Search This Blog

Sunday, July 10, 2022

GANZI YA MOYO - 3

 







    Simulizi : Ganzi Ya Moyo

    Sehemu Ya Tatu (3)



    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kitandani kwa Win baada ya kurudi nyumbani kwake, siku hiyo hapakulalika kwa raha. Aligalagala huku na huko huku kakumbatia mdoli mkubwa aliyekuwa kitandani kwake. Sura ya Eddy na kile kifua alichokiona kwenye gari wakati wanaenda kwake, vyote vilikuwa vinajirudia kichwani mwake kama mechi ya mpira inavyorudia goli lake.



    Maneno ya mashairi ambayo aliyaongea Edson, yalikuwa yakipita kichwani mwake na kuacha mwangwi. Hakusita kuikumbuka ile sura iliyokuwa inavikwa mawani ya macho ilivyokuwa inamwangalia wakati anaenda chumbani kwake.

    Hapo akatabamu na kujikuta mwenye hamu ya kutaka asubuhi ifike ili akimbilie nyumbani kwa akina Edson ili akutane naye.



    “Lakini atakuwa shule sasa.”Alijikwaza mwenyewe kwa maneno hayo. “Ila nitaenda na kukaa na mama yake hadi arudi.” Win alizidi kujipa ukichaa kwa kuongea peke yake usiku ule wa saa saba.

    Maamuzi hayo si kama yalimpa usingizi, bali yalinogesha akili yake na kuifanya ibaki inamuwaza Edson kupita maelezo. Hakutaka kukubali kirahisi kuwa katokea kumpenda kijana kwa siku ile ya kwanza aliyomuona. Na hakutaka kukubali kuwa hampendi yule kijana. Mabishano hayo baina ya moyo na ubongo, yaliisha baadae tena baada ya kubebwa na usingizi. Mapenzi bwana, yaacheni tu.

    ****

    Asubuhi ya siku iliyofuata, Winfrida alikuwa mchangamfu labda kuliko siku zote alizowahi kuishi na wafanyakazi wake. Alipika nao, alifua nao na kula nao kama ndugu zake. Alikuwa na furaha iliyopitiliza mbele ya familia nzima aliyokuwa anaishi nayo. Kukamilisha furaha yake, alipomaliza kazi za nyumbani, aliwabeba wafanyakazi wake wote na kuwapeleka kwenda kufanya manunuzi ya vitu vya ndani na pia kuwanunulia mavazi mapya wafanyakazi wake ambao walikuwa watatu. Wawili wa kike na mmoja wa kiume.



    Ndani ya duka la nguo, Win alikuwa akimchagulia nguo mwanana kijana wake Edson. Hakumchagulia Edson tu, bali na mama yake bila kumsahau yule binti ambaye alipewa taarifa kuwa hukaa na mama wa Edson kwa muda mwingi kuliko mtu mwingine. Na uzuri binti yule alikuwa kamaliza darasa la saba lakini hakuweza kuchaguliwa kuendelea na shule ya Sekondari hata ya kata. Hivyo huyo ndiye akawa msaada mkubwa wa Edson na Mama yake.



     



    BUSARA,



    Katika kila mdomo, kunakuwa na heshima yake itokayo ndani yake. Busara ya mwisho kabisa inaonekana kupitia kinywa chako. Neno busara ni neon dogo sana lakini ni kubwa katika utendaji wake. Kama mdomo wako usipooonesha busara basi tambua hata mavazi ambayo yanaitambulisha busara yako kuwa ya aina Fulani, haitaonekana kwa sababau yam domo wako.



    Unaweza kuvaa mavazi nadhifu na yanayopendeza katika kila macho ya rika. Lakini mdomo tu! Ndio ukatambulisha maana ya mavazi yako. Ndio maana nimesema, busara ya mwisho inaelezewa kwa mdomo na si kitu kingine. Busara ni muhimu katika kinywa chako, kifanye kinywa chako kuwa kitambulisho cha ukivaacho au ukifanyacho.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    ENJOY.



    Baada ya Win kumaliza manunuzi mbalimbali ya siku nzima, aliwarudisha wafanyakazi wake nyumbani. Wafanyakazi ambao siku hiyo walikuwa wamepambwa na tabasamu la ajabu usoni pao. Walishindwa wamshukuru vipi tajiri wao, lakini kusema asante, ilitosha kwa wao kuamini kuwa wamemshukuru sana tajiri wao.



    Baada ya kuwarudisha nyumbani, Win akabadili mavazi yake tena na kisha kutoka nje tayari kwa kwenda kwa akina Edson Lake. Mvulana mdogo aliyeteka hisia za mtu mzima lakini mrembo kupindukia, hayo yote ni mapenzi tu.

    Umri ni namba, usidanganyike na namba katika mapenzi, endapo kungekuwa hakuna namba hizo, sidhani kama kungekuwa kuna kujiona mkubwa au mdogo. Mapenzi hayaangalii namba ambayo ndio umri wako, mapenzi ni hisia za moyoni zinazoundwa kwa fikra pevu baina ya mioyo miwili.

    ****



    Vicheko vya dezo vilitawala nje ya nyumba ya nyumba ya akina Eddy. Baadhi ya wapangaji walikuwa wakicheka kwa sauti za kishangingi kana kwamba wanasuta mtu au labda wapo Uswahilini wanasukana nywele zao.

    Lakini haikuwa hivyo, kila walipotazama gari matata iliyokuwa imeegeshwa karibu na nyumba waliyopanga, wivu na kimsonyoto fulani, vilichachamaa mioyoni mwao na kujiona kama wao ni vinyesi mbele ya mwanadada aliyeingia ndani kwa akina Eddy muda mchache uliopita. Licha ya wanadada wale mashangingi kusalimiwa kwa furaha na Win, lakini bado zege la wivu lilichachamaa na kujenga ukuta mpana mioyoni mwao.



    “He he heee, mwanamke kujishongo kwa katoto ni nomaaa.”Sauti ya shangingi moja ambalo lilikuwa limejikubua hadi rangi yake ya chungwa kuvia damu, ilipenya vema kwenye masikio ya Win na kujikuta akiaanza kujihisi vibaya kwa maneno yale na mengine yaliyokuwa yanawamwagika mashangingi wale.



    “Hakuna kitu kibaya kama mdomo.”Win alishtushwa ghafla na mkono wa mama yake Eddy uliomgusa begani ukienda sanjari na sauti hiyo iliyokuwa inatoka kwa chini sana.

    “Mdomo unaweza kuponza mwili, nadhani wafahamu hilo mwanangu. Vilevile mdomo huu unaeleza vema tabia zako kuliko kiungo kingine chochote cha mwili. Kupitia mdomo, unaweza kumjua mwenye wivu na mkorofi. Kupitia mdomo, unaweza hata kumuua adui. Lakini mdomo huu kama unautumia vizuri, ndio unaoweza kukupa kile unachohitaji.

    Usifadhahike na midomo michafu ambayo haina staha pindi ifunguapo na kutoa neno. U mwana mvumilivu, nakuona katika macho yako ambayo yanaelezea moyo wako. Sidhani kama utayapa kipaumbele haya uyasikiayo. Acha midomo yao iendelee kuelezea tabia zao, hakuna mpambano wa kuku unaoisha bila kupatikana mshindi. Heshima itapakana baada ya pambano.”Alimaliza Mama wa Edson na kukohoa kidogo kabla hajautoa mkono wake kwenye bega la Winfrida Gaula aliyejikuta akitabasamu baada ya maneno ya faraja ya Mama wa Edson.



    Win akajihisi mwenye bahati mbele ya maisha yale ambayo kamwe hakufikiria kama yatafikia sehemu na kumpenda mtu fulani kiasi kile. Akajinyenyekeza kwa Mama wa Edson na kujihisi ni kama mama yake ndiye kafufuka. Akazidi kujihisi faraja kubwa moyoni mwake, akalala juu ya miguu ya mama yule huku huko nje wale washakupaku wakizidi kunya maneno yasiyofaa kusikilika katika kila sikio la kila aliyeelimika.



    Mama Edson naye hakuwa mchoyo wa faraja kama mama wengine walio na mioyo myepesi juu ya wanawake matajiri kuwapenda wana wao. Mama Eddy akawa anachezea nywele ndefu za Win kwa kuzurudisha nyuma ishara ya upendo wa kweli kwa anayetambua kuhusu hilo.

    Ndani ya dakia kumi na tano, Win hakuwa tena katika dunia hii ya wapambe na wambea, alikuwa katia dunia nyingine iliyopelekwa na usingizi mzito akiwa palepale miguuni mwa Mama Eddy, hakika alikumbuka faraja ya mama yae kuliko kitu kingine. Winfrida alikuwa kashikwa na usingizi, eti jamani. Duh.



    Mida ya saa tisa alasiri, Eddy alikuwa kishafika eneo la nyumbani kwao na ni wazi uwepo wa gari la Win nje ya nyumba anayoishi, ulimpa picha nyingine ya furaha moyoni mwake. Akakaza mwendo ili afike ndani na ashuhudie kile ambacho kinaendelea ndani kwake. Muda huo, tayari wale wapambe nuksi walishakaukwa na mate na kuingia vyumbani mwao ambapo wakulala, walilala na wale wenzangu na miye, kuangalia filamu za Kiswahili, ukawa ndio muda wao wa kujiburudisha huku mikanga ikiwa haibanduki miilini mwao.

    Eddy akajongea hadi mlangoni kwa na kisha kwa ustaarabu mkubwa, akafungua mlango na kuingia ndani. Hapo alikutana na ishara ya mama yake akiwa kaweka kaweka kidole cha shahada mdomoni akimaanisha asipe kelele.

    Eddy alipotazama, alimuona Win akiwa kakalia kochi alilolivuta hadi pale karibu na kitanda cha Mama Eddy,kisha akalalia miguu ya mama yule ambaye aliyekuwa hawezi kunyanyuka wala kutembea hasa katika sehemu ya kiuno na kushuka chini. Lakini hiyo ilikuwa si sababu ya kumkataza Winfrida asilale pale kwenye miguu yake.



    Eddy akatabasamu na kisha akaingia chumbani kwake na kubadili nguo kabla hajarudi tena sebuleni ambapo mama yake mara nyingi hujipumzishia hasa mida ya asubuhi hadi jioni. Eddy akamuuliza mama yake kama tayari wamekula, na mama akajibu kuwa Win tayari kaleta chakula ambacho wameshakitabaruku. Eddy akatabasamu tena na kisha akamuomba mama yake ruhusa ya amuamshe Win. Mama akampa ruhusa na kwa ustaarabu, akaanza kumtikisa Win ili aamke.



    “Hey Eddy, umefika saa ngapi.”Win aliamka na kumuuliza swali hilo Edson aliyekuwa kapambwa na tabasamu.



    “Ondoa shaka, sasa hivi ndio nimefika.”Eddy akajibu.



    “Kwa hiyo bado hujala?” Swali lingine toka kwa Win.



    “Ndiyo nakuamsha wewe tule wote.”



    “Haya. Ngoja basi nilete chakula.”Win aliongea huku akinyanyuka lakini Eddy alimkataza na kumwambia asubiri.

    Japo chakula kililetwa na Win, lakini Eddy akajidai yeye ndiye mpishi na kuanza kukiweka mezani. Dah!



    “Haya sasa, karibu dada.”Eddy alimkaribisha Win na kumfanya Win akunje sura mbele ya uso wa Eddy wakati huo kampa kisogo mama yake.



    “Asante.”Win akajibu na kugeuza kochi alilokuwa kakalia mwanzo tayari kwa kujumuika na Eddy katika meza ya chakula.



    “Mmmh! Tunataka kumsahau na mama hapa hapa. Embu tujione kwanza, uchoyo umetujaa tu.”Win aliongea baada ya kuanza kunawa.



    “Nyie endeleeni wanangu. Mimi napenda kuwaona jinsi mnavyokula. Nafarijika sana kuona hivyo.” Mama Eddy aliongea huku akijaribu kupamba uso wake kwa tabasamu mwanana.

    Win kabla hajala chakula kile ambacho kilikuwa ni mtori, pilau na mapochopocho mengine ya ‘kishuani’, akachimba chakula kiasi kwenye kijiko chake na kumlisha Mama Eddy ambaye hakuwa na ajizi juu ya hilo, akatanua mdomo na chakula kile kikapita.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Hichi nacho ulipika wewe mwanangu.”Mama Eddy aliiuliza baada ya kumeza kile chakula.



    “Ndiyo mama.”Win akajibu kiheshima mpaka basi. Ungependa na ungejifunza mengi wewe mtoto wa kike kama ungebahatika kuona heshima aliyokuwa anaionesha Win.



    “Kwani kuna kingine mmekwishakula.”Edson aliuliza huku akiacha kula.



    “Ndiyo. We si umechelewa, tumekula chote hapa hapa, tena kitamu hicho.” Mama Eddy alijibu huku ametabasamu.



    “Kwa hiyo mama umekula bila kunibakizia?”



    “Eee, ndiyo. Hata kesho akileta hupati.” Mama Eddy akazidi kumtania mwanaye huku Win akiwa mwenye tabasamu kwa kuona kile kinachoendelea.



    “Muone kwanza, uchoyo tu umekuzidi.”Eddy naye alimtania mama yake.



    “Ndio ukome. Unajichelewesha kurudi nyumbani kwa nini?”



    “Sawa tu.”Eddy akajibu kiunyonge.



    “Basi mwanangu, kesho nitakubakizia, sawa eeh.”Mama Eddy akaigiza kama Mama anavyopaswa kufanya.

    Eddy akajikuta akitoka pale alipokuwa kakaa na kumfuata mama yake pale kitandani na kumkumbatia. Si kwa sababu aliyapenda yale maneno ambayo mama yake alikuwa anamwambia, la hasha. Eddy alijisikia uchungu baada ya kumkumbuka mama yake yule mzima, mama mpigania haki zake hadi akafanyiwa hila na kupoozeshwa mwili wake baada ya kudungwa sindano ya sumu. Ni hadithi mbaya na kuyasikitisha juu ya mama huyu ambaye ndiye mzazi wa pekee wa Eddy.



    MIAKA MITATU ILIYOPITA.



    Eddy akiwa kafaulu kuingia kidato cha kwanza, ndipo alipopata janga baya la kuondokewa na baba yake. Baba Eddy alikuwa ni mtu maarufu sana nchini Tanzania na nchi jirani kutokana na kazi ya kutibu magonjwa sugu. Mali na utajiri wa fedha, ulikuwa umesheheni katika maisha yake Mzee Lake.

    Lakini ni hila zilezile zilizofanyika kwa familia ya Win na Ibra. Ndugu wa baba wa Edson, wakapanga kumwangamiza mzee yule. Na walifanikiwa kwa asilimia kubwa baada ya kumtumia majambazi ambayo yalimkamata nje ya nyumba yake, usiku wa saa nne tu.



    Mzee yule akiwa anatoka kazini kwake, amekwishafika na nyumbani kwake kabisa. Akapiga honi ya gari ili mlinzi afungue. Akiwa anasubiria mlinzi afungue, ndipo majambazi watatu walipotokea huku yamekamata bastola zenye kiwambo cha kuzuilia sauti. Wakavunja kioo cha gari kwa risasi moja, na kisha wakamchabanga risasi mbili za kifuani Mzee Lake na moja wakaimaliza kwa kumpiga nayo kichwani. Hapo hapo, uhai ukamtoka mzee yule na majambazi yakatokomea haraka kutoka eneo lile.

    Ni kitendo cha dakika mbili tu, hadi mlinzi anamaliza kufungua geti ili tajiri wake afike, tayari Mzee Lake alikuwa mfu. Hapo ndipo shuruba ya maisha ilipoanza.





    NAFASI,



    Nafasi ni jambo pekee ambalo mwanadamu anatakiwa kucheza nalo kuliko jambo lolote katika maisha yake. Sizungumzii nafasi ya kukaa kwenye daladala au nafasi ya kwenye ndege, nazungumzia ‘opportunity’ kwa kiingereza, yaani kupata jambo au kitu na kulitumia vizuri na inavyotakiwa.

    Ni vema kujua nafasi yako katika maisha na usiwe mtu wa kutaka kuchagua nafasi bali itakayotokea, ichukue na ifanyie kazi. Usipende kuchagua bali tumia nafasi zinazokuja.



    ENJOY.



    Edson ambaye alikuwa kafaulu shule za vipaji maalumu, ikawa kwake ndio basi. Mali zikawekwa chini ya ndugu na hakuna ambaye alikuwa anajali mke na mtoto wa Mzee Lake.

    Kazi ya Mama wa Eddy, ilikuwa ni ualimu wa chekechea katika shule moja ambayo ilikuwa ni ya kimataifa. Fedha fulani alizokuwa nazo, zikawafanya wasogeze maisha yao kiasi fulani baada ya kufukuzwa kwenye nyumba aliyokuwa anaishi na marehemu mumewe.

    Mama Eddy akapanga nyumba huko uswahilini na kuendelea na maisha huku akimsihi mwanaye kuhusu elimu zaidi. Na kupunguza gharama, akaamua kumwandikisha mwanaye katika shule ya Kata iliyopo pale Mwanza. Maisha yakaendelea hivyo.



    Katika ile shule ya chekechea ambayo alikuwa anafundisha mama huyu, alikuwa na urafiki mkubwa na mwalimu mkuu wa shule ile. Mwalimu yule mkuu alielewa shida za mama huyu kuliko mtu yeyote katika dunia hii.

    Mama Eddy siku zote alikuwa mtu wa kumuomba ushauri mwalimu yule na naweza kusema ndicho kilichomponza. Kwani siku moja baada ya kumuomba ushauri mwalimu yule mkuu, akashauriwa atafute mwanasheria ambaye ataweza kusimama kwenye chombo cha haki na sheria na kumtetea hadi mali zake zikarudi. Si ushauri mbaya katika dunia ya sasa, lakini ushauri huu ndio ulimsababisha mama Eddy awe mtu wa kulala kitandani asubuhi mpaka asubuhi.



    Mama Eddy akaamua kufanyia kazi ule ushauri na kweli akampata mwanasheria mzuri tu ambaye anajua haki na jinsi ya kuitetea. Hatimaye Mama Eddy akapanda kizimbani na kuanza kutetea mali zake. Alijitahidi kwa nafasi yake, na alikuwa anaelekea kushinda kesi ile. Lakini mioyo ya binadamu, imejaa chuki na masimango yasiyoelezeka.

    Mioyo ya binadamu ni zaidi ya pango lenye giza halafu kuna chatu mkubwa awezaye kuona kwenye giza kuliko kwenye mwanga. Na bila huruma, moyo wa mtu ulivokuwa katili, unaweza kukutumbukiza huko ili upotee kabisa katika uso huu wa dunia.



    Walewale ndugu waliompora mali mama huyu, ndio haohao walimtafutia majambazi na kumdhuru mama huyu.

    Usiku mmoja kabla ya kesi kuisha, Mama Eddy akiwa na furaha isiyosemekana baada ya kuambiwa kesi ile anaweza kushinda, aliingiliwa na majambazi ambao hayakuiba chochote zaidi ya kumchoma sindano shingoni na kutokomea pasipojulikana.

    Hata Mama Eddy alipojaribu kupiga kelele, sauti haikutoka bali ni damu pekee ndizo zilikuwa zinamtoka masikioni, puani na mdomoni. Ni Eddy ndiye aliyesaidia kupiga kelele baada ya kugundua wale majambazi wameondoka.



    Mama wa watu hata pale alipofikishwa hospitali, alikuwa kama zezeta tu. Alikuwa hapepesi macho, wala kuongea au kutikisika. Mbaya zaidi, hata yule Mwanasheria wake, alikutwa hana vidole wala macho. Hiyo ni baada ya yeye pia kuvamiwa na kuuawa kikatili namna hiyo.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Miezi na miezi ikapita bila mama huyu kutoka kitandani. Eddy alikuwa ni mtu wa mihangaiko katika hii dunia kama vile hana akili nzuri. Licha ya hayo yote, hakuacha kwenda shule japo kwa wiki mara tatu.



    Walimu na wanafunzi wenzake walijua ni kiasi gani kijana huyu anaumia kwa sababu ya mzazi wake. Kamwe hawakuwa wachoyo wa fadhila wala watu wa mamneno ya kukatisha tamaa. Mama na wazazi wote, ni zaidi ya unavyofikiria. Heri ukose fedha na mali zote za hii dunia, lakini uwe na mama na baba. Furaha na amani yako itapamba katika maisha yako yote.

    Watu hawa ni sawa na MUNGU wako, wazazi ni sawa na moyo wako, ni sawa na damu katika mwili wako, ni sawa na maji katika maisha haya ya kila siku.



    Wanafunzi na walimu walitambua hilo, kamwe hawakumbugudhi kijana huyu aliyekuwa mwenye upeo mkubwa wa kufikiri kuliko baadhi ya wanafunzi wengine wa shule ile aliyokuwa anasoma.

    Hatimaye Mama Eddy hata kazini kwake akasimamishwa kwani alikuwa si msaada tena. Ilipaswa ifanyike hivyo kwani ile ni shule ambayo inahitaji kuendeshwa na walimu au wafanyakazi wanahuodhuria kazini kila siku. Hutakiwi kulaumu uongozi wa shule kwa hilo.

    Hawakumuacha hohe hahe tu, walimsaidia kwa kila kitu hadi pale mama huyu alipoanza kuchezesha macho na mikono yake. Sindano aliyochomwa, ni wazi iliathiri kiasi kikubwa cha ubongo wake na ndio maana upande mmoja wa mwili wake ukapooza.

    Mwaka mmoja ukatimia, mama yule akiwa palepale hospitali. Alikuwa ni mtu wa kufanya yote hapohapo, wauguzi walifanya kazi ya maana kama kazi yao ilivyowaambia. Hawakuwa watu wa kumtenga mama huyu, kwani leo kwa huyu na kesho ni kwako.

     Ndio maana wanasema ‘MAISHA NI MALAYA’, baada ya kwa yule, yanaenda kwa mwingine na kisha kwako. Huwezi jua MUNGU kapanga nini katika maisha yako. Hivyo ndivyo wauguzi wale walivyoamini, na kazi kweli waliifanya.

    Kazi hiyo kubwa waliyoifanya wauguzi, ndio ilimpa ahueni Edson Lake na kumfanya aende kufanya mitihani ya kuingia kidato cha pili. Alifaulu vizuri sana licha ya matatizo hayo yote.



    Ndugu wa Mama huyu hawakuwa na muda hata wa kuja kusema pole. Wote waliishia kutumbua mali za Baba Eddy, wote walijiona tayari dunia imeegemea upande wao. Hakuna aliyekumbuka hata kumpelekea mabaki ya chakula mama huyu ambaye alikuwa ni mtu mwenye moyo bora kuliko mwanamke yeyote waliyewahi kuishi nao.

    Hata wake zao hawakuwa na moyo mwema kama mama huyu, lakini hilo kwao lilipita tu, ni kama mioyo yao ilikuwa inatobo katikati, yaani hayo yote yalipita katika tobo hilo na kupotea. Hawakuhisi maumivu yoyote. Inasikitisha, lakini MUNGU aliandika hayo, na yametimia.



    Miezi sita mbele, ndipo Mama Eddy aliruhusiwa kutoka hospitali na kuanza kupewa huduma zile akiwa nyumbani kwake ambapo napo walihama na kuhamia huko ambapo wanaishi sasa hivi, hiyo yote ni katika kuokoa gharama za maisha. Walibakiwa na kiasi kidogo sana kwenye visanduku vyao vya fedha vinavyotunzwa na benki. Kidogo nyumbani kukamfanya mama huyu kuanza hata kuongea lakini bado mwili ulikuwa umepooza kama kawaida.

    Mama Eddy akawa kapoteza mali pamoja uwezo wa kufanya kazi baada ya kujiingiza katika kudai haki zake. Huo ndio ukawa mwisho wa matumaini ya kurudisha mali zake.

    ****

    “Eddy, naweza kuongea na wewe hapa nje mara moja.”Winfrida alitoa ombi kwa Edson ambaye alimuangalia mama yake kabla ya kuchukua maamuzi ya kunyanyuka na kutoka nje akiwa na Win.



    “Mimi naonelea, tutoke hapa nyumbani na kwenda kukaa nyumbani kwangu. Kama utapenda lakini.” Winfrida alimwambia Edson kwa sauti ya kukwama kwama kana kwamba alikuwa anaogopa kitu Fulani.



    “Mapema sana Dada yangu.” Edson aliongea lakini aliona uso wa Win ukibadilika na kuwa kama kalamba ndimu.



    “Nishakukataza kuniita dada. Hata mle ndani umeniita hivyo, unaniboha wewe.”Win aliongea kama kwa kufoka na kumfanya Edson acheke badala ya kumshangaa au kununa.



    “Kumbe ukinuna unakuwa mzuri hivyo. Nimekuona mara ya pili ukinuna.” Edson alitania huku akitabasamu zaidi ya pale mwanzo. Ilikuwa yapata kama saa moja na nusu jioni wakati haya yanatokea.



    “Na kwingine wapi uliniona nimenuna.” Win alimuuliza Eddy kwa sauti ya chini na akiwa kalegea. Masikini ya MUNGU, hakufahamu kuwa anaonesha udhaifu mbele ya mwanaume yule mdogo.



    “Jana wakati nipo kwako. Nilipokuwa nakutazama wakati unaenda chumbani kwako.”Eddy alijibu kwa kifupi na kumfanya Win acheke kwa haya kabla hajainua uso wake na kurudi katika kile kilichowaleta pale.



    “Kwa hiyo unakubali kuhama hapa au hautaki.”Sauti mwanana ya Win ilipenya vyema katika masikio ya Edson.



    “Nitakupa jibu kesho basi kwani ni lazima niongee na mama yangu. Siwezi nikasema bila kujadiliana naye. Naomba nijadiliane naye.” Eddy aliongea huku akiwa anamtazama Win kwa macho yake makavu yaliyokuwa hayajavishwa mawani kwa wakati ule.



    “Haya sawa. Basi ngoja nikamuage mama na mimi niende nyumbani. Kesho nitakuja kuwasikiliza mlichoamua.” Win alimwambia Eddy na kisha akaingia ndani ambapo alimuaga Mama Eddy na kutoka nje ambapo napo alimuachia Edson kitita ha fedha halali za Kitanzania.

    Akapanda gari lake na kisha akatitia kutoka katika eneo lile.



    ****

    “Mama, huyu dada kaniomba atuhamishe hapa na kwenda kukaa kwake. Sijui wewe unaonaje kuhusu hili.”Edson alianza kuongea na mama yake katika sauti ya kuomba zaidi.



    “Mapenzi yanaweza kukusababisha ukafanya jambo la ajabu sana ambalo unaweza kushangawa na nusu ya dunia hii. Mapenzi si kitu cha kitoto pale yanapokukumba. Kwa sababu ya mapenzi, unaweza kujikuta ukihamisha hata bahari na kuipeleka pale ambapo mtu umpendaye anataka iende,” Kimya kilikuwa kikubwa katika mwili wa Edson wakati mama yake akiongea haya maneno.



    “Mwanangu…”Mama Eddy aliongea na kumshika Edson kichwani. “Hayo anayoyafanya huyu binti yanasukumwa na mapenzi mazito ambayo anayo juu yako. Nashukuru mapenzi hayo aliyonayo juu yako, ndiyo ambayo kayahamishia na kwangu,” Alizidi kuongea huku akiwa anatabasamu mwanana usoni mwake huyu mama.

    “Lakini nachokuhasa mwanangu, chunga sana kutendewa kitu kwa sababu ya msukumo wa moyo. Huwa napenda kuongea Kiingereza pale naposisitiza jambo fulani kwa sababu Kiingereza kimeshiba kimisemo zaidi ya Kiswahili.” Sura ya Mama Eddy ilibadilika na kuwa yenye kuonya zaidi kuliko hapo mwanzo.





    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    FURAHA,



    Furaha ni hali ambayo inamkumba mtu kwa sababu ya jambo fulani. Ni furaha pekee ndiyo iwezayo kumfanya mtu kuishi miaka mingi bila kusuasua katika mambo yake. Furaha tamu huja baada ya huzuni, na huzuni mbaya huja baada ya furaha. Maisha ni kama shilingi idondokayo kwenye sakafu iliyojengwa kwa saruji nzito, huwezi jua sarafu hiyo itadondokea upande gani.

    Ndivyo maisha yanavyoenda. Huwezi jua kuwa utadondokea kwenye maisha ya furaha au ya huzuni. Yapaswa kuwa tayari kwa hali yoyote katika maisha yako, lakini furaha, ndiyo njia pekee ya kuishi kwa amani na kwa upendo.

    KUWA NA FURAHA.



    ENJOY.



    “Once the heart starting to understand what’s another heart needs, the understanding heart starts to forget the past heart needed. (Pale moyo unapoanza kuelewa moyo mwingine unachokihitaji, moyo huo unaanza kusahau moyo wa zamani ulichokihitaji)” Maneno hayo yakamfanya Edson ainamishe kichwa chake chini akiyatafakari uzito wake. “Sisemi baada ya wewe kuanza kuelewa moyo wa huyu binti utaanza kunisahau mimi, hapana. Hapa na maana kwamba, usije ukasahau mioyo ambayo kwako ilikuongoza katika maisha yako kwa kuwa tayari unaye kiongozi mwingine. Ni jambo jema na la manufaa kwetu sisi sote kutoka hapa na kwenda anapoishi Win. Sina kipingamizi katika hilo kwani ni mwanamke mwenye upendo wa kweli. Kuwa mwenye shukrani kwa MUNGU kwa bahati hii.”Alimaliza Mama Eddy na kumuacha mwanaye hana la kusema.



    “Siwezi kukusahau mama yangu au yeyote aliyenifikisha hapa. Hamna kama ninyi katika maisha yangu. Nitawaheshimu na kuwatukuza daima. Naomba usikasirike mama yangu kwani sasa kidogo tunaweza kusaidiwa na kurudisha kile ambacho ulikikosa kwa muda mrefu.”Edson aliongea baada kimya kifupi kilichochukua nafasi muda mchache uliopita.



    “Mghuu.”Mama Edson aliguna na kutikisa kichwa chake kama mwenye kusikitika. “Eddy, life gives you an opportunities to live, and not the choices. (Eddy, maisha yanakupa nafasi za kuishi, na si machaguo).”



    “Unaonekana mwenye kufanya machaguo katika maisha yako na si kutumia nafasi uliyopewa. Ni wazi umechagua kusaidiwa na huyu binti na si kumpa nafasi ya kukusaidia. Hiyo ni mbaya mwanangu, tena mbaya sana kwani mwisho wa siku utakuwa kama mtumwa katika maisha yako. Usichague bali chukua nafasi.

    Na jinsi ya kuchukua nafasi, ni wewe kutojijengea tabia ya kutoonekana mwenye uhitaji wa msaada zaidi wa mtu. Ridhika na hapa ulipo, kisha ndipo ufanye maamuzi ya kwenda palipo bora zaidi ili hata kama kule pakiwa pagumu, urudi pale ulipotoka.

    Take an opportunity, leave your choices my son. The choice is an exam, but opportunities are the best answers of the exams. Think twice, and make your choice in this. (Chukua nafasi, achana na chaguzi mwanangu. Kuchagua ni mtihani, lakini nafasi ni majibu ya mitihani. Fikiria mara mbili, na fanya chaguzi katika hili)”Kimya kikatanda tena baada ya maneno haya.

    Kifupi Eddy hakuwa akielewa kama anamfuata Winfrida ili asaidiwe shida zake au anamfata Win apate nafasi ya kupumzika kusaidiwa. Hilo ni tatizo kubwa katika maisha ya wengi hasa vijana wa sasa hivi.

    Kamwe usiwe mtu wa kutaka msaada zaidi. Bali kwanza yapasa kujikubali kuwa wewe si muhitaji wa msaada bali unahitaji kupumzika kupewa misaada. Usiwe mtu wa kupokea bila hata kufikiria utalipa nini kwani malipo yake huwa ni utumwa katika maisha yako mwenyewe. Zingatia hilo.



    “Mama. Tunahitaji kutoka hapa na kwenda kuishi kwa Win ili tuweze kupata maangalizo ya karibu na zaidi mimi katika kusoma kwangu. Nakuomba mama, siwezi kwenda kinyume na maneno yako. Nachukua nafasi na si kufanya chaguzi. Kama yatakuwa magumu hata huko, basi tutarudi hapa hapa. Naomba mama yangu.”Maneno ya uhitaji yalimyoka Edson na kumfanya mama yake ashindwe kusema hapana katika hilo bali kumkabalia hasa aliposikia mwanaye anaongelea Elimu yake.



    “Usijali Eddy, sina kinyongo na huyu binti. Ana roho nzuri kuliko unavyojua, na najua anakupenda sana, usitupe moyo wake hata kidogo, mpe moyo wako na kamwe usiruhusu moyo wake uende kwa mwingine. Hapo ndipo utakuwa umeshinda mapigano ya mapenzi dhidi ya mapigano ya hisia. Tutaenda na mwambie nashukuru sana kwa chochote anachokifanya juu yetu.” Edson Lake alijikuta akimkumbatia mama yake baada ya kuambiwa hayo na hakusita kudondosha chozi la furaha kwa sababu ya ruhusa hiyo.

    ****

    Ilikuwa ni furaha pekee iliyotawala katika familia mpya ya Winfrida. Aliwakariibisha Edson na mama yake katika nyumba yake ambayo ilikuwa kubwa na pana. Si Win pekee ndiye alikuwa katika furaha hiyo bali hata mama na kijana wake. Kila muda walipambwa na tabasamu katika nyuso zao.



    Sauti za vicheko zilisikika kila mara katika nyumba ile ya Win. Ni siku nzima ilikuwa ni furaha tu. Hakuna ambaye alikuwa anahuzuni katika moyo wake. Tayari Edson na mama yake walikuwa wamehamia katika nyumba ya Win huku ile nyumba walipotoka wakiicha ile familia ya yule mtoto ambaye alikuwa anakaa na mama yake Edson. Waliacha kila kitu kule na kwa Win walikuja kuanza maisha upya. Walimuamini Winfrida kwa mudam mfupi sana, na walipaswa kufanya hivyo ili kufanikiwa safari nzito ambayo anayo Edson Lake hasa katika elimu.

    Lakini kwa uande mwingine hawakupaswa kufanya hivyo, ni kheri wasingekutana kabisa na Win kwa sababu yeye ndiye chanzo cha mambo mengine kabisa kutokea. Maisha ni kama sarafu inayodondokea kwenye sakafu iliyoumbwa kwa saruji nzito.



    “Win, shukrani sana kwa huu ukarim wako, sina cha kukulipa katika hiuli.” Eddy aliongea wakiwa sebuleni na Win wanapata chakula usiku. Wakati huo mama yake alikuwa chumbani anahudumiwa na wafanyakazi wa nyumba ile.



    “Usijali Eddy, jisikie upo nyumbani na kuwa huru. Ukitaka chochote, nipo kwa ajili yako, utapata tu!” Maneno hayo yakamfanya Edson atabasamu na kujiona mwenye bahati kubwa kwa wakati ule, akaendelea kula chakula ambacho kimeandaliwa.



    Muda wa kulala ulipowadia, kila mmoja alienda kulala katika chumba chake. Ni chumba cha Win ndicho kilikuwa taabani kwa usiku ule. Hakikupumzika kwa sababu mwanadada yule hakuwa amelala kwa sababu ya kumfikiria Eddy. Alikuwa anawaza na kuwazua jinsi ya kumnasa ndege wake. Aligalagala kitandani huku akiwa hoi kwa hisia kila alipokuwa akimfikiria kijana yule mdogo kwake. Win alikuwa kazama katika dimbwi la mapenzi, na Edson pekee ndiye alipaswa kumtoa katika dimbwi lile lenye tope zito la maumivu ya mapenzi.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Jamani Eddy, nakupenda kiukweli. Njoo basi unipooze haya maumivu yangu.” Aliongea kwa masikitiko makubwa Win kana kwamba Edson alikuwa anamsikia au anamuona.

    Binti yule alikuwa kauukubali ukweli kuwa kampenda Edson, na ni yeye pekee (Eddy) ndiye atakayempa furaha mpya. “Sijui nifanyaje jamani, naogopa kumwambia.” Alinong’ona peke yake na mawazo hayo yaliendelea hadi usiku sana tu ambapo alibebwa na usingizi mzito.

    ****

    Zikapita wiki mbili tangu Edson na mama yake wahamie katika nyumba ya Winfrida. Walikuwa wanafuraha kila wakati na kulikuwa hamna ubishi kuwa maisha yao yalikuwa mazuri mno kwa sababu ya uwepo wao wa pamoja.



    Licha ya kukaa wote kwa pamoja kwa siku zote hizo, si Win wala Eddy aliyefungua kinywa chake na kumueleza mwenzake kuwa anampenda japo hisia hizo sasa zilikuwa wazi katika mioyo yao. Kila walichofanya na kila walipokutana, macho yao yaliongea lugha moja pekee ya mapenzi. Walitazamana kila wakati pale walipopata wasaha huo lakini hakuna ambaye alimwambia mwenzake anachokihisi moyoni mwake hadi pale siku moja Winfrida alipomuomba Eddy wakaongee nje. Ilikuwa yapata saa tatu za usiku baada ya kumaliza kula, ndipo wakatoka na kwenda kibarazani ambapo Win alianzisha maongezi huku saa nyingine akikwamakwama kutokana na aibu za kike mbele ya mwanaume.



    “Eddy, siri nzito ya moyo w mwanamke hufungwa kwa aibu yake. Si rahisi mwanamke kuitoa siri kubwa ambayo moyo wake umeibana kwa muda mrefu. Lakini mambo yamuwiapo ugumu, anakuwa hana siri tena. Mwanamke kaumbwa na moyo mwepesi sana katika kutunza siri hasa ambayo inaweza kumtesa hisia zake.” Alianza kuongea hivyo binti yule mrembo, lakini hakuishia hapo, akaendelea “…….Sipo tayari siri hii kunitesa na sipo tayari kukuficha kilichopo katika moyo wangu kwa sasa, naomba unilewe nitakachokwambia.” Alimaliza Winfrida kwa ombi dogo ambalo Eddy hakulipa nafasi na badala yake akaanza kuongea yake.



    “SIRI.” Aliongea Edson kwa sauti ya chini na kisha akamtazama Winfrida usoni huku binti yule asijue ni nini ambacho kijana alitaka kukiongea baada ya neno hilo.



    “Siri ya moyo ni moto, Huchochewa na hisia,

    Moyo hukaa kushoto, U rahisi kuumia,



    Damu pia ina joto, Penzi limeniingia,

    Siri ndani yangu mimi, hadharani naiweka.



    Jipu hili liwivalo, Moyo wako nd’o sindano,

    Hili nilitumbualo, Ni maumivu ya jino,

    Kwa kila nilisemalo, Hakika kwako ni neno,

    Siri ndani yangu mimi, Hadharani naiweka.



    Najua chozi la penzi, Kwako limekudondoka,

    Nitakuwa ni mshenzi, Mpumbavu atacheka,

    Hisia zapaswa enzi, Hata kama zimechoka,

    Siri ndani yangu mimi, Hadharani naiweka.



    Nani chozi hulifuta, Inabaki kuwa siri,

    Na sasa nakufuata, Moyo nitausitiri,

    Najua nitachopata, Lakini siyafikiri,

    Siri ndani yangu mimi, Hadharani naiweka.



    Haya nayosema mimi, Kwako we’ yanasikika?

    Usije kuwa mnyimi, Haya yakakuchomoka,

    Yatokayo kwa ulimi, Kichwani hufikirika,

    Siri ndani yangu mimi, Hadharani naiweka.



    Najua hujanielewa, Ila ukweli nakupa,

    Ni kweli sijachelewa, Na sina wingi wa pupa,

    Kwako nitakuwa dawa, Moyoni sitakutupa,

    Siri hii ninakupa, Nakupenda sana Win.”



    Ni shairi ambalo alipomaliza, Winfrida alikuwa anamtazama kijana yule kwa macho legevu huku akiwa haamini kama anaimbiwa yeye lile shairi. Alijikuta anamfuata kijana yule machachari na kumkumbatia kwa nguvu akisindikizwa kwa maneno machache.



    “Nakupenda sana Edson, naomba niwe wako daima”. Maneno hayo yalikuwa ni ukurasa mpya wa mapenzi baina ya hawa watu. Kilichofuata hapo ni kubadilishana ndimi zao huku kila mmoja akiwa mgeni katika tendo hilo ambalo liliwasisimua kila kiungo cha mwili wao. Hakika walikuwa wanapendana, hilo lilithibitika baada ya wao kuingia chumbani.







    AMANI,



    Kama amani ndio msingi wa maisha ya kila mwanadamu, basi nitaitafuta amani hiyo kwa udi na uvumba, kwa upanga na hata bunduki. Nitahakikisha naipata amani. Lakini swali vipi niklihitaji amani ya moyo? Je nahitaji pesa kuitafuta? Nahitaji panga au bunduki ili niipate? Jibu lake ni hapana.

    Njia pekee ya kuipata amani, ni kuruhusu moyo wake ujawe na furaha. Furaha pekee ndio inayoleta amani ya moyo. Kama hauna furaha, basi ni wazi amani yako itakuwa nusu kwa sababu huna uhakika kwa nini huna furaha.



    ENDELEA.



    Ulikuwa ni usiku mpya kwa wawili wale. Usiku ambao hakuna ambaye angeweza kuusahau kirahisi. Miili yao ilikubali kuwa pamoja kwa kuungana na kukitaabisha kitanda kwa dakika kadhaa zenye kila hali ya kuziita ni dakika za raha na starehe iliyokifani.

    Nasema haya kwa sababu miili hii hapo kabla ilikuwa haijui ladha ya mapenzi toka kwa mtu ambaye inampenda kwa mwili na moyo wote. Usiku huo ulikuwa ni usiku wa watu waliopendana. Mapenzi kati ya Win na Kijana Eddy, yakafunguliwa kwa namna yake.



    “Eddy, sijui nikwambiaje. Lakini naomba kitu kimoja tu!” Aliongea kwa sauti mororo Winfrida akiwa amemkumbatia kwa chati Edson. Akaendelea, “Nipende daima. Usiogope huu mwili au hali yangu ya maisha niliyonayo. Hivi ni vitu vya kawaida tu! Haviangaliwi katika mapenzi, nadhani walijua hilo.”



    “Palipo mazao yaliyostawi na kumea vema, hakika hapo kuna mkulima bora. Na palipo na mkulima bora, hapo ndipo kuna mazao mazuri.” Aliongea Edson na kuweka tu.



    “Una maana gani kwa maneno hayo.” Aliuliza Win huku akiendelea kupapasa kifua hafifu cha Edson Lake.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    “Namaanisha wewe ni zao linalomea vizuri, na hakika wastahiri mkulima bora. Na si mwingine, bali ni mimi.” Akatulia tena Eddy kabla hajaendelea. “Mimi ni mkulima bora, sitacheza na mazao yako. Nitayatunza kadiri ya uwezo wangu. Sitajali ukubwa wa zao linalonichezea kifua changu kwa sasa, bali nitajali kujali hisia zake pekee. Sitaliumiza zao hili kwa kukimbilia zao lingine, bali nitalikumbatia zao hili hadi pale MUNGU atapoamua kulichukua. Hakuna ambacho kitatutenga kwa sasa, nakuahidi hilo Winnie.” Maneno hayo yalimfanya Win ashushe pumzi ndefu na kukaa kimya kwa muda bila kuongea.



    “Eddy. Unajua mimi nimesomea lugha, lakini haya unayoongea, ni zaidi ya lugha kwangu. Siyo kama sijawahi kuyasikia kama haya, la! Ila kwa elimu yako na umri wako, sikudhani unaweza kuwa na maneno konde namna hiyo.” Hatimaye baada ya kimya kifupi, Win aliongea hayo. Hakuishia hapo, alizidi kutiririka. “Sijui nikutunuku heshima gani kwako inayoendana na haya ambayo nayafikiria, hakika umebarikiwa. Na njia pekee ya kufika mbali zaidi, ni wewe kusoma.” Alimaliza kwa busu jepesi kwenda kwa Eddy.



    “Sina budi kusoma. Na ninaomba uwe nguzo yangu imara katika kufanikisha hili. Nitafurahi sana kama nitafikia kiwango cha elimu ambacho wewe na wengine wanacho.” Eddy aliongea naye na taatibu akaupitisha mkono wake kwenye mgongo wa Win. Akapapasa mgongo ule kwa chati na kwa mahaba mazito. Win akawa anasisimka kamamwewe aliyepigwa jiwe la kichwa.

    Walikuja kushtuka wapo katika dunia nyingine kabisa. Dunia yenye raha isiyo na kifani. Dunia yenye kila amsha ya hisia za mwili hadi moyo. Dunia ambayo kwa hakika, ilikuwa na utamu uliopitiliza. Utamu ambao hata ungepigwa risasi za miguu, bado usingehisi maumivu. Walikuwa wakishiriki tendo la ngono kwa mara nyingine. Na huo ndio ulikuwa ukurasa wa kwanza wa mapenzi ya hawa wawili.

    ****

    Ilikuwa ni ngumu sana kwa Win na Eddy kuficha mapenzi yao yaliyochipua kwa kasi katika mioyo yao kwa ni licha ya kujificha na kujibana, lakini mkubwa ni mkubwa tu! Mama yake Edson aliujua ule uhusiano mapema kuliko wao walivyotegemea. Ndani ya wiki moja tu! Mama Edson tayari alikwishafahamu ni nini ambacho mwanaye na Win wanakifanya.



    Licha ya kutokuwa na uwezo wa kusimama toka pale kitandani, lakini aliweza kuona macho ya wawili wale na kutambua ni nini kinaendelea kati yao. Hakusita kuwashauri kutokana na hayo ambayo wameyaanzisha.



    “Wanangu. Katika dunia hii ya mapenzi, hasa dunia yenu ya utandawazi, kuna mambo kadhaa ambayo ninyi kama vijana, yapaswa kuyazingatia.”Alianza kuongea Mama yake Edson Lake. “Mapenzi sikama nyie mnavyodhani yalivyo. Mapenzi ya sasa ni donda, tena donda ndugu ambalo likipona hapa, linajitokeza kwingine.” Maneno hayo yalimtoka Mama yule wakati Edson na Winfrida wapo chumbani kwake wanampa chakula.



    “Mama kwa nini unaongea hayo?” Win aliuliza kwa sauti ya upole.



    “Hakuna kitu ambacho nilikuwa nakiogopa katika maisha yangu kama jicho la mtu mzima hasa mama na baba yangu. Walikuwa wakikuangalia tu, wanaona hadi utumbo wako umelisha nini siku nzima. Nadhani nimerithi jicho la namna hiyo. Unaweza ukamficha kila mtu ambacho kipo moyoni mwako, lakinii huwezi ukamficha mtu kile kilihokatika paji lako la uso.” Mama yule aliongea hayo na kumfanya Win ainamishe kichwa chake kwa aibu. “Eddy, nimekuzaa mimi wewe. Huwezi ukanidanganya hata chembe. Nakujua ukiwa na hasira, nakujua ukiwa na furaha, ninakujua ukiwa katika hali yoyote ile. Upo katika mapenzi mazito. Naona kwa macho yangu.” Mama yule aliongea huku amemtazama Edson, mtoto wake wa kumzaa.

    Edson akatabasamu kwa aibu na kutikisa kichwa kushoto kwenda kulia na kulia kwenda kushoto. Akamuangalia mama yake.



    “Katika maisha yangu, nimesoma kidogo sana hadi sasa hivi. Lakini ukiniuliza ni mwalimu yupi ambaye huwezi kumuacha kumtaja maisha yangu yote, nitakujibu ni mama. Kama nikifika chuo, ukiniuliza ni Profesa yupi ambaye siwezi kumfahamu, nitakujibu ni mama.” Edson aliongea hayo huku akimuangalia mama yake kwa upendo. Akaendelea, “Mama ni zaidi ya walimu wote wa hii dunia. Mama ni zaidi ya maprofesa na madaktari unaowajua wewe. Mama huyu ambaye wengine wanamdharau leo hii, ndiye wa kwanza kukwambia sema Baba.



    Ndiye aliyekwambia sema Mama. Huyu ndiye aliyekukataza ushike moto, ni hatari kwako. Hutu ndiye alkuwa halali pale unaposhikwa na homa kali, hata iwe usiku wa manane. Huyuhuyu ambaye wengine wanamsonya baada ya kufanikiwa, ndiye aliyekuokoa pale ulipotaka kutumbukia kwenye maji ya moto wakati unajifunza kutambaa. Na huyu ndiye aliyekuwa wa kwanza kukufanya utembee. Alikushikilia ili utembee, na alikuachia ili uende peke yako. Ulipojaribu kudondoka, alikuwahi ili usiumie. Hamna anayeweza kufanya hayo, awe Mwalimu au Profesa. Yeye ndiye Profesa wa kwanza kwako Win, na ni Profesa wa pili na pia wa tatu. Profesa wa nne ndio hao wengine.” Edson safari hii aliongea huku akigeuzia macho yako kwa Win.



    Mkono wa mama yake ukashika kichwa chake. Edson akamtazama mama yake na kukutana na tabasamu zito ambalo mara chache sana Eddy aliliona.



    “Sistahili hizo sifa kwa sasa mwanangu……” Mama Eddy hakumaliza maneno yale, Win alikuwa amedakia naye akaanza kushusha falsafa zake.



    “Hapana Mama. U mwenye kustahili sifa hizi, na zinastahili kwa mama yeyote katika dunia hii. Wewe Mama, hata mwanao akutende vipi, akirudi na kuomba msamaha, utamkumbatia haraka. Pale atakapotaka kudondoka, haijalishi anamiaka mingapi, utamkimbilia na kumdaka kama ulivyofanya wakati unaanza kumfundisha kutembea. Pale utakapoona hatari mbele yake, unakuwa wa kwanza kumuonya mwana huyu. Kwa nini hustahili sifa hizi?” Win alimuuliza Mama yule, lakini hamkumpa nafasi ya kujibu. Akaendelea, “Ni kwa sababu upo kitandani? Yaani huna uwezo wa kumnyanyua Eddy? Hapana. Si kweli mama. Unanguvu ambazo hakuna ambaye anaweza kukudondosha. Unanguvu za kuweza kuhamisha mlima Kilimanjaro uje Mwanza. Siri ya nguvu hizo ni busara zako. Siri ya nguvu hizo ni maneno yako ya kujenga. Siri ya nguvu hizo ni yale uliyoyapitia hadi sasa hivi. Bado unastahili yote aliyoyaongea Eddy.” Alimaliza Win na macho ya mama yule yalikuwa hayaamini kile yanachokiona toka kwa Win.



    “Njoeni hapa.” Maneno hayo yakawafanya wote wasogee alipomama yao. “Nikumbatieni.” Mama yule aliongea hayo na wote walicheka kwa furaha na kumlalia mama yule kwa upendo.



    “Lakini mama hujatuambia maana ya maneno yako.” Aliongea Win huku akifuta machozi ya furaha wakati ananyanyuka toka kifuani kwa Mama Eddy.



    “Mimi ni mtu mzima. Nafahamu sura zilizokuwa katika mapenzi. Mmekuwa kama vipepeo au ndege angani ambao wapo katika upendo. Mmekuwa kama watoto. Kucheza-cheza kila mnapoona hamna macho ya watu. Mimi nawaangali tu.” Mama yule aliongea na kumfanya Win azidi kuona aibu.



    “Hamna Mama…..” Win alijikakamua kuongea japo bado aibu kuu ilikuwa imetanda katika uso wake. Mama yule hakutaka Win ajitetee, akawa kamkamata mkono wake ishara ya kumfariji.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Haijalishi upo na nani katika mapenzi yako. Mapenzi si moto wala maji, ila mapenzi ni moto na pia ni maji. Ukiyaingia vizuri utajisikia raha sana kama pale unapoota moto wakati wa baridi kali au kama pale unapokunywa maji ya baridi kwenye joto kali. Lakini ukiyaingia vibaya, ni sawa na moto uliokuchoma mwilini au umezama ndani ya kina kirefu cha maji.” Mama yule mwenye ulimi ulimi uliyojaa busara na raha kuusikiliza, aliongea hayo huku bado kaukamata mkono wa Winfrida Gaula ambaye alikuwa kimya akimsikiliza. Mama akaendelea, “Sikulaumu kumpenda mwanangu wala simlaumu yeye kukupenda wewe, kwa sababu hayo yote ni machaguzi ya mioyo yenu. Huwezi kuukataza moyo pale ulipodondoka lakini unaweza kukataza macho kwa kile ulichokiona. Kuwa na mwanangu, wala usihofu kuhusu mimi. Nimeridhia kwa moyo wote, lakini kumbukeni jambo moja tu! Mapenzi si moto wala maji, ila mapenzi ni moto na pia maji kwa jinsi mtakavyoyaingia. Kuweni huru na shaurianeni yaliyomema hasa elimu.” Mama Edson, alimaliza na kumfanya Win na Eddy watulie kimya wasijue ni nini ca kuongeza na badala yake kubaki kubaki wakimuangalia mama yao akijitahidi kuutafuta usingizi.



    ****



    Mapenzi kati ya Win na Eddy yaliendelea kuwa moto kila kukicha. Haikuwa kificho tena kwa sababu nyumba nzima, kuanzia wafanyakazi wa ndani hadi wa nje, waliweza kuutambua uhusiano ule. Licha ya kuutambua, hawakuwa nyuma pia kushiriki nao katika kuujenga kwa sababu jambo pekee ambalo kwao waliliona bora, ni Win kuwa na furaha. Win alikuwa na furaha kila mara, kiasi kwamba alikuwa anawajali wafanyakazi wake labda kushinda nyakati zote za maisha yao. Kwa njia hiyo pekee, ilitosha kwa wafanyakazi wale kuendelea kulijenga pendo lililomea katika maisha ya Win.







    Kwa upande wa Edson, mambo yalizidi kuwa mazuri kwake. Masomo yalikuwa yanaenda vema kwa sababu sasa mama yake alikuwa katika mikono salama na inayoaminika. Alizidi kufanya vema katika masomo yake kila kukicha. Na zaidi, alianza kunawiri na kuwafanya walimu na wanafunzi wenzake waanze kujiuliza ni wapi alipopata faraja mpya. Na si kuuliza swali hilo tu, bali wapo wanafunzi wa kike ambao walianza kumsumbua kijana huyu kwa sababu ya fedha alizokuwa nazo na uzuri ambao hapo mwanzo ulikuwa umefichwa na makunyanzi wa umasikini. Watoto hao wa kike, hawakupea nafasi katika maisha ya Edson. Mwanaume huyu alikuwa ndani ya furaha kubwa aipatayo kwa Winfrida.



    Mama wa Edson, alikuwa ameanza taratibu kupata matibabu ya kuweza kumfanya anyanyuke kitandani. Hospitali aliyopelekwa, ilitoa tumaini jipya juu ya hali ya Mama Edson na tumaini hilo, ndilo likazidi kunyumbua nyuso za furaha walizokuwa nao wale vijana, yaani Winfrida na Edson.



    Ibrahim Singa, mwanaume mwenye kila kitu katika hii dunia. Kazi nzuri kutokana na makampuni aliyoachiwa na wazazi wake. Mwili mzuri, elimu nzuri na pesa za kutosha. Yeye alikuwa haelewi mabadiliko ya Winfrida yalitokana kwa sababu gani. Hakuwa yule Win ambaye alikuwa anakubali kutoka na yeye muda wowote amtakapo, na wala hakuwa yule Winfrida aliyempigia usiku wa manane na kuanza kuongea naye. Winfrida wa sasa, alimuumiza sana Ibrahim. Alimuumiza moyo pamoja na akili.



    Ndipo Ibra aliamua kufanya uchunguzi na kutaka kujua sababu ya Win kubadilika. Haikuchukua muda sana, na wala haikumpa tabu kwake kutambua kilichokuwa kinamzuzua Winfrida kiasi kile. Na mbaya zaidi, alijikuta akicheka peke yake pale alipogundua kuna kijana wa kidato cha tatu ndiye aliyembadilisha Winfrida.



    “This is crazy. (Huu ni ukichaa)” Aliongea peke yake Ibrahim alipokuwa anatoka nyumbani kwa Winfrida baada ya kuupata ukweli kwa mlinzi wa getini ambaye alimuambia mengi yaliyopo na yale ambayo hayakuwepo, yote ni katika kumfanya Ibrahim amuamini na kumpa kiasi fulani cha pesa. Mlinzi yule alifanikiwa kukamata pesa, lakini tayari alikuwa amekwishatengeneza donge katika moyo mgumu wa Ibrahim Singa, donge ambalo liliambatana na uchungu mkali, uchungu ambao labda maumivu yake yalizidi yale ya kuchanwa kwa kiwembe kipya. “Yaani kitoto cha darasa la kwanza ndicho kimembadilisha huyu mwanamke na kusahau kabisa kuhusu mimi? Ama kweli dunia ni hadaa, ila ulimwengu…..” Ni kama alitaka mtu atokee na amalizie msemo huo, lakini hakutokea hadi pale alipoingia ndani ya gari lake la thamani na kutokomea toka pale.

    ****

    Siku nyingine tena, siku hii labda ilikuwa ni ya kipekee kwa Ibrahim. Nasema ni ya kipekee kwa sababu ndiyo siku ambayo Winfrida alikubali kutoka naye na kwenda eneo fulani na kuanza kuongea mengi sana juu ya maisha yao. Lakini hasa, Ibrahim alikuwa akitaka kuanzisha mahusiano na Winfrida. Na kwa wakati huo, tayari Ibra alikuwa anamjua vema sana Edson Lake. Alimjua kuanzia sura, maisha yake nahadi shule mpya aliyokuwa kahamishiwa ili kujiendeleza kimasomo.



    Bwana Ibrahim, alikuwa uso kwa uso na mrembo wa haja. Mrembo kwelikweli na si mrembo wa nakshi za vipodozi bali akiwa katika ngozi yake ya asili.



    “Eheee! Mwanasheria wangu huyo.” Win aliongea kwa bashasha kedekede wakati anaenda eneo alilokuwa amekaa Ibrahim. Naye Ibrahim aliinuka na kumlaki Win kwa kumbae dogo, kisha wakaketi kila mmoja kwenye kiti chake.



    “Mbona unanifanyia hivi Win?” Alikuwa ni Ibra baada ya salamu na utani wa hapa na pale kuchukua nafasi yake kwa muda wa dakika chache.



    “Vipi tena Ibra?” Aliuliza Win huku bado tabasamu mwanana likiendelea kurindima katika uso wake.



    “Unautesa moyo wangu Win, umeufanya kuwa gharika sasa badala ya kuwa nyakati tamu za mavuno yatokayo shambani.” Aliongea kwa ufupi Ibra huku akimuangalia Win kwa macho makavu. Lakini hakuona badiliko lolote lililotokea wakati akisihi maneno yake. Akaendelea, “Win, hivi kwa nini unaingiza njiti iliyowashwa kwenye petroli angali wajua ni hatari kwa maisha yangu? Kwa nini Win?” Akaliacha swali hilo likielea hewani. Win akamtazama yule bwana kwa macho yake legevu, akacheka cheko ya chini huku akitikisa kichwa chake kushoto kwenda kulia na kulia kwenda kushoto.



    “Nini tatizo lako Ibra? Usiwe mtu wa misemo angali lugha laini ipo na waweza kuitumia na nikakuelewa vema tu!” Win aliongea kwa taratibu na wakati huo, juisi aliyoiagiza ilikuwa imetua mezani kwake.



    “Sina lugha ngumu Win, lakini kitendo cha wewe kuingia katika mahusiano na Eddy, ndicho kinanifanya nitamke haya mbele yako. Kwa nini Win?” Maneno hayo yakamfanya Winfrida acheke zaidi na kisha akamuangalia Ibra kwa macho yaleyale ambayo kamwe hayakuwa yakijieleza maana yake mbele ya Ibrahim.



    “Ibra kaka yangu, yakupasa kunipongeza kwanza kwa hilo.” Aliongea Win na kuamsha mshangao wa haja kwa Ibrahim.



    “Kukupongeza!? Kwa lipi hasa Win? Kuwa na mtoto katika mapenzi?” Akauliza Ibra.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Hapana. Si kwa kuwa na mtoto katika mapenzi bali kupenda. Imenichukua nusu ya maisha yangu kuja kupenda. Nashukuru MUNGU nimependa. Suala la udogo wa Eddy au umri, it doesn’t matter (haijalishi). Age is just a number. (Umri ni namba tu)”



    “Inamaana hujawahi kunipenda Win?” Akauliza Ibrahim.



    “Hapana Ibra. Nakupenda hadi sasa, na ninakupenda sana. Lakini nakupenda kama ndugu au kaka yangu tuseme. Wewe si sawa na Eddy kwa jinsi navyompenda.” Maneno hayo yalimchanganya sana Ibrahim lakini alijipa moyo na kuendelea kutema maneno yake mwanana.



    “Lakini Win. Atakupa nini yule mtoto mdogo? Hana pesa kama mimi, na wala hana chochote ambacho kitakuweka juu kithamani. Win, kuwa na mimi mpenzi wangu. Nakuahidi kukutunza na kukuthamini kwa kila kitu na kwa kila hali.”



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog