Search This Blog

Sunday, July 10, 2022

MOYO WANGU UNAVUJA DAMU - 1

 





    IMEANDIKWA NA : Aziz Hashim - Hash power





    *********************************************************************************







    Simulizi : Moyo Wangu Unavuja Damu

    Sehemu Ya Kwanza (1)



    Ilikuwa ni jumatatu ya kwanza ya mwezi Septemba, asubuhi tulivu yenye anga lililopendezeshwa na rangi ya bluu, jua la asubuhi likiwa ndio linachomoza na kuzidi kuipendezesha siku ya kwanza ya juma.

    Umati mkubwa wa watu waliokuwa wamefurika katika viwanja vya mahakama kuu ulitosha kumfanya yeyote asiyejua kilichokuwa kinaendelea mahali hapo kupigwa na butwaa. Ilikuwa ni idadi kubwa kabisa ya watu kuwahi kutokea tangu mahakama hiyo ilipoanza kufanya kazi rasmi miaka kadhaa iliyopita…



    Kwa kadri muda ulivyokuwa unaenda, ndivyo watu walivyokuwa wanazidi kuongezeka katika eneo la kuizunguka mahakama. Wote walikuwa wamekuja kwa lengo la kutaka kusikiliza mwendelezo wa kesi nzito ya mauaji iliyokuwa ikimkabili kijana mdogo kabisa, ambaye kwa haraka haraka ungeweza kumkadiria kuwa na umri usiozidi miaka ishirini.







    Hiyo haikuwa kesi ya kwanza ya mauaji kutolewa hukumu mahakamani hapo, lakini kesi hii ilionekana kuwa tofauti na kesi nyingine, kwani ilionekana kuzigusa hisia za watu wengi sana.



    Iliwawia vigumu askari wa kutuliza ghasia na wale wa jeshi la polisi kuweza kuwatuliza watu wote waliofurika eneo hilo kwani walikuwa ni wengi sana na walikuwa bado wanazidi kuongezeka kwa kadri muda ulivyokuwa unaenda.



    Ving’ora vya magari ya polisi na kelele za mbwa wa polisi vilizidi kufanya hali ya mahali hapo izidi kuzizima, huku kila mtu akiwa na hamu ya kutaka kujua nini kingeendelea. Vurugu zilizidi kupamba moto na utulivu na amani vikatoweka kabisa katika viwanja vya mahakama wakati gari lililombeba mtuhumiwa likiwa linaingia mahakamani hapo.

    Watu walikuwa wakipiga kelele na kukanyagana kila mmoja akitaka japo amwone mtuhumiwa wa kesi hiyo nzito. Kila mtu alikuwa analikimbilia gari lililombeba mtuhumiwa na muda mfupi baadae gari lote likawa limezingirwa kila upande, kiasi cha kushindwa kuelekea kwenye lango kuu la mahakama .



    Akina mama waliokuwepo eneo hilo walisikika wakiangua vilio kama wanaomboleza msiba mzito, huku vijana na watu wazima wakishindana nguvu na polisi wa kutuliza ghasia waliokuwa wakiwazuia wasimuone mtuhumiwa.



    Kilichoendelea sasa ikawa ni vurugu mtindo mmoja, Polisi virungu na mabomu… raia mawe na fimbo. Polisi wa kutuliza ghasia walioneka kuanza kuzidiwa nguvu na raia hali iliyowalazimu kuanza kufyatua hovyo risasi hewani na kurusha mabomu ya machozi ili kuutawanya umati mkubwa wa watu waliokuwa wamelizingira gari alimokuwemo mtuhumiwa.



    Baada ya nguvu kubwa kutumika kuwadhibiti raia, hatimaye ikalazimu gari lililombeba mtuhumiwa lirudi kwenye gereza kuu mpaka hali itakapokuwa shwari. Baada ya patashika lililodumu kwa takribani masaa mawili, hatimaye hali ilitulia.



    Polisi wa kutuliza ghasia walikuwa wameongezwa maradufu, wengi wakiwa ni wale wa kikosi maalum cha mbwa wakiwa wametapakaa karibu kila sehemu sehemu kuizunguka mahakama.



    Baada ya hali kuwa shwari hakimu aliamuru mtuhumiwa akaletwe na kupandishwa kizimbani tayari kwa kusomewa mashtaka mazito ya mauaji yaliyokuwa yakimkabili.



    Safari hii ilibidi gari lililombeba mtuhumiwa liingie kwa kupitia mlango wa nyuma “Emergency exit” ili kuzuia hali kama ile iliyojitokeza awali.



    Hatimaye mtuhumiwa aliingizwa mahakamani chini ya ulinzi mkali na akapandishwa kizimbani. Utaratibu wa kawaida wa kuendesha mashtaka ukaanza huku Jaji mkuu Profesa kadir Mudhihir Simba akiwa ndiye anayetakiwa kuisikiliza kesi ile na kuitolea hukumu ya mwisho.



    Minong’ono ya chinichini ilikuwa ikisikika kutoka pande zote za mahakama huku watu wakiwa hawaamini kuwa ni kweli yule aliyekuwa kizimbani upande wa kushoto wa hakimu ndio mtuhumiwa aliyeifanya nchi nzima kutetemeka kwa hofu kutokana na mauaji makubwa na ya kutisha aliyokuwa ameyafanya.



    Huyo ndio alikuwa mtuhumiwa aliyezigusa hisia za watu wengi kuliko kawaida kiasi cha kufanya kila mtu awe na hamu ya kutaka kumuona na kujua nini hatma yake. Kijana mdogo kabisa, mrefu wa wastani mwenye rangi ya maji ya kunde, ambaye ungemkadiria kuwa na umri usiozidi miaka ishirini.



    Usoni hakuonyesha wasiwas hata kidogo na alikuwa akitabasamu japokuwa alikuwa akikabiliwa na kesi nzito sana ya mauaji ya kutisha ya idadi kubwa ya watu, akiwa amewaua wote kwa mkono wake. Alikuwa ametulia kimya akisubiri kuona nini hatma yake.



    Minong’ono ilikuwa ikizidi kuongezeka, na zaidi akinamama ambao hawakuweza kujizuia kulia kwa uchungu kwani hakika hukumu ambayo ilikuwa ikisubiriwa huenda ndio ingekuwa kali zaidi kuliko zote zilizowahi kutolewa.



    Kilichovuta hisia za watu wengi ni sababu ambazo zilifanya kijana huyu mdogo kufanya mauaji makubwa na ya kutisha kiasi kile. Ni sababu ambazo ilihitajika mtu makini sana kuweza kutoa hukumu. Na hii ndiyo iliyosababisha kesi hii kuahirishwa mara saba mfululizo licha ya kwamba upelelezi ulishakamilika siku nyingi na vithibitisho vyote vilikuwa vimefikishwa mahakamani.



    Mahakimu wote walikuwa wakijitoa katika hatua za mwisho za kesi huyo huku kila mmoja akitoa sababu zake binafsi. Mwishowe ilibidi jaji mkuu aingilie kati na kuamua kuisikiliza mwenyewe kesi ile baada ya mahakimu karibu wote kuonekana wanaikwepa.



    Waliokuwa wakifahamu kisa na mkasa kilichopelekea kijana yule mdogo kufanya vile, walikuwa wakimsikitikia kwani walijua hakika asingeweza kukwepa adhabu nzito iliyokuwa inamngoja. Hakuna aliyeonekana kuwasikitikia wahanga wa mauaji yale kwani wote walistahili kufa kwa waliyoyafanya.

    “Mwachieni huru mwanetu!”



    Alisikika mama mmoja akiongea kwa jazba iliyofuatiwa na kilio cha kwikwi. Kwa mujibu wa taratibu na sheria za mahakamani hapo, hakuna yeyote aliyeruhusiwa kuongea chochote wakati kesi ikiendelea. Lakini kwa jinsi kesi hiyo ilivyozigusa hisia za watu, mama yule alijikuta ameropoka na kuungwa mkono na umati wote uliokuwemo mle ndani. Ilibidi jaji mkuu atumie busara zake kurudisha utulivu mahakamani kwani vurugu ilikuwa almanusra ianze tena bada ya wanausalama kutaka kumtia nguvuni mama yule kwa kuvunja taratibu za mahakama.



    Baada ya muda mfupi hali ikarudi kuwa shwari. Zilisikika kelele za karatasi tu, za jalada la kesi zilizokuwa zinapekuliwa na jaji mkuu, Profesa Kadir Mudhihir Simba. Watu walikuwa wakiwatazama mtuhumiwa na hakimu kwa zamu zamu. Ungeweza kudhani ni mchezo wa kuigiza kwenye luninga au tamthilia nzuri , lakini haikuwa hivyo.



    Jaji mkuu aliuvunja ukimya uliokuwepo mahakamani hapo kwa kuanza kumsomea mashtaka mtuhumiwa, na kabla hajaendelea kutoa hukumu akamuuliza mshtakiwa…



    “Je! Ndugu mshtakiwa una lolote la kujitetea kabla hukumu haijatolewa?”

    Swali lile lilizua upya minong’ono ambayo iliongeza shauku ya umati ule kutaka kusikia mshtakiwa atajibu nini.



    “Mtukufu hakimu, nashukuru kwa kunipa nafasi hii. Kwangu mimi huu sio utetezi bali ni ushuhuda wa yale yaliyonifanya niwaue mashetani hawa.Ninachoweza kusema ni kwamba, nakiri kufanya mauaji makubwa na ya kutisha kwa mikono yangu. Mikono yangu imetapakaa damu… damu ya kisasi. Sijuti kwa yale niliyoyafanya, zaidi najiona kama shujaa kwa kuweza kulipa kulipa kisasi cha damu kufidia maisha ya ndugu zangu waliouawa mikononi mwa mashetani hawa. Nahitaji kwenda kuungana na familia yangu kuzimu tukapumzike. Nihukumu kunyongwaaa! Nataka kufa! Mungu ibariki kazi ya mikono yangu! Amen.”



    Mahakama yote ililipuka kwa vilio na makelele ya watu waliokuwa wakimsikitikia kijana yule na kuanza kushinikiza aachiwe huru. Watu wote walikumbwa na taharuki na kugubikwa na wingu zito la sintofahamu. Kwa ushuhuda ule mfupi alioutoa, hata wale ambao walikuwa wakimuona kama muuaji na gaidi hatari walianza kumuonea huruma.



    Kila mmoja alionekana kusononeka sana moyoni, hata polisi waliokuwa wamejaa mahakamani mle kila mmoja alionekana kuingiwa na simanzi huku wakijitahidi kuonyesha ukakamavu wao kwa kuyazuia machozi. Hakuna aliyeonekana kuwaonea huruma watu waliokuwa wameuawa mikononi mwa kijana yule, kila mmoja aliunga mkono alichokifanya hata kama ilikuwa ni kinyume na sheria za nchi lakini kwa waliyoyafanya wote walistahili kufa.



    Hali ilitisha. Kelele zile na maombolezo ya watu waliokuwa wakisikiliza kesi ile vilimtisha jaji mkuu ambaye sasa utulivu ulimuisha. Ni kweli kabisa kuwa kijana yule alikuwa na hatia kubwa mbele ya sheria na vithibitisho vyote vya kumtia hatiani vilikuwepo, lakini sababu zilizomfanya kuua ndizo zilizoifanya kesi ile kuonekana kuwa ngumu sana.



    Jaji mkuu alikuwa akihaha kutafuta msaada kutoka kwa wazee wa baraza kuu la mahakama ili kujua nini kifanyike. Tai aliyokuwa ameivaa ilionekana kuwa mzigo kwake, akaivua na kuiweka juu ya meza huku kijasho chembamba kikianza kumtoka. Koti maridadi la suti alilokuwa amelivaa lilionekana kuwa mzigo pia, akalivua na kuliweka nyuma ya kiti alichokuwa amekalia.



    Baada ya vuta nikuvute iliyoendelea kwa muda mrefu, hatimaye Jaji mkuu aliamua kusoma hukumu. Watu wote wakawa kimya kutaka kusikia hukumu ya mwisho ambayo jaji mkuu Profesa Kadir Mudhihir Simba angeitoa.

    Profesa Kadir Mudhihir Simba ni hakimu mwenye uzoefu wa siku nyingi katika medani ya siasa. Alikuwa na ujuzi na utaalamu wa kutosha katika kutoa hukumu za kesi ngumu, kesi zilizoonekana kushindikana au zenye utata. Watu wote walimwamini kwani mara zote hukumu alizokuwa anazitoa zilikuwa ni zenye kuzingatia sheria na haki. Uwezo wake mkubwa wa kuchambua mambo kwa kina na busara alizokuwa nazo, vilimfanya ateuliwe kuwa jaji mkuu miaka kumi na mbili iliyopita.



    Pamoja na sifa hizo zote alizokuwa nazo, kesi hii ilionekana kumchanganya sana kichwa chake na kumkosesha sana raha kiasi cha kumfanya asite kutoa hukumu. Upelelezi ulishakamilika muda mrefu kwani mshtakiwa alijisalimisha mwenyewe mikononi mwa polisi akiwa na vithibitisho vyote vya namna alivyofanya mauaji hayo makubwa na ya kutisha.



    Hakukuwa na sababu yoyote ambayo ingezuia hukumu kutolewa siku hiyo, Lakini bado jaji mkuu alionekana kupoteza mwelekeo. Alitamani aiahirishe kesi ile mpaka siku nyingine, lakini alihofia kupoteza heshima ambayo alijijengea kwa raia. Sasa aligundua ni kwa nini mahakimu wote saba walioteuliwa kuisikiliza kesi ile walikuwa wakijitoa katika hatua za mwisho.



    Aligeuza shingo kumtazama mshtakiwa, kisha wazee wa mahakama na mwisho umati uliokuwa umeijaza mahakama ile. Kwa mara ya kwanza tangu aanze kazi miaka mingi iliyopita, aliuhisi ugumu uliokuwa mbele yake. Japokuwa alikuwa amevaa miwani, macho yake yalionyesha dhahiri jinsi alivyokuwa akibabaika. Usingeweza kuamini kuwa huyu ndio yule jaji mkuu, Profesa Kadir Mudhihir Simba wa siku zote.



    Ni kweli kabisa kwamba kuua, kwa kukusudia au bila kukusudia ni kosa kubwa mbele ya sheria, lakini sababu zilizomfanya kijana huyu mdogo kufanya mauaji makubwa kiasi kile ndilo swala lililoleta ugumu.



    Jasho lilianza kumtoka kiasi cha kuamuru madirisha yote yafunguliwe na viyoyozi vyote vya mle mahakamani viwashwe. Baada ya kubabaika kwa muda mrefu, hatimaye alipiga moyo konde na kuanza kutoa hukumu.

    “Kwa mujibu wa sheria na katiba ya nchi ya mwaka 1962, ibara ya kwanza ya makosa dhidi ya ubinadamu, kifungu kidogo cha kwanza,umepatikana na hatia ya kuua idadi kubwa ya watu kwa kukusudia. Baada ya mahakama kuridhishwa na ushahidi uliowasilishwa dhidi yako, Una..unahukum… unahu……ku……mi……w……”



    Hakuna aliyeamini kilichotokea! Jaji mkuu alianza kubabaika na kushikwa na kigugumizi kikali huku jasho jingi likimtoka kama maji. Mwili wote ulikuwa umeloanishwa kwa jasho na sasa akawa anatetemeka mwili mzima. Alijitahidi kujikaza ili aendelee kusoma hukumu lakini alishindwa. Watu walikuwa wamepigwa na butwaa wakiwa wanashangaa kilichomsibu jaji yule. Alizidi kutetemeka mwili mzima na kuazna kuzitupa hovyo karatasi za jalada la hukumu na mara akadondoka kutoka kwenye kiti alichokuwa amekaa mpaka chini, kisha akawa anaporomoka kwenye ngazi. Hakika hii ilikuwa kali ya kufunga mwaka.



    Ungeweza kudhani kama yanayotokea mle mahakamani ni viini macho au miujiza, lakini haikuwa hivyo. Akiwa pale chini alianza kutupa mikono na miguu huku povu lililochanganyikana na damu likimtoka puani na mdomoni. Ungeweza kuhisi anataka kukata roho. Umati wote wa watu waliokuwa mle mahakani , ulipigwa na bumbuwazi kwa mshtuko mkubwa walioupata. Ilibidi makarani wa mahakama wafanye kazi ya ziada kwa kusaidiana na watu wa huduma ya kwanza.



    Waliwahi kumuinua pale chini na kumkimbiza nje akiwa juu ya machela, na muda mfupi baadae gari la wagonjwa likawa linakimbia kwa mwendo wa kasi kumuwahisha Hospitali. Mtuhumiwa bado alikuwa ametulia kizimbani na yeye akiwa amepigwa na bumbuwazi kwa yale yaliyokuwa yametokea.



    Watu wakaanza kukanyagana kila mmoja akitaka ashuhudie kinachoendelea nje ya mahakama. Askari waliokuwa wamejaa mle mahakamani walifanya kazi ya ziada kuhakikisha mtuhumiwa anarudishwa gerezani. Eneo lote likazingirwa na taharuki huku hali ikiwa tete na ya kuogopesha. Polisi walifanya kazi yao kikakamavu na kuhakikisha hakuna madhara makubwa yanayotokea pale mahakamani.



    Muda mfupi baadae habari kutoka Hospitali kuu ya Blaziniar zilieleza kuwa hali ya afya ya jaji Mkuu Profesa Kadir Simba ilikuwa ikizidi kuwa mbaya kadri muda ulivyokuwa ukienda. Kwa mujibu wa Daktari mkuu Shyroze Mahiza aliyoitoa kwa vyombo vya habari, jaji mkuu alikuwa amepatwa na mshtuko wa moyo na kusababisha mishipa ya damu iliyoko kichwani kupasuka na kuvujisha damu kwenye ubongo.



    Kitaalamu hali hii iliitwa “Venule Rapture due to Hypertension BP”, na husababisha mtu kupoteza fahamu kwa muda mrefu. Hayo ndiyo yaliyokuwa yamemtokea jaji Simba kwani aliendelea kuwa katika hali ya kupoteza fahamu kwa muda mrefu sana.



    Kila aliyemfahamu alimuonea huruma kwa yaliyompata na kila mtu akawa anajiuliza nini kimesababisha hali kama ile itokee. Kila mtu aliongea lake kwani jambo kama hilo halikuwahi kutokea hata mara moja katika historia ya nchi. Wengine waliliona kama muujiza huku wengine wakilihusisha na imani kali za kishirikina. Hali hiyo ilizua hamu na shauku ya watu kutaka kufahamu yule kijana mdogo ni nani na alikuwa ameendesha mauaji yake kwa sababu gani na katika mazingira gani. Uchunguzi wa kina ukaanza kufanywa ili kuupata uhalisia wa kesi ile.



    MANY YEARS AGO-MIAKA MINGI ILIYOPITA

    Khalfan Mwalukasa alikuwa ni mzaliwa wa mkoa wa Nyanda, uliopo kusini mwa nchi ya Blazinia. Alikuwa ni mtoto wa kipekee katika familia yao, na akiwa bado kijana aliamua kuondoka nyumbani kwa wazazi wake na kwenda kujaribu kutafuta maisha katika nchi jirani ya Tanzania. Hata hivyo alipofika Tanzania aligundua kuwa maisha yalikuwa magumu zaidi kuliko kwao Blazinia.



    Alichokifanya aliamua kwenda kwenye visiwa vya jirani vilivyokuwa vikipakana na nchi yake, visiwa vya Banaland vilivyokuwa katika bahari ya Hindi. Visiwa hivi vilikuwa ni sehemu ya nchi yake hivyo hakukuwa na haja ya kuwa na Passport au viza ya kusafiria. Ilimgharimu kiasi kidogo tu cha pesa kupanda meli na siku chache baadae akawa tayari ndani ya visiwa vya Banaland.



    Kwa kuwa kilichomtoa kwao na kukimbilia ugenini ilikuwa ni kutafuta ahueni ya maisha , hakutaka kuchagua kazi kwani hata hivyo hakuwa amejaaliwa kusoma kutokana na wazazi wake kuwa na hali duni ya kimaisha. Alijiwekea dhamira ya kufanya kazi yoyote ambayo ingepatikana ilimradi tu imuingizie kipato. Bahati nzuri alipata kazi ya kuuza genge la mbogamboga na matunda.



    Moyo wa kujituma, heshima kwa wakubwa na wadogo na busara alizokuwa nazo vilimfanya aweze kuishi kwa amani japokuwa alikuwa mbali na wazazi wake. Muda mfupi baadae alifanikiwa kufungua biashara yake mwenyewe na akaanza rasmi kujitegemea. Alifanikiwa kupanga chumba kimoja mitaa ya uswahili na taratibu akaanza kutengamaa kimaisha.



    Mara zote alikuwa akijikumbusha kuwa kilichompeleka pale ilikuwa ni kutafuta maisha, aliahidi kufanya kila alichoweza ili afanikiwe maishani ikiwa ni pamoja na kujiepusha na mambo ambayo alihisi yangezuia ndoto zake.



    Baada ya takribani mwaka mmoja kupita, alikuwa ameshajijengea jina miongoni mwa wafanyabiashara wa mbogamboga na matunda. Aliipenda kazi yake, na faida ndogo aliyokuwa akiipata alikuwa akitumia vizuri na kujiwekea akiba. Wateja wake wengi walikuwa ni wanawake lakini kwa kuwa alikuwa akifahamu alichokuwa anakifanya, hakujihusisha nao zaidi ya uteja wa kawaida.



    Miongoni mwa wateja wake, alikuwepo binti mmoja aliyekuwa na asili kama ya mchanganyiko wa damu mbili tofauti. Alionekana kuwa na mchanganyiko wa kibantu na watu wa visiwa vya ushelisheli. Mchanganyiko huu ulimfanya awe na mvuto wa kimahaba kuliko wasichana wengine wa rika lake.



    Miriam, tofauti na wateja wengine, alikuwa akipenda sana kupiga stori na Khalfan Mwalukasa. Hata baada ya kuhudumiwa kila alichokuwa akihitaji, bado alikuwa akifurahia kuendelea kuongea na Khalfani bila kujali kama alikuwa akichelewa nyumbani kwao.



    Japokuwa alishindwa tu kueleza wazi hisia zake, Miriam alitokea kumpenda Khalfani Mwalukasa lakini alishindwa kumwambia bayana kwa hofu ya kueleweka vibaya. Akawa anaendelea kuumia mtimani siku hadi siku huku akijitahidi kumuonyeshea kwa vitendo kuwa alimhitaji awe baba wa watoto wake. Khalfani Mwalukasa alishaelewa kilichokuwa mawazoni mwa mteja wake Miriam, lakini hakutaka kuwa na papara hasa ukizingatia kilichompeleka kule ilikuwa ni kutafuta maisha na sio mapenzi.



    Pamoja na kujifanya mgumu, Khalfani naye alijikuta taratibu akianza kuvutiwa na urembo wa binti Miriam aliyekuwa na haiba ya kike haswaa…mrefu kama twiga, uso wake wa duara ukiwa umepambwa na macho madogo ambayo muda wote yalikuwa kama yana usingizi, huku sura yake ikiwa imejawa na tabasamu tamu muda wote. Taratibu alijikuta uzalendo ukimshinda na mara wakajikuta tayari wamezama kwenye dimbwi la mahaba.



    “Khalfani hivi kweli utanioa? Au ndio unataka kunitumia mwisho uniache niteseke?”

    Miriam alikuwa akimuuliza huku sauti yake ikwa imejawa na huba.

    “Ningependa uwe wangu wa maisha Miriam, lakini hali yangu nadhani we mwenyewe unaiona…itakuwa ni maajabu kwa muuza mboga kumuoa mtoto wa milionea kama wewe, haitawezekana”



    Khalfani alikuwa akijitetea mbele ya Miriam, lakini baada ya mazungumzo marefu, Miriam alimtoa wasiwasi kuwa yeye hakuhitaji chochote kutoka kwake, zaidi ya kumhitaji awe baba watoto wake bila kuzingatia hali yake ya kimaisha wala kipato.



    Moto wa mapenzi ukaanza kukolea kwenye mioyo ya wawili hawa na baada ya kuwa kwenye uhusiano kwa muda mrefu, hatimaye Miriam alimpeleka “mumewe mtarajiwa” kumtanbulisha kwa wazazi wake. Miriam alikuwa akiishi na wazazi wake wote wawili, Mzee Nurdin Shamsi na mkewe. Walibarikiwa kuwa na maisha mazuri ya kitajiri, utajiri ambao ulitokana na biashara aliyokuwa anaifanya mzee Nurdin Shamsi ya madini ya Ruby. Alikuwa akinunua Ruby kutoka kwa wachimbaji wadogo wadogo na kuisafirisha mpaka nchi za uarabuni (U.A.E). Biashara hiyo ilimuingizia pesa nyingi sana zlizomuwezesha yeye na familia yake kuwa na maisha ya juu.



    Alifanikiwa kujenga nyumba nzuri ya kifahari pembezoni mwa fukwe za bahari ya Hindi alikokuwa akiishi na familia yake. Alinunua pia eneo kubwa kuzunguka nyumba yake, alilolipendezesha kwa bustani nzuri za maua, viunga vya minazi na karafuu. Eneo zima lilikuwa likipendeza mithili ya Edeni ndogo.



    Baada ya kutambulishwa kwa wazazi wa Miriam, Khalfani Mwalukasa aliendelea kuonyesha nidhamu na heshima ya hali ya juu kwa kila mtu, hali ambayo iliwavutia sana wazazi wa Miriam na kuwafanya wamkubalie kwa moyo mkunjufu kumposa binti yao.



    Baada ya kutoa posa, taratibu za ndoa zilianza kuandaliwa na siku chache baadae Khalfan Mwalukasa akawa mume halali wa Miriam Shamsi. Wakayaanza maisha mapya ya ndoa. Kwa kuwa umri wa mzee Shamsi na mkewe ulikuwa umekwenda, na Miriam ndio alikuwa mtoto wao pekee, kitendo cha yeye kuolewa na kwenda kuishi kwa mumewe kiliwafanya wawe wapweke sana. Ikabidi mzee Shamsi amshawishi Khalfan Mwalukasa na mkewe wahamie katika jumba lao la kifahari ili waendelee kuishi wote pamoja. Khalfani alijadiliana na mkewe na wakakubaliana kuhamia nyumbani kwa kina Miriam (Ukweni).



    Khalfani akayaanza maisha mapya ndani ya jumba la kifahari, maisha ambayo hakuwahi kuyaota. Alikuwa amebadili sana mazingira, kutoka kuwa muuza mboga na matunda akiishi uswahilini, mpaka kuwa mume wa binti tajiri akiishi ndani ya paradiso ndogo. Alimshukuru Mungu wake na kuahidi kuwa atampenda mkewe kwa moyo wake wote.



    “Daima nitakuenzi mke wangu, na kamwe sitakufanya utoe machozi ya uchungu, bali utatoa machozi ya furaha”

    Khalfan alikuwa akimpa maneno matamu ya huba mkewe jioni moja wakiwa wameketi kwenye moja ya bustani nzuri zilizokuwa ndani ya kasri la mzee Shamsi. Ndoa yao changa ikatawaliwa na upendo na mahaba ya dhati.



    Kwa jinsi wazazi wa Miriam, Mzee Shamsi na mkewe walivyokuwa wakimpenda mkwe wao, ilibidi wamshawishi Khalfani pamoja na mkewe Miriam wahamie nyumbani kwa Mzee Shamsi. Mzee Shamsi na mkewe hawakuwa na mtoto mwingine zaidi ya binti yao Miriam, hivyo kuondoka kwake na kumfuata mumewe, kuliwafanya wabaki wapweke sana kwenye himaya yao.



    Khalfan na mkewe hawakuwa na kipingamizi chochote, wakakubali kuhamia nyumbani kwa mzee Shamsi, (Ukweni). Maisha yao yakazidi kuwa mazuri siku baada ya siku, na sasa Khalfan akawa ameachana na biashara yake ya mboga mboga na matunda.



    Badala yake akawa akimsaidia mzee Shamsi kwenye shughuli zake za Biashara ya madini ya Ruby. Muda mwingi akawa akitembezwa kwenye gari ndogo aina ya “Mercedes Lexus 5 New Model” ya kisasa, akimwonyesha vitega uchumi vyake na kumwelelekeza jinsi ya kuhudumia mali zote walizokuwa nazo.



    Kwa kifupi mzee Shamsi alimuamini sana Khalfan, kiasi cha kumchukulia kama mwanae wa kumzaa. Hakumficha kitu chochote, alikuwa akimpa mpaka siri zake za ndani. Aliamini kuwa kwa kuwa hakubahatika kupata mtoto wa kiume, basi khalfan ndio atakuwa mrithi wa mali zake zote akishirikiana na mkewe Miriam.



    Alichokuwa akimsisitiza siku zote ni kumpenda kwa dhati mkewe, mtoto wao wa pekee Miriam. Alikuwa akimuonya pia kuwa makini sana na marafiki wa kibiashara ambao atakuwa akishirikiana nao hususani kwenye bashara ya madini kwani akili za mwanadamu hubadilika sana akiona vitu vya thamani. Nasaha alizokuwa anapewa kila siku zilimjenga upya kifikra na kumpa ujasiri kuliko ilivyokuwa mwanzo. Alijiona anaweza kufanya mambo makubwa hata kama hakuwa na elimu kubwa kichwani



    Ilikuwa ni majira ya saa nne asubuhi, Miriam akiwa anamuandalia mumewe Khalfan kifungua kinywa, huku wakitaniana utani wa mume na mke! Kila mmoja alikuwa na furaha kuwa na mwenzake. Wakawa wakitaniana na kucheza kama watoto huku Miriam akiendelea kuandaa kifumgua kinywa.



    Wakati hayo yakiendelea taarifa ya habari iliyokuwa inasomwa kutoka kituo maarufu cha redio, “The Bulletin FM” iliwashtua wote kiasi cha kufanya kila mtu aache alichokuwa anakifanya na kukimbilia jirani na redio ili asikie vizuri taarifa ile.



    Ilikuwa ni habari mbaya ya ajali ya kutisha ya ndege iliyotokea muda mfupi uliopita. Ajali hiyo ilihusisha ndege ya kampuni ya “TRY EMIRATES” aina ya Jet B710 Sossoliso, iliyokuwa inatoka uwanja wa kimataifa wa Blazinair International Airport (BLIA) kuelekea Muscat Oman. Habari ilizidi kuelezea kuwa ajali hiyo ilisababishwa na hitilafu katika moja ya injini zake, hali iliyosababisha ndege hiyo kulipuka muda mfupi baada ya kuruka, kisha ikaangukia baharini.



    Kilichosikitisha ni kwamba abiria wote 67 waliokuwemo kwenye ndege walikuwa wakihofiwa kupoteza maisha katika ajali ile. Habari ilihitimishwa kwa mahojiano na watu walioshuhudia ajali ile ambapo kila aliyehojiwa alikiri kuwa hakuwahi kusikia wala kushuhudia ajali mbaya kama ile.



    Khalfan na mkewe walibaki wakikodoleana macho, wasijue nini cha kufanya. Kilichowashtua ni kwamba ni asubuhi ya siku hiyo masaa machache tu yaliyopita walitoka kuwasindikiza mzee Shamsi na mkewe uwanja wa ndege, wakielekea oman kupeleka biashara yao ya madini ya Ruby.



    Haikuwa kawaida kwa mzee Shamsi kusafiri na mkewe, kwani mara zote yeye aliposafiri mkewe alibaki kuwa msimamizi wa mali zao, lakini baada ya binti yao kuolewa na Khalfan Mwalukasa, shughuli zote za usimamizi wa mali zilibaki kuwa chini ya uangalizi wa Khalfan kwani walimchukulia kama mtoto wao, na kwa pamoja walikubaliana kuwa yeye ndiye atakayekuwa mrithi wa mali zao, pindi mauti yatakapowafika.



    Ni masaa mawili tu yaliyopita majira ya kama saa mbili za asubuhi Khalfan na mkewe waliwasindikiza wazazi wao uwanja wa ndege na wakasubiri mpaka walipopanda ndege ya kampuni ya usafiri wa anga ya TRY EMIRATES tayari kwa safari ya Oman. Ni baada ya kuhakikisha kuwa wamepanda ndege, ndipo Khalfan na mkewe waliporudi nyumbani kuendelea na shughuli zao.



    Wakiwa wanajiandaa kupata kifungua kinywa ndipo taarifa ya kusikitisha na kutia majonzi iliposikika. Hiyo ilimaanisha kuwa mzee Shamsi na mkewe walikuwa wamepoteza maisha katika ajali ile. Msiba mkubwa kiasi gani. Habari ya ajali ile iliwashtua watu wengi, ambao kwa namna moja au nyingine waliwapoteza ndugu, jamaa na marafiki zao waliokuwemo kwenye ndege ile.



    Kwa Khalfan Mwalukasa, licha ya ukweli kwamba aliguswa na vifo vya wakwe zake, hii ilikuwa ni kama bahati ya mtende kuota jangwani, waswahili wanasema kufa kufaana. Ni Khalfan huyu huyu aliyekimbia kwao kutokana na ugumu wa maisha, akawa akifanya biashara ya mbogamboga na matunda, ndiye sasa alitakiwa kuwa mmiliki wa hazina ya utajiri ulioachwa na mzee Shamsi. Hakuwahi kuota wala kutegemea kuwa ipo siku atakuja kumiliki hazina kubwa ya utajiri kama ile. Kweli Mungu alikuwa ametenda miujiza katika maisha yake.



    ********



    Siku ziwaka zinakwenda, sekunde, dakika, masaa! Mara usiku, mara mchana… mawio na machweo. Kumbukumbu ya kuwapoteza wazazi mzee Shamsi na mkewe taratibu ikaanza kupotea vichwani kwa Khalfan na mkewe Miriam. Khalfan akawa anajitahidi kwa kadri ya uwezo wake wote kumliwaza mkewe na kumfaya asahau yote yaliyotokea. Yeye ndiyo akawa baba na kichwa cha familia.



    Mwanzoni ilimuwia vigumu kuweza kusimamia mali zote zilizoachwa na mzee Shamsi lakini kila alipokuwa akikumbuka mawaidha aliyokuwa anapewa na mzee Shamsi, akawa anajipa moyo kuwa hakuna lisilowezekana. Taratibu akawa anapata uzoefu kila siku mpya ilipokuwa ikianza. Hali hiyo ilionekana kumfariji sana mkewe, ambaye sasa akawa na uhakika kuwa kila kitu kitaendelea vizuri na kushamiri japokuwa alikuwa amepoteza wazazi wake.



    Khalfan akawa anajituma kwa bidii kuhakikisha kuwa hakuna kinachomshinda.

    Baada ya miezi saba tangu mzee Shamsi na mkewe wapoteze maisha katika ajali mbaya ya ndege, Miriam akiwa anarudi kutoka hospitali alikuja na habari njema kwa mumewe!



    “Mume wangu, nafurahi kukuambia kuwa baada ya siku si nyingi nitakuzalia mtoto!”

    “Unasema kweli mke wangu? Safi sana!” Khalfan akiwa haamini, alimkumbatia mkewe kwa nguvu… na hapo ndipo naye alipoelewa mkewe alikuwa anamaanisha nini. Mkewe alikuwa mjamzito, furaha iliyoje! Maisha yakawa kama ndio yameanza upya, muda wote wakawa wakicheza kama watoto, wakishinda kutwa nzima katika bustani za maua zilizokuwepo hapo nyumbani.



    Muda ukawa unazidi kwenda, huku Khalfan akiwa anampeleka mkewe Clinic mara kwa mara, kuhakikisha anajifungua salama. Miezi ikawa inakatika, hatimaye miezi tisa ikawa imetimia. Bi Miriam akajifungua salama mtoto wa kiume, mzuri kama mama yake. Furaha katika ndoa yao ikawa imeongezeka mara dufu, na ikawa inazidi kuongezeka kila uchao.



    Wakampa mtoto wao jina la Khaleed . “Mume wangu yaani furaha unayonipa maishani, sikuwahi kutegemea hata siku moja! Nakupenda sana mume wangu na Mungu azidi kuibariki ndoa yetu tudumu mpaka kifo kitakapo tutenganisha” Bi Miriam alikuwa akiongea kwa hisia nzito za mahaba kwa mumewe wakiwa na kichanga chao Khaleed, wakipunga upepo wa jioni.



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog