Simulizi : Kifo Cha Mtu Asiye Na Hatia
Sehemu Ya Nnne (4)
Alisimama wima mbele ya askari magereza wa kike, mtoto wake Alicia akiwa mgongoni, mtoto huyo hakuelewa kitu chochote kilichoendelea aliendelea kulala mgongoni kwa mamaye. Baada ya kujieleza kwa muda mrefu akimbembeleza askari magereza amwitie Prosper ili aonane naye kabla ya kifo chake hatimaye askari alilainika na kuanza kutembea kuondoka eneo hilo na kuingia ndani ya gereza.
Hakurudi mpaka dakika kama kumi na tano hivi baadaye, askari huyo aliporejea mbele yake akiwepo Prosper! Tayari alishavalishwa nguo za wafungwa na alionekana kukonda sana.
Prosper alionekana kutoyaamini macho yake alipomwona Belinda! Alitaka kukimbia kwenda upande wa pili kumkumbatia lakini alizuiliwa na nondo nzito zilizotenganisha ndani na nje ya gereza! Ziliwekwa maalum kuwazuia wafungwa kutoroka.
“Afande nifungulie basi nisalimiane na mke wangu kwa karibu zaidi!”
“Haiwezekani hata kidogo Prosper kwanza si ruhusa leo wafungwa kuonwa nimewafanyia upendeleo vinginevyo ningeweza kukataa kwanza haraka kabla mkuu wa gereza hajaja mnasikia?” Askari magereza aliongea kwa msisitizo.
Hakuna aliyemjibu kitu afande bali Prosper alisogea karibu na uzio wa nondo, Belinda nae alifanya vivyo hivyo mpaka wakakaribiana kabisa na kupenyeza midomo yao katikati ya nondo na kuanza kupigana mabusu mdomoni mbele ya askari bila kuogopa wala kuona aibu.
Ghafla kabla hawajasema lolote hata kusalimiana wote walianza kudondosha machozi na baadaye kulia kwa sauti, walionekana kuwa na uchungu mkubwa mioyoni mwao! Waliangaliana na kukumbuka mambo mengi yaliyotokea katika maisha yao tangu walipokutana mara ya kwanza shuleni, yalikuwa ni mateso makubwa mno waliyoyapitia na bado walikuwa wakiendelea kuteseka.
Waliendelea kulia kwa kwikwi kiasi kwamba hakuna mtu aliyeweza kumwambia mwenzake chochote hadi Prosper alipoanza kuvutwa na askari magereza kurudishwa gerezani! Machozi yalimbubujika Belinda kwa wingi, alimwonea huruma sana Prosper na kabla hajaingizwa ndani aligeuka nyuma na kuwaanglia Belinda na mtoto wake, roho ilimuuma sana na alitamani mambo yangekuwa tofauti na ilivyokuwa, ndani ya nafsi yake Prosper alijilaumu kwa uamuzi wake wa kuyakiri mauaji ambayo hakuyatenda jambo ambalo hata Belinda hakulifahamu.
Mtu aliyekiri mauaji hayo ili amuokoe kutoka gerezani,yaani mama yake tayari alikuwa ni marehemu na dada zake nao walishamtelekeza gerezani baada ya kutoka gerezani na yeye kuingia!
“Nakupenda Belinda, ahsante sana kwa kuja tena, nisamehe kwa kila kosa nililoliyafanya najua sina maisha marefu duniani, kwa sababu watu wenye virusi hufa upesi sana gerezani isitoshe nimeshahukumiwa kifo tayari, namuonea huruma sana mwanangu kwa sababu hataishi kuja kuniona mimi baba yake! Tafadhali Belinda mtunze vizuri mtoto wetu Alicia lakini usije kumwambia niliua!” Alisema Prosper huku askari magereza akisubiri amalizie.
“Prosper elewa ninakupenda sana na nimekwishakukusamehe makosa yako yote na nimesikitika kujua unakufa na kuniacha mimi!” Alisema Belinda akijua hiyo ndiyo ilikuwa mara ya mwisho kuonana na Prosper kwani angenyongwa kama hukumu ilivyotolewa.
Pamoja na kujua Prosper alikuwa na virusi vya Ukimwi kama ambavyo yeye Belinda aliamini kuvipata kutoka kwake na yeye kuvipeleka kwa mtoto wao Alicia, bado Belinda hakuwa tayari kukubali Prosper anyongwe, alimpenda mno na hakutaka kumpoteza! Alitaka waishi pamoja mpaka watakapozidiwa na kufa kwa Ukimwi ikiwezekana siku moja wote watatu.
“Sipendi Prosper anyongwe na ningekuwa na uwezo wa kuliepusha hili ningefanya, siku thelathini za kukata rufaa bado zipo kama ningekuwa na pesa ningeweka wakili ili angalau afungwe kifungo cha maisha si kunyongwa!”
Alishuhudia Prosper akisukumwa na askari magereza kuingizwa gerezani, Belinda alibaki akishangaa bila kujua la kufanya na hakujua baada ya kutoka gerezani angeelekea wapi! Alitamani kurudi nyumbani kwa baba yake lakini kila alipokumbuka yaliyompata mara ya mwisho alipokwenda alishindwa kufikia uamuzi huo.
“Mdogo wangu unaweza kuja Jumamosi au Jumapili, ndiyo siku ya kuona wafungwa!” Alisema askari magereza baada ya kurudi na kumkuta Belinda.
“Ahsante sana dada kwa kweli ninakushukuru mno kwa msaada wako Mungu atakulipa!”
“Huyo ndiye mumeo?”
“Ndiyo na ndiye baba wa mtoto huyu!”
“Ulisema wewe ni mtoto wa mzee Thomson Komba?”
“Ndiyo!”
“Mama yako ni yupi?”
“Mke wake wa kwanza achana na huyu aliyepo hivi sasa ambaye ni mama wa David na John!”
“Kwa hiyo wewe mama yako ni aliyefariki?”
“Ndiyo!”
“Sasa kwanini usirudi ukae nyumbani kwa baba yako kama mumeo amehukumiwa kunyongwa?”
“Dada…wee acha tu!” Belinda aliongea kwa masikitiko.
“Kwanini unasema hivyo?”
“Huwezi kuamini baba yangu hataki hata kuniona, alinifukuza kama mbwa kila ninapokwenda nyumbani hunifukuza!”
“Kwanini?”
“Eti kwa sababu nilipata mimba ya huyu mtoto hawakutaka iwe hivyo nimetengwa kabisa na familia yangu!”
“Pole sana, sasa ukitoka hapa utakwenda wapi?”
“Kwa kweli sijui ila Mungu mwenyewe anaelewa, najua hawezi kuniacha!”
“Ningeweza kukuchukua ukae nyumbani kwangu lakini nina chumba kimoja tu na nina familia kubwa, ninakuhurumia lakini sina la kufanya kukusaidia!”
“Hakuna shida Mungu anafahamu yote!”
*************
Baada ya kuondoka gerezani Belinda alianza kutembea kuelekea kituo cha mabasi cha Segerea, akiwa njiani mvua kubwa ilianza kunyesha na kuwalowanisha yeye na mtoto wake. Alihofia mtoto wake kupata kichomi lakini hakuwa na la kufanya ilibidi aendelee na safari yake hadi kituoni ambako alisimama peke yake akisubiri magari lakini halikupita gari lolote kuelekea mjini, alisongea pembeni na kujikinga mvua chini ya mti na kuendelea kusubiri gari ambalo lingepita.
Akiwa katika dimbwi la mawazo ghafla alishtukia gari moja likipita kwa kasi kubwa na mbele kidogo lilisimama na kuanza kurudi kinyumenyume, Belinda alipoliona alijua ni msamaria mwema amemwona yeye na mtoto wake akawahurumia na kuamua kuwapa msaada wa usafiri.
Alianza kukimbia kulifuata gari hilo wakati likirudi nyuma, alipolifikia alizunguka upande wa dereva na kuinamisha kichwa chake ili aongee naye lakini dirisha liliendelea kufungwa ilionekana watu waliokuwa ndani walikula kiyoyozi cha kasi, dakika moja baadaye Belinda akiendelea kulowa dirisha lilianza kufunguliwa taratibu.
Hakuyaamini macho yake kwa alichokiona ndani ya gari hilo, kulikuwa na watu wanne na kila mmoja wao alikuwa ameshika chupa ya bia mkononi mwake! Walionekana ni watu waliolewa na waliongea kwa sauti ya juu kupita kiasi!
“Wee kuku unakipeleka wapi hicho kifaranga chako?” Ilikuwa ni sauti ya dereva na sauti hiyo haikuwa ngeni kabisa masikioni pa Belinda ingawa dereva mwenyewe alivaa kofia kubwa iliyofunika uso wake na aliongea akiwa ameinamisha kichwa sababu ya kulewa!
Wasichana wote ndani ya gari hilo walicheka kusikia mwanamke mwenzao anaitwa kuku! Dereva alivua kofia yake ndipo Belinda alipotambua alikuwa ni David kaka yake wa kambo! Nyuma alikaa mdogo wake John naye akiwa amekumbatiwa na msichana mrembo kupita kiasi! Kila mtu alikuwa na chupa ya bia mkononi mwake.
“Ingia kwenye buti tukupe lifti kifaranga chako kitapata kichomi!” Lilikuwa ni tusi jingine tena kwa Belinda kutoka kwa mtu waliyechangia naye baba, roho ilimuuma sana Belinda ukizingatia mali zilizowatia kiburi zilikuwa ni za baba yao wote.
“Mpenzi ondoa gari bwana nini achana na kichaa huyo!” mrembo aliyekaa pembeni kwa David alisema na gari lilianza kuondoka kwa kasi likimmwagia Belinda matope mengi! Alisikia kitu kama miba kikimchoma moyoni mwake yalikuwa ni maumivu ya moyo! Akajikuta amekaa chini kuanza kulia.
Belinda aliona dunia kwake ni kama jehanamu, alikuwa akiadhibiwa kwa kosa ambalo hakulielewa, kila upande ulikuwa umemgeukia yeye hakuwa tena na mahali pa kukimbilia, alijihisi kuwa na mkosi.
“Ee Mungu kwanini mimi tu?”Belinda alijiuliza huku akilia machozi.
Sekunde chache baadaye akiwa amekaa chini mvua ikiendelea kumnyeshea, alisikia honi nyuma yake, kumbe alikuwa katikati ya barabara bila kufahamu, gari hilo lilikuwa ni daladala!
“Huyu sijui chizi?” Dereva aliwaambia abiria waliokuwa ndani ya gari.
“Inawezekana ni chizi kweli?” ”Piiiii!Piiiiii!Piiiii!” Dereva alizidi kupiga honi.
Belinda alijinyanyua taratibu kutoka katikati ya barabara huku akipunga mkono kumwomba dereva asimamishe gari ili apande lakini dereva aliondoa gari bila kujali, alisimama aliposikia kelele za abiria zikimwomba asimame na kumsaidia Belinda na mtoto wake.
“Simama bwana umsaidie hata kama ni chizi ana mtoto mdogo anayelowa na mvua!” Mama mmoja aling’aka ndani ya gari.
Gari lilisimama na Belinda alikimbia mbio na kupanda ndani ya gari, nguo zake zilidondosha maji kiasi cha kuwalowanisha abiria wengine ndani ya daladala hilo! Wengi walifoka na watu wote waliokuwa karibu yake walilalamika vibaya, kabla hajakaa vizuri kitini dereva alisikika akipiga kelele kwa sauti ya juu!
“Jamani ajali!Gari linadumbukia darajani!”
Kufuatia sauti hiyo abiria wote walitupa macho yao mbele kuangalia ni kitu gani kilikuwa kimetokea, Belinda alikuwa miongoni mwa watu waliofanya jambo hilo kweli gari lilikuwa darajani tena ndani ya maji ya mto uliokwenda kwa kasi ni sehemu ya juu tu iliyoonekana.
Dereva alipolifikia daraja alilisimamisha gari pembeni na watu wote walishuka na kukimbia darajani kwenda kuona kilichotokea hata Belinda alifuata nyuma akiwa na mtoto wake mgongoni mvua ilikuwa bado ikinyesha!
“John tuna kamba kwenye gari?” Dereva alimuuliza konda.
“Ndiyo!”
“Itoe ili tujaribu kuvuta hii gari tuone itakuwaje inawezekana kuna watu ndani!”
“Poa Suka!”
Dereva na utingo wake walikimbia kwenda mahali lilipokuwa gari na dereva aliligeuza na kuanza kulirudisha kinyumenyume kuelekea darajani, mita kama kumi hivi alilisimamisha na likafungwa kwa kamba na kuanza kuvutwa!
Ilikuwa kazi ngumu lakini kama saa nzima baadaye magari la watu wengi wakiwepo eneo la tukio kutoa msaada gari liliopolewa kutoka majini.
“Masikini kuna watu ndani, tena wamekufa tena wakiwa wamekumbatiana” Mtu mmoja alipiga kelele baada ya kuchungulia ndani ya gari lilipotolewa majini.
Belinda hakutaka kuwa mvumilivu alisogea karibu ili naye ashuhudie kwa macho yake! Tukio hilo lilionekana kumsahaulisha kidogo matatizo aliyokuwa nayo hivyo alisogea karibu. Milango ya gari ilipofunguliwa mbele ya macho yake na maiti kuanza kutolewa, alianguka chini na kulia alipogundua kuwa walikufa walikuwa ni kaka zake waliompita kituo cha basi na kumkebehi, pamoja na kumfanyia kitendo kibaya.
“Ni kaka zangu! Ni kaka zangu! Jamani ni kaka zangu!”Belinda alizidi kulia na kupiga kelele akipita katikati ya makundi ya watu, alionekana kuwa amechanganyikiwa na wanawake wawili walimnyang’anya mtoto na wengine walimshikilia ili asifanye vurugu zaidi.
“Unakaa wapi dada?” Mtu mmoja aliuliza lakini Belinda hakujibu kitu, alishindwa kusema moja kwa moja kuwa aliishi kwa mzee Thomson Komba kwa sababu alikuwa na muda mrefu tangu afike eneo hilo.
“Nyumbani kwenu ni kwa nani dada?” Dereva wa gari hilo naye aliuliza swali hilo hilo!
“Kwa mzee Thomson Komba!”
“Mzee Thomson Komba? Una uhakika?”
“Mimi ndiye mtoto wake wa kwanza na hawa waliokufa ni kaka zangu ila wasichana wao ndiyo siwafahamu!” Belinda aliongea huku akilia machozi.
“Una namba za simu ya nyumbani kwenu?”
“Ndiyo ni 0744-382856, hiyo ndiyo namba ya simu ya baba ya mkononi”
“Jamani nani ana simu kati yetu?” Dereva aliuliza abiria mmoja aliyejitokeza na kutoa simu yake itumike, walimpigia mzee Komba na pia kuwataarifu polisi.
Mzee Komba alipata mshtuko mkubwa sana na saa moja tu baadaye alifika eneo la tukio akiwa na mke wake na kukuta maiti za watoto wake zikiwa zimelazwa chini kwenye nyasi! Alilia machozi kwa uchungu, Belinda alijificha katikati ya watu akilia alimwogopa sana baba yake na alijua angeweza kumuaibisha mbele za watu!
“Watoto wangu hawa niliwaeleza kila siku juu ya tabia yao mbaya ya ulevi na hawakunisikia, hatimaye leo mabaya yamewakuta!” Alisema mzee Thomson Komba kwa uchungu na mkewe aliitikia kwa kilio.
“Masikini sina mtoto tena zaidi, hivi sasa tegemeo langu ni kwa mwanangu Belinda! Nitamtafuta popote alipo ili arudi nyumbani haraka iwezekanavyo! Nitamtafuta kwa gharama yoyote ile!” Alisema mzee Thomson kwa sauti huku akilia, maneno hayo yalimfikia Belinda moja kwa moja akiwa katikati ya watu.
Belinda hakuamini kama maneno yale yalitoka mdomoni mwa baba yake aliyemchukia siku zote! Belinda alijikuta akimwonea huruma baba yake na chuki yote aliyokuwa nayo moyoni juu ya baba yake iliyeyuka! Belinda akitetemeka alianza kutembea kupita katikati ya watu kwenda mbele alitaka amwambie baba yake kuwa alikuwa maeneo yale.
“Baba!Baba!Baba!” Hatua tatu kabla hajamfikia baba yake Belinda alimwita mzee Thomson na aliisikia sauti hiyo na kugeuka nyuma kuangalia na kuanza kumfuata akiwa amepanua mikono yake ili amkumbatie.
“Mwanangu Belinda kaka zako wameku… ! Kabla mzee Thomson hajaimalizia sentensi yake, Belinda kwa macho yake alimshuhudia baba yake akilegea na kuanguka chini kama mzigo na kugeuza macho juu! Belinda akiwa na mtoto wake mgongoni alianguka juu ya baba yake na kuanza kumtingisha baba yake lakini hakuitikia, na alianza kutoa damu mdomoni na puani watu wote walishangazwa na kilichokuwa kimetokea.
“Yaani watoto wamekufa na baba pia?” Abiria mmoja aliuliza kwa huzuni.
Maiti zote zilibebwa na kupakiwa ndani ya magari yaliyokuwepo eneo la tukio na mzee Komba akiwa hoi alipakiwa katika gari lake akifuatana na mkewe pamoja na Belinda akiwa na mwanae mgongoni wote ndani ya gari hilo walilia machozi, ilikuwa huzuni kubwa mno kwao.
Pamoja na kulia kwa uchungu mke wa mzee Komba bado alionyesha chuki yake kwa Belinda waziwazi, kila mara alimwangalia kwa macho ya hasira na kumsonya, alionekana kutopendezwa na kuwepo kwa Belinda na mtoto wake katika tukio hilo.
“Na wewe umefikaje hapa na hicho kitoto chako si nilisikia ulikuwa Tabora?” Aliuliza mama huyo kwa nyodo.
“Mamaaa!” Belinda aliongea kwa sauti.
“Mama yako nani?”
“Tuyaache yote haya ninachotaka kusema ni kuwa tusahau tofauti zetu ili tushughulikie matatizo yaliyopo , David na John wamefariki na baba ndiye huyu anaumwa kupita kiasi!” Alisema Belinda kwa uchungu.
Maneno ya Belinda yalimchoma sana mama huyo moyoni mwake na kumkumbusha watoto wake wawili ambao tayari walikuwa marehemu na walikuwa ndani ya gari lililokuwa mbele yao likielekea chumba cha maiti cha hospitali ya Muhimbili.
Kwake yote yaliyotokea yalikuwa ni kama ndoto! Hakuamini kama David na John walikuwa wamekufa, Belinda alimshika begani na kuanza kumbembeleza ili asilie zaidi lakini aliendelea kulia zaidi, mama huyo aliushika mkono wake na kuutupa pembeni akionyesha kutofurahishwa kabisa na kitu ambacho Belinda alifanya.
“Toka hapa unanibembeleza kitu gani? Si ni heri ungekufa wewe na hicho kitoto chako kama kuzimu wahitajika watu wawili badala ya kufa watoto wangu!” Alisema mama huyo huku akimwangalia Belinda kuanzia miguuni, macho yake yalipofika kichwani yalianza kushuka tena hadi miguuni kisha akasonya kwa nguvu!
Belinda alijisikia kudhalilishwa kiasi cha kutosha alijisikia kama yu uchi wa mnyama! Alitamani kuwa na mama aliyempenda lakini mama yake hakuwepo duniani alishafariki miaka mingi na baada ya kufariki mama yake na kumwacha Belinda akiwa mtoto mchanga ndiyo baba yake alipomuoa mwanamke huyo.
Walipofika hospitali ya Muhimbili walipokelewa, gari lililobeba maiti lilipitiliza hadi chumba cha maiti ambako miili ya John na David pamoja na wasichana waliokuwa nao ilihifadhiwa katika majokofu, baadaye taarifa ilitolewa polisi juu ya ajali hiyo.
Haikuchukua muda mrefu habari zikawa zimekwishasambaa kila sehemu ya jiji la Dar es Salaam kuwa watoto wa mzee Komba walikuwa wamefariki dunia baada ya gari lao kuacha njia na kudumbukia mtoni! Shule ya makongo waliyosoma watoto hao iligubikwa na masikitiko makubwa, karibu kila mtu shuleni hapo hadi walimu walilia.
*********************
“Hiki ni kiharusi mzee huyu alishtuka sana ndiyo maana hali hii ilitokea!”!” Alisema daktari baada ya kumpima mzee Komba
Baada ya kupimwa alichukuliwa na kupelekwa katika wodi ya wagonjwa mahututi, iliyotumiwa na watu wenye pesa na viongozi mbalimbali na kuanza kupewa matibabu ya uhakika, fahamu zake hazikurejea mpaka baada ya siku pili alipozinduka na kumkuta Belinda pembeni ya kitanda chake akiwa na mtoto wake mgongoni.
“Baba!Baba!Baba!” Belinda aliita hakuamini kama baba yake alikuwa amefumbua macho baada ya kukaa bila fahamu kwa masaa zaidi ya arobaini na nane.
Mzee Komba aliangaza macho yake huku na kule chumbani hakuona mtu mwingine zaidi ya Belinda.
“Ma..ma..ya..ko..yu..po..wapi?” Aliuliza mzee Komba.
“Yupo nyumbani baba!”
“Nyumbani wapi?”
“Nyumbani kwetu!”
“Kwani hapa ni wapi?”
“Hapa ni hospitali!”
“Kwanini nipo hapa?” Mzee Komba aliuliza lakini Belinda alishindwa kumsimulia kilichotokea kwa kuogopa kumsababishia matatizo zaidi.
“Kwanini nipo hapa?” Mzee Komba aliuliza tena.
“Uliugua ghafla!”
“Niliugua ugonjwa gani na kwanini?”
Kabla hajajibu mlango ulifunguliwa na daktari akaingia na kundi la wauguzi na madaktari kama watano hivi!
“Ha! Leo mzee Komba anaongea?” Daktari mkuu aliuliza, watu wote walionekana kushangazwa sana na hali hiyo, kila mtu alisogea karibu na kitanda cha mzee Komba na kuanza kushangaa.
“Dada tunaomba utupishe kidogo tumpime mzazi wako!”Daktari alimwomba Belinda na bila kusita alifungua mlango na kutoka nje akiwaacha madaktari bado wanamshangaa baba yake.
Akiwa nje ya wodi mawazo yake yalimrejesha tena gerezani na kuanza kumfikiria Prosper, kila fikra kuwa angenyongwa na kufa zilipomwijia kichwani mwake aliumia zaidi na kulia! Kila upande kwake ulikuwa na maumivu, baba alikuwa mgonjwa na Prosper alikuwa gerezani.
Baadaye madaktari walitoka nje na kumwomba Belinda aingie lakini walimuonya juu ya kuongea habari yoyote ya kusikitisha na baba yake, alipofika ndani alimkuta baba yake akibubujikwa na machozi, Belinda aliinama na kuanza kumfariji.
“Tafadhali nieleze usifiche kitu ni nini kilichotokea hadi nikawa hapa?”
“Uliugua tu baba!”
“Ugonjwa gani?”
“Homa!”
“Homa? Haiwezekani hata kidogo, hii siyo homa mbona mwili wangu umepooza wala sijisikii kabisa?”
“Usiwe na wasiwasi baba utapona tu!”
“Mwanangu Belinda naomba sana unisamehe kwa yote niliyokutendea ni mama yako wa kambo aliyesababisha! Najuta kwanini nilifanya hivyo! Hali yangu ni mbaya na ninafahamu nitakufa, sitaki kukuachia matatizo baada ya kifo changu ninaelewa ni kiasi gani mama yako hakupendi hivyo kuna uwezekano ukakosa kitu chochote kutoka katika mali zangu nenda upesi ukalete karatasi nikuandikie urithi!”
Maneno hayo ya mze Komba yalimtisha Belinda, alijua pamoja na kuonyesha hali nzuri kulikuwa na jambo baya ambalo lingetokea katika muda mfupi!
“Nipe maji ya kunywa kwanza kabla hujaondoka mwanangu!” Mzee Komba alisema.
Mara nyingi Belinda alishasikia watu wakisema kitendo cha mgonjwa kuomba maji akiwa katika hali mbaya ni dalili ya kuaga dunia! Aliyakumbuka maneno hayo lakini hakutaka kuyatilia maanani wala kuyachukulia kuwa ni kweli, aliiona ni imani ya watu na kunyanyuka kwenda kumimina maji katika glasi na kumpa baba yake.
“Belinda fanya haraka uniletee karatasi, sitaki upate shida nina wasiwasi mama yako hatakupa kitu chochote kile baada ya kifo changu!”
Belinda alitoka mbio hadi ofisini kwa wauguzi na kuomba msaada wa karatasi na kalamu, wauguzi walimpatia vitu vyote alivyohitaji na kuondoka mbio ofisini! Hali hiyo iliwashtua wauguzi ikabidi wamfuatilie, walimkuta mzee Komba akiandika maneno fulani kwenye karatasi huku mkono wake ukitetemeka, mwandiko ulikuwa mbaya mno na aliandika maneno machache sana yaliyotaja nyumba mbili zilizokuwa katikati ya jiji la Dar es Salaam kuwa zilikuwa mali ya Belinda tangu siku hiyo! Alipomaliza kuandika aliwapa wauguzi wakaisoma karatasi hiyo.
“Man...esi nyie ndi..o mmes..huhudia jam...bo hili tafadhali nitili...eni sahihi ze..nu hapo juu kabla sijafa!” Alisema mzee Komba na kuwapa manesi karatasi.
“Mzee Komba huwezi kufa utapona tu!”
“Mimi mwenyewe najua hali niliyonayo!”
Bila kusita wauguzi walifanya hivyo na kuanguka sahihi zao juu ya karatasi hiyo nyeupe, wauguzi wote pamoja na Belinda walikodolea macho karatasi na kumsahau mgonjwa kitandani kwa muda! Walipomaliza kutia sahihi waliirudisha karatasi hiyo kwa mzee Thomson Komba lakini hakuipokea ingawa mkono wake ameunyoosha kama mtu aliyetaka kupokea kitu!
Walipoiweka barua hiyo mkononi ilidondoka chini, kila mtu alishangaa sana na Belinda alipotupa macho yake usoni kwa baba yake alichokiona kilimfanya alie kwa sauti ya juu macho ya mzee Komba yalikuwa yametoka nje na alikuwa akitupa shingo yake huku na kule kama mtu aliyekuwa akikata roho!
Mmoja wa wauguzi alipoona hivyo alitoka mbio kwenda hadi chumba cha daktari lakini hakumkuta, alikuwa wodini akiendelea na raundi yake, alikimbia hadi wodini ambako alimkuta daktari na kumpa taarifa za tukio hilo na wote waliondoka mbio kwenda hadi chumbani kwa mzee Komba.
Walipoingia chumbani walimkuta Belinda akilia machozi kwa sauti ya juu! Daktari alinyoosha hadi kitandani na kuanza kumpima mgonjwa, alinyanyua uso wake dakika kama mbili hivi baadaye alikuwa na huzuni kubwa alimkumbatia Belinda na kuanza kumpigapiga mgongoni.
“Binti nasikitika mzee amefariki! Nini kimetokea wakati nimemwacha anaongea?” Alisema daktari.
“Hali yake ilibadilika ghafla!” Alijibu Belinda.
********************
Taarifa za kifo cha mzee Komba zilipelekwa nyumbani kwake ambako shughuli za mazishi ya watoto wake wawili David na John ziliendelea, mke wake alilia kupita kiasi kufuatia habari hizo na kuondoka kwenda hadi hospitali kuuchukua mwili wa mumewe! Ilikuwa ni siku ya huzuni kubwa mno kwake kupoteza watu watatu katika siku moja kila mtu jijini Dar es Salaam alihuzunishwa na tukio hilo na mamia ya watu walikusanyika nyumbani kwa mzee Komba ambako mazishi yalifanyika.
Wote watatu wakawa wamezikwa kwa siku moja na Belinda akiwa nyumbani kwao kushuhudia mazishi hayo, alilia mno kila alipomfikiria baba yake na alijisikia kumsamehe kwa yote aliyomtendea.
Pamoja na kufiwa na baba na ndugu zake bado Belinda hakusahau hata siku moja kuwa Prosper alikuwa gerezani, Jumapili iliyofuata alikwenda tena gerezani na kuonana naye na alimpa taarifa juu ya kifo cha baba yake, Prosper alionyesha masikitiko makubwa sana!
“Bahati mbaya sikuwahi kukutana na baba yako ana kwa ana!”
“Usijali Prosper haikupangwa mkutane!”
Wiki moja tu baada ya kifo cha baba yake matatizo mazito yalianza kumpata Belinda nyumbani kwao, mama yake wa kambo alianza kumfukuza pale nyumbani akidai arudi alikotoka! Hilo halikumsumbua sana Belinda ukizingatia tayari alikuwa na wosia wa kurithishwa nyumba mbili za mamilioni ya pesa katikati ya jiji, alichofanya ni kuondoka nyumbani na kwenda kwenye moja ya nyumba zake na kujitambulisha kwa wapangaji ili wafahamu kama mmiliki wa nyumba walizoishi.
Moja ya nyumba iliyokuwa mtaa wa Mafia namba 30, ilikuwa na chumba kimoja katika ghorofa yake ya pili kilikuwa na kila kitu ndani, kabla ya kifo chake baba yake alikitumia kupumzika kila alipokuwa na mawazo.
Belinda alitafuta mafundi wa ujenzi na mlango wa chumba ukavunjwa, akaingia ndani hicho kikawa ndiyo chumba chake na maisha yake na mtoto wake yakahamia hapo, pesa aliyopata kutoka kwa wapangaji ilimsaidia kuendesha maisha yake ya kila siku. Mambo yalianza kuwa mazuri Belinda alianza kunawiri lakini mawazo yake yaliendelea kubaki kwa Prosper gerezani, wazo la kumsaidia kutoka gerezani lilianza kumwingia akilini.
“Labda nikikata rufaa inawezekana kumfanya asinyongwe, nitauza nyumba yangu moja pesa nitakayopata nitamlipa wakili wa kunisaidia katika kesi kwani nyumba ni bora kuliko Prosper?” Aliwaza Belinda na kweli siku iliyofuata alikwenda moja kwa moja ofisini kwa mzee Rutashobya, mmoja wa mawakili maarufu katika jiji la Dar es Slaam na kumweleza matatizo aliyokuwa nayo ili aone kama angeweza kumsaidia.
“Ni lini hukumu ilitolewa?”
“Wiki iliyopita tu!”
“Basi bado tuna muda wa kukata rufaa nitajaribu kufanya hivyo lakini utanilipa shilingi milioni tano unazo pesa hizo?”
“Pesa sina ila nina nyumba ambayo nitaiuza kisha nitakulipa pesa hiyo!”
“Kwanini usinipe hiyo nyumba mimi tumalizane?” Wakili aliingiwa na tamaa ya kujipatia mali kwa njia rahisi.
“Hapana ni vyema tu niiuze na nikulipe pesa unayodai na nyingine inisaidie mimi na mtoto wangu!”
“Sawa, basi kesho nitasafiri kwenda Tabora kukata rufaa, nitakusaidia binti usiwe na shaka!” Alisema wakili Rutashobya mzee mwenye umri kati ya hamsini na sitini hivi!
Siku iliyofuata Belinda alitafuta madalali wa City Auction Mart na kuwaeleza nia ya kuiuza moja ya nyumba zake na aliwaonyesha barua aliyoachiwa na marehemu baba yake, waliichukua barua hiyo hadi kwa mama yake wa kambo na kumwonyesha, hakuwa na kipingamizi chochote kwa sababu mali aliyoachiwa ilikuwa nyingi zaidi.
Nyumba ikapigwa mnada kwa shilingi milioni 25! Belinda alifurahi kupata pesa na bila kuchelewa alifungua akaunti katika benki ya NBC na kuziweka pesa zote benki ili zimsaidie katika kesi! Alitaka sana kumtoa Prosper gerezani pamoja na kuambukizwa Ukimwi bado Belinda alimpenda kupita kiasi.
“Sitaki afe kwa kunyongwa! Nataka mimi na yeye na Alicia mtoto wetu tuishi pamoja tena tukisubiri kifo chetu cha Ukimwi basi!” Aliwaza Belinda.
Miaka minne baadaye:
Rufaa ilishakatwa na kesi ilikuwa bado ikiunguruma mahakamani kwa miaka minne! Belinda aliendelea kutumia pesa aliyokuwa nayo kuhakikisha Prosper anatoka gerezani, wakili wake alimhakikishia ni lazima angeshinda na kuwa huru.
Maisha ya Belinda yalishabadilika alinawiri na kupendeza, mtoto wake Alicia alisoma shule ya watoto wadogo ya Modern Daycare Centre iliyoko Kijitonyama, ilikuwa ni shule nzuri iliyomfanya aongee kiingereza kizuri! wanaume wengi walimfuata Belinda na kumsumbua wakitaka kumuoa lakini yeye alikataa kwa sababu mbili kwanza aliamini alikuwa ameambukizwa lakini kubwa zaidi mapenzi yake yalikuwa kwa Prosper kuliko mwanaume mwingine yeyote.
“Mom when is dad coming home? Why does he stay there all the time?”(Mama, baba atakuja lini nyumbani? Kwanini anakaa huko muda wote?) hilo ndilo lilikuwa swali la Alicia kwa mama yake kila siku iliyokwenda kwa Mungu, alikuwa ni mtoto mzuri wa sura lakini afya yake haikuwa nzuri sana, aliugua mara kwa mara na ugonjwa wake haukujulikana! Homa hazikukatika katika maisha yake, Belinda alielewa kilichomsumbua mwanae, alijua ni lazima mtoto huyo alikuwa navyo virusi ambavyo alikuwa na uhakika vilimpata kutoka kwa baba yake kupitia kwa wakati wa kujifungua.
*********************
Tarehe 22 mwezi wa Desemba ndiyo siku ambayo hukumu ya Prosper ilitegemewa kutolewa baada ya muda wa miaka minne, ilisikilizwa na jopo la Majaji Belinda na mtoto wake walikuwepo mahakamani siku hiyo, tegemeo lao lilikuwa Prosper kuachiwa huru lakini tofauti na walivyotegemea walijikuta wakiondoka mahakamani wakilia machozi kwani Prosper alishindwa tena hivyo hukumu ya kunyongwa iliyotolewa miaka minne kabla ikabaki palepale na alitegemewa kunyongwa siku mbili baadaye! Belinda alilia mno.
“Belinda tafadhali nakuomba uje gerezani kesho tuongee vizuri juu ya jambo hili ,kuna kitu nataka kukueleza nataka kuongea na wewe kabla ya kifo changu na ninaomba uje na mwanangu!”
“Sawa!” Alijibu Belinda huku akilia machozi.
“Mom why are you crying?”(Mama kwanini unalia?) Alicia alimuuliza mama yake lakini hakupewa jibu.
Siku iliyofuata Belinda alikwenda gerezani kuonana na Prosper, alielezwa kila kitu kilichotokea mpaka Prosper akawa muuaji, Belinda hakuamini alichokisikia kwa masikio yake.
“Sikuua Belinda naomba uniamini ni mama na dada zangu waliofanya jambo hilo mimi nilikuwa shuleni!”
“Sasa kwanini ulikiri?”
“Nilimpenda sana mama yangu na ninajua aliua kwa sababu ya kuteswa na baba!”
Habari hiyo ilimsikitisha sana Belinda usiku wa siku hiyo hakulala na asubuhi ya Desemba 24 siku ambayo Prosper alitegemewa kuchomwa sindano ya sumu majira ya saa 4:30 Belinda aliondoka asubuhi na mapema kwenda ofisini kwa wakili wake na wote waliondoka hadi kwa mwanasheria wa serikali na kumweleza kila kilichotokea mpaka Prosper akatiwa hatiani.
Mwanasheria alisikitika sana na kumpigia simu Rais ikatolewa barua ya kuzuia hukumu hiyo ilitakiwa kuwahishwa gerezani kabla Prosper hajachomwa sindano ya kifo, wakati wanapewa barua hiyo tayari ilikuwa saa 4:10 na Prosper alitegemewa kuchomwa sindano dakika ishirini baadaye.
Kwa msaada wa gari alilopewa na mwanasheria mkuu walifika gerezani saa 4:29:30 zikiwa zimebaki sekunde 30 tu Prosper afe, Belinda alimkabidhi askari magereza mmoja barua hiyo.
“Imetoka wapi?”
“Kwa mwanasheria mkuu!”
“Ya nini?”
“Msimchome Prosper sindano ya sumu hana hatia!”
“Mh! Mh! Mh! Mmechelewa sana hivi sasa ni saa 4:30 kasoro sekunde 20 na anachomwa sindano saa 4:30 hatuwezi kuwahi!”
“Mzee jaribu kuwahi unaweza kumwokoa!” Belinda alisema akiwa amepiga magoti chini.
“Haya ngoja nijaribu lakini matumaini ni kidogo!”
Aliondoka askari huyo akikimbia mbio kwenda ndani ya gereza huku akipiga kelele! Alijua muda huo lazima mzee nyonganyonga alikuwa akijiandaa kumchoma Prosper sindano!
***********************
“Kijana nakuonea huruma sana lakini inabidi tu nitimize wajibu wangu wa kukuchoma sindano hii ya sumu, nisamehe sana kukuondoka duniani, haya si mapenzi yangu!” Alisema mzee nyonganyonga kabla hajamchoma sindano hiyo.
“Choma tu mzee!” Prosper alisema kwa sauti ya unyonge lakini mawazo yake yalikuwa kwa Belinda na mwanae alijua kifo chao kingekuwa cha mateso kuliko chake!
“Haya moja! Mbili….tat….!”
Prosper alilala juu ya kitanda cha chuma pembeni yake akiwa amesimama mzee Nyonganyonga ambaye kazi yake ilikuwa ni kuondoa uhai wa binadamu wenzake! Alilipwa mshahara mkubwa kwa kazi hiyo, prosper alishangaa kuona mzee huyo hamchomi sindano ingawa alikuwa nayo mkononi mwake na muda wa yeye kuchomwa ulishafika alishindwa kuelewa ni kwanini mzee huyo alishindwa kutelekeza wajibu wake.
Prosper alitamani kufa hakutaka kuishi zaidi aliogopa sana kupambana na tatizo la ugojwa wa Ukimwi uliokuwa mbele yake, aliamini hakuwa na uwezo wa kuyastahimili matatizo yanayoambatana na ugonjwa huo!Alijilaumu kwa uamuzi wake wa kukubali kushiriki maisha ya kishoga na mfungwa mwenzake Savimbi ambaye ndiye aliyemwambukiza ugonjwa huo.
“Natamani nisife! Napenda niishi na familia yangu lakini sipo tayari kushuhudia nikikonda taratibu hadi kifo changu!”Aliwaza prosper na aliponyanyua uso wake kumwangalia mzee nyonganyonga alishangaa kukuta sindano ikiwa imezama tumboni kwake mwenyewe.
“Nime…cho….shwa na ….kazi ya ku…..ua ….bina…damu wenza…..ngu! Nita…..mwe..leza nini Mu….ngu ni heri nife sitaki kuitoa roho yako wa sababu huna hatia!” alisema mzee nyonganyonga akiangakua chini na mwili wake kukakamaa na ulimi kutoka nje.
“Mzee nyonganyonga umefanyua nini sasa? Kwanini umejiua wewe wakati ni mimi ninayestahili kufa?”Aliuliza prosper huku akipiga kelele alishindwa kufanya lolote kwa sababu alibanwa na mashine mikononi na miguuni, alianza kupiga kelele kuomba msaada na muda mfupi baadaye waliingia maaskari wawili mmoja akiwa na barua mkononi.
“Vipi kimetokea nini tena?”
“Hata mimi nashangaa nilikuwa nimefumba macho nikisubiri kuchomwa sindano lakini mzee nyonganyonga hakufanya hivyo na nilipofumbua nilikuta sindano imezama tumboni mwake na akaanguka chini!”
“Kweli?”
“Ndiyo! Sasa mnafikiri ni mimi ndiye nimemchoma?”
“Hapana siyo hivyo ila….!”
“Ila nini?” ”Basi tuyaache hayo kakueleza kitu chochote kabla hajajichoma?”
“Alipaanguka chini alianza kusema maneno ingawa kwa shida!”
“Alisema maneno gani?”
“Alisema amechoshwa na kazi ya kuua binadamu wenzake na hakuwa na jambo la kumjibu Mungu!”
“Mungu wangu! Sasa kwanini asingesema tu akabadilishiwa kazi?”
Prosper alibaki ameduwaa akiwashangaa maaskari walionekana kupigwa na mshangao mkubwa na hawakujua ni nini cha kufanya, mzee nyonganyonga alikuwa amelala chini sakafuni, mikono na miguu yake ikiwa imenyooka kuelekea darini! Macho na ulimi wake yakiwa yametoka nje alitisha na picha hiyo ilimuonyesha prosper ni kifo cha aina gani ambacho angekufa.
Aliogopa kupita kiasi na kujikuta akitetemeka mwili mzima lakini kwa sababu alishaamua kufa ili kukwepa mateso ya gonjwa la Ukimwi prosper aliamua kuipuuzia picha aliyoiona sakafuni na kuwageukia maaskari waliokuwa ndani ya chumba hicho.
“Afande!” Aliita na maaskari wote waliokuwa wameinamisha nyuso zao chini wakiushangaa mwili wa mzee nyonganyonga uliolala sakafuni waligeuka kumwangalia.
“Unasemaje prosper?”Wote waliuliza kwa mpigo.
“Sasa mtafanya nini?”
“Kuhusu?” ”Mimi nataka kufa!”
“Hautakufa tena prosper bado una siku nyingi sana za kuishi!”
”Si uchukue hilo bomba la sindano uvute dawa nyingine unidunge kipi kinachokushinda kama mnaogopa basi nitoeni hapa kwenye mashine nijidunge mwenyewe!”
“Haiwezekani tena prosper serikali imeamua kusitisha hukumu ya kifo uliyopewa tena una bahati nafikiri Mungu alikuwa hajapanga ufe kwa sababu mkeo amefika hapa na barua zikiwa zimebaki sekunde ishirini tu! Hapakuwa na njia yoyote ya kuwahi kama mzee Nyonganyonga asingejiua mwenyewe!” alisema mmoja wa maaskari.
“Ni nini mnasema nini nyinyi mbona siwaelewi?”
“Barua ni hii hapa imetoka kwa mwanasheria mkuu wa serikali hivyo haiwezekani kukuchoma sindano tena!”
“Hebu niione hiyo barua!”Alisema prosper kwa ukali kiasi kwamba maaskari walishindwa kumwelewa kwa sababu alitakiwa kufurahia kukwepa kifo akiwa juu ya kitanda cha mauti.
Askari aliyekuwa na barua hiyo mikononi alimsogezea prosper na kuifungua, prosper alianza kuipitia taratibu tangu mwanzo hadi mwisho wa barua lakini badala ya kufurahia alianza kupiga kelele.
“NATAKA KUFA!NATAKA KUFA! MIMI NATAKA KUFA SITAKI TENA KUISHI!” aliongea kwa sauti ya juu huku akijaribu kujitoa kwenye mashine iliyoshika mikono na miguu yake.
Maaskari waliamua kumfungua prosper akatoka kitandani na kusimama wima, wakiwa hawa hili wala lile maaskari walishtukia prosper anatimua mbio kulifuata bomba lililokuwa chini lengo lake likiwa ni kujichoma nalo ili afe alilifikia na kulishika lakini kabla hajalinyanyua na kutimiza azma yake mguu wa askari ulisimama juu ya kiganja chake prosper alipiga kelele sababu ya maumivu aliyoyapata.
“Kwanini unataka kufanya hivyo lakini yaani badala ya kufurahia amenusurika kifo kimiujiza unataka kufanya ujinga?”
“Braza mimi ni mtu mzima na akili zangu ukiona nataka kufanya jambo jiulize mara mbili kuna tatizo gani, hakuna mtu anayetaka kufa binadamu wote tunapenda kuishi! Kwa hiyo niache mimi nifanye ninavyotaka!”
“Haiwezekani! Afande hebu mtoe huyu chumbani mpeleke katika chumba cha washauri nasha nafikiri utakuwa na tatizo ambalo ni vyema tukalifahamu!” Askari magereza alimshika mkono prosper ambaye wakati huo aliendelea kulia mfululizo na kutoka naye hadi nje ya chumba cha kifo mbele kidogo aliingia naye katika chumba kilichoandikwa mlangoni “Ushauri Nasaha!” ambao walimkuta mama wa makamo akiwa amekaa nyuma ya meza kubwa.
“Vipi tena?”
“Hukumu yake ya kifo imesitishwa na serikali baada ya kugundulika dakika chache kabla ya kifo kuwa hakutenda kosa lililopelekea apewe hukumu hiyo!”
“Hongera sana kijana nakushauri ukitoka hapa uwe mwema mbele za Mungu kwani amekupa nafasi nyingine ya kunyoosha njia zako unasikia?”
“Usinipe hongera mama mimi sitaki kuishi na kama kuna uwezekano wa kuniua sasa hivi fanyeni hivyo haraka kwani nitajiua mwenyewe!”
Jipu la prosper lilimshtua mtoa ushauri nasaha, aligundua prosper alikuwa na tatizo kubwa lililohitaji muda mrefu wa kuongea naye!
“Kwanza hebu tufahamiane mimi naitwa mama Mpelumbe wewe mwenzangu unaitwa nani?” Mama huyo alianzaia mbali kidogo.
“Naitwa prosper!”
“Aisee wewe ndiye prosper?”
“Ndiyo mama ni vizuri ukiniita marehemu prosper sababu tayari nimeshakufa! Mimi ni maiti inayotembea!” ”Unamaanisha nini mwanangu?”
“Yaani mama hunielewi ninaposema mimi ni maiti inayotembea!”
‘Sikuelewi hata kidogo!”
“Na si mimi tu hivi sasa vijana wengi ni maiti zinazotembea! Ndiyo maana nataka kufa kwa sababu yaliyoko mbele yangu sitaweza kuyahimili!” ”Unamaanisha nini?”
Badala ya kujibu swali prosper aliyekuwa ametulia alianza kulia machozi.
Belinda alikaa nje ya gereza na mtoto wake mgongoni akiendelea kulia machozi!Alishangaa ni kwanini maaskari walichelewa kiasi hicho kurudi kutoka ndani, alijua kwa vyovyote mume wake alikuwa amekufa! Mawazo hayo yalimzidishia huzuni aliamini asingeweza kupambana na maisha peke yake aliumia juhudi zake zote za kumuokoa prosper zilikuwa zimegonga mwamba.
Ndani na nje ya moyo wake Belinda hakutaka kabisa prosper anyongwe alitaka aendelee kuishi tena wakiwa pamoja na mtoto wao wakisubiri kifo chao ifike n aikiwezekana wafe siku moja! Hakuwa tayari kubaki peke yake duniani akiteseka kumuuguza mtoto wao Alicia pia hakutaka kufa na kumwacha Alicia peke yake duniani kama yeye ndiye angetangulia.
Kifo ni kifo lakini sitaki Prospar afe ghafla kiasi hicho nataka niwe naye niteseke naye hadi mwisho wa maisha yangu! Prospar hana hatia na hastahili kunyongwa!” aliwaza Belinda .
Mom where is dady? Whay is not coming? I wanna talk to him please mom tell them to call him for us”(mama baba yuko wapi? Kwa nini haji? Nataka kuongea naye waambie basi wamwite!) Alicia aliyekuwa mgongoni kwa mama yake alisema maneno yaliyomuumiza moyo mama yake.
Badala ya kujibu swali lake Belinda aliangua kilio kilichomfanya mtoto wake bila kujua kilichomliza mama yake naye aanze kulia. Alicia alimpenda mno mama yake hakuwa tayari kumwona akilia.
“Mom stop Craying! Remember Christimas is just one day from to day and dady will be home to celeblate with us, that is what he told me the last time we came here! He also peomised to buy me a new dress!” (Mama acha kulia! Kumbuka krisimasi ni siku moja tu kuanzia leo na baba aliahidi kuja nyumbani kusherekea pamoja nasi! Aliniambia hivyo mara ya mwisho tulipokuja na aliniahidi ataninunulia gauni jipya!) Alicia alisema hayo bila kujua siku hiyo ndio baba yake alikuwa ananyongwa.!
Kufungwa na kuhukumiwa kifo cha prosper ndicho Belinda hakutata kabisa mtoto wake akijue aliamua kulifanya jambo hilo siri kwa sababu hakutaka kumuumiza moyo mtoto wake aliyeonekana kumpenda sana baba yake, siku zote alimwambia baba yake alikuwa gerezani kufanya kazi na alikuwa hapewi likizo sababu ya kazi nyingi.
Ghafla akiwa katika mawazo hayo Belinda alitupa macho yake upande wake wa kulia kupitia katika dirisha lenye nondo nene lililokuwa pembeni yake, alishuhudia mwili wa mtu ukiwa umebebwa na maaskari wasiopungua wanne ukitolewa ndani ya chumba na kupelekwa upande wa pili kulikokuwa na kijumba kidogo, ukutani mwa kijumba hicho kuliandikwa maneno “Mortuary!”
Picha hiyo ilimwonyesha Belinda wazi kuwa tayari mume na baba wa mtoto wake tayari alishaaga dunia, aliiona dunia imekuwa giza mwili wake ukalegea na ghafla alianguka chini akiwa na mtoto wake mgongoni.
“Mom!Mom! Mom! What has happen with you? Have you fallen asleep? Please wake up mom is time to go home and do chrismas preparation remember dad will be here in no time!(Mama! Mama!Mama! nini kimekupata? Umelala usingizi? Amka basi muda wa kwenda nyumban kujiandaa na krismasi umefika na baba atakuja hapa muda si mrefu!)Alicia aliongea huku akimpiga piga mama yake mgongoni lakini Belinda hakushtuka.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment