Search This Blog

Sunday, July 10, 2022

MUNGU PEKEE NDIYE ATAKAYENISAMEHE - 2

 





    Simulizi : Mungu Pekee Ndiye Atakayenisamehe

    Sehemu Ya Pili (2)









    Ilipoishia jana



    alionekana kuchanganyikiwa kupita kawaida, kila kitu ambacho alikuwa akikifikiria mahali hapo, aliona dhahiri kwamba mtoto wake alikuwa akienda kuuawa, kitu pekee ambacho alikuwa akitakiwa kukifanya ni kumzuia Alan kuingia ndani ya nchi ya Mexico.



    Songa nayo sasa..

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    Bwana Kurt bado alikuwa amechanganyikiwa, kitendo cha Alan kuondoka Washington na kisha kuelekea Texas kwa ajili ya kuingia nchini Mexico kulionekana kumchanganya kupita kawaida. Chumbani hakukukalika tena, akatoka chumbani na kisha kuelekea sebuleni. Akajitupa kochini na kutulia, mawazo yake yalikuwa yakifikiria mambo mengi kwa wakati huo.

    Mkewe, Bertha akatokea sebuleni hapo. Kama alivyokuwa amechanganyikiwa mume wake na yeye alikuwa hivyo hivyo. Kila mmoja alikuwa na uhakika kwamba mtoto wao Alan alikuwa akitaka kuelekea nchini Mexico, sehemu ambayo kulikuwa na mbaya wao namba moja duniani, mzee Sanchez.

    “Ngoja tuone atasemaje. Sikutaka kumuona Alan akielekea nchini Mexico” Bwana Kurt alimwambia mke wake.

    “Ila kwa nini haukumwambia ukweli?” Bi Bertha aliuliza.

    “Ilikuwa ngumu. Alan na Antonio ni marafiki, kama ningemwambia ukweli ningeweza kuutia doa urafiki wao” Bwana Kurt alimwambia mke wake.

    “Tuombe Mungu, nadhani atamlinda huko aelekeapo”

    Bado kila mmoja alionekana kukata tamaa, kitendo cha Alan kuelekea nchini Mexico kiliwanyima raha kabisa. Kila wakati walikuwa wakishikana mikono kama watu ambao walikuwa wakisali, mioyo yao ilikuwa ikimuomba Mungu afanye muujiza japo Alan asiingie nchini Mexico au kama ikishindikana basi aingie lakini asiuawe.

    Usiku ukaonekana kuwa mrefu sana, kitu ambacho walikuwa wakikisikilizia mahali hapo ni simu kutoka kwa Maxwell ambaye angewaambia kile kilichokuwa kimeendelea jijini Texas kama alikuwa amekwishampata Alan au la. Masaa yaliendelea kusonga mbele lakini hakukuwa na simu yoyote ile ambayo iliingia katika simu ya Bwana Kurt kumwambia hali halisi ambayo ilikuwa ikiendelea kwa mtoto wake jijini Texas.

    “Au hawajampata?” Bi Bertha aliuliza huku akionekana kuwa na wasiwasi tele.

    “Ngoja tusikilizie” Bwana Kurt alimwambia mke wake.

    *****

    Ndege ndogo binafsi ya Alan ilikuwa ikitua katika jiji la Texas katika uwanja wa ndege wa Austin-Bergstrom. Ndani ya ndege walikuwepo watu wawili tu, Alan pamoja na rubani wake, Christopher. Ndege iliposimama, Alan hakutaka kubaki ndani ya ndege hiyo, kwa haraka haraka huku akionekana kuwa na haraka akateremka na kisha kuanza kupiga hatua kuelekea nje ya uwanja huo wa ndege kwa kupitia katika mlango binafsi ambao hutumiwa na watu wanaoshuka kwa kutumia ndege za kukodi.

    Alan akapitia hatua zote ambazo alitakiwa kupitia ndani ya uwanja huo wa ndege na kisha kutoka nje kabisa. Katika kipindi hicho kichwa chake kilikuwa kikifikiria kitu kimoja tu, kuelekea nchini Mexico. Mfukoni mwake hakuwa na passport wala hakuwa amegongewa viza, kitu ambacho alikuwa akitaka kukifanya ni kuingia nchini Mexico kwa kutumia fedha tu.

    Kichwa chake kilikuwa kikiamini katika fedha, alikuwa tayari kutumia fedha lakini mwisho wa siku aweze kuingia nchini Mexico. Huo ndio uamuzi ambao alikuwa nao siku hiyo, hakutaka kubaki nchini Marekani, kitu ambacho alikiamini ni kwamba endapo angebaki nchini Marekani basi ilikuwa ni lazima kumuonea huruma Stacie na mwisho wa siku kumrudia na kumuachia Albertina maumivu makali ya mapenzi moyoni mwake.

    Nchini Mexico ndipo kulipoonekana kuwa kimbilio lake kwa wakati huo, hakutaka kabisa kubaki nchini Marekani. Alipofika nje ya uwanja wa ndege huo hata kabla hajakodi teksi, Christopher akapiga hatua kumfuata, alipokaribia kumfikia, akamuita na Alan kugeuka na kuanza kumwangalia Christopher.

    “Mzee akipiga simu kukuulizia nimwambie nini?” Christopher alimuuliza Alan.

    “Hatoweza kukupigia simu” Alan alijibu.

    “Ikitokea amefanya hivyo?”

    “Mwambie nipo njiani kuelekea Mexico” Alan alimjibu Christopher.

    “Ndio unataka kwenda muda huu? Jioni yote hii?” Christopher alimuuliza Alan huku akionekana kushangaa.

    “Nitaondoka kesho asubuhi”

    “Sawa. Kwa ndege au?’

    “Nitapitia mpakani. Ila usimwambie kama nitapitia mpakani, mwambie nitakwenda na ndege. Sawa?” Alan alimwambia Christopher na kumuuliza.

    “Sawa”

    Alan hakutaka kubaki, alichokifanya ni kuingia ndani ya teksi ile na kisha kuondoka mahali hapo. Bado alikuwa na kiu kubwa ya kutaka kufika nchini Mexico, hakutaka kubaki nchini Marekani katika kipindi hicho kwa kuamini kwamba Stacie angeweza kumfuata popote pale ndani ya nchi hiyo. Alitaka kwenda nje ya nchi, mbali kabisa sehemu ambayo Stacie asingeweza kufika, na hata kama angefika basi asingeweza kumpata kwa urahisi.

    Teksi ile ikasimama nje ya hoteli kubwa ya Cowboys Stars ambapo Alan akateremka na kisha kumlipa dereva kiasi cha fedha kilichokuwa kikihitajika na kisha kuingia ndani ya hoteli ile. Moja kwa moja akaelekea mapokezini ambapo hapo akalipia gharama za kuchukua chumba kwa usiku mmoja na kisha kupelekwa ndani ya chumba hicho.

    Muda wote Alan alionekana kuwa na mawazo, alijiona akipitia katika wakati mgumu sana, kitendo cha kumkataa Stacie kilikuwa ni kitu kigumu sana ambacho alikifanya bila kujali kitu chochote kile. Mapenzi makubwa ambayo alikuwa nayo juu ya Albertina yalionekana kumbadilisha kabisa na kumpa ujasiri wa kufanya kitu chochote kile ili kumlinda Albertina asiweze kulia tena.

    Ndani ya chumba kile akabaki akimfikiria Albertina, alikuwa amekwishaanza kumkumbuka, alikuwa na hamu kubwa ya kuwa karibu na msichana huyo ambaye katika kipindi hicho alikuwa katika safari ya kuelekea nchini Mexico. Alipoona kwamba mawazo juu ya Albertina yamezidi zaidi na zaidi, akachukua simu na kisha kumpigia rafiki yake, Brian.

    “Mbona alfajiri sana Alan?” Sauti ya Brian ilisikika simuni.

    “Huku ni mbili usiku kwa sasa. Ninataka kuongea na Albertina. Yupo?” Alan alimwambia Brian na kumuuliza.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Yupo ila amelala kwani ndio kwanza saa kumi na mbili kasoro asubuhi huku” Brian alisikika akimwambia Alan.

    “Naomba kuongea nae kwanza”

    “Kuna tatizo lolote?”

    “Tatizo lilikuwepo ila nimekwishalitatua”

    “Tatizo gani tena?”

    “Kuhusu Stacie”

    “Stace Bruce?”

    “Yeah!”

    “Kwani bado ulikuwa nae?”

    “Ndio. Wazazi walikuwa wanafahamu kila kitu. Baada ya kukutana na Albertina nimeamua kumuacha kwa ajili ya kuwa na Albertina” Alan alimwambia Brian.

    “Si uamuzi mbaya. Ila wazazi wamechuliaje?”

    “Wameshtuka sana lakini nashukuru hawakuniingilia katika maamuzi yangu” Alan alimwambia Brian.

    “Sawa. Ni uamuzi mzuri ulioufanya”

    “Asante sana. Naomba kuongea na Albertina kabla sijaelekea nchini Mexico” Alan alimwambia Brian.

    “Mexico? Kufanya nini tena na wakati baba yako alikukataza kufika kule?” Brian aliuliza kwa mshtuko.

    “Kumtembelea Antonio. Ni muda mrefu sana sijaonana nae. Nahitaji kwenda kuonana nae na pia kuwa mbali na Stacie. Natumaini nikitoka Mexico nitakuja huko kumchukua Albertina” Alan alimwambia Brian.

    “Sawa. Nimekuelewa” Brian alimwambia Alan na kisha kuondoka kuufuata mlango wa kuingilia chumbani kwa Albertina, akapiga hodi, baada ya sekunde arobaini na tano mlango ukafunguliwa na Albertina na kisha kumpa simu ile.

    “Unasikika vizuri sana mpenzi, sauti yako nzuri hata kama umetoka kuamka” Alan alimwambia Albertina.

    “Nashukuru mpenzi. Nimekuota usiku wa leo” Albertina alimwambia Alan.

    “Kweli?”

    “Ndio”

    “Ndoto ya aina gani?”

    “Ndoto ya mapenzi”

    “Asante sana. Kwa siku ya leo sikulala vizuri kabisa, nimelala usingizi wa shida sana na ndio maana hata sikupewa nafasi ya kukuota malaika wangu” Alan alimwambia Albertina.

    “Kwa nini?”

    “Kulitokea mtafaruku kidogo nyumbani”

    “Mtafaruku! Kuhusu nini? Mimi?”

    “Hapana. Kuhusu Stacie”

    “Stacie! Stacie ndiye nani?”

    “Msichana aliyekuwa mpenzi wangu”

    “Imekuwaje sasa?”

    “Wazazi walitaka nimuoe ila nimewaambia kuhusu wewe na kuwaambia kwamba sipo radhi kumuoa Stacie, nataka kukuoa wewe” Alan alimwambia Albertina.

    “Wakasemaje?”

    “Wamekubaliana nami na wamekukubali pia” Alan alimjibu Albertina.

    “Nashukuru kwa kunitambulisha kwa wazazi wako”

    “Usijali. Nipo njiani kuelekea Mexico, nikitoka huko nitakuja Tanzania ili kukuchukua na kukuleta huku. Nataka ndani ya mwaka huu tufunge ndoa” Alan alimwambia Albertina.

    “Unataka tufunge ndoa ndani ya mwaka huu?”

    “Ndio. Au hautaki?”

    “Ninataka. Ninatamani hata iwe sasa hivi”

    “Basi usijali. Tutafunga ndoa, tutakwenda kula fungate katika kisiwa cha Hawaii” Alan alimwambia Albertina.

    “Mmmh!”

    “Mbona umeguna tena?”

    “Nasikia wanaokwenda huko huwa matajiri tu” Albertina alimjibu Alan.

    “Usijali, na sisi tutakwenda tu japo si matajiri. Ningependa ufike huko” Alan alimwambia Albertina.

    “Nitafurahi mpenzi”

    “Basi hakuna tatizo. Nilitaka tu kuisikia sauti yako usiku wa leo. Usiku mwema kipenzi changu” Alan alimwambia Albertina.

    “Usiku mwema tena! Huku ni asubuhi mpenzi”

    “Hahah! Sisi huku ndio tunajiandaa kulala. Nadhani leo nitakuota mpenzi, nitakuwa nawe katika njozi zangu” Alan alimwambia Albertina.

    “Nitafurahi sana” Albertina alimwambia Alan.

    Mpaka Alan anakata simu bado alikuwa na hamu ya kuisikiliza sauti ya mpenzi wake, Albertina. Moyoni mwake, Albertina alionekana ndiye kile kitu, alikuwa akimthamini na kumpenda kwa mapenzi ya dhati sana. Hakukuwa na msichana yeyote yule ambaye alikuwa akimthamini zaidi ya Albertina, msichana huyo kwake alionekana kuwa kama pumzi yake.

    Mawazo mengi juu ya Albertina yakamfanya kupatwa na usingizi saa tano usiku. Akalala usingizi mzito huku akiwa amepanga kwamba ifikapo saa mbili asubuhi siku inayofuatia ilikuwa ni lazima kuendelea na safari yake kuingia nchini Mexico kwa kupitia katika mpaka wa Nuevo Laredo uliokuwa katika upande wa kusini mwa jiji la Texas.

    Kichwani mwake hakujua kwamba baba wa rafiki yake, Antonio ambaye alikuwa akielekea huko kumtembelea ndiye ambaye alikuwa adui namba moja wa familia yake. Endapo Alan angefunguliwa na kuyajua mambo ambayo yangekwenda kutokea nchini Mexico, asubuhi inayofuatia angepanga safari ya kurudi jijini Washington badala ya kwenda nchini Mexico, ila kila kitu ambacho hutokea mbele, usoni mwa mwanadamu huwa sawa na giza nene, huwezi kujua.





    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    Mkuu wa kituo cha polisi jijini Texas, Michael Maxwell alikuwa hatulii ofisini mwake, kitendo cha kupokea simu kutoka kwa Bwana Kurt kilimfanya kuwa katika hali isiyoelewekaeleweka. Tayari alikuwa amekwishapewa taarifa juu ya uwepo wa Alan jijini Mexico na hivyo alikuwa akitakiwa kuhakikisha kwamba Alan anapatikana na kisha kurudishwa jijini Washington.

    Kitu cha kwanza alichokifanya ni kuwaita polisi wake wawili, Smith na Rogan ambao walifika mahali hapo na kisha kuwapa maelekezo juu ya kila kitu kilichokuwa kikitakiwa kufanyika mahali hapo. Mipango ikapangwa usiku huo huo na ni kitu kimoja tu ndicho ambacho kilikuwa kikisubiriwa mahali hapo, kupewa namba ya simu ya rubani Christopher ambaye alikuwa amemleta Alan katika jiji la Texas.

    Kila mmoja alikuwa na uhakika kwamba endapo wangefanikiwa kumpata Christopher basi kwao lisingeonekana kuwa tatizo kabisa kwani kwa jinsi hali ilivyokuwa katika kipindi hicho, Christopher alionekana kufahamu mahali ambapo Alan alikuwepo katika kipindi hicho. Ilipofika saa nne na dakika kumi usiku, meseji ikaingia katika simu ya Maxwell ambapo moja kwa moja akaifungua, akakutana na namba ambayo ilikuwa imetumwa kutoka katika simu ya Bwana Kurt, ikampa uhakika kwamba namba ile ndio ilikuwa ya huyo mtu aitwaye Christopher ambaye alitakiwa kumtafuta kwa wakati huo.

    Maxwell hakutaka kuchelewa, alichokifanya ni kuichukua namba ile na kisha kuipiga. Simu ikaanza kuita, iliita kwa takribani sekunde ishirini, ikapokelewa na sauti ya Christopher kuanza kusikika kutoka upande wa pili.

    “Naongea na nani?” Ilisikika sauti ya Christopher simuni mara baada ya salamu.

    “Unaongea na mkuu wa kituo cha polisi hapa Texas” Maxwell alimjibu Christopher.

    “Sawa. Kuna tatizo lolote mkuu?”

    “Hapana ila tunahitaji kukuona katika kipindi hiki” Maxwell alimwambia Christopher ambaye sauti yake ilikuwa ikisikika kioga.

    “Mbona usiku hivyo?”

    “Ni kwa sababu kuna kitu tunahitaji kufahamu kabla haijafika asubuhi” Maxwell alimwambia Christopher ambaye alikaa kimya kwa sekunde kadhaa.

    “Sawa. Hakuna tatizo”

    “Unaweza kufika hapa kituoni mara moja?”

    “Hakuna tatizo” Christopher alisema na kisha kukata simu.

    Kila mmoja akaonekana kuridhika, kitendo cha Christopher kuja ndani ya kituo kile kiliwafanya kuona kwamba ingekuwa ni rahisi sana kwao kumpata Alan na kisha kumchukua na kumpeleka jijini Washington. Wote watatu walikuwa na uhakika kwamba Christopher alikuwa akifahamu mahali ambapo Alan alikuwepo katika kipindi hicho kwani kama lengo lake lilikuwa ni kwenda nje ya nchi, asingeweza kwenda huko usiku huo.

    “Kuna tatizo mkuu?” Christopher aliuliza mara baada ya kuingia ndani ya kituo hicho na moja kwa moja kupelekwa katika ofisi ya Maxwell ambapo aliwakuta watu wengine wawili mbali na Maxwell.

    “Kaa chini kwanza” Maxwell alimwambia Christopher ambaye akakaa katika kiti kilichokuwa mbele ya meza ile.

    “Tumepokea simu kutoka kwa Bwana Kurt na kutuambia tuongee nawe kuhusiana na mahali alipokuwa mtoto wake, Alan katika kipindi hiki” Maxwell alimwambia Christopher ambaye alikuwa kimya akimsikiliza.

    “Bwana Kurt amewaambia nini?”

    “Kwamba unajua mahali Alan alipo kwani wewe ndiye uliyemleta hapa Texas” Maxwell alimjibu Christopher.

    “Ni kweli nilimleta leo jioni lakini niliachana nae na yeye kuondoka” Christopher alimwambia Maxwell.

    “Kivipi?”

    “Aliniambia nimlete hapa Texas, na kweli nikamleta, baada ya hapo akaondoka zake” Christopher alimwambia Maxwell.

    “Aliondoka kwenda wapi?”

    “Sifahamu”

    “Haukumuuliza?”

    “Sikumuuliza kwani sikutaka kuyaingilia mambo yake. Kama alivyotaka niliweza kufanya na nilikuwa nikitaka kurudi Washington kesho asubuhi” Christopher alimwambia Maxwell.

    “Kwa nini urudi kabla ya yeye kurudi?”

    “Aliniambia kwamba angeondoka kuelekea nchini Mexico”

    “Kufanya nini?”

    “Nadhani hayo ni mambo binafsi, hakuniambia”

    “Alisema anaondoka lini?”

    “Kesho asubuhi”

    “Sasa hivi yupo wapi?”

    “Kusema ukweli sifahamu”

    “Kwa hiyo uliachana nae uwanja wa ndege?”

    “Ndio. Nilitoka nae nje na kuongea nae kidogo, baada ya hapo, akapanda teksi na kisha kuondoka” Christopher alimwambia Maxwell.

    “Ooopppsss...!”

    “Hivyo ndivyo ilivyokuwa”

    “Kwa hiyo haufahamu alipokuwa sasa hivi?”

    “Sifahamu”

    “Unaweza kuifahamu hiyo teksi ambayo aliikodi?”

    “Kwa kuiangalia naweza kuifahamu kwani ina picha ya Che Guevara kwa nyuma” Christopher alimwambia Maxwell.

    “Sawa. Inuka twende” Maxwell alimwambia Chrostopher.

    “Twende wapi tena?”

    “Uwanja wa ndege”

    “Kufanya nini mkuu?”

    “Kuitafuta hiyo teksi” Maxwell alimwambia Christopher.

    Hakukuwa na sababu ya kuendelea kusubiri ndani ya kituo hicho kikuu cha polisi cha Texas. Moja kwa moja wakatoka nje ambapo wakaingia katika gari ya polisi wote wanne na kisha safari ya kuelekea uwanja wa ndege kuanza. Ndani ya gari kila mmoja alikuwa kimya akimfikiria Alan. Kwa Maxwell alikuwa akimfikiria Bwana Kurt, kazi ambayo alikuwa amepewa ilikuwa kubwa na aliamini kwamba ni lazima ingekuwa na kifuta jasho endapo angefanikisha kwa haraka mno.

    Hawakuchukua dakika nyingi wakawa wamekwishafika katika uwanja wa ndege na kisha kuteremka. Kitu cha kwanza wakaanza kuangalia teksi ambazo zilikuwa katika eneo lile la nje ya jengo la uwanja wa ndege, wakaanza kuitafuta teksi hiyo iliyokuwa na picha ya Che Guevara kwa nyuma lakini hawakufanikiwa kuiona kitu ambacho kiliwafanya kumfuata dereva mmoja aliyekuwa na teksi yake pembeni.

    “Hiyo ni teksi ya Marcus, nadhani atakuwa amekwenda nyumbani kwake” Dereva yule alimjibu Maxwell ambaye alikuwa amemuulizia dereva mwenye teksi ile.

    “Unapafahamu kwake?”

    “Hapana. Hapa huwa tunakutana tu, tunafanya kazi lakini hakuna mtu anayepafahamu nyumbani kwa mwenzake” Dereva yule alimwambia Maxwell.

    “Kwa hiyo itashindikana kumpata usiku huu?”

    “Hiyo itashindikana, labda mje kesho asubuhi” Dereva yule alijibu.

    Mtu ambaye walikuwa wamemfuata mahali hapo wakawa wamemkosa. Marcus ndiye ambaye alikuwa akihitajika, kila mmoja alikuwa na uhakika kwamba Marcus angeweza kuwaambia mahali ambapo Alan alipokuwa kwa wakati huo. Walichokifanya ni kuchukua namba ya simu yake, Maxwell alipopiga simu haikuwa ikipatikana na hivyo kuambiwa kwamba alitakiwa kuacha ujumbe ili mwenyewe atakapokuwa tayari kuusikiliza basi ausikilize.

    “Simu haipatikani”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Muachie ujumbe wa sauti” Christopher alimwambia Maxwell.

    “Nadhani hatoupata muda muafaka” Maxwell alimwambia Christopher.

    Dereva ambaye walikuwa wamemfuata mahali hapo kwa ajili ya kuwaambia kwamba Alan alikuwa ameelekea katika hoteli gani hawakuweza kumpata na hata walipokuwa wakijaribu kumpigia simu haikuwa ikipatikana kabisa. Hawakuwa na jinsi kwa wakati huo, walichokifanya ni kuondoka huku wakiahidi kurudi mahali hapo siku inayofuatia huku wakiacha ujumbe kwamba saa moja na nusu asubuhi watakuwa mahali hapo hivyo Marcus alitakiwa kuwasubiria.

    Katika kipindi chote hicho Maxwell alikuwa akifikiria kuhusiana na kazi kubwa ambayo alikuwa amepewa na tajiri mkubwa sana duniani, Bwana Kurt. Alijua fika kwamba endapo kazi ile ingekamilika kwa kumpata Alan na kisha kumpeleka katika jiji la Washington basi mzee huyo angeweza kumwangalia kwa jicho la tatu kwa kumpa kiasi fulani cha fedha.

    Mawazo hayo ya fedha ambayo alikuwa akiyafikiria ndio ambayo yalimfanya kufanya kazi kwa bidii sana na kuhakikisha kwamba Alan anapatikana na hatimae kumpeleka katika jiji la Washington. Usiku hakulala, kichwa chake badala ya kufikiria kumpata kwanza Alan, akaanza kufikiria kiasi cha fedha ambacho angepewa mara baada ya kupata Alan.

    “Kwa jinsi ninavyomfahamu, anaweza kunipa hata dola elfu ishirini” Maxwell alijisemea katika kipindi ambacho alikuwa kitandani amelala.

    “Mmmh! Lakini naona kama dola elfu kumi ndogo. Nadhani anaweza kunipa hata dola elfu hamsini. Kumpata Alan ni kazi kubwa kwa hiyo hata kiasi cha fedha inatakiwa kiwe kikubwa. Mmmh! Tena kuna kitu nimekumbuka. Smith na Rogan nao watahitaji fedha, kwa hiyo kama nitapewa kiasi cha dola elfu hamsini itabidi nao wapate. Yaani elfu hamsini niigawe kwa watu watatu! Haiwezekani, hiyo inabidi iwe yangu peke yangu tena kama inawezekana subiri niwaambie wasije kabisa” Maxwell alisema.

    Kichwa chake kilikuwa kikifikiria fedha tu huku moyo wake ukiwa na tamaa ya fedha. Alikuwa akipenda sana fedha kiasi ambacho alikuwa tayari kufanya kitu chochote kwa ajili ya fedha. Ishu ya kumkamata Alan na kisha kumpeleka jijini Washington halikuonekana kuwa jambo jepesi, lilikuwa moja ya jambo ambalo alitakiwa kuwashirikisha watu wengine na ndio maana alikuwa amewatafuta Smith na Rogan kwa ajili ya kusaidiana katika kulifanya jambo lile.

    Fedha zikaonekana kuharibu kila kitu, mpango ambao alikuwa ameupanga na wenzake ukaonekana kutokuwa mzuri. Alihitaji fedha, fedha zote ambazo angepewa na Bwana Kurt alitaka ziwe peke yake na wala hakutaka kuzigawanya kwa watu wengine, hapo ndipo alipoamua kuwapigia simu Smith na Rogan na kisha kuwaambia kwamba ishu ile ya kumtafuta Alan ilikuwa imekufa kwani alikuwa amekwirudi jijini Washington.

    Baada ya kuwapa taarifa ile, hapo ndipo alipojisikia vizuri, moyoni akajiona mshindi kwa kuona kwamba fedha ambazo angepatiwa na Bwana Kurt zingekuwa zake peke yake na wala asingeweza kuzigawanya kwa watu wengine. Wakati mwingine aliona suala la kumpata Alan wala halikuwa gumu sana kwani kama dereva teksi, Marcus angepatikana na kisha kumwambia hoteli ambayo Alan alikwenda wala kusingekuwa na tatizo lolote lile, angmkamata Alan na kisha kumpeleka Washington bila wasiwasi wowote ule.

    “Ila hakuna tatizo. Alan atapatikana tu” Maxwell alisema na kisha kulala.

    *****

    Mtu huyu alikuwa mlevi kupindukia, alikuwa akinywa pombe za kila aina ambazo zilikuwa na ulevi mkubwa. Macho yake yalikuwa makubwa, uso wake ulikuwa ukionyesha kwamba alikuwa na miaka zaidi ya hamsini na wakati ukweli ni kwamba alikuwa na miaka arobaini tu. Maisha yake yalitawaliwa na ulevi uliopindukia pamoja na uchezaji mkubwa wa kamari.

    Katika maisha yake kila fedha ambayo alikuwa akiipata alikuwa akiitumia katika kunywa pombe pamoja na kucheza kamari ambazo moja kwa moja zilikuwa zikimfanya kusafiri kuelekea katika jimbo la Nevada ndani ya jiji la Las Vegas kwa ajili ya kucheza kamari tu. Kamari pamoja na pombe ndivyo vilikuwa vitu viwili ambavyo vilimtawala maisha yake, kila msahara ambao alikuwa akiupokea alikuwa akiutumia katika kamari na kunywa pombe tu, huyu alikuwa Michael Maxwell, mzee aliyekuwa na umri wa miaka arobaini.

    Maxwell alifanikiwa kuoa miaka kumi iliyopita, alimuoa msichana mzuri aliyekuwa na asili ya Mexico, Jacelyn. Maxwell alikuwa akimpenda sana mke wake, alikuwa akimthamini sana na kumuona kuwa miongoni mwa wanawake wazuri sana ambao alikuwa amekutana nao katika maisha yake. Alimpa kila kitu na kumuonyeshea mapenzi ya dhati.

    Ndoa yao ilidumu kwa muda wa miaka mitano tu, wakaachana huku wakiwa wamepata watoto wawili. Unywaji mkubwa wa pombe pamoja na uchezaji wa kamari ndio ambao ulikuwa umevunja ndoa yao. Jacelyn alimshauri sana mumewe kuachana na pombe pamoja na uchezaji kamari lakini Maxwell hakutaka kusikia, kila siku alikuwa mtu wa kunywa pombe huku kila mwisho wa mwezi akiwa anasafiri kuelekea Las Vegas kucheza kamari tu.

    Hivyo ndivyo vilikuwa vitu viwili ambavyo vilikuwa damuni mwake na alikuwa akivithamini hata zaidi ya alivyokuwa akimthamini mke wake. Tabia yake iliendelea hivyo hivyo hata mara baada ya kuachana na mkewe hakuweza kuiacha. Japokuwa alikuwa akifanya vitu hivyo vyote lakini Maxwell alikuwa mchapakazi mkubwa sana. Alikuwa akifanya sana kazi kila alipokuwa ofisini kitu ambacho kilimfanya kupandishwa vyeo mpaka kufikia cheo cha mwisho kabisa katika ngazi ya upolisi jijini Texas, akawa mkuu wa kituo cha polisi hapo Texas.

    Matukio ya kamari pamoja na unywaji wa pombe hayakuisha, hakuiacha tabia yake. Alikuwa akiendelea kunywa pombe na kucheza kamari kama kawaida. Kila fedha ambayo alikuwa akiipata alikuwa akiitumia katika uchezaji kamari ambao kwake aliuona kuwa wa thamani sana. Kichwa chake kilikuwa kikifikiria sana fedha na ndio maana alikuwa tayari kufanya lolote lile ili mradi apate fedha zitakazomuwezesha kunywa pombe na kucheza kamari kama kawaida yake.

    “Nitaacha kunywa pombe endapo mashamba yote ya ngano duniani yataunguzwa au Mmarekani yeyote ambaye ni mwanamasumbwi wa uzito wa juu atapigana pambano lake ndani ya nchi ya Marekani nje ya hoteli ya MGM Grand, tofauti na hapo, pombe sitoacha” Maxwell alisema huku akiziangalia chupa kadhaa ambazo zilikuwa ndani ya friji yake ambayo alikuwa ameifungua, aliziangalia kwa zamu huku kichwa chake kikijiuliza ni pombe ipi ambayo alitakiwa kunywa.









    Saa moja na nusu asubuhi Bwana Maxwell alikuwa amekwishampigia simu Christopher ambaye alifika katika kituo hicho kwa ajili ya kwenda uwanja wa ndege kumtafuta Marcus ambaye huyo ndiye angewaambia mahali ambapo Alan alikuwepo katika kipindi hicho. Siku hiyo Maxwell hakutaka kufanya kazi na watu wake, Smith na Rogan, alikuwa akitaka kufanya kazi peke yake kwa kuamini kwamba endapo angefanikiwa kumpeleka Alan nchini Marekani basi angepewa kiasi kikubwa cha fedha na hivyo chote kingekuwa chake, asingegawana na mtu yeyote yule.

    Hivyo ndivyo alivyotaka, mara baada ya Christopher kufika katika kituo hicho cha Dallas, moja kwa moja wakaanza kuondoka kuelekea katika uwanja wa ndege wa King County kwa ajili ya kuonana na Marcus. Hawakuchukua muda mrefu wakawa wamekwishafika mahali hapo, wakaambiwa wasubiri kwani muda wowote ule Marcus angeweza kufika mahali hapo na hivyo kuelekea katika sehemu ambayo Alan alikuwepo katika kipindi hicho.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Saa mbili kasoro dakika kumi asubuhi Marcus akawa amekwishafika mahali hapo. Kitendo cha kuiona teksi tu Christopher alikuwa amekwishaitambua hivyo akamuonyeshea Bwana Maxwell na kuanza kuifuta. Iliposimama, Marcus akateremka, kichwani alikuwa na rasta nyingi kama kawaida yake.

    “Where do you wanna to go? (Mnataka kwenda wapi?)” Marcus aliwauliza.

    “Nowhere. I want to ask you questions (Hatuendi popote. Ninataka kukuuliza maswali)” Bwana Maxwell alimwambia Marcus ambaye akaufunga mlango wa gari lake na kisha kuliegemea.

    “About what? (Kuhusu nini?)”

    “I am police officer from DPD, Dallas Police Department (Mimi ni polisi kutoka DPD, Dallas Police Department)” Bwana Maxwell alijitambulisha huku akitoa kitambulisho chake na kumuonyeshea Marcus.

    “What can I help you officer? (Nikusaidie nini ofisa?)” Marcus alimuuliza Bwana Maxwell.

    “I am looking for someone (Kuna mtu ninamtafuta)”

    “Who is he (Ni nani?)

    “Alan” Bwana Maxwell alimjibu Marcus.

    Muda wote Marcus alikuwa akimwangalia Bwana Maxwell usoni tu, uso wake ulikuwa unaonyesha ni kwa jinsi gani alivyokuwa mlevi, alionekana kuwa kama mtu goigoi kutokana na unywaji mkubwa wa pombe lakini ukweli ni kwamba Bwana Maxwell alikuwa shupavu, alikuwa na nguvu nyingi sana.

    Bwana Maxwell hakuishia hapo, aliendelea kumuelezea Marcus juu ya mtu ambaye alikuwa akimtafuta, Alan. Katika kipindi cha kwanza marcus hakuonekana kumfahamu Alan lakini mara baada ya Christopher kuingilia na kumkumbusha kuhusiana na Alan, hapo ndipo Marcus alipoonekana kukumbuka.

    “Nimekwishamkumbuka” Marcus aliwaambia.

    “Yupo wapi?”

    “Nilimpeleka hotelini”

    “Wapi? Hapa Dallas, Houston au Austin?” Bwana Maxwell alimuuliza Marcus juu ya mji ambao alikuwepo Alan katika kipindi hicho.

    “Hapa hapa Dallas katika hoteli ya Cowboys Stars ”

    “Tunaomba utupeleke” Bwana Maxwell alimwambia Marcus.

    Marcus hakutaka kubisha, kwa sababu watu ambao walikuwa mbele yao mmojawapo alikuwa polisi wala hakuonekana kusita, alichokifanya ni kuwataka kuingia ndani ya gari na kisha kuondoka mahali hapo. Ndani ya gari Maxwell alikuwa akiendelea kuuliza maswali mfululizo kuhusiana na Alan, alikuwa akitaka kupata uhakika hasa kwamba huyu Alan ambaye walikuwa wakimfuata hotelini alikuwa ndiye yule Alan ambaye wanamtafuta au alikuwa mwingine.

    “Ndiye mwenyewe. Kama ndiye yule aliyekuja na huyo kijana, ndiye mwenyewe” Marcus alimwambia Bwana Maxwell.

    Saa mbili na robo wakawa wanaingia ndani ya hoteli hiyo, kwa haraka sana bila kupoteza muda wowote ule Bwana Maxwell akateremka kutoka katika gari na kisha kuelekea ndani ya hoteli ile huku akiwa pamoja na Christopher. Walipofika mapokezini, kitu cha kwanza alichokifanya Bwana Maxwell ni kutoa kitambulisho chake na kumuonyeshea dada wa mapokezi ambaye akaonekana kushtuka.

    “Kuna mtu namtafuta” Bwana Maxwell alimwambia dada wa mapokezi.

    “Nani?”

    “Alan Kurt” Bwana Maxwell alimwambia msichana yule. Alichokifanya msichana yule wa pale mapokezini ni kuiangalia monitor ya kompyuta yake na baada ya sekunde chache akayarudisha macho yake usoni mwa Bwana Maxwell.

    “Ameondoka nusu saa ilizopita” Msichana yule alimwambia Bwana Maxwell.

    “Amekwenda wapi?”

    “Sijui kwani hapa inaonyesha kwamba alichukua chumba kwa usiku mmoja tu” Msichana yule alimwambia Bwana Maxwell ambaye akaonekana kuchanganyikiwa.

    “Amekwenda Mexico?” Bwana Maxwell aliuliza huku akionekana kuchanganyikiwa.

    “Sifahamu”

    “Sawa” Bwana Maxwell alisema na kisha kutoka ndani ya jengo la hoteli ile.

    Hapo hakukuwa na muda wa kupoteza, tayari alikwishaona kwamba endapo asingefanya kitu cha ziada basi angeweza kumkosa Alan na hivyo kukosa kiasi cha fedha ambacho alikuwa amehisi kwamba angepatiwa. Wakatoka nje na kisha kuingia ndani ya teksi ile.

    “Tuondoke” Bwana Maxwell alimwambia Marcus.

    “Kwenda wapi?”

    “Fort Worth” Bwana Maxwell alimjibu Marcus.

    Marcus hakuonekana kuwa na wasiwasi, kwa sababu alikuwa akimuendesha polisi sehemu yoyote ile aliyokuwa akitaka, wala hakuwa na mashaka kuhusiana na malipo kwani alijua fika kwamba angelipwa sawasawa na mizunguko yake endapo angekwenda katika kituo kikubwa cha polisi cha hapo Dallas, Texas na kisha kuelezea kila kilichotokea huku Maxwel akitoa taarifa simuni.

    Marcus akaliingiza gari katika barabara ndefu ya 1-30 Fontage ambayo ilikuwa ikielekea moja kwa moja kuingia katika mji wa Aarlington kabla ya kuingia Fort Worth, Magharibi mwa jiji kubwa la Dallas. Kwa sababu Bwana Maxwell alionekana kuwa na haraka, Marcus akaingia katika barabara ya magari yaendayo kasi ambayo ilikuwa na sheria ya kuendesha gari kwa mwendokasi kuanzia mia moja na kuendelea.

    Marcus akibadilisha gia zaidi tu, gari lilikuwa likikimbia kwa mwendo wa kasi sana huku lengo lao likiwa ni kufika Fort Worth mapema zaidi. Muda wote Bwana Maxwell alikuwa akiangalia huku na kule, kila gari ambalo walikuwa wakilipita alikuwa akiliangalia kwa ndani kuona kama angeweza kumuona Alan na hivyo kuliamrisha gari alilokuwepo lisimame.

    Safari ya kuelekea Fort Worth ilikuwa ikiendelea kama kawaida mpaka pale ambapo Bwana Maxwell akaanza kufikiria kitu kimoja ambacho kingekuwa muhimu sana endapo angekifanyia kazi. Hakutaka kufanya kazi isiyokuwa na faida, alijua fika kwamba kuonekana kwa Alan lilikuwa suala gumu sana endapo asingefanya kitu kingine cha ziada. Hakujua kama Alan alikuwa amepanda basi kuelekea mpakani au la, endapo angeendelea kufuatilia kwa kubahatisha basi asingeweza kufanikisha kile ambacho alikuwa amekipanga.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Nipe namba ya Alan” Bwana Maxwell alimwambia Christopher.

    Christopher hakuwa na kipingamizi chochote kile, akachukua simu yake, akaitafuta namba ya Alan na kisha kumpa Bwana Maxwell ambaye akaichukua na kuanza kuipiga kwa kutumia simu yake ya mkononi. Simu ya Alan ikaanza kuita, iliita kwa sekunde fulani, ikapokelewa na sauti ya Alan kuanza kusikika upande wa pili.

    “Naongea na nani?” Sauti ya Alan ilisikika ikiuliza swali.

    “Unaongea na Maxwell. Polisi kutoka katika kituo cha polisi cha hapa Dallas” Maxwell alimjibu Alan.

    “Nikusaidie nini afisa?”

    “Nahitaji kukuona”

    “Itakuwa ngumu kwa sasa”

    “Nahitaji kukuona Alan. Nina mengi ya kuongea nawe”

    “Nadhani unataka kuongea nami kuhusiana na safari yangu, si ndio?” Alan alimwambia Bwana Maxwell na kisha kumuuliza.

    “Hapana”

    “Basi subiri nikirudi utaniona” Alan alimwambia Bwana Maxwell.

    “Nisikilize Alan. Unaelekea mpakani kuingia Mexico, unafikiri utapita vipi hapo mpakani? Unafikiri utaweza kuvuka bila ya kuwa na kibali?” Bwana Maxwell alimuuliza Alan.

    “Nitapita tu”

    “Sidhani. Ila nafikiri unahitaji msaada wangu kama polisi” Bwana Maxwell alimwambia Alan.

    “Sidhani kama una umuhimu sana”

    “Niamini. Unahitaji msaada wangu. Nataka kukusaidia kuvuka kama utakuwa tayari” Bwana Maxwell alimwambia Alan.

    “Nitakuamini vipi?”

    “Ninapokwambia kwamba mimi ni polisi, unaniamini au hauniamini?” Maxwell alimuuliza Alan.

    “Nakuamini”

    “Sasa kama umeweza kuniamini katika hilo kwa nini usiniamini katika hili?”

    “Kwa hiyo wewe ni polisi?”

    “Ndio”

    “Sawa. Ila usijaribu kuniambia kukatisha safari yangu” Alan alimwambia Bwana Maxwell.

    “Sawa. Usijali. Upo wapi?”

    “Nimefika Fort Worth” Alan alimjibu, mji ambao ulikuwa ni njia kuu ya kuelekea katika mpaka wa Nuevo Laredo.

    “Naomba uteremke hapo na nikukute hapo” Bwana Maxwell alimwambia Alan.

    “Sawa” Alan aliitikia.

    Hiyo ikaonekana kuwa nafuu kwa Bwana Maxwell, uongo ambao alikuwa amemwambia Alan kwamba alitaka kuongea nae na kumsaidia kuvuka katika mpaka wa Nuevo Laredo kuingia nchini Mexico na si kumzuia ukaonekana kukubalika kwa Alan. Huo ndio ujanja ambao ulionekana kufaa katika kipindi hicho, alijua kwamba endapo angekutana na Alan na kisha kumuonyeshea bunduki wala Alan asingeweza kuleta jeuri kabisa.

    Walichukua saa moja mpaka kufika Fort Worth ambapo hapo Bwana Maxwell akamtaka Marcus kusimamisha gari. Moja kwa moja akateremka na kuanza kuangalia huku na kule. Alijaribu kumtafuta Alan mahali hapo, aliamini kwamba angeweza kumuona.

    “Yupo wapi?” Bwana Maxwell alijiuliza.

    Alichokiona kufaa kufanywa ni kumruhusu Marcus kuondoka mahali hapo pamoja na Christopher kuelekea Dallas huku yeye akitaka kubaki kumtafuta Alan mahali hapo. Christopher akaonekana kumshangaa, walikuja wote mahali pale kwa ajili ya Alan sasa ilikuwaje yeye aondoke na kisha kumuacha mahali pale? Je endapo Bwana Kurt angempigia simu angemjibu nini?

    “Mbona unaniambia niondoke sasa?” Christopher alimuuliza Bwana Maxwell.

    “Kazi iliyobakia ni ya kipolisi zaidi” Bwana Maxwell alijibu.

    “Lakini si tumekuja wote?”

    “Najua. Wewe ni polisi?” Bwana Maxwell alimuuliza Christopher.

    “Hapana”

    “Ndio maana nakwambia rudi Dallas. Acha nianze kufanya kazi ya kipolisi” Bwana Maxwell alimwambia Christopher ambaye bila ubishi wowote ule akaingia garini.

    “Sasa Bwana Kurt akiniuliza nimwambie nini?”

    “Mwambie yote aniachie mimi, leo hii hii Alan atafika Washington” Bwana Maxwell alimwambia Christopher.

    “Sawa” Christopher aliitikia na Marcus kuwasha gari na kuondoka mahali hapo.

    Bwana Maxwell alipoona anaangalia huku na kule lakini hakuweza kumuona Alan mahali yoyote ile akaamua kuichukua simu yake na kisha kumpigia simu Alan. Simu ikaanza kuita na wala haikuita muda mrefu ikapokelewa na sauti ya Alan kusikika upande wa pili.

    “Upo wapi?”

    “Fort Worth”

    “Nimekwishafika. Wewe upo wapi?”

    “Nipo katika kituo cha mafuta cha Total ndani ya maduka yao ya vyakula na vinywaji” Alan alijibu.

    “Nakuja”

    Kwa haraka bila kupoteza muda wowote ule Bwana Maxwell akaanza kuelekea katika sehemu ambayo ilikuwa na kituo cha mafuta cha Total ambapo alitumia mwendo wa dakika kumi na tano kutokana na umbali uliokuwepo na kisha kuingia ndani ya supamaketi. Kabla hajaendelea mbele zaidi, akapita katika sehemu ya ukaguzi ambapo akakaguliwa na kukutwa na bunduki, akatoa kitambulisho chake kilichomtambulisha kwamba alikuwa polisi lakini akaambiwa aiache bunduki mahali pale, akaiacha. Macho yake yalikuwa yakiangalia huku na kule kumtafuta Alan. Alipomuona, akaanza kumfuata.

    “Unahitajika jijini Washington” Bwana Maxwell alimwambia Alan mara baada ya kumfikia.

    “Haiwezekani kurudi huko kwa sasa” Alan alimwambia Bwana Maxwell.

    “Nimepigiwa simu na baba yako, anakuhitaji. Hataki uende nchini Mexico” Bwana Maxwell alimwambia Alan.

    “Kwa sababu gani?”

    “Sijui”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Haiwezekani. Ninakwenda Mexico. Hakuna wa kunizuia. Yeye hawezi kunizuia na hata wewe hauwezi kunizuia” Alan alimwambia Bwana Maxwell.

    “Utakwenda tu. Ni lazima utakwenda Washington” Bwana Maxwell alimwambia Alan ambaye kwa mbali alionekana kuhofia, kwa muonekano, Bwana Maxwell alionekana kumaanisha huku uso wake ukionekana kumuogopesha Alan.

    “Hapana”

    Bwana Maxwell hakutaka kubaki mbele ya Alan, alichokifanya ni kupiga hatua mpaka katika sehemu ile ambayo aliambiwa aiache bunduki yake na kisha kuitaka, akakabidhiwa na kisha kuanza kumrudia Alan, hakutaka kuificha, alikuwa ameishika mkononi huku akiikoki hali ambayo ilionekana kumuogopesha sana Alan, alijua fika kwamba endapo asingefanya kitu basi angerudishwa jijini Washington.

    “Unategemea nini kutoka kwa baba mara baada ya kunipeleka Washington?” Alan alimuuliza Bwana Maxwell.

    “Sijajua. Ila nimepewa amri ya kukurudisha. Hilo tu” Bwana Maxwell alimwambia Alan.

    “Sawa. Baba anataka unirudishe Washington na kisha hautegemei kupata kitu chochote kutoka kwake, na vipi nikikwambia unifikishe Mexico na kisha kukupa dola elfu thelathini. Dola elfu kumi na tano kunifanikisha kuingia nchini Mexico na dola elfu kumi na tano kunirudisha mahali hapa?” Alan alimuuliza Bwana Maxwell ambaye alibaki kimya kwa muda.

    “Haiwezekani, lazima urudi Washington”

    “Sawa. Hakuna tatizo. Nimekupa ofa umekataa huku ukiivunja ahadi uliyonipa. Hakuna tatizo, unanirudisha Washington halafu nitakwenda Mexico kwa ndege, utakuwa umefanya kazi ya bure isiyokuwa na malipo. Nimekubali, twende Washington” Alan alimwambia Bwana Maxwell.

    Maneno ya mwisho aliyoyaongea Alan yakaonekana kumuingia sana Bwana Maxwell. Ni kweli kwamba alikuwa katika harakati za kumrudisha Alan jijini Washington lakini Bwana Kurt angeweza kumlipa kiasi chochote cha fedha endapo angemfikisha? Japokuwa kichwani mwake alikuwa akifikiria kwamba Bwana Kurt angeweza kumlipa lakini kwa upande wa pili uhakika huo ukaanza kumtoka.

    Alan tayari alikuwa amekwishatangaza dau lake endapo angeweza kufikishwa nchini Mexico, kiasi kikubwa cha fedha ambacho kwa mshahara wake basi angefanya kazi kwa miaka miwili ndipo apokee kiasi hicho cha fedha. Fedha ambazo alikuwa ameziweka Alan mezani zikaanza kumuingia akilini, akaanza kufikiria pombe na kamari.

    “Hebu subiri kwanza” Bwana Maxwell alimwambia Alan kabla ya kutoka ndani ya supermarket.

    “Kuna nini?”

    “Kweli utanipa hizo fedha nikusaidie kuingia nchini mexico?”

    “Siwezi kukudanganya na siwezi kuivunja ahadi yangu kama unavyotaka kuivunja ahadi ambayo umenipa” Alan alimwambia Bwana Maxwell.

    “Sawa. Nitakusaidia kuelekea nchini Mexico. Fedha zenyewe zipo wapi?” Bwana Maxwell alimuuliza Alan, tayari alionekana kuchanganyikiwa juu ya fedha ambazo alikuwa ameahidiwa, fedha ambazo kwa thamani ya fedha za kitanzania zilikuwa ni zaidi ya milioni ishirini na saba kwenda na milioni ishirini na saba kurudi.

    “Twende kwenye ATM. Ila nihakikishie, nitafika nchini Mexico?” Alan alimuuliza Bwana Maxwell.

    “Hilo hakuna tatizo. Yaani hakuna tatizo. Wewe twende kwanza kuzitoa hizo hela” Bwana Maxwell alimwambia Alan.

    “Sawa. Ila nitaanza na dola elfu kumi na tano kama tulivyoahidiana”

    “Hakuna tatizo” Bwana Maxwell alimwambia Alan.

    “Sawa”

    “Nachukua pombe hapa, kama chupa tano, utalipia, utakata katika fedha zangu hizo” Bwana Kurt alimwambia Alan.

    “Hakuna tatizo. Chukua tu na sitokata katika fedha nitakayokupa” Alan alimwambia Bwana Maxwell.

    Macho yalikuwa yakimtoka Bwana Maxwell. Kila alipokuwa akipiga jicho huku na kule na kuzikuta chupa za pombe kali mbalilimbali uroho wa kutaka kunywa pombe zile ulikuwa ukimshika. Ulevi ulikuwa umemtawala kupita kawaida, pombe zile ambazo alikuwa akiziangalia ndizo ambazo zilimfanya kukubaliana na Alan kumfikisha nchini Mexico kwani alikuwa na uhakika wa fedha hizo kuliko fedha za Bwana Kurt ambazo wala hakuwa na uhakika nazo.

    Akachukua chupa kubwa za pombe kali na kisha kuanza kuondoka. Alan akazilipia pombe zile. Hapo ilikuwa ni safari ya kueleka katika sehemu iliyokuwa na mashine ya ATM katika kituo hicho cha mafuta na kisha kutoa kiasi cha fedha ambacho alikuwa akikihitaji Bwana Maxwell na kuongeza dola elfu tano kwa ajili ya matumizi yake binafsi.

    “Kilichobaki ni mimi kuingia Mexico” Alan alimwambia Bwana Maxwell ambaye alikuwa akizihesabu fedha zile.

    “Hakuna tatizo. Twende” Bwana Maxwell alimwambia Alan, tayari fedha zile zilimfanya kuwa muaminifu kumfikisha Alan nchini Mexico.



    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    Asubuhi na mapema Bwana Kurt alikuwa ameamka. Siku hiyo hakutaka kwenda kazini, bado alikuwa akiisubiria simu kutoka kwa Bwana Maxwell ambaye alitarajia kumwambia juu ya kila kitu kilichokuwa kimeendelea Texas, Alan alikuwa amepatikana au la. Muda wote Bwana Kurt na mkewe, Bi Bertha walionekana kuwa wapole, kitendo alichokifanya Alan cha kuondoka kuelekea nchini Mexico kilionekana kuwakasirisha kupita kawaida.

    Muda ulizidi kwenda mbele zaidi na zaidi lakini hakukuwa na simu yoyote ile iliyotoka kwa Bwana Maxwell jambo ambalo lilionekana kuwakatisha tamaa kwa kuona kwamba inawezekana kulikuwa na kitu ambacho kilikuwa kimetokea huko. Muda ulizidi kusogea kama kawaida, walizidi kuisikilizia simu kutoka kwa Bwana Maxwell lakini bado hali ilikuwa kimya kabisa.

    Ilipofika saa nne asubuhi hapo ndipo Bwana Kurt akapata wazo, wazo moja ambalo aliliona ingekuwa vyema endapo angelifanyia kazi. Mtu ambaye alikuwa amekuja kichwani mwake kwa wakati huo alikuwa Christopher. Bwana Kurt alijua fika kwamba kama angemuuliza Christospher juu ya kilichokuwa kimetokea Texas basi angekuwa na chochote cha kumwambia.

    “Unasemaje?” Bwana Kurt alimuuliza Christopher simuni.

    “Nilikwenda nae mpaka Fort Worth” Christopher alimwambia Bwana Kurt.

    “Ikawaje baada ya hapo?” Bwana Kurt alimuuliza.

    “Aliniambia nirudi”

    “Kwa sababu gani?”

    “Kwa sababu sikuwa polisi kwani alitaka kufanya kazi ya kipolisi” Christopher alimwambia Bwana Kurt.

    “Ila amemuona Alan?”

    “Sijajua. Niliondoka kabla ya kumuona Alan” Chrirtopher alimwambia Bwana Kurt ambaye alionekana kuchanganyikiwa.

    “Upo wapi kwa sasa?”

    “Ndio nimeingia ndani ya ndege najiandaa kuja huko” Christopher alimwambia Bwana Kurt.

    “Kwa hiyo Bwana Maxwell anajua kila kitu?”

    “Ndio”

    “Sawa. Asante” Bwana Kurt alimwambia Christopher na kisha kukata simu.

    Kilichofuata ni kuanza kumtafuta Bwana Maxwell simuni. Alijaribu kupiga namba yake ya simu lakini simu haikuwa ikipatikana, kila alipokuwa akipiga aliambiwa kwamba alitakiwa kuacha ujumbe kwa mwenye simu. Hali ile ikaonekana kumkasirisha sana, mtu ambaye alikuwa akimuamini kwa asilimia mia moja kwamba angeweza kufanya kazi alikuwa Bwana Maxwell tu ambaye katika kipindi hicho wala hakuwa akipatikana simuni.

    Hakujua afanye nini kwa wakati huo, hali ilionekana kuchanganya zaidi hasa mara baada ya kumpigia simu Alan nae kutokupatikana. Maswali kibao yakaanza kumiminika kichwani mwake kama Alan alikuwa amekwishaanza safari kuelekea nchini Mexico au la, na kama alikuwa amekwishaanza alikuwa peke yake au na Bwana Maxwell. Katika kila swali ambalo alikuwa akijiuliza mahali hapo lilionekana kutokuwa na jibu kabisa.

    “Hivi inakuwaje?” Bwana Kurt alimuuliza mke wake, Bertha.

    “Kivipi?”

    “Yaani mtu umepanga nae kitu, unampigia simu halafu hapatikani. Sasa mimi nielewe nini?” Bwana Kurt alimwambia mkewe na kumalizia na swali.

    “Na Alan vipi?”

    “Huyo ndiye hapatikani toka jana”

    “Alan....yupo wapi mtoto wangu” Bi Bertha aliuliza huku machozi yakianza kumtoka, tayari alionekana kuogopa, mawazo yakaanza kumjia kichwani kwamba Alan alikuwa amekwishatekwa na mzee Sanchez.

    Alichokifanya Bwana Kurt ni kupiga simu katika kituo kikuu cha polisi cha Dallas hapo jijini Texas kwa ajili ya kupata taarifa zote kama Bwana Maxwell alikuwa ameonekana siku hiyo au la. Simu ikaanza kuita ndani ya kituo hicho, iliiita kwa sekunde chache, polisi mmoja akaipokea na kuanza kuongea nae.

    “Naomba uionganishe simu yangu mpaka kwa mkuu wenu, Bwana Maxwell” Bwana Kurt alimwambia polisi yule.

    “Naongea na nani?”

    “Bwana Kurt hapa”

    “Mkuu hayupo ofisini kwake” Polisi yule alimwambia.

    “Yupo wapi?”

    “Sijajua. Toka nimekuja sikumkuta au kama alikuja na kuondoka kabla ya mimi kuingia hapa” Polisi yule alimjibu Bwana Kurt, jibu ambalo lilimchanganya zaidi.

    Bwana Kurt akakata simu yake, alionekana kuchanganyikiwa zaidi, kila kitu ambacho kilikuwa kikiendelea mahali hapo kilionekana kumchanganya kupita kawaida. Alichokuwa akitaka kujua kwa wakati huo ni kwamba mtoto wake, Alan alikuwa wapi. Mtu ambaye alikuwa akimuamini kwamba angeweza kufanya kile ambacho alikuwa akikitaka cha kumpeleka Alan jijini Washington ndiye ambaye alikuwa amebadilika na kufanya mambo aliyokuwa akiyajua yeye.

    Uamuzi ambao alikuwa ameufikia ni kuchukua tena simu yake na kupiga katika kituo kikuu cha polisi cha jiji la Austin, moja la jiji ambalo lilikuwa likipatikana katika jimbo la Texas. Simu ilianza kuita, iliita kwa sekunde kadhaa na mtu wa upande wa pili kuipokea na kuanza kuongea nae.

    “Unaongea na mkuu wa kituo cha polisi jijini Austin” Sauti ya upande wa pili ilisikika mara baada ya simu kuunganishwa mpaka katika ofisi ya mkuu wa kituo hicho.

    “Kuna kitu nataka unisaidie” Bwana Kurt alimwambia mkuu wa kituo hicho, Bwana Powell.

    “Kitu gani?”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Mtoto wangu yupo Texas kwa sasa” Bwana Kurt alimwambia Bwana Powell.

    “Mtoto yupi? Wewe ni nani?”

    “Mimi ni Bwana Kurt, mmiliki wa McLloyd” Bwana Kurt alijibu.

    “Unamaanisha Alan?”

    “Ndio”

    “Unataka tufanye nini?”

    “Nataka mumlete huku Washington”

    “Kwani amefanya nini?”

    “Naomba mumlete Washington kwanza”

    “Yupo wapi kwa sasa?”

    “Yupo huko Texas”

    “Sawa. Jiji gani?”

    “Dallas”

    “Hakuna tatizo, utasaidiwa katika hilo. Ila ningeomba uwasiliane na Bwana Maxwell kwani yeye ndiye mhusika huko” Bwana Powell alimwambia Bwana Kurt.

    “Nimefanya hivyo kabla lakini sijaona mafanikio yoyote yale, nampigia simu hapatikani, naomba unisaidie katika hilo” Bwana Kurt alimwambia Bwana Powell.

    “Sawa. Nitajitahidi”

    “Hakuna tatizo. Ila ataweza kupatikana?”

    “Bila shaka” Bwana Powell alijibu na kukata simu.

    Bwana Kurt akashusha pumzi ndefu, moyo wake akautoa kwa Bwana Maxwell na kuanza kumuamini Bwana Powell kwamba angeweza kumsaidia katika kila hatua. Japokuwa alikuwa na uhakika wa kusaidiwa na Bwana Powell lakini hakukoma kuendelea kumtafuta Bwana Maxwell na Alan ambao bado hawakuwa wakipatikana simuni.

    “Mpaka mchana kila kitu kikiwa kimya, nitaelekea Texas mwenyewe” Bwana Kurt alimwambia mke wake, Bi Bertha.

    “Na mimi ninataka kwenda huko”

    “Wewe baki mke wangu, huko ni kazi ya kiume ndio itakayokwenda kufanyika” Bwana Kurt alimwambia mke wake.

    “Hapana. Siwezi kubaki na wakati sifahamu mtoto wangu anaendeleaje huko” Bi Bertha alimwambia mume wake.

    Huo ndio uamuzi ambao Bwana Kurt alikuwa ameamua mahali hapo, hakutaka kuendelea kubaki Washington na wakati hakujua ni kitu gani kilikuwa kikiendelea kwa mtoto wake ambaye alikuwa Texas jijini Dallas. Kama kawaida muda ulikuwa ukizidi kusogea huku wote wawili wakionekana kuwa na presha kubwa, masikio yao yalikuwa yakisikilizia kila simu ambayo ilikuwa ikiingia. Ilipofika saa sita mchana, simu yake ikaanza kuita, alipoangalia namba, ilikuwa ngeni.

    “Naongea na nani?’ Bwana Kurt alimuuliza mpigaji mara baada ya kupokea simu ile.

    “Unaongea na Powell. Hii ndio namba yangu ya simu ya mkononi” Bwana Powell alijibu.

    “Umefikia wapi?”

    “Bado vijana wanaendelea. Tumejaribu kuulizia kila sehemu, tumeambiwa kwamba kuna mwanamke alimuona katika supermarket kule Fort Worth” Bwana Powell alimwambia Bwana Kurt.

    “Alikuwa peke yake?”

    “Hapana. Alikuwa na polisi. Anasema kwamba wawili hao walionekana kuwa kama marafiki” Bwana Powell alijibu.

    “Ikawaje baada ya hapo?”

    “Hatujajua ila waliondoka”

    “Walikwenda wapi?”

    “Hatufahamu”

    “Hivi kuna umbali gani kutoka Fort Worth mpaka mpakani Laredo?” Bwana Kurt aliuliza.

    “Zaidi ya kilometa elfu mbili mia tano. Mtoto wako anataka kwenda Mexico?” Bwana Powell aliuliza.

    “Hapana. Nilitaka kufahamu tu. Naomba muendelee kumtafuta” Bwana Kurt alimwambia Bwana Powell na kukata simu.

    Kitendo cha Alan kupanga safari ya kuelekea nchini Mexico alitaka kiwe siri, hakutaka kumwambia tena mtu mwingine kwani aliona endapo angefanya hivyo basi lingekuwa kosa kubwa kwani mzee Sanchez angeweza kupata taarifa na kuwatuma vijana wake wafanye kazi ya ziada ya kumfuatilia Alan, alichokuwa akikitaka ni kusafiri tu kuelekea Texas.

    “Kajiandae, ndani ya nusu saa tunaondoka kwenda Texas” Bwana Kurt alimwambia mke wake, Bi Bertha.

    “Mimi nipo tayari”

    “Sawa” Bwana Kurt alimwambia mke wake, hapo hapo akampigia simu rubani wake na kumwambia aandae ndege tayari kwa kuitumia ndani ya nusu saa kwa ajili ya safari ya kuelekea Texas.

    *****CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Malipo yalikuwa yamefanyika vya kutosha na wala Bwana Maxwell hakuonekana kupunjwa, kila fedha ambayo alikuwa ameahidiwa kulipwa kama malipo kabla ya kuingia ndani ya nchi ya Mexico yalikuwa yamefanyika na kilichokuwa kikisubiriwa kutoka kwake ni msaada wa kumsaidia Alan kuingia ndani ya nchi ya Mexico. Hilo wala halikuonekana kuwa tatizo kubwa kwa Bwana Maxwell, kwa sababu kila kitu kilikuwa kimekabidhiwa, alimhakikishia Alan kwamba ilikuwa ni lazima amfikishe nchini Mexico salama.

    Hawakutaka kukaa sana hapo Fort Worth, walichokifanya ni kuanza safari ya kuelekea mpakani Nuevo Laredo ambapo kulikuwa ni kusini mwa jimbo kubwa la Texas. Kila kitu kilipoonekana kukamilika, wakachukua basi ambalo lilikuwa likifanya safari kuelekea katika jiji la Austin.

    Bwana Maxwell na Alan walikuwa wamekaa katika viti vya nyuma kabisa. Kila mmoja alionekana kuwa kimya, walikuwa wakiifuatilia safari hiyo huku kila mtu kichwani mwake akiwa anafikiria kitu chake. Kichwani mwa Bwana Maxwell kulikuwa kukifikiria pombe pamoja na kamari. Chupa mbalimbali za pombe kali zilikuwa zikikumbukwa kichwani mwake, pombe nyingi za thamani ambazo hakuwa amewahi kuzinywa katika kipindi hicho ndicho kilikuwa kipindi maalumu cha kujiandika kichwani ili aweze kuzinunua katika kipindi ambacho angeteremka kutoka ndani ya basi lile.

    Katika mfuko wake mkubwa aliokuwa amepewa supermarket kulikuwa na chupa tano za pombe kali lakini kwake aliziona hizo kuwa pombe chache ambazo angeweza kuzimaliza ndani ya usiku mmoja tu. Alikuwa akihitaji pombe zaidi tena pombe kali ambazo zingemfanya kuchangamka na kuiona safari ile kuwa fupi.

    Kichwani mwa Alan kulikuwa kukifikiriwa vitu viwili tu. Kitu cha kwanza ambacho alikuwa akikifikiria sana ilikuwa ni hiyo safari ya kuelekea nchini Mexico. Maswali mengi yalikuwa yakizidi kumiminika kichwani mwake kwamba nini ilikuwa sababu ya baba yake kumzuia kuelekea nchini Mexico lakini hakupata jibu japokuwa katika kipindi cha nyuma alifikiri labda kwa sababu Mexico kulikuwa na wasichana warembo ambao wangemfanya kumuacha Stacie.

    Bado hilo halikuonekana kumridhisha, alikuwa akiendelea kujiuliza maswali zaidi lakini mwisho wa siku hakupata jibu lolote lile. Kitu cha pili ambacho kilikuwa kimekuja kichwani mwake kilikuwa ni maisha ya mahusiano yake pamoja na msichana mrembo ambaye alikuwa amemchagua kwa hiyari yake, Albertina ambaye alikuwa nchini Tanzania. Japokuwa alikuwa mzungu lakini kumpenda msichana mweusi na kutaka kumuoa hilo wala halikuonekana kuwa tatizo kwake. Alimpenda sana Albertina zaidi ya msichana yeyote yule na hiyo ndio sababu kubwa ambayo ilimfanya kumuacha Stacie.

    Kiu ya Alan katika kipindi hicho ilikuwa ni kuingia nchini Mexico ndani ya jiji la Monterrey. Alikuwa akitamani sana kumuona rafiki yake, Antonio ambaye hakuwa ameonana nae katika kipindi kirefu kilichopita. Alijiona kuwa na mengi ya kuongea pamoja na Antonio, alikuwa akitamani sana kumwambia kuhusiana na Albertina kwani bado Antonio alikuwa akimfahamu Stacie na wala hakuambiwa kuhusiana na Albertina.

    Alan hakufahamu kitu chochote ambacho kilikuwa kikiendelea kati ya baba yake na mzee Sanchez, hakuwa ameambiwa sababu ambayo ilimfanya kuzuiliwa kuingia nchini Mexico. Alikuwa aking’ang’ania sana kuingia nchini Mexico, sehemu ambayo ilionekana kuwa kama mdomo wa mamba, Alan alionekana kukifuata kifo chake mwenyewe.

    Safari bado ilikuwa ikiendelea. Bado kila mmoja alikuwa kimya. Hawakuongea toka kipindi kile ambacho waliingia ndani ya basi lile. Tayari lilikuwa limepita saa moja na ndio kwanza walikuwa wakiingia Waco. Walipofika hapo ndipo ambapo Bwana Maxwell akachukua mzinga mmoja wa pombe zile alizokuwa amenunua katika ile supermarket iliyokuwa Fort Worth na kisha kuanza kunywa.

    Hapo ndipo ambapo alijisikia kuwa katika hali nzuri. Alijua fika kwamba safari ile ilikuwa ndefu sana na bila kuwa na pombe za kumpa kampani basi angejisikia kuchoka sana. Pombe ndio ilionekana kuwa kampani yake kubwa kuliko Alan. Aliendelea kunywa, basi likaondoka mahali hapo na kisha kuanza kuutafuta mji wa Belton.

    Masaa yaliendelea kukatika zaidi na zaidi. Kutoka Waco mpaka Belton kwa basi la kawaida hutumia zaidi ya masaa matatu kutokana na umbali mkubwa uliokuwepo. Hapo ndipo ambapo safari hiyo ilivoonekana kuchossha zaidi. Bwana Maxwell hakuonekana kuwa na wasiwasi wala kuchoka, pombe ambazo alikuwa akiendelea kunywa zilikuwa zikimpa kampani ya kutosha kabisa.

    “Tutavukaje tukifika mpakani?” Alan aliuliza swali baada ya muda mrefu kuwa kimya.

    “Unaongea na mimi?” Bwana Maxwell aliuliza.

    “Ndio”

    “Umesemaje?”

    “Tutavukaje mpakani?”

    “Tutavuka kawaida tu”

    “Kawaida? Kivipi?”

    “Kawaida kama watu wengine”

    “Hivi unajua kwamba sina kibali chochote hapa?”

    “Unamaanisha nini?”

    “Sina passport”

    “Acha utani. Mbona haukuniambia kabla?”

    “Ningekwambia nini sasa, wewe si umeniambia nitavuka kwa urahisi kabisa?”

    “Sasa bila passport?”

    “Kwa hiyo haitowezekana?”

    “Nafikiri”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Basi nipe fedha zangu kama haitowezekana” Alan alimwambia Bwana Maxwell ambaye akaonekana kushtuka.

    “Subiri kwanza. Huko unakwenda mbali sasa. Utavuka tu”

    “Tutavukaje?”

    “Fedha zitatumika”

    “Fedha hizi nilizokupa?”

    “Yeah! Ila kama hazitotosha itakubidi uongeze”

    “Hakuna tatizo. Ninachotaka ni kuvuka tu mpkani” Alan alimwambia Bwana Maxwell.

    Safari iliendelea zaidi na zaidi. Baada ya masaa nane ndipo wakafanikiwa kuingia Austin huku tayari ikiwa imetimia saa moja usiku. Hawakutaka kuendelea na safari, walichokifanya ni kuchukua vyumba viwili katika moja ya hoteli ya Pasific ambazo zilikuwa zikipatikana sana hapo Texas. Wakapata muda wa kupumzika lakini kwa Bwana Maxwell haikuwa hivyo, kwa sababu hoteli hiyo ilikuwa na Cassino, kama kawaida yake akaelekea huko. Hakwenda huko kwa sababu alikuwa akitaka kuwaona wanawake waliokuwa wakicheza utupu kweye vyuma, alikuwa amekwenda huko kwa ajili ya kucheza kamari tu, ungemwambia nini na wakati alikuwa na dora elfu kumi na tano mfukoni?

    “Nimekuja kuzifuata fedha zangu mlizonishikia hata kabla sijaelekea San Antonio kesho” Bwana Maxwell aliwatishia wacheza kamari ambao walikuwa wamezunguka meza, mchezo wa karata ambao ulikuwa ukijulikana kwa jina la Poker kwenye cassino zote za kimataifa duniani.







    Bwana Kurt pamoja na mkewe, Bi Bertha wakaingia jimboni Texas ndani ya jiji la Dallas. Walionekana kuchanganyikiwa sana, kitendo alichokifanya kijana wao, Alan kilionekana kuwakasirisha kupita kawaida. Muda mwingi walionekana kuwa na mawazo, vichwa vyao vilikuwa vikimfikiria Alan huku wakiendelea kumuomba Mungu aweze kumuepushia kwa kila kitu kibaya ambacho kingeweza kumtokea nchini Mexico, sehemu ambayo alikuwa akikimbilia kwa wakati huo.

    Walipoteremka ndani ya ndege, moja kwa moja wakaelekea hotelini na kisha kutulia. Bado Alan hakuwa akipatikana simuni jambo ambalo liliendelea kuwatia sana wasiwasi. Alichokifanya Bwana Kurt ni kuanza kumtafuta Bwana Maxwell kwa kuona kwamba kulikuwa na uwezekano wa mzee huyo kupatikana na kisha kumuuliza kuhusu kijana wake lakini hata na yeye pia wala hakuwa akipatikana simuni.

    Moyoni mwake alizidi kushikwa na wasiwasi zaidi, hakuamini kama kweli kile kilichokuwa kikiendelea kilitakiwa kuendelea ndani ya maisha yake. Alan ndiye alikuwa mtoto wake pekee ambaye alikuwa akimpenda sana, alikuwa radhi kuupoteza utajiri ambao alikuwa nao lakini si kumpoteza Alan ambaye kwa wakati huo aliamini kwamba alikuwa kwenye safari yake kuelekea nchini Mexico.

    Siku hiyo hotelini hakukukalika, walichokifanya ni kuondoka na kisha kuelekea katika kituo kikubwa cha polisi cha hapo Dallas kwa lengo la kumuulizia Bwana Maxwell. Jibu ambalo walikutana nalo huko ndio ambalo liliwachosha zaidi, Bwana Maxwell hakuwa ameonekana kazini siku hiyo.

    “Kwa sababu gani hakuja kazini?” Lilikuwa swali lililotoka mdomoni mwa Bwana Maxwell huku akionekana kuchanganyikiwa, aliuliza kana kwemba yeye ndiye alikuwa mkuu wa kituo.

    “Hatujui. Ni kawaida yake kutokuja ofisini, kwa hiyo wala hatumshangai kwani hii si mara ya kwanza” Mmoja wa polisi alimjibu Bwana Kurt.

    “Atakuwa amekwenda Mexico pamoja na Alan” Bwana Kurt alimwambia mke wake.

    “Kuna lolote ambalo tunaweza kukusaidia?” Polisi mwingine alimuuliza Bwana Kurt.

    “Ninamtaka mtoto wangu”

    “Mtoto gani?”

    “Nisikilizeni, nilimwambia Maxwell amlete mtoto wangu Washington, sasa mpaka muda huu hajamleta. Simuni hapatikani kabisa” Bwana Kurt aliwaambia.

    “Inawezekana wakawa wamekwenda Las Vegas”

    “Las Vegas! Kufanya nini?”

    “Kucheza kamari”

    “Hapana. Mtoto wangu si mcheza kamari”

    Bwana Kurt bado alikuwa amechanganyikiwa, kila kitu ambacho alikuwa akikiongea mahali hapo kilikuwa kikimtia hasira. Polisi ambao walikuwepo katika kituo kile wakaonekana kutokuelewa kitu chochote ambacho kilikuwa kikiendelea. Bi Bertha alishindwa kuvumilia kabisa, kitendo cha kumkosa mtoto wake mpaka katika kipindi hicho kikamfanya kuanza kutokwa na machozi.

    Moyo wake ulikuwa kwenye maumivu makali mno. Kila wakati alikuwa akimkumbuka mtoto wake, alikumbuka siku ambayo alikwenda katika hospitali ya Washington Medical Centre na kujifungua, hakuishia hapo, alikumbuka hatua mbalimbali ambazo alikuwa pamoja na mtoto wake, Alan, mpaka katika muda huo, hakumuelewa Mungu alikuwa na makusudi gani katika maisha yake.

    “Tuondoke” Bwana Kurt alimwambia mke wake.

    “Kwenda wapi?”

    “Tunakwenda Austin” Bwana Kurt alimjibu Bi Bertha.

    Huo ndio uamuzi ambao ulikuwa umeamuliwa mahali hapo, hawakutaka kuendelea kubaki Dallas na wakati kulikuwa na sehemu nyingine ambayo wangekwenda na hatimae kuendelea kupata ukweli juu ya kila kilichokuwa kikiendelea.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Alikuwa amekwishakumbuka kwamba alitakiwa kuelekea katika jiji la Austin pia kwa sababu alikuwa ameongea na mkuu wa kituo cha polisi cha jiji la Austin, Powell na kumwambia maneno ambayo yalikuwa yamemchanganya sana. Kwa wakati huo alikuwa akitaka kuyasikia maneno yake huku akiongea nae ana kwa ana na pia alitaka kufahamu juu ya kazi ambayo alikuwa amewapa.

    Kwa kutumia usafiri wa ndege wala hawakuchukua muda mrefu, ndani ya saa moja na nusu wakaingia ndani ya jiji la Austin ambapo moja kwa moja wakachukuliwa na gari la kifahari na kuelekea katika kituo hicho cha polisi. Bado walionekana kuwa kama walivyoingia jijini Dallas, wote walionekana kuchanganyikiwa, hawakuamini kama Alan alikuwa akielekea nchini Mexico, nchi ambayo alionywa kuingia bila ya kuambiwa sababu za onyo hilo.

    “Niambie. Mmefikia wapi” Bwana Kurt alimwambia Powell mara baada ya kuingia ofisini kwake na kutulia kitini.

    “Mpaka sasa hivi hatufahamu wapo wapi” Powell alimwambia Bwana Kurt.

    “Yaani pamoja na uchunguzi wenu kama polisi bado hamjafahamu chochote kile kwamba kijana wangu yupo wapi?” Bwana Kurt aliuliza huku akionekana kushangaa.

    “Bado bosi”

    “Hivi kweli mpo makini na kazi yenu?” Bwana Kurt aliuliza huku akionekana kukasirika.

    Powell hakujibu chochote kile, alibaki akimwangalia Bwana Kurt huku akionekana kumshangaa. Ni kweli alifahamu kwamba mzee yule alikuwa tajiri lakini hiyo haikuwa sababu tosha ya kumfanya kutaka kuidharau kazi yake na kutaka kuongea kila alichokuwa akijisikia kuongea.

    “Naomba uiheshimu ofisi hii mzee na ujue unaongea na nani” Powell alimwambia ana Kurt Bwana Kurt huku akisimama, nae alionekana kukasirika.

    “Yaani natoa taarifa mapema kwa ajili ya kumfuatilia mtoto wangu halafu nyie mnazembea, hivi mnajua ni kwa kiasi gani ninaangaika kumrudisha mtoto wangu?” Bwana Kurt aliuliza huku kwa mbali akionekana kutamani kulia.

    Powell hakutaka kuongea kitu kingine, akabaki kimya huku akiwa amesimama. Bwana Kurt hakunyamaza, aliendelea kuongea zaidi na zaidi tena kwa malalamiko makubwa huku akiona kwamba polisi hawakuwa wakifanya kazi kama ilivyotakiwa kufanywa. Aliongea kwa muda mrefu mpaka pale ambapo akaamua kubaki kimya.

    “Umemaliza?” Powell alimuuliza Bwana Kurt ambaye alikuwa amekunja uso kwa hasira.

    “Amemaliza” Bi Bertha alimwambia Powell.

    “Mtoto wenu alionekana katika supermarket jijini Fort Worth” Powell aliwaambia, Bwana Kurt akauinua uso wake na kuanza kumwangalia Powell.

    “Ikawaje?” Bi Bertha aliuliza.

    “Alikuwa pamoja na mtu ambaye alionekana kuwa rafiki yake” Powell alijibu.

    “Huyo mtu ni polisi?” Bwana Kurt akadakia kwa kuuliza swali.

    “Kwa maelezo ya yule dada aliyekuwepo katika supermarket ile alisema ndio alikuwa polisi, tena alikuwa ameiacha bunduki katika sehemu ya kupekuliwa” Powell alimwaambia.

    “Ikawaje?”

    “Baada ya dakika chache, akairudia ile bunduki na kumfuata kijana wako” Powell aliwaambia.

    “Sasa ilikuwaje mpaka baadae wakaonekana kuwa kama marafiki?” Bwana Kurt aliuliza.

    “Hapo sisi ndipo tunaposhangaa, na si sisi tu bali hata wale waliokuwepo pale supermarket nao walishangaa” Powell alimwambia Bwana Kurt.

    “Huyo atakuwa Maxwell” Bwana Kurt alisema kwa sauti kubwa.

    “Maxwell...yupi huyo?”Asubuhi ilipofika, sauti ya mlango uliokuwa ukigongwa ndio ambao

    “Huyo huyo aliyekujia akilini mwako kipindi hiki” Bwana Kurt alimwambia Powell.

    “Haiwezekani”

    “Huyo ndiye niliyekwambia kabla, nilimpa kazi, badala ya kuniletea mtoto wangu sijui nae anataka kuelekea Mexico pamoja nae, yaani nashangaa” Bwana Kurt alimwambia Powell.

    “Kijana wako anataka kuelekea Mexico?” Powell aliuliza kwa mshtuko.

    “Ndio”

    “Kwa hiyo atapitia mpakani au?”

    “Ndio”

    “Basi ngoja tuwafahamishe polisi wa mpakani wafanye kila linalowezekana watu hao wasipite” Powell aliwaambia.

    Mpaka inafika mchana wa siku hiyo wakaamua kuondoka na kuelekea hotelini. Hawakutaka kurudi Washington mpaka pale ambapo wangefahamu ni kitu gani kilikuwa kimeendelea kwa mtoto wao pamoja na mahali alipokuwa katika kipindi hicho. Hotelini, wote walikuwa wakimya na hata muda wa kulala ulipowadia, walilala huku wakiwa wamekumbatiana. Katika vipindi vyote walivyopitia katika maisha yao, kipindi hicho kilionekana kuwa kigumu zaidi ya vipindi vyote.

    *****

    Ulikuwa kama usiku wa wapendao, Bwana Maxwell alikuwa amelala na wanawake wawili ambao walikuwa na mvuto wa kisura na kiumbo. Vifua vyao vidogo ndivyo ambavyo vilikuwa vimemdatisha sana usiku huo. Waliruka ruka kitandani huku hata wakati mwingine wakishuka sakafuni na kuendelekea na mchezo wao wa kuvunja amri ya sita. Bwana Maxwell hakujali kama wale walikuwa wanawake wawili, kwa nguvu za simba ambazo alikuwa nazo alihakikisha kwamba kila mmoja anapewa haki ambayo alistahili kupewa usiku huo.

    Kwa sababu usiku uliopita alikuwa ameshinda dola laki moja na hamsini, hakukuonekana kuwa na tatizo lolote kutoa dola mia tano kuwapata wanawake hao ambao usiku huo walikuwa wamefika chumbani kwa lengo moja tu la kumpa huduma mzee huyo ambaye alikuwa akilalamika usiku kucha. Fedha alikuwa nayo katika wakati huo, Alan alikuwa amekuja katika maisha yake kitu ambacho aliamini kwamba Mungu alikuwa amesikia kilio chake cha kuwa na fedha.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Hakuzitumia ovyo sana fedha zile, alizichezea kamari ambazo zilimuingizia kiasi kikubwa cha fedha zaidi na zaidi. Usiku huo ukaonekana kuwa usiku maalumu kwake, japokuwa alikuwa na wanawake wawili kitandani lakini kwake akauona kuwa kama usiku wa wapendanao. Aliwafanya kila slichotaka kuwafanya mpaka vile ambavyo vilionekana kuwa ni uchafu katika macho ya binadamu, aliringia fedha zake na hata kama wangetaka kuongezwa angewaongeza bila kuuliza swali lolote lile.





    Mpaka wote watatu wanapata usingizi, tayari ilikuwa ni saa kumi alfajiri. Bwana Maxwell alikuwa amelala kama mtu aliyekufa, hawakulala katika mpangilo kabisa kitandani hapo. Kwa Bwana Maxwell, alikuwa amelala huku mguu mmoja ukiwa juu ya kitanda na mwingine akiwa kauning’ing’za kitandani. Msichana mmoja alikuwa amelala huku mguu wake ukiwa usoni mwa Bwana Maxwell na huku msichana mwingine akiwa kalala katika staili kama ya kuchuma mboga, yaani kila mmoja alikuwa amelala kwa staili yake, tena wote wakiwa watupu kabisa.

    Asubuhi ilipofika, sauti ya mlango uliokuwa ukigongwa ndio ambao ulimshtua Bwana Maxwell ambaye akainuka na kisha kuufuata na kuufungua huku macho yake yakiwa mazito, usingizi ulikuwa umemjaa sana. Jicho moja halikuweza kuhimili, akalifumba na kuliacha jicho moja likiwa wazi, alipoufungua mlango, alikuwa Alan.

    “Kuna nini tena? Mbona asubuhi asubuhi?” Bwana Maxwell alimuuliza Alan, yaani alikuwa akiongea huku akisikia usingizi.

    “Tuondoke” Alan alimwambia Bwana Maxwell.

    “Mbona mapema mno?” Bwana Maxwell aliuliza huku akianza kuyumbayumba, yaani alikuwa akijisikia kulala tu.

    “Saa nne asubuhi sasa hivi” Alan alimwambia Bwana Maxwell huku akimuonyeshea saa yake.

    “Bado mapema. Mexico si mbali, tuondoke saa saba” Bwana Maxwell alimwambia Alan na kisha kuufunga mlango ule.

    Kutokana na uchovu mkubwa ambao alikuwa nao mahali hapo akaendelea kuyumbayumba mpaka alipokikuta kitanda na kisha kujitupa. Bado alihitaji muda mwingi wa kulala, hakutaka kuondoka chumbani hapo kuelekea sehemu yoyote ile mpaka pale ambapo usingizi wake ungekata kabisa.

    Ilipofika saa saba na nusu ndio muda ambao Bwana Maxwell aliona kwamba usingizi ulikuwa umekatika kabisa. Alichokifanya ni kuteremka kutoka kitandani na kisha kuelekea bafuni. Akaoga huku akiwa amewaacha wasichana wale kitandani, alipomaliza, akarudi chumbani na kisha kuanza kuvaa nguo zake.

    “Unataka kuondoka mpenzi?” Msichana mmoja ambaye alikuwa ameamka alimuuliza Bwana Maxwell.

    “Ndio. Safari bado inaendelea. Hivi niliwalipa?” Bwana Maxwell aliwauliza.

    “Hapana”

    “Mlisema kiasi gani vile?”

    “Dola mia mbili hamsini kila mmoja” Msichana yule alimjibu Bwana Maxwell.

    “Sawa. Nimekumbuka” Bwana Maxwell akaichukua suruali ambayo ilikuwa pembeni mwa kitanda kile na kisha kutoa dola mia moja kumi na kisha kuwapa, kutokana na mchezo ambao alikuwa amepewa usiku kucha, aliona mabinti wale wakiwa wanastahili dola mia tano kila mmoja.

    Baada ya kumaliza kila kitu, Bwana Maxwell na Alan wakaendelea na safari yao. Katika kipindi hiki safari yao ilikuwa ni kuelekea katika mpaka wa kuingia ndani ya nchi ya Mexico, Nuevo Laredo. Kila mmoja alikuwa akilifikiria lake ndani ya basi, Bwana Maxwell kichwa kilikuwa kikimsumbua, hakujua ni kwa jinsi gani wangeweza kufika nchini Mexico salama.

    “Inatupasa tufanye kitu” Bwana Maxwell alimwambia Alan.

    “Kitu gani?”

    “Tukodi gari”

    “Tukodi gari? Kwa nini?”

    “Ili tuweze kuingia Mexico”

    “Sasa kwa nini tusinunue kabisa? Nadhani tukikodi tutashindwa kabisa kuvuka mpakani kwa sababu ya mambo ya vibali” Alan alimwambia Maxwell.

    “Basi sawa. Tuteremke” Bwana Maxwell alimwambia Alan.

    Hawakutaka mpaka basi litoke nje ya mji, walichokifanya ni kuteremka na moja kwa moja kuingia katika basi jingine ambalo liliwapeleka mpaka mjini, Alan akanunua gari ndogo, teksi kwa dola elfu tano na kisha kuingia na kuendelea na safari yao huku gari ikiwa imeuzwa huku ikiwa na vibali vyote.

    Waliendelea na safari yao huku katika kipindi hiki Bwana Maxwell ndiye akiwa dereva wa gari hilo, alikuwa akiendesha kwa mwendo wa kasi kwani hakutaka watumie muda mwingi kuwa njiani na wakati Mexico wala haikuwa mbali kutoka hapo walipokuwa. Japokuwa walikuwa na gari hilo lakini hawakujua ni kwa jinsi gani wangeweza kuvuka mpakani hapo kwani kulionekana kuwa na ulinzi mkubwa.

    “Tutavukaje?” Alan alimuuliza Bwana Maxwell.

    “Tutavuka tu”

    “Najua tutavuka. Tutavukaje?” Alan aliendelea kuuliza.

    “Kwa upande wa huku kwetu hakuna tatizo, labda kwa upande wa Mexico” Bwana Maxwell alijibu.

    “Kwa nini?”

    “Huku upande wetu, askari wote na wanajeshi wanaokaa huku ni marafiki zangu, ila kule ndio kazi ilipo sasa” Bwana Maxwell alimwambia Alan huku akiendelea kuendesha gari lile.

    “Kwa hiyo tufanyeje?”

    “Kuna kitu nitataka ukifanye”

    “Kitu gani?”

    “Kuingia ndani ya buti?”

    “Kuingia ndani ya buti?”

    “Ndio”

    “Haiwezekani”

    “Kwa leo inabidi iwezekane tu”

    “Hapana”

    “Kama hautaki basi hatutoweza kuvuka salama mahali pale” Bwana Maxwell alimwambia Alan.

    “Kwa hiyo mpaka niingie ndani ya buti ndio tutavuka kwa usalama?” Alan aliuliza huku akimwangalia Bwana Maxwell usoni.

    “Hiyo ndio maana yangu. Kama unataka tuvuke salama basi yakupasa kuingia ndani ya buti, kama unataka tukamatwe na hata Mexico tusifike basi endelea kukataa kuingia ndani ya buti” Bwana Maxwell alimwambia Alan.

    Huo ukaonekana kuwa mtihani mwingine kwa Alan, Iliwezekana vipi kijana kama yeye, msafi aingie ndani ya buti la gari. Alijua fika kwamba ndani ya buti la gari kulikuwa na ufinyu wa hewa na hivyo angeweza kupata tatizo katika kupata hewa safi. Ni kweli alitaka sana kuingia nchini Mexico huku akiwa na hamu ya kumuona rafiki yake na hata kutaka kufahamu kitu ambacho kilikuwepo nyuma ya pazi cha yeye kukatazwa kuingia nchini Mexico.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Hakuwa na jinsi, mara baada ya kubakisha kilometa tatu kabla ya kufika mpakani, Bwana Maxwell akasimamisha gari na wote kuteremka. Wakaanza kwenda nyuma ya gari ambapo Bwana Maxwell akafungua buti la gari na Alan kuingia ndani na kujilaza.

    “Hapa tutavuka sasa” Bwana Maxwell alimwambia Alan na kisha kulifunga buti lile.

    Baada ya hapo, safari ikaendelea. Bwana Maxwell alikanyaga moto mpaka akaanza kuuona mpaka kwa mbali huku kukiwa na magari mengi pamoja na polisi wakiwa na wanajeshi mahali hapo. Bwana Maxwell hakuonekana kuwa na wasiwasi, aliendelea kwenda zaidi na zaidi mpaka pale ambapo akaufikia mpaka, wanajeshi wa kimarekani wakaanza kumsogelea, walipolifikia gari lile na kumuona swahiba wao, wakaanza kupiga stori huku wakionekana kuwa na furaha.

    Huyo ndiye alikuwa Bwana Maxwell. Alikuwa amejijengea heshima kubwa ndani ya Texas, alikuwa akijulikana sana kutokana na sifa zake za kucheza kamari na hata ulevi. Kila polisi na mwanajeshi hapo Texas alikuwa akimfahamu, alifahamika zaidi hata ya cheo chake ambacho alikuwa nacho. Bwana Maxwell alionekana kuwa rafiki na kila mtu, kila aliyekuwa akimuona mpakani pale alikuwa akimsogelea na kuanza kupiga nae stori, alionekana kuwa mchangamfu muda wote.

    “Kuna nini tena?” Mwanajeshi mmoja alimuuliza.

    “Nakwenda kucheza kamari kama kawaida yangu. Nakwenda kuwatia umasikini Wamexico” Bwana Maxwell alijibu, wanajeshi na polisi wakaanza kucheka kwa sauti.

    “Safi sana. Utaishia Mexico?”

    “Nitaweza kwenda mpaka Honduras na nchi nyingine, huko kote ni kwenda kuwatia umasikini tu” Bwana Maxwell aliwaambia.

    Mpakani hapo hasa kwa upande wa Marekani, kwa Bwana Maxwell wala hakukuonekana kuwa na tatizo kwani alikuwa akipita mara kwa mara kutokana na ukaribu wake ambao alikuwa nao pamoja na wale wote ambao walikuwa wakihusika mpakani pale. Kikwazo kikubwa kilikuwa ni kwa upande wa Mexico, huko hakukuwa na mtu ambaye alikuwa akimfahamu, pamoja na hayo, hakutaka kuishia hapo, alitaka kuingia nchini Mexico.

    Hakukaguliwa na wala kuulizwa maswali, akaruhusiwa kuvuka kama kawaida yake. Ukiachana na mambo mengine ya umaarufu, wanajeshi wote walikuwa wakimfahamu kwamba Bwana Maxwell alikuwa mkubwa wa polisi katika jiji la Dallas na hivyo hakuonekana kuwa na tatizo lolote lile. Akavuka salama, akaanza tena kupiga gia, baada ya umbali kama wa nusu kilometa, hapo akakutana na kizuizi kingine, hapo kulikuwa na wanajeshi na polisi wa nchi ya Mexico, huku akiwa mbali tu, akapigwa mkono kabisaa, alipofika pale, akaambiwa aliegeshe gari pembeni na yeye kuambiwa kuteremka.

    “Unakwenda wapi?” Lilikuwa swali la kwanza kutoka kwa mwanajeshi ambaye alimsimamisha.

    “Mexico” Bwana Maxwell alijibu.

    “Unakwenda kufanya nini?”

    “Kumtembelea mke wangu”

    “Umeoa mwanamke kutoka Mexico?” Mwanajeshi yule alimuuliza.

    “Mwenye asili ya Mexico”

    “Anaitwa nani?” Mwanajeshi yule alimuuliza huku akiliangalia gari lile vizuri.

    “Jocelyn”

    “Safi. Vibali vyako vipo wapi?” Mwanajeshi yule alimuuliza Bwana Maxwell.

    “Sina passport, sikuja nayo” Bwana Maxwell alijibu, hakuonekana kuwa na wasiwasi wowote ule.

    “Kwa nini? Utaingia vipi Mexico bila passport?”

    “Nimesahau kuibeba kwa sababu nilikuwa kwenye haraka. Mke wangu alinipigia simu na kuniambia kwamba mtoto wangu kapata ajali ya kugongwa na gari, kuchanganyikiwa kwangu kukanifanya kusahau kila kitu” Bwana Maxwell alimwambia mwanajeshi yule.

    “Kwa hiyo ukasahau passport?”

    “Ndio”

    “Una kibali cha kukuruhusu kuishi Mexico?”

    “Sina ila nafikiri natakiwa hata kuishi huko pia”

    “Kwa nini?”

    “Nimemuoa Mmexico na nimezaa nae watoto wawili ndani ya nchi hiyo” Bwana Maxwell alimwambia mwanajeshi yule.

    Aliposikia hivyo, mwanajeshi yule hakuwa na swali jingine, alichokifanya ni kuanza kulikagua gari lile. Alianza kukagua mbele huku akivikunja viti na kuvikunjua, alifungua hapa na kupafunga na kisha kufungua sehemu nyingine. Alipapasa siti zote kwa kuona kama kungekuwa mzigo wa madawa ya kulevya lakini hakukuwa na kitu chochote.

    “Hiyo bunduki ni ya nini?”

    “Mimi ni polisi. Mkuu wa polisi Dallas”

    “Sawa. Unaweza kunipa kitambulisho chako?” Mwanajeshi yule alimwambia Bwana Maxwell ambaye akatoa kitambulisho chake na kumpa mwanajeshi yule, akakiangalia na kisha kumrudishia. Alichokifanya mwanajeshi yule ni kuanza kumwangalia kwa makini Bwana Maxwell usoni. Kwa mtazamo ambao alikuwa akiutumia mwanajeshi yule kumtazama, Bwana Maxwell akaanza kuingiwa na wasiwasi.

    “Nimelipekua gari lako, u raia mwema. Ngoja nimalizie na sehemu moja. Unaweza kufungua buti la gari lako tuone kama hausafirishi kitu” Mwanajeshi yule alimwambia Bwana Maxwel.

    Swali lile likamfanya kuuhisi mwili wake kama ukipigwa na shoti ya umeme, mapigo yake ya moyo yakaanza kudunda kwa nguvu, mzunguko wa damu mwilini mwake ukaanza kuongezeka, swali lile ambalo alikuwa ameulizwa ndio ambalo lilimfanya kuanza kutetemeka kwa hofu.

    “Fungua buti la gari lako” Mwanajeshi yule alimwambia Bwana Maxwell.

    Bwana Maxwell akajifanya kama kutokusikia, akabaki kimya huku akijifikiria ni kitu gani ambacho alitakiwa kufanya. Mwanajeshi yule hakutaka kunyamaza, aling’ang’ania buti la gari lifunguliwe kwa ajili ya kukamilisha upekuzi wake. Sauti yake ya juu pamoja na mgomo ambao alikuwa akiuonyesha Bwana Maxwell ndio ukawafanya wanajeshi wengine watatu kukusanyika mahali pale.

    “Kuna nini?” Mwanajeshi mmoja ambaye alionekana kuwa kiongozi aliuliza.

    “Hataki kufungua buti la gari lake”

    “Fungua buti la gari lako” Mwanajeshi yule ambaye alikuwa kiongozi alimwambia Bwana Maxwell ambaye alikuwa akitetemeka. Hapo hapo bila kupoteza muda, wanajeshi wale wakaanza kuzikoki bunduki zao.

    “Fungua buti la gari lako” Mwanajeshi yule alimwambia Bwana Maxwell.

    “Mtoto wangu ni mgonjwa hospitalini, ninachelewa, naomba mnisikilize niwahi huko” Bwana Maxwell aliwaambia huku akianza kuutengeneza uso wa huruma.

    “Fungua buti la gari lako. Unavyochelewa kulifungua na ndivyo unavyochelewa kwenda kumuona mtoto wako” Mwajeshi yule alimwambia.

    “Nawaombeni....!” Bwana Maxwell aliwaomba huku akiendelea kutetemeka. Tayari kulionekana kuwa na tatizo, wanajeshi ambao walikuwepo mahali pale walionekana kutokuwa na utani hata kidogo.

    “FUNGUA BUTI LA GARI LAKO....!!!” Mwanajeshi yule alimwambia kwa sauti ya juu yenye ukali, nae akatoa bunduki yake kwani aliona kama Bwana Maxwell alikuwa akimletea utani mahali pale.

    ****CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kelvin bado alikuwa kiendelea kuwa katika mahusiano pamoja na msichana Lucy. Kila siku maishani mwao walionekana kuyafurahia mapenzi japokuwa kiukweli moyoni mwa Kelvin hakukuwa kama jinsi alivyokuwa usoni mwake. Albertina alikuwa amezoeleka moyoni mwake, kila wakati alikuwa akimfikiri msichana huyo ambaye aliamini kwamba alikuwa msichana pekee ambaye alimpa furaha ya mapenzi kama ambavyo alitakiwa kuwa nayo.

    Lucy alikuwa na fedha, Lucy alionekana kuwa na mapenzi ya dhati kwake. Lucy alikuwa msichana wa haraka haraka, alikuwa akitamani kila kitu kifanyike haraka haraka na hivyo aingie katika maisha ya ndoa pamoja na Kelvin.

    Ingawa zilikuwa zimepita siku nne toka aingie katika mahusiano na Kelvin, Lucy akaanza kugusia masuala ya kufunga ndoa. Alionekana kuwa mtu mwenye haraka mno huku akiona kwamba kama asingeweza kufanya hivyo basi Kelvin yule angeweza kuondoka mikononi mwake na kumfuata Albertina na kisha kurudiana.

    Lucy hakutaka kitu hicho kitokee na ndio maana kila siku alikuwa akipenda kuongea na Kelvin kuhusiana na suala la ndoa. Kwa kelvin, katika kipindi hicho hakutaka kukubaliana na Lucy. Ni kweli alijua fika kwamba msichana huyo alikuwa akimpenda kwa dhati lakini hiyo haikuwa sababu ya kumfanya kukubali kufunga ndoa pamoja nae na wakati hawakuwa wamekaa muda mrefu ndani ya mahusiano.

    “Ni mapema mno Lucy” Kelvin alimwambia Lucy mara alipoona anazidi kumwambia kuhusiana na ndoa.

    “Yaani bado ni mapema na wakati ninahitaji kuishi nawe mpenzi. Haunipendi?” Lucy alimwambia Kelvin na kisha kumtupia swali.

    “Nakupenda” Kelvin alijibu.

    “Sasa kwa nini haupendi kumuoa mtu ambaye unampenda kwa moyo wote?” Lucy alimuuliza Kelvin.

    “Si kwamba sipendi”

    “Ila?”

    “Ila bado mapema. Hebu jifikirie Lucy, ni siku nne tu ambazo tumeweza kukaa kwenye mahusiano, hapo unataka ndoa, kweli inakuingia akilini?” Kelvin alimwambia Lucy na kisha kumtupia swali.

    “Inawezekana kama mkiwa kwenye mapenzi ya dhati”

    “Hapana Lucy, unakosea. Maisha hayapo hivyo kabisa. Unakuwa mpenzi wa mtu, unapata muda wa kuzoeana nae zaidi, inatakiwa ujue mpenzi wako anapenda nini na anachukia nini, baada ya hapo ndio unakuja kuzungumzia ndoa” Kelvin alimwambia Lucy.

    “Jamani baby....hiyo sio sababu ya msingi” Lucy alimwambia kelvin.

    “Luccy, wewe ni msomi, umesoma sana na ninajua fika kwamba unajua mengi kuhusiana na mahusiano ya kimapenzi pamoja na ndoa. Hivi unajua huwa ninapenda nini?” Kelvin alimwambia Lucy na kisha kumuuliza.

    “Najua”

    “Niambie”

    “Unapenda kuwa na furaha”

    “Hicho ni kitu ambacho kila mtu anapenda kuwa nacho. Mimi napenda, wewe unapenda na hata yule anapenda pia. Kuna mambo mengine ninayapenda ila wewe hauyapendi, na kuna mengine siyapendi na wewe unayapenda. Hayo ndio mambo muhimu ambayo wewe kama mpenzi wangu unatakiwa kuyafahamu” Kelvin alimwambia Lucy.

    “Sasa nitayafahamu vipi na wakati haujaniambia?” Lucy alimuuliza kelvin.

    “Hapo ndipo linapokuja suala lile lile, nizoee, hayo mambo si ya mimi kukufuata na kukwambia, wewe ndiye yakupasa kuyafahamu” Kelvin alimwambia Lucy.

    “Sasa nisipoyafahamu?”

    “Utakaponizoea zaidi ni lazima uyafahamu” Kelvin alimwambia Lucy.

    Lucy alionekana kuwa tofauti sana na Albertina. Kitu ambacho alikuwa akikifikiria kwa wakati huo kilikuwa ni ndoa tu. Alikuwa akijiamini sana, fedha ambazo alikuwa nazo aliziona kuwa kila kitu katika maisha yake. Alijiona kuwa na nguvu ya kumshawishi Kelvin kuingia katika ndoa pamoja nae lakini kwa upande mwingine pia alijiona kuwa na uwezo mkubwa wa kuimudu ndoa.

    Kila alipokuwa akiwaangalia marafiki zake ambao walikuwa katika ndoa, Lucy alikuwa akiumia moyoni mwake, nae alitamani kuingia katika ndoa. Bado moyoni mwake hakuwa na amani kabisa, Albertina alionekana kumuogopesha kupita kawaida. Alikuwa akihitaji sana kuingia katika ndoa pamoja na Kelvin lakini Kelvin mwenyewe wala hakuwa na habari nae. Kila wakati Lucy alihisi kuibiwaibiwa mtu wake, alikuwa na uhakika kwamba bila ndoa, Kelvin angeweza kurudi kwa Albertina.

    “Mbona mapema sana Lucy?” Rafiki yake, Theopister alimuuliza.

    “Najua ni mapema lakini kwanza yanipasa kumzuia huyu mwanaume, si unajua nimemuiba, sasa bila kufanya haraka haraka unadhani nitafanikiwa?” Lucy alimwambia Theopister na kisha kumuuliza.

    “Hata kama. Hebu jiamini shoga yangu. Una kila kitu, mwanaume atawezaje kukutetemesha?” Theopister alimuuliza Lucy.

    “Si kwamba ananitetemesha”

    “Ila”

    “Naogopa mwenye mali kumfuata”

    “Mwenye mali ni wewe. Mpaka kaachana na huyo msichana basi jua kwa sasa wewe ndiye mwenye mali” Theopister alimwambia Lucy.

    “Sawa. Nimekubaliana na wewe. Hebu nishauri nifanye nini ili nizidi kumteka” Lucy alimwambia rafiki yake.

    “Mpe mapenzi motomoto, mjali na kumsikiliza. Jifanye kama mtumwa kwake lakini akili yako iwe na malengo yako” Theopister alimwambia Lucy.

    “Kingine?”

    “Hakikisha unakuwa nae karibu”

    “Hayo tu?”

    “Yapo mengi sana shoga yangu, mengine sio ya kukwambia hadharani, utatakiwa kuyafahamu” Theopister alimwambia Lucy.

    “Sasa si uniambie Theo”

    “Kuwa mchangamfu kitandani, usiwe kama gogo. Ukiwa kama gogo tu, imekula kwako” Theopister alimwambia Lucy.

    “Hilo la maana ambalo ulikuwa umelificha sasa”

    “Hahaha! Halloooooo...!!” Theopister alicheka kwa sauti kubwa.

    Ushauri ambao aliupata kutoka kwa Theopister akaanza kuufanyia kazi. Kila siku Lucy alihakikisha anakuwa karibu na Kelvin. Hakutaka kumpa nafasi, alijifanya kuwa kama mtumwa huku kichwani mwake akiwa na mlengo ambayo alikuwa amejiwekea. Kitandani hakuwa mvivu tena, alikuwa mchangamfu kitu ambacho kwa mbali Kelvin alionekana kukifurahia.

    Kwa upande wa Kelvin hali ikaonekana kutokubadilika kabisa. Ni kweli alikuwa akipata mengi sana kutoka kwa Lucy lakini bado hakuonekana kuyafurahia mapenzi. Kelvin alitaka kuwa na uhuru, kitendo cha Lucy kumnata kila wakati kilionekana kumkasirisha sana. Lucy aliendelea kuwa karibu nae huku akianza kuonyesha mabadiliko kitandani, mabadiliko ambayo kwa wakati mwingine yalimfanya Kelvin kuhisi kwamba alikuwa amefika lakini moyo wake ukakataa kabisa.

    “Yaani pamoja na kufanya yote haya bado haufurahii jamani” Lucy alimwambia Kelvin huku akiwa amemuegemea kifuani.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Nifurahie nini tena?” Kelvin alimuuliza Lucy.

    “Kufurahia tu. Yaani mpaka mwenzako kiuno kinauma lakini bado haufurahii tu” Lucy alimwambia Kelvin.

    “Ninafurahia Lucy”

    “Upo tayari kunioa”

    “Nipo tayari ila sio kipindi hiki”

    “Jamaniiiiiiii”

    “Kuwa mvumilivu, muda bado”

    Kama alivyoambiwa na Kelvin ndivyo alivyofanya, Lucy akaanza kuonyesha uvumilivu kwa kusubiria ndoa. Mwezi wa kwanza ukakatika na wa pili kuingia, bado Lucy alikuwa kwenye uvumilivu mkubwa. Mwezi huo wa pili ukamalizika na wa tatu kuingia bado uvumilivu wake ulikuwa ukiendelea kuwa moyoni mwake.

    Ndoa ilikuwa ikimsumbua sana, alikuwa akitamani sana kufunga ndoa na Kelvin na yeye kujiita mwanamke aliyekuwa na heshima mitaani na hata kwa marafiki zake. Mwezi wa nne ukaingia, wa tano ukakatika na wa sita kuingia, bado Kelvin alikuwa akimsisitizia Lucy kuwa kwenye uvumilivu mkubwa.

    Kwa kelvin, bado Albertina alikuwa akimsumbua sana moyoni mwake, aliuhisi moyo wake kukosa kitu muhimu sana katika kipindi hicho, kitu ambacho aliamini kwamba aingeweza kukipata sehemu yoyote ile. Ukaribu wake na Albertina katika kipindi cha nyuma ulikuwa mkubwa zaidi ya ukaribu wake na Lucy ulivyokuwa katika kipindi hicho.

    Wakati mwingine kelvin alikuwa akikaa peke yake, mawazo yake yalikuwa yakimpelekea kumfikiria Albertina pamoja na mambo yote ambayo walikuwa wameyafanya katika kipindi cha nyuma, kumbukumbu za matukio mbalimbali ambayo walikuwa wameyafanya yalikuwa yakimuumiza mno, kila wakati alipokuwa akiyafikiria alikuwa akitokwa na machozi tu.

    Hapo ndipo majuto yalipoanza kumkumba, hapo ndipo ambapo aligundua kwamba alifanya jambo moja baya sana kumsikiliza mama yake mpaka kufanya kille ambacho kilikuwa kimefanyika. Kila siku akawa mtu wa kujifungia chumbani kwake na kulia tu, alikuwa akimhitaji sana Albertina wake katika kipindi hicho, mapenzi ambayo alikuwa nayo kwa Albertina yalikuwa makubwa, akashindwa kujua afanye nini kwa wakati huo.

    Miezi sita ilikuwa imekwishaingia na karibia mwezi mwingine wa saba ulikuwa ukikaribia kuingia. Kelvin bado alikuwa akimfikiria sana msicha aliyekuwa mpenzi wake, Albertina. Moyoni mwake alikuwa akitamani sana awe na msichana huyo kwa mara nyingine tena hasa mara baada ya kumuomba msamaha kwa kile kilichokuwa kimetokea.

    Siku hazikumsubiri, mwezi wa saba ukaingia toka aachane na Albertina, siku ziliendelea kusogea zaidi na mwezi wa nane kuingia. Hapo ndipo ambapo Kelvin akashindwa kuvumilia, kitu ambacho alikuwa amekifikiria ni kumfuata Albertina na kisha kumuomba msamaha tu. Moyoni alijipa moyo, kutokana na miezi nane kupita toka kuachana na Albertina alijua fika kwamba msichana huyo alikuwa amesahau kila kitu jambo ambalo lingemfanya kusamehewa na kisha kuanza upya mahusiano na Albertina na kumuacha Lucy kwenye mataa.

    Baada ya siku mbili, Kelvin akaamua kwenda nyumbani kwa mzee Ruttaba. Kitendo cha kufika nyumbani pale kilimshangaza sana, nyumba ambayo alikuwa akiishi mzee Ruttaba pamoja na familia yake ilikuwa imebadilika kabisa, kulikuwa kumejengwa nyumba kubwa ya ghorofa, nyumba ambayo ilitokana na ukarabati wa nyumba ambayo walikuwa wakiishi.

    Nyumba hiyo ilionekana kuwa ya kisasa sana jambo ambalo lilimshangaza sana Kelvin. Kitu cha kwanza ambacho alikuwa amekifikiria moyoni mwake ni kwamba mzee Ruttaba na familia yake walikuwa wamehama ndani ya nyumba hiyo na kisha kuiuza na mtu mwenye fedha aliyeinunua na kuifanyia ukarabati mkubwa zaidi, alichokifanya ni kuufuata mlango na kubonyeza kengele, alichokitaka japo asikie tu mzee Ruttaba na familia yake walihamia wapi.

    “Samahani dada” Kelvin alimwambia msichana ambaye alifungua geti.

    “Bila samahani”

    “Mzee Ruttaba na familia yake bado wanaishi ndani ya hii nyumba au walihama?” Kelvin alimuuliza msichana yule.

    “Bado wanaishi humu”

    “Sawa. Nimemkuta mzee Ruttaba?” Kelvin alimuuliza msichana yule.

    “Hapana. Wamesafiri”

    “Wamekwenda mkoa gani?”

    “Wamekwenda Marekani” Msichana yule alijibu.

    “Marekani! Kufanya nini?”

    “Kwenye harusi ya binti yao”

    “Binti yao! Nani?”

    “Albertina” Msichana yule alitoa jibu ambalo liliufanya mwili wa Kelvin kupoa, miguu ikalegea na kujikuta akichuchumaa.

    “Alibertina anaolewa?” Kelvin aliuliza huku akiwa amechuchuma pale chini na mikono ikiwa kichwani.

    “Ndio”

    “Na nani?”

    “Sijui na nani, ila ni mzungu” Msichana yule alijibu.

    “Harusi inafanyika lini?”

    “Waliondoka majuzi na harusi imefanyika jana. Walisema imefana sana” Msichana yule alimwambia Kelvin ambaye akasimama, hakuongea kitu kingine chochote, alishtukia machozi yakimtoka, akaanza kupiga hatua kuondoka, kilio cha kwikwi kikaanza kusikika, alikuwa amemkosa Albertina, wakati mwingine alijiona kuwa ndotoni ambapo baada ya muda angeamka na kumkuta Albertina akiwa pembeni yake.

    “ALBERTINA...!” Kelvin alilitaja jina hilo kwa sauti huku akionekana kama mtu aliyechanganyikiwa.





    Unaweza ku LIKE, ku COMMENT hata ku SHARE ili iweze kuwafikia wengi zaidi nao wapate kujifunza kitu.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Je nini kitaendelea?

    Je Kelvin atachukua uamuzi gani?

    Je ni kweli Albertina kaenda Marekani kuolewa?



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog