Search This Blog

Sunday, July 10, 2022

GANZI YA MOYO - 1

 





    IMEANDIKWA NA : FRANK MASAI



    *********************************************************************************



    Simulizi : Ganzi Ya Moyo

    Sehemu Ya Kwanza (1)

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kama kupenda ni sheria, basi nitakuwa tayari kuivunja. Na kama kupenda ni matakwa ya mtu basi nitapigana kufa na kupona ili nami niwe mmoja wa matakwa hayo.



    Nitalia ndani ya moyo na kulia nje ya uso wa nimpendaye hadi anielewe ni jinsi gani mwenzake navyohangaika juu ya upendo nilionao kwake.

    Lakini kama moyo wake tayari una mmiliki mwingine, ni kheri nijiweke pembeni kuliko kufanya fitna ambayo mwisho wake huwa tatizo katika maisha haya ya binaadam yenye wingi wa fitna hizo. Sipo tayari kukukosa kwa sababu upo na mtu, na sipo tayari kufanya fitna ili nikupate. Acha nikupende kadiri na niwezavyo. Uliyenaye, acha awe wako daima, mimi nitabaki na Ganzi Yangu Ya Moyo.



    ANZIA HAPA.



    “Win kwa nini unanifanyia mimi hivi? Embu niangalie mwenzako navyolilia penzi lako. Hivi kweli upo tayari kabisa kusema hunitaki kwa sababu ya kale katoto? Kweli Win? Ni kweli kabisa hunitaki kwa sababu ya mtoto wa Sekondari?



    Atakupa nini yule anukaye maziwa? Atakupeleka wapi yule asiyejua kuoga? Kwa nini Win? Embu niangale mimi. Niangalie vizuri tena.

    Hivi mimi naweza kukutenda kweli Win hadi utoe uaminifu wako kiasi hicho juu yangu na kumpa yule mtoto mdogo? Kwa nini unanitesa namna hiyo? Ona navyokonda kwa mawazo tukufu juu yako. Ona chozi langu hadimu kuliona linavyotiririka kutoka kwenye mboni zangu. Ona sura yangu ilivyokuwa ndogo kwa ajili ya kusinyaa kwa machungu juu yako.

    Niangalie Win, usithubutu kuangalia chini wala pembeni hata kidogo. Niangalie hata mavazi, kweli mimi ni wakuvaa hivi Win? Kweli kabisa unanikataa mimi kisa yule mtoto?” Ni sauti yenye uchungu ilikuwa inamtoka Ibrahim Singa kwenda kwa msichana mrembo aitwaye Winfrida Gaula.

    Wakati huo Ibrahim alikuwa amemuomba Winfrida watoke na kwenda sehemu moja tulivu kwa ajili ya maongezi.



    Huku wakiwa wanajipatia vinywaji ndipo Ibrahim alipoanzisha maongezi hayo ambayo yalianza muda mrefu sana. Hadi hapa walipofikia, kama machozi ya Ibrahim yangekingwa sehemu, angekuwa kajaza lita tano.



    “Sikiliza Ibra. Tena nisikilize kwa umakini mkubwa. Utoto wa Edson naujua mimi si wewe. Utamu wa Edson naufahamu mimi, si wewe mkurupukaji, uliyetoka huko na kuanza kukashifu watu. Hujui kuongea na mwanamke, hujui kubembeleza bali kulia na hujui kuomba bali kulazimisha.

    Mimi ni mwanamke, tena mwanamke shupavu. Nisiyetishwa na mavazi, fedha, mali na hata sura ya mwanaume yeyote katika dunia hii. Mwanaume nimpendaye, ndiye mwanaume anayenijali na kuwa muaminifu kwangu.

    Ufukara wake, mavazi yake, umbo lake, maisha yake na elimu yake, kwangu si kitu ili mradi nimempenda na nipo tayari kwa lolote kwa ajili yake. Nipo tayari kumgharamikia mavazi, chakula, elimu, malazi, miundombinu na mambo yote muhimu uyajuayo kichwani mwako. Na zaidi ya hayo, nipo tayari kufa kwa ajili ya Edson.” Maneno ya Win yalikuwa yanatoka kwa mpangilio kinywani mwake na kumfanya Ibrahim abaki kinywa wazi. Win alizidi kutiririka hisia zake.



    “Ooh, Edson Lake, fahari wa moyo wangu, fahari wa maisha yangu, fahari wa furaha yangu. Uko ulipo nadhani MUNGU anakuangazia mwanga wa amani ili uione sura yangu ambayo siku zote naitunza ili iwe kama ulivyoiona mwanzo. Oooh! My sweetie, nadhani upo salama.” Macho ya Win yalikuwa yamefumbwa wakati maneno haya yanamtoka na wakati huo, mikono yake alikuwa kaifumbata katika kifua chake kuonesha yupo katika hisia kali.



    “Embu ona ulivyokuwa Win, ni kama na wewe umekuwa mtoto. Yule wa nini Win? Eeh, nakuuliza Win, yule wa nini? Atakupeleka wapi katika maisha haya ambayo kila neno ni fedha? Atakuja kukudharau bure baada ya kumfanikisha. Njoo kwangu Win ili ujue thamani ya fedha, thamani ya upendo, thamani ya furaha, thamani ya pumzi yako, thamani ya elimu yako na thamani zote ulizonazo.

    Mimi ndiye nikupendaye kwa dhati, mimi ndiye nijuaye maumivu yako Win, mimi ndiye nayejua utakacho Win, mimi ndiye mwenye kila hali ya kukwambia nakupenda, na mimi ndiye mwenye uwezo wa kufanya chochote kwa ajili yako. Nakuomba Win, kuwa na mimi japo katika wakati huu wa mwisho wa hii dunia, japo na mimi hata nikifa niende kumpa taarifa Mzee Singa, baba yangu huko alipo kwa kumwambia nimekufa huku nampenda mwanamke wa furaha yangu, mwanamke wa maisha yangu, mwanamke aliyeteka hisia zangu, mwanamke aliyechukua moyo wangu na kukaa nao na mwanamke pekee mwenye uwezo wa kunifanya niache yote na kumsikiliza yeye.” Alizidi kutema cheche zake Ibrahim, muda huo hata juisi aliyoagiza ilikuwa chungu kupita kooni.



    Win alitabasamu kwa tabasamu lililodumu kwa sekunde mbili na kisha akafungua midomo yake mipana na legevu yenye kila hamasisho la kumfanya mwanaume yeyote atake kuzibusu au japo zitawanyike kwenye paji lake la uso.



    “Sikiliza Ibra. Na safari hii nisikilize kwa ubora kuliko kunisikiliza kwa makini. Mapenzi si kwa sababu tu! Yapo ndiyo tuingie, na wala si kwa sababu yameumbiwa binadamu basi na mimi nijilazimishe kupenda. Mapenzi ni kama pete Ibra, kama haikutoshi achana nayo.

    Na kama si imara, hata ikikaa kidoleni itavunjika na kama umetengenezea madini dhaifu itachakaa mapema sana, tena sana.

    Hivyo ndivyo itakuwa kati yako na yangu kama tukiwa wapenzi. Kwanza mapenzi yetu hayatutoshi, mimi na mali na wewe una mali, nani amsadie mwenzake? Muache masikini kama Edson wangu naye afaidi uwepo wangu, nampenda sana Edson, Ibra. Nikiwa ndani ya penzi na wewe, kamwe halitodumu, litakuwa kama ile pete iliyotengenezwa kwa madini dhaifu.

    Nakuona kama kaka yangu Ibra, sina hisia na wewe kabisa. Lazima mapenzi hayo yatavunjika. Na hata nikijilazimisha kukupenda, mwisho wa siku nitarudi palepale kuwa sikupendi. Na mapenzi hayo yatachakaa kwa kuwa hayakuandaliwa maandalizi yaliyo-bora kama inavyotakiwa.” Win alizidi kumkatisha tamaa kabisa Ibra katika mbio zake za kumpata mtoto yule ambaye waliishi na kukua pamoja katika jiji lile la Mwanza.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Wazazi wa Ibra ambao sasa hivi ni marehemu wote, walikuwa ni rafiki wakubwa wa wazazi wa Winfrida ambao sasa hivi nao hawapo katika dunia hii yenye shibe ya shida na wingi wa ubaguzi.



    “Lakini Win. Kwa nini unakuwa mwingi wa maneno na mchache wa kuelewa? Hivi kweli pendo langu unaliona kama madini yasiyo na ubora? Kwa nini usinipe nafasi ya mimi kukuonesha kuwa penzi langu kwako ni zaidi ya dhahabu, na ni zaidi yaaaa…” Hakumaliza kuongea Ibra, sauti ya mlio wa simu aliyokuwa nayo Win, ikaanza kutoa mlio wa kuita na bila kusita Win alifungua pochi yake na kuitoa.

    Alitabasamu baada ya kumsoma ambaye kafanya mlio ule wa simu kutokea. Na baada ya tabasamu lile, alianza kubofya vitufe vya simu yake kwa ajili ya kujibu mapigo kwa yule aliyekatiza maongezi ya Ibra.

    Alipomaliza akaiweka simu yake mezani, na kunyanyua macho yake tulivu kabisa. Macho yenye sifa ya kuitwa macho. Macho yenye kila hali ya matumaini ya kupendwa na kupenda katika dunia hii. Macho legevu mithili ya yule mtu ambaye anaumwa nusura ya kufa. Macho ya uviringo kama goroli na makubwa kiasi na yenye kupambwa rangi ya ghali kabisa kutokea kwa mwanamke hapa nchini Tanzania, macho yenye rangi ya kahawia. Aliyainua kumuelekezea Ibra, na bila kusita alimuomba samahani kwa kilichotokea kisha akampa ruhusa ya kuendelea kuongea.



    “Ndiyo hivyo Win.”Kwa mfadhaiko na unyonge mkubwa, Ibra alisikika katika ngoma za masikio ya Win.

    “Mimi si mwenye dhambi kwa kusema nakupenda wewe, ila mimi ni mwenye dhambi kwa sababu nimekupenda wewe. Pendo ambalo nitakuwa tayari kufanya chochote ili mradi uelewe ni kiasi gani nakupenda, kiasi gani nakuhitaji, kiasi gani upo moyoni mwangu na kiasi gani umeteka fikra zangu.” Aliongea Ibra safari hii kwa kifupi zaidi na kunyanyua glasi yake ya juisi ambayo ilikuwa imefunikwa vizuri ili nzi na wadudu wengine wasipate kutembelea na kuchafua kimiminika kilichomo humo.



    Kwa madaha na maringo, Win aliunyanyua uso wake mwembamba uliobeba pua ya Kisomali na nywele za Kiarabu. Huku rangi yake ya chokoleti iking’aa vizuri kabisa na kusababisha mwanga hafifu wa sura yake kupenya kwenye akili ya Ibra na kubakiza sura hiyo ambayo ilikuwa inautesa mtima na kuteketeza akili ya Ibra. Sura inayotesa maisha ya Ibra, na inatesa kila macho ya mwanaume atakayetupia jicho kwa mwanadada huyu.



    “Unajua nini Ibra, mimi kwa sasa siwezi kukujibu swala lako kwa kuwa nina mengi ya kuyafikiria na mengi ya kuyafanya. Umeniambia mengi yanayoweza kumfanya mwanamke yeyote dhaifu na asiye dhaifu kukuelewa na kukusikiliza ombi lako. Najua upo kweli katika uongeacho, hivyo na mimi nitakuwa kweli kwa nitakachokujibu. Naomba unipe muda wa kufikiria jibu sahihi la kukupa ili na wewe uridhike na kujiona mwanaume uliye-bora katika dunia hii. Naomba uniache mara moja niende, halafu nikifikiria cha kukujibu, nitakutafuta.”Alimwambia hivyo Ibra huku macho yake yakiwa hayana mgomo na kwepa-kwepa kwenye uso wa Ibra, ambaye baada ya kusikia hivyo alivuta pumzi ndefu na kuishusha kama katoka kushusha magunia mazito Kariakoo.



    “Okey. Sawa Win. Nimekubaliana na wewe na ninakuomba unipe taarifa ili nije kukusikiliza malkia wa masikio yangu, pambo la macho yangu, ahueni wa akili yangu, furaha ya……..” Hakumaliza tena sentensi yake, simu ya Win ilikuwa ikitoa mlio tena. Mlio ule ulikuwa ni wa ujumbe mfupi.

    Akaangalia na kutabasamu tena hadi meno yake meupe na yaliyopangika kistaarabu mdomoni mwake yakaonekana.

    Hakujua kama anazidi kumtesa Ibrahim Singa, hakujua kama alizidi kuufanya moyo wa Ibrahim uzidi kumpenda na hakujua kama anamfanya Ibra azidi kupanga mikakati kabambe ya kumuweka mikononi mwake.



    “Asante kwa kuniruhusu Ibra. Niamini kwa nitakachokiandaa kwa ajili ya kuja kukujibu. Nipe muda tu!”Aliongea Win baada kujibu ujumbe ule aliotumiwa kwenye simu.

    Sauti yake nyororo na ya kubembeleza, ilimfanya Ibra akae kimya bila kujua aseme nini baada ya maneno yale. Alikuwa kabaki akitizama tu wakati Win ananyanyuka kutoka pale kitini na kuanza kuondoka.



    Mwendo wake wa madaha na wa kunyata, uliwafanya wanaume wote wa pale kugeuza shingo zao na kumuangalia yeye akielekea kwenye gari lake la thamani kabisa kupata kutokea hapa Tanzania.

    Umbo lake maridhawa na lililojipinda vizuri maeneo ya kiunoni, liliweza kutengeneza namba nane matata ambayo kamwe huwezi kuipata maeneo yoyote duniani zaidi ya Afrika, hasa Tanzania.

    Lile vazi alilokuwa kaweka mwilini, ndilo haswaa liliufanya mwili wake uonekane kuwa unatingisha hasa maeneo ya nyuma alipokuwa kabebelea mizigo miwili iliyokuwa ipo kichokozi zaidi kuliko kuboha.



    Winfrida alipanda gari lake na kuliwasha kisha akatitia eneo lile huku akimuacha Ibra akiwa anapiga mwayo mmoja mrefu kutokana na kuchoka kuongea mbele ya mwanamke ambaye kwa muonekano alionekana hana mpango kabisa wa kuwa naye.

    Ibra alikuwa kama analazimisha pendo.Pendo ambalo tayari Win alilipeleka kwa mwananume mwingine. Mwanaume ambaye alimfanya Win awe anatabasamu kila akiona ujumbe zake kwenye simu.

    Naam. Ndiye huyo Edson Lake au Eddy kama alivyoitwa na wanafunzi wenzake wa kidato cha tatu, kama alivyoitwa na rafiki zake wa mtaani, na ndivyo hivyo hivyo alivyoitwa na wazazi wake pamoja na mpenzi wake Winfrida.

    Na wakati simu inaita kwenye maongezi yao pale mgahawani, ni Edson alikuwa anatuma ujumbe wa kumuomba Win waonane. Baada ya kupanda gari, Win alianza safari yake ya kwenda kwa Edson.



    **********CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    CHUKI.



    Kama chuki inaweza kuzaa furaha basi ningemuomba MUNGU aniongezee chuki ili furaha hiyo isinitoke maishani. Lakini kama chuki inaleta huzuni na maumivu mioyoni mwetu na tunaowapenda, basi MUNGU ailaani chuki na kwa yeyote atakayebahatika kuwa nayo, naye alaaniwe. Si kwa matakwa yangu, bali ya mwenye uweza wa yote katika dunia hii.



    Chuki ndio mwanzo wa wivu na maumivu katika maisha ya binaadamu. Chuki hiyo ndiyo haswa inayopandikizwa katika mioyo ya watu na kufikia kuitwa uchawi. Si uchawi wa kuroga bali uchawi kutokana na chuki iliyozama ndani ya bwawa la moyo wako ambao ni kama umeumbwa na kitu kisichopokea maumivu bali kutoa maumivu. Nashindwa kutaja kitu hicho, kwani hata jiwe nahisi husikia maumivu pale unapolitumia kufanyia kazi nzito au pale linapopigwa na jua.

    Hata moto husikia maumivu pale unapojiunguza katika mwili wake. Moyo wa chuki, sina cha kuufananisha katika maisha haya.

    Moyo wa chuki ni zaidi ya chuma jinsi ulivyokuwa mgumu, na ni zaidi ya sumu jinsi unavyoweza kuua. Moyo wa chuki, hata mwenye nao akajikata kwa kiwembe, hutoa damu inayoweza kutoboa ardhi au yabisi. Na kamwe huwezi kumjua mtu wa aina hiyo.



    ENDELEA. 



    Wazazi wa Winfrida, Bwana Eleutery Gaula na Josephina Simanyi, walifariki wakati Winfrida ana umri wa miaka ishirini na tatu. Akiwa tayari amekwishaielewa dunia, na zaidi ana elimu ya kutosha ambayo ilimsaidia yeye na rafiki yake Ibrahim kupata mali za wazazi wao bila kudhurumiwa na baadhi ya ndugu ambao muda wote walikuwa wanaomba wazee wale wafe ili warithi mali zile.



    Ikiwa ni majira ya saa sita za usiku, familia zile mbili zilizopendana sana. Familia ya wakina Ibrahim na familia ya Winifrida. Walikuwa wanatoka kwenye sherehe ya watoto wao wapendwa na wa pekee kabisa, Winfrida na Ibrahim ambao walikuwa wanapongezwa kwa kumaliza elimu zao za chuo. Wakati huo Winfrida alikuwa ndiyo kamaliza Oxfod na Ibrahim kamaliza sheria katika chuo cha Dar es Salaam.



    Usiku huo uliyokuwa wenye furaha kwa wazazi hao na watoto, uligeuka kuwa machungu yenye wingi wa huzuni kwa kila aliyeangalia kilichotokea.

    Siku zote familia hizi mbili zilipenda sana kuwaona watoto wao wakiwa pamoja na tena ikibidi wafunge ndoa. Hivyo baada ya kutoka kwenye sherehe ile, walifanya makusudi kuwaachia gari waliyokuja nalo wazazi wa Ibrahim, Bwana Ally Singa na Bi. Habiba Hamidu.

    Na baada ya kuwaachia gari hilo, wao walienda kupanda gari la wazazi wa Winfrida bila kujua wazazi wale walikuwa wana maadui wengi kwa sababu ya mali walizovuna. Maadui hao walipanga kuiondoa familia ile yote kwa pamoja na wao warithi mali hizo.

    Maadui hao hawakuwa wengine, bali ni Shangazi wa Winfrida au dada wa Bwana Eleutery wakiongozwa kwa ukaribu kabisa na Kaka wa Eleutery, Bwana Dickson Gaula.



    Kila kukicha maadui hawa ndugu walikuwa wanatabasamu na kujivika utu muhimu kwa familia ya Bwana Eleutery, lakini ndani yake walikuwa wanapanga jinsi ya kuindoa familia ile na kuifutilia mbali katika upeo wa dunia hii yenye kila sababu ya kuitwa dunia ya wanyama na ndugu wa Shetani.



    ******



    Siku hiyo ya sherehe, walipata taarifa kuwa wazazi pamoja na mtoto wao, wataenda kwenye sherehe hiyo kwa gari moja la familia. Hiyo ndio ikawa nafasi pekee kwao kutimiza lengo walilolipanga kwa muda mrefu sana, lengo lililochukua takribani miaka miwili kulipanga na kulisubiri.

    Walichofanya baada ya kupata taarifa hizo, waliandaa mtu atakayeharibu mtandao wa gari la wazazi wa Winfrida baada ya kufika kwenye sherehe ile. Baada ya kukamilisha mtu huyo, walimpa chake na kumwambia baada ya kazi hiyo wasionane naye tena.



    Mtu yule hakuwa na roho ya utu wala woga katika maisha yake. Alichofanya ni kwenda moja kwa moja kwenye maegesho ya magari, akalitafuta gari la Bwana na Bibi Gaula, na alipolipata akakata breki za gari lile na kuanza kupotea eneo lile huku akibofya simu yake kumpa taarifa Bwana Dickson kuwa kazi yake imekamilika. Bwana Dickson alipopata ujumbe ule, aliusoma na kisha akaufuta pamoja na namba ya mtu yule.



    “Leo ndio mwisho wa nyodo za hawa mbwa.” Aliongea Bwana Dickson akimuelekezea yale maneno Dada wa Eleutery.



    “Washenzi hawa, msyuuu.” Na dada naye kwa kejeli na wingi wa majivuno yaliyojaa ufedhuri na udhandiki uliokithiri moyoni mwake. Akajibu na kumaliza kwa msonyo mrefu, uliomfanya kaka wa Eleutery atabasamu kwa tabasamu lililokuwa na chuki iliyousiriba moyo wake mzima na kutengeza uzio wa ukatili pamoja na ubinafsi wa nafsi ulioifinyanga akili yake na kutengeneza vimelea vya kithilani katika mwili wake.



    Waliendelea kuwa kwenye sherehe ile kama watu muhimu kabisa kupata kutokea katika familia ile. Lakini endapo familia zile mbili zingeelewa ni nini kilicho mioyoni mwa watu wale wawili ambao wao waliwaheshimu kama ndugu na watu muhimu kabisa katika maisha yao, sidhani kama wangewapa hata uwezo wa kukaa nafasi za mbele kabisa kwenye ukumbi ule.



    ******



    Kwa upendo ambao ulikuwa hausemekani kutoka kwa Eleutery, alimuita kaka yake jukwaani na kumpa fursa ya kusema chochote kuwahasa wahitimu wale. Na zaidi Eleutery alimsihi kaka yake awe chachu ya familia ile. Hakuacha kumuomba kakaye aitunze familia ile kwa upendo na amani endapo yeye angetangulia.

    Ilikuwa kama kakiona kifo chake, lakini kutokana na MUNGU kuficha yatakayoonekana mbele, Eleutery hakujua ni nini kaka yake anawaza na ni nini kitakachomkuta baadae.



    Dickson, kaka wa Eleutery. Alikuwa akiongea kwa tabasamu pana na la kuvutia usoni kwake kana kwamba alikuwa hana kinyongo. Kumbe akili yake ailikuwa imejaa tope jeusi, lililoficha aibu na busara, utu na ubinadamu. Kinyume chake lilitengeneza wivu na chuki, dhuruma na ukatili vilivyoenda sambamba na sura yake mbaya, iliyomfanya akose hata mke.



    Aliongea kwa dakika mbili au moja na nusu, akawa amemaliza wosia wake. Wosia ambao ulivunja rekodi ya siku ile kwa kutolewa kwa muda mfupi zaidi, kwani hata yule msichana wakazi ambaye alichukuliwa kama sehemu ya familia katika familia ya akina Ibrahim, aliweza kuongea kwa dakika kumi.

    Lakini sababu kubwa ya Dickson kuongea kwa kifupi vile, ilikuwa ni kutaka sherehe imalizike na familia ile ya mdogo wake iondoke na gari ambalo lingeuchukua uhai wao.

     Kama subira kwa Dickson, ilishavuta heri sana, sasa imebaki heri ya shari ambayo imeutawanya moyo wa kaka yule pendwa wa Eleutery.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Hayo ndiyo maisha. Wakati wewe unampenda fulani kwa moyo na nafsi yako yote, yeye huwa na kijiriba cha roho juu yako. Kijiriba hicho ndicho huzaa kizaa-zaa katika maisha yenu au ya mmoja wenu. Usimuamini yeyote katika maisha haya, jiamini wewe na nafsi yako, wewe na maisha yako, kamwe hata kivuli chako, usikiamini kwani nacho huwa kinaenda kinyume kama muda ukibadilika.” Maneno haya yalikuwa ni ya mwisho katika tafrija ile fupi ambayo familia ya Eleutery na Ally iliandaa kwa watoto wao.



    Yalikuwa ni kama kaa la moto kwa Dickson na Dada yake, kwani Eleutery alitoa maneno hayo kama kuwahasa watoto wale, lakini pia yalikuwa yamewagusa sana Dick na dadaye.

    Walibaki macho chini kama wamesikia habari chafu kutoka kwa wanao wapendwa ambao wao walidhani hawana tabia hizo.

    Mara ya kwanza walidhani wameshtukiwa mpango wao, lakini baada ya kuona Eleutery anawaita kwa furaha waende kupiga picha ya pamoja, amani iliwarudia mioyoni mwao na walijongea pale jukwaani kufanya kilichoendelea.



    ********



    Kama kifo cha nyani miti yote huteleza, basi hii ni kweli bila kificho. Na kama MUNGU hapendi jambo fulani litokee, basi hii nayo ni kweli bila kuuliza.

    Hichi kilikuwa ni kifo cha nyani, kwani licha ya Bwana Eleutery kujitahidi kulipunguza gari lake mwendo, lakini bado liliteleza kutokana na mteremko mkali uliokuwepo eneo lile la barabara.

    Juhudi zote ziliishia kwa gari lile kuangukia mdomoni mwa daraja, na hapohapo injini ikapasuka na kutengeneza kimfereji kidogo cha mafuta ya petroli ambayo nayo hayakuwa na huruma ya kuacha kuwaka baada ya betri la gari lile kugusa boneti ya mbele na kutengeneza cheche zilizodondokea kwenye mfereji ule wa petroli.

    Hapo kama ukuwahi kuona filamu za ughaibuni, basi ni nafasi pekee ya wewe kuona. Ule mlipuko uliotokea pale, ni kama ule wa kwenye filamu za mapigano ya kivita. Hata wananchi na waokoaji walipojaribu kuokoa masalia ya watu, waliambulia majivu pamoja thamani walizovaa wale wazazi.



    Kama MUNGU hapendi jambo fulani litokee, basi halitokei. Kwa nini nilisema haya hapo juu?



    Ni kwa sababu familia ya Eleutery yote, ndiyo ilipangwa kuangamizwa. Lakini kwa sababu ya ukaribu wa zile familia mbili, wazazi wale waliamua kuwaachia wale watoto gari ambalo walikuja nalo familia ya Bwana Sanga na Bi.Habiba.



    Dereva akiwa kijana Ibrahim, alikuwa nyuma ya gari la wazazi wake huku akili na mwili wake ukiwa kando ya mtoto aliyedhani ni wa maisha yake. Namzungumzia Winfrida. Yule mfanyakazi wakina Winfrida, yeye alikuwa katika gari nyingine, tofauti na zile za wazazi na matajiri wake.



    Akili ya Ibrahim ilikuja kupagawa pale alipoona gari aliyopanda wazazi wake pamoja na wazazi wa Win, ikipoteza mwelekeo huku ikiwa katika kasi. Na mwisho wake iliambulia kuangukia darajani, ambapo bila zengwe ilidondokea kidevu na kuifanya boneti yake ifunguke kwa nguvu na kugonga kioo cha cha mbele cha gari ile huku chembechembe zile za kioo zikikutwa kwenye fuvu la Bi .Habiba na Bwana Eleutery waliokuwa wamekaa nafasi za mbele.

    Ni uchunguzi wa Daktari ndio ulionesha hivyo vioo vilivyoingia kichwani mwa wale wawili. Na yasemekana wao waliaga dunia palepale huku ule mlipuko wa gari ile ukiwachukua Baba Ibrahim na Mama Win waliokuwa nafasi za nyuma za gari ile aina ya Noah.



    ******



    Ni kilio kutoka kwa Win na Ibra ndicho kilichofuata baada ya hali ile kuiona wazi bila kificho.

    Wakiwa watu wa kwanza kabisa kufika kwenye eneo la tukio, walisikia sauti ya kike ikilia kwa uchungu uliochanganyika na maumivu ambayo sidhani kama kuna ambaye aliyajua ni kiasi gani yaliingia mwilini mwa yule aliyekuwa analia.



    Sauti ile ililia kwa mara moja na baadaye ilimezwa na mlipuko wa gari lile. Na hapo kulikuwa hakuna sauti iliyoendelea kusikika zaidi ya mabati ya gari ile kuungua na miti pamoja na nyasi zilizokuwa karibu, ambazo nazo zilikuwa kama zinafurahia hali ile kwa jinsi zilivyokuwa zinaushamirisha moto uwake na kuukuza na kuwa mkubwa kuliko pale mwanzo.



    Ibra na Win walibaki wamekumbatiana kama watoto mapacha waliokuwa wanamuogopa muuaji aliyewaua wazazi wao. Mbele walishindwa kwenda kwa sababu ya moto mkubwa uliokuwa umezagaa eneo lile.



    VISA.



    Mwisho wa chuki, huanza visa. Visa ndivyo vinavyoonesha roho ya kutu iliyojikita kwenye mioyo ya wanadamu. Kumchukia pekee mwenzako, haitoshi kumfukuza mahali alipo bali kufanya visa ndio tiketi maalumu ya kumuonesha umchukiaye kuwa humpendi na kumuhitaji.



    Roho ya mwanadamu ni pori zito ambalo limejaa wanyama wa kila aina na visa ndivyo hufungulia aina za wanyama waliojaa kwenye moyo huo. Ni kheri wafunguliwe wanyama ambao unaweza kucheza nao kuliko akifungulia wanyama mwitu ambao wamejaariw njaa na uchu wa kutafuna kila wanachokiona.



    Visa hujenga mtafuruku katika kila sakafu ya nyumba fulani. Ogopa sana mtengeneza visa, kwa sababu amekwishakuchukia mpaka kakomaa mwili huo wa chuki juu yako, anamua kukufanyia visa.



    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    ENDELEA.



    Ibra na Win walibaki wamekumbatiana kama watoto mapacha waliokuwa wanamuogopa muuaji aliyewaua wazazi wao. Mbele walishindwa kwenda kwa sababu ya moto mkubwa uliokuwa umezagaa eneo lile.



    Hadi moto ule unaanza kupotea, ndipo walipotokea kaka na dada wa Eleutery wakiwa na wahka mkubwa tena wenye majonzi na kilio kikubwa ndani yake. Walikuja huku wanakimbia na mwisho wake ulikuwa kwa yule dada kwenda kuwakumbatia Win na Ibra huku yule kaka mtu akijidai kawehuka kwa kwenda mzima-mzima kwenye lile gari lililokuwa bado linawaka moto.



    Hakuna aliyemzuia zaidi ya kelele za watu wachache ambao nao walikuwa katika msafara wa kurudi makwao usiku ule wa saa nane. Kelele zile zilikuwa ni kama kelele za kumzuia lakini kwa kuwa alishajipanga ili kumpiga kanyamazongo Win, alielekea pembeni hadi kulipokuwa na gari lile, huku sehemu hiyo ikiwa salama, yaani haina moto ambao utamdhuru.



    Kwa hamasa aliyodhani itamwingia vya kutosha moyoni mtoto wa kaka yake, alianza kulia kwa uchungu huku akigalagala eneo lile kama mbwa anayejikuna dawa alinayomuwasha. Kilio chake waweza kusema alikuwa hajui nini kiliendelea saa chache zilizopita. Uso wake ulionesha wazi kuumia kwa tukio lile. Na yawezekana kweli aliumia kumuua mdogo wake, lakini kuumia huko yaweza kuwa ndio furaha na amani ya moyo wake uliokuwa umejilimbikiza mtiririko wa chuki uliogandamana kama nta katika moyo wake.



    Hakika, aijuaye siri ya mwanadamu ni yeye na MUNGU wake. Muache MUNGU aitwe MUNGU kwa hii siri kubwa ambayo anatuficha hadi leo. Kama angetupa uwezo wa kuona kwa macho yetu kilicho ndani ya mioyo yetu, hakika nakwambia, Win angemsukumia Baba yake mkubwa katika moto uliokuwa unaendelea kutawala tukio lile.



    “Kaka unaenda wapi kaka?” Sauti ya maumivu ilimtoka Kaka wa Eleutery aliyekuwa kapiga magoti mbele ya gari lililokuwa linateketea. Hakuishia hapo,

    “Umeniachia mzigo mkubwa kaka yako, nitampa nini Win ambacho atakifurahia kama wewe hutokuwepo? Ni nani kama mama? Ni nani kama baba mzazi? Kwa nini umeacha majukumu yako na kuondoka namna hii? Kwa nini umeondoka kabla ya siku Kaka? Rudi mara moja na uongee nasi yale tuliyozoea kuyasikia.” Maneno ya uchungu yalifuatiwa na kilio cha kukauka kutoka kwa Dickson, kaka halali wa Eleutery.



    Ni wasamaria wema ndio walikuja kumuokota pale alipokuwa kapiga magoti na kumwondoa kabisa eneo lile akiwa kalegea utadhani mlevi aliyelewa pombe haramu kama Chang’aa.



    *****



    Mazishi ya wazazi wa vijana wale. Walio-aga dunia wakati wanatoka kusheherekea tafrija ya siku ya watoto wao kumaliza chuo, yalifanyika Wilaya ya Nyegezi na karibu matajiri wa Mwanza wote walihudhuria mazishi yale. Si matajiri hao pekee, bali viongozi na vibopa mbalimbali wa nchi ya Tanzania, walishiriki kikamilifu hatua za kuweka mahala panapostahili majivu na mafuvu ya vichwa ya wajasiriamali wale.



    Wingu zito la huzuni lilitanda katika vichwa vya umati wa watu waliokuwa mazishini. Lakini huzuni kubwa ilikuwa kwa vijana wao wa pekee, Win na Ibra ambao walikuwa wakilia hadi kupoteza fahamu kila wakati. Waliwapa kazi ya kuwapepea wakina mama na vijana rika lao, na hakika walikuwa wameumia kwa vifo vya watu wale muhimu sana katika kubiringisha tairi la maisha yao.



    Shangazi yake Win, hakuwa nyuma kulia hadi kugala-gala kama binadamu anayeanza kupandwa na kichaa. Lakini laiti kama MUNGU angempiga mwanga kichwani mwake na kumuonesha anachowaza, si Win wala Ibra na wananchi wengine wangeacha kumtemea mate kwa alichokifanya. Na wengine wangethubutu kumwondoa duniani ili akawasalimie Kaka na Wifi yake.

    MUNGU endelea kutufumba haya, kwani usipofanya hivyo, ni dhahiri dunia tutaangamizana wenyewe kwa wenyewe. Na yawezekana siku ukifanya hivi, ndio itakuwa mwisho wa dunia. Sitaacha kumsifu MUNGU kwa kazi hii ya kuficha moyo wa binaadam.



    ****



    Mwezi mmoja ukapita tangu mazishi ya wazazi wa Ibra na Win kufanyika. Si rahisi kusahau, lakini inabidi maisha yaendelee, hivyo ndivyo navyotambua.

    Baba Mkubwa na Shangazi wa Win, wao ndio walipewa mamlaka na majukumu ya mali zote za Mdogo wao. Hiyo ni sheria iliyowekwa na familia nzima na hakuna ambaye aliyepinga. Win mwenyewe aliona ni kawaida sana kwa yale yote, hivyo hakuwa mtu wa makuzi mbele ya wazee wale.



    Kwa upande wa Ibra, kulikuwa shwari kabisa. Mali alikabidhiwa yeye kwani hata mirathi ilionesha hivyo. Hakukuwa na matatizo kwake. Na hata kwa Win kulikuwa hakuna matatizo kwa miezi miwili ya mwanzoni. Lakini matatizo yalianza kuchipuka kila siku iendayo kwa MUNGU.



    Alikuwa ni shangazi yake aliyeanzisha vuguvugu la chuki mbele ya binti wa Eleutery Gaula. Lakini kama Shangazi yule aliyekuwa kajaa mwili wake kama gunia la sukari, angejua anamwekea chuki tajiri wake aliyemwajiri, sidhani kama angethubutu hata siku moja kujitapa na kujaribu kumfukuza Win kwenye nyumba ya wazazi wake.



    Ilikuwa hivi.

    “We’ kinyago unayelala hadi sasa hivi na wakati wenzako wote tumeshaamka, una-maana gani.” Sauti chachu ya Shangazi wa Winfrida ilitumbuiza vyema chumbani alipokuwa kajiegesha kitandani kwake akipitia hadithi fulani kwenye simu yake kupitia mtandao wa kijamii.



    “Unaongea na mimi Aunt.” Win aligeuka na kumuuliza Shangazi yake. Alishazoea utani na ndugu zake, hivyo hata aliposikia maneno toka kwa shangazi yake ambaye asubuhi hiyo alikuwa ndani ya badhee la Marehemu Mama Win, hakuhisi kuwa maneno yale yalikuwa yametoka bila utani.



    “Unaniuliza mimi Aunt?” Mama yule kifutu alijibu mapigo kwa kubananisha pua yake jambo lililomfanya Win ashangae kwa kituko kile cha mwaka.

    “Unamwita nani kwa lugha yenu ya ujivuni?” Alizidi kutambulisha chuki zake juu ya Win.



    “Yamekuwa hayo Shangazi.” Ilimbidi Win awe mpole na kuuliza kwa mshangao wa aina yake.



    “Na si haya tu, yanakuja mengine zaidi ya haya. Kaa mkao wa kuyala. Shangingi kubwa wee.” Shangazi mtu alimaliza kwa sonyo moja matata ambayo wakina mama wengi wa Kitanzania wamebarikiwa kuwa nayo.

    Akageuka nyuma na kurudi alipokuwa katokea kabla ya kuingia mle ndani. Win alibaki ghaa! Asijue ni yeye aliyefanyiwa kituko kile au kuna mwingine mle ndani.

     Ikabidi anyanyuke na kuanza kutafuta huku na huko kama anaweza kuona mtu mwingine, lakini la! Hakukuwa na mwingine zaidi yake. Kichwa kikagonga kengele ya hatari. Usomi nao unasaidia kung’amua kifuatacho baada ya nyodo.

    Siku ikatitia huku wanawake wale wamevimbiana kama mafahari wawili waliotoka kupigana pembe.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    *****



    Maisha yakazidi kusonga huku kila mmoja akipanga yake. Win akiwa kagongewa kengele ya hatari na Shangazi yake, na wakati huo Baba yake mkubwa na Shangazi yake, wakiwa katika mkakati kabambe wa kutaka kumiliki mali zote za Eleutery.

    Hata pale waliposhindwa kupata hati zote za mali za mdogo wao, waliamua kutaka kumtoa Win kimabavu. Hawakujua wanacheza na msomi wa chuo cha lugha duniani (Oxford). Na mbaya zaidi, rafiki yake wa karibu, Ibra. Ndio kwanza alikuwa katoka kumaliza School Of Law, alikuwa hajawahi kuitumikia elimu yake. Kama ni kitu, basi naweza kukiita ‘Empty CD’ kwa jinsi kilivyokuwa kisafi lakini kilichotayari kuchafuka kwa kazi iliyoumbwa kuifanya.

    Wale ndugu wawili, wakauvagaa.



    Asubuhi hiyo kama kawaida, likazuka timbwili kati ya Win na Shangazi yake ambaye siku hiyo alikuwa kavalia vitenge vya wax, lakini vikiwa ni mali ya Marehemu.

    Akiwa kaenea kwenye sofa la watu wawili lililo sebuleni, shangazi yule alikuwa kama anasubiri Win atokee na kumwongelesha ili alianzishe.



    “Shikamoo Shangazi.”Win alimsalimia Shangazi kwa heshima zote na kujitua kwenye sofa lingine pale sebuleni. Badala ya kuitikia salaam, mama yule mweusi na asiyependeza kwa mashauzi, alitazama pembeni na kunyonga mdomo wake. Kisha likasikika sonyo refu kama kawaida yake.

    Kwa Win ilikuwa kawaida, wala hakujali. Akakamata limoti ya runinga na kuanza kutafuta stesheni yenye mambo anayoyapenda. Akakwamia kwenye BET, stesheni pendwa ya vijana wapendao burudani ya muziki.



    “Unaona mimi nafaidi sana kuangalia eeh. Au kwa sababu ni mali za baba yako?” Shangazi mtu alikuja juu. “Kumbuka wewe ni Baba yako tu, sisi ni ndugu zake, tumbo moja, toka nikutoke.”Mama yule alizidi kuchombeza.



    “Lakini Shangazi, kwani nimekukosea nini? Au unataka nini?” Win aliuliza huku macho yake yakiwa katika huruma kama ujuavyo wanawake wanapoomba msamaha kwa watu wanaowajali.



    “Nataka uondoke hapa nyumbani. Toka kwenye nyumba ya kaka yetu mbwa mkubwa wee. Limemuua baba yake ili lirithi mali. Tumeshakujua, na utaondoka tu.” Maneno hayo yakawa msumali wa moto kwa Win.

    Hakuwahi kumwambia Baba yake Mkubwa juu ya vituko vya Shangazi yake. Lakini siku hiyo, akaona liwalo na liwe. Akaenda hadi chumba anachotumia Baba yake mkubwa, akagonga. Na uzuri baba yake huyo ndio alikuwa anataka kwenda kufuatilia biashara alizoacha mdogo wake.

    “Baba mbona Shangazi kawa hivi siku hizi?” Win aliuliza huku macho yake yakionesha wazi kuwa atalia muda wowote kama hatobembelezwa.

    Baba yake mkubwa akiwa ndani ya suti ya rangi ya maziwa, lakini nayo ni mali ya Marehemu Mdogo wake. Alizidi kumpagawisha Win kwa jibu lake.



    “Ondoka bwana. Hatukuhitaji. Hatuwezi kukaa na muuaji wa ndugu yetu kipenzi. Nenda zako.” Alijibu Bwana Dick huku anafunga mlango wa chumba chake. Chumba ambacho alikuwa anatumia marehemu mdogo wake na mkewe.

    Baada ya kufunga, alitengeneza koti la suti yake vizuri kisha akampita Win huku akimsukuma kidogo kwa bega lake. Win akayumba kisichana (kilegevu) na kukamata ukuta kama ngao yake. Hadi hapo, Win alishaelewa ni nini kinachofuata.





     HAKI



    Njia ya kumshinda mbaya ni kwenda naye nyama kwa nyama, lakini katika njia inayotambulika kisheria na si kinyume chake.

    Kisasi si njia iliyo salama katika maisha haya ya leo ambayo kila neno ni kifo kama ukiuua. Maisha ya huzuni na yaliyojaa kwa nini, huja baada ya kugundua kuwa ulifanya kosa kwa kulipa kisasi kwa mtu aliyekuharibia mwenendo wa maisha yako.

    Majuto hayo huwa mjukuu hasa pale utakapogundulika na sheria kuwa umelipa kisasi kisichokubalika na serikali au dini. Mwisho wake huwa ni wewe kuishia jela au kifo kama sheria itaruhusu.



    Hakuna kilichobora kama kumwombea adui yako aishi siku nyingi. Na siku zote huwa hivyo. Adui huishi siku nyingi huku roho yake ya uadui ikizidi kugandamana na gundi ya chuki hasa pale anapoona unafanikiwa. Lakini anakuwa hana jinsi na hana cha kufanya hasa pale anapogundua alikutendea ubaya. Hapo utakuwa umelipa kisasi kilichobora kabisa katika maisha yako. Hata MUNGU atakuongezea zaidi ili amnyong’onyeze adui yako.



    ENDELEA.



    Akili kumkichwa, au akili zikacheza. Akatoka na kwenda moja kwa moja kwa Ibrahim Singa na kumpa mkasa uliyomtokea asubuhi ya siku hiyo. Hakuwa na amani hata kidogo, nyumbani hakutaka kurudi bali kubaki na Ibra kama faraja yake.



    Mida ya saa kumi na moja, ndipo alipochukua jukumu la kurudi nyumbani kwao, lakini alichokishuhudia machoni kwake, hata moyo wake ulikataa kuamini.



    Getini, kulikuwa na askari wenye mbwa pamoja silaha za moto. Na mbele yao kulikuwa na mabegi ya nguo zake. Alishindwa kuamini kama ni kweli yale anayoyaona ni yeye anafanyiwa au kuna kiumbe kingine ndicho kinahusika na ule mkasa.



    Kabla hata hajachukua uamuzi wa kuuliza maswali yanayozunguka kichwani mwake. Baba yake mkubwa alitokea huku kavalia mavazi ya kufanyia mazoezi, lakini bahati mbaya nayo hayakuwa ya kwake bali ya Eleutery Gaula. Marehemu mdogo wake.



    “Chukua madudu yako, nenda huko ulipokuwa umeshinda, malaya mkubwa wee.”Sauti ya Dickson ilisikika ikiwa mbali kabisa na Win.



    “Lakini Baba….”



    “Huna Baba wewe, baba yako yupo kuzimu. Mfuate na mwite hivyo, lakini si mimi.” Baba yule mrefu mweusi na mwenye uso wa pembe nne, alimaka bila kusogea pale alipo Win na Polisi aliowaalika. Nadhani yeye mwenyewe aliogopa mbwa ambao muda wote walikuwa ulimi nje kama wameona nyama.



    “Binti chukua chako na uondoke kabla hatujaruhusu meno haya yaingie kwenye makalio yako.” Askari mmoja kati ya watatu alimpa onyo Win huku akimuoneshea mbwa ambaye alikuwa kakamatwa na askari mwingine.



    “Kwa hiyo na nyie askari mmeacha kazi za maana na kuja kushughurika na ujinga huu? Humuoni aibu? Askari watatu wote mmekuja kumwondoa binti mwelewa kama mimi. Hii Tanzania ina-watu wa ajabu sana. Lakini anyway, acha nifate maagizo.” Win alisema lakini hakuna aliyejaribu kumkanya wala kumfokea bali kukaa kimya na kushindwa wampe adhabu gani.

    Alipokusanya mabegi yake na kulidhika na hali hiyo. Aliwaangalia tena askari wale kwa zamu kisha akatikisa kichwa kwa masikitiko.



    “Mtapoteza ajira kwa huu ujinga wenu. Amini nawaambia.” Winfrida aliwaambia wale askari ambao sasa walitaka kuchachamaa na kumpiga Win.



    “We’ binti, usitutishie sisi hata kidogo. Tutakutoa roho yako hapa-hapa kwenu.”Askari mmoja alimpa onyo huku akiwa anamfata na mkono wake kaunyoosha kwenda chini tayari kwa kurusha kofi.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “You all enter in a wrong hole, just wait and you will see (Mmeingia kwenye tundu lisilo sahihi, nyie subirini na mtaona).”Maneno ya kujiamini yaliibukia kwenye kimywa cha Win ambaye badala ya kusubiri ajibiwe na wale askari, alikamata mizigo yake vizuri na kuanza kuondoka eneo lile. Lakini ni kama alikuwa kasahau kitu, akatupa mizigo yake na kuwarudia wale askari.



    “Waambieni hao mabosi wenu wa ndani, nitarudi baada ya siku tatu. Baada ya wao ni nyie.”Alimaliza Win na kurudia mizigo yake huku akiwaacha wale askari wakimtukana na kumkejeli kama mwanamke aliyefumaniwa na mme wa mtu.



    ****



    Safari ya Win iliishia nyumbani kwa Ibrahim aliyekuwa akiishi na ndugu wengine lakini wenye upendo na heshima. Win hakuwa na moyo wa wasiwasi kwa kile kilichotokea. Ungedhani labda mwanadada huyu angedondosha machozi baada ya kufika kwa Ibrahim.



    “Yametukia yaliyopaswa kutukia. Sasa wameamsha mambo yaliyokuwa yamelala.” Winfrida Gaula alitamka hayo akiwa kasimama mbele ya Ibrahim Singa.

    Ibrahim alitabasamu tabasamu la kifedhuli, kisha kwa mapozi yaliyojaa ujivuni ndani yake, akamkaribisha mwanadada yule akae kochini. Kisha Win bila kuchelewa, akaanza kumwaga utamu wote uliotokea aliporudi kwao.



    “Naweza kuingia kazini sasa?” Ibra aliuliza huku akizidisha tabasamu ‘choko’ lake lililoonesha kufurahia kile kitendo cha wale wazee kumfukuza Win.



    “Hapana. Tuingie kazini, lugha hii ya wingi nadhani ni bora kuliko yako ya umoja.” Win alimjibu Ibra huku naye akichanua tabasamu mwanana kama mwamvuli wa kushukia ardhini ukiwa kwenye ndege, namaanisha parachuti.



    *****



    Kama wale askari wa getini walivyopewa malezo ya mwisho kabla ya Win hajaondoka pale kwao, siku ya tatu tangu Win aondoke, Mzee Dickson na Dada yake, walipokea barua ya wito toka mahakamani.



    Wakapagawa wasijue ni nini wameitiwa. Akili zilijichekecha kichwani mwao, lakini hawakupata jibu. Ni kwamba wale askari walipuuzia maneno ya Win, hawakuwaambia mabosi wao maneno ya mwisho aliyoyaongea Win. Hiyo ikawa pasua kichwa kwa ndugu wale wa karibu wa Bwana Eleutery Gaula mbaye kwa wakati huo, yawezekana alikuwa kampuzika kwa amani au bado roho yake ilikuwa inamsimamia mtoto wake afanikishe masuala ambayo yatamkabili.



    Barua ile ilionesha wanahitajika mahakamani siku mbili mbele zijazo, lakini kabla ya hapo, walitakiwa kuonana na wakili upande wa mashitaka ili wapate kuelewa ni nini kinachowakabiri kwenye kesi watakayoenda kuisikiliza.



    Kesho yake, walifunga safari hadi kwa wakili waliyeelekezwa. Huko walikutana na sura mbili. Moja ya Ibrahim Singa na nyingine ya Faustin Mkenge, wakili aliyekuwa anafanya kazi zake kwa kujitegemea. Na ni wakaili huyu ambaye Mzee Eleutery Gaula alimpa mamlaka ya kusimamia mali zake na familia yake pia.



    “Karibu mzee wetu.” Faustin Mkenge au Adv. Mkenge kama kibao chake kilivyoandikwa mezani, alimkaribisha Bwana Dickson aliyekuwa kavalia suti nyeusi na nzito, lakini iliyombana sana hadi kuonekana kama mateso kwake, suti ambayo ilikuwa ya kwanza kwa Marehemu Eleutery kuinunua.

    Baada ya Bwana Dick kukaa, akawa kampa upenyo Adv. Mkenge kukiona kipande cha mama kikiwa ndani ya vazi la kinaijeria. Lakini ubaya vazi hilo, lilikuwa kubwa kuliko mwili wake, lilifunika hadi viatu virefu ambavyo hawezi kuvitembelea, lakini alivaa tu, ili aendane na wakati.

    Vazi lile la rangi ya dhahabu, lilikuwa ni la Bi. Gaula, mke wa Eleutery Gaula. Alipewa zawadi na mke wa Uche Ojiango, ambaye mumewe alitengeneza uhusiano mzuri wa kibiashara na Eleutery Gaula.



    Watu hawa wawili, Bwana Dickson na dada yake, miili yao ilikuwa haiendani na miili ya watu waliorithi nguo zao. Bwana Eleutery alikuwa mwembamba kiasi huku Bwana Dick akiwa kajazia sana japo shida zilikuwa haziishi kugonga nyundo katika maisha yake.



    Mbali na unene na wembamba unaowatofautisha watu hawa, vilevile Dick alikuwa mfupi kuliko Eleutery. Ile suti aliyovaa ilionekana ipo sawa katika urefu, labda kwa sababu ilikuwa ni ya kwanza kununuliwa na Eleutery. Nje ya hapo, kama hilo si jibu, basi jibu lake ni kwamba Bwana Dick alienda kuikata suruali ile ili iendane na yeye. Lakini bado unene ukawa tatizo, koti la suti na mapajani kulivyombana, ni wazi lile vazi lilikuwa si halali yake, na kama lingekuwa na mdomo, lingeomba livuliwe.



    Shangazi wa Win, alikuwa ni mfupi kuliko mke wa Eleutery. Vazi lile la Kinaijeria, likawa limemfanya aonekane kama mwanamazingaombwe wa Kiafrika kwa jinsi lilivyomfunika na hata kiremba alichokuwa kakiweka kichwani. Na vipodozi alivyojipodoa kabla hajaenda ofisi aliyokuwepo kwa wakati ule, huwezi kukataa hizi sifa nazokupa.



    Bi. Gaula, mama wa Win. Alikuwa ni mnene kiasi na kwa kuwa vazi lile hutengenezwa kwa hata wembamba kama Betina, wakilivaa waonekane wanene. Basi kile kifutu cha mama, au shangazi wa Win kwa lugha rahisi, alionekana ndani vazi lile. Vazi ambalo lilikuwa linamvaa hata Mama Win.

    Na ndio maana Mama Win alipopewa zawadi ile, aliiweka tu, hakutaka kulivaa vazi lile kwa kuwa angeonekana kituko. Na mara nyingi, mumewe alikuwa anamcheka sana akivaliwa naa vazi lile.



     Hiyo ilimsababisha Mama Win asilitie vazi lile mwilini bali kuliweka kama ukumbusho. Sasa shangazi yake Win alikuwa ndani yake, otea nini kinachoendelea. Lakini tuyaache hayo, turudi panapotuhusu.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Karibu mama yangu,” Faustin Mkenge alimkaribisha pia Shangazi yake Win akae kwenye kiti kimojawapo kilichomo mle ofisini na kukiacha kiti kimoja kikiwa wazi. “Bado tunamsubiri Win ambaye katoka mara moja kwenda kuongea na simu, hivyo baada ya dakika chache atakuwa kar…..” Hakumaliza kauli yake Mwanasheria yule, tayari Win alikuwa kafungua mlango wa ofisi ile na bila hata kusalimia, alienda kuchukua nafasi iliyokuwa wazi na kutuliza makalio yake kwenye nafasi hiyo.



    “Kwa hiyo mmetuitia nini?” Bwana Dickson alimuuliza Adv. Mkenge baada ya kumpa baadhi ya karatasi azipitie kabla hawajaanza maongezi.



    “Huo niliokupa ni wosia wa Marehemu au Boss wangu, Bwana Eleutery Gaula,” Alianza kufafanua Mkenge. Lakini Dick akadakia,



    “Mimi haunihusu. Na si mimi, hata dada hapa na ndugu zetu wote.” Tehe! Dick bwana. Akasemea mioyo ya watu.





    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog