemea jambo hili.
“Hivi Nadia kweli,muda wote huo haujui kama nakupenda. Mimi nimekutoa kwa wale walevi, nimekuweka sehemu yenye pesa, hujui tu kama nakuhitaji, nafasi yako nimewanyikakina Farida, Jeni ambao umewakuta nimekuweka wewe hujajua tu kuwa nakupenda Nadia.” Alinibembeleza huku nikiwa sijielewi bado kama ni ndoto ama vipi? .
Mara akanikumbatia yule mwanaume aliyekuwa ametanuka kifua chake na kitambi kikiwa kinachungulia.
Nilijaribu kujitetea mwandishi, nilimsihi sana lakini hakunielewa hata kidogo. Alikuwa katika matamanio ya hali ya juu.
Nikiwa bado katika kujitetea akanirusha kitandani.
Mwanaume ni mwanaume tu, ana nguvu na akiamua jambo mkiwa wawili hashindwi kamwe!!
Sijui niseme bosi alinibaka la! Hakunibaka, nilikubali yaishe. Maana tulilala naye hadi asubuhi, nikaoga naye huku kila mara nikona aibu kuitazama picha ya mkewe ambayo ni kama ilikuwa ikinitazama nikifanya uchafu na mumewe pale kitandani.
“Sijapenda iwe hivi mama!!! Nisamehe.” Niliiambia ile picha wakati bosi ameenda kuoga.
Aliporejea alikuwa anatabasamu na kuniambia siku inayofuata nisiende kazini, na atatoa taarifa kuwa sitaenda, nilikubali huku nikijiahidi kuwa nitafanya kila niwezalo nipate kiasi fulani cha pesa nyumbani kwa bosi huyo na kisha nitaacha kazi mara moja. Nikiacha kazi nitasafiri kuelekea Musoma kutimiza azma ambayo haikumalizwa na Jadida.
Kilichokuja kutokea majira ya saa sita mchana ndipo kilitokea kituko cha mwaka ambacho kiliyarejesha majonzi lakini kama hiyo haitoshi niliandika historia nyingine.
Bosi alinikuta nikiwa sebuleni nikiwa nimejifunga kanga za mkewe nikiwa natazama luninga huku nikiyafikiria maisha yangu kwa ujumla. Kwa mara ya kwanza nilikuwa nimeketi kwa utulivu katika nyumba kubwa. Nikiwa na mtu ambaye namuamini pia.
Nikiwa kimada rasmi!!
“Nadia!” nilisikia sauti ikiniita kutoka chumbani.
Nikatambua ni bosi, nikaacha kutazama luninga nikakimbilia chumbani.
Nilikutana na macho makali sana yakinitazama, alikuwa ni bosi lakini huyu alikuwa ana hasira sana sikujkua nimemkosea nini ama kuna nini kimetokea, alikuwa na bukta yake.
“Nadia wewe, wewe…..ni wa kuniletea mimi kisonono!!” aliniuliza huku akitetemeka midomo.
Nikastaajabu bila kujua nini cha kujibu.
“Kumbe unapiga umalaya kimya kimya na kujifanya wewe msafi sana. Nadia Malaya wewe…” alishindwa kuendelea akanivamia akanipiga kibao usoni, sijui ilikuwaje lakini kanga ilifunguka nikabaki uchi, akanikamata na kuanza kunichapa na mkanda, nikajitahidi kuomba msamaha lakini hakunielewa. Alinipiga hadi nikatambua kuwa nikiendelea kuvumilia huyu mtu ataniua. Alikuwa ana mkono mzito sana.
Na huu ulikuwa unyanyasaji wa hali ya juu sana, yaani amenilaghai mwenyewe kufanya naye mapenzi, sikuwa na wazo la kuwa na mwanaume. Nikajiweka mbali nao. Sikatai kuwa yawezekana nilimuambukiza huo ugonjwa lakini alinilazimisha mwenyewe kufanya naye mapenzi.
Nilimsihi pia kutumia kinga lakini yeye mwenyewe akanibiashia akalazimisha kila alichotaka kiwe. Kajiambukiza ama nimemwambukiza? Nilijiuliza!!!
Nikapata jawabu kuwa yule mwanaume ananionea.
Ni hapa nilipoukumbuka ukaidi wa Jadida!! Nikayakumbuka mabavu yake aliyokuwa akiwawekea wanaume!
Kwa mara ya kwanza nikaamua kujitetea, lakini katika kujitetea kwangu nikafanya jambo dogo lililozua balaa huku likinihamasisha kufanya zaidi na zaidi.
Nilijikusanya mwili mzima, kisha kwa kichwa kichwa kama kondoo nikamvamia yule mwanaume nikiwa nimeyaunganisha meno yangu. Nikamchota mithili ya ng’ombe nikamtupa mbali.
Kilisikika kishindo mara moja tu na kimya kikatanda!!
Mwandishi nilikuwa sijawahi kuona maiti, hivi kumbe kufa ni sekunde tu, bosi alijibamiza kichwa chake katika marumaru pale ndani.
Kimya kile kilikuwa kimya cha milele!!
Nilitoweka pale nikiwa nimetaharuki, nisijue nini cha kufanya. Nikavaa nguo zangu vyema, nikatoweka pale ndani huku nikiuruka mwili wa yule mwanaume!!
Hali ilikuwa ya hatari. Hatua kwa hatua hadi nje!!
Nilisikia uzito fulani katika sketi yangu, sikumbuki niliweka nini hapo awali. Nilipojipekua nikakutana n’na kibunda cha pesa.
Bila shaka yule bosi aliniwekea maksudi kama shukrani kwa penzi nililompa. Na hii ni kabla hajagundua kama nimemwambukiza kisonono. Niliondoka mbio mbio baada ya kutoka nje.
Nilirejea nyumbani kwa Chausiku majira ya usiku sana, huyu ndiye msichana ambaye alikuwa akinihifadhi katika chumba chake huku akiwa anafanya kazi katika baa nyingine jirani na ile niliyokuwa nafanya mimi.
“We Nadia wewe…..umemfanya nini tena bosi wako?” aliniuliza huku akiwa na hofu tele.
“Kwani nini?” nilijifanya sijui lolote.
“Bosi wako si amekutwa amekufa wewe..na wanadai kuna uwezekano kuwa ulilala kwake mwenzangu…mbona kazi sasa.” Alinieleza kwa sauti ya kunong’oneza, kisha akaendelea.
“Nadia mimi dada yako nambie nini kimetokea.” Alinisihi.
“Dada Chausiku mi nimemsukuma tu alitaka kunibaka, kanipiga sasa dada kanipiga kidogo aniue nikajitetea kwa kumsukuma mimi sikuua dada!!!” nilimweleza huku nikiwa nalia.
“Nadia, cha msingi wewe ondoka hapa Mwanza, mimi na wewe ni maskini. Na unafahamu hatuna cha kuwabishia wale wenye pesa, Nadia nilikukuta ukiwa na msiba mzito siku nakuchukua tafadhali sitaki nilie tena ukihukumiwa kwenda jela. Ondoka Nadia ondoka!!!” alinisihi dada yule. Kisha akaingia ndani akatoka na kikopo chake cha kuhifadhia pesa. Akakifungua na kutoa pesa aliyokuwa amehifadhi shilingi elfu ishirini akanipatia.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Nilimtazama, sikuichukua ile pesa nikamkumbatia kwa nguvu, nikahisi upendo mwingine ukitoweka kwangu, nikajipekua katika sketi yangu nikalifungua lile burungutu. Nikatoa noti nne nyekundu nikampatia. Akazikataa na kuniambia kuwa nilikuwa ninayo safari ndefu sana mbele yangu. Akanisihi niende kwa amani…..nililia sana!!
Baada ya siku mbili, Nadia nilikuwa natafutwa kwa kosa la kuua!!
Nikaingia rasmi katika safari nyingine ya maisha ya kikimbizi, yaani ukimbizi katika nchi yangu huru kabisa!!!!
Lakini ningefanya nini iwapo nimelaaniwa!!!
Nina njaa naomba twende kula” alimaliza Nadia….akafuta machozi!!
Nilipata mshtuko kusikia kuwa kumbe Nadia aliwahi kupata kesi ya mauaji!! Laiti angekuwa amemuua Desmund wala nisingeshtuka, kumbe aliua katika jiji ambalo yupo kwa sasa. Mwanza!!! Lakini hakupanga kuua.
Halafu kumbe Jadida aliwahi kwenda Musoma…harakati zipi zilimpeleka dada huyo ambaye ni marehemu tayari.
******
Mlo unaoitwa ‘mlo kamili’ uliletwa katika meza yetu ambayo kwa maksudi kabisa tuliiacha izungukwe na viti viwili ili tuwe na uhuru wa kufanya mambo yetu. Hasahasa mazungumzo maana tulihitaji kuwa na faragha kwa kila kitu tulichokuwa tunafanya.
Nadia alipitia orodha ya chakula, safari hii tuliagiza chakula cha kufanana.
Sato na ugali wa dona!!
Hakika Nadia alikuwa na njaa!!
Mbaya zaidi hatukuwa tumepata kifungua kinywa asubuhi ya siku hiyo.
Kila mmoja akajikita katika sahani yake na kushambulia awezavyo, mara kwa mara nikimtupia jicho Nadia niweze kupata kitu cha kuandika hasahasa katika muonekano. Sikutaka kupitwa na tukio hata moja, hata jinsi anavyomeza chakula nilitaka kufahamu ili nikiandika kitu niwe nimeandika kitu chenye uhalisia na safari yangu hii iwaridhishe waliokuwa wanaifahamu na hata pesa zao waone zimeenda kiusahihi kabisa.
Nikiwa nimefikisha ugali wangu nusu ya safari huku samaki aina ya sato akiwa ameteketea upande mzima na macho ya samaki huyo yakiwa wazi yakinitazama. Niligutuka kuwa Nadia alikuwa amesita kula na alikuwa akiangaza macho huku na kule.
Nilimtazama kwa kwa sekunde kadhaa kisha akaonekana kupata kitu alichokuwa akikihitaji, akanyanyua mkono wake akapunga hewani.
“Nini tena Nadia…mbonaa….” Nilimuuliza huku nikiitazama sahani yake.
“Mwenzangu, nimeshiba kama nini?”
“Nadia umeshiba, yaani hivyo vitonge viwili tu Nadia hebu acha utani wewe.” Nilijaribu kubishana naye, wakati huo yule mtu wa kunawisha alikuwa amefika tayari akaanza kunawa mikono.
Nikakosa la kusema!!
“We acha huyo samaki hapo bwana!” nikamzuia yule muhudumu,tamaa zilikuwa zimeniingia tayari, na pia ubahili wa kumlipia samaki yule mkubwa kisha Nadia hata upande mmoja hakuwa amemaliza.
Muhudumu akanitazama kwa jicho la chuki lakini midomoni akatoa tabasamu lao la kawaida. Sikujali kuhusu hilo.
“Lakini Nadia..yaani samaki ndo umedonoa hivyo?” nilimuhoji, kisha nikaendelea,”Au waifungashe tukaisonsomole chumbani”
Nadia akalipuka kwa kicheko baada ya mimi kutumia neno lile maarufu sana kwa wasukuma jijini Mwanza na mkoani Shinyanga. Wakimaanisha ‘kula katika namna ya kufurahia’
“Ujue zamani nilikuwa nakula sana, huyo samaki huyo mbona hata robo tatu ningeweza kumfikisha mimi mwenyewe,unadhani mi huwa nina aibu katika kula, nakula sana tu lakini huwezi amini zamani niliambiwa kuwa mtu ukiwa umezoea kula chakula kidogo sana pasi na matakwa yako basi unajikuta bila kujua tumbo linajibana na kuwa dogo siku ukijaribu kula chakula kingi haiwezekani.
Sikuwahi kuamini, lakini maisha niliyoishi Musoma Vijijini huko yalinifanya niamini kuwa haya mambo yapo. Ile familia ya mzee Marwa ile, basi tu Mungu hakuwapa utajiri. Hakuwapa mali na dhiki zote akaziacha juu yao sijui kwaninihata. Ujue bila wao Nadia mimi ningekuwa nishakufa zamani sana, yaani zamani sana mwandishi. Sawa walikuwepo wanafamilia na mapungufu yao lakini hakika mzee Marwa ni mtu mwema sana japo najua ananichukia sana!!!
Dah! Safari ikiwa una nia mbaya nayo hakika unaweza kuwavurugia hata wengine ambao hawana nia mbaya, yaani jinsi nilivyokuwa nakereketwa hapa kooni, jinsi nilivyokuwa nina hasira nikiwa ndani ya basi. Yaani ilikuwa sawa kabisa mwandishi, yaani kila mtu nilikuwa na hasira naye ndani ya gari. Kila mwanaume nilimuona kama Desmund ama Ramso Rama, na kila mwanamke alifanana na mama yake Desmund huku wasichana wakimfanania yule wifi feki mwanaharamu kabisa. Aliyenigusa nilijikuta natoa tusi zito, kondakta akiwa wa kwanza kisha akafuata abiria ambaye alinigonga bahati mbaya, nikamtapikia matusi ilhali nikijishangaa japo sikuweza kujizuia.
Abiria niliyekaa naye siti moja pia aliipata moto moto ya matusi huku nikitishia kupigana. Watu wakadhani huenda nimechanganyikiwa. Wakaamua kunisusia!!
Safari za usiku sijui kama zina raha yake, lakini nililazimika kusafiri usiku,niliondoka Mwanza na gari ya mwisho kabisa kuelekea Musoma. Sikutaka hata mtu mmoja auone uso wangu. Hofu ilinitawala sana, hofu ya kukamatwa kwa kesi ya mauaji jijini Mwanza hivyo niliamua kusafiri usiku.
Baada ya basi zima kuwa limenichukia mimi naye niliendelea kuchukia zaidi.
Ni basi kuwa Mungu alituzibia namna ya mtu kuweza kuona mambo yaliyo katika moyo wa mwenzako. Lakini abiria wangeuona moyo wangu jinsi ulivyobeba uchungu mzito hakika wangelia na kusaga meno, wanaume wangejilaani huku wanawake wakiinama kwa aibu.
Lakini hawakujua haya yote, nilipoanza kulia ghafla ndani ya gari, wakatambua kuwa ukichaa unaanza kunipanda, nikiongea peke yangu jirani yangu anasogea pembeni kidogo ili nisimdhuru. Hali hii haikuwa njema hata kidogo!!
Hatimaye jirani alipopata upenyo wa kupita akatoweka asirejee tena, siti ya watu wawili nikabaki peke yangu.
Nililia sana, kila mmoja alinitafsiri alivyojua ye mwenyewe mi sikujali tena hayo.
Hatimaye ukafika ule muda wa kutengwa, muda ambao ulinikutanisha na familia nyingine kiajabu ajabu.
Familia ya mzee Marwa!!
Mwendo wa basi ulianza kupungua, kisha waliokuwa mbele wakaanza kutishia amani kwa , maneno yao.
“Tumetekwa…..tumetekwa jamani. Majambazi weeee!!” Alilalamika mwanaume mmoja.
“Mwanaume wewe acha hofu za kijinga jinga nani kasema tume…” kondakta alibwata lakini hakuimaliza kauli yake. Mara kweli tukawa tumetekwa.
Kwanza ikapigwa risasi, bila shaka hewani, lakini kwa wakati ule kila mmoja angeweza kuisikia ikiwa imelia katika sikio lake na labda kujihisi amekufa.
Hata mimi nilihisi nimekufa lakini nikajishangaa kuwa nipo hai katika kiti kilekile, cha ajabu sasa wale abiria waliokuwa wamenikimbia kwa kuhisi mimi nina wazimu, wengi walikuwa wamenikumbatia bila uoga. Wanadamu bwana, hapa huja ile kauli kuwa panapo matatizo wengi watakukimbilia wewe lakini uwapo na tatizo basi watakukimbia wao na usiwakamate katu!!
Mimi sikuwakimbia, na ningeweza vipi kuwakimbia iwapo walikuwa wameniegemea? Basi ukawa mshike mshike!!CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kwangu mimi kidogo ilikuwa salama, mara ghafla msukumo ukazidi kisha nikaanza kusikia milio ya ajabu ajabu akina mama wakilia na wanaume wakilalamika kwa maumivu. Jicho langu likafanikiwa kuona panga si panga jambia si jambia.
Kaka, usiombe kuona ninachokuhadithia mara likanyanyuliwa likashushwa, waaa!! Damu pwaa!! Mkono chini!! Abiria kanyofolewa mkono!!” Nadia akasita akanitazama machoni, bila shaka alitaka kutambua kama nimeguswa na kipengele kile, wacha wee alichokiona anajua yeye, maana mimi kama mimi japo sijioni nilijua kuwa nimekodoa macho sana. Inatisha msomaji!! Mkono kuondolewa!! Eti panga si panga jambia si jambia!! Nadia bwana!! Akaendelea!!
“Watu wakapiga mayowe mimi nikiwa hata uwezo kufungua mdomo sina, wakinamama wakazidi kunilalia, mara jicho langu likaiona panga si panga jambia si jambia likinyanyuliwa tena, mara likatua. Safari hii mlio uliotoka ni paa!! Mwanamama akapiga mayowe alikuwa amepigwa na ubapa wa maana!! Uzito ukaanza kupungua mimi nikiwa sijui nitafanya nini, kumbe ni mmoja baada ya mmoja anatolewa nje.
Nami nikafikiwa, kabla ya kuvutwa nikatoka mwenyewe, nikaenda nje upesi, maana wale waliojichelewesha walipigwa na ile panga si panga jambia si jambia. Niliposhuka ndani ya gari nikavutwa, kushoto. Ndani ya sekunde kadhaa nilikuwa uchi wa mnyama.
Nikasukumwa huku nikiona aibu huku aibu ikaniisha, kila abiria alikuwa uchi wa mnyama.
Kilikuwa kizaazaa. Wakati huo sasa wimbo wa mtaji wa masikini ule wa msanii gani sijui ulikuwa upo bado.
Wale majambazi au watekaji walikuwa wanao, wakawasha redio, Banza Stone…eheee!! Nimemkumbuka Banza anaimba kwenye redio sisi tunacheza uchi. Tena tulitakiwa kucheza kwa bidii huku kila mara mmoja wetu akiingia katikati kunengua mauno. Wakati tunaendelea kucheza ikafika zamu ya dereva kukata mauno, kama ingekuwa filamu hakika ningecheka maana dereva alikuwa kibonge na ana tumbo kubwa!!.
Dereva kibonge, akagoma. Mwandishi ujue alikuwa jirani yangu sana, nilimsihi, nilimsihi akubali yaishe, sijui kama alidhani bado nina wazimu wa kwenye gari lakini mimi nilikuwa nimeona kitu. Mwandishi niliona macho yanayofanana na ya marehemu Jaduda. Macho yasiyokuwa na utani na yanayomaanisha yanachosema. Yule jambazi hakuwa katika utani!!!
Kilikuwa kitendo cha sekunde kadhaa yule mwanaume jambazi ambaye alikuwa akionekana macho tu, aliruka na panga si panga, jambia sijambia.
Ohooo!! Damu ya mwanadamu ni ya moto sana aisee!!, damu ya dereva ikanirukia, alikuwa amechomwa bisu la tumboni.
Wacha watu waanze kupiga mayowe wakilia huku Banza Stone akizidi kuimba mtaji wa masikini ni nguvu zake mwenyewe…..nasi tukitakiwa kucheza. Huku mwenzetu mmoja akipigania uhai bila dalili yoyote ya kufanikiwa!!!
Ilitisha kutazama!!!
Baadaye tukaamriwa kulala chini kifudi fudi, sasa hakuna aliyebisha kila mtu alilala hivyo. Kimya kikatanda, redio ikiendelea kuimba kuwa mtaji wa masikini ni nguvu zake mwenyewe. Sisi tumelala kifudifudi. Uchi wa mnyama….tochi mbili zikitumulika. Tuakendelea kutambua kuwa wale majambazi wapo nasi!! Nusu saa ikakatika.
Mbwa waliokuja kutubwekea na kisha kumng’ata mmoja wetu akapiga mayowe ndio walitukurupua tena……
Kila mmoja akaanza kuhaha akitafuta namna ya kujistiri na hali ile.. Wengine walikuwa na watoto wao, wengine na wake zao, huenda na wengine na baba mkwe zao.
Kizaazaa!! Nani atajali katika hali hii???
Huyu avae ya huyu mara huyu avae ya huyu. Hapakuwa na umoja, huenda hicho kitu ndio kilisababisha hata tukashindwa kuelewana, mtu mmoja akavaa nguo yangu nilipomshika akanitukana akidai mimi ni kichaa.
Umoja ukajengeka, wakamuunga mkono kuwa mimi ni kichaa na sijui ninachokiongea, wengine wakaenda mbali zaidi na kusema kuwa ni mimi nimewazulia balaa lile la aina yake.
Mara nikatengwa maneno yakawa maneno!! Mara nisukumwe mara nitukanwe!! Hakuna aliyekuwa nani mwandishi!! Hakuna hata mmoja!!
Ile nguo aliyoing’ang’ania yule dada ndio nguo ambayo ilikuwa ndani yake nimeishonea ile pesa yangu niliyomuibia marehemu bosi wa Mwanza….na niliamini kuwa lazima itakuwemo, nilishona kwa ustadi mkubwa sana. Wale majambazi wasingeweza kuiona!!
Mwandishi Ni heri ningekaa kimya tu nisijibizane na umati ule …..ni heri ningekubaliana na usemi wa mwenye nguvu ndo mwenye haki.
Nilikosea sana kuthubutu kuongea….nilikosea sana kuidai haki yangu……” kilichotokea ……..
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
***NINI KILIMSIBU NADIA BAADA YA KUIDAI HAKI YAKE…..
#Usikose kipengele atakachoendelea kusimulia tena……ujue kwa mzee MARWA nini kilijiri na alifika vipi??
##TOA MAONI YAKO…..SHARE ZAIDI NA ZAIDI.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment