IMEANDIKWA NA : NYEMO CHILONGANI
*********************************************************************************
Sehemu Ya Kwanza (1)
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Unahitaji kuwa nani baadaye?” lilikuwa swali la kwanza mzee Jackson Gwamaka alimuuliza binti yake aliyeitwa Nandy aliyekuwa akisoma darasa la sita katika Shule ya Msingi Kurasini, jijini Dar es Salaam.
“Nitataka kuwa muimbaji wa nyimbo za Injili, nitataka nimuimbie Mungu mpaka viwete watembee, vipofu waone na wenye matatizo mbalimbali waponywe,” alijibu binti huyo mrembo huku akimwangalia baba yake kwa sura iliyojaa tabasamu pana.
“Unahisi utaweza kumuimbia Mungu maisha yako yote?”
“Ndiyo! Nitamuimbia mpaka naingia kaburini. Nitataka nimtumikie yeye tu katika maisha yangu,” alijibu msichana huyo.
Mzee Gwamaka akamwangalia binti yake kwa mara nyingine, tabasamu pana likatawala usoni mwake. Alimpenda Nandy, alikuwa mtoto wake pekee katika maisha yake.
Moyo wake ulikuwa na faraja kubwa, alipenda kumuona Nandy akizungumzia kuhusu ukuu wa Mungu. Kila siku alimlea binti yake katika mazingira ya kidini huku akimwambia kuhusu ubaya wa wanaume.
Hakutaka kumuona binti yake akipotea, katika maisha yake alitamani kumuona akiendelea kumsifu Mungu mpaka pale atakapoingia kaburini. Mke wake, alifariki dunia siku alipokwenda kujifungua hospitalini. Moyo wake ulimuuma, alilia sana na ndiyo maana kwa Nandy alikuwa roho yake, faraja yake na hakutaka kumuona binti yake huyo akipotea.
Kila siku alimfundisha Nandy Neno la Mungu, alimwambia mambo mengi makuu ambayo Mungu alikuwa akiyatenda tangu kipindi cha Isaka,Yakobo na vizazi vingine vilivyofuata vikiwemo vya Mfalme Daudi na Suleimani.
Mbali na kutamani kumtumikia kumtumikia Mungu, Nandy alikuwa miongoni mwa mabinti waliokuwa na sura nzuri kupita kawaida japokuwa alikuwa akiishi kwenye umasikini mkubwa.
Mtaani hapo Kurasini alipokuwa akikaa, gumzo lilikuwa yeye tu. Alikuwa na umri mdogo lakini kila mtu aliyekuwa akimwangalia aliamini kwamba msichana huyo angekuja kutingisha sana siku za usoni.
Barabarani, wanaume walimtolea macho, kila aliyemwangalia hakuacha kumwangalia mara moja, alimwangalia mara mbili-mbili huku wengine wakidiriki kusimama na kumwangalia mpaka alipopotea katika macho yao.
Shuleni hakuwa msichana muongeaji, alikuwa mkimya huku muda mwingi akipenda kujisomea Kitabu Kitakatifu cha Biblia ambacho alikuwa akienda nacho mpaka shuleni.
Watu walimzoea kwa kumuita Sista kwani alionekana kupenda sana dini kuliko hata kusoma masomo ya darasani. Pamoja na sura yake nzuri, mvuto wake, Mungu alimbariki Nandy sauti.
Alijua kuimba, kila alipokuwa akisimama kanisani na kuongoza pambio watu walichanganyikiwa, sauti yake ilikuwa kali, iliyochujwa kiasi kwamba kila mmoja akamtabiria kuwa muimbaji mashuhuru nchini Tanzania miaka ya baadaye.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Siku zilikatika mpaka pale alipoingia darasa la saba na kumaliza. Uzuri wake uliongezeka, nyonga zikatanuka na kifua kuanza kuchuja. Urembo wake ukaongezeka na wanaume wakazidi kumpenda na hata wengine kuanza kumfuatilia kwa kuwa waliamini kwamba alikua hivyo alistahili kulala naye.
Wanaume wakaanza kumchombeza kwa maneno mbalimbali, wale wasiokuwa na aibu ya kutembea na watoto wadogo hawakumuacha, kwao, kitendo cha kifua kuonekana kimejaa tayari alionekana kuwa mkubwa.
Nandy aliogopa, hakukuwa na mwanaume aliyediriki kusimama naye, kila alipokuwa akiitwa, alikimbia, kwake, kwa malezi aliyokuwa amepewa na baba yake yalimfanya kuwaogopa wanaume kupita kawaida.
Wanaume hawakutaka kukata tamaa, kwao, hizo zilionekana kama changamoto na hivyo kuendelea kumfuatilia. Idadi ya wanaume waliokuwa wakimtaka ikaongezeka, kila mtu akatamani kulala na Nandy na kuwa mwanaume wa kwanza kufanya naye mapenzi katika maisha yake.
Nandy alijichunga, hata alipoingia kidato cha kwanza katika Shule ya Wasichana ya Jangwani bado msimamo wake ulikuwa uleule kwamba hakutaka kulala na mwanaume yeyote yule.
Kila walipokuwa wakitoka shuleni, wanafunzi wa Shule ya Wavulana ya Azania walikuwa wakisubiri nje, kila mmoja alitamani kumuona kwani alionekana kuwa msichana wa tofauti sana huku wengine wakihisi kwamba Mungu aliamua kumuumba msichana huyo wikiendi, kipindi ambacho alipumzika na kumuumba kwa udongo wa tofauti na wengine.
“Nandy!” alijikuta mwanafunzi mmoja akilitaja tu jina hilo.
“Amefanyaje tena?”
“We acha! Yule demu mkali bwana! Demu ni nuksi sana,” alisema mwanafunzi huyo huku akimwangalia rafiki yake na kuanza kucheka.
“Sasa wewe umegundua hilo leo?”
“Hapana! Nimegundua tangu siku ya kwanza nilipomuona. Ninasema hivyo kwa sababu amenichanganya sana. Nandy mzuri mno, demu bomba sana,” alisema mwanafunzi huyo.
Ni stori za uzuri wa Nandy ndizo zilizokuwa zimetawala midomoni mwa wavulana wengi. Walimpenda kwa kuwa alikuwa na sura nzuri, ngozi laini ambayo wanaume wengi iliwafanya kumfuatilia pasipo kumpata.
Nyumbani, mzee Gwamaka aliendelea kukandamiza misumali, kila siku ilikuwa ni kuongea na binti yake na kumwambia mambo mengi kuhusu wanaume, hakutaka kabisa kumuona binti yake akiingia kwenye mahusiano ya kimapenzi kwa sababu tu hakutaka kuona akiumizwa.
Aliwaponda wanaume, akaufanya moyo wa Nandy kuwaona wanaume wana roho ya kinyama, aliwachukia na kila alipokuwa akiitwa, aliogopa na kukimbia.
Aliendelea na maisha hayo ya kuogopa wanaume mpaka alipofika kidato cha nne. Japokuwa alionekana kuwa mkubwa lakini bado aliendelea kuwaogopa wanaume kila siku, hakuacha kuwakimbia kila alipokuwa akiitwa na wanaume.
“Nandy! Tatizo nini kwani?” aliuliza mwanafunzi mmoja huku akiwa amemshika Nandy mkono, hakutaka kumuachia kwani aliwahi kumuita mara nyingi sana lakini msichana huyo alikuwa akimkimbia.
“Niachieee...”
“Nikuachie! Umenikimbia sana, leo niambie ukweli!”
“Ukweli wa nini Mike. Niachieeeee.”
“Nataka uniambie! Unanipenda au hunipendi?”
“Nimesema niachieeeee...”
“Nijibu kwanza.”
“Sikupendi! Sikutakiiiii...” alisema Nandy na kwa kutumia nguvu zake, akajitoa mkononi mwa Mike na kukimbia.
Hilo likaonekana kuwa tatizo, Nandy hakutaka kukubali, alipofika nyumbani tu, kitu cha kwanza kilikuwa ni kumwambia baba yake kilichokuwa kimetokea.
Mzee Gwamaka alivimba kwa hasira, hakuamini kama kungetokea mvulana ambaye angemfanyia hivyo binti yake. Siku iliyofuata, ili kuonyesha kwamba binti yake hakutakiwa kuguswa akaelekea shuleni huko na kuwaambia walimu ambapo baada ya Nandy kuulizwa akamtaja kijana huyo.
Adhabu iliyotolewa siku hiyo, hakukuwa na mwanafunzi aliyediriki kumsogelea Nandy na kumwambia kitu chochote kuhusu mapenzi, wote walimuogopa kwani kila walipokumbuka mzee Gwamaka jinsi alivyokwenda shuleni hapo akiwa amevimba kwa hasira, hakukuwa na mtu aliyediriki kumsogelea.
Mpaka Nandy anamaliza kidato cha nne shuleni hapo bado hakuwa amemjua mwanaume yeyote yule. Aliendelea kujitunza kujitunza huku akimwambia baba yake kwamba malengo yake katika maisha yake yalikuwa ni kumtumikia Mungu mpaka anaingia ndani ya kaburi.
Baada ya kukaa nbaada ya kumaliza kidato cha nne ndipo walipotangaziwa kanisani kwao kwamba kungekuwa na mkutano mkubwa wa injili ambao ulitarajiwa kufanyika katika Viwanja vya Jangwani huku mhubiri mkubwa wa Kimataifa, Benn Hinn akitarajiwa kuhubiri katika viwanja hivyo.
Hiyo ilikuwa ni taarifa njema, kwa kuwa alikuwa na sauti nzuri huku akipewa uongozi katika kuimba pambio, Nandy akaambiwa ajiandae kwani alitakiwa kuongoza pambio katika kipindi chote cha mkutano huo.
Kwake, nafasi hiyo ilikuwa kubwa mno. Alimfahamu muhubiri huyo wa kimataifa aliyekuwa akizunguka dunia nzima huku akilihubiri Neno la Mungu, kitendo cha kuteuliwa kuongoza kikundi cha pambi katika mkutano huo ilionekana kama ndoto yake kuwa kweli.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Matangazo bado yalikuwa yakiendelea kufanyika, makanisani watu walitangaziwa kuhusu mkutano huo mkubwa wa injili. Kila mtu alichanganyikiwa, Wakristo wengi wakatamani kuhudhuria mkutano wa mhubiri huyo aliyekuwa akivuma duniani.
Viwanja vya Jangwani vikaonekana kuwa vidogo kwani Wakristo wengi jijini Dar es Salaam walipanga kwenda huku hata wale waliokuwa mikoani nao wakisafiri kuelekea jijini humo kwa lengo la kusikiliza mahubiri kutoka kwa mhubiri huyo.
Baada ya siku kukatika, hatimaye mkutano mkubwa wa Injili ukaanza katika viwanja hivyo. Siku ya kwanza, alihakikisha anamuimbia Mungu kwa uwezo mkubwa ambao hakuwahi kuimba maishani mwake mwote.
Sauti yake ilipoanza kusikika, watu walichanganyikiwa, kila mtu akaangalia vizuri jukwaani, alitaka kumuona msichana aliyeimba kwa sauti nzuri na kali kiasi kile. Macho yao yalitua kwa msichana Nandy ambaye alinyanyua mkono mmoja juu huku mwingine akiwa ameshikilia kinasa sauti.
Aliimba kwa nguvu, jasho lilimtoka, hakujali, katika kumuimbia Mungu hakujali kitu chochote kile. Mawazo yake na akili yake ilikuwa kwa Mungu wake, alicheza na kurukaruka kiasi kwamba wakati mwingine alionekana kama kuchanganyikiwa.
Mkutano ulipomalizika, kila mtu alimfuata na kumsifia kwani siku hiyo ya kwanza alionekana kuwa moto wa kuotea mbali kwa jinsi alivyomsifu Mungu. Kila alipopongezwa, hakuchukua utukufu, aliwaambia watu kwamba utukufu ulikuwa kwa Mungu aliyekuwa juu.
“Ila umeimba bwana!”
“Nashukuru mama! Utukufu kwa Mungu,” alisema kila alipofuatwa na kusifiwa.
Akaanza kujiandaa, baba yake, mzee Gwamaka alikuwa akimsubiri kwa kuongea na watu mbalimbali. Hakutakiwa kuondoka mapema kwa kuwa kanisa lao ndilo lililoandaa mkutano, alitakiwa kuhakikisha kila kitu kinakaa sawa kabla ya kesho kuja na kuendelea na mkutano.
Wakati akiendelea na marafiki zake kuweka vitu vizuri akasikia akiitwa kwa nyuma, alipogeuka, macho yake yakatua kwa kijana mmoja ambaye alipiga hatua kumsogelea pale alipokuwa.
Kwa kumwangalia kijana huyo, isingekupa kazi kugundua kwamba alitoka katika familia ya maisha mazuri. Alivalia shati jeupe, tai nyeusi na suruali nyeusi huku akiwa na miwani ya macho.
“Bwana Yesu asifiwe Nandy,” alisalimia kijana huyo kwa sauti ya upole kabisa.
“Amen kaka!” alijibu na kuendelea na kazi yake.
“Mungu amekubariki sana, amekupa kitu adimu mno. Umeimba kupita kawaida, hiyo sauti yako, hakika mshukuru sana Mungu!” alisema kijana huyo huku akiachia tabasamu, japokuwa palikuwa na kigiza fulani lakini Nandy aliliona vizuri tabasamu lile.
“Nashukuru! Utukufu kwa Mungu!”
“Naitwa Dickson Kambili!” alijitambulisha kijana huyo na kumpa mkono lakini Nandy hakunyoosha mkono wake kumsalimia.
“Nashukuru kukufahamu!”
“Basi sawa. Ulinzi wa Mungu uwe nawe. Usiku mwema, Mungu akutangulie kama alivyomtangulia baba yetu, Ibrahim,” alisema Dickson maneno mengi ili naye aonekane aliijua sana Biblia.
“Amen!” aliitikia Nandy huku akiendelea kupanga vitu. Dickson hakutaka kujali, huyo akaondoka zake huku akionekana kuwa na furaha kuzungumza na msichana huyo kwa siku ya kwanza.
Dickson alikuwa akisubiria kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa lengo la kwenda kusomea utabibu chuoni hapo. Moyo wake ulikuwa na furaha tele, hakuamini kwamba mara baada ya kupambana kwa kipindi kirefu hatimaye alikuwa akitimiza ndoto yake ya kuwa daktari katika maisha yake.
Tangu alipokuwa kidato cha kwanza, alikuwa akimwambia baba yake mara kwa mara kwamba alitamani sana kuwa daktari, alipokuwa akienda hospitalini, aliumia kila alipokuwa akiwaona wagonjwa wakiugua vibaya na wengine kushindwa kabisa kusimama kama zamani.
Moyo wake uliuma na kujiona kuwa na uhitaji mkubwa wa kuwasaidia wagonjwa hao na hivyo kupanga kusomea utabibu kitu ambacho alikuwa njiani kwenda kukamilisha ndoto yake. Matokeo yake ya kidato cha sita yalikuwa vizuri na alipata alama za juu na hivyo kutakiwa kujiunga katika chuo hicho.
Alikuwa akisubiri siku ya kwanza kwenda kujiunga chuoni huko. Kwa kuwa baba yake alikuwa na pesa nyingi, alichokifanya ili kumfanya mwanaye kuwa na furaha, aone kile alichokuwa amekifanya kilikuwa na thamani sana, akamchukua na kwenda naye nchini Ufaransa.
Hiyo haikuwa mara ya kwanza, tangu alipokuwa kidato cha kwanza, alipokuwa akifanya vizuri alichukuliwa na kupelekwa nchi mbalimbali kutembea. Alikuwa na maisha mazuri, alipata alichokitaka na kila siku aliishi maisha matamu kana kwamba alikuwa peponi.
Wakati akiwa nchini Ufaransa, akapewa taarifa kwamba mhubiri wa kimataifa, Benny Hinn angekuwa nchini Tanzania katika mkutano mkubwa wa siku saba.
Hakutaka kubaki nchini Ufaransa, kwa kipindi kirefu alikuwa akisikiliza mahubiri kutoka kwa mchungaji huyo, aliyapenda, alipenda namna alivyokuwa akihubiri na hata kuwaombea watu hivyo kumwambia baba yake kwamba ni lazima wakatishe ziara yao ya kutembelea sehemu mbalimbali jijini Paris na hivyo kurudi Tanzania.
Hilo halikuwa tatizo, baada ya siku mbili wakarudi nchini Tanzania na hivyo kushiriki katika mkutano huo. Hakuwa na maisha ya wokovu lakini alipenda sana kusikiliza mahubiri. Kila alipokuwa akipata nafasi ilikuwa ni lazima kusikiliza mahubiri mbalimbali huku naye akimuomba Mungu kwamba siku moja baadaye aje kuwa mhubiri mkubwa kama alivyokuwa Benny Hinn.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Japokuwa alipenda sana dini na mahubiri lakini pia Dickson alipenda sana wanawake. Kwake, wanawake walikuwa kila kitu, aliwapenda, alipokuwa akiwaona moyo wake ulifarijika mno.
Mpaka kumaliza kidato cha sita, alikuwa amekwishatembea na wanawake wengi. Alipendwa kwa kuwa alitoka katika familia ya kitajiri lakini mbali na utajiri huo, Dickson alikuwa na sura nzuri mno.
Wanawake walimbabaikia na wengi kumuita Trey Songz kwa kuwa tu alifanana na mwanamuziki huyo kutoka nchini Marekani. Kila msichana aliyekuwa akimuona, hakutaka kumpita Dickson pasipo kumsalimia, kwao, kijana huyo aliitetemesha mioyo yao na hivyo kujikuta akilala na wanawake wengi hata wale ambao hakuwa akiwafikiria kabisa.
Siku ya kwanza ya mkutano huo mkubwa wa injili alikwenda katika Viwanja vya Jangwani huku akiendesha gari la thamani aina ya BMW X6 ya bluu. Alipofika sehemu ya kuegesha magari, akalisimamisha na kuteremka.
Watu waliokuwa pembeni wakabaki wakiliangalia gari hilo. Lilikuwa zuri mno, wengi wakatamani kumuona mtu ambaye angeteremka humo kwani wengi walihisi kwamba angeteremka mtu mzima, mwenye kitambi huku mkononi akiwa na saa ya thamani ya Rolex.
Mlango ukafunguliwa na Dickson kuteremka. Alivalia suruali nyeusi, tai nyeusi na shati jeupe huku akiwa na miwani ya macho. Kila mtu aliyemwangalia kijana huyo, alichanganyikiwa, hawakuamini kumuona kijana aliyekuwa na sura nzuri kama alivyokuwa Dickson.
Hakutaka kujali, aliwaona wanawake wengi wakimwangalia lakini akapiga hatua na kuingia katikatika ya umati wa watu na kutulia. Mkononi mwake alikuwa na Biblia yake, hakutaka kuzungumza na mtu yeyote, mahali hapo, alikuja kwa lengo moja la kumuabudu Mungu, hakufikiria kumfuata msichana yeyote yule japokuwa wakati mwingine moyo wake ulikuwa ukipambana vikali kumkumbusha kwamba alikuwa mkutanoni wakati macho yake yalipotua kwa wanawake warembo.
Baada ya dakika kadhaa, mkutano ukaanza rasmi. Aliyatafakari maisha yake, alijua jinsi alivyokuwa akimchukiza Mungu. Maisha yake yaliteswa na dhambi moja tu ya uzinzi ambayo ilimng’ang’ania kupita kawaida.
Alipambana na dhambi nyingine nyingi, alizishinda lakini dhambi hiyo ya uzinzi haikumuacha hata kidogo. Ilimtesa, kila alipotaka kuyabadilisha maisha yake, alianguka mara baada ya kumuona msichana mrembo.
Siku hiyo alifikiria mambo mengi, alimuomba Mungu msamaha, alihitaji kuwa msafi, hakupenda kuishi katika maisha aliyokuwa akiishi kwa sababu tu alihitaji mabadiliko kwa nguvu zote.
Aliyafumba macho yake, alikiinamisha kichwa chake chini huku akiendelea kumtafakari Mungu na maisha aliyokuwa amepitia mpaka kufikia siku hiyo. Wakati akiwa amekiinamisha kichwa chake, akasikia sauti nzuri kutoka jukwaani.
Sauti ile iliposikika tu, moyo wake ukamlipuka, akakaza moyo wake, hakutaka kuuinua uso wake kuangalia kule jukwaani ili kuona ni msichana gani aliyeitoa sauti hiyo na kuanza kuimba nyimbo za kuabudu.
Moyo wake ukashindana na akili yake. Akili ilimwambia auinue uso wake na kuyafumbua macho yake kumwangalia msichana huyo ila moyo wake ilimwambia kwamba hakutakiwa kufanya hivyo, huo ulikuwa ni muda wa kumfikiria Mungu na hivyo alitakiwa kutulia.
“Haiwezekani!” alisema na kuuinua uso wake.
Macho yake akayapeleka jukwaani, alimuona Nandy akiwa amesimama na waimbaji wengine huku akiwa ameshika kinasa sauti akiendelea kuimba. Hakumuomba vizuri kutokana na umbali aliokuwepo.
Alichokifanya Dickson ni kuanza kusogea kule karibu ya jukwaa kwa lengo la kumwangalia msichana huyo. Alipenyapenya kwa watu mpaka kufika mbele kabisa na kuanza kumwangalia nandy.
Mbali na sauti aliyokuwa nayo, Nandy alikuwa msichana mwenye sura nzuri kupita kawaida. Dickson akajisahau kabisa kama alikuwa kwenye mkutano wa injili, akatulia na kumwangalia Nandy vizuri, sura yake ilimdatisha kupita kawaida.
“Ni msichana wa aina gani huyu?” alijiuliza huku akimwangalia Nandy ambaye alikuwa bize kumuimbia Mungu wake.
Hakutaka kuondoka mahali hapo, alibaki akiwa amesimama huku akimwangalia msichana huyo. Kichwa chake kilichanganyikiwa, kwa Nandy, hakuonekana kuwa msichana wa kumchezea na kumuacha, kichwani mwake kulikuwa na taswira ya kumuoa msichana huyo lakini si kutembea naye na kumuacha kama ilivyokuwa kwa wasichana wengine.
Mpaka Nandy anamaliza kuimba na kuteremka jukwaani, Dickson alikuwa akimwangalia. Alitembea kwa mwendo wa taratibu mpaka katika sehemu iliyoonekana kuwa maalumu kwa ajili ya waimbaji na kukaa.
Dickson alishindwa kuvumilia, hakutaka kuona akimkosa msichana huyo, alitokea kumpenda na siku hiyo ya kwanza kumuona alitamani sana kuongea naye japo kidogo.
Mkutano ulipokwisha, akasubiri, hakutaka kuondoka. Wasichana wengi walikuwa wakimwangalia, alikuwa mzuri wa sura na kila mmoja alitamani hata kuzungumza naye lakini Dickson hakutaka kuwa na habari nao, mawazo na akili yake ilikuwa kwa Nandy tu.
Alisubiri mpaka alipomuona msichana huyo yupo peke yake akipanga vitu vizuri. Kigiza kilianza kuingia, hakutaka kubaki alipokuwa, alichokifanya ni kuelekea kule Nandy alipokuwa na kumsalimia.
Kwa jinsi msichana huyo alivyoitikia, ilionyesha kabisa kwamba hakupenda kufuatwa na kusalimiwa. Akazugazuga kwa kumsifia, alipoona haeleweki akaondoka zake kuelekea garini.
“Kesho nitamfuata tena! Mpaka atanizoea tu,” alisema Dickson na kuingia garini.
Akili yake ni kama ilivurugwa, alichanganyikiwa, hakuamini kama kitendo chake cha kwenda katika mkutano ule basi angekutana na msichana mrembo kama alivyokuwa Nandy.
Alipofika nyumbani, akili yake haikuweza kutulia, alikaa chumbani huku akimfikiria Nandy kupita kawaida. Alitamani kumuona msichana huyo kwa mara nyingine, alitamani kusimama mbele yake na kuongea naye tena.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Usiku huo ukawa wa mateso makubwa, hakula chakula chochote zaidi ya kunywa juisi tu na kulala. Asubuhi alipofika, kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kumfikiria Nandy, sauti yake ilimpagawisha kupita kawaida.
Mbele yake akaanza kuona ndoto ya kuwa na msichana huyo, akaona wakiwa kanisani wakifunga ndoa na hatimaye kuwa mke na mume.
Mchana ulipofika, hakutaka kuchelewa, akaondoka na gari lake kuelekea mkutanoni. Bado wanawake waliokuwa wakimuona walishangazwa, sura yake ilimpagawisha kila mwanamke aliyekuwa akimwangalia.
Wengi wakatamani kuwa naye, wengi wakatamani kumfuata na kupiga naye stori lakini mwenzao hakuwa na mawazo nao hata kidogo, moyoni mwake kulikuwa na msichana mmoja tu, Nandy.
Dickson hakutaka kukaa nyuma, siku hiyo alitaka kumuona Nandy vizuri kabisa. Mkutano haukuwa umeanza, wasichana mbalimbali walikuwa wakiandaa viti vya watumishi wa Mungu akiwemo Nandy aliyeonekana kuwa bize hasa.
Alipomuona, mapigo yake ya moyo yakaanza kwenda kasi, siku hiyo Nandy alionekana kuwa mrembo zaidi ya jana, alionekana kuwa mrembo zaidi ya malaika. Hakukubali kuona akisimama tu pasipo kumfuata msichana huyo na kumsalimia kwani usiku uliopita, ndiye mtu pekee aliyekuwa amekisumbua kichwa chake kupita kawaida. Akaanza kumsogelea.
“Bwana Yesu asifiwe,” alimsalimia mara baada ya kumfikia. Nandy akageuka na kumwangalia.
“Amen!”
“Za tangu jana?” aliuliza Dickson, Nandy akajifanya kama kufikiria hiyo jana yake kama aliwahi kukutana na kijana huyo.
“Tangu jana?”
“Ndiyo! Nilikufuata kukusalimia na kumpa Mungu sifa zake kwa kukupa sauti nzuri,” alisema Dickson.
“Ooh! Ni nzuri tu mtumishi wa Mungu!” alisema Nandy na kuendelea na kazi yake.
“Basi sawa. Naona tumerudi kumuabudu Mungu! Leo nitakaa hapa mbele, nataka utukufu wa Mungu utakapoanza kushuka, na mimi niupate wa kwanzakwanza,” alisema Dickson na kutoa tabasamu, maneno yake yakamfanya hata Nandy kutabasamu.
“Haina shida.”
Dickson akakaa katika kiti cha mbele kabisa huku akimwangalia Nandy ambaye alikuwa bize kufanya usafi. Alikwishaisoma akili ya msichana huyo, hakuonekana kuwa kama wasichana ambao aliwahi kutembea nao kipindi cha nyuma, Nandy alionekana msichana mwenye ari ya kumtumikia Mungu na hivyo hata kama angemwambia kwamba alikuwa akimpenda, alitakiwa kutumia lugha fulani ya kibiblia.
Akakaa kwenye kiti na kuchukua Biblia na kuanza kusoma. Yote hayo ilikuwa ni kumfanya Nady amuone kwamba naye alikuwa bize na Mungu wake. Muda mwingine alikuwa akiifunika na kuanza kumuomba Mungu.
Nandy aliyekuwa pembeni alikuwa akimwangalia kijana huyo. Kwake, alimshangaa, Dickson alikuwa na sura nzuri, alishangaa sana kumuona kijana kama huyo akimuabudu Mungu kwani vijana wengi waliokuwa katika umri wake, uzuri wake walikuwa wakiutumia kwa ajili ya kufanya kazi za kishetani tu likiwemo la kutembea na wanawake wengi.
Kwake, Dickson akaonekana kuwa mwanaume mzuri na mwenye utii hata mbele za Mungu. Alifanya kazi yake lakini naye bado kichwa chake kiliendelea kujiuliza kuhusu kijana huyo.
Alipomaliza, akaelekea chini ya jukwaa na kuanza kubadilisha nguo zake na wasichana wengine. Aliishangaa akili yake, haikufikiria kitu kingine zaidi ya kijana yule aliyekuwa amekutana naye kipindi kifupi nyuma.
Alishangaa, alimuomba Mungu amuondolee mawazo juu ya Dickson lakini hayakutoka kabisa. Alimganda akilini mwake, alichukia na wakati mwingine kuuma meno yake kwa hasira lakini Dickson hakuweza kutoka kichwani mwake.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Mungu! Ni nini hiki? Mbona shetani anaamua kunijaribu hivi,” aliuliza Nandy huku akianza kujiimbia nyimbo mbalimbali lakini bado Dickson aliendelea kung’ang’ania kichwani mwake.
Alipomaliza kuvaa, akatoka chini ya jukwaa na kuelekea kule walipokuwa wakikaa waimbaji. Macho yake yalikuwa yakimwangalia Dickson kwa siri, akahisi kabisa moyo wake ukianza kubadilika na upendo fulani wa ajabu ukianza kuingia moyoni mwake.
“Nandy!” aliita rafiki yake, Nandy akashtuka kama mtu aliyekuwa kwenye lindi la mawazo.
“Abeee!”
“Umemsikia mchungaji, anakuita,” alisema rafiki yake huyo.
Mawazo yake hayakuwa mkutanoni hapo, alikuwa akimwangalia Dickson na kujisahau kabisa. Haraka sana akainuka na kuanza kuelekea jukwaani. Watu wote wakaanza kushangilia akiwemo Dickson mwenyewe.
“Naomba tusimame na tutulie mbele za Mungu aliye hai,” alisema Nandy, watu wote wakasimama akiwemo Dickson ambaye macho yake hayakutulia sehemu moja, mara kwa mara alikuwa akimwangalia Nandy, na msichana huyo, mara kwa mara alikuwa akiyapitisha macho yake kwa Dickson.
“Mungu, naomba uniondolee jaribu hili, naomba umtoe kijana huyu akilini mwangu,” aliomba Nandy kimoyomoyo.
“Mungu, huyu ndiye mwanamke sahihi, naomba unipe nafasi ya kuwa naye katika maisha yangu yote,” naye Dickson aliomba.
Kukawa kama na nguvu mbili zikawa zinashindana.
Kila siku wawili hao walikuwa wakikutana mkutanoni na kuzungumza kidogo kisha kuondoka. Moyo wa Dickson bado ulikuwa na uhitaji mkubwa wa kuwa na msichana huyo huku kila siku naye Nandy akimuomba Mungu ili amuondoe Dickson katika kichwa chake.
Siku zikaendelea kukatika mpaka mkutano ulipokwisha. Alichokifanya Dickson ni kumuuliza Nandy kanisa alilokuwa akisali kwa lengo la kwenda huko na kuungana naye mara moja moja.
Hilo halikuwa tatizo, akamwambia na Jumapili iliyofuata alikuwa kanisani humo akimwabudu Mungu. Bado sauti ya Nandy ilikuwa gumzo kubwa, kila mtu alikuwa akishangaa, msichana huyo alikuwa na karama ya uimbaji ambapo kila alipokuwa akisimama na kuimba, kila mtu alihisi kabisa kwamba Mungu alikuwa akimtumia katika karama yake hiyo.
Wakaendelea kuwasiliana kila walipokuwa wakikutana kanisani na hatimaye wawili hao wakawa marafiki wakubwa. Huyo ndiye akawa mvulana wa kwanza kuwa karibu naye kitu ambacho kilimfanya hata yeye mwenyewe kushangaa kwani hakuwahi kuwa karibu na mvulana yeyote zaidi ya huyo.
Baba yake hakuacha kumuonya, kila siku alimwambia mambo mengi kuhusu wanaume, aliwaambia jinsi walivyokuwa wakiwanyanyasa wanawake, alifanya hivyo kwa kuwa hakutaka kumuona binti yake akiingia kwenye uhusiano wa kimapenzi lakini la kushangaza, katika kipindi hicho akili yake haikutaka kabisa kukubaliana na maneno ya baba yake.
Alimuona Dickson kuwa mwanaume wa tofauti na wale ambao kila siku baba yake alikuwa akiwazungumzia, kwake, Dickson alikuwa na sura ya upole kuliko mwanaume yeyote katika ulimwengu huu, hakutaka kuona akimpoteza mwanaume huyo, alihitaji ukaribu huo uendelee pasipo kuambiana kwamba walikuwa wakipendana.
Kila alipokuwa na kijana huyo, moyo wake ulijisikia tofauti kabisa, alipokuwa akikwazwa na kukutana na Dickson, alihisi mabadiliko makubwa moyoni mwake, akahisi tumaini, upendo mkubwa kuliko kitu chochote kile.
Wakati yeye akiendelea kuteseka, Dickson alikuwa akijipanga, hakutaka kumkosa msichana huyo, kwake, Nandy alikuwa kila kitu katika maisha yake na alikuwa tayari kufanya jambo lolote lile lakini si kumkosa.
Akaamua kuachana na wanawake wake na kuamua kubaki na Nandy ambaye mpaka muda huo hakuwa amemwambia ukweli juu ya kilichokuwa kikiendelea moyoni mwake.
Kila alipotaka kumwambia, aliogopa, hakutaka kumpoteza, kwa jinsi msichana huyo alivyokuwa akimuimbia Mungu, jinsi alivyokuwa akisali aliamini kabisa kwamba kama angemwambia kuhusu mambo ya mapenzi basi huo ungeweza kuwa mwisho wa urafiki wao.
“Nifanye nini? Ngoja nimtoe out, nadhani huko nitamwambia kila kitu,” alisema Dickson.
Hakutaka kuchelewa wala kukaa na jambo hilo moyoni mwake, alichokifanya mara baada ya kukutana na Nandy ni kumwambia kuhusu mtoko huo. Nandy aliposikia, akajifanya kushtuka, alitamani sana kutoka mtoko na kijana huyo lakini aliogopa ni kwa jinsi gani angeweza kumwambia.
Hakutaka kuonekana akifurahia na ndiyo maana akajifanya kushtuka kana kwamba kile alichokuwa ameambiwa kilikuwa kimemshtua mno. Hakukubali, alimkumbuka baba yake, maneno yake aliyokuwa akimwambia kuhusu wanaume yakaanza kujirudia kichwani mwake.
“Hapana! Siwezi,” alisema Nandy huku akionekana kuogopa.
“Nandy! Kwani ukitoka na mimi kuna tatizo?”
“Una uhakika kwamba utakuwa ni mtoko tu?” aliuliza Nandy.
“Ndiyo! Ni mtoko tu!”
“Kweli?”
”Naomba uniamini!”
“Hakuna kingine?”
“Wala hakuna!”
”Basi sawa. Kamwambie baba yangu anipe ruhusa,” alisema Nandy maneno yaliyomshtua Dickson.
“Nikamwambie baba yako?”
“Ndiyo!”
“Mmh! Siwezi!”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Basi haitowezekana Dickson. Siwezi kutoka pasipo baba yangu kujua nilipo,” alisema Nandy.
Huo ulikuwa mtihani mzito kwa Dickson, hakutaka kumfuata baba yake Nandy kwani aliamini ni lazima mzee huyo angefikiria vibaya na hivyo kumwambia aachane na binti yake.
Moyo wake ukanyong’onyea, akaamua kuachana na jambo hilo na kufanya mambo mengine. Aliendelea kukutana na Nandy kanisani, wakawa wanazungumza na kuondoka kuelekea majumbani kwao.
Nandy hakuwa na simu, walipokuwa wakiachana, hawakuwa wakiwasiliana mpaka Jumapili inayofuata. Dickson alijaribu mara nyingi kumpa Nandy simu lakini msichana huyo hakuipokea, aliogopa, hakujua baba yake angemfikiria vipi kwani ni lazima angeulizwa maswali mengi kuhusu simu hiyo kitu ambacho kingemfanya kuonekana kuanza uhuni.
Siku ziliendelea kwenda mbele, baada ya mwezi kukatika, Dickson hakutaka kuvumilia, akajipanga kwa lengo la kwenda kuonana na mzee Gwamaka na kumuomba ruhusa ya kumtoa Nandy mtoko.
Alikuwa akihofu moyoni mwake, hakujua kama angekubalika au kukataliwa, akapiga moyo konde na kuelekea nyumbani kwa mzee huyo. Kwa kuwa mara moja moja alikuwa akionekana kanisa, mzee Gwamaka alimzoea kidogo japokuwa ukaribu wake na Nandy ulimtia hofu kidogo.
Alipokaribishwa, akakaa kwenye kochi lililochakaa sebuleni. Akaanza kuiangalia nyumba ya kina Nandy, hakuamini kama kweli msichana aliyekuwa akimpenda, msichana aliyeyatoa maisha yake alikuwa akiishi katika nyumba kama hiyo.
Msichana mzuri kama Nandy hakutakiwa kuishi ndani ya nyumba hiyo, uzuri wake ulistahili kukaa sehemu kama Osterbay au hata Masaki lakini si hapo Kurasini tena kwenye nyumba mbovu kama hiyo.
Nandy aliogopa, mara baada ya kumkaribisha Dickson nyumbani hapo, hakutaka kukaa sebuleni, akaondoka na kuelekea chumbani kwake huku mapigo ya moyo yakimdunda kupita kawaida.
Huko, alikuwa akimuomba Mungu, alitamani mno baba yake akubaliane na Dickson na hatimaye watoke wote mtoko kwani hakukuwa na mtu aliyekuwa naye karibu na aliyempenda kwa moyo wote kama kijana huyo.
Mzee Gwamaka akakaa na Dickson sebuleni, alimwangalia kijana huyo, hakuonekana kujiamini, moyo wake ulijawa hofu na muda mwingi alikuwa akimwangalia mzee huyo huku akionekana kujishtukia kupita kawaida.
“Karibu sana,” alisema mzee Gwamaka.
“Nashukuru sana!” alisema Dickson.
Wakaanza mazungumzo yao. Dickson hakutaka kumwambia mzee Gwamaka kile kilichokuwa kimemleta mahali hapo, kwanza akaanza kuzungumza naye kuhusu mahubiri ya wachungaji mbalimbali, jinsi Mungu alivyokuwa akifanya miujiza kupitia wao.
Walizungumza kuhusu ibada na hata mikutano ya injili iliyokuwa ikiendelea duniani, Dickson alitaka kuonekana kwamba alifuatilia sana mahubiri hivyo kumwambia mzee huyo kuhusu wahubiri wengi na waimbaji duniani kama Kirk Franklin, Don Moen, kundi la Hillsong kitu kilichomfanya kidogo mzee huyo kuridhika.
“Ila pamoja na hayo yote, nimekuja kumuombea ruhusa Nandy,” alisema Dickson huku akimwangalia mzee huyo.
“Ruhusa?”
“Ndiyo!”
“Ruhusa ya nini?”
“Kutakuwa na kisherehe kidogo nyumbani, ninakwenda kuanza chuo, nimefaulu vizuri hivyo wazazi wanataka kunifanyia sherehe,” alisema Dickson.
“Kwa hiyo inahusiana vipi na Nandy?”
“Nataka ahudhurie sherehe hiyo kwa kuwa amekuwa rafiki yangu mkubwa,” alisema Dickson, mzee Gwamaka akashtuka, akamwangalia vizuri kijana huyo.
“Yaani Nandy atoke hapa, aende huko kwenu halafu arudi usiku?” aliuliza mzee huyo.
“Hapana! Itakuwa mwisho saa kumi na mbili!”
“Kijana unamchezea simba sharubu!” alisema mzee huyo.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Mzee! Naomba uniamini na mimi nitautunza uaminifu wangu kwako. Ni ruhusa ya sherehe, hakuna kingine. Mimi si kijana mbaya kama unavyojifikiria, nimekuja kwako kuomba ruhusa kwa kuwa ninajua thamani ya wazazi, nakuahidi mzee wangu hakuna kitu chochote kibaya ambacho kitatokea,” alisema Dickson.
Siku hiyo Dickson alikuwa mnyenyekevu kuliko siku zote alizowahi kuishi katika dunia hii. Alimuomba sana mzee Gwamaka na hatimaye akakubaliana naye kwa ahadi ya kumrudisha saa kumi na mbili kama alivyokuwa amemuahidi na la zaidi, alimwambia kuwa asithubutu kumvua nguo.
“Sitoweza kufanya hivyo mzee wangu!”
“Basi ruksa umepata.”
Moyo wa Dickson ukawa na furaha tele, hakuamini kama angekubaliwa na mzee huyo kumtoa mtoko Nandy. Hakukuwa na sherehe yoyote ile bali kitu alichokitaka ni kuwa karibu na msichana huyo tu.
Alipoondoka, Nandy ndiye aliyemsindikiza, njiani, alimwambia jinsi baba yake alivyokubali kutoka naye. Nandy akafurahi kwani hata kule chumbani alipokuwa, alimuomba Mungu azungumze na baba yake na hatimaye kutoka na mvulana huyo.
Siku iliyofuata, wawili hao walikuwa katika bwawa la kuogelea katika Hoteli ya Cassanova iliyokuwa Mbezi Beach jijini Dar es Salaam. Kwa Nandy, kila kitu alichokuwa akikiona katika hoteli hiyo alikuwa akishangaa, hakuamini kama kulikuwa na watu walikuwa wakila starehe kama ilivyokuwa kwa watu aliokutana nao ndani ya eneo la hoteli hiyo.
Dickson hakutaka kukaa mbali na Nandy, ilikuwa ni kama alihisi kuwa angeibiwa msichana huyo. Muda wote alikuwa pamoja naye, alipokwenda kwenye bwawa la kuogelea, alihakikisha anakuwa naye na hata alipotoka, alikaa naye sehemu na kuzungumza naye.
Mpaka muda huo hakuwa ameufumbua mdomo wake kumwambia jinsi alivyojisikia moyoni mwake, alikuwa akifikiria ni kwa jinsi gani angeweza kumwambia msichana huyo na hatimaye akubaliane naye na kuingia katika uhusiano wa kimapenzi.
Waliendelea kula raha mpaka majira ya saa kumi na moja ambapo wakatoka na kuingia ndani ya gari. Humo, bado Dickson alikuwa akijiuliza kama muda huo ulikuwa sahihi kumwambia ukweli au raha.
Kwa jinsi msichana huyo alivyokuwa akimuimbia Mungu na kumuabudu, moyoni mwake alihisi kabisa kwamba angemkatalia kile alichokuwa akikitaka na mwisho wa siku kuingia katika ugomvi mzito.
Akanyamaza siku hiyo, alimrudisha kwao na kurudi nyumbani. Hakuzuiliwa kufika nyumbani hapo, siku iliyofuata akarudi na kuanza kuzungumza naye.
Mzee Gwamaka aliridhia kila kitu, japokuwa alimwambia binti yake kuhusu wanaume lakini kwa Dickson ilionekana kugonga mwamba. Kijana huyo alikuwa akimfuata Nandy kwa staili ambayo hata yeye mwenyewe hakuwahi kuifikiria, alimfuata kwa unyenyekevu huku muda mwingi alipokuwa akiongea alilitaja jina la Yesu, yote hayo ilikuwa ni kuendana na mazingira ya msichana huyo aliyokuwa akiishi.
“Nandy! Kuna jambo moja muhimu sana ningependa kukwambia,” alisema Dickson huku akimwangalia Nandy usoni, uzuri wake ulizidi kuonekana.
“Jambo gani?” aliuliza.
Dickson akanyamaza kwanza. Hakujua ni kwa jinsi gani angechukuliwa mara baada ya kumwambia Nandy ukweli, akawa kama mtu aliyekuwa akijifikiria kitu fulani, alipoona kuwa Nandy alinyamaza kumsikiliza, akapiga moyo konde.
“Ninakupenda Nandy,” alisema Dickson huku kwa mbali akionekana kuweweseka.
“Unanipenda mimi?” aliuliza Nandy huku akijifanya kushtushwa, akakunja ndita kidogo, hiyo ikamuogopesha Dickson.
“No! Simaanishi unachokifikiria! Namaanisha upendo wa Agape, kama Yesu aliowapenda wanafunzi wake,” alisema Dickson, alibadilika haraka sana kwani alihisi kwamba Nandy alikuwa amechukizwa na kile alichomwambia.
“Kweli?”
“Ndiyo Nandy!”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Si upendo kama ule wa Romeo aliompenda Juliet?” aliuliza Nandy.
“Nandy! Unajua...daah! Yaani sijui niseme nini...”
“Sema chochote kile, nakusikiliza.”
“Nakupenda sana.”
“Mara ya pili hiyo unaniambia!”
“Najua! Ila naomba uniamini, ninahitaji kukuoa!”
“Kunioa mimi?”
“Ndiyo! Nahitaji kukuoa wewe.”
“Kwa hiyo huo ni upendo wa Yesu aliowapenda wanafunzi wake au mwingine?”
“Nadhani huu ni wa Romeo aliompenda Juliet,” alisema Dickson na wote kuanza kucheka.
Siku hiyo wawili hao wakaingia katika uhusiano wa kimapenzi. Moyo wa Dickson ulikuwa na furaha tele, kwake, kitendo cha kuwa na msichana huyo alihisi maisha yake yakianza kukamilika tofauti na jinsi alivyokuwa kipindi cha nyuma.
Mapenzi yao yakaanza kuwa siri kubwa, waliogopa watu kufahamu kilichokuwa kikiendelea kwa kuwa kanisani msichana huyo alikuwa akiheshimika mno.
Walikuwa pamoja, na mara baada ya kuzoeana sana, ikambidi Dickson amuombe ruhusa mzee Gwamaka kwa ajili ya kumnunulia simu msichana huyo.
Mzee Gwamaka alikataa, alizijua simu, zilikuwa na matatizo mengi, hakutaka binti yake aharibiwe na ulimwengu wa teknolojia, alimwambia Dickson kwamba jambo hilo halikuwezekana, hakutakiwa kumnunulia simu Nandy.
Waliishi hivyohivyo mpaka matokeo ya kidato cha nne yalipotoka, Nandy alifaulu vizuri na hatimaye kujiunga na Shule ya Sekondari ya Benjamini jijini Dar es Salaam huku Dickson akianza masomo yake katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam akichukua utabibu.
Shuleni, Nandy alikuwa mwiba mkali kwa wasichana waliojiona keki shuleni hapo. Alikuwa msichana mwenye uzuri wa ajabu ambapo kila mwanaume aliyekuwa akimwangalia, alimpenda, gumzo kubwa kwa kila mtu shuleni hapo ulikuwa ni uzri wa Nandy tu.
Wanaume hawakutaka kuwa na subira, walichokifanya ni kuanza kumfuatilia kwa lengo la kumtia mikononi mwao lakini kwa Nandy, lilikuwa jambo gumu kumkubali mwanaume yeyote yule kimapenzi.
“Jamani yule demu mkali mno, ila naye mgumu kama nondo,” alisema jamaa mmoja huku akimwangalia Nandy.
“Watu wamemfuata lakini wapi. Ana sauti nzuri ya kumtoa nyoka pangoni lakini ni mgumu sana, hivi kuna mtu anaweza kumpata yule?” aliuliza jamaa mwingine.
“Sidhani! Ila tupambaneni, mwenzenu mimi huwa siamini kama kuna demu mgumu, watu wanazaa na malkia anayewaongoza ndiyo sembuse yeye! Tuweni bize naye tu,” alisema jamaa mwingine.
Miongoni mwa wasichana aliowahi kutembea nao Dickson alikuwa Linda Fabian. Huyu alikuwa msichana mrembo aliyekuwa akisomea sheria nchini Uingereza katika Chuo Kikuu cha Oxford.
Linda alikuwa miongoni mwa wasichana warembo ambao walitoka kimapenzi na Dickson. Katika kipindi ambacho wawili hao walikuwa pamoja walipeana ahadi nyingi za kuwa pamoja mpaka kuja kuoana.
Kwa mapenzi motomoto ambayo Linda alipewa na Dickson, moyo wake ulichanganyikiwa na kuona kuwa katika dunia nzima hakukuwa na mwanamke mzuri kama alivyokuwa.
Dickson hakuwa na mapenzi naye, alimuonyeshea kwa kuwa aligundua kwamba msichana huyo alichanganyikiwa kwake. Walikuwa pamoja, walifanya mambo mengi pamoja na hata wakati mwingine kwenda kutembea nje ya nchi.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Walipendana, kila mtu aliyekuwa akiwaangalia aliona kabisa kwamba wawili hao wangekuwa pamoja siku moja na kutengeneza familia pamoja. Linda alichanganyikiwa, akawaambia wazazi wake kuhusu Dickson kitu ambacho kwa kijana huyo hakupenda kabisa kuona kikitokea.
Penzi likawa wazi lakini bado Dickson alikuwa mtu wa wanawake, hakuwahi kupenda kwa moyo wa dhati, hakuwahi kumwambia mwanamke kwamba alikuwa akimpenda kutoka moyoni mwake.
Kwa uzuri wa sura aliokuwanao aliamini kwamba wanawake walimpenda wao wenyewe na kutaka kulala naye. Hakuwahi kutongoza, wanawake wote aliowahi kulala nao katika maisha yake akiwemo Linda walikuwa wakimtongoza yeye.
Alitembea na wanawake wengi, watoto wa kishua wenzake lakini mtu aliyekuwa karibu naye zaidi alikuwa Linda tu ambaye alimganda kama ruba.
Siku zikaendelea kukatika mpaka siku ambayo Linda alihisi hali ya tofauti mwilini mwake na alipokwenda kupima, akagundua kwamba alikuwa na mimba. Hilo lilimtisha,hakutaka kufanya siri, akamwambia Dickson ambaye aliruka kama ndege na kumwambia kwamba mimba haikuwa yake.
“Kumbe ni ya nani?” aliuliza Linda, kwa jinsi Dickson alivyokuwa amebadilika, hakuamini macho yake.
“Sijajua! Labda ya mwingine, huwezi kujua,” alisema Dickson.
“Kwa hiyo nilitembea na mwanaume mwingine?”
“Kwani mimba mpaka utembee na mwanaume, hujawahi kusikia mimba inayopatikana kwenye bwawa la kuogelea? Linda, mara ya mwisho nilikuuliza kama upo kwenye siku za hatari, unakumbuka ulinijibu nini?” aliuliza Dickson.
“Kwamba sikuwa kwenye siku za hatari!”
“Sasa mimba imeingiaje?”
“Dickson, sikujua kama mzunguko wangu ulibadilika,” alisema Linda.
Dickson hakutaka kukubali, hakutaka kuitwa baba kwa msichana ambaye hakuwa na ndoto zake. Wakaingia kwenye mtafaruku wa kimapenzi na baada ya kuona kuwa mwanaume huyo ameweka vikwazo, akaamua kuitoa mimba hiyo.
Moyo wa Linda ulimuuma lakini hakuwa na jinsi. Uhusiano uliendelea lakini Dickson hakuwa mtu wa kueleweka tena, wakawa kama marafiki, hakuwa mtu wa kumpigia simu Linda na kumjulia hali, kwake, hakutaka kabisa kuwa na mapenzi na msichana huyo.
Maisha yaliendelea kama kawaida mpaka Linda alipoamua kuondoka na kuelekea nchini Uingereza kusoma. Kwake, Dickson alikuwa kila kitu, hakutaka kuona akimpoteza mwanaume huyo, japokuwa aliona kabisa hapendwi lakini moyo wake uliamini kitu kimoja tu kwamba kuna siku angekuja kuwa na mwanaume huyo.
Aliendelea kusoma huku akiweka mipango yake ya muda mrefu, kwa kuwa alipokuwa akiingia mwaka wa tatu chuoni ndiyo kwanza Dickson alikuwa akianza mwaka wa kwanza jijini Dar, akaamua kutulia na kuisubiria siku ambayo aliamini kwamba mwanaume huyo angeukunjua moyo wake na kuwa naye tena.
Hakuacha kuwasiliana naye, alihakikisha anachati naye katika mitandao ya kijamii na hata kumpigia simu. Dickson hakumpenda Linda, alijitahidi kumnyamazia lakini msichana huyo hakukoma, bado imani yake ilimwambia kwamba kuna siku angekuwa na kijana huyo.
“Nimekukumbuka sana Dickson,” alisema Linda kwenye simu.
“Nashukuru sana!”
“Hivi bado unanipenda?”
“Nani? Mimi? Mbona umeniuliza hivyo?”
“Kwa kuwa nataka kujua!”
“Jamani! Sidhani kama unatakiwa kuniuliza hilo swali kwa kuwa ukweli unaujua!”
“Upi?”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Linda! Hebu niambie, masomo yanasemaje huko?”
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment