Simulizi : A Day Too Long (Siku Ndefu Mno)
Sehemu Ya Nne (4)
ILIPOISHIA
Kila siku Tandi akawa msichana wa kujifkiria kama alikuwa akitakiwa kumwambia Selemani au la ili kuyaokoa maisha yake, alipoona kwamba hakutakiwa kumwambia, akaachana nalo huku akisubiri kuona ni kitu gani kingetokea, kama Selemani kuuawa au kuendelea kuishi pamoja kwa raha na mahaba moto moto.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Songa nayo sasa….
Kadri muda ulivyozidi kwenda mbele na ndivyo ambavyo Abuu alivyozidi kuogopa ndani ya handaki lile ambalo wala halikuonekana kuwa sehemu salama katika maisha yake, mwili wake ulikuwa ukitetemeka huku kijasho chembamba cha hofu kikiwa kinamtoka mwilini mwake.
Kila alipotaka kuongea kitu, aliuona mdomo wake kuwa mzito kufunguka jambo ambalo lilimfanya kubaki kimya. Macho yake yalikuwa yakiendelea kumwangalia Mansoor ambaye alikuwa kitandani pale amelala. Huku akiwa hajui nini kilitakiwa kufanywa, watu watatu wakaingia ndani ya handaki lile wakiwa na bunduki mikononi mwao na kumuarisha kukaa katika kiti kilichokuwa pembeni yake.
Bado moyo wake haukuwa na amani hata kidogo, alikuwa akiendelea kuogopa mahali pale. Picha halisi ambayo ilikuwa ikionekana mbele yake ilikuwa ikimtia hofu kupita kawaida. Alitamani kuondoka mahali hapo lakini hakujua ni kwa namna gani angeondoka ndani ya handaki hilo ambalo mpaka katika kipindi hicho, kwake lilionekana kuwa kama jehanamu.
Hapo ndipo akaanza kuelezewa juu ya ugonjwa wa kansa ambao ulikuwa ukimsumbua sana Mansoor ambaye alikuwa hoi kitandani pale. Historia ya Mansoor ikaonekana kumgusa sana Abuu lakini mara alipogundua kwamba mtu yule ndiye ambaye alikuwa ameua watu wengi kwa kufanya ugaidi katika nchi mbalimbali, akajiona akianza kumchukia.
Katika maisha yake yote, kitu ugaidi kilikuwa kikimuumiza sana Abuu, hakuupenda ugaidi ambao wengine walikuwa wakiufanya huku wakijisemea kwamba walikuwa wakipongezwa na Mungu kwa kile ambacho kilikuwa kikitokea. Kila siku katika maisha yake alikuwa akimuomba Mungu aweze kuwafunua magaidi wote duniani ambao kazi yao ilikuwa kuua watu kwa malengo yao binafsi huku wakiwashinikiza hata watu wengine kujitoa mhanga kwa kuamini kwamba wangekwenda peponi kwa kile walichokifanya.
Siku hiyo, Abuu alikuwa mbele ya mtu ambaye alikuwa akitafutwa sana na Wamarekani, na si Wamarekani tu bali hata nchi nyingine za Ulaya kwa kila ambacho alikuwa amekifanya pamoja na kundi lake la kigaidi la Bidar. Japokuwa alikuwa na moyo wa huruma kutokana na hali aliyokuwa nayo Mansoor lakini katika kipindi kichache moyo wake ukabadilika na kutengeneza chuki kubwa moyoni mwake.
Alipopewa maelezo juu ya hali ya Mansoor, hapo hapo Abuu akasimama na kisha kuanza kumsogelea kule alipokuwa huku akitembelea gongo lake, alipomfikia, akaanza kumwangalia usoni.
Mansoor alikuwa kimya kitandani huku akipumua kwa tabu sana. Ufinyu wa hewa halisi ndani ya handaki lile ndio ambayo ilionekana kumpa shida kwa wakati huo, alipomfunua shuka na kisha kumwangalia mikononi na usoni mwake, ugonjwa wa kansa ulikuwa umemtafuna kupita kawaida.
Abuu aliumia, katika maisha yake mpaka katika kipindi hicho hakuwahi kumuona mtu ambaye alikuwa ameteseka kitandani kama jinsi alivyokuwa Mansoor mahali pale. Bila kupenda wala kutarajia, machozi yakaanza kumtoka machoni mwake na kutiririka mashavuni mwake. Huo ndio ulikuwa ugonjwa wa kansa, ugonjwa ambao ulikuwa ukiwatesa watu wengi katika kipindi hicho.
Abuu akaanza kuwaagiza watu wale juu ya vitu ambavyo alikuwa akivihitaji kwa ajili ya kutengeneza dawa na kumponya Mansoor ambaye wala hakuonekana kupata nafuu hata siku moja katika siku za usoni. Ndani ya masaa mawili, vitu vyote ambavyo alikuwa akivihitaji vikaletwa mbele yake na kisha kuanza kutengeneza dawa ya ugonjwa wa kansa, dawa ambayo aliamini ingempa afya nzuri Mansoor.
Ndani ya handaki hilo ndipo kulipokuwa maisha yake katika kipindi hicho, Abuu hakutoka kuelekea katika sehemu nyingine zaidi ya kutembea hapa na pale katika mji huo wa Qalat, tena akiwa chini ya ulinzi mkali.
Dawa ambayo alikuwa amemtengenezea Mansoor ilikuwa ni miongoni mwa dawa kali ambayo baada ya wiki moja, mabadiliko yakaanza kuonekana mwilini mwake jambo ambalo likarudisha furaha katika maisha ya watu wake. Mabadiliko yale yalikuwa yakiendelea zaidi na zaidi na mpaka miezi miwili inakatika, Mansoor alikuwa amepata nafuu kwa kiasi kikubwa sana.
Tayari nguvu ya jeshi lao ikaonekana kuanza kurudi tena katika maisha yao, wakajiona kwamba walikuwa wakitakiwa kufanya mambo mengi ya ugaidi katika maisha yao zaidi ya vile ambavyo walikuwa wamefanya katika kipindi cha nyuma. Kwa Abuu, jambo hilo hakutaka litokee, kitu ambacho alikuwa akikitaka ni Mansoor kuachana na mambo ya ugaidi.
“Haiwezekani Abuu” Mansoor alimwambia Abuu mara baada ya kupona.
“Unapata faida gani unapoua watu wengi?” Abuu alimuuliza Mansoor.
“Moyo wangu unafarijika kila ninapowaua wazungu” Mansoor alimwambia Abuu.
“Ila kumbuka kwamba Allah hapendi. Mimi ndiye niliyetengeneza dawa ili upone ila kumbuka si dawa zangu ambazo zimekuponya bali Allah ndiye aliyetaka upone na kisha kumrudia yeye” Abuu alimwambia Mansoor ambaye alionekana kutokuelewa kabisa.
Mipango ikaanza kupangwa kama kawaida, Abuu hakutakiwa kwenda katika nchi yoyote ile, alitakiwa kuishi hapo Afghanistan tu, hapo ndio sehemu ambayo ingekuwa maisha yake jambo ambalo lilimkasirisha sana Abuu kwa kuona kwamba hakuwa akiitendea haki dunia na wagonjwa wote kwa sababu bado alikuwa akihitajika kwa ajili ya utengenezaji wa dawa.
“Nitamuua Mansoor” Abuu alijisemea.
Hayo ndio mawazo ambayo yalikuwa yamemjia katika kipindi hicho, alijua fika kwamba bila Mansoor basi kundi lile la kigaidi la Bidar lisingeweza kufanya kitu chochote kile, aliona kwamba kama angemuua Mansoor basi hata nguvu ya kundi lile lingeweza kupungua kabisa na hivyo kusambaratika na kuachana na ugaidi ambao kwao ulionekana kuwa kama dini kwa jinsi walivyokuwa wakipenda kuufanya.
Abuu alijua kwamba Mansoor alikuwa amepona kabisa lakini kwa kutumia dawa mbalimbali basi angeweza kumuua Mansoor kwani asingekataa kunywa dawa yoyote ambayo angemtengenezea na kumwamuru anywe kwa ajili ya kuilinda afya yake.
Baada ya kupata wazo hilo wala Abuu hakutaka kuchelewa, alichokifanya ni kuanza kutengeneza dawa hiyo. Mipango ya kufanya ugaidi katika jiji la Washington ilikuwa ikiendelea kupangwa lakini kwa Abuu alikuwa akifikiria namna ya kumuua Mansoor katika ugonjwa ambao ulikuwa ni zaidi ya ugonjwa wa kansa.
Abuu aliitengeneza sumu hiyo kwa muda wa wiki nzima na ndipo ilipokamilika. Sumu ambayo alikuwa ameitengeneza ilikuwa na nguvu japokuwa haikuwa na uharaka wa kuua. Kama mtu alikuwa amewekewa sumu ile mwilini mwake, ilikuwa ikimuangamiza taratibu na kumharibu mwili wake kila siku.
“Nitamuua kwa sumu hii ili niweze kuokoa mamilioni ya watu ambao wangekufa kwa ugaidi wake” Abuu alisema huku akiiweka sumu ile katika kichupa kidogo.
Abuu hakutaka kukaa sana na sumu ile, alitaka kukamilisha kila kitu kwa haraka sana jambo ambalo lilimfanya kumuita Mansoor na kisha kumwambia kwamba alitakiwa kuinywa sumu kwa ajili ya kumpa nguvu mwilini mwake na hivyo kuwa na afya njema.
“Ila mbona nimepona” Mansoor alimwambia Abuu.
“Unajiona umepona, ila bado” Abuu alimwambia.
“Kivipi tena? Kwa sasa ninaweza hata kukimbia, kurusha mabomu, kutumia bunduki na hata kupanga mipango ya kuendelea kuwaua wazungu. Tatizo lipo wapi hapo Abuu?” mansoor alisema na kuuliza.
“Wewe unajiona kuwa mzima wa afya, yaani unavyojiona wewe ni sawa na mtu aliyepata ajali mbaya, mwilini mwake kwa nje, hakuonekani majeraha yoyote yale kumbe ndani ya mwili wake, mwili umeumia vibaya” Abuu alimwambia mansoor.
Mansoor hakutaka kubisha tena, alichokifanya ni kunywa sumu ile huku akiambiwa kwamba ilikuwa dawa, sumu ambayo ilitarajiwa kuuharibu mwili wake katika kipindi cha siku chache zijazo mbeleni mwake. Kitendo cha kunywa sumu ile kwa Abuu kilionekana kumfurahisha kupita kawaida kwani aliamini ndani ya miezi mitatu, Mansoor angekuwa marehemu.
Maisha ya pale uarabuni yalionekana kuendelea kumchosha kupita kawaida, hakuyapenda kabisa. Kila siku alikuwa akikosa uhuru huku kadri alivyokuwa akiwafikiria watu masikini ambao walikuwa wakifa kwa sababu ya ugonjwa wa kansa alikuwa akizidi kuumia moyoni mwake. Kila siku alikuwa akitafuta ni kwa namna gani angeweza kutoroka katika mji ule wa Qalat lakini wala hakupata jibu.
“Wamarekani watafika na kuniokoa. Ngoja nifanye kitu” Abuu alijisemea.
Hakutaka kupoteza muda wake, alichokifanya kwa wakati huo ni kuanza kurudi katika handaki. Hakukuwa na mtu ambaye alikuwa akimhofia, walikuwa wakimuamini kupita kawaida kutokana na msaada wake ambao alikuwa amewapa wa kumponyesha kiongozi wake.
Mara baada ya kufika ndani ya handaki lile, moja kwa moja akaanza kukifuata kitanda chake na kisha kulala na kutoa simu yake ambayo alikuwa nayo katika kipindi hicho. Mara kwa mara network ilikuwa ikisumbua sana lakini alipoiona network hiyo kukaa sawa, akafungua sehemu ya meseji na kuandika ujumbe mfupi uliosomeka ‘ABUUBAKARI SELEMANI’ na kisha kujitumia yeye mwenyewe. Kwa jinsi alivyokuwa amefikiria, katika kipindi hicho aliamini kwamba Wamarekani walikuwa wakimtafuta na hivyo kujua ni mahali gani alipkuwa.
****
Wamarekani waliendelea kumsubiria Abuu ambaye katika kipindi hicho walipewa taarifa na wapelelezi wale walikuwa njiani wakielekea nchini Pakistan ambapo huko wangekwenda moja kwa moja mpaka katika kambi ya kijeshi ya Marekani na kisha kuchukua ndege na kuelekea nchini Marekani na kumkabidhisha Abuu katika mikono ya raisi wa Marekani, Obama.
Muda ulikuwa ukizidi kwenda mbele lakini wala hawakupokea simu yoyote kutokwa kwa wapelelezi hao ambao walitakiwa kuwaambia kwamba katika kipindi hicho walikuwa wamefikia wapi.
Nchini India, bado upelelezi wa kumtafuta Abuu ulikuwa ukiendelea kama kawaida. Japokuwa walikuwa wamefunga mipaka yote ya nchi pamoja na kuchunguza katika magari mengi lakini wala hawakuwa wamempata Abuu ambaye walikuwa wakimtafuta kwa udi na uvumba.
Mara ya mwisho kuwasiliana na wapelelezi wale kilikuwa kipindi ambacho walikuwa Pador ambapo waliwaambia kwamba wangekwenda nchini Pakistan kwa kupitia katika njia za panya na hatimae kufika katika nchi hiyo na kuchukua moja ya ndege ambayo ilikuwa katika kambi yao ya kijeshi. Baada ya hapo, hawakupata simu yoyote ile.
Jambo lile likaonekana kuwatia wasiwasi kupita kawaida, walisubiria simu zaidi na zaidi lakini wala hawakupigiwa simu yoyote ile. Jambo lile likaendelea kuwatia mashaka hali ambayo ikawapelekea kuanza kuwapigia. Simu zao zilikuwa zikiendelea kuita kila siku lakini wala hazikupokelewa jambo ambalo likawafanya kuwa na wasiwasi zaidi.
Walichokifanya ni kuingia katika mitambo yao ya kimataifa na kisha kuanza kutafuta mahali ambapo zilikuwepo simu zile. Walipoona kila kitu kipo tayari, wakaanza kupiga simu zile. Simu zilipoanza kuita tu, skrini kubwa ambayo ilikuwa mbele yao ukutani ambayo iliunganishwa na kompyuta ikaleta ramani kubwa ya dunia na kisha kuanza kuzitafuta simu hizo.
Ramani ile ya dunia ikaanza kujizungusha, ilipofika katika bara la Asia, ikasimama na kisha kuanza kujivuta. Ilijivuta zaidi na zaidi mpaka katika nchi ya Pakistan na kisha kuanza kuzunguka zunguka mahali hapo. Hiyo, kwao ilikuwa teknolojia kubwa sana ambayo katika kipindi hicho haikuwa imesambaa katika nchi yoyote zaidi ya Marekani tu.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Mishale kadhaa ikatokea katika skrini ile na hatiame kuanza kugawanyika na kwenda katika kila upande. Wataalamu wa kompyuta ile walikuwa wakiendelea kufuatailia zaidi mpaka pale mshale mmoja uliposimama Pador, sehemu ambayo ilikuwa mpakani mwa Pakistan na India.
Kompyuta ile ikaanza kupiga picha eneo lile, ikatoa umbali ambao ulikuwa ukipatikana kutoka mahali pale kulipokuwa na simu zile mpaka katika kambi ya kijeshi ya Marekani iliyokuwa nchini Pakistan, walipopata kila kitu walichotaka, wakapiga simu na kuwataka baadhi ya wanajeshi waelekee kule kulipokuwa na simu zile huku wakiwatumia zile picha ambazo zilikuwa zimepigwa na namna ya kufika katika sehemu hiyo.
Baada ya masaa manne wakaletewa taarifa ambayo wala haikuwa nzuri kwao iliyosema kwamba wapelelezi wale walikuwa wameuawa katika mpaka wa kuingilia nchini Pakistan tena kwa njia za panya. Ile ikaonekana kuwa taarifa mbaya ambayo ilimhuzunisha kila mtu mahali pale, hata raisi mwenyewe.
“What about Abuubakar? Is he there? (Vipi kuhusu Abuu? Yupo mahali hapo)” Rais Obama aliuliza huku akionekana kuchanganyikiwa.
“He is not here (Hayupo mahali hapa)
“Where is he? (Yupo wapi?)”
“We don’t know (Hatufahamu)” Lilitolewa jibu ambalo lilionekana kumchanganya zaidi rais Obama pamoja na watu ambao alikuwa amekaa nao ndani ya chumba hicho wakifuatilia kila kilichokuwa kikiendelea nchini Pakistan.
Biashara kubwa ya madawa ya kulevya ilikuwa ikiendelea kufanyika nchini Afrika Kusini, vijana wengi ambao walikuwa wakiishi ndani ya nchi hiyo hasa katika sehemu ya Soweto walikuwa wakiathiriwa sana na matumizi ya madawa hayo ambayo yalikuwa yakipigwa marufuku katika nchi nyingi duniani.
Serikali ya Afrika Kusini kila siku ilikuwa ikiendelea kuzuia utumiaji wa madawa hayo ambayo yalikuwa yakiwaharibu sana vijana walioaminika kuwa taifa la kesho lakini hawakuweza kufanikiwa kabisa kuyazuia madawa hayo kutumiwa nchini humo.
Vijana waliendelea kuharibika, watu wakubwa ndio ambao walikuwa wakiyaingiza madawa hayo ndani ya nchi hiyo huku vijana wale ambao walikuwa katika maisha ya tabu wakipewa kuyajaribu au hata kuyasafirisha kuelekea katika nchi nyingine.
Wafanyabiashara wakubwa wa madawa ya kulevya kama Pokwane ndio ambao walikuwa wakifanikiwa sana katika uuzaji wa madawa yale kuliko vijana ambao walikuwa wakiyatumia au kutumia miili yao kusafirisha madawa yale katika nchi mbalimbali.
Pokwane ndiye mfanyabiashara ambaye alikuwa na mafanikio makubwa sana katika kazi yake yote ya uuzaji wa madawa ya kulevya ndani ya nchi ya Afrika Kusini. Kila siku alikuwa mtu wa kuwatuma vijana wenye shida kusafirisha madawa hayo ambayo yalikuwa yakiendelea kupigwa vita duniani.
Biashara ile ikaonekana kumuingizia kiasi kikubwa cha fedha, alinunua magari mengi ya kifahari pamoja na kujenga nyumba nyingi ambazo zilikuwa na hadhi kubwa katika miji mingi ndani ya nchi ya Afrika Kusini kama Pretoria, Johannesburg pamoja na miji mingine.
Kutokana na fedha nyingi ambazo alikuwa nazo, alifanikiwa kuishi maisha ambayo alikuwa akipenda kuishi kwa wakati huo, alibadilisha wasichana kama alivyotaka katika maisha yake. Kila msichana mrembo ambaye alikuwa akipita mbele yake alikuwa akimtamani jambo ambalo liliwafanya watu wote kujua kwamba Pokwane alikuwa mtu wa sketi tu.
Uwezo wa Pokwane wa kulala na wanawake ulikuwa mkubwa sana kiasi ambacho alikuwa akiweza hata kulala na wanawake watatu kwa siku moja tena wote akiwa nao kitandani na kuwaridhisha alivyotaka. Huyo ndiye alikuwa Pokwane, mtu ambaye alikuwa na fedha nyingi ambazo ziliingizwa kutokana na kuuza madawa mengi ya kulevya.
Ingawa kila siku alikuwa akibadilisha wanawake wengi katika maisha yake lakini akatokea msichana mmoja ambaye alionekana kumpenda kwa moyo wa dhati, msichana ambaye alimthamini sana zaidi ya msichana yeyote katika maisha yake, huyu aliitwa Tandi.
Uzuri wa Tandi ulikuwa ukiutetemesha sana moyo wake. Kila alipokuwa akimwangalia Tandi, Pokwane alikuwa akijiona mtu wa tofauti sana katika maisha yake. Moyo wake ulikuwa umetekwa vilivyo na Tandi ambaye wala hakuwa akipenda kuwa na mwanaume mwenye fedha jambo ambalo lilimpa Pokwane wakati mgumu sana mpaka pale alipofanikiwa kuwa na msaichana huyo ambaye alionekana kuwa na urembo mkubwa.
Pokwane akafanikiwa kuwa na Tandi, wivu ukamjaa moyoni mwake. Uzuri wa Tandi ukawafanya wanaume wengi kuanza kummendea lakini wote walijikuta wakitekwa na kupigwa mikwara, kwa wale ambao walijifanya vichwa ngumu, waliuawa. Pokwane hakuwa na masihala, kwake, Tandi alionekana kuwa kama mke wake wa maisha yake, hakuhitaji kumuona mtu yeyote akimuingilia kwa msichana huyo ambaye alikuwa na mvuto mkubwa.
Tandi hakuzipenda fedha za Pokwane, kitu ambacho alikijali kutoka kwa mwanaume huyo ni mapenzi ya dhati tu. Kila alipokuwa akinunuliwa magari ya kifahari, Tandi alikuwa akiyakataa, kila alipokuwa akitaka kujengewa nyumba ya kifahari hasa katika jiji la Pretoria, Tandi alikuwa akikataa. Kila siku katika maisha yake alikuwa akipenda kukaa katika moja ya maghorofa ya serikali ambayo yaliwawezesha wananchi kupanga tu.
Kila msichana alionekana kumshangaa Tandi kutokana na uamuzi ambao alikuwa amejiwekewa, wengi walimuona kuwa na bahati ambayo alikuwa akiichezea lakini kwa Tandi wala hakuonekana kujali. Mpaka anakutana na Selemani, moyo wake ukawa radhi kumpenda mwanaume huyo na kuamua kuwa nae, tena mbaya zaidi, kuishi pamoja nae ndani ya chumba chake bila kujali kama Pokwane angejua au la.
Tandi hakutaka kumwambia Selemani kuhusiana na Pokwane kwa kuamini kwamba kama angemwambia basi Selamani angeogopa na hivyo kumkosa katika maisha yake jambo ambalo hakutaka litokee kabisa. Kila siku Selemani alikuwa mtu wa kumpa mapenzi moto moto Tandi, mapenzi halisi ya Mtanzania yalikuwa yakifanyika kwa msichana huyo jambo ambalo likamchanganya na kujiona kama malkia katika dunia hii.
Hapo ndipo Tandi alipogundua sababu ya wanawake wa Afrika Kusini kutamani kuwa na wanaume kutoka nchini Tanzania. Kila siku alikuwa akipikiwa chakula jambo ambalo lilikuwa gumu kufanywa na mwanaume wa Afrika Kusini, kila siku alikuwa akiandikiwa kitanda na hata kufuliwa nguo jambo ambalo wala halikuwezekana kufanywa na mwanaume wa Afrika Kusini.
Mapenzi ya Selemani yalikuwa yamemteka sana Tandi kiasi ambacho yakamfanya kujiona kuwa mwanamke mwenye bahati kuliko wanawake wote nchini Afika Kusini. Kila siku Tandi alikuwa karibu na Selemani, hakutaka kumwacha huru kwa kuhofia kuchukuliwa na wanawake wengine wa Afrika kusini.
“Mtoto vipi?” Nyerere alimuuliza Selemani.
“Mambo safi”
“Unafanya kama nilivyokwambia?”
“Tena zaidi ya hivyo. Si unajua mimi mtoto wa Kitanga kutoka barabara ya 13” Selemani alijibu.
“Hahaha! Ila kuna kijiskendo nimekisikia”
“Kijiskendo kipi tena?”
“Huyu demu ana bahasha wake”
“Yupi?”
“Jamaa fulani anauza madawa. Ila kwa sasa hayupo. Yupo Zimbabweeee”
“Sasa wewe unaogopa?”
“Hapana. Siogopi ila yakupasa kuwa makini tu si unajua huku tumekuja kutafuta tu” Nyerere alimwambia Selemani.
“Hilo usitie shaka mkuu. Ila kuna kitu natakiwa kukifanya” Selemani alimwambia Nyerere.
“Kitu gani?”
“Nimchune. Bwana wake si muuza madawa, nadhani atakuwa na fedha. Acha nimchune, au wewe unaonaje?”
“Hilo nalo neno. Tengeneza kibubu kwa ajili ya kuhifadhia mkwanja”
“Haina noma baba wa Taifa” Selemani alisema na kisha wote kuanza kucheka.
Huo ndio uamuzi ambao ulionekana kufaa kwa wakati huo, kumchuna Tandi ndicho kitu ambacho kilitakiwa kufanyika kwa wakati huo. Muda wa miezi minne ambayo walikuwa wameishi pamoja ulitosha kabisa kumfanya Tandi kumuamini Selemani.
Hapo ndipo Selemani alipoanza mishemishe zake za kutaka kumchuna Tandi kwani aliamini kwamba mpenzi wake ambaye alikuwa nae, Pokwane alikuwa na fedha nyingi na za kutosha kutokana na biashara ya madawa ya kulevya ambayo alikuwa akiifanya.
Selemani akaanza kuelezea matatizo mbalimbali ambayo yote kwa pamoja yakawa yakieleweka kwa Tandi ambaye alikuwa akimghawia kiasi cha fedha ambacho alikuwa akikitaka. Selemani hakuwa na uhuru wa kupeleka fedha benki kutokana na kuendelea kuishi nchini hapo kimakosa.
Selemani aliendelea kujikusanyia fedha na baada ya miezi sita, akapata tetesi kwamba Pokwane alikuwa akitarajia kurudi nchini Afrika Kusini ndani ya wiki moja. Hiyo ikaonekana kuwa taarifa mbaya kwa Selemani kwa kuona sasa kilikuwa kipindi chake cha kuuawa kwa kile alichokifanya cha kumchukua Tandi.
Tandi hakutaka kuongea kitu chochote kile, hakutaka kumwambia Selemani kuhusiana na Pokwane, hakujua kwamba mwanaume huyo alikuwa akifahamu kila kitu kilichokuwa kikiendelea. Muda mwingi Tandi hakuonekana kuwa na raha, alijua fika hasira ambazo alikuwa nazo Pokwane katika kipindi ambacho alikuwa akimuona mwanaume mwingine akitembea na mpenzi wake.
Siku ambayo Pokwane alikuwa amefika Afrika Kusini, Tandi hakuonekana kuwa na raha kabisa kwani alijua kwamba ni lazima mwanaume huyo angefika katika vyumba hivyo na kama angefanikiwa kumuona Selemani basi lingekuwa tatizo kubwa.
Saa mbili kamili usiku, mlango wa sebuleni kwake ulikuwa ukigongwa. Huku Tandi akiwa amesimama na kuelekea kuufungua, Selemani akatoka sebuleni pale huku akiwa na taulo na kisha kuelekea katika mlango wa nyuma kuelekea bafuni kuoga.
Tandi akaanza kuufuata mlango ule, alipoufikia akaanza kuchungulia katika kitundu ambacho kilikuwa katika mlango ule, jicho lake likatua usoni mwa kijana mmoja jirani aliyekuwa akiishi katika chumba cha pili. Alipoufungua tu mlango, macho yake yakatua usoni mwa Pokwane ambaye alikuwa na vijana wake waliokuwa wameshika bunduki.
Hata kabla hajaongea kitu chochote kile, Tandi akaamrishwa kuingia ndani na kufanya hivyo huku akitetemeka. Uso wa Pokwane ulionekna kuwa na tabasamu kana kwamba hakukuwa na jambo lolote baya ambalo lilikuwa linataka kutokea mahali hapo. Akamkalisha Tandi kochini na kuanza kumwangalia.
“Unaishi na nani mahali hapa?” Lilikuwa swali moja gumu lililotoka mdomoni mwa Pokwane.
“Peke yangu mpenzi” Tandi alijibu huku akionekana kutetemeka.
“Mbona unajibu huku ukitetemeka sana mpenzi?” Pokwane aliuliza.
“Bunduki. Bunduki zinaniogopesha. Sijawahi kukuona ukija na watu wenye bunduki” Tandi alijibu.
“Usiogope mpenzi” Pokwane alisema huku akiwaambia vijana wake waanze kumtafuta mtu huyo kwa amri moja tu, watakapomuona, basi wamuue.
Vijana wale wakaelekea chumbani na kisha kuanza kumtafuta, walisogeza kitanda huku na huko, wakafungua kabati la nguo na kuendelea kumtafuta mtu ambaye walijua kwamba alikuwa ndani ya chumba hicho lakini wala hawakuona mtu.
“Hakuna mtu” Kijana mmoja alimwambia Pokwane.
“Mmeangalia vizuri?”
“Ndio bo….” Kijana mmoja alijibu lakini hata kabla hajamalizia mara maji yakaanza kusikika kutoka bafuni.
Pokwane akayapeleka macho yake usoni mwa Tandi, uso wake ukawa umekunja ndita kali. Tandi bado alikuwa akitetemeka huku akiwa ameinamisha uso wake chini, aliogopa kumwangalia Pokwane usoni.
“Huyo nani bafuni?” Pokwane aliuliza.
“Hakuna mtu”
“Mbona bomba limeanza kutoa maji?” Pokwane aliuliza.
“Maji yalikuwa yamekatika, sasa ndio yamerudi”
“Una uhakika?”
“Ndio” Tandi alijibu.
Pokwane hakutaka kuridhika, alichokifanya ni kuwaagiza vijana wake waelekee huko bafuni ambapo maji yalisikika yakitoka. Vijana wale wakaanza kushikiria bunduki zao vilivyo na kisha kuelekea kule kulipokuwa na mlango wa nyuma na kuelekea bafuni. Kila mmoja alikuwa akikumbuka amri ambayo walikuwa wamepewa na Pokwane, wamuue yule ambaye wangemkuta ndani ya bafu lile.
****
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Wamarekani bado walionekana kuchanganyikiwa kupita kawaida, hawakujua ni mahali gani ambapo Abuu alikuwa amepelekwa kwa wakati huo. Mbwembwe zao zote za kutaka kuwa na Abuu zikaonekana kuwatokea puani kwa wakati huo, hawakujua ni kwa namna gani watu hao walijua kwamba walikuwa wamemchukua Abuu.
Hawakuwa na jinsi katika kipindi hicho, walichokifanya ni kuanza kupeleleza juu ya mahali ambapo alikuwepo Abuu katika nchi ya Pakistan pamoja na Afghanistan kwani walijua kwamba Abuu asingeweza kuchukuliwa na Waindi bila wao kufahamu.
Upelelezi wa Wamarekani ukaanza, kitu ambacho walikuwa wakikifanya kwa wakati huo si kupeleleza kuelekea katika nchi hizo, bali walikuwa wakipeleleza kwa kutumia kompyuta zao. Kitu ambacho walikuwa wakikitaka kwa wakati huo ni kitendo cha Abuu kutumia simu tu hali ambayo ingewapelekea kufahamu signal ya simu hiyo mahali ilipokuwa huku namba ya Abuu wakiwa nayo mikononi mwao.
Jambo hili halikuonekana kuwa jepesi kutokea, kila siku signal hazikusoma simu ya Abuu jambo ambalo liliwachukua ugumu sana kufahamu mahali ambapo Abuu alikuwepo kwa kipindi hicho. Mwezi wa kwanza ukakatika, mwezi wa pili ukaingia na hatimae mwezi wa tatu kuingia lakini hakukuwa na dalili zozote zile.
Bado Wamarekani walikuwa wakiumiza vichwa vyao kwa wakati huo, hawakujua ni kitu gani ambacho walitakiwa kukifanya, hawakujua ni kwa jinsi gani wangeweza kumtafuta Abuu na kisha kumpeleka katika nchi hiyo kwa ajili ya kufanya kile ambacho walikuwa wakitaka kukifanya.
Hapo ndipo ambapo Serikali ya Marekani ikawasiliana na India pamoja na Tanzania na kuwaambia kile ambacho kilikuwa kinaendelea kwa wakati huo. Serikali ya India ikajitoa hasa mara baada ya kusikika kwamba hata na wao walikuwa wakihitajika kuunganisha nguvu katika kumtafuta Abuu.
Serikali ya Tanzania ikaonekana kuchanganyikiwa, taarifa kwamba Abuu alikuwa ametekwa na watu wasiojulikana lilionekana kuwachanganya kupita kawaida. Taarifa zile zikavuja na hatimae waandishi wa habari kuzitoa katika vyombo mbalimbali vya habari. Kila Mtanzania akaonekana kuchanganyikiwa, mtu ambaye alikuwa amefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuwatibia watu kutokana na dawa zake za kansa alikuwa ametekwa na watu wasiojulikana.
“Tutamtafuta mpaka tumpate” Waziri wa Mambo ya ndani na Nje, Bwana Theo alimwambia rais wa Tanzania, Bwana Baraka Kyomo.
“Tutashukuru sana”
“Ila tukimpata mtatupa zawadi gani?” Bwana Theo aliuliza.
“Tutalizungumzia hilo baada ya kupatikana”
“Hapana. Tukubaliane kwanza kabla ya kupatikana”
“Nyie mnataka nini?”
“Tunataka kuwa nae japo kwa mwaka mmoja. Mtakubali?”
“Hakuna tatizo”
“Basi kama hakuna tatizo. Ngoja tuingie kazini” Bwana Theo alimwambia Bwana Kyomo.
Bado Wamarekani walikuwa wakiendelea na kazi yao kama kawaida, kila siku walikuwa wakiendelea kucheza na kompyuta zao kwa ajili ya kuangalia signal ya simu ya Baraka ingepatikana sehemu gani. Katika siku ambayo hawakuwa wakiitegemea, wakafanikiwa kuipata signal hiyo, signal ya simu ya Abuu ambayo ilikuwa imetuma meseji.
Kwa haraka haraka wakaanza kuifuatilia signal hiyo, mishale kadhaa ikaonekana katika kompyuta yao ikizunguka ramani kubwa ya dunia ambayo ilikuwa katika skrini yao mpaka pale ambapo signal ikasimama katika nchi ya Afghanistan ndani ya mji wa Qalat, sehemu ambayo kulisadikiwa kuwa na makazi ya kundi la kigaidi la Badir.
“Tumeipata. Ni lazima tuelekee huko”
Mawasiliano yakaanza kufanyika kwa haraka haraka, kwa sababu lilikuwa taifa lenye nguvu sana, hata walipotaka kuingia nchini Afghanistan kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa mabomu ya nyuklia, hakukuwa na mtu yeyote ambaye alikataa. Kwa kutumia mgongo wa Umoja wa Mataifa, wanajeshi zaidi ya mia mbili wakaingia katika nchi ya Afghanistan kwa kisingizio cha kuangalia uwezekano wa utengenezaji wa mabomu ya nyuklia kumbe akilini mwao walikuwa na kitu kingine, kumtafuta Abuu katika mji wa Qalat uliokuwa mashariki mwa nchi ya Afghanistan.
Saa kumi jioni, majeshi hayo ya Kimarekani yakaingia katika mji huo, kundi la kigaidi la Badir halikuonekana kukubali, kwa kutumia bunduki ambazo walikuwa nazo, mapigano yakaanza mahali hapo kupigana na wanajeshi wa Marekani, mapigano ambayo yalionekana kuwa makali.
“Hakuna kurudi nyuma mpaka Abuu apatikane” Hiyo ilikuwa kauli ambayo ilitolewa na rais wa Marekani, Obama akiwaambia wanajeshi ambao bado walikuwa wakiendelea kupigana na wanajeshi wa kundi la kigaidi la Badir katika mji huo wa Qalat ambao ulikuwa na milima mingi, ikiwepo milima ya Torabola.
Kila mmoja alikuwa na uhakika kwamba bafuni mule kulikuwa na mtu na hivyo kuziandaa vyema bunduki zao kwa kuona kwamba muda wowote ule walitakiwa kumuua mtu huyo ambaye alikuwa ndani ya bafu lile. Maji bado yalikuwa yakiendelea kusikika yakimwagika katika bomba la mvua hali iliyowafanya wote kujua kwamba kulikuwa na mtu ambaye alikuwa akioga.
Walipoufikia mlango wa kuingia bafuni, wakaufungua na kuingia ndani huku bunduki zao zikiwa mbele. Bafuni hakukuwa na mtu yeyote yule, maji yalikuwa yakimwagika tu jambo ambalo lilionekana kuwashangaza wote mahali pale. Hawakuonekana kuridhika kabisa, wakaanza kuangalia huku na kule, wakafungua hata mlango wa chooni lakini hakukuwa na mtu yeyote yule kitu kilichowafanya kurudi chumbani pale.
“Vipi?” Pokwane aliwauliza.
“Hakuna mtu”
“Mmeangalia vizuri?”
“Ndio bosi. Hakuna mtu” Kijana mmoja alijibu.
Pokwane akasimama na kuanza kumsogelea Tandi na kisha kumshika mkono. Bado Tandi alikuwa akitetemeka tu, uso wake ulionekana kuwa na hofu kubwa kupita kawaida. Pokwane akashusha pumzi ndefu na nzito, akaingiza mkono mfukoni na kutoa pete moja ya almasi ambayo ilikuwa kwenye kiboksi chake na kisha kukifungua.
“Nakupenda sana Tandi” Pokwane alimwambia Tandi kwa sauti ya chini.
“Sitaki mpenzi. Unaonekana kutokuniamini kabisa, unafikiri kwamba ninaweza kukusaliti. Hauniamini kabisa, sioni sababu ya kuendelea kuwa na mtu asiyeniamini” Tandi alisema huku akianza kutokwa na machozi.
“Samahani mpenzi. Kuna wapumbavu walinijaza maneno mengi, nadhani hawapendi kuuona uhusiano wetu ukishamiri na kukua kila siku. Nakuahidi kutokuwasikiliza tena” Pokwane alimwambia Tandi na kisha kuitoa pete ile na kumvarisha.
“Ninataka kukuoa. Hii ni alama ya uchumba wangu kwako. Nataka ikiwezekana hata miezi sita ijayo nikuoe. Upo tayari?” Pokwane alimwambia tandi na kisha kumuuliza.
“Nipo tayari”
“Asante sana mpenzi. Nakupenda sana” Pokwane alimwambia Tandi na kisha kuanza kubadilishana mate.
Pokwane alionekana kuwa mwenye furaha kwa wakati huo, maneno ambayo alikuwa ameambiwa kwamba mpenzi wake, Tandi alikuwa akiishi na mwanaume aliamua kuyapuuzia kwa kuwaona watu hao kutokuupenda uhusiano ambao alikuwa nao pamoja na Tandi na hivyo kutaka wawili hao waachane.
Moyo wake ukazidi kumpenda zaidi Tandi kwa kuona kwamba msichana yule alikuwa mwaminifu na wala hakuwa kama vile watu walivyokuwa wakisema juu yake. Siku hiyo, Pokwane hakulala mahali hapo, kutokana na kazi nyingi ambazo alitakiwa kuzifanya hasa mara baada ya kurudi kutoka Zimbabwe, akaondoka huku akiahidi kurudi mahali hapo mara kwa mara.
Tandi akabaki ndani peke yake, hakuamini kama kweli watu wale walikuwa wameshindwa kumuona Selemani ambaye alikuwa ameelekea ndani ya bafu lile. Tandi hakuonekana kuamini, akasimama na kisha kuanza kuelekea bafuni kule na kuanza kuangalia kwa macho yake, ukweli ulibaki pale pale kwamba Selemani hakuwepo ndani ya bafu lile.
Tandi akaonekana kushangaa, hakujua mahali ambapo Selemani alipokuwa amepitia. Akaliangalia dirisha dogo lililokuwa bafuni mule, lilikuwa limefungwa kama linavyofungwa kila siku. Akilini mwake, Tandi alionekana kuchanganyikiwa, kila alichokuwa akijiuliza mahali hapo, alikosa jibu kabisa.
Baada ya dakika ishirini akasikia mlango wa chumba chake ukigongwa, alipokwenda kuufungua, alikuwa Selemani huku akiwa amevaa taulo. Kabla ya kuongea kitu chochote kile, wakabaki wakicheka huku Tandi akionekana kushangaa kupita kawaida.
“Mimi ni Mtanzania. Kila siku nitaendelea kuwa mjanja” Selemani alimwambia Tandi.
“Tell me what happened? (Niambie kilitokea nini?)” Tandi aliuliza.
“I am Tanzanian man….so mjanja my beautiful. I jump the window there, waliporeach there, sikuonekana…..dissapear like upepo….vuuuuuu” Selemani alijibu huku akionekana kutokuifahamu vizuri lugha ya Kingereza.
Japokuwa Selemani hakuwa akiifahamu vizuri lugha ya Kingereza lakini kila siku walikuwa wakielewana huku nae akiendelea kujifunza lugha hiyo ambayo kwake ilionekana kuwa lugha ngumu. Siku hiyo, kama kawaida walipeana mapenzi moto moto huku Selemani akitumia ufundi wake wa hali ya juu kuhakikisha kwamba anamdatisha Tandi.
*****
Selemani alikuwa amekaa chumbani huku akionekana kuchoka kupita kawaida, muda mwingi alikuwa akikifikiria kiasi ambacho alikuwa amekihifadhi kwenye kibubu chake ambacho kwa kukisia tu, kilikuwa kimefika randi elfu themanini. Hadi kufikia hatua hiyo, hakutaka kuridhika, alikuwa akitamani kuendelea kuchukua fedha za tandi kadri alivyoweza.
Huku akiwa katika lindi la mawazo, akaanza kusikia joto ambalo likamfanya kuinuka, akachukua taulo kwa ajili ya kwenda bafuni kuoga. Hata kabla hajatoka chumbani, akasikia mluzi ukipigwa. Alijua fika kwamba mluzi ule ulikuwa ni wa Nyerere ambaye mara kwa mara alikuwa akimshtua kama alikuwa akitaka kwenda sehemu pamoja nae. Siku hiyo hakuelewa kwa sababu gani Nyerere alikuwa amempigia mluzi usiku, alichokifanya ni kufungua dirisha.
“Ondoka chumbani. Washikaji wanakuja yule jamaa wa kwa Mugabe. Atakuua” Nyerere ambaye alikuwa akiishi katika ghorofa ya chini alimwambia Selemani. Selemani hakutaka kubaki ndani ya chumba kile, hapo akajua kwamba kulikuwa na hatari ambayo ingeweza kumkuta.
Alichokifanya ni kutoka chumbani, alipokutana na Tandi katika kile chumba ambacho kilikuwa kama sebuleni kwao, hakujiwekea wasiwasi wowote ule, alichokifanya ni kuelekea bafuni huku akiisikia mtu akigonga mlango, moja kwa moja alijua kwamba ni huyo jamaa.
Selemani akaingia bafuni, hakujua afanye nini, aliangalia huku na kule lakini hakuiona njia ya kutokea ndani ya bafu lile. Macho yake yalipotua katika kidirisha cha kioo ambacho kilikuwa kwa juu kidogo saizi ya kichwa chake, akaanza kukifungua, alipoona kimefunguka, akapitisha kichwa chake, kulikuwa na bomba kubwa la choo ambalo lilikuwa likielekea chini.
Selemani hakutaka kuchelewa, alichokifanya tena kwa haraka sana, akaufunga mlango, akalifungua bomba la mvua ili atakapoanza kutoka kupitia kioo kile asisikike. Alipoona kila kitu kipo sawa, akaanza kutoka bafuni pale kupitia kidirisha kile ambapo alipojiona yupo nje, akakifunga na kisha kuliparamia bomba la choo ambalo akaanza kushuka nalo mpaka katika dirisha la chumba cha Nyerere na kisha kuanza kugonga na kufunguliwa.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/-
“Vipi?” Nyerere aliuliza.
“Amekuja bwana. Nimesikia akigonga hodi” Selemani alimwambia Nyerere.
“Kwa hiyo hajakuona?”
“Hajaniona. Si unajua mimi ninja” Selemani alimwambia Nyerere.
“Safi sana. Unapokuwa Mtanzania lazima uwe mjanja kuliko waafrika wengine” Nyerere alimwambia Selemani.
“Ila wewe ulijuaje kama jamaa alikuwa akifika hapa?”
“Beatrice aliniambia. Alinipigia simu jamaa walipokuwa wakiteremka garini mwao. Nikaona bora nikushtue” Nyerere alimwambia Selemani.
“Dah! Asante sana aisee. Mbona kungechimbika leo” Selemani alimwambia Nyerere.
Siku hiyo Selemani alikuwa amejiona mjanja kuliko mtu yeyote, msaada ambao Nyerere alikuwa amempa juu ya kumwambia kwamba Pokwane alikuwa akija katika vyumba alivyokuwa akiishi Tandi ulikuwa umemsaidia kupita kawaida.
*****
Dawa ambazo alikuwa amepewa na watu wa kundi la kiroho la WEST AFRICA CHRIST AMBASSADOR ambazo zilikuwa zikimsaidia katika kuikausha kiu ya kutamani kuvuta sigara zilikuwa zimekwishamuishia, katika kipindi hicho, dawa hizo hakuwa nazo tena.
Hapo ndipo tatizo lilipoanza kujirudia tena. Selemani akaanza kushikwa na kiu kali hata zaidi ya mara ya kwanza ya kutamani kuvuta sigara katika maisha yake. Kila wakati alikuwa na sigara mdomoni mwake, uvutaji sigara ukaonekana kumrudia kwa mara nyingine, tena kwa kasi kuliko hata ilivyokuwa kabla.
Uvutaji wake wa sigara ukaonekana kuongezeka zaidi na zaidi, kila siku alikuwa mtu wa kushinda akivuta sigara tu. Selemani hakuweza kubadilika, alikuwa akizidi kuvuta sigara sana kiasi ambacho hata ule ugonjwa wake wa kukohoa mara kwa mara kumrudia tena.
Lile likaonekana kuwa tatizo sana kwake, Tandi akaanza kuangaika huku na kule kwa ajili ya kumtafutia dawa katika hospitali mbalimbali lakini Selemani bado hakupata nafuu hata kidogo. Kwa Tandi, akaonekana kuchanganyikiwa kupita kawaida jambo ambalo lilimfanya kumtaka Pokwane amgawie kiasi kikubwa cha fedha, zaidi ya randi milioni moja.
Kwa Pokwane hilo wala halikuwa tatizo, kwanza alifurahia kuombwa fedha na mpenzi wake huyo. Alichokifanya Pokwane ni kumgawia Tandi kiasi cha randi milioni tatu ili hata pale ambapo angekuwa na tatizo jingine basi aweze kutumia kiasi hicho kingine.
Kiasi ambacho Tandi alikuwa amekiomba akaanza kumuangaikia Selemani katika kumtafutia dawa katika maduka mbalimbali. Kwa Selemani wala hakukuonekana kuwa na nafuu, kila dawa ambayo alikuwa akipewa, haikuwa ikimsaidia kabisa.
Nchini Afrika kusini kulikuwa na hospitali nyingi ambazo Selemani angeweza kupelekwa na kisha kutibiwa ugonjwa wake mpaka kupona kabisa lakini jambo hilo lisingeweza kutokea kutokana na kuishi nchi hapo bila kibali maalumu, hivyo alitakiwa kusubiri nyumbani tu.
Siku nazo ziliendelea kukatika, miezi ikaendelea kukatika mpaka kufikia miezi ile ambayo Tandi alitakiwa kufunga ndoa na Pokwane. Tangazo la ndoa hiyo lilikuwa limetangazwa katika vyombo mbalimbali vya habari. Watu wengi wakaahidi kuhudhuria harusi hiyo ambayo ilikuwa ikijulikana sana kutokana na Pokwane kuwa tajiri mkubwa sana nchini Afrika Kusini.
Taarifa hiyo ikaonekana kuwa kama mwiba mkali kwa Selemani, hakutaka kumuacha Tandi aolewe na Pokwane, kwake yeye, alikuwa tayari kufanya kitu chochote kile, hata kama kufa, acha afe lakini mwisho wa siku, Tandi asiolewe na Pokwane, aendelee kuwa nae mpaka kifo kitakapowatenganisha.
********************************************
Mapigano ndani ya mji wa Qalat bado yalikuwa yakiendelea. Waarabu waliokuwa katika kundi la kigaidi la Badir bado walionekana kutokukubali kushindwa, walikuwa wakipigana vilivyo na jeshi la kimarekani ambalo lilikuwa limevamia katika mji huo kwa kisingizio cha kukamata mabomu ya nyuklia kumbe lengo lao hasa lilikuwa ni kumchukua Abuu na kuondoka nae kuelekea nchini Marekani.
Risasi zilikuwa zikisikika katika kila kona, mabomu yalikuwa yakipigwa katika sehemu ambazo zilikuwa makazi ya watu wa kundi hilo la kigaidi. Hali ikaonekana kutokuwa na amani hata mara moja, Wamarekani wakaonekana kuzidiwa nguvu jambo ambalo liliwafanya kuanza kuomba msaada zaidi.
Dakika zilikuwa zikizidi kwenda mbele, wanajeshi zaidi ya mia mbili ambao walikuwa wamekusanyika katika mji huo walikuwa wamepigwa mpaka kufikia wanajeshi hamsini na mbili tu. Hapo ndipo mawasiliano yalipofanyika na ndege nne za kijeshi kufika katika mji huo wa Qalat.
Ndege hizo ndizo ambazo zilikuwa zimemaliza mapigano yote. Mabomu yenye nguvu yakaanza kupigwa, risasi kali zikaanza kurushwa jambo ambalo liliwafanya waarabu kuanza kukimbilia kwenye milima ya Torabola. Hilo halikuweza kuwasimamisha Wamarekani kurudi nyuma, waliwafuata huko huko na kuzidi kuwashambulia.
Walipoona kwamba Waarabu wale walikuwa wamejificha katika mapango ambayo yalikuwepo ndani ya milima hiyo, hapo ndipo mabomu makubwa ya B52, 1Twelve45 yakaanza kurushwa katika milima hiyo ambayo ikaanza kusambaratika. Hiyo ndio ilikuwa vita kubwa ambavyo vilitokea katika ardhi ya nchi za Kiarabu, vita ambavyo vilichukua zaidi ya saa kumi mpaka kumalizika.
Sehemu ambayo kulikuwa na milima ya Torabola kukabadilika na kuwa sehemu tambarare kiasi ambacho kama mtu angeambiwa kwamba sehemu ile kulikuwa na milima mikubwa basi mtu huyo asingeweza kukubali hata mara moja. Vita vikaisha, Wamarekani wakaonekana kushinda lakini mpaka muda huo, mtu ambaye aliwafanya kuanzisha vita hivyo, Abuu hakuwa amepatikana.
Walichokifanya ni kuanza kuelekea katika maandaki ambayo Mansoor alikuwa akiyatumia kujificha na kisha kuanza kuangalia huku wakitoa vifusi ili kuona kama wangeweza kumuona Abuu. Magari makubwa ya kutoa vifusi yakafika sehemu hiyo na kisha kuanza kutoa vifusi vile. Kazi ya utoaji wa vifusi iliendelea kwa takribani masaa sita na ndipo walipoanza kuiona miili ya watu.
Miongoni mwa miili ile ambayo walifanikiwa kuiona baada ya kutoa vifu vile ulikuwa mwili wa Mansoor ambao ulikuwa ukionekana kupigwa na risasi ubavuni pamoja na vijana wake ambao wote miili yao ilikuwa imetobolewa kwa risasi. Wamarekani wakaonekana kufurahi, kitendo cha kuuona mwili wa Mansoor kuwa miongoni mwa miili ya watu ambao walikuwa wamepigwa na risasi walionekana kuridhika, walichokifanya ni kuendelea kufukua vifusi vile.
Ilipofika saa kumi alfajiri ndio muda ambao wakakutana na mwili wa Abuu ukiwa umefunikwa na mbao, ilionekana kwamba wakati mabomu yanapiga andaki lile, alikuwa amejificha chini ya meza, na hata kifusi kilivyoangaka, meza ilikuwa juu yake na hivyo kumwachia nafasi ya kupumbua kwani uso wake ulikuwa umefunikwa na mbao huku mwili ukiwa umefukiwa na mchanga.
Uso wote wa Abuu ulikuwa na vumbi jingi, Wamarekani wakamchukua na kisha kumtoa, wakasikiliza mapigo ya moyo wake, alikuwa akihema japokuwa ilikuwa ni kwa mbali sana, Wakamchukua na kisha kumpakiza ndani ya gari lao na kuanza kuondoka kuelekea katika sehemu ambazo zilikuwa na ndege zao za kivita.
Abuu akapakizwa ndani ya ndege moja ambayo ikapaa na kuelekea katika kambi yao ya kijeshi iliyokuwa Pakistan kwa ajili ya kumhudumia kwa matatizo yote ambayo alikuwa amekutana nayo. Kutokana na umbali kutoka Afghanistan na Pakistan kutokuwa mbali sana na ndege kuwa za mwendo wa kasi, walitumia muda mdogo kwa ndege hiyo na kuingia ndani ya kambi hiyo ya kijeshi ya jeshi lao.
“He will be just fine (Atakuwa salama)” Daktari mmoja ambaye alikuwa katika hospitali ndogo ya kijeshi aliwaambia wanajeshi ambao walikuwa wamemleta Abuu huku akimfunga dripu na kumuwekea mashine ya hewa safi puani mwake.
Mpaka kufikika hatua hiyo, hali ikaonekana kuwa nzuri, yule mtu ambaye Wamarekani walikuwa wakimtaka katika kipindi hicho wakawa wamekwishampata. Abuu alikaa katika hospitali ile kwa takribani siku mbili na ndipo alipopata nafuu na kuanza kuzungumza tena.
Simu zikapigwa nchini Marekani kwamba Abuu alikuwa salama na hivyo kutakiwa kusafirishwa mpaka nchini Marekani. Hiyo ikaonekana kuwa furaha kwa Abuu, safari ambayo ilikuwa imesitishwa miezi kadhaa iliyopita sasa ilikuwa ikiendelea kuelekea katika nchi ambayo alikuwa akitamani sana siku moja kuingia na kufanya kazi zake kama kujitangaza.
Wamarekani walikuwa na presha kubwa, hawakuamini kama kweli katika kipindi hicho yule mtaalamu wa magonjwa ya kansa alikuwa akiletwa ndani ya nchi yao, wakaandaa sherehe kubwa ya kumkaribisha ndani ya nchi yao. Katika siku ambayo Abuu alikuwa akitua katika uwanja wa ndege kwa kutumia ndege ya rais wa Marekani ya Air Force One ambayo ilikuwa imepelekwa nchini Pakistan kwa ajili yake tu, rais Obama pamoja na Waziri wa mambo ya Ndani na Nje, Bwana Theo walikuwepo uwanjani hapo wakimsubiria.
Abuu akaonekana kuwa mtu maalumu ambaye alikuwa ameletwa duniani kwa ajili ya kuleta ukombozi kwa watu wote ambao walikuwa wakiugua magonjwa ya kansa ambayo yalikuwa yakisumbua sana katika nchi za Ulaya na Marekani. Kitendo cha kupokewa na rais Obama kikaonekana kuwa heshima kubwa na hali ya juu ambayo hata maraisi wengine hawakuwa wakiipata nafasi hiyo katika kipindi ambacho walikuwa wakikanyaga katika nchi ya Marekani.
Siku hiyo, sherehe ya kumkaribisha Abuu nchini Marekani ikaanza kufanyika katika Ikulu ya Marekani, watu walikula na kunywa. Abuu alionekana kuwa mmoja wa familia ya Kimarekani ambaye alikuwa amefika katika nchi hiyo katika muda maalumu ambao watu wengi walikuwa wakihitaji huduma yake.
Rais wa Tanzania, Bwana baraka Kyomo akapigiwa simu na rais wa Marekani, Bwana Obama na kupewa mchakato mzima ambao ulikuwa umeendelea katika nchi ya Afghanistan na kwa jinsi wanajeshi wa Marekani walivyokuwa wamepoteza maisha kwa ajili yake.
Kama makubaliano yalivyokuwa yakisema, Abuu akaanza kazi nchini Marekani kama dokta katika hospitali ya Washington Medical Centre huku akilipwa mshahara wa zaidi ya dola laki tano kwa wiki moja huku akiendelea kutengeneza dawa za magonjwa ya kansa, dawa ambazo zikaonekana kuwa suluhisho kubwa sana katika magonjwa ya kansa ambayo yalikuwa yakiwashambulia sana Wamarekani.
“I want to see my baby (Nataka kumuona mtoto wangu)” Hiyo ilikuwa ni sentensi ambayo Abuu alimwambia dokta Mickey kuhusiana na mtoto wake ambaye aliamini kwamba katika kipindi hicho alikuwa mzima nchini Tanzania.
Kilichofuatia baada ya siku mbili ni Abuu kusafiri mpaka nchini Tanzania kwa kutumia ndege ya kukodi tena huku akiwa na ulinzi maalumu kwa ajili ya kuepuka fitina kutoka katika serikali ya Tanzania. Kwa sababu rais wa Tanzania, Bwana Baraka Kyomo kuwa nchi za nje kikazi, makamu wake, Bwana Adrian Mhina alikuwa amefika uwanjani hapo na kisha kumpokea.
Abuu akaingia nchini Tanzania, akaandaliwa usafiri maalumu kwa kumpeleka katika kila sehemu ambayo alikuwa akitaka kufika kwa wakati huo kama kuwasalimia ndugu, jamaa na marafiki. Akaanza kuelekea katika mtaa ambao alikuwa akiishi katika kipindi cha nyuma kwa ajili ya kumuona bibi yake, Bi Asha ambaye alikuwa akimtumia fedha tu.
Bi Asha alipomtia machoni mjukuu wake, hakuamini, hakuamini kama kweli mjukuu wake alikuwa amerudi nchini Tanzania. Maisha yake kwa ujumla yalikuwa yamebadilika kwa kiasi kikubwa sana. Abuu hakujali jina kubwa ambalo alikuwa amejitengenezea katika kipindi hicho, alichokifanya ni kuanza kuongea na vijana ambao alikuwa amekua nao katika kipindi cha nyuma na kisha kuelekea katika kaburi ambalo mama yake, Bi Jamala alikuwa amefukiwa na kisha kuweka maua kama ishara ya kumkumbuka katika maisha yake yote.
“Inaniuma sana. Nilimuahidi mama yangu kumnunulia gari pamoja na kumjengea nyumba kubwa ya kifahari. Nimepata fedha, yeye hayupo” Abuu alimwambia bibi yake.
“Usijali Abuubakari, kila kitu kilichopita, acha kipite. Allah alikuwa nawe katika kipindi chote hicho, alikuwa na makusudi na maisha yako” Bi Asha alimwambia Abuu.
Abuu hakutaka kuendelea kukaa makaburini hapo, alichokifanya ni kuingia garini pamoja na bibi yake, Bi Asha ambaye muda wote alikuwa akionekana kuwa na furaha na kisha kuanza kuelekea Magomeni alipokuwa akiishi mpenzi wake, Jasmin.
“Nina mtoto bibi” Abuu alimwambia Bi Asha wakati wakiwa njiani kuelekea Magomeni.
“Una mtoto?”
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Ndio. Wakati naondoka kuelekea nchini India miaka mitatu iliyopita nilimuacha Jasmin akiwa mjauzito” Abuu alimwambia Bi Asha.
“Kweli?”
“Ndio. Aliniambia kwamba alijifungua salama. Nina furaha sana kwa ajili ya mtoto wangu” Abuu alimwambia Bi Asha.
Siku hiyo ilionekana kuwa siku ya furaha katika maisha yao wote wawili. Mpaka wanaingia Magomeni, walikuwa wakiongea mambo mengi pamoja huku kila mmoja akionekana kuwa na furaha kupita kawaida.
Kitendo cha Abuu kumtia machoni Jasmin kilionekana kumfurahisha kupita kawaida, hapo hapo Jasmin akaanza kukimbia na kumfuata Abuu. Abuu alitamani kukimbia lakini mguu wake mlemavu ulimkosesha uhuru, Jasmin alipofika karibu yake, akaitupa fimbo yake ya kutembelea na kisha kumkumbatia Jasmin mpaka kudondoka chini.
Hiyo ikaonekana kuwa furaha kubwa katika maisha yao, kwa miaka mitatu hawakuwa wameonana zaidi ya kuwasiliana simuni tu, leo ndio ilikuwa siku ambayo walionana kwa mara nyingine. Kila mtu alikuwa akidondosha chozi, kuonana kwa mara nyingine kulionekana kumfurahisha kila mmoja.
“Nimekukumbuka sana mpenzi wangu” Abuu alimwambia jasmin.
“Hata mimi. Nimekukumbuka sana” Jasmin alimwambia Abuu.
Wote wakaanza kutembea kuelekea ndani ya nyumba hiyo. Uso wa Abuu ukajawa na tabasamu pana mara baada ya macho yake kutua usoni mwa mtoto wake, akaanza kusogea katika kochi ambalo alikuwa amekaa na kisha kumkumbatia.
“Zubeda wangu! Oooh! Zubeda wangu” Abuu alisema huku akimchukua mtoto wake, Zubeda na kumpakata.
“Umefanana nae” Jasmin alimwambia Abuu.
“Kidogo. Asilimia kubwa kachukua kutoka kwako. Inaonekana atakuwa mzuri sana kama wewe mpenzi wangu” Abuu alimwambia Jasmin.
“Ila atakuwa na akili kama zako” Jasmin alimwambia Abuu.
“Kama nimeweza kutengeneza dawa ya magonjwa ya kansa, yeye atatengeneza dawa ya UKIMWI. Nataka familia nzima tuwe wagunduzi wa dawa za magonjwa yaliyo sugu katika maisha ya binadamu” Abuu alimwambia Jasmin.
Siku hiyo waliongea mengi huku wakipanga mipango ya harusi yao ambayo ilitakiwa kufungiwa nchini Marekani. Abuu akaonana na baba yake Jasmin, mzee Hassani pamoja na mama yake, Bi Rukia na kuanza kuongea nao na kujitambulisha rasmi kuwa kama mkwe wao mtarajiwa.
“Unakwenda wapi baada ya hapa?” Jasmin alimuuliza Abuu.
“Kwenda kula chakula Ikulu”
“Ila si rais hayupo?”
“Yeah! Ila amenitaka nifike mahali hapo pamoja na makamu wake. Tutakwenda pamoja” Abuu alimwambia Jasmin.
“Ondoa shaka kipenzi. Ila umewasiliana na John? Rafiki yako wa shuleni kipindi kile?” Jasmin alimuuliza Abuu.
“Hapana. Hivi yupo wapi siku hizi?”
“Nae anataka kuwa daktari, anasoma chuo cha uuguzi, Muhimbili”
“Anataka kuwa daktari! Hilo ni jambo la kumshukuru Mungu. Nadhani nitamuona hata kesho. Nimekuja huku kwa ajili ya kukuchukua tu na wiki ijayo tunaondoka kuelekea nchini Marekani. Kuna vibali kadhaa vinaandiliwa kwa ajili yako” Abuu alimwambia Jasmin
“Hakuna tatizo”
Usiku wa siku hiyo wakaelekea katika Ikulu ya rais na kisha kupata chakula cha usiku. Siku hiyo waliongea mengi na Bwana Mhina na kumuelezea mambo mengi ambayo yalitokea katika safari yake ya kuelekea nchini marekani kutoka India. Ilikuwa ni moja ya safari ambayo ilikuwa ikitia huruma sana katika maisha yake ila mwisho wa siku, Mungu alikuwa pamoja nae.
“Kwa hiyo ratiba yako ipo vipi?” Bwana Mhina aliuliza.
“Kesho nitakwenda katika chuo cha Uuguzi cha Muhimbili kuonana na rafiki yangu na kisha kuondoka wiki ijayo mara baada ya kuwaona wagonjwa wa magonjwa ya kansa ambao wanateseka hospitalini hapo” Abuu alimwambia Bwana Mhina.
“Wewe mtu unatisha sana, sikutegemea kama mambo yangekuwa namna hii kwa muda mchache” John alimwambia Abuu katika kipindi ambacho alikwenda kumsalimia katika chuo cha Uuguzi cha Muhimbili.
“Kila kitu kilikuwa katika mipango ya Mungu. Mungu ameniumba hapa duniani ili watu wengine wapate nafasi ya kuishi kupitia mimi. Namshukuru sana mungu kwa hili” Abuu alimwambia John.
Mara baada ya wanachuo kugundua kwamba mtu ambaye alikuwa pamoja na John kwa wakati huo alikuwa Abuu, mtu pekee duniani ambaye alikuwa akitengeneza dawa ya magonjwa ya kansa, wakaanza kumzunguka. Kila mmoja alikuwa haamini kama yule ambaye alikuwa akimwangalia ndiye alikuwa Abuu mwenyewe ambaye alikuwa amesababisha vita kati ya Marekani na nchi ya Afghanistan pamoja na kuleta uhasama mkubwa ambao bado ulikuwa ukizidi kuendelea kati ya nchi ya Marekani na india.
Abuu alionekana kuwa kijana mdogo sana ambaye wala hakutakiwa kuwa kama vile ambavyo alikuwa katika kipindi hicho. Wanachuo zaidi ya mia saba wakamzunguka na kisha kuanza kuongea nae huku wakimuuliza maswali kadhaa ambayo yalikuwa yakihusiana na ugonjwa wa kansa pamoja na historia yake.
Kwa wanafunzi ambao walikuwa na simu pamoja na kamera, wakaanza kumpiga picha Abuu pamoja na kupiga picha nae. Kwao, kwa wakati huo Abuu alionekana kuwa mtu wa tofauti kabisa, kila mtu alikuwa akimuona mtu huyo kuwa na mvuto mkubwa katika macho yake.
Watu wakapigiana simu juu ya uwepo wa Abuu chuoni hapo jambo ambalo baada ya nusu saa tu, idadi kubwa ya watu wakaanza kumiminika katika eneo la chuo hicho hali iliyopelekea walinzi wa chuo hicho kufunga geti huku zaidi ya watu elfu tatu wakitaka kuingia ndani ya eneo la chuo hicho kwa lengo la kumuona Abuu na kuona anafanana vipi japokuwa walikuwa wakimuona sana katika vyombo vya habari
Siku hiyo, Abuu aliitumia kuwa chuoni hapo. Uwepo wake mahali hapo ukaharibu ratiba nzima ya masomo, kila mmoja alikuwa akitaka kuongea na Abuu ambaye kwao alionekana kuwa mtu muhimu sana. Waandishi wa habari wala hawakukosa, nao walipopata taarifa, wakafika ndani ya eneo la chuo hicho kwa ajili ya kupiga picha kadhaa na kisha kuziweka katika magazeti yao katika siku inayofuatia.
Abuu alipata nafasi ya kuwaelezea historia ya maisha yake. Historia yake ilionekana kumgusa kila mtu, hakukuwa na mtu aliyeamini kama Abuu alikuwa amepitia maisha yale ambayo alikuwa amepitia mpaka katika kipindi hicho. Kila mmoja alimuona Abuu kuwa mpiganaji hasa katika maisha yake, katika kila hatua ya maisha ambayo alikuwa akipitia, alikuwa akiishi kwa malengo makubwa.
Saa kumi na moja Abuu akaondoka katika maeneo ya chuo hicho na kuahidi kuelekea katika hospitali ya Muhimbili siku inayofuatia. Kitendo cha watu kusikia kwamba Abuu angekuwepo katika hospitali hiyo kuanzia saa nne asubuhi, saa moja asubuhi siku iliyofuata zaidi ya watu elfu kumi na mbili walikuwa wamekusanyika katika hospitali hiyo.
Kila mmoja alikuwa na shauku ya kumuona Abuu, kila mmoja alitaka kuhakikisha kwa macho yake kwamba Abuu alikuwa kijana mdogo kama magazeti yalivyokuwa yakisema au la. Hata picha zake ambazo zilikuwa zimetolewa katika vituo mbalimbali vya televisheni watu hawakuonekana kuziamini, walitaka kumuona kwa macho yao wenyewe.
Saa nne, gari aina ya Benzi ya Mjerumani ikaanza kuingia katika eneo la hospitali ya taifa ya Muhimbili. Kila mmoja alikuwa na shauku ya kutaka kumuona Abuu, hata wale watu ambao walikuwa wamefika hospitalini hapo kwa ajili ya matatibabu, wakasahau maumivu yao, nao wakataka kumuona Abuu.
Abuu alionekana kuwa na thamani katika kipindi hicho, alikuwa akionekana kama lulu katika maisha ya WaTanzania wengi. Fujo zikaonekana kutaka kutokea hospitalini hapo kiasi ambacho kikawafanya askari kuongezeka mahali kwa ajili ya kutuliza ghasia ambazo muda wowote ule zingewea kutokea kutokana na kila mtu kutaka kumuona Abuu.
Ikaanza kuonekana fimbo yake ya kutembelea na hatimae Abuu kuteremka. Japokuwa moja ya sheria za hospitalini ni kutopiga kelele, watu wote wakajikuta wakipiga kelele za shangwe, kitendo cha kumtia Abuu machoni mwao kilionekana kuwa kama muujiza. Abuu akatembea kwa hatua chache na kisha kuanza kuwapungia watu mikono huku pembeni yake akiwepo Jasmin ambaye alikuwa amemshika mtoto wake, Zubeda
Manesi na madaktari nao wakashindwa kuvumilia kabisa. Kila mmoja akaiona hiyo ndio kuwa nafasi pekee ya kumuona Abuu katika maisha yake, nao walikuwa wamesimama pembeni mwa watu waliokuwa mahali hapo wakimwangalia Abuu.
Watu walikuwa wakimpiga picha Abuu ambaye alikuwa akitembea kwa hatua za taratibu. Msafara huo, hakuwa Abuu peke yake bali hata Makamu wa raisi, Bwana Adrian Mhina alikuwa pamoja nae. Abuu alitembea mpaka katika sehemu alipokuwa dokta mkuu wa Hospitali hiyo, Dokta Mwamboka na kisha kumsalimia.
“Karibu sana Abuu” Dokta Mwamboka alimkaribisha Abuu.
“Asante sana” Abuu aliitikia na kisha wote kuanza kupiga hatua kuelekea ndani ya jengo la hospitali hiyo.
“Kwa siku, ni zaidi ya wagonjwa saba wanakuja hapa wakiwa na magonjwa mbalimbali ya kansa. Magonjwa haya yamekuwa yakiwatesa sana watu, kama tulivyokuwa na vyumba maalumu vya watu ambao wamevunjika viungo vya mwili kutokana na ajali mbalimbali hasa za pikipiki basi napo tuna chumba maalumu, chumba kikubwa ambacho humu kuna wagonjwa mbalimbali ambao wanaugua kansa katika miili yao” Dokta Mwamboka alimwambia Abuu.
“Siupendi ugonjwa huu. Nitauchukia mpaka kifo changu” Abuu alimwambia dokta Mwamboka.
“Huu ni ugonjwa unaotisha sana. Unawasumbua sana wanawake kutokana na matiti yao kuharibiwa sana na ugonjwa huu. Japokuwa dawa zako zimeanza kusambazwa lakini zimekuwa ngumu sana kupatikana katika bara la Afrika na ndio maana watu wanazidi kuteswa na magonjwa hayo” Dokta Mwamboka alimwambia Abuu ambaye alikuwa akilengwa na machozi.
Bado walikuwa wakitembea tu. Katika kila hatua ambazo walikuwa wakipiga, waandishi wa habari walikuwa wakiendelea na kazi zao za kuwapiga picha kama kawaida yao. Safari ile ikaishia katika chumba kimoja kikubwa sana ambacho kilikuwa kimejaa vitanda ambavyo vilikuwa na wagonjwa kadhaa wa kansa.
Abuu alipowaangalia watu wale tu, machozi yakaanza kumtoka. Kwa sababu muda huo ulikuwa ni muda wa kuwaangalia wagonjwa, watu ambao walikuwa wamekuja kuwaangalia wagonjwa ndani ya hospitali ile walikuwepo pamoja na wagonjwa wao huku wakiwa wamewaletea vyakula mbalimbali.
“Kuna wanawake ambao wanasumbuliwa sana na kansa ya matiti. Asilimia tisini na nane ya wagonjwa wa kansa kwa wanawake wanasumbuliwa na kansa ya matiti ndani ya chumba hiki. Kwa wanaume, wengi wanasumbuliwa na magonjwa ya kansa ya vifua kama huyo mzee na vijana wale kule” Dokta Mwamboka alimwambia Abuu huku akimnyooshea kidole mzee mmoja aliyelala kitandani ambaye alikuwa na mwanamke mmoja aliyeonekana kuwa na majonzi.
“Shikamoo” Abuu alimsalimia mzee yule mara baada ya kumfikia.
“Marahaba” Mzee huyo aliyekuwa amelala aliitikia salamu ile kwa tabu huku akimwangalia Abuu.
“Shikamoo mama” Abuu alimsalimia mwanamke ambaye alikuwa amekuja kumuona mzee huyo.
“Marahaba kijana wangu” Mwanamke yule aliitikia.
“Mzee anaumwa nini tena?” Abuu aliuliza huku akijifanya hajui.
“Anaumwa kifua. Sijui ni kifua kikuu au sijui ni kifua cha kawaida, wala sijui” Mwanamke yule aliyejitambulisha kwa jina la Siwema alijibu.
“Poleni sana. Ila dokta hajawaambia anasumbuliwa na nini?” Abuu aliuliza.
“Kuna nesi alituambia kwamba ana kansa ya kifua” Bi Siwema alimwambia Abuu.
“Ilianza vipi hiyo kansa?” Abuu aliuliza.
“Alikuwa akivuta sana sigara hata kabla sijakutana nae alipotoka Afrika Kusini” Bi Siwema alijibu.
“Baada ya hapo mlikwenda katika hospitali yoyote ile kuangalia afya yake?” Abuu aliuliza.
“Hakuna. Hatukwenda. Kutokana na fedha ambazo alikuwa nazo katika kipindi hicho alikuwa akitumia dawa tu” Bi Siwema alimwambia Abuu.
“Na wewe ulikutana nae kwa muda gani mpaka sasa?” Abuu aliuliza.
“Ni muda mrefu sana. Si chini ya miaka ishirini iliyopita. Ni kipindi kirefu sana mpaka sasa hivi tuna watoto ambao wamemaliza kidato cha nne” Bi Siwema alimwambia Abuu.
“Pole sana mgonjwa na pole sana mama kwa kuwa mvumilivu kumuuguza mzee” Abuu alimwambia Bi Siwema.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Asante sana” Bi Siwema alimwambia Abuu.
“Ugonjwa wake umenigusa sana, sikutarajia kama ningekutana na mtu mwenye kansa ya kifua. Mama yangu alifariki kwa kansa ya matiti lakini nayo ilienea mpaka kifuani. Nilivyosikia ni kansa ya kifua ndio inamuweka hapa tena imetokana na uvutaji mkubwa wa sigara, imeniuma sana. Sijui unaniruhusu nipige nae picha japo ya ukumbusho?” Abuu alimuomba Bi Siwema.
“Usijali baba yangu. Unaweza kupiga nae tu” Bi Siwema alijibu na kisha Abuu kupiga picha na mzee yule ambaye alionekana kuwa hoi kitandani pale.
“Nashukuru sana mama kwa ruhusa yako. Ugua pole mzee wangu” Abuu alimwambia mzee yule.
“Asante sana kijana wangu”
“Usijali mzee wangu. Mimi ninaitwa Abuu, sijui wewe unaitwa nani?” Abuu alimuuliza.
“Naitwa Selemani. Selemani Ramadhani” Mzee yule alijibu.
“Jina lako ni kama la marehemu baba yangu. Ugua pole sana mzee wangu” Abuu alimwambia mzee Selemani.
“Asante sana” Mzee Selemani alijibu na kisha Abuu kuondoka mahali hapo kwenda kuwatazama wagonjwa wengine ambapo napo huko aliendelea kuwafariji.
*****
Tandi na Selemani walionekana kutokuwa na furaha kabisa, tukio la harusi ambalo lilikuwepo mbele yao lilionekana kuwahuzunisha kupita kiasi. Kila mmoja alikuwa akimpenda sana mwenzake katika kipindi hicho na ndio maana walijisikia vibaya sana endapo tukio lile lingekaminilika. Wakati mwingine Selemani alikuwa akijuta, alijuta sababu ambayo ilimfanya kuchelewa kuingia nchini Afrika kusini mpaka kukuta Tandi akiwa tayari ana mtu wake.
Kuolewa kwa Tandi kulimaanisha kuwa mwisho wa kila kitu katika maisha yao ya uhusiano, hiyo ilimaanisha kwamba wasingeweza kulala pamoja wala kuishi pamoja. Tandi ndiye ambaye alikuwa akiumia zaidi, mapenzi, matunzo na moyo wenye kujali ambao alikuwa akionyeshewa na Selemani ndio ambao ulikuwa ukimfanya kujisikia vibaya zaidi.
Alijua fika kwamba kwa Pokwane, asingeweza kuyapata yale ambayo alikuwa akiyapata kutoka kwa Selemani, yale ambayo Selemani alikuwa akimpa yalikuwa yakipatikana kwa wanaume wa KiTanzania peke yao katika bara hili la Afrika.
Siku ziliendelea kukatika kama kawaida, alichokifanya Selemani kwa wakati huo ni kuanza kumchuna hasa Tandi. Kila siku alikuwa akimtumia kuchukua fedha kwa Pokwane jambo ambalo lilimpatia kiasi kikubwa cha fedha katika hazina yake. Zaidi ya randi milioni kumi zilikuwa kwenye hazina yake ambayo wala hakutaka ionekane na Tandi.
Bado maisha yalikuwa yakiendelea, Tandi alijua fika kwamba angeweza hata kukataa kuolewa na Pokwane lakini kwa kufanya hivyo alikuwa akihofia juu ya maisha ya Selemani. Alijua fika kwamba kama angesema akatae na hatimae kuanza kuendelea kuishi na Selemani ambaye ni Mtanzania, basi kijana huyo angeuawa kutokana na chuki ambayo angekuwa nayo Pokwane.
Alikuwa akikubali kuolewa na Pokwane kwa sababu tu alihitaji Selemani aendelee kuishi na ndio maana kila kitu ambacho alikuwa akikihitaji Selemani alikuwa akimpatia bila kuuliza swali lolote lile. Majonzi hayakuisha, kila siku walikuwa wakiendelea kuhuzunika kupita kiasi, harusi ile bado ilikuwa ikiwaondolea furaha kupita kawaida.
“Kwa hiyo itakuwaje?” Nyerere aliuliza.
“Bado sijajua itakuwaje” Selemani alijibu.
“Ila ulifanya kama ulivyopanga?”
“Kufanya nini?”
“Kuchukua chapaa”
“Hiyo kama kawa. Toka lini umeona watoto wa Kibongo tukichelewa kufanya maamuzi katika mambo ya fedha?”
“Hahaha! Mimi nakukubali hapo tu, hurembi hata kidogo” Nyerere alimsifia Selemani huku wakigonganishiana mikono.
“Ila tuache utani. Hivi nishauri nifanye nini juu ya huyu mwanamke” Pokwane alimuuliza Nyerere.
“Kama vipi mtoroshe”
“Nimtoroshe?”
“Ndio. Sasa wewe unaogopa nini hapo? Mwanamke si unampenda na hutaki kumuona akiolewa na mtu mwingine. Mtoroshe tu” Nyerere alimwambia Selemani.
“Kwa hiyo unamaanisha niende nae nchini Tanzania?”
“Hiyo ndio maana yangu halisi” Nyerere alimwambia Selemani.
“Ila si unajua sina vibali?”
“Yeah! Ila njia za panya si zipo kwa ajili ya wasiokuwa na vibali? Tena kwako itakuwa rahisi kwa sababu unarudi nchini kwako”
“Poa. Ngoja nijaribu kuchonga nae, mambo yakiwa mwake, nitatoroka nae” Selemani alimwambia Nyerere.
Hilo ndilo wazo ambalo alikuwa ameambiwa na bila shaka aliliona kuwa la muhimu sana kuliko wazo jingine. Alichokifanya Selemani ni kumfikishia Tandi wazo lile ili aone ingekuwaje. Kwa Tandi, wazo lile likaonekana kufaa kupita kawaida, aliliunga mkono kwa asilimia mia moja.
Wangeanzia wapi? Wangetoroka vipi? Hayo ndio maswali ambayo yalionekana kuwatatiza kwa wakati huo. Kutokuwa na vibali vya kusafiria kulionekana kuwa tatizo kubwa sana kwa Selemani, kama angekuwa na vibali hivyo, kuondoka nchini Afrika Kusini lisingekuwa jambo gumu, kingekuwa ni kitendo cha kupanda ndege na hatimae kuelekea nchini Tanzania tu bila kipingamizi chochote kile.
“Nina wazo” Tandi alimwambia Selemani.
“Wazo gani?”
“Ngoja niwatafute wajanja watutengenezee vibali. Hawawezi kushindwa” Tandi alimwambia Selemani.
Hilo ndilo lilikuwa wazo jingine ambalo liliafikiwa na lilitakiwa kufanywa kwa haraka sana. Alichokifanya Tandi ni kuwatafuta wajanja wa mjini na kisha kuomba kutengenezewa passport kubwa ambayo ingeonyesha kwamba Selemani alikuwa Mtanzania ambaye alikuwa amekuja hapo nchini Afrika Kusini mara moja.
Kwa wajanja wa mjini, hilo halikuonekana kuwa tatizo, walichokihitaji ni randi elfu kumi na kisha kuanza kuangaikia ishu ambayo walikuwa wamepewa na Tandi huku tayari wakiwa wamepewa picha za passport saizi ambazo alikuwa amepiga Selemani. Ndani ya siku mbili tu, kila kitu kilikuwa tayari, passpoti ilikuwa imekwishaandaliwa na ilionyesha kwamba Selemani alikuwa Mtanzania ambaye alikuwa amefika tu nchini Afrika Kusini mara moja.
Kila kitu kilichokuwa kimefanyika katika pasipoti ile kilionekana kuwa sawasawa na pasipoti yenyewe. Hazikuonekana kutofautiana hata mara moja jambo ambalo lilionyesha kwamba wajanja hao wa mjini walikuwa na watu katika kila sekta nchini hapo.
Hawakuishia hapo, bado waliendelea kumtafutia vibali vingine mpaka vilipokamilika. Mpaka kufikia hatua hiyo, kila kitu kikaonekana kuwa tayari na ni safari ya kuelekea nchini Tanzania ndio ambayo ingeanza, wasingeweza kutumia ndege kwani walionekana kutokujiamini, usafiri ambao waliuona kufaa ni kutumia basi ambalo lilikuwa linapitia Mozambique, Malawi na hatimae kuingia nchini Tanzania.
********************************************
Fedha bado zilikuwa zikihitajika kupita kawaida. Selemani alijua fika kwamba alikuwa na kiasi kikubwa ambacho kingemfanya kuyatengeneza maisha yake kama ambavyo alivyotaka yawe nchini Tanzania lakini bado alionekana kuhitaji fedha zaidi. Jambo hilo hakuhitaji kubaki nalo moyoni mwake, alichokifanya ni kumwambia Tandi ambaye alikubali kufanya kila liwezekanalo mpaka wanapata fedha nyingi kadri iwezekanavyo.
Alichokifanya Tandi ni kuwasiliana na Pokwane na kisha kumwambia kwamba alikuwa akihitaji kiasi cha randi milioni tatu kwa ajili ya kusafiri kuelekea nchini Swaziland kuangalia maporomoko ya maji pamoja na rafiki zake huku wakitembelea katika mbuga mbalimbali za wanyama. Japokuwa kilikuwa ni kiasi kikubwa cha fedha lakini Pokwane hakuonekana kujali kabisa, alichokifanya ni kumtumia Tandi kiasi kile katika akaunti yake ya benki.
Tandi hakutaka kuchelewa, siku hiyo akaelekea benki ambapo akatoa kiasi chote cha zaidi ya randi milioni tano na kisha kurudi nacho nyumbani na kumwambia Selemani kwamba kila kitu kilikuwa tayari. Kwa sababu Tandi alikuwa ameonyesha moyo wa mapenzi mazito, Selemani hakutaka kujificha, akakitoa kiasi cha fedha ambacho alikuwa amekitunza katika miaka yote, wakajikuta wakiwa na kiasi kikubwa cha fedha.
Kwa sababu tayari walikuwa na kila kitu katika wakati huo, siku inayofuata ndio ilikuwa siku ambayo walitakiwa kusafiri kuelekea nchini Tanzania. Usiku hawakulala, walikesha wakifanya mapenzi tu mpaka ilipofika saa kumi na moja alfajiri na ndipo hapo safari ya kuelekea Tanzania ilipoanza. Hawakutaka kumuaga mtu yeyote zaidi ya Nyerere ambaye alitakiwa kuwa kimya bila kumueleza mtu yeyote mahali ambapo walipokuwa wamekwenda.
Usafiri wao ulikuwa ni wa basi, wakapanda basi ambalo lilianza safari saa kumi na moja alfajiri. Walikuwa wamekaa katika viti vya watu wawili, muda wote walikuwa wakipiga stori huku wakishikana hapa na pale. Mapenzi yao yalionekana kuwa makubwa katika kipindi hicho, uamuzi ambao walikuwa wameuchukua kwa ajili ya kwenda nchini Tanzania kwao ulionekana uamuzi bora kufanyika katika kipindi hicho.
Safari ya kutoka Johannesburg mpaka Pretoria ilikuwa safari ndefu kidogo lakini wala hawakuonekana kuchoka. Baada ya saa moja na nusu wakaingia katika jiji la Pretoria ambapo hapo wakashuka na kisha kula chakula na safari kuendelea huku wakianza kuingia porini zaidi.
Hapo dereva akaanza kuitafuta Bela Bela na kupita katika mbuga ndogo ya wanyama ambao ilikuwa imetengenezwa kwa ajili ya maonyesho mbalimbali, mbuga ya Combretum ambayo ilikuwa si mbali sana kutoka Bela Bela. Ndani ya masaa matatu, wakaanza kuingia Bela Bela ambapo abiria wakashuka na kisha kuanza kununua vyakula ambavyo vilikuwa vikiuzwa katika hoteli zilizokuwa mahali hapo na kisha kuendelea na safari yao.
Abiria ndani ya gari walikuwa wakiwaangalia kwa macho ya wivu, mapenzi ya wazi ambayo walikuwa wakipeana yalionekana kumshangaza kila mtu mahali hapo. Hakukuwa na mtu ambaye alikuwa akisikia aibu au kujishtua, hawakuonekana kujali kabisa, kitu ambacho walikuwa wakikijali ni kupeana mapenzi ya dhati tu.
“Mmmh! Watu wanavyotuangalia mpaka naogopa” Tandi alimwambia Selemani.
“Achana nao. Mambo haya tunayaweza WaTanzania tu” Selemani alimwambia Tandi na kisha kuanza kupeana mabusu mbalimbali miilini mwao.
Kutoka Bela Bela mpaka Mokopane walichukua zaidi ya masaa matano, wakawa wamefika mahali hapo. Jua lilikuwa kali sana lakini hawakutakiwa kukaa sana hapo Mokopane jambo ambalo walionganisha safari yao moja kwa moja.
Watu ndani ya basi lile walionekana kuchoka kupita kawaida na wengine walikuwa wamekwishaanza kulala. Selemani na Tandi bado walikuwa macho huku wakiendelea kupiga stori za hapa na pale lakini mara baada ya basi kufika Louis Trichardt, wakajikuta wakipitiwa na usingizi.
Walikuja kuamka katika kipindi ambacho basi lilikuwa likipaki Thohoyandou, upande wa Kaskazini mwa nchi ya Afrika Kusini, kiliometa mia nne kutoka katika mpaka wa nchi hiyo na nchi ya Zimbabwe, mpaka wa Musina. Selemani na tandi hawakutaka kulala ndani ya basi, walipoambiwa kwamba safari ya kuondoka hapo Thohoyandou kuelekea mpaka Musina ingeanza saa kumi na mbili asubuhi, wakaondoka na kwenda kulala hotelini.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kama kawaida yao, usiku kucha walikuwa wakifanya mapenzi, kila mmoja alionekana kumtamani mwenzake kiasi ambacho ngono ndio ambayo ilikuwa ikifikirika katika kichwa cha kila mtu. Tandi alikuwa amesahau kabisa kuhusiana na Pokwane, mwanaume mwenye fedha, mwanaume ambaye alikuwa akiuza madawa ya kulevya ambaye alikuwa akitaka kumuoa.
Saa kumi na moja wakaamka kutoka usingizini, wakajiandaa na kisha kuelekea katika sehemu lilipopaki basi lao na kisha kuingia. Saa kumi na mbili kamili, safari ya kuelekea mpakani Musina ikaanza. Kwa wakati huo kila mmoja alionekana kuchangamka, safari ambayo ilikuwa mbele yao kabla ya kuingia Musina wala haikuonekana kuwa mbali.
Baada ya saa moja, wakaingia katika mpaka huo. Hawakuonekana kuwa na wasiwasi kabisa, utengenezaji wa vibali ambavyo walikuwa navyo uliwafanya kujiamini kupita kawaida. Vibali vya abiria wote pamoja na pasipoti zao vikaangaliwa na kisha kuruhusiwa.
Wakaingia nchini Zimbabwe, nchi ambayo wala hawakuwa wamewahi kufika kabla. Kwa sababu lilikuwa ni basi ambalo lilikuwa likitembea nchi kwa nchi, hawakutakiwa kutumia barabara nyingine zaidi ya ile ambayo ilikuwa ikipita katika mbuga ya wanyama ya Gonarezhou, mbuga ambayo ilikuwa Mashariki mwa nchi ya Zimbabwe, tena karibu kabisa na nchi ya Mozambique.
Hapo ndipo kulipokuwa kukichukua kipande kikubwa cha safari yao. Ukubwa wa mbuga ile uliwafanya kuchukua masaa mengi barabarani kiasi ambacho kila mtu ndani ya gari alionekana kuchoka kupita kawaida. Abiria wa basi zima ndani ya gari walikuwa wamelala huku wengine wakikoroma kwa sauti kubwa. Basi bado lilikuwa likiendelea kupita katika mbuga hiyo ambayo bado hakukuwa na dalili zozote za kuimaliza na hatimae kuingia katika Mutare ambapo hapo wangeingia porini kabisa na hatimae kuingia katika mpaka wa Mozambique na Zimbabwe na kisha kuanza kuitafuta nchi ya Zambia hata kabla ya kuingia nchini Tanzania.
*****
Selemani alikuwa katika chumba kilichojaa giza, mwili wake ulikuwa ukimtetemeka kupita kawaida, mbu ambao walikuwa ndani ya chumba kile walikuwa wakimuuma kupita kawaida. Joto ndani ya chumba kile lilikuwa kubwa jambo ambalo liliufanya mwili wake kutokwa na jasho jingi.
Macho yake yalikuwa mekundu, maji maji ambayo yalikuwepo ndani ya chumba kile yalimfanya kujisikia vibaya kiasi ambacho alikosa amani ya kukaa chini. Selemani alikuwa akijuta, hakuamini kwamba katika kipindi hicho alikuwa katika mikono ya Pokwane, mtu ambaye alikuwa akimtorosha mpenzi wake kuelekea nchini Tanzania.
Huku akiwa hajui afanye nini, mlango ukafunguliwa na wanaume wawili wenye miili iliyojazia kuingia ndani ya chumba kile. Selemani alikuwa akiomba msamaha lakini hakukuwa na mtu yeyote ambaye alikuwa akimuelewa. Ugonjwa wake wa kifua ambao alikuwa nao katika kipindi hicho ulionekana kumsumbua zaidi, alikuwa akikohoa ovyo.
Selemani akachukuliwa na kisha kutolewa ndani ya chumba kile. Alibebwa juu juu mpaka katika sehemu ambayo wala hakuwa akiielewa vizuri. Mbele yake kulikuwa na msichana mmoja ambaye alikuwa amefunikwa kichwa chake na kigunia, kile kigunia kilipotolewa na kumwangali, alikuwa Tandi.
Uso wa Tandi ulikuwa umeharibika kupita kawaida, uso mzima ulikuwa umejaa damu kana kwamba alikuwa amemwagiwa ndoo ya damu usoni mwake. Tandi alikuwa akilia huku akiomba msamaha juu ya kile ambacho alikuwa amekifanya, kitendo cha kumsaliti Pokwane.
Hakukuwa na mtu ambaye alionekana kujali. Selemani akachukuliwa na kisha kukalishwa kwenye kiti kingine kilichokuwa mahali pale. Mwanaume mmoja akafika mahali pale huku akiwa na wembe mpya na kisha kuanza kumchana chana Selemani na kuchukua viwaya vidogo na kuvipitisha mwilini mwa Selemani katika sehemu zile alizozichana na kisha kuziweka katika soketi ya umeme na umeme kuwashwa.
Selemani alikuwa akipiogwa shoti, umeme ule ukaonekana kuwa adhabu kubwa mwilini mwake. Selemani akaanza kulia kama mtoto mdogo, shoti ile ya umeme iliendelea kumtesa zaidi na kisha kuachwa na baada ya muda mwanaume mwingine kutokea na kisha kuanza kumwangalia usoni.
“Mimi ndiye Pokwane uliyekuwa ukinisikia” Mwanaume yule alimwambia Selemani na kisha kuanza kumshambulia kwa ngumi nzito.
Selemani akaanza kulia kama mtoto, ngumi mfululizo zilikuwa zikitua usoni mwake, uso wake ukaanza kujaa damu, meno yakang’oka lakini Pokwane hakuonekana kujali kabisa. Selemani alizidi kupigwa ngumi kali tena za mfululizo mpaka akawa hoi.
“Ninawaua wote wawili na maiti zenu kuziwekea mizigo yangu ya dawa za kulevya na kisha kuisafirisha kuipeleka Dubai” Pokwane alisema huku akichomoa bunduki yake.
Kitu cha kwanza alichokifanya Pokwane ni kumfuata Tandi na kisha kumpiga risasi ya mguu, Tandi akaanza kulia kupita kawaida, mguu wake ulikuwa umepata maumivu makali ambayo wala hakutegemea kuyapata kabla. Baada ya hapo, Pokwane ambaye wala hakuonekana kujali akamfyatulia risasi nyingine iliyotua begani, Tandi alikuwa akilia kupita kawaida.
“Haya ndio malipo yako malaya mkubwa” Pokwane alimwambia Tandi na kisha kumpiga risasi ya kichwa na huo kuwa mwisho wa Tandi.
“Bado wewe. Ni lazima nawe nikuue” Pokwane alimwambia Selemani.
Hapo hapo akawaagiza vijana wake kumletea ndoo iliyokuwa imejaa asidi na kisha kuchota kiasi fulani kwa kutumia chombo maalumu na kisha kummwagia Selemani mapajani. Selemani alitoa uyowe mkubwa ambao hakuwahi kuutoa kabla, asidi ile ilikuwa imemuunguza kupita kawaida.
Pokwane na vijana wake wakabaki wakicheka tu, hawakuonekana kuyajali maumivu aliyoyasikia Selemani. Alipoona kwamba ile haikutosha, akachukua ndoo ile, akaibeba na kisha kummwagia Selemani asidi yote mwili mzima. Ule ukaonekana kuwa mwisho wa Selemani.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
********************************************
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment