Simulizi : Viganja Mashavuni Mwangu
Sehemu Ya Pili (2)
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Bila Naseku kuingilia kati basi hali ya Cassian ingekuwa mbaya mahali hapo. Oscar alionekana kukasirika, ilikuwa ni afadhali kucheza na maisha yake lakini si kucheza na dada yake huyo aliyeonekana kuwa kila kitu.
Watu waliokuwa pembeni baada ya kuona Naseku amemzuia mwanaume huyo nao ndiyo wakaingilia na kumzuia. Oscar alikuwa akiongea peke yake huku akiwataka watu hao wamuachie ili amuonyeshee mwanaume huyo kwamba alikuwa mtu hatari aliyekuwa akiheshima katika mtaa huo.
Muda wote huyo Cassian hakuongea kitu, alibaki akiashangaa tu, mambo aliyokuwa akiyafanya mwanaume huyo yalimshangaza lakini akazuia hasira zake kwani kama angeamua kumpoteza kijana huyo, ilikuwa ni kuongea mara moja tu na wasingemuona tena katika dunia hii.
“Mbona mnanishika! Mbona mnagombelezea bhana?” aliuliza Oscar huku akiwa ameshikwa huku na kule.
“Tulia kwanza! Utaua!”
“Mimi nataka niue sasa! Hawa mbung’o ni kuwaua tu! Kwenda kwao kuwapigia misele dada zao hawataki! Jamani si mniache! Mbona mnanishika kama mtoto wenu,” alisema Oscar huku akionekana kuwa na hasira sana.
Naseku ndiye aliyemtuliza zaidi kaka yake na kumwambia kwamba mwanaume huyo hakuwa mtu mbaya, alikuwa mtu mzuri ambaye alifika mahali hapo si kwa lengo la kumtongoza kama walivyokuwa wanaume wengine bali alikuwa hapo kwa ajili ya kumsaidia mama yao.
Kidogo hilo likamfanya Oscar kutulia. Mama yao alikuwa mgonjwa ndani, alikuwa akisumbuliwa na mgonjwa wa miguu kuvimba, alikuwa kitandani mwaka wa pili, kipindi cha nyuma walikuwa wamesumbuka kumpeleka hospitalini lakini kikafika kipindi wakatulia kwani hawakuwa na msaada wowote wa kifedha.
Kidogo Naseku ndiye aliyeonekana kuwa msaada, yeye ndiye aliyekuwa akitafuta pesa kwa ajili ya kumsaidia mama yake na hata kununua chakula cha humo ndani.
Oscar hakuwa akijali, alichokuwa akikiangalia kilikuwa ni ulevi tu. Alikuwa mvuta bhangi na mtafunaji mirungi maarufu hapo Tandale. Maisha yake yaliishia hapo, alijua kabisa kwamba mwisho wa kila kitu ilikuwa ni lazima kufa.
“Kwa hiyo yupo hapa kumsaidia bi mkubwa?” aliuliza Oscar.
“Ndiyo! Wewe kila mtu unayemuona unadhani kaja kunifuata mimi!” alisema Naseku huku akimwachia kaka yake aliyeonekana kunywea.
Hiyo ndiyo ikawa salama ya Cassian. Mpaka kufikia kipindi hicho hakukuwa na mtu aliyegundua kwamba alikuwa yeye. Pale alipokuwa kulikuwa na giza, alizibwa uso na giza lililokuwepo mahali hapo kwani hata Cassian mwenyewe hakumuona vizuri usoni.
Akachukuliwa na kuingizwa ndani, alishangaa kwamba ni kwa namna gani watu walikuwa wakiweza kuishi katika nyumba mbovu kama hiyo. Alibaki akishangaa kila kitu, kulikuwa na harufu mbaya humo ndani, hakukuwa na sakafu ya simenti, kulikuwa na ndoo za maji zilizotobokatoboka.
Hakutaka kujali sana, akapelekwa mpaka katika chumba alichokuwa amelala mama yake Naseku, alikuwa juu ya kitanda huku akiwa amewekewa chandarua kilichokuwa kimetonokatoboka na sehemu nyingine kilikuwa kimeshonwa.
Alichokiona, akashindwa kuvumilia, machozi ya uchungu yakaanza kutiririka mashavuni mwake. Aliumia mno moyoni mwake, mwanamke yule aliyekuwa kitandani alikuwa akiteseka, pale alipokuwa, hakukuwa na kitu kingine alichokuwa akikisubiria zaidi ya kifo tu.
“Tatizo nini?” aliuliza Cassian ambapo Naseku akaanza kusimulia kila kitu huku machozi ya uchungu yakianza kumtoka.
Ilikuwa ni stori mbaya iliyouchoma mno moyo wake. Hakuamini kama kungekuwa na mwanamke ambaye alikuwa amepitia maisha ya kumuumiza kama alivyokuwa amepitia mama yake Naseku.
Mwaka wa pili mfululizo mwanamke huyo alikuwa akiteseka, hakuwa akisimama, wala kutembea, maisha yake yalikuwa kitandani hapo kitu kilichoonekana kumtesa kila siku.
Walimpeleka hospitali lakini baada ya kuambiwa kwamba matatizo yake yangetibiwa kwa shilingi milioni kumi, wakakata tamaa na mwisho wa siku kumuweka ndani wakisubiri siku ifike na kufariki dunia.
Huruma nyingi ikamuingia Cassian kana kwamba aliyekuwa kitandani akiugua alikuwa mama yake wa kumzaa. Hakutaka kuona mwanamke huyo akiendelea kuteseka, kwa kuwa alikuwa akimpenda binti yake kwa moyo wa dhati hakuwa na jinsi kumsaidia mwanamke huyo kwa kuamini kwamba ingekuwa rahisi kwa Naseku kuamini kwamba alikuwa akimpenda.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Nitamsaidia mama,” alisema Cassian maneno yaliyomfanya hata Oscar kushtuka.
Hayo ndiyo yalikuwa maneno yake, hakutaka kusubiri, hapohapo akachukua simu yake na kumpigia kijana wake ambaye alimtaka kufika hapo mara moja kwa kumpa maelekezo kupitia Oscar. Ni ndani ya dakika kadhaa, kijana huyo akafika nyumbani hapo akiwa na gari ambapo moja kwa moja wakamchukua na kuondoka naye.
Huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa maisha yake na msichana Naseku, aliahidi kumsaidia mwanamke huyo, akapelekwa hospitalini ambapo huko matibabu yakaanza kufanyika.
Mwanamke huyo hakuamini kama Cassian alikuwa akimsaidia kwa kiasi hicho, moyo wake ulifurahia na alitamani kusikia mambo mengi kuhusu mtu aliyekuwa akimsaidia.
Kwa kuwa Cassian alitaka kumuonyeshea Naseku kwamba alikuwa akimpenda kwa moyo wa dhati, akawataka kwenda kuishi kwenye jumba lake jingine lililokuwa Mbezi Beach na ile nyumba yao iliyokuwa Tandale kuvunjwa na kuanza kujengwa upya.
Kila mmoja alishangaa, waliijua familia hiyo, ilikuwa miongoni mwa familia choka na masikini iliyokuwa Tandale, sasa iweje nyumba yao ivunjwe na kujengwa upya na wakati hawakuwa na uwezo wowote ule, wengi wakahisi kwamba ilikuwa imeuzwa.
“Mh! Jamani! Hata Oscar haonekani! Hii nyumba waliiuza au?’ aliuliza mwanamke mmoja huku akiangalia mafundi waliokuwa wakiifanya kazi kwa nguvu kubwa, usiku na mchana walikuwa wakihangaika nayo kuhakikisha ndani ya mwezi mmoja kila kitu kiwe kimekamilika.
“Hata mimi mwenyewe nashangaa! Ila tutajua yote hayo,” alisema mwanamke mwingine, hao wawili walikuwa nje wakisukana, kazi yao ilikuwa ni kuongea umbeya, kuwaangalia wakina nani wamepita na nani siku nzima ili wawaseme.
Wakati hayo yote yakiendelea Cassian hakuwa amemwambia Naseku jambo lolote lile, aliamua kunyamaza kwanza, alitaka kuona kwanza akimfanyia mambo mengi mwanamke huyo kama ishara ya kumuonyeshea kuwa alikuwa akimuhitaji kupita kawaida.
Siku zikaendelea kukatika, kule alipokuwa amewaweka, aliwaita wafanyakazi, Oscar na Naseku wakapelekwa katika shule ya kujifunza kuendesha gari na kuwanunulia magari.
Maisha yalibadilika haraka sana, hawakuwa wakiamini walichokuwa wakikipitia, wakati mwingine walihisi kama ni ndoto ambapo baada ya muda fulani wangeamka na kujikuta wakiwa kitandani.
Maisha yalikuwa ya raha, hakukuwa na kulia tena, hakukuwa na machozi tena na baada ya miezi miwili, mama Naseku akapona ugonjwa wa miguu na nyumba ile waliyokuwa wakitengenezewa ikamalizika kabisa.
“Naseku!” aliita Cassian baada ya kipindi kirefu kupita, siku hiyo alitaka kumkumbushia msichana huyo juu ya kile alichokuwa amemwambia nyuma.
“Abee!”
“Umependeza sana! Hakika ninauona uzuri wako kwa sasa. Siwezi kujuta kukuchagua wewe,” alisema Cassian huku akitoa tabasamu pana.
“Nashukuru sana!”
“Kuna kitu nahitaji kukwambia!”
“Kitu gani?”
“Kilekile cha siku zote kwamba ninakuhitaji sana! Ninahitaji nikuoe! Nimekaa na kukufanyia haya yote, ulistahili, ulitakiwa kuwa na maisha ya furaha, ufute machozi yako, uondoe maumivu makali moyoni mwako,” alisema Cassian.
Siku hiyo hakutumia nguvu sana, ilikuwa ni kama kumsukuma mlevi katika mteremko wa mlima. Msichana huyo akakubali kuwa mpenzi wake na hatimaye baada ya mwezi mmoja wakafunga ndoa na kuwa mume na mke.
Ilikuwa ni furaha kubwa kwa kila mmoja, Naseku yule, msichana masikini hatimaye maisha yake yalikuwa yamebadilika na kuwa bilionea mkubwa. Kwa Cassian hicho ndicho kitu alichokuwa akikihitaji, moyo wake ulikuwa na furaha tele, alitaka kuoa na kupata mtoto na mabya zaidi kipindi hicho hakuwa akijua chochote kile kuhusu Evelyne aliyekuwa amemuacha kwa maumivu makali.
“Mume wangu! Sijaziona siku zangu,” alisema Naseku huku akimwangalia Cassian.
“Unasemaje?”
“Sijaziona siku zangu!”
“Hebu rudia tena kwanza! Unasemaje?” aliuliza Cassian huku akionekana kutokuamini.
Wiki mbili tu zilitosha kuonyesha kwamba Naseku alikuwa mjauzito. Cassian hakuamini, kila wakati alikuwa akimwangalia mke wake, hakuamini kama kweli hatimaye alikuwa akienda kuitwa baba.
Alikuwa makini, alihitaji kumpenda mke wake kwa mapenzi ya dhati, alihitaji kumpa kila kitu alichokuwa akikiihitaji. Baada ya miezi minne wakaenda kupima ili kuona jinsi ya mtoto aliyekuwa naye Naseku tumboni.
“Hongereni sana! Mkeo ana mimba ya watoto mapacha,” alisema daktari huku akimwangalia Cassian.
“Unasemaje? Mapacha? Wa kiume wa kike?” aliuliza Cassian huku akionekana kutokuamini.
“Wa kiume.”
“Nashukuru sana!”
Hiyo ndiyo ilikuwa furaha yake, hakuacha kwenda kliniki na mkewe, mara kwa mara walikuwa wakienda huku wakati mwingine wakitumia utra-sound kuangalia jinsi watoto walivyokuwa tumboni mwa mke wake.
Siku ziliendelea, wakati Naseku akiwa amefikisha miezi saba ya ujauzito wake ndiyo hali ya tofauti ikaanza kuonekana kwa mapacha hao. Siku hiyo walikwenda kupima kama kawaida, kuwaangalia watoto waliokuwa tumboni kuona walikuwa wakiendeleaje. Baada ya kuwapiga picha, dokta alionekana kuwa tofauti na siku nyingine na hata ile karatasi ngumu ambayo ingeonyesha jinsi watoto walivyokuwa tumboni hakutaka kuwaonyeshea.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Kuna nini?” aliuliza Cassian.
“Mmh!” aliguna tu daktari.
“Hebu tumabie kuna nini! Hebu nione hiyo karatasi,” alisema Cassian huku akijaribu kuichukua karatasi hiyo ngumu kutoka mkononi mwa daktari.
“Subiri kwanza!”
Cassian hakutaka kukubali, hapohapo akampokonya daktari karatasi ile ngumu na kuanza kuiangalia. Macho yake yalipotua kwenye karatasi ile hakuamini alichokiona, ghafla tu machozi yakaanza kumtoka, akapiga magoti chini na kuanza kulia kama mtoto.
“Mume wangu kuna nini?” aliuliza Naseku huku akimwangalia mume wake, naye mwenyewe alitaka kuiona karatasi hiyo, cha kushangaza mumewe akamzuia, hakutaka kuiona.
“Hapana! Hebu niambie kuna nini! Watoto wamekufa au? Lakini mbona nawasikia wakichezacheza! Niambie kuna nini,” alisema Naseku huku akihitaji kuiangalia karatasi hiyo ambayo Cassian hakutaka kabisa kumuonyeshea kwa kuamini kwamba angeumia sana kitu ambacho hakutaka kuona kikitokea.
Naseku hakutaka kuelewa kitu, aliamini kabisa kulikuwa na tatizo kwa watoto wake na hivyo kutaka kuangalia kile kilichokuwa kimepigwa tumboni mwake, hali ya watoto wake kwani alichohisi ni kwamba walikuwa wamefariki dunia.
Bado Cassian alikataa, msimamo wake ulikuwa uleule, alijua kwamba kama mke wake angekiona kile kilichokuwa kimetokea kwa mapacha wake basi angeumia kupita kawaida.
Naseku hakukubali, bado alihitaji kuona tena huku akilia kabisa kitu kilichomfanya Cassian kumpa karatasi ile ngumu na kuangalia kilichokuwa kikiendelea.
Hakuamini, watoto wake mapacha waliokuwa tumboni mwake walikuwa na kila dalili za kuungana. Moyo wake ulimuuma mno, hakuamini alichokuwa akikiangalia lakini wakati mwingine alihisi kwamba hata kama wangeungana, bado wangeweza kuwatenganisha kwa kuwa tu walikuwa na pesa.
Hiyo ndiyo hali iliyokuwa imetokea, kila mmoja alihuzunika mno, mioyo yao iliuma, ilichoma kupita kawaida. Wakakumbatiana na kumshukuru Mungu kwa kuamini kwamba kila kitu kilichokuwa kikitokea, Mungu alikipanga na kamwe hakukuwa na mtu wa kufanya vinginevyo.
Mara kwa mara walikuwa wakifika hospitalini hapo kwa ajili ya kuangalia watoto wao ambao bado hawakuwa wamezaliwa, Cassian alikuwa na muda mwingi wa kuangalia picha za mapacha walioungana kama watoto wake ambao hawakuzaliwa, alitaka kuangalia maisha yao, waliishi vipi na hata mavazi yao yalikuwaje.
Hapo ndipo akaamua kuwafuatilia mapacha wa aina hiyo, Abby na Brittany Hansel waliokuwa wakiishi nchini Marekani. Kila alipoziangalia picha za mapacha hao moyo wake ulimuuma, hakuamini kama kweli Mungu aliamua kumpa watoto wa namna hiyo na wakati alikuwa amemuomba kwa kipindi kirefu mno.
“Mungu! Kama Abby na Brittany wanaishi, nina uhakika hata watoto wangu wataishi pia,” alijisemea Cassian huku akiangalia picha za mapacha hao, hakuishia hapo tu bali aliangalia za wengine wengi ambao wote kwa pamoja walimgusa sana moyoni mwake.
Siku zikaendelea, Naseku hakuonekana kuwa na furaha, muda mwingi alionekana kuwa na huzuni mno. Mama yake alitumia muda mrefu kumtia moyo, hakuataka kumuona akiwa kwenye hali hiyo kila siku.
Ukiachana na mama yake, pia Cassian alikuwa na kazi kubwa ya kumfariji, alimsisitizia kwamba kila kitu kiilichokuwa kikiendelea ni kwamba Mungu alipanga iwe hivyo, hakutaka kumkatisha tamaa, inawezekana katika mapacha hao kungekuwa na rais wa Tanzania.
“Hutakiwi kulia mpenzi,” alisema Cassian huku akimwangalia mke wake aliyekuwa kwenye maumivu makali.
“Inaniuma sana!”
“Ni bora kupata watoto kuliko kukosa kabisa. Usihuzunike, kuwa na mapacha walioungana si kwamba ndiyo mwisho wa kuishi, bado maisha yanaendelea kama kawaida mke wangu,” alisema Cassian huku akimkumbatia mke wake huyo.
Siku na miezi ziliendelea kukatika mpaka Naseku alipofikisha miezi tisa na hivyo kujisikia uchungu na kwenda kujifungua katika Hospitali ya Ocean Road.
Siku hiyo Cassian alikuwa na presha kubwa, hakuamini kama angekwenda kuwa baba. Moyo wake ulibadilika, huzuni kubwa aliyokuwa nayo tangu agundue kwamba mke wake angejifungua mapacha walioungana ikatoweka na furaha ya ajabu kumuingia moyoni mwake.
Alikuwa nje ya chumba cha kujifungulia akiwa na wazazi wake, hakukaa chini, alikuwa amesimama huku kila wakati mikono yake ikiwa imekutanishwa kana kwamba alikuwa akisali.
“Dad! I am going to be a father, can you believe that?” (nakwenda kuwa kuwa baba, unaweza kuamini hilo baba?) aliuliza Cassian huku akiwa na tabasamu pana usoni mwake.
“I am so proud of you my son!” (najivunia wewe sana kijana wangu)
“They are conjoined twins. It doesn’t matter, I just want to see them,” (ni mapacha walioungana. Haijalishi, ninataka kuwaona tu) alisema Cassian huku kila wakati akiusogelea mlango wa chumba kile na kutegesha sikio lake.
“Come and give me a hug,” (njoo unikumbatie) alisema mama yake ambaye alisimama na kukumbatiana na kijana wake.
Waliendelea kusubiri mpaka baada ya dakika hamsini ambapo mlango ukafunguliwa na daktari kuwaambia kwamba walishindwa kufanya kazi yao ndani kwani ilishindikana kabisa Naseku kujifungua kwa hali ya kawaida kwani watoto hao walikuwa wawili kwa pamoja na njia ilikuwa ndogo.
Hawakuwa na jinsi, wakakubaliana na hali iliyokuwepo hivyo Naseku kujifungua kwa njia ya upasuaji kitu ambacho kilifanikiwa kwa asilimia mia moja. Moyo wa Cassian ukawa na furaha tena, hakuamini kama kweli siku hiyo aliitwa baba baada ya miaka mingi kupita.
Hawakuruhusiwa kumuona Naseku wala watoto siku hiyo, waliambiwa wasubiri mpaka siku mbili zipite ndiyo wangepewa nafasi ya kuwaona watoto hao.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Nyumbani, hakukukalika kwa amani, muda wote Cassian alikuwa akitamani kuwaona watoto wake. Aliwaita watu wa kudesign nyumba na kuweka katika staili ya kitoto na kumkaribisha mke wake, nyumba ilipendeza, kulikuwa na kila kitu ambacho mtoto alitakiwa kuwa nacho, kitanda kikubwa, midoli na vitu vingine vingi.
Hakwenda kazini, muda mwingi alikuwa akishinda hospitalini kuliko hata nyumbani. Baada ya siku mbili, akaruhusiwa kumuona mke wake, macho yake yalipotua kwa mwanamke huyo tu, uso wake ukawa na tabasamu pana, alimwangalia, alikuwa mwanamke aliyemfanya kujiona mwanaume aliyekamilika, akamsogelea mahali pale na kumshika mkono, hapohapo Naseku akafumbua macho yake na kuangaliana.
“Mke wangu...” aliita Cassian huku akimwangalia mke wake aliyekuwa akitabasamu tu.
Moyo wake ukafarijika, akajisikia amani moyoni mwake kuliko kipindi chochote kile. Hapohapo manesi wakamletea watoto wake waliokuwa katika chumba kingine kabisa, alipowaona, japokuwa walikuwa wameungana maeneo ya kichwani, upande wa kulia kwa mtoto mmoja na kushoto kwa mwingine lakini moyo wake ulisikia furaha ya ajabu ambayo hakuwahi kuisikia kabla.
“Watoto wangu!” alisema Cassian huku akiwachukua, machozi ya furaha yalikuwa yakimtoka.
Walikuwa watoto wazuri wa kiume waliochukua sura yake, walikuwa wadogo lakini aliwaona jinsi alivyokuwa amefanana nao. Alitabasamu, alicheka kwa furaha, akamuinamia mke wake na kumbusu shavuni.
“Nashukuru kwa kunipa watoto na kunifanya niwe mzazi,” alisema Cassian huku akimwangalia mkewe, alishindwa kumshukuru vipi mke wake huyo.
Naseku hakujibu kitu chochote zaidi ya kuachia tabasamu pana. Moyo wake ulifurahia, aliwapenda watoto wake, hakuangalia namna walivyokuwa, kwake, hao walikuwa kila kitu katika maisha yake.
Waliendelea kukaa hospitali hapo kwa siku mbili zaidi na ndipo wakaruhusiwa huku Cassian akiwa amewapa watoto wake majina ya Walter na Walker.
Walikuwa na sura nzuri, kila mtu aliyekuwa akifika nyumbani na kuwaangalia, alidiriki kusema kwamba Walter na Walker walikuwa na sura nzuri mno. Kila mtu akawapenda, watu wengi wakasikia habari zao na kutaka kwenda huko kuwaona.
Wengine walimfuata Cassian na kumshauri kwamba alitakiwa kutumia kiasi cha fedha kuwapeleka watoto hao nchini India kwa ajili ya kutenganishwa lakini alikataa, katika maisha yake aliamini kitu kimoja tu kwamba Mungu anaporuhusu jambo fulani kutokea, huruhusu kwa kusudi maalumu.
“Kuungana si tatizo! Mungu aliamua iwe hivyo, kwa nini sisi wadamu tupingane naye?” aliuliza Cassian kila alipokuwa akiambiwa mambo ya kuwatenganisha watoto wake.
Walikuwa watoto wenye afya tele ambao waliungana vichwa vyao. Kwa jinsi walivyokuwa wameungana, hata kama Cassian angekubaliana na kila mtu kwenda kuwatenganisha ingeshindikana kabisa kutokana na watoto hao kuchangia ubongo.
Pale walipokuwa wameungana kulikuwa na mishipa mikubwa, mingi iliyokuwa ikipitisha damu, kitendo cha kuwatenganisha kilimaanisha kwamba ni lazima mishipa hiyo ikatwe na sehemu ya ubongo ambao walikuwa wakitumia pamoja iondolewe kitu ambacho kingemaanisha kifo chao.
Lilikuwa jambo gumu mno kuwatenganisha, Cassian alikubaliana na kila kitu, alikuwa tayari kuwaona watoto wake wakiendelea kukua kwenye hali ile kuliko kuwatenganisha au kuwaua wote.
Watoto waliendelea kuwa kwenye uangalizi mkubwa mpaka baada ya kufikisha miezi miwili ambapo wazazi hao wakaamua kuanza kutafuta mfanyakazi kwa ajili ya kuwaangalia watoto hao.
Kitu cha kwanza kabisa walitaka kwenda kijijini kuchukua msichana wa kuwaangalia watoto hao lakini baada ya siku nne, Cassian akapigiwa na mjomba wake, Marcus ambaye alimwambia kwamba angewapa mfanyakazi mzuri kwa ajili ya kukaa na watoto hao.
“Anajua kutunza watoto?” aliuliza Cassian.
“Hilo si swali! Alimtunza Jackson na Careen mpaka walipoanza kuongea,” alijibu mjomba huyo, wakati huo walikuwa wakiongea uso kwa uso.
“Nashukuru sana! Naomba uniitie huyo msichana, nitamlipa kiasi chochote kile,” alisema Cassian.
“Hakuna shida.”
***
Ilikuwa ni rahisi kwa Evelyne kusahau kila kitu kilichotokea katika maisha yake, kusahau tarehe ya siku yake ya kuzaliwa, kuwasahau watu waliomtendea mabaya kuliko kumsahau Cassia na mambo yote aliyokuwa ameyafanya.
Ilikuwa ni aibu kubwa, hakutoka ndani, kila alipokuwa chumbani kwake alikuwa mtu wa kulia tu, alihuzunika, aliumia moyoni mwake na wakati mwingine alihisi kwamba ilikuwa ni afadhali kujiua kuliko kuendelea kuishi.
Rafiki yake, Mwajuma ndiye aliyekuwa karibu naye, yeye ndiye aliyekuwa akimbembeleza usiku na mchana na hata msichana huyo alipotaka kufanya maamuzi magumu ya kutaka kujiua, Mwajuma alikuwa akimuokoa, alifanya hivyo mara tatu kwa nyakati tofauti.
Alimchukuia Cassian, aliilaani siku aliyokutana na mwanaume huyo, aliwachukia wanaume wote duniani hata kama wengine hawakumfanya kile alichofanyiwa na Cassian. Alilia sana, alihuzunika mno na moyo wake kuchomwa na kitu cha moto kilichokuwa na ncha kali.
Siku zikakatika, alijiapiza kwamba ilikuwa ni lazima kulipiza kiasi kwa Cassian, kama alikuwa amemuumiza kwa staili ile na yeye ilikuwa ni lazima kumuumiza kwa pigo lenye maumivu kama lile.
Kwa mwaka mzima alikuwa chumbani, ni mara chache tu ndizo alizokuwa akitoka ndani, tena usiku, kila alipokuwa akipita kwenye mitandao ya kijamii, watu walimcheka, walimdhihaki kwa kile kilichokuwa kimetokea na hivyo moyo wake kubaki na kidonda kikubwa ambacho hakudhani kama kuna siku kingekuja kupona.
Mwajuma ndiye aliyekuwa akifuatilia kila kitu kilichokuwa kikiendelea, yeye ndiye aliyemwambia Cassian kwamba alikuwa amepata mwanamke mwingine, wa uswahilini, asiyejua hata thamani ya dola ya Kimarekani kwa pesa ya Kitanzania.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Moyo wake ulichoma zaidi, kidonda kikatoneshwa, maumivu yakaongezeka, alizidi kulia na kuomboleza kila siku. Siku zikaendelea kukatika huku Mwajuma akimletea kila kitu kilichokuwa kikiendelea, mpaka aliposikia kwamba mke wa Cassian, Naseku alikuwa amejifungua mapacha walioungana, kidogo moyo wake ukajisikia nafuu kwa kuona kwamba machozi aliyokuwa amemwaga kwa ajili ya mwanaume huyo hatimaye Mungu alikuwa amemlipia.
“Mungu amenilipia, na bado ataendelea kunilipia,” alimwambia rafiki yake, Mwajuma pasipo kujua kwamba huo ulikuwa ni mpango wa Mungu kwa watoto hao kuwa katika hali hiyo.
“Tena sana. Chozi la mwanamke haliendi bure,” alisema Mwajuma pasipo kujua kwamba siku zote machozi ya mwanamke malaya kama walivyokuwa yalikuwa yakienda bure, yaani kama kumwaga maji mtaroni kutoka kwenye ndoo chafu.
Wakajifariji sana, wakazungumza maneno yao ya kujipa nguvu na kujiaminisha kwamba kila kitu kilichokuwa kimetokea kilikuwa ni mpango wa Mungu. Baada ya siku miezi miwili watoto kuzaliwa, Evelyne akapata wazo jingine kwamba hata kama Mungu alikuwa amemlipizia kwa mwanaume huyo kupata watoto walioungana ilikuwa ni lazima kufanya jambo, kuwateka na kuwaua ili Cassian aumie, alie kama alivyokuwa akilia.
Hakujua ni kwa namna gani angeweza kuwapata watoto hao. Cassian alikuwa bilionea, mwenye ulinzi mkubwa ambaye kila kona nyumbani kwake kulikuwa na walinzi waliokuwa na bunduki, alijifikiria sana na baada ya kumtuma Mwajuma kumchunguza kwa undani zaidi, akagundua kwamba familia hiyo ilikuwa ikitafuta mfanyakazi wa ndani wa kukaa na watoto.
“Unasema kweli?” aliuliza Evelyne huku akionekana kutokuamini.
“Ndiyo shoga yangu!”
“Hii ndiyo nafasi yangu!” alijisemea.
Alikuwa na pesa, akaunti yake ilikuwa na milioni tisini, alichuma pesa hizo kwa Cassian, zilikuwa ni zaidi ya milioni mia moja na ishirini ila kwa matumizi ya mwaka mzima zikabaki hizo.
Alitaka kutumia sehemu ya pesa hizo kumuumiza Cassian, kitu alichokifanya ni kuwatafuta vijana watatu kutoka katika Kundi la Fogo lililokuwa na maskani yake Tandale na kuwaambia kwamba alitaka kuona watoto wa mzee mmoja wakitekwa.
“Mzee gani?”
“Anaitwa Marcus!”
“Anaishi wapi?”
“Mbezi Beach.”
“Hakuna shida.”
Akawaelekeza namna ya kuwapata watoto hao, haikuwa kazi kubwa, akawaelekeza shule waliyokuwa wakiishi, gari lililokuwa likielekea shuleni kuwachukua, gari hilohilo lilitakiwa kutekwa.
Ilikuwa ni kazi ndogo sana, watu hao waliokuwa na bastola ambao walitumwa kufanya kazi hiyo kwa malipo ya shilingi milioni kumi wakaanza kufuatilia, ni ndani ya siku mbili tu, tayari watoto wake, Jackson na Careen wakatekwa na hivyo kupigiwa simu.
“Jamani naomba msiwaue,” alisema Mzee Marcus huku akionekana kuogopa.
“Wala usijali! Ukifanya tunachokitaka, hawatokufa, ila usipokifanya, tutaviweka vichwa vyao kwenye boksi na kukutumia,” alisikika mwanaume upande wa pili wa simu.
“Jamani naomba msifanye hivyo! Nitawapendi kiasi chochote cha pesa,” alisema Mzee Marcus.
“Hatuhitaji pesa, tunahitaji kuonana na wewe. Ukishindwa, tunawaua, au ukiwapa taarifa polisi, ndiyo kabisa tunawatumbukiza kwenye pipa la tindikali na hutoona hata maiti zao,” aliskika mwanaume huyo.
“Basi sawa. Tuonane, tuyapange na tutakuachia watoto wako wakiwa wazima wa afya,” alisema mwanaume huyo.
“Wapi?”
“Tandale Sokoni, kesho saa saba mchana, pembeni ya kijana anayeuza mihogo, utamuona amevaa fulana iliyoandikwa Big Man kifuani. Zingatia muda, ukichelewa, tusilaumiane. Saa saba mchana kumbuka,” alisema mwanaume huyo na kukata simu.
Mzee Marcus alikuwa kwenye mawazo mengi, hakujua ni kitu gani alitakiwa kufanya. Alihisi kwamba watu hao walihitaji pesa lakini wazo hilo lilifutika kichwani mwake kwani kama kweli walikuwa wakihitaji pesa ilikuwa ni lazima wamwambie kwamba alitakiwa kwenda na pesa zao kabisa.
Siku iliyofuata mapema tu alifika Tandale Sokoni, kulikuwa na watu wengi na ilikuwa vigumu kwa mtu kama yeye kugundua ni mahali gani walipokuwa wakiuza mihogo. Akaulizia mahali kulipokuwa kukiuzwa mihogo, akaambiwa na kwenda huko.
Macho yake yalikuwa yakiangalia huku na kule, aliogopa, kulikuwa na watu wengi kiasi kwamba hakujua mwema alikuwa yupi na mbaya yupi. Alipoendelea kuangalia huku na kule macho yake yakatua kwa mwanaume aliyekuwa akiuza mihogo ambaye alivalia fulana ya Bluu iliyoandikwa Big Man kifuani.
“Yule pale.”
Akaanza kumsogelea kijana yule na kumsalimia. Ilionekana kama kijana yule hafahamu kitu chochote kile, kwani baada ya kuitikia salamu ile, akaendelea na mambo yake kama kawaida.
Mzee huyo alisimama kwa dakika kadhaa, mara mwanaume mmoja akafika mahali hapo akiwa na pikipiki, akaisimamisha na kumwambia apande ili aondoke naye.
“Watoto wangu wapo wapi?” aliuliza hata kabla ya kupanda kwenye pikipiki ile.
“Wewe twende! Au hutaki?” aliuliza mwanaume huyo, haraka sana mzee huyo akapanda na kuondoka mahali hapo.
Mwendo ulikuwa ni wa kasi, wakaondoka kwa kupitia barabara iliyokuwa ikielekea Kwa Mtogole, walipofika kwenye msikiti wa Bi Mtumwa, wakachukua njia upande wa kulia na kwenda sehemu ambayo ilikuwa na kibanda cha wauza mkaa.
Walikwenda kwa mwendo wa kawaida mpaka wakaingia kwenye kichochoro ambacho ilikuwa ni vigumu sana kuona kama pikipiki ingeweza kupenya, wakaingia na kwenda mbele ambapo ikasimama mbele ya nyumba moja chakavu, wakateremka.
Akaingizwa ndani ya nyumba hiyo, akakutana na vijana watatu waliokuwa na bastola, wakamuamrisha kukaa chini na kumwambia kwamba kulikuwa na kitu alichotakiwa kufanya.
Wakamwambia kwamba watoto wake walikuwa wazima kabisa na ili kumridhisha wakamuonyeshea picha za watoto hao ambao walikuwa wamefungwa vitambaa.
“Naomba msiwaue,” alisema mzee huyo huku akitetemeka.
“Hilo si tatizo! Unachotakiwa ni kufanya tunachotaka ukifanye,” alisema mwanaume mmoja.
Wakaanza kumwambia kile walichokuwa wakikihitaji. Alihitajika kumwambia Cassian kwamba atafute dada wa kufanya kazi za ndani ambaye huyo ndiye angekaa na watoto aliokuwa amewapata na msichana huyo hakuwa na sababu ya kumtafuta kwani walitaka kumpa wao wenyewe.
“Jamaniiii!”
“Kama hutaki basi tuwaue!”
“Naomba msiwaue!”
“Basi fanya tulichokwambia!”
Wakamwambia zaidi jinsi hali ilivyotakiwa kufanywa. Hakutakiwa kubisha, ili watoto wake wawe salama ilikuwa ni lazima kufanya kile ambacho watu hao walimtaka kukifanya. Wakakubaliana na kuondoka huku akiacha namba ya simu.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Siku iliyofuata, akapata ugeni, alikuwa msichana mwenye sura mbaya ambaye ndiye huyo aliyetakiwa kutumwa kwa Cassian kwa ajili ya kufanya kazi za ndani kumbe lengo kubwa likiwa ni kuwateka watoto hao na kwenda kuwaua.
Akampigia simu Cassian, aliongea naye kwa kirefu, akamsifia msichana huyo kwamba alikuwa mtu safi, aliyewalea watoto wake mpaka kukua. Cassian hakuwa na hofu, alimwamini Mzee Marcus na hivyo kuhitaji kuonana na msichana huyo.
Alipomuona tu, kwa jinsi alivyokuwa, akahisi kwamba kweli huyo alikuwa mfanyakazi wa ndani na hivyo kumkaribisha kwa mikono miwili.
“Unaitwa nani?”
“Sikujua!”
“Ooh! Sawa. Karibu sana mama!” alimkaribisha Cassian.
Hakukuwa na mtu aliyegundua kwamba mwanamke huyo alikuwa mbaya, wakatokea kumwamini, kila siku ilikuwa ni lazima wampe majukumu yote ya kuwalea watoto hao kitendo kilichomfanya kuwa karibu na watoto hao.
Kila siku asubuhi walikuwa wakiondoka kuelekea katika majukumu yao, nyumbani alikuwa akibaki msichana huyo na watoto hao tu pamoja na walinzi waliokuwa wakilinda mahali hapo.
Siku zilikatika, watoto wao walikuwa furaha yao kubwa, waliendelea kuwapenda, na kila siku walipokuwa wakirudi, kitu cha kwanza kilikuwa ni kuwajulia hali.
“Oh! My kings!” (Oh! Wafalme wangu) alisema Cassian huku akiwaangalia, hapohapo akaanza kuwamwagia mabusu mfululizo.
Wakati hayo yote yakiendelea Evelyne alikuwa akifuatilia kwa karibu, mara kwa mara alikuwa akiwapigia simu watu hao na kuwauliza ni kitu gani kilichokuwa kikiendelea. Aliwalipa pesa zote na kilichokuwa kikisubiriwa ni kimoja tu, watoto hao watekwe na kuwaua kwa mikono yake.
“Mmefikia wapi?” aliuliza Evelyne.
“Hadija yupo ndani ya nyumba!”
“Sawa. Amekwishawateka?”
“Wewe unataka watekwe lini?”
“Hata kesho!”
“Haina shida!”
Kule ndani alipokuwa, msichana yule alikuwa na simu yake ndogo ambayo hakukuwa na mtu yeyote aliyekuwa akiiona, hiyo ndiyo aliyokuwa akifanya mawasiliano na wenzake waliokuwa wamempa kazi hiyo.
Aliambiwa kitu gani alitakiwa kufanya. Mipango ilikuwa imekamilika na kilichokuwa kikisubiriwa ni yeye kuwateka watoto hao na kuondoka nao.
Siku ambayo alitaka kufanya tukio hilo, akasubiri mpaka Cassian na mkewe waondoke nyumbani, walipofanya hivyo, saa 3:00 asubuhi akaelekea chumbani kwao, akachukua ufunguo wa gari aina ya Range SUV nyekundu na kwenda kufungua.
Mlinzi mmoja aliyekuwa mahali hapo alishangaa, haikuwa kawaida kwa mfanyakazi huyo kufungua mlango wa gari lolote lile, hakutaka kusubiri kuambiwa, akamfuata msichana huyo kwa lengo la kuzungumza naye.
“Sikujua!” aliita mlinzi huku akimsogelea.
“Naam kaka!”
“Vipi tena?”
“Vipi kuhusu nini?”
“Mbona unafungua gari. Kuna lolote?” aliuliza mlinzi huku akimwangalia msichana huyo.
“Nataka niwapeleke hospitali. Mama aliniachia maagizo nifanye hivyo!” alisema Sikujua.
“Uwapeleke hospitali! Eeh! Tangu lini umeanza kuwapeleka hospitali?” aliuliza mlinzi huyo huku akionekana kushangaa sana.
Sikujua hakutaka kujibu hilo, akatoka hapo, akaingia ndani ambapo akawachukua watoto hao, akawaingiza ndani ya gari na kuondoka nao.
Mlinzi alibaki akiashangaa. Kwanza hakuamini kama msichana huyo alikuwa akiwapelekea hospitalini lakini kilichomshangaza kabisa, iliwezekanaje msichana kama Sikujua ambaye kwa muonekano tu hakuonekana hata kujua kupiga honi ya gari awe anaendesha gari?
“Mmh!” aliguna mlinzi.
Hakutaka kubaki kimya, alichokifanya ni kumpigia simu Cassian. Mwanaume huyo aliyekuwa ofisini alipoona simu ya mlinzi wa getini ikiingia, akaanza kuogopa, haikuwa kawaida, akili yake ilimwambia kwamba inawezekana kulikuwa na tatizo limetokea nyumbani.
Kabla ya kuipokea akaanza kujiuliza maswali mengi yasiyokuwa na majibu kwamba kabla ya kuondoka nyumbani kulikuwa na jambo baya gani lililokuwa limetokea nyumbani? Hakuna! Sasa kwa nini mlinzi huyo alikuwa akimpigia simu? Kulikuwa na nini? Akapiga moyo konde na kupokea simu.
“Hamisi! Kuna nini?”
“Eti ulimwambia Sikujua awapeleke hospitalini watoto?” lilikuwa swali la kwanza kabisa, swali ambalo lilimshtua mno Cassian.
“Unasemaje?”
“Sikujua kawapeleka watoto hospitalini. Kachukua gari na kuondoka nalo huku watoto wakiwa humo,” alisema Hamisi maneno ambayo yalimfanya Cassian kuinuka kwenye kiti huku akionekana kuchanganyikiwa.
“Unasemaje?” aliuliza, akasimama, mwili ulikuwa ukimtetemeka na kijasho chembamba kumtoka.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Cassian hakuamini alichokuwa amekisikia kutoka kwa mlinzi, alimuuliza tena na tena na jibu lilikuwa lilelile kwamba dada wa kazi za ndani, Sikujua aliyekuwa akimwamini sana aliondoka na watoto nyumbani kwake, na alipokuwa ameelekea, hakukuwa na aliyepafahamu.
Alichanganyikiwa, haraka sana akakata simu na kuwapigia polisi, alipowapa taarifa, wakamwambia kwamba wangefika nyumbani kwake kwa ajili ya kuzungumza, ilikuwa ni lazima wajue ni kitu gani kilitokea mpaka mfanyakazi huyo kuondoka na watoto.
Yeye mwenye akaondoka ofisini, hakutaka kumpigia simu mke wake kwa kuona kwamba angemchanganya, ilikuwa ni lazima apambane yeye kama yeye kuona ingekuwaje ndipo amwambie mkewe kilichokuwa kimetokea.
Njiani, alionekana kuwa na mawazo mengi, alishindwa kabisa kuyazuia machozi kumtoka, moyo wake uliuma na kuchoma, kile kilichokuwa kimetokea kilikuwa kama ndoto kwake, hakuamini kama Sikujua angeweza kufanya kitu kama hicho.
Hakuchukua muda mrefu akafika nyumbani kwake, hakuliingiza gari, akateremka na kumfuata mlinzi, hata kabla hajamfikia tayari polisi wakafika mahali hapo na wote kumfuata mlinzi ambaye alianza kuhadithia kila kitu kilichokuwa kimetokea.
Ulionekana kuwa uzembe mkubwa, ilikuwaje nyumbani kwa bilionea mkubwa kama Cassian kutokee na mfanyakazi kufanya jambo kama hilo, utekaji uliokuwa umefanyika ulikuwa ni wa kizembe sana ambao hawakuamini kama ungeweza kutokea sehemu yoyote ile.
“Inawezekana vipi?” aliuliza polisi mmoja, maelezo ya mlinzi yalionyesha tukio hilo lilikuwa la kizembe.
Kila mmoja alishangaa, walihisi kulikuwa na kitu kilichokuwa kimetokea. Walianza na mlinzi, walihisi kwamba alikuwa akijua mambo mengi kuhusu tukio hilo lililokuwa limetokea.
Alijitetea kwa upande wake kwamba hakuwa akifahamu kitu chochote kile na kwa sababu Cassian na Naseku walikuwa wakimwamini sana Sikujua, hakuwa na la kuuliza lolote lile kwa kuamini kwamba kwa kila kitu alichokuwa akikifanya kilikuwa sahihi.
“Nitamwambia nini mke wangu? Huu ni mtihani mkubwa sana kwangu!” alisema Cassian huku akionekana kuumia mno.
Simu zikapigwa, polisi wa kila kituo wakapewa taarifa juu ya kilichokuwa kimetokea. Kitu cha kwanza kabisa ambacho kwao kilionekana kuwa na uhakika wa kujua mahali watoto walipokuwa kilikuwa ni kulitafuta gari lake.
Polisi walikimbizana, kutekwa kwa watoto wa Cassian, bilionea mkubwa ilikuwa ni sawa na kutekwa kwa watoto wa rais. Polisi wakaondoka katika vituo vyao na kuingia mitaani, wakasaidiana na trafki kulitafuta gari hilo.
Hawakutaka watu wengine wafahamu kilichokuwa kimetokea, ulikuwa ni msako wa kimyakimya ambao waliamini kwamba usingeweza kuwashtua watu wengi.
Ilipofika saa 10:15 jioni, gari la Naseku likaanza kuingia mahali hapo. Kwanza hali aliyokutana nayo nyumbani ilimshtua, hakukuwa na mlinzi, geti alifunguliwa na mume wake, alibaki akijiuliza maswali mengi pasipo majibu yoyote yale.
Alimfahamu Cassian, alikuwa mwanaume mwenye furaha tele lakini kwa siku hiyo alivyokuwa akimwangalia alionekana kabisa kuwa na kitu kilichokuwa kikimtatiza moyoni mwake kwani hata tabasamu ambalo alijitahidi kumuonyeshea lilionekana kutokutoka moyoni mwake.
“Mume wangu! Kuna nini?” aliuliza Naseku huku akionekana kuwa na hofu kubwa.
“Hakuna kitu!” alijibu Cassian.
“Unajua ni kwa jinsi gani sipendi kudanganywa mpenzi. Niambie kuna nini! Hata kama kuna kitu kinachouma mno, wewe niambie tu kwanza,” alisema Naseku huku akimwangalia mume wake huyo ambaye bado hakuonyesha furaha yoyote ile.
“Tuingie ndani kwanza!”
“Hakuna tatizo?”
“Hakuna!”
“Na mlinzi yupo wapi?”
“Tuingie ndani, tutaongea.”
Cassian akamshika mkono Naseku na kuingia naye ndani ya nyumba hiyo, walipofika sebuleni, macho ya mwanamke huyo yakatua kwa polisi wanne waliokuwa sebuleni. Hilo lilimuogopesha zaidi, akahisi kulikuwa na tatizo kwani haikuwa kawaida kwa polisi kufika nyumbani kwake hapo.
Alitaka kujua, alihisi mapigo yake ya moyo yakiongezeka kudunda, aliogopa, aliyafumba macho yake kwa sekunde kadhaa, akamuomba Mungu amtie nguvu kwa lolote ambalo angelisikia mahali hapo.
“Mke wangu...” aliita Cassian huku akimwangalia Naseku ambaye hakujua kilichokuwa kimetokea lakini cha ajabu kabisa akaanza kulia.
Hakuweza kumwambia mke wake, moyo wake ulimuuma, alijiona yeye kuwa chanzo kwa kile kilichotokea, polisi mmoja aliyekuwa mahali hapo ndiye aliyemwambia Naseku kila kitu kilichokuwa kimetokea.
Mwanamke huyo hakuamini alichokisikia, yaani watoto wake aliowapenda kwa moyo mmoja wawe wametekwa, tena na mfanyakazi wa ndani ambaye walimwamini kupita kawaida?
“Haiwezekani!” alisema Naseku huku akilia.
Ilikuwa kazi kubwa kumbembeleza mwanamke huyo, alilia kwa uchungu mno na ni Cassian ndiye aliyekuwa mfariji wake kwa ajili ya kumbembeleza katika kipindi kigumu kama hicho alichokuwa akipitia.
“Nyamaza mke wangu! Nyamaza bebi,” alisema Cassian huku akiwa amemkumbatia Naseku aliyekuwa akilia kama mtoto mdoo.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Watoto wangu! Watoto wangu wao wapi?” aliuliza Naseku huku akiendelea kulia m,no.
Wakati wakiwa hapo, polisi wakapigiwa simu na kuambiwa kwamba gari aina ya Range SUV lililokuwa na namba za usajili T768NYC lilikutwa katika Ufukwe wa Coco huku likiwa limetekelzwa, walihisi kwamba kama wangeanzia huko wangejua mahali watoto walipokuwa.
“Tunakuja hukohuko” alisema polisi mmoja. Wakawaambia kilichokuwa kimetokea na hivyo wote kuondoka ndani ya nyumba hiyo. Naseku naye hakutaka kubaki, alitaka kujua kilichokuwa kikiendelea hivyo naye kuungana nao na kuelekea huko.
Njiani, hakuwa amenyamaza, bado aliendelea kulia tu. Hakukuwa na kitu alichokuwa akikipenda moyoni mwake kama watoto wake, alikuwa tayari kupoteza kila kitu lakini si kuwapoteza watoto wake aliokuwa akiwapenda mno.
Hawakuchukua muda mrefu wakawa wamefika katika ufukwe huo ambapo moja kwa moja wakaanza kulifuata gari hilo lililozungukwa na watu wengi ufukweni hapo.
Walipolifikia, wakalisogelea na kuufungua mlango wa mbele huku wakiwa na glovusi mikononi mwao, macho yao yalipotua ndani ya gari hilo hawakuweza kuamini, kulikuwa na damu nyingi katika kiti cha pembeni na nyuma picha ambayo ilionyesha kulikuwa na mauaji yaliyokuwa yamefanyika ndani ya gari hilo.
“Wamewaua watoto wangu...” alisema Naseku na kuanza kulia upya, kilio kikubwa kilichowashtua watu wote waliokuwa mahali hapo.
“Damu! Wamewaua hawa watoto,” alisema polisi mmoja, kama ilivyo kwa Naseku na Cassian, hata na yeye moyo ukaanza kuuma, ulikuwa ni ukatili mkubwa ambao hawakutakiw akufanyiwa watoto wadogo kama hao.
Evelyne alikuwa chumbani kwake, kichwa chake kilikuwa kikimfikiria Cassian ambaye bado aliendelea kuumiza moyo wake kupita kawaida. Maumivu aliyokuwa nayo moyoni mwake hayakuisha na ndiyo maana kitu pekee alichokuwa akikihitaji kwa kipindi hicho ni kuwaua watoto wa mwanaume huyo.
Aliwatuma watu ambao walimwambia kwamba iwe isiwe ilikuwa ni lazima kufanikisha kile alichokuwa kikihitaji. Hilo halikuwa tatizo kwani baada ya siku kadhaa, akapewa taarifa kwamba tayari watoto walikuwa waekwishatekwa.
Moyo wake ukawa na furaha tele, akamwambia Mwajuma kwamba tayari kazi aliyokuwa akitaka kwa kipindi kirefu ilikuwa imekamilika, watoto aliokuwa akiwataka walikuwa mikononi mwake.
Mwajuma akafurahia, akaona kwamba mtihani mgumu waliokuwa nao kipindi chote ukawa umekamilika na kwa kuwa alihitaji rafiki yake awe na furaha tele siku zote, akamwambia kwamba kwamba bado alikuwa naye bega kwa bega.
“Wapo wapi tukawaue?” aliuliza Mwajuma huku akionekana kuwa na hasira kali hata zaidi ya alizokuwa nazo Evelyn.
“Subiri! Wanasema wapo njiani!” alisema Evelyne.
Alichukua simu yake na kuwapigia watu wake kwa lengo la kuwaambia kwamba hawakutakiwa kuwaua watoto hao wao bali walitakiwa kumsubiria kwani yeye ndiye aliyekuwa na jukumu la kuwamaliza kwa mkono wake.
Kila alipokuwa akipiga simu, haikuwa ikipokelewa, moyo wake ulikuwa na presha kubwa, alikuwa na kimuemue ambacho hakuwa nacho kabla. Hakuacha, muda wote alikuwa akiwapigia simu lakini majibu yalikuwa yaleyale kwamba simu haikuwa ikipatikana.
Akahisi kulikuwa na tatizo, akahisi kwamba inawezekana watu hao walikuwa wamemgeuka na ndiyo maana walizima simu zao na hawakutaka kuziwasha kwa ajili yake.
Alihuzunika, ilipofika majira ya saa sita mchana akawapigia tena, wakati huo simu ilikuwa ikiita kuonyesha kwamba iliwasha, alisubiri, haikupokelewa kwa wakakati, alikuwa na hamu kubwa, baada ya sekunde kadhaa, simu ikapokelewa na sauti ya upande wa pili kusikika.
“Samahani simu iliisha chaji,” alisema mwanaume aliyesikika upande wa pili.
“Usijali! Imekuwaje huko?” aliuliza Evelyne.
“Sikujua aliwateka watoto, akaondoka na gari lao kisha kwenda kuwamaliza huko, kisha akaitupa miili yao baharini,” alisema mwanaume huyo.
“Mbona hamkuniambia nije kuwaua mimi mwenyewe?” aliuliza Evelyne huku akionekana kuumia sana.
“Alihisi kwamba alikuwa akifuatiliwa, si unajua yule ni bilionea alikuwa na mkono mrefu! Aliogopa na ndiyo maana aliwamaliza. Ngoja nikutumie picha,” alisema mwanaume huyo na kilichofuata ni kumtumia picha kadhaa zilizoonyesha wingi wa damu na kisu ndani ya gari hilo.
Kwa damu zilizoonekana tu, ilionyesha kwamba ni picha za kusikitisha, hazikuishia picha hizo bali kulikuwa na picha nyingine zilizoonyesha mfuko mkubwa wa nailoni huku ukiwa na damu nyingi kiasi kwamba hata yeye mwenyewe alisisimka.
Kilichokuwa ndani ya mfuko ule aliambiwa kwamba ni watoto, badala ya moyo wake kufurahi, akaanza kulia, picha ilimsisimua na hakuamini kwamba yeye ndiye aliyekuwa nyuma ya tukio lile.
Walikuwa watoto wadogo ambao aliamini kwamba Mungu alikuwa akiwalinda, kwa wivu wake, hasira zake akaagiza watoto hao wauawe, kweli wakauawa na kuwekwa kwenye mfuk wa nailoni.
Alishindwa kuyazuia machozi yake, akaanza kulia kwa maumivu makali kiasi kwamba hata Mwajuma akabaki akimshangaa, ilikuwaje alie na wakati yeye ndiye aliyeagiza watoto hao wauawe kama ilivyokuwa?
“Mbona unalia sasa?” aliuliza Mwajuma huku akimwangalia rafiki yake huyo.
“Inauma sana! Sikustahili kuwafanyia hivi watoto hawa. Hivi Mungu atanisamehe kweli?” aliuliza Evelyne huku akiendelea kulia kama mtoto.
**** CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Aliyekuwa akisubiriwa alikuwa ni Sikujua tu, aliwapa taarifa kwamba tayari tukio la utekaji lilikuwa limefanikiwa kwa asilimia mia moja hivyo kitu pekee walichokuwa wakitaka kukiona kwa wakati huo ni watoto kuletwa na kisha wampigie simu Evelyne na kwenda kuwaua kwa mikono yake.
Muda ulikwenda lakini Sikujua hakuwa amefika, walimpigia simu mara kwa mara lakini hakuwa akipokea, walikasirika sana lakini baada ya saa moja, akawapigia yeye na kuwaambia kwamba alikuwa kwenye hatua za mwanzo za kuwaua.
“Unawaua?” aliuliza jamaa mmoja.
“Ndiyo! Nimeanza kuwachinja kama kuku. Mtaona kwenye taarifa ya habari usiku jinsi damu zilivyotapakaa,” alisema Sikujua.
“Mmh! Sawa.”
“Nazileta maiti tu huko!”
“Hapana! Hutakiwi kuzileta, kama vipi nenda nazo baharini, zitupe huko, telekeza gari halafu njoo,” alisema jamaa kwa kutoa maelekezo.
“Haina shida!” alisema Sikujua na kufanya kile alichoambiwa.
Dakika arobaini na tano baada ya kuzungumza naye na kuwaambia kwamba alikuwa kwenye hatua za kwanza za kuwaua watoto hao, Sikujua akafika nyumbani hapo, kwa jinsi alivyoonekana, hakuonekana kuwa kawaida hata kidogo.
Mikono yake ilijaa damu, macho yake yalikuwa mekundu kama mtu aliyekuwa amelia sana, hiyo iliwaonyesha kwamba wakati Sikujua akifanya mauaji hayo, alikuwa akilia kupita kawaida.
“Pole sana! Ndiyo ukubwa huo,” alisema jamaa mmoja na kumkumbatia Sikujua.
“Ila picha inatisha sana. Ninaiona kichwani mwangu jinsi nilivyokuwa nikiwachinja, hakika picha hii haitotoka ubongoni mwangu! Kwa nini nimewaua kinyama hivi?” aliuliza Sikujua huku akilia kama mtoto kiasi kwamba kila mmoja alikuwa akimuonea huruma.
Walichokifanya ni kuwaruhusu watoto wa Mzee Marcus kuondoka mahali hapo kwani tayari walichokuwa wamekitaka kwa muda mrefu tayari walikippata.
“Wapelekeni hao watoto wa yule mzee kwake. Tayari mchakato umekamilika,” alisema jamaa huyo na hivyo watoto hao kuchukuliwa na kurudishwa kwa mzee huyo.
****
Cassian na mkewe, Naseku hawakuacha kulia, mioyo yao ilichoma kupita kawaida na hawakuamini kama walikuwa wakipitia maisha waliyokuwa wakipitia.
Walilia mno, picha ya gari iliyokuwa ikionekana mbele yao iliwaumiza mno. Polisi wakawatoa katika eneo la tukio na kuondoka nao. Kila mmoja alikuwa akihuzunika kwani Walter na Walker walikuwa watoto wazuri mno ambao hawakutakiwa kuuawa kikatili kama ilivyokuwa imetokea.
Wakiwa ndani ya gari ndipo kichwa cha Cassian kikakumbuka kuhusu Mzee Marcus, huyo ndiye mtu aliyekuwa amewaambia kuhusu huyo mfanyakazi na kumchukua. Waliambiwa kwamba alikuwa msichana mwema, aliyejua kukaa na watoto, sasa ilikuwaje msichana huyohuyo aondoke na watoto wao na kwenda kuwaua kikatili.
Hakutaka kupoteza muda, alichokifanya ni kuwasiliana na mzee huyo na kumwambia kila kitu kilichokuwa kimetokea na hivyo kutaka kuonana naye.
“Haina shida,” alisema mzee Marcus huku tayari akiwa amekwishapewa watoto wake.
Majira ya alasiri, mzee huyo akafika nyumbani kwa Cassian na kuanza kuongea naye, taarifa aliyokuwa akipewa ni kama hakuwa akiifahamu, alihuzunika mpaka machozi kumlenga, alimuonyesha Cassian kwamba kama kuchomwa kwa tukio hilo hata na yeye alikuwa amechomwa hivyohivyo.
“Yaani Sikujua ndiye amefanya haya?” aliuliza Mzee Marcus huku akionekana kutokuamini.
“Ndiyo!”
“Sikujua huyuhuyu ninayemjua?”
“Ndiyo!”
Akaanza kutokwa na machozi, maigizo aliyokuwa akiyafanya mahali hapo ilikuwa vigumu sana kugundua kwamba alijua mchongo mzima juu ya kile kilichokuwa kimetokea.
Yeye ndiye aliyetakiwa kutoa maelezo polisi juu ya msichana huyo ili polisi wajue ni kwa jinsi gani alikuwa amempata msichana huyo mpaka kumuamini na kumpelekea Cassian.
Hilo halikuwa tatizo, wakaelekea kituo cha polisi na kueleza kila kitu kuhusu msichana huyo. Kwake, alionekana kuwa mwema kwani aliwahi kuishi naye kwa miaka mingi na hakukuwa na kitu chochote kilichotokea.
“Inawezekana kuna mtu alimtuma kufanya hivi,” alisema Cassian.
“Sijui kwa kweli, ila cha muhimu ni kwamba moyo wa binadamu unaweza kubadilika muda wowote ule,” alisema Mzee Marcus.
Alikuwa akimheshimu sana, hakutaka kuwaambia polisi wamshikilie bali aliamua kuwaambia kwamba wafanye kila linalowezekana mpaka maiti za watoto wake zinapatikana ili kama kwenda kuzizika, basi azizike kwa mkono wake.
Wakaondoka, nyumbani, bado maombolezo yalikuwa yakiendelea, kila mmoja alikuwa akilia sana, walihitaji kuziona maiti hizo, walijua kwamba wangeumia sana lakini hawakuwa na jinsi, siku ya kwanza ikakatika, ya pili mpaka ya tatu bado maiti hizo hazikuwa zimeonekana.
Sikujua alikuwa ndani ya gari, watoto walikuwa pembeni yake, alikuwa akiwaangalia huku moyo wake ukimwambia kwamba siku hiyo alitakiwa kufanya kila liwezekanalo kuhakikisha watoto hao wanauawa mikononi mwake.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Moyo wake ulidhamiria kuua kwa asilimia mia moja, kutoka hapo Mbezi Beach mpaka Mwenge hakukuwa mbali sana kwa kuwa tu hakukuwa na foleni kubwa, aliendesha huku akili yake ikijifikiria ni kwa namna gani alitakiwa kuwamaliza watoto hao ambao wala hawakuwa wakilia, ndiyo kwanza walikuwa wakicheka pale walipokuwa kana kwamba walikuwa wakienda kununuliwa nguo za sikukuu.
Gari lilipofika Makongo, likasimamishwa na msafara wa rais uliokuwa ukipita maeneo ya Mwenge. Alikasirika, alitaka kuwahi kuwamaliza watoto hao kwani iwe isiwe ilikuwa ni lazima kuwamaliza siku hiyohiyo.
Aliangalia huku na kule, magari mbalimbali yaliyokuwa katika msafara wa rais yalikuwa yakiendelea na safari ya kuvuka katika mataa ya Mwenge. Alitulia garini lakini alipoyarudisha macho yake kwa mapacha wale waliokuwa katika kiti cha mbele, kitu cha ajabu kabisa kikaukumba moyo wake, kitu ambacho hakuwahi kukifikiria kama kingemjia moyoni mwake hasa katika kipindi kama hicho.
Moyo wake wa kikatili, ukaingiwa na huruma nzito kiasi cha kumfanya kukosa amani kabisa. Kila alipokuwa akiwaangalia watoto wale, akahisi moyo wake ukisinyaa kabisa.
Akaanza kujuta kwa uamuzi aliochukua wa kukubali kuwateka watoto wale, akabaki akilengwa na machozi, mbele yake akawaona watu wengi wakiwa wamesimama wakimwangalia, wote hao walikuwa wakimlaumu kwa uamuzi aliotaka kuuchukua kipindi hicho.
Alijishangaa, hakuwa hivyo, hakuwa na hali hiyo tangu azaliwe, ni kitu gani kilichokuwa kikimfanya kuingiwa na huruma ya ghafla hivyo. Mbali na huruma hiyo akaanza kuisikia sauti moyoni mwake ikimlaumu kwa kile alichotaka kukifanya kwamba kwa nini aliuruhusu moyo wake kutaka kuwaua watoto wale, malaika wa Mungu ambao hawakuwa na hatia yoyote ile.
Alisakamwa moyoni mwake mpaka akahisi maumivu mazito, akabaki akisikitika kwa kile alichotaka kukifanya. Nguvu ya kutaka kufanya mauaji ikaanza kuondoka moyoni mwake na akajikuta akiingiwa na upendo wa hali ya juu kwa watoto wale.
“Siwezi kuwaua! Siwezi kuuawa watoto wasio na hatia,” alisema Sikujua.
Aliendelea kusubiri mpaka msafara uishe ndipo waliporuhusiwa akaliondoa gari lake mahali hapo na kuondoka. Aliambiwa kwamba ni lazima aende akawaue watoto hao, hakutaka kufanya hivyo hata kidogo hivyo alichokifanya ni kuondoka mpaka katika soko la Mwananyamala ambapo akanunua kuku wawili na kisu kisha kuingia ndani ya gari.
Kwanza hakutaka kuondoka kuelekea baharini, alichokitaka ni kwenda kwa rafiki yake aliyekuwa akiishi Magomeni, alipofika, akamuachia watoto hao kwa lengo la kuwafuata baadaye.
“Wewe! Ndiyo watoto gani hawa?” aliuliza rafiki yake huyo huku akishangaa.
Sikujua hakuwa na jinsi, akamwambia rafiki yake huyo kila kitu kilichotokea kwamba hakutaka kuwamaliza watoto hao, alikuwa kwenye harakati kubwa ya kuokoa maisha yao hivyo ilikuwa ni lazima amsaidie kwa ajili ya kuwa nayo kwa muda wakati yeye akielekea Coco Beach kufanya kile alichotaka kufanya.
“Usichelewe,” alisema rafiki yake huyo na kuondoka.
Kidogo moyo wake ukajisikia amani, akafurahi, akawaangalia kuku wale, walikuwa wakilia, aliondoka nao mpaka alipofika Coco Beach ambapo kwa muda huo hakukuwa na watu wengi, akawachukua wale kuku, akawachinja kisha kunyunyizia damu zile ndani ya gari lile, hakuishia hapo, akawaweka katika mfuko mweupe wa nailoni ambao ulionyesha jinsi ulivyolowa damu huku ndani kukiwa na kitu, akaupiga picha, akaliacha na yeye kuondoka zake kutoa taarifa kwamba mauaji aliyokuwa ameambiwa, yalikuwa yamefanyika.
****
Kila mmoja alikata tamaa, wakajua kwamba watoto wao walikuwa wameuawa kwani damu zilionekana ndani ya gari na kila mmoja aliamini kwamba huo ndiyo ulikuwa mwisho wa kuwaona mapacha hao.
Walikuwa na pesa, kuwapoteza watoto wao kuliwafanya kutokuwa na furaha ya utajiri ule, kuliwafanya kuona kwamba kila kitu walichokuwanazo mikononi mwao kupotea, utajiri huku watoto wako wakiwa wameuawa hakika yalikuwa ni zaidi ya maumivu.
Siku ziliendelea kukatika, Cassian alimuonea zaidi huruma mke wake, alionekana kuwa mwanamke mnyonge ambaye kila siku alikuwa akilia tu, moyo wake ulikuwa na maumivu makali mno na aliamini kwamba kama asingemfariji basi mwanamke huyo angeugua ugonjwa wa moyo na mwisho wa siku kufariki dunia.
Ilipofika siku ya nne huku kila mmoja akiwa na huzuni tele Cassian akaletewa taarifa na daktari ambaye aliichukua damu ile na kwenda kuipima, taarifa ilionyesha kwamba damu ile haikuwa ya binadamu bali ilikuwa damu ya kuku.
Alishindwa kuamini, hapohapo akamfuata mke wake na kuanza kuzungumza naye, akamwambia kuhusu ripoti hiyo aliyopewa na daktari kwamba damu waliyoikuta ndani ya gari haikuwa damu ya watoto wao bali ilikuwa damu ya kuku.
“Unasemaje?” aliuliza Naseku huku akiyafuta machozi yako.
“Ni ripoti ya daktari!”
“Sasa watoto wetu wapo wapi?”
Hilo lilikuwa swali ambalo kila mmoja hakuwa na majibu nalo. Walishindwa kujua mahali walipokuwa watoto wao, mpaka kufikia hatua hiyo, kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kumshukuru Mungu kwa kuwa watoto wao hawakuwa wameuawa kama walivyokuwa wakihisi kabla.
Mbali na swali kuhusu mahali walipokuwa watoto wao lakini pia kulikuwa na swali jingine kwamba kama Sikujua aliwateka watoto wao na kuondoka nao, kwa nini hakuwamaliza? Je, hakuwamaliza kwa kuwa aliuawa yeye au ni kitu gani kilikuwa kimetokea.
Wakawasiliana na polisi na kuwapa taarifa hizo. Wao wenyewe hawakuamini, walijaribu kutafuta kila sehemu, tena wakati mwingine wakiwatumia hata wapelelezi wao lakini hakukuwa na mtu aliyejua mahali walipokuwa.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kazi ikaanza upya, haikuwa kuzitafuta maiti bali kilichokuwa kimetokea ni kutafuta mahali watoto walipokuwa. Walimwambia kwamba wangempa taarifa kwamba watoto wake walikuwa mahali fulani hivyo kumtaka kuwa na matumaini juu ya hilo.
“Kweli watapatikana?” aliuliza Naseku, muda wote alionekana kuwa na hofu tele.
“Wala usijali! Tumuombe Mungu, naamini watapatikana,” alisema Cassian huku akimkumbatia mke wake.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment