Simulizi : I Fail To Forget You
Sehemu Ya Tatu (3)
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Taarifa za ugonjwa uliompata Andrew zilipelekwa shuleni kisha kila mwanafunzi akatangaziwa. Wanafunzi wengi hawakutaka kuamini kama Andrew alikuwa amepooza na hivyo asingeweza kuendelea na shule tena, walipoambiwa kuwa alikuwa amepoteza kumbukumbu walibaki wakitahamaki, hawakutaka kuamini kama Andrew waliokuwa wakimfahamu alikuwa katika hali hiyo. Waliacha ubinafsi na utani waliyokuwa wakimtania na sasa wote wakaungana katika kushiriki pigo ambalo lilikuwa limeipata shule nzima kwa kumpoteza Andrew, si kana kwamba alikuwa amefariki la isipokuwa asingeweza kuendelea na shule tena kutokana na tatizo lililokuwa limempata. Kila mwanafunzi alikuwa akilaani kwa kitendo kilichokuwa kimetokea.
Baada ya kugundua mwanafunzi aliyesababisha yale yote uongozi mzima wa shule uliamua kumfukuza Selestine na kumchukulia Report Book (RB) polisi kwa lengo la kumkamata popote pale ambapo angeweza kuonekana.
Wanafunzi walitokea kumchukia sana Selestine, walimchukia kwa kitendo alichokuwa amekifanya cha kusababisha ulemavu wa Andrew.
“Yani huyu mjinga akikamatwa anatakiwa afungwe kifungo cha maisha jela,” alisema Mwanafunzi mmoja.
“Katili sana,” alisema Mwanafunzi mwingine ambaye alionekana kuchukizwa na kitendo alichokuwa amekifanya.
Miongoni kati ya wanafunzi walioonekana kuumizwa na kile kilichokuwa kimetokea katika maisha ya Andrew, Herieth pia alikuwa kati yao, alijikuta maumivu yakishika hatamu katika moyo wake na muda wote alikuwa akimuhurumia Andrew. Alijua ni maumivu kiasi gani ambayo alikuwa akiyapitia lakini ukweli ulibaki kuwa yeye ndiye alikuwa chanzo cha yale yote kutokea. Hilo lilizidi kumumiza sana moyo wake kuna muda alikuwa akilia machozi lakini aliwahi kuyafuta ili asiweze kuonekana.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Alihisi kumkosea sana Andrew hasa baada ya kusikia kuwa alipooza na pia alikuwa amepoteza kumbukumbu.
****
Moyo wake ulikuwa katika furaha sana, alihisi kutimiza kile alichokuwa amedhamiria kukifanya. Kitendo cha kumpiga Andrew mpaka kuhakikisha anapoteza fahamu kilimfurahisha sana, aliamini kufanikiwa kwa asilimia kubwa.
Lengo lake lilikuwa ni kuona Andrew anapoteza maisha kabisa na hivyo asiweze tena kumfuatilia Herieth msichana ambaye alikuwa akimpenda sana. Kwa wakati ule ambao alikuwa amempiga Andrew aliamua kukimbia na kwenda kujificha mbali kusiko julikana, aliamua kufanya hivyo kwa kuyanusuru maisha yake, aliamini kwa kitendo alichokuwa amekifanya lazima angeweza kuchukuliwa hatua kali za kisheria juu yake.
Mahali ambapo alikuwa amekwenda kujificha alikuwepo mwanafunzi mmoja tu! ambaye alikuwa akipafahamu na ndiye ambaye alikuwa akimletea taaarifa zote zilizokuwa zikiendelea shuleni. Walikuwa wakiishi geto.
“Umefukuzwa shule.”
“Kweli?”
“Ndiyo.”
“Vipi yule shoga imekuwaje?”
“Amepelekwa hospitali ila majibu yake hayajaja vizuri.”
“Kivipi?”
“Amepooza na kupoteza kumbukumbu.”
“Safi sana.”
“Ila kuna tatizo.”
“Tatizo gani tena.”
“Wamekuchukulia RB hivyo unatafutwa kila kona ya mji.”
“Duh! Ishakuwa soo sasa hapa cha kufanya ni kutoroka kwenda mbali.”
“Na shule je?”
“Shule ipi tena wakati nishafukuzwa halafu natafutwa.”
“Dah! “
Yalikuwa ni mazungumzo kati ya Selestine na Derick rafiki yake ambaye alikuwa akimletea habari zote zilizokuwa zikiendelea shuleni, kwa wakati huo kitu alichokuwa akikiwaza Selestine ni kutoroka kwenda mbali akiamini kwa kufanya hivyo asingeweza kukamatwa.
Mkoa uliyomjia kichwani kwake ulikuwa ni Daresalaam. Alipanga siku iliyofuata ndiyo iwe siku ya safari ya kwenda Daresalaam kwa lengo la kujificha ili asiweze kukamatwa na polisi.
Hakutaka tena kuendelea kuishi mkoa wa Kilimanjaro, alichokuwa amekipanga siku iliyofuata aweze kutoroka, alipanga kwenda Daresalaam mahali ambapo aliamini angeweza kujificha na kutokamatwa na polisi ambao tayari walikuwa wameanza kumtafuta. Hakuwa na pesa lakini alidhamiria kusafiri hivyohivyo.
“Sasa nauli unayo?” aliuliza Derick huku akimtazama Selestine ambaye alionekana kuchanganyikiwa baada ya kuambiwa kuwa alikuwa akitafutwa kila kona.
Hilo lilizidi kumfanya azidi kuwaza ni kwa namna gani angeweza kuondoka eneo lile.
“Sele,” aliita Derick huku akiendelea kumtazama Selestine ambaye alikuwa mbali kimawazo. Hakutaka kuishia hapo alimuita tena, safari hii akaamua kumgusa begani kisha Selestine akashtuka kama mtu aliyekuwa ameshtuliwa.
“Nini wewe,” alisema kwa kukurupuka.
“Uko mbali sana?” aliuliza Derick.
“Hapana,” alijibu Selestine.
“Sasa unawaza nini?”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Mbona siwazi kitu?”
“Kesho unasema unaondoka je, nauli unayo?” aliuliza Derick.
Lilikuwa ni swali ambalo lilizidi kumuweka Selestine katika wakati wa mawazo, alipanga kusafiri lakini hakujua ni kwa namna gani angeweza kusafiri mpaka kufika Daresalaam. Hilo lilizidi kumuumiza kichwa mpaka asijue ni nini ambacho alitakiwa kufanya.
Yalikuwa ni majira ya saa mbili za usiku, Selestine bado alikuwa katika mawazo. Alizidi kuwaza na kuwazua mambo mengi sana na mwisho kabisa akapata wazo. Lilikuwa ni wazo la uwizi na alipanga kwenda kuiba usiku huo popote pale ambapo angeweza kupata pesa.
“Nimepata wazo,” alisema Selestine.
“Wazo gani?”
“Itabidi niende nikaibe usiku huu.”
“Ukaibe?”
“Ndiyo ili nipate pesa.”
“Ukikamatwa?”
“Siwezi kukamatwa nitakuwa makini.”
“Ulishawahi kuiba?”
“Hapana ila hii ndiyo mara yangu ya kwanza.”
“Kuwa makini.”
“Usijali,” alisema Selestine.
Hilo ndilo alilokuwa amepanga kwa wakati ule, hakutaka tena kuendelea kujiumiza kichwa chake kwa kufikiria mambo ambayo yalizidi kumuumiza. Aliamini endapo angefanikiwa kwenda kuiba katika usiku ule angeweza kupata pesa ambayo ingemsaidia kumpeleka mpaka Daresalaam. Alikubaliana na wazo lake na alipanga saa sita za usiku ndipo atoke kwa lengo la kwenda kuiba.
****
Moyo wa Herieth ulikuwa katika maumivu makali sana, alikuwa akimfikiria Andrew muda wote, alihisi kumkosea sana katika maisha yake, aliamini yeye ndiye alikuwa chanzo cha yale yote kutokea, alihisi kuwa mkosaji mbele ya Andrew ambaye alitakiwa kumuomba msamaha lakini hakujua kwa namna gani angeweza kufanya hivyo kwani Andrew alikuwa amepooza na kupoteza kumbukumbu zote. Hilo lilizidi kumfanya ajisikie vibaya sana. Alihisi kuubeba msalaba wa dhambi nzito ambao ulikuwa ukimlaani kwa kitendo alichokuwa amekifanya.
Alipokuwa shuleni hakuweza kusoma kabisa, kila alipojaribu kufanya hivyo taswira ya Andrew ilikuwa ikimjia kichwani, ilimfanya mpaka ashindwe kusoma na mwisho wake akabaki akiwa analia. Machozi yalikuwa yakimbubujika mashavuni mwake yakiambatana na maumivu makali aliyokuwa nayo moyoni mwake.
Kila siku ilikuwa ni siku ya vilio na maumivu kwa upande wa Herieth, hakujua ni nini alitakiwa afanye ili aweze kuondokana na hali hiyo iliyokuwa ikimkabili.
“Andrew please forgive me,” (Andrew tafadhali naomba unisamehe,) alisema Herieth alipokuwa chumbani kwake, machozi yalikuwa yakimbubujika mfululizo na kuangukia kwenye mto. Usiku hakupata usingizi kabisa, alikuwa akimkumbuka Andrew, aliutumia muda wake mwingi katika kumuwaza bila kuchoka. Aliikumbuka Barua ambayo alitumiwa na Andrew siku chache kabla hajawa mgonjwa, ilizidi kumuumiza sana, alifahamu alikuwa akimpenda sana japo hakuwahi kumpa nafasi na mara zote alikuwa akimtolea nje na kumdharau kwa kumuita shoga.
****
Andrew alipopata fahamu hospitalini kila mtu aliruhusiwa kwenda kumuona, kwa upande wa Herieth hakutaka kuamini macho yake kama kweli Andrew alikuwa amepooza, kila alipokuwa akimtazama jinsi alivyokuwa amelala pale kitandani machozi hayakumkauka mashavuni mwake. Alikuwa akimlilia Anderw ambaye hakuwa akijua lolote lililokuwa likiendelea. Machozi aliyokuwa akiyatoa Herieth yalimfanya kila mtu abaki akimshangaa kwa kuhisi kuwa Andrew alikuwa ni mpenzi wake.
Ingawa lilikuwa ni kosa la kisheria kwa wanafunzi kujihusisha kimapenzi lakini Herieth hakutaka kujali lolote, alihisi kumpenda sana Andrew ambaye kwa wakati huo alikuwa amepooza na alipoteza kumbukumbu. Moyo wake ulikuwa katika mapenzi mazito na wala hakujua hisia hizo zilikuwa zimetokea wapi hasa.
****
MAHALI: PASUA SOKONI, MOSHI MJINI
MUDA: 6:15 USIKU.
“Mwizi.”
“Mwizi.”
“Mwizi.”
Zilikuwa ni sauti za watu zilisikika maeneo ya Pasua sokoni huku wakiwa wamebeba mawe, mapanga, magongo na vidumu vya petroli. Walikuwa wakimkimbiza mtu waliyedai kuwa alikuwa ni mwizi kwa wakati huo na alikuwa amekimbilia na kwenda kuingia eneo la sokoni. Hawakujua alikuwa amejifichia wapi hivyo walibaki wakiendelea kuita mwizi huku wale waliokuwa wamebeba silaha zao wakianza kulaani kwa kumpoteza kizembe.
Hawakutaka kuamini kama kweli walimpoteza mwizi kizembe kiasi kile, walichoamua kukifanya ni kuanza kupekuwa kila sehemu eneo lile la sokoni wakiamini kuwa wangeweza kumkuta na kumpiga kipigo kikali sana, kila mtu alionekana kutawala na hasira kali sana katika uso wake, hakukuwa na mtu ambaye alikuwa akitabasamu hata kidogo.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Huku hayupo,” alisema jamaa mmoja ambaye alikuwa ameshika rungu kubwa, alionekana kuwa na mwili uliyojengeka vyema kimazoezi, alikuwa ni mtu wa miraba minne.
“Hata huku hayupo pia,” alisema jamaa mwingine ambaye alikuwa ameshikilia panga butu, alionekana kuwa na hasira sana kwa kumpoteza mwizi katika mazingira yale.
“Kwahiyo jamaa ndiyo kasepa na pochi ya yule dada.”
“Watu kama hawa wakikamatwa inatakiwa tuwachome moto kabisa, wamezidi kutuibia sana katika mtaa huu, hatukai kwa amani.”
Kila mtu alikuwa akikilaani kitendo cha kumpoteza mwizi katika mazingira yale, kitendo hicho kilimchukiza kila mtu, walipojiridhisha kuwa hakuwepo eneo lile ilibidi waanze kuondoka eneo lile na baada ya dakika tano hakukuwa na mtu yoyote eneo lile.
Selestine alikuwa amejificha katika mifuko iliyokuwa imeachwa na wafanyabiashara wa soko lile, alikuwa chini ya meza moja ambapo alikuwa amejifunika gubigubi. Mbu hawakuwa mbali katika kumshambulia katika giza lile, hakutaka kujali yale maumivu aliyokuwa akiyapata kwa kuumwa na mbu eneo lile, alichokuwa akijali ni kuona usalama wa maisha yake unaendelea kuwa mzuri, aliamini ule ndiyo ulikuwa mwisho wa maisha yake, kimoyomoyo alikuwa akijaribu kumuomba Mungu aweze kumsaidia ili asiweze kukamatwa, alikiri kuwa hakuwa na njia nyingine ya kufanya zaidi ya kuiba ili aweze kupata pesa. Alifanikiwa katika hilo na kwa wakati huo wale watu waliyokuwa wakimkimbiza walikuwa tayari wameshaondoka. Hakutaka kuamini kirahisi kuwa alisamehewa kuachwa eneo lile akiwa bado amejificha, moyoni alihisi kama ulikuwa ni mtego ambao alikuwa ametegewa hivyo hakutaka kutoka kichwa kichwa, alitumia akili kutoka eneo lile kwa kunyata huku mikono yake ikiwa imeikumbatia pochi aliyokuwa atoka kuuiba. Wasiwasi wa kukamatwa bado uliendelea kumtawala na kila hatua aliyokuwa akiipiga alikuwa akiipiga kwa umakini wa hali ya juu, alihisi wenda alikuwa akifuatiliwa.
“Wewe kijana,” ilisikika sauti ya kiume ikiita kwa nyuma, Selestine akashtuka baada ya kusikia hivyo akahisi kuwa alikuwa ameshakamatwa.
“Usikimbie simama hapohapo,” ilisema tena ile sauti kwa ukali kisha msemaji wa hiyo sauti akawa kama anayemfuata Selestine. Selestine akasimama.
Aliamini ule ndiyo ulikuwa mwisho wa maisha yake, alichoamua kukifanya ni kuanza kusali sala zake za mwisho, aliamini alikuwa amekamatwa na muda wowote angeweza kuchomwa moto ama kupigwa mpaka kufa.
Yule mtu alipomkaribia alimgusa begani kwa kutumia rungu alilokuwa amelishikilia. Kitendo hicho kikazidi kumuogopesha sana Selestine, aliamini alikuwa ni mtu miongoni mwa wale waliyokuwa wakimkimbiza kwa kosa la uwizi aliyokuwa ameufanya muda mfupi, mikononi alikuwa bado ameishikilia ile pochi.
“Unatoka wapi usiku huu?” aliuliza yule mtu kisha Selestine akageuka kumtazama, alikuwa ni mlinzi wa soko lile ambaye alionekana kuwa ni Mzee wa makamo.
“Nimetokea huko ndani sokoni,” alijibu Selestine kwa kujiamini.
“Ulikuwa unafanya nini?”
“Kuna uwizi ulitokea mtaa wa pili sasa tukawa tunamkimbiza huyo mwizi akakimbilia huku.”
“Mwizi?”
“Ndiyo.”
“Yuko wapi sasa?”
“Tayari ameshakamatwa.”
“Kumbe ndiyo nyie nilikuwa nasikia sauti zenu.”
“Ndiyo.”
“Mkononi umebeba nini?”
“Pochi.”
“Pochi ya nani?”
“Mtu aliyeibiwa namfahamu hivyo ndiyo nampelekea hivyo.”
“Unauhakika?”
“Ndiyo Mzee,” alijibu Selestine kwa kujiamini kisha yule Mzee akaweza kumuachia aondoke eneo lile. Hakuamini kama kweli aliachiwa na Mzee yule, aliamini kwa kuendelea kutembea taratibu angeweza kukamatwa tena hivyo alichokifanya ni kuanza kukimbi katika usiku ule.
Alipofika geto mahali ambapo alikuwa akiishi yeye na rafiki yake aliugonga mlango kisha rafiki yake Derick akawahi kuufungua, ni kama vile alikuwa akimsubiri kwa hamu kubwa na alipoweza kumuona rafiki yake amerudi salama hakutaka kuamini.
“Vipi umefanikiwa?” alimuuliza.
“Ndiyo huoni nimekuja na mzigo,” alijibu Selestine huku akiachia tabasamu.
“Hawajakukimbiza kweli?” aliuliza Derick.
“Aisee we acha tu yani leo ilibakia nusu ungesikia nimekufa.”
“Kwanini?”
“Jamaa wamenikimbiza hatari yani kama sio ujanja niliyoutumia nadhani muda huu yangekuwa yanazungumzwa mengine.”
“Ujanja gani tena huo uliyoutumia.”
“Wamenikimbiza sana baada ya kuona nazidiwa ikabidi nikimbilie kule sokoni..yani nilipofika haraka nikawahi kujificha chini ya meza moja na hapo hawakuweza tena kunikamata.”
“Duh! Aisee una michezo hatari sana.”
“Sikuwa na njia nyingine ya kufanya ilibidi nikaibe tu.”
“Kwenye pochi kuna pesa kweli au magumashi?” aliuliza Derick kisha Selestine hakutaka kupoteza muda, akaifungua ile pochi, ndani alikutana na vitambulisho, kadi za benki pamoja na pesa. Hakutaka kukagua sana vitambulisho alivyovikuta wala zile kadi za Benki, alichoamua kukifanya ni kuzichukua zile pesa na kuanza kuzihesabu. Alipomaliza kuzihesabu hakuamini, zilikuwa ni laki mbili, alifurahi sana. Kwa furaha ambayo alikuwa naayo akazirusha zile pesa juu, zikatapakaa chumba kizima, akazidi kushangilia kwa kujiona kuwa mshindi kwa kufanikiwa kuiba pesa nyingi kiasi kile. Aliamini kwa pesa zile zingeweza kumfikisha Daresalaam na kwenda kuyaanza maisha mapya ambayo alitarajia kwenda kuyaanza huko.
“Mbona unashangilia hivyo vipi umeona nini?” aliuliza Derick.
“Zipo laki mbili,” alijibu Selestine kisha uso wake ukaachia tabasamu, alikuwa katika wakati wa furaha,
“Duh! Si mchezo aisee lengo sasa limefanikiwa.”
“Yani limefanikiwa mara dufu.”
“Kwani nauli ni shilingi ngapi?”
“Nahisi itakuwa ni kwenye Elfu ishirini na tano.”
“Hapo sasa kazi ni kwako tu,” alisema Derick.
Kila kitu kilionekana kuwa katika mstari, hakuna kilichoonekana kwenda mrama, muda wote Selestine na Derick walionekana kuwa na furaha, alichoamua kukifanya Selestine ni kutoa shilingi elfu hamsini kisha akampatia rafiki yake.
“Hii ya nini sasa?” aliuliza Derick.
“Hiyo itakusaidia mahitaji yako madogomadogo,” alijibu Selestine.
Derick hakuamini kama aliweza kupewa kiasi kile kwa ajili ya matumizi yake madogomadogo, alizoea kiasi kama kile alikuwa akienda kulipa ada shuleni, kitendo cha kupewa pesa na rafiki yake alikithamini sana alizidi kumshukuru.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Derick alikuwa akiishi kwa kuwategemea wazazi wake ambao ndiyo walikuwa wakimsomesha, kwa upande wa Selestine aliishi maisha ya kipeke yake, hakuwa na wazazi hivyo kila kitu alikiendesha yeye kama yeye. Alikuwa ni baba na mama katika maisha yake ambayo tangu alipofikia umri ule hakuwa amewahi kuwaona wazazi wake, alitelekezwa.
Ilikuwa ni majira ya saa nane za usiku, Selestine akaanza kupanga nguo zake kwenye begi, alikuwa ameshadhamiria asubuhi ya siku iliyofuata aweze kuondoka, hakutaka tena kuendelea kuishi mkoa wa Kilimanjaro kwani alishakuwa amefanya makosa na muda wowote angeweza kukamatwa.
****
Mwili wa Andrew ulizidi kuchoka, kila siku ulikuwa ukipungua hospitalini, hakuweza kula kama ilivyokuwa kawaida hivyo kila siku alizidi kudoofika. Waliyokuwa wakienda kumuona walizidi kujisikia vibaya hasa baada ya kumuona akiwa katika hali hiyo, alisikitisha mno kutazama hasa katika wakati ule ambapo mwili wake ulianza kupungua.
Mama yake alikuwa ni mtu wa kulia machozi muda wote, alikuwa akimlilia mwanaye, alimini ule ndiyo ulikuwa mwisho wa maisha ya mtoto wake, mwisho ambao ulikuwa na mateso mengi sanam hakutaka kuona mwanaye akiendelea kuteseka mpaka kufia mikononi mwake, aliamua kumfuata Dokta Masawwe ofisini kwake na kujaribu kuzungumza naye.
“Dokta hakuna njia yoyote ya kumtibu mwanangu ili aweze kupona?”
“Hakuna njia nyingine kwa ugonjwa aliokuwa nao kupona inawezekana ila itachukua muda mrefu sana mpaka kupona.”
“Itachukua kama muda gani?”
“Siwezi kubunia ila wewe elewa kuwa itachukua muda mrefu mpaka kupona,” alijibu Dokta Masawwe.
Kila alichokuwa akiambia na Dokta Masawwe hakutaka kukiamini kirahisi, alichokuwa akikiwaza katika akili yake ni kutafuta njia mbadala ambayo ingeweza kumsaidia mwanaye. Aliamua kujitoa maisha yake sadaka katika kuyapigania maisha ya mwanaye.
Herieth hakuwa mbali katika kumsaidai katika hilo, kila alipokuwa akitoka shuleni sehemu ya kwanza kwenda ilikuwa ni hospitalini ambapo alikuwa akienda kumuona Andrew, alikuwa akijaribu kumsaidia kumpa pesa mama yake Andrew ambazo zilikuwa zikimsaidia mahitaji madogomadogo ya pale hospitalini. Kila siku hali ya Andrew ilikuwa ikibadilika hospitalini, alizidi kudhoofika mno. Hali hiyo ilizidi kumuumiza sana Herieth kila alipokuwa akimtazama Andrew jinsi ambavyo alikuwa amelala pale kitandani machozi yalikuwa yakimdondoka, alikuwa akilia kwa uchungu.
Moyoni alimchukia sana Selestine, kuna kipindi alikuwa akimuombe mabaya yaweze kumfika katika maisha yake ikiwa kama ni sehemu moja wapo wa malipo hasa kwa ubaya aliyokuwa ameufanya.
Alipokuwa shuleni alikuwa akijihusisha na mahusiano ya kimapenzi na Mwalimu Agustino, moyo wake ulikuwa ukimpenda Andrew hivyo hakutaka tena kuendelea na mahusiano hayo ambayo aliamini yalizidi kumchanganya akili yake.
“Mbona sikuelewi?” aliuliza Mwalimu Agustino.
“Hunielewi nini Mwalimu,” alijibu Herieth huku akiwa amekishika kiuno.
“Usiniite Mwalimu niite jina langu Mpenzi,” alisema Mwalimu Agustino.
“Tena naomba uishie hapohapo, mimi sio mpenzi wako tafadhali kwanza wewe unafamilia yako naomba ujiheshimu tena ukiendelea kunifuatilia nitakufikisha pabaya,” alisema Herieth maneno aliyoyamaanisha, hakutaka tena mahusiano na mwalimu huyo.
“Wewe ndiyo unayeyazungumza maneno hayo?”
“Ndiyo kwani wewe unazungumza na nani?”
“Nini kimebadilika?” aliuliza Mwalimu Agustino lakini Herieth hakutaka kumjibu lolote, alibaki kimya.
Huo ndiyo ulikuwa mwisho wa mahusiano yao, Herieth na Mwalimu Agustino walikuwa katika mapenzi ya kisirisiri lakini katika mapenzi yao hawakuwahi kushiriki kufanya mapenzi hata siku moja, hilo lilizidi kumchanganya sana Mwalimu Agustino, hakutaka kuamini kama ule ndiyo ulikuwa mwisho wa mahusiano na Herieth msichana ambaye alipanga kumchezea kwa kufanya naye mapenzi tu kisha angeweza kuachana naye.
UJUMBE WANGU:
Nisingependa kuimaliza Hadithi hii bila kukuambia kitu ndugu yangu, rafiki yangu, mpenzi wa hadithi unayezifuatilia hadithi zangu.
Katika maisha ya mwanadamu kuna mambo mengi sana huwa yanatokea, inakupasa ujifunze kuishi kwa kuyasoma mazingira. Ishi na watu kiusawa kwa maana maisha ni watu na bila kuwa na watu kusingekuwa na maisha.
Wakati mwingine inakupasa ujifunze pia kusamehe hata kwa kosa la makusudi ulilofanyiwa, lipuuzie halafu wewe songa zako mbele usikubali mtu au watu wawe kikwazo cha kukufanya ushindwe kufanikiwa katika jambo unaloliamini katika maisha yako.
Sikwambii haya kwa kukupandikiza mbegu ya uwoga la. Isipokuwa najaribu kukuambia kuwa jaribu kuwa mtu wa kusamehe kila wakati, usipende kuishi na kinyongo moyoni. Furaha ndiyo itakayokuongezea ushindi wa kuyafikia malengo yako.
Hata kama unapitia magumu kiasi gani ishi maisha ya kujiamini halafu usipende kumuonyesha madhaifu adui yako kwani ataweza kuyatumia madhaifu yako hayohayo katika kukunyanyasa na kukufanya ushindwe kuendelea kuamini katika kile ulichokuwa unakiamini.
Muamini Mwenyezi Mungu, jiamini na jikubali kila kitu kinawezekana.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Ilikuwa ni majira ya saa kumi na moja na dakika arobaini na tano alfajiri 11:45 siku ya jumamosi, Selestine alikuwa tayari ameshafika katika stand ya moshi mjini, moyo wake ulikuwa katika furaha mno, hakuwa peke yake, alikuwa na Derick ambaye ndiye alikuwa amemsindikiza kwa wakati huo.
Ingawa alikuwa na nia ya kutoroka lakini moyo wake ulihisi furaha kubwa sana, hakuamini kama kweli alifanikiwa kupata pesa na hatimaye alikuwa stand ya mkoa kwa ajili ya safari.
“Itabidi uwe makini sana,” alisema Derick huku akimkabidhi begi Selestine ambaye alikuwa tayari ameshakata tiketi, alionekana kutawaliwa na tabasamu katika uso wake.
“Usijali kila kitu kitakwenda sawa,” alisema Selestine wakati huo alikuwa akimuaga Derick kisha akapanda ndani ya basi.
Moyo wake ulizidi kujisikia furaha kwa wakati ule, kwa kipindi kirefu aliishi Moshi mjini bila kusafiri eneo la mbali, safari zake ziliishia katika mitaa mbalimbali ya Moshi mjini kama vile Majengo, Rau, Msaranga, Kiboriloni nakadhalika. Ile ndiyo ilikuwa siku yake ya kwanza kusafiri kwenda mkoa wa mbali.
Ilipofika majira ya saa kumi na mbili asubuhi basi alilokuwa amepanda likaanza kuondoka, huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa safari yake ya kuelekea Daresalaam mahalia ambapo hakuwa na ndugu wala sehemu yoyote ya kufikia.
****
Herieth alizidi kuonyesha msimamo wake, hakutaka kujihusisha kimapenzi na mwanaume mwingine tena. Alikuwa akimpenda sana Andrew kiasi kwamba kuna wakati ulifikia akawa ni mtu wa kuwaza tu. Alikuwa akiwaza kuwa Andrew kapona na tayari walikuwa ni mume na mke. Hilo lilizidi kumuumiza sana, alitamani sana siku moja Andrew aamke kisha amwambie ukweli wa moyo wake kwa wakati ule lakini lilikuwa ni jambo lisilowezekana, ilikuwa ni sawasawa na kuilazimisha ndoto uliyoota ijirudie kwa mara nyingine tena kwa wakati ambao ulikuwa macho ukishuhudia kila kitu kwa uhalisia.
Hakuacha kumuombea Andrew kila siku, alipomaliza kujisomea usiku alipokuwa chumbani kwake hakutaka kulala bila kumuombea Andrew ili aweze kupona, maombi yalichukua nafasi kubwa sana, kila alipokuwa akienda kanisani hakuacha kumuombea Andrew, aliamini maombi ndiyo dawa pekee ambayo ilibakia ya kuweza kumtibu Andrew ambaye haikujulikana angeweza kupona lini na katika muda gani, alikuwa ni sawasawa na mfu kwani hakuwa akifanya lolote muda wote alikuwa amelala kitandani.
Mawazo ndiyo yaliyokuwa yamemtawala Herieth kila siku alikuwa ni mtu wa kuwaza, alikuwa akiwaza kwa jinsi gani angeweza kumsaidia Andrew mpaka anahakikisha anapona na kuwa katika hali yake ya mwanzo. Ingawa alitokea katika familia ya kitajiri lakini ilikuwa ni vigumu mno kuweza kuwaeleza wazazi wake ukweli wa jambo lile mpaka wakaamua kumsaidia, aliamini isingewezekana. Alizidi kuumia sana, kichwa chake kilitawaliwa na mawazo.
“Mbona uko hivyo?” aliuliza Diana rafiki yake na Herieth, wakati huo walikuwa darasani.
“Nikoje?” aliuliza Herieth huku akionekana kushangaa.
“Wewe unajiona uko sawa?” aliuliza Diana.
“Ndiyo mbona niko sawa,” alijibu Herieth.
“Hapana hauko sawa mimi nahisi kuna tatizo.”
“Hakuna tatizo Diana niko sawa.”
“Herieth kuna kitu unanificha na sijui kwanini unanificha.”
“Kitu gani nakuficha Diana?”
“Niambie ukweli mbona unaonekana mwenye mawazo sana?” aliuliza Diana.
Herieth hakutaka kuficha ukweli ambao ulikuwa ukimtesa katika moyo wake, aliamua kumueleza kila kitu rafiki yake huyo ambaye urafiki wao haukuwa wa muda mrefu tangu alipoweza kuhamia katika shule ile, alitokea kumuamini na hiyo ndiyo sababu iliyopelekea mpaka akaamua kumueleza ukweli.
Hakutaka kuficha lolote, kila kitu alikizungumza, Diana akaonekana kushangaa baada ya kusikia kuwa Herieth alikuwa akimpenda Andrew mvulana ambaye alisifika kwa tabia za ushoga lakini kwa wakati huo alikuwa amepooza.
“Inamaana kumbe ni kweli unampenda Andrew yule shoga?” aliuliza Diana.
“Hapana Diana usimuite shoga ni mpenzi wangu,” alijibu Herieth huku akionekana kuchukizwa na maneno ya Diana. Alikuwa akimpenda sana Andrew wala hakutaka kuona mtu yoyote anajaribu kuyaingilia mapenzi yake. Aliamua kuachana na Mwalimu wake kwa sababu ya Andrew, kila mwanaume ambaye alikuwa akimfuata na kumtongoza alimtolea nje, hakutaka kujihusisha kimapenzi na mwanaume yoyote zaidi ya Andrew ambaye alikuwa amelala kitandani.
****
Herieth aliendelea kuishi maisha ya kumuombea Andrew na kumpenda mpaka pale siku ya mtihani wa taifa ilipofika. Wanafunzi wote wa kidato cha nne nchini Tanzania wakafanikiwa kufanya mitihani yao na kumaliza, Andrew hakuweza kufanya mitihani kwa sababu za maradhi aliyokuwa nayo. Machozi yalikuwa yakimdondoka mama yake hasa baada ya mwanaye kushindwa kufanya mtihani wa taifa, mtihani uliyokuwa umebeba maisha yake.
Matokeo yalipotoka Herieth aliweza kufaulu vizuri na yeye ndiye aliyeongoza kimkoa. Waliyomfahamu hawakutaka kuamini jinsi alivyokuwa akiishi maisha ya kumuwaza Andrew na kumlilia usiku na mchana kama kweli aliweza kufaulu kiasi kile tena kwa kupata alama za kuongoza kimkoa.
Wazazi wake walifurahi sana, Baba yake Mzee Thomas kwa furaha aliyokuwa nayo aliamua kumtafutia shule nchini Uganda kwa lengo la kuendelea na masomo yake ya kidato cha tano na Sita katika shule ya St. Mary’s Kitende.
Alimpenda sana mtoto wake, alitamani asome mpaka aweze kutimiza malengo aliyokuwa amejipangia katika maisha yake.
“Unatakiwa uende shule Kampala,” alisema Baba yake Herieth huku uso wake ukiwa umetawaliwa na tabasamu pana.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Kampala?”
“Ndiyo kuna shule nimekutafutia huko nafikiri itakupendeza na pia itaendana na wewe.”
“Tena mwanangu ukienda huko inabidi usome kwa bidii ili uzidi kufanya vizuri kila siku,” alidakia mama yake Herieth.
Herieth hakutaka kuamini kama kile alichokuwa akikisikia kilikuwa ni kweli au la. Alikuwa anakwenda nchini Uganda katika mji wa Kampala ambapo huko alitakiwa kwenda kusoma kwa muda wa miaka miwili. Moyo wake haukutaka kuamini kama masomo yalikuwa yanakwenda kumtenganisha na Andrew.
Moyoni alichukia sana hakutaka kusafiri popote na kumuacha Andrew lakini huo ulibaki kuwa ukweli kwamba alitakiwa kuondoka kwenda nchini Uganda kimasomo.
Usiku wa siku hiyo Herieth hakuweza kulala kabisa alipokuwa chumbani kwake, alikuwa akimfikiria Andrew muda wote. Kichwa chake kilijiwa na mawazo mengi sana juu ya Andrew ambaye siku chache zijazo alikuwa anaenda kutengana naye. Moyo wake ulizidi kumuuma sana, hakutaka kuamini kama kile kilichokuwa kinakwenda kutokea kuwa kilikuwa ni kweli au ni la. Kuna muda akajaribu kuyafumba macho yake akiamini wenda alikuwa katika ulimwengu wa ndoto na muda wowote angeweza kuamka lakini haikuwa hivyo, alikuwa katika maisha ya kweli.
“Andrew siwezi kukuacha peke yako, siwezi,” alijisemea alipokuwa amejilaza kitandani wakati huo alikuwa ameukumbatia mto, machozi yalikuwa yakimbubujika mashavuni mwake mfululizo, alikuwa akilia kama mtoto mdogo hasa baada ya kujua kuwa ilikuwa ni lazima aondoke kwenda nchini Uganda kwa ajili ya masomo.
Moyo wake ulikuwa katika maumivu makali mno, alitamani kuwafuata wazazi wake na kuwaambia ukweli wa kile kilichokuwa kimetokea katika maisha yake na Andrew lakini hakujua alitakiwa aanzie wapi. Yalibaki kuwa ni maumivu ya peke yake, maumivu ya siri yaliyokuwa yakimtesa moyoni mwake.
Alichokumbuka ni kuichukua dayari yake na kuanza kuandika matukio yote muhimu ambayo yaliyowahi kutokea katika maisha yake. Hakutaka kusahau hata tukio moja, yote aliamua kuyaandika. Alikuwa akiandika huku machozi yakimdondoka na kulowanisha karatasi ya dayari aliyokuwa akiiandika kwa wakati ule.
Kabla muda wa safari haujafika aliamua kwenda kununua zawadi ya saa ambayo alikuja kumvalisha Andrew, aliamini ilikuwa ni zawadi ambayo ingeweza kumfanya akumbukwe kipindi ambapo atakuwa masomoni nchini Uganda. Hakuacha pia kumbusu, busu la huba la kumuaga.
****
Selestine alipofika Daresalaam kila kitu kilionekana kuwa kigumu kwake, hakuwa na ndugu wala sehemu ya kufikia, hilo lilizidi kumuumiza sana kichwa chake. Yalikuwa ni majira ya jioni alipokuwa stand ya ubungo bado alikuwa akiwaza ni wapi alitakiwa aende bila kujua lolote, alibaki akiwa amesimama huku mikono yake ikiwa imebeba begi lake la nguo, alionekana kuwa mgeni wa kila kitu, alikuwa akishangaa muda wote.
Wakati ule alipokuwa amesimama huku akiendelea kushangaa mara vijana wawili waliovalia mavazi ya suti nyeusi walionekana wakimfuata, kwa macho ya harakaharaka walionekana kuwa ni watu wenye wadhifa fulani.
“Wewe kijana unaitwa nani?” walimuuliza kwa pamoja walipomfikia, walionekana kuwa kama watu waliojawa na jazba fulani.
“Naitwa Selestine,” alijitambulisha.
“Ok Selestine sisi ni maafisa wa polisi tumekuja kukukamata,” alijitambulisha kijana mmoja kisha akatoa kitambulisho chake na kumuonyesha Selestine ambaye kwa wakati huo woga ulikuwa umeshashika hatamu yake, alionekana kuwaogopa viwajana wale hasa baada ya kugundua kuwa walikuwa ni polisi. Alikumbuka tukio alilokuwa amelifanya mpaka akaamua kutoroka kuja katika jiji lile, aliamini kuwa wenda alikuwa akifuatiliwa na ule ndiyo ulikuwa mwisho wake wa kukamatwa na polisi.
Katika hali ya kushangaza Selestine akaanza kuomba msamaha huku akiwasihi wale vijana wasimkamate, alikiri makosa yake huku akijaribu kuwaomba wasimpeleke kokote.
“Jamani naombeni msinikamate, sijafanya yale kwa kukusudia ni hasira tu! hata hivyo nipo tayari kuwapa pesa lakini msinikamate sina ndugu mimi,” alisema Selestine kwa sauti ya kulalamika.
“Unasemaje?”
“Naomba msinikamate sijafanya yale kwa kukusudia nipo tayari kuwapa pesa.”
“Unataka kutupa rushwa?”
“Hapana.”
“Hapana maana yake nini, nasema unataka utupe rushwa?”
“Hapana afande naomba msinikamate mimi sina ndugu.”
“Una shilingi ngapi?”
“Laki moja na elfu kumi na tano.”
“Haya itoe utupatie kabla hatujakupeleka polisi sasa hivi,” alisema yule kijana aliyejitambulisha kuwa walikuwa ni polisi kisha Selestine akafanya kama alivyoambiwa, akaingiza mkono mfukoni na kutoka na pesa halafu akampatia.
“Mbona pesa ndogo.”
“Ndiyo hiyo niliyokuwa nayo.”
“Una uhakika?”
“Ndiyo afande.”
“Na hilo begi vipi?”
“Hili ni begi langu.”
“Lina nini?”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Nguo zangu.”
“Tutaamini vipi?”
“Kweli nimebeba nguo zangu.”
“Hujaficha madawa kweli.”
“Hapana sijaficha kitu.”
“Embu lilete tukalisachi.”
“Sawa.”
“Usiondoke tusubiri tunakurudishia begi lako sawa?”
“Kwani mnaenda kulisachia wapi?”
“Kituoni au unataka twende wote ili ukakamatwe tena?”
“Hapana.”
“Ok basi tusubiri hapahapa.”
“Sawa,” alijibu Selestine.
Yalikuwa ni mazungumzo machache yaliyofanyika kwa muda mfupi lakini yalionekana kuzaa matunda kwa kiasi kikubwa, Selestine alionekana kushawishika na kuwaamini wale vijana kuwa walikuwa ni polisi mpaka akaamua kuwapa pesa na begi lake la nguo, hakutaka kuwa mtu wa kupinga kila kitu alichokuwa akiambiwa kwa wakati ule na wale vijana waliyojitambulisha kuwa walikuwa ni polisi.
Aliamini hakuwa na njia nyingine ya kufanya zaidi ya ile aliyoamua kuifanya kwani kwa kuendelea kubishana na polisi angeweza kufikishwa mahali pabaya.
Yale yote yaliyotokea hayakuwa na ukweli wowote, wale vijana walikuwa ni matapeli wa mjini na walikuwa na lengo la kumtapeli Selestine ambaye alionekana kuwa mgeni. lengo lao lilifanikiwa na mbali na kupewa pesa pia walifanikiwa kuondoka na begi lake la nguo, kwao ulikuwa ni ushindi mkubwa sana.
Selestine aliendelea kubaki pale stand akiwasubiri wale vijana wamrudishie begi lake, alisubiri kwa muda mrefu bila mafanikio yoyote, wakati huo giza lilikuwa tayari limeanza kuingia.
Watu waliyomuona kipindi alipokuwa akitapeliwa waliamua kumfuata na kumwambia ukweli, hakutaka kuamini kile alichokuwa akiambiwa, hakutaka kuamini kama kweli alikuwa ametapeliwa.
“Wale ni matapeli wa mjini kijana wamekutapeli,” alisema Mzee mmoja ambaaye alionekana kuwa ni mzee wa makamo.
“Sasa Mzee wamenitapeli vipi?” aliuliza Selestine huku akionekana kuchanganyikiwa.
“Umetapeliwa,” alijibu yule Mzee.
Ulikuwa ni ukweli ambao hakutaka kuuamini hata kidogo, kila alipokuwa akifikiria kile kilichokuwa kimetokea na yale aliyokuwa akiambiwa vilikuwa ni vitu viwili tofauti. Machozi hayakuwa mbali, yalianza kumdondoka hasa baada ya kujua kuwa alikuwa ametapeliwa kila kitu, kuanzia pesa mpaka begi lake la nguo. Alikumbuka alihifadhi vitu muhimu sana katika begi lake na vyote alikuwa amevipoteza.
“Mimi naitwa Mzee Antony, wewe unaitwa nani?”
“Selestine.”
“Unaishi wapi?”
“Sina mahali pa kuishi mzee.”
“Ina maana huna ndugu katika jiji hili?”
“Ndiyo.”
“Unatokea wapi?”
“Moshi.”
“Pole sana sasa usiku huu unaenda wapi?”
“Sina mahali pa kwenda Mzee.”
“Ina maana huko utokapo pia huna ndugu au?”
“Ni stori ndefu mzee.”
“Huwezi kuifupisha?”
“Kwa kifupi mpaka nafikia umri huu sijabahatika kuwafahamu wazazi wangu.”
“Una maanisha nini?”
“Siwajui wazazi wangu kabisa hata kwa sura,” alisema Selestine.
Mzee Antony alijikuta akianza kumuonea huruma Selestine na kuamua kumsaidia, hakutaka kumuacha aendelee kubaki pale ubungo hasa katika majira yale ya usiku, alikuwa ni Mzee aliyeufahamu vyema wema na ubaya wa mji ule. Aliamua kumchukua kisha wakaongozana moja kwa moja mpaka mahali ambapo alikuwa amepaki gari lake aina ya Toyota Mark II yenye rangi nyeusi.
“Itabidi nikusaidie kijana, nitaongozana na wewe mpaka nyumbani kwangu.”
“Nitashukuru Mzee wangu, asante sana kwa msaada wako.”
“Usijali,” alisema Mzee Antony kisha akawasha gari na safari ya kuelekea Magomeni mahali alipokuwa akiishi ikaanzia hapo.
Moyo wa Selestine ulihisi furaha baada ya kusaidiwa na Mzee Antony, aliamini Mungu alimleta ili aweze kumsaidia.
Mzee Antony hakuwa akiishi na mke wake, maisha yake alikuwa akiyaendesha mwenyewe. Mwanzoni alikuwa akiishi maisha mazuri na Selestine wala hakumuonyesha tofauti yoyote, hakuwa na mtoto hivyo aliishi kwa kumchukulia kama mtoto wake. Maisha yalikuwa mazuri.
Baada ya kupita miezi kadhaa Mzee Antony alianza kumtumia Selestine katika biashara zake haramu alizokuwa akizifanya kwa siri kama vile kusafirisha madawa ya kulevya, bangi na silaha. Alikuwa akimtumia katika biashara hizo haramu zilizokuwa zikimuingizia pesa nyingi mno, hicho kilikuwa ni kipindi cha mitihani ya taifa ya kidato cha nne, mitihani ambayo hakuweza kuifanya na huo ndiyo ulikuwa mwazo wake wa kutumiwa katiba biashara hizo haramu na Mzee Antony aliyemchukulia kuwa kama Baba yake mzazi.
****CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Hali ya Andrew bado ilikuwa ni ya kusikitisha, hakuwa akizungumza lolote, alibaki akitazama huku akiwa amelala kitandani. Mwili wake ulikuwa umedhoofika mno. Mama yake kila alipokuwa akimuangalia machozi yalikuwa yakimbubujika, alikuwa akilia machozi ya uchungu wa mwanaye aliyekuwa akiendelea kuteseka pale kitandani.
“Mwanangu amka basi uzungumze na mimi mama yako, amka mwanangu,” alisema mama yake huku machozi yakiendelea kushika hatamu yake.
Andrew hakuweza kufanya mtihani wa kidato cha nne kutokana na ugonjwa aliokuwa ameupata. Hilo lilizidi kuwa ni pigo kwa mama yake ambaye alihangaika kumsomesha miaka yote lakini nguvu zake zilionekana kugonga mwamba.
****
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment