Search This Blog

Sunday, July 10, 2022

USIFE KWANZA MPENZI WANGU - 2

 





    Simulizi : Usife Kwanza Mpenzi Wangu

    Sehemu Ya Pili (2)



    Zoezi la kwanza la Rashid kuondoka nyumbani kwao, linakamilika. Zoezi lililokuwa linafuata kwa Levina ilikuwa ni kuhakikisha Deo anaingia nyumbani kwao. Pamoja na mafanikio yale makubwa, moyo wake haukuwa na amani kabisa kutokana na fitna alizomfanyia Rashid.



    Hata hivyo, kikubwa zaidi kwake ilikuwa ni Deo kukubali kwenda nyumbani kwao na baadaye alitamani sana Deo mpenzi wake wa maisha yake yote. Hiyo ndiyo ilikuwa ndoto yake kubwa. Akiwa katika lindi la mawazo, akaamua kumpigia simu Deo.

    Je, nini kitaendelea? Endelea kuisoma...

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    LEVINA aliumia sana ndani ya moyo wake, akaona ni vyema kama angenyanyua simu yake na kumpigia Deo. Alitaka kujua hisia zake zina nini juu yake. Hakutaka kufanya mambo kwa hasara!



    Akachukua simu na kwenda moja kwa moja kwenye Menu, akabonyeza Contacts kisha akaanza kutafuta jina la Deo, alipolipata akabonyeza kwenye kitufe cha kijani ili kuruhusu upigwaji simu.



    Punde tu, sauti ya Deo ikasikika...

    “Vipi Levina mbona usiku sana?”

    “Nina matatizo Deo!”

    “Matatizo gani?”

    “Naomba nikuulize kwanza maswali yangu!”



    “Uliza.”

    “Mimi ni rafiki yako?”

    “Ndiyo!”

    “Unaniamini?”

    “Ndiyo!”



    “Unanipenda?” Levina akauliza kwa sauti ya taratibu, lakini iliyochanganyikana na kilio cha kwikwi kwa mbali.

    Deo hakupata shida sana kugundua kwamba Levina alikuwa analia. Pengine hilo si neno sana, lakini kwanini amemuuliza kama anampenda? Hata kama anampenda, ndiyo alie?

    Kwanini analia?



    Hakujua!

    Kimya cha muda mfupi kikapita, Deo akiwa ametulia kwenye simu na Levina akiendeleza kilio chake cha chini chini huku kwikwi zikisikika kwa mbali.

    “Levina,” baadaye Deo akaita.

    “Bee!”

    “Nini tatizo?”



    “Si tatizo, napenda kusikia ukinijibu!”

    “Uliuliza nini?”

    “Nilikuuliza kama unanipenda?”

    “Ni kweli nakupenda Levina, wewe ni rafiki yangu na umekuwa msaada kwangu kwa kila kitu, lazima nieleze ukweli, nakupenda, kwani wewe hunipendi?”

    “Swali gani hilo Deo?”



    “Samahani kama nimekuudhi, lakini ndani ya moyo wangu natambua kwamba tunapendana, mimi nafahamu hilo, naamini hata wewe ni kama mimi.”

    “Kweli.”

    “Lakini ni kwanini unalia?”

    “Silii ila sauti yangu leo haipo vizuri sana.”

    “Unakohoa?”



    “Ndiyo!”

    “Pole sana.”

    “Ahsante.”

    “Nina swali lingine kwako Deo!”

    “Uliza.”



    “Lakini kabla sijauliza, nataka unihakikishie kwamba utajibu ukweli wako wote na hutanidanganya jambo lolote.”

    “Hilo kabla hujauliza, naamini unatambua kabisa jinsi nilivyo mkweli.”

    “Umewahi kuona mtu akilia?”



    “Mara nyingi sana, hata leo kuna mtoto nimemuona akilia.”

    “Siyo mtoto, nazungumzia mtu mzima.”

    “Ndiyo, kwenye misiba huwa wanalia sana, nimeshaona mara nyingi, kwani kuna nini, mbona unaniacha na maswali?”

    “Lakini vipi kama ukiona mtu mzima analia?”

    “Nitajisikia vibaya sana.”



    “Umeshawahi kumuona mtu akilia kwa ajili yako?”

    “Hapana.”

    “Utapenda siku moja hilo likitokea?”

    “Hapana.”

    “Basi usiku mwema.”



    “Kwanini?”

    “Nimekutakia usiku mwema Deo.”

    “Lakini sijakuelewa kabisa. Mbona leo maneno yako yamekuwa magumu sana kuingia kichwani mwangu? Kwani kuna nini kimetokea?”

    “Hakuna...nilitaka kujua tu unachowaza kichwani mwako!”

    “Nikuambie kitu Levina?”



    “Nakusikiliza.”

    “Nitalala nikiwa na mawazo sana leo. Maneno yako yananiacha na maswali mengi yasiyo na majibu kabisa. Mpaka sasa sijajua maana ya kauli yako.”

    “Siku moja utajua....”

    “Usiku mwema.”



    “Na wewe pia!”

    Wakakata simu zao.

    Deo akapata wakati mgumu sana wa kuwaza mambo kichwani mwake bila kupata majibu. Alikuwa katika wakati mgumu sana wa kujaribu kuwaza kilicho kichwani mwa Levina kitu ambacho kwa hakika kisingekuwa rahisi kuelewa.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Sijajua anamaanisha nini? Anyway itajulikana baadaye!” Akawaza na kujifunika shuka kisha akaishilia usingizini.



    ****

    Siku nzima ilikuwa kama wiki kwa Levina, kichwa kilikuwa kinamuuma mawazo mengi yakimsumbua. Hakuwa na kitu kingine kilichomtesa zaidi ya Deo, aliendelea kuwaza namna ya kumsogeza karibu yake.



    “Nampenda sana Deo, ni kweli kwamba nampenda sana, lazima nitumie kila njia, nihakikishe anakuwa wangu. Hilo lazima nitalifanya,” akawaza Levina akiwa kazini kwake Posta.



    Levina baada ya kumaliza kidato cha sita, wazazi wake walimkabidhi moja ya maduka yao yaliyopo mjini, Levina alipewa duka la simu lililopo Posta Mpya jijini Dar es Salaam.

    Alichojua yeye ni kwamba alikuwa msimamizi wa duka lile kubwa, lakini wazazi wake walipanga kumwachia moja kwa moja kama lake. Walimfanya msimamizi mkuu, akishughulikia kila kitu, mpaka mishahara ya wafanyakazi, walichokifanya wao ni kukagua mahesabu ya fedha zinazoingia na kutoka benki.



    Mali ikipungua dukani, ilikuwa ni kazi ya Levina kuagiza au kwenda nje ya nchi kununua mzigo mwingine wa dukani.

    Akionekana mwenye mawazo tele kichwani mwake, simu yake ikatoa mlio wa ujumbe mfupi wa maneno, mara moja akaufungua na kusoma.



    Ilikuwa meseji kutoka kwa mama yake, alijikuta anarudia kusoma zaidi ya mara mbili ile meseji akiwa haamini kabisa alichokiona.

    Ujumbe ule ulisomeka; “Levina ni wiki moja sasa tangu Rashid ameondoka, hatuna house boy, sasa kama unaweza ni vizuri ukashughulikia hilo, tukapata mtu mwingine haraka.”

    Levina akatabasamu.



    Ilikuwa nafasi nzuri kwake ya kumwingiza Deo nyumbani kwao.

    “Yes, mambo yanakwenda kama nilivyopanga, afadhali,” akasema kwa sauti ya taratibu akiachia tabasamu.



    ***

    Jioni Levina aliwahi sana kurudi nyumbani, akamkuta mama yake sebuleni, baada ya kumsalimia akamwambia...

    “Mama nilipata sms yako ya mchana, nimeanza kuifanyia kazi, ndani ya siku tatu tutapata mtu mwingine.”



    “Oh! Usijali binti yangu, ameshapatikana kijana mwingine kutoka Bagamoyo, atakuja kuanza kazi kesho.”

    Uso wa Levina ukasawagika kwa huzuni.





    KWA sekunde kumi na tano, Levina alikuwa ameganda akimwangalia mama yake, ni kama hakusikia vyema maneno yale, hata kama aliyasikia vizuri lakini yalionekana kuwa magumu sana kupenyeza kwenye ngoma za masikio yake.



    Anamwangalia mama yake kwa macho yanayozungumza jambo fulani, ingawa haijulikani moja kwa moja kuwa anazungumza nini. Mama yake aliweza kugundua tofauti aliyonayo mwanaye haraka sana.



    “Vipi Levina mwanangu, mbona kama hujafurahia?”

    “Siyo hivyo mama?”

    “Bali nini tena?”

    “Nimeshangaa, maana tayari nilishaanza taratibu za kumpata huyo mtu.”



    “Kwani umeshampata?”

    “Kuna dada mmoja ameniambia kwamba jioni ya leo atakwenda kuzungumza naye. Yupo kaka mmoja amesema anaishi Mburahati, kwahiyo akionana naye atajaribu kumweleza.”

    “Ni mfanyakazi au yupo tu, nyumbani?”



    “Anafanya kazi!”

    “Sasa atawezaje kutoka?”

    “Kasema atamshawishi, maana hata pale halipwi mshahara mkubwa, lakini pia atamwambia mazingira ya kazi ni mazuri.”

    “Sawa, ngoja tuone.”



    “Na huyo mwingine uliyesema?”

    “Huyo kila kitu kipo tayari, nimeshafanya naye mawasiliano na tumekubaliana aje kesho!”

    “Sasa itakuwaje? Maana sitaki kuonekana mwongo kwa rafiki yangu.”



    “Kesho tutapata majibu kamili, kama akija huyo wa Bagamoyo sawa, asipokuja basi utanijulisha makubaliano ya huyo kijana mwingine atakayezungumza na rafiki yako leo usiku.”

    “Sawa mama, mimi nipo ndani,” akasema Levina.

    “Sawa mama.”



    Levina akajikongoja mpaka ndani akionekana kuwa na uchangamfu kidogo, bado alikuwa akiomba sana huyo kijana wa Bagamoyo asitokee ili Deo apate nafasi ya kuingia kwao.

    “Itawezekana tu, maadamu moyo wangu umempenda, naamini itakuwa hivyo,” akawaza Levina.



    Baada ya kubadili nguo, aliingia bafuni kuoga, alipotoka alionekana kuwa na nguvu kidogo, akachukua simu na kumpigia Deo.

    “Uko wapi?”

    “Nipo njiani naelekea nyumbani.”



    “Umefika wapi sasa hivi?”

    “Ndiyo nakaribia kushuka Mwembechai!”

    “Ok! ukishuka naomba unisubiri!”

    “Kwani wewe uko wapi?”

    “Nipo home, lakini natoka sasa hivi nachukua taxi nakuja.”



    “Basi jitahidi ufanye haraka!”

    “Usijali, sina muda mrefu sana nitakuwa hapo.”

    “Poa.”

    Levina akabadili nguo haraka na kutoka. Alipopita sebuleni alimkuta mama yake akiwa amekaa pale pale!



    “Haya wapi tena?”

    “Natoka kidogo mama!”

    “Ila saa hizi ni usiku na baba yako hapendi kabisa utoke usiku.”

    “Mama siendi mbali, nakwenda hapo Mwembechai mara moja.”

    “Unatoka na gari?”



    “Hapana, sitaki baba ajue nimeenda mbali kama akirudi mapema, ni bora alione gari atajua nipo jirani!”

    “Kumbe hutakuwa jirani siyo?”

    “Mama...!!! Mwembechai si mbali, lakini ni mbali pia mama. Kwa baba kule ni mbali!”



    Mama Levina akacheka.

    “Uwahi kurudi,” akasema mama Levina akiendelea kutabasamu.

    “Nakuahidi mama.”

    Levina akaondoka zake.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    ***

    Levina alifurahi sana kukutana na Deo, moyo wake ulikuwa ukisisimka sana kila alipokutanisha macho yake na Deogratius.

    Alikuwa mwanaume pekee ambaye aliweza kuutetemesha moyo wake.

    “Nina habari njema Deo!”

    “Juu ya nini?”



    “Unakumbuka mara ya mwisho nilizungumza nini na wewe?”

    “Ndiyo, nakumbuka vizuri sana.”

    “Ilikuwa ni nini?”

    “Kuhusu kazi nyingine!”

    “Halafu?”

    “Kusoma.”



    “Safi sana, kumbe unakumbuka vizuri sana, sasa tunaanza na kimoja baada ya kingine. Kama nilivyokuambia sisi ni marafiki na nitakuwa tayari kutumia kila njia nihakikishe nakufurahisha!”

    ”Nimefurahi kusikia hivyo.”

    “Nimekupatia kazi, tena nyumbani kwetu kabisa.”



    “Unasema kweli?” Deo akauliza akiwa haamini kabisa alichoambiwa na Levina.

    “Kwanini isiwe kweli?” Levina akauliza akitabasamu.



    Tabasamu lililomchoma Deo moyoni, kwa mara ya kwanza alikiri kumuona Levina akiwa ameachia tabasamu zuri zaidi kuliko siku zote!

    Uzuri wa Levina ukawa hadharani!





    Pamoja na taarifa kutoka kwa mama yake kwamba alishapata kijana mwingine wa kazi, bado Levina hakukata tamaa kuhusu Deo. Usiku ule ule akatoka na kwenda kukutana naye Mwembechai.



    Levina akamweleza kwamba amempatia kazi nyumbani kwao, Deo akafurahi sana. Furaha iliyosababisha Levina aachie tabasamu mwanana! Uzuri wake ukawa hadharani!

    Nini kitatokea? Endelea kuisoma...



    DEOGRATIUS akagundua kitu kipya kabisa kutoka kwa Levina, aligundua kwamba alikuwa msichana mzuri kupindukia! Tabasamu lake lililoacha sehemu kubwa ya meno yake nje, lilisababisha aone vijishimo vidogo mashavuni mwake na hivyo kuzidisha urembo wake.



    Alihisi moyo wake kama umepigwa na shoti ya umeme, alikuwa amesimama mbele ya mwanamke mrembo sana tofauti na matarajio yake. Levina alikuwa mzuri zaidi ya alivyofikiria.

    Kwanini anamsaidia sana?



    Kwanini anakuwa naye karibu sana? Hayo yaliendelea kuwa maswali ambayo hayakuwa na majibu ya moja kwa moja kichwani mwake. Alibaki ameganda akimwangalia Levina ambaye sasa aliamua kucheka kabisa. Furaha ya Levina ilikuwa ni kuona jinsi Deo anavyomkubali yeye.



    Hakujali umasikini wake, alichojua yeye ni mapenzi tu. Moyo wake ulianguka kwake, alitamani sana awe mpenzi wake wa dhati ndani ya moyo wake.



    “Deo!” Levina akaita kwa sauti tamu sana.

    “Naam!”

    “Vipi?”

    “Poa.”



    Levina akacheka.

    “Mbona unanicheka?”

    “Sijakucheka Deo!”

    “Bali!”



    “Nimecheka. Unajua kuna tofauti kubwa sana kati ya kucheka na kumcheka mtu. Mimi nimecheka, sijakucheka. Umeona tofauti hiyo?”

    “Haya mama wa Kiswahili, siwezi kushindana na wewe, hapo umenishinda.”

    “Enhee stori nyingine?”



    “Sina!”

    “Basi poa, acha mimi nirudi zangu home, si unajua tena dingi hajaingia, sasa akija na kunikuta sijafika nyumbani mpaka saa hizi haitakuwa sawa!”



    “Sawa basi. Enhee niambie, naanza lini kazi?”

    “Una hamu eeh!”



    “Sasa kumbe ningefanyaje?”

    “Subiri kidogo, mpaka kesho nitakupa jibu kamili la lini utaanza kazi rasmi.”



    “Sawa.”

    “Usiku mwema.”

    “Nawe pia!”



    Deo akaondoka, Levina akaendelea kumkazia macho mpaka alipoondoka. Baada ya hapo akavuka upande wa pili, akachukua taxi nyingine na kurudi zake nyumbani. Kwa bahati nzuri, baba yake alikuwa bado hajafika nyumbani.

    “Una bahati, baba yako hajafika!”



    “Acha tu mama!”

    “Enhee vipi, mambo yanaendaje?”

    “Huyo kijana yupo mama, hata kesho anaweza kuja!”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Sawa basi, lakini naomba tusubiri hadi kesho, kama yule wa Bagamoyo hatakuja basi atakuja huyo, unajua tayari nilishamuahidi na huyo mtu alimuhangaikia sana!”

    “Sawa mama,” Levina akasema kwa sauti ya chini lakini ndani ya moyo wake akiumia sana.



    Alitamani sana huyo kijana asitokee ili Deo wake aweze kwenda nyumbani kwao. Hiyo ilikuwa dua yake kubwa.

    “Mimi naingia chumbani mama.”



    “Sawa, bado nipo hapa naendelea kuangalia taarifa ya habari.”

    Muda mfupi baada ya Levina kuingia chumbani kwake, simu ya Mama yake ikaita. Namba hakuzijua, lakini mara moja akapokea!

    “Nani mwenzangu?” Ndiyo neno la kwanza mama Levina kutamka mara baada ya kupokea simu.



    “Mama Happy wa Bagamoyo...samahani mama Levina, nimekupigia na namba ya kibandani, simu yangu haina chaji!”

    “Usijali, vipi za huko?”

    “Bwana wangu, si salama.”



    “Kuna nini tena?”

    “Yule kijana amefiwa na mama yake, kwahiyo anatakiwa kwenda kwao Morogoro kesho, kurudi ni baada ya wiki mbili!”

    “Duh!”



    “Ndiyo mwenzangu, matatizo yamemfika kijana wa watu, kwa jinsi alivyokuwa na hamu na hiyo kazi, yaani amechanganyikiwa kabisa!”

    “Poleni mwaya, umpe pole na yeye, hakuna jinsi, maana nilikuwa na shida ya haraka sana na kijana wa kazi, sasa nalazimika kutafuta mwingine.”



    “Hakuna shida, haikuwa riziki yake!”

    Wakakata simu zao. Muda ule ule mama Levina akamwita binti yake, ambaye alifika baada ya muda mfupi sana.



    “Levina nimepigiwa simu na Happy sasa hivi, yule kijana amepatwa na matatizo. Amefiwa na mama yake, kwahiyo hataweza tena kuja labda mpaka baada ya wiki mbili, nimemwambia mama Happy kwakuwa nina haraka, nalazimika kutafuta mwingine kwahiyo basi zungumza na huyo rafiki yako, yule kijana aje kesho aanze kazi mara moja!”



    “Sawa,” Levina akajibu kwa sauti ya chini sana, akionekana kuwa na huzuni lakini ndani ya moyo wake alikuwa akishangilia kwamba Deo wake alikuwa anakwenda kuwa karibu naye.



    ****

    Levina alivyoingia tu chumbani kwake, kitu cha kwanza ilikuwa kuchukua simu yake na kumpigia Deo haraka sana.

    “Vipi?”



    “Habari njema zaidi ya zile za saa ile!”

    “Zipi tena Levina?”

    “Unatakiwa kuanza kazi kesho, vipi utaweza?”

    “Nitaweza!”

    “Kweli?”



    “Kweli kabisa.”

    “Basi fanya juu chini, kesho tukutane saa 3:00 asubuhi!”

    “Sawa.”

    Wakaagana.



    ****

    Kama walivyokubaliana, siku iliyofuata walikutana Mwembechai, Deo akiwa na begi lake, tayari alikuwa ameshaacha kazi alipokuwa akifanya mwanzoni na akawa tayari kwenda kuanza kazi kwa akina Levina.



    Wakaingia sebuleni na kukutana na mama yake Levina akiwa anamsubiria kwa hamu...



    “Karibu mwanangu!” Mama Levina akamwambia Deo.

    “Ahsante mama!”

    “Jisikie uko nyumbani!”



    “Ahsante mama.”

    “Nina imani maelekezo yote umeshapewa na Levina, kama bado atakupa. Acha mimi niwahi kazini, nawatakieni siku njema,” akasema mama Levina akisimama na kupiga hatua za kuondoka.



    “Ahsante!” Deo akajibu akiona haya.

    Mama Levina akaondoka zake, akawaacha Deo na Levina tu nyumbani. Levina aliposikia muungurumo wa gari la mama yake nje, akajua tayari ameshaondoka. Akamkazia macho Deo, aliyekuwa amesimama kama mlingoti!



    Mara ghafla akamsogelea na kumkumbatia kwa nguvu! Kilikuwa kitendo cha haraka na ghafla sana, kilichomshtua sana Deo. Akabaki ameduwaa akimwangalia bila majibu!





    Levina alimshangaa Deo kwa kutoonesha furaha kwa kupata kazi.

    “Jamani Deo mbona huoneshi furaha?”

    “Levina mbona nipo happy.”

    “Muongo, au hukupenda kuja kufanya kazi hizi?”

    “Kwa nini nisipende.”

    “Basi Deo nakwambia achana na mshahara utakao lipwa nitahakikisha nakuongezea pesa zaidi ya mshahara wako.”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Nitashukuru Levina.”

    “Basi twende nikakuoneshe chumba chako.”

    Levina alichukua begi la Deo na kumpeleka kwenye banda la uani kulikokuwa na chumba kimoja. Baada ya kuingia chumbani alitoka na kurudi na ufagio na shuka za kumtandikia. Deo alishangaa mtoto wa tajiri yake kumuhangaikia vile, baada ya usafi wa chumba alimtandikia kisha alimkaribisha.

    “Deo karibu hiki ndicho chumba chako.”

    “Asante.”

    “Vipi umekipenda?’

    ”Nimekipenda.”

    Baada ya kumuonesha kile chumba alimuelekeza kazi zote alizotakiwa kuzifanya kisha alimuacha aendelee na majuku ya siku ile. Levina alirudi hadi sebuleni kutaka kujiandaa kwenda mjini kwenye duka.

    Lakini roho haikumpa alisogea hadi dirishani kumtazama Deo aliyekuwa katika vazi la bukta na singland, alijikuta akitabasamu mwenyewe jinsi moyo wake ulivyofurahi kuwa na Deo mwanaume aliyeutesa moyo wake.

    Kuwa mbali na Deo aliona kama kuinyima uhuru nafsi yake, aliamini muda ule ambao wazazi wake hawapo ni muda mzuri wa kujisogeza karibu na Deo. Alitoka hadi uani ambako Deo alikuwa ameanza kazi ya kupunguza majani, alisogea karibu yake huku kidole kikiwa mdomoni kujipa ujasiri.

    “Deo,” alimwita huku akiachia tabasamu pana.

    “Levina si umesema unawahi kazini?”

    “Ndiyo Deo lakini bado nina muda, Deo,” Levina alimwita Deo huku akimtoa majani kichwani.

    “Unasemaje Levina?”

    “Kazi unaionaje?”

    ”Ndiyo naianza lakini siyo mbaya.”

    “Leo kuna kitu nataka kukueleza.”

    “Kipi hicho?” Deo aliuliza bila kumuangalia.

    “Deo acha kwanza kukata majani nisikilize.”

    “Levina hii ndiyo kazi iliyonileta acha niifanye, we wahi kazini jioni tutazungumza nitakuwa nimepunguza kazi si unajua leo ndiyo siku ya kwanza nitaonesha picha mbaya.”

    “Deo ufanye kazi usifanye kazi mimi ndiye mwenye mamlaka, na kukuleta hapa si kufanya kazi hii.”

    “Si kazi hii, kwa kazi gani?”

    “Ili uwe karibu na mimi”.

    “Kivipi?”

    “Deo lazima usome alama za nyakati kila ninachokifanya lazima ujiulize kina maana gani.”

    “Levina mimi na wewe tumefahamiana kitambo umekuwa msichana ambaye umeonesha kunijali, nimekuwa nikivunia upendo wako na kujikuta nikikosa cha kukulipa.”

    “Deo cha kunipa unacho hakihitaji pesa wala nguvu.”

    “Kipi hicho?”

    “Deo lazima leo nikueleze ukweli...na..na..ku...,” Levina hakumalizia aliweka kidole mdomoni huku mkono ukitetemeka baada ya kupoteza ujasiri wa kulitamka neno toka moyoni mwake.

    “Levina unasemaa!”

    Levina aliona aibu na kukimbilia ndani huku akimwacha Deo akijiuliza maswali yasiyo na majibu, alijiuliza Levina alimaanisha anampenda. Kama ni kweli ulikuwa mtihani ambao aliamini kabisa mapenzi ni kikohozi kamwe wasingeyaficha. Kwa muonekano wa haraka ilionekana familia yake ilikuwa ikimpenda sana na kumjali.

    Aliamini kama wazazi wake wakigundua lazima wangemfukuza kazi, alijua lazima atataabika kutokana na kuacha kazi iliyokuwa ikimuingizia riziki. Pia alikuwa na mtihani mwingine kama atamkatalia Levina lazima atamfukuzisha kazi, lakini hakutaka kuingilia sana mawazo ya Levina.

    Levina alikimbia hadi chumbani kwake na kuanza kulia kutokana na kukosa ujasiri kuwasilisha uju mbe wake. Alichukua kitambaa cha mkononi na kufuta machozi. Mara simu ya mama yake iliingia, aliipokea na kuzungumza.

    “Haloo Mamy.”

    “Levina upo wapi?” Alimuuliza kwa ukali kidogo.

    “Mbona hivyo mama?”

    “Hujanijibu upo wapi?”

    “Mamy nipo njiani nakwenda mjini.”

    “Jitahidi uwahi kuna mteja wa jana mlikubaliana afuate simu dukani amefika muda, bado duka halijafunguliwa.”

    “Namjulisha sasa hivi.”

    Alikata simu na kukimbia bafuni kuoga kisha alibadili nguo haraka haraka kuwahi dukani, alitoka hadi uani alipokuwa Deo akikata majani alitembea kwa mwendo wa kunyata alipomkaribia alimgusa begani, Deo alipogeuka alikutana na busu la mdomoni.

    “Deo bai, nawahi kazini kazi njema.”

    “Na wewe pia.”

    Levina alitembea kwa haraka kuelekea kwenye gari lake ili awahi kwenye mihangaiko yake. Nyuma alimuacha Deo na maswali mengi juu ya vitendo vya kimahaba vya Levina, Levina alibadilika kwa muda mfupi hakuwa yule mpole na mnyenyekevu muda wote, alikuwa ni mtu aliyeonekana kuchizika kimahaba.

    Kauli ya Levina ilimfumbulia fumbo zito moyoni mwake la muda mrefu la huduma zote zilizoelekezwa kwake na Levina haikuwa bure na ukweli wake ulikuwa umedhihirika muda mfupi uliopita. Deo alicheka na kuendelea kupunguza majani huku umbile la Levina msichana mrembo tena anayetoka katika familia tajiri lilitawala katika ubongo wake.



    Mbinu za Levina kumuingiza ndani ya jumba lao lilimfanya Deo acheke peke yake kwa kicheko cha chini chini huku akitikisa kichwa, kama alikuwa akizungumza na mtu alisema kwa sauti ya chini.



    “Kweli Levina kiboko, mbinu zake mwenyewe sina hamu.”

    Baada ya kumaliza kukata majani aliyakusanya na kuyapeleka kwenye shimo la takataka lililokuwa nyuma ya banda la ng’ombe.

    ***

    Levina akiwa ndani ya gari lake akielekea kwenye duka lao la simu, macho yake yalikuwa yametazama mbele huku akikanyaga mafuta taratibu kutokana na foleni ya jijini. Pembeni ya barabara alimuona mvulana mmoja na msichana wakitaniana katika hali ya mapenzi.



    Aliwakazia macho mpaka alipowapita, alitabasamu na kuchukua simu yake iliyokuwa kwenye dash boad na kuifungua upande wa picha. Aliifungua na kuijaza picha ya Deo kwenye kioo cha simu, picha ambayo alipiga kwa siri bila yeye kujijua.



    Aliibusu simu na kusema kwa sauti ya chini.

    “Lazima Deo atanielewa si mtoto mdogo.”

    Kutokana na foleni ya barabarani kila gari liliposimama aliiangalia picha ya Deo na kutabasamu. Aliikumbatia simu kifuani katika mahaba mazito na kufumba macho huku akisindikizwa na muziki mtamu wa kizazi kipya wa Suma Usemao Mapenzi ni sumu.



    Alirudia maneno ya kiitikio kimoyomoyo, kumbe wakati huo foleni ilikuwa imeshasogea lakini Levina alikuwa amejisahau na mahaba mazito ya picha ya Deo kwenye simu yake. Hata kelele za honi hakuzisikia kutokana na kujifungia ndani ya gari huku akipulizwa na kiyoyozi. Sauti ya kugongwa dirisha ndiyo iliyomshtua alipofumbua macho aligundua foleni imefika mbele ambapo alibadili gia na kukanyaga mafuta akiwaacha watu wakimsindikiza na matusi mazito ya nguoni lakini hakuyasikia.



    Hata alipofika dukani muda wateja walipopungua alitumia muda huo kuzungumza na Deo huku akimpigia simu mfanyakazi wa ndani ampatie Deo chakula kizuri na kila kitu ambacho baba yake alikitumia wakati wa chakula. Kingine alimuonya mfanyakazi wa ndani kuwa mbali na Deo bila kufanya utani wowote.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Haloo Deo.”

    “Ooh, Levina za kazi?”

    “Zimezidi kuwa nzuri baada ya kusikia sauti yako.”

    “Nashukuru kusikia hivyo.”



    “Vipi unafanya nini sasa hivi?”

    “Mmh, nimepumzika ndiyo nimemaliza kula.”

    “Umekula nini Deo?”

    “Chakula.”



    “Chakula gani?”

    “Ndizi na nyama.”

    “Matunda je?”

    “Nimepata.”



    “Juisi?”

    “Nimepata.”

    “Umeshiba?”

    “Nimeshiba.”



    “Muongo, usione aibu wewe kwa sasa ni zaidi ya baba yangu mzazi.”

    “Kivipi?”

    “Umekuwa mtu muhimu sana maishani mwangu, kuwa nawe karibu nimefarijika. Nilijihisi ufahari siku uliyonikubalia kuja kufanya kazi kwetu.”



    “Mh!”

    “Usigune Deo, lazima niseme ukweli, Deo nakupenda sana.”

    Maneno yale yalimfanya Deo anyamaze kwa muda kitu kilichomnyima raha Levina na kuona mbegu yake huenda hakuipanda muda muafaka. Lakini kwa upande mwingine alijiona yupo sawa kutokana na moyo wa kupenda ulivyo.



    Siku zote macho yakiona moyo unapenda na moyo ukipenda subira hakuna tena na subira ikitoweka aibu hukimbia. Aliamini mchuzi wa mbwa ulitakiwa kunywewa ungali moto.



    Hakujutia kauli yake kumueleza ukweli Deo kuwa anampenda, ulikuwa ujumbe sahihi toka moyoni mwake ambao aliamini kupitia njia ya simu kidogo ujasiri ulikuwepo.



    Lakini kimya cha Deo kilimfanya akose raha moyoni kwake aliamini kama Deo hataafiki ombi lake lilikuwa sawa na kutwanga maji kwenye kinu.



    “Deo,” Levina alimwita baada ya kupita ukimya mfupi.

    “Levina.”



    “Mbona hunijibu, kujivua nguo mbele yako si umalaya Deo, usinihukumu kwa jinsia yangu bali kwa upendo wangu mzito moyoni mwangu.



    Deo sikuwa na njia yoyote ya kukueleza kuwa nakupenda, naomba uheshimu hisia zangu.”

    “Levina,” Deo alimwita Levina kisha alishusha pumzi nzito.



    “Deo,” Levina aliitikia upande wa pili na sauti yenye dalili za kilio.



    “Levina naogopa sana mimi kuwa sehemu ya matatizo yako katika furaha zako za kila siku.”

    “Deo kunikubalia ni kuniingiza kwenye matatizo?”



    “Sina maana hiyo!”

    “Muongo Deo, unataka kuongopa nini?”

    “Levina wewe ni mtu muhimu sana kwangu, nilikuwa na maana kutokana na kujitoa kwangu na mimi kuniona ni sehemu ya furaha yako. Nami najitoa kwako kwa nguvu zote ili kukuhakikishia zile raha ulizokuwa ukizitafuta kwangu unazipata.”

    “Kweli Deo?”



    “Siwezi kukudanganya.”

    “Waooo, I can’t beleave my dear, Thanks God thanks Deo I love you soooo much.”



    Levina alishangilia kukubaliwa ombi lake na kujisahau kama yupo dukani na kuwashangaza wateja waliokuwa dukani wakisubiri amalize kuzungumza kwa simu.



    Hata baada ya kumaliza kuzungumza na simu, uso wa Levina ulionesha dhahiri kuwa amezama ndani ya dimbwi la huba. Aliendelea kuchekacheka mwenyewe kama mwendawazimu bila kujali idadi kubwa ya wateja ambao walikuwa wakisubiri kuhudumiwa. Akili yake ilijawa na taswira ya Deo kiasi cha kusahau kazi.



    “Oya sista vipi? Tumesimama muda mwingi kusubiri huduma we uko bize na simu tu! Tuhudumie tafadhali!”

    Kauli ya mmoja wa wateja waliokuwa wamesimama kusubiri huduma kwenye duka la simu la kina Levina ilimzindua kutoka kwenye mawazo yaliyoiteka akili yake.



    Oops! Im sorry, samahani wateja, hii simu imetoka kwa mtu muhimu sana, enhe, ulisema unataka Nokia toleo gani?”

    “Nokia 5130c-2!”

    “Mimi nakudai chenji yangu, naona simu imekupagawisha kabisa, shemeji nini?”



    Levina aliendelea kuwahudumia wateja waliokuwa wakiingia na kutoka kwenye duka lao la simu. Wakati akiendelea na kazi, majibu ya Deo yalikuwa yakiendelea kuzunguka kichwani mwake kama filamu nzuri ya kusisimua.



    Wateja walipopungua, alichukua simu yake na kuendelea kuitazama picha ya Deo aliyompiga bila mwenyewe kujijua, akawa anaitazama huku usoni akiwa na bonge la tabasamu! Moto wa penzi la Deo ulikuwa umewaka kikweli ndani ya moyo wake, akawa anasubiri kwa hamu muda wa kufunga duka ufike haraka ili akaonane na Deo, kipenzi cha moyo wake.



    ***

    Kuchanganya mapenzi na kazi ni suala ambalo Deo alikuwa akiliogopa sana. Mara kwa mara alikuwa akijiambia mwenyewe kuwa safari ya kutoka nyumbani kwao Shinyanga hadi Dar es Salaam ilikuwa ni kutafuta maisha, hivyo hakuwa tayari kuona anashindwa kutimiza ndoto zake kwa sababu ya kuchanganya mapenzi na kazi.



    Alipofikiria kitakachotokea endapo uhusiano wake na Levina ungegunduliwa na wazazi wa Levina, alijikuta akibatilisha majibu aliyompa Levina siku ile. Alichokiamua ni kutojihusisha kwenye uhusiano wa kimapenzi na Levina, aliamua kuelekeza nguvu na akili zake kwenye kazi.



    Saa zilizidi kuyoyoma na hatimaye muda wa Levina kurudi nyumbani ukawa umewadia. Akilini mwake, Levina alikuwa akiwaza namna atakavyomkumbatia na kumkiss Deo mara atakapowasili nyumbani kwao. Alipanga kufanya kila linalowezekana ili kumfanya Deo ampende kama yeye anavyompenda.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Baada ya kufunguliwa geti na kwenda kuegesha gari lake, Levina alishuka akiwa na hamu kubwa ya kuoanana na Deo.



    Nyumbani kwao hakukuwa na mtu mwingine yeyote zaidi ya mfanyakazi wao na Deo kwani wazazi wake walikuwa bado hawajarejea kutoka kwenye mihangaiko yao.



    ‘Jamani Deo! Nilikukumbuka sana sweetie, yaani nilikuwa naona saa haziendi,’ aliongea Levina kwa sauti ya kudeka na kumkumbatia Deo kimahaba.



    Katika hali ambayo hakuitegemea, Levina alishangaa kumuona Deo akikunja sura na kumsukuma pembeni, kisha akaondoka na kuelekea chumbani kwake na kumuacha Levina akiwa bado haamini kile kilichotokea.



    “Kwa nini unanitesa Deo, nifanye nini ili uamini kuwa ni kweli nakupenda?” Aliongea Levina huku akimfuata Deo.



    “Tafadhali sana Levina, sina maana ya kukutesa lakini naona kama najihatarisha sana pamoja na kukuweka wewe kwenye matatizo.”



    “Kivipi Deo, mi sikuelewi mwenzio?”

    “Namaanisha hivi, nakupenda sana Levina lakini sitaki kuwaudhi wazazi wako!



    Naamini wakigundua watakasirika sana na watanitimua hapa kwenu, nimetoka mbali sana Levina kuja mjini kutafuta maisha, sitaki mapenzi yaniharibie maisha yangu ya baadaye…”



    Wakati Deo akiendelea kujitetea mbele ya Levina, walisikia geti la nje likifunguliwa na gari la wazazi wa Levina likaingia ndani.



    Kwa haraka Deo alitoka nje na Levina naye akaelekea chumbani kwake huku wakiahidiana kuzungumza vizuri baadaye wakiwa peke yao.



    ***

    Deo alijitahidi kuficha hisia zake mbele ya wazazi wa Levina. Bado hofu ilikuwa imeupamba mtima wake.



    Muda wa chakula cha jioni ulipowadia, kama kawaida familia nzima ilijumuika Dinning room kwa ajili ya maakuli.



    Kwa makusudi kabisa, Levina alijisogeza na kukaa jirani na Deo, akamsaidia kumpakulia chakula na kumkaribisha kwa heshima.



    Wakati wakiendelea kula huku wakibadilishana mawazo hapa na pale, Levina alikuwa akimtazama Deo usoni kwa kuibia na kuishia kutabasamu mwenyewe.



    Mchezo ule ulishtukiwa na mama yake Levina, ambaye hata hivyo alijikausha ili awanase vizuri.



    Kwa aibu alizokuwa nazo Deo, alijikuta akishindwa hata kula kwa uhuru kwani mamcho ya Levina yalikuwa hayabanduki kwake.



    Kaamua kujikaza kiume na kumtaza na yeye usoni bila kujali kuwa wamekaa na baba na mama. Macho yao yalipogongana, wote walitabasamu kimahaba, hali iliyomfanya mpaka baba Levina kushtuka.



    Penzi linachipuka kutoka ndani mwa Levina kwenda kwa Deo, kijana anayefanya kazi nyumbani kwao kwa kasi ya ajabu sana. Anashindwa kufanya kazi vyema kutoka na hisia hizo kali za mapenzi. Anajaribu kumweleza Deo, ambaye alimkubalia kwa shangwe!



    Hili lilimfanya afunge duka lake haraka na kurejea nyumbani ili aweze kupata wasaa wa kuzungumza na Deo, lakini jambo la ajabu, alipofika akakuta Deo akiwa na maamuzi mengine mapya! Hakuwa tayari kuwa naye kimapenzi, kiasi cha kumsukuma mbali!



    Baadaye wakiwa kwenye meza ya chakula, Levina alionesha alama zote kuwa anampenda Deo au walikuwa katika uhusiano, jambo ambalo baba yake, aliligundua! Akahisi kuwepo kwa jambo linaloendelea kimya kimya! Je, nini kitatokea? Endelea kufuatilia...



    MZEE Masamu aligundua kitu kupitia macho ya mwanaye aliyekuwa akimwangalia Deo kwa macho yaliyojaa ubembe wa mahaba. Ni kitu ambacho hakukipenda hakika, hakutaka kabisa mwanaye awe na uhusiano na kijana yule. Hakuwa na hadhi ya familia yao.



    Mara ghafla, akasogeza pembeni sahani yake ya chakula na kunawa mikono yake, jambo hilo lilimshangaza sana mke wake.

    “Vipi baba Levina?!”

    “I’m okay!”



    “No dady, you are not okay, vipi chakula hujakipenda?” Mama Levina akasema kwa sauti ya taratibu sana.

    “Nimeshiba mama Levina,” akasema mzee Masamu akimwangalia Levina kwa macho yenye kiashiria kibaya.



    Mama Levina aliweza kugundua kwamba kuna jambo ambalo si la kawaida lilikuwa likiendelea. Anamfahamu vizuri sana mume wake, hakuwa na kawaida ya kushiba haraka kiasi kile, lazima kulikuwa na kitu. Naye akasogeza sahani yake pembeni na kunawa mikono.

    “Mom, kwanini mnasusa chakula?” Levina akauliza kwa mashaka kidogo.



    “Shiiiiii...” mama Levina akamnyamazisha mwanaye.

    Deo akagundua kwamba mchezo wa Levina ulikuwa umegundulika, mara moja akanawa mikono na kukimbilia chumbani kwake. Bwana na Bibi Masamu wote kwa pamoja wakaongozana kwenda chumbani kwako kulala.



    “Mume wangu mpenzi, nini tatizo? Nini kimetokea mpenzi wangu, maana naona haupo sawa kabisa!” Mama Deo akamwuliza mumewe walipoingia chumbani kwao.

    “Unataka kusema hujaona chochote?” Mzee Masamu akasema kwa hasira.

    “Nini tena dear?”



    “Hivi unakumbuka kwanini tulimwondoa Rashid hapa nyumbani?”

    “Ndiyo!”

    “Unaona anayofanya mwanao?”

    “Nani Levina?”



    “Kwani nani mwingine?”

    “Kivipi basi mume wangu?”

    “Hujaona anavyomwangalia yule kijana?”

    “Kwakweli sijawa makini kuwaangalia mume wangu!”



    “Sasa wewe kuwa makini au usiwe makini, lakini nataka kukuambia kwamba, sitaki matatizo katika familia yangu! Deo hana hadhi ya kuwa na mwanangu!”

    “Kwani amesema anataka hivyo?”

    “Hapana, lakini dalili zipo wazi.”

    “Nitazungumza na Levina!”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Siyo utazungumza naye, nenda ukaongee naye sasa hivi, sihitaji matatizo katika familia yangu. Narudia tena sihitaji matatizo katika familia yangu, nenda kazungumze naye tafadhali.”



    “Nimekuelewa mume wangu, ngoja niende nikaongee naye.”

    Mama Levina akatoka haraka na kumuacha mumewe chumbani akiwa amefura kwa hasira. Alipofika sebuleni, alimkuta Levina akiwa anamalizia kuondoa vyombo mezani.

    “Levina nahitaji kuongea na wewe!”



    “Natoa vyombo mama!”

    “Achana navyo isitoshe si kazi yako, kwani Helena yupo wapi? Hiyo ni kazi yake, haikuhusu wewe hata kidogo.”

    “Najua mama, lakini...” Levina akaendelea kujitetea.

    “Wewe tusikilizane!”



    “I’m coming mom!”

    “Hurry up!”

    “Ok mom!”

    Levina akaacha kila kitu na kujisogeza kwa mama yake, aliyekuwa amekaa kwenye sofa kubwa pale sebuleni.



    “Hebu niambie, nini kinaendelea kati yako na Deo?!” Mama yake akamwuliza mara baada ya kukaa sofani.

    “Unamaanisha nini mama?”

    “Macho yako yanaonesha jinsi unavyofahamu ninachomaanisha!”

    “Sijui kitu mama, kwani vipi?”



    “Sasa mimi sina kitu cha kuzungumza zaidi au kubembelezana na wewe, lakini nataka kukuambia kwa kifupi sana, kama una wazo la kuanzisha uhusiano na Deo, futa kabisa wazo hilo!”

    “Uhusiano?”

    “Ndiyo nimekuambia sasa, ondoa wazo hilo kichwani mwako na kama mmeshaanza tafadhali acha mara moja!”



    “Maamaaa...mimi na Deo wapi na wapi mama?”

    “Hili agizo limetoka kwa baba yako!” Mama Deo akaongeza kusema.

    “Mungu wangu, kweli mama?” Levina akashtuka sana.

    “Nadhani unamfahamu vizuri sana mzee Masamu, unajua hasira zake, sasa endelea na upuuzi wako ndiyo utajua kitakachotokea!” Mama yake akasema na kusimama kisha akaondoka zake.



    Levina akabaki pale subuleni akiwa mwenye mawazo mengi sana kichwani mwake. Alimfahamu vizuri sana baba yake, kama ni kweli yeye ndiye alikuwa ameagiza aachane na Deo, basi hali ilikuwa mbaya kuliko alivyofikiria.



    Jambo hilo lilimtisha sana, lakini halikusababisha penzi lake dhidi ya Deo lishuke, bado alihisi penzi zito sana moyoni mwake, alimpenda sana Deo na hakuwa tayari kumpoteza.



    Tayari mambo yamekuwa mabaya kwa upande wa Deo, ambaye Levina anaonekana kumpenda sana, lakini kitu cha ajabu ni kwamba, Levina anashindwa kuficha hisia zake na hivyo kusababisha baba mzazi wa Levina mzee Massamu kuhisi kitu!



    Jambo hilo lilimtisha sana Deo, ambaye aliingia chumbani kwake akiwa na mawazo tele akianza kuhofia kupoteza ajira yake. Akiwa bado ana mawazo, usingizi ukiwa umekataa kabisa kumchukua, akasikia mtu akigonga mlango. Akashtuka sana.



    Alipouliza aliyekuwa akigonga ni nani, hakujibu! Je, nini kitatokea? Endelea kuisoma...



    DEO alishtuka kuliko kawaida, mawazo tele kichwani mwake yakamuandama, kitu kilichoingia kwa kasi sana akilini mwake ni kwamba aliyekuwa akigonga mlango ule alikuwa ni mzee Massamu.



    Hapo hakika ungekuwa mwisho wa ajira yake. Jambo ambalo hakutaka kabisa litokee. Akasogea mpaka kwenye kitasa cha mlango wa chumbani kwake, akasogeza mdomo wake kwenye tundu la funguo, akauliza kwa sauti ya chini kabisa...

    “Nani?”



    “Fungua!” Sasa akajibiwa na sauti ya kike, ambayo haikuwa ngeni sana masikioni mwake.

    Alikuwa ni Levina.

    “We’ Levina, acha ujinga bwana, rudi chumbani kwako.”

    “Fungua kwanza, kuna kitu nataka kukuambia.”

    “Nini?”



    “Fungua.”

    Deo akatumia muda wa dakika mbili tatu kuwaza, kisha akaamua kwenda kufungua ili kuepuka kelele za levina ambazo zingeweza kusababisha matatizo zaidi.

    “Haya unasemaje?” Akamwuliza baada ya kufungua mlango.

    “Kabla hata sijakaa?” Akauliza Levina kwa sauti ya chini, ambayo Deo alishtuka sana kuisikia, akihisi kama ni kubwa.



    “Ongea taratibu bwana...” Deo akasema kwa woga.

    “Niongee taratibu nini? Unamuogopa nani?”

    “Wazazi wako.”

    “Wameshalala bwana.”



    “Kwani unasemaje?”

    “Acha utoto, inamaana hujui kwamba mimi nakupenda?”

    “Najua.”

    “Sasa?”

    “Sitaki tena.”



    “Unasemaje?”

    “Sitaki tena.”

    “Utataka Deo, lazima utake, hujui ni kwa kiasi gani nimehangaika kukupata. Hujui nimefanya mambo mangapi na wakati mwingine kuwakosea watu kwa sababu yako.”

    “Lakini Levina ukumbuke kwamba ulisema unanileta kazini.”



    “Ndiyo nakumbuka.”

    “Sasa?”

    “Lakini si nilikuambia kwamba nakupenda? Unadhani ningeweza kufanya mambo yote hayo hivi hivi tu!”



    “Hivi unajua kwamba haya mambo ni ya hatari sana? Kwanza baba yako anaonekana ameshaanza kuhisi kwamba kuna kitu kinaendelea, huoni kwamba ni tatizo kwangu? Hivi nikipoteza kazi, unadhani nitakuwa mgeni wa nani mimi?”



    “Acha kuwaza mambo ya kijinga...” akasema Levina akivua gauni lake jepesi la kulalia.

    “Acha kufanya hivyo Levina.”



    Levina hakusikia kitu, akalitupa mbali baada ya kumaliza kulivua na kumsogelea Deo, kisha akamsukuma kitandani. Kama mzigo Deo akaanguka kitandani na mara Levina akamzidi ujanja, dakika chache baadaye wakajikuta wakiwa kwenye kiota cha huba ya mapenzi, wakiwa wamesahau shida zote za ulimwengu.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    ***

    “Umeongea naye?” Mzee Massamu akamwuliza mkewe.

    “Ndiyo.”

    “Anasemaje?”

    “Aseme nini?”

    “Kwahiyo hajasema chochote?”



    “Simaanishi hivyo...kifupi amekataa.”

    “Amekataa?”

    “Ndiyo amekataa.”

    “Sasa kuanzia leo anza kuwafuatilia utapata majibu, tena nahisi huenda huwa wanalala pamoja usiku. Ngoja muda uende kidogo, nataka kwenda kuhakikisha mwenyewe leo.”



    “Sawa mume wangu, unajua kama itakuwa ni kweli, utakuwa mchezo mbaya sana.”

    “Siyo mchezo mbaya tu, sitaki mwanangu ajiingize kwenye matatizo. Unajua kuolewa na lofa, ni sawa na kukaribisha ulofa katika familia. Hilo siwezi kuliruhusu likatokea katika familia yangu. Siwezi kabisa.”

    “Ni kweli kabisa baba Levina...itakuwa aibu kwa familia,” akasema mama Levina akiunga mkono kauli ya mumewe.



    ***

    Saa nane na dakika zake za usiku, Mzee Massamu aliamka kitandani na kutoka nje taratibu kabisa. Akaenda moja kwa moja hadi kwenye mlango wa chumba cha Levina. Akatega sikio kusikia kama Levina alikuwa akihema ndani, lakini hakusikia kitu. Kwakuwa taa ilikuwa haijazimwa, akaamua kuchungulia kupitia kwenye tundu la ufunguo kuangalia kama alikuwemo mle ndani.



    Hakuwepo!

    Akashtuka sana.

    Akashika kitasa cha mlango na kukizungusha taratibu, mlango ukafunguka wenyewe. Mzee Massamu akaingia mpaka ndani na kuangalia kila kona, hakuona mtu! Ni kweli Levina hakuwemo ndani.

    “Shiiiti, huyu mtoto amekwenda wapi?” Akawaza.



    Papo hapo likaja wazo lingine, akahisi huenda alikuwa ameingia msalani, kwa bahati nzuri choo kilikuwa mle mle ndani. Kwahiyo akaamua kuita kwa sauti ya chini...

    “Levina...Levina...we Levina...” lakini Levina hakuitika.

    Hapo akaamua kuusogelea mlango wa chooni, akajaribu kuusukuma kwa nguvu! Ukafunguka!

    Levina hakuwepo!



    “Lazima atakuwa chumbani kwa Deo,” akawaza na kutoka chumbani kwa Levina haraka.

    Akapiga hatua za taratibu hadi kufikia mlango wa Deo. Korido nzima ilikuwa kimya kabisa. Alipoufikia mlango wa Deo alitarajia kusikia kelele za mahaba chumbani, lakini hakusikia.



    Chumba kilikuwa kimya kabisa. Hakujiuliza mara mbili, akajaribu kuusukuma ule mlango ambapo ulifunguka mara moja kwakuwa haukufungwa!

    Alihisi kuchangikiwa!

    Akahisi kuzimia!



    Alichokiona mle chumbani, ilikuwa vigumu sana kuamini. Macho yake yaliona gauni la kulalia la mwanaye likiwa chini, huku nguo yake ya ndani ikiwa juu ya kiti! Deo alikuwa amelala na mwanaye wakiwa kama walivyozaliwa!

    Alihisia harufu ya damu!

    Akatamani kuua!



    Lakini akajipa moyo!

    “Deo unamfanya mwanangu hivi?” akajisemea moyoni mwake.

    Haikuwa na maana kwao maana wote walikuwa wameishilia kwenye usingizi mzito, wakiwa kama walivyozaliwa. Busara ya Mzee Massamu ikatumika, akaamua kutoka mle chumbani taratibu na kurudi chumbani kwake. Akamkuta mkewe akiwa macho. Kwa hali aliyoingia nayo, mkewe akajua lazima kulikuwa na kitu kibaya kimetokea.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Vipi mume wangu?”

    “Nenda mwenyewe chumbani kwa Deo ukajionee.”

    “Kuna nini?”

    “Nenda mke wangu,” akasema Mzee Massamu akitoka jasho mwili mzima.





    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog