Simulizi : Viganja Mashavuni Mwangu
Sehemu Ya Nne (4)
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kidogo moyo wa Edmund ukajisikia amani, akahisi kwamba alifanikiwa kwa asilimia mia moja kufanya jambo lile lililompa uhakika kwamba mbaya wake, Walter alikufa katika gesi ile kali.
Akaondoka hospitalini hapo, njiani, redioni ni taarifa za mapacha hao ndizo zilzokuwa zikisikika kila kona kwamba walikuwa wamekufa. Wakati dunia ikihuzika na kulia, kwake hali ilikuwa ni tofauti kabisa kwani moyo wake ulikuwa na furaha kupita kawaida.
Alipofika nyumbani, hakutaka kubaki mahali hapo, ilikuwa ni lazima kuondoka nchini humo kwa kuamini kwamba mara baada ya kugundulika ilikuwa ni lazima kutafutwa kila kona. Akachukua baadhi ya vitu vyake na kuondoka zake huku lengo lake kubwa likiwa ni kuelekea nchini Ireland ambapo aliamini kwamba huko angeishi kwa amani kabisa.
Kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kumpigia simu rafiki yake, Thom na kumshukuru huku akimwambia kwamba alikuwa akijiandaa na safari ya kuelekea nchini Ireland.
“Nimefanikisha. Nashukuru sana,” alisema Edmund, akachukua begi lake lililokuwa na baadhi ya vitu na kuondoka mahali hapo.
Akaingia ndani ya gari lake, akaliwasha, hakutaka kuaga, alipoingia barabarani tu, akasikia ving’ora vya polisi kwa mbali, akapishana nao, yaani wakati yeye akiondoka nyumbani kwao, nao ndiyo walikuwa wakiingia.
“Hamuwezi kunipata!” alisema Edmund huku akitoa tabasamuu pana ambapo alipokuwa akiangalia nyuma kupitia kioo cha gari cha pembeni, akawaona polisi wakiingia katika eneo la nyumba yao. Akaongeza gia na kukanyaga moto. Akapotea eneo hilo.
*
Ilikuwa ni lazima kuondoka kuelekea nchini Ireland, hakutaka kuonekana kwa kuhisi kwamba ilikuwa ni lazima kutafutwa na polisi kwa kile alichokuwa amekifanya. Edmund hakuwa na uhakika kama angegundulika, hakuwa ameziona kamera ndogo za CCTV zilizokuwa zimefungwa kila kona hospitalini hapo.
Aliendesha gari lake kwa mwendo wa kawaida kabisa, hakutaka kushtukiwa na polisi ambao mara nyingi magari yao yalikuwa mitaani yakitembea huku na kule kuhakikisha usalama kila kona hapo London.
Wazo lake kwa wakati huo lilikuwa ni kwenda Olympia London ambapo huko angenyoosha moja kwa moja mpaka Twickenham, huko angepumzika kidogo kabla ya kuelekea katika Jiji la Reading, angeingia Swindon, Bristol ambapo hapo angechukua treni ya chini ya maji mpaka nchini Ireland.
Akaliingiza gari mpaka katika Barabara ya Brixton na kuanza kuelekea Upande wa Kusini huku lengo lake likiwa ni kufika West Noorwood ambapo hapo angechukua barabara nyingine ya Tooting Bec ambayo ingempelekea Upande wa Mashariki mpaka Battersea, huko angechukua Barabara ya S Circular ambayo ingempeleka mpaka Twickenham.
Kuanzia hapo Camberwell alichukua saa tatu mpaka kufika huko. Kila alipopita, hakukuwa na tatizo lolote lile, alihisi kwamba hakukuwa na mtu yeyote aliyekuwa akimfuatilia. Hapo Twickenham akaendelea mbele na baada ya saa moja akafika Felthman ambapo hapakuwa mbali kutoka katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Heathrow.
Hapo ndipo kulipokuwa na barabara mbili zilizoungana, moja ilikuwa ikienda upande wa Kaskazini ambayo ilikwenda mpaka Harmodsworth ambapo kama angekata kulia basi angekwenda mpaka Dorney na kushuka kwa kuelekea chini.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Ilikuwa ni njia ndefu ambayo aliamini angetumia zaidi na saa tano. Kwake, njia hiyo haikuwa salama hata kidogo, kwa kukubali kwenda huko kulimaanisha kwamba ilikuwa ni lazima angekamatwa na polisi kama tu wangekuwa wakimtafuta kwa kuwa barabara hiyo haikuwa mbali na uwanja wa ndege.
Akaamua kuichukua Barabara ya ya Engham ambayo ilimpeleka mpaka Thorpe alipokutana na barabara nyingine ambayo ndiyo ilikuwa ikimpeleka mpaka Bristol.
Katika kila njia alizopita kulionekana kuwa na nafuu kwake, na kwa sababu ilikuwa ni siku ya Jumamosi, siku ambayo mashabiki wa timu za mipira, raga na kriketi walikuwa wakienda viwanjani, njiani alikuwa akipishana na watu wengi kiasi kwamba kwa mhalifu kama yeye ilikuwa rahisi sana kwenda bila kukamatwa.
Aliendesha gari mpaka katika kituo cha mafuta cha Shell ambapo haraka sana akateremka na kuchukua kadi yake, akaiingiza katika kitundu kidogo, akaandika lita alizotaka na kuweka mpitra katika mdomo wa gari lake, akajaza, akaichukua gari lake na kuondoka mahali hapo.
Wakati hayo yote yakiendelea, hakujua kama alikuwa akitafutwa na polisi. Wakati akikaribia Bristol ndipo alipoamua kufungua redio kusikiliza kilichokuwa kikiendelea. Katika kila redio taarifa ambayo ilikuwa ikitangazwa sana ilikuwa ni kuhusu tukio lile lililotokea hospitalini.
Alisikiliza kwa makini, alitaka kujua kama mapacha hao walikufa au la. Kila aliposikiliza, alisikia kwamba walikuwa kwenye hali mbaya m,no ambapo muda wowote ule wangefariki dunia.
Hakuhuzunika, ndiyo kwanza akafurahia kwa kuona kwamba alimkomoa na kama kukosa basi wakose wote. Wakati akiendelea kusikiliza ndipo akapokea taarifa kwamba tayari mtu aliyefanya tukio hilo alijulikana, na mpaka jina lake likatajwa.
Hakushangaa kwani hata alipoondoka nyumbani aliwaacha polisi wakiingia hapo. Aliendelea mbele mpaka kufika Bristol huku akiwa amechoka. Wazo lake kwa kipindi hicho lilikuwa ni kuendelea na safari kwa gari lake mpaka katika kituo cha treni cha Bristol Packway.
Akalipaki gari lake nje ya kituo hicho katika sehemu husika na kisha kuelekea ndani. Alipoanza kushusha ngazi, kitu cha kwanza kabisa alichokutana nacho kilikuwa ni picha zake nyingi zilizobandikwa kwenye kuta mbalimbali.
Alishtuka, hakuamini kama kwa saa chache angekuwa kwenye kila kona nchini Uingereza. Haraka sana akafungua begi lake, akatoa kofia yake nyekundu na kuivaa, baada ya hapo akaanza kutembea kwa kujiamini mpaka sehemu kulipokuwa na watu wengi ambapo walikuwa wakiweka sarafu kwenye kifaa kimoja na chuma kujifungua.
Alipofika, naye akaweka, chuma kikapanda na kuingia ndani. Kwa mwendo wa haraka sana akaanza kuelekea kulipokuwa na watu wengi waliokuwa wakisubiri treni na kusimama hapo.
“Treni itafika baada ya dakika chache, ndiyo inaondoka katika kituo cha Reading, baada ya dakika chache itaingia mahali hapa,” ilisikika sauti nyororo ya msichana kwenye spika zilizokuwa humo.
Moyo wake ulikuwa ukimuomba Mungu, alitaka kuondoka mahali hapo salama kwani kama angeendelea kubaki nchini Uingereza ilimaanisha kwamba huo ndiyo ungekuwa mwisho wake.
Wakati akiwa amesimama mahali hapo, akasikia watu waliokuwa nyuma yake wakilizungumzia suala la mapacha wale kupuliziwa gesi ndani ya gari. Akajificha zaidi lakini ghafla watu wale wakanyamaza kana kwamba waliambiwa wanyamaze, wakati akijiuliza kuhusu ukimya huo wa ghafla, akashtukia akishikwa bega kwa nyuma na kutakiwa kugeuka.
“Turn around, please...” (geuka tafadhali) ilisikika sauti ya mwanaume mmoja nyuma yake.
****
Catherine alikuwa akilia, hakuamini kilichokuwa kimetokea, kitendo cha kuambiwa kwamba rafiki yake, Walter alikuwa amepuliziwa gesi yenye sumu moyo wake ulimuuma mno na kumfanya kulia kila wakati.
Alijiona kuwa yeye ndiye mtu aliyesababisha lile lililotokea, alijihukumu moyoni mwake na muda wote alikuwa akiwaambia wazazi wake kwamba yeye ndiye alikuwa chanzo kwani bila yeye aliamini mapacha hao wasingeweza kupata tatizo walilokuwa wamelipata.
Kwa kuwa alikuwa akijisikia nafuu, hakutaka kubaki katika chumba kile alicholazwa, aliomba sana aende katika chumba walichokuwa mapacha wale ili aone walikuwa wakiendeleaje. Hilo lilikuwa gumu kuruhusiwa kwa kuwa tangu tukio la kupuliziwa gesi iliyokuwa na sumu hakukuwa na mtu yeyote aliyeruhusiwa kuingia ndani ya chumba kile.
Kila kona duniani ni stori za mapacha hao ndizo zilizokuwa zikisikika. Watu waliichukua picha ya Edmund na kuiweka katika mitandao ya kijamii, Watanzania hawakuwa nyuma, wao ndiyo walikuwa watu wa kwanza kuichukua picha hiyo na kuisambaza kwa nguvu zote kwani hakukuwa na mtu aliyehitajika mikononi mwa polisi kama ilivyokuwa kwa Edmund.
Mbali na mapacha hao, Walter na Walker pia wazazi wao walikuwa hoi kitandani. Tangu walipolazwa, mpaka inaingia siku ya pili hakukuwa na yeyote aliyerudiwa na fahamu.
Mapigo ya mioyo yao ilikuwa ikidunda kwa mbali sana hali iliyoonyesha kwamba muda wowote ule watu hao wanne wangefariki dunia.
Wakati hayo yote yakiendelea, tayari taarifa za kwanza zilionyesha kwamba polisi walikwenda nyumbani kwa Edmund siku ileile lakini hawakufanikiwa kumpata na hivyo kuhitaji msaada wa kamera za CCTV. Ilikuwa vigumu kumpata kwa siku hiyo kwa kuwa tu mitaani kulikuwa na idadi ya watu wengi kutokana na Jumamosi kuwa siku ya mechi mbalimbali nchini humo.
Picha zilipigwa, gari lake lilionekana sehemu nyingi likipita, hawakujua mahali lilipokuwa likielekea lakini baada ya kufika Bristol, hakukuwa na mtu aliyejua mahali gari hilo lilipokuwa.
“Lilikwenda wapi?” aliuliza jamaa mmoja.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Hatujui! Au aliondoka kwenda kwenye kituo cha treni kupanda treni?” aliuliza mwanaume mwingine.
“Ni vigumu! Inawezekanaje ukatafutwa halafu ukaenda kupanda treni? Hakuna kitu kama hicho,” alisema mwanaume mwingine kabisa.
Kila mtu hakujua mahali alipokuwa Edmund, alionekana kama mzimu kwani kwa nchi kama Uingereza ilikuwa vigumu sana kumkosa mtu aliyekuwa akitafutwa kutokana na teknolojia yao kuwa juu sana.
Mpaka inafika wiki ya kwanza, hakukuwa na mtu aliyejua mwanaume huyo alipokuwa. Kila mmoja akajiuliza kwamba kama mwanaume huyo aliondoka nchini Uingereza, alipitia wapi mpaka kwenda kwenye nchi nyingine? Kila walipojiuliza, walikosa majibu.
Polisi walikuwa wakihangaika kila kona kumtafuta Edmund ambaye mpaka muda huo hawakujua mahali alipokuwa. Kwenye kamera zao, waliliona gari lake lakini baada ya muda likawapotea. Wakahakikisha wanaweka ulinzi kila kona kuhakikisha mwanaume huyo hatoki kuelekea sehemu yoyote ile.
Polisi waliokuwa katika Kituo cha Treni cha Bristol walikuwa wametulia kuhakikisha ulinzi unakuwa salama mahali hapo. Walimwangalia kila mtyu aliyepita ili kuona kwamba ni lazima wahakikishe kwamba ndani ya kituo hicho, mwanaume huyo haingii kabisa kwani kama wangemkosa mahali hapo na kuondoka kuelekea nchi nyingine basi wasingeweza kumpata tena.
Wakiwa hapo, ghafla polisi wawili wakamuona mwanaume ambaye kwa muonekano alifanana kabisa na Edmund japokuwa alijaribu kuvaa kofia ambayo aliamini kwamba ni lazima ajifiche na asionekane kwa watu wengine.
Hawakutaka kuchelewa, wakaanza kumfuata kule alipokuwa. Kwa jinsi alivyokuwa akitembea huku akiangalia huku na kule, ikawapa uhakika kwamba mwanaume huyo alikuwa Edmund, na alipokwenda na kusimama sehemu kwa ajili ya kupanda treni, wakasimama kwa mbali nyuma yake na kuanza kumwangalia vizuri.
“He is the one, let’s arrest him,” (ndiye yeye, tukamuweke chini ya ulinzi) alisema polisi mmoja.
Wakaanza kumfuata, walipomkaribia, mmojawapo akamshika begani kwa lengo la kumtaka ageuke ili kama ni yeye basi wamuweke chini ya ulinzi lakini kama si yeye, wamuombe radhi.
Edmund alihisi kabisa mtu aliyemshika bega kwa nyuma alikuwa akimfahamu na ndiyo maana aliamua kumfuata na kumtaka ageuke ili atambulike na kukamatwa.
Wakati mapigo ya moyo yakimdunda kwa nguvu tena huku akitetemeka, mara zikaanza kusikika kelele kutoka kwa binti mmoja aliyetoka chooni, alikuwa akikimbia kwa mwendo wa kasi.
“A bomb....a bomb...” (bomu...bomu...) alisema msichana huyo huku akikimbia kutoka chooni.
Vichwa vya Waingereza wengi vilikumbuka tukio ambalo lilitokea mwezi uliopita jijini Manchester ambapo kituo cha treni kililipuliwa kwa bomu lililowekwa na Waarabu kutoka Mashariki ya Kati. Waliposikia hivyo, hakukuwa na mtu aliyebaki, kila mmoja akaanza kukimbia kwa hofu kuyaokoa maisha yake. Pale polisi wale waliposimama, wakashtukia wakikumbwa na watu waliokuwa wakikimbia, walipoinuka, Edmund hakuwepo, naye aliungana na watu wengine kukimbia.
Ilikuwa ni balaa ndani ya kituo hicho, watu wakatawanyika, si wale wanaosimama kwenye kizuizi, bali kila mtu aliyekuwa ndani ya kituo hicho ambao walikuwa ni zaidi ya elfu tatu, walikimbia kuelekea nje.
Edmund hakutaka kurudi, pale alipofika, akalikuta gari lake lakini hakutaka kulifuata, akahisi kwamba kulikuwa na watu waliokuwa wakilifuatilia na kutaka kuona ni mtu gani ambaye angeingia ndani ya gari hilo.
Alichokifanya ni kutembea kwa mwendo wa kasi huku watu wengine wakiendelea kukimbia hovyo. Alipofika umbali fulani, akasimamisha teksi, akaingia na kuondoka.
“Kuna nini?” aliuliza dereva teksi, alishangaa kuona watu wakikimbia huku na kule.
“Kuna bomu!”
“Kuna bomu! Wapi?”
“Kituoni!”
“Acha utani!”
“Kweli! Kuna bomu humo!”
Edmund akamshukuru Mungu kwa kumuwezesha kuondoka salama katika kituo kile pasipo kugundulika. Safari iliendelea, alipokuwa akielekea, hakupajua, wakati mwingine alijisikia kumwambia dereva kwamba wazunguke tu mpaka pale ambapo giza lingeingia.
Wakati wakiwa wanaendelea kuzunguka ndipo akapata wazo kwamba aondoke mpaka nchini Ireland kwa kutumia gari kwani wangepitia katika daraja kubwa lililokuwa likipita kutoka Uingereza mpaka Wales ambapo huko kusingekuwa na kazi kubwa ya kwenda huko.
Wazo hilo lilionekana kufaa, akamwambia dereva kwamba walitakiwa kuanza safari ya kuelekea nchini Wales kitu ambacho hakikuwa na ugumu hata kidogo.
“Kwa hiyo twende Wales?”
“Ndiyo! Twende huko!” alijibu Edmund.
Hakukuwa na tatizo lolote lile, katika muunganiko wa Uingereza, pia kulikuwa na nchi nyingine kama Scotland na Wales ambapo kwa Muingereza kwenda huko hakuhitaji viza kwa kuwa ilionekana kama kutoka sehemu moja na kwenda nyingine.
Ilikuwa ni safari ndefu lakini Edmund hakutaka kujali. Muda wote ambao safari ilikuwa ikiendelea, masikio yake yalikuwa katika redio aliyokuwa akiisikiliza humo garini. Hakutaka kupitwa na wakati, ilikuwa ni lazima kufuatilia kila kitu kilichokuwa kikiendelea ili ajue msako mkubwa wa kumtafuta yeye ulikuwa ukifanyika mahali gani.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Baada ya saa tano, saa mbili usiku wakafika katika eneo ambalo ilikuwa ni lazima magari yaangaliwe kama kulikuwa na kitu cha hatari ambacho kilikuwa kikitoka nchi moja kwenda nyingine.
Hapo kulikuwa na msururu mkubwa wa magari na yote ambayo yalikuwa yakiingia nchini Wales ilikuwa ni lazima kupekuliwa kwanza. Hapo, Edmund akawa na hofu, akahisi kabisa kwamba angeweza kuonekana kitu kilichomfanya kuanza kuzungumza na dereva yule.
“Ninahitaji kupita hapa salama,” alisema Edmund huku akimwangalia dereva huyo.
“Hakuna tatizo! Hatujabeba kitu cha hatari, tunapita bila tatizo lolote lile,” alisema dereva yule kwa kujiamini.
“Najua! Ila hatuwezi kufanya kitu chochote tukapita salama?” aliuliza Edmund.
“Hapa lazima tupite salama! Mbona unakuwa na wasiwasi sana?”
“Yeah! Nataka unifiche. Unajua ninatoroka nyumbani!”
“Kivipi?”
“Baba yangu kanizingua. Ninakwenda kuonana na mpenzi wangu. Familia yetu ni Wazungu, mchumba wangu ni mtu mweusi. Baba hataki niwe naye, amenizuia, nimetoroka nyumbani na ninajua tu kwamba ametuma polisi kunitafuta ili wanirudishe nyumbani kwani hapendi kweli ngozi nyeusi,” alidanganya Edmund.
“Baba yako nani?”
“Steven Powell.”
“Huyu mkuu wa jeshi la polisi?”
“Ndiyo! Naomba unisaidie nipite salama. Sitaki kurudi nyumbani, ninampenda Vanessa, naomba unisaidie katika hili nivuke salama,” alisema Edmund huku akionekana kuomba sana. Na kwa sababu dereva alikuwa na roho nzuri kama papa Francis, akakubaliana naye kwamba iwe isiwe ilikuwa ni lazima kumvusha salama mahali hapo.
“Mom! Where are we?” (mama! Tupo wapi?) lilikuwa swali la kwanza kabisa alilouliza Walter kwa sauti ya chini kabisa.
Aliyafumbua macho yake, mbele yake alisimama mwanamke mnene, aliyevalia nguo nyeupe ya kinesi, kutokana na kutokuona vizuri, hakujua kama mwanamke huyo hakuwa mama yao, alimfananisha.
Mwanamke huyo hakuzungumza kitu zaidi ya kutoka na kwenda kumuita daktari. Walikuwa wamekaa kwa wiki moja hospitalini hapo na hawakuwa wamerudiwa na fahamu kitu kilichoonekana kuwa kibaya kwa afya yao.
Nesi yule hakuchukua muda mrefu, akarudi chumbani hapo akiwa na daktari ambaye uso wake ulionyesha tabasamu pana kwani hakuamini kama vijana hao wangeweza kuyafumbua macho yao, kila mmoja alikata tamaa na kuhisi kwamba huo ndiyo ungekuwa mwisho wao.
“Where are we?” (tupo wapi?) aliendelea kuuliza Walter huku akiangalia kwa macho yake mazito.
Kwa kuwa bado hali zao hazikuwa nzuri, daktari akaagiza wawekewe dripu iliyokuwa na dawa ya Morphometip ambayo ilikuwa na kazi ya kuyaamsha zaidi mapigo yao ya moyo. Kidogo baada ya kuwekewa dripu hiyo, wakapata nguvu na hapohapo Walker naye kuyafumbua macho yake na kuanza kuangalia huku na kule.
Kutokana na hali iliyokuwepo mahali pale, wakagundua kwamba walikuwa hospitalini, hawakujua walifikaje mahali hapo, hawakujua mahali walipokuwa wazazi wao, walishangaa lakini baada ya kukaa kwa dakika kadhaa, wakakumbuka kila kitu kilichokuwa kimetokea kwamba walikuwa wakiingia ndani ya gari na ghafla wakahisi wakiishiwa nguvu na kuanguka chini.
Walihitaji kuwaona wazazi wao, hawakujua mahali walipokuwa, walitaka kuwaona kwani wao ndiyo walikuwa watu muhimu katika maisha yao.
Waliwaulizia lakini madaktari hawakutaka kuzungumza kitu chochote kile, kila walipokuwa wakiulizwa, waliruka na kuliacha swali hilo kitu kilichowafanya kuwa na hofu kwamba inawezekana walikuwa wamefariki dunia ila madaktari hawakutaka kuwaambia ukweli.
Waliendelea kubaki hospitalini hapo, mtu aliyekuwa akiwajulia hali zaidi alikuwa msichana Catherine ambaye hakukuwa na siku iliyokuwa ikipita pasipo kufika katika chumba walichokuwa wamelazwa na kuzungumza nao.
Hakuwaambia ukweli juu ya kile kilichokuwa kimetokea, alijua kwamba ni Edmund ndiye ambaye alisababisha hayo yote, alihofia kuwaambia ukweli kwa kuwa alihisi kwamba wangemchukia kwa kuwa mwanaume huyo alikuwa karibu naye.
Kila siku walikuwa wakiwaulizia wazazi wao, walitaka kujua ukweli kama walikuwa wamekufa au walikuwa hai, na kama walikuwa hai walikuwa mahali gani. Hakukuwa na mtu aliyewaeleza ukweli mpaka pale ambapo walipopewa taarifa kwamba wazazi wao nao hawakuwa katika hali nzuri, walikuwa hapo hospitalini kwani sumu iliyokuwa imewapata, ilikuwa mbaya sana.
“Sumu?” aliuliza Walker huku akionekana kushtuka.
“Ndiyo! Mliwekewa sumu!” alijibu Dk. John.
“Nani alifanya hivyo?”
Hakukuwa na mtu aliyejibu hilo, kila mtu alihofia kwamba kama wangejibu basi wangewafanya mapacha hao wamchukie Catherine ambaye alionekana kuwa karibu na mwanaume aliyekuwa amesababisha hayo yote.
Siku ziliendelea kukatika mpaka pale walipoanza kupata nafuu. Kila mmoja alionekana kuwa na furaha na baada ya siku mbili, wazazi wao ambao hawakujua mahali walipokuwa kipindi cha nyuma, wakakutana nao hospitalini hapo na kuanza kuzungumza nao.
Sumu ile haikuwapata sana kama ilivyowapata wao, katika kipindi chote hicho hata nao walikuwa wakifichwa juu ya hali waliyokuwa wakiendelea nao watoto wao. Walipokutana, wakashindwa kuvumilia, wakakumbatiana kwa furaha, kila mmoja hakuamini kwamba hatimaye familia hiyo iliungana kwa mara nyingine.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Watu wakapewa taarifa kwamba hatimaye mapacha hao walikuwa wameinuka kitandani, kila mtu aliyeziangalia picha zao alibaki na furaha tele kwani kwa kipindi hicho hakukuwa na watu waliokuwa wakipendwa kama ilivyokuwa kwa Walter na Walker.
Hawakuambiwa juu ya mtu aliyewafanyia hivyo ila baada ya kusikia habari na kuona matangazo, wakajua kwamba mwanaume aliyekuwa amefanya hivyo alikuwa Edmund.
Hilo liliwasikitisha, walimfahamu mwanaume huyo kwa kumuona tu, hawakuwa wamezoeana sana, sasa ilikuwaje mpaka kuamua kuwafanyia unyama mkubwa kiasi hicho?
“Kisa?” aliuliza Walter na hapo ndipo Catherine alipoanza kusimulia kila kitu kilichokuwa kimetokea kati yake na mwanaume huyo.
Hapo ndipo wakajua ukweli kwamba Edmund alidhamiria kufanya mauaji hayo kwa sababu tu alihisi kwamba Walter alikuwa mpenzi wa Catherine. Hilo lilimuumiza mno, hakuamini kama kungekuwa na mwanaume ambaye angeweza kufanya jambo kama hilo kwa ajili ya mapenzi tu.
Waliendelea kukaa hospitalini hapo huku kila siku wakifuatilia kuhusu kufuatiliwa kwa Edmund. Kidogo dunia ikatulia, kitendo cha mapacha hao kupona kilimfanya kila mmoja kuwa na furaha tele.
Nchini Marekani, kila mtu akatamani kuwaona watu hao wakielekea huko. Kulikuwa na mashindano makubwa ya America Got Talent ambapo waliombwa kuwa majaji katika shindano hilo lililokuwa kubwa duniani ambalo lilikuwa maalumu kwa watu kuonyesha vipaji vyao mbalimbali.
Ilikuwa nafasi kubwa kwao, hawakuwa na jinsi, kwa kuwa walikuwa watu wa watu, wakapanga kwenda huko ambapo wangekuwa katika siku zote za shindano hilo ambalo lingechukua miezi mitatu.
Wakapanda ndege, Catherine hakutaka kubaki nchini Uingereza, maishani mwake, hakukuwa na mwanaume aliyekuwa na thamani kubwa kama Walter, alimpenda mwanaume huyo, kwake, ngono halikuwa tatizo, alichokuwa akikifikiria ni kumuona mwanaume huyo kila wakati kitu alichoamini kingemfanya kuwa mwanamke mwenye furaa duniani kote.
“Are you going to Las Vegas?” (utakwenda Las Vegas?) aliuliza Walter.
“Yeah! I lost you, I don’t wanna lose you again,” (ndiyo! Nilikupoteza, sitotaka kukupoteza tena) alisema Catherine huku tabasamu pana likiwa usoni mwake.
***
Siku nzima polisi walikuwa barabarani kuhakikisha kwamba mtu aliyekuwa akitafutwa, Edmund anapatikana kwa hali na mali. Hakukuwa na polisi aliyejua kwamba gari moja miongoni mwa magari yaliyotaka kuingia nchini Wales lilikuwa na mtu aliyekuwa akitafutwa kwa udi na uvumba.
Kila mmoja alichoka, hawakuamini kama kweli mwanaume huyo alikuwa njiani kuelekea huko, walichokijua ni kwamba aliendelea kuwa Uingereza hivyo hata kwa jinsi walivyokuwa wakiyakagua magari mpakani hapo, hawakukagaua kama ilivyotakiwa kuwa.
Edmund akapewa kofia kama ya Malboro na dereva yule, akaivaa na kuanza kulisogeza gari kule walipokuwa polisi. Kila mmoja alichoka, walihitaji kuondoka kuelekea nyumbani kwani tangu asubuhi walikuwa mahali hapo, walizikumbuka familia zao, umakini wa kupekua magari uliwatoka na hivyo kuruhusu magari hata kama hawakufanya ukaguzi ambao ulitakiwa kufanyika.
Polisi alimuona Edmund akiwa na kofia, hakumjua, hakutaka kumkagua sana, ilikuwa ni usiku na mwili wake ulichoka mno. Hata kumwambia kuvua kofia ile ili amwangalie vizuri hakuwa na muda huo, akamulika tochi ndani ya gari kizushi, tena kwa haraka na kuliruhusu gari hilo kupita.
Edmund mwenyewe hakuamini, alihisi kama yupo ndotoni, alimwangalia polisi yule kwa makini, hakuamini kama kweli yeye ndiye aliyeliruhusu gari hilo kupita pasipo kufanyika ukaguzi kwa makini kama ambavyo ulitakiwa kufanyika.
Wakapita kirahisi kabisa, na baada ya dakika kadhaa gari likasimishwa nje ya hoteli kubwa ya Wales King ambapo Edmund akateremka, akaelekea mapokezi na dereva yule, akachukua chumba kwa ajili ya kwenda kupumzika.
“Utachukua chumba nikulipie?” aliuliza Edmund huku akimwangalia dereva, bado alimuhitaji, walikuwa na safari ndefu ya kuelekea katika Kituo cha Treni cha Bravein kwa ajili ya kupanda treni na kuelekea nchini Ireland.
“Haina shida. Nichukulie cha chini kabisa, ila kwanza ngoja niende baa kunywa,” alisema dereva huyo na Edmund kufanya hivyo.
Dereva yule akaelekea baa na kuanza kuunywa, nusu ya kiasi cha pesa alicholipwa kama malipo kilimfanya kujiona tajiri, aliamini kwamba kama angemfikisha mwanaume huyo huko alipokuwa akienda basi angepata kiasi kikubwa zaidi.
Kulikuwa na watu wengi ndani ya baa hiyo, kila mmoja alikuwa na chupa ya pombe, wengine waliongea kilevi, wapo walikuwa bize kuwashika makalio wahudumu, na wengine kuwa bize na mambo yao.
Macho ya dereva yule yalikuwa yakiangalia kila kitu kilichokuwa kikiendelea mahali hapo. Baada ya dakika chache alipoyahamishia macho yake kwenye televisheni, akashangaa kuiona sura ambayo haikuwa ngeni kabisa machoni mwake.
Haraka sana akasimama na kuisogelea televisheni ile ili kuiangalia vizuri. Ilikuwa ni sura ya Edmund ambayo ilikuwa kwenye tangazo lililosema kwamba alikuwa akitafutwa na dau la paundi milioni moja iliandaliwa kwa yeyote ambaye angefanikisha kukamatwa kwake.
Moyo wake ukamlipuka, hakuamini kile alichokuwa akikiona. Akaisogelea televisheni zaidi, kile alichokiona akiwa mbali ndicho alichokiona akiwa karibu. Haraka sana akatoka ndani ya baa, nje, kulikuwa na walinzi wawili waliokuwa wakihakikisha usalama mahali hapo, akawasogelea.
“Oya! Mnataka pesa?” aliuliza dereva huku akiwaangalia mabaunsa hao.
“Ndiyo! Kiasi gani?”
“Paundi elfu kumi kila mmoja!”
“Ndiyo! Zipo wapi?” aliuliza, kiasi hicho kilikuwa kikubwa mno.
“Twendeni. Mnamjua yule jamaa anayetafutwa kwenye televisheni?”
“Nani? Edmund? Yule aliyewafanyizia mapacha?”
“Ndiyo!”
“Yupo huku!”
“Wapi?”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Nyie twendeni acheni presha!” alisema dereva na kuwachukua mabaunsa hao na kuanza kuelekea nao katika hoteli ambayo haikuwa mbali kabisa kutoka hapo. Aliamini kwa kutumia nguvu za watu watatu, wasingeshindwa kumkamata Edmund ambaye kwa kuwangalia tu alionekana kuwa goigoi.
Wakavuka barabara na kuanza kuelekea katika hoteli hiyo ambapo baada ya kufika, wakawaambia polisi waliokuwa mahali hapo pia kuongozana nao kwenda katika chumba alichokuwamo kwani kila waliposikia jina la Edmund, waliziona akaunti zao benki kujaa pesa.
Kila mmoja alikuwa na uhakika kwamba Edmund alikuwa ndani ya hoteli hiyo hivyo kuanza kupandisha juu, polisi mmoja na dereva walipanda kwa kwenda huko kwa kutumia lifti huku wengine wakienda kwa kutumia ngazi.
Tayari walikwishazungumza na dada wa mapokezi ambaye aliwaambia kwamba mwanaume waliyekuwa wakimuulizia ambaye aliingia na dereva huyo muda mchache uliopita alichukua chumba namba 62 kilichokuwa katika ghorofa ya saba.
Walikwenda mpaka katika ghorofa hiyo aliyokuwa mwanaume huyo katika chumba hicho, wakaanza kuangalia huku na kule kabla ya kwenda katika chumba hicho. Walipohakikisha kwamba hakukuwa na mtu yeyote yule, wakamtaka mhudumu waliyekuwa naye kuufungua mlango kwa kutumia kadi ya masta.
"Mna uhakika yupo humu?' aliuliza mhudumu yule.
"Ndiyo dada. Fungua haraka asije kuruka dirishani," alisema dereva huku akiwa na presha kubwa.
Yule mhudumu akaufungua mlango huo kwa kutumia kadi ile, wakaingia ndani kwa pamoja huku polisi wale wakiwa na bunduki zao mikononi. Wakaanza kuangalia huku na kule kwa lengo la kumuweka chini ya ulinzi mwanaume huyo lakini kitu cha ajabu kabisa, Edmund hakuwepo chumbani.
"Au chooni," alisema dereva na hivyo kwenda huko.
Hakukuwa na kitu walichoambulia, huko napo hawakufanikiwa kumuona, kila kona chumbani humo palikuwa peupe kitu kilichomfanya dereva yule kushangaa kwani si muda mrefu mwanaume huyo alikuwa ameingia ndani ya hoteli hiyo.
"Au alibadilisha chumba?" aliuliza polisi.
"Sidhani! Hakubadilisha chumba, nina uhakika huo," alisema dereva huku akionekana kuwa na presha kubwa.
Kwa maelezo ya dereva yaliwapa uhakika kwamba bado Edmund alikuwa ndani ya hoteli hiyo, hawakutaka kuishia hapo, walichokifanya ni kuomba ruhusa kwa uongozi wa hoteli na kuanza kuingia kwenye kila chumba. Ilikuwa kazi kubwa sana lakini hawakuwa na jinsi, walikwenda kila chumba na kuangalia kama mwanaume huyo alikuwepo huko lakini hawakupata jibu.
Baada ya dakika arobaini na tano wakateremka mpaka chini, walishangaa, hawakujua mahali alipokuwa Edmund, wakamuuliza mlinzi kama alimuona mtu yeyote aliyetoka ndani ya hoteli hiyo, wakaambiwa kwamba hakukuwa na mtu yeyote.
"Au waulizeni wale vijana," alisema mlinzi huku akiwaonyeshea wanaume wawili waliokuwa wakiingiza takataka kwenye gari la taka.
"Hatujamuona. Kwani alikuja huku? Labda alitoka wakati tumekwenda kuchukua takataka kule," alijibu jamaa mmoja.
"Basi sawa. Popote mtakapomuona, tupeni taarifa," alisema polisi huku akiwaachia namba yao.
Hakukuwa na mtu aliyechanganyikiwa kama dereva, hakuamini kile kilichotokea, alikaa chini huku akiwa ameshika kichwa chake. Kilichomuuma ni kwamba Edmund alikimbia huku akiwa hata hajammalizia malipo yake.
Alikasirika, hakutaka kuondoka, aliamini kwamba mwanaume huyo alikuwa ndani ya hoteli hiyo, kwa kuwa yeye ndiye alikuwa amempeleka mule, akaelekea ndani ya gari na kusubiri humo kwa kuamini kwamba Edmund angerudi na kuendelea na safari kwa kutumia gari lake.
***
Edmund alikuwa chumbani kwake hotelini, kichwa chake kilikuwa kikifikiria mambo mengi yaliyopita, hakuamini kama alifanikiwa kuwamaliza mapacha wale kwani hata alipokuwa akiangalia kwenye televisheni, taarifa pekee ambayo aliipokea kipindi hicho ni kwamba walikuwa kwenye hali mbaya sana.
Moyo wake ulifarijika, hakuamini kama kweli alifanikiwa katika hilo. Hakuwa tayari kupoteza penzi lake, alimpenda sana Christina kiasi kwamba alikuwa tayari kufanya kitu chochote kile lakini si kumuona mwanaume mwingine akimchukua na kuondoka naye.
Alitulia kwa muda, alijiuliza maswali mengi kama alifanya jambo la maana sana kujificha ndani ya gari kwa kisingizo cha kutafutwa na baba yake. Alikuwa na machale, ni kweli alikuwa amezungumza na dereva yule kuhusu kutafutwa kwake na baba yake lakini kwa upande mwingine alikuwa na hofu kubwa kwamba inawezekana dereva huyo akataka kutafuta kile kilichokuwa kimetokea mpaka kuamua kujificha wakati polisi walipokuwa wakipekua kila gari lililokuwa likipita.
Wakati akiwa anafikiria hayo yote akiwa ndani ya chumba kile, akasimama na kwenda dirishani, alitaka kuhakikisha kwamba kila kitu kinakuwa salama na hata pale ambapo alipokuwa kunakuwa salama kabisa.
Akiwa hapo, bado alikuwa akijifikiria mambo mengi mno na baada ya dakika kumi nzima, akamuona kijana mmoja akiwa na mabaunsa wawili wakivuka barabara kuelekea kule hoteli ilipokuwa.
Alimfahamu dereva yule, alipomwangalia, alikuwa na uhakika kwamba alikuwa yeye. Alikuwa akitembea kwa mwendo wa kasi kuelekea katika upande kulipokuwa na hoteli ile. Hofu ikamjia, akahisi kabisa kwamba kulikuwa na kitu kilichokuwa kikiendelea, hakutaka kujiuliza, hapohapo akatoka dirishani, kwa haraka sana akachukua kila kitu alichokuwa nacho kwa lengo la kuondoka mahali hapo.
Alijua fika kwamba kama angepitia mapokezini basi kungekuwa na urahisi wa kukutana na watu hao, alichokifanya ni kupanda ngazi na kuelekea juu ya ghorofa kabisa na kupanga mikakati ya kuondoka hotelini hapo.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Nitaondoka kwa kuruka! Hapana! Nitaweza kuvunjika! Au nishuke kule kule mapokezi? Hapana! Nitakamatwa," alisema huku akizungukazunguka huku na kule.
Alikuwa akitafuta njia ya kuteremka kutoka ghorofani mpaka chini. Hakuona sababu ya kuendelea kubaki kwani hapo hotelini hakukuwa salama tena. Wakati akiwa hapo, akaona bomba kubwa la maji machafu likiwa limeshuka mpaka chini nyuma ya hoteli hiyo, bomba hilo lilikuwa na kazi ya kukusanya mamji ya mvua yaliyokuwa yakikaa huko juu na kuteremka chini.
Hiyo ndiyo ilikuwa nafasi yake, kitu cha kwanza kabisa akalishika bomba hilo na kulitikisa kuona kama lilikuwa imara, halikuonekana kuwa na tatizo na hivyo kuanza kuteremka kuelekea chini.
Alilidandia na kuanza kuteremka kwa kasi kubwa, hakutaka kuchelewa, alijua dhahiri kwamba kama watu wale wangemkosa kule chumbani basi ilikuwa ni lazima kwenda kumtafuta katika vyumba vingine na hata kujaribu kupanda kule ghorofani.
Aliteremka, baada ya dakika tano, akafanikiwa kufika chini kabisa huku akiwa hoi. Hakusimama, alichokifanya ni kuanza kupiga hatua kuelekea sehemu iliyokuwa na parking ya magari ambapo hapo akaliona gari kubwa la takataka likiwa limefika hapo kwa kuondoa taka usiku huo.
"Nitakwenda nalo hilihili," alisema Edmund na kuingia ndani ya garti hilo ambapo kulikuwa na mifuko mingi myeusi, akaichambua na kujificha katikati ya mifuko hiyo na kutulia.
"Nahisi nitaondoka salama mahali hapa," alijisemea huku akiendelea kujichimbia zaidi.
Watu walijaa katika Uwanja wa Ndege wa JFK uliokuwa jijini New York nchini Marekani. Watu wote waliokuwa mahali hapo walitaka kuwaona mapacha walioungana ambao walikuwa na vipaji vya aina yake, Walter na Walker waliokuwa wameiteka dunia kwa kipindi hicho.
Watu waliwaona sana kwenye televisheni, walitaka kuwaona tena na tena. Walijua kwamba siku chache zilizopita walikuwa nchini humo kabla ya kwenda nchini Tanzania, siku hiyo walitaka kuwaona zaidi, kwa wale ambao hawakuwahi hata kuwagusa, walitaka kuwagusa na hata wale ambao hawakuwa wamesainiwa vitabu vyao, walitaka kuona hilo likitokea.
Muda wote watu hao walikuwa wakiangalia saa zao, waliambiwa kwamba ndege hiyo ingewasili mahali hapo majira ya saa tisa jioni lakini cha ajabu, kila mmoja aliona kama muda ulikuwa umefika ila watu hao hawakuwa wameingia nchini humo.
“Jamani! Mbona wanachelewa hivi?” aliuliza msichana mmoja huku akiangalia saa yake, ndiyo kwanza ilikuwa saa 8:17 mchana lakini waliona kama saa tisa ilikuwa imekwishafika.
Uwanjani hapo hawakuwa peke yao, walikuwa na Waziri Mkuu, Bwana Gordon na mkewe ambao nao walitaka kuwaona mapacha hao ambapo kila kona duniani walikuwa wakizungumziwa wao tu.
Dakika zilizidi kwenda mbele na ilipofika majira ya saa tisa jioni, ndege ndogo ya kukodi, Flight 1789 WC ikaanza kuonekana angani, watu wakaanza kujiandaa kwani walijua fika kwamba hiyo ndiyo ilikuwa ndege iliyokuwa imewabeba watu waliokuwa wakiwasubiri uwanjani hapo, ndiyo ilikuwa ndege iliyowabeba watu waliowafanya kuacha shughuli zao na kufika uwanjani hapo.
Ndege ikasimama na watu hao kuanza kuteremka, kila mmoja akaanza kupiga kelele za shangwe, waandishi wa habari waliokuwa na kamera zao wakaanza kusogea kule ndege ile ilipokuwa na kuanza kupiga picha kwa kila kitu kilichokuwa kikiendelea mahali hapo.
Kila mmoja alitaka kuwagusa, hakukuwa na kipindi ambacho walinzi walipata wakati mgumu kama kipindi hicho. Ni kama shughuli zote za ndege zilikuwa zimesimama mahali hapo kwani kitendo cha kuwaruhusu watu kuingia katika ardhi ya uwanja wa ndege tu ilikuwa shida tupu.
“Please Walter! Sign my book,” (naomba usaini kitabu changu Walter!) alisema msichana mmoja huku akikiweka kitabu chake mbele.
Kila mmoja kipindi hicho alitamani kuwa karibu na watu hao, kila mmoja alitaka japo kuguswa na mapacha hao. Hakukuwa na mtu aliyetamani kuwaona watu hao wakiondoka pasipo kufanya jambo lolote lile kwa ajili yako.
Kwa kuwa kila mmoja alikuwa na kiu nao, walichokifanya ni kusaini vitabu vyao na kisha kuingia ndani ya gari na kuondoka mahali hapo. Bi Naseku na mumewe, Cassian walikuwa hawaamini walichokuwa wakikiona, hawakuamini kama vijana wao walikuwa mastaa kiasi hicho, walifurahi, muda mwingine walikuwa wakimshukuru Mungu kwani waliamini kwamba bila watoto wao kuungana namna hiyo basi wasingekuwa mastaa kama walivyokuwa.
Wakafikia katika Hoteli ya Nyota Saba ya 3 Pyramids iliyokuwa hapo New York. Chumbani, kila mmoja alikuwa na furaha, mbali na umaarufu waliokuwa nao lakini pia walikuwa na utajiri mkubwa wa dola milioni 600 katika akaunti yao.
“Shindano no keshokutwa! Nini cha kufanya baada ya hapo?” aliuliza Walker huku akimwangalia ndugu yake.
“Ni kurudi Tanzania! Baada ya hapo, tutafanya mambo mengine mengi,” alisema Walter.
“Na vipi kuhusu Catherine?”
“Nitamuoa. Ila nitaona siku ukioa, tutafunga ndoa pamoja. Umekwishapata msichana wa maisha yako?” aliuliza Walter.
“Bado.”
“Na vipi kuhusu Jackline? Bado hujafikiria kumtafuta?”
“Bado! Ila kuna siku nitamtafuta. Kuna mambo mengi sana. Kuna mchoro nitahitaji kuuchora, wa yule msichana Patricia!” alisema Walker.
“Yupi? Nikuumbushe!”
“Tuliyekutana naye kwenye ndege. Umemsahau?”
“Ooh! Yule Mfaransa?”
“Yeah! Ninatamani sana nimchore kisha nimtumie. Ni msichana mzuri sana. Kiukweli nimetokea kumpenda,” alisema Walker huku akionekana kumaanisha alichokuwa akikizungumza.
“Safi sana. Sema naye.”
Japokuwa alikuwa amekutana na wasichana wengi wauzri lakini Walker alikuwa amekufa na kuoza kwa msichana mmoja tu, Patricia ambaye alikutana naye ndani ya ndege katika kipindi walichokuwa wakitoka nchini Tanzania kwenda Marekani.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Alizoeana na msichana huyo na mara nyingi walikuwa wakichati, walikuwa wakizungumza mengi na kushauriana mambo mengi mazuri. Hakukuwa na mtu aliyemwambia mwenzake, kila Walker alivyotaka kufanya hivyo, alijiona akishindwa kabisa na kitu pekee ambacho aliamini kwamba kingezungumzia hisia zake juu ya msichana huyo kilikuwa ni kumchora tu.
Alikuwa na mawazo tele, hakumfikiria rafiki yake wa utotoni, Jackline ambaye hakujua kipindi hicho alikuwa wapi, mtu pekee aliyekuwa akimfikiria sana alikuwa msichana Patricia tu. Alimwambia ndugu yake, alitamani sana kuona akiwa na msichana huyo zaidi na zaidi ili hata kama ingetokea siku ndugu yake, Walter angekuwa anaona, basi waweze kuoa pamoja.
“Ukichelewa, nitaoa kabla yako!” alisema Walter.
“Huwezi kuoa kabla yangu. Tutaoa pamoja. Wala usijali,” alisema Walker huku akiwa na uhakika wa kumpata msichana huyo.
***
Maisha yalikuwa tofauti, kile alichokuwa amekifanya hakikuleta matokea chanya, akawa mtu wa kuhangaika huku na kule. Edmund alikuwa ndani ya gari la takataka, alifunikwa na taka hizo na kulisikia gari likianza kuondoka mahali hapo.
Hakuamini kama yeye ndiye aliyekuwa akiishi maisha hayo ya digidigi, yaani kisa mapenzi tu leo hii alikosa amani kabisa, na mbaya zaidi kile alichokuwa amekikusudia hakikuwa kimetimia.
Alijuta lakini wakati mwingine aliamua kusonga mbele, alikuwa tayari kuendelea kuishi hivyo na ndiyo maana alikuwa ameondoka kuelekea nchi nyingine kabisa kwa kuamini kwamba angekuwa salama hapo Wales.
Aliikumbuka familia yake, alimkumbuka mpenzi wake, aliwakumbuka marafiki zake, kila kitu alichokiacha nyuma yake huo ndiyo ulikuwa wakati wa kukikumbuka.
Safari ille iliishia katika sehemu iliyokuwa na jumba kubwa ambalo ndani yake kulikuwa na eneo maalumu pa kuchomea takataka. Wakati gari likiwa limesimama kwa lengo la watu kuja kutoa takataka, naye akatoka na kuanza kuelekea sehemu iliyokuwa na mlango mkubwa wa kutokea.
Hakukuwa na watu wengine, humo ndani, watu waliokuwa na zamu ya kuleta gari hilo ndiyo waliokuwa wakiingia humo kwa ajili ya kuzichoma moto taka hizo. Alipofika nje ya jengo lile, akaanza kupiga hatua kuelekea mitaani.
Hapo palikuwa Stonford Pelrr, sehemu iliyokuwa karibu na pori dogo la kutengenezwa la Jumanji. Alitembea kwa mwendo wa haraka katika kipori hicho mpaka alipofika sehemu iliyokuwa imetengwa kwa ajili ya wazazi kuwapeleka watoto wao kwenda kucheza.
Alichoka, alihitaji muda wa kupumzika, pale, hakukuwa na mtu yeyote, palikuwa pamefungwa kwa muda, akayafuta mabenchi yaliyokuwa mahali hapo na kutulia.
Moyo wake ulikuwa na mawazo tele, hapo alipofika, akatamani kuwasiliana na wazazi wake, alitaka kuwaomba msamaha kwa kila kitu kilichokuwa kimetokea kwani hakuwa amekusudia bali kulikuwa na nguvu kubwa iliyokuwa imemuingia ambayo ilimuongoza kufanya jamboo la kipumbavu kama lile.
Akaichukua simu yake iliyokuwa mfukoni mwake ambayo aliizima kitu kiitwacho location na kuizima kabisa, akaiwasha na kuanza kumpigia simu baba yake ambapo baada ya sekunde chache, simu ikapokelewa.
“Baba! Aliita baada ya simu kupokelewa!
“Edmund! Upo wapi?”
“Nimeondoka nyumbani. Baba! Naomba unisamehe, nimefanya jambo la kijinga sana, ninajutia kile nilichokifanya, naomba unisamehe, najua umeumia, sikuwa na cha kufanya, nilifanya hivyo kwa kuwa nilihitaji kulilinda penzi langu, nilimpenda sana Catherine, sikuwa na sababu ya kumpoteza na ndiyo maana niliamua kufanya hayo yote kwa kuamini kwamba ningeweza kulilinda penzi langu kwake,” alisema Edmund huku akitokwa na machozi ya uchungu, aliusikia moyo wake ukichomwa na kitu chenye ncha kali.
“Pole sana. Usijali! Upo wapi?”
“Nimeondoka! Nimekuja huku....” alisema Edmund lakini hata kabla hajamaliza sentensi yake, akasikia vishindo vya watu wakija kwa kasi kule alipokuwa, hapohapo akageuka, macho yake yakatua kwa polisi waliokuwa na bastola viuononi mwao na virungu mikononi mwao.
“Mikono juu! Weka mikono tuione vizuri,” alisema polisi mmoja huku wakimsogelea, hapohapo Edmund hakuwa na jinsi, akaiachia simu na kunyoosha mikono juu huku machozi yakimtoka.
“Halo...halo..” ilisikika sauti ya baba yake kwenye simu.
Kiuhalisia huo ulionekana kuwa mwisho wa Edmund, alinyanyua mikono yake hewani huku akiwa na hofu kwamba hatimaye alikuwa amekamatwa na polisi waliomfikia hapo bustanini na kumnyooshea bastola huku wakimtaka kutulia kama alivyokuwa.
Baba yake aliyekuwa upande wa pili aliendelea kuita pasipo mafanikio yoyote yale. Polisi wale wakazidi kumsogelea, walipomfikia, wakamuweka chini ya ulinzi na kumuuliza maswali juu ya kitu alichokuwa akikifanya mahali pale.
"I was looking for my wife," (nilikuwa namtafuta mke wangu) alisema huku akilala chini.
Walikuwa na taarifa ya mtu aliyejulikana kwa jina la Edmund kutafutwa nchini Uingereza lakini hawakujua kama yule waliyekuwa naye ndiye kijana aliyekuwa akitafutwa kwa udi na uvumba.
Mahali hapo kulikuwa na mwanga hafifu hivyo hata walipomwangalia usoni iliwawia vigumu sana kugundua kwamba alikuwa yeye na maneno ambayo aliwaambia kwamba alikuwa akimtafuta mke wake yaliwafanya kumuonea huruma kwamba alikuwa kwenye matatizo makubwa.
"Where is she?" (yupo wapi?)
"She came here with my son, I don't know where they are!" (alikuja hapa na mwanangu, sijui wapo wapi) alisema Edmund huku akiwa amelala chini, sauti yake kwa jinsi ilivyosikika ilikuwa ni kama ya mtu aliyetaka kulia.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Did you try to call here?" (ulijaribu kumpigia simu?)
"I tried many times but I didn't reach her!" (nilimpigia mara nyingi lakini sikumpata) alijibu.
Hiyo haikuwa mara ya kwanza, ni mara nyingi watu waliokuja wakija mahali hapo walikuwa na malalamiko mengi kuhusu kupotea kwa watoto wao na hata mume na wake zao. Kitendo cha Edmund kuwaambia hivyo, hapohapo wakamfungua pingu na kumuweka kwenye benchi.
Hakutaka kugundulika hivyo kujifanya kulia huku akiuinamisha uso wake. Alijifanya kuwa kwenye tatizo kubwa kiasi kwamba wote wawili wakaanza kumuonea huruma kwa kuona kwamba kweli mwanaume huyo alikuwa kwenye matatizo makubwa hivyo kuhitaji msaada.
Wakamwambia achukue simu yake, akajiandikia namba na kupiga. Simu haikuwa ikipatikana, akawaambia polisi kwamba namba haikuwa ikipatikana hivyo alitakiwa kurudi nyumbani kuona kama mkewe huyo alikuwa amefika nyumbani.
Hawakuwa na jinsi, wakamruhusu, akaondoka mahali hapo kinyonge. Polisi wale walibaki wakimsinidkiza kwa macho mpaka alipopotea na kutokomea zake huku akiwa amenusurika kukamatwa na polisi hao. Moyoni mwake akajiona kuwa na bahati, alimshukuru Mungu zaidi na zaidi kwamba alimuokoa kutoka katika mikono ya polisi hao.
Alipofika barabarani, akasubiri basi la abiria na kuondoka mahali hapo. Alipokuwa akielekea, hakuwa akipafahamu, basi liliendelea mpaka alipofika sehemu ambapo alihisi ndiyo mwisho wa basi hilo, akateremka na kuelekea katika kitu kupumzika. Wakati akiwa hapo, simu yake ikaanza kuita. Haraka sana akaipokea.
"Edmund...You are a superstar," (Edmund...wewe ni supastaa mkubwa) alisikika mwanaume aliyekuwa upande wa pili.
"How?" (kivipi?) akajifanya kuuliza.
"I see you in my television! You about to win an Oscar award!" (nakuona kwenye televisheni yangu, unakaribia kutwaa Tuzo ya Oscar) alisikika mwanaume wa upande wa pili.
Huyo alikuwa rafiki yake wa karibu, Mark aambaye mara nyingi sana walikuwa wakitaniana pasipo kujua ni kwa namna gani mtu fulani alikuwa kwenye hatari ya kupoteza maisha yake. Baada ya kumtania ndipo akauliza kilichokuwa kikiendelea, Edmund hakutaka kumficha, alimwambia kwamba kile alichokuwa akikiona kwenye televisheni ndicho kilichokuwa kimetokea hivyo kutaka msaada kwani alikuwa nchini Wales.
"Hakuna tatizo! Ngoja nimpigie mjomba wangu akusaidie kukupokea," alisema Mark.
Hilo halikuwa hata tatizo, kipindi hicho kitu alichokuwa akikihitaji Edmund ni msaada wa hali na mali kwani ilikuwa ni lazima kuhakikisha kwamba anaondoka salama na kwenda mbali kuishi maisha yake. Mark akawasiliana na mjomba wake huyo ambaye alimwambia kuhusu rafiki yake aliyekuwa akihitaji msaada mkubwa.
Akamwambia sehemu alipokuwa kisha kumpigia simu Edmund na kumwambia juu ya msaada aliokuwa akiuhitaji kupatikana. Akamshukuru rafiki yake huyo na kumsubiri mjomba huyo ambaye aliingia hapo baada ya dakika kadhaa.
"Wewe ndiye Edmun?" aliuliza mjomba huyo.
"Yeah! Ndiye mimi!"
"Ingia twende!"
Hakuwa na hofu yoyote ile, akaingia ndani ya gari na kuondoka mahali hapo. Kidogo moyo wake ukawa na furaha mno, akaamini kwamba kwa kitendo cha rafiki yake huyo kuwasiliana na mjomba wake na hatimaye kumsaidia, kwake ilimfanya kumuona Mark mtu wa maana mno.
Hawakuchukua dakika nyingi wakafika mahali kulipokuwa na nyumba chache ambapo hapo ndipo alipokuwa akiishi huyo mjomba, wakateremka na kuingia ndani, akamuonyesha chumba cha kulala na kumwambia kwamba kuanzia siku hiyo angelala mahali hapo mpaka pale ambapo angetaka kuondoka mwenyewe.
"Nashukuru sana!" alisema Edmund, akaingia ndani na kupumzika.
Mjomba aliyeitwa Vonn alitulia sebuleni. Kitendo cha kwenda kumpokea Edmund na kumuona, hakuamini kabisa kama huyo ndiye alikuwa yule mwanaume aliyetakiwa kwenda kumpokea.
Alimjua, hiyo haikuwa mara ya kwanza kumuona, alimuona kwenye televisheni na kipindi chote hicho mwanaume huyo alikuwa maarufu mkubwa, alionekana kwenye kila kituo cha televisheni huku kukiwa kumetolewa donge nono la pesa ambalo angepewa mtu yeyote ambaye angefanikisha kupatikana kwake.
Sebuleni hakutulia, alikuwa akihangaika, moyo wake ulikuwa ukifukuta, hakutulia, alitamani sana kuwa mwaminifu kwa Mark lakini kila alipokuwa akizikumbuka zile pesa alizokuwa ameahidiwa mtu yeyote ambaye angefanikisha kupatikana kwake, udenda wa tamaa ukamtoka.
"Ni pesa nyingi sana! Hizi zitanifanya kutoa mizigo Ujerumani na kuileta hapa kuendelea na biashara zangu! Siwezi kuziacha pesa hizi," alijisemea huku akiwa sebuleni hapo.
Hakutaka kuchelewa, ilikuwa ni lazima kwenda kituo cha polisi na kutoa taarifa kwamba mwanaume aliyekuwa akitafutwa kila kona alikuwa nyumbani kwake. Akaelekea chumbani, akabadilisha nguo zake, kila kitu alichokuwa akikifanya chumbani humo aliona akifanya taratibu sana kwani alitamani kuondoka haraka sana na kuelekea polisi na kutoa taarifa juu ya mwanaume huyo aliyekuwa chumbani.
Alipomaliza, hakutaka kuchelewa, hapohapo akaelekea sebuleni, akachukua simu yake, akaufuata mlango, alipoufungua tu, macho yake yakakutana na bunduki zaidi ya kumi zilizoshikwa na wanaume waliokuwa wamevalia mavazi meusi ambapo usoni mwao walikuwa wameficha sura zao na kwa nyuma kukiwa na gari lililoandikwa S.W.A.T.
"Don't movie! Hands on your head," (usitingishike! Mikono kichwani mwako) alisema mwanaume mmoja kwa sauti ya chini ambayo hakutaka mtu yeyote ndani asikie chochote kile, hapohapo Vonn akafanya kama alivyoambiwa.
"Where si he?" (yupo wapi?) aliuliza.
"Who?" (nani?)CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Edmund!"
"Who is that?" (ndiye nani huyo?) aliuliza huku akiwaangalia wanaume hao.
Hawakutaka kumwambia ukweli, walichokifanya ni kuanza kuelekea ndani kwa ajili ya kumtafuta mwanaume huyo huku wakiwa na uhakika kwamba alikuwa humo.
Vonn alibaki pale mlangoni, hakuamini kilichokuwa kimetokea, ilikuwa watu hao wajue kama Edmund alikuwa nyumbani kwake na wakati hakumwambia mtu? Wakati mwingine alihisi kwamba Mark alikuwa amewataarifu polisi kwamba mwanaume huyo alikuwa nyumbani kwake.
Zile pesa zilizokuwa kichwani mwake, zikaanza kupotea na kuona kuwa hao polisi wangemuona Edmund ambapo wangemchukua na kuondoka naye bila yeye kupata kitu chochote kile kwani hakuwa ametoa taarifa kama mwanaume huyo alikuwa ndani ya nyumba hiyo.
"Freeze...freeze...frezeeeeee..." ilisikika sauti za watu hao huko ndani.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment