Search This Blog

Sunday, July 10, 2022

KWA NINI MIMI? - 5

 





    Simulizi : Kwa Nini Mimi?

    Sehemu Ya Tano (5)



    ILIPOISHIA>>>



    Tulivyofika nyumbani nikamuambia Thomas sihitaji kukaa pale nyumbani.Bali nahitaji kwenda mbali kwaajili ya kupumzika.Thomas akaniambia nichague sehemu ya kwenda atanipeleka bila ya hiyana, nikachagua nyumbani kwao Thomas.

    Thomas akashangaa lakini ikabidi akubali kunipeleka kwao kwa vile alijua nilikuwa nimekasirika.Nikamuomba namba ya wifi yangu Eve niwasiliane naye, akaniambia hana.Nikamuambia fanya kila njia ili Eve ajue kama naenda nyumbani. Akaniambia kuna jirani yao atampa taarifa,yeye ndiye ataenda nyumbani kutoa taarifa.

    Baada ya siku mbili tulifunga safari na kwenda Kilimanjaro nyumbani kwa akina Thomas.





    ENDELEA>>>>>





    Tuliondoka Dar kwa kutumia usafiri binafsi, na Thomas ndiye aliyekuwa dereva na muongozaji mkuu wa njia kwa vile alikuwa ndiye anayekujua kwao.Safari ilikuwa ndefu na ya kuchosha, tulitembea kwa muda wa masaa nane barabarani.Thomas alikuwa ananieleza yeye ni mwenyeji wa Uru Kishumundu.

    Tulivyofika Moshi mjini nilimshauri Thomas tupitie sokoni kwa ajili ya kununua mahitaji mbalimbali ya nyumbani.Tulipitia sokoni tukanunua mikungu ya ndizi miwili,mchele,unga,sukari na vitu vingine vidogo vidogo kwaajili ya matumizi ya nyumbani

    ******

    Baada ya nusu saa tulifika nyumbani kwao Thomas.Nilikuta nyumba moja kubwa na nzuri, ilikuwa imezungushiwa wigo na pembeni yake kulikuwa na nyumba kuu kuu yaani ile iliyochakaa na ina uzamani ndani yake.Nikamuuliza Thomas,CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    "Kumbe kwenu ni kuzuri hivi?"Thomas akajibu,

    "Ndiyo. Hapa ndipo nyumbani kwetu mama". Niliwaona ndugu zake Thomas ambao walikuwa wamekusanyika kwa ajili ya kumpokea,huku wengine wakawa wanamshangaa huku wakimuambia kwamba amebadilika sana.

    Nakumbuka tulivyofika pale nyumbani ilikuwa ni mida ya saa kumi jioni.Wifi Eve alifurahi sana, alinikumbatia na kunikaribisa ndani. Nikamuuliza,

    "Mama yuko wapi?"akanijibu,

    "Tulia wifi una haraka ya nini karibu anakuja utamuona".Basi tulikaribishwa ndani.

    Siku hiyo walipika ndizi na nyama, tukakaribishwa na baada ya hapo tukaonyeshwa chumba cha kulala. Nikaoga na kubadilisha nguo zangu,sikupenda kupumzika,nikatoka nje na nikawa naongea na wifi Eve.Thomas alikuwa amelala,wakati muda huo ilikuwa ni saa kumi na moja.Ghafla nikamuona mama mmoja akiingia kwenye geti akiwa amebeba mfuko wa sabuni huku akiongea peke yake.Alitupita pale tulipokuwa tumekaa huku akiwa ameshika brashi mkononi.Nilipomsalimia aliniangalia kisha akanichekea na akaendelea na safari yake ambayo iliishia kwenye ile nyumba ndogo kuu kuu, akaingia humo ndani.Nikamuuliza wifi Eve,

    "Huyo mama ni nani?".Wifi Eve akaniambia

    "Huyo mama, ndiye mama yetu mimi na Thomas".Nilipigwa na mshangao na ikabidi nimuulize Eve.

    “ Wewe upo hapa, unaridhika na hali yake jinsi alivyo? Kwanini humpeleki hospitali?"Wifi Eve akaniambia,

    "Hospitali imeshindikana, tumemuachia MUNGU".Kwa kweli pale nilipokaa nilitoa machozi.Nililia sana nikawa namwambia wifi Eve lazima nijue mama ana matatizo gani.Nikanyanyuka pale nilipokuwa nimekaa, nikamfuatilia mpaka kwenye ile nyumba,nikawa nasikiliza anachofanya.Alikuwa anajiimbia mwenyewe nyimbo zisizoeleweka na alikuwa amechukua maji baridi yasiyochemshwa ameyaweka majani ya chai na kuyanywa,huku akiwa anacheka kwa nguvu na kwa sauti kubwa na y juua .

    Ndugu msomaji, nilikaa chini huku nikilia kwa uchungu sana baada ya tukio lile.Wifi Eve akanifuata na kuninyanyua,nami nilinyanyuka pale nilipokaa bila pingamizi.Kwa haraka sana nikakimbia mpaka chumbani.Nilimkuta Thomas anakoroma,nilimtingisha kwa nguvu huku nikimuita

    "Thomas,Thomas tafadhali hamka mama ana hali mbaya tumpeleke hospitali".Thomas aliamka akaniangalia kwa macho makali huku akiwa amekasirika akaniambia,

    "Anne acha kumfuatilia mama yangu, wewe hauna uchungu kama ninavyojisikia mimi.Ugonjwa wake hautibiki hospitali tulishakwenda".Nikamuuliza,

    "Ulihangaika sehemu nyingine lakini kwenye maombi ulienda?"Thomas akanijibu,

    "Nimeshakuambia, muache mama yangu kama alivyo usimguse na wala usijitie kiherehere wa kumtibu".Thomas akarudi kulala kana kwamba suala lile halijamgusa.

    Nililia sana, hata usiku sikupata usingizi mzuri.Nililala usingizi wa mang'amung'amu huku muda wote nilikuwa namuwaza mama yao akina Thomas ambaye kwangu ni mama mkwe.Asubuhi mida ya saa moja nikiwa nafanya usafi, nikamuona mama yao akina Thomas akifungua mlango.Alikuwa amebeba mfuko wenye sabuni ya unga huku mkono mwingine ukiwa na brashi.Akaondoka na kuelekea nje, nilimuangalia yule mama kwa macho yenye huruma mpaka akapotea kwenye upeo wa uso yangu.Nikajiuliza moyoni,

    "Mbona Thomas toka alivyofika jana hajanyanyua mguu wake na kwenda kumsalimia mama yake?".Nikaanza kupatwa na mashaka, nikapanga kumfuatilia mama yake na Thomas mpaka nijue chanzo chake cha yeye kuwa vile na anaelekea wapi. Nikawa naangalia kule getini,wifi Eve akanifuata akaniangalia, akaniuliiza nina shida gani?.Nikamuuliza,

    "Kwani mama amekwenda wapi?”.Wifi Eve akaniambia,

    "Wifi achana na mama endelea na shughuli zako, sikushauri umfuatilie mama kabisa. Utapoteza muda wako na kujiletea matatizo makubwa katika maisha yako".Ikabidi nimsikilize kwa muda ule wifi Eve na nikaendelea na likizo yangu.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Muda mwingi nikiutumia na wifi yangu Eve.Thomas na yeye asubuhi alikuwa akiondoka na kwenda kwenye miradi yake.Alikuwa na biashara zake nyingine hapo Mjini Moshi, hivyo alisema likizo yetu ataitumia kufuatilia baadhi ya biashara zake zilizokuwepo Moshi na Arusha.

    Kwa muda wa wiki moja niliyoishi kwa akina Thomas,sikumuona mama yao amekuja kujichanganyana na sisi wala kutusaliamia.Aghalabu mara moja moja wakati wa usiku nilimuona Wifi Eve akimpelekea sahani ya chakula na kurudi ndani.Kesho yake asubuhi Wifi Eve aliniaga anakwenda Soko la Memoria kwa ajili ya kuchagua nguo kwa sababu siku hiyo ilikuwa ni siku ya mnada.Alivyoondoka tu! Nikapanga kumfuatilia mama yao maana pale nyumbani hakukuwa na mtu.



    Nilichukua kanga, nikajifunika kichwani na mara nikamuona mama yao na akina Thomas akifunga mlango wa nyumba yake kwa ajili ya kuondoka.Kama kawaida yake,mkononi alikuwa ameshika sabuni ya unga pamoja na brashi.Nilivizia mpaka alivyotoka getini, nami nikatoka na kuanza kumfuatilia.Alivyokuwa akigeuka nyuma nilikuwa najificha mahali penye uficho. Mama yao na akina Thomas alitembea mpaka akafika kwenye bonde fulani kisha akateremka na kutokea kwenye mto. Alivyofika pale mtoni, akatoa sabuni ya unga pamoja na brashi akaanza kusugua mawe huku akiendelea kuimba na kuongea peke yake.

    Mara nyingine alikuwa akicheka na kucheza kana kwamba kuna kitu anakifurahia.Nilijisikia uchungu sana, hasa pale alipowa anatumia nguvu sana kuyasugua yale mawe.Ghafla wakapita wavulana fulani waliyokuwa wanakwenda kufua pale mtoni, mmoja wao akaniambia

    "Dada unashangaa nini? Huyo mama amegeuzwa kichaa na mtoto wake wa kumzaa kabisa.Usishangae ondoka, huyo haondoki saa hizi mpaka saa kumi na moja jioni ndio anaondoka”.Nikamuuliza yule kijana,

    " Mtoto wake yupi?"yule kijana akasema,

    "Simjui jina lake".Nililia sana baada ya kusikia yale maneno. Nilivyorudi nyumbani sikuwa na raha hata kidogo wakati naongea. Wifi Eve alikuwa akinishangaa tu!.Thomas alivyotoka kusimamia miradi yake, nilimuambia nimechoka kukaa Mjini Moshi nataka kurudi Dar na wala hakuwa na kipingamizi juu ya hilo.

    ******



    Baada ya miezi minne tangu nitoke Moshi,nilianza kuwa na dalili za uchovu na kichefuchefu.Nikaenda kwenye duka la dawa kisha nikanunua kipimo cha mimba. Yule mtu wa duka lile akanielekeza jinsi ya kupima na nilijikuta kweli nina mimba.Nilifurahi sana, nikapanga kumuambia Thomas kuhusu habari hiyo.



    Jioni nilipika chakula vizuri na kwa kila bashasha huku muda wote nilikuwa naongea kwa furaha.Usiku tukiwa tumelala huku nikimchezea chezea nywele za kifuani za Thomas,nikafungua kinywa changu na kumuambia kwa kuanza kumuita jina lake,

    "Mume wangu……”Nikasita kidogo ili kumsikia kama ataitikia, na kweli akaitika. Nikaenda moja kwa moja kwenye mada.

    “Nimeshika ujauzito mwingine".Thomas alinitoa mkono kwa nguvu pale kifuani kwake nilipokuwa nimepashika na kukurupuka,kisha akakaa kitandani macho pima huku amebadilika usoni kwa kukunja ndita zake akionesha wazi kashituka na ana hasira.







    NI VIZURI KUMUELEZA MTU WAKO WA KARIBU JAMBO LINALOKUSUMBUA, AU LINALOPELEKEA KUFANYA JAMBO FULANI LA HATARI,KULIKO KUKAA KIMYA UKAWA UNAUMIA MWENYEWE NDANI KWA NDANI.



    Alibadilika kabisa, alinyanyuka pale kitandani alipokuwa amelala,akakaa akaniambia,

    "Anne unanipenda?”.Nami nikamjibu ndio.Akaniambia,

    "Please nakuomba uitoe hiyo mimba".Nilimwangalia,na ghafla na mimi nikabadilika sana.Machozi yakawa yanatiririka, nikamwambia Thomas,

    "Kama hutaki nizae, si bora uniambie tutoe kizazi au tutumie kinga kuliko kuniambia nitoe kiumbe wa MUNGU asiyekuwa na hatia ya aina yoyote".Thomas alianza kulia na kunipigia magoti huku ameniinamia miguuni,akajitahidi kunibembeleza tena na tena.

    "Anne nakupenda sana, nionee huruma mpenzi, tafadhali toa hiyo mimba".Nililia sana kwa maneno yake. Nikamwambia kwa vile nakupenda nipo tayari kutoa tena mimba ya pili.

    Thomas alifurahi sana kusikia taarifa zile. Akanikumbatia na kunibusu huku akihaidi kutoniumiza na kunipenda tena na tena, yaani kuniongezea mapenzi zaidi.Kesho yake ilivyofika tuliondoka mimi na Thomas. Kama kawaida akanipeleka kwenye ile hospitali, nikamkuta dokta yule yule aliyenitoa ujauzito wa kwanza.Waliingia ofisini wakaongea faragha yeye na Thomas halafu wakaniita na mimi.Nilikuta kitanda kimekwishaandaliwa nikalala na kutolewa mimba ya pili.Baada ya hapo dokta akanipa dawa za kutuliza maumivu, tukaondoka mimi na Thomas tukarudi nyumbani huku Thomas akiwa na furaha sana,yaani muda wote akawa anacheka.Nilimshangaa sana Thomas,mimi nalia yeye anacheka kwa furaha.Nikabaki mwenyewe ninaumia ndani ya nafsi.

    ******

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Baada ya mwezi mmoja, kampuni ya Thomas ikawa imekuwa kubwa.Akafungua matawi mbalimbali katika baadhi ya mikoa na akawa anapata oda mbalimbali kutoka nchi mbalimbali.Kampuni ya Thomas ilikuwa ikihusika zaidi na usafirishaji wa mizigo, na katika kipindi hicho Thomas alikuwa amepanga kufungua kampuni nyingine huko Arusha itakayokuwa inahusika na kununua madini kutoka kwa wachimbaji wadogo wadogo na yeye atakuwa akisafirisha mpaka nchi za nje.

    Hivyo jina la Thomas likaanza kujulikana Tanzania na yeye akaanza kujulikana kama mfanyabiashara kijana mwenye mafanikio.Kwa upande wa biashara yangu ya duka, ilikuwa nzuri sana.Saluni yangu ikaanza kupendwa na watu maarufu, hata baadhi ya wasanii wakawa wanakuja kwenye saluni yangu kwa ajili ya kujipamba pindi wanapopata kazi zao za kisanii na madili mengine.



    Baada ya miezi mitano, nikashika tena ujauzito. Nilifurahi sana huku nikidhani ile kasumba ya Thomas itakuwa imemtoka. Nilipomueleza Thomas kama kawaida yake, akawa mbogo. Akaniambia ni lazima twende tena tukautoe huo ujauzito.

    Sikuwa na jinsi, ikabidi nikubali tena kwa shingo upande kutoa mimba.Nikawa nimetoa mimba yangu ya tatu.Kwa mara nyingine nililia sana, nikawa nimeumia ndani ya nafsi yangu kwa kuzipoteza roho za wanangu watatu. Sikuwa na jinsi, bali maisha kuyaendeleza.

    ******



    Kutokana na biashara yangu ya duka la vipodozi na saluni kuniletea faida kubwa, sikuwa na hiyana nilifunga safari mpaka Iringa.Nilipofika nikanunua kiwanja kikubwa, nikajenga nyumba kubwa sana.Nayo nilitumia muda mfupi sana kuijenga kwa vile pesa iliongea.Nilitumia muda wa miezi mitano tu kujenga nyumba yangu huku msimamizi mkuu akiwa ni kaka yangu John.

    Mimi nikiwa Dar nikaanza kumkumbuka kaka yangu Zakaria.Nilihangaika kwa muda wa siku mbili kumtafuta katika mitaa mbalimbali ya jiji la Dar-es-salaam,hatimaye nikafanikiwa kuonana naye.Alikuwa yupo katika hali mbaya sana, kwani madawa ya kulevya yalimuathiri sana.

    Nililia sana. Nikamchukua na kumpeleka nyumbani.Nilivyofika nyumbani Thomas alinishauri nimpeleke kaka Zakaria katika kituo cha afya kilichokuwa kinashughulika na watu waliokuwa wameathirika na madawa ya kulevya.

    Nikafanya hivyo huku nikihakikisha kaka yangu yupo sehemu salama.Nikawa naendelea na biashara zangu na Thomas akizidisha mapenzi kwangu.

    ******



    Baada ya mwaka mmoja, nikashika ujauzito mwingine. Kama kawaida Thomas akanibembeleza ikabidi nitoe kwa mara nyingine tena.Lakini sikuwa na amani kabisa hilo kiujumla. Nikawa nimetoa mimba ya nne.

    Siku hiyo nikawa nafanya kazi saluni. Rafiki yangu mmoja anaitwa Sauda akaniuliza,

    "Shoga vipi tena? Upo kwenye ndoa mwaka wa tatu mbona haushiki mimba?".Nikamjibu,

    "Nashika, ila kila nikipata zinatoka kwa bahati mbaya".Sauda alinipa pole akaniambia

    "Usijali best, ipo siku MUNGU atakujalia utapata tu motto”.Nikamjibu

    "AMEN".Kisha nikaendelea na kazi kama kawaida.



    Kaka yangu Zakaria alipona kabisa, alikuwa amekaa kwenye kituo cha afya spesheli kwa waathirika wa madawa ya kulevya kwa muda wa miezi sita.Tulikaa nae nyumbani kwa muda wa wiki moja kisha kaka Zakaria akaomba arudi Iringa kwaajili ya kuendelea na maisha.Niliwasiliana na kaka John, nikamuambia kuhusu na uamuzi alioamua kaka Zakaria.Kaka John akafurahi sana, huku akimshukuru MUNGU kwa kuwa ndugu tumekamilika kwa sababu tulikuwa tumetengana kwa muda mrefu.

    Basi kaka Zakaria akaondoka na kuelekea nyumbani Iringa.

    ******



    Baada ya miezi miwili tangu kaka zakaria kuondoka, nikashika tena ujauzito mwingine.Sikuwa na furaha hata kidogo kwani nilijua nini kitakachokuja kutokea baada ya kumwambia Thomas. Ili kutimiza nilichokiwaza niliamua kumwambia.

    Thomas kama kawaida alibadilika tena na kuwa mbogo.Akaniambia maneno yale yale,

    "Hiyo mimba ni lazima uitoe”.Kiukweli nililia sana na nikaanza kukataa.

    Thomas alinipigia magoti lakini nilikataa katukatu.Thomas alinipiga sana siku ile, ikabidi nikubali nikawa nimetoa ujauzito wa tano.



    Baada ya hapo nilianza kuona ndoa yangu imeingiwa na dosari.Thomas alianza kupunguza mapenzi taratibu, siku za mapumziko tukawa hatutoki tena kama zamani.Na mimi afya yangu haikuwa nzuri nikaanza kupungua taratibu.

    Siku moja Dokta Hans alikuja nyumbani kututembelea.Aliponiona alishangaa sana, akanishauri kesho yake nimfuate hospitali ili anipime afya yangu.

    Siku iliyofuata nikaenda akanichukua damu na kunipima lakini sikukutwa na ugonjwa wowote.Dokta Hans alijaribu kukaa na mimi na kuniuliza maswali kama nimegombana na Thomas, lakini mimi sikupenda kuyaweka wazi masuala yetu na wala sikupenda kumuharibia sifa yake Thomas kwa rafiki yake kipenzi ambaye alikuwa ni dokta mzuri na maarufu katika jiji la Da-es-salaam.

    Basi Dokta Hans akajua ninawaza kutokana na mimba zangu kutoka kwa bahati mbaya.Thomas alimwambia hivyo,akanipa ushauri na pole kisha Dokta Hans akaniruhusu kuondoka huku akiniambia nikipatwa na tatizo nisisite kumtafuta.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Baada ya mwezi mmoja, nikajihisi dalili za ujauzito. Nikaenda hospitali kupima nikakutwa na ujauzito kweli.Sikutaka kumwambia Thomas, nikapanga kulea hiyo mimba niliokuwa nayo mimi mwenyewe.

    Baada ya siku mbili, Thomas alíhisi nina mabadiliko. Muda mwingi nilikuwa namkimbia na kwenda kutapika kwa siri.Kumbe Thomas na yeye alipanga yake moyoni,akawa amepanga kunifuatilia kwa siri.Siku hiyo alinikuta nikitapika sana kwenye sinki, alinivuta mkono kwa nguvu akaniweka kwenye gari,na moja kwa moja akanipeleka kwenye hospitali ya yule dokta aliyekuwa ananitoa mimba. Aliingia ndani na kuanza kuongea na dokta.Yule dokta alinipa chupa akaniambia nimpelekee haja ndogo huku Thomas akinifuatilia.Baada ya kunipima nikamsikia akimwambia Thomas kuwa nina mimba ya miezi miwili.Thomas alimwambia yule dokta anitoe ile mimba.

    Nililia sana nikamuita Thomas muuaji mkubwa asiyependa watoto, hivyo mimba ya sita ikawa imetolewa.

    ******



    Baada ya miezi miwili, Thomas akatangazwa ni moja wa bilionea mkubwa anayeongoza kwa utajiri nchini Tanzania.Nilishangaa sana, nikamuuliza Thomas

    "Wamezingatia vigezo gani?"akanijibu

    "Kujituma kwangu na biashara zangu mbalimbali".Basi tuliendelea na biashara zetu huku mimi nikijitahidi kumkwepa Thomas katika masuala ya kushirikiana nae kimwili.Lakini haikuwezekana kwa sababu baada ya miezi mitano nilishika mimba nyingine.Nikajitoa muhanga na kumwambia Thomas ya kuwa ule ujauzito siutoi na nitajifungua na kumlea mtoto wangu mimi mwenyewe.







    KUKIRI KOSA NI VIZURI, KULIKO KUKAA KIMYA NA NI VIZURI MALI ZAKO UKAWA UMEZIPATA,KIHALALI KULIKO KUTUMIA NJIA NYINGINE ZISIZO HALALI.



    HII NI SEHEMU YA MWISHO.



    Thomas alichanganyikiwa sana baada ya msimamo niliyompa.Akaniuliza mara mbilimbili kama lile jambo ninalomwambia ni la kweli.Nikamjibu ndio.

    Alinipigia magoti huku akiniomba niitoe ile mimba.Nilikataa kabisa akataka kunipiga nikamwambia,

    "Thomas mimi sijawa mjinga, ukinipiga tu! Nitakwenda kwenye vyombo vya sheria vinavyotetea haki za binadamu."

    Thomas aliishiwa na nguvu, siku hiyo nilimshuhudia Thomas akiwa hajaenda kazini.Alijifungia chumbani kwake akiwa analia sana.Moyoni nilimuonea huruma nikatamani nibatilishe maamuzi yangu lakini nikajisema.

    "Hapana amezoea vibaya sana,ni lazima nilee hii mimba na nijifungue.Nikapanga kutoroka kwa siri nikajifiche sehemu mpaka nitakapojifungua.Sikutaka kumshirikisha mtu yeyote zaidi ya rafiki yangu mmoja tu!wa pale saluni.

    Baada ya siku mbili Thomas alienda kazini huku akihama na nyumba na kwenda kulala nyumba ya wageni.Hakutaka kuongea na mimi hata wakati ninamsalimia, hakuijibu salamu yangu.Nilikosa na muda wa kuifuatilia miradi yangu ingawa jioni wafanyakazi wangu walinitafuta na kunikabidhi hesabu za siku.

    Nilivizia Thomas alipoondoka tu! Na mimi nikaingia chumbani na kupanga baadhi ya nguo zangu chache.Nikabeba pesa zangu zote pamoja na kubeba ATM cards zangu,kisha nikaingia kwenye gari na kuelekea mjini.

    Nikatafuta dalali, akanitafutia nyumba yenye vyumba vitatu nikaanza maisha.Hata katika simu yangu nilibadili laini, sikutaka Thomas anitafute.Nikamtafuta Sophia aliyekuwa mtu wa kwetu Iringa,nikamwambia awe anasimamia miradi yangu na kuniletea hesabu.

    ******



    Baada ya miezi minne wakati ujauzito unaingia mwezi wa tano, nilianza kusikia hali ya ajabu katika mwili wangu.Sophia alivyokuja nyumbani akanishangaa sana jinsi nilivyobadilika nikamwambia,

    "Usinishangae mimba ya kwanza inanisumbua".Akanipatia karatasi iliyokuwa imebanwa vizuri ikiwa imeandikwa,

    "ANNE NITAFUTE KABLA HIYO MIMBA HAIJAFIKISHA MIEZI SITA”.

    Nilishtuka nikamuuliza Sophie,

    "Nani amekupa huu ujumbe?".Akanijibu ni Thomas.

    Sophia hakukaa sana, akaondoka zake.Siku hiyo usiku sikulala kwa amani niliweweseka usiku kucha huku nikiona watu na vitu vya ajabu vikinijia na kunizunguka.Muda mwingine wale watu walikuwa wanasema lazima tukutoe mimba uliyobeba.Sikuweza kuvumilia, kesho yake asubuhi na mapema niliamka,hata chai sikuitamani kuitia kinywani. Nikakodi taksi ikanipeleka mpaka nyumbani kwa Thomas.Nilivyofika nyumbani nilimkuta mlinzi yupo kwenye geti kama kawaida yake.Nikamuuliza kama Thomas alikuwepo nyumbani,akanijibu yupo ndani.

    Sikutaka kuongea nae jambo lingine lolote, hapo hapo nikaingia ndani kwa kasi ya ajabu.Nilivyofika sebuleni sikumkuta Thomas,nikaenda hadi chumbani.Nilimkuta Thomas amelala na viatu kitandani akiwa na mawazo sana.Alivyoniona tu akaniambia,

    "Anne nakuomba urudi nyumbani mke wangu".Halafu Anne unaniua hivi hivi ukiwa unaniona?.Nikamuuliza,nakuuaje jamani mbona mimi nakupenda na sitaweza kukuua mume wangu?.Akaniambia rudi nyumbani kwanza jioni ya leo, ninamaongezi mazito na wewe. Itabidi nikuambie ukweli wote.Nikamkubalia Thomas kurudi nyumbani huku moyoni nikasema,

    "Ahsante MUNGU Thomas amejirudi ili tulee ujauzito niliokuwa nao”.Mpaka kufika saa kumi nikawa nimeikabidhi ile nyumba niliokuwa nimepanga.Niliporudi nyumbani nilimkuta Thomas akiwa amekaa akinywa "red wine". Aliniomba nikae ili aniambie ukweli. Sikuwa hata na hamu ya kula nikaa na kuanza kumsikiliza.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    HISTORIA YA THOMAS.



    Mwaka 1998 Thomas na familia yake walikuwa wakiishi maisha ya kimasikini sana. Wakati huo baba yao alikuwa amekwisha fariki.Thomas alitafuta kibarua, akawa anawauzia abiria na watu mbalimbali maji,juice,soda nk,katika kituo kikuu cha mabasi ya Mjini Moshi.Hivyo aliweza kupata pesa ndogo ambayo ilikuwa haikidhi mahitaji yake mbalimbali na ya pale nyumbani kwao.Muda mwingi Thomas aliuchukia umasikini, na kutamani siku moja amiliki nyumba kubwa, nzuri na ya kifahari. Pia alitamani kuendesha gari mbalimbali za kifahari lakini hakuwa na huo uwezo.

    Muda mwingi alibaki akiwaza yeye na nafsi yake.Siku moja wakati Thomas akiendelea na biashara zake alikutana na rafiki yake Nelson.Nelson alikuwa amebadilika sana, alinenepa na na kupendeza sana.

    Nelson alikuwa amekwenda stendi kumsindikiza mke wake aliyekuwa anaelekea jijini Dar-es-salaam.Nelson alisikitika mno alipomuona Thomas yupo katika hali ile.Thomas alimuuliza,

    "Vipi rafiki, mbona upo katika hali hiyo? Umependeza sana aisee".Nelson akamjibu,

    "Siri ya mafanikio yangu naijua mwenyewe, hii si sehemu ya kuongelea.Chukua hii business card yangu ukipata muda utanitafuta".Thomas akapokea business card kisha Nelson akachomoa waleti akampatia Thomas shilingi laki moja.Baada ya hapo wakaagana na Nelson akaondoka.

    Thomas akaendelea na biashara zake japo hukuzifanya kwa raha. Muda wote alikuwa akimuwaza rafiki yake Nelson.Alianza kutamani kuwa kama Nelson.

    Akakumbuka jinsi walivyoanza kutafuta maisha.Nelson alikuwa akiendesha mkokoteni akibeba mizigo ya watu katika soko la Uru Kishumundu na sasa Nelson hakuwa vile tena.



    Ilipofika jioni tu! Thomas alichukua ile business card na kumpigia simu Nelson.Nelson alimuuliza yuko wapi, Thomas akamwambia alipokuwepo na kisha Nelson alimfuata.Akamchukua na gari yake mpaka nyumbani kwake.

    Nelson alikuwa amejijenga kimaisha sana,nyumba yake ilikuwa na vitu vya thamani vingi tu.Tamaa ikamwingia Thomas,akamuuliza Nelson,

    "Mwenzangu nyumba nzuri na ya thamani ghafla umeipata wapi?".Nelson akacheka akamwambia, kwa Babu.Thomas akamuuliza Nelson kwa babu yupi?Nelson akamwambia haya mafanikio nimeyapata kwa babu mganga, usinione hivi nimemwaga damu za ndungu zangu wengi.Je, upo tayari nikupeleke na utatii masharti yake?

    Thomas alishtuka sana,akamwambia Nelson,

    "nipe muda nijifikirie nitakuambia"

    ******



    Baada ya siku mbili Thomas alikubali ombi la Nelson.Akamfuata Nelson na kumwambia yupo tayari.Walianza safari mpaka kwenye milima ya Upareni kwa babu.Kufika kule walimkuta babu, na babu alimuambia Thomas asubiri shughuli itaanza usiku.Usiku ulipofika, Thomas alichukuliwa na kupelekwa kwenye mto aliogeshwa dawa mbalimbali na kuchanjwa. Baada ya hapo akaambiwa amtaje mtu anayempenda akamtaja Peter.

    Peter alikuwa ni mdogo wake anayemfuatia.Baada ya kumtaja akaletewa beseni kisha akapewa kisu na kuambiwa achome atakachokiona kwenye beseni.Sura ya mdogo wake ilipotokea akaichoma.

    Thomas alilia sana baada ya tendo lile hasa alipogundua kuwa kamuua mdogo wake.Babu alimwambia baada ya miezi miwili arudi.Asubuhi wakiwa njiani wanarudi yeye na Nelson,Thomas alipigiwa simu ikimtaarifu mdogo wake Peter amefariki, Thomas alilia zaidi baada ya uthibitisho huo.



    ******

    Baada ya mwezi moja, Thomas alibadilika. Alipendeza akawa anamiliki duka kubwa pale alipokuwa anaishi.Mwezi wa pili ulipofika, akaenda kwa babu tena. Alikuwa na mdogo wake aitwaye Gerald akamtoa kafara tena.Baada ya hapo akamwambia babu anataka ahamishie biashara zake Dar-es-salaam, ila ana mpango wa kujenga nyumba kwanza.Nyumba ikikamilika atahamia huko.

    Babu akamwambia akijenga nyumba atenge chumba ambacho Thomas atakutana na watu ambao watakuwa wanamshauri katika shughuli zake mbalimbali. Asiwe anafunga safari tena za kwenda Upareni.

    Thomas akawa amebakiwa na wadogo zake wawili, Massawe na Eve.Baada ya miezi sita Thomas akaenda kwa mganga yule kisha akampa hirizi, akamwambia mizimu inamtaka mdogo wake Massawe.Na imempenda mama yako ili wewe upate mafanikio haraka.

    Itamfanya mama yako awe chizi na itampa kazi kuanzia saa mbili asubuhi mpaka saa kumi na moja jioni, atakuwa anaosha mawe mtoni kwa sabuni ya unga.Hivyo mdogo wako Eve ndiyo atakaesalimika akimwangalia mama yako.Thomas alilia sana japo ilikuwa kama kinafki, ikabidi akubali masharti kwa shingo upande.



    Thomas akahamia Dar, akapata mafanikio makubwa na biashara yake ikawa nzuri.Kila saa nane usiku akawa akikutana na mizimu ikawa inampa masharti mbalimbali.Thomas akaniambia,baada ya yeye kunisaidia mimi.Mizimu ilimuambia Thomas anitumie mimi, anipe mimba lakini nikipata mimba nitoe na nisizae na hiyo mimba isifike miezi sita, iwe imetolewa.Bila hivyo Thomas atakuwa amekiuka masharti na wanajua adhabu watakayompa.Thomas alimaliza kunisimulia huku akiwa analia sana,na mimi nilikua ninalia sana nikamwambia ndio maana ulikuwa unanikataza kufungua kile chumba na kule Moshi ulikataa nisimfuatilie mama yako.Kumbe kwaajili ya kutaka utajiri ndio umemfanya vile mama yako!?.Unadhambi kubwa ya kujibu mbele za Mungu.

    Thomas akaniambia,

    “ najua Anne naomba unisamehe kabla ya kesho kutwa nitakuwa nimekwishatangulia mbele ya haki”.Nikashtuka sana, nikamwambha Thomas usiseme hivyo akaniambia,

    "Watu waliokuwa wananipa masharti wameniambia lazima nitakufa tu, hapa wamenipa siku mbili nikutafute nikuambie hivyo na lazima mimba yako itatoka tu,na wanahitaji mali zao, watazichukuaje! mimi sijui. Nisamehe sana Anne"CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Nililia sana,nikamsamehe Thomas, nikaendelea kuishi nae ingawa sikuwa na raha.

    ******

    Baada ya siku mbili Thomas alipatwa na ajali ya gari.Gari lake liligonga mti akafariki palepale. Nililia sana, nilijua wale watu wameshmchukua Thomas.Tulisafirisha mwili wa Thomas mpaka Moshi, akazikwa huku watu wengi wakihudhuria mazishi ya Thomas. Nililia sana kumpoteza mume wangu kipenzi.

    Baada ya kumaliza msiba nilirudi Dar nikaendelea kuishi kwenye nyumba ya Thomas.Siku hiyo usiku wa manane nikiwa nimelala.Niliona kwenye ndoto nikiwa nimebebwa na watu watano. Walinipeleka kwenye chumba sikikumbuki ni kipi,kisha wakanitoa mimba.Nilimuona yule dokta aliyekuwa ananitoa mimba wakati nipo na Thomas, nikagundua kumbe alikuwa mwenzao nililia sana.

    Nikiwa kwenye ndoto, wale watu walishangilia sana hapo nikaona giza na sikujua kilichoendelea.Asubuhi nilivyoshtuka tumbo langu lilikuwa dogo na sikuwa na mimba tena.Nilikosa raha, nikawa na mawazo sana. Nilihisi damu za watoto wangu zikinillia,kila nilipokuwa naenda au kukaa,nilikuwa nasikia sauti za watoto wachanga wakilia sana.Nilikosa raha, afya yangu ikaanza kuzorota taratibu.

    Baada ya miezi miwili kuna watu walikuja nyumbani napoishi, wakaniambia nitoke kwenye ile nyumba niwaachie nyumba yao. Niligoma kutoka wakaniambia nitaona.

    Siku hiyo usiku Thomas alinijia kwenye ndoto akiwa na mwili wa mbwa uso wa kwake.Akawa analia sana akaniambia,

    "Anne unanitesa sana huku niliko, napata shida tafadhali toka haraka kwenye hiyo nyumba wamekuja kuchukua nyumba yao”. Kisha Thomas akawa anaondoka huku anabadilika amekuwa kwenye umbo la fisi.

    Kesho yake asubuhi nikasikia kuna panya wameingia kwenye maduka wameku-la bidhaa zote.Baada ya muda nikasikia kampuni zote zimeungua, kuna moto wa ajabu umetokea.Sijakaa sawa kaka John akanipigia simu akanipa taarifa ya kuwa nyumba yangu Iringa inaungua.Wakati natafakari nifanye nini,nikapigiwa simu saluni yangu pia inaungua.

    Nilichanganyijgwa sana, nikasikia tena sauti za watoto wangu wanalia. Nilitafuta kamba na nikaondoka pale nyumbani kwa Thomas. Ile natoka nje tu,niliyakuta magari yote yakiwaka moto. Majirani wakawa wamekusanyika wakiyazima nilichanganyikiwa nikawa sijielewi. Nikakimbia mpaka porini, nililia sana huku nikisema,

    KWANINI MIMI?

    KWANINI HAYA YOTE YANITOKEE?.

    Nilitengeneza kamba, nikaifunga kwenye mti nikapanda kwa ajili ya kujinyonga.Niliitia kamba ile shingoni,kamba ikikazika vizuri.Hapo niliona giza totoro na kilichoendelea sikukijua.



    *****HILI NI FUNZO KWA WATU WOTE. TUTAFUTE MALI ZETU KWA NJIA HALALI.

    MAONI YAKO NITAPENDA ZAIDI.

    MWISHO WA RIWAYA HII.******

0 comments:

Post a Comment

Blog