Search This Blog

Friday, July 15, 2022

NDOTO ZA KIPEPEO - 2

 







    Simulizi : Ndoto Za Kipepeo

    Sehemu Ya Pili (2)

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Baada ya kuachwa huru, kesho yake Maua kabla ya mawio alijidamka kuelekea bustanini. Baada ya kufika huko alikuta hali ambayo ilimvunja moyo. Mazao yaliyokuwemo bustanini yalikuwa si mazao tena, yote yaliliwa na mifugo na kuvurugwa vibaya. Maua chozi lilimtoka kwani alikuwa akiitegemea bustani yake kumhudumia. Hakuwa na namna zaidi ya kuelekea kwa mjumbe asubuhi ile kwenda kutoa taarifa. Alipofika alimkuta mjumbe naye alimsikiliza.



    “Unataka nikusaidie nini Maua?” mjumbe alihoji.

    “Dharau za kijiji hiki nishazichoka. Unaniitaje Maua kama mtoto wa shule? Mimi ni mama nastahili kupewa heshima ya kuwa mama,” Maua alilalamika.



    “Ondoa wazimu hapa. Wewe ni mama wa nani? Mama wa marehemu si mama. Tutajuaje, yawezekana hata huyo mfu ulimkwapua kwa wenyewe ukamhadaa mmeo. Hufai kuitwa mama kwani mwanao ni mfu. Wewe ni Maua, basi!” alisema mjumbe kwa kejeli.



    “Mjumbe, hayo tuyaache. Niiteni vyovyote iwavyo lakini Mungu anajua. Shauri langu ni hilo, bustani yangu kama nilivyokueleza. Si mchicha, mhindi wala mnyanya, vyote wamegeuza malisho. Nataka mhusika akamatwe na anilipe,” alieleza Maua.



    “Unamjua ng’ombe au mbuzi aliyekula mazao yako?” alihoji mjumbe.



    “Kumjuaje huyo ng’ombe au mbuzi? Namjua mfugaji kijijini hapa ni mmoja tu. Ni Malecha peke yake!” alieleza Maua.



    “Hivyo Malecha ndiye amechunga kwenye bustani yako?” aliuliza mjumbe.



    “Ndiyo!” alijibu.



    “Usiwe mpumbavu Maua. Kati ya ng’ombe na mfugaji, nani kala mazao yako?” mjumbe aliuliza.



    “Ng’ombe! Lakini mchungaji ndiye alimpeleka,” alijibu Maua.



    “Maua usiwe mjinga kama alivyokuwa mmeo. Jibu sahihi ni la kwanza kwamba, ng’ombe ndiye kala mazao yako. Sasa unataka Malecha ashitakiwe ili iwe nini? Kula ale ng’ombe mashitaka ashitakiwe Malecha. Naona shauri lako halifai hata kufikishwa kwa mjumbe. Tena hata karani wa baraza hapaswi kujuzwa hili. Ili kuupata ukweli, italazimika mashahidi wa kueleza ilivyokuwa. Hao ng’ombe nani atawasikiliza? Mchungaji atasema walikula ng’ombe, sasa ng’ombe watajiteteaje?” Alijibu mjumbe kwa maelezo marefu.



    “Mjumbe, haki yangu Mola atailipa. Kama kweli nililima na kuihudumia bustani kwa jasho, nitalipwa. Yeyote aliyetia mguu bustanini kwangu na kuchunga, moto utawaka juu yake,” alieleza Maua kwa huzuni.



    “Laana za mnazi hazimpati mkwezi maana hata mwezi humcheka. Wewe ongea vizuri na watu uvalishwe viatu Maua. Utaishije kama mchawi peke yako bila tulizo la bwana? Ee mama! Nifae kwa jua nami nikufae kwa mvua. Kama jua hutawala mchana basi mwezi nao utawale usiku. Mzee kwa mzee wakiwa, wakiungana upweke huushinda,” mjumbe alisema. Maua alikuwa akimsikiliza na kumtazama mjumbe usoni kwa makini. Wakati huo mjumbe alimpelekea mkono kiunoni kumtekenya. Maua aling’aka na kunyanyuka kuondoka. Hasira zilimjaa akaenda kama mtu aliyefumwa na jini makata.



    Akiwa njiani, Maua hakusema na mtu zaidi ya kuongea na nafsi yake. Alipofika nyumbani, kwenye mti wa mzambarau uliokuwa pembeni ya nyumba yake palikuwa na watoto. Mmoja alikuwa juu akitikisa zambarau na wengine walikuwa chini wakiokota.



    Maua baada ya kuwaona alisimama na kuyaangaza macho yake mtini. Aliwakemea na kuwataka waondoke. Walikaidi kuondoka ndipo Maua alipoamua kwenda hadi kwenye uchanja wa kuni na kuchomoa ukuni mwembamba akitaka kuwatisha ili waondoke. Hamadi! Mtoto aliyekuwa juu ya mzambarau alimwona Maua akiwa na fimbo mkononi, alitaharuki. Alianza kuteremka haraka. Kwa kuwa jasho lilimtoka kutokana na hofu, aliteleza na kuporomoka. Alijigonga kwenye matawi hadi kuifikia ardhi. Puuu! Alitua chini na kutulia kimya. Damu zilianza kumtoka puani na mdomoni. Watoto wenzake baada ya kuona hivyo walitimka mbio kwenda kwa wazazi wao. Maua alibaki kaduwaa. Baada ya sekunde chache akiwa kapigwa butwaa, Maua alipiga hatua kumsogelea mtoto na kutaka kumnyanyua.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    “Mwananguuuuu! Kafanyaje mwanangu!” Siahi ilimgutua Maua. Alivyogeuza kichwa chake, ana kwa ana alikutana na Koi aliyeongozana na mkewe. Hapo vikawa vilio wakipokezana hadi wanakijiji walizisikia kelele zilizojaa kilio. Walikusanyika na kumshuhudia mtoto akiwa kanyooka na kujawa damu puani na mdomoni. Walijaribu kumzoazoa, lakini waligundua kuwa alikuwa tayari ameagana na dunia. Maua alikuwa bado kaduwaa, chozi lilikuwa likimiminika kama ng’ombe.



    “Huyu mama ni mchawi! Maua ni mchawi na kijiji hiki atatumaliza,” alifoka Koi wakati akimzoazoa mtoto wake. Alikuwa mwanaye wa kwanza wa kiume kwa mkewe ambaye aliozeshwa na babaye. Mtoto wake wa pili alikuwa msichana ambaye umri wake ulikuwa bado wa kubebwa mgongoni mbali na kutambaa. Tukio hilo lilizalisha minong’ono mingi. Kijiji kizima kilirusha mzigo wa lawama kwa Maua kuwa yeye ndiye alisababisha kifo cha mtoto yule. Walimlaumu na kumjuza kuwa, asingeokota ukuni kuwafukuza watoto, kifo hicho kisingeweza kutokea. Kwa fikra za wanakijiji ilimpasa Maua kuhukumiwa.



    ****

    Minong’ono ya kutuhumiwa kwa Maua ililifikia baraza la kijiji. Maua alihojiwa kama mtoto mdogo katikati ya wanaume wengi. Kila alipojaribu kujitetea alinyamazishwa. Katikati ya kikao kile kabla ya maamuzi kutolewa, Huruma alifika barazani akiwa mbio.



    “Baba, ng’ombe wanakufa, wanakufa!” alisema Huruma. Wakati huo alikuwa kamfikia baba yake. alimweleza kuwa, baada ya ng’ombe kutoka machungani mchana ule, baada ya kunywa maji watano walianguka palepale na kutoa kelele nyingi. Kila mmoja alitoa kelele na kunyamaza kisha tumbo lake liliumuka na kuwa kubwa kama kichuguu. Matumbo yalijaa na kuwa kama yalijazwa upepo na kuwafanya miguu ielee hewani wangali wamelala chini. Malecha alistaajabu. Kwa kuwa aliketi karibu na mjumbe, aliaga kutaka kwenda kushuhudia. Mjumbe alimuuma sikio baada ya kumtoa chemba akimweleza maneno ambayo aliyasema Maua baada ya kwenda kushitaki kuwa bustani yake ilivurugwa na mazao yake yaliliwa na mifugo. Tayari Majaliwa alihisi kuwa ng’ombe wake walipewa sumu na Maua. Alichukua baiskeli na kwenda mbio hadi kwake. Haikumchukua muda mrefu, alirudi akiwa mnyonge. Kikao cha baraza kilikuwa kikiendelea.



    “Kijiji chetu kimekuwa na hamaniko kila siku ijayo usoni. Kila uchwao, kumekuwa na vilio na sononeko. Mambo haya hatukuyazoea enzi na enzi lakini tangu Maua na mmewe wafike hapa kutokea Pwani, kumekuwa na kimbunga. Ndugu zangu, wasiwasi wangu ni kuwa, Maua na mmewe walikuja hapa na pepo wabaya,” alieleza mjumbe. Alimtazama Maua aliyekuwa akiendelea kumwagikwa na machozi.



    “Pamoja na hayo, jana baraza lilimwonya Maua kutotenda kosa ndani ya siku arobaini. Sasa baada ya onyo hilo, leo hii hata jua halijachanua, maafa kayasababisha Maua. Mtoto kwa kijana wetu amefariki tena nyumbani kwa Maua. Kabla hilo halijaisha, taarifa za maafa kwa mifugo ya Malecha imetufikia. Ng’ombe watano wamekufa tena hata saa moja haijapita. Jambo hilo nalo linamhusu Maua ambaye alifika kwangu leo asubuhi na mapema kushitaki. Alisema kuwa, bustani yake imevurugwa na mazao yameliwa na ng’ombe. Wakati nikijaribu kumshauri, hakunisikiliza zaidi ya kula kiapo akisema, aliyetia mguu bustanini atakiona. Kukiona kwenyewe naona ndiyo huku!” Mjumbe alidondoa maneno. Wanakijiji vinywa viliwabaki wazi. Walimtazama Maua kama mtu hatari asiyefaa kutazamwa na kusogelewa.



    “Hatufai mtu huyu. Kijiji hiki kimtende kama atendavyo,” alisema Malecha.



    “Tena auawe, shauku yangu ni kuiona damu yake ikimwagika mikononi mwangu,” alisema Koi. Wanakijiji walijawa simanzi. Nafsi zao ziliwafanya kuamini kuwa, Maua alikuwa mtu mbaya. Walinong’ona na wengine waligumia kwa sauti za kuogofya. Wengine waliokota madongo na vipande vya mawe na kumrushia. Maua hakuwa na jingine, chozi lilimwagika na kuuchafua uso wake. Hakuwa na rafiki kwani alivishwa nishani ya kuwa mchawi aliyekubuhu.



    “Akumulikaye mchana, usiku atakuchoma. Tuchukue hatua japo mapema. Akiendelea kubaki hapa maafa yanaweza kulipuka kila kona ya kijiji chetu,” alisema mjumbe.



    “Tupe mwongozo mjumbe,” alisema Koi.



    “Laana ya mke aliyefiwa mume na mtoto wa kumzaa ni kubwa. Anafaa kung’olewa kama mgomba mbovu shambani. Ukiachwa utaweza kuambukiza miche yote na shamba zima litakuwa halina faida,” alieleza mjumbe. Alimtazama Maua na kutema mate kwa kejeli.



    “Hukumu yake iwe masikioni mwenu wanakijiji. Maua hapaswi kuuawa kwa upanga wala ncha ya mkuki. Anapaswa kusindikizwa hadi tawala ya kijiji kingine. Huko akifikishwa jogoo wa kijiji hiki watafanya yao ili kuagana naye kwa ujasiri. Lazima kumuenzi, wafurahipo jogoo wetu furaha itakirudia kijiji kizima. Anung’unikapo kwa maumivu ibilisi wake na watu wake atawaingia,” alieleza mjumbe.



    “Mali zake je? Mashamba, nyumba, miti na bustani,” alihoji Koi.



    “Kulingana na mila zetu, mali zote zitakuwa chini ya uangalizi wa mjumbe. Atazimiliki kwa mwaka mmoja. Baada ya hapo itakabidhiwa familia ambayo imempoteza mtoto wa kwanza wa kiume,” alieleza mjumbe.



    “Mjumbe, hiyo nyumba itaingiwa na mtu bila kuleta ahamani?” alihoji Koi.



    “Nyumba inapaswa kuchomwa moto pamoja na nguo iliyoligusa jasho la Maua ili moshi wake upate kulisafisha anga la himaya yetu,” alisema mjumbe. Baada ya mjumbe kusema, wanaume walisimama na kuanza kuelekea kwa Maua. Walitangulia wachache na wengine walibaki barazani wakichanganya tope na majivu. Walimkandika Maua usoni na mwilini kama jumba la miti. Walimlowesha kwa maji na nguo zake walizichanachana.



    Maziwa yake yalining’inia yakiwa kama embe mtini, yalibembea. Walimchukua mzobemzobe wangali wakiimba.



    Sikawende mlozi,

    Kinawana kuwaua

    Mlozi awafayetu!

    Nawana kuwalozi

    Sikawende ufe

    Shetwani mloe

    Alafaye mwana!



    Wakati wakiimba walikuwa wakikimbia mchakamchaka. Maua alikuwa mbele katangulia akichechemea na kukimbia kwa shida. Kila baada ya mwendo mfupi kiongozi mmoja alitaja jina la kijana mmoja kumchapa Maua kwa fimbo zilizokuwa zikinesanesa. Kila alipochapwa, Maua alichanika. Kila fimbo ilipoufikia mwili wa Maua, vijana walipiga mbinja kushangilia. Kila mmoja alivyojisikia. Wengine walienda wakikimbia na kumpita wakawa mbele zaidi. Waliimba wakirudi nyumanyuma, wakimfikia walimvuta ziwa lake na kumwachia. Kelele za watu waliofurahia zilikuwa kinywani mwao. Maua alikuwa hoi bin taabani. Hakuwa na hali, machozi yalimkauka. Alinong’ona na Mungu wake katikati ya waonevu, ‘lililojema, roho yangu itwaliwe.’



    Mchakamchaka kutoka kwa mjumbe ulifika kwa Maua. Vijana waliivamia nyumba kama nyuki. Waliingia ndani wakavitoa vitu vyote nje mbele ya hadhara. Maua walimwanika, hawakumbakizia siri kwani hata vibwende vya Maua alivyovihifadhi kwa matumizi yake vilielea kwa hadhara. Walivipekua vibwende kimoja baada ya kingine bila kificho wakimrushia usoni. Vilindo vya unga na mboga za kukaushwa vyote walivimwaga. Hatimaye vijana walikiendea kijinga cha moto na kuilipua nyumba. Iliwaka moto na kuteketea mbele ya macho ya wanakijiji ambao walikuwa wakimtazama Maua kwa dharau.



    Furushi la nguo chache, kuukuu alirushiwa baada ya kuwa zimetiwa kwenye gunia la mkonge. Aliliokota na kulinyanyua akiwa kashikwa na fadhaa. Hakuwa na msaada. Japo walikuwepo waliotaka kumsaidia, nafsi zao walizipa onyo kwani nao wangeweza kuunganishwa katika vurugu zile. Nyumba ya Maua na jiko vilikukuwa jivu. Walimchukua Maua moja kwa moja kuifuata njia iliyokuwa ikielekea kwenye mto Kisare ambao ni mpaka na kijiji cha Amani, njia panda ya Tuamoyo. Muda huo msafara ulifika karibu na shule ambapo Carolina alikuwa akisoma. Watu wengi walimiminika kushuhudia. Katikati ya kundi kubwa, Carolina pia alimwona mwanamke huyo akisulubiwa. Aliingiwa huruma japo hakuweza kumtambua kwa jinsi alivyokuwa kabadilika baada ya kukandikwa tope na majivu. Hali yake ilikuwa mbaya, Carolina ilimkaa akilini!



    Ulikuwa mwendo mrefu hadi kuufikia mpaka ambapo Maua alipaswa kwenda. Huko walibaki wanaume wachache hasa vijana. Wazee hawakuuweza mwendo mrefu, waliishia njiani. Vijana walimbeba Maua juujuu na wakati walipumzika. Walimfanyia kadri ya agizo la mjumbe kuwa walipaswa kumfurahia ili furaha irudi kijijini kuutoa msiba. Maua alifanyiwa hila na walimfanya mke kinyume na matakwa yake. Pamoja na uchovu, maumivu yalikuwa juu yake. Alitelekezwa kwenye ukingo wa mto na hapo alianza kuyakusanya maisha yake. Hakuwa na mjomba wala shangazi wa kumtetea. Alibaki peke yake. Aliikumbuka historia ya familia yake aliyoianzisha na Majaliwa tangu Pwani na hatimaye kuoana kwa furaha.



    Hakuacha pia kujiwa na kumbukumbu mbaya za mateso ndani ya ndoa hatimaye kupotea kwa mmewe na kifo cha binti yake. Aliumia!



    Safari ya Maua ilijaa mashaka njiani. Aliyemuumba alimchukua kutoka pale watu wa Hamaniko walimtelekeza. Alijikokota kama gari bovu. Kila alipopiga hatua kuelekea asikokujua nguvu zilimwisha naye aliamua kupumzika. Kuumaliza msitu uliofuata baada ya mto ule mkubwa lilikuwa jambo gumu. Kwa kiu na njaa aliyokuwa nayo asingefaulu. Fika alijua siku yake ya mwisho ilifika.



    Wakati akihangaika, usiku uliingia. Hakutaka kwenda mahali zaidi ya kujibanza alipoona pangemitiri. Mawio ya iku iliyofuata alikazana kutembea kwa tumaini kuelekea kule alihisi kungekuwa salama yake. Safari kwa miguu yake iliyolegea iliishia kwenye njia ambyo alijua fika ilikuwa ikiwapitisha watu kwenda na kutoka masafa ya mbali kuviunganisha vijiji vingi vilivyokuwa mbalimbali. Hapo alifika kwenye mti mmoja mkubwa akaketi zingali nguvu zilimwisha. Alichutama na kujiinamia. Alizikumbuka nyimbo zote za majonzi alizokuwa akizisikia tangu Pwani hadi alipohamia Hamaniko. Maua katikati ya fikra na kumbukumbu hizo alijiwa na wimbo akaanza kuuimba:CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    Tamati Rabi natua

    Mola fanya asadi

    Nijibishe lenye sura

    Gharika asinikumbe

    Utu watu kutu

    Wamejaa hiana

    Yangu hali naweka

    Kwako usinitupe

    Niokoe mja wako

    Pitisha yako rehema.



    Malimwengu hamaniko

    Laana waondolee

    walipe kwa pepo

    Wapatie jamala

    Sihukumu kwa upanga

    Wapatie ahua



    Palipo inkisari

    Pafanye shwari

    Tuma wako hua

    Anitwae malishoni

    Furaha inikae

    Moyo utuame

    Niokoe!



    Maua aliuimba wimbo mara nyingi akiurudiarudia wakati kichwa chake kikienda na kurudi upande upande. Hatimaye nguvu zilimwisho kwa sababu ya maumivu, kiu na njaa kali. Alitulia na kujilaza kama mzoga.



    Majira yale ya jua lilianza kupanda, kulikuwa na wafanya biashara za masafa walikuwa wakipita na punda wao kuipita njia ile. Ilivyo bahati kwake, baba mmoja aliyepita karibu na eneo hilo alimwona. Alisimama na kumsogelea. Alimwendea na kumnyanyua akiwa hajiwezi. Kwa kuwa alikuwa na nguvu, mwanaume yule alimbeba na kumweka kwenye kwama lililokokotwa na punda. Moja kwa moja aliwatimua punda wake mbio hadi kulivuka daraja la miti kuuvuka mto mkubwa hatimaye kukiingia kijiji cha Tuamoyo. Alipofika nyumbani kwake, mwanaume yule alimtaka mkewe kumhudumu Maua ili hali yake iwe ya mtu wa kawaida. Ukarimu ulimfanya Maua kuhudumiwa kwa kila hali, tangia majeraha hadi chakula na mahali pa kuishi. Familia ile ilimpenda na Tuamoyo pakamkaribisha kwa bashasha.



    _______Baada ya miaka 6_____



    Wakati Maua akitimiza miaka sita ya furaha kijijini Tuamoyo, Carolina mambo yalianza kuchacha. Akiwa na miaka 13, jina la Chausiku lilififia na kusahaulika. Chausiku lilimezwa na jina ambalo mwalimu wake alikuwa akilitumia. Walimu na wanafunzi walimuita naye kuitika kwa jina hilo alilolipenda. Chausiku aliyejibatiza Carolina maisha ya shule yalimhamisha na kumfanya maarufu shule nzima. Alikuwa na bidii darasani na mwenye kumheshimu kila mmoja aliyekuwa mbele yake.



    Wakati akiendelea na masomo ya shule ya msingi, alikuwa nyota isiyoweza kuzimwa. Si kwa tamaa, choyo wala huba, kwake alisimama imara kwa tabia njema kujilinda. Alikuwa na akili nyingi darasani. Sauti yake kama chiriku ilimpamba na kumfanya malkia wa sauti shuleni. Kila aliposikika akizungumza waliomsikia walitamani aendelee kuongea. Alikuwa kinanda. Aliposhiriki katika mashindano ya UMITASHUMTA, kwaya yao ilishinda kwaya zote zilizoshiriki. Hakika wengine wote hawakufua dafu.



    Uhalali wa jina lake alikolezwa kwa ubatizo wa maji kadri ya imani yake ilivyomtuma. Carolina lilikuwa jina lake alilojivunia na kujiimarisha nalo. Binti wa Lola hakujaliwa sura pekee, Maulana alimtunuku mwili ulio na mvuto. Umbo lake lilikuwa la kuvutia. Alifanana kwa umbo na namba nane iliyosimama. Kiuno chake kilikuwa kama dondola na makalio yalijaa ambapo kila nguo aliiyoivaa ilimkaa kumsitiri. Hata kama alivaa nguo ronya, zenye kuchukiza wengine na kuwafanya manungayembe, kwake alionekana ni malkia mbele ya hekalu la mfalme. Ngozi yake ilikuwa mororo laini kama mgongo wa chupa. Mahulutu umbo lake, mvuto wake wa hamu, kiu kwa wana kuizidisha, hamu yao kumchuuza iliongezeka kila walipomtupia jicho. Alikuwa mrembo. Hakutumia vipodozi kuuchuna mwili wake, bali mafuta ya mgando kwake yalimtosha. Sabuni yake ilikuwa komesha, ilimfanya mwili kuulinda. Hakuwa na tamaa ya nikwata, kiguu kwenda na jua kali kwa uroho, yeye alisimama jadidi kuilinda yake saada. Carolina hakumfahamu mwanamume, yake shime ilikuwa madaftari na kazi nyingi za shamba. Alikuwa mshamba wa shamba, tamaa hakuweza kujitwalia. Kila jambo la heri, muda alilipatia. Kisomo kilimnanga na kumfanya mateka wake. Hakupuuza kuuliza, lengo lake kueleweshwa. Siku moja kwa shauku, niaye jazanda hakulitaka, mwalimuwe wa sayansi somo alilifundisha. Kwa ujinga hakunyamaa, kauli yake ilimlea, kwa swali kama mkunga, lilimtoka kwa sauti.



    “Kiungo hiki cha uzazi, mwanaume twamsemea, kinamfupa ama sponji, nieleze nielimike?” Mwalimuwe hakunyamaa, alimjibu kwa ustadi. Kwake alielewa, pasi shaka alifaulu. Wenzake macho ya koroboi, mbavu zao ziliwapasuka. Kwa tekenyo la ulizo lake walimwita mshamba kwa kejeli. Iweje awe kipepeo bubu, katikati ya bahari ya elimu? Kweli asouliza jambo, halijui ajifunzalo. Carolina hofu hakuishiba, ilikuwa haramu kwake.

    Carolina njema yake tabia, ilimfanya waridi shule nzima. Wengine kwa mikogo, wavulana walimmendea. Mate yaliwamiminika, wakihitaji kuonja asali. Mlinzi wake hakuwepo, pekee alijibeba. Alikuwa mwenye bidii ya kazi, mchwa hakufua dafu. Tunu ya uongozi ilimvaa kila hatua alipokuwa shuleni. Sauti yake ilimfanya mteule kwa kila shindano la kuimba. Kwaya ilimpandisha, kileleni na kumsimika, malkia wa Hamaniko.



    Carolina hakuwa bora tu mshindi, bali mshindi bora katika mashindano ya taifa. Mafanikio hayo yote yalikuwa ni kwa sababu ya sauti yake iliyoweza kumsisimua kiziwi na kufanya aelewe alichokiimba na kukisema. Ingekuwaje leo? Sauti yake Carolina ingemtajirisha maradufu. Angejijengea majumba ya kifahari na pengine angemiliki magari na kutukuka kote ulimwenguni. Kama angeimba muziki, hakika usingemkataa. Sura yake runingani, ingesawiri ustawi wake. Hata kama angeimba taarabu, sauti yake ingekonga nyoyo za wengi na kuwafanya wanaume wenye uchu wa kuyafisadi maisha ya warembo, wamtafute kwa kuzipoza njaa zao.



    Ingawaje wahenga walisema, Mola hamtupi mja wake, Carolina alitelekezwa. Hakuwa mbumbumbu wala mbongompozeni, lakini matokeo ya darasa la saba yalimsaliti. Hakuchaguliwa kuendelea na kidato cha kwanza. Ilionesha hakuwa na bahati ya maisha ya elimu. Jambo hili liliiumiza sana nafsi yake. Kila alipokumbuka kuikosa nafasi hiyo, alibubujikwa na machozi kwa uchungu uliomtafuna akiihurumia nafsi yake. Alipenda kusoma, naye hakutaka kushindwa.



    Katika familia aliyolelewa walikuwa ni wafugaji wa ng’ombe. Familia hiyo kwa kadirio la karibu walikuwa na ng’ombe wasiopungua mia mbili. Kila rangi na kila aina ya ng’ombe walifugwa. Alikuwa akijihesabu ni mzaliwa pacha wa familia hiyo. Alijua hata kama angeamua kusoma katika shule za watu binafsi angeweza kufanya hivyo kwani mali ilikuwepo. Kwa kuwa alifahamu abu yake ni Malecha, mwenye mifugo isiyohesabika ilibidi amvae jioni moja. Alikusudia kumweleza nia thabiti ya moyo wake. Niaye ni kusoma kuufukuza ujinga.



    *****



    “Majaliwa, pole sana kwa yaliyokusibu. Pamoja na pole nikupayo yapasa nikupongeze. Umekuwa mtu mwema na jasiri tangu vijana wangu wakulete hapa. Sehemu hii ni ya amani na haina vurugu za aina yoyote. Yaliyokupata hata siku niliyokuona ukifikishwa mbele yangu, nilijua hutapona na ungefikwa na umauti,” alieleza mzee Ganda. Alikikupua kiko chake na kuuruhusu moshi kuutoroka mdomo. Nywele zake zilikuwa ndefu, zilisimama kama mkia wa tausi. Alikuwa akikamua maji ya majani yaliyopondwapondwa na kuyajaza kwenye gofu lililokuwa jumba la konokono. Alichukua ungaunga wa rangi ya kahawia akaumiminia ndani ya gofu. Alianza kuukoroga unga kwa kutumia kijiti ukachangamana na majimaji yale ya kijani. Hakuacha kukoroga mpaka ungaunga ukayameza maji ya majani na kuwa kama uji mzito wa chapati za kumimina.



    “Mzee Ganda, napaswa kukushukuru wewe. Bila kuwalea vijana wako katika maadili mema, wasingeweza kunifikisha hapa kwako. Hata kama wangenifikisha, bado pia ungeweza kukataa kunipokea na kunitunza kama hivi ufanyavyo. Umenipatia tiba kwa muda mrefu sana. Miaka yote umehangaika namimi hata senti sijawahi kukulipa. Nakula, kunywa na kulala bure, ni nadra sana kukarimiwa na yeyote duniani hapa. Kweli hapa ni Amani. Asante sana,” Majaliwa alishukuru.



    “Hupaswi kunishukuru Majaliwa. Hii ni kama jina lako, ni majaliwa ya Muumba. Hebu egama kwenye kitanda chetu nikuwekee dawa,” alisema Ganda. Majaliwa alinyanyuka kwa kujikokota akiuvuta mguu wake mmoja kwa shida. Mkono mmoja nao ulimpa shida.



    “Yalah! Mola niponye,” alisema Majaliwa.



    “Ameshakuponya. Kabla hujataja ombi lako kwake tayari Mola ameshasikia na kutenda. Hadi hapa ushapona. Si kama ilivyokuwa awali,” alieleza mzee Ganda. Majaliwa alikuwa tayari kalala na kuegama kwenye kitanda. Kilitengenezwa kama uchanja wa kuanikia vyombo ila tu kilitiwa nyasi na juu yake kulitandikwa gunia la mkonge. Juu yake pia palikuwa na blanketi lililokuwa limechokachoka. Mzee Ganda alisimama akamshika paji la uso kwa mkono wa kushoto. Mkono wa kulia alikomba ule uji kutoka kwenye gofu la konokono na kuupachika kwenye jicho la kulia la Majaliwa.



    “Yalah! Umenitia pilipili leo?” alilalama na kuuliza Majaliwa.



    “Si’ pilipili wala mshubiri. Naona sasa tiba yetu inaelekea ukingoni. Masharti ya dawa hii, ukimtibu mgonjwa asihisi chochote baada ya kuitumia ujue bado ugonjwa wake umemkalia vibaya. Lakini ukimsikia anaugulia kwa maumivu, jua atakuwa akielekea kupana afueni. Hivyo, umepona,” alisema mzee Ganda.



    “Ahsante. Heri nipone, ingawa jicho nimelipoteza sijapoteza uhai,” alisema Majaliwa kwa huzuni.



    “Waliosema heri chongo kuliko jicho bovu hawakukosea. Nimetumia kila aina ya uganga wangu kuyanusuru macho yako yote mawili, lakini imeshindikana. Hili limegoma kabisa. Kwa hili moja litakufaa. Hata gari bovu huwa japo na taa moja. Chongo utaizoea na mwanga utauona,” alisema Ganda.



    “Nimeshapata ubini tayari. Kwa mazoea ya kwetu, mtu mlemavu jina lake hufuatwa na kasoro aliyonayo. Ubini wake husahaulika bali kasoro ndiyo huchukua nafasi. Utasikia tu wakiniita; Majaliwa chongo! Majaliwa jicho moja! Majaliwa taa moja! Potelea mbali, kilema si ugonjwa,” alieleza Majaliwa wakati akinyanyuka baada ya kutiwa dawa jichoni. Kiganja chake kimoja alikipachika kulifunika jicho.



    “Mzee Ganda, nakosa maneno ya kueleza. Wema wako umezidi kiasi. Pia napenda leo tuzungumze kwa kina maana siku zote kila nikitaka kusema huwa unanikata kauli na kusema bado naumwa ningoje siku nikipona. Si busara kukaa na mtu usiyemfahamu shina wala mzizi wake. Niruhusu nami nikujuze, unifahamu japo zaidi ya jina,” aliomba Majaliwa.



    “Ondoa shaka Majaliwa. Leo utanihadithia mwanzo mwisho. Wakati tukienda kwa mazoezi ya mguu wako na mkono bila shaka tutapata wasaa wa kukaa kitako tuzungumze,” alieleza Ganda. Majaliwa alibaki kuugulia na baada ya muda maumivu ya dawa yaliisha. Hali yake ilikuwa ya kupendeza japo alikuwa bado akihangaika kuikusanya afya yake iliyokuwa vipandevipande.



    *****CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Jua halikugoma kutua. Hatimaye jioni iliingia na upepo wa baridi uliambaa kote na kukifunika kijiji cha Amani. Hali hiyo iliwaruhusu mzee Ganda na Majaliwa kutoka wakielekea matembezini ili kukamilisha siku kwa mazoezi. Hali ya vilima na mito iliyozunguka kijiji hicho ilitosha kuzalisha hali ya hewa ya kuvutia na kila neema kwa wakazi wa kijiji kile.



    Baada ya kuiona hali imetulia, Majaliwa na mzee Ganda waliongozana. Majaliwa aliushika mkongojo maalumu kwa ajili ya mazoezi wakati Ganda yeye alikuwa na fimbo ndefu ambayo upande mmoja ilikuwa na mkuki. Majaliwa alitangulizwa mbele. Walitembea taratibu kadri ya mazingira yalivyo waruhusu. Iliwachukua kama saa zima wakiwa wanafanya matembezi.



    Safari yao iliwapeleka na kuwafikisha hadi kwenye eneo lililokuwa na majabali makubwa, eneo lisilo na uoto wa aina yoyote. Majabali yalikuwa yamesimama kama viti ndipo nao walivutika hadi kuyafikia. Waliyafikia na kuketi kitako wakaanza kusogoa kama ahadi yao.



    “Naona sasa umekuwa imara. Umetembea umbali ambao hapo awali sikutegemea kama ungeweza. Mguu sasa naona umekaza na mkono taratibu unaendelea vema. Kwa jicho tupo mwishomwisho kulitibu jeraha. Sasa unaweza kufanya mazoezi hata peke yako bila hofu,” alieleza mzee Ganda.



    “Namshukuru Mungu nawewe pia uzipokee,” alijibu Majaliwa.



    “Miaka mingi sasa imepita, hatujuani kwa undani. Unaweza kunieleza unachokikumbuka?,” alisema mzee Ganda.



    “Kama nilivyoeleza mara baada ya kuzinduka nikiwa mikononi mwa ukoo wako, naitwa Majaliwa bin Kisenhi. Ni mzaliwa wa pwani. Nilifika ukanda wa bara miongo kadhaa iliyopita kama sehemu ya utafutaji riziki. Mara baada ya kuwa nimepata mchumba nilifunga ndoa na Maua ambaye hadi nafikwa na haya, ndiye mke wangu. Tangu hapo tuliishi kwa raha isiyo kifani japo tulichelewa kupata mtoto. Tulimpata mtoto baada ya miaka mingi. Binti yetu wa kwanza ni Lola ambaye hadi kipindi napatwa na hamaniko alikuwa akingoja majibu baada ya kuhitimu shule ya msingi. Kwa kifupi, kilitokea kisa ambacho kilisababisha pengine hadi leo hii niwe hapa napengine ningekuwa nimeacha jina tu. Binti yangu Lola alikutwa na ubaya, alibakwa usiku wa mkesha wa Noeli moja. Kulingana na maadili ya kila tawala, Hamaniko waliliamua jambo hili kwa hila. Niliamuliwa kulipa haka ili kuendelea kuishi kijijini pale. Nilipaswa kulipa fahali kwa kuwa sikumtunza binti yangu hadi akapatwa na mabaya yale,” alieleza Majaliwa. Mzee Ganda alikuwa akimsikiliza kwa makini. Majaliwa alieleza yote aliyoyakumbuka.



    “Hamaniko ni himaya ya ajabu sana. Huwa sitamani kabisa kufika huko tangu baba zangu wauwawe na wanyang’anyi enzi za biashara za masafa kipindi kile. Hamaniko ni hamaniko kweli,” alidokeza mzee Ganda.



    “Kumbukumbu yangu ya mwisho ni pale ambapo nilikuwa bondeni nikimchunga fahali niliyeamuliwa kumlipa baada ya kumnunua. Walinivamia vijana wawili na walichonifanya nadhani kilikuwa kibaya zaidi. Nilipoteza fahamu mpaka pale nilipokuja kuzinduka nikiwa hapa kwako. Yaliyoendelea sikuyajua hadi sasa sijui ni nini kilitokea baada ya hapo na kunifanya nifike hapa,” alieleza Majaliwa.



    “Pole sana Majaliwa. Ninayo imani, utapata wasaa wa kukutana na familia yako tena. Kilichopo kwanza upone na upate nguvu. Na kabla ya hapo, nitatuma kijana wangu hadi huko apeleke salamu na pia akachunguze hali ilivyo maana huwezi kujua kinachoendelea,” aliongea mzee Ganda.



    “Uliyoeleza yote sikuyafahamu. Bali nakumbuka jinsi vijana wangu walikupata hadi kukuleta nyumbani. Siku hiyo waliondoka majira ya jioni kwenda mtoni ambako huwa wanaenda kulaza mitego yao ya samaki. Wakati wakihangaika kutega mitego yao kwa ajili ya kuwanasa samaki ndipo maporomoko ya maji yalikufikisha na kukutua kwenye mtego. Walitaharuki sana. Lakini baada ya kujaribu kukuondoa kwenye kimia, waligundua kuwa ulikuwa bado hai. Walikuopoa na kukuhudumia kuyatoa maji uliyokuwa umeyanywa. Haraka walikubeba na kukufikisha nyumbani ukiwa na majeraha mengi. Mkono wa kushoto ulivunjika, kisogoni kulikuwa na kidonda kikubwa ambacho kilionekana wazi kuwa ulipasuliwa na kitu chenye ncha kali. Jicho la kulia lilikuwa limetoboka na damu zilikuwa zikimiminika. Yalikuwa mengi, mguu mmoja nao ulikuwa umevunjika na kila sehemu ya mwili ilikuwa na jeraha. Hukutamanika!” Alieleza mzee Ganda.



    “Asante sana ndugu yangu,” Majaliwa alishukuru.



    “Siku hiyo nilihangaika sana. Nilikoka moto na kuchemsha maji na dawa nyingi nilizotumia kukukanda na kukuogesha. Baadhi nilikunywesha na wakati nilitumia dawa kavu kukuvutisha. Hadi siku tatu hukuwa na uwezo wa kufanya chochote bali mwili ulikuwa ukionesha kuwa ulikuwa hai kama mtu mwenye usingizi mzito. Uliendelea kuwa hivyo hadi ulipozinduka. Ulikaa hapa karibu miaka mitatu ukiwa mzima lakini huelewi chochote. Umekuwa ukisema hovyo, unaweweseka na wakati unakuwa kama mgonjwa wa akili ukitaka kufanya mambo ya ajabuajabu. Miaka zaidi ya mitano hali hiyo umekaa nayo ikienda na kurudi. Namshukuru Mungu, mengi nimefanya na hadi sasa akili yako imerudi mahali pake, umepona,” aliendelea kufafanua mzee Ganda.



    “Nashukuru sana ndugu yangu,” Majaliwa alishukuru tena.



    “Mimi naitwa Ganda. Hamaniko kuna mdogo wangu aliolewa na ukoo mmoja wa wafugaji miaka mingi iliyopita. Walimchukua akiwa katoto kadogo. Walimlea angali hata miaka kumi na mitano hakuwa nayo. Baba zangu walienda kufanya biashara huko, wakati wa kurudi walikuja na wageni ambao mmoja wao alimtamani mdogo wangu na kusema angefaa kuolewa na kijana wake. Walimchukua kwa makubaliano ya kibiashara na baba yangu. Walipofika huko nilipata habari kuwa wazee wangu waliuawa mara baada ya kuwa wameenda kukamilishiwa malipo ya biashara zao. Tangu miaka hiyo hadi leo sijapata habari zao za dhati japo niliwaza sana namna ya kuwafikia nijue japo habari zao. Kulipa kisasi sikutaka. Ndiyo maana sasa nataka niagize kijana aende hadi kwa familia hiyo, kupitia hapo ndipo nitapata nafasi ya kujua hali ya kijiji kizima. Nafahamu ni hatari kumtuma mpelelezi asiye na wenyeji, watamuua na kumwangamiza. Yapasa aende kwa namna hiyo. Nina imani tutafanikiwa kupata taarifa za huko kwa muda muafaka,” alieleza mzee Ganda. “Yafaa sasa pangali mapema turudi nikamwandae kijana wangu ili kesho asubuhi na mapema aende huko,” aliongeaa.



    “Nitashukuru sana kupata taarifa za huko. Mungu atamwongoza na atafika salama na kurudi na taarifa kamili. Nimeikumbuka sana familia yangu na inawezekana kabisa kuwa walishakata tamaa na kujua niliuawa,” alieleza Majaliwa.



    “Lazima wapate wasiwasi. Akienda nataka awajuze kuwa upo huku bali ajue kama wapo na wanaendeleaje na maisha baada ya wewe kutoweka,” alieleza mzee Ganda. Muda huo walikuwa wakinyanyuka na kuanza kujikongoja kurudi nyumbani. Giza lilikuwa limeanza kukitalii kijiji cha Amani tayari kuwafanya watu wake kuingia ndani ya majumba yao kulala.



    “Pamoja na kuwa afya yako inatengemaa, mpakani mwa kijiji cha Amani japo ni mbali kutoka hapa kuna hospitali. Ningependa sana siku moja ufike huko wakutazame hali yako. Wajua sisi waganga wa miti shamba hatuna vipimo vya kitaaluma. Huko wataweza kutupatia jibu kamili kuwa umepona na uko imara kuanza kufanya chochote kwa jasho,” alieleza mzee Ganda.

    “Nimepona mzee Ganda. Sina haja ya kukusumbua tena. Nitakuwa salama,” alijibu Majaliwa.



    “Sawa Majaliwa. Fahari ya macho ni kuona kilicho juu ya mwili pekee. Tiba yetu ya jadi haina uwezo wa kuona ndani ya mwili. Yapasa wenye macho ya ziada wakushauri. Sijawahi kumtibu mtu wa majeraha makubwa namna yako tena kwa kipindi kirefu namna hii. Yafaa kuwashirikisha. Wewe ndugu yangu, usihofu vijana watakupeleka,” alieleza mzee Ganda. Wakati huo walifika nyumbani na kama ilivyokuwa desturi walifika na kuweka kituo kwenye moto uliokuwa umewashwa kwenye magogo. Kama alivyomweleza Majaliwa, mzee Ganda alimjuza kijana aliye mwamini kuwa, kulikuwa na safari ya kwenda Hamaniko.



    *****



    Siku hiyo anga lilikuwa jeupe, pe! Lilipauka na kuwa yatima. Hakuna wingu wala tai waliokuwa wakiruka kwa mikogo, wote walitoweka. Upepo uliokuwa ukivuma na kuifanya miti mirefu kukumbatiana kwa furaha, ulikoma. Miali ya jua la utosi ilisafiri, fya kama mshale wa msasi kisha kuchupa ndani ya ardhi. Udongo uliimeza miali na kutema joto kali lililomkera kila kiumbe aliyekuwa juu ya uso wa dunia. Miche ya nyanya na vitunguu iliyokuwa bustanini yote ilipigwa simanzi kisha kujiinamia kwa huzuni. Wadudu watambaao walijibanza kwenye miti mikubwa na wengine chini ya mashimo ili kulingoja jua kutua.



    Jua kali la mwezi Oktoba lilishika kasi yake. Ndege wa porini makoo yaliwakauka. Waliruka kila upande na kutua juu ya matawi yenye kivuli. Kwa zamu, walitua kwenye dimbwi la maji yaliyokuwa yakitumika kumwagilia bustani. Wima! Kwa pembeni, mti mkubwa wa maua mazuri ulisimama. Kupitia maua yake yaliyopepea mti ulipumua harufu nzuri yakuvutia. Nyuki na vipepeo walivutwa kama sumaku wakiruka na kutua kwa zamu. Mbawa zao kwa mikogo walizitanua na kuzikunja huku tabasamu kubwa lilichanua kwa kila ua walipolitoka. Shangwe iliwashika kwa utamu waliouonja. Hebedari ilikuwa ni ndoto zao kuzitimiza, kufyonza na kujipatia chavua.



    Ingawaje jua liliwaka na kuzalisha joto kali, Carolina alikuwa pekupeku. Ndoo yake aliishika mkononi akiingia na kutoka dimbwini ili kuinywesha maji miche ambayo ilizubaa kwa kiu. Baada ya kuhakikisha kila mche umekunywa na kukinai maji, Carolina aliamua kupumzika kwa dakika chache chini ya kivuli cha mti. Aliichukua kanga yake ambayo mji wake ulitoboka kisha kuikunjua na kuitandaza chini ya mti ule wenye maua mazuri. Alijilaza ili kulingoja jua kupungua ukali. Sekunde chache zilipopita, Carolina alihisi usingizi kumteka. Aliusikia mwili wake ukilalamika kwa maumivu kutokana na kazi za kutwa alizozifanya katika bustani yake.



    Kabla hajatopea usingizini, Carolina alisikia kishindo pembeni yake. Alihisi kulianguka ua au jani kutoka juu ya mti huo wenye maua mazuri. Kishindo kilifuatiwa na kelele za majani makavu yaliyokuwa yametanda chini ya mti baada ya kupukutika kwa kulihofu jua. Carolina aliyafumbua macho yake na kukinyanyua kichwa kwa haraka. Aliyaangaza macho ya duara kuelekea kule sauti na kelele vilitoka na kubaini kulikuwa na jambo lililokuwa likiendelea. Alinyanyuka na kuchukua kipande cha mti na kujongea karibu.



    “Ohh! Mungu wangu! Kulikoni kipepeo na kinyonga kuwindana?” Carolina aliongea peke yake wakati akijaribu kumchokonoa kinyonga kwa kijiti alichokiokota. Rangi ya kinyonga ilifanana sawia na rangi ya kipepeo mzuri aliyekuwa mdomoni mwa kinyonga. “Kweli Kinyonga hana huruma. Kipepeo kakosa nini hadi atiwe mdomoni kwa uchu?” Alisema Carolina peke yake. Alichunguza kwa makini na kumwona kipepeo akiwa kanasa kwenye ulimi mrefu wa Kinyonga. “Kipepeo hana hila kwa kiumbe yoyote duniani. Upenzi wake kwa maua umemponza” Carolina aliendelea kutafakari juu ya alichokiona.



    Alishika miti miwili ili kutaka kumnasua kipepeo kwa huruma. Kinyonga kwa hasira alivimba na kutoa sauti ya hasira. Alimsogeza kipepeo vizuri mdomoni na kumzamisha tumboni. Alisimama wima kwa ukakamavu wakati rangi yake taratibu iligeuka na kuwa ya manjano kama gauni alilokuwa amelivaa Carolina.



    “Haaa! Kinyonga kigeugeu! Amebadili rangi na kuwa kama gauni langu. Maajabu ya kinyonga,” Carolina alipigwa butwaa. Alijiuliza maswali mengi kwa tukio aliloliona. Hakuwa na la kufanya kwani kipepeo tayari alikuwa kwenye ulimwengu wa tumbo la kipepeo. Macho ya Carolina yalibaki kumtazama kinyonga kwa mshangao wakati alipokuwa akiondoka sehemu ile kwa madaha.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Alitokomea kichakani na kwenda zake.



    Punde! Njaa ilianza kumsokota Carolina. Alikusanya kuni kisha kuchota maji na kuanza mwendo kurudi maskani kwa ajili ya chakula cha mchana. Kila alipopiga hatua kukipanda kilima cha njia aliyoifuata kutoka bondeni, alihisi zilizala. Kwenye bega la kuume alipachika jembe, mkono wake wa kushoto ulibeba galoni la maji wakati kichwani aliibeba ndoo pia ilijaa maji. Mgongoni alifunga furushi la kuni lililokuwa limetuna kama mtoto. Aliikaza miguu iliyovaa kandambili ili kuongeza mwendo kwa ujasiri kukipanda kisha kukimaliza kilima cha njia iliyomwongoza hadi kwao. Kila alipopiga hatua, kuni zilimchoma na kufanya atikisike na kuifanya ndoo iliyokuwa kichwani kwenda homahoma.



    Ilimchukua muda mfupi hadi kufika sehemu ambayo aliishi. Alilitua dumu dogo kisha kuzifungua kuni zilizokuwa mgongoni. Aliziachia zikaanguka chini na ktoa sauti, kwachala! Aliitua ndoo na kuiweka kandokando ya mtungi mkubwa ambapo alisimama kando. Jasho jekejeke lilimtiririka hadi gauni lake lilikuwa chepe na kuganda mwilini sehemu ya mgongo. Alikishika kipande cha kanga yake kisha kujipangusa usoni hadi shingoni akilitoa jasho lililokuwa likimtoka.



    “Ah! Ukisikia kula kwa jasho ndo huku. Wakati wengine wakila kwa feni mie…kwa jasho!” Aliongea wakati akiyaagiza macho yake kulitazama gauni lake ambalo pamoja na kulowa lilikuwa na tope kila pahala. “Ona, hata sabuni ya kulifua gauni hili sijui itatoka wapi? Potelea mbali, Mungu anajua. Mzee wetu mwenyewe na ng’ombe wote hawa, kuipata sabuni hadi upige goti. Nitatumia majani ya mlenda hasa watumiao kwa mrenda kuzifua nguo zangu.” alisema Carolina. Alilitazama gauni vizuri, lififia rangi na kufanya michirizi kama chujio la magadi. Alilizoa gauni lake kwa chini na kujikokota kisha kuketi kwenye kiambaza cha mlango wa nyumba yao. Aliangaza macho yake kila upande tena na tena lakini hapakuwa na mtu.



    “Huruma!...Huruma!” Carolina aliita kwa sauti. Bado hapakuwa na mtu ambaye aliweza kuitikia sauti ile. Alikaa kimya akiendelea kuyazungusha macho yake kukagua pande za nyumba yao. Kiganja cha mkono wake kilikuwa kimeliegemea shavu kwa huzuni. Mawazo yalimteka na kumsafirisha hadi anga ya tafakari kwenye maswali asiyo na majibu yake. Moyo ulimkaba na kumlazimisha kunung’unika.



    “Carolina mie. Nitakuwa mgeni wa nani? Kwa nini?... juhudi zangu za kusoma zote zimegeuka njozi bustanini. Badala ya kuwa darasani, nimekuwa mkulima kijiko mkononi. Mchicha, nyanya, vitunguu mashina sabini vitanifikisha wapi? Dimbwi la maji nalo linaelekea kukauka. Nitafanya nini baada ya hapa. Shamba ni mali, lakini kwa mtindo wangu sitafika mahali,” Carolina alijiuliza utitiri wa maswali ambayo hakuweza kuyajibu. Machozi yalimlengalenga machoni. Alilitazama zizi la ngombe lililokuwa mbele ya macho yake kisha alikitikisa kichwa kwa huzuni.



    Hakukoma huwaza na kujiuliza, aliendelea. “Hivi, iweje baba yangu tajiri kiasi hiki asinipeleke shuleni kusoma?” Muda huo aliikusanya mikono yake. Aliipandisha na kuishusha pumzi kwa nguvu. Tayari macho yake ya gololi yalitengeneza vijito vya machozi yaliyoshindana kufanya michirizi kwenye mashavu yake mororo. Aliutuma mkono kuyazuia, lakini hakufaulu. Kifua kilimtuna kwa huzuni na uchungu uliunguza mtima wake, alilia kwa uchungu. Kamasi jepesi lilimiminika, alilidaka kwa kanga yake na kulifikicha. Tayari macho yaligeuka rangi na kuwa mekundu kama kaa la moto. Moyo wake uliingiwa fadhaa kwa kuwaza.



    Msicha huyu hakuwa na mtu wa kumsimulia masahibu yake. Kijiji alichoishi kilikuwa na vipaza sauti wengi ambao punde wapatapo taarifa za mtu huziuza kwa midomo. Kulijaa wambea ambao wakisikia moja wao huongeza kumi kwa hila. Kuwaza na kuwazua ikawa sehemu yake. “Safari yangu ya maisha ni kitendawili kigumu. Ni kama hadithi za jongomea kwa mtu anayeishi. Mafanikio yangu ayajua Muumba. Kama nafsi iliyoshiba hukinai sega la asali, basi mimi ni nafsi yenye njaa. Nimekuwa kama ndege aendaye huko na huko mbali na kitundu chake. Katika kuwaza kwangu, majawabu siyapati. Mola nijulishe mwisho wangu na kiasi cha siku zangu za kuishi ulimwenguni. Tazama, umefanya siku zangu kuwa shubiri. Matumaini yangu kwako, usiyanyamalie machozi yangu. Mimi ni mgeni wako uniachilie nikunjue uso japo siku moja kwa furaha. Maji yamefika mpaka nafsini mwangu. Ninazama katika matope mengi pasipowezekana kusimama. Nimefika penye maji ya vilindi, mkondo wa maji utanichukua. Kulia nimechoka, koo limenikauka. Macho yangu yamedhoofu, ndoto zangu zinafifia kama kipepeo mdomoni mwa Kinyonga,” alilalama Carolina. Mfuatano wa fikra ulimsonga.



    Akiwa mateka wa fikra, alisikia mshindo wa nyayo zikitokea nyuma ya nyumba yao. Kwa haraka tena aliyafikicha macho yake kukificha kilio chake. Hatimaye sauti ilimgutua.



    “Dada Caro. Mbona unaonekana mwenye huzuni?” aliuliza Huruma. Huruma alikuwa ni mtoto wa mwisho wa Malecha. Muda huo naye alitokea kisimani. Aliitua ndoo karibu na pale Carolina aliketi. Alimsogelea na kumshika bega akimtazama dadaye kwa huruma na upole. Carolina aliyazungusha na kuyakaza macho yake kwa ujasiri. Alijilazimisha kulitoa tabasamu na asifanikiwe.



    “Si kitu Huruma.”



    “Hapana dada. Mbona leo huna furaha kabisa? Hata macho yamekuiva, kulikoni?”



    Maswali ya Huruma yalichochea huzuni nafsini mwa Carolina. Machozi yalizidi kumbubujika kama chemchemi kandokando ya mto. Huruma alimpangusa kwa kiganja chake. Aliendelea kumdadisi ili kuujua ukweli wa kilichokuwa kimempata.



    “Dada, niambie ukweli. Kwa nini huna furaha? Tena unalia, kwani kuna nini?” alidodosa Huruma. Alimkumbatia na kumbembeleza dada yake.



    “Hapana Huruma. Amini nipo sawa. Hakuna tatizo lolote mdogo wangu!” Carolina hakuweza kusema wakati huo. Alimshika shavuni na kumtazama kwa upole. Huruma naye aliingiwa huzuni wa kile asichokijua naye chozi lilimtoroka pasipo kutarajia.



    “Huwezi kunificha dada. Lazima kuna tatizo. Angalia, hata macho yako yanakushitaki, yameiva na kusinyaa kwa huzuni! Nitawaambia baba na mama unalia,” alisema Huruma.



    “Hapana Huruma,” Carolina alijibu kwa mkato. Alitazama kila upande kabla hajainamisha kichwa kwa sekunde chache. Alimtazama tena Huruma, alitikisa kichwa kwa unyonge.



    “Kuna nini…niambie?” Huruma alizidi kumdadisi dada yake ili ajue kile kiliyasibu maisha yake. Kwa kuwa nafsi huamini chozi limtokalo kuku si bure, bali kuna mwewe kamuuzi, Huruma hakukata tamaa kumchimba dada yake akitaka kujua sababu ya kilio chake.



    “Dada, niambie basi mdogo wako!” Huruma alimsihi Carolina ambaye macho yake alikuwa kayakaza kwa ujasiri na kuupiga moyo konde. Aliipandisha pumzi kisha kuishusha akimtazama Huruma.



    “Nimewaza mengi sana mdogo wangu. Wewe bado hujayajua ya dunia. Mwisho wa maisha yangu ni upi? Hata wewe sijui mwisho wako utakuwa upi japo bado unasoma shule ya msingi. Nimehitimu shule ya msingi, isivyobahati sikuchaguliwa. Napenda sana kusoma Huruma,” alisema Carolina. Aliinama tena na kuyafuta macho yake kwa gauni. Huruma alikuwa kapigwa na butwaa asijue la kusema. “Kwa nini mimi naishi maisha kama kijakazi? Kutosoma nahisi nitakuwa kipofu katikati ya msitu wenye miiba,” alisema Carolina. Alipomaliza kusema alinyanyuka. Aliingia ndani na kuelekea chumbani alikokuwa akilala. Huruma naye alimfuata ili kupata kuujua ukweli.



    “Nisubiri dada Caro,” Huruma aliita.



    Alimfikia dada yake na kujaribu kumtuliza ili aache kulia na kuishi katika simanzi.



    “Huruma mdogo wangu, nayaogopa maisha ya kijiji hiki. Tazama, wanaume wengi wazee kwa vijana wanavyonisumbua kwa maneno na zawadi nyingi. Wote wanataka kunioa jambo ambalo siafiki. Ningekuwa shuleni hakuna ambaye angeweza kunibabaisha. Kwani wanaona jinsi niishivyo kuwa sina jipya zaidi ya kunitaka. Naumia sana!” alifafanua Carolina. Huruma hakuwa na msaada zaidi ya kubaki kimya akimtazama. Alimtaka amjulishe baba yao juu ya nia yake huenda angemkubalia.



    Maisha ya Carolina yalifunikwa na vitendawili vingi vigumu. Tangu akiwa mwanamwali aliota kuelimika. Nia yake ni elimu. Hakuacha kuwaza juu ya jambo hilo. Alihisi kulikuwa na hiana ambayo ililenga kumpoteza katika rada ya mafanikio.



    Baada ya kuwa wametayarisha chakula cha mchana kwa siku hiyo, wote walikusanyika chini ya mti wa mwembe palipokuwa na kivuli na ubaridi wa kutosha. Wanawake hawakupaswa kula chungu kimoja na wanaume kama desturi za jamii yao ilivyowapasa kufanya. Wanaume waliketi sehemu yao vilevile Mama Saraganda, Carolina na Huruma nao iliwalazimu kuketi kundi lao. Carolina alitia maji ya kunawa kwenye beseni na kulitenga katikati ya kundi ambapo Malecha aliketi na kibarua wake akiwemo Saraganda pacha wa hiari na Carolina. Kwa kuwa desturi iliwapasa wanaume kupata chakula kabla ya wanawake, Carolina alikifuata chungu cha ugali akiwa amekifunika kwa adabu. Alipiga magoti na kukitenga chini kisha kufuata chungu kilichokuwa na mboga. Baada ya kuwa ametenga, alijongea pembeni kidogo yangali magoti yameishikilia ardhi. Aliikusanya mikono yake kwa adabu na kuwaalika kwa chakula huku akitabasamu. Walishukuru wakanawa kisha kuendelea na kile walikarimiwa na binti huyo.

    Baada ya dakika arobaini kupita, Carolina aliitwa kwenda kutoa vyombo. Alienda haraka na kutekeleza alichopaswa kukifanya.

    Alifagia kwa mfagio sehemu ambayo mabaki ya chakula yalionekana. Alipotoka hapo, alifuata maji aliyoyaandaa na kuyatia kwenye kata kubwa akamkabidhi baba yake. Aliendelea kuchutama akisubiri baba yake kumaliza kunywa maji likiwa goti lake tuli ardhini. Alipomaliza kunywa maji, Carolina aliipokea kata na kunyanyuka. Moja kwa moja alienda hadi ndani kumchukulia baba yake sigara na kaa la moto alilolibana kwa magunzi ya mhindi. Zamu ilikuwa imeisha, alitekeleza matakwa ya mlezi wake.



    Hatimaye ilifika zamu ya akina mama kujipatia chakula kama stahiki na desturi yao. Walikula huku wakipiga soga wakirejea matukio mbalimbali katika jamii yao. Baada ya chakula, Carolina na Huruma walianza zoezi la kuchota maji kwa ajili ya matumizi ya nyumba nzima. Wakiwa njiani kutoka kisimani, Carolina alijikwaa kwenye jiwe. Ndoo ilimponyoka ikajipigiza chini na kupasuka. Kidole kimoja cha mguu wake wa kushoto kilichunika vibaya na kufanya damu nyingi kumtoka. Japo watu wa kale walisema, heri kujikwaa dole kuliko ulimi, Huruma alihamaki sana kwa tukio lililompata dada yake.



    “Dada, pole! Umeumia sana?” Aliuliza Huruma. Aliinama kutazama kwa makini sehemu iliyokuwa ikitokwa damu mguuni kwa Carolina.



    “Hapana. Sijaumia sana, bali nahisi kidole kimechunika vibaya,” Carolina alijibu wakati akiipangusa damu iliyokuwa ikiruka kutoka kwenye kidonda cha mguu wake.



    “Naona damu nyingi sana inakutoka. Ngoja nikukamulie maji ya mkonge,” Huruma alisema wakati ambao alitimua mbio hadi sehemu palipokuwa na mkonge kisha kuchuna jani moja changa. Mbio tena alirudi hadi pale Carolina alikuwa kaketi akiugulia kwa maumivu. Huruma alilikamua jani la mkonge likatoa maji mengi yaliyotua kwenye kidonda. Kwa taratibu damu ilianza kupunguza kasi ya kutoka. Alichana kipande cha kanga na kumfunga dada yake vizuri.



    “Asante mdogo wangu. Sasa tunaweza kwenda,” alisema Carolina wakati akinyanyuka na kuokota masalia ya ndoo yake. Alishikilia kandambili moja mkononi na taratibu walijongea hadi nyumbani. Walipofika nyumbani, Mama yao alimtia Carolina chumvi kwenye kidonda. Hakika ilimsababishia maumivu makali hadi alihisi haja nyepesi kumtoroka.



    Jioni ilipofika, giza lilikuwa limekimeza kijiji cha Hamaniko. Redio ya Malecha ilinguruma kwa taarifa ya habari usiku huo. Ilikuwa saa mbili usiku. Miji yote iliyokuwa katika kijiji hicho ilikuwa imefunga milango na kujisitiri ndani. Mitaa ilibaki ukiwa na kimya kama waombolezaji wa kifo cha mtu mashuhuri. Hapakuwa na yeyote aliyerandaranda usiku kutokana na hofu ya kuvamiwa na wanyama wakali waliokiumbua kijiji kile.



    Carolina na Huruma walikuwa ndani ya chumba chao kwenye kijumba kilichojitenga na nyumba ya wazazi wao. Waliwasha kibatari kilichotoa moshi mzito. Huruma alikohoa mfululizo akijitahidi kulisafisha koo ili apumua vema. Dada yake alikuwa akifunga siku yake kwa sala akimshukuru Mola. Alitimiza nia yake kisha kujitupa kitandani. Carolina aliikusanya pumzi na kukipuliza kibatari ambacho kilizima na kukiacha chumba kikiwa giza kama pango katikati ya msitu mnene. Moshi wa kibatari ulitawanyika na kuifanya hewa ya chumba kuwa nzito isiyoweza kuvumilika. Hali hiyo ilimfanya Carolina kunyanyuka na kupapasa kwenye kitundu cha dirisha na kuliondoa gunia lililokuwa limeziba. Kipande hicho cha gunia kiliongeza kasi ya kikohozi kwakuwa kilitimka vumbi jingi. Alikohoa na kupiga chafya mfululizo wakati akipanda kitandani tayari kwa kupumzika. Alipotulia kidogo, kumbukumbu ya tukio la mchana lilimjia.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Huruma!” Aliita kwa sauti ya chini kwani asingeweza kupayuka kwa sauti ya juu ambayo ingeweza kusafiri hadi umbali mrefu na kukifikia kijiji kizima.



    “Abee dada!” Huruma aliitika akiwa ameshikwa lepe la usingizi. Aligeukageuka akiwa katikati ya giza nene lililokimeza chumba chao.



    “Nikajua umesinzia tayari. Bado upo macho?” Carolina alisema wakati akijifunua shuka kichwani vingali vumbi na moshi vikiendelea kukimiliki chumba chao.



    “Ndiyo dada, sijasinzia bado. Kwani unasemaje?” Huruma alihoji. Aliendelea kukohoa na kutema mate kwenye sakafu ya vumbi laini ndani ya chumba chao.



    “Mh! Kuna kitu nimekumbuka nataka nikwambie. Yaani we’ acha tu,” Carolina alisema huku akijiandaa kuketi.



    “Kitu gani dada. Kimetokea wapi?” Huruma alitaka kufahamu. Masikio yalimsimama kama mbwa koko aliyesikia mluzi wa bwanake amwitiaye chakula.



    “Kilitokea leo mchana nilipokuwa bustanini,” alijibu Carolina.



    “Bustanini! Mbona unanitia wasiwasi dada. Au yule mbaba alikufuata tena?” Aliuliza Huruma.



    “Mbaba ndiye nani?” Carolina alihoji akijaribu kukumbuka.



    “Koi nawe! Umesahau siku ile alitufuata kisimani akitaka umkubali akuoe,” Huruma alijaribu kumkumbusha kisa kilichokuwa kimetokea juma moja ambalo lilikuwa limepita. Siku hiyo Koi aliwafuata kisimani akimtaka Carolina kuwa mke wake na angempatia zawadi ya dume la ng’ombe na shamba kubwa.

    “Ha-ha-ha! Yule mwendawazimu, unadhani ni mzee. Maisha ya shamba yashamfanya kibabu kabla hata ya umri wake. Sawa lakini ni kibabu maana atuzidi umri yapata mara tatu zaidi. Hana adabu hata chembe. Na ubaba wake ule, pamoja na kusoma na mwanaye Tunu darasa moja, kutwa kiguu na njia kuwafuatilia mabinti za watu. Wala si yule mzee. Ni jambo tofauti sana,” Carolina alieleza kisha alicheka.



    “Kweli dada, ulisoma na Tunu na sasa mwenzio tayari kaolewa. Mbaba yule impendi! Tunu angesoma, angekuwa bonge la dada, si unajua alivyo?” alisema Huruma.



    “Ndo hivyo, ukiwa na baba wa hivyo heri kuwa yatima. Lakini hata mimi sielewi huyu mzee anawazaje. Huenda akawa anawaza kuniozesha mimi na wewe utafuata!” alisema Carolina.



    “Ha! Sasa nani wa kuoa katoto kama mimi, wewe ndo wanakuita mchumba hata vibabu!” alisema Huruma.



    “Thubutu! Mimi ni mtoto bado. Kwenye somo la uraia hujaelimishwa, mtoto hadi miaka 18. Chini ya hapo mtoto tu,” alisema Carolina na kutulia kidogo. Kwanza usinikatishe nilichokuwa nataka kukwambia,”



    “Ndiyo, nilikuuliza ukasema ni tofauti, Tofauti gani hiyo. Niambie upesi nataka nilale ili kesho niwahi shuleni. Maana fimbo zinaimba siku hizi, walimu hawataki kucheka na nyani….!” Huruma alisema wakati akinyanyuka kuketi.



    “Kisa kimoja cha kipepeo na Kinyonga.”



    “Wamefanyaje dada Caro?” Huruma alihoji. Alicheka kidogo na kuguna chinichini kwa mshangao.



    “Maajabu duniani hayawezi kuisha. Maana, hata wadudu huoneana.” Carolina alimsimulia Huruma kisa kizima kama ilivyokuwa bustanini.



    “Kwani dada, kipepeo na kinyonga wanakuhusu hadi uhangaike nao?”



    “Nilimhurumia kipepeo. Aliuawa bila huruma. Wewe huoni kama kipepeo hana hatia dhidi ya mdudu hata mnyama yoyote? Kipepeo lake ua, ua nayeye wala hana makuu.”



    “Kinyonga je? Hujui kinyonga ni mpole na mtaratibu sana? Huwezi jua, mpole kwa mtaratibu wamekosana nini,” Huruma aliongea kisha kujilaza na kuivuta shuka yake. Alijifunika gubigubi.



    “Hujajua nini nawaza kwa nilichokiona.”



    “Kwani unawaza nini dada?”



    “Kila ukionacho duniani ni mwalimu muhimu sana. Maisha ya kipepeo na kinyonga yamenipa mtazamo mpya.”



    “Nieleze, nini ati?” Huruma alidadisi.



    “Kisa cha kipepeo na kinyonga kimenijengea taswira pana akilini. Hebu fikiria, kipepeo awe ni msichana mzuri anayependeza. Anazo ndoto zake nyingi. Anataka kutua kwenye kila ua zuri ili apate kujisitiri kwa haja zake. Sasa atokee kinyonga ambaye hugeukageuka kwa rangi akijifananisha na rangi za ua analolipenda kipepeo kisha amtie mdomoni na kummeza. Unadhani kipepeo atatimiza ndoto zake kwa mazingira hayo?” Carolina alijieleza kwa fumbo.



    “Mie sijui dada. Maana mara kipepeo! Mara kinyonga!…hata sikuelewi” Huruma aligeuka kitandani akiuelekea ukuta tayari kwa usingizi.



    “Kesho dada utanisimulia vizuri. Siku hizi unataka kuwa bibi, hadithi nay eye. Mchana ulikuwa unalia wala hujaniambia kisa nikakuelewa,” alisema Huruma.



    “Haya. Jitie kutoelewa, najua siku ipo utanielewa. Lakini kaa ukijua, wewe pia ni kipepeo mchanga. Vinyonga wako wengi watakuwinda tu. Kwa mimi, lazima nitimize ndoto zangu. Siwezi kuwa kama kipepeo wa mchana,” Carolina alimsihi Huruma kisha alilala usingizi fofofo.



    Uchwao hauachi kuchwa. Asubuhi ilifika. Carolina alikuwa tayari zizini akiwakamua ng’ombe maziwa. Kidole chake kilikuwa kikiendelea kumuuma na kumfanya atembee kwa kuchechemea. Carolina hakuwa goigoi bali alikuwa hodari katika kazi za kila aina. Ilikuwa hebedari yake kuamka mapema kuwahudumu wanyama kabla hawajakwenda malishoni. Angali bado akimkamua ng’ombe wa mwisho, Malecha baba wa familia alijongea hadi lilipo zizi. Mwili aliuhekemua, mikono aliitawanya baada ya kukiachia kitanda muda mfupi. Alikishika kidevu chake kuzipapasa ndevu zake huku macho yake yakiambaa zizini kuwahakiki mifugo mamia waliokuwa zizini. Aliwajua mifugo kwa sura, maumbo na hata wengine aliwapatia majina. Wakati huo upepo ulifanya fujo na kusababisha vumbi zito kufunika eneo hilo. Carolina kwa haraka aliliziba zela alilokuwa akikamulia kwa mfuniko. Alisimama kuuacha upepo upite. Haikuchukua muda upepo uliokuwa ukienda kwa kujiviringaviringa ulikoma pakawa na utulivu kama kawaida. Carolina aliendelea kuwakamua ngombe hadi alipomaliza angali Malecha akiwa bado mlingoti akimngoja ayafungashe maziwa tayari kuyapeleka mjini.

    Wakati akiyahifadhi maziwa kwenye chombo cha kusafirishia, Carolina alikumbuka ushauri aliokuwa amepewa na mdogo wake. ‘Mwambie baba huenda akawa kabadili msimamo wake.’ Huruma alimshauri kumkumbusha baba yake kuhusu nia yake ya kutaka kujiunga na masomo ya sekondari. Aliyapakia madumu yote kwenye sanduku ambalo baadae alilifunga kwenye kitako cha baiskeli na kuiegesha kwenye ukuta wa nyumba yao. Malecha aliingia ndani kujiandaa tayari kwa safari ya kupeleka maziwa kwenye mji wa Tumaini uliokuwa mbali nao. Akiwa mwenye tafakari, Carolina alisimama asadi akimngoja huku macho yake kayatumbua kuuelekea mlango wa nyumba ambamo baba yake alikuwa. Haikuchukua muda mrefu, baba yake alitoka akiwa tayari kwenda mjini. Alimsogelea huku kamkazia macho na kupiga magoti mbele yake.



    “Baba!” Carolina aliita. Malecha aligeuka na kumtazama. Carolina alikuwa akiifikicha mikono yake kwa hofu. Familia nzima haikutaka kumzoea kutokana na msimamo na maamuzi yasiyo tabirika. Malecha alizikunja ndita kisha kumsogelea Carolina. Carolina alimtazama usoni kwa ujasiri.



    “Baba, mimi ninaombi,” alisema Carolina. Alijivuta pembeni kwa hofu kwani baba yake alimtazama kwa macho makali.



    “Ombi! Ombi gani asubuhi asubuhi? Hapa si kanisani mama,” Malecha alisema.



    “Kuhusu shule baba. Nataka kusoma. Muda unazidi kwenda nachelewa.”



    “Nyanyuka uendelee zako kafanye kazi. Jambo lako nitalishughulikia. Lakini….basi,” Malecha alitaka kusema lakini alikatisha na kukimeza. Carolina alinyanyuka na kuchechemea akielekea kilipokuwa kijumba chao cha majani. Aliingia ndani na kujibanza mlangoni akichungulia kumtazama baba yake akiondoka. Alimwona Malecha akiikokota baiskeli kisha kuirukia akielekea njia iendayo mjini. Jawabu ambalo alipewa halikuwa la kutia tumaini. Kila alipokumbuka alivyojibiwa,... ‘lakini….basi’ wasiwasi ulimzidi. Alihisi hapakuwa na namna zaidi ya kungojea ili apate jawabu kamili. Aliamini wakati ni ukuta hivyo muda ungefika wa yeye kupata jibu sahihi.



    Aliichukua ndoo na galoni pamoja na jembe kisha kuondoka zake. Alitembea hadi bustanini. Akiwa huko alimwagilia mimea hadi pale alipomaliza. Jua lilikuwa limeshika hatamu. Kama alivyokuwa amezoea, alijongea hadi kwenye mti wa maua aliokuwa ameuzoea. Aliyapepesa macho yake kila upande na kuridhika kuwa hapakuwa na tatizo lolote. Aliichukua kanga yake na kuitandika chini kisha kujilaza kifudifudi. Anga lilikuwa kama jangwa wakati jua likiwa limeshika kasi kwa hasira kuiunguza dunia. Hamu ya moyo wake ilimjia tena.



    “Nikifanikiwa kwenda shule..nitasoma mpaka kieleweke, hadi madarasa yatabomoka” Carolina alijiwazia. Alikuwa akijipa shime kama mamaye ambaye maishaye yaliishia njiani. Nafsi yake ilibubujikwa furaha na tumaini kuwa angeweza kusoma na kufanikiwa maishani. Akiwa katikati ya matamanio hayo, alisikia nyayo zikimnyemelea kutoka kwa nyuma. Alihesabu hatua na kusikia zikimkaribia. Majani makavu yaliyotapakaa chini ya mti ule ndiyo yalifanya atambue hilo. Alisikiliza kwa makini pasipo kugeuka, alijua nyayo hizo zilikuwa za binadamu ambaye si hatari kama mnyama. Taratibu alianza kuikunja shingo yake kama kitara ili apate kuona pasipo kugundulika. Akiwa hajaweza kutazama, ghafla macho yake yalizibwa kwa viganja kutokea kwa nyuma. Carolina aliogopa na kupiga kelele.



    “Nani wewe?” Hakusikia sauti ya mtu aliyekuwa amemfunika uso kwa kumbato la viganja vyake. Mwili ulimsisimka akajaribu kuvuta kumbukumbu za mtu mwenye mazoea ya kumfanyia hivyo.



    “Huruma! Lakini mh!” Carolina aliingiwa na wasiwasi. Hakupata jibu zaidi ya kuingiwa na tashwishi. Akili yake ilimjuza kuwa, mtu yule hakuwa Huruma hasa kutokana na kimo pia ukubwa wa viganja vya mikono yake. Huruma alikuwa bado shuleni na asingeweza kufika bustanini kwa wakati huo. Akiwa katikati ya tafakuli hiyo, uoga ulizidi kumwingia. Aliituma mikono yake kumpapasa mtu aliyekuwa ameufunika uso, lakini alimkwepa. Carolina aliirudisha mikono yake kwenye viganja na kuanza kuvifuata kwa kuvipapasa. Mwili ulimsisimka na kuota vipele kama fenesi baada ya kuwagusa malaika wakubwa kwenye ngozi ya aliyemkumbata.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Niacheee!” Alijikaza kujinasua kwa nguvu. Alikuwa na hofu.

    Mchana ule wa jua kali wakati Carolina akiwa bustanini, Roy alikuwa akitokea shuleni. Walikuwa wameruhusiwa kurudi nyumbani baada ya masomo ya kutwa nzima. Yapata mwaka mzima tangu aandike barua kwa Carolina lakini cha ajabu hakuwahi kupata jibu alilosisitiza kupatiwa. Kamwe katika maisha yake hakuwahi kukutana na Carolina uso kwa uso na kumweleza ambacho alikusudia zaidi ya kumwandikia barua. Kila wakati ambao alimwona Carolina akikatiza mbele yake alibadili njia kisha aliishia kusononeka. Kwa uoga hakuweza kumsemesha ili kumweleza nia ya moyo wake. Roy alikuwa hawafu asiye jiweza mbele ya binti aliyempenda. Jambo rahisi kwake ilikuwa kumwandikia barua.



    Roy alikuwa ni mwanafunzi wa kidato cha pili katika shule ya sekondari ya kata ambayo ilikuwa katika kijiji cha Hamaniko. Alimtangulia Carolina mwaka mmoja kuhitimu katika shule ya msingi waliyosoma pale kijijini. Baada ya jua kuwa limeuchoma mwili wake vya kutosha, Roy alilivua sweta lake la kijani ili apate kulirushia kichwani limsitiri dhidi ya miali ya jua. Alitembea wanguwangu akiteremka bondeni ili aweze kupanda kilima na kufika sehemu ambayo waliishi. Njia yake ilimchukua kwa karibu sana na ilipokuwa bustani ya Carolina. Bustani ya familia yake pia ilitazamana macho kwa pua na bustani ya Carolina.



    Akiwa amemaliza kukishuka kilima na kutumbukia bondeni, aliyapepesa macho yake hadi ng’ambo ya pili ambako ndiko kulikuwa na bustani hizo. Macho yake hayakukiamini kile alikuwa akikiona. Alisimama kwa mshangao kama nguchiro kwenye kichuguu na kutazama tena na tena kwa makini. Bado macho yake hakuyaamini. Alijaribu kuyafuta akihisi yalikuwa yamejawa utando na kumfanya aone kitu ambacho hakuwahi kukifikiria.



    “Ha! Yule si Carolina. Na-na-nani huyo? …Mh! au nakosea?” Roy aliuliza na kuyajibu maswali yake mwenyewe. Hakufikiria hata kuota siku moja kumwona Carolina akiwa kakumbatiwa na mwanaume ambaye si yeye. Alimjua Koi kuwa ni mtu mzima katika kijiji kizima kuweza kuwa karibu hivyo na Carolina ambaye kwa umri alifaa kabisa kuwa bintiye wa kumzaa. Ilikuwa ni wakati ambao Roy ilimlazimu kuukubali ukweli wa macho yake. Ingawaje alistaajabu, wivu ulimea moyoni mwake na hasira zilimjaa. “Haiwezekani. Leo acha nimfunde adabu. Atanitambua,” aliahidi Roy.



    Aliuweka mfuko wake wa daftari na sweta chini na kuchukua kipande cha mti kilichokuwa kimekauka . Aliwanyemelea polepole. Carolina mpaka muda huo hakuwa amemtambua mtu aliyekuwa amemfunika uso na macho yake. Alijaribu kujinasua lakini hakuweza kuachiwa.



    “Niachie, nani wewe?” Carolina alisema huku akifurukuta. Aliposikia maneno ya Carolina, Roy alipata picha kuwa haikuwa hiari ya Carolina kufanyiwa vile. Alikinyanyua kipande cha mti na kukishusha kwa nguvu, alimtandika mtu yule mgongoni.



    “Unamfanya nini? Huna haya, unataka kubaka!” Roy alifoka. Mtu yule alimwachilia Carolina ambaye alijitupa chini kisha kugeuka kumtazama. Mtu yule aibu ilimvaa aibu mdomo ukawa wazi na macho aliyatumbua. Carolina baada ya kumtazama aliyekuwa amemkumbata, hakuyaamini macho yake. Aliiona sura ya mwanaume ambaye kichwa kilianza kujaa unga. Makunyanzi usoni yalikuwa yametanda kama malinda ya pulizo la mashine ya unga. Carolina aling’aka kwa hasira. “Koi! Shetani mkubwa.” Carolina aliangua kilio. Kilio cha huzuni na uchungu wa kudhalilishwa. Macho yake aliyakodoa kwa hasira. Uvumilivu ulimuisha, mikono yake aliiagiza kuliokota jembe lililokuwa karibu yake. Timutimu! Koi alitimka mbio na kutoweka kama duma mawindoni. Carolina maneno yalimtoroka mfululizo, alibwata, “Mungu na akulaani uchomwe jua kama nikwata mwambani.” Alisema hayo huku macho yake yakimtazama kwa karibu Roy aliyekuwa kasimama na kukishika kiuno chake.



    Carolina alimfuata Roy na kumkumbatia akimshukuru kwa kumsaidia. Alijua pasipo Roy, Koi angeweza kumfanyia unyama wa aina yoyote. Siku hiyo ilikuwa adimu kwa Roy, mbali na kuwaza kumsemesha Carolina uso kwa uso, alipata kumbato ambalo lilimfanya moyo wake upoe kama barafu kwenye jokofu na kuzifuta hasira zake zote.



    *****

    Baada ya juma moja kupita, kidonda cha mguu wa Carolina kilikuwa kimepona kwa maji na moto. Hakuwa amelipata jawabu kutoka kwa baba yake ambaye hapo awali alimwambia kuhusu nia yake yakutaka kusoma. Japo hakuchaguliwa alijua kuna njia ambayo Malecha angeweza kuitumia ili kumfanya mwanaye aweze kusoma na kujipatia elimu aliyoitamani. Carolina alikuwa kaketi kwenye kigoda akichambua mboga huku akitafakari yaliyomsibu. Aliukumbuka usemi aliofundishwa shuleni na mwalimu wake kuwa, ‘ukiona kimya fahamu umekataliwa’ lakini aliipinga kauli hiyo akiamini kuwa kimya kingi kinamshindo. Carolina hakuwa mwenye kukata tamaa kwa wepesi.



    Akiwa bado katikati ya msitu wa mawazo, alikumbuka pia masahibu yaliyomtokea juma moja nyuma kule bustanini. Alikumbuka vile Koi alimfuata, pia hakuacha kukumbuka usumbufu ambao huwa anampatia. Nia yake yote ni kutaka kumrubuni na kumfanya akubali kuolewa naye. Hapohapo tena alikikumbuka kisa cha kipepeo na kinyonga na jinsi alikielewa. Mawazo yalimfanya asiendelee kuchambua mboga kama alivyokuwa amekusudia. Hakufahamu hata kama kulikuwa na mama yake aliyekuwa kasimama akimtazama kwa muda mrefu. Carolina akiwa bado kwenye msitu wa mawazo alikitingisha kichwa chake kwa huzuni. Aliyarudisha matembele kwenye ungo akijishika shavu kwa huzuni. Pumzi alizikokota akipumua kwa nguvu huku akijipiga kiganjani kwa hasira. Mama yake aliyashuhudia yote.



    “Carolina! Una nini leo?” Mama Saraganda alimuuliza. Alimsogelea.



    “Hapana kitu mama. Niko sawa,” Mkono wake aliutuma kuchukua majani ya matembele yaliyokuwa kwenye ungo na kuendelea kuchambua. Mama yake alipomfikia hakuwa na mengi ya kusema zaidi ya neno moja ambalo Carolina lilimuumiza sana.



    “Najua unataka kusoma. Tazama, wewe ni binti hupaswi kuhuzunika. Riziki ya mzaliwa wa kike anayo mumewe. Utaolewa na kuipata toka kwa mumeo. Inatia shaka sana kama baba yako ataafiki kukupeleka shule za kulipia ingali msichana. Hofu yake ni kwamba, unaweza kusoma halafu ukaolewa. Unadhani faida ni ya nani kama si mmeo. Ukizingatia wewe ni mpitaji tu!” Mama Saraganda alizungumza hayo pasipo kufahamu kama Carolina aling’amua kitu.



    Carolina aliposikia hayo, alimtazama mamaye kwa makini kisha kunyanyuka akielekea chumbani. Wakati huo Saraganda ambaye ni mtoto pacha na Carolina alikuwa akifika nyumbani akitokea shuleni. Alikuwa na barua mkononi.



    “Mama, barua hii nimepewa shuleni,” alisema Saraganda. Mama yake aliipokea. Aliigeuzageuza na kuyasoma maandishi, bado hakutosheka. Alitaka kujua kilichokuwa kimeandikwa. Baada ya kuifungua na kuisoma, alikuwa na maneno.



    “Hii barua inamhusu Carolina. Mngonjee baba yenu arudi atatoa jibu kama atampeleka kwenye shule hii au la, gharama ni kubwa sana,” alisema mama Saraganda. Saraganda aliyekuwa kasimama alimsikia mama yake akiongea hayo lakini alionekana kutoelewa.



    “Mpelekeni dada shuleni, namhurumia sana. Atakuwa mgeni? Ulimwengu wa kesho unahitaji elimu si kudra pekee za kuzaliwa nazo. Hata wanaume hawataki golikipa mama?” alisema Saraganda. Hakubaki pale, aliondoka.



    Ndani alikokuwa Carolina aliendelea kujiuliza na kuwaza. “Kwa nini mama anasema mimi ni mpita njia? Halafu kwamba mimi ni binti nitaolewa. Haiwezekani! Lazima nitasoma ili niishi maisha ninayoyatamani. Hakika, lazima nitasoma kwa njia yoyote nitasoma. Lakini…ah,” Carolina alijiuliza nafsini. Alitia nia ya kutimiza ndoto zake akiwa katika umri ule wa kufaa. Majibu ya mama yake yalimtelekeza akiwa njiapanda.



    Carolina alikuwa ameketi juu ya kitanda cha kamba ambacho kilifumwa kwa ngozi za wanyama. Kitundu cha dirisha dogo kilipitisha mwanga ndani ya chumba kile kwa shida. Japo jua lilikuwa kali, mwanga ndani ya chumba bado ulikuwa hafifu. Carolina alijaribu kujilaza lakini nia yake haikutimia. Mawazo yalimzidi na kukifanya kichwa chake kimuume. Akiwa katikati ya tafakari ya jinsi maisha yake yangekuwa, Carolina alikumbuka kuwa kipindi alipokuwa darasa la saba kuna shajara alitengeneza yeye na rafiki zake. Alinyanyuka kitandani na kuinama uvunguni na kuvuta kilindo ambacho alikuwa amekijaza daftari zake tangu darasa la kwanza hadi alipohitimu darasa la saba. Alianza kupekua daftari moja baada ya jingine. Alipekua karatasi kwa karatasi huku akichunguza kwa makini. Alichokuwa akikitafuta hakukiona.



    Alitulia kutafakari ili kukumbuka muundo na rangi ya shajara aliyotengeneza kipindi akiwa shuleni. Kumbukumbu zilimjia! Alianza kurudia kupekua tena na tena hadi alipokutana na daftari dogo. Daftari hilo lililochorwa picha ya ua kubwa na alama ya moyo uliotiwa mshale. Alilichomoa na kulikung’uta ili kulitolea vumbi lililokuwa limefunikwa nalo. Alilitupia kitandani wakati akijihimu kuzirudisha daftari zote ziliyokuwa chini ndani ya kilindo. Alimaliza. Alikisukuma kilindo kikapotea chubwi uvunguni mwa kitanda. Aliifuta mikono kwa gauni lake. Tabasamu lilimtawala mdomoni baada ya kuipata shajara ya ndoto zake. Aliichukua na kuitia mkononi akiuangalia usanifu aliokuwa ameufanya juu ya jalada lake.



    “Mh! Ua kubwa jekundu, mkuki moyoni! Nazipenda picha hizi,” Carolina alinong’ona lingali tabasamu halikufutika. Alianza kufungua ukurasa mmoja baada ya mwingine kutafuta kile ambacho alikusudia kujikumbusha. Katika ukurasa wa kwanza alikutana na jina lililoandikwa kwa herufi kubwa: CAROLINA CHAUSIKU MALECHA. Hili lilikuwa jina lake. Aliyashusha macho yake chini kidogo na kukutana na herufi kubwa zilizoandikwa kwa wino wa kukoza: LY 2000. Alipoyaona maneno hayo, alivuta hisia kali zilizomfanya aendelee kupekua kurasa zilizofuata. Kabla hajapekua ukurasa wa nne, aliona kipande cha karatasi kikipeperuka na kuanguka chini. Alitaka kujua kilikuwa ni kitu gani hivyo aliinana kukiokota. Kilikuwa kimekunjwa na kutiwa pini. Alipokishika mkononi alijua fika kuwa kilikuwa hakijafunguliwa na kusomwa. Aliiweka shajara pembeni akakigeuzageuza na kusoma juu yake kikiwa na maneno: Kwa, CCM, toka kwa ROC. Carolina alikipachua kipini na kukichomoa. Alikikunjua kipande cha karatsi ile. Alikutana na maandishi ambayo aliyasoma:

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mpendwa Carolina,



    Salaam sana. Ama baada ya salaam, mimi ni buheri wa afya. Hofu na mashaka ni juu yako wewe unayeutesa moyo wangu. Kwani upo mbali na upeo wa macho yangu.



    Wakati naandika barua hii nilihisi upo mbele yangu. Barua hii ni ujumbe wa kukujulisha jinsi moyo wangu umekufa na kuoza juu yako. Kila msichana nimtazamaye shuleni namwona kama mvulana mwenzangu lakini nikuonapo tu, mapigo ya moyo wangu hulipuka kama fataki wakati wa sherehe za mwaka mpya nikuonapo. Kwa kifupi mimi nakuzimia. Sina hali wala hila kwako ila majibu yako nikiyapata.



    Usijiulize kwa nini nimeandika barua na kuichomeka katika daftari zako badala ya kukufuata na kukuambia moja kwa moja. Nimefanya hivyo kwa sababu kuu mbili; Moja: Mimi napenda ufahamu kuwa, barua ni zaidi ya maneno ya mdomo kwani nimetumia viungo vyangu muhimu, kwa utulivu kufanya hivyo. Kila kiungo changu ni shahidi wa vile nakupenda na kukuthamini.

    Mbili: Ni vigumu kukutana na wewe na kuzungumza niyawazayo kwani, mazingira ya shule ni magumu. Walimu hasa mwalimu wa nidhamu na mashushushu wake wangeweza kugundua na kufanya tuadhibiwe vikali.



    Hizo ni sababu chache bali zipo nyingi natamani kukueleza tukikutana. Nakupenda Carolina, tafadhali naomba unipende pia. Palipo upendo penzi huota pasipo na fitina. Yaelewe maneno yangu.



    Kila siku nikuwazapo hata nikila huwa siwezi kushiba. Kiu yangu haipozwi kwa maji hata usingizi ukinijia huwa nakuota wewe pekee. Ua langu la waridi moyo umeuchoma mkuki. Nakupenda! Nakupenda! Nakupenda! Nakupenda pia nitakuoa.

    Naomba majibu haraka.



    Niandikie barua ukaifukie kwa mchanga chini ya mti mkubwa wa mkaratusi, karibu na kengele ya shule, nitaiona.

    Majibu muhimu. Mtima wangu unaugulia.

    Wako akupendaye,



    ROC



    Sikiliza wimbo — Kipenzi Maua.



    Maneno ya barua hiyo yaliuteka moyo wa Carolina na kuusafirisha katika ulimwengu ambao hakuwahi kuufikiria. Alirudia kuyasoma maneno yale tena na tena, bado hakukinai. Alihisi kuna wimbo mzuri aliimbiwa na aliyekuwa akiandika barua hiyo. Moyo wake ulitaka kumfahamu. Alijaribu tena na tena kukumbuka kama kulikuwa na yeyeto pale shuleni ambaye aliweza kuiandika barua ile. Katu hakufanikiwa, hata jina lenyewe kila alipojaribu kuliunganisha hakuweza kumpata mwenye jina hilo. Aliwakumbuka vijana wengi na walimu mbalimbali wa kiume vile walivyomhangaisha alipokuwa katika mazingira ya shule. Hakuwa mmoja bali walikuwa wengi. Hatimaye ilimjia akilini, alikumbuka mwandishi alimtaka kuusikiliza wimbo, Kipenzi Maua. Akaukumbuka na kuuimba.



    Kushoto kwako kuna simba

    Nyuma kwako kuna faru

    Kulia kwako kuna chui

    Tazama mbele nipo binadamu

    Kwa nini hunioni

    Kukuokoa natamani

    Nifanyeje kukuokoa kipenzi?



    Dunia gunia maji halibebi

    Uje kwangu nyumbani

    Sebuleni utafaa

    Chumba nitakupa safi

    Utandike tupumzike

    Karibu ndani karibu

    Mchumba wangu Maua njooo



    Wasiwasi wa nini

    Mimi bado sina jiko

    Usiishie mlangoni, hapa ni kwako malaika

    Kwangu wewe malkia

    Maua njooo!



    Nakutegemea kipenzi njoo

    Nakuhitaji tuishi wote Maua

    Silaha ya upendo ni tabia njema

    Kwangu imejaa gunia

    Sina kidumu wala ndoo Edina

    Wewe ni pekee ua

    Pokea penzi langu limeze

    Usilitapike mchangani

    Wewe chaguo langu Maua



    Alipouimba wimbo huo maarufu masikioni mwa watu waliopendana, Carolina alijawa furaha. Moyo wake ulitabasamu, mdomo aliukenua. Alitamani kumjua aliyemtumia barua ile, bado hakupata jibu. Nia ya kuendelea kuipekua shajara yake ilimjaa. Aliichukua na kuikunja barua hiyo kisha kuipachika kwenye ukurasa wa mwisho wa shajara. Alifunua ukurasa ambapo hapo awali alikomea. Aliifungua kwa makini akakutana na majina ya rafiki zake wote aliowapenda na ambao alipotezana nao kwa muda mrefu. Wengine walikuwa wameshaolewa na wengine walikuwa masomoni mbali na mkoa aliokuwa akiishi. Alifungua ukurasa uliofuata akakutana na maandishi yaliyosomeka: CHAKULA NIKIPENDACHO. Maneno hayo yalifuatiwa na majina ya vyakula: wali kuku, samaki wa kubanika, ugali dagaa, viazi vitamu. Carolina alicheka peke yake baada ya kukumbuka vile alivyokuwa ameandika.



    Hatimaye alipekua ukurasa uliofuata. Ulikuwa na orodha ya vinywaji alivyovipenda. Orodha ilikuwa: fanta baridi, sharubati kola, zabibu, maji ya kisima, maziwa ya ng’ombe, togwa na wanzuki. Ukurasa huo ulimkumbusha mambo ambayo alitamani kuyapata kama kinywaji. Moyo wake uliingiwa furaha. Alipata picha kichwani jinsi alivyokuwa na furaha alipokuwa na wasichana wenzake. Akilini bado alikumbuka mambo mengi ambayo alikuwa bado hajajikumbusha. Carolina alifunua ukurasa uliokuwa na namba za masanduku ya barua ya kila rafiki yake. Aliyaruka na kufungua kwenye nyimbo alizozipenda. Ukurasa huo ulikuwa na majina ya nyimbo kumi. Jicho lake likakutana na wimbo uliokuwa namba moja na ni ule uliokuwa katika barua aliyoandikiwa na kutakiwa ausikilize. Alifurahi sana.



    Ukurasa ambao alikusudia kuusoma aliukuta baada ya kurasa tano kutoka kwenye nyimbo. Hapo alisoma neno moja baada ya jingine akiwa mpole usoni kwake. Carolina alipata kumbukumbu nzuri ambayo alihisi kumjaza nguvu ya kupambana na kuzitimiza ndoto zake. Ukurasa huo uliandikwa, KANUNI NA MIIKO YA BINTI MWENYE NDOTO PEVU. Maneno hayo yalifuatiwa na orodha ya kanuni hizo.



    1. Kutambua ndoto zake na kuzitimiza hata kwa kuyapoteza maisha yake.



    2. Ndoto lazima ziinufaishe jamii kwani yeye baadae atakuwa ni mama.



    3. Kujiepusha na uhusiano usiofaa kati ya binti na wanaume au wasichana makuwadi.



    4. Kuwaheshimu watu wote kama maandiko ya imani yapasavyo kuwa.



    5. Kusimama imara kama kutatokea shambulio la kutaka kumwangusha binti.



    6. Kutambua kuwa, adui mkubwa ni tabia, ni lazima kwa binti kujitunza mwenyewe kwanza.



    7. Kusoma kwa bidii na kufanya kazi kwa bidii.



    8. Kutokusababisha madhara duniani.



    9. Kutotumia kileo ambacho kitapunguza uelewa na utambuzi wa mema na mabaya.



    10. Kutokubali kurubuniwa kwa fedha, cheo, mali na kuanguka kwenye zinaa.



    11. Kutumia elimu na mapaji kumsaidia binti popote awapo ili ajikomboe.



    12. Kuwa mwaminifu kwa kila hatua.



    13. Kujiamini kwa kila hatua.



    14. Kuwa mvumilivu kwa kila hatua.



    15. Kutotegemea kusifiwa na yeyote kwa lolote.



    16. Kuwa viongozi kwa mema.



    17. Kutotegemea kuolewa au kupendwa.



    18. Kuamini kuwa siku binti atafanikiwa.



    19. Kutoogopa kuchukua hatua.



    20. Kujitunza wenyewe pasipo shinikizo.



    21. Kutambua majukumu hayataisha kwa binti.



    22. Kuwa na malengo thabiti.



    23. Kuwa wabunifu.



    24. Kuomba ushauri kwa mtu anayefaa.



    Pumzi alizishusha baada ya kuwa amezipitia tena na tena kanuni hizo. Kwa kipindi alichokuwa amefikia, aliziona kanuni hizi sawa na mwalimu wake aliyemwongoza. Aliwaza sehemu ambayo angeenda kujipatia ushauri ili aweze kukivuka kizingiti kilichokuwa kikimkabili. Akiwa katika kutafakari, alisikia mama yake akimwita. Aliichukua shajara na kuipachika ndani ya shuka alilokuwa akijifunika. Alitoka na kuelekea ambako mamaye alimwita ili kwenda kumsikiliza.



    Uchomwapo na mwiba wa kupenda nafsi huangamia na kuoza kabisa. Hii hutokana na kumpenda mtu ambaye anafaa kuwa mwenzi wa maisha lakini nafsiye haijui. Lakini kuna wakati kupenda huwa ni ujinga, ujuha usioweza kuvumilika. Haijalishi umri ambao mtu huwa nao dhidi ya ule wa ambaye hutamani kuwa naye karibu. Nafsi ikitamani hujipa ushindi hata pasipowezekana, hivyo ndivyo ilikuwa kwa Koi. Kwa kutokujua ama kwa uzuzu wa kuzaliwa nao, pumbazo la nafsi lilimfanya Koi kuyakanyagakanyaga maadili na mila za jamii yake. Vyote alivifukia topeni akitaka kujenga wasifu mpya. Wakati ushaibu ukimfuata alijiona kama barobaro mwenye umri sawa na binti kipusa Carolina.



    Akiwa amejawa na fikra za kumpata, Koi alifanya hila. Aliwaza jinsi Carolina aliumbika na kumtamani kila amtupiapo macho. Alimwona kama dhahabu isiyommiliki kwakuwa Carolina hakuwa na mwanzo wala mwisho aujuao. Aliikumbuka siku ambayo alimkumbatia na kuyafunika macho yake kabla ya kukatishwa na Roy. Koi hakuweza kuvumilia. Alinyanyuka alipokuwa ameketi wakati ule wa alasiri yenye jua kali. Aliikurupua baiskeli ili kwenda kwa Malecha angalau apate kuyalisha macho yake chakula ambacho yalikitamani. Alilikung’uta vumbi ambalo lilikuwa limeishika suruali yake nyeusi. Aliituma mikono yake mfukoni kukitoa kipande cha kioo na kuitazama sura yake. Meno aliyakenua kuangalia kama kulikuwa chochote chenye kumtia mashaka. Hakuridhika! Alilifuata galoni la maji lililokuwa chini karibu na mlango. Aliliinamisha na kukinga kiganja chake wakati akiyamimina na kuyatia maji kinywani. Alisukutua meno kwa kidole na kutema kuuondoa utando wa ugoro na sigara. Tayari! Alirudi kwenye kioo tena kujikagua. Wakati huo mikunjo usoni na mashavuni vilimnyima furaha. Hakufa moyo, bado alitabasamu na kujipa hamasa. “Utu uzima dawa, lazima Carolina nitampata. Carolina yatima hawezi kunishinda. Nitatumia kila hila kumtega. Nipo tayari kwa lolote,” alisema Koi nafsini mwake. Alitaka kuidandia baiskeli ili aondoke haraka. Mkewe aliyekuwa jikoni akiandaa chakula cha mchana alipomwona katika harakati za kuondoka ilimbidi atoke nje.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    “Koi, Safari ya wapi hata kuniaga mkeo hakuna? Tena nakuona mwenzangu unajikagua kama mtoto wa shule, kulikoni!” Mama Tunu alikuwa kasimama na mwiko mkononi. Macho yalikuwa yakibubujikwa machozi ambayo yalisababishwa na moshi mkali wa kuni na magunzi aliyokuwa akipikia. Koi alikuwa kasimama akingojea mkewe amalize kuzungumza.



    “Mama Tunu, mtu mzima haulizwi aelekeako, huulizwa atokako! Hivi umri huu unaweza kuuliza ninakoelekea? Sawa. Naenda kwa Malecha. Kuna jambo muhimu nataka nikamwone, sasa hivi tena nishachelewa,” Koi alieleza. Aliipanda baiskeli na kutokomea. Alimwacha mama Tunu akiwa kasimama akimsindikiza kwa macho. Alikitingisha kichwa wakati akiondoka kurudi jikoni.



    Koi aliendesha baiskeli kwa kasi. Jua lilikuwa kali hivyo alifanya hima afike lingali bado halijamchoma. Alipokaribia nyumbani kwa Malecha, alisimama kwenye mti mkubwa ili kulikausha jasho lililokuwa limemtoka. Pua zake alizielekeza kwenye makwapa afahamu endapo alikuwa hatoi harufu ya jasho. Baada ya muda aliipanda baiskeli na kuingia upenuni kwa Malecha kwa mikogo.

    “Hodohodi wenyewe!” Koi alibisha hodi. Moja kwa moja alielekea kwenye mwembe mkubwa. Huko Malecha alikuwa kajilaza akipunga upepo wakati huo wa jua kali.



    “Oh! Karibu Koi. Karibu sana. Naona umetukumbuka! Tangu harusi ya Tunu hadi leo hatujaonana. Ulipotelea wapi?” Malecha alimkaribisha Koi huku akimfikishia mkono wa salamu.



    “Kweli kabisa, siku nyingi zimepita. Nilikuwa na kazi nyingi, kutwa-kucha. Na huu ukame, basi najikuta nashinda bustanini nikihaha kupata maji. Lakini leo nikaona lazima nije japo kwa dakika chache kukujulia hali,” Koi alizungumza. Macho aliyapepesa ili apate kumwona Carolina. Malecha alichukua kata na kuchota maji yaliyokuwa kwenye sufuria dogo. Aliyatia kinywani na kuyameza.



    “Vipi, Tunu huko chuoni kwake hajambo?” Malecha aliuliza. Tabasamu lilienea mdomoni.



    “Hajambo kabisa, tena afya imemjaa tele. Tumbo jema huzaa chema. Tunu hajambo na kizuri zaidi chuo amekifuzu. Kwa sasa anangojea kutunukiwa shahada ya uhodari,” aliongea Koi. Tabasamu lilikuwa likining’inia mdomoni. Alitoa taarifa ya kuwa, Tunu ambaye alikuwa darasa moja na Carolina aliolewa na tayari alikuwa mjamzito. Malecha alimpongeza. Malecha alishikwa na kikohozi kilichomfanya anyanyuke na kwenda kulitema kohozi shambani. Koi aliwaza jinsi ya kufanya ili apate kumwona Carolina japo kwa macho. Kama akipaparika kama kuku atafutaye mahali pa kulitaga yai. Alikosa utulivu.



    “Leo umebaki peke yako kama mkia wa mbuzi?” Alihoji Koi. Muda huo aliyaangaza macho yake sehemu ambayo alihisi Carolina angekuwa. Malecha hakufahamu hawaa aliyokuwa nayo Koi hadi kuuliza swali lile.



    “Hapana. Ushaona mwanakichuguu huishiwa mchwa? Sipo peke yangu. Carolina yupo jikoni anaandaa chakula,” Malecha alijibu. Koi alifikwa furaha kusikia hilo. Ilimpasa kutafuta njia bora ambayo ingeweza kumfikisha Carolina mahali pale. Alizipanga mbinu kichwani kama mcheza bao. Baada ya sekunde chache, alipata mbinu. Aliliangalia sufuria la maji ya kunywa lililokuwa karibu yake. Alikikokota kigoda alichokuwa nacho upande upande akiwa kakusudia kufanya hila. Nia yake ilikuwa kuyamwaga maji yote. Alijisogeza kama mwenye kuikwepa miali ya jua iliyojipenyeza katikati ya matawi ya mwembe. Hatimaye aliligonga sufuria na maji yote yalimwagika. Ardhi iliyokuwa na kiu iliyameza mara moja.



    “Samahani Malecha. Naona maji yote yame…” Kabla hajamaliza kuongea Malecha alidakia.



    “Bila samahani. Usidhani kiu tunayo peke yetu, hata ndugu walioko chini nao wanayo. Hivyo hii ni stahiki yao,” Malecha alisema kwa upole. Aliliokota sufuria na kuliweka wima. Koi alitulia kidogo akijaribu kukiweka kigoda sawa. Ilipita dakika chache wakiwa katika mazungumzo yaliyorukia hekaya mbalimbali za maisha ya ulimwengu. Japo walizungumza mengi, Koi alikuwa akitia maongezi makusudi akitafuta nafasi ya kuchomeka yake. Alitaka kufanya jambo ambalo tayari mtego wake ulikuwa tayari ukifanya kazi.



    “Malecha, nahisi kiu kunikaba, mazungumzo na jua kali yataka kipozeo. Naweza kupata maji ili angalau koo langu nilifurahishe?”



    “Koi, hapa kwako. Tangu lini mwenye mji akawa mtumwa ndani ya nyumba yake? Mji wangu wako, wako wangu. Ngoja nimwite binti atusaidie,” Malecha aliita kwa sauti. Carolina aliyekuwa jikoni akianda chakula aliitika.



    “Abee baba! Nakuja,” Carolina alitoka jikoni. Aliyafikicha macho yaliyotokwa chozi kwa sababu ya moshi mkali wa kuni. Alipofika alipiga magoti na kumsalimia Koi kwani ilikuwa adabu kwa mtoto kumsalimia mtu mzima. Usoni kwa Carolina hapakuwa na bashaha. Aliukumbuka udhalimu wa Koi na hakufurahishwa na uwepo wake. Baada ya salamu, Malecha alimtaka Carolina kuwapatia maji. Alienda na kuwajazia maji kwenye sufuria kisha kuwatengea. Wakati Carolina anaondoka, jicho la Koi liliganda kumtazama kwa nyuma juu chini. Malecha alimkazia macho Koi akimshangaa. Aliuchukua mkongojo na kumdokoa mguuni kumgutua.



    “Koi! Lawalawa za watototo wazitolea macho!”



    “Ah! Mtoto amekua. Hujapata posa aolewe? Umri alionao unaelekea kupata lawama. Mabinti siku hizi hawatakiwi kutunzwa kama mbegu za boga, watabunguliwa,” Koi alizungumza akiwa kamkazia macho Malecha.



    “Kila jambo lina wakati wake. Sijapata wa kumposa bado. Lakini Koi unajua kuwa binti huyu si mwanangu wa damu. Nina mtihani mkubwa maana anataka kusoma. Tena hajui kama si mwanangu wa damu. Tangu mama yake afariki na mimi kumchukua akanyonya kwa mke wangu, anajua ni wa hapa,”



    “Malecha, sisi ni marafiki muda mrefu, tangu lini mgomba ukabeba kole la nazi? Haiwezekani kusomesha mtoto wa kike kama Carolina. Tena sio kwa sababu ya usichana wake tu, huyu ni laana! Kwanza si mwanao. Pili hana ukoo. Unategemea akisoma atakujua? Fanya aolewe na huko ataanzisha ukoo wake?” Koi aliyatoa maneno mfululizo. Malecha yalimwingia akabaki kimya.



    “Mguu wangu na jua hili, nimekuja kwa hilo. Si busara kuona nyumba ya jirani inafuka moshi pasipo kumjuza kabla haijaungua. Nimekuja kukufunulia fumbo,” alisema Koi. Malecha alishikwa fadhaa kumsikia Koi akisema maneno hayo. Koi alimsogelea Malecha sikioni.



    “Carolina si mwanamwali.”



    “Una maana gani Koi?”



    “Najua umesikia. Huyu ni komamanga lenye chongo mtini. Siku likionekana kuiva litakuwa limeoza na halifai tena kuliwa. Wanaume wameshamtuma sokoni na kikapu,” Mzee Koi alizungumza kwa kujiamini. Malecha aliduwaa. Kila alipojaribu kutafakari hakuyaamini maneno ya Koi. Alimdadisi Koi ili kuujua ukweli. Alimwamini Carolina kuliko watoto wa kike wote waliokuwa katika kijiji hicho. Koi alieleza mambo mengi yaliyojaa chumvi dhidi ya Carolina. Koi hakuwa ametosheka, aliendelea kumchanyanta Carolina.



    “Unajua mie sivai miwani hadi nisiweze kuona nikiwa sijaivaa. Kwa macho yangu haya, uso kwa uso nilimkuta binti akicheza tarazia kama samaki majini. Tena matusi na kijana wa Dendego, mchana kweupe chini ya mwembe,” Koi aliongeza. Malecha alihamaki.



    “Ehh! Wapi huko? Na—na—ni nani huyo kijana wa Dendego?” Aliuliza Malecha wakati mdomo ukimcheza. Povu lilikuwa limeanza kumtoka kwa hasira. Fadhaa ilimvaa kwa kuvuliwa nguo. Moyo ulizizima kwa aibu. Mapigo ya moyo yalimshuka na mwili kunyong’onyea. Hakuwahi kuwaza kama Carolina angeweza kuwa chakaramu akifanya mambo ya aibu hadharani. Upande mwingine nafsi ilimshawishi kumwamini Koi.



    “Mtoto wa Dendego jirani yangu! Yule kijana aliyezaliwa masika moja kabla ya mamaye na Carolina kufariki. Ni yule anayesoma shule yetu ya kata pale ng’ambo ya mto. Chunguza utagundua. Huyu binti ni sawa na mlanguzi hekaluni, hana ibada lakini sadaka anachukua. Usipoangalia atakuletea laana juu ya nyingine. Hana baba wala mama, tena atakuletea mjukuu asiye baba wala shangazi. Mjumbe hauawi, yangu ni hayo naenda zangu,” Koi alisema na kuidandia baiskeli yake, aliteleza kwenda kwake. Nafsi ya Koi ilishangilia kuupata ushindi, ilitulia. Alijua Carolina angepatwa timbwili ambalo lingefuatwa na misukosuko ili aweze kumpata kwa wepesi.



    Akiwa kaketi chini ya mwembe, Malecha tumaini lilimtoka. Moyo uliingiwa simanzi. Alikuwa njia panda akiiwaza barua ambayo alipewa ikimtaka kumpeleka Carolina katika shule binafsi ili ajipatie elimu yake ya sekondari. Akiwa anawaza, Carolina alifika kutenga maji ya kunawa na chakula. Alipiga magoti kumkaribisha baba yake kwa chakula cha mchana. Malecha alimtazama Carolina usoni pasipo kusema neno. Carolina alihisi kuwepo kwa tatizo kwani kabla ya ujio wa Koi alikuwa na uo wa furaha. Alihisi lilikuwepo jambo lililokuwa limeenda upogo mbele ya baba yake.

    Chakula ada yake kuliwa, Malecha alikula chakula akiwa katikati ya msitu wa maswali. Aliuahidi moyo kuzifuatilia nyendo za Carolina ili kuubaini ukweli.



    *****

    Saa 7:59 alasiri, kengele ya shule iligongwa. Sauti yake iliyaumiza masikio ya kila mwanafunzi. Usikivu ulipotea huku kila aliyekuwa akimalizia zoezi lililoachwa na mwalimu alijitahidi kuikamilisha. Waliokuwa wamechelewa walichukua daftari za marafiki na kunakili majibu ilimradi kukidhi matakwa ya kukusanya baada ya kengele kugongwa. Hatimaye viranja wa madarasa walikusanya daftari hadi ofisini kwa walimu. Waliingia na kuyafutika madaftari juu ya meza na kutoka pasipo kuongea. Wakati wakiingia walimu walikuwa kimya wakiwangoja viranja kutoka ili waendelee na mjadala uliokuwa ukiendelea. Ilionesha walingojea dakika chache kufikia hitimisho.



    Wanafunzi wote baada ya muda walikuwa wakimiminika kama siafu kuelekea kwenye mistari. Walijipanga kwa kufuata utaratibu wa madarasa kama walivyozoea. Kiranja wa zamu alisimama mbele na kutoa amri walizozizoea. Wimbo wa taifa uliimbwa, ulifuatiwa na wimbo wa shule tayari kuimaliza siku. Bendera nzuri ya rangi nne ilipepea—njano, nyeusi, kijani na bluu ilipunga mkono kila upande. Jua lilikuwa limesimama wima katikati ya vichwa vya wanafunzi ambao matumbo yalikuwa yakiwasokota kwa njaa. Baada ya wimbo wa shule, kiranja aliwaamuru kugeuka — kushoto, kulia, mbele na nyuma. Wote walitii amri kwa kujikokota. Jambo hilo liliwafanya kupandwa na jazba, walianza kunong’ona. Kiranja alijaribu kuwanyamazisha lakini hawakunyamaza. Wakati kiranja akitaharuki, mwalimu wa zamu alitoka ofisini. Mkono wa kushoto alishika kipande cha karatasi na mkono wa kuume alishika rundo la henzirani. Uso ulijaa ndita kama matuta kwenye mteremko wa mlima. Alitembea kwa ukakamavu hadi mbele ya bendera. Alisimama na kuutupia chini mzigo wa henzirani. Vumbi laini lilichokozwa, lilielea kwenda zake. Wanafunzi waliokuwa mbele bado waliendelea na minong’ono. Mwalimu aliyazungusha macho kutokea kulia hadi kushoto kwa ghadhabu, hakusema neno. Aliyaelekeza macho upande wa kushoto kutoka pale aliposimama, bado wanafunzi walikuwa wakisukumana na kutekenyana. Alimtazama mwanafunzi ambaye alikuwa kachelewa kufika mstarini kwa sababu ambayo hakuijua. Macho yalimtoka mdomo nao ulifunguka kufoka.



    “Kauzeni pita mbele, haraka!” Alisema mwalimu akiwa anaikunja mikono ya shati lenye madoadoa kama chui.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Atamia mchanga,” alisema mwalimu. Alimsukuma mwanafunzi, uso wake ukaliparamia dongo jekundu. Wakati mwanafunzi anajifuta lile vumbi, guu la mwalimu lilitua mgongoni kumkanyaga. Mwanafunzi alitulilia, kifua kililifuata vumbi kwa kasi, aliliatamia. Hofu ilizidi kumtikisa. Kila alipojaribu kuzungumza alihisi kumpandisha hasira mwalimu aliyekuwa na kiboko mkononi. Mwalimu alikinyanyua kiboko juu na kukitua kwa ujazo matakoni. Kilitoa mshindo kama kuni kavu iliyolazimishwa kuvunjika. Siahi zilimtoka mwanafunzi akijaribu kuurudisha mkono mmoja nyuma. Aliyapapasa makalio na kulalama. Kilifuata cha pili na kumfanya mwanafunzi amkumbuke mama yake. Meno aliyakutanisha akazizima kwa uchungu. Aliutuma tena mkono kujipangusa. Hakujua, maumivu ya henzirani hayafutwi kwa kiganja.



    “Ukishika nafuta,” mwalimu alitamka. Alijiandaa kuvunja kuni nyingine ya tatu. Mapigo ya moyo yalimwenda mbio barobaro yule huku chozi likimwagika kwa uchungu.



    “Simama!” alisema mwalimu. Tai iliyokuwa shingoni ilipepea kushoto na kulia. Mwanafunzi alinyanyuka. Aliifuta mikono wakati macho yake yakiwa kwenye unasi wa wanafunzi waliokuwa katika mistari.



    “Ulikuwa wapi hadi uchelewe, tena unatembea kama dume la nyani. Tazama, shati hujachomekea!?” Mwalimu alimsaili mwanafunzi wake.



    “Mwalimu, tumbo linanisokota. Naendesha mwalimu!” Alijibu mwanafunzi. Macho yake yalikuwa yamefurika machozi. Shati jeupe lilijaa vumbi wakati mgongoni lilikuwa limekolea alama ya nyayo ya kiatu cha mwalimu aliyemwadhibu.



    “Rudi mstarini haraka,” Mwalimu aliamuru. Alimsindika kwa kiboko komoja mgongoni. Mwanafunzi alikimbia kuelekea mstarini kujipanga. Wanafunzi walimtazama mwalimu kwa jicho la kuiba. Waliokuwa wakisogoa walinyamaza kama redio baada ya umeme kukatika. Kimya kilitawala. Jua lilizidi kusimama katikati ya anga na kuwaunguza. Mwalimu aliendelea kuwatazama wakiwa kimya, mashati yao yalipepea kwa upepo uliokuwa ukivuma na kulikusanya vumbi hadi miguuni mwao. Mwalimu alisogea mbele kidogo, alisimama. Macho yake makubwa kama bundi aliyazungusha kama kinyonga akiwatazama.



    “Mguuuuu-pande!” Mwalimu aliwaamuru. Wanafunzi walitanua miguu yao. “Mguuuuu-sawa!” Mwalimu aliendelea. Wanafunzi waliikusanya miguu wakiwa wamekakamaa. Aliwatazama wakiwa mguu sawa, walitikisika kama tufe kwenye upepo. Hiyo yote ni sababu ya njaa. Mwalimu aliwaamuru tena na tena kisha alitoa amri nyingine. “Nyumaaaa-geuka!” Waligeuka kwa kujikokota. Baada ya muda palikuwa na ukimya wa kutosha.



    “Wimbo wa nidhamu unafuata, imba!” aliwaamuru. Wanafunzi kwa ukakamavu na kwa sauti waliimba kwa kupokezana, wasichana kwa wavulana. Wavulana waliimba kwa sauti nzito wakati wasichana waliitikia kwa sauti nyembamba. Wimbo uliimbika vizuri, wanafunzi nao waliimba kwa madoido. Kwa muda wote hawakufahamu kilichokuwa kikiendelea. Wengi walijua muda wa kwenda majumbani ulitimia.



    Baada ya muda mfupi, walimu watano walitoka ofisini na kujongea mbele ya mkusanyiko wa siku ile. Walitembea hadi pale mwalimu wa zamu alikuwa amesimama. Wote walikuwa kimya na sura zao zilikula ndimu. Mwalimu wa zamu alikinyosha kuelekea kwa mvulana aliyekuwa mbele ya mstari waliposimama wanafunzi wa kidato cha tatu. Alifanya ishara kumuita.



    Mwanafunzi alitoka kuelekea kwa mwalimu. Aliagizwa kufuata kiti kirefu cha mbao kilichokuwa ofisini. Alipokuwa anarudi wanafunzi waliguna. Muda huo walianza kuhisi jambo kwani kiti kile hutolewa wakati wa kutoa adhabu maalum. Kila mmoja mapigo ya moyo yalianza kumdunda kama kitenesi juu ya sakafu. Kiti kiliwekwa mbele na wanafunzi walikitazama kwa hofu. Kitendawili hakikuwa kimepatiwa jibu. Mwalimu wa zamu aliuvunja ukimya. Aliifungua karatasi iliyokuwa mkononi na kuitalii kwa macho. Aliwatazama na kubaki kimya kidogo.

    “Wanafunzi hamjambo?”



    “Hatujambo, shikamooo mwalimu!” Umati uliitikia kwa sauti.

    “Marahaba,” mwalimu aliitikia. Alisimama thabiti na kuzivuta pumzi. “Mniwie radhi mchana wa leo kwa kuwachelewesha kwenda makwenu. Bila shaka mnafahamu kuwa kiti hiki mbele yenu huwa kinafuatwa na jambo zito.”



    “Ndiyo mwalimu,” Wanafunzi waliitikia kwa unyonge.

    “Kuna utovu wa nidhamu uliopindukia miongoni mwenu. Tunalazimika kulikomesha hili ili iwe fundisho kwa yeyote. Shuleni ni mahali pa kujipatia elimu wala si sehemu ya kufanya uasherati. Mnanisikia?” alieleza mwalimu.



    “Ndiyo mwalimu,” wanafunzi wachache waliitikia. Mwalimu aliichukua tena karatasi, alimuita kiranja mkuu na kumpatia. Kiranja mkuu hakujua afanye nini. Alielekezwa kusogea mbele ya wanafunzi ayasome maandishi yaliyokuwa kwenye karatasi ile kwa sauti.



    Kiranja alisoma:



    Kipenzi Carolina,



    Salamu sana.



    Ama baada ya salamu, mimi ni mzima wa afya ingawaje roho inaniuma. Nimekuwa nikiwaza kila wakati kwa nini umebaki kimya tangu barua yangu nikuandikie wakati ulipokuwa ukijiandaa kuhitimu darasa la saba. Bila shaka ni kipindi kirefu kimepita tangu wakati huo lakini najua unakumbuka.



    Kinachoniuma sana ni mara baada ya kukukuta umekumbatiana na Koi kule bustanini. Jambo hilo halikunipendeza bali liliniumiza sana. Kila nikiingia darasani kusoma nahisi napoteza muda. Kila mwalimu aingiapo naona kama ananipotezea muda wa kuendelea kutafakari hatima ya upendo wangu kwako.



    Kwa barua hii, nakujulisha kuwa nipo tayari kwa lolote ili tuweze kuishi pamoja. Wewe ni msichana mdogo hustahili kuwa na wazee wasio mbele wala nyuma. Niamini nitakuoa. Wewe ndiye malkia na mama wa watoto wangu. Ukinikubali nitasoma kwa bidii ili nitafute riziki ya watoto wetu utakao nizalia. Kwa kifupi mimi nakusomea wala usihangaike na kazi za bustani.



    Tafadhali nakuomba, upatapo barua hii unijibu kwa haraka ili kutuliza wahaka moyoni mwangu. Majibu naomba unipatie kwa barua. Mpatie Huruma ili aniletee na kama utashindwa kumpatia, ifukie barua kwenye mchanga pale njiapanda ya kwenda shuleni kwetu karibu na jiwe kubwa, kata jani la mwembe uliweke juu yake, nitajua kwa urahisi.



    Nakutakia siku njema. Nakupenda sana kuliko maisha yangu.

    Tamati namaliza, moyo wangu unaumia.

    Usiponijibu utaniua kwa huzuni.



    Ni mimi nikupendaye,



    Roy au ROC!





    Wakati yakisomwa maandishi katika karatasi ile, wanafunzi wote walikuwa kimya. Saraganda ambaye ni kaka yake Carolina alikuwa katikati ya msitu wa mawazo. Aliposikia jina la Carolina hakupata jibu kama ilimhusu dada yake pacha. Muda uleule alihisi kuwa ndiye kwani ni yeye pekee mwenye jina hilo ambaye alikuwa mwenye kazi ya bustani. Kilichokuja kummalizia utata ni kutajwa kwa Huruma katika barua ile. Saraganga furaha haikuwa naye, alijawa huzuni. Alikumbuka jinsi alivyojaribu kumpigania ili apate elimu ya sekondari. Hatimaye chozi lilimtiririka Saraganda kimyakimya. Alishindwa kulizuia. Roy aliyeandika barua alikukuwa akitetemeka mwili mzima. Jasho jekejeke lilimtoka akijuta kuiandika barua. Alitafakari jinsi walimu waliipata barua, ukweli alikuwa amechelewa kuujua. Alichokuwa akikikumbuka ni kuwa, aliipachika barua hiyo kwenye daftari la hisabati usiku wakati akifanya zoezi na huko ndiko alisahau kuitoa. Kwa kuwa kipindi cha hisabati kilikuwa cha kwanza, alijikuta akilikusanya daftari likiwa na barua ndani. Alijutia kupitiwa kwake.



    Baada ya barua kusomwa, walimu waliendelea kunong’ona. Mwalimu wa zamu alimwita Roy na kumtaka kupita mbele. Uso wake ulijawa hamaniko wakati machozi yalitiririka na kudondoka kama matone ya mvua. Hukumu iliyofuata ilikuwa kali.

    “Roy, unaijua barua hii?” Mwalimu aliuliza.



    “Ndiyo mwalimu,” Roy alijibu. Wanafunzi waliokuwa mstarini wote waliguna kisha kunyamaza.



    “Carolina unamjua?” Alidadisi mwalimu. Roy alinyamaza kidogo akiyapepesa macho yake harakaharaka kama mtu aliyekuwa akikaribia kulia.



    “Ndiyo namfahamu. Ni dada yake Saraganda. Anaishi kijijini hapa, lakini hasomi,” Roy alijitetea. Mwalimu aliposikia jina la Saraganda aliunyanyuo uso kumtazama Saraganda. Saraganda alijiinamia kama mgomba ulioelemewa na mkungu. Mwalimu hakutaka kumsumbua wala kumshirikisha kwa jambo hilo. Wanafunzi vilevile waliyaelekeza macho kwa Roy. Minong’ono iliendelea huku sauti nyingi zikisikika kusema kwa utani, ‘shemejiii!’



    Ilipaswa Roy kuadhibiwa kutokana na kukosa nidhamu. Kila mwalimu aliyekuwepo alimchapa viboko vitano vya nguvu. Alilia na kupiga kelele kama mbuzi achukuliwaye kwenda machinjioni. Machozi yalimtoka na kamasi jepesi lilimiminika kutokana na ukali wa viboko. Roy aliahidi kutotenda kosa tena bali alisema angekuwa na tabia njema.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Baada ya Roy kuadhibiwa, wanafunzi waliruhusiwa kutawanyika. Kila mmoja alielekea makwao. Njiani kote wanafunzi walisimuliana na kuzungumza juu ya tukio la siku hiyo. Kila alipopiga hatua, Saraganda alihisi dunia kumzomea na kumfanya ajawe na aibu kubwa. Furaha ilimtoka na kuwa mnyonge asiyeweza kujitambua.



    Roy alienda zake akiwa peke yake. Hapakuwa na ambaye alimsindikiza ama alienda naye njia moja kwa hofu kuwa angedhaniwa kuwa ni ndege wa kundi moja. Alinung’unika kuwa aliadhibiwa pasipo ukweli kuwa Carolina alikuwa mpenzi wake au la. Alijikaza kisabuni na kuupiga moyo konde akiamini kuwa lenye mwanzo lingekuwa na mwisho. Wakati huo aliapa kumpata Carolina kama mpenzi kwa udi na uvumba.



    Akiwa njiani, Saraganda alikuwa na maswali mengi fikrani. Kilichomuumiza zaidi ni kutajwa kwa Koi kwenye barua kuwa ndiye alikutwa kamkumbatia Carolina bustanini. Hakuweza kuamini kama kweli dada yake alifanya hayo pasipo yeye kuwa hata na chembe ya fununu.



    Roy aliuonja uchungu uliotokana na siri aliyoikumbatia. Alikuwa amefunga siku yake ya masomo kwa chozi ambalo ampendaye hakuwa akijua. Macho yake yaliiva na kuvimba kwa kilio. Kila aliyekutana naye alitambua kuwa alipatwa na tashwishi. Alitembea wanguwangu huku mwili wake ungali ukiyasikia maumivu makali. Tembea yake kisha ilimfikisha kwa Koi. Aliyatupa macho na kuwaona wakicheza karata. Roy alirusha salamu kuwasabahi, mama Tunu aliitikia wakati Koi alibaki kimya.



    “Mtoto huyu laana tupu! Simpendi kama haja ya mbwa njiani?” Alisema Koi. Mama Tunu alishangaa kuyasikia maneno hayo yakitoka kinywani mwa mmewe. Alizifutika karata kwenye mkeka kisha kumsindikiza Roy kwa macho.



    “Anatatizo gani hadi salamu yake usiitikie? Kama salamu mtoto kakusalimia nawe hutaki kuitikia. Kuna nini?” Mama Tunu alimhoji mmewe. Koi alikuwa kimya. Alimkazia macho mkewe angali kichwani alikuwa akitunga jawabu la kujibu.



    “Hivi hujasikia kuwa huyu ndiye kuwadi aliyemvuruga Tunu hadi akaribie kukataa kuolewa. Na sasa huyuhuyu anampa jeuri binti wa Malecha asiweze kuolewa. Eti wanadanganyana anataka asome. Kuwadi wa kiume huyu. Anajidai kijogoo kokoriko wakati akiona mwewe anajificha mbawa. Hana adabu hata chembe. Kwa taarifa yako, nilimkuta mdomo kwa ulimi na Carolina mchana kweupe. Uliza alikuwa anafanya nini sasa? Yakitandani yalishuhudiwa na kivuli cha mwembe,” Koi alidondoa maneno. Mama Tunu alishikwa bumbuwazi kwa aliyoyasikia. Koi alinyanyuka na kuondoka. “Wanawake akili huwa mnaziacha tumboni mwa mama zenu. Hata jambo usilolijua unataka tu kuamini unavyodhani wewe. Hujui hata komba-mwiko hujidai anaweza kula nyama wakati yake ni majani. Tangu lini kinda la kuku likamshinda mbio mwewe. Huyu anajisumbua tu. Nimemwambia Malecha sijaacha hata irabu moja,” Mzee Koi alisema wakati akiingia ndani.



    Wakati akiwa kagubikwa na unyonge, Saraganda aliwasili nyumbani kwao. Ilivyokuwa desturi ya Carolina, kila alipomwona kaka yake akiwa anatoka shuleni, alimkimbilia kumpokea mkoba. Siku hiyo haikuwa njema kwa Carolina. Alipomkaribia tayari kuushika mkoba wa daftari, kaka yake alimsukuma. Carolina alianguka chini. Alijizoazoa kutoka vumbini na kulikung’uta vumbi lililokuwa limelichafua gauni lake. Alimtazama kaka yake ambaye alikuwa akiingia ndani pasipo kusema neno. Mama Saraganda na mumewe ambao walikuwa kwenye mti wa mwembe waliona kila kitu kilichokuwa kikitokea. Hali ile iliwastaajabisha na wote waliingiwa taharuki. Ilipita dakika chache, Huruma naye alifika kutoka shuleni. Akiwa na shauku ya kukutana na kaka yake, kwanza alienda mbio akapiga magoti kuwasalimia wazazi wake. Aliponyanyuka aliingia ndani huku akiwa anaita kwa sauti ya juu.

    “Kaka Sarrr!” Aliita Huruma. Kaka yake hakuitikia. Huruma alipoingia ndani alikutana na kaka yake akiwa njia moja kutoka nje ya chumba chake. Alimsalimia kwa adabu lakini alibaki kimya akimtazama kwa jicho ambalo alidhani ni utani wa kaka yake. Saraganda alifura hasira. Huruma aliunyosha mkono kulishika shati la kaka yake huku akiendelea kuita.



    “Kakaaa! Njaa gani mpaka usiitikie salamu mdogo wako nakusalimu!?” Huruma alihoji. Saraganda hakutoa neno, alimkazia macho. Hasira zilimpanda akauchomoa mkono wa kulia. Alikikunjua kiganja na kumzaba kibao. Huruma alianguka vumbini wakati kilio kilifuata. Alinyanyuka na kwenda mbio walipokuwa wameketi wazazi wake. Malecha na mama Saraganda walinyanyuka baada ya kusikia siahi aliyoipiga. Walimtazama usoni na kuuona uso ukiwa umevimba na kutapakaa alama ya vidole vya Saraganda.



    “Kwa nini leo umejawa kisirani? Kisa cha kumpiga mdogo wako! Hata siku moja sijawahi kukuona ukifanya hivi. Kwa nini Saraganda? Wamekukosea nini au tayari umejiunga na wavuta bangi huko shuleni?” Alifoka Malecha. Saraganda alijibu kwa kupiga hatua hadi kwenye mti wa mwembe. Aliufikia mkeka na kuketi. Aliliegemea shina la mwembe akiwa bado katikati ya tafakuri nzito. Carolina bado hakujua tatizo lililokuwa limemsibu kaka yake. Alichukua chakula kwenda kumtengea akijua alikuwa na njaa. Saraganda hakutaka chakula. Hasira iliikomesha njaa yote. Katika maisha yake hakupenda kufedheheshwa kwa lolote. Alipenda ahukumiwe na atambulike kuwa ni mnyoofu na familia nzima alipenda kuwa kama mawazo yake yalivyomtuma.



    Carolina alipofika alikitenga chakula juu ya mkeka kwa heshima. Alipiga magoti na kumualika kama alivyokuwa amezoea. Saraganda alikitazama chakula kisha kumtazama Carolina usoni kwa hasira. Alinyanyuka na kukipiga teke chakula kikamwagika na kutawanyika kwenye mchanga. Carolina kwa uoga alivikusanya viganja vya mikono yake na kuufunika mdomo akiwa kajawa mshangao. Saraganda alinanyuka na kuchepua miguu yake kuingia ndani. Alilichukua panga na kulichomeka kiunoni akitokomea kuifuata njia iliyokuwa ikipita kwa Koi. Familia walibaki wameduwaa wakimsindikiza kwa macho.

    Wakati Saraganda akitoka nyumbani na silaha mkononi, Dendego alikuwa ameketi mbele ya nyumba akipunga upepo. Roy alikuwa ndani akipata chakula cha mchana baada ya kutwa nzima yenye mateso. Hakuwa ameyasahau maumivu yaliyoufanya mwili kuchemka. Macho yake yaliangaza nje kupitia kwenye mlango uliokuwa wazi na kumfanya amwone yeyote aliyekuwa akikatiza mbele ya nyumba yao. Alipoyaangaza macho nje, alimwona Saraganda akiwa kavaa fulana nyekundu. Alikuwa akitembea kwa kasi. Alihofu kuwa, ujio wa Saraganda ungeweza kumfanya baba yake kujua jambo ambalo alikusudia kulifanya siri. Alikuwa amekusudia kulificha jambo hilo ndani ya mvungu wa moyo wake.



    Akiwa mwenye wasiwasi, Roy alikisukuma chungu cha ugali pembeni. Alinawa na kunyanyuka. Japo alitamani kujificha, dhamira yake ilimtuma kukabiliana na chochote ambacho kingetokea. Aliupiga moyo konde akiamini kuwa, kulikwepa tatizo si njia ya kulisuluhisha bali ni kupambana nalo. Aliishika kata ya maji ya kunywa na kuyamimina maji mdomoni. Saraganda alikuwa hatua moja mbele aingie upenuni kwao. Dendego aliuinua uso na kukutana uso kwa uso na Saraganda aliyekuwa akipumua kama mbwa aliyeponyoka kwenye domo la fisi. Macho yalimuiva wakati kijasho chembamba kilimtanda usoni.

    “Shikamooo!” Saraganda alimsabahi Dendego.



    “Marahaba. Mbona hivyo? Kuna tatizo?” Dendego alihoji. Alimpatia Saraganda Kigoda.



    “Mwanangu, kuna tatizo gani? Mbona pumzi zimetangulia mbele yako?” Dendego aliuliza. Kifua cha Saraganda kilimwenda juu kisha kilishuka kwa ghadhabu. Koo lilimkauka. Alijaribu kuyameza mate lakini hayakuwepo. Saraganda alikipokea Kigoda na kukitupia chini. Alibakia kusimama wima. Dendego alimtaka Roy kutoka nje. Roy alipotoka, Saraganda alimsogelea na kumkwida. Alilichota koromeo na kumfanya apumue kwa shida. Roy na Saraganda waling’ang’aniana na kuangushana chini. Mzee Dendego alibaini kitu, kiunoni kwa Saraganda kulikuwa na panga. Alimwendea na kulikwapua.



    “Saraganda nisamehe. Sijakusudia. Nisamehe,” Roy aliomba msamaha wakati akijaribu kujinasua mikononi mwa Saraganda. Dendego alijaribu kuwaachanisha lakini alishindwa.



    Alipolichukua lile panga na kulisugua chini, Saraganda alimwacha Roy na kumvaa Dendego. Alimparamia na kumfanya aliachie panga. Alilizoa na kumfuata Roy. Alimpalaza Roy sikioni na kumpatia jeraha lililosababisha damu kuchuruzika. Dendego alikuwa ameshaingia ndani na kutoka na mkuki. Baada ya kuyaona hayo, Saraganda alilitupia chini panga na kutokomea zake. Alikwenda njia nzima akiwa anafoka. “Sitaweza kuwasamehe. Wewe na Koi lazima mlipe. Aibu mliyoiletea familia yangu ni kubwa. Hatumalizii hapa mpaka kieleweke.”

    Kwa kuwa Dendengo hakujua lolote, alibakia kuduwaa kama mlevi asiyejua chanzo cha vurugu zile. Roy aliufumba mdomo. Macho yalimtoka wakati akilifungafunga jeraha kwa mshubiri. Damu ilikoma yangali maumivu yalikuwa yangalipo. Machozi yalimlengalenga, alijua siri ilikuwa katikati ya kijiji kama mtama kwa kuku wengi ugani.



    Saraganda alipoondoka kurudi nyumbani aliendelea kuyarusha maneno. Sauti yake ilimfikia Koi. Masikioni yake yaliyokuwa kama sinia yalifikiwa na kila neno ambalo Saraganda alikuwa akilitamka na kumtaja. ‘Hatutamaliza. Koi ni nani? Roy ni nani mpaka yatokee haya. Nawaambia mtalipa kwa jasho hata kwa damu.’ Maneno ya Saraganda yaliyomwingia Koi na mkewe wakiwa wamesimama mbele ya nyumba yao baada ya kuzisikia vurumai. Kila mmoja kwa nafsi yake alibaki akijiuliza maswali aliyokuwa hawezi kuyajibu.



    Jua lilipopunguza hasira, Carolina alikuwa bado hajajua sababu iliyomfanya kaka yake kufura kwa hasira hadi amsukume na kumzaba kibao Huruma. Hata kama alikuwa amechukia alijua kuwa, muda mfupi uliofuata Saraganda angerudi kwenye hali yake ya kawaida. Alichuchukua ndoo na jembe na kuianza safari kwenda bustanini. Wakati huo hakuenda peke yake, aliongozana na Huruma.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Walipokuwa njiani walizungumza na kutaniana, Carolina aliiga vile kaka yao alimsukuma na kumzaba kibao Huruma. Wote hawakujua kama kulikuwa na jambo ambalo lililotokea shuleni na kumfanya Saraganda kuwa katika hali aliyokuwa nayo. Wakati Huruma na dada yake wakitokomea kuelekea bondeni, Saraganda alikuwa ameshafika nyumbani. Alikuwa kasimama na kuuegemea moja ya miti iliyotumika kulijenga zizi la ng’ombe. Alitaka kuupata ushaidi kama ni kweli Carolina alikuwa anahusika na yote ambayo yalitokea mchana ule. Pia alikusudia kujua kama Koi alikuwa na uhusiano wa huba na Carolina. Aling’oa nanga kutoka alipokuwa, macho yake yaliangaza kuwachungulia dada zake kama kweli walienda bustanini. Aliiona njia ikiwa nyeupe, hapo alijipatia jibu kuwa walikwenda.

    Alirudi hadi mlangoni kwa dada zake. Aliusukuma mlango na kuingia chumbani ambamo walikuwa wakilala. Alikiwasha kibatari na kuinama uvunguni ili aweze kumulika. Uso kwa pua macho yake yalikutana na mijusi wakiukimbia mwanga uliokuwa ukiwamulika. Alivuta kilindo kilichokuwa na daftari za Carolina. Alianza kupekua moja baada ya jingine lakini hakuona chochote chenye kutia wasiwasi. Aliyakodoa macho kuelekea kila upande wa chumba kile. Nia yake ilimwongoza kukipekua kikapu kilichokuwa na nguo lakini bado hakupata kiashiria chochote kibaya.



    Akiwa kakata tamaa, alisimama na kukishika kiuno wakati akitazama juu kwenye fito za nyumba pasipo macho yake kuona alichokuwa akihitaji kukipata. Alijikongoja na kuketi kwenye kitanda cha Carolina akitafakari. Mkono wake ulimtoroka ukaenda kuuchukua mkoba aliokuwa akitunzia daftari Huruma. Aliyamwaga madaftari yakatawanyika juu ya kitanda. Alianza kuyapekua madaftari moja baada ya jingine. “Mjinga nini?” Saraganda alifoka peke yake. Alikuwa kakutana na matunda ya zambarau ambazo Huruma alijikusanyia wakati akitoka shuleni. Alinyanyuka ili atoke nje ya chumba kwani hakuona alichokuwa akikitafuta. Wakati miguu yake ikimlazimisha kutoka, nafsi ilimshauri na kumtaka asitoke kwani angepata kitu. Nafsi ilipata ushindi.



    Alirudi ndani hadi chumbani. Aliivuta shuka iliyokuwa juu ya kitanda cha Huruma na kukiacha kitanda uchi. Alilibinua godoro la sufi ili macho yake yaone chochote, hakuona zaidi ya kulitimua vumbi zito lililomfanya akohoe na kupiga chafya. Alizibinya pua zake wakati kamasi jembamba likimmiminika. Alilirudishia godoro kama lilivyokuwa awali wakati pua aliibinya mara kwa mara.



    Macho yalikitazama kitanda cha Carolina kwa ukali. Alilishika shuka na kulivuta akitandua. Hamadi!. Alikiona kitu kikiwahi kuifuata sakafu yenye vumbi. Vidole vyake vilishindana akakidaka na kukitia kiganjani. “Loh…!” Saraganda alifoka. Mikono yake ilikuwa imeshika sodo lililotokana na kibwende cha kanga kilichokuwa kimegandamana. Kilikuwa kipande cha kanga ambacho dada yake alikuwa tayari kakitumia kujihifadhi kwa mwezi huo. Saraganda hakufa moyo, nia yake ilikuwa bado thabiti. Alilikung’uta shuka lililokuwa limekunjwa, aliliona daftari likidondoka chini. Aliinama kuliokota na kuketi kitandani kuanza kulipekua daftari ukurasa mmoja baada ya mwingine. “Afanaleki! Ya msichana haimsitiri wa kiume!” Saraganda alisema na nafsi yake. Saraganda alipekua daftari zima hadi mwisho. Alihisi hapakuwa na kitu chochote cha maana zaidi ya kujifunza mambo ya Carolina.



     Saraganda alilifunika daftari akitaka kulirudisha kama lilivyokuwa. Alivyoliweka akitaka kulifunika aliona kipande cha karatasi kikiwa kimechungulia tofauti na urefu wa kurasa za kawaida za daftari lile. Alizituliza fikra na kuviagiza vidole vyake kukichomoa. Alikigeuza juu akasoma maandishi yaliyokuwa yameandikwa kwa kifupi. Jicho liliganda kama barafu kwenye neno lililokuwa limeandikwa kwa hati kubwa na kusomeka, ROC. Harakaharaka aliikunja karatasi hiyo na kuizika kwenye mfuko wa kaptula yake na kutoka. Hakutaka kutandika vitanda aliondoka na  kuviacha kama vilivyokuwa kwa mshawasha wa kutaka kujua yaliyokuwa ndani ya barua ile. “Mola hamfichi mnafiki, leo nitaujua ukweli. Umdhaniye siye kumbe ndiye. Leo atanitambua,” alijisemea Saraganda wakati akiharakisha kutembea kutoka kilipokuwa chumba cha dada zake. Aliingia na kuketi kwenye kitanda kilichokuwa chumbani kwake. Aliikunjua barua na kuanza kuisoma mstari kwa mstari. Alipofika mstari wa tatu alihisi hakuwa na amani pale. Alinyanyuka na kutoka chumbani akielekea kwenye mti mkubwa. Alikwea mtini hadi kwenye tawi kubwa. Aliketi vizuri huku mgongo wake na mabega ukiliegemea tawi jingine. Alianza kuisoma barua kwa makini. Alichungulia kuiangalia njia iliyotokea bondeni kila wakati. Alipomaliza kuisoma barua neno kwa neno, Saraganda aliami kuwa Carolina na Roy walikuwa marafiki wa siri. Aliikunja barua na kuichomeka mfukoni na kwenda chumbani kwake kujilaza. Alijawa na mshawasha wa kumweleza baba yake kile ambacho alihisi kilikuwa ni chanzo cha yeye kukosa furaha tena kwa ushahidi wa barua. Wasio hili wala lile Carolina na Huruma walikuwa bustanini wakiinywesha miche. Hawakujua kama kaka yao aliwakagua chumbani na kuokota barua. Huruma na dada yake walipomaliza, waliyachota maji na kuanza kurudi nyumbani. Walipofika walizitua ndoo kisha kusimama kwa sekunde kadhaa kabla ya kuandaa chakula cha jioni. Kipindi chote cha mizunguko yao hapo nyumbani, hawakumwona kaka yao. Alikuwa ameshaamka kitandani na kwenda kufuatilia ng’ombe ambao walikuwa malishoni. Huruma na dada yake walishirikiana kuyakamilisha mambo ya jikoni ili wanafamilia wapate mlo kwa jioni ile. Baada ya kuona mambo yalikuwa sawa, huruma aliondoka kwenda chumbani kubadilisha nguo ili aweze kwenda bafuni kuoga. Alipofika chumbani macho yalishuhudia vitu vikiwa vimevurugika. Alipigwa butwaa. “Dada! Da-Caro! Njooo!” Huruma aliita. Wakati huo alikuwa na hofu kwa kile alichokuwa amekiona. Carolina alienda mbio hadi chumbani. Alipofika Huruma hakuongea zaidi ya kuitandaza mikono akionesha kwa ishara. “Nani aliingia na kuvurugavuruga hivi? Ha! Kwa nini?”



     Carolina alihoji. Huruma alikusanya na kurudishia vitu vyake ndani ya begi. Carolina hakuwa na shaka yoyote alichokifanya kilikuwa ni kukitandika kitanda vizuri na kuichukua shajara iliyokuwa juu na kuirudisha sehemu ambayo alipenda kuiweka baada ya kuipata. Baada ya kumaliza kukitandika kitanda na kuifunika shajara ndipo kumbukumbu zilimjia. Aliichukua shajara tena na kuanza kuipekua mwanzo hadi mwisho. Alikuwa akikitafuta kipande cha barua aliyokuwa ameandikiwa na mtu ambaye hakuwa amemfahamu. Kilichomfanya aitunze barua ile kilikuwa ni maneno matamu yaliyoutekenya moyo wake. Kila ukurasa aliupekua lakini hakukiona kipande kile cha barua.  Alisimama kukishika kiuno wakati akitafakari. Mkono wake wa kuume ulienda kichwani na kujikuna japo hakuwa akiwashwa kwa lolote. Hofu ilianza kumnyemelea. “Leo nimepatikana. Inawezekana ameichukua ile barua. Yawezekana ndio maana amekasirika,” alibashiri Carolina. Wakati huo Huruma aliyekuwa hajui lolote, alihoji akitaka kujua. Carolina alimweleza kuhusu barua na jinsi alivyoipata na kuitunza ndani ya shajara yake. Wasiwasi ulizidi kuimeza furaha wakati mapigo ya moyo yalimwenda mbio kama mshale wa saa. “Maskini, leo nimeumbuka, nitasemaje maana hata jibu sina? Kama simjui aliyenitumia kwa nini nimeitunza barua mpaka leo? Kama namfahamu aliyenitumia je ni nani nikiambiwa nimtaje? Siku ya kufa nyani miti yote huteleza. Nahukumiwa kwa kosa nisilolitenda,” Carolina alinung’unika. Mwili ulimtikisika kwa hofu. Furaha iliondoka na kumfanya asimame kama gofu lililoachwa baada ya vita kali. Baridi ilimwingia, tumbo lilimsokota akaihisi haja kumtoroka. Aliinyanyua miguu yake kutoka chumbani hadi msalani ambako hakupata haja yoyote. Hatimaye mwili ulishikwa na ugonjwa wa fadhaa uliomfanya aongoze kitandani kwenda kulala na kujifunika shuka gubigubi.



    Limtokalo mtu kinywani si kelele, bali asojua maana hulipuuza. Baada ya Saraganda kuyarusha maneno na kuondoka, Dendego alibaki katika ulimwengu wa mashaka. Hakutaka kupuuzia neno lolote alilolisikia likitoka kinywani mwa kijana aliyekuwa amekasirika. Alimwita Roy ili amjuze sababu ambayo ilimfanya Saraganda kuwa kifaru kwa mapambano. Alipoulizwa, Roy alibaki kimya akitafakari angali akijaribu kuipandisha na kuishusha pumzi. Hatimaye alimjuza baba yake kisa chote tangu alipokuwa shuleni hadi muda ule ambao Saraganda alifika kumshambulia. Mzee Dendego alilitega sikio lake na kusikia kila neno alilolizungumza Roy. Binafsi hakupenda kuona mwanaye akiwa chanzo cha patashika katika kijiji hicho. Baada ya kuwa amelisikia jina la Koi katika tukio zima, alistaajabu kusikia mtu mzima aliingia katikati ya sakata la watoto wadogo. Dendego alimweleza mwanaye maneno mengi ya kukemea.



    “Mwanangu, japo wahenga walisema, ujana ni maji ya moto hayaunguzi nyumba, mimi naipinga kauli hii. Kwako ujana ni moto wa kifuu katikati ya nyika iliyojaa majani makavu na upepo. Kwa miaka dahari tangu utoto wangu, sijawahi kufanya jambo la fedheha kama ulilolifanya. Jambo hili litasambaa kama mwanga wa jua na kuifikia kila nyumba hapa kijijini. Watu wote katika kijiji hiki watakuona wewe ni jogoo mkorofi na watakunyoshea vidole vya lawama. Je, mimi baba yako nitauficha wapi uso wangu kwa aibu hii? Bila shaka unafahamu, binti chongo lawamaze kwa mamaye lingali kengeza jichoni kwa mwanamfalme ni udhaifu wa babaye. Umenivua nguo mchana kweupe tena katikati ya unasi. Kaa ukijua, kinukiacho hakivumi bali kinukacho,” Dedengo alisema akimkemea mwanaye kwa mafumbo mazito. Roy alikuwa kimya, alinyanyuka na kupiga magoti akiomba msamaha.



    Baba yake alimtazama na kutingisha kichwa kwa huzuni.

    “Usipojenga mzinga wako asubuhi, mchana huwapati nyuki. Wakati wa ujana ni wa kujijengea msingi wa maisha ili uzee ukija uishi kwa heshima. Ukiutunza ujana utakuwa kama kito cha thamani ambacho kila mmoja hukitamani. Utajipatia kila kitu ukitakacho. Elimu ni silaha kushinda zote. Leo utahangaika kuwawinda wanawake usiku na mchana lakini hutawapata kwa kuwa wewe ni lofa. Ukivumilia hadi kuvuna matunda ya elimu, watakufuata na kukulilia kama makinda ya ndege yenye njaa. Kama unataka kuoa, acha moja ushike ulitakalo maana huwezi kupiga mbiu ungali na mnofu mdomoni. Yakupasa twende kuomba msamaha kwa Malecha. Aombaye radhi ni muungwana,” Dendego alizungumza kwa hekima. Alimwalika mwanaye kwenda kuomba msamaha. Waliianza safari kwenda kwa Malecha. Kiguu na njia Roy na baba yake waliukaza mwendo. Njia nzima Roy alikuwa akiilaumu nafsi yake iliyomtuma kuandika barua iliyozalisha tufani wa taharuki tangu shuleni hadi kwenye kiji hicho.



    *****



    Kama ilivyo ada, mwanamwali humkumbata mamaye, naye mwanamfalme shupavu humuuma sikio babaye. Saraganda aliketi kitako na babaye akimwagia kisa kizima kilichotokea siku ile. Mbele kidogo ya walipokuwa wameketi kulikuwa na moto uliowashwa kwa magogo makubwa ya mti. Cheche ziliruka na moto uliachama kama domo la simba kwa ukali. Saraganda alizungumza kwa hisia kali na kumpatia baba yake kipande cha barua ambacho alikipata ndani ya chumba cha dada zake. Malecha alimsikiliza kwa makini na kutafakari kwa kina. Katika mazungumzo, jambo lililomstaajabisha ni kuwaKoi alikuwa katika mkumbo huo. Nafsi ilimtuma kusema pasipo kuwa ametarajia.



    “Kweli kikulacho ki nguoni mwako. Koi wa kunifanyia mimi hivi? Yawezekana ndiyo maana alikuja mbio kama mtoa habari za msiba kunishtakia juu ya Carolina. Kumbe alikuwa na lake jambo,” aliongea Malecha. Mishipa ya kichwa ilisimama wima kwa hasira. Macho yalibadilika yakawa yanametameta kama paka pale gizani. Aliuchukua mkongojo na na kuiadhibu ardhi kwa nguvu. Saraganda alibaki kimya. Aibu ambayo Carolina aliisababisha ndani ya familia ilimfanya Malecha kujawa ghadhabu. Alijuta kwa vile alijitahidi kumlinda na kumtunza japo hakuwa mwanaye wa damu.



    “Haiwezekani. Kweli wema utendee mtende, hamali atakusaliti. Ukarimu wangu kwa miaka kumi na mitano leo navuna aibu. Carolina nilimpenda na kumhifadhi kama mwanangu wa kumzaa. Amenivua nguo mbele ya kijiji kizima. Carolina!” Malecha alifoka. Saraganda alikuwa katika tafakari kuhusu maneno aliyoyasikia kutoka kinywani mwa baba yake. Alijiuliza, ‘iweje mzee aseme amemkarimu Carolina kwa miaka kumi na mitano kama mwanaye wa kumzaa.’ Neno “kama” lilimweka njia panda.



    Ukiwaondoa Malecha na mkewe, familia yao haikuwa na mtu aliyejua ukweli kuhusu Carolina. Hata wanakijiji wengi walijua kuwa Saraganda na Carolina walizaliwa pacha katika familia hiyo. Akiwa njiapanda, nia ya kutaka kumuuliza baba yake ilimvaa kama utando wa buibui. Alikifungua kinywa kumuuliza baba yake ambaye alikuwa akiugulia kwa uchungu.



    “Baba, kwa nini unasema hivyo? Kwani Carolina…”



    “Shime usitake kunipandisha mori. Jambo usilolijua usilitolee maana. Kwa nini utake kuicheza ngoma ambayo mapigo yake huyajui. Wewe bado mwanakitumbo. Jambo hili usilizungumzie nakusihi,” Malecha alimhadharisha Saraganda na kumfanya ayameze maneno yake. Wakati Saraganda na baba yake wanazungumza, Carolina alisikia yote. Wasiwasi ulimwingia baada ya kumsikia Malecha akiyasema maneno ya kumkana. Aliondoka kwenye kisiki cha mti mkubwa alipokuwa amejibanza na kuingia ndani. Alipokuwa akiishilia chumbani aligeuka na kuwaona watu wawili wakiwa wameongozana. Hakuwafahamu mara moja kutokana na giza lililokuwa limefifisha mwonekano wao.



    “Hodi wenyewe!” alibisha hodi Dendego aliyekuwa na kijana wake Roy. Malecha aliposikia sauti aligutuka. Baada ya tafakari aliitambua sauti ya Dendego mapema.



    “Karibu Dendego. Karibu uketi,” Malecha alikaribisha. Aliwapatia kipande cha gogo la kukalia yeye na kijana wake. Roy alimsabahi Malecha ambaye aliitikia kwa mkato. Saraganda hakuwa na lolote la kuzungumza bali alipishana nao punde tu walipokuwa wakifika mahali pale. Roy akiwa na baba yake ililazimu kumkabili Malecha. Dendego alikuwa anatafakari namna nzuri ya kuyaanza mazungumzo kutafuta suluhu.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Ndugu, mguu umenifikisha hapa usiku huu, kuna jambo. Nimefikiri ni busara tuzungumze ili kuiondoa tofauti iliyopo,” alisema Dendego. Malecha alikuwa kimya akisikiliza. “Ni kuhusu kijana wangu, aliteleza,” aliendelea Dendego. Roy aliliachia gogo na kupiga magoti mbele ya Malecha.



    “Naomba unisamehe mzee. Sikukusudia yatokee haya,” alizungumza kwa unyenyekevu ingali hofu imemjaa. Aliishika miguu ya Malecha ambaye alikuwa kimya akikitingisha kichwa na kuutafuna mdomo.



    “Dendego, najua unanifahamu vizuri,” alisema Malecha. Alimsukuma Roy kutoka miguuni kwa mkongojo.



    “Hasaa! Nakufahamu ni mtu usiyependa makuu. Na hilo ndilo limenifanya nije mbio tuondoe udhia,” Dendego alijibu.



    “Isiyo kilevi ikivunda huwa kilevi hatari. Usiuchukulie upole na ukimya wangu kuwa mimi hunudi unaweza kunifanya utakavyo. Kama kuna siku umenikosea na huyu chekeamwezi basi ni leo,” Malecha aliongea kwa ukali.



    “Mzee mwenzangu, ningekuwa na hila nisingejihima usiku huu kuja. Naomba upokee ombi la msamaha yaishe,” Dendego alimsihi Malecha.



    “Jambo hili si jepesi kama unavyofikiri. Limezalisha utitiri wa mambo ambayo sikutaka kujulikana hadharani. Wewe unajua siri kubwa juu ya Carolina,” Malecha alizungumza kwa kuishusha sauti.



    “Ndiyo nafahamu. Ni miaka mingi imepita….,”



    “Naam! Hata Koi kaingia kwenye kikaango cha moto. Hivi nyie mmekusudia kunifedhehesha kwa nini?” Malecha alizungumza wakati akisimama wima.



    “Usiukane msamaha. Mtoto amepitiwa, tusamehe!” Dendego alizidi kuomba.



    “Sihitaji kuzungumza juu ya jambo hili. Nitakachokifanya mtajuta kuzaliwa. Mmelianzisha najua mtalimaliza pamoja na Koi,” Malecha alizungumza. Aliondoka taratibu na kuingia ndani. Aliliokota sime na kutoka kuelekea walipokuwa Roy na baba yake. Mkewe Malecha alimwona mmewe akilitwaa sime.



    “Baba Huruma, sime la nini usiku huu?” alihoji mama Saraganda. Baada ya kuyasikia maneno ya mama Saraganda, Roy na baba yake walitokomea gizani. Walijua Malecha hakutaka maelewano. Malecha alijaribu kuwafuata wakati akiendelea kufoka. Hakuwapata. Baada ya kurudi, alikielekea chumbani kwa akina Carolina. Sime lake lilikuwa mkononi likitaka kuikata kiu.



    “Carolinaa! Toka nje kirukanjia wewe!” Malecha aliita na kufoka. Carolina muda huo baada tu ya kumsikia baba yake alifadhaika. Alitamani sakafu ipasuke ajichimbie kumkwepa baba yake. Katika giza alijibanza ukutani akiunyemelea mlango taratibu. Alikuwa akitikisika kama kifaranga kilichonyeshewa mvua kwa sababu ya kuogopa kukabiliana na baba yake.



    “Kweli asiyeridhiki hapewi amana. Nilikutetea na kukupamba wakati kijiji kizima kikitaka kukutupa mtoni sababu wewe ni laana. Sasa nimejua, unastahili kifo. Mkono wangu lazima uhusike ili laana hii ikome,” Malecha alizidi kusema.



    Aliusukuma mlango na kuingia ndani. Alipokifikia chumba baada ya kuiacha sebule alijigongesha kwenye tendegu la kitanda. Goti lilipigwa ganzi na maumivu yakasafiri kama mwenye kupigwa na nishati ya umeme. Malecha aligugumia, maumivu yalimfungua mdomo kwa kutoa sauti.



    Carolina aliyekuwa kaufikia mlango wa kutokea nje alimsikia baba yake akiugulia. Aliuvaa mlango kutoka. Isivyo bahati alijikwaa na kuanguka vumbini. Malecha alimsikia. Alitoka mkuku kumfuata. Kabla hajanyanyuka, Carolina alitiwa mkononi na baba yake. Alijiviringaviringa wakati sauti kali ya hofu ilimtoka. Alipoona baba yake alikuwa na ala mbaya ya kumdhuru, kwa ujasiri alilisukuma goti likampata Malecha na kuzigonga hasua zake. Alijichomoa kutoka mikononi akitaka kutimua mbio. Malecha alilinyanyua sime kumkata Carolina koromea. Kwa kuwa alikuwa kaanza harakati kujiokoa, sime lilimpata na kuichuna ngozi ya juu ya koromea pasipo kuzama ndani kwa kina.



    Binti wa Lola alitimua mbio kumkimbia baba yake aliyebaki kuugulia kwa maumivu. Damu zilimtoka Carolina sehemu ambayo alikatwa. Alipoziona damu kwenye kiganja hofu ya kuipa kisogo dunia ilimjaa. Jasho jembamba lilimtiririka wakati akiwa bado mbio akielekea machakani.



    “Huwezi kunishinda, nitakupata tu. Nyumba yangu sifugi kahaba,” Malecha alizidi kufoka wakati akijaribu kumfuata Carolina sehemu alikokimbilia.



    “Kunguru hazai bata nimeamini. Mama kahaba mtoto jini mahaba…..! Nilifanya kosa kukaa na huu msukule,” Malecha alisema. Alivyoona hakukuwa na haja ya kuendelea kumfuata Carolina, alirudi hadi kwenye moto. Alichukua kijinga cha moto na kuelekea sehemu kilipo kijumba ambacho walikuwa wakilala Carolina na Huruma. Aliyavuta majani na kuyaunganisha kwenye kijinga cha moto na kuanza kupuliza ili moto ulipuke. Alilokusudia alilijua yeye. Baada ya kuona baba yake anataka kufanya jambo la ajabu, Huruma alitimka na kuingia ndani ya kijumba chao.



    “Vitu vyangu baba! Madaftari yangu!” Huruma alitamka akiwa mbio kuingia ndani. Babaye alikuwa kauwasha moto uliokuwa ukiruka na kukatika vipandevipande. Aliurusha moto juu ya kijumba ukashika na kuanza kutawanyika kwa kasi. Huruma alikuwa bado yupo ndani. Mama yake alikimbia kutaka kumwokoa.



    “Tena hata naye mwache aungue humo maana akili zake zitakuwa sawa na huyo mwenziwe,” alifoka Malecha akimkaripia mkewe. Mama Saraganda aliufikia mlango na kumhimiza Huruma kutoka. Huruma alifanikiwa kutoka akiwa na mfuko wake wa daftari pekee. Vitu vingine aliviacha kuteketea kwa moto.



    “Laana zote naziondoke na moshi huu,” Malecha alisema akiwa kasimama kando ya kijumba hicho kilichokuwa kikiteketea. Baada ya kuuona moto ukilisabahi anga usiku ule, wanakijiji walimiminika ili kushuhudia tukio lililokuwa likiendelea.



    Carolina alipouona moto ukipanda angani kwa mafungumafungu alijua maishaye yalikuwa shakani. Aliichukua kanga aliyokuwa kajifunga kuipangusa damu iliyokuwa ikitiririka kutoka shingoni. Damu haikukatika mara moja jambo ambalo lilimzidishia hofu. Alilichana bwende la kanga yake na kulifanya bandeji shingoni akizizuia damu kutiririka. Kichwa kilivurugika. Hakujua ukweli wa aliyoyasikia kutoka mdomoni mwa Malecha. Mama Saraganda wakati huo alisimama kimya akimtazama mmewe.



    “Baba Huruma, usiku huu….? Kakosa nini na ataenda wapi sasa? Miaka kumi na mitano anapajua hapa ni kwao leo unam…..”



    “Funga bakuli lako. Usitake kunivuruga mwanamke. Tangu lini shetani akaishi na kundi la malaika? Carolina ana laana. Laana! Kama unamtetea, mfuate na usirudi kwangu na mikosi,” Malecha alifoka dhidi ya mkewe. Mama Saraganda aliufumba mdomo wake kwa maneno mazito ambayo yalitolewa na mmewe. “Nakwambia ukimfuata……” Malecha alionya.



    Mama Saraganda alirudi kwa unyonge na kuingia ndani akigugumia. Saraganda na wanakijiji waliomjua Carolina hawakuamini kilichokuwa kikitokea. Ndoto za Carolina zilianza kufifia katika giza lisilo tumaini. Hakuwa amelijui kosa lililomfanya ahukumiwe vikali hata atake kuuawa na mtu ambaye kwa miaka mingi alimjua kuwa ni baba mzazi.

    Mbio za Carolina usiku ule zilimchukua hadi kwenye kichaka kilichokuwa karibu na bonde lililokuwa na bustani yake. Macho yake aliyaangaza kulishinda giza lililokuwa limemzunguka. Kila hatua aliyoipiga alihisi ilisikika kwa jinsi eneo zima lilivyokuwa limefunikwa kwa ukimya, “Kosa langu nini?” Carolina alijiuliza.



    Taratibu alijongea hadi kwenye kisiki cha mti mkubwa na kuketi akiwa kauegemea. Mikono yake aliielekeza shingoni kwenye jeraha kulipapasa. Kwa kupitia vidole vya mikono, alijua kuwa damu ilikuwa ikiendelea kumtoka. Kipande cha kanga alichokuwa amekizungusha shingoni kilikuwa kimelowa chepechepe. Bado chozi lilimtiririka akigugumia kwa uchungu, “Nitakufa. Baba. Nakufa mie,” alijisemea kwa kukata tamaa.



    Alijizoazoa kutoka sehemu ile hadi ilipokuwa bustani yake katika giza lile. Alipofika moja kwa moja aliingia kwenye dimbwi la maji na kulichukua galoni bovu lililokuwa pembeni. Wakati huo mbalamwezi ilikuwa ikiangaza na kuzalisha mwanga hafifu. Kipande cha kanga kilichokuwa kimebaki alikiviringa tena kuliziba tundu kubwa lililokuwa likivujisha maji kwenye galoni. Aliyachota maji akapiga hatua chache kwenda pembeni. Alipiga magoti na kuinama kulifungua jeraha lililokuwa likivuja damu nyingi. Alikiloweka kipande cha kanga chenye damu na kukikamua. Aliendelea kukifuta kidonda kuziondoa damu. Alimkumbuka Huruma ambaye alimsaidia bega kwa bega kuwa hakuwa naye wakati huo. Mbinu ya Huruma alivyomkamulia maji ya jani la mkonge baada ya kukichuna kidole chake ilikuwa kitendo cha uungwana. Alitamani kupata mkonge afanya vilevile. Asingeweza kupata jani la katani muda ule kwani alikuwa mbali na sehemu bustanini.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Damu, zinazidi kunitoka bila kukoma. Eeh tumaini langu uko wapi Mungu!” Alijisemea Carolina wakati ule aliojikokota hadi kuufikia mgomba uliokuwa kwenye bustani ya akina Roy. Aliitumia mikono yake miwili kulishika moja ya chane la mdizi uliokuwa mchanga. Mkono wake ulikifikia kilindachozi kilichokuwa kimening’inia na kukinyonga kwa nguvu.



    Alikinyofoa na kuielekeza sehemu iliyotoa utomvu kwenye jeraha lake. Kwa kuwa kilikuwa na utomvu mwingi, uliingia kwenye kidonda sawia. Alijaribu kusimama, jelezi akalihisi kumfuata ndipo aliamua kujifutika chini.



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog