Search This Blog

Sunday, July 10, 2022

GANZI YA MOYO - 2

 







    Simulizi : Ganzi Ya Moyo

    Sehemu Ya Pili (2)





    “Kama huo haukuhusu wewe, basi sidhani kama hayo mavazi yanakuhusu pia. Pili, usiseme hata dada yako hayamhusu, mwache aseme yeye mwenyewe.” Adv. Mkenge aliongea huku akichukua karatasi ile na kumpatia Shangazi wa Win. Dickson akakaa kimya.

    Shangazi mtu akaanza kuiangalia ile karatasi huku saa nyingine akiileta karibu kabisa macho yake kama aangaliaye maandishi madogo au kitu kidogo kinachotakiwa kuangaliwa kwa ukaribu zaidi. Hapo mguu wa Win ukasogea kiuficho na kumkanyaga Ibra na kumfanya ashindwe kuvumilia na kujikuta akicheka lakini cheko ile aliibadilisha na kuwa kikohozi kikali kilichofanya asishtukiwe kuwa alikuwa akicheka.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Mwanangu, unadhani mimi naona basi hapa kitu? Hata miwani yenyewe sina.” Shangazi mtu akaona isiwe tabu, ya nini kuzuga unasoma wakati kusoma kwenyewe tatizo? Ikabidi ajitetee kwa kuisingizia mawani.

    Acheni tu, ukitaka kudhulumu kwanza jipange. Sio hujui hata maana ya hati ya nyumba kwa kiingereza, halafu unataka kufanya dhuluma, utaaibika hivihivi.



    “Embu leta hapa.” Dickson alimpora karatasi ile Dada yake na kuanza kuipitia kwa umakini huku ofisi nzima ikiwa kimya.

    Baada ya dakika chache, alikuwa kamaliza kilichoandikwa na nadhani kijasho chembamba kilikuwa kinamtoka mgongoni na kutambaa kwenye mfereji wa uti wa mgongo na kushuka hadi chini kwenye ‘mstari wa neva’.







     SHERIA.



    Ukiijua haki yako ni ipi na unaihitaji kwa wakati gani, basi unaweza kuhamisha mlima tok sehemu moja kwenda nyingine. Kusimama kwenye sheria ni njia ya busara kuliko kupinda nje ya sheria. Maisha ya kudhurumiwa hata kile ambacho umekitafuta kwa jasho lako, yakupasa kuachana nayo na kuanza kuijua sheria kuwa ipo n itakusaidia kukutoa katika udhandiki ambao umejikita kwenye mioyo ya wenye chuki.



    Hakuna jambo zuri kama kuijua sheria na kucheza nayo. Na hakuna jambo tamu kama sheria hiyo ikaenda katika mstari ambao unatakiwa, yaani bila kupindishwa. Fuata sheria, haki yako ipo huko.



    ENJOY.



    “Kwa hiyo sasa kwani, sasa kwani ndiyo kwani eeh…..” Maneno yasiyokamilika yalianza kubwabwajika toka kinywani kwa Dickson Gaula.



    “Mh! Mzee vipi.” Advocate au kwa kifupi Adv au kwa lugha yetu hadhimu ya Kiswahili, Mwanasheria Mkenge, alimuuliza bwana Dick huku akionesha mikono yake kwa msisitizo wa swali lake.



    “Kwani nini kimeandikwa hapo Kaka?” Shangazi wa Win alimuuliza Kaka yake huku yeye katandaza miguu yake mifupi mle ofisini kama yupo kwake. Na shingo yake iliyojichimbia ndani huku weusi fulani wa kung’aa uliokolezwa na mpangilio mbovu wa vipodozi, ukimpamba kwa mbwembwe, hata ungeambiwa yule mama ni mchawi, usingekataa hasa kwa wale wanaoweza kuhukumu kwa kuangalia.



    “Kwanza wewe ni nani wa kuandika haya.” Dickson alikuja juu na kumuuliza Mwanasheria. Wakati huo wote, Ibra na Win walikuwa kimya wakijitazamia burudani ya ajabu iliyoshushwa na wao wenyewe.



    “Ohooo! Samahanini sana wazee wangu. Naitwa Faustin Mkenge. Kampuni yangu inaitwa Mkenge’s Free Advocate au MF - Advocate. Ni kampuni ambayo watu wengi hutumia wanasheria wa hapa kuweka mambo yao kisheria zaidi. Na Bwana Elly au Eleutery kwa jina lake lote, alifanya hivyo hapa kwangu. Kama uonavyo, kuna sahihi yake na mhuri wake pia. Hapo kulia, kuna sahihi na jina la kampuni yetu, pia mhuri wetu.” Faustin Mkenge alimpa maelekezo na kujitambulisha kwa Dickson.



    “Kwa hiyo mnataka nini sasa.” Shangazi mtu aliuliza swali la kibwege kabisa. La kibwege kwa kuwa mali walizotaka kudhulumu, zilikuwa zinajieleza kwenye karatasi ile aliyopewa. Kutokana na elimu yake ndogo iliyoishia kidato cha kwanza, hakuweza kusoma lugha ya Kiingereza bali kusingizia kuwa hana mawani. Tatizo kubwa linalowasibu wadhulumaji wengi.



    Shangazi yake Win, enzi za ujana wake, alipata mimba akiwa kidato cha kwanza. Hali hiyo ilimfanya afukuzwe shule aliyokuwa anachukua masomo yake. Wazazi wake walimfokea sana tena sana. Kwa hasira zake, aliamua kwenda kuitoa mimba ile. Huko ndipo alipokutana na maswahibu yanayomfanya achukie watoto wa ndugu zake.

    Mimba ilifanikiwa kutoka, lakini wakati wa chakua-chakua ya kutumia vitu vya ncha kali wakati wa utoaji mimba, ncha zile kali zikagusa mfuko wa uzazi na kuutoboa. Hata daktari pori aliyekuwa anamshughurikia hakujua alichofanya, yeye alidhani amekwishamaliza kazi.



    Baada ya wiki moja, Shangazi yule alianza kupatwa na uchungu mkali sana wa tumbo. Akakimbizwa hospitali, huko akaambiwa kuwa mfuko wake kizazi umeoza, ni wa kuutoa tu. Ugumba ukaanzia hapo na chuki juu ya watoto wa ndugu zake, ukazaliwa. Chuki hizo zikaenda na kusababisha wivu juu ya mdogo wake Eleutery, kwa nini anamtoto na mali kuliko wao? Akawa wa kwanza kwenda kumrubuni kaka yake mkubwa ambaye naye licha ya kuwa na elimu kubwa tu, lakini MUNGU hakumpa mtoto wala mali, na hata mke pia kwa kuwa alikuwa hana nguvu za kiume. Wanawake walimkimbia kama wameona kimbunga.

    Kaka mtu akajiunga na dada mtu kwa ajili ya kumuhangamiza mdogo wao.



    “Mama,”Alianza kuita Mwanasheria wa Eleutery huku akiinua mgongo wake kutoka kwenye kiti chake cha kuzunguka na mikono yake kukita kwenye meza ya kiofisi iliyokuwa mbele yake. “Karatasi hiyo, inamaelezo yote juu ya mali za Bwana Eleutery Gaula. Mali hizo zote, licha ya wewe kuwa na hati zake pamoja na kadi za magari yake, haziwezi kuwa mali zenu kama Winfrida Gaula hajatia saini yake kwenye huu mkataba wa kuruhusu mali hizo.” Mkenge alitoa faili moja na kulionesha juu akimaanisha mle ndimo penye mkataba huo.



    “Embu tuone hapa.” Bwana Dickson akataka kufata lile faili, lakini Mkenge akamsimamisha kwa kumwoneshea mkono kama afanyavyo mwanausalama wa barabarani.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Haya utayaona mahakamani kesho au keshokutwa.” Dickson akawa mpole na kurudisha makalio yake taratibu pale yalipokuwepo mwanzo. Hakika yalikuwa yanamshuka yaliyokuwa yamempanda.

    “Lakini mimi sijawahitia hapa hayo. Nachotaka kuwaambia ni kwamba, malalamiko ya mwana wenu nimeyapata na ndio maana nimewataka mje hapa. Mnaweza kuongea na mwana wenu na kuyamaliza bila mahakama. Na pia mnaweza kwenda kutafuta mwanasheria, hata hapa wapo. Mkamueleza nia yenu na yeye akawasaidia kuja kutetea yanayowakabili.

     Mkifanya hivyo, msisahau kuja na vithibitisho vya umiliki wa mali mnazozililia,” Faustin Mkenge alikuwa anatoa maelezo yake vizuri kabisa na kuwafanya wazee wale wawe kimya kabisa. “Chaguzi ni lenu.” Alimaliza Mkenge.



    “Mimi nadhani nitaenda kutafuta Mwanasheria aje kutetea kesi hiyo. Vithibitisho tunavyo. Hati miliki tunazo, na kila kitu tunacho. Msitutishe ni mikataba yenu.” Dickson aliongea na kuungwa mkono na kile kipande cha mama kilichojitandaza kwenye kochi pekee la mle ofisini.



    “Sawa. Hamna tatizo. Ila nadhani Winfrida ana cha kuongea kabla hamjafika huko,” Mkenge aliongea hayo huku akimgeukia Win. “Win,”Alimuita Win na kumpa ishara ya kumruhusu aongee. “Go on.”



    “Kwa kuwa mnadhani huo ni mkataba wa uongo, na kwa kuwa mna-kila kitu mikononi mwenu, basi sasa natakiwa kuonesha kuwa hivyo mlivyonavyo haviwahusu. Kadi za benki zote mnazo nadhani, naanza na hizo. Hamtotoa hata senti moja baada ya nyie kutoka hapa. Tuone huyo Mwanasheria wenu mtamtafuta kwa njia gani. Labda kama mtatumia akaunti zenu za benki zisizo na hata na fedha ya kununulia maji ya Kandoro.” Win alimaliza na kutoa simu yake na kubofya namba kadhaa.

     Sekunde chache, aliweka simu sikioni na kufanya alichokusudia. “Funga hizo hadi nitakaposema fungua.” Amri ikatoka kumfanya Dickson atumbue macho kama anakamuliwa jipu au kakabwa na jinamizi.



    “Sijamaliza bado. Kule kwenye kampuni uliyopo Baba, ooh! Sorry, Dickson. Nakumbuka ulinikataza kukuita baba. Kule napo hutaruhusiwa kwenda tena kuanzia nilipokata simu hii. Na kama mmekuja kwa kutumia gari la baba yangu, nadhani mtakaporudi mtakuwa mnasaidia kuliweka mahala pake tu. Hamtoruhusiwa tena kwani hata nyumba mnayoishi kwa kujitanua kama matausi, itawabidi muondoke leo hii hii.” Win alimaliza maneno yake na kumfanya Shangazi yake kutoa jasho lililoharibu uso wake kutokana na vipodozi alivyokuwa kavipaka kuanza kuchuja pamoja na jasho. Hata pale alipojifuta, alijikuta anajipaka kitu kama rangi za jeshi usoni pake.



    “Sasa mwanangu tutaishi vipi mwanangu.” Shangazi wa Win aliamua kutoka pale kwenye kochi na kumpigia magoti Win huku akionesha sura ya huruma. Lakini yale marangi yaliyokuwa yamechujia usoni mwake, hakika hata wewe ungecheka. Na ndicho kilichotokea kwa akina Win na Ibra.



    “Leo hii nimekuwa mwanao?” Win aliuliza huku bado kicheko kikiwa kimemwandama. “Okay Aunt, usijali. Ila nataka uniambie wale Askari wanapatikana wapi.” Win alimuuliza swali ambalo Shangazi yake yule alibwabwaja kama kawekewa vocha. Akataja kituo walichowatoa na uongo mwingi walioutumia huku hongo ikiwa inatembea katika kituo kile kama Bwana Mapesa kakitembelea.



    “Sawa Aunt. Sasa fanya hivi, wewe na Dick, nendeni nyumbani. Kisha kachugueni chochote mnachokitaka. Kama ni nguo, bebeni zote, kama kitanda au TV au redio au chochote kasoro msivyoweza kuvibeba tu! Hata hati za nyumba chukueni, kisha ondokeni. Tukutane kesho mahakamani. Na kama mnaweza, bebeni hata nyumba muondoke nayo. Ila magari na vingine kama hivyo, hamtaruhusiwa kuvichukua kwani kutakuwa na walinzi wa kuvisamamia vitu hivyo.

    Vingine, chukueni tu. Masaa manne mtapewa na wale walinzi, zaidi ya hapo. Mtatolewa kama mbwa. Kazi ni kwenu.” Win alimaliza na kusimama kwa ajili ya kuondoka lakini Shangazi mtu alimng’ang’ania miguu huku akilia kwa nguvu akiomba amsamehe kwa yale yote aliyomfanyia.

    Win alikuwa akiangalia juu lakini sauti ya mama yule ilipenya vema mtimani mwake na kujikuta huruma ikimwingia. Mwema ni mwema tu.



    Hata alipomwangalia Baba yake mkubwa, aliona wazi anaangaliwa kwa macho ya naomba msamaha. Na alipomwangalia mwanasheria wa baba yake, aliona kitu kilekile. Lakini hakuwa tayari kufanya kile kwa wakati ule. Ikambidi afanye maamuzi magumu ya kuomba Shangazi yake amwachie miguu yake aliyoikumbatia kwa mikono miwili.



    “Niache niondoke bwana. Mimi si mwana wenu, mnakumbuka?” Win aliongea kwa hasira huku anajaribu kujing’oa toka mikononi mwa Shangazi yake. Mara ghafla Shangazi yake alimwachia na kuanza kubwabwaja mambo ya ajabu huku akilia na kugala-gala ndani ya ofisi ile.



     Elimu nayo ni kitu muhimu sana maana kule unaweza kujifunza hata kukaa na siri ndani ya moyo wako, lakini kwa Shangazi wa Win, kutikiswa kidogo tu, akajikuta anabwabwaja mambo ambayo kila siku Kaka yake, Bwana Dickson Gaula, alikuwa anamsihi awe makini asije akayaongea.



    “Yuwiii tata wee. Elly tulidhani tumefanikiwa kukuondoa ili tumiliki mali, lakini hakuna kitu tulichokipata hapa duniani zaidi ya kuaibika tu. Tutaenda wapi kuficha hizi sura zetu. Tutaenda kwa nani na haya madhambi yetu, yuwiiii tata weweee…” Shangazi kipande cha mtu, alisikika akilia hivyo hali iliyofanya ofisi nzima kubaki imeduwaa isiamini kile ambacho imekisikia sekunde chache zilizopita.



    “Aunt umesemaje?” Win alitaka kuhahakisha kama yale maneno kayasikia kweli toka kwa Shangazi yake au alikuwa anaota tu. Au labda kayasikia kwenye maigizo ya kwenye runinga.



    “Tumekulaza mchangani Elly kisa mali na wivu, tumekutoa duniani kisa hila zetu. Leo unatupiga makofi kupitia mtoto wako. Yuwiii.” Shangazi mtu ni kama alikuwa kaambiwa endelea kufunguka. Akazidi kubwabwaja maneno mengi zaidi ya haya uliyosoma.



    ‘Embu nyamaza mjinga wewe.” Ilibidi kaka yake amnyamazishe kwa kofi zito la kisogoni.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    MAPENZI.



    Mapenzi si maneno matamu au utanashati wako, au wewe ni nani katika hii dunia. Mapenzi ni kama ukuaji wa binadamu. Huzaliwa, hutambaa, husimama na baadae hutembea. Hata mapenzi hupitia njia kama hizo.

    Kwanza humuona mtu, unavutiwa naye, mnakutana na baadae mnakuwa wapenzi. Kuwa na maneno mengi matamu hayo si mapenzi kwa yule ambaye kayazoea kuyasikia maneno hayo. Mvuto au mali zako si kigezo cha kupendwa na mtu ambaye unadhani unatakiwa kuwa naye kimapenzi. Mapenzi ni hisia ambazo zinauteka ubongo wako kwa vitu vidogo sana.

    Mapenzi ni hisia ziutekazo moyo wako kwa udogo wa punje ya nusu ya sukari. Mapenzi si porojo dada na kaka zangu.



    ENJOY.



    “Ninyamaze nini. Wakati tumefanya ujinga huu kweli. Wivu na chuki zisizo na sababu ndo tumemuua mdogo wetu. Unataka ninyamaze nini? Tumeua hadi ambao hawana hatia, japo tunacheka lakini dhambi hii inatutafuna. Na njia pekee ya kuacha kutafunwa ni kusema ukweli tu. Tumemuua mdogo wetu na wazazi wa Win pamoja na Ibrahim. Hamna ubishi.” Sura mbaya ya mama yule ilikuwa inamuangalia kaka yake huku chembechembe za herufi fulani zikimtoka mdomoni na kutengeneza maneno yaliyoeleweka kwenye ubongo wa kila aliyeofisini.

    Kaka mtu ikabidi atulie tuli kama wale wengine ambao walikuwa wamekumbwa na butwaa la mwaka.



    “Kwa nini umewaua wazazi wangu?” Ni tendo la ghafla lilifanywa na Ibra na kujikuta kamkwida Bwana Dickson na kumbania ukutani.

    Win naye ni kama alikuwa kaamshwa usingizini na kujikuta akimkalia tumboni shangazi na kuanza kumkwangua kwa kucha zake, si wajua ugomvi za wanawake. Mara anakwangua, mara anafinya, mara anavuruga nywele za mtuhumiwa, basi ni shida tupu.



    “Kwa nini mmewaondoa wazazi wetu, wamewakosea nini?” Win aliongea kwa uchungu huku anaendelea kuvuruga kichwa cha Shangazi yake. Wakati huo Faustin Mkenge alishindwa kuamulia ugomvi ule hivyo akakimbilia nje ya ofisi ile kwenda kutafuta msaada.

    Baada ya dakika zisizozidi mbili, alikuwa amerudi na vijana watatu ambao wanafanya kazi katika kampuni ile na kuanza kuwachomoa wale vijana wenzao kutoka katika miili ya wale wazee ‘size’ ya kati.



    “Mjinga we.” Ni Ibrahim aliyekuwa kakamatwa na watu wawili alitupa tusi hilo dogo huku akibembea na kurusha teke la angani na likampata Bwana Dickson usoni.

    Bwana Dickson akatoa mguno wa maumivu kama mbwa aliyepigwa jiwe la mbavuni.



    “Mnafanya nini hiki ofisini kwangu?” Mkenge alifoka kwa hasira baada ya vijana wale wawili kutolewa miilini mwa watuhumiwa wao.

    Ibra na Win walikuwa wanapumua kwa kasi kama wametoka kukimbia mbio za mita mia tano. Wakati huo sura ya Bwana Dick ilikuwa imevimba baada ya kupokea dochi la kiatu cha Ibra na Shangazi mtu alikuwa kishasimama na kujibanza kwenye pembe mojawapo ya ofisi ile huku nywele zake zikiwa timu-timu na uso wake kuvuja damu ndogo-ndogo kutokana na kukwanguliwa.



    “Hawa wameua wazazi wetu. Au huoni hilo.” Ibra alifoka kwa hasira akijibu swali la Mwanasheria.



    “Kwa hiyo mkageuza ofisi yangu uwanja wa mapigano, si ndio eeh.” Faustin akatupa swali lingine lililokuwa gumu sana kwa Ibrahim. Ikabidi ainame chini kuonesha kuwa kakosa au tuseme kakubali kuwa kafanya kosa, hawezi kubisha.  “Nitawaacha humu ili muwaue vizuri halafu tuone kama mkono wa sheria utawasikiliza maelezo yenu. Acheni ujinga vijana.” Faustin alimaliza na kurudi katika kiti chake.

    Si Ibra wala Win, wote walikuwa wapole na kufanya wale waliowaamulia kuwaacha na kutoka mle ofisini. Kazi ikabaki mle ndani, sheria na mambo mengine yakafata. Habari za kuchukua mali, zikapotea ghafla. Mjadala mkubwa ukawa juu ya mauaji ya wazazi wa wale vijana wawili.

    Mwisho wa yote hayo, ilikuwa ni Bwana Dickson na dada yake kupelekwa mahakamani na kusomewa mashtaka yanayowakabili.



    Kulikuwa hakuna chenga za hapa na pale kwani hakuna aliyekataa kosa siku ya kwanza tu, walipopelekwa mahakani. Japo baadhi ya ndugu wa Eleutery walihamaki na kudiriki kutaka kukataa, lakini ukweli ulibaki vilevile. Na hata hukumu ya vifungo vya maisha vilivyotolewa kwa watu wale, hakuna ambaye aliona wameonewa kwa sababu walikiri makosa.

    Mwisho wa ubaya, ukawa umefikia tamati kwa wale wazee. Sheria ikafanya kazi yake

    *****

    Miaka ikaenda na kupotea huku urafiki wa karibu ukizidi kuchukua nafasi baina ya Winfrida na Ibrahim. Mali zote za wazazi wa Winfrida, alikabidhiwa Win kwa kutumia sheria za nchi na siyo tena familia. Hata familia waliona ni sawa tu, na kwa kuwa Win hakuwa mtu mwenye makuu, alikuwa mstari wa mbele kuwasaidia ndugu wa baba yake na mama yake pia. Hakuwatenga kamwe. Aliwapa chochote wanachohitaji katika sehemu ya mali za wazazi wake.

    Hakuacha kuendesha mashirika aliyoyaacha wazazi wake. Alifanya kila kitu katika mpangilio uliovutia na kuwavutia wengine. Hayo ndio yakawa maisha mapya ya Win.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Lakini kuna jambo likawa linamsumbua sana moyoni mwanadada huyu. Licha ya kujaribu kuwa karibu na Ibrahim, hakuwahi kuhisi msisiko wa mapenzi juu ya kijana huyu msafi na mzuri wa sura. Hakuwahi hata mara moja.

    Ibrahim alikuwa ni bingwa wa kuongea maneno matamu na makali kwenda kwa Win, kama ujuavyo Wanasheria. Lakini kwa Win alikuwa anaona maneno yale ni ya kawaida tu. Yalikuwa hayamsisimui hata kinyweleo kimoja cha mwili.



    Maneno hayohayo ambayo Ibra alikuwa anayetema kwa Win, akienda kwa mwanamke mwingine na kuyatumia, basi mwanamke huyo anajiona kama Malaika. Kila muda humpigia simu Ibra ili apewe hayo maneno. Hata mtoto wa Raisi mstaafu wa Marekani ambaye alikuja Tanzania kujifunza Kiswahili, alijikuta akimsasambulia nguo zake zote Ibrahim na kumpatia usichana wake kwa sababu ya maneno yale matamu.

    Ibrahim alikuwa ndani ya penzi zito na kimwana Win. Lakini kila alipotupa kete zake, alikuwa kama anacheza kamali ya korokoro. Yaani anaambulia tabasamu la matumaini ambalo linamfanya aendelee kucheza kamali ile.



    Hali ile ya kuambulia tabasamu na maneno ya matumaini, yakawa yanatengeneza maswali. Ina maana yale aongeayo hayamgusi moyo Win? Au labda hayataki? Na maswali mengine kama hayo ndio yalichukua nafasi katika kichwa cha Ibrahim.

    Majibu yake yakawa ni kujaribu kwa wasichana wengine. Akatafuta wanawake kwa wanawake, matajiri kwa matajiri ili wasitamani pesa zake bali yeye. Wote aliowapata walikuwa hawalali usiku bila kusikia maneno ya Ibrahim.



    “Sasa tatizo ni nini?” Siku moja Ibrahim alijiuliza baada ya kutoka kuagana na mtoto wa Raisi mstaafu wa Marekani aliyekuwa kampigia simu ili asikie falsafa za Ibra.

    Ibra alijua kutumia ulimi kutengeneza maneno ya mapenzi. Lakini alikuwa hajui kuwa mapenzi ni hisia za mtu na si kupendwa kwa sababu ya ulimi wako kutema sumu na maneno ya kulevya wanawake.

    Hakujua kuwa kuna wanawake hawaambiwi wala hawasikii mbele ya mpenzi wao bubu. Sasa Bubu anamaneno gani matamu toka kinywani mwake? Hata hilo hakutambua, hata swali hakujiuliza. Na vipi wale wasiosikia maneno na wanaangukia katika mapenzi mazito juu ya watu wao. Hata hilo hakuliona Ibrahim.



    Yeye akawa mtu kutengeneza misemo kila kukicha. Hakujua kuwa si wanawake wote hutekwa kwa maneno matamu japo asilimia karibu tisini hutekwa. Kumi nzima hapo haipo, na hiyo kumi yawezakuwa Winfrida akawemo ndani yake. Hakujua hilo na hakutaka kulifanyia kazi bali kila siku alikuwa anatumia njia ileile iliyoshindikana.

    Mapenzi hisia na damu kuelewana. Wengine hupenda mwenza wao awe mcheshi na mwenye maneno mengi-mengi kama mimi Masai hapa. Tehe, msinitafute lakini.



    Na wengine hupenda mwenza wao awe kila muda kanuna, siriasi kama katili la kwenye filamu. Hayo yote ni mapenzi na jinsi ya kuteka hisia za mwenza wako. Ibra alikuwa na maneno mengi sana matamu na yenye mafumbo au mitego tuseme, maana Wanasheria navowajua wana-maneno ya mitego sana.

     Sema sisi wa nje ya sheria tunasema mafumbo. Na wao wanapendelea kuyaita mafumbo, ila mimi nasema mitego. Kwani swali moja anaweza kukuuliza mara mbili katika muda tofauti. Anaweza kukuuliza eti wakati marehemu anajipiga risasi wewe ulikuwa wapi? Halafu akaanza kukupiga maswali mengine ya kero kama mia hivi. Akiona umekereka, anarudi palepale mwanzoni, wakati marehemu anajipiga risasi wewe ulikuwa wapi? Na wewe kwa kuwa ulishakerwa na maswali, unajikuta unaropoka tu.

    Ukiropoka tofauti, tayari umempa ‘point’ za kuzidi kukubana. Sasa hayo si mafumbo, ni mitego tu. Tuwaachie wao hayo, yawezekana sipo sahihi au nipo sahihi, siwezi jua. Tuendelee na yetu.



    Ibrahim akawa bingwa wa kutengeneza misemo kwa ajili ya Win, lakini hakuteka hisia zake hata kidogo. Alishasahau kuwa mwanadada yule mrembo alikuwa ni bingwa wa lugha, hivyo maneno yale yalikuwa kama nyongeza ya elimu ambayo alikuwa hataki kuisikia tena kwa kuwa tayari alikuwa kaipata ya kutosha.

    Ibra akawa anajishangaa huku akijiuliza kwa nini. Na hata alipomfatilia Win, hakuona kama anamtu mwingine. Akashusha pumzi ndefu ya kukata tamaa. Kupenda anapenda, na kujitahidi kuteka hisia, anajitahidi sana tu. Na hata majaribio kadhaa alishayafanya kwa wanawake. Akajiona kama msaliti wa penzi lake. Akaamua kutulia bila kufanya majaribio tena bali kuendelea kujaribu kuteka hisia za Win.



    Winfrida naye kwa kuwa alikuwa hana hisia za mapenzi kwa mwanaume yule waliyekua kwa pamoja, akajiona kama hisia hizo hazikuwepo tena kwa wanaume wote wa dunia hii. Ni uongo, kulikuwa hakuna ukweli wa suala hilo alilolifikiria Win, kwani hatimaye alimpata yule aliyeamsha hisia zake.

    *****

    Ni Jumatatu moja ya saa saba mchana lakini ilionekana kama ni saa moja au saa mbili asubuhi kutokana na hali ya mawingu iliyotanda katika jiji la Mwanza. Hiyo ni baada ya mvua kubwa kunyesha siku ile na bado ilizidi kunyea ardhi ya jiji lile hadi muda ule ambao Win alikuwa anatoka kazini kwake.



    Akiwa ndani ya gari lake, alimwona mwanafunzi wa Sekondari akiwa kajikunyata pembeni ya banda la kusubiria usafiri wa uma (daladala mfano). Alikuwa kalowa nguo zake na kuonesha kuwa hali ile ilimtesa muda mrefu sana.



    .

     HISIA.



    Katika kila andiko lililotoka kichwani mwangu kuhusu mapenzi, sijawahi kwenda kinyume kuhusu mapenzi kuwa ni hisia.

    Hisia ndio nguzo pekee inayoendesha mioyo ya kila mwanadamu. Kama hun hisia, amini wewe hujakamilika. Hisia za moyo ndizo chachu ya maamuzi ambayo hapo kabla hujawahi kuyahisia na kuyafanya. Acha hisia zako ziendane na kukubaliana moyo wako, kubana hisia, ni kuumiza nafsi na moyo wako.



    ENJOY.



    Win akashuka toka garini mwake na kumfuata yule mwanafunzi aliyekuwa peke yake pale kwenye kibanda. Win akafungua mwamvuli aliokuwa kaubeba ndani ya gari lake, na kisha akamfuata yule kijana pale kwenye kona aliyokuwa kajikunyata huku kachutama.



    “Kijana.” Win alimuita yule Mwanafunzi ambaye aliitika kwa kumwangalia usoni.

    Hapo Win alikutana na sura nyeupe huku macho yakiwa ndani ya miwani ya macho. Hakusisimka kwa wakati ule, bali alimuonea huruma kwa jinsi meno yake yalivyokuwa yanagongana kwa sababu ya baridi iliyokuwa inachukua nafasi wakati mvua ile ya lasha-lasha ikiendeleza tambo zake Jijini Mwanza.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Nyanyuka twende kwenye gari langu lile pale.” Mwanafunzi yule wala hakuwa na mapozi ya kujivunga-vunga, mara moja akasimama na kwenda na Win kwenye gari lake.

    Aliponyanyuka, ule urefu wake uliomzidi kidogo Win, ulionekana na kumfanya Win anyooshe mkono kidogo kwenda juu ili asimguse-guse kichwani kwa mwamvuli yule mwanafunzi aliyekuwa tepe-tepe sababu ya kulowana mavazi yake.



    Mwanafunzi aliingia nafasi ya nyuma ya gari lile na Win hakuchelewa kuanza kumpa huduma muhimu itakayoondoa baridi mwilini mwa kijana yule.

    Akafungua kiyoyozi cha joto kilichomo mle ndani ya gari. Na kisha akampa sweta fulani ambalo alikuwa nalo mle ndani ya gari. Kijana wa watu bila kuuliza, akafungua vifungo vya shati lake la shule na kuliondoa. Hakuishia hapo, ile vesti aliyokuwa kavalia ndani ya shati la shule, nayo akaitoa na kubaki kifua wazi.



    Winfrida akiwa tayari kaingiza gari barabarani, aliweza kushuhudia kifua kipana lakini kichanga na cheupe cha kijana yule. Kwa mara ya kwanza akahisi kusisimkwa kwa kumwangalia tu yule kijana wa kiume. Akajikaza kiuanamke huku akimeza funda mbili, tatu za mate ya uchu.



    “Unakaa wapi kijana.” Win alimuuliza baada ya kijana yule mwanafunzi kuvaa sweta alilopewa na kuwa na ahueni kwa baridi ile kupungua.



    “Mimi nipo hapahapa Nyegezi karibu na pale uwanjani.” Alimjibu.



    “Na unaitwa nani?”



    “Naitwa Edson.”



    “Edson Kuku au?” Aliuliza huku akitabasamu Win.



    “Hapana. Edson Lake.”



    “Kwa nini upo pale hadi sasa hivi Edson.”



    “Nimekosa nauli ya kurudia nyumbani. Nimefukuzwa ada tangu saa nne. Nikatoka pale shuleni hivyohivyo na mvua, ndo’ nikaenda pale uliponikuta kwa ajili ya kusubiri mvua ipungue ndio niende nyumbani.” Edson alimjibu Win.



    “Oooh! Pole sana. Unadaiwa shilingi ngapi shuleni?”



    “Kule nadaiwa elfu thelathini kwa ujumla.” Win akatikisa kichwa kwa masikitiko baada ya kusikia mtu anarudishwa nyumbani kwa kuwa kakosa elfu thelathini ambayo yeye anaichoma kwa siku kwa ajili ya kujaza mafuta kwenye tanki la gari yake.

    Ama hakika kama hujui thamani ya kitu, MUNGU hukuonesha bila wewe kujua kama ni MUNGU ndiye kafanya hivyo. Win alioneshwa na MUNGU ni kiasi gani hiyo fedha anayochoma mafuta watu wanaihitaji kuliko yeye.



    “Okay. Pole sana. Basi twende kwanza nyumbani. Halafu utabadili nguo na kupata chakula, kisha nitakusindikiza hadi kwenu.” Win aliongea huku akikata mitaa ya Nyegezi kwa kutumia gari lake. Edson hakuwa mbishi.



    Walipofika nyumbani kwa Win, Edson alikuwa ni mtu wa kushangaa tu, asiamini kama kuna binadamu anaishi maisha matamu kama yale. Wafanyakazi nadhifu wa mle ndani pamoja na samani zilizozagaa kila pembe mwa nyumba ile, zikamfanya aamini hayo.



    “Karibu Ed…son.” Win alimkaribisha huku akiwa hana uhakika wa jina lile analomwita Edson kama analipatia au.



    “Waweza kuniita Eddy pekee, yatosha.” Edson akamrahisishia mambo dada wa watu na Win akajikuta mwenye kutabasamu baada ya maneno hayo ya Eddy.



    “I think it will be better, than to call you full alphabets of your name. (Nadhani itakuwa vema kuliko kutamka herufi zote za jina lako)” Win aliongea kwa Kiingereza bila kujitambua kutokana na Umagharibi kumkaa sana.



    “I saw that too, that’s why I simplify the things. (Nimeona hilo pia, ndio maana nimerahisisha mambo)” Edson alimjibu na kufanya Win akodoe macho na kutoamini kama maneno yale yametolewa na kijana yule ambaye licha ya kuonekana fukara, pia alionekana hamna kitu darasani.



    “Unasoma kidato cha ngapi?” Win alimuuliza huku akimruhusu akae kwenye kochi moja mle sebuleni.



    “Hapana dada, nimelowa.” Edson alionesha hofu ya kulowanisha makochi ya pale.



    “Just sit. Oh! Sorry. I mean, we kaa tu.” Win alikuwa anajing’ata-ng’ata sana kutokana na kutumia Kiingereza mahala pasipo kuwa na uhitaji huo.

    Alikuwa anakipenda sana Kiswahili, hivyo kitendo cha kuwa anachanganya madawa ya lugha, kilikuwa kinamkera sana. Si yeye mtumiaji pekee ndio kilimkera, bali hata waliomsikiliza hasa hawa wafanyakazi wake ambao aliwatoa kijijini na elimu yao ilikuwa unga-unga mwana.



    “Nipo kidato cha tatu dada.” Alijibu swali la Win, Edson alipokaa kwenye kochi kama alivyoamriwa.



    “Kidato cha tatu unaongea kiingereza kilichotulia kama hicho? Na tena si kidato cha tatu kilichokamilika, ni mwezi wa pili huu. Hivyo umeingia kidato cha tatu mwezi uliopita. Na isitoshe kwa hiyo nembo yako ya shule, inaonekana wazi unasoma Shule ya Kata ambazo shule hizi Serikali yetu imezipa kisogo kabisa.” Winfrida aliongea maneno mengi lakini ukweli ulibaki palepale tu, kuwa Edson alikuwa kidato cha tatu.



    “Ndiyo hivyo dada yangu, kiingereza ni lugha tu ambayo ukiikazania sana unaiweza.”Alijibu Edson baada ya maneno mengi ya Win.



    “Haya bwana. Hongera kwa kukijua mapema Kiingereza.” Win alimpa hongera huku akinyanyuka na kuanza kuondoka pale sebuleni kwa lengo la kwenda chumbani kwake.

    Huku nyuma akampa upenyo Edson ya kumtathimini vizuri uzuri wake ambao alikuwa anautazama juu juu hasa usoni tena pale anapoombwa na Win mwenyewe amtazame usoni.



    Hatua kama tatu, Win ni kama alikuwa kashtukia kuwa kijana yule anamtazama. Akageuka kwa kushtukiza na kweli alikuta macho ya Edson yakimwangalia umbo lake hasa ile kuanzia kiunoni kushuka chini.



    “Na wewe una-tabia za mtaani?” Win alimuuliza Edson ambaye baada ya Win kugeuka na kumwona, yeye alirudisha macho yake chini haraka na kujifanya alikuwa hajamwangalia.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Am, am, am.” Edson akawa wa kujing’ata bila kutamka neno. Mara Win akasitisha safari yake na kurudi kwenye kochi alilokuwepo mwanzo huku uso wake ukiwa umekunjamana kwa ghadhabu. Edson akawa mtu wa kumchungulia mwanadada yule kwa jicho moja tu.



    “Nakuuliza. Na wewe una tabisa za mtaani?” Win alirudia tena swali lake.



    “JICHO.” Edson alitamka neno hilo huku akionesha kwa kidole cha shahada jicho lake. Win akawa katulia asijue ni nini kijana yule anataka kuongea.



    “Baba aliniambia, jicho linaponza mwili.

    Jicho linaweza ua, jicho ni silaha kali.

    Hutambua, hukosoa, pia husema ukweli.

    Jicho langu limeona, jicho langu limekwaza.



    Mama hakukosa neno, hichi ni kiungo tete. (Huku anaoneshea kidole jicho lake)

    Jicho si kama mkono, japo hugusa chochote.

    Linaweza ona nono, likadhani ni ubwete.

    Jicho langu limeona, jicho langu limekwaza.



    Samahani dada yangu, jicho langu limekwaza.

    Nono li jichoni mwangu, kweli hilo nimewaza.

    Nikiwazacho ni ukungu, ni fikra kuzipendeza.

    Jicho langu limeona, jicho langu limekwaza.



    Jicho hili ni silaha, leo mwili lauponza.

    Laumbwa kiufasaha, kuliko viungo wenza.

    Nakuomba msamaha, nipo chini kama funza. (Edson akashuka kochini na kuanza kugala-gala)

    Jicho langu limeona, jicho langu limekwaza.



    Edson akamaliza shairi fupi ambalo alilitunga papo kwa hapo na kumuimbia Win ambaye muda wote alikuwa kama haamini kile anachokisikia masikioni mwake na kukiona. Alikuwa kimya kwa muda mrefu akitafakari ujio wa kijana huyu matata.



    Kwanza alimsisimua garini wakati wanakuja nyumbani kwake. Ikawa ni mara ya kwanza kusisimka baada ya kuona kifua cha mwanaume. Sasa kaisisimua akili yake ambayo ilikuwa haijawahi kusisimuliwa kwa maneno licha ya kuyasikia mara zaidi ya milioni kutoka kwenye vinywa mbalimbali vya wanaume.



    “Nimepatikana.” Win alijiwazia kichwani baada ya mawazo yale machache kupasua ubongo wake. Hakika alipatikana, hata alipomwangalia mara nyingine kijana yule aliyekuwa kapiga magoti huku kajiinamia akisubiri hukumu yake, alijihisi kutaka kumkumbatia, lakini alishindwa.



    “Inuka ukae. Nakuja sasa hivi.” Win alikata shauri na kuondoka eneo lile la sebuleni haraka kabla hajafanya uamuzi wa ajabu mbele ya kijana yule aliyemwokota mjini.

    Edson akashusha pumzi ndefu aliyokuwa kaibana kwa sababu ya uoga. Hakujua kama tayari alikuwa kamteka ubongo na akili mwanamke yule. Hakujua kama tayari kinono alichokiona kwenye jicho lake, naweza sema jicho la bahati. Tayari kinono hicho kilikuwa kimekubali kuwa cha ubwete kwake. Edson akarudisha mwili wake kwenye kochi na kukaa ili kumsubiri mwanadada yule.



    Hivyo ndivyo mapenzi huanza kujengwa. Mapenzi ni kama kutengeneza chai. Unaenda hatua kwa hatua. Utatenga sufuri motoni, utatia maji, utasubiri yachemke, utaweka majani ya chai na baadae utamalizia sukari. Sukari ndio kila kitu kwenye chai ya Kitanzania. Nasema Tanzania kwa sababu nchi nyingine hasa China, huwa hawaweki sukari kwenye chai yao. Hunywa chai kama kahawa.



    Na mapenzi yapo hivyo. Yatengee muda wake na kuyapa nafasi akilini. Tia hisia za mapenzi akilini baada ya kuyawekea muda. Subiri mtu muafaka aje kwa ajili ya mapenzi hayo, usikurupuke kumwagia majani ya chai kwenye maji yasiyochemka, kwa sababu yakichemka yatafuruma, yatamwagikia motoni. Utapoteza kiasi cha chai yako uliyoitenga.





    MOYO,

    Moyo ni kiungo ghali naweza kusema kuliko vyote katika mwili wa binadamu. Moyo ukisimama, basi ujue na maisha yako ndio yamesimama. Lakini mikono ikisimama, haimaanishi kuwa ndio umekufa au macho au mdomo. Hivyo moyo ndio kila kitu katika mwili wa binadamu.



    Lakini moyo naouzungumzia mimi, ni huu unaomaanisha hali Fulani. Kuna mioyo ina hali ya ukatili, na mingine hali ya huruma au moyo wa kutoa. Basi kama MUNGU kauumba moyo wako katika hali Fulani, heshimu hali hiyo. Moyo ndio kila kitu katka maisha ya binadamu. Heshimu hisia zitokazo katika moyo wako kuliko kichwani mwako.



    ENJOY.



    Baada ya kumpata mtu unayedhani unampenda, weka vionjo kwenye mapenzi yako. Weka sukari katika mapenzi yako, lakini hakikisha sukari hiyo isizidi wala kupungua kwani itakuwa kero ndani ya mahusiano. Kila mara wewe ni wa kupiga simu na kuanza kuongea misemo ya mapenzi na nahau kama vile mhenga, haileti ladha hasa kwa yule aliyezowea kuyasikia maneno hayo mengi kama kuku katoka kutaga.



    Mapenzi ni kama muunganiko wa punje moja ya mchele ambayo inatengeneza wali jikoni. Mapenzi ni kama punye moja ya sukari ambazo ukiziweka kiasi fulani kwenye chai, huifanya chai iwe na ladha ya kipekee.

    Hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa Win. Japo alikuwa haamini kuwa ipo siku itatokea akasisimkia mwanaume, lakini alijiweka tayari katika mapenzi. Hakutaka kuzama ndani ya mapenzi ambayo hayakuwa sahihi kwake. Sasa kakutana na huyu kijana wa kidato cha tatu, Edson Lake.

    *****



    “Karibu huku mesini Eddy.” Edson alitolewa katika mawazo aliyokuwa kayajaza kichwani kwa sauti ya Win.

    Akaenda moja kwa moja huko mesini ambapo ni maalumu kwa ajili ya kupatia chakula au kifungua kinywa.



    Alipofika chumba kile, alikuta meza imeandaliwa ipasavyo. Kila aina ya vinywaji laini, alivishuhudia pale mezani. Kila aina ya kifungua kinywa aliweza kuvitia machoni. Kila aina ‘makorokocho’ ya kula, yalikuwa yanamtazama pale alipoyatazama. Akatikisa kichwa chake kuonesha kuwa kakubali kuwa kuna watu wanajua kutumia fedha kwa kuijenga miili yao.

    Alipoangalia kwenye meza ile, ambacho yeye aliweza kukijua kwa haraka ni Juisi ya embe na boksi la maziwa ‘freshi’. Vingine vyote vilikuwa vigeni kwake.



    “Karibu Eddy.” Win alimkaribisha tena Edson lakini Edson bado alijiona kuwa hayupo sawa hasa katika baadhi ya mavazi ya chini aliyovaa, yalikuwa yamelowa.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Ohoo. Halafu ujue umenisahaulisha kutokana na shairi lako lile. Nilikuwa nataka nikakuchukulie nguo chumbani, ila wewe ukaanza utani wako.” Aliongea Win huku akiwa anatabasamu mwanana usoni pake.

    Akatoka pale mesini na kuelekea chumbani tena. Alipotoka alikuwa kakamata nguo za kimichezo (tracksuit) na kumkabidhi Edson na kumwonesha sehemu ya ufichoni atakayoitumia kuyaweka au kuyavaa mavazi yale.



    Baada ya dakika mbili, Edson alirudi na kuungana na dada yule.



    “Eddy, tumia chochote hapo. Jisikie upo nyumbani.”Win aliongea huku bado tabasamu limetawala usoni.



    “Lakini hivi vitu mi sivijui. Siwezi kuvitumia. Nataka chai tu.” Edson alijitetea maana kuna wengine wakikaribishwa na wapenzi wao kama hivyo, basi kila chakula watagusa. Matokeo yake huwa ni kuchafuka kwa tumbo na baadae kwenda kuchafua maliwato. Edson hakutaka aibu kama hiyo.



    “Okey basi. Kunywa hii juisi au haya matunda. Yanaitwa stroberi, unachovyea humu kwenye Vanilla.” Alisogezewa hivyo vitu Edson. Akachukua boksi lililokuwa na juisi na kumiminia kwenye gilasi mojawapo kati ya nyingi zilizokuwa zimeletwa pale mezani.



    “Sasa unakunywa juisi peke yake?”Win aliuliza kwa hamaki.



    “Nimekwambia nataka chai, umenipa hivi. Sijui hata kimoja hapo zaidi ya hii juisi.” Edson alimjibu huku akiweka gilasi juu ya meza baada ya kupiga funda moja la kistaarabu.



    “Okey. Basi chukua na haya matunda, sitaki useme nayo huyajui.” Win alimsogezea sahani moja baada ya kuifunua. Ilikuwa na matufaa sita.



    “Unajua nini dada.” Edson akakatishwa kabla hajaendelea.



    “Niite Win. Naitwa Winfrida Gaula. Niite Win tu, yatosha.”



    “Sawa, nitafanya hivyo.”



    “Ehee, niambie ulichokuwa unataka kuniambia.”



    “Mama yangu anahitaji hivi vitu kuliko mimi navyovihitaji. Yupo kitandani nyumbani. Mwezi wa tatu huu hawezi kunyanyuka wala kujigeuza. Awezacho yeye ni kuongea, tena kwa shida. Kula kwetu ni kwa shida, na maisha kwa ujumla ni ya shida. Sasa napoona unanijazia mimi hivi vitu wakati tangu asubuhi sijui mama yangu kala nini, sijui anaendeleaje na mvua kubwa hii iliyonyesha, nakuwa napata mashaka na hali yake huko nyumbani. Tafadhali, naomba nivibebe nikampe mama yangu, nitakula naye huko kwa furaha kubwa sana. Hapa utakuwa unanilazimisha tu. Ni chai pekee ndiyo inaweza kuingia mwilini kwani nahisi baridi.” Maneno mengine yakagusa moyo wa Win.



    “Kwa nini huyu kijana anapoongea maneno akiwa siriasi yananigusa sana moyo wangu?” Win alijiuliza wakati yupo kwenye gari lake anaelekea anapoishi Edson na mama yake. “Nimesikia historia kama hizi kwa wangapi? Kwa nini huyu aisisimue akili yangu namna hii? Nataka kupenda nini? Ooh! No. Not this one, please GOD.”



    “Kata hapo, nyumba ya kwanza ndio nyumbani.” Win alikatishwa mawazo yake kwa sauti ya Edson ikimwelekeza pa kupita ili afike kwao.

    Win akafanya alichoelekezwa na sekunde kadhaa alikuwa kasimama nje ya nyumba ambayo alikuwa anaishi Edson Lake na mama yake.



    Ilikuwa ni nyumba ndefu lakini haina ubora kabisa. Mabati hata milango yake, ilionekana wazi ni nyumba ambayo haijafanyiwa ukarabati kwa muda mrefu. Licha ya hayo, pia katika ukuta wake wa mbele kulikuwa kuna alama kubwa ya X kwa chini yake iliandikwa BOMOA.



    Ilikuwa ni nyumba ya kupanga lakini kwa wale watu wa hali ya chini sana. Edson akagonga mlango mmojawapo na hapo msichana mmoja mwenye umri kati ya miaka kumi na minne na kumi na sita, alifungua mlango.



    “Anaendeleaje mama.” Edson alimuuliza binti yule. Wakati huo Win alikuwa nyuma yake akifatilia kwa makini kila jambo.



    “Yupo vilevile kama siku zote.”Alijibu yule binti na hapo Edson alimuomba aingie ndani na kufuatiwa na Win ambaye alikuwa amekamata mifuko miwili mikubwa ya ‘super market’ na mwingine mmoja alikuwa nao Edson.



    Licha ya nyumba ile kwa nje kuonekana chakavu lakini ndani, wanapoishi wakina Edson, kulikuwa ni pasafi kuliko Win alivyodhani. Hali ya hewa ilikuwa ni safi japo mama wa Edson alikuwa ni mtu wa hapo-hapo.



    Macho ya Win yalituwa kwenye mwili wa Mama Edson na kushuhudia hali aliyokuwa nayo mama yule. Mipira ilipita puani na sehemu nyinginezo ziwezazo kupitisha taka au chakula kasoro mdomoni.



    “Eddy. Huyu nani.” Mama Edson alimuuliza Edson kwa sauti ya chini.



    “Ni rafiki yangu. Kanisaidia leo.” Edson alijibu huku anamkaribisha Win aje pale alipolala mama yake.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Umemsaidia mwanangu?” Mama Edson aliuliza huku anakipapasa kichwa cha Win na tabasam likiwa limemtawala.



    “Ndiyo mama. Unatatizo gani lakini.”Win alijibu kwa heshima na kuuliza kwa unyenyekevu uliojaa huruma ndani yake.



    “Usijali mwanangu. Kwa kuwa umemsaidia mwanangu, umenisaidia na mimi pia. Najua hadi mwanangu kakubali kuwa kasaidiwa, ni kweli alikuwa anahitaji msaada. Asante sana.” Mama Edson alizidi kumshukuru Win tena na tena kila alipoongea.



    Win alikaa nyumbani kwa akina Edson hadi muda wa usiku. Alikula na kunywa nao na baadae akapewa mkasa mzima uliomtokea mama yake hadi ukamfanya ‘apararaizi’ sehemu kubwa ya mwili.

    Win akaahidi kuwasaidia kadiri ya uwezo wake.

    *****



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog