Search This Blog

Sunday, July 10, 2022

NISAMEHE MAMA - 1

 







    IMEANDIKWA NA :  JUNIOR NICKSON





    *********************************************************************************



    Simulizi : Nisamehe Mama

    Sehemu Ya  Kwanza (1)





    "Nimekulea kwa tabu sana hadi ulipofikia leo hii mwanangu. Hata siku moja sikuwa kufikiri kama utafika hapo ulipo.

    Iliwahi kuninyeshea mvua ya mawe wakati nikihangaika huku na kule kutafuta kazi ya kufanya pindi mgambo wa jiji walipoamua kuchukua vifaa vyangu ambavyo vilikuwa vikiwafanya watu kuniita mama ntilie. Sikuwalamu wao bali nilimuona baba yako ndiye mwenye makosa kwani kama asingeamua kunitelekeza nikiwa na mimba yako ya miezi mitatu, mabaya yote hayo yasingenikumba.

    Kama hiyo haitoshi, niliwahi kukumbana na tukio lililonifanya niwaone wauaji wanaume wote. Bado u mdogo mwanangu hivyo mengine si busara kuyatamka.

    Mwanangu elimu nd'o itakayokusimamia popote pale hata kama uhai wangu utakuwa umeshaniondokea." Aliongea mama yule huku machozi yakimtoka kwa fujo mbele ya mwanae wa kiume aliyempatia jina la Steven. Steven akamkumbatia mama yake bila kufungua kinywa chake kuongea lolote.

    Ndipo akamsikia mama akiongea kwa mara nyingine huku akimuonyesha mguu.

    "Nitizame mwanangu. Mguu uliunguzwa kwa pasi ya umeme miaka kumi na saba iliyopita na mama mmoja wa kiarabu kipindi nafanya kazi ya upishi katika famili yake. Hakujali maumivu nitakayoyapata. Akanifukuza kama mbwa ndani ya nyumba yake usiku wa saa tatu. Ilikuwa ni kipindi cha baridi sana. Wakati huo mimba ilikuwa kubwa na iliyokuwa ikihitaji uangalizi wa hali ya juu.

    Nikaanza kuizunguka mitaa ya mji wa Shinyanga. Sikuwa na ndugu,huku marafiki niliokuwa nao ni wale watoa ushauri wakati wa nafuu na si wale watoao msaada wakati wa tabu. Maumivu ya mguu wangu yalikuwa makubwa mno.

    Niliendelea kutembeatembea usiku ule uliofunikwa na kiza totoro. Bahati mbaya sikuwa nafuatilia siku zangu za kujifungua. Kumbe siku hiyo ilikuwa nd'o maalumu kwa wewe kuuona ulimwengu.

    Nikasaidiwa kujifungua na mama mmoja ambaye hadi leo hii huwa simjui ni nani. Hakuwa akiongea. Sijui alikuwa bubu ama lah! Akanisaidia hadi nilipojifungua salama. Akaondoka na kuniacha pale kwenye mtaro.

    Niliendelea kuwa na matuamaini ya kuwa labda atarudi lakini wala hakurudi". Mama yule alipofika hapo akasita kidogo kusimulia. Ukimya kwa muda ukatawala kisha akaendelea.

    "Mwanangu usiku wa siku hiyo ulinifanya nikumbuke kitenge nilichonunuliwa na baba yangu mzazi enzi za uhai wake, halafu kwa hasira nikakichanachana kwa wembe eti kisa mama yako mdogo kanunuliwa gauni la bei kubwa kuliko kitenge hicho.

    MUNGU anisamehe kwani mama yako mdogo alishatangulia mbele za haki halafu namuongelea kwenye mambo ya kipumbavu kama haya.

    Usiku huo nililazimika kuvua nguo zangu za juu na kukufunika wewe ili hali yako iwe sawa kwa kiasi fulani. Maumivu ya mguu, kujifungua pamoja na baridi kali, vilinifanya kuiona dunia kisiwa cha tabu. Kulipopambazuka nikavaa nguo zangu na wewe nikakuweka kifuani mwangu ili angalau nikaangalie sehemu ambayo nitapata maji ya kuoga kwani hali ya mwili wangu haikuwa ikitamanika.

    Kila kona niliyopita watu walinigeuka na kutema mate kwasababu ya harufu niliyokuwa nikiitoa". Alipofika hapo mama yake na Steven, akashindwa kuendelea kumsimulia mwanaye kutokana na kilio cha kwikwi alichokitoa. Steven alimuacha mama yake alie hadi aliponyamaza mwenyewe.

    Wakati historia hiyo ikipenya kwenye ngoma za masikio ya Steven, ilikuwa yapata majira ya saa kumi na mbili za asubuhi. Siku hiyo ilikuwa ni ya pekee sana katika kupiga hatua ya pili kielimu kwa upande wa Steven pamoja na wenzake. Siku ambayo alitakiwa kufanya mtihani wa kuhitimu kidato cha nne.

    "Mwanangu nakupatia baraka zote mtihani wako ukawe mwanga wa kuyamulika maisha yako yajayo." Aliongea mama yule ambaye hali yake kiafya haikuwa ikiridhisha lakini mbele ya mwanae alikuwa imara kama zege.

    Steven akaagana na mama yake kisha akaelekea shuleni huku akiwa na matumaini makubwa ya kuufanya mtihani kwa utulivu ili siku moja ayafute machozi ya mama yake.

    Mitihani yake ya kwanza ilikuwa ni Mathematics pamoja na Civics. Aliifanya kwa umakini mkubwa mno akiwa hataki kumuangusha mama yake ambaye ada yake alikuwa akiitoa kwenye kilimo cha pamba.

    Baada ya taratibu kumalizika akarudi nyumbani na kumkuta mama yake akiwa anamalizia kupika. Wakapata chakula lakini shauku ilikuwa kubwa mno moyoni mwa Steven. Alihitaji kujua ilikuaje hadi yeye akawa hai wakati mama yake alikumbwa na maswahibu mengi.

    "Mama hujanimalizia ulichokianzisha". Alikuwa ni Steve nusu saa baada ya kumaliza chakula cha usiku huku wakiwa wamekaa kwenye mkeka nje ya kijumba chao kibovu. Kijumba ambacho upepo ukija kinarekebishwa.

    Kauli yake ikaibua machozi kwa mara nyingine katika mboni za macho ya mama yake. Hakutaka kumtaka radhi, akamuacha hadi alipokuwa tayari kuzungumza.

    "Sikujali vitendo vyao hao walionitema mate. Nikatembea kwa mwendo wangu uliojawa na maumivu ya hali ya juu hadi kwenye bwawa lililoko pale Maganzo. Hapo nikaoga na kufua nguo zangu.

    Nikiwa nasubiria zikauke, akatokea mama mmoja ambaye alionekana kuguswa na hali yangu. Akanisogelea na kuniuliza kama n'naweza kuhitaji msaada wake. Msaada nilikuwa nauhitaji sana".

    "Ni wachache sana wenye mioyo ya wema na wakadumu. Wengi huchukuliwa na muubaji wetu na kuwaacha kwenye wakati mgumu wenye uhitaji nao. Anastazia akafariki kwa ajali ya gari kabla hajatimiza ahadi zake kwangu.

    Mwanangu ulimwengu unayo mengi yenye kuumiza mno. Yahitaji uvumilivu wa hali ya juu mwanangu”.

    “ Akaningojea hadi nguo zangu zikakauka ndipo nikaongozana naye hadi mahali alipokuwa akiishi. Anastazia alikuwa ni nesi katika hospitali ya Maganzo. Akanipatia huduma zote zihitajikazo kwa mama aliyejifungua.

    Ukarimu wake ukanifanya nijione mpya ndani ya jamii. Muda wa mwezi mzima nilioishi naye sikuwahi kumuona akicheka. Mara zote alitoa tabasamu tu. Sikuwahi kuwaona hata ndugu zake kabla ya ajali aliyoipata. Anastazia ni kama alishajua kifo chake kipo karibu.

    Mwezi uliofuata, akaniambia nia yake ya kukupeleka kwenye kituo cha kulelea watoto yatima pale Shinyanga mjini. Nilikubaliana naye ndipo tukakupeleka pale kama mtoto yatima". Alipofika hapo akatawaliwa na ukimya na kilio kilichoambatana na kwikwi kikasikika.

    "Pole sana mama." Aliongea Steven lakini wala haikusitisha kilio cha mama yake. Alilia sana lakini alipokoma akaendelea kumsimulia mwanae;

    "Wakati tunatoka kukupeleka kwenye kituo hicho, teksi tuliyokuwamo ikagongana na basi lililokuwa likitokea Mwanza.

    Wakati macho yangu yanaanza kuona kiza, nilishuhudia shingo ya Anastazia ikikatwa na kipande cha kioo. Ndipo kwa tabu nikawa nalitamka jina lake kwa kulikatakata. Ana.... Anaa.. Staziiiaaa.

    Sikujua kilichoendelea kwani fahamu zilinipotea. Nilipozinduka nilikuwa hospitali huku sehemu mbalimbali za mwili wangu zikiwa zimebandikwa bandeji. Cha kwanza nililitamka jina la Anastazia kadiri nilivyoweza hadi pale dokta alipokuja na kunichoma sindano iliyonisababishia usingizi.

    Niliposhtuka toka usingizini, maumivu yalikuwa ni makubwa mno. Daktari alikuwa pembeni akinitundikia dripu ya maji."

    "Yuko wapi Anastazia??" Ni swali nililomuuliza daktari pindi nilipoamka.

    "Tulia yote utayajua pindi hali yako ikitengamaa." Aliongea dokta huku akiondoka.

    “Nilikaa pale hospitali kwa mwezi mzima bila kupatiwa taarifa za Anastazia. Si kwamba nilikuwa nimepona majeraha yangu. La hasha! Gharama za matibabu zilikuwa kubwa na sikuwa na uwezo huo. Zile za kwanza zililipwa na mwanaume ambaye sikumfahamu na wala hakutaka nimtambue japo hadi leo hii huwa nahisi ni baba yako.

    Nikatakiwa kuondoka pale hospitalini. Uwezo wa kutembea nilikuwa nao japo kwa kupepesuka. Cha kwanza nilielekea ilipokuwa nyumba ya Anastazia.

    Sikuamini nilipofika na kukaribishwa na maandishi makubwa yaliyokuwa kwenye msalaba juu ya kaburi lake. Maandishi ambayo yalielezea tarehe ya kuzaliwa kwa Anastazia pamoja na tarehe ya kifo chake. Ilinisikitisha mno lakini sikuwa na namna.

    Nikalisogelea kaburi lake ili niweze kuliwekea hata mchanga pamoja na kumuomba MUNGU alilaze roho yake mahala pema peponi. Nilipoanza kuweka tu mchana, akatokea mama mmoja ndani ya nyumba na kudai eti mimi ni mchawi hadi nimemloga mtoto wake. Nikafukuzwa bila huruma huku nikimwagiwa mchanga na kunifanya nionekane kituko mbele za watu. Nikaondoka eneo lile ili kuepuka balaa.

    Nikanyoosha kituo ulichokuwepo ili kuangalia kama u mzima. Nikakuta afya yako inazidi kuimarika japo ulikuwa ukikuzwa na maziwa ya chupa. Hakuna aliyetambua kama mimi ni mama yako. Bali walinitambua kama mama yako mdogo ambaye sina uwezo wa kukutunza. Niliporidhika na hali yako, nikaondoka na kukuacha hapo. Nikatafuta sehemu iliyokuwa na mti wenye kivuli na kukaa chini yake kwani jua lilikuwa kali kuliko maelezo". Alipofika hapo, akashindwa kuendelea kumsimulia mwanae Steven. Akamtaka wakalale kwani hata siku iliyokuwa inafuta kama uzima upo hatasita kumuhadithia.

    Japo Steven alihitaji kuendea kusikiliza, lakini hali aliyokuwa nayo mama yake ikabidi amuache na kuingoja siku ya kesho kwa hamu.

    "Kumbe mama kapitia magumu mengi namna hii? Je vipi kuhusu baba yangu mzazi? Alikuwa hai hadi nikaitwa mtoto yatima?" Ni maswali yaliyokuwa yakipita kichwani mwa Steven kabla ya kupitiwa na usingizi.

    Kesho yake asubuhi na mapema, mama yake alimtaka kujiandaa kuelekea shuleni ili kuendelea na mitihani yake ambayo alitakiwa kuifanya kwa muda wa wiki moja.

    Asubuhi ile hakutaka kumgusa mama'ake kwa maswali ya udadisi. Akajiandaa na kuagana na mama yake ambaye alirudia kauli ya jana yake ya kumtakia heri katika mitihani ile.

    Siku hiyo alifanya mitihani miwili pia,wa somo la Geography na Kiingereza.

    Majira ya jioni akarejea nyumbani ambapo hakumkuta mama yake. Hakujua ni wapi kaelekea. Akachukua jukumu la kupika chakula.

    Akiwa anaendelea kupika, mama yake akarejea huku jembe likiwa begani.

    "Mmh! Mama nawe! Hadi jua namna hii uko shambani tu!" Steven alimwambia mama'ake baada ya salamu. Mama yake aliishia kucheka na kulia kwa wakati uleule. Kwa mara ya kwanza Steven akaona ni kitu cha ajabu sana. Mtu kulia na kucheka kwa wakati mmoja.

    "Mwanangu usiyatafsiri machozi ya mtu kama maumivu ndani ya moyo wake. Vilevile usikitafsiri kicheko cha mtu kama furaha ndani ya moyo wake." Maneno hayo yalimtoka mama yake Steven.

    "Unamaanisha nini mama unaposema hivyo?" Steven alimuuliza mama yake.

    "Mwanagu kuna kipindi jua unaliona ni starehe linakusulubu". Aliongea mama yake huku akiondoka mahali pale.

    Steven akabaki njia panda na kauli za mama'ake. Alitaka kumdadisi tena lakini akasita alipomuona mama yake akiweka maji kwenye karai ili aweze kuelekea bafuni kuoga. Lakini alijawa na mshangao alipomuona mama'ake akiyachota maji kwenye karai kwa kutumia kiganja na kuyarudisha huku akiwa anayatizama kama mtu anayekumbuka kitu.

    Alitumia muda mwingi kufanya hivyo lakini katu Steven hakuthubutu kumuuliza chochote. Alitambua fika kuna kitu anakikumbuka na kinamuumiza nafsi. Akaendelea na mapishi hadi alipomaliza.

    Muda mchache baadaye mama'ake akatoka bafuni. Wakajumuika wote katika kupata chakula. Wakiwa wanaendelea kupata chakula, mama akasita na kubaki ameshikilia tonge la ugali mkononi. Machozi yakaanza kumtiririka huku ukimya ukitawala.

    Hali ile ilimuumiza mno Steven ndipo akamwambia mama'ake huku na yeye machozi yakianza kuonekana kwenye macho yake.



    Muda mchache baadaye mama'ake akatoka bafuni. Wakajumuika wote katika kupata chakula. Wakiwa wanaendelea kupata chakula, mama akasita na kubaki ameshikilia tonge la ugali mkononi. Machozi yakaanza kumtiririka huku ukimya ukitawala.

    Hali ile ilimuumiza mno Steven ndipo akamwambia mama'ake huku na yeye machozi yakianza kuonekana kwenye macho yake.

    "Najua inakuuma sana mama'angu lakini tafadhali usilie. Ulishayavuka na haistahili yakunyong'onyeze tena nafsi yako". Pamoja na maneno hayo lakini mama alizidi kulia.

    Takribani dakika tano alikuwa akilia tu. Ulikuwa ni wakati wa kupata chakula lakini ukageuka wasaa wa kilio. Chakula kikasahaulika kwa wote,si Steven wala Mama'ake aliyekuwa akishughulika na chakula kile.

    Baada ya dakika hizo kupita, mama akafungua kinywa chake na kuendelea kumuhadithia mwanaye kilichomtokea katika maisha yake kipindi cha nyuma.

    "Nikiwa nimepumzika chini ya ule mti njaa ikaanza kunitesa. Sikuwa na kiasi chochote cha fedha ambacho kingenisaidia kupata chakula mahali popote pale. Endapo ningeendelea kubaki eneo lile, nadhani isingekuwa busara. Njaa iniue kisa kuogopa jua? Nikainuka na kuanza kutembea kurudi Shinyanga mjini.

    Yale mabandeji niliyokuwa nimebadikwa yakaanza kuniletea maumivu makali kutokana na hali ile ya jua kali". Alipofika hapo kilio kikamkuba tena.

    Alionekana ni mama ambaye moyo wake ulikuwa kwenye maumivu makali kila alipokumbuka historia yake ya nyuma. Steven akamuacha alie kwani kumnyamazisha asingeweza. Takribani dakika moja alilia. Alipokoma akaendelea;

    "Maumivu yalikuwa makali lakini nikaendelea kujikakamua kutembea. Hali yangu ilisikitisha lakini hakuna aliyejali hilo.

    Kila mmoja alikuwa na mihangaiko ya maisha yake. Mbali na yote sikufungua mdomo wangu na kutamka MUNGU umeniacha.

    Nikafika mahali maumivu yakazidi. Njaa nayo ikanilegeza miguu. Nikashindwa kuendelea na safari. Nikasogea kandokando ya barabara nikaketi. Baada ya maumivu yangu kupungua, nikainuka na kuendelea na safi hadi nilipofika mahali ambapo nilikuta umati mkubwa wa watu ukiwa umefurika barabarani. Hata magari yalikuwa yamepanga foleni kutokana na umati ule. Japo nilikuwa katika wakati mgumu lakini niliamini pale ni ajali imetokea. Hakuna kitu nilichokuwa nakiogopa kama ajali. Ilisababisha nimpoteze rafiki yangu Anastazia aliyekuwa amejitolea kunisaidia.

    Ikanisababishia kuwa kwenye maumivu ya majeraha sehemu mbalimbali za mwili wangu. Hakika ajali nilistahili kuichukia. Yale maumivu yangu yakanipotea na kunifanya nijipenyeze katikati ya umati ule hadi nikafanikiwa kufika mbele.

    Ilikuwa imepita miaka kumi na moja pasipo kumuona baba yako kwani mara ya mwisho nilikuwa nimekutana naye ghafla katika mkutano wa vyama vya siasa akinadi sera zake japo hakuchaguliwa. Pale nilikuwa namuona lakini akiwa hatamaniki. Alikuwa ni baba yako mzazi pamoja na mama yako wa kambo wakiwa wametulia kimya huku pembeni yao gari dogo aina ya suzuki likiwa limepinduka. Hawakuwa na jeraha lolote katika miili yao wala sikuona chembe za damu. Iliniweka katika mshangao wa aina yake. Lakini sikuthubutu kuiweka ajali ile katika mambo ya ushirikina.

    Muda mfupi wakafika maaskari eneo lile la tukio. Tukio ambalo kila mmoja alilichukilia kwa jinsi alivyojua yeye. Wakafanya vipimo vyao na kuondoka na miili ile. Sikufuatilia hospitali lakini kwake nilifika kesho yake ambapo nilikuta msiba. Niliamua kusamehe yote aliyonitendea kwani tayari nilikuwa naishi na damu yake.

    Mazishi yalifanyika siku mbili baada ya ajali ile ya ajabu. Nikaondoka pale kwenye msiba kwani sikuwa na cha kudai juu yako kwasababu hukuwa mtoto wa ndoa na wala hakuna aliyekuwa akifahamu uwepo wako.

    Kifo cha baba yako ni kama kilinipatia unafuu wa maisha kiasi fulani kwani niliweza kupata msamaria mwema aliyenigharamikia hadi nikapona kabisa majeraha yangu. Mwanamama Minza akaniajiri kwenye hoteli yake iliyokuwa pale stendi ya Shinyanga. Nilikuwa nikilala palepale hotelini. Maisha yenye furaha yakarejea.

    Kila baada ya wiki moja nilikuwa nikikutembelea pale kituoni. Kwa muda wa miaka miwili niliweza kufanya kazi na Minza ambaye ujira wangu alinipatia kila lipofika mwisho wa mwezi. Hakuwahi kuninyima ujira wangu. Fedha yangu ya miaka miwili nilionainastahili kufungua biashara yangu ya kuuza hoteli lakini si pale mjini. Nikahamia Maganzo." Akasita kusimulia hodi ilipobishwa na mtu nje.

    Akafuta machozi yake kwa kutumia khanga yake ambayo ilikuwa si chakavu na wala si mpya. Akaingia mama Sung'wa.

    Ujio wa mama Sung'wa ulisababisha chakula kikumbukwe. Tena baada ya salamu wakashirikiana kukimalizia kile chakula. Baada ya uhitimisho wa zoezi lile, ndipo mama Sung'wa akaeleza ujio wake.

    "Mwenzangu nimeona si busara nifanikiwe mwenyewe katika hili. Kuna mradi wa uchimbaji madini utaanzishwa eneo hili hivyo kama na wewe utaridhia basi tukubali hili wanalitaka." Aliongea mama Sung'wa.

    "Kwani kuna nini haswa."

    "Mradi huu utafanyika eneo hili ambalo linakujumuisha wewe, mimi pamoja na majirani zetu wawili. Watoto wetu watasomeshwa bure hata kama hawatafaulu hadi pale watakapopata kazi. Vilevile tutahamishwa na kujengewa nyumba saehemu nyingine na kampuni itakayosimamia mradi huo. Ilimradi tukubali kuhama eneo hili." Aliongea mama Sung'wa maneno ambayo yaliamsha furaha za ajabu moyoni mwa Mama Steven pamoja na mwanae.

    Waliona ni muda wao kuishi misha yaliyotawaliwa na furaha zaidi ya yale. Si maisha kama waliyokuwa wakiyaishi kwenye kile kijumba kibovu. Mvua ikinyesha hawalali kama ni usiku.

    "Mimi sina kipingamizi katika hilo. Tena nitakuwa nimepumzika na haya maisha magumu ninayomsomeshea mwanangu Steven japo sijayachoka." Waliendelea na maongezi ya hapa na pale hadi mama Sung'wa alipoaga na kuondoka.

    Huku nyuma furaha iliyoambata na machozi kati ya mama na mwana ilitawala. Lakini kwa upande wa mama alilia mno. Wakabaki kusubiri kama litatimia lile waliloambiwa. Hata ile hadithi haikuendelea tena.

    ****

    Siku hiyo majira ya jioni mama'ake na Steven hakuelekea shambani kulima kama ilivyokuwa kawaida yake. Badala yake akaelekea kusaga unga huku mwanaye akijikita katika kupitia yale aliyofundishwa hapo kabla.

    Kesho yake alitakiwa kuingia kwenye chumba cha kufanyia mtihani. Masomo mawili alitakiwa kuyafanya hiyo kesho yake. Chemistry pamoja na Kiswahili.

    Aliyapitia masomo yale kwa umakini pasipo kuichosha akili yake. Ilipotimu majira ya saa moja, ndipo aliachana na madaftari yake wakati huo mama yake akishughulika na suala la chakula cha usiku.

    Akaingia bafuni na kuoga. Alipohitimisha zoezi hilo, akaketi pembeni ya jiko kuota moto huku stori zilizojaa utani zikiendelea kati yao. Vicheko vilitawala kwa wingi hadi pale mama alipoanza kusonga ugali.

    Chakula hiki ndicho kilikuwa kikuu kwa wakazi wa Shinyanga,hivyo haikuwa ajabu familia kula ugali kwa wiki nzima mfululizo bila kukichoka chakula hicho. Kuzungusha miko miwili tu akashindwa kuendelea. Machozi yakaanza kumbubujika. Dhahiri shahiri kuna kitu alikikumbuka ndiyo maana alianza kutokwa na machozi ghafla.

    Steven akachukua jukumu lile na kumalizia kusonga ugali wakati huo mama yake hakuwa amekoma kulia. Alipomaliza kusonga ugali na kuuweka kwenye sinia, akasikia sauti ya mama yake ikilitamka jina lake.

    "Steven mwanangu."

    "Naam, mama."

    "Wiki mbili tangu nilipofungua biashara yangu ya kuitwa mama ntilie, nilikumbwa na kitu kilichonifanya nirudi kwenye hali ngumu kiamisha. Tena nikiwa na wewe." Akanyamaza na kujifuta machozi kwa kiganja chake. Kichwani mwa Steven akabaki kwenye sintofahamu.

    Ilikuaje hadi aseme alirudi kwenye wakati mgumu tena akiwa na mimi ilihali tayari nilikuwa nikilelewa katika kituo cha watoto yatima? Akashindwa kuvumilia na kujikuta akimuuliza swali mama yake.

    "Mbona ulivyoanza tu kusonga ugali hali ya kulia ikakukumba?" Kimya cha dakika kadhaa kikatawala baada ya swali lile. Kilichosikika ni koo zikipitisha mafunda ya mate.

    "Steven." Alirudia kuita kama awali mama yake.

    "Ni mimi mwanao nakusikiliza lakini nakuomba usilie."

    "Nakiri bila wewe mimi nisingekuwa hai hadi muda huu. Ningeshajiondoa uhai wangu kutokana na maswahibu yaliyokuwa yakiniandama kila ilipoitwa siku mpya. Lakini kama ningejiua bila shaka ningekuacha katika maisha ambayo yangekufanya unyanyasike zaidi yangu.

    Siku hiyo nilipoanza tu kusonga ugali, wakatokea mgambo waliokuwa wakisafisha wale wote waliokuwa wakifanya biashara maeneo yasiyoruhusiwa. Na mimi nilikuwa mmoja wao. Sufuria langu la ugali likapigwa mateke kisha likabebwa na kupakiwa kwenye gari lao. Wakati huo mimi nilikimbia na kuwaangali kwa mbali.

    Si mimi tu aliyefanyiwa vile bali ni wengi. Lakini mimi niliona kama nimeonewa kutokana na magumu yangu kimaisha. Huo ulikuwa ni utawala wa rais Benjamin William Mkapa. Akiwa na mwaka mmoja tangu aingie madarakani akimpokea Mwinyi. Nilimchukia japo kura yangu nilikuwa nimempa.

    Mkapa ndiye chanzo cha mimi kutopiga kura tena hadi leo hii. Sikutaka tena kushiriki kumuweka mtu madarakani halafu nipate tabu ambayo angeweza kuizuia. Alitaka nikauze mirungi? Au bangi? Au gongo haramu ambayo inawaharibu vijana wetu wengi?" Hapo pia alinyamaza ghafla na kufunua goti lake la mguu wa kushoto.

    Akamuonyesha mwanae ambapo Steven alishuhudia goti la mama yake likiwa limepishana, japo hakuwa amepiga X-ray lakini lilionekana wazi.

    "Kipi kikufanya hivi mama?"

    "Sistahili kukuambia kilichonipata hadi goti langu likatenguka namna hii,lakini tambua lilinitesa sana hadi kupona. Nisamehe kwa kutokuweka wazi kwa hilo mwanangu Steve".

    "Sawa mama."Steve akaitika.

    “Wakanifukuza kama mbwa na mimi sikutaka kufuatilia suala hilo tena,lakini baadaye nilipata taarifa kuwa kituo kile kilisambaratika na baadhi ya watoto waliingia mtaani na kuwa machokoraa.

    Wale wadogo walichukuliwa na wale waliowapeleka pale kama ilivyokuwa kwangu kukuchukua wewe..

    Kituo kilisambaratika kwa sababu fedha zilizokuwa zimetumwa ziendeshe kituo,ziliingia mifukoni mwa wachache”.Yule mama aliendelea kumsimulia mwanaye mkasa uliokuwa umemsibu katika maisha yake.

    "Siku mbili tangu mgambo wale wanirudishe nyuma kimaisha, nilikwenda kwa Minza. Yule mama alieyekuwa ameniajiri. Nikashangaa kukuta ukarabati wa ile hoteli ukifanyika. Mmiliki hakuwa yeye tena bali alimuuzia jamaa mmoja ambaye alitaka kuweka nyumba ya kulala wageni pamoja na hoteli yenye hadhi.

    Hizo ni taarifa nilizozipata kwa mmoja wa kijana aliyekuwa mteja wetu. Kwa namna hiyo sikutarajia ajira tena mahali hapo.

    Nilipotoka hapo nikatembea kuja kituoni kwenu ili kuangalia maendeleo yako. Ndipo nikukuta wewe pamoja na wenzako ambao umri ulikuwa bado mdogo katika uvumilivu wa njaa, mkiwa mnalia. Nyote mkanizunguka huku wenye uwezo wa kuongea wakidai niwapatie chakula. Wakati huo neno njaa ulikuwa ukilitamka kwa tabu.

    Mlikuwa zaidi ya kumi na tano. Wale walezi wenu hawakuwepo hali iliyoibua maswali mengi sana kichwani mwangu. Mmoja wenu ambaye tayari akili zake zilishaanza kukomaa akaniambia tangu asubuhi hamkuwa mmepata chochote cha kuweka tumboni. Na walezi wenu hawajaonekana tangu asubuhi.

    Mwanangu Steve, ilibaki kidogo nizimie kwa taarifa hiyo niliyopewa na binti mdogo ambaye umri wake haukuwa ukizidi miaka sita. Nakumbuka nilikuwa nimevaa sketi ya mifuko. Nilipoingiza mkono mfukoni nikakutana na noti ya shilingi elfu tano. Enzi zile za utawala wa Mkapa shilingi elfu tano ulikuwa unanunua vitu vya kutosha.

    Nikakimbia haraka dukani na kununua maandazi. Nikawaletea mkatuliza njaa yenu. Nikakuweka mgongoni na kuelekea kwa aliyekuwa mtendaji wa kijiji ili kumpatia taarifa zenu.

    Nilipofika kwake, nikamkuta mkewe akiosha vyombo. Kulikuwa na sufuria la wastani likiwa na wali. Nikaanza kumuelezea kilichonipeleka pale. Wakati naendelea kutoa maelezo, nikashuhudia ule wali akiumwaga tena akicheka.

    Ilinisikitisha mno kuona watoto wadogo wanalia kwa ajili ya njaa halafu mtu ambaye alitakiwa kuwa mstari wa mbele kuwasaidia anamwaga chakula na tayari taarifa anayo. Kumbe wakati namueleza yote hayo na yeye kunisikiliza alikuwa ananikejeli kwani taarifa alikuwa nayo kabla. Hilo nililithibitisha pale alipotokea mme wake ambaye ndiye alikuwa mwenyekiti wa kijiji."



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog