Search This Blog

Sunday, July 10, 2022

SIPENDI UJINGA MIMI - 5

 







    Simulizi : Sipendi Ujinga Mimi

    Sehemu Ya Tano (5)



    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    Wote kwa pamoja wakaingia alipolazwa mgonjwa wao. Mama Salehe alipomuona mama Juma machozi yakaanza kumtiririka, kakumbuka maovu mengi aliyomfanyia, akakumbuka alivyojaribu kumuua. Hakika nafsi yake ilimuuma mno. Akashindwa kujizuia kuangusha chozi na akashindwa kuongea lolote. Mdidi alivyoona hali inakuwa ivyo ikabidi amtoe mama Juma nje kwa muda ili wampe nafasi mama Salehe aweze kutulia. Baada ya dakika 10, akapoa na apo wakapata nafasi ya kumuona na kuongea naye,

    “Pole sana shoga yangu,” alisema mama Juma.

    “Sidhani kama nastahili pole yako mama Juma, nimekukosea sana,” alisema mama Salehe huku machozi yakimtoka.

    “Usijali ndugu hamna binadamu aliyekamilika wote tunamapungufu yetu, kikubwa ni kusahau yaliyopita”

    “leo ndio nimeamini kuwa si kila akuchekeaye ni rafiki wengine ni maadui wakubwa, nimekuwa na marafiki wengi mtaani lakini angalia hamna hata mmoja aliyekuja kunitazama, ila ninyi ambao niliwachukulia kama maadui zangu leo ndio mmeacha shughuli zenu na kuja kuhangaika name,” aliongea huku akizidi kulia.

    “Mama Juma na Mdidi naomba mnisamehe sana kwa yote niliyowafanyia, mimi kisayanisi sina ugonjwa wowote na najua nani aliyesababisha mimi kuwa hivi. Ukweli mimi hadi kupatwa na hali nilikuwa na mpango wa kumuangamiza kabisa Mdidi”

    “Nini!”

    wote waliokuwa pale walishtuka mno na kauli ile Mdidi mwenyewe ikabidi amsogelee mama Salehe ili asikie vizuri kile alichosema,

    “Naongea nikiwa na ufahamu wangu kamili na ninamaanisha kile nisemacho, nina muda mfupi sana wa kuishi katika dunia hii, adui yangu ana nguvu kuliko nilivyofikiri lakini kabla sijaondoka nataka nisawazishe pale nilipokosea. Nyie watu wawili nimewakosea sana ingawaje wapo wengine niliowakosea ila ninyi ni Zaidi,” aliendelea kuongea mama Salehe huku machozi yakimtoka.

    “Hapana uwezi kufa mama Salehe! Daktari amesema wewe ni mzima na huna ugonjwa wowote ivyo ondoa shaka,” alisema Mdidi.

    “Vita ya ulimwengu wa giza ni kubwa kuliko ile ionekanayo kwa macho ya nyama, sina nguvu ya kupambana, nimefanya kosa na lazima waniadhibu kwa kifo”

    “Wakina nani hao watakao kuadhibu?” akauliza mama Juma.



    *************************



    Mama Ashura baada ya kuona mpango wake umeenda kama alivyoupanga, akaanza harakati za kutaka kummaliza kabisa Mdidi. Swala la mama Salehe kuwa hospitali hakuwa na shaka nalo kwani aliamini giza tu litakapoingia mama Salehe hatoweza kuona jua la siku inayofata. Hakujua kuwa wakati huo shoga yake alikuwa akifichua siri isiyostahili kufichuliwa,

    “Mdidi wewe ndio kikwazo changu cha mwisho, nikifanikiwa kukuondoa wewe nitakuwa Malkia na wote watanieshimu na kunisikiliza, yeyote atakayeingilia kati kukutetea sitomuacha mzima. Nimeanza na shoga yangu wewe unafata usiku huu”.



    Aliongea mama Salehe huku akiingia katika chumba ambacho kinaonekana kutotumika kwa muda mrefu, akaingia moja kwa moja hadi upande wa kushoto wa chumba icho ambapo palionekana kama ni sehemu ya kufanyia ibada ya kichawi, kwani kulizungukwa na mishumaa, ubani na udi pia kulikuwa na matunguru alikadharika beseni la maji. Mama Ashura akawasha mishumaa, kisha akawasha ubani na udi, akajifunga kitambaa chekundu kichwani na kuanza kuongea maneno yasiyoeleweka kisha akalisogelea beseni la maji na kunyunyuzia kitu flani cha unga unga. Akafanya hivyo kwa sekunde kadhaa kisha taswira ya mama Salehe ikatokea kwenye beseni lile, akaona kila kitu kilichokuwa kinaendelea hospitali, akakuta lile swali ambalo mama Juma alimuuliza mama Salehe. Mama Ashura akashtuka sana kuona vile, akahisi uenda atapoteza nafasi ya kumteketeza Mdidi endapo atamuacha mama Salehe aendelee kuzungumza.





    “Haina haja ya kuuliza zaidi mama Juma, tayari ameshasema vita vyake ni katika ulimwengu wa giza, kuna mambo mengine hatutoweza kuyastahimili endapo yatafichuliwa Zaidi. Mama Ashura lakini unajua kuwa hakuna lishindikanalo kwa Mungu, weka tumaini lako kwake naamini hakuna kitu chochote kitakachokudhuru chini ya jua,” alisema Mdidi.

    “Naona aibu hata kumuomba huyo Mungu maana vitendo nilivyovifanya havisameheki,” alijibu mama Salehe.

    Mdidi akamtazama, kisha akamwambia subiri akatoka haraka na baada ya dakika 5 akarudi akiongozana na daktari,

    “Dokta kama unavyomuona mgonjwa amepata ahueni, hivyo sioni sababu ya kuendelea kumuweka hapa. Naomba ruhusa yake turudi nae nyumbani,” alisema Mdidi.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Daktari akamsogelea mama Salehe na kumpima mapigo ya moyo, akakuta yapo sawa, akampima presha akaona ipo sawa, hakuwa na la ziada Zaidi ya kuwaruhusu warudi nyumbani. Ikabidi wakodi bajaji ambayo itawapeleka hadi nyumbani. Safari ikaanza na baada ya kwenda umbali wa kama nusu safari bajaji ikaanza kusumbua, dereva akailazimisha hivyo hivyo hatimaye wakatokea mtaani kwao na walipokaribia kufika kabisa bajaji ikazima kila ilipowashwa haikukubali. Kwa kuwa hapakuwa mbali ikabidi mama Salehe ashuke akiongozana na mdogo wake Nasra akiwa na mama Juma, Mdidi akamlipa dereva kisha akawa anawafata kwa nyuma. Wakati wakiendelea kuikaribia kabisa nyumba yao upepo mkali mtithili ya kimbuka ukazuka na kufanya wasione vizuri wanapoelekea, watu wakaishangaa sana ile hali kwani haikuwa ya kawaida kwa mazingira ya uswahilini kama yale kutokea. Baada ya muda mfupi akatokea ng’ombe aliyekuwa na kichaa mwenye pembe kali zilizochongoka akawa anakimbia kuelekea upande wa mama Salehe. Watu wakaanza kupiga kelele za hofu kumuona mnyama yule bila kuelewa wapi alipotokea. Nasra na mama Juma walivyoona ng’ombe anakuja upande wao wakashindwa kujizuia ikabidi wamuachie mama Salehe ambaye hakuwa na nguvu za kutembea vizuri. Mama Salehe akajikuta akipiga magoti huku yule ng’ombe akiinamisha kichwa chake tayari kumvaa mama Salehe. Mdidi aliponyanyua kichwa chake akastaajabu kuona lile jambo ikabidi kwa haraka naye asogee alipo mama Salehe walau ajaribu kumsogeza pembeni lakini kabla hajafanya hivyo naye akahisi miguu kama imefungwa hakuweza kusogea mbele wala kurudi nyuma…

    Mama Salehe alipotazama nyuma akaona Mdidi akiwa katika hali kama yake wake hawezi kwenda mbele wala kurudi nyuma. Kimbunga kikawa kikali Zaidi ikabidi watu waingie ndani kukwepa vumbi lililokuwa likitimuliwa pia kuepuka hatari ya kujeruhiwa na vitu kama matawi ya miti na vinginevyo, kimbunga kile kilikuwa cha ajabu sana kwani ni mtaa wa Faru tuu ndio ulipatwa na janga hilo ila mitaa mingine ilikuwa shwari kabisa. Mama Salehe akacheka kwa nguvu sana swala ambalo lilimshtua hata Mdidi, akashangaa inakuaje katika hatari ile yeye acheke vile,



    “Mdidi wakati wako wa kufa umefika,” alisema mama Salehe.

    “Unamaanisha nini?”

    “Mipango imeenda sawa na nilivyopanga kwani haujui kwamba hata mimi mchawi?”

    “Mhmhmhm! Mama Salehe acha utani jitahidi tutoke hapa la sivyo huyo ng’ombe atakudhuru”

    “Huyo sio ng’ombe ila ni shoga yangu mama Ashura, anakuja kumaliza kazi tuliyoipanga”

    “Inamaana mama Salehe yale yote yalikuwa ni kiini macho?”

    “Hahahahahahahah! Sipendi ujinga mimi, umezidi kufatilia na kuharibu mambo yasiyokuhusu na haya ndiyo malipo yako,” alijibu mama Salehe kwa ukali huku macho yake yakibadirika na kuwa mekundu.

    Mdidi ikabidi ajikongoje kusogea pembeni lakini miguu haikuwa na nguvu na tayari yule ng’ombe alikuwa sentimita chache kutoka sehemu alipo, hakuwa na jinsi ya kufanya ikabidi afumbe macho kukabiriana na hali ile.

    “Fumbua macho yako hutakiwi kufa bila kuona nani anayekuua,”

    Ilikuwa sauti ya kike ambayo ilipenya masikioni mwa Mdidi, alipofungua akakutana uso kwa uso na mama Ashura, akashangaa sana. Mama Salehe akakumbatiana na mama Ashura kuonesha kuwa wapo pamoja kwa kila jambo.

    “Moto wa gesi hauzimwi kwa maji, tumekula kiapo cha damu unafikiri eti kirahisi vile nianze kukuomba msamaha wewe na mama Juma alafu ni kubali kufa kizembe vile, ooh! Mdidi ulishindwa kutambua Sanaa yangu,” alisema mama Salehe kwa kejeli.

    “Hamna kati yenu anayeweza nidhuru isipokuwa yule aliyeniumba na kunilinda toka nikiwa tumboni mwa mama yangu. Mnajisumbua bure na angalieni wakati umewadia chuya zitajitenga na mchele”.



    Mama Ashura akanyoosha mkono na kukatokea na kitu kama shoti vikampiga Mdidi na papo hapo akatokea Mdidi mwingine na mama Salehe mwengine ila tofauti ni kwamba hawa wa sasa wakawa na majeraha kadhaa katika miili yao na hawakuwa na fahamu. Mdidi alishangaa sana kwani mtu aliyelala pale chini alifanana na yeye kwa kila kitu.

    “Hahhahaha! Mchezo umekwisha hata upelekwe hospitali gani hawezi amka kwani lile ni gogo tuu,” mama Salehe akasema kisha kwa pamoja wakatoweka eneo lile.

    Tahayaruki ikawa kubwa sana, watu wakajazana huku wakiwa hawaamini kile walichokuwa wakikishuhudia, Mdidi na mama Salehe wakawa chini huku wote wakiwa hawajitambui damu zikawa zinawatoka mdomoni na puani,

    “Bado wanapumua tuwawaishe hospitali,” alisema mzee mmoja aliyewasogelea wawili hao.

    “Aaah! Tusubili polisi waje kufanya uchunguzi hiyo kesi eti,” alidakia mtu mwingine.

    “Acha ujinga yaani tuwaangalie tuu wakifa wakati uwezo wa kuwasaidia tunao, hao polisi watafanya uchunguzi wao baadae.

    Muafaka wa kuwapeleka hospitali ukafikiwa wakafanya utaratibu wa kukodi gari, Nasra na mama Juma hawakuamini tukio lile lilitokea walihisi kama wanaangalia sinema au wapo ndotoni maana ni tukio ambalo kiukweli liliacha maswali mengi vichwani mwa watu wengi.



    *****************************CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    Ni katikati ya msitu mmoja mzito sana, Mdidi akiongozwa na wanawake wawili makatili sana mama Salehe na shoga yake alizidi kustaajabu uwepo wa eneo lile lililojaa watu wengi waliodhoofu kiafya huku baadhi wakionekana na upungufu wa viungo katika miili yao. Alihuzunika mno na kulaani sana uovu ule ambao watu wasio na hatia wanafanyiwa.

    “Siku sio nyingi utakuwa kama hao, na kwetu ni faida kwani tutapanda vyeo na kuheshimiwa na kila mtu,” alisema mama Ashura.

    “Mungu wangu sio mjinga kuruhusu haya yatokee ni wazi amekubali mimi nipitie huku ili nipate kushuhudia uovu wenu hadharani,” alijibu Mdidi.

    “Hahahahahahahahaha! Huo ulimi unaokupa jeuri ya kuongea tutaukata usiku wa leo,” alijibu mama Salehe.

    Mdidi alimtazama sana mama salehe akakumbuka jinsi alivyohangaika kumsaidia na kumpeleka hospitali akakumbuka msamaha na yale machozi ya kinafki, nafsi yake ilikaangika sana, akajipa moyo kuwa huku kumbukumbu ya maneno ya wahenga ikizunguka kichwani mwake,

    “Siku zote Nuru haichangamani na giza, palipo na Nuru uovu ujitenga pembeni, Mdidi ni nuru ya familia hata walioko huku nao ni familia pia kwa uwezo wa Mungu watu hawa watafikiwa na Nuru na hawa mashetani wataaibika,” alisema Mdidi kwa sauti ya chini bila kusikika na yeyote.



    Watu mbalimbali walijitokeza katika hospitali ya taifa muhimbili kujua hali ya Mdidi na mama Salehe baada ya ajali ile ya kuvamiwa na ng’ombe aliyesadikika kuwa kichaa,

    “Ukweli tuzidi kumuomba Mungu bahati nzuri viungo vyao viko sawa ni majeraha madogo madogo ya nje ila kinachotupa wasiwasi ni mapigo ya nyoyo zao kuwa ya chini sana, nadhani tuvute subira kidogo tuone jinsi hali zao zitakavyokuwa”.

    Yalikuwa majibu ya daktari kwa watu wengi waliojitokeza kuwaona wagonjwa wale, Aida aliumizwa mno na matukio ya mara kwa mara yanayomkuta Mdogo wake,

    “Najua Mungu unamakusudi yako kuruhusu haya yatokee, lakini kwanini kila siku mdogo wangu ni mtu wa kutaabika! Tafadhali Mungu naomba umnusru mdogo wangu katika hili,” alisema Aida huku machozi yakimbubujika.



    ******************************



    “Mama Salehe itabidi uendelee kuishi katika dunia hii walau kwa siku chache ili kutowapa watu nafasi ya kuhisi lolote,” alisema mama Ashura.

    “Usijali Shoga yangu mie teena nitavumilia tuu kikubwa kazi yetu tumeikamilisha kwa asilimia 90, bado kidogo tutapewa tuzo ya heshima”.

    “Sasa itabidi mkae hapa na hawa wenzenu nitarejea usiku kwa ajili ya kufanya mambo mengine,”

    “Sawa shoga yangu”

    Mama Ashura akatoweka na kuwaacha Mdidi na mama Salehe katika msitu ule uliojaa vitu vingi vya ajabu na vya kutisha. Mdidi akamtazama sana mama Salehe ambaye kwa wakati huo hawakutofautiana sana, sababu wote walishapoteza nguvu katika dunia ya kawaida,

    “Ushawahi kufikiria nini kitatokea katika maisha yako endapo shoga unayemuamini akaamua kukusaliti?” akauliza Mdidi.

    “Mfyuuu! Baada ya kuwaza maisha yako unawaza ya wenzako, huhuhuhu! Mdidi huna pa kutokea safari hii,” alijibu mama Salehe.

    “Je wewe unatofauti gani na binadamu hawa wanaoteseka hapa?, wote ni kama wewe wamepoteza maisha katika ulimwengu wa kawaida watu wengi wanadhani kuwa wameshafariki ila wapo huku wakiteseka. Je hali hiyo ni tofauti na yako wewe uliyekuwa mahututi katika ulimwengu wa kawaida kumbe upo huku ukiwa uelewi hatima yako,” alisema Mdidi.

    “Huo ulimi unaokupa jeuri dawa yake inachemka, Mdidi huwa sipendi falsafa zako za kijinga umechangia kukwama kwa mambo yetu mengi na leo mkuu atakapo kuona atafurahi sana”.

    “Hamna aliye mkuu Zaidi ya Mungu aliyeumba dunia na vyote vilivyomo, tumaini langu lipo kwake hivyo sina hofu mtaweza kuudhuru huu mwili wa nyama lakini hamuwezi kuifanya lolote roho yangu”

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Waliendelea kuongea kwa muda mrefu huku Mdidi akikosoa kila ambacho mama Salehe anakiongea. Hofu ikaanza kumjaa akawaza itakuaje kama mama ashura ataamua kumsaliti. Atawezaje kuishi katika ulimwengu ule wa mateso, hakajikuta akiishiwa nguvu na kukaa chini huku akijikunyata.

    Muda ukazidi kwenda hatimaye giza likaanza kuwa kali Zaidi, ile hali ya kuwa usiku ikatawala akili za Mdidi na mama Salehe. Kila mmoja akawa kimya akiwaza lake ghafla kukasikika kishindo kikubwa kikija upande waliopo, wakashangaa kuona wale watu waliodhoofu wakianza kulia na kusogea nyuma kukimbia kile kishindo, Mdidi akajaribu kuuliza kulikoni lakini hakuweza kupata majibu kwani binadamu wale walipoteza uwezo wa kuongea siku nyingi zilizopita pindi tu walipofikishwa katika dunia ile.

    Kishindo kilizidi kuwa kikubwa kuwakaribia hatimaye moshi mkubwa ukazuka watu wote wakatulia kama wamegandishwa papo hapo likatokea joka kubwa lenye ulefu na unene ambao si rahisi kuukadilia, joka lile likajisogeza katikati ya watu na kutanua kinywa chake kisha akawaviliga watu watatu kwa mkupuo na kuwameza kisha likajitikisa na kutoweka. Hakika lilikuwa tukio la kutisha ambalo mama Salehe hakuwahi kukutana nalo katika maisha yake,

    “Hii inamaana kama mama Ashura hatokuja huku na mimi ipo siku nitamezwa kama wale,” alisema mama Salehe huku akitetemeka kwa hofu.



    Mdidi akamtazama bila kusema lolote, akasimama na kuangalia pande zote za msitu ule hali ilikuwa shwari kabisa na haikuwa rahisi kugundua ni njia ipi ya kutokea. Wakiwa katika hali ile ya sintofahamu mama Salehe akiwa na watu wengine watano wakatokea.

    “Pole na hongera kwa kuvumilia shoga yangu,” alisema mama Ashura.

    “Asante shoga japo hayazoeleki”

    “Umekuwa huku kwa siku 5 sasa”

    “Nini! Siku 5!” kwa mshangao mkuu.

    “Ndiyo shoga yangu, yule joka huja kila baada ya siku 7 na nilivyowaleta ilikuwa siku mbili baada ya yeye kuja, ila usijali wakati umefika wa kurudi katika maisha yako ya kawaida”

    Mama Salehe alifurahi sana kusikia hivyo akaanza kucheka kwa kebehi huku akimtazama Mdidi ambaye tayari alianza kudhoofu ingawaje aliona ni siku moja tuu.

    Wale watu waliokuja na mama Salehe wakamfunga Mdidi kitambaa cheupe asione lolote litakaloendelea, kufumba na kufumbua wakajikuta wapo katikati ya kundi la watu huku ngoma za shangwe zikiendelea,

    “Tulimsaka toka akiwa tumboni mwa mama yake, ametusumbua sana lakini leo tumempata ni furaha sana kwetu,” alisema mzee mmoja kwa sauti kubwa iliyojaa mtetemo na watu wote wakashangilia.

    “Anastahili kuadhibiwa vikali mno,” aliongea mama Salehe.

    “Hahahahahahaha! Huyu hapaswi kupewa adhabu yeyote, kwanza ananyota kali inayokubarika na kila mtu kama tutamtumia katika kazi zetu ni wazi atasaidia kuleta waumini wengi upande wetu,” alisema yule mzee.

    “Tutawezaje kumtumia katika hali hii?” aliuliza mama Ashura.

    “Tunapaswa kumfanya awe mkuu, aishi na kunena kama sisi,” alijibu mzee yule.

    “Yatawezekanaje hayo?”

    “Tunahitaji kafara la damu ya mwanadamu mwenye mahusiano ya karibu naye kuyakamilisha hayo, akili zake zitabadirika tutauchota ufahamu wake na atafanya kama tutakavyo sisi”

    Ilikuwa habari njema sana kwa watu wa ulimwengu ule wa giza ingawa halikuwa swala la kufurahisha kwa mama Salehe kwani alitegemea itakuwa nafasi ya kumfanyia ukatili Mdidi ila ndiyo kwanza imekuwa nafasi yay eye kupata cheo.

    “Ni bora mniue kuliko kutumikia kazi zenu,” alisema Mdidi.

    Watu walicheka tuu hakuna aliyeinua kinywa chake kumjibu sababu walijua ni hali ya mfa maji siku zote haachi kutapatapa.



    Hali ya Mdidi katika hospitali ya muhimbili haikuwa ya kuridhisha kwani kadri siku zilivyokuwa zikienda hakukuwa na dalili yeyote ya yeye kupona. Aida kwa namna ya pekee alipeleka jina lake kwa kiongozi wa kanisa ambaye ni padre walau apite kwa ajili ya kumpa sakramenti ya mpako wa wagonjwa.



    Mpako wa wagonjwa ni ibada maalumu kwa ajili ya wagonjwa inayotumiwa na Wakristo wa madhehebu mbalimbali kufuatana na desturi ya Mitume wa Yesu na agizo la Barua ya Yakobo. Kwa Kanisa Katoliki, Waorthodoksi na madhehebu mengine machache ni sakramenti iliyowekwa na Yesu Kristo, ingawa Injili haisemi. Pamoja na Kitubio ni kati ya sakramenti mbili za uponyaji, zinazolenga kumrudishia Mkristo afya ya roho na mwili, iliyoathiriwa na dhambi na ugonjwa. Kadiri ya imani hiyo, Mpako wa Wagonjwa ulianzishwa na Yesu, kama sakramenti zote. Mafuta ya wagonjwa yanamaanisha lengo la kuwaponya na kuwarudishia nguvu na uzuri. Kama kawaida, maneno yanaweka wazi zaidi kuwa lengo si kuponya mwili tu, Bali hasa roho kwa kuitia msamaha na faraja katika mateso ambayo huenda yakaendelea. Kwa kuwa Mungu haponyi mwili kila mara, isipokuwa kwa faida na wokovu wa mgonjwa na wa wengine.

    Padri ambaye alipewa dhamana ya kutoa huduma iyo kwa Mdidi akakubali na kuahidi kwenda siku inayofata asubuhi wakati akipita na kwa wagonjwa wenye uhitaji sawa na Mdidi,

    “Usijali dada huruma ya Mungu ni kubwa kuliko unavyoifikiria, tuzidi kudumu katika sala naamini Mungu atalegeza vifungo alivyofungwa Mdidi na atapona kwa sifa na utukufu wa jina lake,” alisema padre baada ya kupokea jina na kulihifadhi katika faili lake.



    Kwa mara ya kwanza toka apoteze fahamu mama Salehe anafumbua macho yake na kujikuta yupo katika chumba cha ugonjwa mahututi. Anaangaza huku na huko lakini haoni mtu Zaidi ya mipira aliyofungiwa ili imsaidie katika kupumua. Akanyanyuka na kukaa kitako, muuguzi aliyekuwa zamu siku hiyo alistaajabu mno kwani si kawaida kwa mtu aliye mahututi kupona moja kwa moja na kuwa na nguvu kama alizokuwa nazo mama Salehe.

    “Usinyanyuke tafadhari utajiumiza,” alisema muuguzi.

    “Mboni mmenileta hapa wakati mimi ni mzima wa afya,” aliuliza mama Salehe.

    “Dada yangu wiki moja iliyopita uliletwa hapa ukiwa na hali mbaya sana, hatukutegemea utapona haraka kiasi hiki ila ashukuriwe Mungu, ngoja nimuite daktari”

    Muuguzi akatoka na baada ya dakika kadhaa akarudi na daktari, akafanyiwa vipimo upya na hakuonekana na tatizo lolote alionekana yu mzima wa afya. Daktari hakuwa na la ziada Zaidi ya kumruhusu,CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Unaruhusiwa kurudi nyumbani sasa, ila nasikitika kukwambia yule mwenzako hali yake bado sio nzuri kwani hajarudisha fahamu na mapigo yake yapo chini sana, tuombe Mungu aliyekuponya wewe na ampe ahueni yeye pia,” alisema daktari.

    Mama Salehe akajikuta akiangua kicheko mbele ya daktari, alicheka mno hadi daktari akapata wasiwasi na kuhisi labda akili zake hazipo sawa.

    “Usijali daktari atapona tu,” alisema mama Salehe.

    Nasra akafurahi sana kuona dada yake amerejea katika hali ya kawaida ikabidi achukue nguo na kuanza safari ya kurudi nyumbani,

    “Dada kabla hatujaondoka tukamuone Mdidi, kwani matatizo aliyoyapata ilikuwa kwa lengo la kukusaidia wewe”

    “Maskini Mdidi Mungu amponye jamani namuhurumia sana, sawa twende tukamjulie hali”



    Wakaongozana moja kwa moja hadi jingo la pili ambapo Mdidi amelazwa, kutokana na hali aliyokuwa nayo hakuruhusiwa mtu yeyote kuingia kumtazama Zaidi ya dada yake Aida. Wakafika na kumkuta Aida amekaa kwenye benchi huku akiwa na watu wengi wa mtaani waliokuja kumtazama.

    “Ina maana bado Mdidi ana watu wengi kiasi hiki, sasa si bora tuu afe. Dunia hii anakubarika hivi kule napo wanataka kumfanya awe kiongozi sasa si atatawala huku mpaka kule, huu ujinga sasa,” alisema mama Salehe kimoyo moyo.

    “Ooh! Ashukuriwe Mungu mama Salehe hatimaye umepona, ila mdogo wangu bado hali yake si nzuri,” alisema Aida baada ya kumuona mama Salehe.



    “Isingekuwa mimi Mdidi asingalikuwa katika hali aliyo nayo sasa, ni bora ningeendelea kuumwa mimi Mdidi apone, amenisaidia sana,” alisema mama Salehe huku akilia kinafiki.

    Aida alimfariji mama Salehe na kumwambia kuwa ni kazi ya Mungu ivyo haniana haja ya wao kulalamika sana maana kila kitu hutokea kwa sababu. Mama Salehe akaaga na kurejea nyumbani kwa ajili ya mapumziko na mipango mingine.



    *********************



    Jioni ya siku hiyo padre akaenda kumtazama Mdidi hospitali, Aida alishangaa kidogo maana aliahidi kuja asubuhi ya siku inayofuata.

    “Usishangae! Nimekuja kumpa huduma Mdidi maana nafsi yangu imekosa Amani kila ninapolifikiria jina la kijana huyu na hali aliyokuwa nayo,” alisema padre.

    “Nashukuru sana Father, karibu njia ni hii,” alisema Aida huku akimuelekeza padre njia ya kupita.

    Kwa kuwa haikuruhusiwa kuingia mtu Zaidi ya mmoja katika chumba alicholazwa Mdidi ikabidi wapate ruhusa kutoka kwa daktari ambaye ana jukumu la kuhakikisha wagonjwa wanakuwa salama, wakaruhusiwa na kuingia moja kwa moja hadi katika kitanda alicholazwa Mdidi.

    “Uandae moyo wako kwa ajili ya ibada fupi ya kumuombea ndugu yetu Mdidi, ambaye amedhoofishwa na magonjwa ya ulimwengu huu, tuombe huruma ya Mungu ili anyooshe mkono wake wa uponyaji na kusawazisha sehemu zote zinazomgandamiza kijana huyu,” alisema padre.

    Aida akaunganana padre katika ibada hiyo, wakasali kwa kirefu kidogo kisha padre akachukua mafuta matakatifu na kumpaka Mdidi.

    “Sasa tusubili majibu kutoka kwa Mungu na kumbuka kuwa Mungu wetu siku zote hakawii wala hawai ila anatoa majibu katika wakati unaofaa, usiteteleke katika Imani yako tuendelee kumtumainia yeye siku zote,” alisema Padre na kuanza safari ya kwenda kuwatazama wagonjwa wengine wenye uhitaji wa huduma hiyo.



    **********************



    Hayawi hayawi sasa yamekuwa wanachama wote wa ulimwengu wa giza wakakusanyika ili kufikia azimio la kubadilisha ufahamu wa Mdidi na kumtumia katika mambo yao ya kishetani. Safari hii watu kutoka sehemu mbali mbali za nchi walifika utaratibu wa awali wa kutoa taarifa juu ya majukumu waliyopeana ukafanyika, waliofanikisha wakapongezwa na walioshindwa walishushiwa rungu la adhabu kali. Baada ya tukio hilo kupita mkuu wao akasogea mbele na kupaza sauti yake yenye mitetemo na ya kuogofya,

    “Leo ni siku ambayo tuliisubiri kwa hamu sana, hatuna cha kupoteza tutamvuta dada yake Mdidi awe kafara la kuubadili ufahamu wa mdogo wake na hatimaye aweze kuifanya kazi ya kupotosha watu kwa ufasaha”.

    Watu wote wakashangilia kwa makofi na vicheko vya ajabu, kisha kila mmoja akatulia na kupiga magoti. Mdidi akasogezwa mbele yao kila mmoja akainua kichwa kumtazama.

    “Ni wakati wa kumvuta dada yake” alisema mkuu wao.

    Kukatengenezwa kitu mithiri ya kaburi kisha kiongozi wao akawataka wote watazame pale akasogea kabisa na kuchukua kibuyu na usinga akaanza kupunga huku akiita jina la Aida,

    “Aida…! Aida…! Aida…!”

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Upepo mkali ukazuka ardhi ikatetema kufumba na kufumbua Aida akatokea mbele yao, watu wote wakashangilia sana. Baada ya shangwe za muda mfupi wakatulia kisha yule mkuu wao akatoa kitu chenye ncha kali na kutaka kumchoma Aida shingoni lakini alipojaribu kumkaribia kukatokea na radi iliyompiga na kumrusha pembeni.



    Wote wakaingiwa na uoga, walipomtazama Mdidi wakakuta anang’ara mithili ya mwezi mpevu, mama Ashura ikabidi apige atua fupi fupi kumsogelea Mdidi lakini kadri alivyozidi kumsogelea ndivyo mg’aro ukazidi kuwa mkubwa akaogopa na kurudi nyuma,

    “Huyu ni mchawi kuliko sisi,” alisema mama Salehe.

    “Leteni damu ya msichana bikra,” alisema kiongozi wao.

    Kwa haraka sana damu ikaleta na wakaanza kuinyunyiza alipo Mdidi, ghafla mlipuko mkubwa ukatokea watu wakawa kama wameshikwa na bumbuazi wasijue la kufanya, Aida akatoweka na Mdidi akabaki katika hali ile ya kung’ara. Mama Salehe na mama Ashura wakaanza kucheka hovyo, huku watu wengine wakiugulia maumivu yaliyosababishwa na mlipuko ule. Wakuu wote wakaungana kupambana na hile hali lakini hawakufanikiwa lolote kwani hata Mdidi naye akatoweka.

    ***********************

    Ni asubuhi nyingine tena katika wodi ya wagonjwa mahututi Mdidi anarejewa na fahamu, Nesi anapoona ile hali anafurahi sana na kutoka nje ambapo alimpa habari njema Aida ambaye alikuwa hapo siku zote kumtunza mdogo wake. Habari ile inakuwa ya furaha sana hasa baada ya daktari kuthibitisha kuwa Mdidi yu mzima na ataruhusiwa kurudi nyumbani siku hiyo.

    “Mhmhm! Ni ajabu sana jinsi watu hawa wanavyopona maana wanafanana kila kitu na yule mama tuliyemruhusu jana,” alisema daktari.

    “Kweli ni jambo la kushangaza ila tumshukuru Mungu kwa hili maana nilimuhurumia sana dada yake ambaye kila siku yupo hapa hata kulala vizuri hajalala.

    Baada ya Muda mfupi Mdidi akaruhusiwa na safari hii dada yake hakutaka warudi kwenye nyumba ya mzee Kobelo,

    “Hapana dada turudi tuu pale pale,” alisema Mdidi.

    “Mdogo nyumba ile ina vita sana, naogopa usije patwa na tatizo lingine”

    “Mungu wetu ni mkuu tutashinda dada, shaka ondoa”

    Ikabidi wakodi Tax ambayo iliwapeleka moja kwa moja hadi nyumbani kwa mzee Kobelo, wakati wakiwa wameshaingia mtaani wakashangaa kukuta umati wa watu umejazana karibu na nyumba yao, ikabidi Aida ashuke akaangalie nini kinachoendelea. Alipofika hakuamini kile alichokishuhudia akakuta mama Salehe akiwa kama amechanganyikiwa, watu walionekana kuwa na jazba nyingi na tayari baazi walianza kumshambulia kwa mawe.

    “Msinitisheeee! Mimi ni mchawi! Mtaa huu hakuna Zaidi yangu labda mama Ashura peke yake, huhuhuhu! Atupendi Ujinga, nilimuua Upendo, mama Ashura akawaua wale vijana 10 na kuwatoa kafala hukoo kwenye ulimwengu wetu,” alilopoka mama Salehe akiwa hajielewi.

    “Piga huyoooo! Mwanga mkubwa sie tunalia misiba ya ndugu zetu wao kumbe wamewala nyama pumbavuuuu,” alisema baba mmoja wa makamo kwa jazba sana.

    “Inaoenakana wameenda kuwanga sehemu mbaya ndio maana wameumbuka, kamleteni na huyo shoga yake tumuadhibu,” alisema mama mmoja.

    Vijana watatu wakaenda hadi kwa mama Ashura lakini wakamkuta akiwa na hali mbaya sana, asiweze kuongea wala kujisogeza. Hali ile iliwatisha sana wale vijana ikabidi warudi kutoa taarifa juu ya lile, watu wengi wakaenda kuona kile kilichomkuta mama Ashura, wengi walikuwa na jazba lakini pindi macho yao yalipotua kwake kila mmoja akajikuta akimuhurumia.

    Aida alipoyaona yale yote ikabidi arudi kwa haraka na kumtaarifu Mdidi kile kilichotokea. Ikabidi wamruhusu dereva aondoke kisha taratibu wakajisogeza maeneo hayo hili kujua nini kinaendelea,

    “Hahahahahaha! Shoga yangu pole tulitaka kumuangamiza Mdidi ona Mungu alivyokuadhibu,” alisema mama Salehe huku akiwa bado amechanganyikiwa.

    Watu walipomuona Mdidi maeneo yale walifurahi sana wengi walimpa pole kwa yaliyomkuta kwani mama Salehe aliongea yote.

    “Mdidi unamoyo wa kipekee sana ingekuwa mtu mwingine sidhani kama angevumilia kwa haya yote uliyofanyiwa,” Alisema mzee Kobelo baada ya kusikia na kushuhudia yote toka kwa mama Salehe na mama Ashura.

    “Binafsi nimefurahi kwa kuwa wengi mlikuwa kwenye giza la ujinga na mliamini kile mlichokisikia, lakini leo mtu yule ambaye ilisadikika kuwa na hatiya juu ya maafa yaliyoukuta mtaa huu amesafishika wengi wenu mmeamini sasa mzee Kilonda au mama Juma hawakuwa watu wabaya isipokuwa hawa wawili,” alisema Mdidi.

    “Daah! Kweli asee tumechuma dhambi za bure,” alisema Yahaya ambaye hakutaka kupitwa na tukio hilo.

    “Mimi sina kinyongo nao nimewasamehe hivyo kwa pamoja tusaidiane kuwapeleka kituo cha afya kwa matibabu aidha tuzidi kumuomba Mungu awapunguzie mateso haya hatimaye waweze kurudi katika hali ya kawaida”.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    BAADA YA MWEZI MMOJA



    “Bwana Mdidi! Tumeusoma utafiti wako ulioufanya katika kata ya Mnyamani lakini sasa tunataka tusikie wote kwa pamoja kama bodi ya utendaji hili tuweze kujua namna gani ya kuinua elimu na kujenga maadili mema katika eneo hilo,” alisema Mkurugenzi wa wizara ya elimu.

    “achilia mbali sababu za kiuchumi kama wazazi kuwa na kipato kidogo au upungufu wa vifaa vya kusomea na kufundishia, pia zile sababu za kijamii kama makundi mabaya ambayo utakuta vijana wengi wanajishughulisha na uvutaji wa bangi pia uchezaji wa Kamari aidha ile miziki yenye dhima mbovu ambayo imewakaa sana vijana na watoto akilini kiasi cha kutowapa nafasi nzuri ya kusoma. Sababu ya nguvu za giza ni kubwa pia watoto wengi wamekuwa wakichezewa na kupunguziwa uwezo na hamu ya kusoma kwa kupuliziwa roho chafu kama ilivyo kazi ya mama Ashura,” alisema Mdidi.

    “Sasa unafikiri sisi tufanyaje?”

    “Ukiangalia sehemu ya 5 ya utafiti huo, utakuta kuna mapendekezo ambayo nimeyaandika ambayo jamii kwa pamoja inapaswa kuyafanya, kama kujenga hofu ya Mungu na kumwamini yeye pekee, aidha wazazi wanatakiwa wawalee watoto katika maadili mazuri, pia serikali isambaze vifaa vya kusomea na kujenga madarasa mengi hili watoto wasome kwa kujinafasi Sababu hatupendi ujinga uendelee kutawala katika akili za watu”.



    MWISHO



0 comments:

Post a Comment

Blog