Search This Blog

Sunday, July 10, 2022

GANZI YA MOYO - 5

 







    Simulizi : Ganzi Ya Moyo

    Sehemu Ya Tano (5)



    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    “Kijana tatizo lako umeingia choo kichafu halafu imejulikana kuwa wewe ndiye uliyekichafua. Sasa ni kheri ungeelewa somo kuliko kujidai nunda. Tumekuonya mara ngapi juu ya yule mwanamke lakini bado ukang’ang’ania kuwa naye?” Aliuliza jamaa mmoja ambaye alikuwa kifua wazi huku kakamata waya wa umeme.

    Edson alihangaika kuinua uso wake na kumtazama yule jamaa kwa macho makali, kisha akainamisha kichwa chake bila kuongea neno.



    “Hilo ndilo tatizo lako kijana. Unakiburi sana…” Bwana mwingine aliongea hayo na kumfuata Edson na kuanza kumpiga virungu kwenye magoti yake. Edson alilia kama mtoto lakini hakuna aliyejali zaidi ya kucheka kile kitendo kinavyoshika nafasi yake.



    “Acheni kwanza.” Sauti kali ilisikika mlango wa kuingilia chumba kile na yule mpigaji alijikuta akiwa kaganda huku kanyanyua Rungu lake, halafu kageuka nyuma kumuangalia yule aliyekuwa amemkataza kutoa adhabu.

    Akajikuta akiacha kazi ile na kwa heshima kubwa akasogea pembeni wakati huo yule bwana akiyekataza Eddy asipigwe alikuwa anasogea pale alipotundikwa Edson.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Edson kwa shida sana akanyanyua uso wake na kumtazama yule bwana aliyekataza ule msalaba asiendelee kuubeba, hapo alijikuta akitabsamu na kusikitika bila kupenda.



    “Sitaki kuamini kama mapenzi ndio sababu ya wewe kufanya hivi.” Edson aliongea kwa shida wakati yule mtu anazidi kusogea pale alipotundikwa.



    “Tatizo ni kwamba, umeingilia pale ambapo tayari mwenzako nimeweka moyo wangu. Kwa nini kijana?” Aliuliza yule bwana.



    “Tatizo ni kwamba, moyo ule hukuwekwa wewe.” Alijibu Edson kwa utulivu na maneno yalimfanya yule bwana aende kwa kasi na kutaka kumpiga Edson.



    “Nitakupiga wewe mtoto.” Aliongea kwa hasira kali.



    “Umeshawaamrisha vibaraka wako wanipige, sitashangaa wewe kuendelea kunipiga. Lakini tambua kuwa, hata nikifa, moyo wa Win hautokuwa wako. Umenielewa Ibra?” Edson aliongea kwa nguvu kidogo na kwa kujiamini.

    Ibrahim Singa, muhusika mkuu wa kumteka nyara Edson, alikuwa kafura kwa hasira mbele ya kijana yule. Kila neno lililomtoka Eddy, basi lilikuwa mkuki wenye ncha ya moto unaoingia kwenye moyo wake.



    “Unaonekana huogopi kifo.” Aliongea tena Ibra safari hiikwa utulivu bila kufoka.



    “Nilikwishakufa juu ya Win. Kwa hiyo hapa nathibitisha kifo hicho tu! Siogopi kufa, ila naogopa Win kufa. Na wewe ndiye utakayemuua yule mwanamke.”



    “Hapana. Wewe ukifa, moyo wa Win lazima utahamia kwangu. Na hadi sasa hivi moyo huo umeanza kuja kwangu.” Alijibu Ibra kwa kejeli.



    “Hapana, mimi nikifa moyo wa Win utakuwa katika ganzi, ganzi ya moyo. Hatokuwa na njia nyingine, bali naye kufa tu! Baada ya yeye kufa, utafuata wewe kwa sababu na wewe utakuwa umekumbwa na ganzi kama alilolipata Win.” Ibrahim alicheka sana kwa maneno hayo ya kujiamini kutoka kwa Edson.



    “Dogo upo vizuri kwenye kutunga. Kwa nini usitoe muvi? Itafana sana. Lakini nasikitika hapa ndio mwisho wako.”



    “Najua hapa ni mwisho wangu, lakini sina mwisho kwenye moyo wa Win. Atanifata tu!”



    “Nyamazaa. Mbwa wewe.” Maneno hayo yalienda sambamba na Edson kupokea kofi zito la shavuni. Aligugumia maumivu kwa dakika kadhaa lakini baadae alimtazama Ibrahim kwa macho yake makavu na kisha akacheka tu.



    “Mapenzi ni moyo na wala si kulazimisha. Moyo uliyondani ya penzi, si rahisi kuhisi maumivu hata ya kisu pale unapochomwa. Usilazimishe moyo wa Win kukupenda kwa sababu tayari moyo ule unakuona wewe huna thamani yoyote juu yake. Ukilazimisha sana kupendwa, utajikuta unatumbukia katika penzi la manyanyaso. Utanyanyaswa kisa umependa. Mshukuru Win anaroho nzuri sana. Hakutaka kuunyanyasa moyo wakona kuuvunja kama changarawe. Mshukuru nakwambia.” Maneno hayo yalikuwa yanatoka mdomoni kwa Edson kwa shida sana lakini yalisikika vema kwa wote waliokuwamo mle.



    “Linapokuja suala moyo wangu kupenda, basi nitafanya lolote lile ili moyo huu uapate kile unachokitaka. Nitacheza kwa nguvu, na ninacheza kwa nguvu zangu zote ili kushinda moyo wa Win. Naimani kuwa nitashinda baada ya kifo chako.” Tabasamu pana lilirindima katika uso wa Ibra wakati anaongea hayo lakini Edson alisikitika na kujikuta mwenye kucheka tu.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Naona unatumia msemo wa kipendacho roho hula nyama mbichi. Lakini hujui huu msemo unamaana gani. Kwa kuwa umependa, basi upo tayari kula nyama mbichi, si ndio?” Edson alimuuliza Ibrahim.



    “Yeah!” Akajibu Ibra kukubali yale.



    “Basi wewe utakuwa mtumwa wa mapenzi tu. Kama upo tayari kula nyama mbichi, wewe ni mtumwa. Na mwisho wake utakuwa bwege. Wenzako kama mimi tutatokea na kula mzigo wakati wewe unanyimwa huko ndani.” Maneno hayo yalimfanya Ibrahim azidi kuvimba kwa hasira lakini yalikuwa yanaukweli mkubwa sana katika maisha yake.



    Hakuna ambaye yupo tayari kula nyama mbichi eti kwa sababu moyo wake umetaka kufanya hivyo. Huo ni utumwa wa nafsi. Kama nafsi itakupelekesha, basi tambua kuwa hutofikia malengo yako katika suala lolote katika dunia hii. Fanya kitu kwa matakwa yako na kioneshe faida. Usile nyama mbichi kwa sababu moyo umependa na nafsi imekusukuma. Utaishia kukufuru kila siku kuwa mwanamke huyu alinifanya nile nyama mbichi, halafu leo hii ananiacha. Au mwanaume huyu kanifanya niwaache wanaume wengine wote lakini leo hii ananitenda. Hanijali, hanithamini wala kuzielewa hisia zangu. Hayo ndio yatakuwa malalamiko kama utalazimisha moyo wa mtu. Na mwisho wa yote, utakonda kwa mawazo, utakuwa mlevi na mwishowe utafanya mambo ya ajabu kama aliyoanza kuyafanya Ibrahim. Mapenzi ni vita, lakini si vita ya mioyo inayopendana bali ile isiyopatana. Ibrahim anataka kuingia vitani na Win.



    “Unaonekana mjuzi wa Kiswahili, umemfundisha hadi Win. Embu mshusheni kwanza. Mleteni hapa mezani.” Ibra aliongea hayo huku anaelekea sehemu moja ambayo ilikuwa inameza yenye karata za wale mabwana.

    Wale majamaa wenye miili, walifanya kama Ibrahimalivyotaka na kisha kumburuta Edson hadi mbele ya Ibra. Wakamkalisha kwenye kiti na kisha wao wakasogea pembeni.



    “Hichi ni nini?” Ibrahim alimuuliza Edson baada ya kuweka bastola juu ya meza.

    Edson akatabasamu baada ya kuona silaha ile.



    “Mapenzi bwana. Yanaweza kukufanya ufanye mambo ambayo hapo mwanzo hukuwahi kuwaza kuyafanya. Haya leo nabebewa bastola kisa mapenzi. Kweli mimi ni shujaa.”



    “Hamna shujaa wa mapenzi dogo. Kwanza huko nje unasambaziwa mambo kibao. Nadhani ulikuwa unapewa ujumbe na Win.”



    “Haijalishi, lakini moyo wa Win haukuhusu.” Ibrahim alinyanyuka kwa hasira na kumtandika kofi Edson. Kijana yule akagugumia kwa maumivu makali lakini alijikaza na kumtazama tena Ibrahim. “Unajua kitu kikukwa katika maisha ni kukubali kushindwa lakini usikate tamaa kushindana tena. Wewe umekubali umeshindwa, lakini hutaki kuamini kuwa umeshindwa, matokeo yake unajiumiza tu.”



    “Dogo. Kuna jambo moja kubwa sana katika maisha wewe hulijui. Hakuna mshindi katika mapenzi. Penzi wanasema ni kiti cha basi tu! Unaposhuka wanakaa wengine. Hakuna mwanamke wa sasa anayeweza kupita kwenye mkono wa mwanaume mmoja tu! Waliweza mama zetu, lakini wanawake wa sasa, kwa asilimia kubwa sana, karibu asilimia tisini na nane, wanapita kwa wanaume zaidi ya watano ndipo anakuja kuoelewa.” Aliongea Ibrahim.



    “Kwa hiyo asilimia tisini na nane wanapita kwa wanaume wengi kabla ya kuolewa. Halafu asilimia mbili ni wale wanaopita kwenye mkono wa mwanaume mmoja tu! Huyo huyo ndiye anayemuoa.” Edson aliongea kama anauliza lakini alikuwa anafafanua kauli ya Ibrahim.



    “”Exactly (Sawasawa). Naona somo limekuingia.” Ibra alimsifia Edson.



    “Hapana. Nataka kukwambia kuwa, katika asilimia hizo mbili, ndimo Win yumo. Kapita na atapita kwenye mikono yangu tu” Maneno hayo yalimfanya Ibrahim ananyanyuke kwa kasi na kumvaa Edson. Vaa hiyo ikawadondosha wote chini lakini Ibra akiwa kamkalia kifuani Edson na kuanza kumtandandika ngumi za usoni kijana yule. Akaona haitosha, akachukua bastola yake na kuanza kumpiga kwa kitako chake. Edson alikuwa analia kwa maumivu makali lakini alishindwa afanye nini kw wakati ule.







    Kitako kile cha bastola kilikuwa kinatua vema kwenye upande wa kushoto wa uso wa Edson. Upande ule ulitengenezwa jeraha kubwa sana la kidonda lakini Ibrahim hakuacha kumpiga Edson kwa sababu tayari alikuwa kadhamiria sana kummaliza kabisa kijana yule.



    “Yatosha bosi. Tutamuua huyu wakati si lengo letu.” Jamaa mmoja kati ya wale watekaji watatu alimkamata mkono wenye bastola Ibrahim na kumuambia amuache Edson kwa sababu tayari kijana yule alikuwa amekwishanyamaza muda tu.

    Ibrahim akamuangalia yule bwana kwa macho makavu lakini yule bwana hakukwepesha macho yake wala hisia zake za kuumia baada ya kuona matendo anayofanyiwa yule kijana tena kisa kikuu kikiwa ni mapenzi, ama kweli mapenzi ni maji ya moto, nadhani Edson atayakumbuka maneno ya mama yake.



    “Wewe unamuonea huruma huyu mpumbavu?” Ibrahim alimuuliza yule bwana kwa hasira kidogo.



    “Si mpango wetu kumuua dogo. Nadhani tulikubaliana bosi. Kama wataka afe, basi si mbele ya macho yetu na wala si kwa sasa hivi. Sisi tutahusika kwa asilimia kubwa sana huyu dogo kufa kwa sababu ndio watekaji. Hivyo hatutoruhusu huyu dogo kufa.” Aliongea yule bwana kwa makini zaidi.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Unahuruma sana yaonekana. Ni mara ya kwanza kuona mtu anauawa? Au ni mara ya kwanza wewe kuteka? Au labda wewe hujawahi kuua. Lakini niliwalipa kwa sababu hii, na si kwa sababu nyingine.” Ibrahim aliongea huku akipepesa angali mkono wake uliokuwa umekamata bastola.



    “Hapana Bosi. Nimekwishateka sana, nimeua sana na nimeshudia hadi wazazi wangu walivyouawa. Lakini sijawahi kuua au kutumwa kuua eti kisa kiwe mapenzi. Yaani kuua kwa sababu ya mwanamke. Sisi huwa tunatoa onyo tu huku tukifikisha ujumbe tuliotumwa na bosi kuwa atauawa. Ndio maana mateso yetu ni viboko na makofi. Tunabastola wote hapa, lakini tumeziweka mbali. Tulichofanya ni kumkanya tu Dogo. Tunajua wazi akitoka hapa hatorudia tena na ndio maana hatukutaka wewe uje hapa. Sasa tunashangaa kukuona angali unajua kuwa atakutaja huko uraiani.” Alizidi kutabainisha yule mtu ambaye alikuwa na mwili mkubwa kuliko ule wa Ibra.



    “Ujue sikuelewi kijana. Ni kwamba unanidharau mimi kuua kwa sababu ya mapenzi au unanitisha. Nimekuja hapa nikiwa na akili zangu timamu na si kulazimishwa. Najua wazi kuwa huyu bwege atanitaja na ndio maana nataka kumuua ama la! Nitatumia hii.” Aliongea Ibra na kutoa bomba la sindano mfukoni pamoja na kichupa kidogo cha dawa. “Inaitwa MEMOPONOMINI. Ni dawa mpya kabisa duniani. Kazi yake ni kumpoteza kumbukumbu kiumbe chochote duniani. Na kumbukumbu hizo hupotea kwa miaka kumi na tano. Lakini ukitaka zipotee kabisa, basi kila mwezi uwe unampa kidonge kimoja, hichi hapa.” Akatoa pakiti ya vidonge na kuwaonesha wale majamaa ambao walikuwa kimya wakifuatilia yale maongezi. “MEMOPILLISM. Ndio jina lake. Navyo ni vipya duniani. Kazi yake ni kuzidi kufuta kumbukumbu kabisa. Inakwangua kumbukumbu zote za kichwani, unaanza upya. Na kitu kizuri kabisa kuhusu hii dawa….” Akashika tena ile dawa ya maji kwa ajili ya sindano, MEMOPONOMINI. “Ukimdunga sindano hii, anakuwa kila wakati anataka ngono tu! Huyu atakuwa mbakaji mkubwa duniani. Dawa hii imetengezwa kwa ajili ya wanyama wa mwituni wale wanaoibwa nchi fulani na kupoelekwa nchi za huko ughaibuni.” Alimaliza maongezi yake ambayo kwa wale jamaa yalikuwa ni mazuri sana na walipata faraja lakini maneno ya mwisho yakawashangaza tena.



    “Bosi. Dawa ya wanyama unamdunga binadamu?” Jamaa mwingine alimuuliza Ibrahim kwa hamaki.



    “What’s a poblem? (Nini tatizo?)” Ibrahim alijibu swali hilo kwa swali.



    “Lakini huoni kuwa ukimchoma hiyo sindano, kama mihemko ya mwili ikiwa mikubwa, Win atamsaidia?” Swali hilo likamfanya Ibrahim ajikune kichwa na liliulizwa na yule jamaa mwingine aliyemkataza asiendelee kumpiga Eddy.



    “No. Nasema hapana. It can’t happen (Haiwezi kutokea)” Alilalama Ibra. “Kalete maji tumuamshe huyu bwege.” Ibra aliongea na jamaa mmoja akakimbia haraka na aliporudi alikuwa na maji ya baridi kwenye chupa. Akammwagia usoni Edson lakini hakuamka na badala yake maji yale yakachanganyika na damu nyingi ambayo ilikuwa haijakata.

    Jamaa yule akammwagia tena Edson safari hii kwa fujo zaidi. Edson akafumbua macho na kikohozi juu lakini alishindwa kunyanyuka na alikuwa katika maumivu makali sana.



    “Karibu tena kidume. Naona ulikuwa umeenda nusu kuzimu. Niambie, umeonana na Shetani au MUNGU?” Ibra aliongea kwa kejeli baada ya kuona Eddy kazinduka.



    “Niue…” Edson aliongea kwa sauti ya chini. Akaendelea, “Lakini kabla hujafanya hivyo, naomba nimuage Win. Sitakutaja.” Kwa sauti ileile Edson alitoa ombi na bila kufikiria Ibra akaomba simu moja ya mabwana ambao huwa hawakai na line moja ya simu kwa sababu ya kazi zao. Yaani wakishamaliza kazi walizotumwa, line zile wanazivunja na kuzitupa.



    “Ibra akachukua simu moja na kubofya namba fulanifulani. Kisha akamuinua Eddy na kumkalisha, akamuwekea sikioni simu. Simu iliita kwa sekunde kadhaa na baadae ilipokelewa na msichana.



    “Hey Wife. Edson hapa.” Kwa sauti ileile ya chini na iliyojaa maumivu, Edson aliongea. Upande wa pili wa simu ulikumbwa na taharuki kwa sauti ile lakini Edson hakuacha kuongea japo kwa taratibu sana. “Unakumbuka niliwahi kukwambia kuwa siwezi kukuondoka bila kukwambia kwa heri?” Hakusubiri tena ajibiwe na upande wa pili. Akaendelea, “Nataka kukuaga Win. Tutaonana MUNGU akipenda. Usilie sana wala kufanya chochote juu yakifo changu. Mwambie mama alikuwa sahihi kunikataza nisitoke siku ile. Mwambie nampenda sana, lakini sina jinsi. Kwa heri.”Maneno hayo ya mwisho toka kwa Eddy, yaliwafanya wale watekaji wakuu waumie sana moyoni lakini walificha hisia hizo na kusubiri ni nini tajiri wao ataamua.



    “Kumbe huwezi kunitaja wewe. Hiyo namba wala siyo ya Win. Nilijua tu utataka kuongea naye hivyo nilikuandalia mtu spesho kwa ajili ya kujaribu kuona kama utanitaja kwenye maongezi yako. Sasa nampigia Win orijino. Jipange.” Edson akatabasamu kwa shida usoni kwake akiwa na jeraha kubwa sana la kidonda. “Huyu hapa Win.” Ibra akamuwekea tena ile simu sikioni Edson. Simu ilipokelewa na sauti ya Win ilisikika vema katika masikio ya Eddy.

    Edson akatabasamu kwa furaha na kujikuta tabasamu hilo linaambatana na kutokwa na damu mdomoni. Kijana wa watu akaanzakulia kwa uchungu baada ya kuona kuwa tabasamu lake limegeuka damu, damu ambayo inamwagika kwa sababu kapenda. Alizidi kulia baada ya kusikia sauti ya Win ikiita bila kujibiwa.



    “Wiiii…..niiii.” Sauti kavu ya Edson iliita kwa uchungu mkubwa huku akiwa kang’ata meno kwa nguvu akijaribu kutoonesha maumivu ya moyo anayoyapitia. Ama kwa hakika alikuwa anaumia kijana yule, kuanzia mwili, akili mpaka moyo.



    “Eddyyy.” Sauti kali iliita kwenye simu na kusababisha Eddy aangue kilio kwa nguvu zaidi ya mwanzo. Aliachia machozi yatiririke, aliona ni bora kulia kuliko kubana pumzi.

    Wanasema njia kubwa ya kupunguza maumivu ni kulia tu! Hata kama ulikuwa umeumizwa kiasi gani, lakini ukilia, maumivu yale hupotea mara moja. Uwe umeachwa, uwe umeiumizwa kwenye mapenzi au vyovyote vile, kulia pekee ndio njia rahisi ya kukata maumivu hayo kwa haraka.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Win. Kwa kheri mama. Kwa kheri mke wangu. Kumbuka nilikwambia kuwa siwezi kuondoka bila kukuaga. Mama nilimuaga, na sasa ni zamu yako Win…” Edson alijikaza na kutamka maneno hayo yaliyojaa uchungu mkubwa.



    “Eddy noo. Please. Huwezi kuondoka, huwezi nakwambia. Bado nakuhitaji mme wangu, bado mama anakuhitaji Eddy. Please. Fikiria hilo.” Alisikika Win akilalamika kwa uchungu kwenye simu.



    “Natakiwa kwenda Win. Unakumbuka Ganzi Ya Moyo?” Eddy alimuuliza Win na Win hakujibu lolote. “Hivyo ndivyo ilivyotokea kwetu. Kumbuka nakupenda sana tena sana. Lakini natakiwa kutangulia. Sijawahi kufanya lolote ambalo umelisikia, huo ndio ukweli wangu wa pekee.” Baada ya maneno hayo, Ibra alitoa sikioni simu ile na kisha akawa anasiikiliza Win anavyolalamika. Akaamua kuikata simu ile na kumuangalia Edson.



    “Bravo. (Hongera)” Maneno hayo yalienda sambamba na Ibra kupiga makofi huku simu na bastola yake vikiwa mikononi. “Lakini hamna jinsi.” Ibrahim bila kutegemewa na wengine wote mle ndani, alimpiga risasi ya kichwa Edson na mwili wa Eddy ukadondoka sakafuni ukiwa hauna uhai. Akaona haitoshi, akampiga risasi zingine za kifuani.

    Mwili wa Eddy ukawa umelala sakafuni damu zikiwa zimetapakaa mahali hapo kana kwamba kuna bahari kubwa ya damu.



    Maisha ya mwanadamu ni safari fupi sana ambayo huwezi kujua ni wapi itaishia. Nakumbuka wakati simulizi hii inaanza. Edson alikutwa na Win akiwa kajikunyata baada ya mvua kubwa kumnyea mwilini. Win akamchukua Edson na kwenda naye nyumbani kisha akampa huduma nzuri ya kutoa baridi katika mwili wake. Tabasamu la Edson, macho yake yalivyomwangalia Win, pamoja na matendo yake, yakamvutia Winfrida na kujikuta kwa mara ya kwanza anamvulia mwanaume nguo zake na kufanya naye mapenzi. Maisha yao yakawa ya furaha. Maneno ya ushauri toka kwa mama yake Eddy ndio yalikuwa chachu kubwa ya kudumisha penzi lao lililomea kama magugu maji.

    Siku zenye furaha zilitawala katika maisha yao ya mapenzi. Walicheza kwa pamoja katika jumba lao kubwa. Walikuwa kama watoto wadogo vile. Wafanyakazi walikuwa ni watu wa kucheka na kufurahia kila walipowaona wapenzi hawa wanavyobishana na kutaniana ndani mle.



    Yakaja mambo kubadilika baada ya FITINA kuingilia kati penzi lao. Mambo yalikuwa magumu sana kwao, lakini walipiga moyo konde na kusonga bila kuyafatilia mambo wanayoambiwa na binadamu. Kuna muda Win alikwishaanza kuamini maneno yale, lakini hakuwa tayari kumuacha Eddy, aliapa kuwa atambadilisha kama kweli anafanya vile.

    Ukapita ule wakati ambao Eddy alitekwa mara ya kwanza na kuachiwa. Na sasa ni wakati mwingine wa maumivu. Yote kisa ni mapenzi tu! Mapenzi ya wivu na fitina. Kama MUNGU angekuwa anamuonesha binadamu mambo yatakayomkuta mbele, Edson asingechagua kuanzisha mahusiano na Win. Lakini yote yanabaki kuwa ya MUNGU. Na kila siku atapishangiliwa na ataimbiwa kwa nyimbo nzuri zote. Muacheni MUNGU, aitwe MUNGU.



    MAPENZI ni nini? Furaha au maumivu? Maji au moto? Hilo ni swali ambalo hakuna anayeweza kulipa jibu sahihi. Kila mmoja atalijibu kwa njia yake. Utayalaumu mapenzi, lakini si ruhusa kuyalaumu bali laumu nafsi yako iliyokubali kuyaingia.



    Mwili wa Eddy ulikuwa chini kifudifudi huku macho akiwa bado kayakodoa. Alikuwa hana uhai Edson, mtoto aliyekulia kwenye maisha magumu sana. Lakini kabla hajafurahia maisha mazuri yaliyokuwa yameanza kumea hivi karibuni, uhai wake unaokotwa.

    Aaaah! MAPENZI, MAPENZI, MAPENZI, MAPENZI.

    MAPENZI NI NINI?







    “Umefanya nini bosi?” Baada ya kimya kifupi swali lilimtoka mtekaji mmoja na bila kufikiria, Ibrahim aligeuka haraka na kumpiga risasi yule bwana ambayo ilimkuta katika paji lake la uso. Jamaa akatokwa nauhai.

    Wakati wale wawili waliobaki wakiwa wanajifikiria, tayari Ibrahim alikuwa kawageukia nao akawapiga risasi. Mmoja alichukua ya kichwani na mwingine ambaye alitaka kukimbia, alijikuta akipokea risasi ya mgongoni ambapo ilitokeza kifuani. Jamaa alitulia tuli kana kwamba alikuwa amekufa.

    Ibra akamsogelea na kutaka kumpiga risasi nyingine ya kichwani lakini kwa bahati mbaya risasi zilikuwa zimekwisha na wakati huo kelele kadhaa zilikuwa zinasikika nje baada ya milipuko ile bastola ambayo ilikuwa imepaa hadi maeneo wanapoishi watu.



    “Utafia hapa, bwege wewe.” Ibrahim Singa akaondoka ndani ya nyumba ile haraka na kwenda kwenye gari lake ambapo wala hakuchukua muda, akaliwasha na kuondoka huku miili ya watekaji na Edson ikiwa inachuruzika damu.

    ****

    Watu waliokuwa wanaelekea kule milio ya risasi ilipotokea, walipishana na gari lakini hawakulitilia maani na badala yake wao walikuwa wanakimbilia huko wakiongozwa na Mjumbe pamoja na kundi la Sungusungu.

    Walifika katika eneo husika na ukimya uliopo ukawapa imani kuwa wamekwishachelewa sana kumpata mhusika wa milipuko ile. Wakaingia ndani na walichokutana nacho, hakika kiliwatoa machozi. Edson akiwa bado hajayafumba macho yake, akiwa bado mdogo kabisa, ndiye aliyewafanya wale wasamaria wema wadondokwe na machozi.



    Lakini kulikuwa hamna muda wa kupoteza, haraka simu ilipigwa polisi na wakati yanatendeka hayo, bwana mmoja aliokota simu ambayo ilitumiwa na Ibra kumpigia Win. Kulikuwa na simu karibu ishirini zimepigwa katika namba ile, lakini zote zilikuwa za mtu mmoja. Ndipo akakabidhiwa ile simu Mjumbe wa mtaa ule.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mjumbe hakuchelewa, akaipiga ile namba na moja kwa moja sauti iliyoitika upande mwingine ilikuwa ni Winfrida. Mwanamke yule alielezwa tukio zima lilivyokuwa linaonekana, na akaelezwa mtaa ambao tukio hilo limetokea. Mara moja Win alikata simu na kutoka nje ikiwa tayari ni saa nne usiku. Akakwea ndani ya gari na safari ya kwenda alipotaarifiwa kuwa mpenzi wake yupo, ikashika hatamu.

    ****

    Saa tano Win alikuwa eneo la tukio lakini alikatazwa kuingia ndani kwa sababu polisi walikuwa wakifanya uchunguzi wao. Hakuna mtu aliyeruhusiwa kuingia ndani kwa sababu hizo za polisi. Na hakuna mwili ulioguswa na yeyote, hata wale waliowahi kufika eneo la tukio hawakuthubutu kufanya hivyo ili kutopoteza ushahidi.



    “Kuna mmoja nasikia anapumua.” Ilikuwa ni sauti ya mtu mmoja pale nje na sauti hiyo ilipenya vema masikioni kwa Win. Win akajikuta anataka kujua zaidi ni nani ambaye anapumua, yawezekana akawa Eddy.



    “Afande. Mimi ndiye nilikuwa namtafuta kijana wangu aliyepotea siku tano za nyuma. Nimesikia yupo huku ndio maana nimekuja kumuangalia. Naomba unisaidie Afande.” Aliongea Win baada ya kuwa anarushwa roho na hadithi za nje.



    “Dada, subiri polisi wamalize kazi zao, halafu tutakuita uje utambue miili. Sawa dada, kuwa na subira tu.” Maneno yale yakamfanya Win atulie na kungoja hilo aliloambiwa na yule Afande.

    Akakaa pembeni na kuanza kusali sala zake zote ambazo alifunzwa katika maisha yake.



    Baada ya nusu saa, miili ikaanza kutolewa na hapo Win alinyanyuka na kwenda kwenye gari la hospitali tayari kwa kutaka kuiangalia miili ile. Ndipo kabla mwili mmoja mmoja haujaingizwa, ukawa unafunuliwa mbele ya Win.

    “Huyo simjui.” Aliongea Win baada ya kuona maiti ya kwanza. Ikapita miili miwili, mwili wa tatu ulipofunuliwa, Win alifikicha macho yake kwanza. Akashikwa na kigugumizi cha ghafla. Alitaka kuongea lakini hakujua aongee nini.



    Edson alikuwa amefumbwa macho yake lakini jeraha la risasi pembeni ya kichwa chake, lilikuwa linatoa damu iliyokuwa inachafua hadi kitanda cha kubebea wagonjwa.



    “Dada unamjua huyu?” Sauti ya askali, kitengo cha upelelezi ilikuwa inamuuliza Win ambaye alikuwa ameganda kwa muda huku haamini kile anachokiona.



    “Ni Edson huyu. Mzima au kafa?” Win alikuwa kaanza kama kuchanganyikiwa kwa jinsi alivyokuwa anaongea.



    “Hapana. Tumempoteza kijana. Mzima ni huyo hapo lakini hali yake naye ni mbaya sana.”Askari yule aliongea kwa taratibu huku akiamini Win atamuelewa lakini haikuwa hivyo, Win alianza kulia na kukataa katakata kuwa Edson hajafa.



    “Hapana MUNGU. Hapana, Eddy hajafa jamani. Nakataa Eddy wangu hajafa. Kwa nini afe sasa? Kwa nini afe eti hata kabla sijamuona mara ya mwisho? Eddy, haiwezekani Afande, haiwezekani nasema….” Kilio cha uchungu kilimtoka Win na kuwafanya eneo lile likumbwe na majonzi ndani ya dakika chache kwa sababu ya kilio chake.

    Kifo cha Edson kilikuwa ni cha kushtukiza sana katika maisha ya Winfrida, hakutegemea kama kijana yule anaweza kufa kwa wakati ule ambapo kama kumependa alikuwa kampenda sana tu!



    “Mchukueni. Mpelekeni sehemu salama.” Aliongea yule Afande na hapohapo polisi wawili walikuja kumtoa eneo la tukio na kuacha matabibu wakipandisha miili ya marehemu pamoja na yule majeruhi. Hali ilikuwa ya kusikitisha sana wakati Win alipokuwa anaondolewa eneo la tukio, alilia kwa uchungu aking’ang’ania kupanda gari lile la wagonjwa.



    “Dada twende kwenye gari lako tutaongozana nao hadi hospitali.” Aliongea kijana mmoja ambaye alikuwa amemuona Win wakati anaingia na gari lake.



    “Wewe unajua kuendesha gari?” Aliuliza askari mmoja na yule kijana aliafiki kwa kukubali kuwa anaweza kuendesha gari. Hivyo akawa msaada mkubwa kwa kuendesha gari la Win hadi hospitali. Akili ya Win ilipokaa sawa, alimpigia Ibrahim na kumpa hali halisi.



    Ibra alikwenda haraka eneo la hospitali na kumkuta Win amejikunyata kama kifaranga cha kuku kilichochapwa na mvua.



    “Vipi Win. Pole sana na msiba.” Ibrahim aliongea na hapohapo Win alinza kulia huku akilalamika na kuwalaani vikali waliofanya vile. Hakika alikuwa anauchungu na alihitaji faraja kubwa. Ndipo Ibra akamkumbatia japo harufu ya damu bado ilikuwa inanuka mwilini mwake, lakini Win hakujua kitu. Naye akamkumbatia.

    ****

    Win hakulala usiku uliopita na asubuhi alidamka mapema sana tayari kwa kuweka hali ya msiba nyumbani kwake. Tayari ndugu kadhaa walikwishafika na kumpa pole Win lakini walishindwa kwenda kwa Mama yake Eddy kwa sababu walijua itakuwa ngumu sana kwa mama yule kuelewa kilichotokea kwa mwanaye. Lakini Win alijikaza na kwenda hadi kwa Mama Eddy.



    “Mama shikamoo.” Alianza Win huku akijikaza asilie wala asioneshe hali yoyote ya msiba.



    “Marhaba. Vipi mnaendeleaje?” Mama Eddy aliuliza huku akiwa makini na uso wa Win. Win akakaa pembeni ya kitanda na kuanza kuongea na mama yule.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Mama. Katika dunia hii kuna mambo mengi sana ambayo mengine yana maana na mengine hayana maana. Yaliyo ya maana hayapewi nafasi kubwa kama yale ambayo hayana maana, lakini mwisho wa haya yote huwa ni sehemu moja tu! Kaburini.” Win akanyamaza nakumuangalia mama yule aliyekuwa kamakinika sana kumsikiliza Win. “Mauti humkumba kila binadamu na kila binadamu yatamkumba kwa mtindo wake na kwa muda wake. Hakuna ambaye atakikimbia kifo katika dunia ya leo. Kila kiumbe chenye damu na nyama, kitaonja umauti. Usisikitike sana mama endapo utapoteza yeyote katika hii dunia, ni MUNGU ndiye mpanga yote.” Bado mama yule hakuongea neno zaidi ya kuwa kimya akimuangalia Win. “Mama…” Aliita Win, “Eddy hatunaye tena.” Maneno hayo ambayo yalisindikizwa na machozi toka kwa Win yalipokelewa vingine na Mama Edson. Mama yule aliposikia mwanaye amefariki, mara alipandisha kifua chake juu huku macho kayakodoa, kisha akashusha pumzi ndefu ambayo ilifanya na kifua chake kushuka chini. Alibaki kakodoa macho na chozi moja jembamba lilitiririka kutoka kwenye jicho lake.



    “Mama…” Win alimuita yule mama. “Mamaa…” Aliita tena lakini mama yule alikuwa kabaki vilevile kakodoa macho. Mama Edson alikuwa kaiaga dunia kwa shinikizo la damu kutokana na taarifa alizozipata toka kwa Win. Hakuna ambaye angeweza kuzuia jambo hilo, ilikuwa ni lazima mama yule apewe taarifa. Hata kama ungetumia maneno matamu kama asali, lakini ukweli ungebaki kuwa Eddy amefariki.

    “Mamaaaaaaa…….” Win aliita kwa sauti ya kilio na hapohapo akadondokea mwili wa Mama Edson, Win akapoteza fahamu hapohapo.



    Alizinduka siku mbili mbele na kitu cha kwanza kilikuwa ni kuulizia Eddy na Mama yake. Ndipo akajibiwa kuwa wamezikwa. Win alilia sana tena sana lakini haikubadili ukweli kuwa watu aliowapenda kwa moyo wake wote alikuwa hawapo naye tena.

    ****

    Taarifa za kipelelezi zililetwa na ilijulikana kuwa Ibrahim ndiye aliyoyafanya yale yote baada ya vidole vyake pamoja risasi zilizokutwa mwilini mwa marehemu wote kuwa moja kwa moja ni vyake. Alikamatwa na kuwekwa mahabusu. Walipopekuwa ndani kwake, walikuta bastola iliyotumika.



    “Kwa nini umefanya haya Ibra.” Win alimuuliza kwa uchungu sana Ibrahim ambaye sasa alikuwa anajutia yote aliyoyafanya.



    “Mapenzi Win. Ni mapenzi...” Ibra alijibu huku analia na kumfanya Win apandwe na hasira atamani hata kumpiga lakini alizuiwa na wazu ambao ulikaa katikati yao wakati wa maongezi.



    “Mapenzi? Mapenzi ni nini wewe mpumbavu hadi ufikie hatua ya kuwaua watu wangu muhimu? Watu walionipa furaha maishani mwangu. Mapenzi ni nini?” Win aliuliza kwa chuki zilizomjaa mwili mzima.



    “Sijui mapenzi ni kitu gani.”



    “Na kweli hujui mapenzi ni nini ndio maana umekurupuka. Ahsante Ibra kwa malipo yako. Ahsante baba.” Win alisimama na kutoka nje ya kituo cha polisi ambapo alitaka kuongea na Ibrahim.



    Alipotoka hakujua anataka kwenda wapi au anataka afanye nini. Alijikuta kasimama mlangoni akiwa hana nguvu za kuamua walakufanya lolote.



    “GANZI YA MOYO.”Win aliongea peke yake maneno hayo. “Ganzi ya Moyooooooo.” Win alipayuka maneno hayo na mara hiyohiyo akaanza kuvua nguo zake na mwishowe akabaki hana vazi lolote. Wanawake wenzake walijaribu kumstiri lakini haikuwezekana, kila ambacho alikuwa anavalishwa, alikivua huku wimbo wake mkubwa ukiwa ni GANZI YA MOYO. Win alikuwa kichaa ghafla. Ni jambo la ajabu na la kusikitisha sana. Mapenzi haya, tuyaache yaitwe mapenzi tu!



    Ilibidi wamkamate na kumpeleka hospitali. Huko ilionesha kuwa amepatwa na kichaa na tiba ya ugonjwa huo, inapatikana Hospitali ya Milembe Dodoma na Muhimbili. Lakini ilibidi apelekwe Dodoma baada ya Muhimbili kushindwa. Hali ilikuwa tete kwa Winfrida.



    Milembe walikuwa wanampa vidonge na sindano za usingizi ili asiwe msumbufu, lakini alipozinduka, hali ilikuwa vilevile. Wimbo wa Ganzi Ya Moyo ulikuwa unaimbwa sana kinywani mwake.



    Hatimaye ikawadia siku ya siku ambayo kila mwanadamu hapendi wala hataki kuifikiria siku hiyo. Ni siku ambayo si mimi wala mtu yeyote anaitamani.

    Win aliruka uzio wa hospitali ile na kuanza kukimbia kwa kasi kuelekea mjini huku akitamka maneno kwa sauti kubwa. “GANZI YA MOYOOOO”. Lakini kwa bahati mbaya maneno hayo hayakuenda hadi mwisho, gari kubwa la mchanga, lililokuwa linakwenda kasi, lilimgonga Win na kumpaisha mbali sana. Alipotua chini, kichwa chake kilikuwa kimepasuka huku barabara ikipambwa na damu yake pamoja na ubongo.



    Hakuna binadamu ambaye anaombea siku hii inayoitwa mauti. Nasema tena, HAKUNA anayeipenda siku hii. Win hakuwa tena duniani.

    ****

    Upande wa Ibrahim Singa. Alifungwa kifungo cha maisha jela baada ya kukiri makosa yake japo ndugu zake walimuwekea mawakili nguli katika dunia hii. Na iligundulika kuwa alitumia madawa ya kulevya siku wakati anafanya mauaji yale. Ibra akahukumiwa kifungo hicho wakati huo alikuwa kapata taarifa kuwa Win kawehuka punde tu alipotoka pale kituoni kuongea na yeye.



    Siku ya pili ya kifungo chake, alikutwa amejinyonga ndani ya gereza alilofungwa kwa kutumia shuka alilolifunga kwenye kitanda cha juu. Mezani aliacha ujumbe wa karatasi ambapo aliomba kalamu ili aundike. Ulisome maneno machache.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Mara ya mwisho Edson aliongea na Win. Kisha akafa kwa mimi kuuchukua uhai wake. Mtu wa mwisho kwa Win kuongea naye akiwa timamu, alikuwa ni mimi. Mama yake Edson aliongea na Win mara ya mwisho kabla hajafa. Hakika mwanamke huyu kapitia GANZI YA MOYO. Nisameheeni wapendwa.” Ujumbe ulisomwa hivyo baada ya mwili wa Ibra kukutwa hamna uhai.



    IMEANDIKWA HIVI: Maisha ya mwanadamu katika dunia hii ni mafupi sana. Ukipenda yafurahie ukiwa nayo kwa sababu wakati wewe unatembea ukiwa na amani tele, wapo wanaokuwinda kama swala aliyenona. Maisha si yetu. Tumuombe MUNGU kila siku za uhai wetu kwa sababu pumzi unayovuta sasa, si yako na kamwe haitokuwa yako. Maisha ni safari ambayo mwisho wake huwa mauti.



    MWISHO.







0 comments:

Post a Comment

Blog