IMEANDIKWA NA : MARYAM SAID AMOUR
*********************************************************************************
Sehemu Ya Kwanza (1)
Niliyagandisha macho yangu juu ya mwili wa mke wangu ambaye
alikuwa akiondoa vyombo juu ya meza baada ya kumaliza kupata
kifungua kinywa. Moyoni nilijisifia kwa kupata mwanamke mzuri wa umbo na tabia kitu ambacho ni nadra katika dunia ya leo, ukupata mwanamke mzuri wa sura basi tabia yake mbaya.
Lakini si kwa mke wangu Minza mtoto wa Kisukuma naweza sema
nimelamba dume la mchezo. Kwa kweli lazima nijisifie kwa chaguo la macho yangu lililosababisha kuwa kipenzi cha moyo
wangu.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Nilimpenda akanipenda naweza sema mimi ndiye mwanaume wake wa kwanza kumuingiza kwenye anga ya mapenzi. Japo si mimi niliyemtoa usichana wake lakini mambo mengi katika mapenzi alikuwa hayajui alijifunzia kwangu.
Kila siku machoni mwangu nilimuona kiumbe kipya, kila nilipomuona moyo alipasuka na kwenda kwa kasi hata sijui ni kwa nini.
Wengi huamini wanawake wazuri ni weupe lakini ni tofauti na moyo wangu. Minza alikuwa binti mweusi tii, weusi wa kitusi unaong'ara. Hakuwa mrefu sana ila alikuwa na kila kitu nilichotakiwa kuwanacho mwanamke mlimbwende.
Macho yake yalikuwa yamevimba kidogo kama ametoka singizini, mboni zake hazikuwa nyeupe bali za njano ya mbali, meno yake ya shaba wengi huuta meno ya kuungua.
Macho yake ukimuangalia kama amekula kingu manga kila akiniangalia kama ananiita. Kifua chake kilichosheheneza matiti yaliyojaa kama ndimu maji yaliyokipendezesha kifua chake. Nyuma, mmh! Hakuwa haba mwenyezi mungu alimpendelea. Kwa kweli Minza alipendeza kila idara alikuwa hachoshi machoni hata kama huna kitu ukimuona Minza utajiona tajiri.
Nilirudisha kumbukumbu nyuma ya miaka miwili toka nionane na Minza. Nakumbuka vizuri ilikuwa jumapili, siku ambayo huwa siendi popote hupumzika nyumbani baada ya mihangaiko ya wiki nzima.
Nikiwa natoka zangu gengeni kununua vitafunwa vya chai nilikutana na msichana mmoja ambaye alikuwa mgeni machoni mwangu. Kule kumuona tu moyo ulinilipuka na kujiuliza ni nini kilicho ufanya ushtuke vile, nilimuangalia yule binti kwa chati hakuniona alikuwa akichota maji.
Nilijiuliza yule binti atakuwa anaishi wapi, nilijikuta naahilisha safari yangu na kumfuatilia nyuma nyuma hadi nyumba aliyoingia kwenye nyumba iliyokuwa jirani yangu. Nilijisemea kumbe alikuwa hakai mbali na sehemu niliyo kuwa ninaishi.
Niligundua yule msichana aliye kuwa kwenye mavazi machakavu ni mzuri sana ila alichokosa ni mavazi. Nilijiuliza huenda ni mgeni maana sikuwahi kumuona siku za nyuma. Niliachana na yule msichana na kurudi nyumbani kwenda
kupata kifungua kinywa.
Baada ya kifungua kinywa niliendelea na shughuli ndogondogo za usafi kama ujuavyo wasela jumapili ndiyo siku yetu ya usafi. Ikipita basi usubiri jumapili nyingine. Kama kawaida yangu baada ya usafi nilikwenda sokoni kununua
kitoweo kwa ajiri ya mboga ya mchana mara zote niwapo nyumbani nilipenda kula chakula cha kujipikia mwenyewe.
Baada ya manunuzi nikiwa najiandaa kurudi nyumbani moyo ulinipasuka baada ya kumuona tena yule msichana wa asubuhi akiwa ameshikia kikapu kilichokuwa na mahitaji muhimu ya chakula cha mchana.
Japo safari hii alikuwa amebadili nguo, lakini bado zilikuwa za hadhi ya chini. Gauni alilovaa lilikuwa linamikunjo, lilionekana limetolewa kwenye mfuko wa Rambo na kuvaliwa. Yule msichana alinipita na kuelekea njia ya nyumbani niliangalia kama yupo na mtu aliyefuatana naye, lakini niligundua yupo peke yake.
Nilichepua mwendo ili nijaribu bahati yangu, kabla ya kumfikia nijiuliza maswali na kujijibu mwenyewe. Nilipomkaribia nilimsabahi.
"Hujambo binti."
"Sijambo, shikamoo kaka," alinijibu kwa lugha yenye rafudhi ya Kisukuma huku akipiga magoti kuonesha heshima.
"Marahaba, wewe ni mgeni?"
"Ndiyo."
"Umetokea wapi?"
"Uzinza."
"Hapa una muda gani?"
"Kama mwezi sasa."
"Oooh vizuri, unaitwa nani?"
"Minza, kwani we nani? Mbona unanihoji wewe ni sungusungu?”
(askari wa jadi)CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Hapana mimi ni raia mwema," nilimjibu kwa sauti ya upole.
"Ulikuwa unataka nini?"
"Samahani Minza, leo ni mara yangu ya kwanza kukuona lakini
nimetokea kukupenda na kutaka uwe mke wangu."
"Mmh! Haiwezekani."
"Kwa nini?"
"Mimi nimekuja mjini kufanya kazi sikufuata hayo."
"Lazima uelewe, nawe unataka kuwa na familia yako hivyo naomba ukubali uwe mke wangu ili shughuli kama hizi uzifanye ukiwa kwako."
"Na mama nitamwambiaje?" Majibu ya Minza yalinionesha bado ushamba haujamtoka.
"Umwambieje kuhusu nini?"
"Yeye alinifuata kijijini nije nifanye kazi sasa asikie eti nataka kuolewa atakubali?"
"Maisha yako Minza yapo mikononi mwako, yeye anataka kazi bila
kujali maisha yako, hata kipato ni kidogo kwani anakulipa kiasi
gani?"
"Elfu ishirini."
"Ooh maskini! Ni ndogo sana, Minza umesoma?"
"Ndiyo."
"Mpaka darasa la ngapi?"
"La saba."
"Ooh! Minza, yaani umesoma mpaka la saba bado unaona kazi za
ndani ni bora kuliko kuwa na nyumba yako ambayo hata wazazi
wako watakuja kukutembelea mtoto wao bila wasiwasi. Hivi
unafikiri hata ndugu zako wakija utawapeleka wapi, kingine hata
ukivuja kitu unakatwa mshahara au kufokewa hata kupigwa. Lakini
ukivunja kwako nani wa kukugombeza?"
"Mmh! Kweli, tena jana nimevunja sahani mbili na glasi tatu
nimeambiwa mshahara wa mwezi huu siupati."
"Unaona sasa Minza, kijua ni hiki usipo uanika sasa, utautwanga mbichi
kubali uwe mke wangu. Tena sitaki kukuchezea nipeleke kwa wazazi
wako ili nijitambulishe na kulipa mahari kisha nipate idhini yao ili
uwe uke wangu wa halali."
"Mimi nimekubali sijui mama kama atakubali."
"Yeye hana mamlaka ya maisha yako, la muhimu twende kwa wazazi wako kama nilivyo kueleza."
"Sawa, sasa tutakwenda lini?"
"Jumapili ijayo."
“Hakuna tatizo, nitamwambia mama”
“Hapana, ukimwambia anaweza kukuwekea kauzibe.”
“Sawa siwezi kumwambia.”
Niliagana na Minza nikiwa na furaha tele moyoni, ilionyesha hakukuwa na mwanaume yeyote aliyewahi kuongea naye mambo ya mapenzi. Nilijiona mtu mwenye bahati kwa kupata nguo nzuri kwenye mitumba kwa bei rahisi ambayo haijavaliwa sana.
***
Jumapili niliondoka na Minza hadi kwao Uzinza kwa kuvuka ziwa victoria. Nilipofika Uzinza nilikutana na wazazi wake ambao nao hawakuwa na
pingamizi. Nilimuacha Minza kwao wakifanya mipango ya harusi
mimi nilirudi hadi Nyumbani kuwataarifu ndugu na jamaa. Baada ya wiki mbili nilimuoa Minza na kuwa mke wangu wa ndoa.
Baada ya ndoa na kumtengeneza kwa mavazi na mapambo, kila aliye muona Minza aliniuliza dhahabu ile nimeichimbua wapi. Niliwajibu kuwa mbona mjini zimejaa tatizo wengi huwapenda wanawake aliojipamba kumbe wapo wazuri sana kushinda hao wanaoongezwa uzuri kwa kukomboa sura zao. Siku zote muhogo mtamu ni ule uliochimbwa na kuliwa. Siyo uliosafiri mjini na kuchanganywa na vitu vingi vinavyosababisha kupoteza uharisi wake.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
*********
Hapo ndipo nilipo yaanza maisha yangu kama mume wa Minza ambaye ndani ya miezi miwili alishika ujauzito. Baada ya miezi tisa alijifungua salama mtoto wa kike aliyemwita jina la mama yake Shikilwa. Leo ni mwaka wa pili bado nikimuangalia Minza hamu hainiishi, utafikiri nimemuona ndiyo siku ya kwanza kumuona, kila siku amekuwa mpya machoni mwangu.
Sababu kubwa za kumpenda mke wangu Minza ilitokana na mapenzi na
uaminifu wake kwangu, nami nilikuwa nikijifunza mambo mengi kama
ukarimu. Japo nami nikuwa mkarimu lakini kwa Minza nilikuwa mwanafunzi.
Minza alikuwa mpole mcheshi mwenye huruma kwa watu wote alikuwa achagui wala habagui.
Tukiwa tumemaliza kupata kifungua kinywa wakati huo mtoto
wetu Shikilwa alikuwa na mwaka mmoja, ni juzi tu tumesherehekea
siku yake ya kuzaliwa kutimiza mwaka mmoja.
Kama nilivyokwisha kueleza mwanzo kuwa kila muda nilimuona
mke wangu mpya, hata sijui ni nini. Nilikuwa nipo tayari kuitwa limbukeni kwa ajili ya kumpenda mke wangu. Niligundua kuwa Minza ni chaguo la moyo wangu burudisho la nafsi yangu.
Kila nilipomuona nilihisi kupata farijiko hata kama una maudhi ya wanadamu au uchovu wa mwili na fikra. Nikiwa bado nausanifu mwili wa mke wangu Minza, pamoja na kuwa na mtoto mmoja lakini ukiambiwa hajazaa utakubali.
Hata alipogeuka alikutana na macho yangu, kitu kilichomfanya aachie tabasamu pana lililoufanya moyo wangu uchanue na kuufanya mwili uhisi baridi moyoni.
"Baba Shikilwa mbona unaniangalia sana," aliniuliza mke wangu.
"Aaah! We acha tu."
"Kuna nini mume wangu, maana si leo mara nyingi hukuona
ukiniangalia na kuachia tabasamu huku ukitingisha kichwa?"
"Mke wangu wewe mrembo."
"Asante mume wangu kwa kunisifia pia nawe u mwanaume mzuri sana."
"Asante mke wangu, lazima kwanza nimsifu Muumba kwa umahiri
alioufanya kukuumba kwa utulivu mkubwa, pili wazazi wako kwa
malezi mazuri waliokupa, tatu wewe mwenyewe kwa kuwa mke
mwema mwenye upole na huruma."
"Asante mume wangu, nami sina budi kumshukuru Mungu kwa
kunipa mume mwema, kwani siku zote mume au mke mwema
hupewa na Mungu. Pili wazazi wako kwa kukufunza tabia njema
yenye upendo usiochanganywa na chembe wa chuki na
hasira...Najiona ni mmoja wa wanawake aliyependelewa na
Mungu. Mwisho kwako wewe mume wangu kwa kunifanya mimi
kuwa chaguo lako...Asante sana mume wang......"
Mke wangu alikatwa kauli na mlio wa simu yake ya mkononi iliyokuwa pembeni yangu. Sikupokea haraka niliitazama wakati huo mke wangu alikuwa akimalizia kupanga vyombo kabatini.
“Nani?” Aliniuliza.
“Ni namba tu.”
“Pokea,” kutokana na kuaminiana hakuna aliyekuwa akiificha simu ya mwenzake hata kupokeleana bila kutiliana wasiwasi. Nilibofya cha pokelea na kuweka simu sikio na kuongea:
"Haloo, nani mwenzangu?"
"Samahani naomba kuongea na Minza mama Shikilwa ."
Ilikuwa sauti ya kike, nilimpa mke wangu bila kuhoji ni nani
aliyepiga aliipokea simu na kuongea:
"Haloo nani mwenzangu?...Eeeh ndiyo mimi...Etiii… Aaah…”
Hakumalizia kuongea nilishangaa kumuona mke wangu akidondoka
chini na simu ikimponyoka.
Nilishtuka na kujiuliza mke wangu amepata taarifa gani ambayo
zimemshtua kiasi hicho. Nilimuwahi lakini nilikuwa nimeisha
chelewa alikuwa ameishaanguka chini na kupoteza fahamu. Nilikimbia haraka kwenye simu ili nihoji ni habari gani alizopewa kipenzi mke wangu ziliyo mweka kwenye hali ile.
Mkosi mwingine simu ilipoanguka na kujipigiza chini ilipasuka kila
kitu kilisambaa. Niliachana na simu na kurudi kumpa msaada mke
wangu wakati huo mwanetu Shikilwa naye alikuwa ameamka na
kuanza kulia.
Niliona kweli mitihani ya Mungu inapokuijia huwa aiangalii upo kwenye mazingira gani. Nilimwacha Shikilwa alie ili nimshughulikie mama yake. Nilimpa huduma ya kwanza ambayo nilifanikiwa kumrudishia fahamu. Nilipepea mpaka aliporudi kwenye hali ya kawaida, cha kwanza alimtaka mtoto wake aliyekuwa bado analia, nilimpeleketea alimpakata na kuanza kumnyonyesha huku akiendelea kububujikwa machozi.
Nilishindwa kumuuliza nilimwacha kwanza amnyonyeshe mtotto,
lakini moyoni nilikuwa na swali zito nikijiuliza mke wangu
amepata habari gani zilizo muweka kwenye hali ile. Mawazoni
nilifikiria huenda ni habari za msiba na kama ni msiba atakuwa amekufa nani?
Nilimwacha amnyoshe mtoto mpaka aliposhiba na usingizi kumpitia, alimlaza na kuanza kulia tena safari hii kwa sauti kitu kilichonifanya nihoji kwa sauti ya upole:
"Mke wangu kuna tatizo gani?"
"Mama amekufa."CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Ha! Unasema?" Japo nilikuwa nimemsikia lakini sikumuelewa.
"Lazima mama atakuwa amekufa tu."
"Mbona sikuelewi amekufa, atakuwa amekufa una maana gani?"
"Najua wananidanganya mama atakuwa amekufa tu."
"Atakuwa amekufa kivipi kwani taarifa inasemaje?"
"Eti mama ni mgonjwa sana ninatakiwa haraka, kama sio amekufa ni
nini? Najua wamenificha mama atakuwa amekwisha kufa tu," kufikia
hapo mke wangu alianza kulia kwa sauti ya juu kidogo, niliingia kazi ya kumbembeleza.
"Nyamaza mke wangu kwani ulikuwa una taarifa zozote kuhusu
ugonjwa wa mama?"
"Nashangaa yaani kumbe mama anaumwa siku zote hizo wasinipe
habari mpaka amefariki ndio wananijulisha?" Mke wangu alisema kwa uchungu.
"Nani kakwambia mama amekufa...Usimchulie mama badala ya
kumuombea kwa Mungu apone wewe unamuua kabisa."
"Sio hivyo mume wangu, moyo umekuwa na wasiwasi huenda wamenidanganya."
"Nina imani hawajakudanganya mama ni mgonjwa la muhimu
uondoke sasa hivi ukamuone mama pia nitakupa pesa za kumsaidia
kwenye matibabu la muhimu ni kumuombea mzazi wetu apate
nafuu ya ugonjwa na apone upesi."
"Sawa mume wangu wacha niondoke asubuhi hii niwahi nikamuone
mama si tutakwenda wote?"
"Hapana wewe tangulia ila mimi nitakuja kesho, la muhimu nijulishe
mgonjwa ana hali gani kama kuna tatizo zaidi nijulishe ili tufanye
mpango wa kumleta hospitali kubwa."
"Sawa mume wangu hata sina haja ya kuoga tena wacha nijiandae
niondoke asubuhi hii."
Minza aliingia ndani kujiandaa kwa ajili ya safari ya ghafla na
kuniacha nikiwa na mawazo tele juu ya ujumbe uliomfikia mke
wangu una ukweli gain. Mmh! Kama ni kweli mawazo ya mke
wangu ni sawa hakuna mgonjwa bali ni kifo nilijua patakuwa
hapatoshi.
Jinsi mke wangu alivyokuwa akimpenda mama yake sikujua
itakuwaje. Nikiwa katika ya lindi la mawazo nilikatishwa na sauti ya Minza:
"Baba Shikilwa hubadili nguo utanisindikiza hiyohiyo bukta yako?"
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment