IMEANDIKWA NA : NYEMO CHILONGANI
*********************************************************************************
Simulizi : A Day Too Long (Siku Ndefu Mno)
Sehemu Ya Kwanza (1)
Malumbano baina ya msichana Jamala pamoja na mpenzi wake, Selemani bado yalikuwa yakiendelea kusikika kutoka katika nyumba moja kuu kuu ambayo ilikuwa maeneo ya Kibaha Maili moja. Kadri malumbano yale yalivyokuwa yakizidi kusikika na ndivyo ambavyo watu wakazidi kusogea mahali pale karibu na nyumba ile na kutegesha masikio yao vizuri huku wakiwa na hamu ya kufahamu ni kitu gani ambacho kilikuwa kikiendelea katika kipindi hicho ndani ya nyumba ile.
Muda ulikuwa umekwenda sana huku ikiwa ni saa 2:15 usiku. Malumbano yale tayari yalikuwa yamechukua takribani masaa mawili lakini hakukuonekana kuwa na muafaka wowote ambao ulikuwa umeafikiwa. Japokuwa mara kwa mara Selemani alikuwa akiongea kwa mikwara mingi lakini Jamala hakutaka kuogopa, kadri Selemani alivyozidi kupanda juu, nae Jamala alipanda juu.
Malumbano yale ambayo yalikuwa yakiendelea kusikika ndio ambayo yalizidi kuwavuta watu wengi mahali pale, baada ya kipindi fulani, wazee wakaanza kuisogelea nyumba ile kwani tayari walikwishajua kwamba kuna kitu ambacho kilikuwa kikiendelea kwa wakati huo. Wazee wale walipoufikia mlango wa nyumba ile, wakaanza kuugonga.
Ingawa Selemani na Jamala walisikia jinsi mmoja wa wazee wale alivyokuwa akipiga hodi lakini hakukuwa na mtu yeyote ambaye alikwenda kuwafungulia. Wazee wale waliendelea kusimama nje ya mlango wa nyumba ile huku wakiendelea kupiga hodi lakini bado hakukuwa na mtu ambaye alikuja kuwafungulia kitu ambacho kiliwapelekea kujaribu kuufungua mlango ule. Walipojaribu kuufungua, mlango ukafunguka na kuingia ndani.
Wakaanza kuwaangalia Selemani na Jamala ambao bado walikuwa wakiendelea kulumbana bila kujali kwamba kuna watu walikuwa wameingia mahali hapo. Kila mmoja alionekana kuwa na hasira kipindi hicho, hakukuwa na mtu ambaye alikuwa tayari kutulia kimya kumsikiliza mwenzake, kila mtu alikuwa akiongea yeye hali ambayo ilionekana kutokuwa na maelewano kabisa mahali pale.
“Haiwezekani. Haiwezekani kabisa. Kwani mwanaume lijali ni mimi peke yangu?” Selemani alisema kwa sauti huku akimwambia Jamala ambaye alikuwa akiendelea kulumbana nae.
“Unaniona mimi malaya! Au kwa sababu nilikutanulia mapaja yangu ndio maana kwa sasa unaniona malaya? Umewahi kuniona wapi nimetembea na mwanaume mwingine?” Jamala aliuliza kwa sauti ya juu.
Ingawa wazee wa mahali pale walikuwa wameingia ndani ya nyumba ile kwa ajili ya kusuluhisha malumbano yale ambayo yalikuwa yakiendelea ndani ya nyumba ile lakini mara baada ya kuingia ndani hakukuwa na mtu yeyote ambaye alidiriki kufanya kile ambacho walikuwa wamekusudia kukifanya mahali hapo, wakabaki wakiwaangalia tu. Kila mmoja alikuwa bize kulumbana na mwenzake jambo ambalo lilikuwa likiwashangaza wale wazee.
Selemani na Jamala walikuwa wapenzi ambao walionekana kuwa kwenye mapenzi ya dhati kupita kawaida. Walikuwa wakipendana sana katika kipindi cha nyuma kiasi ambacho baadhi ya watu walijua fika kwamba mwisho wa siku watu wale wangekuja kuoana huko mbeleni. Japokuwa Jamala alikuwa akiishi jijini Dar es Salaam ndani ya mtaa wa Tandale na Selemani kuishi Kibaha Maili moja lakini watu hao walionekana kushibana katika mahusiano yao.
Mara kwa mara Jamala alikuwa akielekea Kibaha ambako huko alikuwa akielekea katika nyumba ambayo Selemani alikuwa akiishi. Kitendo cha Jamala kufika katika nyumba ile mara kwa mara kikawafanya watu ambao walikuwa katika mtaa ule kumfahamu sana. Kila mtu ambaye alikuwa akikutana nae alikuwa akimuita ‘shemeji’ huku wengine wakimuita ‘wifi’, majina ambayo yalionekana kumfurahisha sana Jamala.
Kwa mara ya kwanza Selemani alikutana na Jamala katika kipindi alichokwenda kumsalimia mjomba wake katika nyumba yake iliyokuwa maeneo ya Mwananyamala jijini Dar es Salaam, mtaa ambao haukuwa mbali na mtaa wa Tandale ambapo alipokuwa akiishi Jamala. Siku hiyo ndiyo ambayo wawili hao wakaonana katika ngomba ya Kitanga, Baikoko ambayo ilikuwa ikipigwa karibu na nyumba ya mjomba wake Selemani, mzee Hussein.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Ingawa siku hiyo hawakuwa na uhuru mkubwa wa kuongea, wakaamua kutoka mahali hapo na kwenda sehemu fulani kuongea. Siku hiyo waliongea mengi tu na kutokana na uzuri ambao alikuwa nao Jamala, Selemani akaamua kulielezea dukuduku lake ambalo lilikuwa moyoni mwake juu ya msichana huyo ambaye alionekana kuwa mrembo sana usoni mwake.
“Unanipenda?” Jamala aliuliza huku akicheka kwa chini chini.
“Ndio. Nimetokea kukupenda sana” Selemani alijibu.
“Haiwezekani bwana. Naona bado mapema sana” Jamala alijitetea.
“Haiwezekani?. Huu ni muda muafaka sana wa mimi kuwa pamoja nawe” Selemani alimwambia Jamala.
“Utakuwa umenitamani tu. Yaani unataka kulala nami tu tena kwa usiku mmoja wa leo tu” Jamala alimwambia Selemani.
“Hapana. Kitu gani kimekufanya kusema hivyo?”
“Kwa ajili ya hizi ngoma. Yaani unavyoona wanawake wanaonyesha matiti yao hadharani nadhani umepagawa na umeamua kuniambia jambo hilo mapema na kwa haraka sana” Jamala alimwambia Selemani ambaye alikaa kimya kwa muda.
“Hapana. Sijakutamani”
“Umenitamani tu”
“Sidhani kama kuna mtu anaweza kumtamani msichana gizani” Selemani alimwambia Jamala.
“Kwani wewe unafikiri kila mtu anayemtamani msichana huwa mwangani tu?”
“Ndio. Labda ameona mapaja yake manene ya kuvutia, au ameona vikuku vyake vya miguuni, au wakati mwingine hata shanga za kiunoni” Selemani alimwambia Jamala ambaye alianza kucheka.
“Katika vitu vyote nilivyovitaja hapo, kuna chochote nimekiona kutoka kwako?” Selemani aliuliza.
“Hapana” Jamala alijibu.
“Basi ndio maana nimekwambia kwamba nimetokea kukupenda” Selemani alimwambia Jamala.
Japokuwa Selemani alikuwa akisikika kuongea kiutani lakini ndio alikuwa akizidi kupiga hatua zaidi na zaidi na mwisho wa siku Jamala kutoa kauli yake ya mwisho kwamba alikuwa tayari kuingia katika mahusiano na Selemani. Japokuwa ilikuwa mapema sana na kwa haraka sana lakini maneno matamu ya Selemani pamoja na hali ya kujiamini ndivyo ambavyo viliweza kumpa ushawishi mkubwa Jamala wa kumkubali na kuanza mahusiano ya kimapenzi.
Kuanzia siku hiyo wakaamua kupeana namba za simu na kuanza kuwasiliana. Walipokuwa wakitaka kuonana, walikuwa wakionana. Siku ya kwanza ambayo Jamala alikwenda katika nyumba ya mzee Hussein, mjomba wake Selemani ndio ilikuwa siku ambayo wakaamua kufanya kila kitu. Mambo yote yakaanza kutokea chumbani tena kitandani, dakika kumi baada ya Jamala kuingia ndani ya chumba kile, akawa mtupu kama alivyozaliwa na kisha kuanza kufanya ngono zembe pamoja na Selemani.
Kuanzia siku hiyo ndio ikawa mchezo wao. Mara kwa mara walikuwa wakikutana na kufanya kitendo kile ambacho kwao hasa kwa wakati huo wala hakikuonekana kuwa na madhara kabisa. Walifanya takribani kila siku mpaka pale ambapo Selemani alipoamua kurudi Kibaha. Kutoka na Jamala kuupenda sana mchezo ule, akajikuta mara kwa mara akielekea Kibaha ambapo mechi ilikuwa ikichezwa zaidi na zaidi huku akijulikana na watu wengi kule Kibaha kwamba alikuwa msichana wa Selemani.
“Nina mimba?” Jamala alimuuliza Dokta ambaye alikuwa amempima.
“Ndio” Dokta alijibu.
Siku hiyo Jamala hakukaa kwa raha, tayari mawazo yake yakaanza kumfikiria Selemani huku akizikumbuka siku zote ambazo alikuwa pamoja na Selemani na kuucheza mchezo ule ambao tayari ulikwishaanza kuonyesha madhara yake. Alichokifanya Jamala siku hiyo jioni ni kuondoka kuelekea Kibaha ambapo akaamua kumwambia Selemani juu ya hali ambayo alikuwa nayo kwa wakati huo.
Selemani akaonekana kuwa mkali kama mbogo, kwake hakutegemea kuwa na mtoto kwa wakati huo. Kwanza alijiona kutokuwa tayari kulea kutokana na maisha yake kuwa ya kuungaunga sana. Siku hiyo ndio ambapo malumbano yale yalipoanza mpaka wale wazee kuingia ndani ya nyumba ile. Jamala alikuwa akimwambia Selemani kwamba ujauzito ule ulikuwa wa kwake lakini Selemani alikuwa akikataa kwa nguvu zote.
“Nitawezaje kuamini kama huo ujauzito ni wangu? Unaishi Dar kumbuka” Selemani alimwambia Jamala.
“Kwa hiyo nikiishi Dar ndio nini?”
“Nawajua vijana wa Dar wewe kwamba wakiamua kukufuatilia utafikiri wanafuatilia kazi. Naujua mchezo wao sana. Mimba hiyo itakuwa ya kijana mmoja wa huko huko” Selemani alimwambia Jamala.
“Huu ni ujauzito wako Sele”
“Nasema hivi, huu si ujauzito wangu” Selemani alimwambia Jamala.
Malumbano yalikuwa yakizidi kuendelea zaidi na zaidi. Hakukuwa na mtu ambaye aliibuka kuwa mshindi siku hiyo, kila mmoja alijitahidi kutaka kuibuka mshindi. Bado wale wazee ambao walikuwa wameingia ndani ya nyumba ile walikuwa kimya huku wakiwaangalia vijana wale ambao bado walikuwa wakiendelea kulumbana kama kawaida yao. Muda ulizidi kusogea zaidi na zaidi mpaka kufika saa tatu kasoro usiku.
“Jamani! Kuna nini tena?” Mzee mmoja aliuliza lakini hakukuwa na mtu ambaye alijibu chochote kile zaidi ya kuendelea kulumbana tu.
Huku akionekana kuwa na hasira, Jamala akaondoka mahali hapo na kutoka nje ambapo akaanza kukimbia kuelekea barabarani huku akilia kama mtoto. Kichwa chake kwa wakati huo kilikuwa kimechanganyikiwa, hakujua afanye kitu gani. Kuna mawazo mawili ambayo yalikuwa yakimjia kichwani kwa wakati huo, wazo la kwanza lilikuwa ni kuitoa mimba ile huku wazo la pili likiwa ni kuiacha kwa sharti moja tu, endapo mtoto angezaliwa, angeweza kumtelekeza mahali popote pale.
“Nitafanya chochote kile. Huyu mtoto tayari kashakuwa mtoto wa haramu” Jamala alisema huku akiwa amekwishafika kituoni na kisha kuingia ndani ya daladala kurudi jijini Dar es Salaam.
Ndani ya gari, bado Jamala alikuwa akiendelea kulia tu, hakuamini kama mwanaume ambaye alikuwa akimpenda na kumthamini mpaka kufikia hatua ya kumvulia nguo ndiye ambaye leo hii alikuwa amekataa kwamba ujauzito ambao alikuwa amempa haukuwa wake. Lile likaonekana kuwa kama pigo kubwa kwa Jamala, hakujua ni hatua gani ambayo angeanza kumwambia mama yake ambaye mara nyingi sana alikuwa akimsisitiza kumpenda Allah kuliko kitu chochote maishani mwake, hakujua ni kitu gani angemwambia mama yake ambaye alikuwa akimsisitizia sana kwenda msikitini kuswali ili apate muongozo mzuri wa maisha yake ya sasa na yajayo.
“Sitokubali kukaa na mtoto wa haramu” Jamala alijisemea kwa sauti ya chini huku akiendelea kulia ndani ya daladala ile.
Jamala alikuwa na mawazo kupita kawaida, akili yake kwa wakati huo ilikuwa ikimkumbuka Selemani ambaye alikuwa ameukataa ujauzito ule. Alikuwa akilia mfululizo, hakuamini kama mwanaume yule angeweza kuukataa ujauzito ule ambao alikuwa amempa. Jamala hakuonekana kuwa na raha, muda wote alionekana kuwa mnyonge kupita kawaida.
Muda ulizidi kwenda zaidi na zaidi, ilipofika saa nne na nusu usiku akafika nyumbani kwao na moja kwa moja kuingia chumbani kwake. Akajifungia na kuanza kulia. Kumbukumbu zake zikaanza kujirudisha nyuma kama mkanda wa filamu, akaanza kukumbuka siku ya kwanza ambayo alikua amekutana na Selemani katika ngoma za Kitanga za Baikoko Mwananyamala.
Katika usiku huo alikumbuka mambo mengi ambayo walifanya pamoja mpaka kipindi kile ambacho walifanya mapenzi kwa mara ya kwanza. Kwa kila kitu ambacho alikuwa akikikumbuka kwa wakati huo kilikuwa kikimuumiza kupita kawaida. Hakuamini kama Selemani yule ambaye alimvua kuanzia gauni mpaka nguo ya ndani ndiye ambaye alikuwa ameamua kuukataa ule ujauzito wake ambao alikuwa nao.
Jamala hakuonekana kuikubali hali ile japokuwa ilikuwa imetokea, alichokuwa amekifikiria kwa wakati huo ni kuitoa mimba ile pasipo kujali ni kitu gani kingetokea lakini kwa wakati huo hakuwa radhi kuwa na mtoto. Usingizi siku hiyo haukuja mapema kama siku nyingine mpaka ilipofika saa tisa usiku ndipo alipolala.
Siku iliyofuata asubuhi na mapema akaamka na kuanza kufanya vitu vyake ambavyo vilikuwa katika ratiba yake siku hiyo. Kila kitu ambacho alikuwa akikifanya katika kipindi hicho alikuwa akijaribu kukifanya kwa haraka haraka sana kwani alikuwa akihitaji kwenda katika maabara moja ya uswahilini kwa ajili ya kuonana na daktari na kisha kuitoa ile mimba ambayo alikuwa nayo.
Ilipofika saa 4:10 asubuhi, moja kwa moja akaanza safari ya kuelekea katika maabara hiyo ambapo baada ya kufika, akakaa kwenye foleni na zamu yake ilipofika kuingia ndani. Jamala akabaki akimwangalia Dokta kwa muda huku uso wake ukionekana kuwa na wasiwasi kutokana na kile ambacho alikuwa akitaka kukifanya kwa wakati huo.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Karibu” Dokta alimkaribisha Jamala ambaye alikaa kitini.
“Asante”
“Unaumwa nini dada yangu?” Dokta alimuuliza Jamala ambaye akabaki kimya kwa muda.
“Unaumwa nini?” Dokta alimuuliza tena kwa sauti iliyojaa upole.
“Nimekuja kutoa mimba” Jamala alisema huku akijipa ujasiri.
“Gharama yake ni shilingi elfu thelathini kama mimba hiyo itakuwa na muda wa mwezi mmoja. Shilingi elfu arobaini kama mimba hiyo itakuwa na muda wa miezi miwili na shilingi elfu hamsini kama mimba hiyo itakuwa na muda wa miezi mitatu” Dokta alimwambia Jamala ambaye alibaki kimya kwa muda.
“Yako ni ya muda gani?” Dokta alimuuliza.
“Mwezi mmoja”
“Sawa. Una kiasi hicho cha fedha?”
“Hapana. Nina pungufu”
“Kiasi gani?”
“Elfu ishirini”
“Mmmh! Ulikwishawahi kutoa mimba kabla?” Dokta alimuuliza.
“Hapana”
“Ok! Ila kama utakuja siku nyingine naomba ukumbuke hilo. Umenielewa?”
“Ndio”
“Sawa. Nenda nje wengine waje. Kwa sababu kazi yako ni ya muda mrefu kidogo na ya siri kubwa, nitakuita” Dokta alimwambia Jamala ambaye akatoka nje.
Jamala akakaa kwenye benchi, akili yake kwa wakati huo wala haikutulia kabisa. Alikuwa akiifikiria hali ambayo alikuwa nayo katika kipindi hicho. Kichwa chake kilikuwa na mawazo mfululizo, kadri dakika zilivyozidi kwenda mbele na ndivyo ambavyo hofu ilivyozidi kuongezeka zaidi na zaidi moyoni mwake.
Hakuwahi kutoa mimba lakini alijua fika matatizo ambayo walikuwa wakiyapata wanawake ambao walikuwa wakitoa mimba. Mara nyingi njia za kutolea mtoto zilikuwa zikiharibika huku wakati mwingine mishipa ya damu ikikatika jambo ambalo lilikuwa likisababisha damu kutoka mfululizo na kutoa vidonda sehemu za siri.
Kadri alivyokuwa akifikiria hivyo na ndivyo ambavyo hofu ilivyozidi kumshika zaidi na zaidi. Moyoni mwake kulikuwa na mvutano mkubwa, wakati mwingi alikuwa akisikia kwamba kile ambacho alikuwa akitaka kukifanya ndicho kilikuwa kitu sahihi lakini upande mwingine ulikuwa ukimuonya kufanya kile ambacho alikuwa akitaka kukifanya.
Jamala alikuwa akichanganyikiwa zaidi, hakujua ni upande gani ambao alitakiwa kukubaliana nao. Aliendelea kubaki benchii pale mpaka pale alipoitwa na Dokta na kuingia ndani ya ofisi nyingine ambayo ilikuwa na kitanda kidogo na kutakiwa kulala huku akiitoa nguo yake ya ndani na kuipanua miguu yake.
Jamala akafanya kama alivyoambiwa huku bado akionekana kuwa na wasiwasi mkubwa. Dokta akatoka na aliporudi, alikuwa tayari kwa kila kitu. Uso wa Jamala ulikuwa ukionyesha wasiwasi mkubwa jambo ambalo lilimfanya Dokta kumshangaa.
“Mbona upo hivyo?” Dokta alimuuliza.
“Vipi?”
“Unaonekana kuwa na hofu”
“Hapana. Sina hofu”
“Hautakiwi kuwa hivyo. Kuwa huru, wala hauwezi kupata tatizo lolote lile. Nina ujuzi mkubwa na kazi hii. Kwanza hela yangu ipo wapi?” Dokta alimwambia na kumuuliza na Jamala ambaye akachukua kiasi kile cha fedha alizokuwa amefunga kwenye pindo la khanga na kumgawia Dokta kiasi kile cha fedha ambacho kilikuwa kikihitajika.
“Nakwenda kuanza kazi sasa”
“Sawa” Jamala alijibu.
Bado mvutano wa pande mbili moyoni mwake ulikuwa ukiendelea kama kawaida. Upande mmoja ukaonekana kushinda kwa wakati huo. Ghafla Jamala akabana miguu yake na kisha kushuka kitandani huku akionekana kuwa na haraka hali ambayo ilionekana kumshagaza Dokta kupita kiasi.
“Vipi tena?” Dokta aliuliza huku akionekana kushangaa.
“Hapana. Siwezi” Jamala alijibu huku akimtaka Dokta amrudishie fedha zake na kuondoka mahali hapo.
Dokta hakuonekana kumuelewa kabisa, alikuwa akimwangalia huku akimshangaa kutokana na uamuzi wake kubadilika katika hatua za mwisho za kufanya jambo lile. Dokta hakuwa na kipingamizi, alichokifanya ni kuzichukua zile fedha ambazo alikuwa amekwishaziweka mfukoni na kisha kumrudishia Jamala ambaye kwa haraka akatoka ndani ya chumba hicho na kuanza kukimbia.
Jamala alikuwa akikimbia kuelekea nyumbani kwao huku akilia kupita kawaida. Alikuwa akijuta kwa kuchukua uamuzi wa kwenda kuutoa ujauzito ule katika maabara ile. Kitendo kile ambacho alikuwa akitaka kifanyike tayari kilionekana kuwa kosa kubwa na dhambi kwa Mungu ambaye alikuwa akimuabudu.
Muda wote alikuwa akiyalaumu maamuzi yale ambayo alikuwa ameyachukua. Bado Jamala alikuwa akkikimbia, aliendelea kukimbia mpaka kufika nyumbani kwao na kuingia ndani ya chumba chake. Mara mama yake akaingia ndani ya chumba chake na kutaka kujua ni kitu gani ambacho kilikuwa kimetokea. Mama yake, Bi Asha akaanza kupiga hatua na kumsogelea kitandani pale alipokuwa amelala.
“Kuna nini Jamala?” Bi Asha alimuuliza.
Jamala hakutaka kujibu chochote kile, bado alikuwa akiendelea kulia kupita kawaida. Mto mmoja ulikuwa umeficha uso wake. Moyo wake ulikuwa kwenye maumivu makali kupita kawaida, kile kitendo ambacho alikuwa akitaka kukifanya katika kipindi kilichopita bado kilionekana kumuumiza kupita kawaida.
“Kuna nini Jamala?” Bi Asha alirudia swali lake.
“Nina mimba” Jamala alijibu.
Bi Asha akabaki kimya, hakuonekana kuamini kile ambacho alikuwa amekisikia kwa wakati huo. Ukimya ukaanza kutawala ndani ya chumba kile. Tayari Bi Asha akajiona kuwa na bahati mbaya, watoto wake wawili ambao walikuwa dada zake Jamala walikuwa wamepata mimba na kujifungua huku baba wa watoto wale wakiwa hawajulikani nyumbani hapo.
Bi Asha alibaki akiwa amepigwa na mshangao, hakuamini kwamba mahusia yote ambayo alikuwa amempa Jamala kuhusiana na mimba za bahati mbaya kabla ya ndoa hayakuwa yamesaidia kitu chochote kile. Bi Asha akasimama na kuanza kutoka ndani ya chumba kile huku dhahiri akionekana kukasirika.
“Nisamehe mama” Jamala alimwambia Bi Asha ambaye alikuwa akitoka nje.
Siku ziliendelea kukatika zaidi na zaidi huku nayo miezi ikizidi kusogea. Miezi tisa ikatimia na hatimae Jamala kuelekea hospitalini kwa ajili ya kujifungua. Bi Asha ndiye ambaye alikuwa mtu pekee ambaye alikuwa akimsaidia kwa wakati huo japokuwa bado alikuwa hajafurahishwa na kile kilichotokea.
Alipofika hospitalini, akajifungua salama mtoto wa kiume, mtoto ambaye alikuja kusababisha mambo mengi duniani, mtoto ambaye alisababisha umwagaji wa damu katika mataifa makubwa, huyu ndiye alikuwa mtoto ambaye alisababisha vurugu, mauaji na fujo za kila aina duniani, mtoto huyu ndiye ambaye alionekana kuwa tofauti na watu wengine.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
**********************************************
Tayari Jamala akawa mzazi. Mtoto wake wa kiume akaamua kumpa jina la Abuubakari. Maisha kama mzazi yakaanzia mahali hapo. Muda mwingi alikuwa akiaa pamoja na mtoto wake huku akiendelea kumpa huduma kama alivyotakiwa kufanya.
Maisha hayakuwa rahisi hata kidogo, muda mwingi Jamala alikuwa akimfikiria Selemani ambaye mpaka katika kipindi hicho alikuwa kimya kabisa. Jamala ndiye alikuwa mama wa mtoto huyo na yeye ndiye alikuwa baba wa mtoto huyo. Mama yake, Bi Asha alikuwa akijitahidi kwa hali na mali kumsaidia Jamala katika kumtunza Abuu.
Kadri siku zilivyozidi kwenda mbele na ndivyo ambavyo maisha yalivyozidi kuwa magumu hali iliyompelekea Jamala kuanzisha biashara ndogo ya genge la viungo mbalimbali pamoja na mboga za majani. Kwa asilimia chache maisha yakaanza kubadilika, Jamala akaanza kupata nafuu katika maisha yake na hata wakati mwingine kununua dawa mbalimbali ambazo alikuwa akiambiwa kuzinunua kila alipokuwa akimpeleka Abuu kliniki.
Uzuri ambao alikuwa nao Jamala katika kipindi hicho haukuwepo tena, mwili wake ulionekana kuchoka kupita kawaida. Matiti yake yakawa makubwa na mwili wake kupungua sana. Mabadiliko hayo ya mwili yakawafanya watu wengine kumwangalia kwa jicho la tatu, alionekana kutokustahili kupata mtoto katika umri ambao alikuwa nao kwa wakati huo..
Mara kwa mara Jamala alikuwa akihudhuria kliniki katika hospitali ya Halmashauri ya Tandale na kuungana pamoja na wazazi wengine. Biashara zake ndogo ndogo bado zilikuwa zikiendelea kama kawaida, fedha ambazo alikuwa akizipata ndizo ambazo zilikuwa zikiyaendesha maisha yake nyumbani hapo.
Selemani hakuonekana nyumbani hapo, hali ilionyesha kama hakuwa na taarifa kama kwa wakati huo Jamala alikuwa amejifungua mtoto wa kiume. Moyo wa Jamala ulikuwa ukimuuma sana kiasi ambacho alikuwa akijuta sababu zilizompelekea kuwa na mahusiano na mwanaume kama Selemani. Kila siku alikuwa mtu wa kuhuzunika tu, aliuhisi moyo wake ulikuwa kama umechomwa na msumali wa moto.
Kwa kipindi hicho wala hakumpenda tena Selemani, alimchukua hata zaidi ya alivyokuwa akimchukia shetani. Mapenzi ambayo alikuwa nayo kwa Selemani, kwa wakati huo hayakuwepo tena. Jamala alijiona kutengwa, alijua fika kwamba kama angeshirikiana na Selemani katika kumtunza mtoto Abuubakari wala kusingekuwa na tatizo lolote lile.
Siku ziliendelea kukatika, miezi ikaendelea kukatika na hatimae mwaka mzima kupita. Abuu akawa amefikisha umri wa mwaka mmoja. Hapo ndipo ugonjwa mbaya wa degedege ulipomuanza. Muda wote mwili wake ulikuwa ukitetemeka kupita kawaida huku mboni yake nyeusi ya jicho ikiwa haionekani kabisa.
Ugonjwa ule ukaonekana kumtisha sana Jamala jambo ambalo lilimfanya kuogopa. Japokuwa alikuwa akiendelea kumpeleka mtoto wake hospitalini, kesho yake hali ilirudi na kuwa vile vile. Madaktari wakamshauri kununua dawa kwa ajili ya ugonjwa ule ambao kila ulipokuwa ukimpata, alikuwa akiyagongagonga meno yake hali ambayo ilileta hofu zaidi.
“Itakupasa kumuwekea kijiko kila wakati meno yake yanapogonganagongana” Nesi alimwambia Jamala.
“Hiyo itasaidia nini?” Jamala aliuliza.
“Kwa sababu ya ulimi wake. Anapogongagonga meno yake machache, kuna uwezekano ulimi ukaja mpaka katika mafizi yake, atakapougonga ulimi huo kunaweza kumletea matatizo” Nesi alimwambia Jamala.
“Sawa. Nitafanya hivyo. Na vipi kuhusu hizo dawa za degedege? Wanauza kiasi gani?” Jamala aliuliza huku akiangalia karatasi ambayo alikuwa amepewa.
“Wanauza shilingi elfu mbili” Nesi alijibu.
“Mmmh!” Jamala aliguna.
“Mbona umeguna?”
“Gharama kubwa sana. Sijui kama nitaweza kuzimudu” Jamala alimwambia nesi.
Gharama zile zilionekana kuwa kubwa sana, kiasi cha shilingi elfu mbili ndicho ambacho kilikuwa faida ya biashara ambayo alikuwa akiifanya nyumbani hapo. Faida hiyo ndio alikuwa akiigawa katika chakula pamoja na matumizi mengine madogo madogo.
Hali haikupata unafuu wowote ule, kila siku maisha yalikuwa ya shida kupita kawaida kiasi ambacho wakati mwingine Jamala alikuwa akijuta sababu zilizompelekea kukubali kumzaa mtoto Abuubakari badala ya kuitoa mimba ile.
“Hali itaendelea hivi hadi lini mama? Kila siku maisha yanaendelea kuwa ya shida hivi. Shida mpaka lini?” Jamala alimuuliza mama yake, Bi Asha kwa uchungu huku akipanga mafungu ya nyanya.
“Hakuna kitakachodumu milele Jamala” Bi Asha alijibu.
“Nafahamu mama. Naona mambo yanazidi kuwa magumu zaidi” Jamala alimwambia mama yake, Bi Asha.
“Kuna siku yatakuwa mazuri. Amini kwamba Allah yupo na kuna siku tu tutafurahi” Bi Asha alimwambia Jamala.
Maisha yalikuwa yakiendelea zaidi na zaidi. Hakukuwa na unafuu hata kidogo, kila siku walikuwa wakiishi maisha ya tabu ambayo hawakuwa wakiyapenda kabisa. Biashara haikuongezeka zaidi, iliendelea kuwa vile vile kama ambavyo ilivyokuwa katika kipindi cha nyuma.
Mwaka wa pili ukakatika, ugonjwa ule wa degedege ambao ulikuwa ukimwandama mtoto Abuu ukaongezeka zaidi na zaidi. Kwa wakati huu hali ikaonekana kuwa mbaya zaidi. Kila wakati ugonjwa ule ulipokuwa ukimshika, alikuwa akitetemeka zaidi na zaidi huku macho yake yakiwa meupe kupita kawaida.
Jamala hakuonekana kuwa na raha, ugonjwa wa degedege ambao ulikuwa ukimuandama sana mtoto wake ndio ambao alikuwa akiuchukia kuliko magonjwa yote. Safari za kwenda hospitalini hazikumuisha, mara kwa mara alikuwa akielekea hospitalini kwa ajili Abuu kupatiwa matibabu.
Maisha yaliendelea kuwa ya tabu kama kawaida. Mwaka wa tatu ukakatika na hapo ndipo Abuu alipoanza shule ya chekechea. Abuu alikuwa mtoto mtundu ambaye wala hakuwa akitulia darasani. Mara kwa mara Jamala alipokuwa akienda shuleni pale na kumuacha, Abuu alikuwa akilia tu.
Mwaka wa nne ukaingia huku Abuu akiendelea na elimu yake ya chekechea. Kwa sababu alionekana kuwa mtoto mtundu, muda wote walimu walikuwa karibu nae kuliko watoto wengine wote. Kidogo hali ya Abuu kwenda shuleni ikamfanya hata Jamala kupumzika huku akifanya kazi zake kama kawaida bila ya kubughudhiwa na fujo za Abuu ambaye alionekana kuzidi kuwa mtundu sana.
Hapo ndipo Jamala alipoamua kuanzisha biashara nyingine ya kuuza mkaa mtaani alipokuwa akiishi. Ingawa mtaji wake ulikuwa mdogo lakini akaweza kuanza kidogo kidogo mpaka pale alipofanikiwa na hatimae biashara ile kuwa kubwa. Mpaka kufikia hatua hiyo, kidogo maisha yake yakaanza kubadilika.
Mara kwa mara alikuwa akiuziwa magunia ya mkaa kutoka katika magari makubwa ambayo yalikuwa yakitoka mikoani huku yakiwa na magunia mengi na makubwa. Biashara ile iliendelea zaidi na zaidi, alikuwa akipata fedha za kutosha ambazo zilimfanya kuyarahisisha maisha yake kila siku.
Mwaka wa tano ukaingia. Abuu akajifunza kusoma na kuandika japokuwa hakuwa na uwezo mkubwa zaidi. Penseli ambayo alikuwa akipewa mara kwa mara alikuwa akitafuna ufutio pamoja na penseli nzima. Utundu wake haukukoma kabisa, bado alikuwa akiendelea kuwasumbua walimu wake.
Kila alipokuwa akirudi kutoka shuleni, Jamala hakutaka kuendelea kukaa nae mahali hapo, alichokifanya ni kumuanzisha madrasa iliyokuwa katika mtaa huo. Jamala alikuwa akijitahidi kufanya mambo mengi katika maisha yake pamoja na mtoto wake, alijua fika kwamba hakuwa na uwezo wa kifedha kabisa lakini katika kipindi hicho alihitajika kumtunza zaidi mtoto wake.
Kutokana na utundu wake pamoja na kutembea tembea ovyo, Abuu akajichoma na kipande cha chupa mguuni. Kilio kikaanza kusikika mpaka pale ambapo Jamala akafika mahali pale na kisha kumchukua na kumpeleka hospitalini ambapo kidonda kile kikasafishwa.
Siku zikaendelea kwenda mbele, kidonda kile kikaonekana kutokupata nafuu jambo ambalo lilimfanya mara kwa mara kutakiwa kumpeleka Abuu hospitalini kwa ajili ya kuatiwa matibabu ikiwa ni pamoja na kuchomwa sindano mguuni.
Katika kipindi cha nyuma Jamala alikuwa akimpeleka Abuu katika hospitali ya Halimashauri ya mtaa wa Tandale ila kutokana na foleni kubwa hospitalini hapo akaamua kuanza kumpeleka katika maabara ndogo ndogo. Huko ndipo ambapo matatizo yakatokea, Abuu akachomwa sindano ya mguuni, sindano ambayo ilichomwa vibaya na hivyo kuufanya mguu wake wa kulia kulemaa.
Hilo likaonekana kuwa kama pigo, moyo wa Jamala ukaumia kupita kawaida. Hakukuwa na jinsi tena, mtoto Abuu akanunulia gongo dogo kwa ajili ya kutembelea. Mguu wake ukalemaa kwa asilimia mia moja.
“Inaniuma kumuoa mtoto wangu kuwa hivi. Lakini kwa nini mimi?” Jamala alikuwa akijiuliza kila alipokuwa akimwangalia Abuu katika kipindi ambacho Abuu alikuwa akitembelea gongo dogo.
***************
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Maisha yalikuwa yakiendelea kama kawaida huku Jamala akijitahidi kumtunza mtoto wake katika mazingira ya shida. Hakuwa radhi kumuona mtoto wake akikaa na njaa kwa muda mrefu, alikuwa akipigania maisha kila siku huku kwa kiasi fulani mafanikio yakianza kuonekana. Baada ya kufikisha miaka saba, Abuu akaanza darasa la kwanza katika shule ya msingi ya Makurumla iliyokuwa Mwembe Chai jijini Dar es Salaam.
Uwezo wake wa kusoma na kuandika uliwafanya walimu wengi kumpenda huku wakijaribu kumwambia kwamba alikuwa na nafasi ya kuwasaidia wanafunzi wengine kusoma na kuandika. Abuu akaonekana kuwa mfano wa kuigwa shuleni pale, japokuwa alikuwa kilema ambaye alikuwa akitembelea gongo lakini uwezo wake ulimfanya kuonekana kuwa mtu wa tofauti sana.
Abuu aliendelea kusoma katika shule hiyo mpaka pale ambapo alifika sarasa la sita. Jamala alijitahidi kila siku kumficha Abuu kuhusiana na baba yake, hakutaka kumwambia kwamba baba yake alikuwa ameikataa mimba ile katika kipindi cha nyuma kwani kwa kufanya hivyo aliamini kwamba Abuu angeumia kupita kawaida na hivyo kumuharibia hata maendeleao yake shuleni hapo.
Uwezo wake ulikuwa mkubwa sana, Abuu akawa miongoni mwa wanafunzi ambao walikuwa wakilipenda sana somo la Sayansi. Kuongoza kwake shuleni hapo lilikuwa jambo la kawaida sana. Mara kwa mara alikuwa akipewa zawadi na walimu wake kama sehemu mojawapo ya kumuhamasisha kwa kile ambacho alikuwa akikifanya.
Hakukuwa na mwanafunzi ambaye alikuwa akiongoza sana shuleni hapo kwa wanafunzi wa darasa la sita kama Abuu ambaye kadri siku zilivyokuwa zikizidi kwenda mbele na ndivyo ambavyo alikuwa akiongoza zaidi na zaidi. Ingawa Abuu alikuwa akipendwa sana na walimu lakini baadhi ya wanafunzi hawakuonekana kumpenda kabisa.
Hali ya kutokupendwa na baadhi ya wanafunzi ilitokana na uwezo wake wa darasani lakini wengine walikuwa wakimchukia kwa sababu ya ulemavu ambao alikuwa nao. Mara kwa mara Abuu alikuwa akilia tu kila alipokuwa akiambiwa maneno yaliyokuwa ya dhihaka juu ya hali ambayo alikuwa nayo mwilini mwake.
Mama yake, Jamala pamoja na bibi yake, Bi Asha ndio ambao walikuwa wakimfariji kwa kila hali ambayo alikuwa akipitia katika kipindi hicho. Maisha yaliendelea huku Abuu akizidi kuongoza zaidi na zaidi. Uwezo wake mkubwa wa darasani uliwafanya hata walimu wengine kumshangaa kupita kawaida, hakukuwa na mwalimu ambaye aliamini kama kuna mwanafunzi ambaye alikuwa na uwezo mkubwa kama ule.
Mwaka ukakatika na hatimae kuingia darasa la saba. Hapo Abuu akaongeza kasi zaidi na zaidi, uwezo wake ukaongezeka na kuwa mara tatu zaidi ya vile ambavyo ulikuwa kabla. Abuu hakuwa mchoyo, muda mwingi alikuwa akiwafundisha wanafunzi wengine masomo mbalimbali darasani. Miezi ikakatika mpaka pale ambapo wanafunzi wa darasa la saba walipofanya mtihani wa Taifa.
Mitihani ilifanyika huku wanafunzi waliokuwa na uwezo akiwepo Abuu wakiwa na uhakika kwamba ni lazima wangefaulu mitihani hiyo. Japokuwa Abuu alikuwa na ulemavu lakini hakutaka kumuona mama yake akifanya kazi peke yake, siku zote alikuwa akimsaidia mama yake kazi mbalimbali za nyumbani hapo.
“Kuna siku nitakuwa tajiri sana mama” Abuu alimwambia mama yake, Jamala.
“Kuwa tajiri utaweza lakini yakupasa kusoma sana” Jamala alimwambia Abuu.
“Kwani utajiri mpaka usome sana mama?”
“Hapana. Unaweza kuwa tajiri bila kusoma hata darasa moja” Jamala alimwambia Abuu.
“Nitataka niwe tajiri mkubwa sana maishani mwangu. Nitataka nikununulie nyumba nzuri pamoja na gari” Abuu alimwambia mama yake, Jamala.
Hayo ndio yalikuwa mawazo yake ya kila siku. Abuu alionekana kuchoka sana kuishi katika maisha ambayo alikuwa akiishi kwa wakati huo. Biashara ya mkaa ambayo mama yake alikuwa akiifanya haikuonekana kumfurahisha. KIla alipokuwa akiiangalia nyumba ambayo walikuwa wakiishi hakuonekana kuipenda kabisa.
Alitamani kumjengea mama yake nyumba kubwa na ya kifahari pamoja na kumnunulia gari la kifahari ambalo litawafanya watu wote ambao hawamheshimu kuanza kumheshimu. KIla kitu ambacho alikuwa akikifikiria kwa wakati huo, elimu ndio aliiona kuwa njia sahihi na ya urahisi kupata kile ambacho alikuwa akikitamani sana katika maisha yake.
“Nataka kuliona kaburi la baba yangu” Abuu alimwambia mama yake, Jamala.
“Unasemaje?” Jamala aliuliza kwa mshtuko.
“Nataka kuliona kaburi la baba yangu” Abuu alimwambia Bi Jamala.
Jamala hakusema kitu, alibaki kimya kwamuda huku akianza kutokwa na machozi. Maneno ambayo aliongea Abuu yalionekana kumkumbusha maisha yake ya nyuma. Akaanza kumkumbuka Selemani ambaye aliikataa mimba ile katika kipindi ambacho alimpa taarifa kuhusiana na ujauzito ule.
“Mbona unalia mama?” Abuu alimuuliza mama yake, Bi Jamala.
“Inaniuma” Jamala alijibu.
“Pole sana mama” Abuu alimwambia mama yake.
Abuu hakutaka kuendelea kuuliza swali lolote lile kuhusiana na baba yake, alijua fika kwamba mama yake alikuwa akiumia sana kila alipokuwa akimuuliza kuhusu baba yake ambaye aliambiwa kwamba alikuwa amefariki katika kipindi ambacho alikuwa mdogo. Abuu akabaki kimya, hakutaka kuongea kitu chochote kile kuhusiana na baba yake japokuwa kila siku alikuwa na hamu kubwa ya kuliona kaburi hilo la baba yake.
Baada ya miezi kadhaa, matokeo ya darasa la saba yakatolewa. Wanafunzi wengi wa shule ya Makurumla walikuwa wamefaulu isipokuwa mtu mmoja tu ambaye alikuwa akiongoza sana darasani, Abuu Selemani. Hilo likaonekana kuwa kama pigo kubwa, baadhi ya walimu wakashtuka, wanafunzi wakashindwa kuelewa ni kitu gani ambacho kilikuwa kimetokea.
Kutokufaulu kwa Abuu kukaonekana kutokuwafurahisha sana walimu na wanafunzi, kuna mchezo fulani ukaonekana kuchezwa. Hilo lilikuwa pigo kubwa kwa Abuu ambaye alikuwa na uhakika wa asilimia mia moja kwamba angefaulu mtihani wa darasa la saba. Abuu akaonekana kutokuwa na furaha, amani ikapotea moyoni mwake, akaanza kushinda ndani akilia.
Jamala na Bi Asha ndio watu wa karibu ambao walikuwa wakimfariji katika kile ambacho kilikuwa kimetokea. Japokuwa alikuwa akifarijiwa lakini hakuweza kufarijika kabisa. Bado moyo wake ulikuwa na huzuni kupita kwaida.
Miezi ikakatika na hatimae wanafunzi wa kidato cha kwanza ambao walikuwa wamefaulu wakaanza kuelekea shuleni. KIla wakati Abuu alipokuwa akiwaangalia wenzake walivyokuwa wakielekea shuleni, alikuwa akibaki akilia tu.
“Nasikia matokeo yake aliuziwa mwanafunzi mwingine ambaye baba yake ana uwezo kifedha” Mwanamke mmoja alisikika akiongea huku wakimwangalia Abuu ambaye alikuwa amekaa kibarazani huku akiwa ameshika tama.
Hiyo ndio ambayo ilikuwa imetokea. Matokeo yake ambayo yalimuonyeshea kwamba alifaulu vizuri na kuchaguliwa kujiunga na shule ya Wavulana ya Kibaha yalikuwa yameuzwa na kupewa mwanafunzi mwingine. Hakukuwa na mtu aliyelifahamu hilo ingawa baadae siri ilionekana kuvuja kwa watu wengine.
Abuu hakusoma tena shule katika kipindi hicho zaidi ya kukaa nyumbani na kumsaidia mama yake kazi. Fedha za kumpeleka shule za kulipia hazikuwepo, hivyo alihitajika kubaki nyumbani mpaka pale ambapo mama yake angepata fedha na kisha kumpeleka katika shule ya kulipia na kuanza kidato cha kwanza.
“Hivi nitasoma tena mama?” Abuu alimuuliza mama yake.
“Utasoma tu. Nitakwenda kukopa fedha mpaka usome tena” Jamala alimwambia Abuu.
Jamala hakutaka kufanya kazi siku hiyo. Miezi miwili ilikuwa imekatika lakini Abuu hakuwa ameanza shule kidato cha kwanza. Alichokifanya Jamala ni kwenda katika shirika moja la mkopo na kisha kukopa kiasi cha shilingi milioni tano huku akikubaliana kuiweka hati ya nyuma yao kuwa kama bondi katika shirika hilo.
Fedha hizo ambazo walikuwa wamezipata ndizo ambazo ziliwafanya kupanua biashara yao zaidi ya kuuza mkaa na kisha kiasi kingine kumpeleka Abuu shuleni kuanza masomo kidato cha kwanza katika shule ya Sekondari ya Baptist iliyokuwa Magomeni jijini Dar es Salaam.
Hiyo ilionekana kuwa kama ndoto kwa Abuu, siku ya kwanza kuingia shuleni hapo na kuanza kusoma hakuonekana kuyaamini macho yake. Japokuwa alikuwa amechelewa kuanza masomo yake kwa muda wa miezi miwili baada ya masomo kuanza lakini wala hakuonekana kujali, kwake, alijiona kuwa afadhali alikuwa shuleni hapo.
Ulemavu wake ukawagawa wanafunzi, wengine hawakuonekana kuvutiwa nae, ulemavu ule kwake ukaonekana kuwa kama laana. Wanafunzi wengi walimchukulia Abuu kuwa mwanafunzi wa kawaida sana ambaye wala hakuwa na uwezo wowote darasani. Hakukuwa na mwanafunzi ambaye aliamini kwamba Abuu alikuwa na uwezo mkubwa, hakukuwa na mwanafunzi ambaye alifahamu kwamba uwezo wa Abuu haukutakiwa kumfanya kuwa katika shule hiyo, uwezo wake ulikuwa mkubwa ambao ungemfanya kuwa katika shule yenye watoto wenye vipaji, uwezo ambao ungewafanya wanafunzi wote kushangaa japokuwa alikuwa mlemavu wa mguu mmoja.
**********************************
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Maisha ya shule yalikuwa yakiendelea zaidi na zaidi. Hali ambayo ilikuwa ikitokea shuleni ilionekana kuwa kama changamoto katika maisha yake. Idadi kubwa ya wanafunzi walikuwa wamemtenga Abuu, ni idadi ndogo kabisa ya wanafunzi ndio ambao walikuwa wakionyesha upendo kwa Abuu.
Hali ile ilionekana kumuumiza kupita kawaida, muda mwingi alikuwa akionekana kuwa na mawazo. Katika maisha yake alikuwa akitamani sana kuingia shuleni na kisha kuanza masomo jambo ambalo aliamini lingempa furaha zaidi lakini katika kipindi hiki hali ikaonekana kuwa tofauti na matarajio yake.
Furaha yote ambayo alikuwa ameitarajia kuipata shuleni pale ilikuwa imepotea kabisa. Kutengwa na baadhi ya wanafunzi ikaonekana kutokumpa furaha kabisa. Ulemavu ambao alikuwa nao ndio ambao ulikuwa umemfanya kuwa katika hali ile. Ingawa wanafunzi wengi walikuwa wamemtenga huku wengine wakionekana kuwa karibu nae, ni mvulana John tu ndiye ambaye alionekana kuwa karibu nae sana.
John ndiye mwanafunzi ambaye alikuwa karibu nae sana, mara kwa mara walikuwa pamoja huku wakipiga stori pamoja. Ukaribu wao haukuwa nje ya darasa tu bali hata darasani walikuwa wakikaa karibu karibu sana. Urafiki ule ukaonekana kudumu zaidi na zaidi, John akaonekana kuwa mtu muhimu sana katika maisha ya Abuu shuleni pale.
John hakuwa ametoka katika familia ya kimasikini kama ilivyokuwa kwa Abuu, yeye alitoka katika familia ambayo ilikuwa na uwezo fulani kifedha. Fedha ambazo alikuwa akipewa kwa ajili ya matumizi ya shuleni, siku zote alikuwa akitumia pamoja na Abuu ambaye alikuwa hapewi fedha yoyote ya matumizi zaidi ya fedha ambayo alitakiwa kuitumia kama nauli mara aendapo na arudipo shuleni.
Urafiki wao ulikuwa mkubwa kiasi ambacho kiliufanya shule nzima kuuona urafiki ambao ulikuwa wa ajabu sana. Ulemavu ambao aliendelea kuwa nao Abuu ulionekana kuwa kama kero kwa wanafunzi wengine. Maneno mengi yalikuwa yakiongelewa lakini kwa Abuu hakuonekana kujali kitu chochote kile.
“Mmmh! Maisha haya yananifanya hata shule nimalize mapema niondoke” Abuu alimwambia John katika kipindi ambacho walikuwa wakinywa chai muda wa mapumziko.
“Kwa nini?” John aliuliza.
“Angalia watu wanavyoniangalia kwa jicho la chuki. Yaani kwa hali hii mpaka naichukia shule” Abuu alimwambia John.
“Usijali. Utamaliza shule tu na kuondoka mahali hapa” John alimwambia Abuu.
“Nitashukuru Mungu” Abuu alimwambia John.
Maisha ya shule yaliendelea zaidi na zaidi mpaka katika kipindi cha majaribio mbalimbali ya mitihani yalipoanza shuleni hapo. Majaribio yale yakafanyika na Abuu kuongoza kwa kiasi kikuba sana. Kila mwanafunzi alionekana kushtuka, hawakuamini kama Abuu angeweza kuongoza kwa kiasi kile na wakati alikuwa amechelewa kufika shuleni hapo.
Fitina zikaanza mahali hapo, wanafunzi wengi wakaanza kuwaambia walimu kwamba Abuu alikuwa akiingia katika chumba cha mtihani huku akiwa ameandika majibu ya mtihani katika gongo lake ambalo alikuwa akilitumia kutembelea. Maneno yale yakaonekana kumuumiza sana Abuu, mara kwa mara alikuwa akiitwa ofisini na kuulizwa na walimu juu ya zile tetesi.
“Sijawahi kufanya kitu kama hicho” Abuu alimwambia mwalimu Mshana.
“Sasa mbona kila mwanafunzi anasema hivyo?”
“Sijui kwa nini mwalimu. Sijawahi kudanganya katika chumba cha mitihani” Abuu alijitetea.
Mwalimu Mshana akachukua gongo ambalo alikuwa akilitumia Abuu kutembelea na kisha kuanza kuliangalia. Alichukua muda mrefu kidogo kuliangalia lile gongo kwa umakini, alipomaliza akamrudishia.
“Umekwishayafuta majibu ya mtihani ambayo uliyaandika?” Mwalimu Mshana alimwambia Abuu.
“Hapana mwalimu. Sijawahi kudanganya kwenye mtihani” Abuu aliendelea kujitetea.
“Sawa. Nenda. Mwisho wa siku tutakuja kujua ukweli. Na kama tukifahamu kwamba unadanganya kwenye mitihani, tutakufukuza shule” Mwalimu Mshana alimwambia Abuu.
Abuu akaondoka ndani ya ofisi hiyo, machozi yalikuwa yakimlengalenga, na alipofika nje ya ofisi hiyo tu, machozi yakaanza kutiririka mashavuni mwake. Moyo wake ulimuuma sana, hakuamini kama jitihada ambazo alikuwa akizifanya kusoma ndizo ambazo ziliwafanya wanafunzi kuhisi kwamba alikuwa akidanganya katika mitihani ya shuleni pale.
****
Baadhi ya wanafunzi wakabaki wakimwangalia Abuu ambaye alikuwa akitoka ndani ya ofisi ile ya walimu huku akilia. Wengi hawakujua ni sababu gani ambayo ilikuwa ikimliza Abuu katika kipindi kile japokuwa wengi wao walikuwa wakifurahia kuyaona machozi yake ambayo yalikuwa yakitiririka mashavuni mwake.
Abuu alitembea kwa mwendo wa taratibu huku akitumia gongo lake mpaka kuingia darasani. Akatulia kitini huku akiwa ameinamisha kichwa chake juu ya meza na kuendelea kulia. Maneno ambayo aliongea mwalimu Mshana yalionekana kumchoma kupita kawaida, kitendo cha kusingiziwa kudanganya katika chumba cha mitihani kilionekana kumuumiza sana moyoni mwake.
Kwa wanafunzi ambao walikuwa wakimchukia sana Abuu walionekana kuwa na furaha kupita kawaida, muda wote ambao walikuwa wakimuona Abuu akilia walionekana kuwa na furaha kupita kawaida. Abuu aliendelea kuwa katika hali ile mpaka pale rafiki yake, John alipokuja mahali hapo na kuanza kumfariji.
Maneno ya faraja ambayo alikuwa akiyaongea John ndio ambayo yalionekana kumuumiza sana Abuu, alimfanya kuendelea kulia zaidi na zaidi mahali pale. John hakuacha kumfariji rafiki yake, alijua fika kwamba alikuwa katika kipindi kigumu shuleni hapo, kwa hiyo ukaribu wake pamoja na faraja yake ni vitu ambavyo vingemfanya kumtia moyo katika kila hatua ambayo alikuwa akipitia shuleni pale.
Abuu hakutaka kuwa kimya, mara baada ya kufika nyumbani akaanza kumhadithia mama yake, Jamala juu ya kile ambacho kilikuwa kimeendelea shuleni kule. Jamala alionekana kuumia sana, maneno mbalimbali ambayo alikuwa akiambiwa mtoto wake yalikuwa yakimuumiza kupita kawaida.
“Mungu atakuwa pamoja nawe” Jamala alimwambia Abuu.
Siku zikaendelea kukatika, mitihani mingine ikazidi kufanyika shuleni pale. Hali haikuonekana kubadilika kabisa, bado Abuu alionekana kuwa juu kuliko wanafunzi wote wa kidato cha kwanza. Hali hiyo ndio ambayo iliwafanya walimu kuanza kumwangalia kwa mtazamo wa tofauti kabisa. Halikuwa jambo la kawaida kwa mwanafunzi yeyote shuleni pale kupata alama zote mia moja katika masomo yote saba.
Abuu akaitwa tena katika ofisi ya walimu, katika kipindi hali ilikuwa ni tofauti kabisa, hakuitwa kwa sababu kulikuwa na tetesi za kudanganya kwenye chumba cha mtihani bali walimu walikuwa wakitaka kufahamu mengi kutoka kwake na kumpongeza katika kile ambacho alikuwa amekifanya shuleni pale katika mitihani ile.
“Hongera sana” Mwalimu mkuu wa shule ile, Mkwasa alimwambia Abuu.
“Asante” Abuu alijibu.
Abuu akaonekana kuanza kuonyesha kile ambacho kilikuwa kichwani mwake katika kipindi hicho. Hakutaka kubaki nyuma katika masomo, alionekana kuwa mwanafunzi wa ajabu sana. Hakuwa akisoma sana kama wanafunzi wengine lakini kile ambacho alikuwa akikisoma au kufundishwa darasani kilikuwa akitoki kichwani mwake.
Uwezo wake wa kukumbuka na kuelewa ulikuwa ni wa hali ya juu sana jambo ambalo hata wanafunzi wengine wakapigwa na mshangao kupita kawaida shuleni pale. Huyu Abuu ambaye alikuwa mlemavu, huyu Abuu ambaye alikuwa akitengwa na wanafunzi wengi shuleni pale ndiye ambaye akawa lulu katika kipindi hicho.
Wanafunzi wengi wakahitaji msaada wake, walimu wengi ambao walikuwa wakiingia darasani na kufundisha, walikuwa wakimpa Abuu nafasi ya kuweza kuwafundisha wanafunzi wenzake pale ambapo hawakuwa wamepaelewa. Chuki ambazo zilikuwepo ndani ya mioyo mingine ya wanafunzi zikaanza kupotea, tayari Abuu akaonekana kuwa mtu muhimu sana katika masomo ya kila mwanafunzi.
Miezi ikaendelea kukatika mpaka mitihani ya mwisho wa mwaka kuingia. Kama kawaida yake, Abuu alikuwa amefanya vizuri kwa asilimia mia moja jambo ambalo lilionekana kuwashangaza sana walimu. Tayari Abuu akaonekana kuwa mtu muhimu ambaye hakutakiwa kupotezwa shuleni hapo, walimu wakahitajika kuwa karibu na Abuu.
“Huu mtihani hadi aibu” Mwalimu wa hesabu, Kenani aliwaambia walimu wenzake.
“Vipi tena?” Mwalimu Lucy aliuliza.
“Huyu Abuu Selemani amepata hesabu zote. Yaani nilijaribu kutoa hesabu ngumu lakini amepata zote” Mwalimu Kenani aliwaambia walimu wenzake.
Hali hiyo haikuwa kwa mwalimu wa hesabu tu bali hata walimu wengine walikuwa wakizungumzia kitu hicho hicho. Mwisho wa mwaka huo Abuu alionyesha makali yake katika masomo yote shuleni. Hali ya kuwa na uwezo darasani haikuishia hapo, ilizidi kuendelea zaidi na zaidi mpaka pale walipoingia kidato cha pili na cha tatu.
Katika miaka yote hiyo mitatu bado Abuu alikuwa akiendelea kuongoza kama kawaida yake. Wanafunzi wengi ambao walikuwa wakimtenga kutokana na ulemavu wake kwa wakati huu asilimia kubwa walikuwa marafiki zake ambao alikuwa akiwasaidia kila siku katika masomo.
Kila mwanafunzi alikuwa na hamu ya kuwa karibu na Abuu ambaye alionekana kuwa na akili za kuzaliwa. Abuu hakutaka kuwa mbinafsi, bado alikuwa akiendelea kuwafundisha wanafunzi wenzake pale ambapo palikuwa pakihitajika msaada wake.
Wasichana wengi wakatokea kuvutiwa na Abuu ambaye alionekana kuwa lulu shuleni hapo na hata katika shule za jirani ambazo huko napo alikuwa akiwaongozea katika kila mitihani ya wilaya ambayo ilikuwa ikifanyika mara kwa mara.
Japokuwa alikuwa na uwezo mkubwa darasani na kumfanya kufaulu vizuri lakini moyo wake ulikuwa kama binadamu wengine. Kama walivyo binadamu wengine, Abuu nae akatokea kumpenda msichana mmoja ambaye alitokea kuvutiwa nae kupita kawaida. Msichana huyu alikuwa Jasmin Hamisi.
Moyo wa Abuu ulikuwa kwenye mapenzi kwa asilimia mia moja kwa msichana Jasmin ambaye alikuwa hafahamu kama mvulana ambaye alikuwa akiongoza sana shuleni hapo tayari alikuwa ameangukia katika mapenzi yake. Kutokana na kutokuwa mtu wa wasichana kama vijana wengine, Abuu alikuwa akimuogopa sana Jasmin ambaye alikuwa na mvuto mkubwa machoni mwake.
Kila siku Abuu alikuwa akijifanya kuwafundisha wanafunzi wengine lakini huku lengo lake likiwa moja tu, kuongea na Jasmin ambaye alionekana mkimya kupita kawaida. Moyo wake ulikuwa na hofu sana, hakujua kama ingetokea siku ambayo angeweza kusimama mbele ya Jasmin na kumwambia kwamba alikuwa akimpenda sana.
Ni mara nyingi alikuwa akimuona Jasmin akiwa amekaa peke yake huku akiwa amezungukwa na viti vilivyokuwa wazi lakini Abuu hakuwa na uwezo wa kumfuata Jasmin na kumwambia ukweli juu ya jinsi alivyokuwa akijisikia moyoni mwake kwa wakati huo.
Jasmin ndiye ambaye alikuwa moyoni mwake, kila alipokuwa akilala kitandani, mawazo yake yalikuwa yakimfikiria Jasmin tu. Kila siku usiku alikuwa akikata shauri kwamba siku inayofuatia ilikuwa ni lazima amfuate Jasmin na kumwambia ukweli juu ya jinsi alivyojisikia, lakini alipofika shule na kumuona Jasmin, woga ulirudi na hivyo kutokumfuata.
“Mbona unamuangalia sana Jasmin?” John alimuuliza Abuu ambaye muda mwingi alikuwa akimkodolea macho Jasmin.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Ninampenda sana” Abuu alijibu kwa sauti ya chini.
“Kama unampenda mfuate tu umwambie ukweli” John alimwambia.
“Unafikiri ni kazi rahisi? Ni bora nipewe hesabu za kidato cha sita nizifanye nitaweza kuliko kumfuata Jasmin na kumwambia kuhusu hisia nilizo nazo moyoni mwangu juu yake” Abuu alimwambia John.
“Kwa hiyo utateseka mpaka lini juu yake?”
“Nafikiri mpaka pale nitakapoamua kumwambia ukweli”
“Lini sasa?”
“Sijui” Abuu alijibu kinyonge.
Hiyo ndio ilikuwa hali ambayo ilizidi kuendelea zaidi na zaidi moyoni mwa Abuu. Jasmin, kwake alionekana kuwa kama malaika ambaye alishushwa duniani kwa makusudi ya kumjaribu yeye. Urembo wa Jasmin ulikuwa ukizidi kuuteka moyo wake kila siku. Kumfuata na kumwambia ukweli lilionekana kuwa jambo gumu sana kufanyika.
“Au nimwandikie barua?” Abuu alimuuliza John.
“Mmmh! Usifanye hivyo. Ushahidi huo” John alimwambia Abuu.
“Ushahidi! Kivipi?”
“Akikukataa na kuamua kuipeleka kwa walimu. Hauoni ni tatizo hilo” John alimwambia Abuu.
“Kwa hiyo nifanye nini sasa?”
“Mfuate na kumwambia ukweli” John alimwambia Abuu.
“Haiwezekani hata kidogo. Hilo ni jambo gumu sana kufanyika kwani kama nikifanya hivyo halafu akinikataa, vile vile anaweza kwenda kuwaambia walimu” Abuu alimwambia John.
“Afadhari iwe hivyo, hapo unaweza kujitetea kwamba haukumwambia maneno kama hayo” John alimwambia.
“Unafikiri walimu wataniamini?”
“Kwa nini wasikuamini?”
“Kwa sababu Jasmin si kichaa mpaka aseme hivyo”
“Kwa hiyo unaona uamuzi wa kuandika barua ndio mzuri?”
“Ndio. Kwani naamini siwezi kuionea aibu karatasi wala kalamu”
“Acha hizo Abuu. Hilo litakuwa tatizo kubwa. Kama ukishindwa kuongea nae, achana nae kuliko kuamua kumwandikia barua” John alimwambia Abuu.
“Kwa hiyo unashauri kumwambia mdomo kwa mdomo ndio uamuzi sahihi?”
“Ndio maana yake”
“Basi ngoja nijaribu. Mmmh! Ila naogopa sana mpaka nashangaa wale wanaweza huwa wanakuwa na moyo gani” Abuu alimwambia John na kisha kuchukua gongo lake na kuanza kutoka nje huku akijipitisha karibu na kiti alichokuwa amekalia Jasmin.
Mateso yakaongezeka zaidi moyoni mwake, kuumia kwake kukaongezeka zaidi na zaidi. Wivu wa mapenzi ukazidi kumkamata kila alipokuwa akimuona Jasmin akiongea na wavulana wengine iwe wa mule darasani au wavulana wengine wa vidato vingine. Bado alikuwa akitamani sana kumfuata na kumwambia ukweli lakini tatizo lilikuwa moja tu, uoga.
Ingawa alikuwa kidato cha tatu lakini uoga juu ya wasichana ulikuwa mkubwa moyoni mwake, kila alipokuwa akimuona Jasmin machoni mwake, alikuwa akitetemeka huku mapigo ya moyo wake yakidunda kwa kasi sana. Mzunguko wake wa damu ulikuwa mkubwa kupita kawaida, Jasmin alionekana kuwa mtu wa tofauti moyoni mwake.
Siku ziliendelea kukatika mpaka walipomaliza kidato cha tatu na kisha kuingia kidato cha nne. Bado hali iliendelea kuwa vile vile. Shuleni alikuwa akiendelea kuwaongoza lakini na moyo wake uliendelea kuumia zaidi na zaidi.
Miezi ikakatika mpaka kufikia siku ambayo aliamua kumwambia Jasmin ukweli. Hakujali ni kitu gani kingetokea au angeonekana vipi mbele ya macho ya msichana huyo, kitu ambacho alikuwa akikitaka kwa wakati huo ni kuushusha mzigo mzito ambao ulikuwa moyoni mwake kwa zaidi ya mwaka mmoja na nusu.
“Naweza kuongea nawe?” Lilikuwa swali ambalo Abuu alimuuliza Jasmin ambaye alionyesha tabasamu pana.
“Yeah! Unaweza. Kuna nini?” Jasmin alimuuliza Abuu huku akitoa tabasamu pana ambalo lilimchanganya sana Abuu.
“Ningependa kuongea nawe kipindi hiki” Abuu alimwambia Jasmin.
“Kuongea na mimi! Kuhusu nini?” Jasmin alimuuliza Abuu.
“Mahusiano” Abuu alijibu huku kwa mbali kijasho chembamba cha uoga kikianza kuonekana usoni mwake.
“Mahusiano gani?” Jasmin aliuliza.
Abuu akakaa kimya kwa muda, swali ambalo alikuwa ameulizwa mahali hapo lilikuwa jepesi sana kujibika lakini kulitoa jibu lake lilihitaji ujasiri wa hali ya juu. Hali ya uoga ikazidi kumuingia zaidi Abuu, mapigo yake ya moyo yakazidi kudunda zaidi, ujasiri wote ambao alikuja nao ukaanza kupotea. Katika kipindi hicho aliombea kitu chochote kitokee darasani hapo ambacho kingemfanya kuondoka mbele ya uwepo wa Jasmin.
“Abuu” Jasmin alimuita.
“Naam”
“Mbona hauongei tena?” Jasmin alimuuliza.
“Najaribu kukufikira kidogo” Abuu alimjibu.
“Kunifikiria?”
“Ndio”
“Kunifikiria kuhusu nini?”
“Uwezo wako wa kusoma hisia, yaani saikolojia ya mtu” Abuu alijibu.
“Mmmh! Mbona unanichanganya?”
“Usichanganyikiwe. Jaribu kusoma saikolojia ya mtu Jasmin” Abuu alimwambia Jasmin na kisha kuchukua gongo lake na kuondoka mahali hapo.
Jasmin alibaki kimya huku akimwangalia Abuu ambaye alikuwa akiondoka taratibu kukifuata kiti chake. Maneno ya mwisho ambayo alikuwa ameyaongea yalionekana kuanza kujenga mambo fulani moyoni na akilini mwa Jasmin. Aliyafikira maneno yale kwa muda wa zaidi ya dakika moja, moyo wake ukaanza kupata hisia fulani juu ya maneno ambayo aliongea Abuu.
“Ananipenda.” Jasmin alijisemea huku uso wake ukionyesha kuwa na tabasamu.
Abuu alipokifikia kiti chake, akakikalia huku John akiwa pembeni yake akicheka kisirisiri. Abuu alionekana kutokuwa katika hali ya kawaida kabisa, alionekana dhahiri kuwa na hofu kubwa moyoni mwake. Akajiona kuutua mzigo mkubwa ambao ulikuwa umemuelemea moyoni mwake.
“Vipi?” John alimuuliza Abuu.
“Mmmh! Moyo unavyodunda……..naweza kufa muda wowote ule” Abuu alijibu na wote kuanza kucheka kisiri.
*******************************
Siku ziliendelea kukatika zaidi na zaidi, Abuu hakutaka kuongea tena na Jasmin japokuwa alikuwa amekwishaushusha mzigo mkubwa ambao ulikuwa moyoni mwake. Wote wawili wakabaki wakiangaliana kimapenzi tu darasani, moyo wa Jasmin tayari ukaanza kuvutiwa na Abuu ambaye bado makali yake ya masomo yalikuwa juu.
Abuu aliendelea kumuogopa Jasmin huku nae Jasmin akimuogopa Abuu. Kuogopana huko ndio ambacho kiliwafanya kutokuongea kabisa japokuwa mioyo yao ilikwishaanza kupendana. SIku zikaendelea zaidi na zaidi mpaka kufika kipindi ambacho ugonjwa wa kansa ya ziwa ulipoanza kumsumbua mama yake Abuu, Jamala.
Ugonjwa huo ulianza taratibu sana, kidonda kidogo kilikuwa kimetokeza karibu kabisa na chuchu yake. Kwa mara ya kwanza Jamala alikichukulia kuwa kidonda cha kawaida sana. Akaanza kwenda hospitalini na kuchomwa sindano huku akipewa dawa za kuweza kukikausha kidonda kile.
Dawa zikaonekana kutokusaidia jambo ambalo lilikifanya kile kidonda kuzidi kadri siku zilivyozidi kwenda mbele. Muda mwingi kidonda kile kilikuwa kikiwasha sana hali ambayo ilichangia kukaa ndani huku akiwa anakikuna mara kwa mara. Kwa kadri ambavyo alivyokuwa akikikuna na ndivyo ambavyo kidonda kile kilizidi kuwasha zaidi na kuwa kikubwa.
Baada ya mwezi kupita, Jamala akaamua kuelekea hospitalini tena kwa ajili ya matibabu zaidi. Dokta hakusema kitu chochote japokuwa alionekana kuwa na kitu moyoni ambacho alikuwa akihofia kukisema. Baada ya kuambiwa kukisema ndipo alipoamua kumwambia kwamba kansa ya ziwa ndio ilikuwa imemuanza na ilikuwa imeenea katika ziwa lote kiasi ambacho ikasababisha kidonda hicho.
Hiyo ilikuwa ni taarifa mbaya kwa Jamala, akaanza kulia mahali hapo. Ingawa kidonda kile kilionekana kutokuwa kikubwa sana lakini kansa ile ilikuwa imeenea katika ziwa lote kwa ndani. Jamala akaonekana kukata tamaa, kansa ile ikaanza kulimaliza ziwa lake.
Kansa ile ilianzia kwenye ziwa lakini kadri siku zilivyozidi kwenda mbele na ndivyo ambavyo ilizidi kuenea zaidi na zaidi. Matibabu ya kuweza kuitibia kansa ile mpaka ili ipone kabisa ilihitaji kiasi kikubwa cha fedha cha zaidi ya shilingi milioni saba. Umasikini wa kutokuwa na fedha ndio ambao ulisababisha hali yake kutokuwa na unafuu hata mara moja.
“Naiona kansa inakwenda kuniua” Jamala alimwambia mama yake, Bi Asha.
“Hapana Jamala, utapona tu” BI Asha alimwambia Jamala maneno ya kumfariji juu ya hali ambayo alikuwa nayo katika kipindi hicho.
Maneno yale hayakuonekana kumfariji Jamala, bado kansa ya ziwa ikaonekana kuongezeka zaidi na zaidi. Kansa ikasambaa sana na kuanza kuingia kifuani. Kwa kifupi, ziwa lake lote lilikuwa limekwishaanza kuoza. Hiyo ilikuwa ni siri yake, hakutaka mtu mwingine yeyote wa mtaani afahamu jambo hilo, tena hakutaka hata Abuu afahamu kama alikuwa na ugonjwa huo.
Siku zikaendelea kukatika zaidi, Abuu akaonekana kuhisi kitu hasa mara baada ya kumaliza kidato cha nne na kuanza kutumia muda wake mwingi nyumbani. Kila siku alikuwa akimuona mama yake, Jamala kuwa mpole kupita kawaida, ziwa lake alikuwa akilifunga kwa kutumia bandeji kubwa ambayo ilikuwa juu ya pamba.
Tayari Jamala akaona kwamba kitu ambacho kilikuwa kimebaki katika maisha yake kilikuwa ni kufa tu ila hakutaka kufa bila kujaribu. Hapo ndipo alipoanza kutumia dawa mbalimbali za mitishamba kama Ngoka 12 na Ngetwa lakini nazo hazikuweza kumsaidia kitu chochote kile juu ya ugonjwa wa kansa ambao ulikuwa umelitafuna sana ziwa lake.
“Nina kansa” Jamala alimwambia Abuu ambaye alionekana kushtuka.
“Unasemaje?” Abuu aliuliza kwa mshtuko kana kwamba hakusikia vizuri.
“Nina kansa ya ziwa. Kansa imelitafuna sana ziwa langu na kwa sasa imehamia kwenye kifua changu” Jamala alimwambia Abuu.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Ilikuwa ni taarifa mbaya hata zaidi ya msiba, bila kupenda, machozi yakaanza kutiririka mashavuni mwa Abuu. Kila alipokuwa akimwangalia mama yake alikuwa akijisikia kulia tu. Huo ndio ulikuwa ukweli wa hali ambayo ilikuwa ikiendelea. Jamala akawa akishinda chumbani kwake huku akiugulia maumivu makali ya ziwa lake pamoja na kifua ambacho kilikuwa kimeanza kushambuliwa.
Tarehe 9 mwezi Novemba mwaka 2005 siku ya Jumatano saa mbili asubuhi ndio ilikuwa siku ambayo Jamala akakaa kimya milele, alikuwa amefariki kitandani kwake. Moyo wa Abuu ukamuuma kupita kawaida, kila alipokuwa akikumbuka kwa jinsi ambavyo mama yake alivyokuwa akisumbuka kutafuta tiba ya ugonjwa wa kansa, alikuwa akiumia sana.
Katika maisha yake akatokea kuvichukia vitu viwili. Kitu cha kwanza kilikuwa ni umasikini. Aliamini kwamba mama yake alifariki kwa sababu tu alikuwa amekosa fedha za kumsafirisha na kumpeleka nje ya nchi kwa ajili ya kutibiwa ugonjwa huo ambao ulikuwa umemsumbua sana. Ukiachilia mbali na umasikini, pia akatokea kuuchukia ugonjwa wa kansa, hapo ndipo alipoona kila sababu ya kusoma sana na kuwa daktari mkubwa na kuanza kupambana na ugonjwa huo wa kansa.
Siku ambayo mama yake, Jamala alipokuwa akifukiwa kaburini, Abuu alilia kama mtoto. Moyo wake ulikuwa ukimuuma sana, alijua fika kwamba baba yake alikuwa amekufa kama alivyoambiwa na mama yake, na katika kipindi hicho, mama yake mpendwa nae alikuwa amekufa kwa ugonjwa ambao ulionekana kutokuwa na dawa kwa watu masikini kama wao.
“Pole sana Abuu” Jasmin alimwambia Abuu.
Katika kipindi hicho hawakuogopana kabisa, walikuwa wakipendana na kutembeleana huku kila mmoja akiwa na kiu ya kutaka kujua matokeo ambayo yalikuwa yakitarajiwa kutolewa mwezi wa kwanza mwishoni mwezi ujao. Abuu alikuwa amesoma sana huku akihitaji kufaulu vizuri na kumuonyeshea mama yake kwamba alikuwa katika harakati za kukimbia umasikini maishani mwake, katika kipindi hicho alionekana kukata tamaa kabisa, hata kama matokeo yangekuwa mazuri hapo baadae bado angeshindwa kujivunia kwa mama yake.
Siku zikaendelea kukatika mpaka mwaka kumalizika na baadae matokeo kutolea. Hakukuwa na mtu ambaye aliamini kile ambacho alikuwa amekiona, walimu pamoja na wanafunzi wakashikwa na butwaa hasa mara baada ya kuliona jina la Abuu likiwa limeongoza wanafunzi wote ambao walikuwa wamemaliza kipindi hicho nchini Tanzania.
Shule ya Baptist ikajiwekea historia ambayo waliamini kwamba hata miaka mingapi ingepita kusingekuwa na mtu ambaye angekuja kuifuta historia hiyo shuleni hapo. Kwa sababu alionekana kuwa na uwezo mkubwa, Abuu akachaguliwa kujiunga na shule ya vipaji ya Sekondari ya Kibaha.
Maisha bila mama, maisha bila baba huku akiwa mlemavu wa mguu mmoja yalionekana kuwa magumu sana kwake. Kila siku alikuwa akisoma shuleni hapo lakini mawazo yake yalikuwa yakimfikiria mama yake ambaye alikuwa amemuonyeshea upendo mkubwa sana katika maisha yake katika kipindi ambacho alikuwa hai.
Uwezo wake haukuishia katika shule ya Baptist tu bali aliendelea kuongoza mpaka katika shule ya vipaji ya Kibaha. Uwezo wake ulikuwa mkubwa sana, wanafunzi wote ambao walikuwa wakisomea masomo ya Sayansi wakaanza kumgeuza kuwa mwalimu wao. Ingawa alikuwa akiendelea kusoma sana lakini mawazo ya Abuu yalikuwa yakifikiria kitu kimoja tu, kutafuta tiba ya kuweza kupambana na magonjwa yote ya kansa.
Akaanza kushinda katika chumba cha kompyuta kwa ajili ya kujifunza mambo mengi kuhusuiana na magonjwa ya kansa. Alikutana na dawa nyingi ambazo zilikuwa zikipambana na kansa lakini hakuona dawa yoyote ambayo ilikuwa ikifanikiwa kupambana moja kwa moja na ugonjwa huo.
“Nataka kutengeneza dawa yangu ya kupambana na ugonjwa wa kansa” Abuu alimwambia rafiki yake, Ezekiel shuleni.
“Elimu yetu ndogo sana. Yaani kama unataka kufanya hivyo, haina haja ya kusoma mahali hapa, itakupasa kwenda kusoma Ulaya au hata hapo India” Ezekiel alimwambia.
Masomo yaliendelea zaidi na zaidi huku katika kipindi cha likizo akikitumia kukaa na bibi yake, Bi Asha pamoja na mpenzi wake, Jasmin ambaye walikuwa wakionana mara kwa mara. Mpaka wanaingia kidato cha sita, tayari walikuwa wamejiwekea ndoto moja mioyoni mwao, ya kuishi pamoja na kuwa mume na mke.
Kila mmoja aliamini jambo hilo kutokea hapo baadae, kila mmoja aliona kuwa umuhimu wa kutunza uhusiano wao ambao bado walikuwa wakiuona kuwa mchanga sana. Walikuwa makini kwa kila kitu ambacho kilikuwa kikitokea katika maisha yao, walipendana na kujaliana.
Miezi ikakatika na hatimae kufanya mitihani ya kidato cha sita. Mara baada ya kumaliza mitihani hiyo, wakapata muda wa kuwa pamoja zaidi. Wakawa huru kufanya mambo mengi likiwepo ngono. Walifanya mchezo huo kila siku kama njia mojawapo ya kujifariji na kipindi kigumu ambacho walikuwa nacho kipindi cha nyuma.
“Nina mimba” Yalikuwa maneno ambayo yalisikika masikioni mwa Abuu kutoka kwa Jasmin.
“Unasemaje?” Abuu aliuliza kana kwamba hakusikia vizuri.
“Nina mimba yako” Jasmin alimwambia Abuu ambaye alionekana kama kuwa na wasiwasi fulani usoni mwake.
****
Abuu alionekana kuwa kama mtu ambaye alichanganyikiwa, maneno ambayo aliyaongea Jasmin kwamba alikuwa na mimba yalionekana kumshtua kupita kawaida. Akabaki akimwangalia Jasmin mara mbili mbili huku akionekana kutokuamini kile ambacho alikuwa amekisikia kwa wakati ule.
Ni kweli kwamba alikuwa akipenda sana kupata mtoto na kutengeneza familia moja iliyokuwa na upendo mwingi pamoja na amani lakini wala haikutakiwa kuwa katika kipindi hicho. Abuu alibaki kimya kwa muda huku akionekana kufikiria kitu fulani kichwani mwake. Mdomo wake ukawa mzito kabisa kuongea kitu kingine chochote kile.
Akili ikawa inafanya kai ya ziada katika kufikiria, akaanza kuyafikiria maisha yake, alipenda sana kumuona mtoto wake akikaa katika mazingira mazuri, ni kweli kwamba alikuwa ameishi kwa miaka mingi katika maisha ambayo yalikuwa na shida nyingi ila hakutaka kabisa kumuona mtoto wake akiishi katika mazingira ya shida kama ambavyo aliishi yeye.
Alichokifanya kwa wakati huo ni kumsogelea Jasmin na kisha kumkumbatia tu. Hakuwa na uwezo wa kumwambia kwamba mimba ile haikuwa yake, hakuona sababu ya kuukataa ujauzito ule au kutoa ushauri wa kipumbavu kwamba ni lazima mimba ile itolewe, kitu ambacho alikiona kufaa kwa wakati huo ni kumfariji Jasmin na kumuahidi kuwa pamoja nae katika kipindi chote.
“Tutamlea tu mtoto wetu” Abuu alimwambia Jasmin ambaye alionekana kufarijika kupita kawaida.
“Niahidi juu ya hilo”
“Nakuahidi mpenzi. Mtoto wetu atakapozaliwa, ataishi katika maisha ya raha, kamwe sitotaka apate shida yoyote kama ambazo nimepitia” Abuu alimwambia Jasmin.
Hayo ndio ambayo walikuwa wamekubaliana kwa kipindi kile, waliahidiana kumtunza mtoto ambaye angezaliwa kadri ya uwezo wao. Japokuwa hawakuwa na fedha katika kipindi hicho lakini Abuu aliendelea kuamini kwamba angeweza kupata fedha za kutosha japokuwa hakujua ni wapi pa kuanzia.
Siku ziliendelea kukatika mpaka pale ambapo matokeo ya kidato cha sita yalipotangazwa. Kama kawaida yake, Abuu alikuwa amefanya vizuri kabisa na kuiongoza Tanzania nzima kama ambavyo alifanya katika kipindi ambacho alikuwa kidato cha nne. Walemavu wote ambao walikuwa wamekata tamaa katika kusoma wakaonekana kutiwa nguvu, walijiona nao kwamba walikuwa na uwezo wa kufanya vizuri hata kama walikuwa katika mazingira ya shida.
Serikali ikatoa nafasi tatu kwa watu ambao walikuwa wamefanya vizuri katika mitihani ya kidato cha sita kwa kuwapa nafasi za kwenda kusoma nje ya nchi. Ingawa wanafunzi wawili wakachagua kwenda kusoma nchini Marekani lakini kwa Abuu hali ikawa tofauti sana, akachagua kwenda nchini India kwa kusomea masomo ya udaktari.
Siku ambayo alikuwa akiagana na Jasmin ilikuwa ni moja ya siku ya majonzi makubwa sana kwao wote. Walibaki wakiangaliana huku machozi yakiwatoka tu. Abuu akambusu Jasmin na kisha hapo hapo kumfuata bibi yake ambaye alikuwa amemsindikiza katika uwanja huo pamoja na watu wengine ambao walitakiwa na serikali kumsindikiza na kisha kuwaaga na kuingia ndani ya jengo la uwanja wa ndege.
Jasmin hakuamini kile ambacho alikuwa akikiona mahali hapo, hakuamini kama mtu ambaye alikuwa akimpenda sana kwa wakati huo alikuwa akielekea ndani ya eneo la uwanja wa ndege na kisha kupanda ndege na kuelekea nchini India kwa ajili ya masomo. Hiyo wala haikuwa ndoto kwa Jasmin, lilikuwa ni tukio la kweli ambalo lilikuwa likitokea katika ulimwengu halisi.
“Nitakupenda milele mpenzi” Jasmin alisema kwa sauti ndogo huku akiamini kwamba Abuu alikuwa akiisikia.
**
Macho ya Abuu yalikuwa yakiangalia maghorofa marefu ambayo yalikuwa yamejengwa katika jiji kubwa la Mumbai nchini India. Majengo yale makubwa yakaonekana kumshangaza sana kutokana na jinsi yalivyokuwa. Yalikuwa yamekwenda sana angani huku yakiwa mapana kupita kawaida. Katika kila hatua ambayo ndege ilikuwa ikiendelea kutembea pale ardhini, Abuu hakutaka kuyatoa maho yake kutoka katika maghorofa yale ambayo kwake yalionekana kuwa na mvuto mkubwa.
Ndege ikasimama na hivyo abiria wote kutakiwa kuteremka, Abuu pamoja na abiria wengine wakaanza kuteremka. Hali ya joto katika kipindi hicho ilikuwa sawa sawa na hali ya hewa ya jiji la Dar es Salaam. Watu mbalimbali ambao walikuwa wakiremmka kutoka katika ndege ile, mavazi yao yalikuwa ni nguo nyepesi ambazo zilikuwa zikiwafanya kutokusikia joto kali.
Abiria wakaanza kutembea na kuingia ndani ya jengo la uwanja ule na kisha kuambiwa kupita katika mlango mmoja ambao ulikuwa maalumu kwa ajili ya kuwaangalia kwa undani abiria ambao walikuwa wameteremka katika ndege ambazo zilikuwa zikiingia katika uwanja huo wa kimtaifa wa ndege wa Mumbai.
Mara baada ya Abuu kupita pamoja na gongo lake, akaanza kuelekea katika sehemu ambayo aliruhusiwa kuchukua begi lake na kisha kuanza kuelekea nje ya uwanja huo ambao kulikuwa na watu wengi waliokuwa wameshika mabango mbalimbali ambayo yaliandikwa majina ya ndugu, jamaa na marafiki ambao walikuwa wamefika mahali hapo kwa ajili ya kuwapokea.
Abuu akaanza kuangalia katika mabango yale, macho yake yakatua katika bango moja lililoandikwa ‘Abuubakari Selemani’ ambapo akaanza kumfuata mtu ambaye alishika bango lile na kisha kujitambulisha kwamba yeye ndiye alikuwa Abuu yule ambaye alikuwa ameandikwa katika bango lile.
“You are welcome (Karibu)” Jamaa huyo alimkaribisha Abuu huku akimsaidia begi lake na kisha kuelekea nje ya jengo la uwanja ule.
Muda mwingi Abuu alikuwa akiangalia mandhari ya jiji la Mumbai, kwake, jiji lile likaonekana kuchangamka kupita kawaida, idadi ya watu mitaani ilikuwa kubwa sana, katika kipindi hicho, Abuu hakutaka kutembea haraka haraka, alilitumia gongo lake vizuri kutembea mwendo wa taratibu huku akiangalia katika kila upande.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Safari yao ikaishia katika gari moja la kifahari ambalo liliandikwa ‘Ambassy of United State of Tanzania’ (Balozi wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania). Jamaa yule ambaye alikuwa amefika mahali hapo kwa ajili ya kumpokea Abuu, akamfungulia mlango na kisha Abuu kuingia ndani.
Kwa mara ya kwanza katika maisha yake toka azaliwe, hiyo ndio ilikuwa mara yake ya kwanza kuingia ndani ya gari lililoonekana kuwa la kifahari. Gari lile lilionekana kuwa na mandhari mazuri kwa ndani. Upepo wa kiyoyozi ulikuwa ukizidi kupepea ndani ya gari lile, harufu nzuri ya manukato yalikuwa yakizitetemesha pua zake. Ndani ya gari lile, viti vilikuwa vikiangaliana huku kwa mbele kidogo kukiwa na kiuzio ambacho kilimfanya dereva kutokuonekana na watu ambao walikuwa wakikaa katika viti vya nyuma ya gari lile.
Gari lile lilionekana kuwa katika mazingira mazuri sana kwa ndani, katika kila kitu ambacho kilikuwa kikionekana machoni mwake ndani ya gari lile, kumbukumbu zake zikaanza kujirudia kichwani, katika kipindi kile ambacho alikuwa akimwambia mama yake kwamba ilikuwa ni lazima apigane na asome sana katika maisha yake mpaka apate fedha za kujenga nyumba na kununua magari, kwa jinsi alivyokuwa akiliona gari lile, akaanza kuona kwamba ndoto zake zingetimia japokuwa hakujua ni wapi ambapo alitakiwa kuanzia kwa wakati huo.
Gari lile likaanza kuondoka mahali pale. Abuu hakutaka kuacha kuangalia nje ya gari lile, idadi kubwa ya watu bado ilikuwa ikimshangaza sana machoni mwake. Japokuwa jiji la Dar es salaam lilikuwa likisifika sana na idadi kubwa ya watu, kwa jijini Mumbai, hali ilionekana kuwa mara tatu ya jiji la Dar es Salaam.
Safari yao iliendelea kwa zaidi ya dakika thelathini na ndipo wakaanza kuingia katika nyumba fulani kubwa ambayo ilikuwa imezungushiwa ukuta mkubwa huku kukiwa na seng’enge kwa juu na geti kubwa likionekana likifunguliwa na gari lile kuingizwa ndani. Bendera ya nchi ya Tanzania ilikuwa ikipepea katika mlingoti wake ambao ulisimamishwa katikati ya eneo la nyumba ile kubwa ambayo iliandikwa kwa maneno makubwa Embassy of United State of Tanzania.
Gari liliposimama, wote wakateremka na kisha kuanza kuelekea ndani ya ubalozi ule. Muda mwingi Abuu alikuwa akiutumia kuangalia maeneo kadhaa ya nyumba ile kubwa, kila kitu ambacho alikuwa akikiangalia katika eneo lile, alionekana kuvutiwa nacho.
“Karibu Abuubakari” Mwanaume mmoja ambaye alikuwa na ndevu chache nyeupe alimkaribisha Abuu ambaye alikuwa amekaa kwenye kochi moja la kifahari.
“Asante. Shikamoo Baba” Abuu aliitikia na kisha kumsalimia.
“Marahaba” Mzee yule, balozi wa Tanzania nchini India, Bwana Maliki aliitikia.
Katika kipindi hicho, Abuu alitakiwa kuwa katika ubalozi huo kwa muda wa masaa kadhaa hata kabla ya kupelekwa katika chuo ambacho serikali ya Tanzania ilikuwa imekitafuta kwa ajili yake. Siku hiyo ubalozini hapo, alikula vyakula ambavyo hakuwahi kula toka azaliwe, alikunywa vinywaji ambavyo hakuwahi kuvinuywa toka azaliwe. Mpaka kufikia hatua hiyo, akili yake ikafunguka kwa kuona kwamba umasikini ndio ambao ulikuwa ukimnyima vitu vingi sana ambavyo vilikuwa vizuri kwa kuviangalia na hata kuvionja.
“Nitapigana na umasikini tu hadi mwisho” Abuu alimwambia Bwana Maliki.
“Unasemaje?” Bwana Maliki aliuliza huku akionekana kutokusikia.
“Nina uhakika mpaka sasa hivi bibi yangu atakuwa hajala chakula chochote kile” Abuu alimwambia Bwana Maliki.
“Kwa nini unasema hivyo?”
“Bibi yangu ni masikini sana. Nimekulia katika maisha ya masikini mpaka unaniona hapa. Mama yangu alikufa kwa ugonjwa wa kansa na hivyo kubaki bibi yangu tu. Mama ndiye alikuwa akitoa kila kitu nyumbani, alipofariki, hakuna mtu ambaye aliweza kuangaikia chakula kwa ajili ya bibi yangu” Abuu alisema kwa sauti ya majonzi.
“Pole sana Abuubakari”
“Asante sana”
“Na vipi kuhusu huo mguu wako?”
“Huu mguu wangu umetokana na umasikini ambao ulikuwa umeikumba sana familia yetu. Nilijichoma na kitu chenye ncha kali ila kwa sababu mama alikuwa akitafuta unafuu na kuepuka foleni, akaelekea katika maabara za uchochoroni ambapo nilichomwa vibaya sindano” Abuu alimwambia Bwana Maliki.
“Pole sana. Kipi kilitokea kwa mama yako mpaka afariki?”
“Ugonjwa wa kansa. Au acha niseme kwamba umasikini. Mara nyingi mtu ambaye anakuwa na fedha huwa ngumu sana kufa kwa ugonjwa wa kansa hasa anapoiwahi. Mama yangu alijua mapema kabisa kwamba alikuwa na kansa, ila angefanya nini sasa? Kama angekuwa na fedha, angekwenda hospitalini ambapo angetibiwa na kupona. Hakuwa na fedha, akasubiri sana nyumbani kwa kungojea muujiza wa Mungu. Matokeo yake hakupata muujiza wa Mungu ambao alikuwa akiusibiria katika maisha yake, kansa ile ya ziwa ikamuua hasa mara baada ya kuenea mpaka kifuani” Abuu alimwambia Bwana Maliki ambaye alionekana kuwa kwenye masikitiko.
“Pole sana”
“Asante sana”
“Hapa ndipo India, miongoni mwa nchi zenye watu wengi sana duniani, nyuma kidogo ya China. Kwa sababu umefika hapa, naamini utakwenda kusahau mengi yaliyotokea katika maisha yako ya nyuma” Bwana Maliki alimwambia Abuu.
“Inawezekana kusahau lakini si kumsahau mama yangu, umasikini pamoja na ugonjwa wa kansa. Nimeingia leo nchini India nikiwa masikini sana, ila nataka nitakapoondoka hapa niwe tajiri mkubwa sana” Abuu alimwambia Bwana Maliki.
“Yote yanawezekana kama ukijituma”
“Naamini hilo. Nitakachokifanya ni kuwasaidia watu ambao ni masikini kama alivyokuwa mama yangu, sitotaka kuwaona wakifa kama alivyokufa mama yangu. Mama yangu alikufa kwa sababu tu alikuwa masikini, sipendi kuwaona masikini wengine wakifa kwa sababu ya umasikini wao ambao utasababishwa kukosa dawa za ugonjwa wa kansa ambao unaendelea kuwamaliza watu wengi duniani. Ngoja nisome, najua kila kitu kitakuwa sawa japokuwa kila mtu anaweza kunidharau kutokana na ulemavu ambao ninao mwilini mwangu” Abuu alimwambia Bwana Maliki.
Siku hiyo, Abuu alikuwa akiongea mambo mengi kuhusiana na ugonjwa wa kansa, umasikini pamoja na kumzungumzia sana mama yake, Jamala ambaye alikuwa amekufa kipindi kirefu kilichopita. Moyo wake bado ulikuwa katika maumivu makali sana, alijiona dhahiri kuwa na hasira ya kusoma sana ili kuepukana na umasikini ambao ulikuwa ukimkabili katika maisha yake. Kusoma sana ndicho kitu ambacho kilionekana kuweza kumtoa katika hali ambayo alikuwa nayo katika kipindi hicho.
Si kwa sababu alikuwa mlemavu basi alitakiwa kukaa barabarani na kuanza kuomba msaada. Alijiona kuwa na nafasi ya kubadilisha kila kitu maishani mwake, kuanzia mitazamo ya watu ambao walikuwa wakiamini kwamba walemavu hawakuwa wakiweza kufanya kitu chochote kile katika maisha yao. Alijua fika kwamba kichwani mwake alikuwa na kitu cha ziada, kitu ambacho kingeweza kuyabadilisha maisha yake.
Hakutaka kuiacha Elimu ambayo ilikuwa kichwani mwake isifanye kazi au kuyabadilisha maisha yake, aliamini kwamba Mungu alimpa uwezo mkubwa wa darasani kwa sababu tu alitaka uhai wa masikini wengine ambao walikuwa na magonjwa ya kansa basi yaweze kuokolewa na yeye.
Saa kumi na moja jioni, Abuu alitakiwa kuelekea chuoni ambapo Bwana Maliki ndiye ambaye alitakiwa kumsindikiza. Abuu akaoga na kisha kuvaa nguo nyingine na muda ulipofika, wakaingia ndani ya gari na kuanza kuelekea katika chuo cha Taifa cha Mumbai. Ndani ya gari, bado Abuu alionekana kuwa na mawazo mengi, kitu ambacho alikuwa akikitaka kwa wakati huo ni kufika chuoni hapo haraka iwezekanavyo na kuanza masomo mara moja.
Kiu yake kubwa ambayo alikuwa nayo katika kipindi hicho ilikuwa ni kuingia darasani na kisha kuanza masomo yake haraka iwezekanavyo. Alikuwa akitamani sana kuyabadilisha maisha yake, kila alipokuwa akifikiria namna ambavyo Bibi yake, Bi Asha alivyokuwa akiishi ndani ya jiji la Dar es Salaam katika mtaa wa tandale, moyoni mwake alikuwa akishikwa na kiu kubwa ya kusoma zaidi na kubadilisha picha halisi ya maisha yake na maisha ya bibi yake.
Baada ya dakika ishirini, gari likaanza kuingia katika eneo la chuo kikubwa cha Mumbai. Abuu akabaki akishangaa ukubwa wa chuo kile, majengo na hata idadi kubwa ya wanachuo ambao walikuwa wakionekana machoni mwake. Furaha kubwa ikamuingia Abuu, hakuamini kama kweli katika kipindi hicho alikuwa amefika katika chuo ambacho kilikuwa kikisifika kwa kutoa madakatari wakubwa duniani.
Abuu akaanza kutokwa na machozi, hakuamini kama katika maisha yake yote angeweza kufika katika chuo hicho na yeye kuwa miongoni mwa wanachuo ambao wangesoma ndani ya chuo hicho ambacho kila mwanachuo duniani alikuwa akitamani sana kufika mahali hapo na kusoma. Gari liliposimama, wakaanza kuteremka.
Wanachuo walikuwa bize, kila mmoja alionekana kuwa katika mishemishe zake katika kipindi hicho hivyo hawakutaka kuangalia ni mtu gani ambaye alikuwa akiteremka katika gari lile. Abuu akateremka huku akiwa amelishikilia gongo lake na huku akiwa ameuzungusha mguu wake uliolemaa katika gongo lile na kisha kuanza kuelekea katika ofisi ya mkuu wa chuo pamoja na Bwana Maliki.
Kila kitu kikawa kimemalizwa na hatimae Abuu kusajiriwa na kuwa mwanachuo kamili wa chuo hicho cha Mumbai. Kwa sababu ndio ulikuwa mwaka wake wa kwanza, akapelekwa katika chumba ambacho kilikuwa katika moja ya majengo yaliyokuwa ndani ya eneo la chuo hicho kikubwa kuliko vyuo vyote nchini India.
Katika chumba kile, Abuu akakutana na wanachuo wengine wawili ambao nao ulikuwa ni mwaka wao wa kwanza ndani ya chuo kile. Wote wakatambulishana na kugundua kwamba wao wote watatu ambao walikuwa ndani ya chumba kile walikuwa ni watu ambao walitoka katika nchi tatu tofauti nje ya India. Abuu alikuwa ametokea nchini Tanzania, Kendesh aliyetokea nchini Malaysia na Katashi aliyetokea nchini Korea Kusini.
Kwa sababu ilikuwa ni siku ya kwanza, hawakutaka kuongea sana, ilipofika usiku, wote wakalala na hivyo kujiandaa na siku ya kesho ambayo masomo yalitakiwa kuanza rasmi katika chuo hicho. Usiku mzima, Abuu alijiona kama yupo ndotoni ambapo baada ya muda mfupi angeshtuka na kujikuta akiwa katika kitanda chake cha kamba nchini Tanzania, ndani ya jiji la Dar es Salaam katika mtaa wa Tandale huku akiwa amelala katika usingizi wa mang’amung’amu usiku mzima.
“Nitasoma sana. Nitasoma sana mpaka watu wanishangae” Abuu alijisemea katika kipindi ambacho alikuwa akijifunika shuka mwili mzima kama alivyozozea.
*************************************************************
Asubuhi ya siku hiyo Abuu aliamka asubuhi na mapema hata kabla mwanga haujaanza kuonekana nje. Usingizi wote ukamuisha, akainuka kitandani na kisha kukaa. Chumba kilikuwa na giza, hali ya hewa wala haikuwa ya joto kabisa kutokana na feni lenye nguvu kuendelea kuwapepea kwa kasi kubwa.
Abuu akaanza kuyafikiria maisha yake ya nyuma, hakuamini kama katika kipindi hicho alikuwa nchini India kwa ajili ya kuanza masomo yake ya kuwa daktari mkubwa hapo baadae. Akili yake ilikuwa ikiwafikiria watu ambao bado walikuwa wakiendelea kuishi katika maisha ya kimasikini tu, akili yake ilikuwa ikiwafikiria masikini ambao walikuwa wakifa kutokana na kukosa fedha za kuwawezesha kuwapeleka hospitalini na kutibiwa dhidi ya magonjwa ambayo yanawasumbua.
Abuu hakuishia hapo, akaanza kumfikiria Bibi yake, Bi Asha ambaye alikuwa amemwacha nchini Tanzania huku akiendelea na maisha yake ya kimasikini. Abuu aliumia kupita kawaida, aliyakumbuka maisha ambayo alikuwa akiishi pamoja na Bibi yake, yalikuwa maisha yaliyojaa dhiki, maisha ambayo kila alipokuwa akiyakumbuka, alikuwa akitokwa na machozi tu.
Kwa wakati huo alijua fika kwamba bibi yake alikuwa akiendelea kuwa na maisha ya kimasikini. Moyoni alitamani aanze chuo na kisha awe anafanya kazi za hapa na pale kwa ajili ya kupata fedha ambazo moja kwa moja angemsaidia bibi yake ambaye alikuwa kwenye dhiki kubwa kupitiliza.
Hali yake ikaonekana kuwa tatizo kwake, asingeweza kufanya kazi yoyote ile kwa sababu asingeweza kuwa imara kutokana na mguu wake mmoja kupooza na hivyo kuhitaji kutembelea gongo kila alipokuwa akienda. Wazo lake la kufanya kazi na kujiingiza kipato likaonekana kuwa gumu kutokea, asingeweza kufanya kazi kabisa.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Hapo ndipo alipofikiria zaidi kuhusu kusoma zaidi na zaidi, kujikwamua kwake kutoka katika hali ya umasikini kulimhitaji sana kusoa kuliko kitu kingine. Kwa wakati huo, tayari alikuwa nchini India tayari kwa kuanza kusoma masomo ambayo aliamini kwamba mara baada ya miaka kadhaa angekuja kuwa daktari mkubwa hapa duniani. Katika alfajiri ya siku hiyo, Abuu alikuwa akifikiria mambo mengi ambayo yalikuwa yakimtoa machozi kitandani pale.
Mpaka mwanga unatokea, Abuu hakulala, bado alikuwa macho na hivyo kuanza kujiandaa tayari kwa kwenda darasani. Siku hiyo ikaonekana kuwa furaha kwake, alipoanza kupiga hatua kuingia darasani, Abuu alijiona kama anaota, hakuamini kama yeye ndiye ambaye alikuwa akipiga hatua kuingia ndani ya darasa hilo.
Wanachuo wote ambao walikuwa ndani ya darasa hilo wakabaki kimya na kuanza kumwangalia Abuu ambaye alikwenda na kutulia katika kiti kimoja ambacho kilikuwa wazi. Abuu, kwao alionekana kuwa mtu wa tofauti sana, kwanza, darasa zima yeye ndiye alikuwa mtu mweusi na pili, darasa zima yeye ndiye alikuwa mlemavu. Watu wakabaki wakimwangalia, hali yake ikaonekana kumhuzunisha kila mmoja darasani hapo.
Siku hiyo masomo yalianza rasmi. Kutokana na Abuu kuwa na hamu ya kusoma sana, akajikuta akiituliza akili yake katika kila somo ambalo alikuwa akilisoma kwa wakati huo. Alijua fika kwamba alikuwa na akili ya kuzaliwa, lakini jambo hilo halikuwa sababu ya kumfanya asisome kwa bidii. Alijua kwamba nchini India, watu wengi walikuwa na akili nyingi, hivyo kama asingetumia hata muda wa ziada kujisomea, asingeweza kufanikisha kile ambacho kilikuwa kimeleta mahali pale.
Abuu akawa mtu wa kusoma usiku na mchana, kila siku alikuwa bize akijisomea. Kadri alivyokuwa akiufikiria umasikini pamoja na ugonjwa wa kansa na ndivyo ambavyo alisoma zaidi na zaidi. Alihitaji kuwa daktari mmoja mkubwa katika dunia hii, daktari ambaye asingekuwa na mpinzani yeyote yule. Alihitaji kuwa bize muda wote, hata wakati wa kwenda kula, yeye alikuwa akisoma tu.
“Utaumwa kichwa. Pumzika”
Abuu aliisikia sauti moyoni mwake, hakujua kama ilikuwa sauti yake au ya nani.
“Haiwezekani. Nitapumzika nikimaliza chuo. Nitapata muda mwingi wa kupumzika hata zaidi ya huu upatikanao”
Abuu alisema huku akikiweka kitabu chake vizuri.
Hayo ndio yalikuwa maisha yake ya kila siku. Mwezi wa kwanza ukakatika na kuingia mwezi wa pili chuoni hapo. Mwezi wa pili, wa tatu na wa nne ukakatika huku akiendelea kuwa na maisha yake chuoni hapo. Abuu akawapata marafiki mbalimbali ambao alikuwa akisaidiana nao.
Tayari uwezo wake ukaanza kuonekana, maelekezo yake ambayo alikuwa akiwapa watu wengine katika masomo mbalimbali yakamfanya kuonekana kuwa mtu wa tofauti sana.
Tofauti na kujisomea sana, Abuu akaonekana kuwa na kitu cha ziaida katika kichwa chake, kitu cha ziada ambacho hata walimu wenyewe hawakuwa nacho. Hapo ndipo wanachuo wengi walipokuwa wakihitaji ukaribu wake zaidi. Kila siku Abuu akawa mtu wa kuwafundisha wengine.
Si wanachuo wote ambao walikuwa wakimpenda Abuu, wengine walikuwa wakimchukia kupita kawaida japokuwa alikuwa akionyesha moyo mkuu wa kuwafundisha wengine. Wengine walimchukia kwa sababu alikuwa mlemavu wa mguu, wengine walimchukia kwa sababu alikuwa mtu mweusi kutoka Afrika lakini pia kulikuwa na wengine ambao walimchukia bila sababu, wao walijikuta wakimchukia tu.
Abuu alilifahamu hilo. Moyoni alikuwa akiumia kupita kawaida lakini hakuwa na cha kufanya zaidi ya kuendelea na maisha yake ya kila siku. Kila siku marafiki kwake walikuwa wakiongezeka lakini napo maadaui walikuwa wakiongezeka pia. Abuu hakukata tamaa, Abuu hakuvunjika, bado alikuwa akiendelea na maisha yake kama kawaida.
Mwezi wa tano ulipoingia, wanachuo wakapewa taarifa kwamba walitakiwa kujiandaa na mitihani chuoni hapo. Kwa Abuu ilikuwa ni furaha lakini kuna kitu ambacho alikuwa akikifikiria, hakutaka kuingia katika mitihani huku akiwa na mawazo juu ya bibi yake ambaye bado alikuwa akiendelea kuishi katika maisha ya kimasikini.
Alichokifanya ni kupanga safari ya kuelekea katika ubalozi wa Tanzania nchini India na kisha kuanza kuongea na Bwana Maliki, Abuu hakutaka kuficha, alimkumbushia Bwana Maliki kwamba bibi yake alikuwa akiendelea kuishi katika maisha ya dhiki na hivyo alihitaji msaada wake mkubwa.
“Kwa hiyo nimsaidie vipi?” Bwana Maliki alimuuliza Abuu.
“Naomba umtumie kiasi cha fedha nami nitakurudishia mambo yangu yatakapokaa sawa”
Abuu alimjibu Bwana Maliki.
“Kiasi gani kitamtosha kwa mtazamo wako?”
“Hata laki tano”
“Hizo ndogo sana. Nitamtumia milioni mbili kwa ajili ya matumizi yake ya hapa na pale” Bwana Maliki alimwambia Abuu ambaye kwa furaha akajikuta akianza kutokwa na machozi.
“Asante sana” Abuu alimwambia Bwana Maliki.
“Usijali Abuu. Tutaendelea kuwa pamoja nawe katika maisha yako. Cha msingi soma sana, naona una ndoto kubwa sana moyoni mwako ambayo sijawahi kuiona kwa mtu yeyote yule. Soma sana Abuu” Bwana Maliki alimwambia Abuu huku akiwa amemkubatia.”
“Ninasoma. Ninasoma sana kwa ajili ya kuyabadilisha maisha yangu, sipendi kuona bibi yangu akiendelea kuishi katika maisha ya kimasikini” Abuu alimwambia bwana Maliki.
“Mafanikio yako yapo katika elimu yako Abuu. Kama ukisoma sana ninaamini kwamba utakwenda kufanikiwa sana zaidi ya jinsi unavyofikiria kwa sasa” Bwana Maliki alimwambia Abuu.
Kama ilivyopangwa na ndivyo ilivyokuwa. Bwana Maliki akamtuma mtu aliyekuwepo nchini Tanzania kwa ajili ya kumpelekea Bi Asha kiasi cha shilingi milioni mbili kwa ajili ya matumizi yake ya hapa na pale kiasi ambacho kilikuwa kikikubwa sana kukipokea katika maisha yake.
“Imetoka kwa Abuu” Kijana ambaye alikuwa amempeleka kiasi kile cha fedha alimwambia Bi Asha.
“Asante sana. Oooh! Mjukuu wangu Mungu akufanikishe kwa kila jambo ulipangalo, akupe maisha marefu yenye furaha na amani. Ewe Mola! Mwangalie mjukuu wa Abuu” BI Asha alisema huku akinyanyua mikono juu kama ishara ya kumshukuru Mungu.
****************************
Siku ya mitihani ikafika na hatimae wanachuo wote kufanya mitihani yao. Kwa Abuu, wakati huo alifanya mitihani huku moyoni mwake akiwa na amani kwa kuona kwamba bibi yake alikuwa amesaidiwa kiasi cha fedha ambacho aliahidiwa na Bwana Maliki. Mitihani, kwake ilionekana kuwa ya kawaida sana japokuwa kwa wanachuo wengine mitihani ile ilionekana kuwa migumu kupita kawaida.
Walitumia wiki mbili kufanya mitihani ile na ndipo wakapewa muda wa mapumziko. Wanachuo wengine wakaamua kwenda nyumbani kwao kwa ajili ya wiki moja ya mapumziko. Abuu hakutaka kwenda sehemu yoyote ile zaidi ya kubakia chuoni hapo. Japokuwa Bwana Maliki alikuwa amemuita aende akaishi nyumbani kwake lakini Abuu akakataa.
Alijua fika kwamba nyumbani kwa Bwana Maliki angeishi maisha ya raha ya kula alichokitaka na kunywa alichokitaka. Hakuyapenda maisha hayo kwa wakati huo, asingependa kuishi maisha ya raha na wakati muda huo huo bibi yake ambaye alikuwa akiishi nchini Tanzania alikuwa akiishi maisha ya tabu. Uamuzi ambao aliuchukua wa kubaki chuoni ndio ambao ulionekana kuwa bora kwake katika kipindi hicho.
Chuoni hapo alipobaki, Abuu aliendelea kusoma kwa bidii kana kwamba masomo yalikuwa yakiendelea. Usomaji wake uliwashangaza sana watu wengine, hawakuamini kama duniani kulikuwa na mtu ambaye alikuwa akipenda sana kusoma kama alivyokuwa Abuu katika kipindi hicho. Muda mwingi alikuwa bize katika maktaba ya chuo au hata katika kompyuta yake aliyonunuliwa na Serikali huku akiperuzi huku na kule kwa ajili ya kupata mambo mbalimbali.
Baada ya wiki moja, chuo kikafunguliwa na hatimae matokeo kutolea. Watu wakaona kuwa kawaida kwa Abuu kuongoza katika mitihani ile kutokana na jinsi ambavyo alikuwa akisoma. Abuu alipata alama za juu, watu wakashtuka pale ambapo walikuja kufahamu kwamba alama alizokuwa amezipata Abuu zilikuwa ni za juu zaidi ya Rajeesh ambaye alikuwa akishikiria rekodi ya kupata alama za juu katika chuo hicho toka mwaka 1960.
Abuu akaonekana kuvunja rekodi ambayo ilikuwa imewekwa chuoni hapo. Walimu wake hawakuamini kama kungekuwa na mtu ambaye angeweza kuivunja rekodi ile ambayo ilikuwa imewekwa katika chuo hicho. Taarifa zile zikaanza kutangazwa katika sehemu mbalimbali kwamba Abuu alikuwa amefanikiwa kuvunja rekodi hiyo ambayo ilidumu kwa mudamrefu sana.
“Nitafanya hata zaidi ya hili”
Abuu alijisemea katika kipindi ambacho alipewa taarifa juu ya kuvunja rekodi ile ambayo ilidumu kwa muda mrefu chuoni hapo.
Hivyo ndivyo ilivyotokea. Kwa sababu alikuwa amevunja rekodi ambayo ilikuwa imewekwa ndani ya chuo hicho kwa muda mrefu, Abuu akapewa zawadi mbalimbali kutoka katika serikali ya India ambayo macho yake yalikuwa yameelekezea katika chuo hicho. Serikali ya India ikaamua kumpa ofa ya kuwa mmoja wa madaktari katika hospitali ya Taifa ya hapo India mara baada ya kumaliza masomo yake.
Hiyo ikaonekana kuwa kama heshima kwa Abuu, heshima ambayo wala hakuwa akiitarajia kuipata. Juhudi zake za kusoma ziliendelea zaidi na zaidi, aliamini kwamba kama angeendelea zaidi basi kuna mambo mengi yangeweza kutokea katika maisha yake. Kila siku alikuwa mtu wa kusoma zaidi na zaidi.
Katika kila mitihani ambayo ilikuwa ikitokea chuoni hapo, bado Abuu alikuwa akiendelea kuongoza kama kawaida yake. Kuongoza kwake kukaonekana kuwa kawaida kwa wanachuo wengine, Abuu akaonekana kuzoelekea katika uongozaji wake. Wale ambao walikuwa wakimchukia katika kipindi cha nyuma wakajikuta wakianza kumpenda na kumhitaji katika maisha yao ya kila siku.
Mwaka wa kwanza ukakatika na wa pili kuingia. Hapo ndipo ambapo Abuu akaanza kupata wazo moja, wazo ambalo alitakiwa kulifanyia kazi kubwa sana mpaka kupata kile ambacho alikuwa akikifikiria kwa wakati huo. Kwanza, wazo hilo hakutaka kumtaarifu mtu yeyote, alitaka abaki nalo moyoni mpaka pale ambapo atakapoanza kulifanyia utafiti wa kina.
Abuu hakutaka kulipuuzia wazo hilo, alichokifanya siku iliyofuata ni kuanza kuingia katika mitandao mbalimbali na kuangalia vitu ambavyo alikuwa akivihitaji. Hakuishia hapo, alikwenda mpaka kuonana na madaktari wakubwa ambao walikuwa wakimueleza kwa kina kile ambacho alikuwa akikihitaji kwa wakati huo jambo ambalo lilimpa uhakika kwamba kile ambacho alikuwa akikitarajia kingeweza kufanikiwa.
“Kumbe inawezekana kabisa” Abuu alijisemea.
“Nitaanza leo hii hii kutengeneza dawa ya magonjwa ya kansa”
Abuu alijisemea huku akisimama na kuanza kwenda maktaba kuchukua vitabu kadhaa kabla ya kuelekea katika maabara kubwa chuoni hapo
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
*********************************
**** Je nini kitaendelea?
**** Je Abuu ataweza kutengeneza dawa ya magonjwa ya kansa?
***** Utamu unazidi kuendelea hapa joka la hadithi, endelea ku LIKE ku COMMENT na hata ku SHARE
****ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment