Simulizi : Ganzi Ya Moyo
Sehemu Ya Nne (4)
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Nasema hivi, hata kama ungeniahidi dunia yote iwe mali yangu, sipo tayari kuwa na wewe kwa sasa na labda daima. Si kwa sababu sihitaji mali zako, bali pia sina sababu za kukuhusudu, kwani kipendacho roho ni thamani ya moyo. Upo hapo Ibra?” Win alimuuliza mwanaume yule lakini hakumpa nafasi ya kujibu swali lake, akazidi kukomelea maneno yake aliyoyakusudia. “Nayasema haya yote toka mtimani na wala siongopi kwa sababu sipo hapa kwa hilo. Nakushauri tafuta mwingine kwani ni wengi tu wapendao vidani vya dhahabu, hereni, mikufu na gari za kutembelea. Lakini miye Win,” Akajitazama binti yule kama vile anajishusha thamani, kisha akaendelea, “Ni lofa. Ila Edson mwana wa Lake tu, ndiye chaguo la Winfrida.” Sura ya Ibrahim ikabadilika zaidi baada ya kumsikia Win akitamka hayo, lakini alijikuta akiacha mdomo wazi pale alipoyasikia maneno ambayo Win alizidi kuyatamka, “Eddy, upo wapi kijana wewe? Ninavyokuhusudu ni kama chai ya rangi uswahilini. Ungejua, usingetokea katika maisha yangu, lakini sina jinsi, maisha yangu yote nakukabidhi. U-wapi kipenzi changu? U-wapi nakuuliza? Potelea mbali hali yako ya kifedha, lakini ipo siku, tutafurahi pamoja.” Maneno hayo yalikuw yanamtoka Win ambaye alikuwa kafumba macho yake na hisia kali zikitawala kichwani kwake, hakika binti huyu alikuwa kazama kwenye dimbwi zito la mahaba.
Ibra ambaye alikuwa haamini kile anachokiona na kukisikia, alijikuta mwenye kutikisa kichwa kwa masikitiko na asijue ni vipi anaweza kumshawishi mwanadada yule aelewe kile kilichokuwepo moyoni mwake.
“Looh! Ama kweli nimeamini kuwa hasidi chakula chake ni asidi. Na uzuri wako wote huo, Win veje unampenda kijana wa manati kama Eddy? Huoni kuwa hakufai? Hebu tazama ulivyonyororo, utaweza kweli siku akikuambia acha mali zako zote twende tukashike jembe? Tazama nywele zako laini juu ya kichwa chako dhaifu cha kupendeza, kitaweza weka kuni mkiamua kwenda kuishi kijijini kwao? Tazama pua yako ya Kimanga, macho ya kigoroli na midomo ya kitoto, itaweza kuhimili kweli moshi kwenye jiko chakavu?” Ibrahim aliongea maneno ambayo ama hakika yalikuwa kama kituko mbele ya Winfrida aliyekuwa ndani ya penzi zito na kijana Edson. Ibra alizidi kumfungua kichwa Win lakini hakikufunguka athilani. “Tazama rangi yako ya ki-mirinda, makalio ya kisambusa, tumbo la kibamia, shingo ya kitausi na miguu ya kimataifa. Je? Vyaweza kuhimili safari ndefu ya kwenda na kurudi toka shamba, vyaweza kuhimili vumbi la nchi yetu? Angalia juu ya maisha bora Win, usijekujutia baadae, muda ndio huu. Mwili wako haupaswi kuingia kwenye maisha kama kaburi, penda aliyenacho ili uzidi kuwa nacho kwani asiyenacho hathamini, unajishusha Win.” Alimaliza Ibra na kumuangalia Win kama anaelekea kwenye mtego wake.
“Eddy hanitoki wala simtoi kamwe moyoni mwangu, hata machoni pangu. Sishangai kwa nini, lakini nashangaa kwa sababu nimempenda kabla hajaniambia lolote. Amejaa pomoni rohoni mwangu, kila tone la damu linapoungana na jingine na kutengeneza mzunguko kamili wa damu, ni Eddy. Ni Eddy tu rohoni mwangu, nashindwa kutumia uma kwa sababu nimekubali umasikini alionao Eddy. Loh! Eddy mwana wa Lake, ama kweli we ni Lake (Ziwa) kwangu. Nimezama ndani yako, na sihitaji kukombolewa na yeyote. Nakupenda na nakuthamini kuliko hata jicho langu. Angalia thamani yake kwangu, tafadhali Ibra. Mimi pia ni mwanadamu nimezaliwa, udhaifu wangu kwa Eddy ni sawa na ule wa mwendawazimu kwa uchafu. Kheri kuwa vyovyote kuliko kukosa Edson Lake.” Maneno hayo hayakumfanya Winfrida asimame na kuondoka, la hasha! Ni kama hakumaliza maongezi. Aliendelea kukaa na ndipo nafasi ya kuongea aliichukua Ibrahim Singa.
“Nashangaa sana Win, kwa nini u-mgumu kuenilewa. Chachu ya roho yangu, yazidi ile ya ndimu juu yako. Win, nilitegemea rehema kubwa kubwa toka kwako, tamu zaidi ya chochote toka kwako. Pendo langu kwako, limenikoroga bongo yangu na kuniacha nusu uchi, ni neema zako tu! Zinaweza kunisitiri, sina jingine juu yako. Ila naomba niwe wako. Nipo tayari kutoa chochote na nipo tayari kuwa vyovyote kwa ajili yako.” Safari hii Win alimtazama kijana Ibrahim kwa huruma yenye uchungu, kisha akabinua midomo yake iliyonakshiwa kwa rangi nyeusi kwa mbali.
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Nasikitikika na kukushangaa sana Ibra, kwani naona hujanielewa. Uchungu wa mwana……. Aujuaye ni mzazi. Potelea mbali matatizo ya kimaumbile. Mimi na Eddy ni sawa na ulimi na mate, penzi langu kwa Eddy ni sawa na sehemu mojawapo ya kiungo changu. Damu yangu yote imejaa Eddy tu. Hivi Ibra? Hadi hapo hujanilielewa tu kuwa sikuhitaji, sikutaki wewe kuwa mpenzi wangu? Penzi halilazimishwi, penzi ni kama pete, kama haikutoshi, achana nayo.” Ibrahim alivuta pumzi na kuzishusha kitakatifu.Macho yalikwishaanza kumuwiva na kunyong’onyea kama kuku aliyejua kuwa anataka kuchinjwa. Hali ya kukata tamaa tayari ilikwishaanza kujionesha dhahiri machoni pake. Alibaki akimtazama mtoto Win kwa jicho la huruma na unyenyekevu wa kikondoo huku machozi kwa mbali yakianza kumtiririka lakini alijikaza kisabuni akisubiri tamko lenye nguvu toka kwa Win. Pengine alifikiri kuwa majibu aliyojibiwa yalikuwa ni danganya toto, kutokana na walipotoka yeye na Win.
“Win, tuache utani. Tuzungumze kwa kina juu ya suala hili. Tuache lugha za Kiwahili-swahili ingawa utani hujenga undugu. Win, mwenzako nimeelemewa sana juu ya penzi lako, penzi zito lisilopimika katika mzani, penzi lenye kila aina ya bashasha, penzi takatifu lenye baraka na neema zote toka kwa wazazi wetu, penzi litakalozidi kukugeuza Win kuwa Malkia wa wapendanao. Sijui nikupe dawa gani Win ili uwezenijaza pomoni katika roho yako. Sijui niweze nena nini ili unielewe. Maneno yako ya awali ni sumu ya roho yangu ingawa naelewa kuwa Win huwezi nitia kapuni. Samahani Win, sema nikuelewe.” Baada ya maneno yenye chachu toka kwa Ibrahim, Win aligeuza shingo yake ya kitausi taratibu na kumtazama kwa kinyaa kijana nadhifu na mtanashati, si mwingine ni Ibrahim.
Sauti nyororo mithili ya ute wa yai ikapasua kinywa chake, “Umemaliza?” Ibrahim hakujibu lolote ila sura ya uchovu ilijichora. Taratibu Win aligeuza sura yake hadi bega la kushoto na kufanya kitendo ambacho kamwe Ibrahim hakuwaza kuwa atakuja kufanyiwa na Win. Win alitema mate kwa kinyaa, “Nitatapika.” Na kunena kwa dharau.
“Win, nini umefanya?” Kwa mshangao Ibra alimuuliza Win. Wakati akimshangaa akajikuta anadondosha chozi. Hakika alikumwa na fadhaa mwanaume yule. “Leo hii wewe wa kunitema mimi? Kwa kosa gani yaani? Kwa sababu nimekupenda Win? Ni kwa sababu mimi ni pete isyokutosha? Win? Kweli Win unanifanyia haya mimi? Aaah! Siamini kabisa.” Akaongea kwa masikitiko Ibrahim.
Win akatabasamu na kumuangalia tena Ibrahim alivyopaa kwa kile alichooneshwa na Win muda mfupi uliopita. Win akiwa na tabasamu pana, akatikisa tena kichwa masikitiko.
“Pole sana Ibra, pole we…., nakuonea huruma we…. mpaka nasikia kinyaa kutokana na shombo chafu ya maneno yako.” Ibra akapunguza munkari baada ya kugundua ni maneno yake yaliyomfanya Win afanye kile kitendo. Akakaa kimya na kumsikiliza mwanamke yule, “Ibra, nielewe sasa….. mimi sikupendi kabisaaa, tena wapoteza muda wako bure kutaka mimi niwe mpenzi wako. Sikupendi na sina haja na wewe. Nikupende kwa nini sasa? Pesa!?” Win hakusubiri ajibiwe swalio hilo, akazidi kumnyambua Ibrahim, “Sina haja na pesa, kwanza sikuzaliwa nazo ila jina Eddy, nimezaliwa nalo na lipo damuni. Kila kunapotokea mdundo mmoja wa moyo, roho ulipuka kwa sauti za Eddy, Eddy, Eddy nyingi. Halafu, wanawake wengi sana siku hizi, au vipi Bro Ibra? Pesa ndio tatizo lao, mbona upo nyuma sana Ibra? Toka lini sifuri ongeza sifuri ikawa nne? Toka lini mali ongeza mali ukasaidia masikini? Hiyo ni kuwabana wasiyo na kitu kama Eddy wangu kukosa msaada,” Ibra akainamisha kichwa chini na ni wazi alikuwa anaanza kukata tamaa hasa kwa maneno yenye nguvu toka kwa Winfrida. “Najisikia vibaya sana neno Win linapotoka kwenye mdomo wako, mbaya zaidi mimi ni kama dada yako lakini unanitaka kimapenzi. Au wewe Shetani mahaba nini? Sipendi kusikia unamsemea vibaya Eddy, sijui masikini, mara kijijini mara sijui nini. Sipendi kabisa sauti yako, naweza hata kuharisha ukiendelea na huo ujinga.” Ama kwa hakika Ibra alikuwa kakutana kisingi cha mpingo. Na safari hii, nadiriki kusema kuwa Ibra alikutana na maneno makali kuliko kipindi chochote cha maisha yake.
“Win kwa nini unanifanyia mimi hivi? Embu niangalie mwenzako navyolilia penzi lako. Hivi kweli upo tayari kabisa kusema hunitaki kwa sababu ya kale katoto? Kweli Win? Ni kweli kabisa hunitaki kwa sababu ya mtoto wa Sekondari?
Atakupa nini yule anukaye maziwa? Atakupeleka wapi yule asiyejua kuoga? Kwa nini Win? Embu niangale mimi. Niangalie vizuri tena.
Hivi mimi naweza kukutenda kweli Win hadi utoe uaminifu wako kiasi hicho juu yangu na kumpa yule mtoto mdogo? Kwa nini unanitesa namna hiyo? Ona navyokonda kwa mawazo tukufu juu yako. Ona chozi langu hadimu kuliona linavyotiririka kutoka kwenye mboni zangu. Ona sura yangu ilivyokuwa ndogo kwa ajili ya kusinyaa kwa machungu juu yako.
Niangalie Win, usithubutu kuangalia chini wala pembeni hata kidogo. Niangalie hata mavazi, kweli mimi ni wakuvaa hivi Win? Kweli kabisa unanikataa mimi kisa yule mtoto?” Ni sauti yenye uchungu ilikuwa inamtoka Ibrahim bila kutambua kuwa maneno yale, Winfrida alikuwa hayataki si kuyasikia tu! Bali kuyaona na kuyagusa. Yalikuwa ni machafu kuliko uchafu wa mariwatoni.
“Naona hunielewi, nisikilize sasa Ibra. Tena nisikilize kwa umakini mkubwa. Utoto wa Edson naujua mimi si wewe. Utamu wa Edson naufahamu mimi, si wewe mkurupukaji, uliyetoka huko na kuanza kukashifu watu. Hujui kuongea na mwanamke, hujui kubembeleza bali kulia na hujui kuomba bali kulazimisha.
Mimi ni mwanamke, tena mwanamke shupavu. Nisiyetishwa na mavazi, fedha, mali na hata sura ya mwanaume yeyote katika dunia hii. Mwanaume nimpendaye, ndiye mwanaume anayenijali na kuwa muaminifu kwangu.
Ufukara wake, mavazi yake, umbo Lake, maisha yake na elimu yake, kwangu si kitu ili mradi nimempenda na nipo tayari kwa lolote kwa ajili yake. Nipo tayari kumgharamikia mavazi, chakula, elimu, malazi, miundombinu na mambo yote muhimu uyajuayo kichwani mwako. Na zaidi ya hayo, nipo tayari kufa kwa ajili ya Edson.” Maneno ya Win yalikuwa yanatoka kwa mpangilio kinywani mwake na kumfanya Ibrahim abaki kinywa wazi. Win alizidi kutiririka hisia zake, “Ooh, Edson Lake, fahari wa moyo wangu, fahari wa maisha yangu, fahari wa furaha yangu. Uko ulipo nadhani MUNGU anakuangazia mwanga wa amani ili uione sura yangu ambayo siku zote naitunza ili iwe kama ulivyoiona mwanzo. Oooh! My sweetie, nadhani upo salama.” Macho ya Win yalikuwa yamefumbwa wakati maneno haya yanamtoka na wakati huo, mikono yake alikuwa kaifumbata katika kifua chake kuonesha yupo katika hisia kali.
“Embu ona ulivyokuwa Win, ni kama na wewe umekuwa mtoto. Yule wa nini Win? Eeh, nakuuliza Win, yule wa nini? Atakupeleka wapi katika maisha haya ambayo kila neno ni fedha? Atakuja kukudharau bure baada ya kumfanikisha. Njoo kwangu Win ili ujue thamani ya fedha, thamani ya upendo, thamani ya furaha, thamani ya pumzi yako, thamani ya elimu yako na thamani zote ulizonazo.
Mimi ndiye nikupendaye kwa dhati, mimi ndiye nijuaye maumivu yako Win, mimi ndiye nayejua utakacho Win, mimi ndiye mwenye kila hali ya kukwambia nakupenda, na mimi ndiye mwenye uwezo wa kufanya chochote kwa ajili yako. Nakuomba Win, kuwa na mimi japo katika wakati huu wa mwisho wa hii dunia, japo na mimi hata nikifa niende kumpa taarifa Mzee Singa, baba yangu huko alipo kwa kumwambia nimekufa huku nampenda mwanamke wa furaha yangu, mwanamke wa maisha yangu, mwanamke aliyeteka hisia zangu, mwanamke aliyechukua moyo wangu na kukaa nao na mwanamke pekee mwenye uwezo wa kunifanya niache yote na kumsikiliza yeye.” Alizidi kutema cheche zake Ibrahim, muda huo hata juisi aliyoagiza ilikuwa chungu kupita kooni.
Win alitabasamu kwa tabasamu lililodumu kwa sekunde mbili na kisha akafungua midomo yake mipana na legevu yenye kila hamasisho la kumfanya mwanaume yeyote atake kuzibusu au japo zitawanyike kwenye paji lake la uso.
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Sikiliza Ibra. Na safari hii nisikilize kwa ubora kuliko kunisikiliza kwa makini. Mapenzi si kwa sababu tu! Yapo ndiyo tuingie, na wala si kwa sababu yameumbiwa binadamu basi na mimi nijilazimishe kupenda. Mapenzi ni kama pete Ibra, nimekwishakwambia hili hapo kabla, kama haikutoshi achana nayo.
Na kama si imara, hata ikikaa kidoleni itavunjika na kama umetengenezea madini dhaifu itachakaa mapema sana, tena sana.
Hivyo ndivyo itakuwa kati yako na yangu kama tukiwa wapenzi. Kwanza mapenzi yetu hayatutoshi, mimi na mali na wewe una mali, nani amsadie mwenzake? Muache masikini kama Edson wangu naye afaidi uwepo wangu, nampenda sana Edson, Ibra. Nikiwa ndani ya penzi na wewe, kamwe halitodumu, litakuwa kama ile pete iliyotengenezwa kwa madini dhaifu.
Nakuona kama kaka yangu Ibra, sina hisia na wewe kabisa. Lazima mapenzi hayo yatavunjika. Na hata nikijilazimisha kukupenda, mwisho wa siku nitarudi palepale kuwa sikupendi. Na mapenzi hayo yatachakaa kwa kuwa hayakuandaliwa maandalizi yaliyo-bora kama inavyotakiwa.” Maneno yalikuwa mengi sana kati ya Winfrida na Ibrahim. Na wakati wanaendeleza maneno hayo, ujumbe mfupi ukaingia kwenye simu ya Winfrida.
Mwanadada yule alitabasamu baada ya kugundua ni Edson ndiye alituma ujumbe ule. Lakini tabasamu lake halikuwa tu kwa sababu ni Eddy, bali liliongozwa na utamu wa ujumbe ule.
U-hali gani faraja yangu
Pumziko la moyo wangu
Fikra za kichwa changu
Tamu yangu isiyo na chungu
U-salama kwa kudra za MUNGU
Naamini ulipo hamna hata ukungu
Najua hilo, na ndio tegemeo langu
Natamani kukuona mpenzi wangu
Nipo salama pia mke wangu
Usidhani nimesahau kukujuza yangu
Nipo njiani narudi kwangu
Najua umefurahia neno la mwisho (Kwangu)
Ujumbe kama huo, hakika ungemfanya mwanamke yeyote atabasamu peke yake. Ndivyo ilvyotokea kwa Winfrida. Alitabasamu hasa mstari wa mwisho. Siku zote Win alikuwa akimsisitiza Eddy aseme kuwa anarudi kwake na si kwa Win au kwa mtu fulani. Win aliamini kuwa pale ni nyumbani kwa Eddy, hivyo haipaswi yeye kusema narudi kwako au nyumbani balia aseme narudi kwangu.
“Nakuja kukufuata mpenzi.” Alipomaliza akaiweka simu yake mezani, na kunyanyua macho yake tulivu kabisa. Macho yenye sifa ya kuitwa macho. Macho yenye kila hali ya matumaini ya kupendwa na kupenda katika dunia hii. Macho legevu mithili ya yule mtu ambaye anaumwa nusura ya kufa. Macho ya uviringo kama goroli na makubwa kiasi na yenye kupambwa rangi ya ghali kabisa kutokea kwa mwanamke hapa nchini Tanzania, macho yenye rangi ya kahawia. Aliyainua kumuelekezea Ibra, na bila kusita alimuomba samahani kwa kilichotokea kisha akampa ruhusa ya kuendelea kuongea.
“Ndiyo hivyo Win.”Kwa mfadhaiko na unyonge mkubwa, Ibra alisikika katika ngoma za masikio ya Win.
“Mimi si mwenye dhambi kwa kusema nakupenda wewe, ila mimi ni mwenye dhambi kwa sababu nimekupenda wewe. Pendo ambalo nitakuwa tayari kufanya chochote ili mradi uelewe ni kiasi gani nakupenda, kiasi gani nakuhitaji, kiasi gani upo moyoni mwangu na kiasi gani umeteka fikra zangu.” Aliongea Ibra safari hii kwa kifupi zaidi na kunyanyua glasi yake ya juisi ambayo ilikuwa imefunikwa vizuri ili nzi na wadudu wengine wasipate kutembelea na kuchafua kimiminika kilichomo humo.
Win akamtazama mwanaume yule na kabla hajamjibu lolote, simu yake ikaita tena kwa mlio kama ule wa mara ya kwanza. Ulikuwa ni ujumbe mfupi kutoka kwa Edson Lake. Akaufungua na kwa tabasamu lilelile, akabonyeza vitufe kujibu ujumbe ule. Ujumbe wa Edson ulisomeka hivi.
Nakusubiri wangu wa moyo
Penzi ni doa usinipe jakamoyo
Nipe lote tena bila ya choyo
Usichelewe kuja napiga mwayo
Nashindwa nikuambie kipi kizuri
Ila sitafanya mapenzi yawe shubiri
Yetu yawe yetu tuyafanye yawe siri
Wanafki wa nje waambulie sifuri
Naimani penzi litakuwa takatifu
Ndoa yetu itapitia dini zetu tukufu
Tutafuata ushauri kuhusu uaminifu
Hakika kati yetu hakutokuwa na mchafu
Kumbuka kati yetu hamna mkamilifu
Turekebishane tusipopita panyoofu
Maneno ya nje tuyakimbie kama wafu
Tusiwaangalie, mapenzi kwetu yawe upofu
NAKUSUBIRI.
Ujumbe wa Eddy uliishia hivyo na Win akajikuta akijibu “Nakuja” huku tabasamu lake likizidi kurindima katika uso wake. Akamtazama Ibrahim na kumuomba radhi tena. Kisha akatumia njia hiyo kumuaga.
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Unajua nini Ibra, mimi kwa sasa siwezi kukujibu swala lako kwa kuwa nina mengi ya kuyafikiria na mengi ya kuyafanya. Umeniambia mengi yanayoweza kumfanya mwanamke yeyote dhaifu na asiye dhaifu kukuelewa na kukusikiliza ombi lako. Najua upo kweli katika uongeacho, hivyo na mimi nitakuwa kweli kwa nitakachokujibu. Naomba unipe muda wa kufikiria jibu sahihi la kukupa ili na wewe uridhike na kujiona mwanaume uliye-bora katika dunia hii. Naomba uniache mara moja niende, halafu nikifikiria cha kukujibu, nitakutafuta.”Alimwambia hivyo Ibra huku macho yake yakiwa hayana mgomo na kwepa-kwepa kwenye uso wa Ibra, ambaye baada ya kusikia hivyo alivuta pumzi ndefu na kuishusha kama katoka kushusha magunia mazito Kariakoo.
Licha ya kugundua kuwa hana chake, Ibrahim alijikuta akimruhusu Winfrida aende anapohitaji huku akimsisitiza ampe jibu mapema pale atakapofikiria.
Win alinyanyuka taratibu na kuanza kuondoka kingamia, macho yakiwa yamemwiva kwa sababu ya kuongea. Minenguo ya kiuno chake na mimeng’enyo ya jungu lake, lilimfanya kila mtu kutoa pongezi kwa Muumba. Ibra alibaki akishangaa hadi kudondosha denda la uchu huku akiijutia bahati yake. Alitikisa kichwa kwa huzuni na uchungu huku akimsindikiza Win kwa macho ya tamaa. Akafikicha macho yake na kusema, “Ee Mola nimekukosea nini kiumbe wako dhaifu? Nausubiri utukufu wako”. Alitikisa kichwa na kujishika tama kwa unyonge na wakati huo Win alikuwa amekwishotoweka kabisa katika peo za macho ya watu waliokuwepo eneo lile.
****
Safari ya Win iliishia shuleni anaposoma Edson ambapo hapakuwa mbali sana na pale ambapo alikuwepo. Breki ya gari ilifunga mbele ya Eddy na Edson alitabasamu kwa tabasamu ambalo hakika lilinakshiwa kwa furaha na amani tele.
Kioo cha gari ambacho kilikuwa cheusi tupu, kilifunguliwa na Win alitoa uso wake mwanana na kumuita Eddy kwa furaha. Kijana wa watu akaelekea upande mwingine wa gari na kuingia. Akaweka begi lake la madaftari kwenye viti vya nyuma na kisha akamgeukia Win ambaye alikuwa amekaa nyuma ya usukani. Win alikuwa akimtazama bila kuongea neno lolote.
“Twende sasa nyumbani.” Edson aliongea huku tabasamu pana likiwa limechanua usoni pake baada ya kuona macho ya Winfrida yakiwa yanaongea lugha fulani ya upendo, kujali na mapenzi.
“Kwa hiyo nikikufuata kila siku itakuwa hivi?” Aliuliza kwa deko Win?
“Kivipi jamani mke wangu na wewe.” Eddy aliongea kwa utani huku akishika mashavu mwanana ya kimwana Winfrida.
“Yaani hata busu hamna.” Win akazidi kudeka.
“Ahaaa! Usijali.” Eddy alikuwa haraka sana kutimiza kila neno ambalo alihisi Win analihitaji kuliko chochote.
Akashika shingo ya Win na kumvuta kwake kidogo, kisha akambusu busu nyevu (busu la ulimi). Winfrida alikuwa kama kichaa pale ulimi wa Eddy ulipokuwa ukiingia kwenye kinywa chake na yeye kuudaka na kuutendea haki. Na raha zaidi alikuwa akiipata pale anapompa ulimi wake Eddy na Edson anapounyonya kwa staha huku meno yake makavu yakiwa kama yanaung’atang’ata ulimi wa Win. Hakika msichana yule alipatikana kwa Edson. Na si kama Edson alikuwa hampendi, la! Kijana yule alikuwa chizi mara zaidi ya Win. Alikuwa hawezi bila Winfrida na Win alikuwa hawezi bila Edson.
Hakika umebarikiwa.
Ujuzi umepewa.
Najihisi mwenye mbawa.
Napaa nikiwa nimechachawa.
Sijui pa kutua
Na sihitaji kutua
Raha umenipatia
Mwili wangu umezisikia
Maneno yalimtoka Win baada ya ndimi zao kuachana na Edson alijikuta akitasamu baada ya kusikia maneno yale toka kwa Winfrida.
“Na wewe umeshaanza kuwa mtunzi wa mashairi eeeh! Basi nitabadilisha, sitatumia tena mashairi kwa sababu tayari umeshayajua.” Aliongea Edson baada ya shairi hilo fupi toka kwa Win.
“Ndio maana yake, nimekaa karibu na Waridi, wacha tu ninukie. Ukibadilisha, nitakufuata napo hadi niweze.” Aliongea Win kwa furaha huku akipasha mashine ya gari lake moto na kuliingiza barabarani tayari kwa safari ya kurudi wanapoishi.
****
Zikapita siku kadhaa, hatimaye wiki na mwezi ukakatika bila Ibrahim kupata mualiko wowote toka kwa Win. Kila alipojaribu kuwasiliana na mwanamke yule, aliambulia majibu ya kuwa ‘bize’ na mara hana nafasi kwa sababu kazi zimenibana.
Ibra alikuwa akishusha pumzi ndefu na kama mapenzi ni moto, basi huyu alikuwa anaungua ndani yake. Ibrahim alikuwa kama chizi wa mapenzi mbele ya Winfrida, lakini Win yeye alikuwa katika hali hiyo kwa mtu mwingine kabisa, namzungumzia Edson Lake.
Hakuna asiyependwa katika hii dunia, lakini hamna anayejua ni nani anayempenda au anapendwa na nani. Na mara nyingi katika hili, unakuta yule unayempenda, yeye hakupendi na yule anayekupenda, wewe humpendi. Mwisho wa siku unajikuta umeoa au umejiingiza katika mapenzi na mtu ambaye hukuwahi kufikiria kuwa ipo siku utampenda au atakuwa mpenzi wako. Hayo ndio mapenzi, na ndivyo yalivyo.
Lakini kama umependa pale ulipopendwa, yaani moyo wako umedondokea sehemu ileile ambayo ulikuwa umeipanga, hapo sasa ndipo tunapaita ubavuni. Huyo ndio wangu wa ubavu. Maneno kama hayo yanasikika kwa wale ambao wanapendana na wameshibana.
Hilo ndilo lililopo kati ya Win na Eddy. Walikuwa wameshibana na kulikuwa hakuna cha kuwatenganisha zaidi ya kifo, wao walinena hivyo kila walipokuwa wanayaongelea mapenzi yao. Na mara nyingi wakiwa katika mazungumzo ya kujenga penzi lao zaidi ya hapo, basi hujikuta wakibingilishana kitandani huku miili yao ikiwa inanena lugha moja ya kimapenzi.
Lakini wakati wao wanabilingishana kitandani kama majongoo yanayopigana kwenye nyasi zinazoteleza, yupo ambaye alikuwa anaumia sana kila anapofikiria ni wapi katoka na mwanamke yule na sasa kaporwa na mtoto wa shule. Inauma sana tena sana hasa pale unapoona mtoto uliyemzidi kwa kila kitu, yeye kakuzidi kitu kimoja tu ambacho kwako ni kikubwa kiasi kwamba ukichanganya vyote ulivyomzidi, haviwezi kulingana na hicho alichokuzidi. Ibrahim alizidiwa na Eddy kuushinda moyo wa Win.
“Mkuu, huyu dogo nataka umuoneshe kuwa kaingia choo kibaya. Mfanye vile nilivyokutuma.” Sauti ya Ibra ilikuwa inatoka kwaukali kidogo mbele ya mwanaume mmoja mwenye mwili wa mazoezi.
“Usitie shaka kaka. Kajitakia mwenyewe, acha akione.” Alijibu yule bwana aliyekuwa kaivuta mawani yake hadi katika paji la uso.
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
FITINA.
Wivu ni kipande kidogo sana cha damu ambacho kinajikita katikati ya moyo. Na jinsi damu hiyo inavyozunguka katika mwili wa binadamu, basi kipande hicho nacho hukuwa taratibu na baadae kusambaa mwili mzima. Kikishasambaa kwenye mwili, basi huzaa FITINA.
Ibrahim alimuonea wivu Eddy kwa kuupata moyo wa Win. Wivu huo haukuwa na manufaa hata kidogo kwani badala ya kujenga ushindani na yeye apate kama kile mwenzake alichokipata, basi wivu huo kwake ulijenga chuki dhidi ya Eddy. Ndipo akapanga kumuadabisha kijana wa watu. Yeye alisema kumuadabisha kwa sababu ya yule kijana kumchukua mwanamke wake. Lakini haikuwa hivyo, Win ndiye alimchagua Edson.
“Malipo na mambo mengine, ni baada ya kazi kufanyika. Ntaka akione cha moto.” Alilisitiza Ibrahim mbele ya kibaraka wake.
Baada ya kumaliza hayo, yule kibaraka aliaga na kuondoka eneo lile huku akiwa kapewa siku mbili tu! Ya kutimiza kile alichopangiwa.
Na kweli, baada ya siku mbili, Eddy aliokotwa pembezoni mwa Ziwa Viktoria akiwa hajitambui na mwili wake ulikuwa umepatwa na majeraha mengi ya kuchomwa na sigara pamoja na kuchanjwa na viwembe.
Hali ya kijana huyu ilikuwa tete sana ndani ya siku tatu walizokuwa wakihangaika kumtafuta. Chanzo kikuu ni wivu wa mapenzi. Je? Mapenzi yanaua? Jini hapana, roho ya mtu ndio inaua. Mapenzi hayauwi athilani. Roho na moyo wa mtu ndio vinaua.
“Basi mwanamke aliwaza hayo na kiukweli yalimsumbua sana. Si kama hakumpenda yule mfalme wa nchi jirani, la hasha! Alimpenda lakini si kimapenzi japo mara kwa mara walitoka kama wapenzi. Ndipo ikatokea bahati Malkia akapata kijakazi mpya wa kiume. Kijakazi yule alikuwa mtaratibu na mwenye uelewa mkubwa. Punde tu, Malkia akampenda sana kijakazi yule. Na alipokuja kushtuka, aligundua kuwa anampenda kijakazi kuliko yule Mfalme mwenzake. Hakuwa na jinsi, akampa moyo kijakazi, na kijakazi akampa wake…….” Ilimbidi Win akamtishe Edson hadithi yake.
“Leo unataka kuongea nini Edson?” Win alimuuliza baada ya kuona hadithi ile kama inalenga maisha yake.
“Nataka nikwambie kitu kinachoitwa GANZI YA MOYO.” Akajibu Eddy kwa taratibu.
“GANZI YA MOYO.” Akarudia kwa sauti ya chini maneno hayo, Winfrida.
“Ni Ganzi Ya Moyo. Unajua ipo vipi mke wangu?” Aliuliza Edson.
“Nieleweshe.” Akatoa ombi Winfrida ambalo lilipokelewa kwa mikono miwili na kijana yule machachari.
“Pale mioyo miwili inapokutana na kutengeneza pendo, halafu ukatokea moyo mwingine na kuanza kuharibu pendo lile, basi mioyo ile ittakumbwa na Ganzi. Ganzi hilo ndiyo naliita Ganzi Ya Moyo.” Alielezea kwa kifupi Edson Lake.
“Kwa hiyo wale watoto wa viongozi walikumbwa na Ganzi ya Moyo?” Aliuliza Win.
"Ndio,” Alijibu Edson na kisha aliendelea. “Baada ya yule Malkia kumpenda kijakazi wake, mapenzi kwa Mfalme yakapungua kabisa. Hakuwa kama yule wa zamani. Mfalme alipojaribu kumuuliza, binti yule hakumpa jibu maalumu bali alisingizia mambo kadha wa kadha ya kiuongozi.
Ndipo yule mfalme alipochukua jukumu la kufanya upepelezi ambao wala haukumpa shida sana. Siku chache pekee zilitosha kwa mfalme kugundua kuwa Malkia alikuwa anatoka na kijakazi wake. Hapo sasa ikawa taflani katika mioyo hii. Mfalme alicheka kwa dharau lakini kicheko chake kiligeuka kilio punde tu alipogundua kuwa kazidiwa kete na masikini wa kutupwa kama yule kijakazi. Jambo hilo lilimuuma sana katika moyo wake na lilitafuna fikra zake kwa wingi mno. Ndipo baadae alipoamua kufanya jambo la hatari sana, jambo ambalo lilikuwa ni ganzi ya moyo.” Alimtazama Win na alimuona yupo katika usikivu mkubwa wa hadithi ile.
“Alifanyaje?” Win alimuuliza Edson baada ya kuona kimya kimetawala sana.
“Yule mfalme alianzisha vita kati ya nchi yake na ile ya malkia. Baada ya kupigana kwa muda mrefu, Mfalme alifanikiwa kuingia katika kasri analokaa Malkia na huko alimkuta kijakazi akiwa anaogopa sana vita vile. Mfalme alifurahi sana kumkuta kijakazi yule na hapohapo akaanza kumwambia kuwa kafanya vile kwa sababu yake. Kijakazi alishangaa, kwa sababu alikuwa hajui kama mapenzi yake na Malkia ndiyo yangeleta yale yote.
Yule mfalme akaropoka mengi lakini mwisho wa yote, alimchoma kwa upanga yule kijakazi na kupoteza maisha yake. Lakini kwa bahati mbaya, Malkia alikuwa anashuhudia yale yote yaliyokuwa yanatokea. Alisikitika sanaalipomuona mpenzi wake anauawa, ndipo ganzi ya moyo ilipomkumba. Akatoka sehemu aliyokuwepo huku akiwa haamini kama maiti iliyokuwa imelala kwenye miguu ya mfalme ilikuwa ni ya mpenzi wake. Malkia alishindwa alie au afanye nini. Moyo na mwili ulikuwa umeshikwa na ganzi. Na yule mfalme alikuwa hategemei hali ile, alikuwa anampenda sana Malkia lakini katu alikuwa hataki ajue sababu ya vita vile.
Malkia kwa hasira akamfata yule Mfalme na kutaka kumchoma na kisu kifupi chenye ncha kali sana. Lakini yule mfalme alimuwahi na kumtandika kofi zito kisha akaanza kulalamika ni kwa nini Malkia alifanya yale yote. Alilalamika mengi lakini mwishowe yule Malkia alimvamia bila kutegemea yule Mfalme, na Mfalme alimchona na upanga wake yule Malkia. Upanga ulitokeza mgomgoni. Malkia akafa na Ganzi ya Moyo ikamkumba yule Mfalme baada ya kuona miili miwili iliyopendana ikiwa imelala mbele yake. Kwa mara ya kwanza alijikuta analaumu maamuzi yake na adhabu aliyoiona ni sahihi, ni yeye kujiua pia kwa sababu Ganzi ile ya Moyo, asingeweza kuihimili daima. Akapanda juu ya kabisa ya jumba lile na kuangalia chini ambapo mapigano yalikuwa yanaendelea. Mfalme akajitupa na alipodondoka chini, alikuwa hana uhai. Hata vita iliishia hapo baada ya kumuona kiongozi amekufa.” Alimaliza Edson kusimulia mkasa huo na Win alivuta pumzi ndefu kama mtu aliyetoka kukimbia mbio za Marathon.
“Inasisimua sana hadithi yako. Nimeipenda mno.” Aliongea Win baada ya pumzi hizo alizozipumua.
“Kawaida tu! Nina nyingi zaidi ya hizi, ila hii nimekupa tu!” Alijibu Eddy na baada ya hapo walianza kuongea mengi mengine ya kujenga zaidi.
****
Katika maisha ya mapenzi, kuna kupendwa sana kiasi kwamba unaweza usione lolote ambalo mpenzi wako analifanya hata kama ni baya. Lakini kwa Win na Eddy, mambo yalikuwa tofauti sana tena sana. Waliwekana sawa pale mambo yalipokwenda kombo. Walijizuia mambo yao yasiwe hadharani na kila mtu akajua kuwa wale wamegombana.
Hivyo ndivyo mapenzi yalivyo. Ya wawili, yawe ya wawili pekee na yasiwe hadithi kwa wengine au faida kwa wengine. Kama mmeamua kupendana, basi ni vema kuhakikisha pendo lenu linakuwa lenu peke yenu, hata kitanda mnachokilalia hakikisheni kuwa hakijui kama mmekilalia.
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Nayasema haya kwa sababu baada ya wiki mbili, mambo yalianza kubadilika katika mapenzi kati ya Win na Eddy. Mtoto wa kike alianza kupokea shutuma nyingi sana toka kwa watu kuwa Edson anawachukulia wanawake wao. Na mara kadhaa kuna wanawake walikuwa wanakuja kumuulizia Eddy huku wakijitambulisha kuwa ni wapenzi wake.
Kingine kibaya zaidi ya vyote, ni pale alipokuja bwana mmoja na kumuonya Win kuwa Edson akiendelea kumchukua mke wake, basi atamfanya kitu kibaya kuliko kile alichomfanyia miezi kadhaa iliyopita.
Hakuna moyo ambao ungeweza kuvumilia maneno kama hayo toka kwa watu mbalimbali. Na kwa asilimia fulani, maneno yale yalimuingia Win. Edson alipoulizwa na Win juu ya suala lile, Edson alimwambia Win neno moja tu! FITINA. Baada ya neno hilo, hakuongeza neno lingine zaidi ya kumsihi Win akae mbali na maneno ya watu.
FITINA.
Ni kweli ilikuwa Fitina. Ni Fitina toka kwa Ibrahim. Alitumia pesa zake kufitinisha ili mapenzi kati ya Win na Eddy yakwame. Lakini haikuwa hivyo, kila siku aliwaona watu wale wakiwa wanacheka kwa pamoja kana kwamba kulikuwa hamna maneno yalikyokuwa yanawakwaza kila kukicha. Cheko na furaha za watu wale, ndizo zilikuwa zinamfanya Ibrahim azidi kuichukia dunia. Kila siku alikuwa anawaza ni vipi ataweza kuwatenganisha watu wale.
Lakini siri kubwa ya furaha ya Eddy na Win ilikuwa ni jambo dogo sana, linaitwa SIRI. Walitunza siri zao za ndani ambazo zilikuwa zinawapelekea hata kununiana kwa siku mbili na zaidi. Lakini walipotoka kwa pamoja, ni kama walikuwa hawana jambo linaloitwa ugomvi. Hapo hata yule mfitinishaji, lazima aone kuwa kachemka. Jambo kuu katika mapenzi yanayoingiliwa na wapinzani, ni SIRI. Kamwe usiwe mtu wa kutoa mambo yako nje eidha kwa kuwaambia watu au kuonesha wazi kuwa umegombana na mtu wako.
“Lakini huyu mtoto ananitakia nini? Mbona mimi sitaki kabisa kumtenda? Yaani licha ya haya yote lakini bhado anaendelea kulala na mtu ninayempenda? Haiwezekani, anatakiwa kutendwa zaidi ya hapa.” Alikuwa anaongea peke yake Ibrahim baada ya kuona fitina zake zinagonga mwamba mbele ya mahusino yale yaliyokuwa yanazidi kushika nafasi kubwa kila kukicha. “Asubiri sasa kinachofuata baada ya hapa.” Alijiapiza tena kama kawaida yake Ibrahim Singa.
****
Ilikuwa Jumamosi moja tulivu sana. Hali ya mama yake ilikuwa inaendelea vema kuliko miaka yote lakini kitandani alikuwa bado hawezi kunyanyuka mwenyewe japo sasa aliweza kukaa na saa nyingine kula mwenyewe. Ilikuwa ni ahueni kubwa sana mbele ya familia inayomuhudumia kwani walikuwa hawapati ugumu kama ule wa mwanzo.
Siku hii ya Jumamosi ilikuwa ya kipekee sana katika familia ile. Winfrida alikuwa ameenda kazini kwake na Edson alikuwa anajiandaa kwenda kujisomea maktaba. Lakini kabla hajaondoka, alienda chumbani kwa mama yake kwa ajili ya kumuaga.
“Mama naenda Mktaba kujisomea, nitarudi baadae.” Alikuwa akiongea Edson baada ya kukaa kwenye kitanda kipana alicholala mama yake.
“Leo kwa nini usibaki mwanangu tukae tucheke mara moja? “Mama wa Edson alimuuliza mwanaye baada ya kupata taarifa hiyo toka kwa mwanaye.
“Natamani kufanya hivyo Mama, lakini nabanwa sana na haya masomo. Nitawahi kurudi lakini. Na Win naye kasema atawahi kurudi kwa sababu anataka tutoke leo jioni.” Aliongea Eddy kwa furaha lakini mama yake hakuwa sawa kabisa.
“Lakini mimi naonelea ubaki mwanangu. Sitaki uende huko leo hii. Kwa nini usikae tu.” Alisisitiza mama mtu.
“Hapana Mama, nahitaji kusoma sana ili nifikie lengo.” Eddy naye aliweka msisitizo kwenye kile alichokuwa kakianza.
“Haya baba. Nenda kasome lakini moyo wangu leo hautamani kabisa kukuona umeondoka hapa. Ni kama ile siku baba yako alipokuwa anaenda kazini. Nilimsihi sana asichelewe kurudi, na kweli hakuchelewa lakini yaliyomkuta, hadi leo sitaki kuifikiria ile picha.” Aliongea kwa masikitiko mama yake Edson. Edson akasogea karibu na kitanda cha mama yake. Kwa faraja kubwa akamsisitizia mama yake aondoe hofu kwa sababu anaenda kutafuta kilichobora kwake na si jambo lingine.
Mama wa watu ikabidi amuache mwa wake aende kutafuta maisha kupitia Elimu. Mama Edson aliujua umuhimu wa Elimu, lakini siku hiyo hakuwa tayari kumuona mwanaye anaondoka pale nyumbani. Atafanya nini na wakati yeye anapenda mwanaye asome? Ikabidi amuache tu!
Lakini kama Edson angejua ni nini kinaenda kutokea mbele yake, sidhani kama angekubali kuondoka ndani ya nyumba ile. Lakini wanasema, ni MUNGU pekee ndiye anayajua maisha yetu ya mbele. Hakuna ambaye anapanga kufa kesho, lakini wapo wanaopanga kuwa watanunua kitu fulani kesho. Hamna anayewaza kupatwa na mabaya kesho, bali mazuri pekee. Hayo ndio maisha ya mwanadamu wa siku hizi.
“Naenda shule mama. Kwa kheri.” Alimuaga tena mama yake wakati anashika kitasa cha kutokea mle ndani.
“Njoo tena mwanangu nikukumbatie.” Aliongea Mama Edson na Eddy alirudi kitandani na kumkumbatia kwa nguvu mama yake.
“Kasome mwanangu. MUNGU akulinde.” Yalikuwa maneno ya mwisho ya mama yule Eddy kuyasikia katika masikio yake, na kumbate lile ndilo lilikuwa la mwisho katika maisha haya ya kila siku.
“Usijali mama. Naenda kutengeneza maisha.” Eddy alinong’ona taratibu huku akimuachia mama yake na yeye kuondoka mle chumbani kuelekea ilipo maktaba ya mkoa wa Mwanza.
Ilikuwa kama utani pale gari moja kubwa na pana ilipofunga breki miguuni kwa Eddy na kisha kwa haraka wakashuka wanaume watatu waliovalia kininja na kumkamata Edson kisha wakamtupia ndani ya gari halafu kwa kasi ya ajabu wakaondoka eneo lile ambalo lilikuwa si mbali na anapoishi Edson, na kwa bahati mbaya kulikuwa hamna watu walioona lile tukio la haraka sana.
****
Taarifa zilizagaa mkoa mzima wa Mwanza kuwa kijana wa kidato cha tatu amepotea siku ya tatu tokea Jumamosi ile alipoagana na mama yake. Hakuna aliyekuwa analala kwa amani kila alipokuwa anafikiria kuwa Edson hajaonekana. Si mama yake wala Winfrida aliyekuwa anaamani baada ya Edson kutoonekana kwa siku hizo tatu. Lakini licha ya hayo yote, Winfrida hakuwa tayari kumkatisha tamaa mama yule. Kila mara alikuwa akimpa moyo kuwa mwanaye angepatikana na maisha yangeendelea. Lakini kama angelijua kuwa kuwa kuna Ganzi Ya Moyo itaikumba familia ile, basi asingelikuwa anayaongea maneno ya kumpa moyo mama wa Eddy.
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kwa upande mwingine, Edson alikuwa kaning’inizwa kwenye chumba kimoja huku mwili wake ukiwa unavuja damu na uso wake kuvimba kama aliyeumwa na nyigu. Alisikitisha kwa kumwangalia tu! Lakini roho za watu aliokuwa amekutana nao, walikuwa hawaju hilo. Walimpiga kadiri walivyoweza ili tu kutimiza lengo lao. Eddy alikuwa amening’inia kama vile mbuzi aliyekuwa anavuliwa ngozi, alionesha wazi kuwa amepoteza tumaini la kuishi.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment