Simulizi : Usife Kwanza Mpenzi Wangu
Sehemu Ya Tatu (3)
Mzee Massamu ametoka chumbani kwa Deo na kushuhudia akiwa amelala na mwanaye Levina, akamwamsha mkewe na kumwambia aende akajionee mwenyewe chumbani kwa Deo. Nini kitatokea? Endelea...
MAMA Levina ni kama alikuwa haelewi kabisa anachoambiwa na mumewe. Alimwangalia bila kupata majibu ya moja kwa moja. Kwanini anamwambia aende akajionee mwenyewe chumbani kwa Deo.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Mume wangu, niambie tafadhali, kuna nini?”
“Nenda mama, nenda ukaoane mwenyewe!”
Mama Levina hakutaka kuuliza swali lingine zaidi, akatoka na kunyata hadi kwenye mlango wa Deo, kwa haraka za mzee Massamu, hakuufunga ule mlango, kwa hiyo mama Levina alivyotokeza tu akaona kila kitu!
Nusu azimie!
Akajikaza sana, lakini akashindwa, macho yake yakaanza kumwaga machozi. Hakutaka haraka, akaufunga ule mlango na kuwaacha waendelee na usingizi wao. akatoka haraka hadi chumbani kwao.
Huko akamkuta mumewe akiwa amejiinamia kwa mawazo tele. Mama Levina naye akaungana naye, yeye akaenda kujitupa kwenye sofa kubwa na kuyatupa macho yake juu ya dari.
Akawaza alichowaza!
Majibu hayakupatikana!
Lakini akiwa katikati ya mawazo hayo, kumbukumbu za zamani zikaanza kurejea kama sinema ya kusisimua! Akakumbuka jinsi Levina alivyomweleza kuhusu kijana wao wa kazi aliyepita, ambaye alifukuzwa baada ya kumuonesha meseji za mapenzi akimtongoza!
Ni Levina yule yule!
Iweje leo alale na kijana wa aina ile ile? Mama wa watu akawaza lakini hakupata majibu.
“Hii ni laana, huu ni upuuzi mtupu,” akajisemea moyoni mwake.
Lakini ghafla kuna kitu kilianza kuingia kichwani mwake kwa kasi ya ajabu, kwamba kuna uwezekano mkubwa Levina alimsingizia yule kijana wa mwanzoni ili aweze kupata nafasi ya kumuingiza yule kijana nyumbani kwao.
Hilo lilikuja kichwani mwake hasa kutokana na kukumbuka tukio la kumweleza Levina kwamba alikuwa amepata kijana mwingine kutoka Bagamoyo, akalipokea bila furaha. Lakini baadaye aliposikia kwamba kijana huyo amefiwa na alitakiwa kusafiri kwenda kwenye msiba, zikawa taarifa njema kwake na kumleta Deo!
Kila kitu kikafunguka kama sinema ya kusisimua. Akagundua uchafu wote alioufanya Levina.
“Shiiit! Kumbe ndiyo maana alikuwa anafanya yote yale ili aweze kuja kufanya uchafu wake na huyu mpuuzi siyo?” akawaza kichwani mwake mama Levina.
Baba Levina alikuwa kimya kabisa, hakuelewa kilichokuwa kikiendelea. Alimpenda sana mwanaye, siku zote aliamini bado alikuwa kigori, lakini kitendo cha kushuhudia uchafu wake, tena mbele ya macho yake kabisa kilimchoma sana moyo wake.
“Mama Levina...” baba Levina akaita.
“Abee mume wangu!”
“Umeona?”
“Acha tu!”
“Sasa?”
“Sasa nini tena, zaidi ya kumtimua huyo mpumbavu hapa nyumbani?”
“Sawa, tulale, hili nitalimaliza mwenyewe asubuhi!”
“Sawa mume wangu, lakini ukweli ni kwamba sijaamini kabisa kama Levina angeweza kutuabisha kiasi hiki!”
“Hata mimi pia, sina amani kabisa. Nahisi kama dunia nzima inaniangalia mimi. Huyu mtoto ametuvua nguo kabisa!”
Wakaamua kulala, lakini wakiwa na majonzi tele mioyoni mwao.
***
Mzee Massamu aliamka mapema sana siku hiyo, lakini kila alipokuwa akitaka kutoka nje, alijikuta miguu yake ikikataa kabisa. Alihisi alikuwa na hasira kali ambayo ingeweza kusababisha madhara makubwa.
Baada ya kujishauri kwa muda mrefu, akatoka hadi sebuleni huku akiendelea kufunga tai yake shingoni.
Akiwa sebuleni, akafungua pazia kuangalia nje, akamuona Deo akikatia majani ya fensi, akahisi moyo wake kwenda mbio sana.
Akaketi kwenye kiti, akachukua viatu vyake, akafunga kamba na kutoka nje. Alipofika mlangoni, akajikuta anasita kuinua mguu wake kupiga hatua nyingine.
“Deo,” akajikuta ameita.
“Naam baba,” Deo akaitika haraka na kukimbia alipokuwa amesimama mzee Massamu.
“Shikamoo baba!” akasalimia Deo.
“Mar-haba bwana, mzima?”
“Sijambo!”
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Hata mimi naona hujambo!” Mzee Massamu akamjibu.
Kwa mara ya kwanza alimuona mzee huyo akiongea naye kwa muda mrefu, tena maneno ambayo yalionekana kuwa na mafumbo ndani yake. Moyo wake ukapiga kambi!...Puuu!
“Mchezo umeshtukiwa nini?” akawaza.
“Hivi hapa ndani una mke?” swali hili likazidisha utata kichwani mwake.
“Mke?”
“Kwani umekuja kuoa au kufanya kazi?” Lilikuwa swali gumu kidogo kujibu. Akabaki anababaika akikosa cha kuongea.
“Hivi, unajua huyu Levina nimeteseka naye kwa kiasi gani?” akamwuliza tena.
Deo akanyamaza kimya.
“I’m talking to you!” akasema kwa Kiingereza, hapo ndipo Deo hakuelewa chochote kabisa.
Deo bado aliendelea kubaki kimya.
“Sikia kijana...huwa nina roho nzuri sana, lakini pia nina roho mbaya sana. Naweza kukutwanga risasi kufumba na kufumbua...naomba ndani ya dakika tano, uwe umeshaondoka hapa kwangu...haraka sana naomba ufutike!”
“Sawa mzee.”
“Ingia ndani uchukue kila kilicho chako, uondoe nuksi nyumbani kwangu!” akasema Mzee Massamu akionekana kuzidiwa na hasira.
Deo akabaki anatetemeka, hakuwa na neno lolote la kuongea, kwa hali aliyoonekana kuwa nayo Mzee Massamu, kama angeongea neno lolote, angeweza kuishia kupigwa risasi na kufa pale pale. Mzee Massamu akaondoka na kuingia kwenye gari lake, hapo Deo akaingia ndani na kuchukua nguo zake, akaondoka.
Hakumuaga Levina wala mama yake. Alijua ni kiasi gani angepata matatizo kama angefanya hivyo! Akatokomea mitaani akiwa anajuta. Usiku mmoja tu, ndiyo chanzo cha matatizo yale. Alikuwa anarudi kwenye dhiki ambayo tayari alishaisahau. Anarudi kwenye maisha yake ya mitaani!
Akaikumbuka Singida!
Alitakiwa kurudi kwao Singida!
***
Alikuwa amezama kwenye kumbukumbu ambazo zilibaki kuwa historia, Deo anaumwa, risasi zimepenyeza kwenye bega lake. Hana matumaini tena ya kufunga ndoa na mpenzi wake Cleopatra. Akiwa ameyatoa macho yake pale kitandani, sasa ameweza kumkumbuka vizuri mwanamke yule mrembo aliyekuwa amesimama.
Yes, alikuwa ni Levina!
Levina Massamu!
“Pole na kuumwa!” Levina akatamka akimkazia macho.
Deo hakujibu!
“Pole sana mwaya, kwahiyo ndoa itaahirishwa?” akauliza tena Levina.
Uso wa mwanamke huyu, ulikuwa wa upole, lakini aliachia tabasamu mwanana wakati wote alipokuwa akizungumza. Tabasamu ni kitu cha ajabu sana kwa wakati huu ambao Deo anaugulia maumivu kitandani.
Anatabasamu na wakati yeye yupo kitandani? Tena na tundu la risasi begani! Moyo wa Deo ukaingiwa ubaridi, mara akajihisi kuumia sana, machozi kama maji yakaanza kumiminika machoni mwake. Punde, akamuona mpenzi wake akija uelekeo ule. Mpenzi wake mpya ambaye alikuwa bibi harusi mtarajiwa!
Cleopatra!!!
Deo amefukuzwa nyumbani kwa mzee Massamu alipokuwa anafanya kazi, haijulikani alipoelekea, lakini upande wa pili anaonekana akiwa amelezwa hospitalini Muhimbili. Mbele yake amesimama mwanamke ambaye sasa amemkumbuka vizuri, ni Levina aliyekutana naye sokoni Tandale akiwa anauza mchele.
DEOGRATIUS aliyakodoa macho yake akiwa hajui la kufanya, akamwangalia Levina kwa umakani, lakini akiwa na maswali mengi sana kichwani mwake. Mosi, Levina alijuaje kwamba yeye anaumwa? Nani alimpa taarifa hizo?
Hata hivyo, hayo hayakuwa maswali magumu sana, swali gumu zaidi ambalo lilimchanganya kichwa chake ni akina nani wale waliompiga risasi na kwanini walifanya hivyo?
Akiwa katika maswali hayo, anamuona mwanamke mwingine akija uelekeo wa kitanda chake akitokea mlango mkubwa wa kuingilia pale wodini. Alimfahamu vizuri sana.
Ni Cleopatra!
Macho ya Cleopatra yalikuwa na wasiwasi mwingi, lakini alipokaribia yakaonesha ukali kidogo. Ukali uliosababishwa na kiumbe kilichokuwa mbele ya kitanda cha Deo.
Levina!!!
“We’ malaya unafanya nini hapa?” Cleopatra akauliza kwa sauti ya chini lakini iliyojaa ukali.
“Umeniita nani?”
“Malaya!”
“Nani?”
“Malaya!!! Kwani hujasikia au hutaki? Au hufahamu kwamba wewe ni malaya?”
“Cleopatra mimi ni malaya?”
“Tena mchafu!”
“Ok! Ahsante sana, ahsante sana mama, sikuja kwa ugomvi, nilikuja kwa ajili ya kumsalimia mgonjwa!”
“Mgonjwa?”
“Ndiyo Deo!”
“Anakuhusu nini Deo?”
“Ni boyfriend wangu wa zamani, kwahiyo sina tatizo kuja kumsalimia akipata matatizo!”
“Kwanza aliyekupa taarifa za Deo kuumwa ni nani? Tena haraka kiasi hicho?”
“Unataka kumjua?”
“Ndiyo!”
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Ipo siku utamjua, lakini kwa leo hupaswi kumjua...kwaheri...kwa mara nyingine tena Deo pole sana mwaya, najua unaumia na una maumivu mawili! Ya kuugua, lakini pia una maumivu ya kusogeza ndoa yako mbele, pole sana...” akasema Levina na kuanza kupiga hatua kuondoka pale kwenye kitanda cha Deo.
Deo hakuzungumza chochote, Cleopatra naye hakuwa na la kuzungumza zaidi ya kumsindikiza kwa macho mpaka alipopotea mbele ya macho yake. Akamgeukia Deo aliyekuwa ameyatoa macho yake kwa kukata tamaa kabisa. Akapiga magoti pale na kumbusu usoni mwake.
“Pole mwaya Deo wangu!”
“Ahsante...” akaitikia Deo kwa taabu kidogo.
“Unajisikiaje sasa?”
“Nina nafuu!”
“Utapona mpenzi wangu, naamini hadi siku ya ndoa yetu utakuwa umeshapona kabisa na utaweza kwenda kanisani kutimiza ahadi yetu ya muda mrefu!”
“Siamini Cleopatra!”
“Kwanini?”
“Nakufa Patra, nakufa mpenzi wangu!”
“Hapana baby, usife kwanza mpenzi wangu kabla hatujafunga ndoa yetu...subiri kidogo mpenzi wangu, unioe kwanza...” akasema Cleopatra akilengwa na machozi machoni mwake.
“Siamini kama nitapona mpenzi, moyo wangu una maumivu makali sana, lakini hata mwili wangu naona unauma, sioni tumaini kabisa, nakufa mpenzi wangu!”
“Hufi baba!”
“Nakufa!”
“Usife kwanza mpenzi wangu, nakupenda Deo!”
Deo hakujibu kitu, alikuwa na mambo mengi sana kichwani mwake. Alikuwa na maumivu ya kupigwa risasi, lakini pia alikuwa na maumivu na ndoa yake na Cleopatra!
Alimkumbuka sana Levina, kila alipojaribu kukumbuka sababu ya kuachana kwao, hakuona kama alistahili!
Akazidi kulia.
“Unalia nini mpenzi wangu?” Cleopatra akauliza.
“Maumivu mpenzi!”
“Pole sana!”
“Ahsante!”
“Hivi dokta ameshakuja kukuona?”
“Sijajua!”
“Namaanisha baada ya kuzinduka!”
“Hapana.”
“Ngoja niende kumwita mara moja,” Cleopatra akasema na kusimama mara moja kisha kwenda ofisini kwa daktari.
Muda mfupi baadaye daktari alikuwa ameshafika kitandani kwa Deo na kuanza kumpima na kumjulia hali yake.
“Pole sana Deo, unajisikiaje sasa?” Dokta akamwuliza.
“Kidogo nina nafuu.”
“Usijali, kilichotokea ni mshtuko tu, hujaumia sana, utakuwa sawa wala usiwe na hofu!”
“Lakini dokta kama nilivyokuambia, wiki tatu zijazo tunafunga ndoa, anaweza kuwa ameshapona kabisa?”
“Bila shaka, tutajitahidi kadri ya uwezo wetu, maadamu yupo chini yetu, kila kitu kitakuwa sawa, kikubwa ni kumuomba Mungu tu!”
“Ahsante sana, naweza kumpa chakula kwa sasa?”
“Umemletea nini?”
“Ndizi nyama!”
“Sawa, lakini hakikisha anakula chakula laini na chenye kumpa hamu ya kula. Unaweza kumpa.”
“Ahsante Dokta.”
Dokta Pallangyo akaondoka zake na kumuacha Cleopatra akiwa na mgonjwa wake. Akatayarisha chakula na kuanza kumlisha kwa upendo.
“Nakupenda sana Deo wangu, sipo tayari kukupoteza katika maisha yangu, usijali utapona!”
“Ahsante mpenzi wangu kwa kunipa moyo!”
Muda wa kuwaona wagonjwa ulipoisha, Cleopatra alitakiwa kuondoka na kumuacha Deo peke yake, jambo ambalo lilimuhuzunisha sana. Moyo wake uliumizwa sana na jambo hilo, lakini hakuwa na jinsi, alitakiwa kuondoka!
“Nitakuja kukuona mpenzi wangu, ugua pole na ulale salama.”
“Ahsante, msalimie mama!”
“Sawa, nitamsalimia.”
Akaondoka.
***
Macho yake yalikuwa yanagoma kufumbuka kabisa, alihisi kama yanauma kwa mbali, hata hivyo hakuwa na tatizo la macho, alikuwa na tatizo la bega, lakini macho yake yalikuwa yakipambana na nuru ya asubuhi baada ya kuzoea giza kwa usiku mzima.
Akajilazimisha kuyafumbua, akayafumbua kwa tabu kidogo. Alipofumbua tu, akakutanisha macho yake na sura ambayo haikuwa ngeni kwake hata kidogo. Alimfahamu vizuri sana msichana aliyekuwa amesimama mbele yake.
Alikuwa ni Levina!
“Habari za asubuhi Deo? Samahani nimekuja kukusalimia, nimefika mapema sana hapa, lakini sikuona sababu ya kukusumbua katika usingizi, ndipo nikaamua kukusubiri uamke mwenyewe...pole sana,” akasema Levina akiweka uaridi jekundu mezani kwa Deo.
“Ahsante Levina!”
“Unajua kwanini nimekuja mapema yote hii?”
Deo hakujibu kitu, alitingisha kichwa kuashiria kwamba hakujua sababu.
“Nilitaka kuwa wa kwanza kuijua hali yako baada ya kuamka leo, lakini pia nilitaka kukuthibitishia kwamba huyo Cleopatra wako hakupendi kama anavyokudanganya, kama angekuwa anakupenda asingeweza kulala usingizi ukiwa wewe unaumwa, alipaswa awahi kukuona...upo hapo?” Akasema Levina akimwangalia Deo usoni.
Deo hakujibu kitu!
Akabaki anashangaa, akiwa katika hali ya mshangao huo, akamuona Cleopatra akiwa anaingia wodini. Sekunde chache baadaye alikuwa amesimama mbele yake.
Levina amekuwa wa kwanza kufika hospitalini kumwona Deo akiwa na uaridi mkononi mwake. Anaeleza hisia zake jinsi alivyokuwa akimpenda. Akiwa amesimama pale Cleopatra akaingia wodini akitembea kwa kunyata, baadaye anafika na kusimama mbele ya kitanda chake!
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
ALIONEKANA kabisa kuchukizwa na kitendo cha Levina kufika hospitalini kumuona Deo, tena kabla yake. Akamwangalia Levina kwa macho yaliyojaa hasira sana, akabenua midomo na kurudisha macho yake kwa Deo aliyekuwa pale kitandani. Akamwonea imani.
“Lakini Levina unatafuta nini kwangu?” Cleopatra akamwuliza.
“Kivipi?’
“Hujui?”
“Nimekuuliza kivipi? Mtu anayeuliza maana yake ni kwamba hajui; mimi sijui ndiyo maana nakuuliza. Haya niambie kivipi?”
“Kwanini unakuja kumwangalia mpenzi wangu?”
“Kuna ubaya gani?”
“Ubaya upo?”
“Upi?”
Cleopatra akakaa kimya!
Ni wazi kwamba hakuwa na jibu la haraka na la moja kwa moja. Maana ni kweli hakukuwa na ubaya katika kumjulia hali mgonjwa.
“…najua unaogopa kusalitiwa? Ni kweli?” Levina akamwuliza akimwangalia usoni.
Cleopatra akaendelea kubaki kimya.
“Mbona kimya? Unaogopa nitakuibia Deo wako siyo?”
“Ndiyo!”
“Lazima uwe na woga huo….lazima…tena ni kawaida kabisa. Maana siku zote mwizi huwa na hofu sana ya kuibiwa…kwasababu wewe ni mwizi wa waume za watu, ndiyo maana unahofia nitakuibia, mwanamke huna haya kabisa…hivi unajua nilimtoa wapi Deo? Alikuwaje na nilifanya nini hadi ukamkuta akiwa katika hali hii?
“Unajua? Leo unajifanya unampenda, unajua alikuwaje kabla hajaanza kukuvutia? Unajua hali aliyokuwanayo kabla ya kuwa handsome na kupata kazi nzuri? Wewe ni mpumbavu sana mtoto wa kike.
Kwa taarifa yako sina haja na Deo tena, ninachokifanya hapa ni ustaarabu tu wa kuja kumjulia hali kama binadamu mwingine, si zaidi ya hapo. Mwone alivyo na sura ya huruma? Utadhani ni mkarimu kumbe muuaji mkubwa!” Akasema Levina kisha akashika njia ya kutokea nje.
Cleopatra akabakia akimwangalia Levina anavyoishia.
“Amekuambia nini?” Cleopatra akamwuliza Deo aliyekuwa amelala kimya kitandani.
“Amenipa pole!”
“Kingine?”
“Kaniletea ua!”
“Amesema kuwa anakupenda?”
“Hapana.”
“Wewe unahisi nini?”
“Kwakweli siwezi kujua, lakini naona kikubwa hapa ni mimi na moyo wangu. Sidhani kama nitabadilisha uamuzi wangu. Bado wewe ni wangu, nitafunga ndoa na wewe. Nakupenda sana Cleopatra, usiwe na wasiwasi na hilo mama, nakupenda sana.”
“Kweli?”
“Niamini.”
Cleopatra akainama pale kitandani kisha akamwangushia busu mwanana shavuni mwake, machozi yakaanza kumiminika kama maji.
“Naomba asikudanganye kwa lolote, nakupenda mpenzi, lazima tutimize dhamira yetu.”
“Usijali mpenzi wangu.”
Akamnywesha uji na kumpa matunda akala. Muda wa kuwaona wagonjwa ulivyoisha, akaaga na kuondoka zake.
***
Ilikuwa asubuhi mbaya zaidi kwa Deo, zaidi ya jana yake. Alikuwa akimuwaza sana Levina. Tena safari hii alikuwa akimuwaza kama mwanamke asiye na hatia. Ni kweli hakuwa na sababu za kumuacha na kutaka kuoana na Cleopatra. Kulikuwa hakuna njia yoyote ya kubadilisha kilichokuwa mbele yake, ni kweli alikuwa anakwenda kufunga ndoa na Cleopatra.
Tena wiki mbili na siku chache baadaye. Tayari ndoa ilikuwa imeshatangazwa kanisani, kwahiyo isingekuwa rahisi hata kidogo kughairi. Akayatupa macho yake juu ya dari, mawazo tele yakamjaa. Kwa hakika alimkumbuka sana Levina. Mawazo yake yakarudi asubuhi ile ya fumanizi.
Siku ambayo alifukuzwa na mzee Massamu nyumbani kwao na Levina. Akaikumbuka siku hiyo na mtiririko wa matukio mengine mengi yaliyoonesha mapenzi ya dhati kutoka kwa Levina. Matukio yale yakashuka kama sinema ya kusisimua…
Akakumbuka vizuri…
***
Kitu cha kwanza Deo kufanya alipofika Magomeni kwenye mataa, ilikuwa ni kumpigia simu Levina, lakini simu yake ilikuwa haipatikani. Akarudia tena na tena, lakini jibu liliendelea kuwa lile lile, haipatikani! Akachanganyikiwa.
Hapo akajua alitakiwa kuanza maisha yake mapya, ambayo kwa vyovyote yangekuwa ya tabu na shida nyingi! Hakuwa na jinsi ndivyo hali halisi ilivyokuwa…na alitakiwa kukabiliana nayo!
Hakuwa na kitu kingine chochote zaidi ya begi lake dogo mgongoni lililokuwa limehifadhi nguo zake. Ndani ya begi hilo, pia alikuwa na kiasi cha shilingi laki mbili na arobaini elfu, alizokuwa amezihifadhi wakati akifanya kazi ya kuuza mchele sokoni Tandale! Alikuwa na mawazo tele kichwani, huku akikosa uamuzi wa muelekeo.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Alisimama pembeni mwa sheli, karibu kabisa na geti la kuingia katika Hoteli ya Travertine. Akaangalia barabara nne, moja ya Kawawa ikitokea Ilala kwenda Kinondoni, nyingine ya Morogoro ikitokea Ubungo kuelekea Posta.
Akaanza kuwaza atumie ipi? Aende wapi? Kwa nani?
Hakuwa na majibu ya haraka ya wapi aelekee, lakini kikubwa zaidi ni kwamba, aliumizwa sana na kitendo cha kuingia kwenye mateso kwa sababu ya starehe ya usiku mmoja. Hilo lilimchoma sana moyo wake.
“Lakini nilimwambia Levina hakusikia…sasa ona sasa sina kazi, nabaki nahangaika,” akawaza Deo, lakini hilo haikuwa dawa.
Alitakiwa kujua anaelekea wapi baada ya tukio hilo. Wazo lililoingia haraka kichwani mwake ni kwenda kutafuta kwanza gesti kwa ajili ya kujibanza kwa siku kadhaa wakati akitafuta kazi. Sehemu pekee ambayo aliamini angepata chumba cha bei nafuu ni Manzese.
Akaingia kwenye gari la Ubungo, akashukia Manzese – Tip Top na kukata mitaa, akakodisha gesti ya elfu mbili kwa siku!
“Utakaa siku ngapi?” Mhudumu akamwuliza.
“Kwasasa nitakulipa elfu kumi kwa ajili ya siku tano, kama nitaendelea nitakuongeza pesa nyingine.”
“Sawa, nenda namba sita.”
“Ahsante sana.”
Deo akaondoka na kwenda kufungua mlango wa chumba namba sita kama alivyoelekezwa, akaingia na kujitupa kitandani. Mawazo tele kichwani mwake. Akiwa bado hajatulia vizuri, simu yake ikaanza kuita, akaichukua haraka, jina lilioonekana kwenye kioo, lilikuwa la Levina.
Akapokea.
“Umeridhika sasa siyo? Naamini roho yako ipo kwatu sasa…” akasema Deo kwa sauti iliyojaa hasira kwenye simu.
“Niridhike na nini Deo?”
“Kunisababisha nifukuzwe kazi? Sasa maisha yangu yameharibika kama ulivyokuwa unataka siyo?”
“Sina maana hiyo Deo, kumbuka kwamba mimi nakupenda na sipo tayari kuona maisha yako yanaharibika. Ndiyo maana nimekupigia simu, kwanza uko wapi? Nataka kukutana na wewe!”
“Kukutana na mimi?”
“Ndiyo!”
“Unataka nini kwangu?”
“Ni juu ya maisha yako. Nia yangu ilikuwa kukusaidia, bado nahitaji kukusaidia.”
Licha ya Levina kumsababishia afukuzwe kazi, bado Deo hakati tamaa ya maisha na anaendelea kujipa moyo kuwa ipo siku mambo yake yatatulia.
Levina analazimika kufanya kazi ya ziada ili kubadili fikra za Deo anayemchukulia kama mtu aliyepania kumharibia maisha yake. Baada ya kumshawishi kwa muda mrefu, Deo anakubali kukutana tena na Levina na wanajikuta wakifungua ukurasa mpya katika maisha yao. Endelea mwenyewe…
Kitendo cha kupoteza kazi kwa sababu ya mapenzi kilikuwa ni pigo lililomgharimu Deo kwa kiasi kikubwa. Kumbukumbu za yote aliyofanya na Levina ilikuwa ikipita kichwani mwake mithili ya mkanda wa sinema ya kusisimua, hakuamini kuwa kila kitu kimeharibika na kufikia mwisho kwa sababu ya mapenzi.
Wakati hayo yakiendelea kupita kichwani mwake, alikuwa akifikiria juu ya ombi la Levina kutaka kukutana naye tena.
“Unataka nini kwangu? Deo alirudia kuuliza swali lile, na majibu ya Levina yakawa ni yaleyale, kwamba alikuwa akimpenda na alikuwa tayari kumsaidia.
“Siwezi kukuruhusu unione tena, najua lengo lako ni kuniharibia maisha yangu, niache nife peke yangu ili ufurahi.”
“Usiseme hivyo Deo, lengo langu ni kukusaidia na sitokata tamaa mpaka hapo nitakapofanikiwa,” alijibu Levina kwa sauti iliyoonesha kuwa alikuwa akilia kwa uchungu. Mazungumzo kwa njia ya simu yaliendelea lakini msimamo wa Deo ukawa ule ule, hakutaka kuonana tena na Levina.
Deo akiwa amejilaza pale kitandani, aliendelea kusanifu mandhari ya chumba kile cha kulala wageni alichofikia. Kwa hakika hakuwa na hadhi ya kukaa kwenye chumba kama kile, ila kutokana na yaliyomsibu aliamua kuvumilia na kuyaacha yote yapite.
Usiku wa siku ile aliuona kama mwaka mzima kwani mpaka kunapambazuka alikuwa hajapata hata tone la usingizi. Kulipopambazuka tu, Deo aliinuka pale kitandani na kwenda kupiga mswaki, lakini kabla hajatoka, simu yake iliita tena na alipoitazama aligundua kuwa ni Levina ndiye aliyekuwa akipiga. Aliitazama simu ile bila kuipokea kwa dakika kadhaa hadi ilipokatika.
“Anataka nini kwangu? Sihitaji tena kuwa na mpenzi, bora peke yangu,” alijisemea Deo kimoyomoyo. Akiwa bado anatafakari, simu ya Levina iliingia tena, akaipokea kwa jazba…
“Si nilishakwambia uniache Levina? Sitaki uendelee kunifuatilia tafadhali,” kabla Deo hajamaliza Levina alimkata kauli…
“Najua unanichukia sana Deo kwa yaliyotokea, lakini amini nakuambia ipo siku utaelewa kuwa nina lengo zuri sana na wewe. Naomba unielekeze mahali ulipo, nina jambo muhimu sana la kukuambia ambalo ni lazima nikuambie leo,” aliongea Levina kwa hisia, jambo lililomfanya Deo arudishe moyo nyuma.
“Njoo mpaka Manzese, mwambie konda akushushe Tiptop.”
“Nakuja na usafiri binafsi, wala usihofu na nitakuwa hapo baada ya muda mfupi,” alijibu Levina kwa furaha na akaanza kujiandaa.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Jamani Deo, nisamehe kwa yote yaliyotokea, nakupenda na niko tayari kukufanyia lolote, amini kuwa sina lengo la kukuharibia maisha yako,” alianza kujitetea Levina mara baada ya kufika Manzese alikoelekezwa na Deo.
Kitendo cha kumkuta akiwa amepanga chumba katika gesti chafu, yenye mashuka machafu na kitanda kibovu huku dari na kuta zikiwa katika hali mbaya kilimuumiza sana Levina, akashindwa kuificha huzuni yake.
“Siridhishwi na wewe kuishi mahali hapa, kuonesha kuwa kweli nimepania kukusaidia nataka nikutafutie nyumba nzuri ili tupange vizuri malengo ya maisha yetu ya baadaye,” aliongea Levina huku akiwa amemkumbatia Deo.
Baada ya mazungumzo ya kina yaliyochukua muda mrefu, Deo alikubali msaada wa Levina na wakatoka kwa ajili ya kwenda kutafuta nyumba ya kupanga.
Kwa msaada wa madalali aliokuwa akifahamiana nao, walifanikiwa kupata nyumba nzuri ya kuishi maeneo ya Sinza Bwawani, wakakamilisha malipo ya kodi ya mwaka mzima iliyotolewa na Levina ‘cash’, kisha mipango ya kuhamia makazi mapya ikaanza kufanywa mara moja.
“Mimi nafikiri tukitoka hapa tukanunue kitanda na godoro zuri, kisha vitu vingine vidogo vidogo vitafuata,” alisema Levina.
“Sawa mama, mimi nakusikiliza wewe.”
Mpaka jioni ya siku ile inafika, tayari Deo alishanunuliwa vitu vyote muhimu vya kuanzia maisha vikiwemo kitanda kizuri na godoro, meza, zulia na viti. Deo akaanza maisha mapya. Angalau sasa alianza kuamini kuwa Levina alikuwa na mapenzi ya dhati kwake.
Maisha yakawa yanasonga mbele huku mapenzi kati ya Deo na Levina yakizidi kuchanua siku baada ya siku. Ikafika mahali Deo akayasahau machungu yote aliyopitia maishani mwake, akawa anazifukuzia ndoto zake zilizoonekana kupotea kwa kipindi kirefu.
“Uliwahi kuniambia kuwa una malengo ya kujiendeleza kimasomo, huoni kuwa huu ni muda muafaka,” Levina alimuuliza Deo wakiwa faragha.
“Ni kweli baby, lakini naona kama nitakuwa nakupa mzigo mkubwa sana, natamani kuja kuwa mhasibu lakini kila nikitazama naona kama kuna kazi nzito mbele yangu.”
“Wala usihofu Deo, nilishakwambia kuwa nataka kuyabadili maisha yako, amini nakwambia kuwa nitashughulikia masuala yote ya wewe kuanza masomo, cha msingi jiweke tayari.
“Hamna shida sweet, sitakuangusha.”
Siku chache baadaye Deo akaandikishwa kuanza rasmi masomo ya muda mfupi (Qualifying Test) ili kujiweka tayari kabla ya kujiunga na chuo cha Uhasibu kwani ndoto zake zilikuwa ni kuja kuwa mhasibu.
Deo akayaanza maisha mapya ya uanafunzi. Licha ya kwamba umri wake ulikuwa mkubwa, hakuona aibu kujichanganya na vijana wadogo katika masomo ya elimu ya sekondari kwa muda mfupi (QT).
Hiyo ilimpa nguvu kubwa kwani hatimaye alikuwa akielekea kutimiza ndoto zake za siku nyingi kwa msaada mkubwa wa Levina.
Aliahidi kumpenda na kumfanyia mema Levina kwani aliyoyafanya kwa ajili yake hayakuwa na kifani.
Deo na Levina wameanza ukurasa mpya wa maisha yao ya kimapenzi kiasi cha kusahau yote yaliyowahi kuwasibu. Kwa msaada mkubwa wa Levina, Deo anaanza maisha mapya akiwa katika makazi mapya na anajitahidi kuzifukuzia ndoto zake, hasa ya kusoma na kupata kazi, lakini ghafla mambo yanaanza kubadilika. Shuka nayo…
Deo aliendelea na masomo ya kujiendeleza na akawa anaonesha juhudi kubwa katika kila anachokifanya. Alijiapiza kuwa ataendelea kumpenda na kumheshimu Levina kwa maisha yake yote kwani alimbadilisha kabisa.
Kutokana na juhudi alizozionesha kwenye masomo, haikumchukua muda Deo akawa na uwezo wa kufanya vizuri mitihani na kujibu maswali kwa ufasaha mkubwa, hali iliyomfanya awe kivutio kikubwa kwa wanafunzi wenzake.
Wasichana wengi walianza kumshobokea na kujifanya wanataka awafundishe. Kwa kuwa alishajiwekea nadhiri ya kutomsaliti Levina, alikaa nao mbali.
Maisha yalizidi kusonga na hatimaye Deo akamaliza masomo yake kwa mafanikio makubwa. Alifaulu vizuri mtihani wake na kupata vyeti vilivyomuwezesha kujiunga na Chuo cha Uhasibu cha Planet Link Accountancy ambako alisomea stashahada ya uhasibu.
Kwa kipindi chote hiki maisha ya kimapenzi kati yake na Levina yalikuwa yakizidi kupamba moto siku baada ya siku.
“Deo malengo yako si yanakaribia kutimia? Bila shaka haitakuwa vibaya tukianza kufikiria kujenga familia yetu, au unasemaje?”
“Ni kweli sweet, lakini kwanini tusisubiri nimalize kabisa halafu nikishapata kazi ndiyo tuanze kufikiria hayo?”
“Unajua mimi ni mwanamke niliyekamilika, siwezi kuendelea kukaa hivihivi, wenzangu wataanza kunicheka kwamba sizai, mi nataka nikuzalie mtoto wakati wewe unaendelea na masomo yako,” alisema Levina kwa sauti ya mahaba akiwa amejilaza kifuani kwa Deo.
Licha ya Deo kukwepakwepa, lakini hatimaye aliukubali ushauri wa Levina, wa kutafuta mtoto wa kuupamba uhusiano wao.
“Lakini huoni kwamba litakuwa tatizo kuzaa kabla hatujafunga pingu za maisha,” alihoji Deo huku akizichezea nywele za Levina wakiwa kitandani.
“Sidhani kama hili litakuwa tatizo, nimehiyari mwenyewe na hakuna wa kunizuia. Nakupenda sana Deo.”
***
MIAKA MITATU BAADAYE
Deo alifanikiwa kumaliza salama masomo yake na kupata kazi kama mhasibu wa Kampuni ya Usafirishaji Mizigo ya Snox Carries LTD ya jijini Dar es Salaam. Kwa upande wa Levina tayari alishajifungua mtoto wa kike aliyekuwa na umri wa mwaka mmoja na miezi kadhaa, waliyempa jina la Precious wakiwa na maana ya kitu cha thamani.
Baada ya kupata mtoto, maisha yalibadilika sana na sasa wakawa wanatumia muda mwingi kumuhudumia na kumfikiria mtoto wao kuliko wanavyojijali wao.
Deo alikuwa akirudi nyumbani kutoka kazini anamsaidia mkewe malezi ya mtoto wao Precious. Pesa walizopata walizitumia pamoja kufanya mambo mbalimbali ya kimaendeleo. Maisha yao kwa ujumla yalibadilika na usingeweza kudhani kuwa huyu ndiye Deo wa miaka ile.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Levina! Nadhani sasa wewe ni mke wangu na nina mamlaka yote juu yako na wewe una mamlaka juu yangu,” aliongea Deo jioni moja wakiwa wanapunga upepo kwenye bustani ya maua nje ya nyumba wanayoishi.
“Ni kweli mume wangu!”
“Lakini mbona siku hizi hutaki mimi niguse simu yako kama zamani, unapigiwa simu usiku halafu unaenda kupokelea nje na wakati mwingine unaikata mbele ya macho yangu, tatizo nini?”
“Wewe nawe kwa wivuu! Hakuna anayekuzidi mume wangu kwa kila kitu, siwezi kutoka nje na kukusaliti, amini nakwambia Deo, mimi ni wako peke yako…” alisema Levina huku akimsugua sugua mumewe mgongoni kimahaba.
Licha ya kujibiwa hivyo, Deo alibaki na dukuduku moyoni kwani mabadiliko ya mkewe yalishaanza kumtia hofu. Tangu mkewe aache kunyonyesha miezi michache iliyopita, alianza tabia za ajabu ambazo zilimfanya ahisi anaibiwa mali zake. Mkewe alikuwa akichelewa kurudi nyumbani bila sababu za kueleweka, na alipokuwa akimuuliza kisingizio kikubwa kilikuwa ni ubize wa kazi.
Siku nyingine alikuwa akirudi nyumbani ananukia pombe, hali iliyotoa ishara kuwa tayari mwenzake anamsaliti. Shughuli zote za kumlea mtoto zikabaki kwa Deo na msichana wa kazi aliyetafutwa kwa lazima baada ya kuona Levina ameanza kubadilika. Ilifika mahali hata suala la kufurahishana faragha likaanza kupungua taratibu.
“Najua umenisaidia sana maishani Levina, Bila wewe nisingekuwa hapa nilipo leo, lakini kaa ukitambua kuwa mabadiliko yako ya tabia unayonionesha kwa sasa yanauumiza sana mtima wangu.
“Kama kuna kosa nililokuudhi niambie na naahidi nitajirekebisha kwani bado nakuhitaji Levina wangu.” Uzalendo ulishaanza kumshinda Deo, ikafika mahali akawa anamwaga machozi mbele ya mkewe akimsihi ajirudi kama alivyokuwa hapo mwanzo.
Jibu la Levina siku zote lilikuwa ni kwamba anampenda Deo na kamwe hawezi kumsaliti, lakini kumbe nyuma ya pazia alikuwa akimfanyia mambo ya kusikitisha sana.
Usiku mmoja, Deo akiwa na mwanae mdogo Precious sebuleni, mkewe alichelewa kurudi, na hata aliporudi saa tano usiku alikuwa akipepesuka na kunuka pombe. Alipoingia ndani, aliweka simu yake mezani na kupitiliza bafuni kwenda kuoga.
Akiwa bafuni, ujumbe mfupi wa simu uliingia kwenye simu yake, Deo akaiwahi na kuichukua kutaka kujua ni nani aliyemtumia meseji mkewe usiku wote ule.
Alipoifungua na kuisoma, hakuamini macho yake…akarudia kuisoma tena… akajikuta mwili wote ukiishiwa nguvu. Wakati anaisoma kwa mara ya tatu, mkewe akawa anatoka bafuni. Macho yao yakagongana.
Baada ya Deo kufukuzwa nyumbani kwa akina mzee Massamu Magomeni, ameamua kwenda kuanza maisha mapya katika gesti moja iliyopo Manzese Tip Top. Levina amewasiliana naye na amefika hadi kwenye gesti hiyo ambapo ameonesha nia yake ya kumsaidia.
Tayari ameshampangia nyumba yenye vyumba viwili, Sinza. Deo amesoma elimu ya sekondari kwa miaka miwili na baada ya hapo akasomea masomo ya Uhasibu katika chuo kimoja jijini Dar.
Akiwa anaendelea na masomo, Levina anamweleza Deo nia yake ya kuzaa mtoto, lakini jambo hilo Deo anapingana nalo. Je, nini kitatokea? Endelea...
SUALA la kuzaa na Levina lilikataa kabisa kupenya kwenye ubongo wa Deo, alijaribu kuvuta picha ya miaka mitatu ijayo akaona hatari kubwa kuzaa na Levina. Hakujua ilikuwaje, lakini akahisi kwamba Levina angeweza kubadilika na kumsababishia jakamoyo la mapenzi moyoni mwake.
Aliona kuzaa naye, ingekuwa tiketi ya kuingia kwenye matatizo, lakini pia aliona wazi vita iliyokuwa mbele yake ikimuhusisha yeye na wazazi wa Levina. Hilo hakutaka kabisa litokee.
“Levina haiwezekani, kama nilivyokuambia siwezi kuzaa na wewe!”
“Kwanini unanifikiria vibaya lakini?”
“Vipi?”
“Kwamba nitakusaliti?”
“Ni kweli, lazima baadaye utanigeuka na kuninyanyasa.”
“Kwanini unahisi hivyo?”
“Lakini kwani ni vibaya kukueleza hisia zangu? Nilichokifanya ni kukueleza nilichokuwa nahisi kichwani mwangu. Sijui kwanini sina amani na wewe, nahisi matatizo tupu kuendelea na wewe katika uhusiano huu tena na kuzaa.”
“Mh! Siamini kama huniamini kwa kiwango hicho?”
“Siyo hivyo Levina, nawajua wanawake mimi, tena wale wanaotoka kwenye familia za kitajiri.”
“Unajua nini sasa?”
“Sikiliza nikuambie Levina, wewe mpaka sasa hivi unaishi kwenu na unatambua kabisa kwamba nilifukuzwa kwenu baada ya kugundulika nina uhusiano na wewe, unadhani baba yako akigundua kwamba una mimba yangu itakuwaje?”
“Lakini atakayekuwa amebeba mimba ni mimi au yeye?”
“Ni wewe ndiyo, lakini atakayepata matatizo ni mimi!”
“Basi tuachane na hayo mpenzi wangu, tatizo si kuhusu mtoto tu siyo?”
“Ndivyo!”
“Basi huo mjadala tuukatishe kwasasa tusiharibu penzi letu kwa jambo dogo, mambo mengine tutajua baadaye!”
“Sawa.”
“Enhee lini sasa utakuja kulala kwangu?”
“Kwahiyo ndiyo unanifukuza au?”
“Sina maana hiyo, muda utakaoondoka, si vibaya lakini hata nikikuambia muda huu. Hapa ni kwako mama.”
“Ahsante sana mpenzi kwa maneno yako matamu!”
“Nakupenda sana Levina wangu!”
“Nakupenda pia Deo!”
“Lakini bado hujaniambia ni lini utakuja kulala kabisa hapa?”
“Mh! Mpaka nipange safari ya uongo...acha nifikirie kwanza nitakujulisha mpenzi wangu!”
“Sawa mama!”
Waliendelea na mazungumzo hadi saa mbili za usiku, ndipo Levina alipoondoka Sinza kuelekea nyumbani kwao Magomeni.
***
Usiku mzima Deo aliendelea kufikiria kuhusu Levina, alishindwa kuelewa ni kwanini mawazo yake yalienda mbali kiasi kile. Hakujua ni kwanini aliwaza kusalitiwa na mwanamke ambaye amekuwa chachu ya mafanikio yake.
Hata hivyo, alijitahidi kuubembeleza usingizi hadi alipofanikiwa kulala.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/-
***
Levina aliendelea kuwa msada mkubwa sana katika maisha ya Deo. Alimsaidia kwa kila kitu kwa siri, alifanya uhusiano wao kuwa siri kubwa, kwani wazazi wake wasingekubali awe katika uhusiano naye wakati hali ya maisha yake ikiwa chini sana.
Alihakikisha anaendelea kufanya kazi kwa bidii, mtaji wake haushuki na badala yake faida inazidi kuongezeka. Jambo hilo lilizidi kuwafurahisha wazazi wake, kwani alionekana msichana mwenye bidii kubwa katika kazi zake.
Siku moja aliamua kuvunja ukimya kwa kuamua kumshirikisha mama yake kuhusu uhusiano wake na Deo. Ilikuwa kazi ngumu sana lakini ilikuwa lazima amweleza ukweli ili kujua kama mama yake angemuunga mkono. Ilikuwa Jumamosi, ambapo mzee Massamu alikuwa kazini.
“Mama kuna kitu nataka kukuambia muda mrefu sana lakini nashindwa, ila naona leo ni muda muafaka wa kukuambia.”
“Ni nini mwanangu?”
“Mama nina mpenzi ambaye nataka kumtambulisha hapa nyumbani.”
“Umeanza lini tena hayo mambo mwanangu?”
“Lakini muda umefika mama, umri wangu unaniruhusu!”
“Sawa, ni nani huyo mwanaume mwenyewe!”
“Unamaanisha nini?”
“Ni wa hapa mtaani kwetu?”
“Hapana!”
“Ni wa wapi?”
“Kwasasa anaishi Sinza.”
“Sawa, kama ni kijana mwenye heshima zake na mmependana, mwambie atume ujumbe wa wazee tutawasikiliza, lakini chunga asije kuwa ni mzururaji asiye na mpango mzuri na maisha yako ya baadaye!”
“Hapana si mzururaji, lakini sidhani kama mtamkubali!”
“Kwanini?”
“Ni Deo mama!”
“Deo?”
“Ndiyo!”
“Deo gani?”
“Yule aliyekuwa akifanya kazi hapa nyumbani?”
“Wewe una kichaa kabisa, baba yako hawezi kukubaliana na hilo jambo, yaani unataka kuolewa na houseboy?”
“Hapana si houseboy tena, sasa anamalizia masomo yake ya Uhasibu!”
“Lini alianza kusoma?”
“Tangu kipindi kile, nilikutana naye akasema kwamba kuna mfadhili amejitolea kumsaidia, ndiyo huyo anayemlipia mpaka sasa hivi!”
“Kwa ninavyomjua baba yako, sijui kama atakubaliana na wewe.”
“Ndiyo maana nimeoomba msaada wako mama, nampenda sana Deo!”
“Nitajaribu kuongea naye, ingawa sina uhakika kabisa kama atakubaliana na jambo hili!”
“Nisaidie mama!”
“Nitajaribu!”
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment