Search This Blog

Friday, July 15, 2022

VIGANJA MASHAVUNI MWANGU - 1

 





    IMEANDIKWA NA : NYEMO CHILONGANI



    *********************************************************************************



    Simulizi : Viganja Mashavuni Mwangu

    Sehemu Ya Kwanza (1)



    Cassian alikuwa kimya, macho yake yalikuwa yakiangalia baharini huku mawazo yake yakiwa mbali kabisa. Moyo wake ulichoka, maumivu aliyokuwa akiyasikia moyoni mwake hayakuweza kuelezeka.

    Alikuwa bilionea mkubwa, mwenye makampuni mengi, migodi ya dhahabu na kila kitu ambacho kingemfanya kustahili kuitwa bilionea. Alimshukuru Mungu kwa utajiri aliokuwa nao lakini tatizo lilikuwa moja tu, hakuwa na mtoto.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Hilo lilikuwa pigo kubwa katika maisha yake, wakati mwingine alikuwa akimuuliza Mungu juu ya kilichokuwa kimetokea. Kwa nini alimpa utajiri mkubwa na kumnyima mtoto? Utajiri ungekuwa na maana gani kama tu hakuwa na mtoto ambaye angekuja kuurithi baada ya yeye kufa?

    Hakuwa na furaha hata kidogo, kila siku moyo wake ulichoma kama moto kiasi kwamba alimuonea aibu mkewe, hata kukutana naye wakati mwingine aliogopa kutokana na tatizo lililokuwa mwilini mwake.

    Hapo ufukweni mawazo yake yalikuwa mbali kabisa. Alitulia ndani ya gari huku akionekana kuwa na mawazo lukuki, alikaa garini kwa dakika kadhaa ndipo akaamua kutoka na kuanza kutembea. Kwa jinsi alivyokuwa akiwaza mpaka wakati mwingine machozi yalikuwa yakimtiririka mashavuni mwake.

    Aligombana na dada zake kwa sababu hakuwa na mtoto. Kipindi cha kwanza ndugu hao walifikiri kwamba mwanamke aliyekuwa akiishi naye ndiye alikuwa na matatizo lakini baada ya kupima katika hospitali tatu, zote zilionyesha yeye ndiye alikuwa na matatizo.

    Hakutaka kuwaambia ndugu zake ukweli, alikuwa tayari kugombana nao na hata kuchukiana maisha yake yote lakini si kuwaambia ukweli kwamba tatizo la kutokupata mtoto lilisababishwa na yeye na si mpenzi wake kama walivyokuwa wakihisi.

    “Kwa nini wanamuonea? Kwa nini hawataki kuniuliza ili wajue ukweli kwamba Evelyne hana tatizo?” alijiuliza huku machozi yakimtiririka mashavuni mwake.

    Hayo ndiyo yalikuwa maisha yake ya kila siku. Moyo wake ulimuuma mno, hakuona thamani ya utajiri, bila kuwa na mtoto maisha yake yangekuwa hivyohivyo mpaka kifo chake na mali kubaki kwa ndugu zake.

    Si kazini, si nyumbani au barabarani, kila alipokuwa Cassian alikuwa myonge, hakuwa muongeaji, wakati mwingine alihisi kabisa mwili wake ukianza kupungua kutokana na matatizo aliyokuwa nayo.

    Alipenda kuwa na mtoto, kila alipowaona wanaume wenzake wakiwa na watoto barabarani moyo wake ulimuuma, alitamani kuona kama ingekuwa yeye, alitamani kuona naye akiwabeba watoto wake kama walivyofanya watu wengine.

    Mpenzi wake ambaye alimchukulia kama mkewe, Evelyne ndiye aliyekuwa akimfariji kila siku, alimwambia kwamba hakutakiwa kukata tamaa na ipo siku ambayo Mungu angetenda muujiza na hatimaye kupata watoto.

    Alimwangalia Evelyne machoni, aliyaona maumivu yake, aliona jinsi msichana huyo alivyokuwa akiumia kwa kuwa tu hakuwa na mtoto. Alimuona kuwa mwanamke mwenye uvumilivu sana, aliyevumilia maneno ya ndugu na wakati hakuwa na tatizo bali tatizo kubwa lilikuwa kwake.

    “Pole sana mke wangu,” alisema Cassian huku akimwangalia Evelyne.

    “Usijali mume wangu! Maneno ya watu huwa hayanisumbui hata kidogo! Mimi nimekupenda wewe, katika shida na raha hakika tutaendelea kuwa pamoja na kamwe sitokuacha,” alisema Evelyne maneno ambayo kwa Cassian yalionekana kuwa faraja kubwa.

    “Ila sina uwezo wa kumpa mimba mwanamke!” alisema Cassian.

    “Hata kama! Nimekupenda wewe mpenzi, mtoto ni majaaliwa ya Mungu,” alisema Evelyne huku akimwangalia mpenzi wake huyo machoni mwake.

    Japokuwa mkewe alijitahidi sana kumfariji lakini hakufarijika, bado alijiona kuwa na mzigo mkubwa kichwani mwake. Alimuomba Mungu kila siku bila kukoma, maombi yake makubwa yalikuwa ni kupata mtoto.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Ni kama alimuona Mungu akiwa ameziba masikio, alijitahidi kufunga na kuomba lakini matokeo yalikuwa yaleyale kwamba hakupata mtoto. Hilo lilimuuma mno, alichokifanya ni kwenda kwa madaktari wengi pamoja na mkewe, katika kila hospitali aliyofika, aliambiwa kwamba alikuwa na tatizo kubwa katika mfumo wa utengenezaji mbegu, hazikuwa na nguvu za kumpa mimba mwanamke.

    Kila aliposikia sehemu kuna mikutano ya injili, yeye alikuwa wa kwanza, wakati mwingine alimuacha Evelyne nyumbani na kwenda huko, alitaka kumuona Mungu akimtendea muujiza lakini alimuona Mungu kuchelewa kwani kwenye kila alipofanyiwa maombezi aliambiwa kabisa kwamba angepata mtoto lakini matokeo yalikuwa yaleyale, hakupata mtoto.

    Maumivu hayakupungua moyoni mwake, alikuwa mtu wa majonzi na kulia kila siku. Hakuona thamani ya utajiri, wakati mwingine alimwambia Mungu kwamba alikuwa tayari kupoteza kila kitu lakini mwisho wa siku aje kuwa na mtoto lakini maombi yake yote hayo yalionekana kama si kitu mbele za Mungu.

    “Mchungaji! Kwa nini Mungu hajibu maombi yangu?’ aliuliza Cassian huku akionekana kuchanganyikiwa.

    “Kuna siku atafanya jambo. Nakwambia kwamba kuna siku utapata uzao wako wa kwanza,” alisema mchungaji huku akimwangalia Cassian.

    “Kweli?”

    “Unachotakiwa ni kuamini. Uwe na imani hata kama ni ndogo kama mchanga, hakika Mungu atafanya jambo,” alisema mchungaji huku akimwangalia Cassian.

    Aliteseka usiku, hakulala vizuri, kila wakati alikuwa akishtuka usiku na alipoyafumbua macho yake kitu cha kwanza kilikuwa ni mtoto tu. Evelyne alimuonea huruma, wakati mwingine msichana huyo aliinuka kutoka kitandani na kwenda sebuleni, huko alikuwa akilia kama mtoto, hakuamini kama alikuwa akipitia maisha yake, alimpenda sana Cassian, alitamani siku moja wawe na familia yao lakini jambo hilo lilishindikana kabisa.

    Cassian alipokuwa akiamka na kumkosa mkewe kitandani, alimfuata sebuleni na kumkumbatia, alimfariji kwa kumwambia kwamba kuna siku wangepata watoto hivyo hakutakiwa kuwa na hofu hata kidogo.

    “Kuna siku Mungu atatupa familia yetu! Usilie mpenzi, amini kwamba kuna siku tutakuwa na familia yetu,” alisema Cassian huku akiwa amemkumbatia Evelyne.

    “Ninaamini mume wangu!” alisema Evelyne huku akilia kilio cha kwikwi.



    “Shoga mwenzako najuta kwa nini sikuwa nikichoma sindano za kuzuia mimba! Yaani umalaya wangu huu leo unanifanya nikose mtoto! Nimetoa mimba nyingi, mwisho wa siku leo hii nakosa mtoto! Hivi kweli mimi wa kukosa mtoto?” aliuliza Evelyne huku akimwangalia rafiki yake, Mwajuma.

    “Mmh! Shoga ila na wewe ulizidi. Kila ulipopata mimba, kazi ilikuwa ni kutoa tu, ona sasa, unamfanya mume wako akose amani, alie kila siku, kwa nini lakini? Tena hata sindano za kuzuia mimba ulikataa kuchoma, ” aliuliza mwajuma.

    “Wewe acha tu. Kwanza hapa ninachokitaka ni kufunga naye ndoa tu ili hata kama kuna siku mambo yataharibika basi yaharibike tukiwa kwenye ndoa ili tugawane mali manake bila hivyo naweza kuachwa kibudu,” alisema Evelyne.

    “Hilo kweli Eve! Siku mumeo akigundua kwamba hata tatizo lolote ni lazima atakuacha. Umemdanganya sana! Kila nikimwangalia namuonea huruma bilionea wa watu. Wewe mwanamke mbaya sana,” alisema Mwajuma na wote kuanza kucheka.

    Mwajuma alikuwa shoga pekee wa Evelyne aliyejua kilichokuwa kikiendelea. Aliyajua maisha ya Evelyne tangu kitambo, walikua wote utotoni na kusoma pamoja. Katika maisha ya ujana waliyopitia wasichana hao yalikuwa ni maisha ya kujirusha na kila mwanaume aliyekuwa akipita mbele yao.

    Waliendekeza ufuska, walitembea na kila mwanaume aliyeonekana kuwa na pesa. Walipenda maisha ya starehe kiasi kwamba wakati mwingine walikuwa wakijiuza katika mitandao ya kijamii wakitafuta pesa na kwenda nchi mbalimbali kutafuta mabwana.

    Maisha yao yaliharibika, wanaume ndiyo waliokuwa wakiyaendesha maisha yao. Kutokana na kujiona mjanja zaidi, Mwajuma aliamua kujichoma sindano za kuzuia mimba ila kwa Evelyne, aliogopa kabisa kufanya hivyo. Evelyne alipokuwa akipata mimba, kitu cha kwanza kilikuwa ni kutoa. Mpaka anakutana na bilionea kijana, Cassian, alitoa mimba zaidi ya kumi na mbili.

    Wakawa wapenzi, wakaanza kuishi pamoja. Kwa kuwa alimpata mwanaume mwenye pesa, Evelyne akatulia, akataka kujenga maisha na kutengeneza familia yake ila tatizo lilikuja pale alipogundua kwamba hatoweza kushika mimba kwa sababu mfuko wake wa uzazi (uterus) na ukuta uliokuwa ukishikilia mfuko huo (cervix) vyote vililegea na mimba isingeweza kukaa tena.

    “Huwezi kushika mimba. Mfuko wako wa uzazi umeharibika vibaya kiasi kwamba hauwezi kuruhusu kijusi kutengenezwa,” alisema daktari kwa sauti ya huruma huku akimwangalia Evelyne aliyekuwa akilia pembeni ya rafiki yake.

    Hicho ndicho kitu kilichomuumiza mno, hakuamini kama tabia yake ya kutoa mimba ndiyo ingemfikisha mahali hapo. Alilia na kujuta sana huku wakati mwingine akitamani muda urudi ili arekebishe pale alipokosea lakini hakuweza kuurudisha muda huo.

    Alijua kabisa kwamba kama angemwambia mumewe kuwa tatizo alikuwa nalo yeye angemuacha na kutafuta mwanamke mwingine, hivyo alichokifanya ni kutumia pesa zake, kwa kila hospitali waliyotakiwa kwenda kesho, kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kumtuma Mwajuma huko, alionana na daktari aliyetakiwa kuwapima siku inayofuata na kumpa kiasi kikubwa cha pesa ili aseme kwamba mwanaume ndiye aliyekuwa na tatizo.

    Huo ndiyo ulikuwa mchezo wao, walifanikiwa, Cassian hakujua kilichokuwa kikiendelea, kwenye kila hospitali waliyokuwa wakiingia, majibu yalitoka na kusema kwamba yeye ndiye aliyekuwa na tatizo kitu kilichomnyima furaha katika maisha yake.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Wakati hayo yote yakiendelea, Evelyne hakutaka kuonyesha kitu chochote ndani ya nyumba, alimuonyeshea Cassian mapenzi ya dhati kwamba alikuwa akimpenda hivyohivyo kumbe dhamira yake kubwa ilikuwa ni kufunga ndoa na mwanaume huyo ili hata kama kuna siku wangeachana basi wagawane mali.

    “Nakuonea huruma mke wangu,” alisema Cassian huku akimwangalia Evelyne.

    “Hutakiwi kunionea huruma mume wangu! Nilikwishakwambia kwamba mimi na wewe mpaka kifo kitutenganishe,” alisema Evelyne huku akimwangalia mwanaume huyo.

    “Ila sina uwezo wa kumpa mimba mwanamke!”

    “Hilo hutakiwi kujali! Nilikupenda wewe, nakupenda jinsi ulivyo, unaniheshimu, unanithamini, hivyo ni vitu pekee ambavyo kila msichana huvipenda kutoka kwa mtu wake,” alisema Evelyne, wakati akizungumza hayo, tabasamu lilikuwa likionekana kwa mbali.

    Bado Cassian alikuwa na mawazo tele, kila siku alipokuwa akimwangalia msichana huyo alijiona mkosefu katika maisha yote. Msichana mrembo kama Evelyne alitakiwa kuwa na mwanaume mwenye uwezo wa kumpa mimba mwanamke si kama yeye.

    Mwanamke huyo alimuonyeshea uvumilivu, hakujua kama yeye ndiye mwenye tatizo na si kama alivyofikiria. Kwa kuwa alikuwa amejitolea kumpenda maisha yake yote, kuishi naye basi akataka kufanya kile alichokihitaji, kufunga naye ndoa pasipo kugundua mbinu za mwanamke huyo zilikuwa ni kugawana mali.

    Akamwambia kwamba alikuwa tayari kufunga naye ndoa, hiyo ilimpa furaha Evelyne ambapo baada ya kuwa peke yake, akachukua simu yake na kumpigia rafiki yake kipenzi, Mwajuma kwa lengo la kumpa taarifa hiyo.

    “Vipi? Mbona asubuhi asubuhi?” aliuliza Mwajuma kwenye simu.

    “Mambo yametiki!”

    “Umepata mimba?”

    “Hapana bhana! Ameniambia nianze kufanya mipango ya harusi,” alisema Evelyne huku akionekana kuwa na furaha tele.

    “Kweli?”

    “Kwa nini nikudanganye? Tuanze kufanya mipango shoga kabla huyu mpuuzi hajagundua lengo langu,” alisema Evelyne.

    “Eeh! Unamuita mpuuzi tena!”

    “Hahah! Sasa nimuiteje? Mwanamke wa kukudanganya tena kizembe namna hii! Huyu ni mpuuzi,” alisema Evelyne na kuanza kucheka.

    Mipango ikaanza kusukwa, Evelyne akajitoa vilivyo, akawataarifu marafiki zake wote kwamba alikuwa akijiandaa kufunga ndoa na mwanaume wake wa ndoto. Hakufikiria mapenzi, kichwa chake kilifikiria pesa ambazo aliamini kwamba mara baada ya kuachana na Cassian basi angeweza kuzipata.

    Marafiki zake wakampongeza, wengine wakamuonea wivu kwani hawakupenda kumuona akiolewa na mwanaume mwenye pesa kama yeye, kila mtu alitaka kuwa na mwanaume mwenye pesa kama Cassian.

    Akawasiliana na marafiki zake waliokuwa Dubai, akawaambia wamuandalie shela kwani alitaka kuvaa vazi hilo kutoka nchini humo. Akawapigia simu marubani wake wa ndege ndogo ya mpenzi wake aliyokuwa akiitumia kwenda huku na kule, akawaagiza kwamba wajiandae kwani walitakiwa kuondoka kuelekea katika Visiwa vya Comoro kula fungate yao baada ya kufunga ndoa.

    Siku haikuwa imefika lakini Dar es Salaam nzima walikuwa wakifahamu kilichokuwa kikiendelea. Evelyne alimpa taarifa kila mtu aliyekuwa akimfahamu, alitaka watu wote wajue kwamba alikuwa akienda kufunga ndoa na bilionea mkubwa Afrika Mashariki.

    “Tuna wiki mbili tu! Kila kitu kipo tayari kwa upande wako?” aliuliza Cassian huku akimwangalia Evelyne.

    “Ndiyo mpenzi! Hofu kwako!”

    “Huku kwangu kila kitu kipo poa. Nimewasiliana na Mchungaji Sebastian Mark kutoka nchini Ufaransa, amejitolea kuja kutufungisha ndoa. Nimeandaa boti nzuri na ya kifahari ambayo tutafungia ndoa huko katikati ya bahari,” alisema Cassian huku akitoa tabasamu, japokuwa alikuwa na moyo wa furaha lakini suala la kukosa mtoto lilimkosesha amani.

    “Kwenye boti?”

    “Ndiyo!”

    “Waooo! Jamani baba watoto...” alisema Evelyne na kumkumbatia mwanaume huyo.

    Siku hazikuwasubiri, ziliendelea kukatika kama kawaida. Baada ya kubaki wiki moja, maandalizi yakachachamaa, Evelyne hakutulia, kichwa chake kilifikiria mali, kwa jinsi alivyokuwa na presha aliona kama watu aliowaweka kwenye kamati walikuwa wakimchelewesha.

    “Mwajuma! Wamesemaje?” aliuliza Evelyne.

    “Kila kitu kipo tayari! Hoteli imekwishaandaliwa huko Comoro! Fungate tu ndiyo inasubiriwa,” alijibu msichana huyo baada ya kumpigia simu.

    “Nashukuru sana shosti!”

    “Halafu kuna kitu umesahau! Hivi umewaalika wale madaktari ambao walikusaidia kuficha siri?” aliuliza Mwajuma.

    “Mungu wangu! Nilikuwa nimesahau! Ngoja niandike meseji halafu niwatumie wote kwa pamoja,” alisema Evelyne na kuanza kuandika ujumbe huo.

    Aliandika harakaharaka, akakumbuka kwamba alitakiwa pia kumpigia Cassian na kumpa taarifa kwamba tayari hoteli ilikuwa imeandaliwa kwa ajili yao. Mara baada ya kuandika ujumbe huo wa kuwashukuru madaktari kwa mchezo walioufanya, na kwa sababu jina la Cassian lilimkaa sana kichwani, kwenye kutuma, akamtumia na Cassian, anakuja kushtuka baada ya ujumbe huo kwenda huko.

    “Mungu wangu! Nimemtumia na Cassian pia!” alisema Evelyne, hapohapo kwa kuchanganyikiwa, akadondosha simu. Mapigo ya moyo yakaanza kumdunda kwa nguvu.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Cassian hakuwa na furaha kabisa, moyo wake ulikuwa na mawazo tele. Kila wakati alikuwa akimfikiria mpenzi wake, Evelyne, alionekana kuwa mwanamke shupavu, mwenye uvumilivu ambaye alikuwa tayari kufanya kitu chochote kile lakini si kumpoteza.

    Alijiona kuwa na bahati kubwa, hakuwa na mawazo kwamba kitu alichokuwa akikihitaji msichana huyo kilikuwa mali zake na si mapenzi kama alivyokuwa amefikiria.

    Akampigia simu rafiki yake aliyeitwa Osman na kumwambia kwamba alitaka kuzungumza naye, alihitaji kuwa bestman wake katika harusi hiyo iliyokuwa imebakiza siku moja kabla ya kufungwa katika boti moja ya kifahari aliyokuwa akiimiliki.

    Kwa kuwa lilikuwa jambo muhimu, hakutaka kuzungumza naye kwenye simu, alichokitaka ni kuonana naye na kumwambia kwamba walitakiwa kuonana Serena Hotel kwa ajili ya kuzungumza suala hilo muhimu.

    “Serena ni mbali sana. Kwa nini tusionane hapa Manyema?” aliuliza Osman kwenye simu. Alichokuwa akikiangalia zaidi kilikuwa ni foleni kubwa ya magari.

    “Ipo wapi?”

    “Hapa Kinondoni! Makaburini Mkwajuni!” alijibu Osman maneno yaliyomfanya Cassian kushtuka.

    “Yaani nije kuonana na wewe Kinondoni?”

    “Ndiyo! Njoo bwana!”

    “Poa. Ila ninahitaji ulinzi, nisije kudandiwa na wahuni,” alisema Cassian, hilo halikuwa tatizo, kila kitu kiliandaliwa.

    Cassian akatoka ofisini kwake, alijua kwamba alikuwa akienda katika mitaa ya Kiswahili hivyo hakutaka kwenda na gari lake la kifahari la Jaguar bali akachukua gari la mfanyakazi wake, Opa na kwenda nayo huko.

    Hakutaka kugundulika, alijua kwamba kama angefika mahali hapo na gari la kifahari kila mtu angelitolea macho na kuangalia kuona ni mtu gani angeteremka katika gari hilo.

    Njiani, kichwa chake hakikutulia, bado alimfikiria Evelyne, alimuona kuwa mwanamke shupavu, mwenye moyo wa chuma ambaye alijitolea maisha yake kwa asilimia mia moja kuishi naye japokuwa hakuwa na uwezo wa kumpa mimba.

    Hakuchukua dakika nyingi akafika mahali hapo. Akapaki gari lake na kuteremka. Kwa kuwa lilikuwa gari la kawaida, hakukuwa na mtu aliyelitolea macho.

    Hakutaka kugundulika, hivyo akachukua miwani yake ya jua na kuvaa kisha kuanza kupiga hatua kwenye sehemu ya kulia chakula ambayo ilikuwa maarufu Kinondoni nzima kwa kupika ugali mzuri na nyama ya kuchoma.

    “Karibu bwana. Umebadilika! Hiyo miwani kama komando,” alisema Osman, ndiyo ilikuwa kawaida yake, kila walipokuwa wakikutana, kitu cha kwanza kilikuwa ni kumtania kutokana na muonekano wowote aliokuwa nao.

    Wakakaa na kuagiza chakula. Macho ya Cassian hayakutulia, yalikuwa yakiangalia huku na kule, hakuonekana kujiamini, swali lililokuwa kichwani mwake ni nini kingetokea mahali hapo kama tu watu wangegundua kwamba alikuwa yeye.

    Wakati akiangalia macho yake huku na kule, yakatua usoni mwa msichana mmoja, mrefu kidogo, msichana aliyekuwa na sura nzuri, kifua kidogo huku uso wake tu ukiwa na tabasamu la asili.

    Cassian akabaki kimya, akamwangalia msichana huyo kwa muda. Aliuona uzuri wake lakini tatizo kubwa alilokuwa nalo ni umasikini uliokuwa ukimwandama.

    Alibalia khanga moja iliyoonekana kuchoka, kwa ndani alikuwa na gauni lake refu na blauzi ya rangi nyekundu. Japokuwa alionekana kuwa masikini kwa muonekano wake tu lakini msichana huyo alikuwa mchangamfu mno, aliongea na wateja kana kwamba alikuwa akimjua kila mtu.

    “Mbona unamwangalia sana Naseku?” aliuliza Osman mara baada ya kumuona rafiki yake akimwangalia sana msichana huyo.

    “Naseku! Ndiye nani?”

    “Si huyo msichana unayemwangalia. Ngoja nimuite aje kutuhudumia,” alisema Osman na hapohapo kumuita msichana huyo.

    Bila hiyana, huku uso wake ukiwa kwenye tabasamu pana Naseku akaanza kupiga hatua kuelekea kule walipokuwa wanaume hao. Macho yake Cassian hayakutoka kwa msichana huyo, alikuwa akimangalia mpaka alipofika mahali pale.

    Mapigo yake ya moyo yalikuwa juu, alisahau kwa muda kwamba nyumbani alimuacha msichana ambaye kila siku alimwambia kwamba alikuwa akimpenda kuliko wanawake wote katika dunia hii.

    “Naseku! Kutana na mshikaji wangu huyu,” alisema Osman huku akimtambulisha Cassian kama rafiki yake. Cassian alipovua miwani na kumwangalia vizuri msichana huyo, Naseku akashtuka.

    “Umeshtuka sana kumuona Cassian hapa kwenu. Ndiye huyo unayemuona! Hebu msikilize kwanza,” alisema Osman.

    Cassian alibaki kimya kwa muda, alikuwa akimwangalia msichana huyo kwa mshangao. Hakuamini kama angekutana na msichana aliyekuwa mrembo kama alivyokuwa.

    Umbo lake maridadi, sauti yakena sura yake ya kitoto vilimfanya kuishiwa nguvu na kumsifu Mungu kwamba alikuwa akijua sana kuumba.

    “Unaitwa Naseku?” aliuliza.

    “Ndiyo!”

    “Bila shaka Mmasai?”

    “Ndiyo!”

    “Nimefurahi kukufahamu! Una chakula gani?”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Ugali na nyama choma!”

    “Huna baga au pizza?” aliuliza Cassian na wote kuanza kucheka kwani walijua kwamba alikuwa akitania.

    “Tuna sandwich!” alijibu Naseku kwa utani, vicheko vikazidi.

    “Naomba ugali na nyama choma.”

    “Sawa.”

    Wakati anaondoka, mwanaume huyo alibaki akimwangalia kwa nyuma. Naseku alikuwa mrefu mwenye umbo maridhawa lililomfanya Cassian kuchanganyikiwa.

    “Kaka una mke!” alisema Osman.

    “Mke au mchumba! Unataka kunibania nini?” aliuliza Cassian na wote kucheka mpaka kugongeana mikono.

    Naseku hakuchukua muda, akapeleka chakula mezani pale na wanaume hao kuanza kula. Kila mmoja alikuwa na furaha, walikuwa wakizungumza mambo mengi kiasi kwamba hakukuwa na mtu aliyechoka.

    Muda wote huo Cassian hakumwambia Osman kilichokuwa kimemfanya kupigia simu na kukutana, alitaka wamalize kula na ndipo wazungumze.

    Wakati wakiendelea kula, mara simu ya Cassian ikatoa mlio uuliomaanisha kwamba kulikuwa na ujumbe mfupi uliokuwa umeingia kwenye simu. Haraka sana akaingiza mkono mfukoni na kuitoa simu hiyo.

    Macho yake yakatua katika kioo cha simu hiyo na kuliona jina la Evelyne. Moyo wake ukapiga paa kwani kwa jinsi alivyokuwa akimpenda, kila alipokuwa akiona ujumbe wake moyo wake ulifarijika mno, hivyo akaufungua ujumbe huo na kuanza kuusoma.

    Haukuwa ujumbe mrefu sana, aliposoma mstari kwa mstari, alijikuta akibadilika, hakuamini kama ujumbe ule ulikuwa umetoka kwa msichana aliyekuwa akimpenda. Ulikuwa ni ujumbe uliobeba maumivu mazito, hakuamini kile alichokiona, akashusha pumzi nzito kiasi kwamba mpaka Osman akashangaa.

    “Vipi?”

    “Osman! Osman! Osman!” alijikuta akiliita jina hilo bila kuzungumza lolote.

    “Kuna nini?”

    “Evelyne! Evelyne!” alisema Cassian huku akimpa simu rafiki yake huyo na kuanza kuusoma ujumbe huo ambao uliandikwa ‘Dokta! Nashukuru sana kwa kunifichia siri ya kutokushika mimba. Mume wangu hajui lolote, anahisi tatizo ni lake. Naomba uje kuhudhuria harusi yangu wiki ijayo. Nitakupa taarifa zaidi’

    “Mungu wangu!” alijikuta akisema Osman huku akiiweka mezani simu hiyo.

    Cassian alishindwa kuvumilia, machozi yakaanza kumtoka. Moyo wake ulisikia maumivu makali ambayo hakuwa ameyategemea hapo kabla. Kila siku alijua kwamba yeye ndiye alikuwa na tatizo la kutokumpa mimba mwanamke lakini kwa meseji ile ilionyesha kabisa kwamba hakuwa na tatizo lolote lile.

    Lawama zake za kwanza zilikwenda kwa madaktari ambao aliwaamini na kuwaambia wampime, wao ndiyo waliomwambia kwamba mpenzi wake hakuwa na tatizo lolote lile bali aliyekuwa na tatizo alikuwa yeye.

    “Cassian! Unatakiwa kutulia, yaani usifanye maamuzi yoyote mabaya,” alisema Osman huku akionekana kumfariji sana rafiki yake huyo.

    “Osman! Yaani huyu malaya ananifanyia hivi? Yaani ananifanya nijione sina uwezo wowote wa kumpa mwanamke mimba! Yaani ananifanyia hivi mimi!” alisema Cassian huku akilia kwa uchungu mkubwa.

    Hakuweza kuvumilia, akainuka na kuelekea ndani ya gari. Osman akasimama na kumfuata kulekule. Kila mtu aliyekuwa ndani ya mgahawa ule alibaki akiwashangaa, si wao tu bali hata msichana Naseku naye alikuwa akishangaa na hakujua ni kitu gani kilikuwa kikiendelea mpaka Cassian kuinuka na kuelekea ndani ya gari lake huku akionekana kuwa tofauti.

    Kazi ilikuwa kwa Osman, alikuwa akimpoza rafiki yake huyo ambaye alionekana kuumia kupita kawaida. Alijua kwamba kwa hali moja au nyingine ilikuwa ni lazima kufanya jambo kama tu angekwenda nyumbani akiwa katika hali hiyo. Alikaa naye ndani ya gari na kumpoza sana na mwisho wa siku mwanaume huyo kurudi katika hali ya kawaida.

    “Nifanye nini?” aliuliza Cassian.

    “Kitu cha kwanza kabisa hutakiwi kuonyesha hali yoyote ya kuupata huu ujumbe!” alisema Osman.

    “Sawa.”

    “Kama ni furaha, muonyeshee, usimfanye ashtukie kitu chochote kile, halafu huo ujumbe wake ulioingia, ufute. Halafu kesho nitakupeleka katika hospitali ya swahiba wangu akakufanyie vipimo tena,” alisema Osman.

    “Sawa. Nitashukuru!”

    Hicho ndicho alichoambiwa, hakutaka kuonyesha tofauti yoyote ile. Hakutaka kuondoka muda huo, alikaa mpaka ilipofika usiku ambapo akajiandaa na kuelekea nyumbani.

    Alipofika, kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kumkumbatia Evelyne kwa furaha tele, alimletea unafiki, hakuonyesha tofauti yoyote ile machoni mwake, kama ilivyokuwa juzi na jana ndivyo ilivyokuwa siku hiyo kiasi kwamba msichana huyo akahisi hakukuwa na jambo lolote baya na inawezekana ujumbe ule haukuenda, na kama ulienda basi hakuuona.

    Wakati Cassian akiwa amekwenda bafuni kuoga, haraka sana Evelyne akachukua simu ya mpenzi wake huyo na kuanza kuangalia. Akaenda sehemu ya meseji na kuangalia katika uwanja wa kuwasiliana naye, hapo, hakukutana na ujumbe wowote mpya kuonyesha kwamba kumbe meseji hakuwa ameipata.

    Kidogo moyo wa Evelyne ukarudi kwenye amani, furaha ambayo ilikuwa imepotea ikarudi tena. Cassian alipomaliza kuoga, akarudi chumbani, akamnyanyua Evelyne na kumtupa kitandani ambapo akaanza kumvua nguo moja baada ya nyingine na kuanza kufanya mapenzi.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mpaka kufikia hatua hiyo msichana huyo hakujua kama mwanaume huyo alijua kila kitu, hali aliyokuwa amemuonyeshea siku hiyo ilikuwa kama siku nyingine, wakalala na siku iliyofuata Cassian kuaga kwamba anaelekea kazini lakini ratiba yake ya kwanza kabisa ni kuwasiliana na Osman ambaye akamwambia hospitali ya kwenda na kuonana huko.

    Hawakutaka kuchelewa, moja kwa moja wakaingia ndani ambapo Osman akamwambia tatizo alilokuwa nalo rafiki yake huyo ambapo daktari huyo hakuwa na tatizo lolote lile zaidi ya kuanza vipimo.

    “Huna tatizo lolote lile. Mbegu zako zina nguvu za kuzalisha hata watoto ishirini! Wewe tu,” alisema daktari baada ya saa kumi za kusubiri majibu.

    “Kweli?”

    “Ndiyo! Kwani kuna mtu alikwambia huna uwezo?”

    “Ndiyo! Kwa hiyo mambo yapo poa?”

    “Kabisa kabisa. Mwanaume ngangari kama chuma,” alisema daktari huyo huku akimpongeza Cassian kwa kumpigapiga mgongoni.

    Wakati Cassian akiwa amekwishapata majibu yake, Evelyne akampigia simu Mwajuma na kumwambia kwamba alitaka kuonana naye. Wakaonana na kuumuhadithia kila kitu kilichokuwa kimetokea, jinsi alivyowaandikia meseji madaktari na kwa bahati mbaya kumtumia mpenzi wake.

    “Una hatari sana!”

    “Wewe acha tu! Lakini hakushtukia. Angejuaaaa! Nafikiri angenichinja usiku ule,” alisema Evelyne huku akionekana kuwa na furaha tele.

    “Mmh! Umecheza kama Pele. Kwa hiyo!”

    “Sasa hivi hata kutuma meseji za kijinga siwezi. Nisije kukosea tena. Ile haikwenda, nikirudia tu, inakwenda,” alisema msichana huyo pasipo kugundua kwamba Cassian alijua na alitaka kumfanyia mchezo hatari, kumkataa siku moja kabla ya harusi.



    Evelyne alikuwa na presha kubwa, alitaka kuona akifunga ndoa na mwanaume huyo bilionea ili aweze kufanikisha ile adhma yake aliyokuwa ameipanga. Alimpigia simu Mwajuma na kumwambia kwamba alitaka harusi yake iwe bab’kubwa hivyo kuendelea kuwaambia watu wengine.

    Akaona hiyo haitoshi, akazungumza na waandishi wa habari wa mitandaoni na magazetini, aliwalipa kiasi kizuri cha pesa kwa ajili ya kutangaza harusi hiyo ambayo ingefanyika siku ya Jumamosi inayofuatia.

    Waandishi hao na wale waliokuwa na kurasa zao katika mitandao yao wakaanza kuwataarifu watu wengi kwa kuposti matangazo kuhusu harusi hiyo kubwa ambayo ilitarajiwa kufanyika hivi karibuni.

    Ni ndani ya siku chache tu, gumzo kubwa katika mitandao ya kijamii ilikuwa harusi hiyo, kila mtu alitaka kuona ni kitu gani kingetokea kwani kwa jinsi ilivyokuwa ikitangazwa kwenye mitandao hiyo, kila mmoja akahisi kwamba ingekuwa harusi kubwa na ya kifahari hata zaidi ya ile ya Beckham alipomuoa Victoria.

    “Hii harusi kiboko! Inafungwa ndani ya boti!” alisema jamaa mmoja huku akionekana kushtuka sana, hakuamini kama kungekuwa na Mtanzania ambaye angeamua kufunga ndoa ndani ya boti ya kifahari badala ya kanisani.

    “Kaka hiyo ni pesa. Unachotakiwa ni kuiamkia pesa, hilo tu,” alisema jamaa mwingine.

    Wakati hayo yote yakiendelea, Cassian hakuwa na furaha hata kidogo, alikuwa mtu wa mawazo tele, alipokuwa akikaa ofisini kwake, hakuamini kama Evelyne angemfanyia mambo kama yale aliyomfanyia lakini wakati mwingine alibaki akimshukuru Mungu kwa muujiza alioufanya.

    Alikuwa na kila kitu, alikosa mtoto tu, alikata tamaa kwa kuhisi kwamba huo ndiyo ungekuwa mwisho wa kila kitu lakini mwisho wa siku daktari akabainisha kwamba hakuwa na tatizo lolote lile kitu kilichomfanya kumshukuru Mungu sana.

    Mapenzi yote aliyokuwa nayo kwa Evelyne yakaanza kupotea na chuki kuanza kuingia moyoni mwake. Alihitaji kuwa peke yake, alihitaji kuwa na msichana mwingine, asingeweza kuendelea kukaa na msichana huyo, alitaka kumuondoa maishani mwake na kumuingiza mwanamke mwingine.

    Alimuumiza mno, hakutaka kumuacha hivihivi pasipo kumuumiza kama alivyokuwa amefanya. Alipanga kumuacha siku moja kabla ya kufunga ndoa. Alijua jinsi Evelyne alivyokuwa akihaha huku na kule kuhakikisha kwamba harusi inafungwa haraka iwezekanavyo hivyo alichokitaka ni kumuumiza kwa kukataa kumuoa msichana huyo.

    Akapanga na Osman kila kitu ambacho walitakiwa kufanya, ilikuwa ni lazima Cassian apange kwenda kulala na msichana huyo hotelini siku moja kabla ya kufunga ndoa hiyo halafu amtelekeze hukohuko na kuondoka hotelini hapo, hilo wala halikuwa tatizo lolote lile, wakapanga hivyo na kukubaliana na mwanaume huyo kwamba hicho kilitakiwa kufanyika haraka sana.

    Bado Cassian hakutaka kuonyesha tofauti yoyote kwa Evelyne, alimuonyeshea mapenzi ya dhati kwamba bado alikuwa akimpenda mno, kila alipokuwa naye, uso wake ulikuwa na tabasamu pana na muda wote alikuwa akikenua japokuwa moyoni mwake kulikuwa na maumivu makali.

    Hakuacha kumsisitiza msichana huyo kufuatilia kila kitu kilichokuwa kikiendelea, alimharakisha sana kwani siku zilibaki chache na kama asingeweza kukamilisha kwa kipindi kifupi basi kila kitu kingeharibika.

    “Waandishi umewaandaa kuja harusini?” aliuliza Cassian huku akimwangalia mpenzi wake huyo.

    “Ndiyo! Tena niliwasiliana na waandishi wa habari wa BBC nao wamesema watakuja,” alisema Evelyne huku akionekana kuwa na furaha tele.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Safi sana. Nakupendea hapo tu. Hakuna mwanaume asiyependa kuwa na mwanamke mwenye kasi ya kufanya mambo kama wewe mpenzi,” alisema Cassian, hapohapo akamvuta msichana huyo na kumkumbatia.

    Uso wake ulikuwa tofauti na kile kilichokuwa moyoni mwake, alikuwa na hasira kali, alimchukia mno msichana huyo japokuwa hakutaka kumuonyeshea ni jinsi gani alikuwa na chuki kali dhidi yake.

    “Nakupenda mpenzi!” alisema Cassian huku akimwangalia Evelyne usoni.

    “Nakupenda pia mume,” alisema msichana huyo.

    Siku ziliendelea kukatika, ilipofika Ijumaa, Cassian akampigia simu Osman na kumwambia kwamba siku hiyo ndiyo ilikuwa ya kufanya mpango waliokuwa wameupanga. Akamwambia kwamba kila kitu walichokuwa wamekubaliana kilikuwa juu ya mstari na kilichobaki kilikuwa ni wajibu wa kufanya hicho walichokuwa wamepanga.

    Ilipofika majira ya saa moja usiku, Cassian akampigia simu Evelyne na kumwambia kwamba siku hiyo walitakiwa kulala hotelini ili asubuhi wajiandae na harusi iliyokuwa imepangwa kufanyika siku hiyo.

    Hilo halikuwa tatizo, kwa kuwa alimwamini sana Cassian na aliamini kwamba hakuwa akifahamu kitu chochote kile, akaondoka nyumbani na kuelekea katika Hoteli ya Twiga iliyokuwa Masaki na kukutana huko.

    Kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kukumbatiana kwa furaha, wakaenda bafuni kuoga, walipomaliza, wakatupana kitandani na kuanza kuvuana nguo. Akilini mwa Evelyne aliyaona mapenzi mazito ya mwanaume huyo, aliamini kwamba kusingekuwa na mwanamke yeyote ambaye angemtoa katika ulimwengu wake.

    Walipomaliza kufanya mapenzi, simu ya Cassian ikaanza kuita, alipoliona jina la Osman wala hakujiuliza, akaipokea simu ile na kuanza kuzungumza naye.

    “Umekwishafika? Ndiyo...ni kesho...ooh! mchungaji ndiyo amefika! Umempeleka hoteli gani? Serena...safi sana...anataka kuniona...basi sawa nakuja...” alisema Cassian na kukata simu.

    “Nani?”

    “Osman! Anasema kwamba mchungaji Mark ameingia kutoka Ufaransa! Hivyo anataka nikamuone mara moja,” alisema Cassian.

    “Sawa. Ila usichelewe kurudi mpenzi!”

    “Usijali!” alisema Cassian, hakuishia hapo tu, akamvuta Evelyne na kumbusu mfululizo kisha kuondoka.

    Msichana huyo akabaki na amani moyoni mwake, hakuamini kama kweli siku inayofuata ndiyo ilikuwa ya kufunga ndoa na kuwa mke halali wa mwanaume huyo. Alikuwa na tamaa ya utajiri, alijitahidi kuficha siri ambayo hatimaye alijua ndiyo ilikuwa imedumu pasipo kugundulika mpaka hapo alipokuwa akitaka kufunga naye ndoa.

    Hapohapo akampigia simu Mwajuma, akajisifia sana kwamba alikuwa mwanamke wa shoka aliyemkamata vilivyo Cassian na mwisho wa siku kutaka kufunga naye ndoa huku akiwa amemdanganya vya kutosha kuhusu kuzaa watoto.

    “Shoga kesho ndiyo naanza safari! Nikitoka hapo, ni kuleta vituko, akiniacha kesi inakwenda mahakamani tunagawana utajiri,” alisema Evelyne huku akionekana kuwa na furaha ya ajabu.

    “Jamani shoga mpaka nakuonea wivu! Unakwenda kuuchukua ubilionea hivihivi!” alisema Mwajuma.

    “We acha tu! Ndiyo tayari nishatajirika!” alisema Evelyne.

    Cassian akashuka mpaka chini ya hoteli, akaingia ndani ya gari lake na kuondoka mahali hapo. Mtu wa kwanza kuzungumza naye alikuwa mlinzi wa nyumbani kwake, akamwambia kwamba Evelyne hakutakiwa kuingia ndani ya nyumba hiyo na kama angemruhusu kuingia basi angemchukulia maamuzi magumu mno.

    Mlinzi huyo hakuleta ubishi, alimheshimu bosi wake, tena baada ya kuona kwamba mlinzi mmoja asingetosha, Cassian akapiga simu mpaka katika kampuni ya ulinzi ya Knight na kuwaambia kwamba alihitaji ulinzi wa watu watano nyumbani kwake ambapo bila tatizo lolote walinzi watano waliokuwa na bunduki wakaelekea huko.

    “Osman upo wapi?” aliuliza Cassian.

    “Nyumbani!”

    “Hebu twende Albert Lounge tukale bata kidogo!” alisema Cassian huku akiendesha gari kwa kasi kuelekea Albert Lounge. Msasani kwa ajili ya kuonana na mshikaji wake huyo.



    Muda ulikuwa ukisonga mbele, msichana Evelyne alikuwa ndani ya chumba cha hoteli, mara kwa mara alikuwa akimpigia simu Mwajuma na kuzungumza naye, alikuwa akimtambia kwamba hatimaye alikuwa akienda kufanikiwa kwa kile alichokuwa amekipanga.

    Cassian alikuwa na utajiri mkubwa, makampuni mengi ambayo aliamini kwamba kama wangekuwa mume na mke kisha kuachana basi akaunti yake ingesoma zaidi ya bilioni kumi za Kitanzania.

    Hakuwa radhi kuona akikikosa kiasi hicho cha pesa na ndiyo maana alipambana kuhakikisha anaolewa na kufanya uchafu huo akiwa ndani ya ndoa. Hapo chumbani, kichwa chake kilikuwa kikifikiria mambo mengi, alitaka kuona kila kitu kikienda harakaharaka kama alivyokipanga, alitaka kuona asubuhi ikiingia, aende saluni na mpambe wake na baadaye aende kwenye boti ambayo walitakiwa kufungia ndoa.

    Aliiamini simu aliyopigiwa Cassian na kuambiwa kwamba tayari mchungaji kutoka nchini Ufaransa alikuwa amekwishaingia nchini na kilichokuwa kimebaki kilikuwa ni kufunga ndoa tu.

    Pale chumbani hakutulia, kila wakati alikuwa akiishika simu yake na alipoona muda unazidi kwenda na mwanaume wake harudi chumbani hapo, akaanza kumpigia simu.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Hakukuwa na majibu yoyote yale, simu ilikuwa ikiita tu lakini haikuwa ikipokelewa. Alishindwa kujua kulikuwa na tatizo gani lakini kila alipofikiria kwamba alikwenda kumpokea Mchungaji Mark, alihisi kwamba mwanaume huyo huyo alikuwa bize katika kufanya mazungumzo na mchungaji.

    Muda ulizidi kusogea, mpaka inaingia saa tisa usiku wa manane bado majibu yalikuwa yaleyale. Hilo kidogo likaanza kumtia hofu na kitu kimoja na cha kwanza kilichomjia kichwani mwake ni kwamba Cassian alikuwa amepata ajali mbaya.

    Akahisi mwili wake ukipigwa ganzi, hakutaka kuona hilo likitokea, kitu alichokuwa akikihitaji ni kuona akifunga ndoa naye na hata kama angepata ajali na kufa, basi kitu hicho kitokee wakati wakiwa ndani ya ndoa.

    “Mpenzi nina wasiwasi,” alisema Evelyne, alikuwa amempigia simu Mwajuma.

    “Wasiwasi wa nini tena?”

    “Cassian. Aliondoka kwenda kuonana na Mzungu ambaye ndiye atakuwa mchungaji wa kesho. Hajarudi mpaka sasa hivi,” alisema Evelyne.

    “Aliondoka saa ngapi?”

    “Tangu saa tatu usiku!”

    “Mmh! Lakini usijali! Inawezekana kaenda sehemu kunywa. Si unajua wanaume,” alisema Mwajuma.

    Maneno ya rafiki yake huyo hayakumuingia kichwani, bado alikuwa na hofu kwa kuhisi kwamba kulikuwa na kitu kilichokuwa kikiendelea upande wa pili.

    Muda ulizidi kusogea, hakupata usingizi, ilikuwa ni heri kukosa kitu chochote kile lakini si kuikosa ndoa ambayo iliutesa moyo wake, ndoa ambayo aliamini piga ua ilikuwa ni lazima kuyabadilisha maisha yake.

    Ilipofika saa kumi na moja na kuona kimya, hakutaka kuendelea kubaki hospitali, haraka sana akatoka na kuanza kwenda katika hospitali zilizopo karibu, alihisi kwamba mwanaume wae huyo alikuwa huko. Alikwenda kwenye hospitali tatu lakini huko hakufanikiwa na ndipo akapata wazo la kwenda nyumbani kwa Cassian.

    Hakuchukua muda mrefu akafika nyumbani hapo. Hali aliyoikuta ikamtia hofu, nje kulikuwa na walinzi kadhaa waliokuwa na bunduki, hakujua sababu ya watu hao kuwa mahali hapo, kitendo cha wao kuwa hapo kikampa majibu kwamba kulikuwa na tatizo, inawezekana Cassian alikuwa amekamatwa na polisi.

    “Unakwenda wapi wewe mwanamke?” aliuliza mlinzi mmoja huku akimsogelea Evelyne.

    “Naingia kwangu!”

    “Humu kwako?”

    “Ndiyo!” alijibu huku akimwangalia mlinzi yule.

    “Nyumba yako hii?”

    “Ni kwa mume wangu mtarajiwa, na leo tunafunga ndoa!” alijibu Evelyne kwa mbwembwe zote, alikuwa akimwangalia mlinzi huyo kwa jicho la dharau, jicho lililoonyesha moyo wake kusema ‘nikiingia ndani utanikoma mshenzi wewe’.

    “Wewe si ndiye Evelyne?”

    “Ndiyo!”

    Wale wenzake waliokuwa pembeni waliposikia jina hilo, nao wakajisogeza kule alipokuwa msichana huyo na kumwangalia. Evelyne alishangaa, hakujua kitu kilichokuwa kikiendelea mahali hapo, akahisi kulikuwa na tatizo.

    “Hutakiwi kuingia humu!” alisema jamaa mwingine.

    “Siruhusiwi kuingia humu?”

    “Ndiyo!”

    “Na nani?”

    “Huyo unayejidaia ni mpenzi wako!”

    “Cassian?”

    “Ndiyo!”

    “This is insane! I got get inside,” (huu ni uwendawazimu! Inabidi niingie ndani) alisema Evelyne kwa Kiingereza cha harakaharaka.

    “No! You have to leave!” (hapana! Unatakiwa usepe) alisema mwanaume mwingine, hakuishia hapo, akaanza kukoki bunduki yake.

    Mara ya kwanza msichana huyo alifikiri ni utani lakini baada ya kuwaona watu hao wakimwangalia huku wakionekana kumaanisha walichokuwa wakimwambia, akahisi kabisa hapo hakukuwa na utani wowote ule. Akanywea ila kitu pekee kilichomjia kichwani ni kwa sababu gani Cassian hakutaka aingie ndani.

    Akaona hilo halitoshi, akawaomba walinzi hao wamuitie mlinzi wa kila siku nyumbani hapo, hilo halikuwa tatizo, mlinzi huyo akafika na kuanza kuzungumza naye.

    “Jamaa ndiyo aliagiza usiingie ndani! Hata huu ulinzi umeongezwa kwa ajili yako,” alisema mlinzi huyo kitu kilichompelekea Evelyne kuhisi kama akimwagiwa maji ya baridi kabisa.

    Machozi hayakutaka kusubiri, hapohapo yakaanza kumtoka na kutiririka mashavuni mwake, akaanza kusikia maumivu makali, hakuamini kile kilichokuwa kikiendelea, alihisi kwamba alikuwa ndotoni akiota kila kitu kilichokuwa kikiendelea mahali hapo.

    Hiyo ilimaanisha kwamba Cassian hakutaka kuwa naye, ilimaanisha kwamba hakukuwa na ndoa tena, yaani alichwa siku ya harusi. Lilimuumiza moyoni, alitamba sana kwamba alikuwa akienda kuolewa, mitandaoni, gumzo lilikuwa ndoa hiyo, kila kona ilizungumziwa harusi hiyo.

    Akarudi ndani ya gari, kabla ya kuondoka akalalia usukani, mbele yake akayaona maisha yake yakiwa yamejaa giza, hakujua sababu iliyomfanya Cassian kuchukua uamuzi ule na wakati mpaka mara ya mwisho mwanaume huyo alipokuwa akiagana naye alionyesha sura ya tabasamu, penzi zito lilionekana kupitia macho yake, sasa iweje abadilike ghafla hivyo?CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Akaanza kuifikiria mitandao ya kijamii, alitumia kiasi kikubwa cha pesa kutamba huko, kama kila mtu alikuwa akijua kwamba alikaribia kufunga ndoa na mwanaume huyo siku hiyo ilimaanisha kwamba hata hapo alipoachwa kwenye mataa basi kila mmoja angejua kwamba ameachwa solemba.

    Alilia sana, hakutaka kumpigia simu Mwajuma na kumwambia, alichokifanya ni kuwasha gari na kumfuata huko. Mawazo juu ya Cassian yalikuwa makubwa mno, hakuamini kama kweli mwanaume huyo alimuacha katika kipindi kigumu kama hicho.

    Aliendesha gari huku akiwa na mawazo hayo ya kuachwa yakimsumbua kichwani mwake. Kila alipokuwa akipita na kupishana na watu, aliona kama wote hao tayari walijua kama aliachika.

    Alipofika Sinza Makaburini, akakata kulia ambapo aliendesha mpaka katika nyumba moja iliyokuwa na wanawake wengi kwa nje, akasimamisha gari na kuwafuata wanawake hao, akawasalimia na kuingia ndani.

    Alikijua chumba alichokuwa akikaa Mwajuma, moja kwa moja akaelekea mpaka katika chumba hicho na kugonga, mlango ukafunguliwa na msichana huyo ambapo baada ya kumuona tu, akaanza kulia.

    Mwajuma alishangaa, ilikuwa ni asubuhi sana hata kutoka ndani hakuwa ametoka, alijiuliza sababu ya msichana huyo kulia namna hiyo, alionekana kuumia, alionekana kuwa na kitu moyoni mwake, ilikuwaje alie kwa uchungu namna ile na wakati siku hiyo ilikuwa ni ysiku ya kufunga ndoa na bilionea mkubwa Afrika Mashariki.

    Alijaribu kumbembeleza anyamaze lakini Evelyne hakunyamaza, alikuwa akilia mfululizo, tena kilio kikali kilichojaa kwikwi. Aliendelea kulia kwa dakika ishirini nzima ndipo akanyamaza na kuanza kumwambia Mwajuma kilichokuwa kimetokea.

    “Haiwezekani!” alisema Mwajuma huku akimwangalia rafiki yake huyo.

    “Ameniacha! Cassian ameniacha,” alisema Evelyne huku kila wakati akiyafuta machozi.

    Huo ndiyo ulikuwa ukweli, aliumia mno moyoni mwake, kilichokuwa kimetokea hakukiamini, aliona kila kitu kilichokuwa kikiendelea kama ndoto fulani ambapo baada ya dakika chache angeshtuka kutoka usingizini.

    Hawakujua sababu ya Cassian kuchukua uamuzi wa ghafla namna hiyo kwani usiku uliopita tu alikuwa na furaha tele na alimuonyeshea msichana huyo mapenzi yote, sasa iweje abadilike namna hiyo?

    “Au ile meseji uliyomtumia ndiyo chanzo?” aliuliza Mwajuma.

    “Hapana! Haikumfikia?”

    “Una uhakika? Kwako ilionyeshaje? Kama meseji haikwenda inakuonyeshea kwa kuweka kialama chekundu, sasa kama ile ilikwenda, kwa nini kialama hakikuonekana?” aliuliza Mwajuma maswali ambayo yalianza kumpa jibu Evelyne.

    “Mmh!”

    “Nahisi meseji aliipata ila aliifuta na hakutaka kukuonyeshea dalili zozote zile!” alisema Mwajuma huku akimwangalia msichana huyo.

    “Inawezekana!”

    “Kwa hiyo utafanyaje?”

    “Nimeaibika Mwajuma. Cassian ameniumiza. Kwa pesa nilizokuwa nazo kwenye akaunti yangu, nitazitumia hata zote kumuua mwanamke yeyote atakayekuwa naye, kama kuumia, na yeye aumie kwa kumuua msichana ampendaye!” alisema Evelyne huku akionekana kuwa na hasira kali.

    “Wewe tu! Na mimi nitakusaidia. Ukiua kwa kisu, nitaiweka maiti kwenye gunia, sitokuacha ila huyu mbwa lazima tumkomeshe,” alisema Mwajuma huku naye akionekana kuwa na hasira sana kwani mafanikio ambayo angeyapata rafiki yake yangekuwa sawa na mafanikio yake.



    Cassian aliamshwa na alamu ya simu yake, haraka sana akashtuka kutoka usingizini, mwili wake ulikuwa umechoka kwani usiku uliopita alichelewa kulala kutokana na kwenda baa kunywa huku akiwa na rafiki yake, Osman.

    Akaanza kuangalia huku na kule, hakuwa sawa, akayapeleka macho yake katika saa yake ya ukutani ambayo ilimuonyesha kwamba tayari ilikuwa ni saa 12:00. Akapeleka mkono wake pembeni kwa lengo la kumgusa mpenzi wake, Evelyne, alikuwa amesahau kile kilichotokea usiku uliopita, alipomkosa, kumbukumbu zake zikamjia kwamba aliachana na msichana huyo.

    Hapo ndipo mawazo juu ya Evelyne yalipoanza kurudi kichwani mwake. Alijiona shujaa, alifanya kitu ambacho kwa wanaume wengine wasingeweza kufanya, alipoteza muda wake, alilia kwa kuwa aliumia sana lakini baadaye, kila kitu kilichokuwa kimetokea hakikuwa kama kile alichokuwa amekifikiria.

    Wakati akiwaza hayo, picha ya msichana mmoja ikaja kichwani mwake, hakuwa msichana mwingine zaidi na Naseku. Alimkumbuka binti huyo wa kimasai, jinsi alivyokuwa mrembo, umbo matata ambalo lilitosha kumfanya mwanaume yeyote duniani kuwa kwenye mhemko mkubwa.

    Akatoa tabasamu, kwa jinsi alivyokuwa, alihisi kabisa kwamba msichana huyo alistahili kuwa mke wake, alikuwa msichana masikini, aliyetafuta maisha kwa kuwa mhudumu katika mgahawa uliokuwa Kinondoni, hakutaka kujali kwa kuwa alikuwa na pesa, aliamini kwamba angeweza kumbadilisha na kuwa na muonekano mzuri kama ilivyokuwa kwa Kim Kardashian.

    Hakuwa amezoeana naye, ila aliamini kwamba kama angemtumia rafiki yake, Osman ingekuwa rahisi kuonana na msichana huyo kisha kuzungumza naye. Hapohapo pasipo kuchelewa akaichukua simu yake na kumpigia rafiki yake huyo.

    “Vipi mzee mzima?” ilisikika sauti ya Osman kwenye simu.

    “Poa tu! Una nafasi leo?” aliuliza Cassian.

    “Yeah! Hasa kwa mtu kama wewe ukiuliza hivyo! Kuna ishu?” aliuliza Osman.

    “Ndiyo! Nataka unipeleke kwa yule msichana!”

    “Msichana gani?”

    “Naseku!”

    “Duh! Mpaka jina lake umelikariri! Wewe noma!”

    “Hahaha! Itawezekana?”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Haina shida!”

    Huyo ndiye mtu aliyekuwa akimfikiria muda huo, taswira ya Naseku ilipomjia kichwani, ilimkaa vilivyo. Alitabasamu na muda mwingine kutoa kicheko cha chini. Aliamini kwamba kama angezungumza na msichana huyo basi angeweza kukubaliana naye na kuwa mpenzi wake.

    Akajiandaa, alipomaliza, akaondoka zake kuelekea ofisini. Njiani, alikuwa akiangalia huku na kule, kila alipowaangalia watu aliokuwa akipishana nao, moyo wake ulikuwa na furaha kwani alihisi kila mtu aliyekuwa akimwangalia alijua kilichokuwa kimetokea kati yake na msichana aliyetokea kumchukia mno, Evelyne.

    “Bosi! Karibu sana,” alimkaribisha sekretari wake huku akiwa na tabasamu pana.

    “Ahsante sana!”

    “Na leo kumbe unakuja kazini!”

    “Kwa nini nisije sasa?”

    “Si unakwenda kwenye harusi!”

    “Harusi gani?”

    “Jamani! Yaani umesahau?”

    Cassian hakujibu kitu zaidi ya kutoa tabasamu na kuingia ofisini kwake. Moyo wake ulikuwa na furaha tele, alijisikia amani kuliko siku nyingine. Alijua kwamba Evelyne alichanganyikiwa lakini hilo hakutaka kujali.

    Kila mfanyakazi alishangaa, wengi waliamini kwamba siku hiyo ilikuwa ni siku ya harusi ya bosi wao. Wanakamati walikamilisha ripoti yao, wakatengeneza ratiba lakini kilichowashtua ni kumuona bosi wao akiwa ofisini, ilikuwaje awe mahali hapo na wakati siku hiyo ilikuwa ni ya kufunga ndoa na Evelyne.

    Kila mmoja alikuwa na maswali mengi, alilijua hilo, alichokifanya ni kutoka na kuanza kuzungumza nao. Aliwaambia kwamba hakukuwa na harusi, aliahirisha kila kitu baada ya msichana yule kumdanganya.

    “Alikudangany? Kivipi?” aliuliza mfanyakazi mmoja.

    “Alinifanya nijue sina nguvu ya kumpa msichana mimba!”

    “Kumbe unazo?”

    “Tena nyingi! Naweza kujaza hata mbuga ya wanyama!” alisema Cassian na wote kucheka kwa sauti.

    Huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa kuvujisha kile kilichokuwa kimetokea. Kila mfanyakazi aliyeipata, akachukua picha ya Evelyne na kuiweka mtandaoni, kama alivyokuwa ametamba sana katika mitandao ya kijamii ndiyo hiyohiyo iliyotumika kumchafua.

    Waandishi wa habari hawakuwa mbali, baada ya kuipata taarifa hiyo, kitu cha kwanza kilikuwa ni kumpigia simu Evelyne, simu yake iliita bila kupokelewa mpaka pale ilipozima.

    Mitandaoni kila sehemu stori kubwa ilikuwa ni kuachwa kwa msichana Evelyne, wengi walimsikitikia kwa kuona kama kile kilichotokea alikuwa ameonewa huku lawama zao nyingi zikiwa kwa Cassian ambaye alikuwa akiheshimika kila kona nchini Tanzania.

    Baada ya kuwekwa sababu ya watu hao kutokufunga ndoa, kila mmoja akabadilisha moyo wake na kuanza kumchukia msichana huyo. Posti mbalimbali zikawekwa katika mitandao ya kijamii wakikilaani kitendo alichokifanya msichana huyo, wengine walimdhihaki, wengine walimcheka kwa kumwambia kwamba mbwembwe zote alizokuwa amezifanya mitandaoni kumbe hakuwa na uwezo wa kushika mimba.

    “Halo halo! Mwanamke mtu mzima hata aibu hana,” alisema msichana mmoja aliyekuwa saluni akisukwa, mkononi alikuwa na simu yake ya Tecno, muda wote alikuwa akicheka tu.

    Tanzania nzima ikajua kilichokuwa kimetokea, mbwembwe zote zikaisha na hakukuwa na harusi tena. Wale waliokuwa wamejiandaa, wakapewa taarifa kwamba kitu kama hicho kisingekuwepo tena.

    “Mwajuma! Nitamuua Cassian! Nitamuua Cassian,” alisema Evelyne huku akionekana kuumia mno, kilichokuwa kikiendelea katika mitandao ya kijamii kilimuuma kupita kawaida.

    Wakati yeye akihuzunika na kulia, upande wa pili Cassian alikuwa na mpango wa kuonana na msichana Naseku. Alihakikisha kwamba ni lazima afanye kila liwezekanalo kumpata msichana huyo.

    Wakakubaliana kuonana na Osman sehemu na baada ya hapo kuanza kuelekea katika mgahawa ule. Hawakuchukua muda mrefu, wakafika huko ambapo macho ya Cassian yalipotua kwa msichana Naseku, moyo wake ukapiga paaa!

    Wakafuata meza moja na kukaa hapo. Macho yake hayakutoka kwa Naseku, alikuwa akimwangalia tu, siku hiyo alionekana kuwa tofauti, alionekana mzuri zaidi ya siku ya kwanza alipomuona mahali hapo.

    Kama kawaida yake ndani alivalia gauni lake refu huku kwa nje akiwa na khanga iliyofubaa. Alimwangalia, kichwani alisuka mabutumabutu, kwa kifupi alionekana msichana mshamba mwenye umasikini mkubwa.

    “Leo nahitaji wali na nyama,” alisema Osman baada ya Naseku kufika mezani hapo.

    “Sawa. Kaka hapo?”

    “Nahitaji kuzungumza na wewe tu!” alisema Cassian na Naseku kuanza kucheka kwani alihisi kama utani fulani.

    “Hahaha!”

    “Naseku! Ninahitaji kuzungumza na wewe!” alisema Cassian huku akimwangalia msichana huyo, mtazamo wake ulibadilika, hakuonekana kuwa na utani hata kidogo kwa kile alichokuwa akikizungumza. Kidogo Naseku naye akatulia.

    “Kuzungumza na mimi?”

    “Ndiyo!”

    “Kuhusu nini?”

    “Usijali! Mimi si mtekaji! Naweza kuzungumza na wewe?” aliuliza Cassian.

    “Mmh!”

    “Dakika kumi tu!”

    “Nyingi sana! Au baada ya kazi!”

    “Haina shida!”

    “Sawa.”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Unatoka saa ngapi?”

    “Saa moja usiku!”

    “Nitakufuata!”

    Hiyo ndiyo ilikuwa shida yake siku hiyo, hakuwa na haja ya kula chakula ila alikuwa tayari kulipia kiasi chochote cha pesa mahali hapo. Alibaki akimwangalia Naseku, msichana huyo mpole alikuwa akitembea kwa mwendo wa taratibu, alionekana kuwa na hofu, alimfahamu Cassian, alikuwa mwanaume mwenye pesa, alipojiangalia yeye, hakujiona kuwa na pesa yoyote ile, sasa kwa nini mwanaume huyo alitaka kuzungumza naye?

    Hakufikiria ishu ya kimapenzi hata mara moja, alijiangalia jinsi alivyokuwa, maisha yake na hata jinsi alivyokuwa akivaa, hakustahili hata kumgusa Cassian si kuwa mpenzi wake tu. Kila alipokuwa akiwahudumia wateja, alipomwangalia Cassian, naye mwanaume huyo alikuwa akimwangalia vilevile.

    Baada ya Osman kumaliza kula, wakaondoka, njiani, Cassian alikuwa na mawazo tele, kichwa chake kilivurugika, mawazo yakamuingia, alikuwa akimfikiria msichana huyo kuliko kitu chochote kile.

    “Ninataka nimuoe Naseku!” alisema Cassian huku akimwangalia Osman.

    “Umuoe Naseku?”

    “Ndiyo!”

    “Mhh!”

    Alimaanisha, aliondoka mpaka nyumbani kwake, alikaa kidogo na kurudi tena kulekule kazini kwa kina Naseku huku saa yake ikimwambia kwamba tayari ilikuwa ni saa 12:26 jioni. Alipofika hapo, akamuulizia msichana huyo na kuambiwa kwamba aliondoka.

    Moyo wake ukamuuma, aliumia kupita kawaida, alihisi kudharauliwa, hakutaka kukubali, kwa jinsi alivyotokea kumpenda msichana huyo, hakuwa radhi kuona akilala pasipo kuzungumza naye. Akauliza alipokuwa akiishi, akaambiwa kwamba ni Tandale Kwa Mkunduge.

    “Ninakwenda sasa hivi!”

    Akaondoka mgahawani hapo mpaka huko. Alipofika, akaulizia na akaelekezwa mahali msichana huyo alipokuwa akiishi. Alipoteremka na kuifuata nyumba hiyo, alipoiona tu akashindwa kuvumilia, machozi yakaanza kumtoka, hakuamini kama msichana aliyekuwa akimpenda kwa moyo wa dhati alikuwa akiishi katika nyumba mbovu kama hiyo.

    Ilikuwa nyumba yenye ukuta uliochoka, bati lenye kutu ambalo lilikuwa na matairi ya gari, kulikuwa na kila aina ya uchafu katika paa la nyumba hiyo, mbali na vyote hivyo, mlango wake ulikuwa mbovu kiasi kwamba kama ungeuegemea tu basi ungeanguka nao mpaka ndani.

    Alibaki nje huku akiwa amesimama tu, hakujua ni kitu gani alitakiwa kufanya kama ni kwenda kugonga au kusubiri mpaka msichana huyo atokea.

    Huku akiwa mahali hapo na mawazo mengi, akamuona msichana akija kule alipokuwa huku akiwa na ndoo ya maji kichwani mwake. Akamwangalia msichana huyo vizuri, hakutaka kujipa maswali mengi kwamba alikuwa nani, alikuwa Naseku.

    “Naseku!!!” aliita huku akianza kumfuata msichana huyo ambaye aligeuka, alipomuona Cassian, akashtuka.

    “Cassian!”

    “Naam!”

    “Umefuata nini?”

    “Nimekufuata wewe!”

    “Umenifuata mimi?”

    “Ndiyo!”

    “Hadi nyumbani?”

    “Ndiyo!”

    “Nani alikwambia ninapoishi!”

    “Kazini kwako! Naweza kukaa nawe sehemu kuongea na wewe?”

    “Hapana! Nataka kwenda kupika. Mama yangu ni mgonjwa, inatakiwa nimpikie!” alisema Naseku huku akimwangalia Cassian.

    “Anaumwa nini?”

    “Ni habari ndefu.”

    “Habari ndefu ambayo haisimuliki?”

    “Cassian! Naomba uondoke. Kaka yangu mkali sana, akikuona hapa, atakushikia panga!” alisema Naseku.

    “Anishikie panga! Mimi?”

    “Cassian! Naomba uondoke. Tutaonana kesho kazini! Nakuomba,” alisema Naseku.

    “Kuondoka siondoki!”

    “Oscar atakukuta!”

    “Acha anikute! Kama kunikata mapanga, bora anikate lakini hapa siondoki! Kama ni treni ishafika Kigoma,” alisema Cassian, hapohapo akaenda kibarazani kwa kina Naseku na kukaa kabisa.

    Naseku hakujiamini, alikuwa akiogopa, alimjua kaka yake, alikuwa mtemi Tandale nzima, alikuwa mtu wa kushika panga, hakupenda kuona mwanaume yeyote akimmendea dada yake, alijua wanaume wengi walikuwa wadanganyifu.

    Aliwakata mapanga wanaume wengi, walimuogopa na kumuona Naseku kama ukoma, hakukuwa na mtu aliyemsogelea. Naseku alimwambia hilo Cassian lakini hakutaka kujali, hakutaka kusikia kitu chochote kile, kwake alichokuwa akikitaka ni kuzungumza na msichana huyo tu.

    Wakati Naseku akiwa amepeleka ndoo ya maji ndani, mara Oscar akaanza kuonekana kwa mbali, kama kawaida yake alikuwa akija kwa kasi ya ajabu, alikwishatoa onyo kwamba hakutaka kumuona mwanaume yeyote nyumbani kwao, kitendo cha kumuona Cassian alijua kabisa alifika nyumbani hapo kwa ajili ya dada yake tu.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Alipomfikia Cassian, hakutaka kuuliza alikuwa nani, akalipandisha shati lake, akatoa panga. Watu wote waliokuwa wakimuona wakajua kabisa kwamba Oscar hakuwa akitania, hakuwa na historia ya kurudisha panga pasipo kufanya kazi.

    Cassian alibaki akimwangalia mwanaume huyo aliyeonekana kuvimba kwa hasira. Hapohapo akamrushia Cassian panga, bila kukwepa lilikuwa likimpiga kichwani.

    “Umekwepa! Unajiona ninja!” alisema Oscar na kuanza kumsogelea tena, kitendo cha Cassian kukwepa panga lake ilionekana kuwa kama dharau kwani tangu awe mtemi wa mtaa, hakukuwa na mtu aliyewahi kulikwepa panga hilo.



    ITAENDELEA



0 comments:

Post a Comment

Blog