Search This Blog

Friday, July 15, 2022

NDOTO ZA KIPEPEO - 1

 







    IMEANDIKWA NA : JOHN WISSE



    *********************************************************************************



    Simulizi : Ndoto Za Kipepeo

    Sehemu Ya Kwanza (1)

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Shangwe huwa siku ya kuzaliwa, dunia huchekelea. Mtoto awapo hadharani, ulimwengu humpokea na kumtia akilini. Katikati ya msitu wa walimwengu, mtoto huchipuka na kustawi kwa nasaba na haiba. Kwa kimo hujitangaza mbele ya kila mzaliwa. Lakini upo wakati huja pasipo hiari, akuaye huchagua wa kuambatana naye. Kwa usuhuba au huba, ni hiari ya moyo wa mtu imtumavyo. Mwisho wa yote umri mtu humuongoza, kumpata wake wa sirini, mme au mke. Hiyo ndiyo sifa ya maisha ya muumbwa kwa damu na nyama.



    Vilevile ulimwengu uliwakutanisha watu wawili kutoka katika familia mbili; Majaliwa akiwa mtoto wa pekee kwa mama yake, Bi. Lola Muksin, mwenyeji wa Pwani na Maua binti wa Jackson, mzaliwa wa bara. Kukutana kwa wawili hawa kulikuwa kama pambazuko la kuyatimiza yasiyo hiari mwilini mwao, walipendana. Nia yao iliwafanya wachaguane ili kuyaishi maisha ya uchumba hatimaye ndoa, walioana. Ilikuwa fahari kubwa kwa ulimwengu kuwapokea wawili hao kama mke na mme walioshibana.



    Hatimaye waliokotana na kuvutana hadi bara, nia ikiwa ni kujitafutia riziki waliyopangiwa na Maulana. Wakiwa bara ilipita misimu kumi na mitano ya masika na kiangazi wakiwa na furaha. Furaha waliyokuwa nayo, ilifukuza ila zote kutoka kwa watu wenye inda. Walicheka na kufurahi pamoja. Msibani waliomboleza pamoja na hata harusini walikuwa chanda na pete.



    Hawakuachana hata hatua moja kama kumbikumbi. Walistahili kuwa baba na mama wa mfano. Lakini je, lingewezekanaje hilo pasipo kutokewa na uzao? Hivyo iliwapasa kukazana kumwomba aliyewaunganisha wakimtaka mzaliwa wao wa kwanza.



    Ndoa ya Majaliwa na Maua katikati ya kijiji cha Hamaniko ilikuwa ya mfano. Maua alikuwa badii jamali kwa sura, umbo na sauti. Majaliwa nafsi ilimsifu na kumpandisha kwa fahari na kujiona akiwa kileleni mwa mlima mgumu kuukwea. Kila alipokuwa akimtazama Maua, hakuisha hamu ya kutaka kumsogelea japo amtekenye na kuisikia sauti yake nyembamba tamu kama kinanda. Walishibana na kushabikiana. Maua alijua mmewe alikuwa mtanashati kuliko waume wote aliopata kuwatia machoni, vilevile Majaliwa alijua fika kuwa, ahali yake alikuwa hana wa kufanana naye kwa kila kitu. Walisifiana!



    Siku zilikatika, miezi hatimaye miaka ikawa imewapa kisogo, kitanda chao hakikuwahi kumbeba mwana hata binti mchanga wa kumzaa. Walikuwa bado wakibarizi kama wachumba. Wahenga walisema; juhudi haishindi kudra, hatimaye ndoa ya Majaliwa na mkewe ilijibu baada ya miaka mingi. Wakati ambao jirani zao walikazana kuwanyoshea vidole vya lawana, Rabana alijaza furaha chumbani mwao. Maua alishika ujauzito.



    Shauku ya kumpata mwana kwa Majaliwa ilikomaa moyoni. Maua yeye hakutaka kutabiri wala kutangaza tamaa ya jinsia ya mtoto alomtaka kuwa naye. Alitaka mtoto, awaye yeyote, mwana hata binti kwake ilikuwa zawadi na tunu katika ndoa yake. Maua hakuisha kudeka naye alidekezwa. Majaliwa alimtunza mkewe zaidi ya bustani mbele ya kasri la kifalme. Hakuna alichokitaka Maua ambacho Majaliwa alishindwa kumtimizia. Hata kama ilimlazimu Majaliwa kumwaga jasho jingi kwa kwenda mbali kwa miguu kutafuta limau, hiana hakuwa nayo, alitii. Hata kama Maua ingefika siku akahitaji mzizi wa mlima, Majaliwa angejipiga kifua akitaka kuung’oa mlima Kilimanjaro. Hakutaka mkewe aingiwe huzuni hata kwa sekunde moja kutokana nay eye kushindwa jambo. Alitaka mke awe na siha njema na akili tulivu ili amzalie mwana, mrithi wa amali na fahari zake.



    Miezi kenda haikuwa muda mfupi kwa Maua aliyepitia kila aina ya changamoto. Kwa kuwa hakuwahi kuwa na hali ile tangu kuzaliwa, ilimpasa kuwauliza rafikize waliokuwa wakifika kumjulia hali. Kuna wakati miguu ilimvimba na wakati mwingine hasira zilimchukua bila sababu na kuhisi kumchukia mme wake. Kuna wakati Maua alitamani harufu ya maua mabichi na kumlazimu Majaliwa kuyatafuta kondeni asubuhi hata mchana wa jua kali. Kwa Majaliwa miezi kenda aliyoipitia Maua ilikuwa si chochote. Muda kwake ulienda kama konokono tofauti na hamu yake iliyokuwa ikienda kwa kasi kama mshale wa msasi mawindoni. Alitaka kumwona mzaliwa wake wa kwanza. Si kumwona tu, bali alitaka kumwona mwana ambaye alifanana naye kwa haiba na nasaba. Hali hiyo ingeweza kumwondolea laana na fununu za majirani ambao walikuwa wakimbandika sifa ya kutokuwa mme. Walikuwa hawaishi kumzushia kuwa alikuwa chapapunga.



    Hayawihayawi mwishowe ikawa. Usiku wa saa tisa Maua alishikwa na uchungu. Majaliwa aliikupua akiba yake yote fedha na kumpeleka Maua kwa mkunga wa kijiji hicho. Alijifungua salama usiku uleule baada tu ya Majaliwa kuipa kisogo nyumba ya mkunga. Majaliwa ambaye alikuwa na shauku ya kuitwa baba, hakupatwa na usingizi. Hakuwa akijitambua na asingeweza kufanya lolote bila kumfikiria Maua. Hamu yake ni mwana, mrithi wake kutoka kwa ubavu wake.



    Mapema alfajiri hapajakuchwa, Majaliwa aliwasili kwa mkunga. Hapakuwa na siri tena ya kumfanya Majaliwa asitambue ukweli. Sauti ya mtoto ilimpokea angali akiwa hatua chache kabla hata hajafika ugani kwa mkunga. Furaha ilibisha hodi nafsini mwa Majaliwa, mwili ulimsisimka hadi vinyweleo vikasimama wima baada ya sauti ya kichanga kuisikia. Alitaka kupayuka kwa furaha kutangaza ujio wa damu yake, lakini alijipa muda. Aliharakisha kutembea ili awahi, hatimaye alifika mlangoni na kubisha hodi ili afunguliwe.



    “Amejifungua Maua, kipenzi changu?” Majaliwa aliuliza baada ya kufunguliwa. Akiwa na shauku ya kujibiwa. Mkunga alisita kidogo kumjibu lakini baada ya kuona Majaliwa alitaka kumpita mlangoni bila adabu, alimpatia ushuhuda.



    “Ndiyo baba, amejifungua. Hongera sana, Mungu awakuzie,” alisema mkunga. Majaliwa alikuwa tayari kaingia ndani. Alikuwa kasimama sebuleni. Koroboi iliyokuwa ikiwaka haikutoa mwanga wa kutosha na kumfanya aweze kuona chumbani alimokuwa Maua. Baada ya Majaliwa kumpita kama mshale pale mlangoni, mkunga naye aliingia. Alipitiliza moja kwa moja hadi kwa Maua aliyekuwa kapumzika baada ya kazi nzito ya kumleta shuhuda wa kizazi chake.



    “Mama, mtoto gani?” Aliuliza Majaliwa. Alitamani mkunga amjibu papo kwa hapo kabla hata hajamaliza kuuliza. Masikio yake yalisimama wima kama mbwa mwitu ili apate kusikia. Moyo wake uligonga kwa kasi ikiwa hamu ya kujua imeuzidi mwili mzima. Mkunga bado aliendelea kuwa kimya kwa sekunde chache kama hakulisikia swali kutoka kwa Majaliwa. Hatimaye aliamua kumjibu ili kumtoa wasiwasi.



    “Mrembo kama mama yake. Mrefu kama baba yake. Mke mwenzangu huyo,” alijibu mkunga. Majaliwa hakujibu kitu wala hakuuliza tena. Joto la furaha lilizima na kuufanya mwili kujaa baridi. Ukimya wake haukuweza kutabirika, lakini aliamua kuuvunja baada ya kutafakari sana.



    “Maua haliye ikoje, maana simsikii akinena. Anaendeleaje, mke wangu?” Aliuliza Majaliwa.



    “Hajambo, lakini amelala tu kwa uchovu. Nataka apumzike kwanza. Nakuomba kaninunulie mafuta ya nazi au ya karanga ingali mapema. Kama kuna nguo za kubadilisha, nenda kaniletee vitenge pea moja na kanga doti mbili. Hivi sasa navihitaji ili akiamka niendelee kumhudumia. Yakupasa pia kumpeleka hospitali,” alieleza mkunga.



    “Hospitalini kwa lipi tena mama? Kama kajifungua salama si mambo yamekwisha!” Alihoji Majaliwa. Jambo la kwenda hospitalini tena lilikuwa kama habari mpya kwa Majaliwa. Hakutaka na wala hakuwa na wazo la kwenda hospitali tena. Akili yake ilijua kufika kwa mkunga mambo yote yaliishia pale. Mkunga alilazimika kumfahamisha sababu ya kwenda hospitali.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Mwanangu, dunia ya zama zenu ni tofauti na ya sasa. Mambo huenda yakibadilika kizazi hadi kizazi. Ukienda hospitali, huko watamchunguza hali yake kiafya pia watampatia mtoto karatasi ili aweze kupata cheti cha kuzaliwa. Siku hizi kila kitu ni mpaka cheti cha kuzaliwa. Ni nyaraka muhimu sana usipuuzie,” mkunga alieleza.



    “Sawa mama. Lakini mambo haya ya cheti kila uendako, yananisumbua sana hata mimi. Kama mara mbili au tatu nakosa kupatiwa stahiki zangu nyingi, nikidaiwa cheti cha kuzaliwa au kitambulisho cha uraia. Sasa mimi nawashangaa sana watu hawa. Tangu lini mtu aliyezaliwa chini ya mwembe kama mimi akawa na cheti cha kuzaliwa? Kama mwembe ulikuwa na uwezo wa kutoa cheti basi siku nitawapatia waendelee kungoja. Lakini kwa huyu, ni jambo jema umenifumbua macho. Acha nifuate nguo kwanza ndipo nitarudi ili twende huko hospitali,” alisema Majaliwa. Alitoka na kutokomea alikokuwa akiishi na mkewe kwa ajili ya kuchukua alivyokuwa ameagizwa.



    *****



    Baada ya kuwa wamempata binti katika uzao wao wa kwanza, Majaliwa alipendekeza jina. Ilipaswa mtoto kuitwa Lola. Jina hilo lilikuwa la mama yake ambaye alikuwa akipenda sana kujitazama kwenye kioo. Tabia hiyo ndiyo ilipelekea wazazi wa mama yake Majaliwa kumbandika mama yake jina hilo ambalo lilikuwa na maana ya mpenda kioo. Wakati uliendelea kuyoyoma, Lola alikua na kuchipuka kama mche wa mgomba kwenye rutuba. Alikuwa na afya njema iliyowafurahisha wazazi wake wote.



    Majaliwa ambaye alikuwa akitegemea kumpata mwana badala ya binti hatimaye moyo wake aliushauri kukubaliana na ukweli. Alijua fika, uzao ule ungefuatwa na uzao wa kiume kama matamanio yake. Alijipa imani hiyo baada ya kudodosa ndani ya ukoo alimozaliwa, hapakuwa na uzao mkubwa wa watoto wa kike. Alimpenda Lola na kumfanya mwanaye na kumtukuza.



    Baada ya Lola kufikisha umri wa kwenda shule, Majaliwa alianza kumtilia mashaka mkewe. Hakukuwa na dalili yoyote ya kushika ujauzito zaidi ya Maua kuongezeka kwa unene. Maua alinenepa na kuwa na uzito mkubwa. Majaliwa hakukoma kulalama akimlaumu mkewe kuwa alikuwa amefanya hila ili asiweze tena kujipatia mtoto aliyemhitaji. Maua yeye hakuwa na wasiwasi, fika alijua siku ingefika ambayo angempata mtoto wa pili kumfuata kifungua mimba wao.



    Wakati Lola akianza darasa la kwanza hadi anahitimu darasa la saba, Maua na Majaliwa walikuwa wakiwa. Hawakuwa tena na mtoto zaidi ya Lola jambo ambalo Majaliwa lilimvuruga akili. Hakuwa akishinda nyumbani wala hakuwa akimganda mkewe kama hapo awali. Kutwa alikuwa akihangaika na kazi zake za juakali. Mapenzi aliyokuwa akiyaonesha kwa Maua hapo awali yalipungua. Tabasamu lake lilikuwa nadra sana kuliona.



    Lola ililazimu kulelewa kwa kiasi kikubwa na mamaye.

    Kwa kuwa miongoni mwa sifa za mama, ni kumlea mwanaye ili aweze kuwa mfano wa kuigwa kwa mema, Maua alikuwa mzazi mwema. Pamoja na sadfa ya kumfanya mtoto kuwa juu ya kilele cha tabia njema na vurugu za mme kutaka mwana, Maua alibaki kuwa nguzo muhimu. Isingeweza kuwa familia bora bila uwepo wa mama bora. Hii sawa na ujenzi wa nyumba, haiwezi kuwa nyumba pasipo kuwa na nguzo imara kuinyanyua. Kwa uhitaji huo, baba yeye huwa kama chumvi, hukoleza uhai na ladha kwa kusimamia miiko na misingi imara. Hivyo katika nyumba, Majaliwa alikuwa msingi wa nguzo kusimama japo alikuwa kasongwa na fadhaiko.



    Maua hakuisha kumnasihi bintiye kwa maneno ya kila aina. Ilipolazimika kucheka naye walicheka na ilipobidi kumkanya kwa maneno makali alifanya. Palipohitaji kumpatia peremende alimpatia na palipokuwa na pakihitaji mshubiri napo hakusita kumjazia. Hakutaka mtoto wake akue na kuwa kama chaza ajianikaye mwambani. Alitaka Lola awe mfano mwema ili kumwaminisha Majaliwa kuwa, Lola alikuwa mtoto sahihi kwake.



    Siku ya kumnasihi tena Lola ilifika. Umri wake ulihitaji kukumbushwa kila wakati kwa kemeo na ushauri ili akue na kukivuka kipindi kigumu cha usichana wake baada ya kuvunja ungo. Lingali jua limefifia likichomoza kwa shida, Mama Lola alitoka shambani alikokwenda kuchuma kisamvu. Alimwita mwanaye na kumtaka wasaidizane angali akisema naye.



    “Lola mwanangu, sasa wewe ni embe bivu mtini. Kama halikuliwa changa kwa chumvi na pilipili, sasa watakiwa kuishi tofauti. Kila apitaye karibu yako analitamani tunda ili kuituliza njaa yake,” alisema mama Lola angali akiendelea kuchambua kisamvu.



    “Abee!” Lola aliitikia. Alionesha kutoelewa kile mama yake alisema.



    “Nisikilize mwanangu. Maisha siku zote ni utu kwa watu, endapo watageuka afriti, ubaya wao huuzidi ule wa mnyama. Tangu utoke tumboni mwangu, Mola amekujalia afya, waishi salama. Unapaswa kumshukuru kwa kila hali. Ninacho kusisitiza ni kimoja ufahamu; ulimwengu hauna mgumu, kwake wote laini mithili ya mkate kwa chai. Halahala binti wa Majaliwa, ichunge haiba yako nasi pia usituvue nguo. Ushakua mwanangu, kote kusi na kasi vijana wakutazama,” alisema Mama Lola. Alikisogeza kinu alichokuwa amekiandaa kwa ajili ya kulitwanga samvu lililokuwa limejaa tele kwenye kapu.



    “Mama, huishi mafumbo. Kila kukicha kuniasa kama mie kiziwi nisiyeweza kusikia. Ninajitambua mama’ngu, kamwe sitaweza kuwavua nguo. Njia yangu nyoofu najua waifahamu, namtumaini Mungu pekee. Mwalimu wangu wa somo la Kiswahili alishasema mara nyingi kuwa, miluzi mingi humpoteza mbwa. Nakuomba uamini na uniamini mwanao. Najitunza ili ndoto zangu zisiende na mwezi,” alijibu Lola wakati akimnyang’anya mamaye mchi na kuanza kukitwanga kisamvu. Mamaye alimtazama kwa makini usoni. Aliupeleka mkono wake mmoja shavuni na kuubandika kisha kuuegesha kwenye goti lake. Aliendelea kumpekua Lola kwa macho, tangu unyayo hadi ncha ya unyewe.



    “Hivi Lola, upitapo mitaani siku hizi hali ikoje?” Aliuliza mama Lola.



    “Mama, ushaanza, maswali yako kama mpelelezi. Mitaani ni kawaida tu. Hakuna ubaya, lakini……..”



    “Hapo ishia…. Hiyo lakini naitaka, hasa ndipo nikaamua kukuuliza. Nishaliona jua likichomoza kabla yako miaka mingi iliyopita. Niulizapo maana yangu ni kubwa. Hebu nieleze, lakini ina nini ndani yake?” Aliuliza mama Lola.



    “Mama’ngu we acha tu, kila nikatizapo mbele ya wanaume, vijana hata wazee, haweshi kuziacha hamsini zao na kunikazia macho. Tena, hunitazama tangu chini ya miguu hadi unywele. Basi hunisindikiza kwa macho na utawasikia tu wakirusha maneno ya chinichini, ni aibu hata kuyasema,” alieleza Lola.



    “Aibu ee mama! Aibu kaburi la nafsi, siri sema na mamayo, kijakazi usimsiri. Ushakua nimesema. Enhee, wanasemaje? Maana hapo ndipo palipo na lile ninalotaka kukuasa,” aliendelea mama Lola.



    “Mama nitakwambia, acha kwanza nimalize kutwanga kisamvu niinjike. Wauona wakati wakimbia kama mshale. Nataka baba’ngu arudipo kutoka kondeni ajipatie mlo mapema,” alieleza Lola.



    “Kumbe wamjua vema baba yako. Tangu akiwa barobaro na ukoko shingoni, yeye chakula kwanza mengine hungoja. Haira zake za mkizi akikosa mlo kwa wakati ndipo utazijua,” alisema mama Lola kisha kuangua kicheko. Jicho tena liliendelea kumtazama Lola wakati akitingishika kila alipousukuma mchi kwenda kwenye kinu.



    “Mashallah!” Alistaajabu mama Lola.



    “Mama jamani, wanitazamaje kama sanamu la maonyesho kwa makini namna ile? Hadi naogopa, au kuna jambo mama’ngu walijua wataka kunijuza. Basi niume sikio unitoe wasiwasi,” alisema Lola.



    “Nikutazamapo nayakumbuka mengi sana. Nazikumbuka enzi ambazo nilikuwa nikimwaga maji kichwani, yalienda haraka chini kumwagika. Mwili ulikuwa mororo na ulikuwa ukimeremeta kama embe dodo bivu. Kila mwanaume alitaka japo nimpe mkono kabla ya salamu. Cha ajabu nakiona sasa, baada ya baba yako kunioa, hatimaye kukuzaa wewe mambo tofauti. Mwili ushakuwa kama gunia la mkonge, ukitia maji kichwani pengine yaweza yasifike chini, huishia pasipojulikana. Salamu tena za vijana na wababa zishakoma,” alisema mama Lola.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Mama nawe, mpaka uzunguke kama tiara. Najua unachotaka kusema, we niambie mwanao nakusikiliza,” alisema Lola.



    “Haya, pakua hilo samvu, litie kwenye chungu, nenda kaliinjike na urudi hapa. Kabla baba yako hajarudi nikupe yangu ya moyoni. Binti na mamaye, mwana na babaye hivyo nisiposema utanilaani uzeeni,” alisema mama Lola.



    Mama Lola alibaki kimya kajiegesha kwenye mti wa kivuli. Ulikuwa mti mkubwa wa mzambarau. Dusumali lake kichwani lilipepea kwa upepo uliokuwa ukivuma hasa baada ya dalili ya mvua kutaka kunyesha. Alikuwa akiwaza jinsi ya kusema na mwanaye kuhusu maisha hasa wakati ule wa usichana ulioiva. Lola hakukawia kuinjika kisamvu alichokuwa amekiandaa. Alipomaliza, alitia kuni ili apate moto wa kutosha, kisha alipiga hatua kurudi kwa mamaye aliyekuwa akimngoja.

    “Ushatia kuni za kutosha jikoni?” Aliuliza mama Lola.



    “Ndiyo mama, tena naona leo zitawahisha kisamvu kuiva,” alijibu Lola.



    “Haya tega sikio na sikia. Niyasemayo hapa hutayasikia popote mpaka utaenda kaburini,” aliongea mama Lola. Usoni tayari aliuvaa umama ambao haukuwa na chembe ya masihara. Lola alibaki kimya, moyo ulimdunda kwa shauku ya kujua kile mamaye alitaka kumjuza.



    “Nianulie kanga yangu hapo kambani ndipo uje tuendelee,” Mama Lola alimwagiza mwanaye. Lola alinyanyuka na kuivuta kanga iliyokuwa imekauka. Mji wake ulikuwa umepambwa kwa samaki wadogo wengi wakiwa wamemzunguka samaki mkubwa ambaye alipanua domo. Lola aliketi kwenye kigoda kumsikiliza mamaye.



    “Watoto wa leo kwa kutaka laana! Unajua maana ya kuketi juu ya kigoda wakati unazungumza na mama yako? Teremka jikalie hapo mkekani. Mwiko kwa msichana asiyeolewa kukalia kigoda angali akizungumza na wazazi wake,” Mama Lola alifoka. Lola alinyanyuka kisha kuketi mkekani.



    “Haya, uko tayari kunisikiliza?”



    “Ndiyo mama.”



    “Naomba nieleze bila kuficha, ushaanzisha usuhuba na mvulana au mwanaume wa aina yoyote tangu nikuzae?”



    “Aka! Sijawahi mama. Mbona wauliza una…”



    “Shhhhhhi! Taratibu. Nijibu hatua kwa hatua.”



    “Sijawahi mama.”



    “Vizuri! Umehitimu darasa la saba, sasa wangojea matokeo. Je, wataka kuendelea na shule ama umefika kikomo?”



    “Mamaaa! Kikomo ndo wapi?”



    “Umefikia mwisho wa ndoto zako?”



    “He! Mama, mie nataka kusoma hadi madarasa yasiwepo huko mbeleni. Ndoto yangu ni kusoma –kusoma-kusoma mpaka nitamanicho nikifikie,” alijibu Lola.



    “Vizuri. Nakuuliza haya kwa maana kubwa. Tazama, rafikizo wote sasa wanaeleka mabegi mgongoni tena mapema baada ya kuzivua sare za shule. Wamezalishwa nao wanalea. Wao pia hawaitaki shule kabisa, wanasema kuketi darasani kwa binti ni utumwa. Wao wasema kuwa, wasomewa na bwana zao. Wanaringisha makalio yao kuwa wakikalia sana viti, watapigwa pasi kama wachina. Isiwe nawe wasomewa na bwana’ko,” alieleza mama Lola.



    “Mama, nataka kusoma kwa juhudi zangu mwenyewe. Nataka kupata kila kitu changu kwa akili na nguvu alizonijalia Mola. Sihitaji upendeleo wala kumtegemea mtu kama dhamana ya maisha yangu,” alieleza Lola.



    “Isome hii kanga. Imeandikwa nini?” Mama Lola alisema kisha alimpatia Lola kanga. Lola aliizungusha kanga kuiweka vema ili aisome.



    “Imeandikwa; avumaye baharini ni papa, dagaa mjichunge.”



    “E-waaa! Haya, niambie ina maana gani?”



    “Ina maana kuwa, papa ni kiumbe mkubwa ambaye anapaswa kuogopeka baharini. Kwamba, dagaa wajihadhari wasije kuingia hatarini kwenye domo lake maana atawala bila huruma,” alijibu Lola.



    “Yaonesha mwalimu alokufundisha Kiswahili hajambo. Safi kabisa.”



    “Ahsante mama.”



    “Je, kati ya papa na hao dagaa, wewe unajifananisha na kipi?” aliuliza mama Lola.



    “Hee mama! Mie dagaa tu, tena mdogo kabisa.”



    “Haya, nadhani sasa utaelewa maneno yangu kwani akili yako yaonesha kupevuka. Hapa duniani ni sawa na bahari, papa ni wanaume wenye hila. Ni wale watumiao vipawa vyao na mionekano yao kuwahadaa mabinti. Jichunge dhidi ya wanaume walaghai watakao kuonekana katikati ya dagaa,” alieleza mama Lola. “Hivi kanga uloivaa unajua imeandikwaje?” Mama Lola aliendelea kudadisi. Lola aliikagua kanga yake kisha kutoa jibu.



    “Imeandikwa; mbuzi na ng’ombe wamoja, mtu mbali ni kondoo,” alisoma Lola.



    “Waelewa nini napo?” aliuliza mama Lola.



    “Mama mie sielewi. Niambie wewe,” alijibu Lola.



    “Asiyejua maana haambiwi maana. Lakini ukae ukifahamu kuwa, huwezi kuwa mwerevu na mjuvi kwa kila jambo. Umeweza kujibu vema mafumbo nilokuuliza, yumkini hili dogo limekuacha ugenini. Namaanisha kuwa, wenye mali na kauli ndio hushirikiana; nao ni ng’ombe na mbuzi. Humkandamiza kondoo ambaye ni sawa na mtu mjinga ama mpole, kichwamaji asiyeweza kujieleza na kujitetea. Sasa ukae ukijua mwanangu, duniani kuwa mwema kiasi, wema ukizidi sana huwa upumbavu. Msabihi Mungu wako, kwa kudra atazinyanyua juhudi zako uifikie pepo.”



    “Ahsante mama. Ndoto zangu mie nataka kusoma tu, hakuna kingine. Sihitaji kuolewa katika maisha yangu kabla sijakamilisha matakwa ya nafsi yangu. Kwani mama, kutoolewa ni dhambi?” Alihoji Lola.



    “Nisingeolewa ungetoka wapi?” alijibu mama Lola kwa swali.

    “Nisingezaliwa pengine?”



    “Usiwe mbumbumbu. Kuolewa si dhambi, lakini namna ya kuolewa na mtu wa kuolewa naye ndicho huzaa dhambi. Jitunze, soma na fikia malengo yako kisha Mola atakupa mume umtakaye. Ulimwengu unaoupokea usichana wako umejaa mashaka. Usiuharakie ujana na kuupa kisogo utu wema,” alieleza mama Lola. “Nakumbuka ulisema wataka kuwa mwanasheria, bado unaota kuwa hivyo ama ushageuka kama mlevi kitandani?” Alihoji mama Lola.



    “Hapana mama. Ndoto zangu hazitabadilika maana ndilo chaguo langu,” alijibu Lola.



    “Haya binti wa Majaliwa, nitakapopata wasaa nitakujuza mengi, lakini leo nimekumbuka shairi la malenga mmoja. Anaitwa Sudi Bin Hamood Akwaay, alikuwa akiimba tungali Pwani minazini. Ni vema nikuimbie upate kujitwalia ujumbe alotaka wasichana wajue juu ya nikuusiacho.”



    “Mama, napenda sana mashairi. Hebu niimbie, Pwani naona uliikaa na ikakukaa sawia,” Lola alieleza.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Haya shairi sikia, laitwa KIPEPEO:



    Kipepeo we mpole, maishayo ya shakani

    Humjui mwendapole, kinyonga akutamani

    Yake nia akupole, furahayo kichakani

    Ona wala lako dole, kipepeo kwenye jani



    Haraka guu chepusha, kinyonga atafutani

    Yake shida kukurusha, yako ndoto kufitini

    Sijifanye kumrusha, yaja siku kichakani

    Zako ndoto tazikosha, fahamu kuziruhani



    Ndefu safari meenda, heshimayo darasani

    Ngazi nne kuzipanda, kujifunza kwa hisani

    Utelezi njia panda, sisahau kurehani

    Kwa vitabu utapanda, safariyo toka pwani



    Kipepeo binti yangu, nakusihi sijizini

    Kinyonga na nyungunyungu, takukuna kwa thumuni

    Barobaro kama jungu, hakinai kukutani

    Ujichunge kwa majungu, kwa zawadi takubani



    Takuletea nikama, tamaayo kwa kidani

    Kingayo wima simama, kuupinga ushetwani

    Ilimu hima ni mama, babayo awe ilani

    Hishimayo kwa ulama, uombe tena sirini



    Sijifanye we chuchunge, taliwa tena domoni

    Utajipatia nunge, dunia itakuzini

    Shauri langu kinange, hima kijazi sizini

    Saharani na kinange, waombee kwa imani



    Nachoka jipendekeza, harusi si msibani

    Ujingao takutweza, kwa inda na baniani

    Kwetu mie ni jinaza, siyendi kwao Mazini

    Takutia kwa jeneza, ndoto yako ukutani



    takushika kwa upaja, njaa kenda sebuleni

    Nimechoka kubwabwaja, pira natia kwapani

    Kipepeo wewe mja, simtukuze shetwani

    Sasa valia pambaja, kinyonga mwache chakani



    “Mamaaaaa! Kipepeo ndiye nani katika shairi hilo?” Aliuliza Lola.



    “Kipepeo asili yake ni maua, maua asili yake ni urembo. Katika shairi, Bin Hamood alimlenga sana msichana mbichi anayechipuka. Sawa kabisa na wewe binti yangu. Wewe ni kipepeo ambaye wapaswa kukaa macho dhidi ya maadui wengi. Wapaswa kujilinda dhidi yao,” alieleza mama Lola.



    “Kipepeo kwahiyo ni msichana! Amakweli sikuwa nafahamu hilo. Ahsante mama, nimelipenda sana shairi hilo,” Lola alisema. Muda huo alifika babaye akitokea kondeni.



    “Karibu baba’ngu. Shikamoo!” Lola alimkaribisha na kumsabahi baba yake.



    “Marahaba mwanambee! Kuna heri hapa?” Mzee Majaliwa aliitikia na kudadisi. Alikuwa akihema kwa shida kwani alifika pale akiwa mbiombio.



    “Baba, naona umekuja mbimbio, kuna usalama utokako?” Alihoji Lola.



    “Nawe baba yako hata hajapumua ushamjaza maswali ya mkimbizi mpakani. Mwache apumzike kwanza ndipo maswali yako muulize,” mama Lola alifoka.



    “Acha wivu mke wangu. Haki yake mtoto kutaka kujua siha ya babaye. Ama kafanya kosa?” Alieleza Majaliwa. Alimsogelea mke wake aliyekuwa akiutandua mkeka ili kuingia ndani. Wingu na upepo vilishindana. Upepo ulipotulia wingu nalo lilisimama wima, upepo ulipovuma na kufanya fujo, wingu nalo lilikimbia kwa kasi angani.



    “Wewe waonaje, ni sawa afanyavyo? Anapaswa akukaribishe, akupokee kisha uketipo kitako ndipo aje kwa adabu akusabahi. Sasa wamdekeza kama yai, siku akikengeuka utanigeuka najua,” mama Lola aliendelea kunung’unika.



    “Mke wangu yeshe! Mi najua mtoto ni haki yake,” alijibu Majaliwa.



    “Haya, mkeo hujaniona? Maana tangu uniache kitandani alfajiri, huna hata hamu ya kunijulia hali. Jicho lako kwa huyo mama yako, mwanambee mja wa Vuga,” alilalama mama Lola.



    “Maua mke wangu, acha gubu. Huyu ni mwanetu sote. Kusema sijakutakia heri nalo linatoka wapi? Usiku kuchwa tumelala wote, nilijidamka nik’enda kondeni nikitaka uendelee kupumzika, sasa imekuwa nongwa? Kweli hila imekosa pa kwenda. Kibuyu akitiwa kunde hulalama kavimbiwa, akitiwa maji hutapika yashamkinai, tosheka na penzi nikupalo mke wangu,” alijibu Majaliwa.



    “Majaliwa mume wangu, siku hizi si kama zamani. Nilikuwa kama yai kwako kabla sijamzaa huyu mrembo wako. Hukuwa ukibanduka hapa nyumbani na wala hukuwahi kuniacha kitandani. Hata uk’enda kokote, hujawahi kurudi bila kunibebea kijizawadi na kuniuzia maneno matamu. Tena, niliyapokea mbali kabla hata hujafika nilipokuwa nimesimama. Mahaba yashakwenda na maji ya moto sasa waniona kama kibuyu cha siagi. Saweni bwana, mpende mwanao,” Mama Lola alilalama.



    “He! Mke wangu nisamehe. Sikudhani kama utawaza yote hayo. Nyakati hazifanani, nitakuwa mwema basi yaishe,” alijibu Majaliwa.



    “Mie nakubali yaishe lakini yanaishaje hapo ndipo unapaswa ujirekebishe. Fahari ya mume ni mke, na fahari ya mke ni mume,” alieleza mama Lola.



    “Mama Lola usitake kuamsha yaliyolala. Tena naomba yaishe kwa wema tu,” alisema Majaliwa angali akiwa kaingiwa na kijiba rohoni.



    “Hebu yaamshe yaliyolala niyasikie. Yepi hayo yalolala nisiyajue yakufanye hadi unisahau mkeo. Mapenzi yote sasa tangu nimzae Lola yashakwisha kabisa. Hutulii mwanaume kwa mkeo, kutwa kiguu na njia wala hujali kama nahitaji hata tucheze bao kama zamani. Au wataka niende mtaani kukaa kitako na wanawake makuwadi, si utakata kauli wewe?” alisema mama Lola.



    “Makuwadi, kina nani hao?”alihoji Majaliwa.



    “Kina mama Koi na hao vijuso wengine, wale wa mtaa wa maduka. Huwajui mashambenga na makuwadi! Hadi midomo ishawaenda upande kwa kuwasema watu kwa mabaya. Kila mmoja anawanyoshea kidole wale jini walivyo na midomo mirefu?” alifafanua mama Lola.



    “Usitake nicheke ningali naugulia moyoni. Unawaitaje mashambenga na makuwadi? Naona akili zako zote ushaziacha Pwani juu ya mnazi ungali ukija katika kijiji hiki. Unapaswa kuwaheshimu. Tena unatakiwa ukikutana nao njiani, unawapisha wapite na kuwasabahi kwa heshima. Uwapo kisimani wakifika unawapisha kwanza wachote maji na wewe uwatwishe. Wale ni wake za watu, wake wanaostahili kusalimiwa asubuhi na waume zao. Si wewe Maua, hustahili kabisa salamu na matunzo ninayokupatia hadi unakuwa kama faru umenenepa humu kwangu,” alieleza Majaliwa. Mama Lola alikuwa kasimama kwenye kizingiti cha mlango angali mumewe akiwa ndani. Lola alikuwa jikoni akiendelea na maandalizi ya chakula. Mvua ilikuwa imeanza kudondosha matone ya rasharasha.



    “Majaliwa, kosa gani nililokutenda hadi wanitusi namna hiyo? Ulitaka mtoto nikakuzalia Lola, tena kwa shida nusura niupoteze uhai wangu. Hiyo haitoshi, nimekuwa nikitii kila agizo lako la kutoubandua mguu wangu hapa na kwenda kwenye magenge ya wanawake na vikundi vya upatu. Bado waniona hayawani nastahili matusi. Si bure bwanaweye! Utakuwa umeshapata bibi mwingine zaidi yangu naona anakuzuzua. Hata huku kutoka hapa alfajiri ninapata shaka sasa, si ajabu unaenda kumalizia usingizi huko kwa bi mdogo. Mlete basi tuhangaike naye hapa,” alieleza mama Lola.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Maua shida yangu ni moja tu….”



    “Ipi? Looh, huna hata haya Majaliwa. Ushakua achana na tabia za barobaro.”



    “Bado hujazaa. Kabisa hujazaa hata familia yangu naiona ikipaparika kwa ukiwa, haiheshimiki. Tunaonekana wote kama wanawake.”



    “Unasema nini Majaliwa?”



    “Umesikia. Usijitie kiziwi eti hujasikia. Nataka dume humu ndani. Ningetaka mwanamke si wewe unatosha, yanini ningeoa sasa. Nizalie mshika fimbo si mwiko, hapo ndipo utajua Majaliwa alizaliwa Pwani na kulelewa bara kwa bahati mbaya.”



    “Mungu wangu! Majaliwa kumbe siku zote ukimya wako umeficha hayo! Ni kwa sababu ya kukuzalia Lola, msichana na si mvulana. Sasa leo nimeelewa. Hata hiyo elimu yako ya darasa la nne haijakusaidia kabisa. Mtoto ni mtoto tu, jinsia ni maumbile,” alisema mama Lola.



    “Toka mbwa! Ukiwa na rununu ya tochi nawe utajilinganisha na mwenye rununu ya video na picha? Utafananishaje mtoto wa kiume na wa kike. Haunazo kabisa Maua, leo ndo nimefahamu. Mtoto wa kiume ndiye mshika fimbo na mkuki. Ndiye mshika sanda kunitwaa kaburini. Sasa huyu mshika mwiko wako anaweza kunizika? Anaweza kunitetea kwa kuushika mkuki na fimbo dhidi ya maadui!” alifoka Majaliwa.



    “Kinywa changu umekitia shubiri. Usemayo hata sielewi kama wayasema weye.”



    “Lione, usinisimamie wima kama nyonya damu. Keti hapo kitini uipishe mvua inyeshe japo tupate kulima,” alisema Majaliwa.



    “Haya naketi, lakini Majaliwa leo umenikata kauli,” alilalama mama Lola angali akiingia ndani. Alikivuta kiti tayari kukikalia. Alipokifikia ili kuketi, kiti kilivunjika akajibwaga sakafuni.



    “Haya umeona, kwa dhambi zako hukumu ishaanza kukupata ingali asubuhi. Maua niliyekuwa nimeoa alikuwa mrembo. Alikuwa mwembamba, kiuno kimekatika kama dondola, umbo la kibuyu cha maziwa. Shingo yake ilikuwa ndefu kama twiga. Kifua chake kipana, kiwiliwili kilikuwa kimeumbika na kuvutia. Mdomoni alikuwa amejaa meno meupe na tabasamu. Ibara ya nywele zake sasa, laini kama hariri. Midomo kama kaswiba, waridi kasingiziwa. Kula kwake kidogo alishiba na kwa usowe nuru ilicheza na kumfanya anighuri. Hayo ndiyo yalinifanya niache kazi zangu na kukimbia mbio kwenda kumkumbatia kila wakati. Tazama, sasa ushakuwa dubwana kama mcheza mieleka. Mdomoni ndo kabisa, meno yote yashapuruka kama muuza ugoro. Hujulikana kichwani na miguuni wapi. Umenenepa mpaka unachukiza. Sasa unadhani wewe ndiye nilikuoa miaka iliyopita. Umeharibika sana na umejisahau, kisa tu tayari nishakuoa huna la kukufanya. Ujitunze kama vile ulivyokuwa kwa baba yako naweza kukuona tena. Punguza kula, utanilaumu bure,” Majaliwa alieza.



    Mama Lola alikuwa amejizoazoa na kuketi. Kifua kilijaa kwa hasira. Alimtazama Majaliwa akitamani japo kumrarua na kumfanya vipandevipande. Chozi lilianza kumtiririka wakati akilia kwa uchungu. Majaliwa alikuwa kaeleza ya fikrani mwake. Maua alipaswa kuyasikia na aliyasikia na kuyajibu kwa kilio.



    “Majaliwa mume wangu, leo umeniambia maneno ambayo sikutegemea kuyasikia toka kwako. Nisamehe na Mungu atasikia kilio changu. Kama yote haya ni sababu ya kumzaa Lola, basi atafanya namna nitakupatia mtoto wa kiume. Hakika Mungu hana choyo,” alisema Maua kwa uchungu.



    “Maua ulishachelewa kuamua. Lola ndiye fungua na funga mimba kwa uzao wetu mimi na wewe. Sitegemei kama kutakuja muujiza wa kwenu, labda utoke kwa shetani. Hata kama vitabu vya dini vinawataja watu wengi kuwa walizaa watoto wakati wa machweo, kwako haiwezekani,” alisema Majaliwa.



    “Sawa Majaliwa. Hata hivyo, Lola atakufaa najua ipo siku. Hata kama si yeye, uzao wake utakufaa wakati wa uzee wako. Amini Mungu anayo makusudi. Tumpende na kumlea bila kuonyesha hakustahili kuzaliwa hapa. Tu wazazi wake ujue,” Maua alieleza.



    “Haya, maneno yako ni sawa na kelele za mlango. Nishakuzoea, mwambie alete chakula nile hapa maana kazi za shamba zimenifanya kurudi mbio,” alisema Majaliwa.



    Lola alikuwa tayari kaivisha chakula. Aliandaa kama kawaida ya alivyolelewa. Alimtengea baba yake chakula. Baada ya baba yake kutosheka, yeye na mamaye walitenga chakula wakala. Mama Lola alikuwa mnyonge jambo ambalo Lola alilazimika kulihoji. Siku hiyo ilikuwa ikiondoka ifuatiwe na siku ya mkesha wa Noeli.



    “Mama, kesho nitafanya kazi za hapa nyumbani mapema. Nitakwenda kwenye mkesha wa Noeli kama nilivyozoea ili nawe upate nafasi ya kwenda asubuhi. Muda huo mimi nitakuwa naandaa chakula cha siku,” alieleza Lola akimjuza mamaye.



    “Nishakuzoea binti yangu, ibada na wewe hamkwepani. Jitahidi kuamka mapema ili uyakamilishe yote kwa wakati tena kwa ufanisi zaidi,” alijibu mama Lola. “Utaenda na nani safari hii kanisani wakati huo wa usiku? Nakumbuka Pasaka, ulienda na akina Joyce ambao sasa hawapo.”



    “Nitaenda mwenyewe mama. Siwezi kuogopa kitu maana mbalamwezi sasa huchomoza mapema. Nitatembea harakaharaka bila shaka nitafika na kurudi. Wakati wa kurudi ndo kabisaa, watu wengi sana nitaongozana nao,” alisema Lola.



    “Haya mwanambee, kuwa makini maana usiwe na mazoea na binadamu. Kila siku iendayo kwa Mola kuna visanga vingi. Huwezi kuota nani anakuwazia yepi, Mungu tu akuongoze.”

    “Sawa mama.”



    Hatimaye walimaliza kula chakula cha mchana. Lola aliviokota vyombo ili apate kuviosha. Mvua iliyokuwa imesheheni wingu zito na upepo ilinyesha. Hali ya mchana wa saa nane ilikuwa kama jioni ya saa kumi na mbili. Kila mmoja alijifungia ndani akitafakari yaliyotokea siku ile. Hakika ilinyesha hadi jimbi la kwanza kuwika usiku ule.

    Lola, binti mwembamba, tula kwa kimo, sura ya yai na rangi ya mwafrika halisi aliingia mashakani. Si kwa shambulio la guruneti wala mishale ya msasi, ila kwa hila za waja walioasi. Lola angali mwanamwali, alifikwa hamaniko. Gauni lake jeupe ndilo lilikuwa la kwanza kuusema ukweli. Damu zilizokuwa zikimwagika baada ya kuupoteza usichana wake kwa shida, zilisema kwa sauti iliyojaa uchungu kuyaeleza yaliyomsibu.

    Maumivu aliyoyahisi Lola hayakuwa ya kipimo cha macho, bali ilitosha kwa kila aliyemtazama kudondokwa chozi.



    Walimhurumia.



    Alilishika tumbo lake, mkonowe ulisimama chini ya kitovu akijaribu kujinasua kutoka kwenye kichaka alikokuwa ametelekezwa. Chozi kama chemchemi lilibubujika na kuifukuza haiba ya uzuri wa macho yake ya duara. Aliyumba, kushoto kisha alirudi kulia kabla hajaanguka chini kama fuko la taka. Mithili ya mlevi aogopaye mwanga wa jua, aliyabinya macho yake akitazama. Kwa makini alitazama kitu kilichokuwa kikining’inia, kilishikwa na uzi mwembamba wa gauni lake. Yalah! Lola alitulia kidogo. Pumzi bado zilikuwa za kuokoteza. Alitazama na kuuona mkufu ukibembea. Akili yake tayari ilimtaka kuutuma mkono wake, aliushika mkufu na kuutia kiganjani. Aliunyanyua uso kuangaza mbele akiwa kasimama wima akitikisika. Alitafakari kidogo wakati akiyahisi maumivu yaliyokuwa yakiumiliki mwili wake. Hatimaye nafsi yake ilisema, ‘Mola wangu, niokoe dhidi ya hili tufani liutekalo mwili.’



    Kulikoni! Jicho lake liliuendea tena mkufu kuutazama. Uchungu ulimzidi. Taratibu kiganja cha mkono alikikunja kuushika usimponyoke. Ulikuwa kitu muhimu kwake kwa hisi na fikra za wakati ule. Lola aliendelea kujivuta kuifuata njia ambayo ilikuwa karibu na kile kichaka. Zuzu si zuzu, mlevi si mlevi, mgonjwa si mgonjwa, Lola aliweweseka. Nguvu zilimhama, maumivu yalimkalia na kuishinda miguu.



    Alichutama kupumzika. Hakufahamu kilichotokea hadi afikwe na unyama ule. Aliuagiza mkono wake katikati ya mapaja, hakuamini, alitoa siahi, ‘ala!’ Hakuwa na nguoye ya ndani. Alikuwa uchi, gauni lake jepesi lilipepea juu ya mwili ulio tupu. Hatua chache akiikaribia ile njia ya wote, macho mengi yalimmulika kwa mshangao. Kila aliyemtazama alikifunika kinywa chake kwa viganja. Ilikuwa aibu isiyoelezeka.



    Utamu wa mwili na faragha vyote vilikuwa kama chelezo kwenye maji ya bahari. Taarifa za kubuni na kuona zilizagaa kama upepo na kuufikia kila mlango wa kijiji cha Hamaniko. Kwa chuku na chumvi waswahili habari walizisambaza.Wasifu wa Lola wakati ule ulikuwa mdomoni mwa kila mpika maneno kwa kipimo sawa na hata kwa kutia chumvi nyingi.



    Hatimaye wake kwa waume, wana kwa mabinti, wote kama siafu walimiminika kutaka kushuhudia kwa macho. Wote walimwelekea wakijaribu kumsaidia. Lakini haikuwa muda sahihi. Lola hakuhitaji msaada tena. Muda wa kumnusuru dhidi ya unyama uliokuwa umetendeka zamani ulipita. Akiwa bado yupo chini, alijaribu kunyanyuka. Hakuweza. Aliunyosha mkono wake wa kushoto kuelekea kwa makutano waliofika kumshuhudia. Aliwakodolea macho akiwashangaa wangali nao walikuwa wakimshangaa. Mkono wake wa kuume aliupachika tena katikati ya mapaja na kujikunja kama kikongwe akificha aibu yake. Sauti ilimtoroka, “Nimefanyiwa-unyama!” Alitamka kwa shida wakati sura yake ikiwa imejaa simanzi. Alikusudia kuwaeleza jambo watu wale, lakini hawakuelewa.



    Alijaribu tena na tena kuunyosha mkono ili watu waone na kuelewa alichokusudia waelewe. Bado hakuna aliyeelewa kwa haraka. Aliunyanyua mkono uliokuwa na mkufu uliofumwa kwa shanga na kuvishwa kikaragosi chenye ramani ya Afrika, bado hawakuelewa. Macho yake aliyalazimisha kuitazama nuru ya jua lililokuwa likianza kuchomoza, hakuweza kusadiki. Uso wake ulijaa mashaka. Yalimkuta!CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    Mwanaume mmoja alimsogelea Lola akiwa kajawa mshangao. Alimkazia macho kutoka usoni hadi unyayoni. Alimpekua kwa macho tokea chini hadi juu akiwa mkimya. Lola alikuwa peku mguu wa bata. Hereni moja ilining’inia sikioni. Sikio la pili lilikuwa tupu ila tu kulikuwa na kidonda kilichokuwa kikitoa damu. Uso ulikwaruzika na kupambwa kwa mistari mingi. Mdomo wake uliokuwa mzuri kama ua waridi ulikuwa na mipasuko na kuufanya uvimbe. Mwanaume huyo fahamu ilimjia na kumfanya aite kwa sauti, “Lola!” Wakati akiita katikati ya mshangao, aliyashusha macho yake hadi kwenye mkono uliokuwa katikati ya mapaja ya Lola. Zilimpokea damu nyingi zilizoshuka na kufanya michirizi mingi kuelekea kwenye nyayo za miguu yake. Nafsi ya mwanaume huyo ghafla ilijaa uchungu. Uzalendo ulimjaa kisha kutangaza kwa sauti, “Amebakwaaa!”



    “Mkononi ana nini?” Sauti nyingine ya kike ilihoji. Ilikuwa sauti ya mama wa makamo aliyekuwa akijongea kumsogelea Lola. Aliushika mkono wake na kuuchukua mkufu uliokuwa mkononi.



    “Wa nani?” Mama msamaria alimhoji Lola. Lola alibaki akimtazama. Uchungu ulimzidi kisha aliangua kilio kwa sikitiko. Katikati ya kilio lilimtoka neno kumjibu mama yule, “Aliyenibaka!” Kila sikio la aliyefika eneo lile lilijua. Lola alifanyiwa kitendo cha aibu. Mwanaume na yule mama pamoja na wasamaria walimshika Lola kisha walimkokota na kumpeleka hadi kwa mjumbe kutoa taarifa ya kilichotokea.



    *****

    Kabla ya kuelekea kanisani kwenye mkesha, Lola aliamka mapema na kuzifanya kazi za nyumbani. Alifagia nyumba na uwanja, aliteka maji, aliosha vyombo na tayari alikuwa alijiandaa kwenda dukani kufuata mahitaji ya siku.



    Ilikuwa siku muhimu, tarehe 24 mwezi wa Desemba. Ni siku ambayo kila mwaka aliitumia kutwa akijiandaa kuipokea Noeli ambayo huja kila tarehe 25 ya kila mwaka. Hata siku hiyo, Lola alikusudia kukusanya mahitaji yote ya msingi mapema. Aliamini kufanya hivyo angeweza kupata wasaa mzuri wa kwenda kuabudu usiku ule kwa nafasi.



    Akiwa na kusudi lake akilini, aliingia ndani ya chumba chake. Aliangaza juu ya sanduku ambalo alilitumia kuhifadhi nguo zake. Macho yake yalitua kwenye shajara ya matukio ya kanisa. Aliifunua na kuichomoa noti moja, ilikaa mkononi. Aliikunja kisha kuifunga kwenye pembe ya kanga isipotee, aliitunza. Miguu aliinyanyua kutoka nje. Aliufikia mlango na kusimama akitafakari mahitaji ya kwenda kununua. Hatimaye alianza kutafakari moyoni, ‘Mchele, unga wa ngano, mafuta, sukari, viungo vya pilau na….’ Lola hakuendelea kuwaza. Aligundua kuwa, pesa aliyokuwa nayo haikutosha. Alirudi ndani na kuzitwaa pesa zote zilizokuwa kwenye shajara. Kwa haraka tena alitoka moja kwa moja alielekea dukani.

    Kutoka maskani alipoishi hadi lilipokuwa duka, ilikuwa pua na mdomo. Hivyo, alipokuwa akilikaribia dirisha la duka, aliifungua pesa yake na kuishika kiganjani. Aliyatuma macho kutazama pembeni, alimwona kijana aliyekuwa kaketi juu ya jiwe moja kubwa. Ada yake ni salamu, hakuwa na chuki na yeyote, hivyo kwa kutoa salamu ilikuwa kama hewa aivutayo bure.



    “Habari za asubuhi kaka,” Lola alisabahi. Magoti aliyatua chini kwa adabu.



    “Safi! Sijui wewe mrembo! Uko salama?” Kijana yule alijibu. Macho yake yalimsaliti akimtazama Lola kwa hamu. Alikitingisha kichwa chake. Mdomo ulimcheza akitaka kuzitangaza sifa za Lola japo kwa upepo uliokuwa ukivuma. “Kama kuumbwa, wewe ulizidishiwa. Mungu kakutunuku haiba isiyo mfano…,” aliongeza kijana yule baada ya salamu. Lola hakujali, aliondoka zake. Fahari ya ulimwengu kwake ilikuwa ni kudra za Mungu na juhudu ndizo zilikuwa za binadamu.



    “Oliii! Acha kumtani’ mteja wangu….” Sauti kutoka dukani ilionya. Oli alibaki kimya kidogo akitafakari. Jicho lake lilikuwa bado limeganda nyuma, chini ya mgongo wa Lola. Mate alikuwa akiyameza ingali nafsiye ikimtaka kufanya jambo.



    “Kwa nini nisiuvunje ukimya, Koi? Ukweli husemwa. Heri mfalme asemaye kwa kinywa kuliko mtwana afaye kwa ukimya. Muungwana asemapo la moyoni nafsi huwa huru na hupata tiba. Au….” Oli alijibu.



    “Ungelijua hilo, hakika ungelikuwa umetuma washenga kwenda kumposa,” Koi alisema wakati akimtayarishia mahitaji Lola. Binti wa Majaliwa alikuwa kaufumba mdomo wake. Hakutoa neno lolote kuingilia mazungumzo yaliyokuwa yakilenga kumnasa. Baada ya kuwa mahitaji yake yamekamilika, aliubeba mfuko akiondoka kurudi nyumbani. Alipowapa kisogo, Oli na Koi walianza kusogoa wakimteta.



    “Hivi tutaendelea kula kwa macho hadi lini?” Koi alihoji. Aliufunga mlango wa chumba wa kuingilia dukani. Alitembea hadi alipokuwa Oli.



    “Hawezi kutushinda binti mdogo kama huyu. Unajua kumchinja kobe lazima umvizie, ikilazimu hata kulivunja gamba.” Maneno yalimtoka Oli wakati mdomoni akiwa na sigara iliyokuwa ikifuka moshi.



    “Unadhani tutafanyaje kumpata? Kijiji kizima, binti hawezekani. Tangu Kinesi hasomeki, Kilima hashikiki hata Tareta kote huishia kumtazama na mate kuwashuka. Vitongoji vyote wamemshindwa. Hamaniko nzima, warumbi ninaowaamini kwa porojo na mpunga, katu kasimama imara. Watu huenda kwa hamu kumhadaa kwa maneno matamu na nyimbo lakini bado hang’oleki. Wapo waliojaribu kumhonga mapesa, lakini mtoto hajasikia hata shairi moja la mtu. Sasa unijibu, kijiji kizima hiki unataka kuniambia ni mabwege?” Alisema Koi angali akimpoka sigara rafikiye na kuitia mdomoni.



    “Kweli usemayo. Lakini umekaona kalivyoondoka hapa kwa mbwembwe? Kama dudu washa vile. Tikiri-tikiri, tatara-tatara!...mtikisiko huko nyuma utadhani kafungiwa furushi la sufu. Mbona tunalo!” Oli alizungumza. Alisimama na kuiga mtembeo alioondoka nao Lola. “Moyo wangu vumilia, ukishika mawili moja litaniponyoka,” aliongeza Oli.



    “Huwezi kujua, inawezekana kakawa na tatizo. Mwamba!” Koi alisema kwa kusisitiza.



    “Mwamba? Haiwezekani katoto kazuri hivyo kawe na mwamba. Hapo ni shamba darasa unajipandia mbegu kwa maarifa yako,” Oli alijibu kwa msisitizo.



    “Labda kanataka kuingia utawani. Iweje, kijiji kizima hiki hata mmoja! Anaishije bila kupata hamu ya kusalimiana na wajinsia tofauti naye?” Koi alisema kwa kulalama.



    “Mtawa wa Hamaniko?” Oli alisema kisha kucheka kwa kejeli.



    “Haiwezi kutokea. Jimbi wawikao kijiji hiki ni wengi kuliko mtetea. Leo uniambie haka kawe kuku wa banda la uani, katikati ya jimbi wenye ugwadu? Haiwezekani. Siku zinahesabika, tutampata tu. Tena tazama atokapo, kwa Majaliwa pale hapana hata uzio tutashindwa nini!” Oli alizungumza kwa msisitizo. Aliunyosha mkono wake kuelekea mdomoni kwa Oki. Aliipoka sigara na kuitumbukiza mdomoni kwake. Aliivuta kwa pupa na kuukupua moshi kupitia kwenye tundu za pua na mdomo. Moshi uliruka juu na kuelea hewani wangali wakiendelea na mazungumzo yao.



    “Hewala si utumwa! Umezungumza kuhusu utawa. Hakika nimekumbuka jambo muhimu,” Koi aliongea. Alitabasamu na kuyaacha meno yake makubwa kuonekana hadharani.



    “Leo usiku kuna mkesha wa Noeli ujue. Ni lazima Lola atapita hapa usiku kunywa soda. Karibu kila mkesha ni lazima hufanya hivyo. Sasa hii ndiyo nafasi pekee ya kumpata,” Koi alianika siri kwa ujasiri wakati tabasamu likiwa limechanua. Macho yake makubwa kama bundi yalikuwa yakizunguka na kudondosha chozi baada ya kuivuta sigara kubwa iliyomtatiza. “Au unasemaje?” Koi aliongeza.



    “Fyekeo linamhusu. Ukiongeza na zana zako, mia tutampata,” Oli alijibu.



    “Fyekeo kwa majani makavu hapana. Tutaumbuka mapema,” Koi alihadharisha. Alimnyoshea kidole rafikiye.



    “Tumtie kiberiti kisha reki tumzoe.”



    “Kiberiti, Koi! Una maana gani? Eleza mpango mzima.”



    “Kwenye soda tu, nywiii! Cha Kolombia kitamtuliza. Tutamzoa kama tawi la mti tuumalize mchezo kwa ulaini,” Koi alipendekeza.



    “Cha Kolombia kinapatikana wapi kijijini hapa?” Oli aliuliza.



    “Ondoa shaka. Japo nilisahau kuja nacho kutoka mjini wakati huu, najua hatuwezi kukosa,” Oli aliongeza.



    “Nakuamini, jungu kuu halikosi ukoko. Unakumbuka uliniletea kipindi kile. Ninayo akiba kidogo itamtosha,” Koi alieleza.



    “Kweli mwanajeshi haishiwi silaha. Lazima tukatie adabu. Tena….!” Oli alichombeza kwa furaha. “Unajua kuwa, maji ukiyakamia sana, huyanywi?” Oli alimpiga kijembe rafikiye. “Usije ukaishia kushika pembe na maziwa wakanywa wenzio.”



    “Samaki mjanja majini, nchi kavu kitoweo. Hakuna kumkosa. Ushawahi kuona dagaa aliyekikaangoni akaruka na kutoroka? Huliwa hata mfupa usionekane. Tena, nina hakika zote kwa zote, katakuwa bado mdomo wa chupa. Wa kwanza mimi sajenti, halafu mtafuata nyie mlio wavumilivu. Nitaka…..!” Koi hakumaliza mazungumzo. Mteja alifika na kumtaka Koi kunyanyuka kwenda kumhudumia.



    ***

    Jua lilikuwa limetua na kupumzika kuliruhusu giza kutawala. Ilikuwa saa nne usiku. Mbalamwezi ilipambana kujinasua kutoka mikononi mwa mawingu meusi yaliyokuwa yakijitahidi kuikumbata kwa nguvu. Mwanga wake ulijipenyeza na kusafiri kwa usawa kisha kulifanya anga lote kujaa nuru. Wakati huo, Lola alikuwa tayari kahitimisha maandalizi ya siku. Alikuwa kaanza maandalizi kwa ajili ya mkesha.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Baada ya dakika chache, alisikia kengele ya kanisani ikiliteka anga lililokuwa tulivu kwa tafakari. Alinyanyuka na kuitwaa ndoo ya maji. Aliingia bafuni kuusafisha mwili wake. Hakuwa ameikumbuka sabuni aipendayo, alirudi ndani kuifuata. Alijitwalia Yolanda-sabuni ndipo aliporudi tena bafuni. Alimaliza kuoga, kanga yake aliitumia kuukausha mwili. Aliziokota nguo tayari kurudi ndani ya chumba chake. Macho aliyaangaza kulitafuta kopo la mafuta ya kupaka. Mkono wake wa kuume ulimsaidia kupapasa kitandani. Alilipata kopo alilolifunua na kujipaka mafuta ya mgando. Sanduku la nguo zake alilifungua. Alichomoa nguo yake ya Noeli aliyoipenda. Aliitupia kitandani kabla ya kupiga hatua kwenda nje palipokuwa na moto mkali wa kuni.



    Muda huo alibaki na kanga moja nyepesi iliyoushika mwili. Alikichukua chungu kitupu na kukiinjika jikoni, alirudi ndani kuvaa. Gauni jeupe pee alilitupia mwilini. Lilimwagika hadi unyayoni na kumfanya aonekana malaika katikati ya mawingu meusi. Lola aliinama, macho yake yalielekea uvunguni alikochomoa viatu avipendavyo. Chubwi! Miguu yake aliitumbukiza kwenye loso kisha kuzikaza kamba sawia. Mkononi alizipachika bangili zake za shaba. Heleni alizipachika masikioni zikaning’inia kama pilipili mbuzi. Alikichukua kioo kujikagua akiutumia mwanga hafifu wa kibatari kilichokuwa kikiangaza chumbani usiku ule. ‘Nimependeza!’ Nafsi yake ilimsifu.



    Lola alikirudisha kioo kisha kukokoa mafuta ya mgando kwa vidole vyake. Alikijaza kiganja. Hatua alizipiga kuelekea ulipo mlango wa kutokea. Macho yalimsafirisha hadi kwenye chungu alichokiinjika. Kilichemka na kuwa chekundu kama kaa la moto. Alivifikicha viganja kuyalainisha mafuta kabla hajayakandika kichwani zilipo nywele zake fupi. Aliendelea kuzifikicha hadi zikayameza mafuta yote. Naam! Lola alikusudia kuzijali nywele zake zilizoukoleza uzuriwe wa asili.

    Macho aliyaangaza, kushoto kisha kulia pale sakafuni. Aliliokota tambara lililokuwa limelowa na kulifanya shikio. Alikitwaa chungu cha moto na kukipitisha kichwani akikizungusha kila sehemu yenye nywele. Sawia! Kusudi lake lilitimia. Huyooo! Lola aliingia ndani hadi kwenye kioo na kujikagua. Ng’aring’ari! Nywele zililala na kuwa kama zilipitiwa na ulimi wa ng’ombe. Maandalizi ya Lola yalikuwa tamati, fika moyo wake uliridhika.



    Kengele ya pili ya wito kanisani ililia kumkumbusha. Aliitwaa noti kutoka kwenye shajara na kuitia kiganjani wakati akiharakisha kutoka nje. Aliwaaga wazazi wake waliokuwa wakiota moto usiku ule. Chapuchapu! Aliifuata njia yake iliyomchukua karibu na duka ambalo hulitumia kutwaa mahitaji yake. Baada ya kulikaribia, nafsi yake ilimvuta na kumsaliti. ‘Soda! Kesho sitapata muda wa kunywa soda. Kila mmoja atakuwa na hamu ya soda hadi watu watagombania. Ngoja ninywe kesho ipite.’ Lola aliukubali ushauri wa moyo wake. Aliichepusha miguu yake hadi dukani.



    *****

    Baada ya hamu kumzidi, Lola mate yalimwagika, Shwaa! Utamu kolea. Mdomo ukahitaji kuupatia kilichopaswa kunywewa wakati huo. Moyo ulimsukuma kuifungua noti iliyokuwa mkononi na kumpatia Koi, muuza duka. “Nipatie Punto ya baridi.” Aliagiza Lola angali akiyapepesa macho yake upande wa nje ya duka lile. Aliwaona vijana wengi wakizagaa katika uchanjaa wa duka lile kama siafu. Wengine walikuwa wakitimua moshi wa sigara katikati ya mazungumzo waliyokuwa wamependezwa nayo. Wengine kwa kujipumbaza, walisimama mlingoti vikundivikundi wakipata machozi ya simba ili kujipumbaza. Yote ilikuwa ni namna ya kuupokea mkesha wa Noeli. Lola hakuwajali. Hamsini zake zilikuwa kwenda kanisani na hamsini zilizosalia ni kuinywa soda aina ya Punto ambayo aliitamani. Baada ya sekunde chache, Koi alimnyoshea mkono kumpatia.



    “Hii hapa, nimeshakufungulia… Au?” Koi alihoji. Tayari soda alikuwa ameifungua.



    “Nachelewa, nipe bwana!” Alisema Lola wakati akiipokea na kuitundika kinywani. Aliimimina mdomoni ikapita kooni. Aliuhisi utamu ukilipapasa koo na kuufanya mwili kusisimka. Aliitua chupa kupitia dirisha la duka lile. Alimkazia macho Koi aliyekuwa akiushauri moyo wake kuwa na subira. Kifua cha Lola kilikubali kuipokea soda tamu. Alitabasamu kwa utamu asili alioumeza.



    “Nipe baki yangu,” Lola alitaka baki ya fedha yake. Kiganja cha mkono wake alikifungua kuipokea fedha aliyokuwa akiihitaji.



    “Hujui kama hiyo ni sadaka ya leo?” Lola alinong’ona wakati mkono wake ukizipokea fedha kichele toka kwa Koi. Kushoto-kulia, Lola aliinyanyua miguu yake kuelekea kanisani. Fikra ya aendako ilimjia akilini, kanisani na hakuwaza kingine.

    ‘Leo lazima niimbe kwa nguvu, tena soda hii imenitia nguvu maradufu.’ Yalikuwa mawazo ya Lola aliyekuwa akiumaliza uga wa duka lile kisha kuishika njia iliyokuwa ikielekea kanisani kwao. Wakati akitokomea, Koi alikuwa na furaha isiyo kifani. Alimwita kijana ambaye walizoeana na kushibana naye. Alilitungua shati lake lililokuwa limeshikiliwa na msumari ukutani. Alilivaa mwilini haraka kama mtu aliyefumaniwa akizini. Alivifunga vishikizo kwa mkono mmoja wakati mkono mwingine uliuvuta mkufu uliokuwa umefunikwa na shati. Aliutoa na kuuacha ukionekana shingoni sawia.



    “Niangalizie, muda si mrefu narudi,” Koi alisema. Kijana aliyemwalika kumsaidia alikubali. Koi alitoka mbio kuelekea ilipokuwa maskani ya Oli. Haikuwa mbali, mara baada ya kupiga kona na kuupita uchochoro wenye kuta za mabua, tayari alifika dirishani kwa Oli.



    “Dege limeruka, twende!” Koi alimnong’oneza Oli kupitia dirishani. Baada ya kusikia hivyo, Oli alitoka na kuurudisha mlango wa chumba chake. Walianza kutembea kuifuata njia aliyokuwa ameipita Lola. Macho waliyakodoa kupitia kwenye mwanga wa mbalamwezi iliyokuwa ikitamalaki.



    “Ametoka kitambo?” Oli alihoji.



    Koi alikohoa kidogo kabla ya kujibu, “Ameondoka muda si muda. Nina hakika hawezi kukatisha kile kichaka cha njia panda. Unalijua zigo la Kolombia lilivyo! Kila hatua atakayoipiga damu itazidi kuchemka nalo zigo litampanda kichwani. Atakuwa tayari amecheua,” Koi aliongea wakati sigara akiitia mdomoni. Alikilipua kiberiti na kuiwasha sigara. Kama jadi yake, moshi aliukupua kupitia vitundu vya pua na kumalizia mdomoni. Baada ya kumaliza alimdakisha rafikiye. Miguu yao iliongeza kasi. Macho walizidi kuyakodoa kutazama kwa mbele. Lahaula! Mtu alionekana mbele yao, vazi lake lilikuwa likichangamana kabisa na mwanga wa mbalamwezi iliyokuwa hafifu. Oli alimshika bega Koi kumtaka asimame. Walisimama wima.



    “Amevaa nguo ya rangi gani?” Oli aliuliza.



    “Nyeupe. Tulia kwanza, namwona akiinama na kusimama,” Oki aliunyosha mkono kumwonesha Oli.



    “Tayari mzigo umeshamchukua nini?”



    “Tayari kashikwa mdondo. Kilichopo tunatia hatua hadi alipo. Tunamchota mpaka kichaka kile pembeni,” Koi aliongea. Kidole alikielekeza kumwonesha Oli sehemu ya kichaka kilichokuwa hatua chache na alipokuwa kachutama Lola.

    Wakati Koi na Oli wakijadili jinsi ya kumchota Lola, yeye alikuwa katikati ya jongomeo na kitala. Alipokuwa akitembea, ghafla alihisi joto kali kuuteka mwili. Alijipepea kwa kitambaa lakini hewa haikumtosha. Alihisi wingu zito jeusi kumvamia na kuufunika uso kisha kuiteka fahamu yake. Tayari, zilizala lilimvamia. Lilimtikisa upandeupande likitaka kumdondosha, alilibishia. Alikiagiza kiganja kuyafunika macho aliyoyafumba ili asione kilichokuwa kikimkumba. Wasiwasi ulianza kumwingia binti wa Majaliwa. ‘Mungu, nini kinatokea?’ Alihoji Lola. Akiwa hajapata jawabu, kichwa kilianza kupasuka kwa maumivu. Kilisikia maumivu makali kikigonga kama nyundo ya mhunzi. Alisimama wima. Koo lilimkauka. Tetemo liliitembelea miguu yake na kuipiga vikali. Kila kiungo kilimsaliti mwenzake. Aliyumba kama mti uliopigwa kimbuka jangwani akikubali kuporomoka kwenda chini.



    ‘Mungu, nakufa pasipo kujua sababu. Sijakutenda dhambi. Kama unanichukua nichukue kwa amani. Nisamehe dhambi zangu, wewe ni muweza.’ Lola alinong’ona kwa kutubu. Mikono na miguu ilikuwa uji wa mhogo ikiegama kwenye majani yaliyopembeni ya njia hiyo. Fahamu zilimhama na uono ulitoweka. Udende wa teja ulimiminika akiwa nusu hai nusu mfu. Aliishi katika dunia mbili kwa wakati mmoja, ile ya wafu na ile ya uzima.



    Kama fisi mawindoni, Oli na Koi walimfikia Lola. Walisimama na kuyaangaza macho yao kama kurunzi, walikagua kila upande. Palikuwa tulivu bila hata dalili ya mpita njia wa kuweza kuwakatisha kuikata kiu yao. Walikuwa rafiki wa giza, waliokusudia kufanya kwa hamu ya matamanio yao.



    “Hakuna noma,” alisema Oli baada ya kuyaangaza macho yake kila upande. Kweli hapakuwepo na mtu karibu na pale. Mkono kwa mkono walimpakata Lola. Kushoto Koi wakati kulia alikuwako Oli. Binti aliikokota miguu yake chini akiwa hajitambui. Safari ya fisi wenye njaa iliongoza hadi kichakani.



    “Pale kwenye giza,” domo la Koi lilipendekeza. Walikisogelea kichaka kilichokuwa kimestawi. Majani mengi ya kijani yalikoleza giza eneo lile. Chini walimtua Lola kama furushi la ulezi. Alianguka na kulala chali akiliangalia anga. Mkono mmoja suheli na mwingine kadimu. Pumzi alizikokota angali mwili ulimkana kuusogeza. Nguvu za kujisogeza popote ama kuipaza sauti yake nyembamba kuwafikia watu kwa msaada, yote ilizima. Ulimwengu ulimsaliti!



    “Wa kwanza mimi!” Koi alinguruma. Alimsukuma kwa nguvu rafikiye.



    “Mimi…ah!” Sauti ya ukali ilimtoroka Oli aking’aka kama simba kwenye mzoga. Toba! Mikono ya Koi ililichana gauni la Lola kutoka shingoni hadi kitovuni. Kweli rafiki wa kweli Rabuka, wengine wasaliti. Hamadi! Aibu ilikuwa ikiandikwa katikati ya mapaja ya mwanawali mrembo. Mkono wa Oli ulijipenyeza na kulipasua kufuri lililoulinda mji wa malkia. Gigidi-gagada! Oli alilazimisha kupata upenyo wa kutuliza kiu yake. Ghafla guu la Koi lilimparamia usoni na kumgonga Oli. Lilimsukuma na kumbwaga chini kichakani. Kasi ya kulionja tunda walilolitamani siku nyingi iliongezeka maradufu. Utu wa Koi ilibaki hewani ukielea kwenye vichaka vilivyokuwa vikistaajabu ya binadamu. Mkono wa kushoto ulikazana kuufungua mlango wa mfalme. Alimtembelea malkia pasipo kubisha hodi, aibu isiyo tumainiwa.



    Mzigo wa huba ulimkalia Koi akilini na kifuani. Alijihisi peke yake ndiye aliweza kuitawala dunia pasipo nguvu kubwa. Sherehe ilipiga kambi moyoni, kijana aliongeza juhudi kuulinda umahiri wake juu ya asiye na fahamu. Kushoto alienda, kulia pia alienda. Mbele na nyuma alibembea akitafuta maficho. Mapigo ya moyo yalimwenda omo! Kwa nguvu alijituma kuupasua mwamba. Mwamba wa mawe ya dhahabu ambao Lola aliulinda kwa kipindi chote cha maisha yake ulivamiwa kwa ubaya. Mlango wa malkia haukubisha, ulikubali kufunguka na kumkaribisha mfalme ambaye hakuwa na kibali. Koi alijivuta kama konokono akijaribu kujipenyeza hadi chumba ambacho alihisi malkia alihifadhi asali. Joto kali lilimkaribisha kisha alishikwa fadhaa. Yai lilivunjika, likaukinai moyo wake naye alitapika chakula chote alichokitunza kwa kiangazi chote. Asali aliyoilamba haikuwa na thamani tena. Koi alitoka chumbani akijifuta vumbi lililokuwa limemtanda wakati ule.



    “Hakika ulisema, mwamba!” Koi alitoa ushuhuda. Oli naye alimparamia Lola kwa uchu. Kama mtangulizi wake, alicheza tarazia na kila ngoma alizofundwa na asili yake. Hamu na midadi vilimpandisha mbingu ya anasa. Hakulijua jina lake wala asili ya wazazi wake.



    “Ewaa!” Oli aliafiki kumuunga mkono mtangulizi wake. Alikipanda na kukishuka kilima cha huba kwa kasi. Pumzi zilimuisha. Alijiachia fedhuli kifuani kwa Lola na kumkumbatia kama boya lililo baharini kuwaokoa manusura wa tufani. Lola alihisi kusafiri anga ya shetani. Hakuwa hai na hakuwa mfu, alikuwa katikati ya jongomeo na uzima. Kama mwenye kuota ndoto chafu za mahaba, aliweweseka akijaribu kukinyanyua kichwa chake. Kwa alivyokuwa taabani, hakuweza kuihamisha mikono wala miguu pia. Kwa mbali, alihisi maumivu yakimnyenga angali hakuweza kutambua ukweli.



    Firauni, wanaharamu, fidodido na kila aina ya jina baya ilikuwa sifa halali kwa Koi na Oli kuitwa. Kiu yao ilikatika. Akili ya utu iliwavamia wakawa tayari kuondoka. Walichepuka hadi kwenye njia iliyowaongoza na kuwafikisha walipomchota Lola kama mche wa mgomba.



    “Koi!” Sauti ilibisha hodi masikioni mwao. Walisimama na kuchungua kwa makini. Walikuwa na shaka, hawakumjua mtu aliyewaita usiku ule.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Mbona wanguwangu. Tena kichakani, kuna heri kweli?” Alihoji kijana aliyekuwa mrefu na mwembamba kama mlingoti. Alimkwida Koi na kuliviringa shati lake shingoni. Koi alihisi mambo yalienda omo. Alijua fika, kijana yule naye alikuwa miongoni mwa waliomaliza soli za viatu vyao kumfuatilia Lola. Wazo lilimrukia akapata cha kufanya. Alimsogelea kijana yule mrefu na kumvuta pembeni. Alimnong’oneza, “Lola, ameingia mkenge. Yupo kichakani,” Koi alimwaga mtama. Kijana yule alisimama kimya asiyaamini maneno yale. Hatimaye hamu ya kuona naye ilimjaa.



    “Sema haki ya nani?” alisema kijana yule wakati akimvuta Koi kumrudisha kwenye njia iliyoelekea alikokuwa Lola. Mkufu wa Koi baada ya kukwidwa katika vurumai ile ulikatika na kubaki mkononi mwa kijana yule mrefu.



    “Nakwambia ni kweli. Tumeshamaliza yetu. Kama unataka kukizima kichungi cha sigara, mzimaji yupo….,” Koi alikatiza. Kijana yule ambaye aliongozana na rafikiye baada ya kumwona Lola walistaajabu. Ibilisi aliwavaa kutaka kujua mbivu ama mbichi kwa walivyomfahamu Lola. Tajiri msafisha makombo kikombe hatumii. Aliuachia mkufu ukaangukia shingoni kwa Lola kisha alikibinua kikombe na kukifunika. Kwa zamu, kila mmoja aliizima sigara yake angali Lola akiyoyoma upande upande kama mbuzi achunwaye kwa kitoweo.



    Waonevu! Miti iliyokuwa ikimpepea Lola ilitamka pasipo kusikiwa. Kweli waonevu, tena zaidi ya ibilisi. Dunia ilikuwa ikiwazomea walioutesa mwili wa mwanamwali angali taabani kwa hashishi. Hakika yalitokea. Ndoto aliyoiota wakati ule si ya mchana wala usiku wa maanani, bali ndoto katikati ya wanaharamu waliomtamani kwa huba. Maji yalishakwisha kumwagika, kuzoleka hayakuweza. Historia iligeuka na kuwa kumbukumbu yenye mtihani usio na majibu.



    *****



    Baada ya kutomwona Lola usiku mzima, mzee Majaliwa hakuwa na kituo. Alikuwa mwenye kuzunguka kila pahali. Aliingia ndani na kutoka. Alizunguka kila upande wa nyumba na kuikagua njia itokayo kanisani. Hakupata kumwona. Hakuwa na usemi bali alikuwa akitamani japo amwone Lola ndipo angeweza kutulia. Maua yeye alituliza akili zake akitafakari.



    “Baba Lola, usihangaike huko nje mme wangu. Usiku huu mkubwa huwezi kujua utakutana na nini. Najua Mola atamleta Lola akiwa mzima kwani alikoenda ni mahali salama,” alisema mama Lola kumsihi mmewe.



    “Nyamaza kinyamkela. Usitake nikufanye kile kinamngoja kumpata nuhusi wako,” alisema Majaliwa akimjibu mke wake. Povu lilimjaa mdomoni kisha staha ilimhama.



    “Nuhusi wangu wataka kimpate nini? Unajua kile kimemkawiza kufika, Baba Lola!” Aling’aka Mama Lola. Hakutaka mmewe amhukumu bintiye kwa jambo asilokuwa na uhakika nalo. Aliendelea kuwa na imani kuwa, Lola angerudi akiwa salama.



    “Saa kumi kasoro hii! Kanisa gani linasalisha waumini usiku kuchwa?” Majaliwa alisema baada ya kuitazama saa yake iliyokuwa ikimkonyeza. “Maua, Lola alishakushinda na leo mmeamua namimi nijue. Baada ya mkesha wa Noeli umegeuka kuwa mkesha wa…”



    “Majaliwa nyamaza! Weka akiba ya maneno mme wangu. Kwa nini uhukumu ungali huna uhakika. Utajuaje kilichomkuta?” Alifoka Mama Lola. Hali ikawa si hali. Vuta n’kuvute ikawa sehemu ya wawili hao wakipingana kwa ambacho hakuna kati yao alikuwa akikifahamu.



    “Unaona! Nilishakuonya siku nyingi Maua. Leo sijui utanieleza nini?” Mzee Majaliwa alifoka kumgombeza mke wake. Mama Lola alinyamaza kimya. Alijikunyata kama paka jikoni asiye na la kufanya. Aliikusanya mikono yake akimwomba Mola kumsaidia. Alijawa hofu.



    ‘Lola mwanangu! Hujawahi kuniletea jefule kama leo. Uko wapi Lola? Njoo kabla babako hajanimaliza.’ Mama Lola alinong’ona nafsini akisema na roho yake. Mzee Majaliwa bado alikuwa akienda humahuma kila upande. Kila pahali kwenye uga uliotanda mbele ya nyumba yake aliufikia kama kifaru. Mkongojo ulikuwa mkononi akiyaangaza macho yake kila kona. Mishipa ya kichwa ilimsimama wima.



    “Leo utanitambua! Aibu gani unataka kuniletea kijijini hapa? Hamaniko yote leo masikio yatawasimama kusikia mtoto wa Majaliwa amelala uchi nyumba ya jirani. Tena!” Majaliwa alitamani kumwona Lola akifika ili kumwadabisha.



    “Ndiyo maana! Shikamoo-Shikamoo Majaliwa! Zimekuwa nyingi hadi sijui kwa nini? Barobaro wengi shikamoo wananirushia kama mwalimu wa shule? Ah! Leo nimepata jibu zuri sana. Kumbe shikamoo zikizidi inapaswa kufuga mbwa wakali. Shikamoo nanyinyi, pumbafuuu!” Majaliwa alifoka. Alielekea upenuni kilipokuwa kiti chake ambapo aliketi. Alimtazama mkewe kwa jicho la husuda.



    “Wewe makorokoro, huyu kahaba alikuaga kuwa atalala kwa nani? Maana wanaonitupia shikamooo ni wengi hawahesabiki. Ni wengi kama nyota za anga pevu,” alihoji Majaliwa.



    Kwa jazba Mama Lola alibwatuka, “Nikuulize na wewe. Ndiyo!..maana alituaga wote kisha kwenda zake. Saa ngapi aliniaga mie peke yangu? Baba Lola usinitafute. Ni kawaida yenu wanaume, binti akikengeuka tayari maneno huwafyatuka fyaa! Kafuata ujinga wa mamaye. Mwana akienda nginganginga, kafuata ukoo wa mamaye. Nimechoka Mzee Majaliwa! Nyie mazuri ya watoto ndo yenu, mabaya yote upande wa mama. Kulea jukumu la wote,” mama Lola alifoka. Mzee Majaliwa alikuwa akiutingisha mkongojo wake kwa ghadhabu.



    “Hivyo unaniambia mtoto wa kike anaweza kufuata tabia za baba yake? Tangu lini? Ungenizalia dume la mbegu, dafrau hii ningeiona wapi? Shida umenizalia jini mahaba, malalo ufukwe wa bahari. Nitawachinja ili Hamaniko isimame kwa hofu,” mzee Majaliwa aliongea angali akiingia ndani na kulichukua jambia lake. Ilikuwa yapata saa kumi na moja na nusu ikielekea saa kumi na mbili muda huo. Haraka aliufikia mlango akitoka kwenda zake.



    “Naenda kwa mjumbe kutoa taarifa. Akija huyo maarasi wako, katu asikanyage kwenye upenu wa nyumba hii. Nimkute kachutama hapo katikati ya uga nimtolee sadaka ya jongomeo,” alisema Majaliwa wakati miguu yake akiisukumiza ndani ya katambuga zilizokuwa mlangoni. Alitoweka na kwenda zake. Mama Lola aliugulia kwa uchungu. Hakuwa anajua hatua sahihi ya kuchukua zaidi ya kichwa chake kujawa na vurugu.



    ‘Miaka dahari tumekuwa tukiomba mtoto, hatimaye Mungu alijibu kwa kutupa Lola. Maua mie. Majaliwa hampendi Lola, mtoto wetu wa pekee. Leo anadai ningemzalia dume ungali wakati ushatupa kisogo. Kwani Lola gumegume, eh! Mungu anajua.’ Mama Lola alizungumza peke yake yangali machozi yakimlengalenga.



    Haikuchukua muda mrefu, Majaliwa aliwasili kwa mjumbe. Alipewa kiti na kuketi. Walianza mazungumzo kama Majaliwa alivyokuwa amekusudia.



    “Ndugu yangu, yaliyompata fila sasa yanampata na lila. Nipe pole ndugu yangu,” Majaliwa alisema. Alikichezesha kichwa chake ungali mkongojo wake ukiwa wima mkononi.



    “Hee! Majaliwa punguza maneno ndugu yangu. Pwani na bara ni vitu viwili kama kisogo na ugoko. Wamaanisha nini kuwa lililompata fila sasa limempata lila?” mjumbe alihoji.



    “Yamenikuta! Kibibi wangu hapo nyumbani kanitia shombo. Hajalala nyumbani leo hadi asubuhi inagonga hodi,” alisema Majaliwa.



    “Lahaula! Usemayo kweli? Huyu bintiyo, Lola au kibibi gani tena?” Alistaajabu mjumbe.



    “Kwani nina binti wangapi hapo kwangu, mjumbe? Ni Lola pekee,” alijibu Majaliwa.



    “He! Ulimwengu umekwisha. Kama Lola huyu ninayemfahamu amekuwa jicho upande, basi kijiji hiki kimejaa laana,” aliendelea kustaajabu mjumbe.



    “Nishasema kitambo, kulea binti bara ni sawa na kumtosa chura kwenye bwawa la samaki, ataliwa tu kwa vyovyote. Sasa Lola kawa samaki, chakula cha Noeli kwa vijana. Nishakata tamaa na hivi sihitaji kabisa kumwona,” alilalama Majaliwa.



    “Majaliwa, mzazi hasusi. Bintiyo kanyea kono huwezi kulikata. Vuta subira yatapita. Sasa, unajua kalala kwa nani?” alihoji Mjumbe.



    “Hata sielewi. Shikamoo mtaani ziko nyingi siku hizi tofauti na hapo awali. Sasa nimebaini salamu kwa barobaro wa kijiji hiki zinamaana kuwa Lola kakua. Hata sijui atakuwa kwa nani,” alijibu Majaliwa.



    “Sasa waamuaje, mzee mwenzangu?” alihoji mjumbe.



    “Vichwa viwili ni baraza. Nimekuja kukujuza, unishauri nduguyo,” alieleza Majaliwa.



    “Haya. Kikubwa kwanza atafutwe alikolala. Akipatikana ndipo tutajua hatua ya kuchukua. Una mashaka na kijana gani tuanzie huko?” mjumbe aliuliza.



    “Hata sijawahi kuota. Mzunguko wa binti yangu huishia dukani. Sasa kama dukani walimkuwadia basi itakuwa shuku yangu ya kwanza kwao,” alijibu Majaliwa.



    Angali mjumbe hajatoa jibu juu ya jambo la kufuata, kelele ziliyafikia masikio yao. Ghafla walinyamaza kimya wakisikiliza. Hekeche! Hekeche! Mjumbe alijihekemua kunyanyuka. Aliyakodoa macho yake kutazama upande ambao sauti zilikuwa zikitokea.



    “Haya sasa, kila sikukuu na viroja vyake. Starehe waponde wao, karaha mbio kwa mjumbe! Sijui waletwa nini umati ule wote?” Mjumbe alijaribu kubashiri ungali umati haujamfika karibu.



    Wima, mzee Majaliwa alisimama mlingoti kama korongo ufukweni. Mwaa! Macho yake yalisafiri hadi katikati ya umati uliokuwa ukiwasogelea. Kama zumbukuku, alibaki kaduwaa. Mdomo ulimfunguka kama mamba mtegoni. Domo lake la kuloloma lilipigwa ganzi na kusinyaa. Kimya! Alinyamaza yangali macho yake yaliganda katikati ya umati uliokuwa umewasogelea karibu. Macho aliyahamisha na kumtazama mjumbe kisha kuyahamisha tena kwa kwenda pale yalipokuwa awali. Mkono wake wenye mkongojo aliunyoosha kuelekea pale macho yake yaligonga mhuri wa moto.”



    “Lola!?” Majaliwa alitorokwa na maneno akimwita bintiye. Miguu yake ilishindana kuupokea umati ule. Demedeme! Lola alijikokota akidema kama mlevi aliyeutundika mtama na kumfanya taabani. Mwilini aliviringwa kwa kanga aliyohisaniwa na mama msamaria. Alikuwa bado akipepea kama bendera mlingotini. Aliegama kushoto na kulia kwa watu waliomshikilia. Mguuni hakuwa na kiatu, alikuwa peku kafunikwa na tope. Macho ya mzee Majaliwa yalishuhudia binti asiyemfahamu.

    Mwili wenye afya na angavu ulikuwa vungevunge, ulidhoofu na kunyong’onyea. Uzuri ulipotea, machoni, alitazama kama mwenye degedege. Michirizi ya machozi ilipiga kambi nakujitangazia utawala kwenye mashavu yake mororo.



    “Mwananguuu!” Mzee Majaliwa alipiga nduru. Alimwendea mwanaye akitaka kumkumbata. Pwata! Lola alijibwaga kwenye uga wa mjumbe uliokuwa umeyameza maji na kuvimbiwa. Tope lililojaa utelezi lilimchukua hadi kumfikia baba yake. Wasamaria walimzunguka wangali wakinong’ona, “amebakwa! Semeni haraka, amebakwa!” Zilisikika sauti katikati ya umati ule. Mjumbe alikuwa bado koo limemzuia kutamka lolote. Yeye pamoja na mzee Majaliwa walikuwa kodo wamemkodolea macho Lola. Hawakuwa na kauli.



    “Binti huyu kafanyiwa unyama usiku mzima. Amebakwa! Tena, kama samaki kikaangoni…” Mama msamaria alibwabwaja angali akiliweka sawa gauni lake bwangabwanga. Mzee Majaliwa aliufumba mdomo kisha kuketi chini akikisahau kiti alichokuwepo. Mikono yake aliirudisha kisogoni kwa huzuni.



    “Nani kafanya unyama huu? Nani naulizaaa?” Majaliwa alifoka.



    “Huyu hapa!” Mama msamaria aliunyanyua mkono kumpatia mjumbe ule mkufu.

    “Yuko wapi nimchanechane kwa panga langu?” Mzee Majaliwa aliruka kama chui akitaka kumtia mkononi mwanaume aliyesaidia kumfikisha Lola pale. Umati ulipiga kelele kupinga uamuzi wa mzee Majaliwa.



    “Siyo huyooo!” Majaliwa alimwachia mwanaume yule. Mjumbe aliunyosha mkono kumpatia Majaliwa ule mkufu ambao alikuwa kaupokea.



    “Hiki kikaragosi kimemfanyia binti yangu aibu?” Mzee Majaliwa alifoka. Aliutupa chini mkufu alipokaa Lola. “Hamuwezi kuniambia kidubwana hiki kinaweza ku-ku….ah!..mwanangu.”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Mzee Majaliwa, piga moyo konde. Mimi nadhani kidubwana hiki kitasaidia kumpata aliyetenda unyama huu. Au mnasemaje?” Mjumbe aliuliza mbele ya ule umati.



    “Ndiyoo!” Kelele na mbinja vililifunika eneo lile. Wengine kwa chinichini walinong’ona, “muuza duka!” Sauti hizo zilijirudiarudia hadi kuyafikia masikio ya mjumbe na mzee Majaliwa

    Baada ya kujua kile kilimpata Lola, mjumbe na Majaliwa hawakuwa na ziada. Ilikuwa na wasaa wa mjumbe kukata shauri juu ya hatua ya kuchukua. Ilimlazimu kuitisha kikao cha baraza la kijiji ili wasaidiane kuutafuta ukweli. Mwanaume msamaria ndiye alikasimiwa jukumu la kupiga mbiu kuwaalika wanakijiji. Alienda kila kona akiipiga ngoma yenye mlio mkubwa. Kila baada ya mapigo ilijipenyeza sauti yake kuwaalika wananchi kujumuika kwa mjumbe. Kila sikio kijijini lilifikiwa na wito huo.



    Ilichukua muda mfupi, yapata saa moja ndipo kila mkazi wa kijiji cha Hamaniko alitia mguu wake kikaoni. Ilikuwa wito wa dharula maana lilikuwa jambo la nadra sana kuisikia ngoma hiyo ikialika watu. Hatimaye baraza la kijiji liliketi tayari kuanza kutafuta ufumbuzi wa jambo lililomkumba Lola. Kilichodaiwa kuwa ushahidi wa shauri la Lola dhidi ya mtu asiyejulikana kilikuwa mikononi mwa mjumbe. Lola alikuwa kaketi pembeni juu ya jiwe kubwa akingojea kumjua aliyemfanyia unyama ule. Fikrani mwake kulijaa fukuto akiwaza kwa bashiri kuhusu mbaya wake. Jicho lake la duara alilizungusha kama kinyonga kumwelekea kila kijana aliyekuwa mbele ya baraza. Macho yake yalisafiri na kuzikagua shingo za vijana ambao wote walikuwa na tabia ya kuvaa mikufu shingoni. Nani alihusika? Hili ndilo lilikuwa swali kuzidi yote kwa uzito katika hisi zake. Lola aliingiwa wasiwasi kila wakati ambao macho yake yalitua shingoni kwa Koi. Hakuwa na mkufu kama walivyokuwa vijana wengine. Haikuwa kawaida ya Koi kutoka maskani kwao akiwa hana mkufu wake. Moyo wa Lola ulianza kumpatia jawabu. ‘Itakuwa Koi, hata leo hana mkufu shingoni’ Lola aliwaza. Alimkazia macho Koi kwa muda mrefu bila kupepesa macho. Sura aliikunja kama aliyemeza ndimu. Koi aliunong’oneza moyo wake kwa hofu. Macho yake yalimsuta ikamlazimu kuyakwepesha kwa aibu. Hatimaye nafsi ikamsemesha, ‘Lazima nijilinde. Lazima Lola aondoke hapa maana atanifanya nikose utulivu.’ Koi aliishauri nafsi yake. Alimtazama Lola kwa jicho kali ili aogope. Lola hakuhamisha macho yake ambayo yaliiva kama kaa la moto. Hatimaye Mjumbe alisimama wima kuwasabahi wananchi waliokusanyika.



    “Wajumbe, nalifungua baraza kujadili kisa cha binti wa Majaliwa. Ni jambo la aibu katika kijiji chetu. Hivyo lazima tuanze kulijadili. Wajumbe karibuni,” mjumbe alimaliza kuwaalika wananchi, aliketi. Koi aliunyanyua mkono wake kabla hata mjumbe hajafika chini kuketi.



    “Ninalo neno mjumbe,” Koi alizungumza. Alimkazia mjumbe macho ili amruhusu kuzungumza. Wakati huo Lola, mama Msamaria na mamaye Lola walikuwa wameketi peke yao. Walikuwa pembeni na pale wanaume walikuwepo. Wanawake wengine hawakuruhusiwa kufika mbele ya baraza kwa kuzingatia miiko ya Hamaniko.



    “Karibu Koi, zungumza,” mjumbe alimruhusu. Kabla hajazungumza, Koi alimtazama Lola kwa jicho la kuiba. Alilisafisha koo lake kwa kukohoa kisha kumeza funda la mate.



    “Wazee wangu, kama ulivyo utaratibu wa mabaraza yetu, wanawake hawapaswi kusimama mbele ya wanaume. Inawapasa kuketi uani kungojea taarifa kuhusu uamuzi kufikiwa. Hivyo, Lola wa Majaliwa aondoke. Atupe nafasi wanaume tuamue.” Vijana wa rika lake walimuunga mkono kwa kumpigia makofi. Wazee wengi pia walimuunga mkono kwa kutingisha vichwa vyao. Pakiwa na ukimya wa sekunde chache, mwanaume mmoja ghafla alisimama. Hakuwa ameruhusiwa kuipaza sauti yake na mjumbe ambaye ndiye alipaswa kumpa ruhusa. Umri wake haukuwa mdogo kama Koi bali alikuwa na umri wa kati.



    “Wazee wa Hamaniko tunakosea. Tusikubali kukosea wakati tukimtafuta mkosaji. Binti Majaliwa ni mhimili katika uamuzi katika baraza hili. Tena si peke yake, na yule mama msamaria ni mwanga atumulikie kuyajua waliyoyaona gizani. Lola ndiye mtendwa na shahidi wa nafsi yake. Anao ushahidi. Tukimwondosha, nani atatueleza ukweli wa yaliyomtokea? Au tutapiga ramli?” Alimaliza kuzungumza mwanaume huyo na kuketi. Koi alisimama akiwa amejawa jazba. Hapakuwa na haja tena ya kungoja kibali cha mjumbe ili kuzungumza.



    “Dendego nyoka wa kilindoni, chakula chake unga! Mambo ya kike waachie wanawake. Wazee wangu, kwanza kawakosea adabu huyu. Amesimama bila ruhusa, halafu anaongea utumbo. Tangu lini jogoo wa uani akapambana na mwewe paani?” Koi alifoka kisha aliketi. Wazee waliafiki hoja ya Koi na kuipuuza ile ya Dendego. Mjumbe tena alisimama na kuyaagiza macho yake hadi pale alipokuwa Lola, mama msamaria na mamaye Lola.



    “Mama zangu, naomba mtupishe tulijadili jambo hili kwa upana. Tutawaita kuwapatia majibu,” mjumbe aliongea kwa taratibu. Lola hakuwa tayari kuondoka. Shauku yake ya kusikia kinagaubaga ilitoweka ghafla. Si mamaye wala msamaria aliyefurahishwa na uamuzi ule. Japo alionesha kukaidi, macho ya wazee yalimfukuza. Hakuwa na lolote la kufanya kwani hakujua mipaka ya haki zake dhidi ya baraza la kijiji alichozaliwa. Koi alihisi kuupata ushindi, alitabasamu. Mzee Majaliwa alikata tamaa, fika aliijua hila iliyokuwa ikifanywa na wanakijiji kumkandamiza mwanaye.



    Kisha wasaa wa hoja ulifika. Koi alisimama, “Hamanikooo!!” aliwasabahi wanabaraza nao waliitika, “Haki itadumu.” Koi aliendelea, “Ndugu wana wa Hamaniko, hatuwezi kuendelea na baraza hili. Sisi kama vijana tungependa mjumbe atukumbushe kwanza kanuni za kijana mwadilifu katika kijiji hiki. Tunatakiwa kukumbushwa ili tuweze kulijadili jambo hili kwa kuzingatia sheria na kanuni zetu,” Koi alihitimisha kueleza na kuketi. Umati ulimuunga mkono kwa nguvu. Mjumbe alisimama na kuwataka wanakijiji kumsikiliza.



    “Hamaniko, kijiji chetu kinayo miiko na sheria. Nitataja kwa kifupi na kwa haraka kama ifuatavyo:



    1. Watoto wa kike hawapaswi kuwa nje ya nyumba za wazazi wao nyakati za usiku.



    2. Ni kazi ya mzazi kuwalinda binti zake wasizagae kijijini usiku.



    3. Mzazi ambaye binti yake atapatikana akizagaa usiku atafukuzwa au kutozwa haka ya fahali mmoja ambaye ataliwa na kijiji kizima.



    4. Binti ambaye atakutwa na ahamani nje ya nyumba ya mzazi wake usiku, hatasikilizwa bali atahesabiwa mhalifu.



    5. Vijana wa kiume watakuwa walinzi wa kijiji, wataruhusiwa kufika kila sehemu ya kijiji wakati wowote.



    6. Watoto wa kike wenye umri wa miaka 14 na kuendelea watalazimika kuolewa ili kuendeleza koo na jamii za kijiji chetu.



    7. Binti atakaye zini kabla ya ndoa, atasindikizwa na kuuawa kwenye mto wa Kisare.



    8. Hairuhusiwi kwa binti mdogo kuketi mbele ya baraza la wazee kwani hulifedhehesha.



    9. Wanawake wote hawapaswi kwenda mazikoni hata kuketi mbele ya baraza la maamuzi la wazee.



    10. Kila atakayeivunja sheria ya kijiji cha Hamaniko, adhabu yake kubwa itakuwa kuuawa kwa moto au kusindikizwa hadi tawala nyingine baada ya kufukuzwa. Wana wa Hamaniko, hizo ndizo amri kumi za kijiji chetu,” mjumbe alihitimisha kueleza, aliketi. Dendego aliunyosha mkono wake juu. “Ndugu zangu. Miiko na sheria hizo zilishapitwa na wakati. Kila mmoja anastahili kupewa nafasi ya kujitetea na kuishi kwa furaha kama wengine. Tusiwabague wenzetu.” Dendego aliongea kisha kuketi. Kelele za kumzomea zilimwandama huku wengine wakimcheka kwa dhihaka.



    “Sheria na kanuni zetu zimetueleza ukweli wa kila jambo,” aliongea mjumbe. Aliyazungusha macho yake kwa vijana. “Koi, unalo neno la kutuambia?” Mjumbe alihoji. Dendego alisimama mara nyingine kuzungumza.



    “Haiwezekani! Kwa sababu baba yake ni tajiri kijjijini hapa ndicho kifanye asikilizwe kila asemalo! Siyo haki,” Dendego alifoka. Sauti ilisafiri hadi kumfikia mjumbe pamoja na Koi. Kwa pamoja walimwendea na kumnyanyua wakimfukuza kutoka katika kikao cha baraza. Koi alijawa hasira.



    “Hatuna cha kujadili hapa. Mjumbe, kanuni zetu zote zinajieleza. Hapa mzee Majaliwa na binti yake wanatakiwa kuwajibishwa. Nashauri tujadili adhabu wanayostahili kwani wameenenda kinyume na matakwa ya kijiji chetu,” Koi alisema kwa msisitizo. Mzee Majaliwa alijaa kifua kwa hasira. Alinyanyuka.



    “Hamaniko kijiji cha wanafiki. Nani aliyembaka mwanangu? Niambieni kama ni halali kwa kilichompata mwanangu. Kosa nitendewe halafu na adhabu nipewe mimi. Uonevu! Au kwa sababu Majaliwa ni maskini mnataka kumfanya mnavyotaka. Sawa, kwa mwenye kiraka hapawekwi msiba lakini machozi humwagika. Hatumalizi hapa..naapa! mtalipa,” Majaliwa alifoka kisha kusimama akiondoka. Mjumbe alimzuia na kumtuliza. Macho yake aliyaangaza akimtazama Koi kwa gadhabu.



    “Kama sheria ni msumeno, basi unakata upande mmoja. Haki lazima ipatikane. Mjumbe..eh! nipe…” Aliongea Majaliwa angali akimpoka mjumbe ule mkufu wa shanga. “Mhalifu wangu ni mwenye kidubwana hiki….angalieni..yuko hapa na mnamlinda kwa kuwa baba yake tajiri! Laana na itamwandama hadi kizazi chake,” Majaliwa alifoka tena angali macho yake alimkazia Koi. Tena alisimama na kutokomea zake. Walimsindikiza kwa macho kisha Koi alimzomea kwa dhihaka.



    Baada ya mzee Majaliwa na Dendego kuondoshwa katika baraza, mjumbe alisimama kutoa hukumu.



    “Jambo hili limefika tamati. Hukumu inayotolewa iko wazi na iko ndani ya kanuni na sheria zetu. Majaliwa anapaswa kutulipa fahali mmoja ili tumchinje na kumla kijiji kizima. Adhabu ya pili, binti yake lazima tumsindikize hadi tawala nyingine, aondoke katika kijiji hiki,” mjumbe alihitimisha. Aliangaza macho yake na kuuona mkono ukiwa umenyoshwa juu.



    “Malecha, karibu uchangie,” alialikwa Malecha ambaye alikuwa kimya kwa kipindi kirefu. Malecha alisimama kisha kuyaangaza macho kwa wanabaraza wote.



    “Nalishauri baraza. Tusimtwishe Majaliwa gunia la misumari. Hebu tuchague moja ambalo litakuwa na manufaa kwa kijiji chetu ndilo tulichukue. Kama kumfukuza, Majaliwa afukuzwe na familia yake, na kama kumbakisha Majaliwa, basi haka ya ng’ombe itamtosha kubaki na familia yake,” Malecha aliongea kwa kudondoa neno mojamoja kisha aliketi.



    Mjumbe alisimama na kuwahoji, “Mmeelewa?”



    “Ndiyo!” Waliitikia. Hatimaye kukawa na minong’ono ya chinichini, “afukuzwe” wengine “nyama!” jambo hilo lilimlazimu mjumbe kuchukua maoni ya wengi.



    Aliwahoji tena, “Wanaotaka afukuzwe mnyoshe mikono juu!” Mjumbe alihesabu kisha kuchora chini. “Wanaotaka Majaliwa alipe haka ya fahali wanyoshe mikono juu,” mjumbe alihesabu, pia aliweka alama chini. “Mmechagua Majaliwa abaki kwa kulipa haka,” aliwajuza. Watu wote barazani walipiga makofi kwa shangwe.



    Mjumbe alikuwa bado akiendelea, “Haka hii itolewe ndani ya juma moja. Mjulisheni Majaliwa kufanya hivyo. Akishindwa tutamtenga,” mjumbe aliongeza. Koi hakuwa na furaha. Alihisi kubaki kwa Majaliwa kijijini pale ingekuwa jambo la hatari kwake. Kila mmoja alinyanyuka na kwenda zake. Koi na Oli walisherehekea ushindi kwa hila japo nia yao haikuwa imetimia.



    *****



    Juma moja liliyeyuka kama siagi kikaangoni. Lola alikuwa akipokea matibabu ya maji na moto kutoka kwa mamaye. Furaha ilimhama akiwa mwenye kuweweseka kwa mawazo. Mzee Majaliwa kwa hofu, alilazimika kulipa haka aliyokuwa ameamriwa. Alikubali yaishe ili kuilinda amani ya familia yake. Aliafiki kuuza shamba lake la miwa, michungwa na mahindi kwa baba yake Koi ambaye alimpatia fedha alizotumia kumnunua fahali mkubwa mnadani. Angali bado fahali hajamwasilisha kwa baraza, alimswaga hadi bondeni kwa ajili ya malisho na maji. Alimfunga kamba kisha alijivuta hadi kwenye jabali kubwa aliloliegemea na kuanza kutafakari. ‘Haki ni pesa, maskini aitoe wapi? Mwanangu amefanyiwa unyama na adhabu abebeshwe. Shamba langu! Tumaini langu pekee nalo limeenda! Mwenye nacho huongezewa. Wenye umaskini huongezewa na manyanyaso, wenye mali na maamzi huwa juu yao. Kama hasira ya bwana kwa waonevu, iwafuate mpaka vizazi vyao. Hamaniko imegeuka himaya ya wanyang’anyi, humpora hata maiti. Miungu watu wamejipa haki ya kuhukumu kwa maono yao. Sisi walalia ngozi hatusikilizwi,” mzee Majaliwa aliteta na moyo wake. Usingizi ulimchukua angali kajiegesha kwenye jabali kubwa. Kwenye anga ya utulivu na ndoto za mateso alisafiri kimawazo. Muungurumo kama mashine ya kuchakata vyuma ulimtoka wakati udenda ukimmiminika. Alikuwa taabani kachoshwa na mawazo pia mihangaiko ya kila uchwao.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    Wakati akiwa kalala fofofo, Koi na Oli walikusudia kumhujumu. Hawakupenda wala kutaka kuona Majaliwa analipa haka na kubaki katika kijiji kile. Walichokitaka ni kuona Majaliwa anashindwa kulipa ili asindikizwe kutoka katika kijiji chao. Kila hatua aliyokuwa akiipiga, walimfuatilia kwa karibu. Koi na Oli waliteta wakati wakiterema kule bondeni alikokuwa ameelekea.



    “Huyu mzee tumnyamazishe. Tukishindwa ipo siku atatuumbua,” Oli alipendekeza. Walikuwa wamekaza miguu kueleke bondeni. Baada ya mwendo wa dakika chache, Koi alisimama na kumshika bega mwenzake.



    “Lazima Majaliwa akihame kijijini hiki. Akifanikiwa kulipa haka, lazima tuichome nyumba aangamie yeye na watu wake. Lakini tukifanikiwa kumhujumu asifikishe huyu fahali kwa baraza, lazima atachukuliwa hatua kali,” Koi alipendekeza.



    “Unadhani tutafanya nini angali na fahali tayari akingoja siku kufika?” Oli alihoji.



    Alibaki kimya kidogo baadaye aliendelea, “Lazima tuhakikishe yule fahali anatoweka. Tufanye namna ili asiweze kupatikana tena,” Koi alitoa pendekezo kwa urefu.



    “Sawa. Ujue mzee yule si pono bali ni mtu wa fikra. Tumwendee kwa makini,” Oli alionya.



    “Akituletea ushari tutamzima kama mshumaa. Hakuna jingine tunaloweza kufanya dhidi yake,” alisema Koi. Muda huo waliteremka toka kilimani wakiliingia bonde lililokuwa limejaa majani ya kijani. Macho yao hayakutulia sehemu moja. Waliangaza kila pahala ndipo walipomwona fahali mkubwa akila majani pembeni ya mto uliokuwa ukitiririsha maji kwa kasi. Walimnyemelea kama chui afanyavyo kummendea swala.



    “Haraka, mfungue twende naye,” Oli alitoa pendekezo kwa kunong’ona sikioni mwa Koi.



    “Tukimchukua tutampeleka wapi?” Koi alihoji.



    “Nenda kamfungue, tumchukue hadi mnadani. Fanya haraka angali bado kizee kasinzia,” Oli alinong’ona. Koi alinyata na kumfikia fahali. Aliifungua kamba na kuanza kumswaga taratibu. Mzee Majaliwa wakati huo alikuwa akiweweseka ndotoni. Hamadi! Dume la ng’ombe lilisiahi kwa sauti. Usingizi ulimtoroka Majaliwa na kumfanya ayafumbue macho na kuangaza akitazama kila upande.



    “Nimekuona! Unanitafuta nini wewe mwanaharashi?” Majaliwa alifoka wakati akimfuata Koi kwa karibu. Aliendelea kumswaga ng’ombe bila kujali tisho dhidi ya Majaliwa. Oli baada ya kuona Koi angeadabishwa na Majaliwa, aliita kwa nyuma. Mzee Majaliwa hakujua kama kulikuwa na Oli kwa nyuma. Aligutuka na kusimama. Aliigeuza shingo yake na kumwona Oli akiwa kabebelea jiwe kubwa mkononi. Angali akimtazama Oli, kijana Koi alimrukia, Majaliwa alianguka chini. Pamoja na kuwa alichomoa jambia lake, halikumsaidia.



    “Leo lazima nitoe salamu kwa kijiji hiki. Kuonewa nimechoka,” mzee Majaliwa alinong’ona angali akiwa bado akijaribu kufukuta pale chini. Jambia lake lilimkaa sawa mkononi. Aliunyosha mkono kumlarua Oli baada ya kunyanyuka. Akiwa hajatekeleza azma yake, tayari Koi alimvaa tena kwa kumrushia jiwe lililotua kisogoni kwake. Chali! Mzee Majaliwa alianguka kisha kujiviringaviringa kama kambale aliyetupwa nchi kavu kutoka bwawani. Tuli! Alitulia. Mikono yake ililiachia jambia lililoanguka mbali naye. Koi alimwendea na kumtikisa wakati macho yake akiyapepesa kila upande. Mbio! Koi alitimka hadi kwa Oli.



    “Mzee kakata kauli! Imeshakuwa adha. Mswage ng’ombe kamuuze mnadani. Timkia mjini tutawasiliana nipate mgao wangu. Naenda kumtumbukiza mtoni ili maji yamtwae tupoteze ushahidi,” Koi alisema. Alirudi hadi alipokuwa mzee Majaliwa na kuishika miguu yake. Alimkokota kama rukwama na toroli hadi mtoni. Alimtosa kwenye maji yaliyokuwa yakishindana kubeba kila kitu kilichoelea ndani ya mto ule. Vingirivingiri! Maji yalimchukua Majaliwa. Yalimchekecha na kumgongesha kwenye kingo za mto na kumviringa kisha kutokomea naye. Hakuonekana tena kwenye upeo wa macho ya Koi. Hasidi! Koi alitabasamu na kujipa sifa iliyomjaza furaha. Majaliwa alitoweka kama bua la mhindi mtoni.



    Ilikuwa asubuhi, kisha mchana hadi machweo, Majaliwa hakuonekana akirudi nyumbani kwake. Mkewe na bintiye Majaliwa walijawa hofu. Haikuwa tabia ya Majaliwa kukawia kiasi kile kurudi nyumbani. Wanafamilia, mke na bintiye waliamua kuifuata njia ielekeayo bondeni kumtafuta. Lahaula!



    Hawakuweza kumwona wala kupata fununu za kujua alikoelekea. Waliamini kuwa, mwenye kwake hafungwi na muda, hivyo huenda angerudi usiku na muda atakao. Walihisi huenda aliamua kumchukua fahali hadi sehemu aliyoona yeye ilifaa kwa malisho. Kwa kuwa usiku uliingia, Lola na mamaye waliishika njia kurudi nyumbani. Mioyo yao ilifungwa na wasiwasi mwingi.

    Wakati ambao Lola na mamaye wakiwa katikati ya hamaniko, Oli alikuwa tayari akiambaa kuingia mjini baada ya kumuuza fahali mkubwa wa dhuluma. Koi yeye aliendelea na biashara dukani kwa baba yake aliyekuwa mfanyabiashara za masafa kuvizunguka vijiji vya tawala ile.



    Kitendawili kigumu kilikuwa kikingoja kuteguliwa. Majaliwa hakuonekana tena na siku ya kulipa haka ilikuwa puani tena mapema asubuhi ya kesho yake. Mama na binti walilala usingizi wa mang’amung’amu wakisikiliza kila kishindo kilichosikika kutokea nje ya nyumba yao. Kila wakati walihisi mtawala wa mji aliwasili. Kamwe! Majaliwa hakurudi. Asubuhi ilifika bila kumtia machoni. Mama Lola alirauka hadi kwa mjumbe kwenda kutoa taarifa za kutopatikana kwa mumewe. Mjumbe hakuwa na njia zaidi ya kuwatangazia wanakijiji kuhusu kutoweka kwa Majaliwa. Kila mmoja alibaki gizani isipokuwa Koi ambaye ndiye aliujua ukweli uliokuwa umejificha nafsini mwake.



    *****



    _________Baada ya miezi 15___________



    Familia ya Majaliwa ilibaki kuwa ya mama na binti. Sauti ya baba aliyekuwa akiwakemea haikusikika tena. Lola na mama yake walibaki wakiwa wasiojua kule mpendwa wao alikuwa.



    Hawakujua wala kuota kama Majaliwa alikuwa hai au mfu. Pamoja na kutoweka kwa Majaliwa, wanakijiji hawakuhangaika kumtafuta. Kila wakati Mama Lola alipohoji kuhusu mumewe walimjibu kwa mkato kuwa, ipo siku mumewe angerudi. Wengine walimbeza wakisema, Majaliwa alitoroka na kuikimbia familia yake. Wengine walimjuza kuwa, Majaliwa alienda kutafuta haka aliyokuwa ametozwa na jamii yake. Yote hayo hayakupata wasaa wa kumwingia akilini mama Lola. Umuhimu wa Majaliwa aliye hai ulionekana ndani ya familia. Pamoja na kuwa aliwachachafya kwa kemeo na suto za kila mara, hawakutaka kumpoteza. Mama Lola mwili aliokuwa nao ulinyauka na kuwa kama muugua unyafuzi. Mashavu yalimsinyaa wakati uso wake uliokuwa na tabasamu angali na Majaliwa ulikuwa wa mwombolezaji. Macho yake hayakukaukwa machozi, kila uchwao alikuwa akibubujikwa na machozi yasiyo kikomo.



    Pamoja na kuishi na mamaye, Lola mambo yalimwendea shelabela. Alikuwa mtu mwenye shibe tangu siku apatwe na hamaniko. Awali hakuwa na hamu ya chakula kwa sababu ya mawazo mengi juu ya tukio lililomkuta. Baada ya muda kutoweka, hali ile ilimwachia bali shibe ilikuwa juu ya mwili wake. Kitumbua kilitiwa hamira hivyo kuumuka ni jadi yake. Hakuwa na shibe ya chakula alichokipenda wala shibe ya uji wa mgonjwa bali alishiba mshindo wa mtu mzima. Mdundiko alioubeba mbele chini ya kifua chake ulimfanya kupata karaha na mateso mengi. Ilikuwa tayari miezi kumi na mitano tangu Lola agundulike na ujauzito usiomjua baba. Kwa aliyofanyiwa ilikuwa ni kitendawili kumjua aliyehusika. Mkanganyiko ulizidi kila siku juu ya hali yake. Aliishi kwenye mawazo yasiyo mshauri zaidi ya mama yake ambaye alisimama kama baba kuiendeleza familia pweke.



    Hamaniko! Lola alikuwa mtu wa kuwaza asiye na pumziko. Aliwaza kutwa mchana na hata usiku. Hakuisha kuihoji nafsi yake. ‘Mungu, kwa nini umeruhusu haya kunikuta. Kwa nini familia yetu imeingiwa tufani? Nani baba wa mtoto nitakayemzaa? Simfahamu, naomba unioneshe wewe. Walionitenda unyama huu niliisha wasamehe. Nifahamishe japo mwanangu apate wa kumwita baba. Baba yangu katoweka, nimebaki bila yeye. Mwanangu naye awe mpweke kama mimi? Hapana Mungu, nisaidie.’ Lola alisema na wa sirini mwake kwa imani. Kila wakati aliulaani uamuzi wake uliomtuma kwenda kwenye mkesha. ‘Mungu, uliniita nifedheheke? Uliniita unitese? Hapana. Najua mimi mdhambi. Umefanya kusudi, naangamia. Nakubali kosa langu nitalitubu, lakini nionyeshe baba wa mwanangu.’ Lola aliendelea kulalama kisha alipiga magoti na kumlilia aliyemuumba. Macho yake yaligeuka chemchemi kwa machozi yaliyofurika na kutiririka hadi mashavuni. Yaliilowesha shimizi aliyokuwa ameivaa jioni ile. Kitendawili, hakikuteguliwa!

    ‘Baba, nisamehe dhambi zangu. Nilikusudia kukiangamiza kiumbe tumboni mwangu kwa kila aina ya uganga, lakini ulisimama imara nikashindwa. Najua mwanangu unamakusudi naye aishi. Nisamehe nitamzaa na kumtunza kwa mapenzi yako. Ukipenda mateso haya kuyaondoa kwangu yaondoe sasa. Kwa nini? Mungu kwa nini? Wake wa watu huenda miezi kenda wakashikwa uchungu na kuwaleta wana. Kwa nini mimi miezi yote hii sijapata kumwona mrithi wangu. Naamini, mapenzi yako ni mema, lazima yatimizwe. Nimechoka! Kama unataka kunitwaa nichukue kwa amani usiku huu. Kitegue kitendawili hiki kigumu!” Lola aliendelea kunena kwa simanzi. Aliyapangusa macho kwa kanga kisha alinyanyuka na kulitupia macho anga lililokuwa limeshiba mawingu likitaka kuitapika mvua. Hofu ilimjaa.



    ‘Eh! Wingu limesheheni, ikinyesha sina pa kuuficha ubavu wangu. Panavuja kila kona kama mwembe.’ Aliongea Lola wakati akitoka na kusimama kisiki akiiangaza njia iliyokuwa ikipita karibu na nyumba yao. Alimsindikiza kwa macho kila aliyepita na kutokomea zake. Akiwa katika tafakari na msongo wa mawazo, sauti ilibisha hodi masikioni mwake.



    “Hujambo mama katumbo?” Ilikuwa salamu kutoka kwa Koi aliyekuwa akipita kuelekea kwao akitokea kwa mjumbe. Lola alimtazama kwa kukata tamaa kisha hasira zilimjaa. Alimkazia macho.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Sijambo baba katumbo,” aliitikia Lola. Koi alitaharuki kusikia maneno hayo. Alisimama kisiki na kumtazama Lola aliyekuwa akikukuruka na tumbo lake.



    “Umesemaje we’ mwendawazimu? Umebeba tembo? Mwaka na kitu unagalauka tu. Mwaka huu unalo!” Koi alisema kwa kejeli.



    “Mtoa jamala Mola, ndiye rafiki aujuaye mwisho wangu. Laiti kwa yeyote aliyehusika..nhe! Nikifa atalitafuta kaburi langu kuniomba msamaha na atakuwa amechelewa,” Lola aliongea wakati akiushumburua mdomo wake. Koi baada ya kuyasikia maneno hayo alighadhabika.



    “Ukitaka kujua uzuri wa mke, mpe pakacha abebe. Loh! Kachoka kama mbwa wa maskini hata hatamaniki. Ngoja nikuonyeshe kwa nini samaki haishi nchi kavu,” Koi alinguruma chinichini angali akiokota kipande cha kuni akimfuata Lola. Chubwi! Kama nguchiro kwenye tundu la kisuguu Lola aliingia ndani na kujibanza chumbani kwake.



    *****



    Baada ya wingu zito kutanda angani, ulifuata upepo mkali uliokifagia kijiji kizima cha Hamaniko. Upepo ulivyokoma, mvua kubwa iliyoambatana na radi ilitapakaa na kukifunika kijiji kizima. Giza lilizidi kuwa zito, dhoruba si dhoruba, kila pahala. Ulikuwa usiku wa ajabu katika mwezi wa pili wa mwaka wenye mvua. Mwezi ambao walimwengu kwa mahaba waliwatumia wapenzi wao maua na mavazi mekundu. Mwezi huo uliwakutanisha waliopendana na kushibana kwa huba. Ilikuwa mwisho wa mwezi wa wapendanao kama adhimisho la Mtakatifu Valentino. Siku hiyo, wenye vibarua walitarajia kuchwe haraka ili waweze kujipatia ujira wao. Usiku uleule, hatimaye yakawa!



    Tarehe ya mwisho wa mwezi ilisomeka 29.02, Lola uchungu ulimshika. Nyonga zilimbana nazo pumzi zilimtoroka. Chwaa! Kama kiwembe, maumivu ya uchungu yalimkata tangu kiunoni kuzunguka kinena na kusambaa mwili mzima. Aliugulia vikali wakati uchungu ukimkwida. Mdomo wake aliupanua na kutoa siahi kumwita aliyemzaa, “Mamaa!” Uchungu wa kumzaa kichanga asiye baba wala babu ulimkolea. Tena aliita, “mamaaa!” Kimya! Hakuna aliyemsikia na kukipokea kilio chake. Mama Lola alilala chumbani kwake fofofo. Hata kama angelikuwa macho, kelele za radi na upepo mkali ziliyaziba masikio na kumfanya kujikunyata kama paka kando ya jiko.



    Shime! Alijikaza. Binti Majaliwa alijikokota akitambaa kukifuata kijinga cha moto uliokuwa ndani ya sebule yao. Baridi kali ilimsugua na kuugandisha mwili wake lakini cha ajabu, jasho lilimmiminika. Hakuweza kusimama. Alijiokota kwa shida kama kenge aliyetenguliwa uti wa mgongo akitaka kuupita mlango wa kutokea chumbani kwake, nguvu zilimwisha. Alipumzika kidogo ingali radi iliendelea kupiga na kumfanya aone sehemu ya kushika, alijivuta tena na tena. Alipofika sehemu iliyokuwa na moto, ilikuwa giza. Moto ulizima kutokana na matone yaliyokuwa yakitoka juu ya paa la nyumba yao iliyoezekwa kwa nyasi. Alijiegesha kwenye jifya akijaribu kuzivuta pumzi upya. Alizipandisha hatimaye alizishusha akijiweka sawa wakati ule wa hangaiko.



    Yalaaa! Sauti ya uchungu ilimwelemea. Jasho jembamba katikati ya baridi liliongezeka na kulivuruga tumbo. Pwaaa! Kwa haraka alitapika. Aliipandisha tena pumzi na kuishusha taratibu. Hali hiyo hakuwahi kuizoea wala kuhisi kumpata, hivyo aliingiwa na shaka. Aliita kwa nguvu katikati ya ngurumo za radi, “Mamaaa! Ma..” Lola aliita kisha kunyamaza. Alihisi bado nyonga ziliendelea kumbana kila alipovuta pumzi kwa pupa. Alianza kutweta kama jibwa wakati wa jua kali. Nguvu zilimwisha tena na kumfanya atulie wakati kajiinamia. Alitulia kwa sekunde chache. Tena! Tumbo lilimvuruga na kuuruhusu mdomo wake kutapika, pwaa! Alitapika. Mate yalimtiririka naye alikishika kiuno na kujinyonga. “Shiiiiih! Mamaa!” Lola alikuwa akiongea na kuita. Uchungu wa kumzaa mtoto hakuwahi kuufahamu zaidi ya kusimuliwa na watangulizi wake. Simulizi za watangulizi ndizo zilimjaa. Tafakari ilimhamisha na kumfanya akumbuke mengi ambayo wenye nzao walivyokuwa wakisimuliana jinsi ya kuweza kupata nguvu na kumzaa kichanga. Lola alijipa shime, ‘Mdomo funga, pumzi nijae mwana aisabahi dunia.’ Alijipa moyo. M-nhhhh! Sauti ilimtoka akiufunga mdomo na kusukuma kingali kijasho kiliendelea kumiminika. Tena na tena akiwa kalala chali pale sakafuni palipolowa maji, Lola alijikaza. Bado safari ilikuwa ikimtaka kujaza pumzi upya. Hakufundwa kufanya hivyo bali ilimtokea kwa kudra. Tena aliufumba mdomo wake akaipandisha pumzi nyingi. Kimoyomoyo alijipa shime kwa kuhesabu, ‘moja..mbili..tatu’ alizibana pumzi na kusukuma. Aah! Kazi ilikuwa ukingoni. Alipumua harakaharaka kama mwimba mziki wa kufokafoka kisha kujiegesha kwa ubavu akiinamia mikono yake. ‘Mungu, mtoe kiumbe wako.’ Alijinong’oneza. ‘Mnh a—a-a-ah!’ Kelele alizipiga. Kama karatasi, mwili wake ulimpwaya. Pumzi alizivuta tena akihisi kuutua mzigo mzito uliokuwa umemwelemea. Sauti ilimtoka tena, “Mamaaa!” Kimya! Hakumsikia mtu. Hakusikia kilio cha kichanga bali aliuhisi mtikisiko kidogo. Nguvu hakuwa nazo kwani hata sauti haikumtoka. Kisha usingizi ulimchukua akalala taratibu.



    Kichanga hakulia wala hakutapatapa baada ya kuzaliwa. Alikuwa mzima au alikuwa si riziki, hayo yote angeyajua aliyemshuhudia kwa mara ya kwanza. Mvua iliendelea kunyesha na radi ilimulika kwa taratibu. Mama Lola aliyekuwa kalala fofofo alihisi kibofu chake kushindwa kuyabeba maji yaliyochujwa mwilini mwake. Chapa! Miguu yake aliishusha kitandani na kuitua kwenye sakafu iliyojaa maji.



    “Ha! Maji au?” Alishangaa Mama Lola. Jubwi! Jubwi! Alitembea akiyakanyaga maji yaliyofurika chumbani mwake. Aliagiza mkono kupapasa ukutani kwenye msumari na kuitwaa kurunzi. Alikiagiza kidole chake kwenye kitufe cha kuwashia na kukisukuma, kwacha! Kurunzi ilicheka na mwanga wake kuking’arisha chumba. Alipiga hatua kuuelekea mlango uliompeleka sebuleni. Mguu wa kwanza ulitoka na kutua salama ukifuatiwa na ule wa pili. Mkono wake aliuzungusha kumulika sebuleni kabla hajatoka.



    “Afanaleki!” Alitamka mama Lola baada ya macho yake kumsaliti. Biwi la damu! Bintiye alikuwa kanyooka na kidubwana katikati ya mapaja yake.



    “Mama yangu, Lola!” Sauti ya hamaniko ilimtoka. Alidumbukia chumbani kwake kama mshale. Wembe, uzi na kanga mkononi alijitwalia na kurudi akiwa bubu. Alikiviringa kichanga kwa kanga baada ya kukitenga na mama yake. Chumbani kwake tena aliingia na kukilaza kitandani kwake kisha kukifunua kidogo.



    “Chausiku wewe!” Mama Lola alikipachika jina kitoto tumbo mara moja. Lola wakati ule alikuwa akiweweseka pasipo ufahamu. Damu nyingi ilimtoka na kuitwaa siha yake shimoni. Alihitaji msaada wa haraka wakati ule. Mama yake alifika, alimshika na kuanza kumvuta akimtoa kwenye biwi la damu na maji. Baada ya kumtoa alimpakua nguo zote na kumfunika kwa vitenge.



    Aliendelea kumkokota hadi kitandani alipomlaza kichanga wake. Hakuwa na fahamu wala hakujua kilichokuwa kikiendelea. Mamaye aliushika mkono kuunyanyua akijaribu kuuachia, ulienda na kutulia. Alimtikisa na kumgeuza kichwa kushoto na kulia, hakuweza kutoa tumaini. Mama Lola aliingiwa hofu.



    “Lola,” aliita mama Lola. Kila alipomtikisa na kumwegesha kwenye mapaja yake, aliifuata sakafu. Bintiye hakuwa buheri, jongomeo kulimuita. “Lola mama!” Aliita tena na tena mamaye, kimya lilikuwa jibu sahihi. Aliichukua kurunzi na kummulika machoni. Kodo! Macho yalimtazama kwa buriani. Yaliachana na dunia, kila moja likiwa na uelekeo wake. Jingine kushoto jingine kulia, yalitazama moja kwa moja.



    “Mwaa-na-nguuuu!” Kilio kilimtoroka mama Lola na kutapakaa kijiji kizima. “Mamaaaaa! Mwananguuuu-wiii!” Alipiga nduru kwa nguvu. Nguo zilimvuka lakini hakujua zaidi ya kumtaka mwanaye aamke na kusimama. Alikiendea kichanga na kukifunua kisha kukishika kifuani. Kimya! Akili ilizidi kumhama. Alikinyanyua tena na kukipakata akihaha kila upande. Hapakuwa na alilolifurahia.



    Siahi za mama Lola ziliwaalika majirani. Walifika kuitikia wito wa mbiu aliyoipiga mama mlezi wa familia ya kukeni. Bado mama Lola aliendelea kupiga mbiu kwa uchungu akiwa tayari maji ya moto alishayakosa na mwana pia alikuwa kamtoka.



    “Nitakuwa mgeni wa naniiiii! Mwanangu---Uhhhh!” Aligugumia kwa uchungu. Hofu ya kubaki ukiwa, peke yake pasipo wa damu yake ilimzidishia uchungu. Mume alimpoteza katika mazingira ya kutatanisha, bintiye na mjukuu pia kisogo walimgeuzia.

    Mama msamaria alikuwa wa kwanza kuingia ndani ya chumba cha Mama Lola. Moja kwa moja alimwendea Lola. Alimtazama kwa macho kupitia mwanga ule hafifu kisha alibaki bila kauli. Alitafakari.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    “Maua, Lola ametupa kisogo,” aliongea mama msamaria kwa sauti ya ombolezo.



    “Binti yangu! Waliokufikisha huku watalipwa kwa kipimo sawa. Pumzika kwa amani,” alimalizia mama msamaria. Alielekeza mikono yake hadi kwa kichanga, alikishika kifuani na kuhisi joto la uzima lingalipo. Alikikanyanyua na kukapigapiga kifuani. Kimya! Alikitazama kisha aliguna. Alikinyanyua tena na kukipigapiga tena na tena kifuani kwa awamu kisha sauti ilitoka, ‘nghaaa-ah!’ Sauti ilimpa tumaini jipya. Mdomo ulimfunguka na kutoa ushuhuda, “Mzima,” mama msamaria alijiridhisha. Hakujali giza wala maji wakati ule. Alijua kichanga alipigwa na baridi na alichoka wakati wa safari yake ya kuifuata dunia ya ndoto zake.

    Alikurupua kipande cha tandiko na kukichana kisha kukitia kiberiti kikawaka. Alilitwaa kopo la samli akaitia mkononi na kukipasha joto kiganja. Alikipaka kichanga mwilini kisha kukifunika ili kipate kupumzika.



    Naam! Binti Majaliwa hakuwa mzima tena. Baada ya kujifungua mtoto wake wa kwanza na wa mwisho, alikata kauli. Damu nyingi iliyomtoka ilimfanya apitilize kuliko mauti. Yalikuwa ni majonzi yasiyoweza kuelezeka. Buriani kwa Lola ndilo lilikuwa neno jepesi kuwatoka wanakijiji waombolezaji. Walimpenda wengi ingawa wachache walimchukia na kukifurahia kifo chake.

    Baada ya kujiridhisha kuwa Lola aliipa kisogo dunia, wanakijiji walijuzana. Walikusanyika na kuitisha baraza ili kufahamu namna ya kufanya. Mzee Godigodi aliipaza sauti yake.



    “Ahadi ya Maulana haina mwamana. Binti yetu katutoka ingali tunamhitaji sana. Pamoja na hayo, inatupasa kutilia maanani miiko yetu. Wanahamaniko wote tunafahamu mila zetu hasa kutokana na aina ya tukio kama hili,” alieleza mzee yule mwenye nyusi nyingi nyeupe.



    “Kweli mzee mwenzangu! Mila zetu zinatuzuia kumsitiri binti ambaye jamii nzima haijanywa mtama toka kwa mume. Hii ni ishara mbaya kwetu. Tukishiriki jambo hili tutakuwa tumetibua mikosi katika ardhi yetu,” alieleza mjumbe.



    Mzee Godigodi aliendelea, “Kwenu Wanahamaniko! Binti ametutoka kwa aibu. Je, tufanyeje wazee wangu?” alihoji.



    “Kanuni za tawala yetu hazijafutika. Hata kama zimefifia inapaswa kuzikoleza kwa kwenda kuutupa mwili wake kwenye mto wa Kisare. Tumpeleke mpakani na kijiji cha Amani. Hiyo itanusuru hali yetu dhidi ya gharika,” aliongeza mzee Godigodi, baba yake na Koi.



    “Mtoto je?” Mjumbe alihoji.



    “Naye hukohuko! Hatufai kuwa naye. Ni mkosi, huoni hata mama yake hakuwa na mume na amesababisha kifo chake! Tumpeleke pamoja naye. Hata kama tutamwacha, nani atamlelea na atamlelea wapi?” mjumbe alisema.



    “Ndugu zangu, tunahitaji mabadiliko katika kijiji chetu. Nawaomba tuyape kisogo maisha ya gizani. Maisha ya wahenga si sehemu ya maisha yetu. Ulimwengu ulishabadilika, tunapaswa kuuacha ujinga uende na wajinga tubaki na werevu. Tusiukatae usasa na kuukumbatia ukale unaonuka. Mimi siamini yote ambayo mjumbe na mzee Godigodi wanasema,” Malecha alisema.



    “Basi mchukue wewe usiye binti kwa miaka dahari!” Godigodi aling’aka. Wazee waliokuwa pembeni walinong’ona chini chini, “Hapana! Haiwezekani! Lazima watupwe mama na mwanaye.” Wakati huo mtu mmoja alinyosha mkono na kutoa hoja.



    “Wazee wangu, naomba mniwie radhi kwa niyasemayo,” alisema na kunyamaza. “Nawaomba sana, tufanye yanayompendeza Mungu kama maagizo yake. La Mungu halina ibilisi wazee wangu! Tunao wajibu wa kuyarejea mafundisho ya Mungu kwa umoja wetu. Marehemu hajatukosea na wala hatuna haja ya kumkosea. Yeye aliye sirini anajua mapungufu yake. Sisi tutimize wajibu wetu. Tusihukumu kwani hata nasi siku moja tutahukumiwa!” Dendego alijieleza kisha kuketi. Kimya kilitawala. Wazee walijigawa magengemagenge. Waliteta, baadhi yao walianza kutoka na kususia shughuli hiyo.



    “Ndugu zangu, Hamaniko ina matatizo mengi sana. Pia familia hii bado tunaidai haka. Majaliwa alitukimbia. Sasa tutawezaje kuendelea kuwahudumia wangali hawataki kufuata miiko ya tawala yetu? Hii ni aibu sana. Kuweza kufuta aibu hii, familia ya Majaliwa watulipe kwanza haka ndipo nasi tuwasaidie. Mchelea mwana kulia, hulia yeye,” mzee Godigodi alikazia kwa kufoka.

    “Wazee wangu, binti huyu alikuwa muumini wa matendo mema. Hata hajawahi kwa makusudi kumtenda mtu ubaya. Tunaomba tumzike, haikuwa chaguo lake,” Dendego alizungumza kwa upole akiwabembeleza wazee. Koi alijitahidi kumuunga mkono baba yake, mzee Godigodi na kumpinga Dendego vikali. Mjumbe alinyamaza kimya akisema na moyo wake. Kila mmoja alionekana mkimya mwenye kutafakari. Kisha mwanaume mmoja ambaye ni msamaria aliunyosha mkono na kuufungua mdomo wake.



    “Hakika, wazo la Dendego ni dawa.”



    “Hivi Dendego na mzee Godigodi, nani alitangulia kuliona jua? Nakuuliza, nani?” Angalia! Kuna mamlaka gani inayoruhusu uchafu wa Lola?” Mjumbe alibwata.



    “Mjumbe, shuka kidogo tuelewane,” aliongea msamaria.



    “Marehemu hakufanya kosa hili kwa makusudi. Ilikuwa nje ya matakwa yake. Tambueni,” aliongeza.



    “Namuunga mkono Dendego kwa maneno yake ya busara. Tumzikeni kwa imani yake. Kama ni mdhambi atahukumiwa na aliyemuumba. Kwetu sisi hatuna alilotukosea na hatujamuumba, iweje leo tumhukumu?” alisema Malecha.



    Mzee Godigodi na mwanaye, Koi walisimama na kuanza kuondoka. Baadhi ya wazee wa kijiji waliingiwa na maneno ya Malecha. Wakati minong’ono ikiendelea, mzee mmoja alijitokeza na kuuamsha ulimi wake. Alikuwa mpiga domo ayari mwenye ulimi mtamu.



    “Ndugu zangu, naomba tukumbushane mafundisho ya wazee wetu; mauti ni siri aijuaye mfu. Na je, nani afahamuye kesho yake itaanzia na kuishia wapi? Kama tunaweza kumsamehe tudhanie ni mwovu, basi tumezisamehe nafsi zetu. Tusitengane kwa jambo dogo. Tumzikeni watakavyo, katu hatutapata makovu!” aliongea mzee kwa taratibu kwa msisitizo mkubwa. Alipokwisha kuyanena maneno hayo, Malecha, Msamaria na Dendego pamoja na wanakijiji walimuunga mkono. Mazishi yaliandaliwa na walikubaliana kumsitiri Lola kwenye makaburi ya kijiji cha Hamaniko. Malecha alimchukua kichanga na kumlea kama mwanaye akiungana na mtoto wa kiume ambaye alizaliwa usiku ule wa huzuni.



    *****

    Maisha ya Chausiku yaliendelea vema pasipo shida katika familia ya kigeni. Kwa siri iliyokuwa imewekwa, hakupata kujua japo fununu kuwa mamaye alikuwa mfu. Mamaye ambaye ni Lola alikuwa ameshaanza kusahaulika masikioni mwa kijiji cha Hamaniko. Hakukumbukwa, dunia haikuwa na nafasi ya kumkumbuka ambaye hakuwa na thamani kwayo. Mola aliyemuumba ndiye alimkumbuka kwa kumtwaa mapema.



    Naam! Chausiku sasa alikua. Umri wa miaka saba ulikuwa juu ya historia yake. Kimo na umbile la kuonekana kwa watu lilimtangaza kijijini kuwa alistahili kuwa msomi. Ilikuwa wakati wa kuufuta ujinga na kuinoa bongo tayari kuyamudu maisha ya dunia gumegume. Haikuhitaji kudra pekee, juhudi ilikuwa kiungo muhimu ili kujiongezea thamani. Ulimwengu haujawahi kumthamini mtu zaidi yake mwenyewe kujitia shime. Hivyohivyo, Chausiku alipaswa kuanza kujipatia kinga kwa kuyavuka madarasa akiushinda ujinga. Chausiku, binti mzaliwa wa usiku, asiye baba wala mama, aliyepatikana kwa uchungu uliomtwaa mamaye alichipuka. Kama mche wa amani katikati ya kijiji cha watu bedui alipaswa kuanza kuijenga haiba yake. Kijiji chenye watu wasiojali utu wa mtoto wala wajihi wa vitendo vyema, kwao matamanio ya nafsi zao ilikuwa ni kumhujumu.



    Katika kujijengea ngome ya umahiri, siku ilifika kama upepo wa demani. Ulikumsukuma kusema maono ya ndoto zake baada ya kuwaona wenye umri kama wake wakienda shuleni. Macho yake yalimtoka baada ya kuwaona wenzake wakiwa na vikombe mkononi. Alivyowatazama aliwafurahia na kuhisi fahari naye kuwa kama wao. Hamu ya kuwa darasani ilimfuma kama mkuki na kumshona kutaka kuwa darasani. Katikati ya jua kali lililosimama wima alimwendea baba yake, Malecha kumweleza niaye.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Baba, nataka shule,” Chausiku alimjuza baba yake nia ya moyo wake. Malecha hakuwa na fikra ya kutaka kumwandika Chausiku kwa masomo ya msingi. Yeye aliwaza, Chausiku angelikua na kuwa msichana wa haja ndipo angeweza kumwozesha kwa yeyote mwenye kumpatia mahari nono ya kustawi. Alikusudia. Kuwaza kwa Malecha kulikuwa kama hekaya za Kingange, kutaka kukiteka kivuli chake na kukifanya msaidizi wake ili yeye apumzike. Chausiku alikuwa malaika mchanga, aliwaza kusoma. Hakuelewa tofauti ya mwanamke na mwanamke japo aliwaona na kuwatofautisha kwa sura na mavazi. Pamoja na kueleza nia mbele ya baba yake, Malecha hakumjibu Chausiku. Alimtazama kama mwendawazimu asiye na thamani mbele ya jaa akichekura makombo na kuyatia kinywani. Hii ilisadifu usemi kuwa, uona kimya, majawabu mawili yahusika; kukataliwa ni moja na la pili ni kukubaliwa. Chausiku hakulijua hilo. Akili yake bado haikuwa pana kwa tafakari.



    Nia ya Chausiku ilistawi kila kukicha na kumfanya binti mwenye kiu ya kuijua shule. Ndoto zake zilianza kumfuma na kumfanya ashikamane kuzitii. Angefanyaje kama babaye mwenyewe hakujali bali alisikiliza agizo la moyo wake la kutaka amali kwa mahari ya binti kiokote!



    Baada ya juma moja kuaga kwa mchanganyiko wa fikra zisizoelewa matamanio wala kiu ya baba wa kufikia, Chausiku alichukua hatua ya ujasiri. Hatua yake ilikuwa ni kutii ukweli wa ndoto zake. Ndoto za kuutoa ujinga na kujielimisha ilisimama mbele yake na kumvuta kuelekea shuleni. Akiwa anacheza kwenye mchanga, Chausiku alifikwa na kundi la watoto wenzake, walewale wa siku zilizopita. Walikuwa na kimo na umri kama yeye. Wao walivaa sare za shule na kupendeza tayari kwa masomo. Alipowaona alisimama na kutafakari sana. Alijikagua na kujilinganisha na watoto wenzake. Alijikataa na kujikana, “sijapendeza! Sina nguo za shule….lakini hapana! Lazima niende shuleni na mimi,” Chausiku alikata shauri. Aliwafuata wanafunzi wale hadi shuleni. Hakuwa na kiatu wala sare ya shule. Hakuwa na daftari wala penseli. Hakuwa na kitu zaidi ya mwili uliobeba kichwa chenye akili zake.



    Chausiku alikuwa na ndoto. Ndoto kuu ilikuwa ni kusoma kama mama yake alivyokuwa na ndoto za kuyamaliza madarasa yote akijielimisha. Fauka ya Chausiku ilikuwa ikitaka kufuata hekima na fikra za mamaye ambaye ni nasaba ya asili yake. Hakujali jinsi alivyoonekana mbele ya watu alipofika shuleni. Alichokuwa akijua pekee ilikuwa ni utu wake pengine kuwa ulikuwa kwenye wazo lake aliloliheshimu. Hakuwa na uoga bali alikuwa jasiri tofauti na umri pia kimo alichokuwa nacho. Wanafunzi ambao aliongozana nao walikuwa wameyazoea maisha ya shule. Baada ya kufika shuleni walikuwa tayari kuingia darasani. Chausiku hakuliingia darasa lolote, alibaki akishangaa. Alisimama nje si kwa uoga wala kutopenda, bali alikuwa akitafakari njia sahihi ya kule angeelekea. Miguu yake iliyokuwa peku ilijaa vumbi la kiangazi. Aliibandika na kuibandua, kushoto kisha kulia alielekea ofisi ya walimu. Hakuhofu wala kumwogopa mtu.



    Ndani! Chausiku alijitoma ndani ya ofisi ya walimu walimokuwa wameketi na kufanya kazi zao, walisogoa pia mambo mbalimbali yaliyowahusu. Mtoto Chausiku tayari alisimama wima katikati ya uwazi uliokuwa umezunguwa na meza za walimu. Kimya!



    Walimu wote walinyamaza na kumtolea macho wakimshangaa. Yeye hakushangaa bali aliwatazama kwa zamu akiwa kimya. Alitabasamu. Kimya chenye maarifa kilichojaa udadisi machoni kilifuatiwa na mhamo wa macho kwa kila picha iliyokuwa ukutani ndani ya ofisi ile. Wanyama, ramani na vingine vingi alivimulika. Jicho lake lilisafiri hadi kwenye meza iliyokuwa bila mwalimu.



    Huyoooo! Chausiku aliisogelea meza ile. Aliona kitu juu yake. Aliifikia meza na kuuagiza mkono wake kwa haraka kukichomoa kiboko kimoja kati ya rundo lililokuwa mezani pale. Alikichunguza kisha kukirudisha. Mdomo ulimfunguka, “Punda haendi bila mjeledi,” maneno yalimtoka Chausiku katikati ya walimu waliokuwa kimya wakimshangaa. Maneno yake yaliwatekenya walimu na kuwafanya waangue kicheko kwa pamoja.



    “Wewe mtoto, kakufundisha nani kusema hivyo?” Mwalimu mmoja aliuliza baada ya kuwa vicheko vimepungua.



    “Baba yangu. Kila siku huwa akinichapa husema..Punda haendi bila mjeledi,” alijibu Chausiku. Alilisukasuka gauni lake lililo chakaa na kubadilika rangi kwa uchafu. Nywele zake kichwani zilikuwa kama mkutano wa nzi, zilijisokota na kujaa mchanga na vumbi. Walimu walipigwa bumbuwazi. Chausiku alikuwa mtoto mwenye tafakari na hekima nyingi. Japo alikuwa mtoto mdogo, alitosha kumfanya mtu kuutambua uwepo wake kwa muda mfupi.



    “Unataka nini hapa shuleni? Nenda kacheze..au unataka mpaka tukutandike mijeledi?” Mwalimu mmoja alisema kwa kumtisha. Chausiku hakuogopa. Alimkazia macho mwalimu yule kisha kutabasamu. Hakuonesha uoga wowote, macho yake yalionyesha ujasiri wake.



    “Chura hamzuii ng’ombe kunywa maji,” Chausiku alisema. Maneno yake yalimwongezea ukubwa kwa waliokuwa wakimtazama kwa kimo chake. Mara hiyo walimu wote walisimama kwa mshangao.



    “Wewe mtoto, umetumwa? Au……” mwalimu mmoja alihoji.



    “Unataka nini hapa, nenda nyumbani kacheze. Au chukua pipi hii uende zako,” Mwalimu mmoja wa kike alisema wakati akipekua mkoba wake na kutoa peremende kisha kumpatia. Chausiku aliipokea kisha kuitia mdomoni. Aliitafuna kama punje ya hindi na kuimeza. Aliendelea kuwasumbua kwa maneno.



    “Peremende ni tamu..lakini imeisha,” alisema Chausiku. Alikenua kinywa chake na kuyafanya mapengo yake mdomoni kuonekana sawia. Bado aliendelea kuwatazama walimu waliokuwamo ofisini mule.



    “Unataka nini wewe mtoto? Tupishe tufanye kazi zetu,” alifoka mwalimu. “Mtoto huyu sijui mzuka ametumwa, maana kijiji cha Hamaniko ni mauzauza kila kukicha. Tokaaa!” mwalimu aliongeza. Alimfukuza kwa nguvu akimtoa kwa kumvuta.



    “Sitoki, nataka kusoma,” Chausiku alieleza nia yake. Mwalimu mmoja aliyekuwa kakishika kiboko alikitupia sakafuni palipokuwa pamejaa vumbi.



    “Pipi ni tamu lakini imeisha! Mtoto huyu ana falsafa kubwa. Sasa anataka kusoma. Pipi tamu lakini imeisha, elimu je? …ni bahari haiishi utamu,” Mwalimu aliwaza wakati kamkazia macho Chausiku.



    “Njoo hapa wewe mtoto,” Mwalimu mwingine aliita.



    “Unajua kusoma?”



    “Najua.”



    “Nyoosha mkono wako, pitisha kichwani ushike sikio upande wa pili nione kama umekua,” Mwalimu aliamrisha. Chausiku alitii kwa kufanya alichoagizwa. Mikono yake ililishika sikio. Mwalimu alipiga makofi.



    “Kweli umekua. Una miaka mingapi?” mwalimu aliuliza.



    “Mingi tu….”



    “Unajua kusoma nini?”



    “Kichwa, pua, nywele, tumbo, sikio, mdomo…” Chausiku alitamka wakati akishika kila kiungo alichokitaja.



    “Safi sana. Unaitwa nani?”



    “Chausiku.”



    “Baba yako nani?”



    “Malecha.”



    “Mwalimu Caro, njoo msajili mtoto ajiunge na shule.” Mwalimu alimwita mwalimu mwenzake. Chausiku alivyomwona mwalimu aliyeitwa alitabasamu. Alionekana kujawa furaha hadi alianza kurukaruka.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    “Caro ndo nani?” Chausiku alihoji.



    “Mie, naitwa Carolina Kimbo,” alijibu mwalimu yule wa kike. Alitabasamu na kuufanya mwanya wake mdomoni kuonekana bayana. Chausiku alimsogelea mpaka miguuni kwake na kusimama mbele yake alipokuwa ameketi.



    “Na mimi hivyohivyo. Naitwa Carolina Malecha,” Carolina alijipa jina jipya.



    “We’ nimesikia unaitwa Chausiku. Mbona unataja jingine tena mtoto mzuri?” mwalimu alidodosa.



    “Hilo la nyumbani na hili la shule.”



    “Hapana. Mpaka niwaulize wazazi wako juu ya hili. Kwani wako wapi?”



    “Hawapo. Mimi ni Caro pia,” Chausiku alisema kwa kusisitiza.



    Kila mwalimu alipojaribu kutaka kumsisitiza atumie jina la Chausiku aliangua kilio. Basi mwalimu alimwandika kwa majina matatu, Carolina Chausiku Malecha. Hapo ndipo maisha ya Chausiku yalianza kama mchezo wa kuigiza. Baada ya kuandikwa alipelekwa darasani kujiunga na wenzake. Wengi walimshangaa kwa kuwa hakuwa na sare za shule.



    *****

    Baada ya kumpoteza mmewe na hatimaye kifo cha mtoto wake wa pekee, Maua alibaki mpweke. Alikuwa mkiwa asiye mtu wa kusema naye hata kubadilishana mawazo. Nyumba yake ilikuwa ya mkono mmoja. Alikuwa akifungua na kufunga mlango pasipo tegemeo la kumsikia mtu mwingine. Furaha hakuwa nayo, mwili wake ulidhoofu wakati fikra zake zilikuwa kama mwenye kurukwa na akili. Kila njia aliyoipita ikimchukua kuelekea popote, njiani alizungumza peke yake. Watu waliokutana naye walistaajabu na kujua huenda alikuwa na wazimu. Maisha yalimsukasuka na kumchukua hadi ambako hakutarajia kufika.



    Carolina wakati huo alikuwa tayari na kimo cha kuweza kumwona pia kumwagiza japo kusogeza sahani. Kwa kuwa damu ni nzito kuliko maji, Maua alipoona Carolina kawa na kimo cha kutosha pia akili ya kupambanua mambo, hakukauka kwenda kwa Malecha. Carolina alikuwa mwenye furaha kila wakati ambao alikutana na Maua akimwita bibi. Familia ya Malecha ilimkataza Maua kumjuza lolote. Walitaka Carolina akue akimjua Maua kama jirani na mtu baki katika kijiji hicho.



    Kutokana na hali hiyo, Carolina hakufahamu chochote kuhusu uhusiano wake na Maua zaidi ya jirani aliyekuwa akimpenda. Akilini mwake na fikra, Maua alikuwa akimtazama na kumchunguza mjukuu wake vema. Alifanana sana kwa sura na umbile na mama yake. Alimshukuru Mungu.



    Japo Maua alikatazwa kuwa karibu na Carolina, nafsi aliiahidi kutafuta siku ambayo angemchukua Carolina na kwenda naye kwake. Alimtamani awe akimsaidia mambo mbalimbali ya nyumbani kama mjukuu wake. Siku haikuwa imefika na aliingoja ifike kwa hamu.



    Dua azitoazo mtu kwa Mola, tena kwa uaminifu na tumaini, hujibiwa kwa wakati. Hatimaye nafasi ya kumpata Carolina ilipatikana. Maua alimwendea Carolina mapema kabla hajatoka shuleni. Alimsubiri njia panda kwenye mti mkubwa mpaka wakati ule ambao yeye na wanafunzi wenzake waliruhusiwa kuondoka shuleni. Baada tu ya kumwona, Maua alimwita mjukuu wake. Carolina hakusita kuambatana na Maua kwa kuwa naye alimpenda kuliko hata mama aliyemlea. Baada ya kuongozana, walifika nyumbani ambako alimpatia kila aina ya upendeleo wa kula na kunywa. Kila alichokitaja alipatiwa. Siku hiyo alijihisi mwenye uhuru na furaha ambayo hakuwahi kuipata. Maua alikuwa na furaha kuu siku ile, hakuacha kumjuza Carolina pamoja na udogo wake kiumri, kila kitu alimsimulia. Carolina alikuwa haelewi, alidhani alikuwa akipiga porojo za kumfurahisha.



    Familia alikoishi walingoja kwa muda bila kumwona. Walianza kumtafuta lakini hawakumwona. Baada ya kutafakari na kujiuliza kule Carolina alitamani kwenda, waliamua kwenda kwa Maua.



    “Hodi hapa, Maua?” Malecha alibisha hodi nyumbani kwa Maua.



    “Karibu!” aliitikia Maua angali hajamwona mtu abishaye hodi. Muda huo Carolina alikuwa amelala usingizi juu ya mkeka nyuma ya nyumba palipokuwa na mti mzuri wa kivuli. “Karibu sana baba,” Maua alimkaribisha Malecha mara ya pili. Wakati huo alikuwa na wasiwasi kwani alimjua Malecha hakuwa akipenda masihara. Pamoja na maonyo yake ya kila mara, alivunja makubaliano.



    “Nimekaribia! Hivi Carolina yupo huku ama la!” Alihoji Malecha.



    “Ndugu, muungwana huketi ndipo maneno hufuata. Hapa kwako pia baba,” alijibu Maua.



    “Maua, sijaja kwa marumbano. Kwangu pia kuna viti lakini nimeviacha. Nijibu kama huyu yupo hapa au la!” alisisitiza Malecha. Maua alisita kidogo akiwaza.



    “Ukimya wako unanipa mashaka,” Malecha alisema. Alisimama kutoka pale alikuwa ameketi. “Carolina! We Carolina!” Malecha aliita. Hakukuwa na sauti ya kuitikia kutoka pande yoyote.



    “Malecha, wewe ni kijana wangu. Kwani Carolina akiwa kwangu ni kosa?” alihoji Maua.



    “Nilishakueleza, Carolina hapaswi kujua lolote kuhusu wewe. Naona hutaki kuelewa. Niambie yuko wapi ili niondoke naye sasa,” Malecha alifoka.



    “Carolina ni mjukuu wangu wa damu. Anapaswa kunitambua vizuri kama bibi yake. Sikatai aishi kwako, lakini mimi pia ninayo haki ya kuwa naye. Yupo amelala huko nyuma. Naomba hata uimsumbue. Akiamka nitamleta na mzizi wa fitina utaisha,” alieleza Maua.



    “Hujui ulitendalo. Tangu Carolina nilivyomnusuru dhidi ya kifo walichokusudia Wanahamaniko, si wako tena. Huyu ni haki yangu. Usitegemee chochote. Je, nisingemchukua leo ungemwona wapi?” alihoji Malecha. Alipiga hatua kuelekea upande wa nyuma ya nyumba ambako alimkurupua Carolina. Maua aliwahi kumzuia. Malecha alijivuta kwa nguvu lakini bado Maua alikataa katukata. Maua alivyozidisha usumbufu, Malecha alimzaba kibao kilichompeleka chini. Alivyonyanyuka alikuwa kapandwa hasira. Alimvaa Malecha na kumng’angania. Malecha ilimlazimu kumniga shingoni kwa kumbana na mkono. Maua ili kujinasua alimng’ata Malecha mkononi. Tayari Malecha baada ya kuona hayo, alimwachilia Maua. Vurumai zilikuwa kubwa hadi kuwakusanya watu wengi waliokuwa wakipita sehemu hiyo. Bado Malecha alimnyanyua Carolina kama paka na kuondoka akimburuza.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Baada ya Malecha kuondoka na jeraha, hakukubali kubaki bila kuchukua hatua. Alikwenda kwa mjumbe ili kumpa taarifa ya kile kilimkuta. Mjumbe kama kawaida yake, hakuamua mambo kwa fikra yake pekee. Ililazimu kesho yake asubuhi kuitishwe kikao cha baraza kulijadili jambo ambalo Maua alilisababisha. Siku hiyo mashahidi walioshuhudia waliitwa na kusimama mbele ya baraza. Wote walieleza jinsi Maua alivyomshambulia Malecha na kumjeruhi. Ilifika zamu ya kutolewa hukumu ambapo Maua alipaswa kuhukumiwa.



    “Ndugu zangu, kwa mujibu wa sheria za Hamaniko, kosa la Maua linahitaji asamehewe kwa sharti. Endapo atatenda kosa jingine ndani ya siku arobaini, atapaswa kuhukumiwa kwa makosa yote. Atahukumiwa kwa kosa la awali na lile atakalokuwa amelitenda wakati ule,” mjumbe alitaja hukumu. Wanakijiji walinyamaza kimya. Koi na familia yake hawakuwa na furaha kwani kwa kipindi chote hawakupatana na Maua. Kosa la Maua lilimpa wasaa wa kuendelea na maisha yake kama kawaida.



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog