Simulizi : Moyo Wangu Unavuja Damu
Sehemu Ya Pili (2)
Baada ya miaka miwili wakapata mtoto mwingine wa kiume, tofauti na kaka yake, yeye alifanana mno na baba yake. Watoto wakawa na afya njema, furaha na walipewa malezi bora.
Khalfan sasa akawa baba wa familia, mkewe Miriam naye akawa mama kama alivyokuwa akitamani siku zote. Waliyafurahia sana maisha yao. Muda mwingi walikuwa sambamba wakisaidiana kuwapa malezi bora watoto wao na kuwafundisha maadili mema. Utajiri nao ukawa unazidi kuongezeka kila kukicha, shamba na bustani zao za maua zikawa zinazidi kushamiri na kuwa “Evergreen” huku mazao yakistawi sana.
Wapo watu walioyahusisha mafanikio yale na imani za kishirina wakihisi kuwa huenda Khalfan Mwalukasa alikuwa akitumia nguvu za giza ili kupata mafanikio. Wapo walioanza kummezea mate wakiona kuwa hakustahili kuwa na mafanikio makubwa kama yale. Wala maneno ya walimwengu hayakuwarudisha nyuma. Walikuwa waimwamwini Mungu wao na walijitahidi kuishi vizuri na kila mtu, wakitoa misaada mingi ya kijamii kwa watu wenye shida na wanaoishi katika mazingira magumu.
Waliwasaidia pia watoto wenye shida mbalimbali hasa wale waliokuwa wakiishi kwenye mazingira magumu bada ya kufiwa na wazazi wao ama kutokana na hali duni za wazazi wao. Walijtahidi kwa kadri ya uwezo wao wote kugawana kile walichojaaliwa na Mungu kwa wale ambao hawakuwa nacho. Kadri muda ulivyokuwa unaenda wakazidi kujijengea jina na umaarufu huku kila mwenye shida akikimbilia kwao kuomba msaada.
Walifanikiwa pia kuanzisha kituo cha kulelea watoto yatima na wale wa mitaani, na wakaamua kukipa jina la “Shamsi Memorium Orphanage” ikiwa kama kumbukumbu ya mzee wao Shamsi na mkewe waliokuwa wameshatangulia mbele za haki.
Baada ya miaka kadhaa kupita, walikuwa na jumla ya watoto watano, wazuri wenye furaha na afya njema. Khalfan sasa akiitwa “mzee” khalfan na mkewe Bi Miriam waliyafurahia sana maisha yao na familia yao. Muda mwingi walikuwa sambamba na watoto wao wakiwafundisha maadili mema . Utajiri ukawa unazidi kuongezeka kila kukicha, familia yao ikiwa gumzo kila kona ya mtaaa . Wengine waliendelea kuamini na kuhusisha mafanikio yale na ushirikiana , huku wengine wakiamini kwamba mzee Khalfan alikuwa amebahatisha
Lakini ukweli ni kuwa juhudi na maarifa ndivyo vilivyofanya maisha yao yawe gumzo kila sehemu . Siku zikawa zinakwenda, lakini kama walivyosema waswahili penye riziki hapakosi chuki , na ili ufanikiwe zaidi unahitaji kuishi vizuri na kila mtu ingawa huwezi kukwepa kuwa na maadui, taratibu mzee Khalfan akaanza kuhisi kuwa na maadui wasiopenda mafanikio yake, alianza kuhisi marafiki zake anaoshirikiana nao katika shughuli zake za biashara wameanza kumfanyia hila kutokana na mafanikio anayoyapata, hakukosea kabisa . Hivyo ndivyo ilivyokuwa.
Wengi wa marafiki zake waliokuwa wakija kumtembelea pale nyumbani kwake walikuwa wakiyamezea mate mafanikio yake. Wengi walimwona kama hastahili kumiliki mali nyingi na za thamani kama alizokuwa nazo, wakaanza kupanga njama kila mmoja kwa wakati wake , wote wakitaka kumiliki mali zilizokuwa chini ya uangalizi wa khalfan na mkewe Bi Miriam. Hilo halikuwapa sana hofu khalfan na mkewe kwani waliamini Mola wao atawapigania kwa haki kwa kwa hakuna lolote baya walilomfanyia , wala hawakuwa na roho mbaya kwa mtu yeyote yule. Wote waliokuja kuomba misaada ya kimaisha walipewa walichohitaji kwa moyo wa ukarimu.
Ilikuwa ni kawaida ya familia yao kwenda kubarizi ufukweni mwa bahari kila mwisho wa wiki , siku za jumamosi na jumapili wakipendelea kukaa sehemu tulivu wakipunga upepo mwanana wa baharini huku wakibadilishana mawazo na kucheza na watoto wao.
Ilikuwa ni jumapili tulivu , majira ya jioni kabla ya jua halijazama… Khalfan na mkewe walikuwa wakirudi kutoka ufukweni walikokuwa wamekwenda kubarizi pamoja na watoto wao . Bi Miriam ndiye aliyekuwa akiendesha gari huku mumewe akiwa amekaa pembeni yake na watoto wakiendelea kucheza siti ya nyuma , baada ya muda mfupi wakawa wamefika kwenye geti la kuingia kwenye himaya yao . Bi Miriam alipiga honi mfululizo na mlinzi akatoka mbio kuja kuwafungulia.
Baada ya mlinzi kufungua mlango Bi Miriam aliingiza gari mpaka sehemu ya maegesho , akashuka na kumfungulia mumewe mlango naye akashuka kisha wakawashusha watoto wao. Kwa muda wote huo mlinzi alikuwa amesimama pembeni yao akionekana kuwa na jambo alilotaka kumwambia bosi wake, mzee Khalfani. Alisubiri wamalize kushushana ndipo ampe ujumbe aliokuwa amepewa muda mfupi uliopita kabla hawajarudi .
Khalfan aligundua kuwa mlinzi hayuko katika hali ya kawaida ikabidi amsogelee palepale alipokuwa amesimama . Mlinzi alitoa ujumbe aliokuwa amepewa na kumkabidhi mzee Khalfan, ilikuwa ni bahasha ya ukubwa wa kati iliyokuwa imefungwa vizuri. Nje ya bahasha ile hakukuwa na anuani wala jina la mtu aliyetumiwa , ila yalisomeka maandishi makubwa ya wino mwekundu “SIRI”.
Kilichomshtua khalfan ni jinsi mlinzi alivyokuwa na hofu wakati akimkabidhi ujumbe ule, alijaribu kumhoji juu ya mtu aliyeileta barua ile lakini akawa anamjibu kwa kubabaika. Alieleza kuwa muda mfupi uliopita gari ndogo nyeusi na ya kifahari ikiwa na vioo “TINTED” vya rangi nyeusi iliwateremsha wanaume wawili waliovalia makoti marefu meusi na kofia kubwa zilizoficha sura zao, mmoja akaenda mpaka pale mlangoni na mwingine akawa amebakia kwenye gari.
“Bila hata salamu akanipa bahasha na kusema nikupe wewe ukirudi!” Aliendelea kueleza mlinzi. Khalfan hakutaka kuhoji zaidi, akachukua ile bahasha na kuingia nayo ndani. Muda huo mkewe alikuwa ameshatangulia ndani na watoto akawa anaendelea kuwaandalia chakula cha jioni. Akapitiliza mpaka chumbani na kwenda kuifungua bahasha ile.
Alijikuta mikono ikianza kutetemeka alipoanza kuifungua bahasha ile akakutana na maandishi ya wino mwekundu ambayo yalisomeka vizuri. Ulikuwa ni ujumbe uliojaa vitisho na maneno ya kibabe, ukimtaka eti ‘ahame hapo nyumbani kwake yeye na familia yake yote bila kuchukua kitu chochote kwa sababu yeye Khalfan hakuwa mmiliki halali wa eneo hilo. Ujumbe ule ulizidi kutishia kwamba wanampa siku saba za kuwa ameshaondoka na onyo kali likatolewa kuwa asijaribu kutoa taarifa sehemu yoyote kwa kuwa kwa kufanya hivyo angehatarisha uhai wake.’
Alijikuta akicheka kwa dharau na kisha akatoka na ile bahasha mpaka sebuleni alikokuwa amekaa mkewe na watoto wake wakiangalia luninga. Mkewe alishtuka kumuona mumewe ameanza kubadilika, ingawa usoni alikuwa akicheka lakini alionekana kuchanganyikiwa sana akampa ule ujumbe ili na yeye ausome.
“Unatakiwa uhame hapo unapoishi wewe na familia yako bila kuchukua kitu chochote. Huna haki ya kumiliki eneo zuri kama hilo, wamiliki halali tupo na tulikuwa tunangoja muda ufike tukuambie.
Usijaribu kutoa taarifa sehemu yoyote , polisi wala jeshini kwani kwa kufanya hivyo utahatarisha usalama wako na hizo takataka zako (mkeo na watoto) unapewa siku saba za kutekeleza amri hii na ukiipuuza utaona matokeo yake”
NB. Uhai hautafutwi ila mali zinazotafutwa
By
Wamiliki
Bi Miriam alishusha pumzi ndefu baada ya kumaliza kuisoma, huku akiwa amepigwa bumbuwazi asijue nini cha kufanya. Kwa muda wote huo Khaflan alikuwa akizunguka-zunguka pale sebuleni akiwa haelewi anatafuta nini . watoto walikuwa hawana habari wakawa wanaendelea kucheza na kuruka kwenye masofa ya kisasa yaliyokuwepo pale sebuleni.
Khaflan alirudia kuisoma barua ile kisha akatoka kwa kasi kumfuata mlinzi nje. Alianza kumhoji upya ni nani aliyeleta ujumbe ule na mlinzi akarudia maelezo kama aliyoyatoa mara ya kwanza. Safari hii alionekana kuhofia zaidi baada ya kumuona bosi wake amechanganyikiwa.
Hakujua mle ndani mliandikwa nini lakini kwa hal aliyokuwa nayo bosi wake ilionyesha kuna jambo baya. Mzee Khalfan alirudi ndani na kumuelekeza mkewe awape chakula watoto haraka kisha akawalaze . Alipitiliza mpaka chumbani na kujitupa kitandani kama mzigo.
Maswali mengi yalikuwa yakipishana kichwani kama umeme wa gridi ya taifa . Alijalibu kuwaza na kuwazua ni akina nani walioleta ujumbe ule, hakupata jibu. Muda mfupi baadae mkewe akawa ameshamaliza kuwapa chakula wanae na akaenda kuwalaza kwenye chumba chao. Ama kwa hakika usiku huo ulikuwa ni usiku wa mauzauza kwao. Mpaka jogooo la kwanza linawika kuashiria mapambazuko, Khalfani na mkewe walikuwa hawajapata hata tone la usingizi.
Usiku kucha walikuwa wakijadiliana wafanye nini, hakuna aliyekuwa na jibu. Mwisho wakafikia uamuzi wa kwenda kutoa taarifa kituo cha polisi ingawa barua ile iliwaonya vikali juu ya uamuzi huo.
“Lakini mume wangu , si ni bora tuondoke tu tuwaachie wafanye wanachotaka ? nahofia usalama wa wanangu, tuondoke tu Mungu atatusimamia huko tuendako kwani mali hutafutwa lakini uhai hautafutwi.”
Wazo hilo halikuingia akilini mwa mzee Khalfani, kwani kufanya hivyo kungemaanisha yeye ni mwanaume dhaifu asiyeweza kuilinda familia yake aliamua kutetea msimamo wake.
”Mke wangu siko tayari hata kwa mtutu wa bunduki kuruhusu watu wengine wayaharibu maisha yetu! niamini nitafanya kila niwezalo kukulinda mke wangu na wanangu na mali zangu zote! Hakuna wa kuchukua chochote kutoka mikononi mwetu, siwezi kusalimu amri kirahisi namna hii, niamini…”
Kwa jinsi alivyokuwa akiongea kwa kujiamini, mkewe akapata imani kuwa usalama wao utalindwa kwa kila namna. Kulipopambazuka tu, mzee Khalfani na mkewe wakaanza kujiandaa kwenda kutoa taarifa kituo cha polisi cha Blazinia Central Police Post”.
Walichukua barua ile kama ushahidi wa maelezo yao. Mzee Khalfan aliendesha gari lao huku mkewe akiwa pembeni yake. Hakuna aliyemsemesha mwenzake! Kila mtu alikuwa kwenye lindi zito la mawazo, maneno ya barua ile yalikuwa yakijirudiarudia vichwani mwao.
*******
Kulipopambazuka tu, Khalfani na mkewe wakaanza safari ya kwenda kutoa taarifa kwenye kituo kikuu cha polisi cha Blazinia “Blazinia Central police post”. Walienda na barua ile waliyoletewa kama ushahidi wao. Dakika chache baadae walikuwa wameshafika kituoni na wakashuka na kuingia ndani mpaka kaunta ambapo waliomba kukutana na mkuu wa kituo. Muda mfupi baadae wakawa ndani ya ofisi ya mkuu wa kituo, Luteni Lauden Kambi, aliyekuwa akifahamika kwa jina la utani kama “Luteni Fuvu” kutokana na ukatili wake.
Mzee Khalfan alianza kueleza kila kitu kuanzia mwanzo mpaka mwisho, na Luteni akawa anaandika kila kitu kwenye faili jeusi. Alipomaliza kueleza, Luteni Lauden Kambi aliwajibu kwa kifupi kuwa waende nyumbani kwao baada ya kuacha maelezo yote ya msingi ya mahali na mtaa wanakoishi, jeshi litawapa ulinzi baada ya siku hizo saba kupita. Aliwatoa hofu kuwa vile ni vitisho vya kawaida ambavyo vinahitaji ujasiri kuweza kukabiliana navyo. Aliwapa pia maelezo kuwa warudi siku ya sita hapo kituoni ili waambiwe nini cha kufanya. Baada ya kuridhika na maelezo waliyopewa, Khalfan na mkewe waliaga na kurudi nyumbani kwao wakiwa na matumaini makubwa ya kupewa msaada na jeshi la polisi
Siku zikawa zinasonga mbele kwa haraka mno, mara ikafika siku ya sita…yakiwa yamesalia masaa Ishirini na nne tu kabla ya siku ya mwisho waliyoambiwa kuwa wanatakiwa wawe wameondoka katika eneo lile, siku ya Jumapili. Hawakuwa na wasiwasi tena wakiamini wako salama wa kuwa walishahakikishiwa kuwa watapewa ulinzi. Walichokifanya ni kwenda kutoa ripoti Polisi siku moja kabla, yaani Jumamosi Kama walivyokuwa wameelekezwa na mkuu wa kituo cha polisi, Luteni Lauden kambi “Fuvu”.
Wakajitayarisha kwa safari ya kwenda tena Blaziniar Central Police post wakiwa na matumaini makubwa ya kupewa ulinzi. Safari hii gari lao liliendeshwa na Bi Miriam huku Khalfan akiwa ametulia siti ya pembeni. Walipofika waliomba tena kuonana na Mkuu wa kituo. Yule Askari aliyekuwa pale kaunta aliwapa taarifa kuwa Mkuu wa kituo ameanza likizo yake ya mwezi mzima kuanzia siku ya Ijumaa, yaani jana yake na kwa muda huo alikuwa ameshasafiri kurudi kwao alikoenda kuimalizia likizo yake.
Alizidi kuwaambia kuwa shughuli za ukuu wa kituo alikuwa amepewa mtu mwingine ambaye naye alikuwa safarini kikazi. Maelezo yale yalionekana kuwachanganya mno Khalfan na mkewe. Yale matumaini waliyokuwa nayo yakawa yamepotea Kama barafu inavyoyeyuka kwenye moto mkali. Walionyesha hofu na woga waziwazi vikiambatana na kupoteza matumaini Kiasi cha kumfanya yule Askari aliyewapa taarifa ile kushtuka. “Kwani kuna tatizo gani mzee! niambieni labda naweza kuwasaidia hata kama Mkuu hayupo”
Ilibidi mzee Khalfan aanze tena kueleza upya kuanzia mwanzo. Baada ya maelezo yake
yule Askari aliwaomba waongozane mpaka kwenye Ofisi ya Mkuu wa Kituo, wakatafute faili ambalo maelezo yao yalihifadhiwa pamoja ile barua waliyokuwa wameileta kama uthibitisho. Dakika chache baadae wakawa tayari ndani ya Ofisi ya Mkuu wa Kituo. Yule Askari akaanza kutafuta faili lenye maelezo yao.
‘’Unasema mlikuja kutoa ripoti siku gain?” Yule askari alimhoji mzee Khalfan.
‘’Jumatatu iliyopita afande…‘’
Aliendelea kutafuta maelezo yale kwenye mafaili moja baada ya jingine.
‘’Aliweka maelezo yetu kwenye faili jeusi pamoja na ile barua’’ alizidi kusisitiza Bi Miriam huku wote wakimkodolea macho yule askari aliyekuwa akiendelea kupekua faili moja baada ya jingine. Baada ya kutafuta kwa muda mrefu karibu kila mahali, yule askari aliwageukia mzee Khalfan
na mkewe na akawaambia kuwa labda wasubiri kidogo ampigie simu bosi wake hata kama yuko likizo angewaelekeza alipolihifadhi faili lile.
Wakatoka Ofisini na kurudi kaunta ambako yule askari alinyanyua mkonga wa simu na kuanza kuongea na mkuu wa Luten Lauden Kambi. ‘’Amesema msiwe na wasiwasi, rudini nyumbani ila muache ramani ya mtaa mnakoishi, jina la mtaa, jina la balozi na namba ya nyumba eti ameshaacha maagizo na polisi watakuja kuwapa ulinzi wa kutosha kuanzia majira ya jioni.’’
Alimaliza yule Askari kuwapa maelezo aliyopewa na Mkuu wa kituo kwenye simu. Mzee Khalfan ali shusha pumzi ndefu kisha akamgeukia mkewe, wakatazamana kwa muda kisha yule askari akawapa
Karatasi kwa ajili ya kuacha maelezo ya mahali nyumba yao ilipo, jina la mtaa, jina la balozi na namba ya nyunba. Mzee Khalfan akaanza kuandika upya. Baada ya kuhakikisha kuwa maelezo waliyoyaacha ni sahihi mzee Khalfan na mkewe wakaaga na kuondoka.
Kengere ya hatari ilishalia kichwani mwa Khalfan, akahisi kuna mchezo mchafu unaotaka kuchezwa na askari wale askari. Iweje watoe maelezo mara ya pili ilhali walishahakikishiwa usalama wao?
Hakutaka kumwambia mkewe alichokihisi kwa kuogopa kumuongeza hofu. Wakapanda garini na safari ya kurudi kwao ikaanza safari hii pia hakuna aliyekuwa akimsemesha mwenzake… kimya kimya
mpaka nyumbani.
Masaa yakawa yanazidi kuyoyoma, saa kumi jioni… kumi moja… kumi mbili, mara saa tatu usiku… nne tano kasoro… Hakukuwa na dalili yoyote ya polisi kufika eneo hilo kama walivyoahidiwa na Luten Lauden ‘’Fuvu”. Kwa muda wote huo mzee Khalfan alikuwa nje pamoja na walinzi wake watatu na wengine wawili aliwakodi kwa ajili ya kuhakikisha usalama wa eneo zima la kuzunguka nyumba yao ili kulinda usalama.
‘’Boss! hao polisi uliosema watakuja tusaidiane nao kazi mbona hawaji na muda ndio unazidi kwenda? saa tano usiku sasa!’’ Alihoji mlinzi mmoja kwa niaba ya wenzake. Mzee Khalfan hakuwa na jibu la kuwapa, zaidi swali lile lilionekana kumchanganya akili. Tangu saa moja jioni alikuwa akiwapa darasa walinzi wake ikiwa ni pamoja na kuhakikisha bunduki wanazotumia (magobore) yako katika hali ya utayari kwa kazi muda wowote. Alihakikisha pia kuwa bastola yake aliyoachiwa na marehemu mzee Shamsi imejaa risasi za kutosha.
Wote wakawa wamejiandaa vya kutosha wakitegemea muda wowote polisi wangefika kuungana nao kuwasubiri hao wanaotaka kuwadhulumu mali zao kwa nguvu. Walijiandaa kutoa upinzani wa kutosha kwa yeyote ambaye angethubutu kuleta ujeuri wa aina yoyote ile katika eneo lile. Bi Miriam naye alikuwa amewahi kuwaingiza watoto wake ndani mapema kuliko siku yoyote. Wakawahi kula chakula cha usiku kisha wote wakaenda kulala. Alihakikisha milango yote na madirisha yamefungwa ipasavyo.
Mzee Khalfan hakutaka kuingia ndani. Alitaka ashirikiane bega kwa bega na walinzi hata kama polisi hawatafika. Walinzi walimshauri aende ndani kwani walikuwa wakijiamini kuwa wanaweza kazi. Baada ya mabishano kidogo, hatimaye mzee Khalfan alikubali kurudi ndani huku bastola yake ikiwa mkononi “standby” kwa lolote. Muda ukazidi kuyoyoma…mara saa sita usiku… Saa saba na hatimaye saa nane.
Eneo zima lilikuwa kimya kabisa huku giza nene likiwa limetanda kila sehemu. Walinzi walikuwa waki zunguka huku huko kuhakikisha hakuna mtu anayesogelea eneo lile. Bunduki zao zilikuwa “standby” mikononi wakisaidiwa na mbwa mkubwa wa mzee Khalfan. Giza lilikuwa likizidi kushamiri na kufanya hali
ya eneo lile izidi kutisha. Ilishatimia saa tisa usiku huku bado kukiwa kimya kabisa.
Ghafla zilianza kusikika kelele za mbwa aliyekuwa akibweka na kukimbilia kwenye geti kubwa la kuingilia. Walinzi wakajua mambo yameanza, kwa umakini mkubwa nao wakaanza kunyata kuelekea kule mbwa alikokuwa anakimbilia. Alizidi kubweka na walinzi nao wakawa wanazidi kusogea kuelekea kule getini. Mara walishtukia kuona mbwa akipigwa risasi nyingi kichwani kisha akadondoka chini, Puuuh! Ile milio ya risasi ilitosha kuwamaliza kabisa ujasiri wote waliokuwa nao wale walinzi, kwani ilionekana dhahiri maadui zao wamekuja na bunduki nzito za kivita.
Hawakuelewa risasi zimetokea upande gani wakawa wanaangalia huku na huko. Wakiwa bado wanashangaa walishtukia kujikuta wote wamemulikwa na tochi kali kisha mvua ya risasi ikaanza kuwanyeshea. Sekunde chache baadae walinzi wote watano walikuwa chini wakitapatapa kukata roho baada ya shambulizi la ghafla risasi zilikuwa zimepenya vichwani mwao kisawasawa.
Kelele za shambulizi lile ziliwafanya wote waliokuwa ndani ya nyumba ya mzee Khalfan kushtuka. Watoto walianza kupiga mayowe hovyo ya kuomba msaada. Bi Miriam naye alikuwa hajitambui kwa hofu. Mzee Khalfan akapiga moyo konde na kunyanyua bastola yake, akaikamata kisawasawa. Akafungua mlango wa chumbani na kuanza kutoka huku akinyata kwa tahadhari kubwa. Mkewe alijaribu kumzuia asitoke lakini wapi! Akanyatia mpaka sebuleni. Akiwa katikati ya sebule, alishuhudia mlango wa nje ukivunjwa kwa jiwe kubwa kisha watu wapatao saba, wote wakiwa wamevalia makoti marefu meusi, usoni wakiwa wamevaa vitambaa vya kuficha sura zao (masks) , mikononi wakiwa na bunduki nzito za kivita kila mtu ya kwake wakiingia kwa kasi na kumzunguka pale aliposimama…
‘’Weka silaha chini! ‘’ Mmoja wa majambazi yale alimuamuru mzee Khalfan kwa sauti ya ukali mno. Akajikuta akitetemeka mwili mzima kiasi cha kuhisi haja ndogo ikimtoka bila ya ridhaa yake. Hakuwa na cha kufanya zaidi ya kudondosha bastola yake chini kisha kuinua mikono juu kusalimu amri. Yale majambazi yakaanza kumshambulia kama mpira wa kona. Alipigwa na kitako cha bunduki kichwani akadondoka chini kama mzigo.
Yakaanza kumshushia kipigo cha nguvu kwa zamu zamu. Alijitahidi kujitetea lakini alizidiwa nguvu. Majambazi wengine wakaingia vyumbani na kuwatoa Bi Miriam na watoto wake wote. Kipigo kikaendelea kwa wote… hata mtoto wao mdogo wa mwisho ambaye na miaka miwili tu! Ikawa ni kichapo mtindo mmoja.
Mtoto wa kwanza wa Mzee Khalfan, Khaleed, ambaye kwa kipindi hicho alikuwa na miaka kumi na tatu, alifanikiwa kujificha chini ya meza kabla ya majambazi hayajamuona. Aliendelea kushuhudia jinsi baba’ake, mama’ake na wadogo zake walivyokuwa wakisulubiwa. Uchungu ulimuingia mno kiasi cha kushindwa kuvumilia. Kwa haraka alitoka chini ya meza na kunyanyua chuma kilichokuwa sakafuni, kisha akakinyanyua kwa nguvu zake zote na kukirusha kwa jambazi mmoja. Kilitua sawia kichwani kiasi cha kufanya jambazi lile lidondoke chini.
Akajikuta amedakwa juu juu kama kifaranga cha kuku mbele ya mwewe. Kisha naye akaanza kusulubiwa. Sekunde chache tu baadaye naye akawa ameloa damu mwili mzima kama wenzake. Kichapo kiliendelea mpaka wote wakawa hoi taabani. Yale majambazi yakawafunga wote kwa kamba, mikononi na miguuni na kuwajaza matambara midomoni mwao. Kisha yakaanza kuwaburuza mpaka nje ambako yalianza kuwapakiza kwenye gari yaliyokuja nayo. Yalikuwa yakiwarusha kama magunia,wakati yaiwapakia kwenye Landrover. Gari likawashwa na kuanza kuondoka kwa kasi ya ajabu kuelekea kusikojulikana. Eneo zima liliachwa likiwa limetapakaa damu na maiti tano za walinzi zikiwa zimelala chini. Ukimya ukatawala eneo zima, tena safari hii kukiwa kunatisha zaidi kwani hakuna aliyekuwa amesalia akiwa hai eneo lile.
Saa kumi na nusu alfajiri gari aina ya ya landrover 110 lilikuwa likiacha barabara kuu na kuingia barabara ya vumbi kuelekea pori la gamutu . Gari lilikuwa likiendeshwa kwa kasi kubwa mno, na dereva hakupunguza mwendo wakati akikata kona kuiacha barabara ya vumbi na kuingia katikati ya vichaka. Gari lilizidi kutokomea ndani kabisa ya pori kisha likasimama katikati ya pori.
“Hebu washusheni hao wanaharamu haraka!”
Sauti ilisikika ikitoa amri kwa ukali . Lilikuwa ni gari la yale majambazi yaliyowateka mzee Khalfan na familia yake. Kutokana na kipigo walichokuwa wamekipata kutoka kwa majambazi yale yenye roho mbaya kupindukia wote walikuwa wamepoteza fahamu isipokuwa Mzee Khalfan aliyekuwa akiendelea kuguna kutokana na maumivu makali aliyokuwa akiyahisi baada ya kula kichapo kikali.
Kwa msaada wa tochi kubwa zenye mwanga mkali, majambazi yale yalianza kuwashusha toka garini mmoja baada ya mwingine. Mzee Khalfan ndio alikuwa wa kwanza kushushwa. “Huyu mfungeni peke yake kwenye huo mti mkubwa”
Jambazi mmoja aliyeonekana kuwa ndio kiongozi wao alitoa amri kwa sauti nzito.
“Hawa wengine wafungeni watatu kwenye miti hii miwili” Kilichofuata ikawa ni utelekezaji wa amri iliyotolewa. Kamba za katani zikaanza kufungwa kwenye mashina ya miti kisha wakaanza na Mzee Khalfan, akafuatia Bi Miriam aliyeunganishwa na kufungwa na mabinti zake wadogo wawili. Alifuatia mtoto wao wa kwanza Khaleed ambaye kwa muda wote huo fahamu zilishamrudia naye akawa akishuhudia kila kitu kilichokuwa kinaendelea . Yeye alifungwa pamoja na wadogo zake wawili kwenye mti mmoja.
Mzee Khalfan hakuwa na cha kufanya zaidi ya kutokwa na machozi ya uchungu wa kuonewa kwani aliamini huo ndio mwisho wao kwani wasingeweza tena kutoka salama ndani ya pori lile. Kilichomsikitisha zaidi ni aina ya kifo kilichokuwa kinawangoja, kuwa kitoweo cha simba kabla ya mapambazuko… ilitisha.
Baada ya kumaliza kuwafunga wote, majambazi yale yalimsogelea Mzee Khalfan na kumuinua uso pale chini aliofungwa, kisha yule aliyeonekana kuwa na amri zaidi akaanza kumsemesha kwa sauti kavu na nzito iliyokwaruza.
“Pole Khalfan kwa kuwa muda si mrefu wewe pamoja na familia yao mtakuwa chakula cha simba wa Gamutu. Laiti kama ungetii amri uliyopewa, usingepatwa na balaa hili… ila ubishi wako ndio umekuponza. Kabla hujafa ningependa ujue kwamba sisi ni watekelezaji tu, hii kazi tumetumwa na wenzako mnaofany nao Biashara… The Holly Trinity wakiongozwa na swahiba wako Musa Mtaki na Pius Bagenda. Bila shaka unawafahamu vizuri kwa kuwa ni marafiki zako wapendwa. Hao ndio waliotutuma tukumalize… haa! Haa! Haa!… majambazi yale yaliangua vicheko vya dharau huku yakigongeshana vitako vya bunduki zao. Walichokifurahia ni donge nono la mamilioni ya pesa waliyoahidiwa na “The Holly Trinity” Umoja wa wafanyabiashara wakubwa watatu wakiongozwa na rafiki mpendwa wa mzee Khalfan, Musa Mtaki.
“Salamu zao kuzimu kwani hamuwezi kunusurika na mauti! msisahau kusali kabla simba hawajafika kuwatafuna…” vicheko vya kebehi vikaanza upya, kisha wakaanza kuondoka kulifuata gari lao. Muda mfupi baadaye yakawa yameshaingia ndani ya gari lao na kutoweka eneo lile kwa kasi.
Mzee Khalfan alishindwa kujizuia kutoa machozi… sasa alikuwa ameshapata picha kamili ya watu waliokuwa nyuma ya tukio lile, “The Holly Trinity”. Hawa walikuwa ni marafiki zake wa kibiashara “Business friends” wa siku nyingi aliokuwa akishirikiana nao katika shughuli mbalimbali za kibiashara. Kundi hilo la lilikuwa likiundwa na Pius Bagenda, Musa Mtaki na Jamal Maziku, wote wakiwa ni wafanyabiashara wa madini na vito vya thamani.
Mawazo yalianza kupishana kichwani akijaribu kuwaza na kuwazua kuwa aliwakosea nini rafiki zake hao mpaka wakafikia hatua ya kumfanyia unyama wa kiasi kile? Hakukumbuka kama alishawahi japo kuwakwaruzana na yeyote kati yao! Sasa kwa nini wafanye vile?... hakupa jibu.
Kwa muda wote huo mwanae wa kwanza Khaleed alikuwa kimya akimuangalia baba yake. Alimuonea huruma kwa jinsi alivyokuwa akisikitika. Aliyasikia pia mazungumzo ya yale majambazi na akaelewa vizuri waliohusika kuwafanyia vile kwani hata yeye alikuwa akiwafahamu vizuri sana, Mzee Mtaki ambaye licha ya kuwa alikuwa akiwatembelea mara kwa mara nyumbani kwao, pia alikuwa akisoma darasa moja na mwanae kwenye shule ya kimataifa ya St Benedict -Blaziniar wote wakiwa kidato cha kwanza. Alijikuta akiwachukia mno wote waliohusika kuwafanyia unyama ule na akajiapiza kuwa lazima aje kulipa kisasi!
“I must revenge…”
Alijikuta akifoka kwa hasira maneno yake yalimshtua baba yake aliyekuwa amezama kwenye lindi la mawazo machungu. Alishindwa kujibu kitu kwani matambara aliyojazwa mdomoni yalimpa shida ya kuzungumza. Akilini mwake alimhurumia mwanae kwani alikuwa ameshuhudiaukatili wa kutisha usiku huo, tena akiwa bado mdogo, na zaidi aliwahurumia wanae, kwani aliamini wasingeweza kutoka salama porini Gamutu. Aliamini Simba wa Gamutu wangewamaliza palepale bila ya mtu yeyote kujua . Alibaki kusali kimoyomoyo ili Mungu wao awaepushie kifo cha namna ile.
Ilikuwa imeshatimia saa kumi na moja alfajiri, giza likiwa limeanza kupungua polepole. Khaleed alikuwa akijaribu kujinasua kwa nguvu kutoka pale alipofungwa. Baba yake alikuwa akimtazama huku akimkataza kwa ishara kwani kwa kuendelea kufanya vile angezidi kujiumiza kwani kila alipojaribu kuinuka, kamba zilizopita mwili mzima zikawa zinamrudisha chini.
“Baba!... Baba!... Ona wanarudi tena”
Aliongea Khaleed akimuonyeshea baba yake upande ambao vitu kama tochi vilikuwa vikiwasogelea. Mzee Khalfan alipojigeuza kwa shida na kuangalia upande ule alioonyeshwa na mwanae Khaleed, nguvu zilimwishia kabisa akajikuta ametamka kwa sauti ya kukata tama… Mungu wangu !!
Khaleed kwa uelewa wake mdogo alidhania ni watu walioshika tochi nyingi ndio waliokuwa wakiwasogelea, lakini haikuwa hivyo! vile vilivyoonekana kama tochi yalikuwa ni macho ya Simba wa Gamutu waliokuwa wakiwasogelea. Macho ya simba yalikuwa na tabia ya kuwaka gizani kama tochi.
“shiiii…shiiii…”
Mzee Khalfan alijaribu kumzuia Khaleed asipige kelele kwani kwa kufanya hivyo ndio kuongeza hatari iliyokuwa ikiwakaribia. Sekunde chache baadae, mti aliofungwa Khaleed na wadogo zake wawili ulizingirwa na simba wapatao saba waliokuwa wakitoa ngurumo za kutisha wakionyesha meno yao makali. Khaleed hakuwahi kuwaona simba ana kwa ana zaidi ya kuwaona kwenye TV, kitendo kile cha simba wale kuunguruma kwa njaa kali waliyokuwa nayo, tena wakiwa karibu kabisa… kilimfanya Khaleed ahisi kama yuko ndotoni. Mwili wote ukafa ganzi akawa akitetemeka kupita kiasi.
Kufumba na kufumbua wale simba waliwavamia kwa kishindo kikuu na kukatakata kamba walizokuwa wamefungwa . Khaleed alijaribu kujitetea kwa kuwatisha samba lakini haikusaidia kitu. Kwa macho yake alishuhudia mdogo wake wa kwanza akiraruliwa kwa meno na makucha makali ya simba wenye njaa… akiwa bado amepigwa na butwaa , alishuhudia mdogo wake wa pili naye akiraruliwa vibaya na simba , ikabakia zamu yake…
Akili yake ilifanya kazi kwa kasi ya ajabu, akakumbuka mbinu aliyowahi kufundishwa shuleni na mwalimu wake wa somo la Biology, akajinyoosha taratibu chini na kubana pumzi kiasi cha kufanya aonekane kama amekufa. Wale Simba wakaanza kumnusa huku na huko wakijiandaa kumrarua. Akazidi kubana pumzi na kujifanya amekufa…aljitahidi mno kujibana na kweli akaweza…Simba wakahisi ni mzoga , wakamuacha palepale chini. Muda mfupi baadae alisikia wale simba wakiburuza miili ya wadogo zake na kutokomea nayo gizani. Alizidi kujibana pale chini mpaka alipohakikisha wale simba wametokomea kabisa vichakani. Eneo zima likawa limetapakaa damu. Alipoinuka na kumtazama babaake mzee Khalfan, naye alikuwa amejikausha kama amekufa huku naye akiwa amezibana pumzi zake.
Baada ya Simba kuwavamia pale chni ya miti walipokuwa wamefungwa, Khaleed anatumia mbinu kali ya kubana pumzi na kujifanya amekufa, mbinu ambayo inamuokoa kutoka kwenye shimo la mauti. Anashuhudia wadogo zake wawili wakiburuzwa na kwenda kuwa kitoweo cha simba wenye njaa. Anamgeukia baba yake ambaye naye amejikausha kama amekufa ili kukwepa kuliwa na Simba.
Alipougeukia mti aliofungwa mamaake, alimuona akiwa bado hajitambui kutokana na kipigo cha yale majambazi kilichomfanya apoteze fahamu. Wadogo zake wawili waliosalia ambao walikuwa wamefungwa pamoja na mama yao, nao walikuwa hawajitambui kwa majeraha makubwa waliyoyapata na kusababisha wapoteze damu nyingi.
Matumaini ya kunusurika yalikuwa yamefifia kabisa, kwani kwa mbali kidogo ilisikika mingurumo ya wale simba wakijichana mawindo yao. Roho ilimuuma sana Khaleed na akawa anahisi kama yuko ndani ya ndoto ya kutisha. Haikuwa ndoto…Alijikuta akishindwa kujizuia kulia kimya kimya kwa kuomboleza.
Akili yake iliacha kufanya kazi kwa muda akiwa kama mtu aliyepigwa na ‘shock’ ya umeme. Hakutaka kuamini kama yale matukio yalikuwa ni ya kweli lakini ukweli ukabaki kuwa uleule. Walikuwa wakisubiri kifo cha kuliwa na simba muda wowote.
Mara akaanza kuhisi manyunyu ya mvua yakianza kudondoka. Alipotazama angani, wingu zito la mvua lilikuwa likitanda kila mahali na kuimeza kabisa ile nuru hafifu ya alfajiri iliyokuwa imeanza kuonekana. Radi kali zikaanza kupiga na kumulika huku na kule na kufanya hali iwe ya kutisha kupita kiasi. Radi na ngurumo ziliendelea huku manyunyu yakizidi kuongezeka. Mara Khaleed akaanza kusikia tena sauti za wale simba zikisogelea pale chini ya miti walipokuwa wamefungwa.
Akawa anatetemeka akijua zamu yake imefika. Akiwa anahaha kujiokoa ndipo alipogundua kuwa zile kamba alizokuwa amefungwa kumbe zilikuwa zimekatwakatwa wakati walipovamiwa na samba kwa mara ya kwanza. Kwa haraka alinyanyuka huku miguu ikiwa inatetemeka kupita kiasi. Sauti za wale simba zilizidi kusogea jirani na sasa zikawa zinasikika mita chache tu kutoka pale walipokuwa wamefungwa. Kwa ujasiri wa ajabu, Khaleed aliinuka na akakimbilia pale alipokuwa amefungwa baba yake na kwa kasi ya ajabu akaanza kumfungua kamba alizokuwa amefungwa mwili mzima.
Radi zilizidi kuongezeka na manyunyu nayo yakawa yanaongezeka kwa kasi kuashiria mvua kubwa. Mzee Khalfan alishtuka kuona akiguswa akidhani ni wale simba wameishafika, lakini alipoinua uso alimuona mwanae Khaleed akihangaika kumfungua. Alijikuta akipata nguvu na matumaini mapya ya kunusurika na kifo kibaya kama kile.
khaleed alimtoa baba yake matambara aliyojazwa mdomoni na akawa anaendelea kumfungua kwa kasi.
‘’Kazana nwanangu! Do it hurry my son… simba wameishafika!”
Mzee Khalfan alikuwa akimhimiza mwanae kuongeza kasi ya kumfungua kwani tayari Simba walikuwa jirani kabisa.
Alipomaliza tu kumfungua, kundi kubwa la simba lilikuwa limeshafika pale chini ya miti walipokuwa. Mtu na baba yake wakabaki kutazamana wasijue cha kufanya.
‘’What can we do dad?’’
Khaleed alimuliza baba’ake kwa sauti ya kunong’ona huku akijificha nyuma yake. Ile Bunduki ilikuwa mbele yao umbali wa hatua chache, jirani kabisa na kundi la wale simba ambao walikuwa wakizidi kuwasogelea. Swali likabaki kuwa wataichukuaje ilhali simba nao ndio walikuwa wakizidi kusogea huku wakinguruma kwa sauti za kutisha.
Mzee Khalfan akiwa bado anatazamana na wale simba ana kwa ana, akili yake ikawa inafanya kazi kwa kasi ya ajabu. Wazo jipya likamjia… akakumbuka kuwa mfukoni alikuwa na kibiriti cha gesi. Akamwita Khaleed kwa ishara na kumwelekeza kitu cha kufanya. Kwa haraka Khaleed akavua shati lake na kuliwasha moto kama alivyoelekezwa, akampa babaake kisha wakaanza kusogea mbele taratibu wakiwasogelea wale simba.
Simba kuona moto ukiwasogelea, wakaanza kurudi nyuma huku wakizidi kunguruma kwa hasira . Mzee Khalfani alijikaza kiume na akawa anazidi kusogea mbele huku mwanae Khaleed akiwa anamfuata mgongoni. Walizidi kusogea mbele na wale simba wakawa wanazidi kurudi nyuma huku wakionesha meno yao makali. Walisogea mpaka walipoifikia ile bunduki iliyokuwa chini kwenye majani. Walipoifikia, Mzee Khalfani alimpa ishara Khaleed aiokote upesi wakati yeye akizidi kuushikilia moto usizimike.
Khaleed alifanya kama alivyoelekezwa. Kwa haraka aliiokota na kuishika mikononi mwake huku akitetemeka. Mvua nayo ilianza kumwagika kwa kasi na kusababisha ule moto uzimike. Wale Simba kuona moto umezimika, wakawa wanarudi kwa kasi, safari hii wakiwa wengi kuliko awali. Kwa kasi ya ajabu, Mzee Khalfan aliichukua ile bunduki kutoka mikononi mwa Khaleed na kufyatua risasi mfululizo hewani.
Hiyo ndio ikawa ponapona yao kwani milio ya risasi iliwachanganya wale simba na wakatawanyika kwa kasi na kupotelea vichakani.
Mzee Khalfan alizidi kufyatua risasi nyingi kuwafukuzia mbali wale Simba. Sekunde chache baadae eneo lote likawa kimya. Baada ya kuhakikisha kuko salama, Mzee Khalfan alimgeukia mwanae Khaleed aliyekuwa nyuma yake, wakakumbatiana kwa nguvu.
“You are a real soldier my son, grow brave-hearted! Im proud of you” (hakika mwanangu wewe ni mwanajeshi kamili, endelea kukua ukiwa na moyo shujaa kama huu! Najivunia kuwa nawe)
Mzee khalfan aliongea kwa furaha kubwa huku akizidi kumkumbatia mwanae Khaleed kwa nguvu. Japokuwa alikuwa bado na umri mdogo alikuwa shujaa mno, hali ambayo ilimshangaza hata baba yake. Mvua ilikuwa ikizidi kumwagika na kuzidi kulifanya pori la Gamutu lizidi kutisha. Baada ya kupongezana, Kwa haraka khaleed na baba yake wakaanza kupanga namna ya kuwaokoa wenzao.
Bi Miriam na wanawe walikuwa wamepoteza fahamu tangu walipotekwa na kupigwa vibaya na majambazi nyumbani kwao usiku uliopita. Baridi kali iliyokuwa ikiambatana na mvua kubwa iliyokuwa inanyesha alfajiri ile iliwafanya wazinduke na kurejewa na fahamu zao. Fahamu zilipomrudia Bi Miriam alianza kupiga mayowe kama aliyerukwa na akili huku akimuita mumewe.
Hakujua hapo walipo ni wapi na wamefikaje. Mzee Khalfan akawa na kazi ya ziada kumtuliza mkewe huku Khaleed naye akiwanyamazisha wadogo zake waliokuwa wakilia kwa maumivu makali wakati wakiwafungua zile kamba walizokuwa wamefungwa.
Mvua kubwa ikawa inaendelea kunyesha ikisindikizwa na ngurumo kali za radi. Ilibidi watafute sehemu ya kujificha ili wasizidi kuloana. Wakangia ndani ya pango lililokuwa chini ya mti mkubwa. Mvua ilikuwa haiingii kabisa mle ndani ya pango. Wakakumbatiana huku kila mmoja akitetemeka kwa baridi kali waliyokuwa wakiihisi. Mzee Khalfan, bunduki yake ikiwa “Standby” mkononi, alikuwa amekaa tayari tayari kuilinda familia yake endapo Simba wangerudi tena.
Wakiwa ndani ya lile Pango wakawa wakisali kumshukuru Mungu wao kwa yote. Japokuwa tayari walikuwa wameshawapoteza wenzao wawili, walimshukuru Mungu kwa kuwanusuru mpaka muda ule kwani hakuna aliyetegemea wangekuwa hai mpaka muda ule. Mvua kubwa iliendelea kunyesha mpaka kulipopambazuka kabisa. Hali ya hewa ikaanza kubadilika na kuwa shwari.
Baada ya muda, jua lilianza kuchomoza na miale yake kupenya vivuli vizito vya miti mikubwa iliyofungamana ndani ya msitu wa Gamutu. Ile mvua kubwa iliyonyesha na kuutetemesha msitu wote tangu alfajiri ikawa imekatika kabisa. Hali ya hewa ikaanza kuwa ya kupendeza huku zikisikika kelele za ndege wa kila aina waliokuwa wakiimba na kurukaruka juu ya matawi ya miti mikubwa ya pori la Gamutu wakifurahia mpambazuko ya siku mpya.
Licha ya kuwa Mzee khalfan na mkewe Bi Miriam walikuwa tayari wamewapoteza watoto wao wawili wa kike walioliwa na Simba porini Gamutu, walizidi kumshukuru sana Mungu wao kwani hakuna aliyetegemea kama wangeiona siku hiyo mpya.
Kwao ilikuwa ni kama miujiza kubaki hai mpaka asubuhi hiyo. Walikuwa wameshakata tamaa kwa yaliyowatokea usiku, lakini Mungu alitenda miujiza kwao, kitu ambacho hakuna aliyekitegemea. Pamoja na kunusurika kuliwa na simba usiku uliopita, mzee Khalfan na familia yake iliyosalia bado hawakupata jibu namna ambavyo wangeweza kutoka salama ndani ya msitu wa Gamutu.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment