Simulizi : Kifo Cha Mtu Asiye Na Hatia
Sehemu Ya Tatu (3)
“Na wewe hicho kitoto chako unakipeleka wapi?” Walimuuliza Belinda kwa kejeli lakini hakuwajibu kitu alizidi kusonga mbele kuelekea nyumba kubwa waliyoishi.
Alikuwa nyumbani kwao kwa mara nyingine baada ya kukaa na kuteseka nje kwa muda mrefu, hakujua ni kitu gani kingetokea baada ya kukutana na baba yake lakini hilo hakulipa nafasi sana, alichotaka ni kukutana na baba yake na kumuomba msamaha basi!
Kabla hajaingia ndani mlango ulifunguliwa na baba yake alitoka nje na kumkuta, palepale sura yake ilibadilika.
Belinda aliendelea kulia akiwa amemshika mtoto wake Alicia mkononi na Prosper aliendelea kumbembeleza asilie lakini hakusaidia kitu! Kadri alivyobembelezwa ndivyo Belinda alivyozidi kutokwa na machozi, alilia akimwangalia mtoto wake kwa macho ya huruma.
Alikuwa na wasiwasi na hofu kubwa sana moyoni mwake, alijua kama kweli kifo cha Savimbi kilisababishwa na Ukimwi basi hata Prosper alikuwa ameambukizwa! Na kama Prosper alikuwa ameambukizwa Belinda alikuwa na wasiwasi ni lazima na yeye pia alikuwa ameathirika kwa sababu alikutana naye kimwili na matokeo yake yakawa mimba iliyowapa mtoto wao Alicia.
Wasiwasi wake haukuishia hapo ulivuka mpaka hadi kwa mtoto wao, Belinda alijua kama yeye alikuwa ameathirika lazima na mtoto wao pia alikuwa katika hali hiyohiyo! Hakuna kitu alichokiogopa maishani mwake kama ugonjwa wa Ukimwi! Aliujua ulivyotesa watu kabla ya vifo vyao, roho ilimuuma sana Belinda na kujikuta akimwaga machozi na kumtupia lawama nyingi Prosper.
“Prosper kwanini ulijiingiza katika mchezo huo na Savimbi?” Belinda aliuliza.
Badala ya kujibu swali aliloulizwa Prosper aliinamisha kichwa chini na kuendelea kulia, moyoni mwake alikuwa na maumivu makali na alijuta kwa uamuzi aliouchukua, hakuwa na namna ya kujitetea mbele ya Belinda, aliyoambiwa yote yalikuwa kweli tupu!
“Prosper naomba unijibu swali langu!”
“Darling huu sio wakati wa kunilaumu ninahitaji msamaha wako na msaada mkubwa wa mawazo! Niliingia katika mtego bila kujua hata mimi ninajuta! Nina uhakika nimeambukizwa na mwisho wa maisha yangu upo karibu, ingawa najua nitanyongwa kwa kesi niliyonayo Mahakamani nisingependa hata kidogo kufa kwa Ukimwi! Nisamehe mke wangu” Alisema Prosper huku akilia.
Maneno ya Prosper yaliuchoma moyo wa Belinda na kumfanya agundue kuwa kweli hakutakiwa kumtupia lawama nyingi kiasi hicho kwa wakati mgumu aliokuwa nao! Hilo alilifahamu lakini bado maumivu yaliendelea kuwepo moyoni mwake, hakutaka kuukubali ukweli kuwa alikuwa ameambukizwa Ukimwi na hakuwa tayari kulipokea jibu hilo hata kama angepimwa.
Moyo wa Belinda haukuwa tayari kwa matokeo ya Ukimwi na alijua angekuwa marehemu siku moja baada ya kupewa majibu ya damu! Jambo ambalo hakutaka kabisa litokee kwa sababu kufanya hivyo kungemaanisha mateso kwa mtoto wake Alicia ambaye angekuwa Yatima tangu siku hiyo.
Alipenda sana kujua hali yake kiafya lakini aliogopa kupima damu! Alichofanya Belinda ni kumshawishi Prosper apime na majibu ambayo angepata ndiyo yangeonyesha kama alikuwa ameambukizwa au la!
“Lakini kuna watu huwa wanatembea na watu wenye virusi vya Ukimwi na hawaambukizwi, acha nisimtupie lawama nyingi sana Prosper mpaka apime damu yake inawazekana hakuambukizwa lakini hata kama ni hivyo nitawezaje kuwa na mwanaume shoga?” Alijiuliza Belinda bila kupata majibu ya maswali yake na machozi yaliendelea kumbubujika.
Muda mfupi baadaye huku Prosper na Belinda wakiendelea kulia mlango wa chumba ulifunguliwa na maaskari Magereza wawili wakaingia hadi ndani ya chumba walichokuwa wameketi Belinda na Prosper.
“Dada muda umekwisha tunakuomba sasa uondoke!” Alisema mmoja wa askari Magereza, mwanamke mwenye umri kati ya miaka ishirini na tano hadi thelathini aliyemwangalia Belinda kwa macho ya huruma.
“Ahsante dada naondoka sasa hivi!” Alijibu Belinda huku akinyanyuka na kumfunga mtoto wake mgongoni kwa kutumia khanga ndogo ya India.
“Belinda umenisamehe mke wangu?” Prosper aliuliza wakati maaskari wakimnyanyua kutoka sakafuni alipokaa.
Belinda hakulijibu swali hilo alianza kutembea kuelekea nje ya Gereza, kichwani kwake kulijaa mawazo mengi kupita kiasi! Mbele yake aliona giza, kimawazo alijiona tayari yupo kitandani hoi akiugua Ukimwi kwa sababu tu ya uzembe wa Prosper!
“Wanawake wengi sana wanaponzwa na wanaume zao katika suala hili la Ukimwi, nimejitahidi kadri ya uwezo kuwa mwaminifu kwa Prosper lakini ameniangusha!” Aliwaza Belinda akitembea kuelekea kituo cha basi.
Mwili wa Belinda ulikuwa bado ukitoa harufu kwa sababu ya tundu alilolipata wakati wa kujifungua, kabla hajafika kituo cha basi kumbukumbu juu ya matatizo yaliyompata katika mabasi aliyopanda zilimrejea kichwani mwake, hakutaka kuzomewa tena na hakutaka tatizo lake limsumbue wala kumkosesha raha mtu yeyote! Kwa sababu hiyo Belinda aliamua kutembea kwa miguu kuelekea mjini Tabora.
****************
Aliingia Tabora mjini saa nane mchana jua likiwa linawaka kweli kweli, alitafuta kivuli na kuketi huku akitafakari nini cha kufanya, alipofikiria kwenda hospitali ya Kitete moja kwa moja alishindwa kwa sababu zilikuwa zimebaki siku saba kutimiza mwezi kabla hajarudi, alijua manesi wasingempokea mpaka tarehe aliyopewa kurudi hospitali ifike!
Uamuzi uliomwijia akilini mwake wakati huo ni kwenda kijijini Tutuo kusubiri mpaka tarehe ifike ndiyo aende hospitali kurekebishwa tundu lake, alisubiri kwa hamu kubwa sana siku hiyo! Alitamani sana kupona na kurejea katika hali yake ya kawaida, alikuwa amechoshwa na kuzomewa pamoja na masimango aliyokuwa akiyapata.
“Na hili tundu ni kipimo tosha kama nina virusi vya Ukimwi au la! likipona nitakuwa sijaambukizwa lakini likikataa kupona nitakuwa navyo!” Belinda aliwaza kulingana na taarifa zilizokuwepo mitaani juu ya uponaji wa vidonda vya watu wenye Ukimwi.
Baada ya kuwaza kwa muda mrefu akiwa amekaa chini ya mti wa Mwembe karibu kabisa na shule ya sekondari ya Mihayo, Belinda alinyanyuka na kuamua kutembea hadi kituo cha basi ambako alipanda basi lililomfikisha hadi kijijini Tutuo, mtoto wake Alicia alilia kwa njaa lakini Belinda hakuwa na kitu cha kufanya ilikuwa ni mpaka afike nyumbani kwao na Prosper ndipo apike uji na kumpa.
Alisababisha usumbufu mkubwa sana ndani ya basi lakini hakuna mtu aliyegundua kuwa ni yeye aliyesababisha hali hiyo itokee, alipoteremka kituoni alitembea moja kwa moja hadi nyumbani kwao na Prosper, njiani watu wengi walionekana kumshangaa na hakuelewa sababu ilikuwa ni nini! Aliifananisha hali hiyo na mara ya mwisho alipokuja kijijini na kukuta mama yao Prosper amefariki.
“Sijui kimetokea nini tena leo?” Alijiuliza Belinda.
Mita chache kabla hajafika nyumbani alishangaa kuona ukuta mkubwa wa mabati ukiwa umekizunguka kiwanja chote cha nyumba ya akina Prosper! Belinda alishindwa kuelewa ni nini kilitokea ila alijua lazima kulikuwa na tatizo na aligundua ni kwanini watu walikuwa wakimshangaa.
“Nikusaidie dada?” Aliuliza mtu aliyemkuta mahali pale, aliyeonekana kama mlinzi.
“Nauliza waliokuwa wakiishi hapa wamehamia wapi?”
“Walikiuza kiwanja chao kwa mwarabu mzee Mohamed na sijui wamehamia wapi!”
Belinda aliishiwa nguvu miguuni na kujikuta amekaa chini bila kujua la kufanya, alishindwa kuelewa angekwenda nyumbani kwa nani na kuishi mpaka tarehe ya kwenda hospitali ifike! Kwa hali aliyokuwa nayo na harufu aliyoitoa alijua kusingekuwa na mtu ambaye si ndugu kijijini pale ambaye angevumilia kuishi naye ndani ya nyumba yake.
“Kwani vipi dada?”
“Kwani wewe hunifahamu mimi?”
“Ndiyo nilikuwa nakuona nyumbani kwa Mwarabu Mzee Mohamed lakini sikufahamu vizuri!”
“Nilikuwa naishi hapa na akina Nyamizi na Kasanda kabla sijaanza kazi nyumbani kwa Mwarabu mzee Mohamed, niliacha kazi nilipotakiwa kwenda kujifungua na baada ya hapo nilikwenda nyumbani kwetu Dar es Salaam na sasa nimerudi tena Tutuo nategemeo langu lilikuwa kufikia hapa hapa!” Alisema Belinda huku akimtoa mtoto wake aliyekuwa akilia mgongoni na kujaribu kumnyonyesha lakini maziwa hayakuwemo kifuani kwake.
“Ukweli ndio huo dada sasa sijui utafanya nini!”
“Kaka yangu nina matatizo makubwa nafikiri hata hapo ulipo unasikia harufu ninayotoa, ni kazi ngumu sana kwa mtu yeyote kuishi na mimi ndani! Ninatakiwa hospitali ya Kitete kutibiwa ugonjwa wangu siku saba kuanzia leo yaani tarehe nne, ninachokuomba kama binadamu mwenzangu mwenye huruma nisaidie niwe naishi hapa ndani mpaka siku hiyo ifike!”
“Dada lakini nyumba hii itabomolewa tarehe tatu! Ninaweza kukusaidia mpaka tarehe mbili baada ya hapo itabidi utafute utaratibu mwingine sababu mzee Mohamed anataka kuweka mashine zake za kusaga”
“Ahsante sana kaka na sijui nikushukuru vipi!”
“Usijali dada yangu matatizo ni ya wote, nyumbani kwangu ni kijiji jirani lakini nitakusaidia chakula mpaka hiyo tarehe mbili, kila nitakacholetewa na mke wangu tutakula pamoja!”
“Mungu akubariki sana kaka yangu!” Alisema Belinda huku akinyanyua mfuko wake wa rambo na kuingia ndani ya ngome ya mabati baada ya mlinzi kufungua mlango.
Nyumba ilikuwa haijabomolewa ila ndani yake hapakuwa na kitu chochote, si kitanda wala jamvi! Kasanda na Nyamizi walishachukua kila kitu, Belinda aliwashangaa sana wasichana hao kwa kitendo chao cha kuuza shamba na kumsahau kaka yao aliyekuwa gerezani.
Alichukua kitenge alichokuwa nacho ndani ya mfuko na kukitandika chini na yeye pamoja na mtoto wake wakalala na kujipumzisha, Alicia hakulala sababu ya njaa! Mlinzi ambaye baadaye Belinda alimtambua kwa jina la Juma alikuja ndani kuuliza ni nini kilikuwa kinasumbua.
“Ni njaa! Hajala kitu tangu jana na maziwa kifuani kwangu hayatoshi”
“Subiri nije!”
Mlinzi alitoka nje na aliporudi alikuwa na chupa ya maziwa na kumkabidhi Belinda.
“Mnyweshe hayo maziwa!”
“Ahsante sana kaka! Si ninahitaji kuyachemsha?”
“Ukiweza kufanya hivyo ni vizuri zaidi!”
Belinda aliipokea chupa na kuiweka pembeni alitamani kuyachemsha maziwa hayo lakini kwa sababu hakuwa na sufuria alishindwa na kulazimika kumnyesha Alicia maziwa ya baridi, alijua kulikuwa na magonjwa kama Kipindupindu, Kuhara, Kifua kikuu ambayo hutokana na kunywa maziwa yasiyochemshwa lakini yote hayo alimwachia Mungu.Baada ya kunywa maziwa hayo Alicia alitulia na kulala usingizi.
***************
Belinda alikaa ndani ya nyumba hiyo kwa msaada wa mlinzi Juma mpaka tarehe mbili nyumba ilipobomolewa! Hakuwa na mahali pa kuishi tena ilibidi ampe shukrani zake Juma na kupanda basi lililompeleka moja kwa moja hadi mjini Tabora, siku hiyo alishinda na kulala mtaani na siku iliyofuata saa kumi na mbili za asubuhi alikuwa ameshafika hospitali ya Kitete.
Saa mbili kamili aliingia katika chumba cha daktari aliyefurahi kumwona Belinda tena.
“Belinda mwanangu umerudi?”
“Ndiyo baba!”
“Pole sana najua umeteseka kiasi cha kutosha lakini mateso yako leo yanafikia mwisho!”
“Kweli baba?” Belinda alimuuliza daktari.
“Ndiyo mwanangu!” Alijibu daktari huku akiandika kitu fulani kwenye karatasi, alipomaliza alinyanyuka na kumwomba Belinda amfuate na waliongozana hadi katika chumba kilichoandikwa Laboratory! Wote wawili waliingia hadi ndani.
“Mzee Simba naomba umpime huyu binti damu!”
“Sawa daktari!”
“Daktari!” Belinda aliita.
“Naam Belinda!”
“Unataka kunipima damu?”
“Ndiyo! Ni lazima tujue!”
“Lakini mimi sitaki kufahamu!”
“Hutaki kufahamu nini?”
“Sitaki kufahamu kuwa nina virusi vya Ukimwi!”
“Siyo hivyo Belinda hatukupimi Ukimwi! Tunataka kufahamu una damu kiasi gani kwa sababu utafanyiwa operesheni leo”
“Kama ni hivyo sawa!” Aliitikia Belinda.
Daktari na mzee Simba wote waliangua kicheko kwa woga aliouonyesha Belinda.
“Kwanini mnaogopa sana kupimwa Ukimwi?” Daktari alimuuliza Belinda.
“Basi tu mimi sipendi!”
Usiku wa siku hiyo baada ya majibu kuwa mazuri Belinda alipelekwa chumba cha upasuaji na kurekebishwa kasoro yake akawa mwanamke kamili tena lakini wasiwasi wake uliendelea kuwa juu ya Ukimwi.
*****************
Mwezi mmoja baadaye:
Hali ya Belinda ilikuwa nzuri kabisa, hakuwa na harufu tena! Furaha ilijaa maishani mwake kasoro pekee iliyomchukulia sehemu ya furaha yake ni tatizo la Prosper! Lakini aliendelea kujipa moyo kuwa huenda Prosper hakuambukizwa virusi vya Ukimwi na Savimbi.
Uhakika pekee angeweza kuupata kwa kuongea na Prosper mwenyewe na kupata taarifa za majibu ya damu aliyomwomba apime! Baada ya kutoka hospitali aliamua kwenda moja kwa moja gerezani Isanga lengo lake likiwa kwenda kuyaona majibu ya damu ya Prosper.
*****************
Prosper alikuwa amekonda na alionekana mwenye mawazo mengi kupita kiasi na muda wote wakati wakiongea aliendelea kulia akimwomba Belinda msamaha kwa yote yaliyojitokeza.
“Prosper nieleze juu ya majibu yako ya damu!” Belinda aliuliza.
Walikuwa watu watatu tu ndani ya chumba Prosper alipoanza kueleza kila kitu kilichokuwa kikiendelea mwilini mwake.
“Nieleze kwanza juu ya majibu, hayo mambo ya homa na kuharisha yaache kwanza, nieleze kwanza juu ya majibu nataka kujua ukweli huo!” Belinda alizidi kumbana.Dunia ilionekana kubadilika na kuwa sehemu ya mateso makubwa kwa Belinda. Hakuamini kama binadamu wote waliishi katika shida kama alizokuwa nazo yeye, alibadili matatizo kama nguo! Likitoka hili linaingia jingine, Belinda alihisi kukata tamaa. Baya na lililomsumbua zaidi lilikuwa ni la virusi za Ukimwi ambavyo alihisi Prosper aliambukizwa na Savimbi katika mchezo wa wanaume kwa wanaume kuingiliana gerezani.
Belinda alikuwa ameamua kuufahamu ukweli
wa majibu ya damu kutoka kwa Prosper ili auondoe wasiwasi moyoni mwake
“Ulipimwa damu?”Belinda alimuuliza
Prosper!
“Ndiyo nilipima
Belinda!”
“Majibu yako
wapi?”
“Ninayo!”
“Nipe basi
niyaone!”
“Naogopa
kukupa!”
“Kwa nini? Wewe nipe
tu!”
“Sijui kama utaweza
kuyakubali!”
“Kwani una virusi katika damu yako
Prosper?”
“Nd….i…o Belinda ila nisamahe sana!”
Prosper alianza kulia machozi na alishindwa kumwangalia Belinda
usoni.
“Kweli?” Belinda aliuliza tena, hakuliamini
jibu alilopewa.
“Prosper tafadhali nionyeshe cheti chako
cha majibu!” Aliendelea kusisitiza Belinda.
“Niamini na naomba unisamehe sana
Belinda!”
“Nipe cheti Prosper siwezi kuamini hivi
hivi!” Belinda alisema kwa ukali.
Katika maisha yake Prosper hakuwahi
kumwona Belinda katika hali hiyo, ilimlazimu aingize mkono ndani ya kaptura
yake, alionekana akivuta kitu fulani ndani ya nguo yake ya ndani na mkono
ulipotoka ulikuwa na kikaratasi kidogo kilichokunjwa kikiwa kimelowa jasho
alimkabidhi Belinda!”
Huku akitetemeka Belinda alianza
kukikunjua kikaratasi hicho na kuanza kukisoma, kadri alivyozidi kusoma ndivyo
machozi yalivyozidi k ummiminika hatimaye alijikuta akilia machozi huku kichwa
chake akiwa amekiinamisha chini! Kilionyesha tayari Prosper alikwishaambukizwa
virusi vya Ukimwi.
“Hivi mimi nina mkosi
gani?”
“Wewe huna mkosi hata kidogo Belinda,
mwenye mkosi ni mimi niliyewaua wewe na mwanangu bila
hatia”
“Prosper ni heri ningekufa mimi kuliko
Alicia ana makosa gani mtoto huyu?” Aliongea Belinda huku akizidi
kulia.
Prosper alipomwangalia mwanae Alicia
mikononi mwa mama yake naye alijikuta machozi mengi zaidi yakimtoka, alijilaumu
kwa kila kitu kilichotokea na alijilaumu kwa kuua watu wasio na hatia,
alijisikia mkosaji mbele za Mungu na mbele za Belinda na Alicia! Kwa kosa hilo
aliamini hakustahili kuishi.
“Prosper nimejitahidi kuwa mwaminifu kwako
lakini bado umeniua, nimeacha mambo mengi pamoja na utajiri wa baba yangu kwa
ajili yako na ninateseka leo hii tena umenitia virusi vya Ukimwi mwilini
mwangu!”
“Belinda ni shetani aliniingia usinilaumu
sana Belinda utanifanya nikose sababu ya kuishi!” Prosper alipiga magoti mbele
ya Belinda na kuanza kumshika miguu kama ishara ya kumwomba
msamaha!
“Hii haitoshi Prosper umekwishaniua basi
inatosha!”
“Sikujua itakuwa hivyo Belinda ilitokea
kama ajali na kama ningepewa nafasi nyingine nisingefanya hivyo na ninajuta
moyoni mwangu nisamahe Belinda kwa kukatisha maisha
yako!”
Belinda hakujibu kitu alibaki amesimama
wima mtoto wake akiwa mgongoni, alihisi akili yake kuchanganyika, ubongo wake
kusimama kufanya kazi sawasawa, alijilaumu kwa kila kitu alichokifanya maishani
mwake.
Hakuwa na kimbilio tena maishani kwake na
alikiona kifo chake kikija kwa kasi! Katika maisha yake hakuna kitu alichoogopa
kama kifo cha Ukimwi kwani kiliwatesa watu wengi na kilionekana kama kifo cha
aibu na hakutaka kufa katika jina la umalaya kama jinsi watu wengi
walivyokitafsiri kifo cha Ukimwi, Belinda aliamini hakuwahi kuwa malaya katika
maisha yake.
“Prosper!”
“Naam
Belinda!”
“Sitakusamahe maishani mwangu na hata kama
nitakusamahe basi sitasahau siku zote!” Alisema Belinda na kuanza kutembea kwa
haraka kutoka chumbani kwenda nje ya gereza.
“Belinda! Belinda! Belinda usiondoke!”
Prosper aliita wakati Belinda akitoka chumbani lakini hakugeuka kuangalia
nyuma alizidi kutembea kwa haraka huku akilia.
*****************
Alitoka hadi nje ambako alitembea hadi
kituo cha mabasi madogo na muda mfupi baadaye daladala moja lilikuja na kusimama
pembeni yake, alimbeba vizuri mtoto wake na kuingia ndani na kuchukua kiti cha
nyuma kabisa, alikuwa bado na hofu ya kusababisha harufu lakini alipokumbuka
kuwa alishafanyiwa operesheni na kuwa mkavu hofu hiyo ilitoweka mara
moja.
Belinda aliendelea kububujiwa na machozi
hadi wakati anafika mjini, watu wote ndani ya gari walimshangaa na walipomuuliza
ni kwanini alilia machozi kiasi kile hakueleza
chochote.
Alipomwangalia mtoto wake mzuri Alicia,
aliyekuwa ameketi mikononi mwake roho yake ilimuuma zaidi, alikuwa mtoto mzuri
mno kufa kwa Ukimwi! Ilimuuma sana Belinda kujua kuwa hata mtoto wake hakuwa na
maisha marefu mbele yake, lakini Alicia hakuwa na taarifa na kilichokuwa
kikiendelea aliendelea kutabasamu huku akimpigapiga mama yake
usoni.
Alipofika mjini Tabora aliteremka ndani ya
basi, alihisi kukata tamaa ya kila kitu! Hakuona sababu ya kurudi tena Tutuo,
kijijini kwao Prosper alichofikiria wakati huo ni kurudi tena Dar es Salaam
kwa baba yake na kujaribu kumwomba msamaha! Lakini alipokumbuka jinsi baba yake
alivyomfukuza kama mbwa roho iliingiwa wasiwasi na kujikuta akisita kuchukua
hatua hiyo.
“Kwa kweli baba asingekuwa na matatizo
ningerudi Dar , acha tu nirudi Tutuo!”
Baada ya kuwaza sana hatimaye mawazo yake
yalimfikisha katika hatua hiyo lakini alipokumbuka kuwa nyumba aliyofikia
ingekuwa tayari imekwishabomolewa na mwarabu aliyeinunua ili ajenge mashine,
Belinda alikosa mahali pa kuelekea kwa sababu hakuona mahali pengine popote
pa kufikia kijijini Tutuo.
“ Lakini acha tu niende, Wanyamwezi ni watu
wakarimu sana, nitaomba kukaa kwa mtu yeyote au nitarudi tena kuomba kazi
nyumbani kwa Mwarabu Mzee Mohamed nafikiri safari hii atakubali kwa sababu sina
mimba na sinuki kama ilivyokuwa zamani!”
Belinda aliamua kurudi kijijini na
alichofanya ni kwenda stendi ya basi ambako alipanda basi la kumpeleka kijijini
Tutuo, njia nzima aliendelea kulia alijua maisha yake yalikuwa yamefika mwisho!
Alihisi hakuwa na maisha tena mbele yake, binafsi hakujionea huruma sana
aliyemtia simanzi zaidi alikuwa ni mtoto wake
Alicia.
“Masikini Alicia anakufa kwa kosa lisilo
lake akini kwanini hasa mtu amuue mtoto asiye na hatia? Prosper alishindwa
kuvumilia shida? Nasema sitaki kumwona tena maishani mwangu!” Alisema kwa
uchungu Belinda, hakujua alikuwa akiongea kwa sauti kiasi kwamba watu wote ndani
ya basi waligeuka kumwangalia.
*******************
Gerezani:
Baada ya kuachwa chumbani Prosper
alinyanyuka kwa unyonge na kutembea hadi chumba cha mahabusu na kwa muda mrefu
aliendelea kulia na hakuona tena sababu ya kuendelea kuishi, alitamani kufa
kukwepa aibu ya kuwaua mke na mtoto wake kwa Ukimwi lakini alishindwa kuelewa ni
kwa njia ngani angeweza kujitoa uhai akiwa ndani ya
gereza.
Alilia usiku mzima hadi asubuhi, alijuta
kwa yote aliyoyafanya na alitamani sana kuonana tena na Belinda ili apate
kuongea naye na kumwomba msamaha! Alijua hilo lisingewezekana hata kidogo
kwani alikuwa na uhakika Belinda asingerudi
tena.
“Laiti ningejua nisingejiingiza katika
mchezo huo mbaya, shida za gerezani zingeniua mbona watu wengine wanaishi?”
Aliwaza Prosper huku akilia.
Prosper alikuwa na watu wengi sana wa
kuwalaumu kuhusiana na suala hilo lakini watu waliopaswa kuzibeba lawama zote
hizo walikuwa ni mama na dada zake kwa kitendo chao cha kumuua baba yake, bila
wao kufanya hivyo Prosper aliamini asingeingia gerezani katika maisha
yake!
“Ni wao ndio walilaumiwa niliingia gerezani
kumwokoa mama na dada zangu, mama mwenyewe amekwishakufa na hata hao dada zangu
hakuna hata mmoja anayefika hapa gerezani kunitembelea na bado nyumba na
kiwanja alichoacha baba wameuza na kupotea, huu ni ukatili wa hali ya juu sana!”
Aliendela kuwaza Prosper.
Baada ya siku hiyo Prosper hakuwaona tena
Belinda na mtoto wake Alicia, kesi yake iliendelea katika mahakama kuu kanda
ya Tabora na miezi mitatu baada ya Belinda kuondoka kesi hiyo ilifikia hukumu
yake, alionekana kuwa na hatia mbele ya sheria baada ya yeye mwenyewe kukiri
mauaji hayo ya baba yake mzazi mbele ya jaji Mohamed Simbila na kuhukumiwa
kifo kwa kuchomwa sindano ya sumu
Mahakama nzima ilipigwa na butwaa baada ya
hukumu hiyo, Prosper hakuonyesha huzuni wala kulia badala yake alitabasamu
kwa furaha baada ya hukumu hiyo kutolewa.
“Una namna yoyote ya
kujitetea?”
“Sitaki kujitetea Mhesimiwa Jaji, hukumu
yako ni sahihi na hii ndiyo niliyoisubiri ili iniepushe na kifo cha mateso
kilichopo mbele yangu!Nakushukuru sana mheshimiwa jaji na ninakupongeza sana
kwa hukumu hiyo nzuri!” Alisema Prosper huku
akicheka.
Bila kuchelewa maaskari walimpiga pingu
mkononi na kumwondoa mahakamani, jaji aliyemkuhumu alibaki na maswali mengi sana
kichwani mwake, alishafanya kazi ya kuhukumu watu kwa miaka karibu ishirini na
alishahukumu watu wengi kifo lakini hakuwahi hata siku moja kumhukumu mtu kifo
akicheka! Wengi walilia na kuomba kupunguziwa kifungo!
Siku iliyofuata Prosper ilitolewa amri
Prosper ahamishiwe gereza la Keko jijini Dar es Salaam ambako angepambana na
kifo chake! Alipakiwa ndani ya treni la abiria kutoka Mwanza kwa safari ya
kwenda Dar es Salaam.
Prosper alilia lakini hakulia sababu ya
hukumu ya kifo aliyopewa ila alilia kwa sababu alikuwa anapelekwa kufa bila
kuonana na mke na mtoto wake kwa mara ya mwisho, alikuwa anakwenda kufa bila
Belinda kufahamu ukweli juu yake! Pia alilia sababu yeye alikuwa anakwenda kufa
na kuwaacha mkewe na mwanae wakiteseka kwa ugonjwa wa Ukimwi aliowaambukiza
yeye.
*****************
Alicia, kijijini
Tutuo:
Tayari alishazoea maisha ya nyumbani kwa
mzee Mohamed, alifanya kazi kwa nguvu zake zote ili aweze kumridhisha mama
mwenye nyumba, alipewa chumba kidogo ambacho alilala na mtoto wake kwa kutandika
jamvi chini kila siku!
Ilikuwa ni kawaida yake siku zote kudamka
mapema na kufanya kazi zote za ndani na ilipotimu sawa nne aliacha kazi hizo na
kuanza kupasua kuni, baada ya kupasua kuni alianza kupika chakula cha mchana
na baadaye alianza shughuli za ufuaji wa nguo za kila mtu
nyumbani.
Zilikuwa ni kazi ngumu lakini Belinda
alizifanya ili aweze kuishi na mtoto wake, katika miezi yote aliyokaa
nyumbani kwa mwarabu Mzee Mohamed hakuwahi kumkumbuka Prosper lakini asubuhi ya
siku hiyo akipasua kuni kumbukumbu za Prosper zilimsumbua kichwani, alitamani
sana kumwona na aliona uamuzi aliouchukua haukuwa wa busara kwa sababu
usingeweza kuubadilisha kitu chochote katika maisha yake kama ni virusi
alishavipata na ni lazima yeye na mtoto wake
wangekufa.
“Ninaamini hivi sasa Prosper anahitaji
msaada wangu kuliko wakati mwingine wowote katika maisha yake!” Aliwaza Belinda
huku akiendelea kupasua kuni.
Alimfikiria Prosper kwa muda mrefu hatimaye
aliamua kuliweka shoka pembeni na kuketi chini, mawazo juu ya Prosper
yaliendelea kumiminika mwake.
“Hapana nakwenda gerezani!” Alisema Belinda
na kulitupa shoka pembeni, akambeba mtoto wake mgongoni na kwa kutumia khanga
yake iliyochanika alimfunga vizuri na kuondoka kuelekea ndani ambako alimkuta
mke wa mzee Mohamed na kumwomba ruhusa lakini hakuruhusiwa
kuondoka.
“Belinda wewe hapana ondoka iko kazi nyingi
leo!”
“Hapana mama ni lazima nikamwone Prosper
nikishindwa leo ni mpaka wiki ijayo!”
“Hapana!” Mke wa mzee Mohamed alikataa
katakata.
“Mama nimekwishasema naondoka,nitafanya
kazi nikirudi!” Belinda alisema na kunyanyuka.
“Wewe ondoka kwa nguvu eh! Pana rudi
hapa!”
“Sawa
mama!”
*****************
Alifika gerezani saa nne asubuhi, kitu cha
kwanza alichofanya ni kuomba kuitiwa Prosper.
“Dada yangu ulikuwa wapi siku zote
hizi?”
“Nilikuwa safarini!” Belinda
alidanganya!”
“Karibu
sana!”
“Ahsante! Prosper
yupo!”
“Prosper?” Askari magereza
aliuliza.
“Ndiyo mbona unauliza kwa
mshangao!”
“Amesafirishwa jana kwenda gereza la Keko
Dar es Salaam, alihukumiwa kifo!
Belinda alichanganyikiwa na kwa kutumia
basi alirudi hadi mjini ambako alipanda basi jingine lililompeleka hadi Tutuo.
Hakukaribishwa tena nyumbani kwa mzee Mohamed na kwa sababu hakuwa tena na
haja ya kufanya kazi aliomba mishahara yake na kuondoka tena hadi stesheni ya
treni mjini Tabora ambako alipanda treni jioni ya siku hiyohiyo kurejea Dar es
Salaam lengo lake likiwa ni kuishi kabla Prosper
hajanyongwa!
*******************
Treni iliingia Dar es Salaam saa saba
mchana, Belinda aliona bado muda ulimruhusu kwenda gerezani Keko kuonana na
Prosper, hakutaka kabisa afe kabla hajaongea nae na kumjulisha kuwa tayari
alishamsamehe yote yaliyotokea.
Kutoka stesheni ya reli ya Dar es salaam
hadi gereza la Keko ilikuwa kama nusu kilometa hivi, kwa umbali huo mdogo
Belinda hakuhitaji gari alitumia njia ya mkato hadi kufika
gerezani.
“Dada mwenye mtoto nikusaidie nini?” Askari
magereza aliyekuwa akilinda nje ya gereza
alimuuliza
“Nimekuja hapa kumwona mume
wangu!”
“Leo siyo siku ya kuwaona wafungwa njoo
Jumamosi ama Jumapili umesikia!”
“Sawa lakini……..!” Alisema Belinda huku
akimsogelea askari.
“Lakini nini? Dada hiyo ni sheria ya
gereza!”
“Nilikuwa naomba kukuuliza kitu sababu
sijui!”
“Kitu
gani?”
Belinda alimsimulia askari huyo kila kitu
juu ya Prosper na kwamba alitaka kuhakikisha kama kweli alikuwepo gerezani au
la!
“Katokea gereza
gani?”
“Isanga
Tabora!”
“Nisubiri hapa niulizie!” Alisema askari
huyo na kuingia hadi ndani ya gereza na alipotoka alikuwa na jibu la
Belinda.
“Nasikitika
hayupo!”
“Hayupo? Hayupo vipi wakati mimi Tabora
wamenieleza amehamishiwa gereza hili!”
“Amepelekwa gereza la Segerea sababu hapa
hakuna nafasi ya wafungwa kama yeye!”
“Ah! Sawa nashukuru sana kaka yangu!”
Belinda alishukuru lakini hakuwa tayari kusubiri hadi jumamosi ndio aonane na
Prosper alihisi kufikia siku hiyo tayari angekuwa
amekwishayongwa!
“Na nitakwenda huko segerea
wakinizuia nitatumia hata hii pesa kidogo niliyonayo mpaka nimwone!” Aliwaza
Belinda.
Kutoka gerezani Keko hadi kituo cha mabasi
cha Shule ya Uhuru ambako mabasi ya Tabata na Segerea yaliegeshwa ilimchukua
dakika 30 na kutoka shule ya Uhuru sababu ya ubovu wa barabara ya Tabata
ilimchukua saa nzima hivyo alifika gerezani segerea saa tisa na nusu ya jioni
na kwenda moja kwa moja hadi mapokezi ambako alimkuta askari magereza wa
kike.
“Shikamoo dada!” Belinda
aliamkia.
“Marahaba, nikusaidie nini mdogo
wangu?”
‘Dada unavyoniona hivi ninatoka Tabora,
huyu ni mwanangu nimekuja hapa kumfuata mume wangu anaitwa Prosper, yeye
kahamishwa kutoka gereza la Isanga huko Tabora ni mfungwa aliyehukumiwa kifo,
nataka kumwona kabla ya kifo chake.
“Kwani vipi mbona unanieleza vitu vingi kwa
wakati mmoja?” Askari magereza aliuliza.
“Nisaidie dada, nisaidie mimi mwanamke
mwenzio!” Aliendelea kusema Belinda na baadaye kumsimulia askari huyo kila kitu
kilichotokea katika maisha yake na Prosper, askari alishindwa kujizuia na
kujikuta akichukua kitambaa chake na kujifuta machozi usoni
mwake.
“Ni sawa nimehuzunishwa sana lakini sina
jinsi ya kukusaidia kwa sababu si rahisi kukuingiza gerezani siku ya leo mdogo
wangu,nenda uje Jumapili!”
“Dada tafadhali
nisaidie!”
“Haiwezekani labda nimwite tu umwone kwa
mbali lakini siwezi kukuruhusu uingie ndani ya gereza, kwani unaitwa
nani?”
“Naitwa
Belinda!”
“Belinda
nani?”
“Belinda Thomson
Komba!”
“Thomson Komba yule
mfanyabiashara?”
“Ndiyo!”
“Sawa wewe mbona una hali
hiyo?”
“Maisha tu dada yangu!” Belinda alijibu
huku akilia.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment