Simulizi : Lidake Tena Chozi Langu
Sehemu Ya Tano (5)
YULE mzee pembeni yangu alinitazama katika namna ya kunitilia mashaka. Awali nilidhani ataishia kunitazama mara moja na kuachana na mimi lakini ajabu sasa alizidi kukazia kuwa anamashaka na mimi. Ubaya ni kwamba huyu hakuwa wa kabila langu labda ningeweza kumsihi na angeweza kuwa ha huruma. Nilijaribu kumpuuzia yule mzee lakini sasa alimgusa bega abiria mwingine. Alipogeuka akamwonyeshea kidole kuja kwangu. Wakagusana kadhaa na kisha mmoja akasimama na kunifuata pale nilipokuwa. “Msinigusie mwanangu nasema….” Mama alikaripia baada ya wale watu walipoanza kunizongazonga wakidai wana mashaka juu yangu. “Watu wanabeba misukule wanatuletea mikosi tu safarini.” Ilikuwa sauti ya kondakta wakati huo akiwapangua abiria kadhaa na kunifikia. Sasa mjomba wangu alisimama na kunikingia kifua, akadai kuwa ikiwa kondakta anataka shari basi athubutu kunigusa. Hapo zikaanza vurugu, kundi kubwa likitupinga, nadhani walikuwa sawa kabisa kutuona kuwa sisi ni watu wabaya lakini wangejua magumu yote niliyoyapitia si wanawake si wanaume wote wangefunikwa nyuso zao na machozi. Kondakta alifika na kumsukuma mjomba wangu na hapa ndipo nikaelewa nini maana ya damu nzito kupita maji. Mjomba alifyatuka na kumtandika kichwa kikali sana yule kondakta. Palepale akaanza kuvuja damu na hapo watu wengine wakatishika. “Wapumbavu wakubwa nyie.,.. wapuuzi kabisa na imani zenu dhaifu kabisa. Gari lenu bovu mnaanza kubughudhi watu… sasa mwingine anayejiamini amsogelee mpwa wangu!!” aling’aka. Nikayakumbuka maneno ya mama ambayo aliwahi kunieleza zamani sana kuwa ana mdogo wake ambaye ni mpole sana lakini ukitaka kumkera wewe mguse tu ndugu yake ama rafiki yake. Hasira yake haipoozwi kwa namna yoyote na yupo radhi ajeruhiwe lakini si mwepesi kukubali kushindwa. Hakuna mtu aliyesogea, yule kondakta akajaribu kumtupia teke mjomba. Kilichomtokea akadakwa mguu na kisha kutupwa mbali. Kikasikika kilio cha maumivu!! “Tupatie nauli yetu na tutashuka!! Tuwaache na gari lenu bovu!!” alizidi kuwaka mjomba wangu ambaye mwili wake ulikuwa wa wastani tu. Mjomba akiwa hajui hili wala lile mara ghafla dereva wa lile basi aliingilia kati, akarusha ngumi mjomba akaikwepa akarusha teke likampata mjomba. Mjomba akiwa hajatulia mara nikashuhudia yule dereva akijipekua na kutoka na bisibisi, nikapiga kelele lakini nilikuwa nimechelewa sana yule dereva akamfikia na kumchoma begani. Kizaazaa!! Mjomba aliendelea kupambana huku mama akijaribu kuachanisha ugomvi ule. Mwisho wa hili tukio hili tulisukumwa nje ya gari kwa sababu mjomba alikuwa amejeruhiwa tayari hivyo hakuweza kupambana. Basi abiria wakatusukuma nje. Nikiwa sina hata mkono mmoja nikaanguka na kujipigiza kichwa chini katika barabara ya vumbi. Kumbe wakati naanguka mama yangu alimuona mwanamke ambaye alinisukuma, nilipogeuka nikakuta vurumai ya hali ya juu sana. Mama alikimbia na kumchomoa yule mwanamke kutoka katika kundi la abiria wale na kuanza kumshushia kipigo huku akizungumza maneno mengi. “Unamjua huyu mtoto nimepitia naye uchungu gani we mwanahizaya.. sasa leo utatambua nini maana ya uchungu wa mwana aujuaye mzazi” alimgalagaza yule mwanamke pale chini. Yule mwanamke alipiga mayowe ya uchungu mama akaendelea kumkaba huku akimpa kichapo cha uhakika. Nikiwa pale chini nikazitazama mbingu na kumshukuru Mungu kwa sababu alikuwa akinionyesha maana ya pendo la mama. Nilijisikia fadhaa sana kwa sababu sikuwa na mikono ya kumsaidia. Laiti kama ningekuwa mzima nilikuwa nakaribia kuingia chuoni na bila shaka baada ya hapo ningekuja kumsaidia mama yangu, kumtoa katika dimbwi la umasikini na shida zile zilizopitiliza. Wakati nayawaza haya mara nilimuona mwanaume mmoja akimwendea mama yangu na hapo akampiga teke kali mgongoni. Ndugu msikilizaji, mama alimwambia yule mwanamke kuwa uchungu wa mwana aujuaye mzazi. Hii ikawa zamu yangu kumwonyesha yule bwana kuwa licha ya kwamba sina mikono lakini siwezi kuhimili kushuhudia mama yangu akiumizwa vile. Nilijikuta nipo wima na mbio mbio nilimfikia yule mwanaume. Ilikuwa kama nilivyomkabili yule mwanasiasa. Na huyu nikamtia meno katika bega lake na hakuweza kuchomoka kirahisi hadi nilipomwachia akaanguka chini huku akilia kwa uchungu mkubwa!! Wakati huo gari lilikuwa limetengemaa, wakambeba yule mwanaume na kumpakia garini. Kisha tukatengwa na kuachwa pale chini. Mimi, mama na mjomba wangu ambaye lile jeraha lilikuwa limemlegeza sana na mama yangu alikuwa ameumizwa na lile teke alilopigwa na na yule bwana. “Majaliwqa mwanangu, huwezi amini nina furaha kubwa sana moyoni, ninafurahi kwa sababu nipo hapa na wewe. Ukifa nitakufa mwanangu sitakuwa na sababu yoyote ya kuishi bila wewe. (akasita kisha akamgeukioa mjomba)… Emma asante sana mdogo wangu, yaani umenipa sababu ya kutabasamu. Asante kwa kumtetea mwanangu. Najisikia vibaya sana kwa sababu hatujaweza kufika tunapotakiwa kufika lakini hebu tuungane na kumuombha Mungu maana ni yeye anayeruhusu haya yote yatokee. Tazama tupo jangwani hapa sijui hata ni wapi hakuna nyumba za kuishi wala maeneo yoyote ya biashara lakini amini kuwa yeye anatuona na anajua kuwa kwa akili zetu hapa hatuwezi kutoka. Amini kuwa asipotutumia msaada basi atakuwa pia ametupangia jambo ambalo ni jema kwake…” mama alizungumza kwa sauti ya chini huku sasa akisimama na kujikongoja huku akiwa ameinama, bila shaka alikuwa akipitia maumivu makali ya mgongo baada ya kukanyagwa na yule bwana. Alinifikia na kunikumbatia kisha tukasogea hadi alipokuwa ameketi mjomba. “Naishiwa nguvu na ninahisi kizunguzungu… sijui kama nitapona… najisikia vibaya sana…” mjomba alilalamika huku akiwa analigandamiza bega lake. Alikuwa amevuja damu sana hakika na kama alivyosema ilikuwa ni nadra sana kupona hasahasa eneo kama lile ambalo hatukuwa na msaada. Mama shujaa hakuacha kauli ya mjomba iwe neno la mwisho. Akaondoka na kunisihi nisisogee popote pale nitulie na mjomba wangu. Akaondoka kwenda kutafuta msaada wowote ambao utapatikana. Alitumia takribani dakika thelathini, nikaanza kupatwa na mashaka juu ya baya lolote ambalo limemkuta mama yangu. Tatizo aliniambia nisitoke pale kabisa alipokuwa amejilaza mjomba. Yale mashaka juu ya mama yakanifanya kwa muda nisahamu kumtazama mjomba. Na nikiwa bado pale mara nikaona gari ikitokea mahali kuja upande wetu. Nikamshtua mjomba ili aamke kuitazama gari ile ndogo. “Mjomba… mjomba…” nilimuita lakini hakunijibu na ile gari ilizidi kukaribia eneo tyulilokuwepo. Nilimtikisa mjomba wangu lakini hakusema neno lolote.] Hatimaye gari likafika tulipokuwa, mjomba hakuwa ameamka na ndani ya gari akashuka mama akiongozana na wazungu wawili. Akawaonyeshea kwa kidolea lipokuwa mjomba. Walau kidogo nikapata nafuu. Kwani nilikuwa nimeingiwa na mashaka kuhusu mama yangu. Nikatabasamu lakini tabasamu lile halikudumu kabisa baada ya wazungu wale kuzungumza kwa lugha ya kiingereza kuwqa mjomba wangu alikuwa amekufa tayari. Ndugu msikilizaji nililia sana hakika, nililia kupita maelezo. Mama kiutu uzima alijikaza lakini macho yake yalikuwa mekundu sana. Wale wazungu wakajadiliana na kisha wakapiga simu. Baada ya muda mrefu kiasi ikafika gari ya kubeba wagonjwa na kuubeba mwili wa marehemu mjomba wangu. Mjomba aliyenipigania hadi dakika yake ya mwisho, mjomba aliyekufa kwa sababu alikuwa akinipigania mimi. Niliumia na hadi ninaposimulia mkasa huu maumivu yale hayajaisha katika moyo wangu. Naam! Tukaondoka na gari ile ikawa ni safari ya kuelekea Dodoma lakini mimi nilizungumza na wale wazungu na kuwaeleza ni kiasi gani nitaishi maisha ya mashaka nikirejea Dodoma. Wale watu walikuwa na utu sana walilalamika sana juu ya imani hizo dhaifu na baada ya pale wakakubaliana kuwa mmoja kati yao atangulie na mimi jijini dare s salaam na mama akashughurikie suala mla kumzika mjomba. Mama hakuwa tayari kuniacha katika mikono ya mtu yeyote yule na hakutaka kumuamini mwanadamu. Akagoma katakata!! Akasema ni heri aambatane nami kila kona!!*************Mama aliendelea kusimamia msimamo wake uleule kuwa hayupo tayari kuamini mtu yeyote tena. Ataandamana na mimi kila sehemu ilimradi tu auone mwisho wangu aidha uwe mzuri ama mbaya.Msimamo wa mama ukasababisha liibuke wazo jipya kutoka kwa watu wale waliokuwa wamekusudia kutusaidia.Wakaniuliza juu ya ndugu tuliokuwanao Dodoma, nikamuuliza mama swali lile kwa sababu wao waliniuliza kwa kiingereza. Mama akasema hatukuwa na ndugu kule.Basi kwa sababu hatukuwa na ndugu tukaona ni vyema na haki kumpumzisha mjomba katika kijiji kile tuwatafute wasamaria kadhaa tulichimbe kaburi na kumpumzisha pale.Hilo tukaliafiki kwa pamoja!!Kweli ikawa, mjomba akalala katika ardhi isiyokuwa yake.Naam! Haikuwa sawa lakini tusingekuwa na la kufanya kwa sababu mambo yalikuwa mabaya haswa!!Baada ya hapo safari ya kuelekea jijini ikafuata.Tulisafiri usiku na alfajiri ilitukuta tupo jijini Dar es salaam.Hakika mama alikuwa amemaanisha aliposema ataandamana nami popote iwe kwa heri ama shari.Mama hakukubali kulala chumba tofauti na mimi.Alisema kuwa ameishi nami miaka yote akinilea mwenyewe na sasa sina mikono linabaki kuwa jukumu lake kunilea mimi upya hivyo ni sawa tu nitalala naye vchumba kimoja hadi hapo hali ya hewa itakapokuwa tulivu.Wale wazungu hawakupinga, tukalazwa chumba kimoja na mama akawa mtu wa mwisho kabisa kuufunga mlango. Akanilaza kitandani na yeye akaketi katika kochi ambalo alikuwa ameliweka mlangoni kiusalama.Nilimuonea sana huruma mama yangu, maisha yale ya mashaka yalimfanya akakakonda sana. Alikonda kiasi kwamba ukimuona kwa mara ya kwanza na kuelezwa kuwa hapo awali alikuwa ni mnene utakataa katakata.Lakini uwepo wa mama yangu, mwanamke na mwanadamu pekee niliyekuwa namuamini kulinitia faraja na hata kusinzia nilisinzia vizuri.Mama yangu alikuwa nami bega kwa bega alinifanyioa kila kitu kasoro kuniogesha tu ndio nilisaidiwa na wale wazungu!Baada ya siku mbili hatimaye tukapata miadi ya kufika shirika la kutetea haki za wanadamu lililokuwa na ofisi zake kubwa hapohapo jijini.Wazungu wale hakika walikuwa wameonyesha nia ya kutusaidia.Niliusimulia mkasaa wote katika shirika lile, kadri nilivyokuwa nawasimulia yote niliyoyapitia wakawa wanatoka machozi jambo hili likanifanya nijikute na mimi nikitokwa na machozi. Nilijiuliza ikiwa hawa watu maneno tu yalikuwa yanawaliza vipi kuhusu mimi ambaye niliyapitia maumivu makali kabisa moja kwa moja katika mwili wangu.Nilimtaja hadi yule mwanasiasa kwa majina yake juu ya hujuma aliyotaka kuifanya ili kuniua na kumfunga bila makosa daktari aliyeniokoa ambaye hadi wakati ule nilikuwa sijui nini hatma ya yeye na familia yake.Nilipotaja kuhusu yule daktari. Wale watu walinizuia kisha mmoja akanieleza jambo zito.Yaani kumbe baada ya mkasa ule wa pale mahakamani, waliniteka mimi lakini hawakuiacha hivihivi familia ya daktari, familia ilikutwa imeuwawa kinyama, mama pamoja na watoto wake.Daktari alivyopata ushuhuda ule akarukwa na akili na hadi wakati huo alikuwa katika hospitali ya vichaa mirembe akipata huduma.Nilijikuta nakuwa mkimya kwa takribani dakika mbili nikimtafakari yule mwanasiasa na hapo nikajiuliza swali moja la msingi. Ikiwa huyu mwanasiasa hana uwezo wa kumpenda mtu mmoja mmoja ataanza vipi kuipenda na kuipigania jamii yake ikiwa atapewa madaraka.Kufikia wakati ule hadi sasa nikajikuta naichukia sana siasa!!Siku mbili baadaye nilifanyiwa mahojianon katika vituo mbalimbali vya runinga, awali niliona kama inasaidia sana lakini kadri nilivyokuwa nikisikia taarifa za mauaji kuendelea nilijiona kama ninayekata tamaa.Yule mwanasiasa hakupatikana alipokuwa na familia yake haikujulikana wapi ilipo. Nikajisemea kuwa huenda alikufa akiwa katika jumba lile baada ya kumngáta vibaya sana yeye na mkewe.Hilo la kuhisi kuwa huenda alipoteza uhai lilinifurahisha sana kwa sababu hakika alistahili.Kumbe kule kuonekana kwangu katika runinga na kujitambulisha kwa majina yangu yote mawili kukayafikia masiko ya mtu mmoja. Mtu yule akampigia mama yangu simu.Siku hiyo baada ya mahojiano katika kituo kingine cha runinga nilirejea mahali alipokuwa mama na kumkuta akiwa mnyonge sana. Nilikuwa ninao mpamgo wa kumueleza kuwa kuna mtanzania mmoja amejitolea kunipeleka ujerumani ili niweze kuwekewa viungo vya bandia yaani mikono na sikio, nikajikuta naghairi!!Upesi nikajua kuna tatizo. Nikamuuliza mama ni kitu gani kilikuwa kinatokea…. Mama alitabasamu kisha akaniita na kunikalisha pembeni yake.“Mwanangu kuna mtu amepiga simu hapa!!” aliniambia kinyonge.“Nani huyo wa kupiga simu hadi unakuwa mnyonge kiasi hiki mama yangu …” nilimdadisi.“Amepiga simu baba yako, amekuona kwenye televisheni anadai ameumizwa sana na yote yaliyokutokea na anahitaji sana kufika hapa tulipo….” Mama alinieleza huku akibetua midomo yake.Nilishindwa kuzungumza kitu chochote kile kila nikijaribu kufungua kinywa changu nakosa neno sahihi.Hatimaye nikaweza kuzungumza.“Mama ukimruhusu huyo shetani kukanyaga hapa nitamuua…” Mama alinitazama kisha akanisihi sana kuwa iwe isiwe yule ndiye baba yangu na ana haki ya kuniona na kunijulia hali. Alisihi sana mama lakini sikujiona kabisa kama nilikuwa tayari kukutanisha macho yangu na baba yangu mzazi. Alinisaliti vibaya sana baada ya kugundua kuwa nilizaliwa nikiwa na ulemavu wa ngozi inakuwaje sasa hivi aonyeshe kuguswa na haya yaliyonitokea.Kwanini basi hakuguswa zamani sana baada ya kusikia nimezaliwa nikiwa mlemavu. Ni kwanini alinisaliti na kunikimbia!!Jamani duniani kuna watu wanajua kusuka mipango!! Looh! Imeshawahi kusukwa mipango mingi lakini huu ulikuwa hatari zaidi.Baada ya mama kunisihin sana kuonana na mzee wqangu, nikamweleza sawa nitaonana naye lakini sihitaji kabisa aanze kuniita mimi mtoto wake naomba aje kunisalimia kama muhanga wa kawaida tu!!Mama akamweleza mzee wangu akakubali na kuahidi kufika siku inayofuata!!Siku aliyofika alifika na kitoto kidogo, ambacho pia kilikuwa na ulemavu wa ngozi.Baada ya kuwasalimia watu wote hatimaye tukaachwa kama familia yaani mimi mama pamoja na yule mzee na kile kitoto.Baba akazungumza sana akadai kuwa anasikitika sana kwa sababu alijaribu kukikimbia kiitu ambacho aloikuwa amepangiwa.“Mama Majaliwa nakiri kuwa nilikuwa nasumbuliwa na ujana nikakukimbia na kukuacha na mtoto, nilikuwa mjinga hakika. Lakini hata mwanamke wa pili niliyempata na yeye akaishia kuzaa mlemavu wa ngozi. Huyu unayemuona hapa ni mtoto wangu wa pili na nimetambua kuwa Mungu alinipangia tu kumpata mlemavu wa ngozi ili nimuonyeshe upendo wote kutoka moyoni…. Majaliwa mwanangu huyu ni mdogo wako anaitwa Catherine tafadhali sana naomba umpende kama unavyompenda mama yako. Najua mimi haunipendi hata kidogo lakini mpende mdogo wako yaliyopita yamepita mwanangu.” Baba alinieleza yale maneno kwa sauti iliyojaa hekima.Dah! Sijui nd’o kurogwa ama ni kitu gani kile lakini nikajikuta eti namuona baba kuwa yupo sawa kabisa na kosa alilofanya ni kwa sababu ya akili za ujana tu. Na ule uwepo wake pale na mtoto mndogo yule ambaye anayo ngozi kama yangu kukanifanya nimpende na kuiona familia ikiwa kubwa na yenye amani. Nikajikuta nasimama na kumkumbatia mzee wangu na kumweleza kuwa nimemsamehe. Mama akatabasamu tabasamu pana kabisa bila shaka lilitoka moyoni. Siku ile baba alikaa pale hadi usiku kabisa Cathe akapitiwa na usingizi baba akampigia simu mama yake Cathe na kumweleza kuwa anamuacha cathe kwa kaka yake, mama yake akaruhusu. Na hapo baba akaaga na kuondoka.Ama hakika damu inabaki kuwa damu hakuna maji yanaweza kuiziti uzito damu.Nikajiona niliukosa upenbdo wa baba yangu kwa muda mrefu na nikajikuta namtamkia kuwa kesho pia aje tushinde wote pale.Sura ya baba yangu ni sawa nilikuwa najitazama katika kioo, sema yeye alikuwa mweusi tu!!Tulifanana sana!!Kweli kesho yake mapema kabisa baba akafika akiwa na nguo za Cathe za kubadili!!Akaniletea na zawadi kadha wa kadha na hakusita kila mara kunikumbusha kuwa anajutia kila kitu alichofanya enzi za ujana wake!!Nilimwambia asijali kabisa!!Sikujua hata ni kitu gani alikuwa anakiwaza kwa wakati huo!!Na hapa huwa unakuja ule usemi LAITI NINGELIJUA!!!JIFUNZE!!Usiamini kila unachokiona, subiri kile unachokiona kikuonyeshe kwa matendo kuwa hautakosea ukikiamini. Lakini pasi na matendo tafadhali usikiamini!!*****************************ILIKUWA SAFARI za kuja na kuondoka kwa takribani juma moja. Hakika baba alijitahidi sana, kila siku alikuwa akifika asubuhi ananisaidia kuniogesha ananilisha kisha anaondoka kuingia katika shughuli zake nma baadaye mchana anakuja tena ananilisha na kuniogesha tena ikiwa nitahitaji. Baada ya hapo ananichukua tunatembea kidogo na kurejea nyumbani.Nilipata amani sana kuwa pembeni ya baba yangu, ni kweli nilikuwa nina hasira naye kiasi fulani lakini sikutaka kuendelea kuifuga kwa sababu mtu mzima alikuwa ameomba msamaha tayari ya nini kumwekea ngumu kiasi kile?Baada ya juma moja nikajikuta nikiwa na watu wawili wa kuwaamini kwa kiasi kikubwa, baba yangu pamoja na mama yangu.Maisha yakaendelea tukiwa chini ya uangalizi wa wale wazungu ambao walidai kuwa michango itakayopatikana kwa kutumwa na watu ambao wanaguswa na kilichonitokea basi wataongezea na pesa yao kwa ajili ya kunipeleka nchini ujerumani kuwekewa viungo bandia ilimradi tu niweze kurejea darasani kusoma tena.Juma la pili mzee aliendelea kunihudumia vyema na ni kama kuna kitu alisubiri niulize na kweli ikafikia siku nikadai kuwa nimemkumbuka sana mdogo wangu Catherine. Akanambia kuwa alikuwa na homa asingeweza kumchukua kutoka kwa mama yake, akaniambia ikiwa vyema basi siku moja niende kumsalimia nyumbani kwani hata yeye kila siku alikuwa ananiulizia.Sikupinga lile wazo nikaona heri tu kwenda kumsalimia mdogo wangu, nikamueleza mama akakniambia tu niwe makini kabisa nisiende usiku huko na nikifika nisikae sana.Nilimshangaa mama kuwa licha ya kwamba yule alikuwa ni baba yangu mzazi lakini bado alikuwa hamuamini pia.Sikutaka kumwambia jambo lolote la kumkera na badala yake nikamweleza kuwa sitaenda nje ya ushauri wake.Siku iliyofuata tukaaga nikiwa na baba kuwa tunaenda kumsalimia Cathe.Tukaondoka hadi zilipokuwa Taksi. Tukapanda na baba akatoa maagizo kuwa tupelekwe Kinondoni maeneo ya Biafra!!Sikuwqa nayafahamu maeneo mimi nilichowaza ni kwenda kumuona Cathe kisha tucheze naye akinitania na kunisumbua sumbua hiyo ndo ilikuwa furaha yangu mpya!!Baada ya mwendo wa kama nusu saa hivi gari lilisimama na watu wawili wakaomba lifti. Dereva akakataa lakini mzee akawaombea tu waingie kwa sababu pale kituoni palikuwa na tatizo kubwa la magari.Wakaingia mwanaume mmoja na mwanamke!!Sikujua kuwa ni mpango ulikuwa umesukwa na ukasukika kuanzia ile taksi, dereva wa taksi na hao wawili walioomba lifti pamoja na baba yangu mzazi. Mimi tu ndo nilikuwa sijui lolote, nikaendelea kuyashangaa maghorofa ya jijini Dar.Hatimaye taksi ikaingia katika jumba ambalo lilikuwa la kifahari kiasi fulani japokuwa halikuwa limekamilika bado.Ni hapo ndipo nikajikuta nikisalitiwa na baba yangu wa kunizaa kabisa, yaani kumbe alinichukia kuanzia aliponizaa nimeteseka sana lakini bado alikuwa na mpango wa kunitumia mimi kujipatia kipato.Niliposhuka tu nikakamatwa kwa nguvu sana, nilimuita baba hakuitika wala hakunitazama machoni.Na mara akasema yeye si baba yangu nisirudie kumuita kwa cheo kile.Ndugu msikilizaji, hapakuwa na na Cathe wala mama yake ule ulikuwa ni mpango tu wa kuziteka akili zetu ili wanipate kirahisi.Baada ya kuwa wamenikamata vizuri wakawa wanabishana kuhusiana na mimi.“Sasa mzee hapa sisi tunachukua nini, mikono umegawa tayari, sikio moja hakuna, dole gumba mmegawa.. hapa kwa ile bei hapana mzee…” walimlalamikia baba yangu. Mzee alifikiri kidogo kisha akawaambia, “ Lakini sehemu za siri bado zipo na hapo ndo bei yetu ilipolalia…” Dah! Yaani kiujasiri kabisa baba majaliwa, baba yangu mzazi anazungumzia kuuza viungo vyangu vya mwili… nilijikuta natokwa na chozi huku nikitabasamu.Ama kweli dunia hadaa na huu ulimwengu ndo shujaa!!“Milioni kumi hatutoi mzee, hapa tuachie tatu ya nauli…” walilalamika.Mzee akafikiri kidogo na kisha kwa mara ya kwanza kabisa akanitazama machoni. Nikamjibu kwa tabasamu, akapatwa haya akakwepesha macho.Katika simulizi hii niliwaambia kuwa ikiwa mnataka niwape mfano wa upendo wa kweli basi upendo wa mama ni upendo wa kweli. Simaanishi muwachukie ama kuishi kwa mashaka na baba zenu la! Mimi nimewaambia kwa kitu nilichoshuhudia tu, wapo watu wanalalamika kuwa mama zao ni wabaya lakini kwangu mimi hakika baba yangu si mfano wa kuigwa hata kidogo na sijui ilikuwaje tukakutana tena.Baada ya muda mzee akatoa jibu.“Milioni saba na nusu bei ya mwisho… nawapa na mkono wa yule mtoto…” Jamani!! Yaani mwanadamu anafikia hatua ya kuzungumzia kumuuza mwanadamu mwenzake kirahisi hivyo, damu ikanisisimka sana nilipokafikiria kale katoto kadogo. Bila shaka hakuwa mwingine bali Cathe.Biashara ikakubalika. Mzee akanisogelea na kunikumbatia akaninongóneza kinanifiki.“Nakupenda sana Majaliwa” nikatabasamu na kumjibu, “Sitakufa kabla sijakuuliza nini thamani ya pesa linapokuja suala la utu…” Akaondoka, kisha wale watu wakaniingiza ndani ya lile jumba… kadri tulivyozidi kwenda ndipo tuliingia gizani zaidi.Hatimaye tukaufikia tena mwanga!!Aisee palikuwa kama hospitali…. Wale watu wakaanza kuchanganya madawa yao katika vichupa kisha wakavuta katika sindano na kunichukua wakanilaza kitandani.Nikaona nakufa nikakiona kifo mpenzi msikilizaji.Nikawauliza swali moja lililonijia akilini.“Naupata uchungu kama mnaoweza kuupata nyinyi, nimeumia sana mikono hii ilikatwa bila ganzi, kidole, sikio vyote hivyo bila ganzi. Maumivu ni makali sana tafadhali siwazuii kunifanya mnavyohitaji lakini naomba kama ipo sindano ya usingizi ama ganzi ama hata sindano ya sumu naomba mnichome kabla hamjanitenda mtakavyo….” Walinisikiliza kwa makini na kila mmoja akapokea kwa jinsi alivyopokea, mwingine alicheka na kutaka kupuuzia, na mwingine akaonyesha kunielewa sana. Akawashauri wenzake wanifae kwa vile nilivyoomba.Ikawa kama nilivyoomba, wakatafuta madawa mengine na kisha wakachanganya na kunichoma sehemu zangu za siri na hapo sikuwa nahisi kitu chochote, ilikuwa sindano ya ganzi.Wakanichukua na kunilaza kitandani tayari kwa kunikata sehemu za siri.Wakati hawajanifanya kitu chochote mara mlango ulifunguliwa. Nikadhani kuna msaada wowote ulikuwa umefika lakini hapakuwa na msaada. Alikuwa ni baba yangu mzazi na aliingia akiwa amekibeba kile kitoto kidogo, Catherine!Kilikuwa kimesinzia na alikuwa amekikumbatia kana kwamba alikuwa yu na mapenzi ya dhati sana kwake.Akakifikisha na kukilaza katika kitanda kingine pembeni yangu.Kilikuwa kinatabasamu!!Nilijisikia vibaya sana jamani, niliumia sana kukitazama kitoto kile.“Baba… tutakutana mbele ya haki kamwe sitasema lolote njema juu yako. Ulaaniwe wewe nba wote watakaonufaika na pesa hiyo uliyoipokea kwa kuuza utu wangu na huyu mtoto. Nakuchukia sana baba yangu!!” nilimwambia, akatoa tabasamu kisha akaondoka na kuufunga mlango.Visu vikatolewa mahali pake wakanifunga uso wangu kwa kitambaa cheupe kisha wakanifunga na kamba zilizopita kifuani kwangu na miguuni.Sikuweza kutikisika, mwisho wakauziba mdomo wangu!! Ama hakika nilipitia magumu jama, sihitaji mtu wa kusema badala yangu kwa sababu nilikuwa mimi na mimi ndiye niliyeshuhudia haya!!Naam! Majaliwa katika wakati mgumu sana. Yu kitandani amefungwa kamba tayari kwa kufanyiwa kitendo cha kikatili!! ***********************Hatimaye niliyafumba macho yangu na kuyauma meno yangu kwa nguvu sana ili kuweza kupambana na uchungu ambao ungefuata baada ya muda mfupi. Japokuwa nilikuwa nimechomwa sindano ya ganzi lakini bado nilitambua kuwa kitakachofuata ni maumivu.Mwanadamu anaenda kunifanya asichopenda kufanyiwa yeye hata kidogo!!Nilimuomba Mungu ikiwqa vyema basi kamwe asiwasamehe kwa maovu yale waliyokuwa wakitaka kunifanyia mimi na pia nikakumbuka kumuomba anikutanishe nao baada ya vifo vyao niwaone wakiteketea katika moto ule wa milele.Lakini kabla ya kukubali kuwa nilikuwa naenda kufa kwa kuvuja damu nyingi sana nilikumbuka kuwa Mungu wetu yu tayari kusikia kilio cha kila mtu hapa duniani.Kama anaweza kusikiliza kilio basi hata maswali pia anaweza kujibu.Nikamuuliza swali nilililoona kuwa ninastahili kabisa kupewa jibu lake.“Mungu baba yangu wa haki. Hivi ni lini nimekukosea kiasi cha kustahili adhabu kubwa kiasi hiki, kama nimewahi kukukosea baba nichukue huku ukiwa umenisamehe, lakini kama ahuhusike na haya yanayonitokea baba sasa ingilia kati sitaweza kustahimili kinachoenda kunitokea hapa. Mungu wetu wewe hauwahi wala hauchelewi lakini naomba nikukumbushe sasa kuwa nakuhitaji. Ingilia kati, washike mikono yao wasifanye wanachotaka kukifanya!!!” nilimaliza kutoa ombi langu kimyakimya.Na mara nikaisikia sauti ya kile kitoto kidogo nikayafumbua macho na kugeuka, nilimuona bwana mmoja akiwa amelowana damu mikononi na mtoto alikuwa analia.Maskini wee!! Alikuwa anamkata mkono wake.Ndugu yangu unayenisikiliza ikiwa unapitia mambo magumu sasa hivi tambua kuwa mimi nilipitia na pia kuyashuhudia mambo magumu zaidi tena yenye kuumiza sana nafsi. Nilitetemeka sana na baridi ikayakumba matumbo yangu, yaani wale watu shetani alikuwa amewapa uziwi hawakusikia kabisa kilio cha katoto kale.Wakaendelea kabisa huku wakijua wazi kuwa Mungu hapendi wanachokifanya.Naam! Wakiwa katika shughuli yao ile haramu ya kukemewa vikali kabisa ukawadia ule wakati uitwao hakuna marefu yasiyokuwa na ncha na fanya ufanyavyo lakini kamwe huwezi kuishi nyuma ya kivuli cha uongo milele.Nikausikia mlango ukipigwa kwa nguvu sana na aliyeingia ndani alikuwa ni mzee wangu.Nikakata tamaa kwa sababu nilidhani kuwa alikuwa ni mtu aliyekuja kunikomboa.Lakini safari hii aliingia na kuanguka huku akiwa amepiga magoti chini, nikajitahidi kumtazama nikagundua kuwa alikuwa amepasuka usoni.Kabla sijajua ni kitu gani kilikuwa kinaendelea, ikasikika sauti ikiamrisha kuwa kila mtu ambaye yupo pale ndani basi atulie kama alivyo.Bado sikuweza kugeuka vizuri kwa sababu zile kamba zilikuwa zimekazwa barabara!!Lakini kamba zile hazikufungwa masikioni eti nisiweze kusikia.Niliweza kuisikia ile sauti ambayo hata liwe giza hata uwe mwanga iwe kwa mbali hata karibu bado naweza kuitambua. Hasahasa ikiwa katika masikitiko.Naam! Alikuwa ni mama yangu mzazi.“Mamaa!!”niliita kwa saquti ya juu huku nikijitikisa kutoka katika kamba zile.“Calm Down majaliwa!!”niliisikia sauti ikinisihi na hapo aliuekuwa akizungumza akasimama mbele yangu.Alikuwa ni mmoja wapo kati ya wale wazungu.Sikuamini kabisa kuwa lile jambo lilikuwa limetokea.Upesi nikayafumba macho yangu kisha safari hii ilikuwa kwa sauti ya juu kidogo nikazungumza.“Asante sana Mungu baba yangu wa haki kwa sababu umekuja nilipokuita!! Haujanifedhehesha mbele ya watu wabaya, jina lako lisimame na kuheshimiwa daima na milele.” Nilizungumza huku machozi yananitoka.Baada ya muda akaingia mama yangu, alikuwa analia sana alikuwa anamlaani baba yangu.“Yaani baba Majaliwa.. haikutosha kunitelekeza nikiwa na mtoto mdogo, haikutosha kabisa ulinijaza mimba nikafukuzwa nyumbani hii yote haikukutosha umeamua kurejea tena uniulie mwangu yaani mtoto ambaye ni damu yako kweli?? Alilalamika sana mama yangu, hakuna aliyejaribu kumbembeleza kwa sababu alikuwa katika uchungu maradufu.Nilishangaa ni kwanini sikufunguliwa zile kamba. Lakini baada ya nusu saa hivi askari waliovalia kiraia waliingia pale ndani, upesi yule mtoto akachukuliwa hapa ni baada ya kupiga picha. Wale wauaji akiwemo baba yangu mzazi wakatiwa pingu na hapo nikafunguliwa na kuwa huru tena.Napenda kukueleza ewe msikilizaji kuwa kama kifo kinayo ladha basi mimi mwenzenu niliwahi kuionja kabisa tena si mara moja wala mbili.Lile swali langu la ni kwanini sikufa mapema, ni kwanini nimekoswakoswa sana kupoteza uhai nalipata jibu hili wakati huu unaponisikiliza nikikusimulia haya. Labda nisingekusimulia haya kamwe usingeamini kuwa albino tunateseka, labda nisingesimulia haya huku ukiniona ungeamini kuwa yasemwayo juu yetu kuwa tunanyanyaswa ni propaganda tu.Baada ya pale tulifikishwa hospitali, yule mtoto aliyeitwa Catherini alitibiwa vyema. Ilikuwa bahati kuwa mkono wake ulikluwa haujakatika hivyo aliweza kupata tiba na hatimaye kuwa sawa.Nami nikatazamwa sikuwa na tatizo lolote, wale watu waliokamatwa wakiwa katika jaribio la kutukata viuongo vyetu walihukumiwa kifungo cha maisha jela.Zile pesa ambazo walikuwa wamepeana kwa ajili ya kununua viungo vyetu zilichukuliwa na hizo zikapangwa kutumika katika kunisaidia mimi kununuliwa viungo vya mwili.Lakini nikiwa mbele yenu leo nakiri kuwa nimekataa sihitaji tena viungo bandia, natambua kuwa kuna wenzangu wengi wamekatwa mikono na hata miguu yao na hawana msaada kabisa kama huu ambao nilikuwa nimepangiwa mimi kuupata.Ushuhuda huu bila shaka ni zawadi katika maisha yangu, ushuhuda huu uwe fimbo ya akili yako ewe mwenye mawazo potofu.Jisikie vibaya kutuona albino tukilia kila kukicha,tupo wachache sana jama! Ni amani gani tunawakosesha kwa kuishi kwetu?? Kama tunawatia kichefuchefu tafadhali andikeni katika katiba kuwa hamtuhitaji ipigwe kura tupokelewe katika nchi ambazo hatutabaguliwa.Ikiwa ni haki kwako kutukata viungo vyetu wewe wajisikiaje pale mwanao anapojikwaa tu na kutoka ukucha?? Wajisikia vibaya sana lakini waona ni haki kwetu kuuwawa.Jamani kama mnaamini kuwa kufa kwetu ni kupotea na kamwe maiti haionekani, kama mnahisi sisi tukikatwa hatuumii basi leo nipo mbele yenu hapa nimewasimulia mengi sana, jamani niliumia nilipokatwa mikono, niliumia nilipokatwa sikio. Niliumia sana na ninahisi maumivu hayo ni sawa kabisa na nyinyi.Sasa chukia kabisa kuliona chozi letu.Simama wewe, yule na nyote kwa pamoja mlidake tena chozi letu!!!Mkitupuuzia hamtakuwa mkitutendea haki!!SISI NI WANADAMU KAMA NYINYI, SISI NI WATANZANIA!!!USICHOKE KULIDAKA TENA CHOZI LANGU.JIFUNZE!MAISHA hayana tafsiri ya moja kwa moja. Usijiweke katika kundi la kuwatega albino, kumbuka kuwa mama na baba zao ni watu weusi, nawe ni mweusi je? Kesho keshokutwa na wewe ukizaa mtoto albino utafanya nini? Ama ndo utakuwa na roho mbaya kama ya baba Majaliwa ukamkimbia mtoto? Na kama ukimlea je utakubali kuona akiteswa??Kama jibu ni ndio basi badilika kuanzia hivi sasa.SIMULIZI HII YA MAISHA YA LIDAKE NTENA CHOZI LANGU NI SIMULIZI ITOKANAYO NA KISA CHA KWELI KABISA CHA KIJANA ALBINO ALIYEKARIBIA KUINGIA KATIKA MASOMO YAKE CHUO KIKUU LAKINI AKAISHIA KUKATWA MIKONO YAKE YOTE MIWILI NA KUKATISHA NDOTO ZAKE.
0 comments:
Post a Comment