Simulizi : A Day Too Long (Siku Ndefu Mno)
Sehemu Ya Pili (2)
Ilipoishia
Hakuishia hapo, alikwenda mpaka kuonana na madaktari wakubwa ambao walikuwa wakimueleza kwa kina kile ambacho alikuwa akikihitaji kwa wakati huo jambo ambalo lilimpa uhakika kwamba kile ambacho alikuwa akikitarajia kingeweza kufanikiwa.
“Kumbe inawezekana kabisa” Abuu alijisemea.
“Nitaanza leo hii hii kutengeneza dawa ya magonjwa ya kansa”
Abuu alijisemea huku akisimama na kuanza kwenda maktaba kuchukua vitabu kadhaa kabla ya kuelekea katika maabara kubwa chuoni hapo
Songa nayo sasa…
Mara baada ya Jamala kuondoka ndani ya chumba chake, Selemani akakifuata kitanda chake na kisha kukaa. Uso wake ulionekana kuwa na hasira kupita kawaida, malumbano ambayo alikuwa ameyafanya pamoja na mpenzi wake yalionekana kumkasirisha sana. Muda wa kuwa na mtoto kwake haukuonekana kuwa tayari, bado alikuwa akihitaji maisha ya kuwa peke yake na wala hakutaka kusikia jambo lolote lile kuhusiana na mtoto.
Selemani akaonekana kuyachukia mahusiano yake pamoja na jamala ambaye alikuwa ameondoka ndani ya chumba kile muda mchache uliopita. Wazee wale ambao walikuwa ndani ya chumba chake kwa ajili ya kusuluhisha malumbano yale ambayo yalikuwa yametokea walibaki wakimwangalia Selemani ambaye alionekana kuwa na hasira kupita kawaida.
Selemani hakuonekana kuwa tayari kusikia kitu chochote kile kwa wakati huo, alikichukia kila kitu ambacho kilitokea katika maisha yake pamoja na jamala. Usiku wa siku hiyo, Selemani hakulala, muda wote alikuwa akimfikiria Jamala. Moyoni mwake, alijua wazi kwamba jamala alikuwa msichana muaminifu sana na alikuwa na uhakika pia kwamba mimba ile ilikuwa yake na wala haikuwa ya mwanaume mwingine, ila alikuwa akibisha kwa sababu katika kipindi hicho wala hakuhitaji mtoto yeyote yule.
Huo ndio ukawa mwisho wa kumsikia Jamala katika maisha yake. Selemani hakutaka kumkumbuka Jamala, katika kila kitu ambacho kilikuwa kimetokea, historia yake akaifuta katika kipindi hicho. Maisha yaliendelea zaidi mpaka pale ambapo Selemani akaja kumpata msichana mwingine, Farida ambaye akaanzisha mahusiano nayo.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kwa Farida, akaamua kuwa makini, hakutaka tatizo ambalo lilitokea kwa Jamala litokee tena kwa Farida. Alijijua fika kwamba hakuwa na uwezo wa kutumia mpira kwa sababu hakuwa akisikia raha yoyote ile, kwa hiyo, kwa wakati huo, alijitahidi kuwa makini ili asiweze kumpa mimba Farida na kutokea matatizo mengine.
Uhusiano ule uliendelea zaidi na zaidi mpaka pale ambapo Selemani akaanza kuugua ugonjwa ambao kwa mara ya kwanza hakuuelewa ulikuwa ukisababishwa na nini. Kila siku alikuwa mtu aliyekuwa kwenye maumivu makali sana jambo ambalo likamfanya kuanza kuelekea hospitalini.
“Figo yako moja imeharibika sana” Daktari alimwambia Selemani ambaye akaonekana kushtuka kupita kawaida.
Hakutarajia kama angekuwa na tatizo kama lile katika maisha yake. Hakuwa mvutaji sigara wala mnywaji pombe lakini Dokta alimpa taarifa kwamba figo yake moja ilikuwa imeharibika. Kwa Selemani, ile ikaonekana kuwa taarifa mbaya sana ambayo wala hakuitegemea,
Akayageuza macho yake na kumwangalia Farida ambaye alikuwa pembeni yake, wote wawili, nyuso zao zilikuwa katika majonzi makubwa. Alichokifanya Dokta ni kumpa baadhi ya dawa ambazo alitakiwa kuzitumia katika kipindi chote mpaka pale ambapo angemaliza dozi ile na kwenda kuchukua nyingine.
“Mbona dawa zenyewe gharama hivi?” Selemani alimuuliza Dokta Mtimo wa hospitali ya Tumbi.
“Shilingi elfu kumi ndio gharama yake halali. Utatakiwa kununua dawa hizi au kama utashindwa basi haina budi kuitoa figo yako moja ambayo imeharibika” Dokta Mtimo alimwambia Selemani ambaye alionekana kuwa kwenye huzuni kubwa.
Hiyo ndivyo ambavyo ilitakiwa kufanyika, japokuwa gharama zile zilikuwa kubwa sana kwake lakini alitakiwa kuzimudu. Kwa kiasi cha shilingi elfu kumi na tano ambacho alikuwa nacho kwa wakati huo, ilimpasa kutoa shilingi elfu kumi kwa ajili ya kupata dawa zile ambazo aliambiwa kwamba zingeweza kumsaidia katika kipindi hicho. Alipoona kwamba amezinunua dawa zile, wakaondoka mahali hapo.
Maisha ya selemani katika kipindi hicho yalikuwa yakitegemea kazi yake ya ujenzi ambayo alikuwa akiifanya kwa wakati huo. Mara kwa mara alikuwa akiitwa kwa ajili ya kuzikarabati baadhi ya nyumba ambazo zilikuwa zikihitaji kurakabatiwa kwa kiasi ambacho wala hakikuwa kikimtosha sana katika matumizi yake pamoja na mpenzi wake, Farida ambaye alikuwa akiishi nae katika nyumba yake kama mke wake.
“Kuna tatizo gani?” Selemani aliwauliza watu ambao walikuwa wamekuja nyumbani kwake.
“Nyumba yako inahitajika kubomolewa kwa ajili ya utanuzi wa barabara” Mwanaume mmoja ambaye alikuwa amevalia suti alimwambia Selemani.
“Kwa hiyo mtanilipa shilingi ngapi baada ya kuibomoa?” Selemani aliuliza.
“Hatukulipi kiasi chochote”
“Kwa nini msinilipe na wakati mnaibomoa nyumba yangu?”
“Kwa sababu imejengwa katika eneo la barabara” Mwanaume yule alimwambia Selemani.
“Hapana bwana. Hili si eneo la barabara” Selemani alimwambia huku akionekana kuanza kuchanganyikiwa.
“Unaiona nguzo ile ya umeme?” Mwanaume yule alimuuliza huku akimuonyeshea nguzo moja ya umeme.
“Ndio naiona. Imefanya nini sasa?”
“Nyumba zote ambazo zimejengwa nyuma ya nguzo ile, zipo eneo sahihi na ndizo ambazo zikibomolewa, wenye nyumba watalipwa, ila kwa nyumba ambazo zipo mbele ya nguzo ile, basi nyumba hizo zitabomolewa bila malipo yoyote yale” Mwanaume yule alimwambia Selemani ambaye alibaki kimya.
“Ila huu ni uonevu”
“Hapana. Huu si uonevu kabisa. Wewe uliyejenga nyumba hii ndiye uliyefanya makosa” Mwanaume yule alimwambia Abuu.
“Huu ni uonevu. Mbona haukututaarifu mapema na mmekuja kwa kushtukiza?”
“Hii nyumba ulijenga wewe?”
“Hapana”
“Alijenga nani?”
“Marehemu baba”
“Basi hilo ndio tatizo. Baba yako ilibidi akwambie kwani alipewa taarifa miaka kumi iliyopita. Alijua kila kitu. Kwa maana hiyo, yeye ndiye aliyefanya makosa ya kutokutekeleza kile ambacho alitakiwa kutekeleza kama kutafuta nyumba nyingine mapema” Mwanaume yule alimwambia Selemani.
“Sasa mimi nitakwenda kuishi wapi?” Selemani aliuliza huku akilengwa na machozi.
“Tafuta pa kuishi. Ndani ya miezi sita, nyumba itakuja kubomolewa” mwanaume yule alimwambia Selemani na kisha kuondoka mahali hapo.
Selemani akabaki akiwa na mawazo, akili yake katika kipindi hicho ilionekana kuchanganyikiwa kupita kawaida. Mfukoni hakuwa na fedha za kutosha, kazi zake za kuzikarabati nyumba ndizo ambazo zilikuwa zikimpatia kipato kidogo cha kuweza kumsogezea siku za kuendelea kuishi hapa duniani.
Katika maisha yake, hakuwa akilifikiria suala la kulipa kodi kwani alikuwa akiishi katika nyumba ambayo alikuwa ameachiwa na marehamu baba yake.
“Nitakwenda kuishi wapi sasa?” Selemani alijiuliza lakini hakupata jibu.
Maisha yake yakaanza kuvurugika hata kabla nyumba haijabomolewa, kila wakati akawa mtu wa mawazo mengi, hakujua ni kitu gani ambacho alikuwa akitakiwa kukifanya kwa wakati huo. Kuchanganyikiwa huko ndicho kilikuwa kitu ambacho kikamfanya kugombana na Farida kila siku hali ambayo haikuwa nzuri katika maisha yao ya mahusiano.
“Nenda kwenu sio lazima uishi na mimi malaya mkubwa wewe” Selemani alimwambia Farida kwa ukali katika siku ambayo walikuwa wakigombana.
“Ndio nakwenda. Kwani sina kwetu. Mwanaume gani wewe. Mwanaume hujui hata kujipanga” Farida alimwambia Selemani huku akimwangalia kuanzia juu mpaka chini.
“Nitakupiga makofi wewe mwanamke” Selemani alimwambia Farida huku akimsogelea.
“Unipige makofi! Hebu jaribu kama sijaiharibu hiyo figo yako iliyobakia” Farida alimwambia Selemani ambaye kwa kiasi fulani alionekana kuhofia.
Siku hiyo ndio ilikuwa ambayo Farida akaonyesha makucha yake, japokuwa kipindi cha nyuma alikuwa akionekana mwanamke mkimya asiyejua kuongea lakini siku hiyo ilikuwa ni balaa kubwa. Selemani akapewa maneno yake mpaka akabaki kimya akimwangalia Farida ambaye alikuwa akiongea kama kafungwa mota mdomoni.
Siku hiyo ndio ilikuwa siku ya mwisho kuwa katika uhusiano pamoja na Farida ambaye alionekana kuwa mkali kama pilipili. Maisha ya upweke yakaanza kumpata Selemani kiasi ambacho akaanza kupungua mwili wake. Mawazo mengi yakaanza kukipata kichwa chake kiasi ambacho muda mwingi alionekana kuwa mpweke kupita kawaida.
Hakuwa amejiandaa katika maisha yake, baada ya miezi sita, nyumba ile ikabomolewa. Ndugu zake wote wakaanza kumkimbia, Selemani akaanza kupata tabu katika maisha yake. Kwa sababu alikuwa katika maisha ya tabu hapo ndipo alipoamua kwenda kwa mjomba wake aliyekuwa akiishi Dar es Salaam kwa ajili ya kuhitaji hifadhi, alipofika huko, mjomba wake hakuwepo, alikuwa amehama na kuhamia sehemu isiyojulikana.
Kwa Sulemani ile ikawa kama laana, akaanza kuiona dunia kumbadilikia, muda mwingi akawa na mawazo, maisha ya kurandaranda ndani ya jiji la Dar es Salaam yakaanza rasmi. Vituo vya basi ndipo kulipokuwa na kitanda chake cha usiku. Alipoona kwamba maisha yanaendelea kuwa mabaya, hapo ndipo alipoanza rasmi kazi ya kuwakaba watu na kuwapora mali zao.
Hayo ndio yakawa maisha ambayo alikuwa ameyachagua kwa wakati huo. Mali ambazo alikuwa akizipora ndizo ambazo zilikuwa zikimpa fedha kila alipokuwa akiziuza. Maisha ya Selemani yakabadilika. Moyoni mwake hakujua kabisa kwamba ile ilikuwa ni laana ambayo ilianza kumtafuna taratibu, laana ambayo ilisababishwa kwa kuikataa mimba ya msichana Jamala ambaye alijifungua mtoto ambaye alikuwa mlemavu kwa kipindi hicho. Laana ile haikuwa na dalili ya kuisha, bado iliendelea kumtafuna zaidi na zaidi huku mara kwa mara figo yake ikiendelea kumletea matatizo katika afya yake.
Selemani aliiona dunia ikiwa imemgeuka, hakukuwa na mtu ambaye alikuwa akimjali, watu wote wakaonekana kutokumuona kwa jinsi alivyokuwa akiteseka kila siku. Japokuwa bado alikuwa akiendelea kufanya unyang’anyi lakini fedha ambazo alikuwa akizipata hazikuweza kuyabadilisha maisha yake, aliendelea kuishi katika maisha yake ya shida kila siku.
“Mungu wangu! Mbona umeniacha mimi mja wako?” Selemani aliuliza huku akiwa amekaa stendi ya daladala.
“Ni laana” Aliisikia sauti moyoni mwake, sauti ambayo hakujua ni nani alikuwa ameizungumza.
**********************************************
Mara kwa mara msichana jasmin alikuwa akilishika tumbo lake ambalo ndani yake kiumbe kidogo kilikuwa kimeanza kujitengeneza. Kila wakati alikuwa akionekana kuwa na furaha, hakuamini kama katika kipindi hicho alikuwa na mimba ya mwanaume ambaye alikuwa akimpenda kwa moyo wake wote, Abuu.
Hali ile wala haikuonekana kumuogopesha Jasmin, uamuzi wake wa kukubali kubeba mimba ulionekana kuwa uamuzi mzuri ambao wala hakuwahi kuujutia hata siku moja. Jasmin hakutaka kunyamaza kimya, alichoamua ni kumwambia mama yake ambaye alionekana kushtuka kupita kawaida.
Kwanza hakuamini, hakuamini kama Jasmin angeweza kuuruhusu mwili wake kupata mimba katika kipindi hicho, kipindi ambacho bado alikuwa akihitajika kusoma sana ili kukamilisha ndoto ambazo alikuwa amejiwekea katika maisha yake. Bi Rukia hakuonekana kukubali na kile alichoambiwa na binti yake, akaanza kumgombeza.
“Kwa nini umekubali kubeba mimba?” Bi Rukia aliuliza huku akionekana kukasirika.
“Nimeamua mama” Jasmin alimwambia mama yake ambaye aliliona jibu lile kuwa kama dharau kubwa sana kwake.
“Kwa hiyo umeamua tu?”
“Ndio”
“Mimba ya nani?”
“Abuubakari”
“Yule kiwete wako?”
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Ndio”
Majibu yale ndio yalionekana kumcharua zaidi Bi Rukia, hapo ndipo alipoongeza nguvu zake katika kumfokea Jasmin kwa uamuzi ule ambao alikuwa ameuchukua. Moyoni mwake, hakumpenda kabisa Abuu japokuwa binti yake, Jasmin alikuwa haambiwi kitu chochote kuhusu mwanaume huyo ambaye kwake alionekana kuwa furaha yake moyoni mwake.
Katika kila neno baya ambalo Bi Rukia alikuwa akiliongea mahali hapo, Jasmin hakuongea kitu chochote kile, alibaki kimya huku akilia tu. Hakuamini kama mpaka katika kipindi hicho bado kulikuwa na watu ambao hawakuwa wakiwapenda walemavu kwa kuona kwamba watu hao hawakuwa watu sahihi kuwa pamoja na watu ambao hawakuwa na ulemavu miilini mwao.
Jasmin aliumia, aliumia zaidi ya alivyokuwa akitarajia. Alitamani kuufumbua mdomo wake na kumtukana mama yake ambaye alikuwa akiendelea kumfokea sana huku akitoa maneno ya dharau juu ya Abuu. Jasmin alipoona kwamba kulikuwa na kila dalili za kushundwa kubaki kimya na hivyo kumtukana mama yake, akainuka na kisha kuanza kuelekea chumbani kwake.
Jasmin alibaki akilia, maneno ambayo alikuwa ameongea mama yake yalionekana kumuumiza kupita kawaida. Si kwamba lawama zile zilimuumiza, hapana, maneno ya kejeli ambayo aliyaongea mama yake juu ya Abuu ndio ambayo yalionekana kuwa kama msumali wa moto moyoni mwake.
Jasmin hakutaka kutoka nje, alijua fika kwamba kama angeyaruhusu macho yake kumuona mama yake basi moyo wake ungekuwa na hasira zaidi na hivyo kuongea naneo lolote baya kitu ambacho wala hakutaka kitokee kabisa. Aliendelea kubaki chumbani kwake mpaka ilipofika saa mbili usiku ambapo mlango wa chumba chake ulipoanza kugongwa, alipoufungua, alikuwa baba yake, mzee Muksin.
“Tatizo nini Jasmin?” Mzee Muksin alimuuliza alimuuliza.
“Mama amenifokea”
“Kisa nini?”
“Nina mimba” Jasmin alimwambia baba yake, mzee Muksin.
Mzee Muksin hakuongea kitu, akabaki kimya kwa muda huku akionekana kufikiria jambo fulani. Ni kweli alikuwa akimpenda sana binti yake lakini suala la kumwambia kwamba alikuwa na mimba lilionekana kumkasirisha sana. Jasmin alikuwa binti yake, mtoto pekee katika familia yake, hakutaka kumkasirisha, Jasmin alionekana kuhitaji msaada wao katika kila jambo.
“Mimba ya nani?”
“Ya Abuubakari” Jasmin alijibu huku akitokwa na machozi.
“Yule kijana mlemavu?”
“Ndio. Ila mama amemtukana” Jasmin alimwambia baba yake, mzee Muksin.
Kilio hakikupungua, bado Jasmin alikuwa akilia tu. Maneno ya mama yake ambayo alikuwa ameyaongea dhidi ya Abuu yaliendelea kujirudia kichwani mwake jambo ambalo lilikuwa likimuuma kupita kawaida. Kila wakati alikuwa akizidi kulia zaidi na zaidi, macho yake yakaonekana kuwa kama kisima kikubwa cha machozi ambayo yalikuwa yakitiririka mashavuni mwake.
“Usijali Jasmin. Kilichotokea kimetokea” Mzee Mukisin alimwambia Jasmin huku akimkubatia.
Hali ambayo alikuwa nayo Jasmin katika kipindi hicho ilionekana kutokubadilika hata kama angesemwa na watu wote duniani. Mzee Muksin akakubaliana na hali hiyo, hapo ndipo alipoamua kuwa bega kwa bega na mtoto wake katika kumpa moyo kwa kila kitu ambacho kingeendelea kuhusiana na ujauzito ule.
Siku zikazidi kwenda mbele na ndipo dalili hasa za kuwa mjamzito zilipoanza kujionyesha mwilini mwake. Akaanza kutapika ovyo huku mwili wake ukichoka kupita kawaida. Muda mwingi Jasmin alikuwa akiutumia kuwa ndani ya chumba chake akiwa amepumzika. Matunda machachu kama maembe mabichi ndivyo ambavyo vilikuwa vitu ambavyo alikuwa akipenda sana kuvitafuna kwa wakati huo.
Mawazo ya Jasmin bado hayakuacha kumfikiria Abuu, mwanaume ambaye alikuwa akimpenda na kumhitaji, mwanaume ambaye katika kipindi hicho alikuwa ameubeba ujauzito wake. Siku ziliendelea kwenda zaidi na zaidi, japokuwa Jasimn alitakiwa kujiunga na chuo Kikuu cha Dar es Salaam lakini kutokana na hali ambayo alikuwa nayo katika kipindi hicho wala hakujiunga, alisubiria mpaka katika kipindi ambacho angejifungua mtoto wake.
Ingawa katika kipindi cha nyuma mama yake, Bi Rukia alikuwa akionyesha ukali na chuki za waziwazi lakini kikafika kipindi ambacho hata yeye pia ilimbidi kukubaliana na kile kitu ambacho kilikuwa kikiendelea mwilini mwa Jasmin, akaanza kumpa ushirikiano katika kila kitu ambacho alikuwa akikihitaji.
Baada ya miezi tisa, Jasmin akaanza kujisikia uchungu jambo ambalo likamfanya kupelekwa hospitalini na kisha kujifungua mtoto wa kike. Hiyo ikaonekana kuwa furaha kwake, mtoto yule alikuwa amefanana nae kwa kila kitu huku baadhi ya viungo akifanana na Abuu.
Mtoto huyo ndiye ambaye alionekana kumpa furaha Jasmin, furaha ambayo ilikuwa imepotea katika kipindi kirefu ikaanza kurejea, hakuamini kama katika kipindi hicho alikuwa amejifungua mtoto na kuitwa mama huku baba wa mtoto huyo akiwa Abuu, mwanaume aliyekuwa mlemavu, mwanaume mwenye akili za kuzaliwa, mtu ambaye alikuwa ameamua kuanza kutengeneza dawa za magonjwa ya kansa kwa lengo la kuzisambaza bure duniani kuwasaidia masikini.
****
Abuu alishinda katika maabara, kichwa chake kilikuwa kikifikiria mambo mengi kwa wakati huo. Pembeni mwake alikuwa na vitabu vingi ambavyo vilikuwa vimeandikwa na baadhi ya madaktari waliokuwa wakubwa duniani. Alikuwa akikipitia kitu kimoja baada ya kingine. Macho yake hayakuonekana kuridhika, katika kipindi hicho alikuwa na nia moja ya kutengeneza dawa ya magonjwa ya kansa, dawa ambayo ingesambazwa dunia nzima hasa katika nchi masikini.
Katika kipindi hicho, magonjwa ya kansa yalikuwa yakizidi kuiteketeza dunia hii. Wagonjwa wengi walikuwa wakifariki mahospitalini kutokana na magonjwa hayo ambayo yalikuwa yakiwatafuna sana. Msaada mkubwa ulikuwa ukihitajika, madaktari walikuwa wakiangaika kila siku lakini wala tiba ya magonjwa hayo wala haikupatikana.
Abuu alishinda katika maktaba ile kwa masaa kumi na mbili, mpaka anakwenda kulala, hakuwa amekamilisha kile ambacho alikuwa akikihitaji. Alichokifanya kwa wakati huo ni kuamua kuwasiliana na Bwana Maliki na kisha kuanza kumuomba msaada wake kwani alijua kwamba bila yeye, asingeweza kukamilisha kile kitu ambacho alikuwa akitaka kukifanya.
“Nikusaidie nini Abuu?” Bwana Maliki alimuuliza Abuu.
“Nataka unisaidie chumba chako kimoja nyumbani kwako nikigeuze na kuwa maabara” Abuu alimwambia Bwana Maliki ambaye alionekana kushtuka.
“Unasemaje?”
“Ndio hivyo. Naomba unisaidie”
“Huko chuoni si kuna maabara?”
“Ipo lakini akili yangu wala haitulii. Kila wakati watu wanaingia ingia na kunitoa katika umakini” Abuu alimwambia Bwana Maliki ambaye katika kipindi hicho alimchukulia kama baba yake wa kumzaa.
“Dah! Sasa unataka kufanya nini hasa?”
“Nataka kutengeneza dawa ya magonjwa ya kansa” Abuu alimjibu Bwana Maliki.
“Usinitanie Abuu”
“Huo ndio ukweli. Naomba unisaidie. Nimekwishapata kila kitu, yaani kuna baadhi ya vitu nitahitajika kununua na kisha kazi kuanza” Abuu alimwambia Bwana Maliki.
“Utaweza kweli?”
“Asilimia mia moja”
“Basi hakuna tatizo. Vitu gani unataka nikununulie?” Bwana Maliki alimuuliza Abuu ambaye akaanza kumuagizia vitu hivyo.
Kila kilichopangwa na ndicho kilichofanyika, baada ya siku mbili, Bwana Maliki akakitenga chumba kimoja na kuwa maabara ndogo ya Abuu ambayo angeitumia katika kutengeneza dawa zake ambazo alikuwa akitaka kuzitengeneza. Abuu alipofika ndani ya chumba hicho, akafurahi sana kwani kila alichokuwa akikihitaji, kilikuwa kikipatikana.
“Unakumbuka nilikwambia nini?” Abuu alimuuliza bwana Maliki.
“Uliniambia mengi tu”
“Achana na hayo. Lile ambalo nilisema kwamba nimekuja hapa nikiwa masikini”
“Nimekumbuka. Ulisema kwamba ungeondoka ukiwa tajiri” Bwana Maliki alimwambia Abuu.
“Sawa sawa. Una kumbukumbu sana baba. Kazi inaanza. Nahitaji utulivu” Abuu alimwambia Bwana Maliki.
Abuu akaanza kazi yake. Alikaa kwa masaa zaidi ya ishirini huku akiendelea kufanya kila liwezekanalo kuhakikisha kwamba anatengeneza dawa ya magonjwa ya kansa. Hakula chakula, alikuwa akiifanya kazi yake ambayo aliamini kwamba kupitia hiyo angeweza kufanikiwa sana katika maisha yake.
“Masaa ishirini. Nahitaji kupumzika kwa dakika tano kisha kuendelea na kazi yangu. Sirudi chuo mpaka kila kitu kikamilike hata kama itanichukua mwaka mzima” Abuu alisema katika kipindi ambacho alikuwa akiufungua mlango na kutoka nje ya chumba kile.
********************************************
Maisha wala hayakuweza kubadilika, laana ambayo ilikuwa juu yake ikaonekana kuwa kubwa hata zaidi ya mwili wake. Matatizo hayakumuisha Selemani, kila alipokuwa akitoka katika tatizo hili, alikuwa akiingia katika tatizo jingine hali ambayo ilimfanya kusurubika kupita kawaida.
Kichwa chake hakikuweza kukumbuka kwamba kila kitu ambacho kilikuwa kikiendelea kutokea katika maisha yake kilisababishwa na laana, laana ya kuikataa mimba ambayo alikuwa amempa msichana Jamila. Maisha ya shida ndio ambayo yalikuwa yakiendelea katika kipindi hicho ndani ya maisha yake, hakuonekana kuwa na amani, hakuonekana kuwa na furaha hata kidogo.
Kila siku alikuwa akiendelea kufanya unyang’anyi lakini hakuwa akipiga hatua za maendeleo kimaisha maishani mwake. Leo alikwapua simu ya shilingi laki mbili na kuiuza elfu ishirini kiasi ambacho kwake yeye kilionekana kuwa kikubwa sana.
Akili yake haikuonekana kufanya kazi sawa sawa. Kikafika kipindi ambacho akaamua moja kwa moja kuanza kutumia sigara, kitu ambacho hakuwahi kukitumia katika maisha yake yaliyopita. Kampani za marafiki zake ambayo alikuwa nayo ndio ambayo ilionekana kumuingiza ndani ya utumiaji wa sigara. Kwake yeye, alijiona kuwa mjanja kama watu wengine kama ambavyo angekuwa akitumia kilevi hicho ambacho kutokana na hali yake ilivyokuwa mbaya kilizidi kumuongezea matatizo zaidi.
Kila siku moyoni mwake alikuwa akinung’unika, aliona kama Mungu alikuwa amemuacha katika njia panda ambayo hakujua ni upande upi alitakiwa kwenda katika muda huo. Selemani hakupunguza manung’uniko yake, alipokuwa akikosa mtu wa kumfanyia unyang’anyi, kwake akaona kwamba Mungu siku hiyo hakuwa pamoja nae.
Tangu alipoanza kutumia sigara, kuna tatizo moja ambalo likaanza kutokea mwilini mwake. Hakujua tatizo hili lilikuwa likisababishwa na nini. Kwa kuwa alikuwa akivuta sana sigara, siku ambayo alikuwa akikosa sigara, mwili wake ulikuwa ukimuwasha kupita kawaida.
Muda mwingi alikuwa akijikuna ovyo, mwili wake ulikuwa umekwishazoea sigara kupita kiasi japokuwa alikuwa ameanza miezi kadhaa iliyopita. Alipokuwa akiwashwa sana, alipotumia sigara, miwasho ile ilikuwa ikipotea mwilini mwake.
Hayo ndio yakawa maisha ambayo alikuwa akiishi mitaani. Uvutaji wake sigara wala haukukoma kabisa, kila siku alikuwa akivuta sana sigara kiasi ambacho hata wale ambao walikuwa wamemshawishi kuvuta sigara wakawa wanamshangaa kutokana na uhodari wake katika uvutaji.
“Unatisha Sele. Sigara ya ngapi hiyo?” Chopa, mmoja wa marafiki zake wakubwa alimuuliza.
“Ya saba”
“Toka asubuhi mpaka sasa hivi?” Chopa aliuliza kwa mshangao.
“Ndio. Si unajua bila hii kitu maisha hayaendi. Sisi wengine tunaonekana kama tuna nuksi tu, Mungu katupa kisogo, zamu zetu za neema zinakuja halafu anajifanya kama hatuoni vile anawapa wajinga wengine” Selemani alimwambia Chopa.
Alianza na sigara moja, akapandisha mpaka kufikia sigara mbili, akaona haitoshi, akazidisha nyingine zaidi na zaidi mpaka kufikia uwezo wa kuvuta sigara saba kwa siku. Kitendo kile cha kuvuta sana sigara kikamfanya hata kujituma zaidi katika kazi zake ili mladi atafute fedha ya kununulia sigara.
Alikuwa akivuta sana sigara, kwake zilionekana kama kumpenda lakini ukweli ni kwamba sigara hazikuwa zikimpenda kabisa. Uso wake wa ujana ukaanza kupotea, mikunjo pajini mwake ikaanza kuonekana hata katika kipindi ambacho alikuwa akitabasamu, uso wa Selemani ukaanza kubadilika zaidi na zaidi.
Sura ya kizee ikaanza kumsogelea, sura ikazidi kumkomaa kila siku. Alikuwa akionekana kuwa mzee wa miaka arobaini na wakati alikuwa kijana wa miaka ishirini na tano tu. Sura yake ikawa imeanza kufanana na wale watu ambao wanakunywa pombe haramu ya gongo au chang’aa.
Ndani ya miaka miwili na nusu alikuwa akiendelea kufanya unyang’anyi kwa ajili ya kujipatia chakula cha kila siku pamoja na kununua sigara ambazo katika kipindi hicho zilikuwa zikiuzwa shilingi 60 tu. Siku zikaendelea kukatika zaidi, maisha yake hayakuonekana kuwa na unafuu hata kidogo, hakuwa akifanya lolote la maana zaidi ya kuendelea kuteseka katika maisha yake.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Hapo ndipo ambapo aliamua kuanza kuwa mpiga debe wa daldala. Kila daladala ilipokuwa ikisimama kituoni, Selemani alikuwa akipiga debe kuwaita abiria. Kwa kiasi fulani japo si sana kazi ile ikaonekana kuanza kumlipa. Kiasi cha shilingi 100 ambacho alikuwa akilipwa katika kipindi hicho kwa kila daladala ambayo alikuwa akiitia abiria ikaonekana kuwa kubwa kwake.
Kila alipokuwa akianza kazi yake asubuhi mpaka usiku, alikuwa akifanikiwa kupata zaidi ya shilingi elfu mbili ambayo kwake ilionekana kuwa kiasi kikubwa sana ambacho kilimfanya hata kuongeza idadi ya sigara ambazo alikuwa akizivuta kwa siku.
“Tutapiga debe mpaka lini sasa?” Chopa alimuuliza Selemani.
“Mpaka Mungu atakapofungua milango ya neema” Selemani alijibu.
“Lini sasa?”
“Sijui lini. Ila atafungua tu” Selemani alimwambia Chopa.
“Hivi hatuwezi kutafuta mchongo mwingine wa kufanya?”
“Kama upi?”
“Wowote tu ili mladi tuweze kutoka”
“Labda tungekuwa tumesoma Chopa”
“Hata kama hatujasoma. Hivi hatuwezi kufanya chochote kutoka?”
“Mmmh! Ngumu sana”
“Sikiliza. Kuna mchongo nimepewa na wana jana”
“Mchongo gani?”
“Kusepa Bongo”
“Kusepa Bongo! Kwenda wapi?”
“Kwa George H Bush kula bata” Chopa alimwambia Selemani huku akimtaja rais wa kipindi hicho, George H Bush, baba wa rais aliyefuata baada ya Clinton, George W Bush.
“Acha utani wewe. Tutakwenda vipi?”
“Tunakwenda kwa meli”
“Kwa hiyo tunazamia”
“Pigia mstari”
“Hapana. Hiyo noma sana”
“Acha uoga mtoto wa mama wewe. Maisha ukiyaogopa hautoki. Kama vipi jiandae, sisi ndio tunaondoka kesho kutwa pamoja na wana wengi wa kule Kivukoni” Chopa alimwambia Selemani.
“Kwa meli gani?”
“Meli ile kuleee. Unaiona? Meli ya Kimarekani ile”
“Ile ya Kimarekani au ya Kigiriki?”
“Nadhani ya Kimarekani. Kwani lile neno Greece linamaanisha nini?”
“Wala sijui. Inawezekana linamaanisha Marekani” Selemani alimwambia Chopa.
“Ndio hivyo. Kuna wadau kama saba tunakwenda nao. Jiandae vya kutosha nikuunganishe nao. Huwezi jua bwana. Unaweza kukuta Mungu kakuandalia mchumba mzuri wa Kizungu huko mbele” Chopa alimwambia Selemani.
Japokuwa moyo wake ulikuwa ukisita kukubaliana na Chopa lakini mwisho wa siku akajikuta akikubaliana nae kutokana na maneno mengi ya mbwembwe ambayo alikuwa akiongea Chopa mbele yake. Maneno mengi yenye kutia matumaini, maneno mengi yenye kuvutia yakafanya Selemani kuona kwamba kulikuwa na maisha mengine mazuri ambayo Mungu alikuwa amemuandalia ukiachilia maisha ya nchini Tanzania ambayo yalikuwa yamemtesa sana.
Wote wakaanza kujiandaa na safari na siku iliyofuata, Selemani akatambulishwa kwa vijana saba ambao wote walikuwa wakiungana kwa pamoja kutaka kuzamia kwenda nchini Marekani kwa kutumia meli ambayo wao walifikiri ni meli ya Kimarekani kumbe ilikuwa meli ya Kigiriki, wazee wa bahari ambao walikuwa na roho mbaya kupita kawaida.
Walichokifanya ni kuendelea kujiandaa. Japokuwa zamani ilikuwa ni lazima uingie ndani ya meli kabla ya wiki moja meli kuondoka lakini katika kipindi hiki mambo yalionekana kuanza kubadilika, ilikuwa inawezekana kuingia hata siku moja kabla ya meli kuondoka na kila kitu kuwa safi.
“Ulishawahi kuzamia?” Jamaa mmoja, Ibra alimuuliza Selemani.
“Bado”
“Kwa hiyo hata njia za panya za kuingia melini huzijui?”
“Yeah”
“Ok! Usijali. Unajua kuogelea?”
“Sana tu”
“Hilo si tatizo. Nimefanikiwa kupata ratiba ya meli ile. Inaondoka saa tisa usiku. Sisi tutakachokifanya ni kuingia melini saa saba usiku wa leo” Ibra aliwaambia wenzake.
“Hakuna tatizo”
Kila kitu ambacho kilipangwa ndicho ambacho kilifanyika. Walichokifanya ni kuanza kuogelea mpaka pale ambapo kulikuwa na meli na kisha kuelekea katika upande ambao wala haukuwa na watu kabisa huku wakiwa wamebeba mabegi yao ambayo yalikuwa na biskuti na juisi kwa ajili ya kuwasaidia kwa chakula njiani.
Walifanikiwa vizuri kuingia ndani ya meli hiyo ya mizigo ambayo ilikuwa ikielekea katika nchi za Ulaya. Walichokifanya mara baada ya kuingia ndani ya meli hiyo ni kuanza kutembea kwa kunyata mpaka katika sehemu ambazo zilikuwa na mizigo mingi na kisha kujificha huku kila mmoja akionekana kuwa na furaha kwani walijua kwamba safari yao ya kwenda Ulaya ilikuwa imekubali.
Saa tisa usiku, nanga ikatolewa na meli ile kuanza kuondoka kuelekea upande wa Kusini huku lengo likiwa ni kuingia Afrika Kusini na kisha kupita mpaka katika nchi za Ulaya, safari ambayo ingewachukua zaidi ya miezi mitatu mpaka kufika huko.
“Nimeshaanza kuwaona watoto wa kizungu machoni mwangu” Chopa alimwambia Selemani ambaye alibaki akitabasamu tu ndani ya meli ile ya Kigiriki.
Maisha kwao yalionekana kuwa ni upofu. Mioyo yao ilikuwa ikifikiria kwenda Ulaya tu kwa wakati huo, kamwe hawakuamini kabisa, hawakuamini kama watu kama wao wangeweza kufanikiwa endapo wangeendelea kubaki nchini Tanzania. Kwa sasa, wameanza safari, safari ya kuelekea nchini Marekani. Hakuna aliyekuwa akijua maisha yao ya mbele ambayo yangewapata katika safari hiyo, na endapo wangejua kile ambacho kingewapata, wangeendelea kubaki nchini Tanzania, ndani ya jiji la Dar es Salaam kuendelea kupiga debe katika daladala mbalimbali.
*****
Abuu alikuwa akijiona kuwa nyuma ya muda, mara kwa mara alikuwa akifikiria namna ambayo angefanikiwa katika lile ambalo alikuwa akilifanya kwa wakati huo. Kichwa chake hakikuisha mawazo, bado alikuwa akiwafikiria watu ambao walikuwa wakiishi katika maisha ya kimasikini ambao hawakuwa na uwezo hata wa kununua dawa ambazo kwao zilionekana kuwa bei kubwa kuzinunua.
Kwake, alijiona kuwa mkombozi wa watu ambao walikuwa wakiendelea kuwauguza ndugu zao ambao walikuwa wakiendelea kufa kwa sababu ya kukosa tiba ya magonjwa mbalimbali ya kansa. Abuu alikaa sebuleni kwa dakika tano tu, akarudi katika maabara ndogo ya muda na kisha kuendelea na utengenezaji wa dawa ya magonjwa ya kansa.
Uwezo wake mkubwa wa akili ndio ambao ulimfanya kufanya mambo mengi kwa wakati huo, mambo ambayo wala hakuwa ameyategemea kabla. Mara kwa mara Bwana Maliki alikuwa akiingia ndani ya chumba hicho kuangalia kile ambacho Abuu alikuwa akikifanya lakini kwake, hakuelewa kitu chochote kile.
Siku ya kwanza ikakatika, siku ya pili ikaingia mpaka kumalizika na ya tatu kuingia lakini bado Abuu alikuwa akiendelea na kazi yake kama kawaida. Katika kipindi hicho hakutaka kutoka nje ya nyumba ile, alikuwa akishinda ndani tu mpaka pale ambapo dawa ile ingekamilika na hatimae kuthibitishwa na kuanza kupewa watu ambao walikuwa wakiendelea kuteseka na magonjwa ya kansa duniani.
“Bado tu?” Bwana Maliki alimuuliza.
“Kazi kubwa. Ingekuwa dawa ya magonjwa ya kawaida kama kichwa, tumbo na magonjwa mengine, ingekuwa tayari kitambo sana” Abuu alimwambia Bwana Maliki.
“Kwa hiyo utachukua muda gani tena?”
“Kama wiki nzima”
“Ningependa sana kuona unafanikiwa juu ya hili unalolifanya. Kama kuna kitu kitahitajika, naomba unitaarifu” Bwana Maliki alimwambia Abuu na kisha kutoka ndani ya chumba kile.
Utengenezaji wa dawa haukuwa mwepesi hata mara moja. Kuna kipindi alikuwa akitengeneza na kisha kugundua kwamba kulikuwa na vitu ambavyo alitakiwa kuviweka lakini akasahau, wakati mwingine alikuwa akitengeneza na kugundua kwamba alitakiwa kufanya hiki na si kile ambacho alikuwa amekifanya.
Siku zikaendelea kukatika kama kawaida lakini Abuu aligoma kutoka ndani ya nyumba ile mpaka pale ambapo angefanikiwa kile ambacho alikuwa akitaka kufanikiwa kukipata kwa muda huo. Shuleni, wanachuo walikuwa wakimtafuta Abuu kwa ajili ya kuwasaidia katika masomo mbalimbali lakini Abuu wala hakuonekana machoni mwao.
Mara kwa mara walikuwa wakielekea ndani ya chumba chake na kuwauliza wenzake juu ya mahali alipokuwa lakini hakukuwa na mtu ambaye alikuwa akifahamu jambo ambalo likaonekana kuwatia wasiwasi hasa mara baada ya kufika katika meza ya uongozi wa chuo kile.
Mtu muhimu kwao alionekana kupotea katika mazingira ya kutatanisha, walikuwa wakimhitaji sana Abuu arudi chuoni hapo kwa ajili ya kuendelea kuwafundisha wenzake katika sehemu ambazo hawakuwa wakielewa lakini wala hakuonekana. Wanachuo wakaanza kuwa wanyonge kupita kawaida, nyuso zao zikajawa na huzuni ambayo ilionyesha kwamba walikuwa wamekosa kitu fulani katika maisha yao.
“Au alirudi nchini kwao?” Jamaa mmoja aliuliza.
“Mmmh! Sijui”
“Sasa itakuwaje ghafla haonekani?”
“Hata sisi tunashangaa kama unavyoshangaa”
“Kuna namna. Inawezekana watu wenye wivu wamemfanyia kitu kibaya”
“Kama kitu gani unavyofikiria wanaweza kumfanyia?”
“Kumuua”
“Usifikirie hivyo, utaanza kututia wasiwasi”
Siku ziliendelea kukatika zaidi na zaidi, wiki ya pili ikaingia lakini wala Abuu hakuonekana chuoni hapo. Kila mmoja alikuwa na hamu ya kumuona Abuu akirudi ndani ya chuo hicho na hatimae kuendelea kuwafundisha wenzake kama kawaida.
Kwa upande wa Abuu, bado alikuwa akiendelea kutengeneza dawa ambayo alikuwa akiisitisha na kuongezea vtu vingine. Katika utengenezaji wake wa dawa hiyo, Abuu alichukua mwezi maima na ndipo dawa hiyo ilipokamilika na hatimae kumuonyeshea Bwana Maliki.
“Namshukuru Mungu nimekamilisha” abuu alimwambia Bwana Maliki.
“Sasa itaitwaje?”
“Abja2” Abuu alijibu.
“Ndio jina gani hilo?”
“AbuuJamalaJasmin”
“Mmmh! Kwa hiyo itatumikaje?”
“Hii dawa itatakiwa kutengenezwa kwa staili ya vidonge viwandani na kisha kuanza kusambazwa bure kabisa. Sitohitaji kulipwa hata senti tano katika dawa hizi” Abuu alijibu.
“Sawa. Kuna chochote unahitaji?”
“Nataka kuonana na Waziri wa Afya wa hapa India pamoja na dokta mkuu wa hospitali ya Taifa” Abuu alimwambia Bwana Maliki.
“Hilo si tatizo. Kuna jingine?”
“Labda utakapokwenda kuwaita, naomba umtumie bibi yangu kiasi fulani cha fedha. Nadhani zile zitakuwa zimekwisha” Abuu alimwambia Bwana Maliki.
“Usijali. Nitafanya hivyo” Bwana maliki alimwambia Abuu na kisha kuondoka mahali hapo kwenda kuwaita watu ambao walikuwa wakihitajika. Japokuwa mawasiliano ya simu yalikuwepo lakini Bwana Maliki hakutaka kutumia simu, alitaka kuwafikishi salama mdomo kwa mdomo.
**********************************************
Bwana Maliki akatoka nje ya nyumba yake na kisha kuanza kulifuata gari lake ambalo lilikuwa limepakiwa ndani ya eneo la nyumba yake, akamwambia mlinzi afungue geti na kisha kuanza kuondoka nalo mahali hapo. Japokuwa kulikuwa na dereva ambaye kazi yake ilikuwa ni kumuendesha katika kila sehemu ambayo alikuwa akitaka kuelekea lakini kwa haraka ambayo alikuwa nayo mahali hapo, hakutaka dereva kumuita dereva huyo kwa kuona kwamba angemchelewesha tu.
Bwana Maliki alikuwa akiendesha gari lake kwa kasi lakini mara baada ya kufika katika njia za mitaani, akaanza kuendesha gari kwa mwendo mdogo kutokana na idadi kubwa ya watu kuwepo barabarani. Mawazo yake katika kipindi hicho yalikuwa yakifikiria kuutua mzigo mzito ambao ulikuwa moyoni mwake, mzigo ambao alitakiwa kumwambia Waziri wa Afya nchini India pamoja na daktari mkuu wa hospitali ya taifa ya hapo India.
Bwana Maliki aliendesha gari mpaka alipoingia katika mtaa wa Bujalpur, mtaa wa watu wenye fedha nchini India, mtaa ambao ulikuwa na ofisi nyingi za viongozi wa serikali ya nchi hiyo. Akaanza kuelekea katika sehemu ambayo ilikuwa na ofisi ya Bwana Kumir, waziri wa Afya nchini India kwa ajili ya kumwambia kile ambacho alikuwa amekifanya Abuu katika kipindi hicho.
Japokuwa nchini India kulikuwa na idadi kubwa ya watu lakini katika mtaa huo hakukuwa na watu wengi kabisa, watu walikuwa wachache tena wa kuhesabu hesabu tu. Bwana Maliki akaendesha gari lake mpaka pale ambapo kulikuwa na ofisi ya Bwana Kumir na kisha mlinzi kufungua geti na kulipitisha gari lake hadi katika eneo la ofisi ile.
Bwana Maliki akateremka na kisha kuanza kupiga hatua kuelekea katika mlango wa kuingilia ndani ya jengo la ofisi ile, alipoufikia mlango, ukajifungua na kisha kuingia ndani. Akaendelea kupiga hatua mpaka kufika katika sehemu ya mapokezi na kisha kuelezea shida yake ambayo ilikuwa imemleta mahali hapo na kisha kuruhusiwa kuingia ndani ya ofisi ya Bwana Kumir na kisha kuanza kuongea nae.
“Naona kama unanitania?” Bwana Kumir alimwambia Bwana Maliki.
“Huo ndio ukweli”
“Inawezekana vipi mtu mwenye digrii moja akatengeneza dawa?” Bwana Kumir aliuliza huku uso wake ukionyesha dhahiri kushangaa.
“Kipaji”
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Hata kama. Sidhani kama kipaji kinaweza kuwa kwa namna hii. Kwa staili hii, tunaweza kuwaua wagonjwa badala ya kuwatibia” Bwana Kumir alimwambia Bwana Maliki.
“Sawa. Ila cha msingi ningeomba kwanza uonane nae na pia ufanye mipango ya dawa yake kuchunguzwa, inaweza ikasaidia sana” Bwana Maliki alimwambia Bwana Kumir.
Kilichoendelea ni kupigiwa simu kwa Dokta Patel ambaye alikuwa akihitajika katika ofisi hiyo kwa ajili ya kuongozana na Bwana Maliki kuelekea katika nyumba yake na kuonana na Abuu huku wakiwa pamoja na Balozi wa Tanzania nchini India, Bwana Maliki.
Ndani ya dakika thelathini, Dokta Patel akafika katika ofisi hiyo na kisha kuanza kumsikiliza Bwana Maliki. Maneno ambayo alikuwa akiongea mahali hapo yalionekana kuwa kama kichekesho katika masikio yake, hakuamini kama kile ambacho alikuwa akikisikia kilikuwa ni kitu ambacho kilikuwa kikitokea kwa wakati huo.
Mwanafunzi mwenye digrii moja kwa wakati huo alikuwa amekwishatengeneza dawa yake ya kansa ambayo alihitaji ifanyiwe uchunguzi na kisha kuanza kusambazwa nchini India kabla ya kusambazwa dunia nzima. Jambo hilo likaonekana kuwa gumu sana kuaminika ndani ya mioyo yao japokuwa Bwana Maliki alikuwa akiendelea kusisitiza kwamba dawa hiyo ilikuwa ipo vizuri.
Hawakutaka kuandikia mate kwa wakati huo, walichokuwa wakikihitaji ni kuelekea katika nyumba hiyo na kisha kuiona dawa hiyo. Hawakutaka kuendelea kubaki ndani ya ofisi hiyo, walichokifanya ni kuanza kuelekea katika nyumba ya Bwana Maliki kwa ajili ya kuiona hiyo dawa ambayo ilikuwa imetengenezwa na Abuu.
Baada ya nusu saa, gari hilo likaanza kuingia ndani ya eneo la nyumba hiyo ambapo moja kwa moja wakateremka na kuanza kupiga hatua kuufuata mlango wa kuingilia ndani ya jengo hilo la nyumba hiyo. Walipoufikia mlango, Bwana Maliki akaungua na kisha kuingia ndani.
Abuu alikuwa amekaa katika moja ya makochi ya kifahari ambayo yalikuwepo ndani ya nyumba ile sebuleni pale. Akawasalimia na kisha Bwana Maliki kumtambulisha Abuu kama mtu ambaye alikuwa ametengeneza dawa ile. Wote wakaanza kumwangalia huku wakionekana kutokuamini.
Kwanza Abuu alionekana kuwa mtu tofauti sana katika macho yao, hawakuamini kabisa kwamba mtu huyo ndiye ambaye alikuwa ametengeneza dawa ambayo walikuwa wamepewa taarifa kabla ya kuiona. Abuu kwao alionekana kuwa mtu wa kawaida sana, machoni mwake hakuwa na miwani ya macho kitu ambacho kwao kingewafanya kwamba mtu huyo alikuwa na uwezo wa kufanya jambo fulani kubwa, uvaaji wa miwani kwao ulionekana kuwa maalumu kwa watu ambao walikuwa na akili nyingi, hasa madaktari.
“Haiwezekani” Bwana Kumir alijikuta akisema huku akimwangalia mara baada ya utambulisho ule.
“Kwa nini?”
“Kwa sababu ni mdogo mno” Bwana Kumir alijibu.
Kimue mue cha kuwaonyeshea dawa ile bado kilikuwa kikiendelea ndani ya moyo wa Bwana Maliki, alichokuwa akikitaka ni kuwaonyeshea kwamba kijana wa Kitanzania kwa wakati huo alikuwa amefanikiwa kutengeneza dawa ya magonjwa ya kansa, dawa ambayo ilionekana kuwa mkombozi wa wagonjwa wote ambao walikuwa wakiugua ugonjwa huo.
Wote kwa pamoja wakainuka, kitu kingine kikaonekana kuwashangaza, ukilema wa Abuu. Dharau za watu wa India ambao asilimia kubwa walikuwa wakiwatenga walemavu zikaanza kuonekana nyusoni mwao, hawakuwa wakiamini kama kungekuwa na mlemavu yeyote duniani ambaye angeweza kufanya jambo lolote la mabadiliko, hawakuwa wakikumbuka kwamba Abuu alikuwa mlemavu wa mwili na si mlemavu wa akili.
“Hii ndio dawa ambayo nimeitengeneza kwa ajili ya magonjwa ya kansa” Abuu aliwaambia huku akiwaonyeshea.
“Inaitwaje?” Bwana Patel aliuliza huku akiiangalia vizuri.
“Inaitwa Abja2” Abuu alijibu.
Wote wakaichukua dawa ile ambayo ilikuwa katika kopo moja na kuanza kuiangalia. Dawa ilionekana kuwa kama kwenye unga unga fulani ambayo ilihitajika kuwekwa sawa na kutengenezwa katika mtindo wa vidonge na hata wakati mwingine ingefaa kutengenezewa kama dawa mojawapo ya kuchomwa kwa kutumiwa sindano.
“Kuna mambo matatu nadhani itatakiwa kuchagua moja” Dokta Patel aliwaambia mara baada ya kuangalia kwa makini dawa ile.
“Mambo gani?”
“Wewe mtengenezaji ungependa dawa hii iwe katika mfumo gani? Vidonge au kimiminiko?” Dokta Patel aliuliza.
“Vidonge” Abuu alijibu.
“Sawa. Itahitajika kufanyiwa uchunguzi kwanza. Baada ya kuonekana kufaa, tutakuita na kuongea nawe, tukiona haifai, usijisumbue tena kutengeneza dawa ya namna hii” Bwana Kumir alimwambia Abuu.
Hawakutaka kuendelea kubaki mahali hapo, walichokifanya ni kuondoka pamoja na ile dawa kwa ajili ya kuifanyia majaribu ili kuona kama ingefaa au isingefaa.
“Itafaa tu. Tena itafaa mpaka watashangaa” Abuu alimwambia Bwana Maliki.
****
Jopo la madaktari wakuu ishirini wa nchini India walikuwa wamekutana ndani ya chumba cha hospitali kuu ya Taifa ya nchini hapo India kwa ajili ya kuongelea jambo ambalo lilikuwa limewatatiza sana kwa wakati huo, jambo ambalo lilikuwa limevichanganya vichwa vyao kupita kawaida.
Dawa ambayo alikuwa ameitengeneza Abuu ndio ambayo ilikuwa ikianza kujadiliwa mahali hapo, dawa ile ndio ambayo iliwafanya madaktari hao wakuu kuitana mahali hapo kwa ajili ya kuizungumzia dawa hiyo ambayo ilionekana kuwa ni ya kitofauti sana kuliko dawa zote ambazo ziliwahi kutengenezwa katika dunia hii.
Dawa ile ilikuwa imekwisafanyiwa majaribio zaidi ya mara kumi, kwa kila mgonjwa wa kansa ambaye alikuwa akitumia dawa ile, alikuwa akipata nafuu na mwisho wa siku kupona kabisa ugonjwa ule. Dawa ile ikaonekana kuwa kali kupita kawaida juu ya magonjwa yote ya kansa ambayo yangekuwa yakiwapata watu mbalimbali.
Kikao hicho kilikuwa ni kizito na cha siri sana, katika kipindi hicho walikuwa wakitaka kufanya kitu kimoja tu, kumdhulumu Abuu kutokana na kile ambacho alipoteza muda wake mwingi kukitengeneza. Madaktari hawakuonekana kuamini kama mwanafunzi wa mwaka wa pili alikuwa ametengeneza dawa ya kansa na wakati wao walikuwa na zaidi ya digrii moja lakini wala hawakuwa wamefanikiwa kutengeneza hata dawa ya mafua.
Jambo lile kwa wakati huo likaonekana kuwaumiza vichwa vyao kupita kawaida. Kijana mdogo Abuu alikuwa amefanya jambo moja kubwa ambalo wote lilikuwa limewafanya kujikuna vichwa vyao huku wakifikiria kupita kawaida juu ya kipi ambacho kilikuwa halali kufanyika katika kipindi hicho.
Uamuzi ambao ulikuwa umetolewa katika kipindi hicho ulikuwa mmoja tu, kumdhulumu Abuu dawa ile na kisha wao kujitangaza kwamba ndio walikuwa wameitengeneza kwa ajili ya kuiuza na kisha kujipatia kiasi kikubwa cha fedha. Hawakuonekana kufahamu kwamba Abuu alikuwa ametumia muda mrefu sana kuwa ndani, kujinyima kwa kila kitu mpaka dawa ile ilipokamilika, walichiokuwa wakukufikiria wao kwa wakati huo ni kumdhulumu tu.
“Hilo wazo zuri. Kwanza mtu mwenye ngozi nyeusi. Achana nae, hii itakuwa ikiuzwa kwa jina letu” Dokta Patel aliwaambia madaktari wengine.
Wazo la kumdhulumu likaonekana kupitishwa na kila daktari ndani ya ukumbi ule, kila mmoja aliona wazo la kumdhulumu Abuu dawa ile na kujimilisha wao lilikuwa ni jambo jema ambalo lingewaingizia kiasi kikubwa sana cha fedha katika maisha yao.
Utu ukawaondoka mioyoni mwao, walichokuwa wakikifikiria kwa wakati huo ni kutengeneza fedha tu katika maisha yao. Dawa ambayo Abuu alikuwa ameitengeneza kwa lengo la kuisambaza bure dunia nzima kwa wakati huo madaktari wenye digrii nchini India walikuwa wameamua kwa moyo mmoja kutaka kuisambaza dawa ile, tena si bure kama Abuu alivyotaka iwe, isambazwe kwa wanaoihitaji, tena kwa malipo makubwa.
***************************************
Safari ya kuelekea nchi za Ulaya kwa kupitia Afrika Kusini bado ilikuwa ikiendelea kama kawaida. Ndani ya meli ile, wazamiaji akiwepo Selemani walikuwa wakila biskuti ambazo walikuwa wamezibeba pamoja na kunywa jusi ambazo zilikuwa katika mabegi yao madogo.
Kila mmoja kwa wakati huo alikuwa akiifikiria safari hiyo, hamu ya kuingia katika nchi mojawapo ya Ulaya ilikuwa imewashika kupita kawaida. Hawakuwa wakifikiria kitu chochote kwa wakati huo zaidi ya kufikiria kile ambacho wangeweza kukutana nacho katika nchi za Ulaya.
Maisha ya kuishi nchini Tanzania yalikuwa yamekwishawachosha kupita kawaida, kwa wakati huo, walikuwa wakielekea Ulaya, sehemu ambayo waliamini kwamba maisha mazuri yangepatikana katika maisha yao. Hakukuwa na mtu yeyote ambaye alikuwa akifikiria shida, kitu ambacho waliamini vichwani mwao ni kwamba kila mtu ambaye alikuwa akiishi Ulaya, maisha yake yalikuwa mazuri na si msoto kama ilivyokuwa Tanzania.
Siku ya kwanza ikakatika, bado walikuwa ndani ya meli ile. Juisi pamoja na biskuti zilionekana kuwasaidia sana katika kuyadanganya matumbo yao kwamba walikuwa wakiyashibisha. Siku ya pili ikaingia, bado safari ilikuwa ikiendelea zaidi na zaidi.
Maisha yao ndani ya meli ile ya mizigo wala hayakuwa na uhuru kabisa, walikuwa wakitumia muda mwingi kukaa chini kuliko kusimama au kutembea. Siku ya tatu ikaingia na hatimae wiki nzima kukatika mpaka vyakula ambavyo walikuwa wakivitumia kuisha na hivyo njaa kali kuanza kuwashika.
Hali ikaonekana kuwa mbaya sana kwao, kadri siku zilivyokuwa zikizidi kwenda mbele na ndivyo ambavyo njaa kali zilivyozidi kuwashika zaidi na zaidi. Japokuwa hakukuwa na mtu ambaye alikuwa radhi kutoka ndani ya chumba kile kwa kuogopa kukamatwa lakini kikafika kipindi ambacho hawakuwa na jinsi, walitakiwa kutoka nje ya chumba kile kwa ajili ya kutafuta chakula.
Hawakujua ni kwa namna gani wangeweza kupata chakula lakini walijua fika kwamba kama wangejaribu kutoka ndani ya chumba kile na kuanza kutembea tembea ndani ya meli ile basi wangefanikiwa kupata chakula ambacho walikuwa wakikitumia baharia ambao walikuwa wakifanya kazi katika meli ile.
“Nani aanze kutoka kwenda kututafutia chakula?” Lilikuwa swali ambalo liliulizwa na kila mtu kichwani mwake.
Wote wakaanza kuangaliana, kila mmoja alikuwa akihofia kwa wakati huo japokuwa walikuwa na njaa na hivyo walikuwa wakihitaji vyakula. Ibra ambaye ndiye alionekana kuwa kiongozi wa msafara ule akaamua kumchagua Chopa kwamba ilikuwa ni lazima atokea ndani ya chumba kile na kwenda kutafuta chakula, walitakiwa kufanya hivyo kwa zamu.
Japokuwa hakuwa akitaka kufanya hivyo lakini Chopa akajikuta akitoka ndani ya chumba kile huku ikiwa ni saa saba usiku. Akaanza kutembea kwa mwendo wa kunyata kuelekea katika sehemu ambazo alijua fika kwamba kungekuwa na mabaki ya vyakula kutoka kwa baharia ambao walikuwa wamevibakiza vyakula vyao.
Mapigo yake ya moyo yalikuwa yakidunda kupita kawaida, kijasho chembamba kilikuwa kikimtoka huku mwili wake ukitetemeka kana kwamba alikuwa akisikia baridi. Chopa akafanikiwa kufika katika sehemu ambayo ilikuwa na vyakula vingi vilivyokuwa vimebakishwa na baharia wa meli ile na kisha kuanza kuvikusanya na kuondoka navyo mahali hapo.
Japokuwa vyakula vile vilikuwa ni mabaki lakini kwao vikaonekana kuwa vyakula safi na vilifaa kuliwa. Kutokana na njaa ambayo walikuwa nayo, wakala haraka haraka mpaka walipomaliza, lakini hawakuwa wameshiba, hivyo walihitaji vyakula vingine.
“Nenda kachukue vingine” Ibra alimwambia Chopa.
“Hapana bwana. Zamu ya mwingine sasa” Chopa alimwambia Ibra ambaye akaanza kuangalia huku na huku na kumchagua Selemani.
“Wewe, zamu yako sasa” Ibra alimwambia Selemani.
“Nani? Mimi?” Selemani aliuliza kana kwamba hakuwa amelisikia swali hilo.
“Ndio. Zamu yako”
“Naomba zamu yangu iwe kesho”
“Hapana. Zamu yako ni leo. Nenda kachukue vyakula vilivyobaki” Ibra alimwambia Selemani.
“Lakini mimi naumwa”
“Unaumwa nini?”
“Kifua. Si mnaona jinsi ninavyokooa kisiri” Selemani alimwambia Ibra.
“Hata kama. Nenda katuchukulie chakula” Ibra alimwambia Selemani kwa ukali.
Kila mmoja mahali hapo alikuwa akimng’ang’ania Selemani aelekee kule katika sehemu ya kulia chakula kwa ajili ya kuchukua mabaki ya chakula kiasi ambacho Selemani hakuwa na jinsi. Kila mmoja alikuwa akijua fika kwamba Selemani alikuwa na tatizo, tatizo ambalo lilikuwa likimfanya kukohoa mara kwa mara pamoja na kujikuna sana kutokana na kukosa sigara kwa kipindi kirefu, lakini pamoja na kujua hivyo, walimtaka kuelekea kule.
Selemani akasimama na kisha kuanza kuelekea huko. Mapigo yake ya moyo yalikuwa yakimdunda kupita kawaida. Alitembea kwa mwendo wa kunyata huku katika kipindi ambacho kikohozi kilikuwa kikimpata, alikuwa akiufunika sana mdomo wake na kukohoa kisiri sana.
Selemani aliendelea kutembea mpaka pale alipofika katika sehemu ambayo kulikuwa na mabaki ya vyakula vingi na kisha kuanza kuvikusanya. Kutokana na kuwa na hamu ya sigara, macho yake yalipotua katika vipisi kadhaa vya sigara, hakutaka kuviacha, akavichukua pamoja na kiberiti na vyakula na kisha kurudi kule ndani ya chumba kile.
Kila mmoja alimuona Selemani kuwa mjanja kupita kawaida kutokana na kuja na vyakula vingi kuliko vile alivyokuja navyo Chopa. Wakampokea na kisha kuviweka chini na kuanza kula. Walitumia muda wa dakika kumi kula, kila mmoja akajiona kushiba.
“Asante Mungu! Nilikuwa nakufa kwa njaa” Dullah aliwaambia wenzake.
“Safari bado ndefu sana. Kila nikichungulia kwenye hiki kitundu naona hakuna hata dalili ya kisiwa wala mji wowote ule” Ibra aliwaambia huku akichungulia katika kitundu kidogo kilichokuwa mahali hapo.
Selemani akachukua kipisi kimoja cha sigara ambavyo alikuwa amevitoa katika sehemu ile alipokwenda kuchukua chakula na kisha kukiwasha na kuanza kuvuta. Kila mmoja akaonekana kumshangaa, hakutakiwa kuvuta sigara ndani ya chumba hicho kutokana na moshi wa sigara ile kusambaa katika sehemu kubwa.
Kila mmoja alijaribu kumuonya Selemani juu ya uvutaji wa sigara mahali pale lakini kutokana na hali ambayo alikuwa nayo katika mwili wake, aliona ni vigumu sana kukubali kuacha kuvuta sigara ile. Selemani aliendelea kuvuta zaidi na zaidi mpaka katika kipindi ambacho wakaanza kusikia vishindo vya watu wakianza kusogea kule walipokuwa.
Ghafla, wazamiaji wote wakabaki kimya, Selamani akaizima sigara ile na kisha kuanza kuchungulia kule kulipokuwa na mlango wa kutokea ndani ya chumba kile. Watu wanne ambao walionekana kuwa na miili iliyojazia wakatokea katika sehemu ya mlango ule na kisha kutegesha pua zao kama ambavyo watu ambao walikuwa wakitaka kuisikia harufu fulani.
Watu wale wakaanza kuongea Kigiriki hali ambayo iliwafanya wazamiaji wale kutokuelewa kitu chochote kile. Mwanaume mmoja akaondoka mahali hapo huku akiwaacha wengine wakiwa wamesimama pale mlangoni. Kila mzamiaji alikuwa na wasiwasi mwingi, tayari hali ile ikaonekana kuwatia wasiwasi kupita kawaida kwa kuona kwamba tayari kulikuwa na kitu cha hatari kwao ambacho kingeendelea mahali hapo.
Mara baada ya dakika mbili, mwanaume yule akarudi pamoja na wanaume watano ambao walikuwa na bunduki mikononi mwao. Kila mmoja akaonekana kushtuka kupita kawaida, tayari hatari ikaonekana kuwa karibu yao, kila mmoja akaanza kusali kimoyo moyo kwa kuona kwamba ni msaada wa Mungu tu ndio ambao ungewafanya kutokuonekana na watu wale.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Wanaume wale wakaingia ndani ya kile chumba kikubwa na kisha kuanza kufanya upekuzi wao huku wakiwa na tochi zao zilikuwa na nguvu kubwa. Wakaanza kumulika huku na kule, wakatoa mizigo hii na ile mpaka pale ambapo wanafanikiwa kuwaona wazamiaji ambao walikuwa wakiwatafuta.
Wote wakaweka chini ya ulinzi, walikuwa wakitetemeka kupita kawaida. Hawakutaka kubaki chumbani pale, wakaanza kuondoka nao kuelekea katika sehemu nyingine kabisa. Hawakupelekwa kiusalama zaidi, walikuwa wakipigwa ngumi na mateke jambo ambalo likaanza kuwachana nyuso zao.
“Tusameeniii” Kila mmoja alisema lakini hakukuwa na mtu ambaye alionekana kuwaelewa.
Wote wakapelekwa mpaka katika vyuma vya meli ile, pembezoni kabisa mwa meli ile na kisha kuamriwa kusimama. Wakaanza kuhesabiwa na kisha mapipa manne kutupwa baharini. Kila mmoja alijua fika kwamba ni kitu gani kilichotakiwa kuendelea mahali hapo.
Kama kawaida yao, Wagiriki hawakuonekana kuwa na huruma, nyuso zao zilikuwa zikitoa tabasamu yalioonyesha kwamba walikuwa wamefurahia sana kuwakamata wazamiaji wale. Bila kushikwa, wakaambiwa kimatendo kwamba walitakiwa kujirusha ndani ya bahari ile.
Kabla ya kujirusha, wakayapeleka macho yao katika kila upande, hakukuwa na dalili yoyote ya nchi kavu au kisiwa wala meli yoyote mahali pale. Eneo zima la bahari lilionekana kutokuwa na kitu chochote kile. Walichokifanya mara baada ya kuona kwamba wazamiaji wale walikuwa wakiogopa kufanya kile walichokuwa wakitaka kukifanya, kujitosha baharini, ikapigwa risasi moja hewani, wote wakajikuta wakijitupa baharini na kisha kuanza kupiga mbizi kuyaendeea mapipa yale ambayo yalikuwa yametupwa baharini na kisha kuyashika.
Kwa macho yao, wakaiona meli ile ikiendelea na safari kama kawaida huku baharia wale wakicheka kwa shangwe kwa kuona kwamba walikuwa wamefurahia kile ambacho walikuwa wamekifanya katika kipindi kile, kuwatosa majini wazamiaji wale ambao walionekana kutokuwa na msaada wowote ule.
“Sigara yako imetuponza. Sigara yako imekatisha safari yetu mjinga wewe” Ibra alimwambia Selemani kwa sauti ya juu yenye ukali.
Selemani hakusema kitu chochote kile, alijua fika kwamba yeye ndiye alikuwa chanzo cha tatizo lile lakini kwa wakati huo haukuwa muda wa kulaumiana tu, walitakiwa kusubiri meli yoyote ipite mahali hapo na kisha kuomba msaada wa kuweza hata kurudishwa nchini Tanzania kwani mpaka kufikia mahali hapo, hawakujua walikuwa katika eneo la nchi gani, hakukuwa na nchi kavu yoyote ambayo ilikuwa ikionekana machoni mwao baharini mule. Mikono yao ilikuwa imeshika mapipa yale tu.
***********************************************
Kitu kilichokuwa kimepangwa cha kumdhulumu Abuu dawa yake ndicho ambacho kilitakiwa kufanyika kwa wakati huo. Hakukuwa na swali lolote la nyongeza ambalo walitakiwa kujiuliza, iliwapasa kufanya kile ambacho kwa wakati huo walikuwa wamepanga kukifanya.
Dawa ile ikachukuliwa na kisha kupelekwa katika maabara ya hospitali ya Taifa ya India na kisha kuanza kuangalia vitu ambavyo vilikuwa vimetumika katika utengenezaji wa dawa ile. Waliangalia kuanzia kitu kimoja mpaka kingine. Kila kitu ambacho kilikuwa kimechanganywa ndani ya dawa ile kilikuwa kikijulikana, mchanganyiko wake ulionekana kuwachanganya sana.
Akilini mwao hawakuamini kama kweli mchanganyiko wa vile vitu ambavyo alikuwa amevichanganya katika dawa ile vingeweza kuleta dawa ya magonjwa ya kansa. Waliendelea kuichunguza zaidi na zaidi, mwisho wa siku wakagundua kwamba kulikuwa na vitu vitatu zaidi ambavyo vilikuwa vimechanganywa katika dawa ile tofauti na vile ambavyo walikuwa wakivifahamau. Walijaribu kuviangali vitu hivyo vitatu, hawakuonekana kuvifahamu kabisa. Walionekana kuchanganyikiwa zaidi mara walipoona kwamba vitu hivyo vitatu ambavyo hawakuwa wakivifahamu navyo vilikuwa vimehanganywa na vitu vingine vitatu ambavyo navyo hawakuwa wakivifahamu japokuwa walikuwa na digrii vichwani mwao.
Mpaka kufikia hatua hiyo, Abuu akaonekana kuwa bora zaidi kwao, elimu yake kuhusiana na utengenezaji wa dawa ile ukaonekana kuwa mkubwa hata zaidi ya walivyokuwa wakifikiria. Madaktari wale wakaonekana kuchanganyikiwa kupita kawaida jambo ambalo liliwafaya kuitana tena ndani ya kile chumba kwa ajili ya kuzungumza tena.
“Mmmh! Huyu mtu si mtu wa kawaida” Dokta Patel aliwaambia madaktari wenzake mara baada ya kikao hicho kuchukua zaidi ya dakika arobaini.
“Mlipochunguza mligundua nini?” Dokta Rajeev, mtaalamu wa magonjwa ya wakinamama aliuliza.
“Dawa yake imefanyiwa mchanganyiko mkubwa sana, mchanganyiko ambao wala hatuufahamu kabisa” Dokta Patel alijibu.
Wote wakaonekana kuchanganyikiwa kupita kawaida ila hawakutaka kushindwa kabisa kujua vile vyote ambavyo vilikuwa vimechanganywa katika dawa ile. Walichokifanya kwa wakati huo ni kuwapigia simu daktari mkuu wa Urusi pamoja na daktari mkuu kutoka nchini China kwa ajili ya kuja nchini India na kisha kuangalia vile ambavyo vilikuwa vimechanganywa katika dawa ile.
Mara baada ya siku mbili, madaktari wale wakafika nchini India na moja kwa moja kupelekwa katika maabara na kupewa ile dawa na kisha kuanza kuichunguza. Akaanza Dokta wa China, Dokta Cheung Li kuichunguza dawa ile. Alitumia muda wa dakika arobaini na tano kuichunguza, alipomaliza, akauinua uso wake na kisha kumwangalia Dokta Patel na wenzake.
“Hii dawa inafanya kazi kweli?” Dokta Li aliuliza kwa mshangao.
“Tena sana. Ina nguvu hadi inatuogopesha” Dokta Patel alijibu.
“Mchanganyiko wake ni wa ajabu sana. Nimejua baadhi ya vitu ambavyo vimechanganywa pamoja lakini vitu vingine wala sivijui kabisa na wala sijawahi kuviona japokuwa nina digrii mbili za udaktari” Dokta Li aliwaambia.
Kila mmoja akaonekana kushangaa, tayari dawa ile ilionekana kuwa dawa yenye utofauti sana na dawa nyingine na ndio maana ilikuwa na mchanganyiko wa ajabu ambao hakukuwa na Dokta yeyote ambaye alikuwa akiufahamu. Hapo hapo wakamuita dota Usmanov kutoka Urusi ambaye alikuwepo ndani ya chumba kile na kisha kuanza kuichunguza dawa ile kwa kutumia vyombo maalumu vya kuchunguzia dawa ambavyo vilikuwepo mahali pale lakini nae hakuona kitu.
“Huyu aliyetengeneza dawa hii ana digrii ngapi?” Lilikuwa swali la kwanza alilouliza Dokta Usmanov kutoka Urusi.
“Ana digrii moja” Alitoa jibu ambalo likamfanya hata Dokta Li kushangaa.
“Unasemaje?”
“Ndio hivyo”
“Huyu mtu ana akili za ziada sasa. Naweza kumuona?” Dokta Usmanov alimuuliza Dokta Patel.
“Hapana. Hilo haliwezekani” Dokta patel alijibu kwani alijua fika kama angeonana nae, basi ishu yao ingevurugika.
Hivyo ndivyo ilivyokuwa, dawa ambayo alikuwa ameitengeneza Abuu ilionekana kuwachanganya kupita kawaida. Muda wote walikuwa wakiichunguza kwa kuangalia kila kitu ambacho kilikuwa kimechanganywa katika dawa ile lakini wala hawakuweza kupata jibu. Vitu vitano ndivyo ambavyo vilikuwa vimechanywa, na vitu vitatu, vilikuwa vimechanganywa na vitu vingine vitatu, ni vitu gani sasa? Hakukuwa na mtu ambaye alikuwa akifahamu.
Dokta Patel na wezake wala hawakutaka kukata tamaa, walichokifanya ni kuanza kuwasiliana na Dokta Mickey kutoka nchini Marekani kwa ajili ya kuja nchini India na kufanya kazi ile ambayo walikuwa wakitaka ifanyike kwa wakati huo. Kila mtu alikuwa na imani na Dokta Mickey kwa sababu alikuwa ni Dokta mkubwa na mwenye uwezo mkubwa.
Dokta Mickey ndiye alikuwa Dokta mkuu nchini Marekani ambaye alikuwa akifanya kazi katika hospitali ya Washington Medical Centre ambayo ilikuwa nchini Marekani. Dokta Mickey ndiye alikuwa akiaminika sana nchini Marekani kutokana na uwezo mkubwa ambao alikuwa nao katika kipindi hicho.
Wagonjwa wengi wenye matatizo mbalimbali walikuwa wakikusanyika katika hospitali hiyo kwa ajili ya kutibiwa na Dokta Mickey ambaye uwezo wake ulimfanya mpaka rais wa nchi hiyo kipindi hicho, Barack Obama kumfanya kuwa Dokta pekee wa familia yake.
Dokta huyo alionekana kushindikana kabisa katika magonjwa mbalimbali japokuwa nae hakujua tiba ya ugonjwa wa kansa ilikuwa ni nini. Alipofika nchini India n kuambiwa kwamba kulikuwa kumepatikana dawa ya kansa, kwanza alionekana kushtuka kupita kawaida, hakuamini kama kungekuwa na Dokta ambaye angeweza kutengeneza dawa ya kansa kabla yake yeye kuigundua dawa ile kwani alijiona kuwa bora zaidi ya madaktari wote duniani.
Mara baada ya kufika, moja kwa moja akapelekwa hotelini na kisha siku iliyofuata kupelekwa katika chumba kile kilichokuwa kikifanyika mikutano ile na kisha kuanza kuichunguza dawa ile kwa kutumia vipimo maalumu ambavyo alikuwa navyo na alikuja navyo kutoka nchini Marekani.
Dokta Mickey aliichunguza dawa ile zaidi na zaidi lakini wala hakupata jibu lolote lile hali ambayo ilionekana kumchanganya sana. Lengo lake kwa wakati huo ni kuangalia mchanganyiko wa dawa ile ili atakapofika nchini Marekani basi aweze kutengeneza dawa yake ambayo angeisambaza dunia nzima na kisha kutengeneza fedha zaidi ya zile ambazo alikuwa nazo katika kipindi hicho.
Alichukua muda wa saa moja, hakufanikiwa, akaona haitoshi, akaomba muda wa mapumziko zaidi ya saa moja jingine na kisha kurudi na kuanza kufanya uchunguzi wake huku kijasho chembamba kikimtoka lakini napo hakuambulia kitu jambo ambal;o lilionekana kumshangaza.
“Hii dawa kweli inaponesha?” Dokta Mickey aliuliza.
“Tena sana. Yaani ina nguvu kupitiliza. Tumewatibu watu kumi, wote wamepona” Dokta Patel alimjibu.
Dokta Mickey akaonekana kushtuka zaidi, hakuamini kama kweli dunia ilikuwa imepata dawa ya ugonjwa ambao ulikuwa ukiua sana watu duniani katika kipindi hicho. Moyoni alikuwa na hamu ya kutaka kufahamu namna ambavyo dawa ile ilivyotengenezwa lakini wala hakuwa amejua ni mchanganyiko wa vitu gani ambavyo vilikuwa vimetumika katika kutengeneza dawa ile.
Dokta Mickey akataka kuonana na mtengenezaji wa dawa ile. Dokta Patel na madaktari wengine wakaonekana kutokuwa na jinsi, wakamruhusu kuonana nae kwa masharti ya kutokumwambia kitu chochote kile juu ya dawa ile jambo ambalo Dokta Mickey akaonekana kukubaliana nao.
Kwa mara ya kwanza macho yake yalipotua kwa Abuu, Dokta Mickey hakuonekana kuamini kile alichokuwa akikiona, hakuamini kama mtu yule ambaye alikuwa akimwangalia alikuwa ndiye mtu ambaye aliitengeneza dawa ile ambayo ilionekana kuwa na nguvu ya kutibu magonjwa ya kansa. Akamwangalia Abuu mara nyingi nyingi usoni, akayarudisha macho yake kwa Dokta Patel na bwana Maliki.
“Ndiye huyu?” Dokta Mickey aliuliza.
“Ndiye mwenyewe” Dokta patel alijibu.
“Acheni utani. Namuulizia mtu ambaye alitengeneza dawa ile” Dokta Mickey aliwaambia.
“Ndiye huyo”
“Hivi leo ni siku ya wajinga duniani?” Dokta Mickey aliuliza.
“Hapana. Huu ni mwezi wa tisa”
“Sawa. Naomba mniitie basi mtu huyo. Sina muda wa kupoteza” Dokta Mickey aliwaambia.
“Ndiye huyo hapo”
“Acheni utani bwana”
“Huyo ndiye kijana aliyetengeneza dawa hiyo”
Dokta Mickey alibaki akiwa na mshangao mkubwa kupita kawaida, kila alipokuwa akimwangalia Abuu alishindwa kuamini kama kijana yule ndiye ambaye alikuwa ametengeneza dawa ile. Kichwa chake kabla kilikuwa kikifikiria kwamba mtu ambaye alikuwa ametengeneza dawa ile alikuwa mtu mkubwa mwenye ndevu nyingi ambaye alikuwa na digrii ya udaktari, kumbe alipokuja kukutana nae, alikuwa kijana mdogo sana, yaani kama angekuwa na watoto ishirini, basi angekuwa mtoto wake wa mwisho.
Siku hiyo Dokta Mickey akabaki akiongea nae tu, hakutaka kuacha kuongea na Abuu na kumwambia juu ya mchanganyiko ambao alikuwa ameutumia katika dawa ile. Abuu hakuwa wazi kusema kitu chochote kile, kila kitu kilikuwa siri yake. Dokta Mickey hakuonekana kuwa na jinsi, moyoni alitamani sana kuwa karibu na Abuu kwa kuamini kwamba mtu huyo alikuwa na vitu vya ziada kichwani mwake.
“Ni lazima nisafiri na wewe kwenda nchini Marekani. Hauna hadhi ya kukaa huku Asia” Dokta Mickey alimwambia Abuu maneno ambayo yalimshtua sana Dokta patel kwa kuona kwamba kulikuwa na uwezekano kama wasingefanya juhudi za ziada, Abuu alikuwa akiondoka kuelekea nchini Marekani, nchi ambayo kwa muonekano tu wala asingeweza kukataa.
“Hawezi kuondoka kwenda popote pale. Hiyo ni mali yetu sasa” Dokta Patel akaingilia.
Hapo kukatokea malumbano kadhaa huku Dokta Mickey aking’ang’ania kwamba ilikuwa ni lazima Abuu apelekwe nchini Marekani kwa ajili ya kuwasaidia watu wengi ambao walikuwa na magonjwa ya kansa lakini kwa Dokta Patel alionekana kulipinga hilo.
“Ni lazima aelekee nchini Marekani. Haijalishi mtataka au hamtotaka, huyu mtu ni lazima afike Marekani” Dokta Mickey aliwaambia.
“Si nyie tu, hata nchini kwao mtu huyu hatokwenda. Yupo India na ataendelea kuwa India, haondoki kwenda popote pale, hata nchini kwao hatokanyaga” Dokta Patel alimwambia.
“Utake usitake. Atafika Marekani tu, tena mwezi huu huu” Dokta Mickey alimwambia Dokta Patel na kisha kuondoka mahali hapo huku Abuu akibaki kuwa na mshangao.
******************************************
Wazamiaji bado walikuwa wameshikilia mapipa ambayo yalikuwa yametupwa ndani ya bahari ile. Mawimbi yalikuwa yakiendelea kupiga zaidi na zaidi lakini hakukuwa na mtu ambaye alikuwa tayari kuyaachia mapipa yale ambayo walikuwa wameyashika.
Hali ya hewa ndani ya bahari iile ilionekana kuwatisha kupita kawaida, mawimbi yale ambayo yalikuwa na nguvu kubwa yalikuwa yakiendelea kuwapiga kupita kawaida. Hali ya mahali hapo ilikuwa ni baridi kali, miili yao ilikuwa ikitetemeka kupita kawaida.
Mpaka jua linachomoza, bado hali zao hazikuwa nzuri, walikuwa wakiendelea kupigwa na mawimbi yale zaidi na zaidi. Kila walipokuwa wakiangalia huku na kule, hakukuwa na dalili zozote za nchi kavu au kisiwa chochote kile jambo ambalo waliona kwamba huo ungekuwa mwisho wa maisha yao katika bahari hiyo.
Katika kipindi hicho, walitamani sana kuona meli au boti yoyote ikiwa inaelekea kule walipokuwa lakini jambo hilo wala halikuweza kutokea kabisa. Hawakujua ni wapi kulikuwa upande wa mashariki, Magharibi, Kaskazini au Kusini, kote kulionekana kutokuwa na kitu chochote kile.
Miili yao ilikuwa ikitetemeka kupita kiasi na kutokana na mawimbi yale ambayo yalikuwa yakiwapiga, yakawafanya kuanza kusikia njaa. Hakukuwa na chakula mahali hapo, hakukuwa na msaada wowote ule japokuwa walitamani sana jambo hilo litokee mahali hapo.
Saa la kwanza likapita, likaingia saa la pili na mpaka kufikia masaa kumi, bado walikuwa wameendelea kushilia mapipa yale. Katika kipindi hicho hakukuwa na mtu ambaye alikuwa radhi kuyaachia mapipa yale, kila mmoja alikuwa na imani kwamba ni laizima kungekuwa na msaada ambao ungeweza kutokea mahali hapo na hicyo kuokolewa.
“Kuna msaada kweli unaweza kutokea?” Chopa alimuuliza Selemani huku akitetemeka kupita kawaida.
“Ngoja tuendelee kusubiri, nadhani tutapata msaada” Selemani alimwambia Chopa huku nae akiwa anatetemeka na huku akiwa amelishikilia pipa moja pamoja na Chopa.
Masaa yalizidi kukatika mpaka usiku unaingia, bado hakukuonekana msaada wowote ule jambo ambalo lilionekana kuwakatisha tamaa kabisa. Siku nzima wakawa wameitumia ndani ya bahari hiyo ya Hindi. Mpaka usiku unaingia, hakukuwa na msaada wa meli yoyote ambao ulionekana karibu nao.
Katika usiku huo, baridi lilikuwa kali zaidi baharini, walikuwa wakitetemeka kupita kawaida kiasi ambacho ngozi za miili yao zikaanza kujikunja kunja. Kila mmoja akaanza kujuta, walijuta sababu ambazo ziliwapelekea kupanga mikakati ya kuzamia na kuelekea nchi za Ulaya au marekani.
Siku nzima wakawa wameitumia katika bahari ile huku kila mmoja akionekana kuchoka kupita kawaida. Matumbo yao yakazidi kusikia njaa zaidi na zaidi lakini hakukuwa na chakula chochote ambacho walikuwa wamekipata. Kazi yao kubwa kwa siku nzima ilikuwa ni kunywa maji ya bahari ile ambayo yalikuwa na chumvi kupita kawaida.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Siku ya pili ikaingia, hali haikubadilika, bado ilikuwa vile vile. Njaa zilizidi kuwauma kupita kawaida, kila mmoja akaona mwili wake ukiishiwa nguvu. Mikono yao ikaanza kuonekana kuchoka kushikilia mapipa yale jambo ambalo kila mtu alikuwa akitamani kuyaachia na hatimae kuzama baharini na kufa. Hali ilionekana kutisha kupita kawaida, siku ya pili ikaingia na kukatika, bado walikuwa wakiendelea kuwa katika bahari ile. Katika siku ya tatu ya kuwa baharini pale, wakaanza kukata tamaa.
Akaanza Dullah, mwili ulikuwa umechoka kupita kawaida, ngozi yake ilikuwa imejikunja kutokana na baridi pamoja na kukaa baharini kwa muda mrefu, akaviona vidole vyake vikikosa nguvu kabisa.
“Nimechoka. Siwezi kushikilia zaidi” Dullah alimwambia Ibra huku akionekana kuchoka zaidi.
Dullah alitamani kuendelea kulishikilia pipa lile lakini vidole vyake havikutaka kabisa kuleta ushirikiano na akili yake. Vidole vikaanza kuliachia pipa lile na hatimae kuanza kuzama baharini. Kila mtu alikuwa akimumwangalia, mioyo yao ilikuwa na maumivu sana lakini hawakuwa na jinsi, tayari kwa jinsi hali ilivyokuwa ikiendelea kwenda mbele na ndivyo ambavyo walizidi kuchoka zaidi na zaidi.
Bado msaada haukuonekana kabisa machoni mwao baharini pale, waliendelea kushikilia mapipa yale zaidi na zaidi. Mtu wa pili kuachia pipa alikuwa Halidi, kijana ambaye alikuwa na ndoto nyingi sana za kufanya katika kipindi ambacho angefika Ulaya.
Bado kila mmoja alionekana kuwa na wasiwasi, vidole vyao vilikuwa vimechoka sana kuyashikilia mapipa yale. Miili yao ilikuwa imeanza kuota mabaka ambayo yalisababishwa na kukaa kwa muda mrefu ndani ya maji yenye chumvi nyingi.
Mmoja baada ya mwingine akaanza kuchia pipa ambalo alikuwa amelishika na hatimae kuzama. Hali ilionekana kuwa ngumu zaidi, hata Chopa mwenyewe nae akaamua kuachia pipa lile jambo ambalo lilimfanya kuzama na kufa baharini.
Safari ya kwenda Ulaya, kulala na wanawake wa kizungu, kutafuta fedha na hatimae kuyabadilisha maisha yao ilikuwa imeishia katika bahari ile. Vijana wote ambao walikuwa wametangulizana nao walikuwa wameyaachia mapipa yale na hatimae kufa na hivyo kubakia watu wawili tu, Selemani na Ibra.
Wote walikuwa wameshikana mikono jambo ambalo liliwafanya kudumu kwa muda mrefu baharini pale. Usiku ukaingia. Baridi la siku hiyo lilikuwa kali kuliko siku nyingine zilizopita. Muda wote walikuwa wakitetemeka kupita kawaida. Mioyo yao ilikuwa ikisali ili Mungu aweze kuwaokoa katika pipa hali ambayo walikuwa nayo.
“Yaani tunakufa baharini kabla ya kufika Ulaya?” Chopa alimuuliza Selemani huku akionekana kuchoka kuishikilia mikono ya Selemani.
“Hatutokufa. Tutapata msaada” Selemani alimwambia Chopa japokuwa alijua fika kwamba huo ndio ulikuwa mwisho wa maisha yao.
Mpaka inaingia alfajiri ya siku ya nne, bado walikuwa baharini pale. Miili yao kwa wakati huo ikaonekana kutisha kupita kawaida. Miili ilianza kuota vitu vya kijani kama maji ambayo yalikuwa yamekaa sehemu moja kwa muda mrefu. Macho yao yalikuwa mekundu kupita kawaida kutokana na maji kuwapiga machoni kila wakati.
“Nimechoka” Alisema Chopa kwa sauti ya chini ambayo kwa kuisikia tu, ilionyesha dhahiri kwamba alikuwa amechoka.
“Jitahidi. Usiniache peke yangu” Selemani alimwambia Chopa huku aking’ang’ania mikono yake.
Hali hiyo haikuweza kusaidia kitu chochote kile, Chopa akaonekana kuchoka kupita kawaida, akaanza kuiachia mikono ya Selemani na hivyo kuanza kuzama, alikuwa amechagua kufa kuliko kuendelea kuteseka baharini pale. Selemani akaonekana kuumia kupita kawaida lakini wala hakuwa na jinsi, kile ambacho kilikuwa kimetokea wala hakuwa na uwezo wa kukizuia kabisa. Chopa akawa amezama baharini na kufa.
Wazamiaji wote wakawa wamekwishazama na kubakia Selemani peke yake ambaye alikuwa akiendelea kulishikilia pipa lile. Moyo wake uliumia kupita kawaida, alikuwa akitamani kulia lakini wala machozi hayakuweza kumtoka kabisa. Siku hizo zilionekana kuwa siku za mateso kuliko siku zote katika maisha yake, hakuwa na uhakika kama angeweza kunusurika katika bahari ile.
Usiku ukaingia, siku hiyo ikaonekana kuwa mbaya kuliko siku zote, bahari ikachafuka. Mawimbi yakaanza kupiga kupita kawaida. Pipa likaanza kupelekwa huku na kule lakini Selemani hakutaka kuliachia japokuwa alikuwa amechoka kupita kawaida.
Kuchafuka kwa bahari ile kuliendelea kwa dakika zaidi ya arobaini na ndipo bahari ile ikaanza kuwa katika hali ya kawaida. Selamani alionekana kuchoka zaidi ya siku nyingine, tumbo lake lilikuwa limeingia ndani, asilimia kubwa ya mwili wake ulikuwa umeota vitu vya kijani kuonyesha kwamba alikuwa amekaa sana ndani ya maji yenye chumvi.
Siku ya tano ikaingia huku Selemani akiendelea kuwa baharini pale. Mwili wake ukakosa nguvu, japokuwa alikuwa ameshikilia kwa kipindi kirefu lakini kwa wakati huo hakuona kama angeweza kushikilia zaidi. Bila kupenda, akaviona vidole vyake vikianza kuliachia pipa lile. Moyoni aliumia, hakuamini kama safari ya kwenda Ulaya ilikuwa ikiishia mahali hapo. Alitamani kuendelea kulishikilia pipa lile, ila vidole havikuweza kuendelea kulishikilia.
“Mungu! Naomba unisamehe kwa kila kibaya nilichokifanya” Selemani alisema huku akiwa amekwishaachia pipa lile na kuanza kuzama ndani ya bahari ile.
*****
Mawasiliano yakaanza kufanyika kupitia kati ya Dokta Patel pamoja na Waziri wa Afya nchini India, Bwana Kumir. Mawasiliano hayo kwa njia ya simu yalikuwa ni kutaka kumuelezea kile ambacho Dokta Mickey kutoka nchini Marekani alikuwa amekizungumza katika kipindi ambacho alikuwa amefika nchini hapo na kuonana na Abuu ambaye alikuwa ametengeneza dawa ya magonjwa ya kansa.
Wazo ambalo walikuwa nalo madaktari wa India kwamba ilikuwa ni lazima waidhulumu dawa ile na kisha kuanza kuitoa wao tayari lilikuwa limefutika katika vichwa vyao, kwa wakati huo walikuwa wakitaka kukaa na Abuu kwani tayari alionekana kuwa tayari kuliletea sifa taifa hilo ambalo lilikuwa likisifika kuwa na madaktari walio mabingwa duniani.
Bwana Kumir akaonekana kushtuka kupita kawaida, tayari alikwishaona kama wasingefanya jambo fulani basi Wamarekani wangeweza kufanya kile ambacho walikuwa wakitaka kukifanya, kumchukua Abuu kinguvu na kisha kumpeleka nchini Marekani, sehemu ambayo angeweza kuliletea sifa taifa hilo.
Alichokifanya Bwana Kumir ni kuanza kuwasiliana na rais wa nchi hiyo, Bwana Ranjit ambaye akataka kuonana nae ili apate kumuelezea kwa kina kile ambacho alikuwa ameongea nae simuni. Bwana Kumir akaanza kuelekea Ikulu ambapo baada ya kufika, moja kwa moja akakaribishwa na kuingia ndani.
“Umesemaje?” Rais, Bwana Ranjit aliuliza huku akionekana kushtuka.
“Kama nilivyokwambia Mheshimiwa. Wamarekani wanaweza kumchukua mtu huyu” Bwana Kumir alimwambia Rais.
“Haiwezekani, labda mimi nisiwe rais” Bwana Ranjit alisema huku akijiapiza kwamba kamwe Abuu asingeweza kuchukuliwa na Wamarekani.
Rais Ranjit hakutaka kusema kwa maneno tu, akaanza kufanya kwa vitendo. Kitu cha kwanza alichokifanya ni kumgawia Abuu nyumba ambayo alitakiwa kuishi humo, akapewa gari la kifahari ambalo lilitakiwa kujazwa mafuta kila baada ya siku mbili, akafunguliwa akaunti ya benki na kisha kuingiziwa kiasi cha dola milioni mbili kama kianzio cha kumfanya kuvutika kwao zaidi.
Hawakuishia hapo, walichokuwa wakikifanya kwa wakati huo ni kuhakikisha kwamba Abuu anabaki kwao. Kitu kingine ambacho kilifanyika ni kumpa ajira katika hospitali ya Taifa ya nchini India, sehemu ambapo angefanya kazi kama Dokta wa kawaida huku akiwa amesaini mkataba utakaomlipa kiasi kikubwa cha fedha, mara mbili ya kile alichokuwa akilipwa Dokta mkuu wa hospitali hiyo, Dokta Patel.
Taarifa za uwezo wa Abuu zikaanza kutangazwa katika vyombo mbalimbali vya habari, nchi ya India ikajitangaza rasmi kwamba mtu wao ambaye alikuwa akisoma katika chuo kilichokuwa nchini kwao alikuwa ameleta neema kwa watu wote waliokuwa wakiishi katika dunia hii mara baada ya kupata dawa ya magonjwa ya kansa.
Kila mtu akashtuka, hawakuamini kama duniani kungekuwa na mtu ambaye angeweza kutengeneza dawa ya aina hiyo. Taarifa zile zikaendelea kutangazwa zaidi na zaidi, kwa wakati huo, kila mtu akataka kumuona mtu huyo, na hata pale ambapo picha yake ilipotolewa, hakukuwa na mtu ambaye aliamini kwamba Abuu angeweza kutengeneza dawa hiyo.
Watu walikuwa wakifikiria kwamba mtu huyo angekuwa mzee na mwenye umri mkubwa lakini alionekana kuwa tofauti kabisa. Alionekana kuwa kijana mdogo ambaye alikuwa na miaka ishirini na moja tu, mtu mweusi ambaye alikuwa na ulemavu wa mguu mmoja.
Serikali ya Tanzania nayo ikaonekana kucharuka hasa mara baada ya kuona kwamba yule mtu ambaye alikuwa ametengeneza dawa ya kansa alikuwa ni Mtanzania ambaye alikuwa amekwenda nchini India kwa ajili ya kusoma tu tena huku akiwa anadhaminiwa na Serikali ya Tanzania.
Watanzania wakamtaka mtu wao arudi katika nchi yake, hawakuwa radhi kuona taifa la India likipata sifa kupitia kwa mtu ambaye wala hakuwa wa taifa hilo. Hapo ndipo maneno mbalimbali yalipoanza kusikika kutoka kwa Watanzania, tayari waliona kwamba nchi ya India ilikuwa ikiendelea kujipatia umaarufu duniani kupitia mtu wao jambo ambalo wala hawakulifurahia.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Rais akaambiwa kwamba ilitakiwa afanye kitu kimoja, kuhakikisha kwamba Abuu analetwa nchini Tanzania. Rais wa Tanzania, Bwana Baraka Kyomo alipoongea na rais wa India na kumuelezea kile kilichotakiwa kufanywa, nchi ya India ikawatoa madaktari kumi ambao walikuwa na uwezo mkubwa ili kuachiwa nafasi ya kuwa na Abuu ambaye kwa wakati huo alionekana kuwa juu zaidi ya madaktari wote.
Hilo halikuonekana kutosha kwa Watanzania, kitu ambacho walikuwa wakikitaka kwa wakati huo ni kumuona Abuu akiletwa nchini tu. Kazi ilionekana kuwa kubwa kwa rais wa Tanzania, kila alipokuwa akiongea na rais wa India, aliulizwa alikuwa akitaka kitu gani zaidi ili awaachie Abuu ambaye tayari dawa zake zilikuwa zimeanza kusambazwa na watu kupona.
“Watanzania hawatonielewa kabisa. Wanachotaka ni kumuona Abuu akirudishwa nchini tu” Rais wa Tanzania, Bwana Baraka Kyomo alimwambia rais wa India, Bwana Ranjit.
“Jambo hilo gumu sana. Acha sisi tumtangaze halafu tutawapeni mtu wenu” Bwana Ranjit alimwambia Bwana Baraka Kyomo.
“Hilo gumu sana pia”
“Wale madaktari kumi hawatoshi tuongeze wengine?”
“Kwa ajili ya Abuu, hata ukiwaleta madaktari wote wa India bado hawatotosha” Bwana Kyomo alimwambia Ranjit.
“Basi tutawajengea hospitali ya kisasa. Unaonaje hapo?”
“Dah!”
“Usijali. Kila kitu kitakuwa safi” Bwana Ranjit alimwambia rais Kyomo.
Kama alivyoongea ndivyo ambavyo ilivyofanyika, baada ya siku tano, ujenzi wa hospitali kubwa ukaanza ndani ya jiji la Dar es salaam. Kutokana na fedha kumwagwa sana, ujenzi wa hospitali ile ukaendelea kwa kasi ya ajabu sana na baada ya miezi mitatu tu, kila kitu kilikuwa tayari.
Bado, hali haikuonekana kuvumilika kabisa, Watanzania hawakuonekana kuelewa, walijua fika kwamba Waindi walikuwa wamefanya vile kwa sababu walikuwa wakitaka kubaki na Abuu ambaye kwao alionekana kuwa na faida kubwa kupita kawaida huku wakiingiza fedha kwa njia ya ujanja ujanja.
Kila walipokuwa wakipiga kelele, Watanzania wakaonekana kutokueleweka jambo ambalo likawafanya watu kujipanga na kutaka kuuchoma moto ubalozi wa India pamoja na hospitali ile ambayo ilikuwa imejengwa na Serikali ya India. Jambo hilo kidogo likaonekana kuleta hofu moyoni mwa rais Kyomo ambaye akaanza kuwasiliana tena na rais Ranjit na kisha kumwambia kile ambacho Watanzania walitaka kukifanya.
Rais Ranjit akaonekana kuhofia, tayari aliona kwamba kulikuwa na matatizo ambayo yangeweza kutokea, hivyo ilikuwa ni lazima ampeleke Abuu nchini Tanzania japokuwa hakutaka jambo hilo litokee kabisa. Alichokifanya ni kuanza kuwasiliana na Waziri wake wa Afya, Bwana Kumar na kisha kumwambia kile ambacho alitakiwa kukifanya, kumsafirisha Abuu kuelekea nchini Tanzania kabla mambo hayajaharibika.
Kwa sababu Abuu alikuwa akiendelea kusoma chuoni, Bwana Kumar akawatuma vijana wake na kisha kuelekea katika chuo hicho kwa ajili ya kumchukua Abuu na kumpeleka katika ofisi yake. Vijana wale wakafika katika chuo kile na kisha kuanza kumuulizia Abuu ambaye alikuwa maarufu sana katika kipindi hicho.
“Mmmh! Aliondoka leo mchana” Mwanachuo mmoja alijibu.
“Kwenda wapi?” Mmoja wa vijana waliotumwa na Bwana Kumir aliuliza.
“Kuna gari la wazungu fulani lilikuja chuoni na kisha kumpandisha, walipoelekea, hatujui” Mwanachuo huyo alijibu.
Maneno yale yakaonekana kuwashtua vijana wale, walichokifanya ni kuwasiliana na Bwana Kumir na kisha kumwambia kile ambacho kilikuwa kimeendelea kule chuoni. Bwana Kumir akaonekana kuchanganyikiwa, kitendo cha kusikia kwamba kulikuwa na wazungu ambao walikuwa wamefika na kumchukua Abuu kilionekana kumfanya kuhisi jambo.
“Wamarekani” Ilisikika sauti ya Bwana Kumir.
Bwana Kumir akazidi kuchanganyikiwa, hapo hapo akaanza kuwasiliana na rais Ranjit na kisha kuanza kumwambia kile ambacho kilikuwa kimeendelea, rais Ranjit akaonekana kuchanganyikiwa zaidi, tayari alijua fika kwamba Wamarekani walikuwa wamewachezea mchezo mchafu. Hapo hapo bila kuchelewa akachukua simu yake na kumpigia rais wa Marekani, Barack Obama na kumwambia kuhusu kile kilichofanyika.
“Hatujafanya kitu kama hicho” Ilisikika sauti ya Obama simuni.
“Una uhakika?”
“Asilimia nyingi tu”
“Sawa. Nimekuelewa. Msako unaanza, tutakayempata nae, tunawaua na miili yao kuichoma moto kama zawadi kwa mungu wetu, Bhuddha” Rais Ranjit alisema kwa hasirira.
“Subiri kwa…..” Obama alisema lakini hata kabla hajamaliza sentensi yake, simu ikakatwa.
Kwa haraka bila kupoteza muda rais Ranjit akaanza kutoa taarifa kwa mkuu wa jeshi la polisi ambaye akaitangazia nchi ya India kwamba kuna watu ambao ni wazungu walikuwa wamefika nchini hapo na kumteka Abuu, hivyo, mipaka ya nchi ilitakiwa kufungwa, uchunguzi ufanyike kwa kila mtu ambaye alikuwa akitaka kusafiri kupitia uwanja wa ndege, kila gari ambalo lilikuwa likitaka kutoka nje ya nchi lilitakiwa kupekuliwa.
Hapo ndipo msako rasmi ulipoanza. Kila mmoja alikuwa akitaka kumuona Abuu akirudi mikononi mwao kwa wakati huo. Ukiachana na hiyo, Watanzania bado walikuwa wakimtaka mtu wao aweze kurudishwa nchini mwao.
“Sikuamini. Sikuamini hata kidogo, huo utakuwa mchezo mchafu mnaotaka kutufanyia” Rais Kyomo alisikika simuni.
“Ndio ukweli. Nilimtuma waziri wa Afya kwenda kumchukua chuo ili tumsafirishe lakini akakuta Wamarekani wamemchukua” Rais Ranjit alimwambia .
“Huo ni mchezo tu. TUNAMTAKA ABUU WETU” Iliskika sauti ya rais Kyomo na kisha kukata simu.
********************************************
***** Je nini kitaendelea?
*****Je ni kweli Wamarekani wamemchukua Abuu? Na Abuu ataweza kupatikana?
***** Je Selemani atakufa baharini?
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
***** ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment