Search This Blog

Friday, July 15, 2022

NDOTO ZA KIPEPEO - 3

 







    Simulizi : Ndoto Za Kipepeo

    Sehemu Ya Tatu (3)



    Muda mchache ulipita akiwa kajiinamia. Alijishika kwenye kidonda na kupata habari njema. Damu ilikuwa imepunguza kasi. Moyo ulipata faraja ingawaje hakujua kama damu ilikoma kwa sababu ya kilindachozi ama ilikuwa imepungua mwilini. Hakuisha kuwaza,“Usiku huu mchanga nitaelekea wapi? Wazazi wangu hawanitaki. Wananihukumu kwa kifo. Wapi nitaenda wakati kila sehemu ni mgeni. Tangu nizaliwe sijawahi kuijua nyumba nyingine zaidi ya nilipotoka,” Carolina alisafiri mbali kimawazo. Hakika hakujua sehemu ya kuelekea, alikuwa mwenyeji wa wa familia moja aliyoipenda na kuitumaini.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    Usiku huo Roy na baba yake walikuwa kwa mjumbe kutoa taarifa kutokana na maneno ambayo Malecha aliyasema. Maneno hayo yalimkosesha furaha Dendego akihisi anaweza kudhurika.



    “Mjumbe, nimefika kwako kwa jambo moja kubwa. Bila shaka umeyasikia yanayoendelea katika kijiji hiki,” Dendego alieleza. Mjumbe alikuwa kalitega sikio kwa makini.



    “Bila shaka Dendego. Taarifa nimezipata tangu alasiri iingie na punde tu nimepata taarifa za mkasa uliotokea kwa Malecha,” alisema mjumbe.



    “Sawa. Kilichotokea kwa Malecha chanzo chake ni huyu kijana wangu. Hivi tumefika hapa kukujulisha kuwa, Malecha amefura kama mbogo. Tulienda kutaka kuyamaliza kwa amani, kilichotokea huko imetupasa kuja mbimbio kwako.



    Malecha aliingia ndani na kulitwaa sime akitaka kutudhuru. Tulipoondoka tu, kwa nyuma tuliona limbuko la moto mkubwa ukitokea kwenye mji wake. Hatuelewi kama kuna usalama huko. Mjumbe hauawi, taarifa hii kaa nayo na uangalie namna. Kijiji hiki kimeingiwa shetani,” Dendego alieleza.

    “Asiyesikia la mkuu huvunjika guu. Malecha aliyataka matatizo mwenyewe. Unakumbuka kipindi kile baraza la kijiji lilipendekeza kichanga cha binti Majaliwa kitupwe mtoni. Malecha kwa tamaa ya mtoto wa kike aliungana na mkewe kumtaka. Kwa kuwa kijiji huwaheshimu wenye ukoko basi wote waliufyata na kumwacha afanye atakavyo. Lakini nilijua ipo siku kijiji kingevurugika. Na ndicho ukionacho sasa,” mjumbe alijieleza. Wakati huo Roy hakufahamu kile walichokuwa wakikizungumza. Alibaki kashikwa na bumbuwazi.



    “Tena hapa moto ndiyo kwanza umeanza kuwaka. Utakiwakia kijiji hiki mpaka adabu itawashika. Carolina atawapepeta kama mchele kwenye ungo. Si wana wala ninyi wazee. Laana hufuata kizazi hadi kizazi, itawafuata,” mjumbe alisisitiza.



    “Sasa tutafanye nini? Hili tatizo ni kubwa hata madhara tunayaona yameanza kutapakaa,” Dendego aliuliza. Alizungumza wakati macho yake yakiangaza upande ambako kundi la watu lilikuwa likikaribia kufika. Kila mmoja alishika.



    “Mjumbe!” Malecha aliita akifuatwa na wanakijiji wengine.



    “Kulikoni Malecha? Upige moyo konde. Jambo hili halihitaji hasira,” mjumbe alimtuliza Malecha.



    “Naomba msamaha wanakijiji wenzangu. Baada ya miaka mingi leo nimefahamu ukweli. Carolina hafai kuwa mtoto. Laana ya kijiji hiki sasa imeanza. Iwezekanaje mtoto mdogo awavuruge wana hadi wazee wao?” alieleza Malecha.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Hewala mwana wa Hamaniko,! Heri umeona mwenyewe! Umeonaeee!” Mjumbe aliitikia.



    “Lazima hadhari ichukuliwe. Auawe binti huyu kabla mguu wake haujaiacha ardhi yetu. Damu yake ikimwagika itakuwa imekisafisha kijiji chetu na tutaishi kwa amani na mshikamano,” mjumbe alipendekeza. Wakati huo vijana wenye umri kama Roy hawakufahamu lolote. Walivyokuwa wakimfahamu Carolina ni tofauti na maelezo yaliyokuwa yakitolewa pale. Walinong’ona lakini hawakupata jawabu.



    “Puliza mbiu tumsake ungali usiku haujakomaa,” mzee mmoja alitoa pendekezo. Mjumbe hakukaidi, aliipuliza parapanda iliyokuwa imechongwa kwa pembe ya mnyama na habari ziliwafikia wanakijiji wote. Wanaume wote walimiminika kwenda kwa mjumbe. Hapakuwepo mwanamke ambaye aliruhusiwa kufika katika kutano hilo.



    “Ndugu zangu, yaliyosemwa leo yametimia. Bila shaka kila mmoja anamfahamu msichana anayeitwa Carolina,” mjumbe alihoji.



    “Ndiyo mjumbe,” Waliitikia wanaume wengi waliokuwa wamekusanyika hapo. Vijana wengi hawakuitikia kwani waliwaza na kuwazua kile ambacho Carolina alikifanya na kuwafanya wakutane.



    “Atafutwe usiku huu popote alipo. Akipatikana aletwe mbele ya baraza atueleze sababu inayomfanya kukichanganya kijiji chetu,” mjumbe aliagiza.



    “Kwa kuwa ni usiku, hamtachelewa kumpata. Hawezi kwenda mbali. Mtafuteni shambani, mtini hata bondeni, awe mfu au hai aje hapa,” mjumbe aliongezea kwenye agizo lake. Kila mmoja alisimama na kuokota kile alihisi kingefaa kuwa mkononi wakati wa msako.



    Wakati ambao wanamsako wa kijiji walijiandaa kumsaka Carolina, yeye aliendelea kuwaza sehemu ya kuelekea. Usiku ulizidi kukomaa. Mbu nao waliendelea kumtafuna kwa furaha. Anga wakati huo lilibadilika na kujaa baridi iliyomiminika na kumfunika. Alijibanza kwenye shina la mgomba akijikinga dhidi ya upepo wa baridi uliokuwa ukimiminika kimyakimya. Macho yake hayakuweza kuona mbali na pale alipokuwa amejisitiri kutokana na wingu kuwa limeufunika mwezi. Maumivu ya kidonda yalikuwa yakiendelea kumsulubu. Hofu ya kuwaogopa wanyamamwitu haikuwa sehemu ya fikra zake. Aliwahofia binadamu hasa baba yake aliyekuwa kakusudia kumkatili maisha kwa kisa asichokifahamu. Aliwaza jinsi Rabani alimnusuru dhidi ya kifo kilichokusudiwa kumpata kwa ncha ya upanga. Alibaki mkiwa kulikabili baridi.



    Wanamsako walitawanyika kumsaka Carolina. Roy aliwaza jinsi Carolina angeadhibiwa kwa jambo asilolifahamu. Japo hakuwa na uhakika juu ya uhusiano wa Carolina na Koi, kwa fikra alijihoji mengi. “Iweje Carolina peke yake ahukumiwe. Hapana, sitakubali jambo hili litokee. Kwa nini Koi hajaulizwa hata swali kuhusu uhusika wake kwa Carolina? Mimi naujua ukweli na nitasema nilichokiona ili naye aweze kupata haki yake. Lakini…., inawezekana wanamlinda. Ngoja Carolina apatikane, nina hakika kila mmoja ataeleza ukweli wake. Carolina! Unazidi kuyaweka maisha yangu mashakani.” Roy aliwaza wakati akiwa shambani wakimtafuta Carolina.

    Kila kichaka kilichokuwa katika mashamba hawakukiacha bila kukipa misukosuko kwa kukimulika kwa kurunzi na kukivuruga kwa marungu. Chini na hata juu ya miti kote waliangaza lakini hawakubahatika kumwona. Uwanda wote uliokuwa na mashamba ulitapakaa mianga ya kurunzi na kuyafanya mashamba kuwa kama mji uliokuwa ukionekana kwa mbali.

    Angali katika msako huo, Koi aliwaza tofauti na wenzake. “Leo nitaumbuka. Anayeujua ukweli wa hili ni Roy na Carolina. Sasa akipatikana nitajiteteaje? Atasema ukweli, atasema tena nitazidiwa kwa idadi ya ushahidi. Roy na Carolina ni kura mbili dhidi yangu. Haiwezekani jambo hili litokee. Lazima auawe angali bado kulifikia baraza,” Koi aliwaza na kukata shauri.



    Baada ya kuvimulika na kupekua vichaka vya mashamba yote, walianza kuteremka kuelekea bondeni. Sehemu ile ilikuwa yenye giza kupita kiasi. Hawakutumaini kumpata Carolina katika eneo hilo lililoogopesha wakati ule wa usiku. Kila mmoja alijitahidi kuikaza miguu yake kuelekea bondeni. Mianga ya kurunzi ilionekana kwa mbali ikiwa bado kilimani. Carolina aliyekuwa chini ndani ya bonde lile aligutuka baada ya kuona mianga iliyokuwa ikimulika na kuangaza kama nyota. Ilikuwa ikichezacheza na wakati ilielekea upandeupande ikimulika. Moyo ulimdunda na kujua alikuwa katika kipindi kingine kigumu cha kuutetea uhai wake.



    Carolina aliingiwa na wasiwasi. Maumivu ya mwili tena hakuyasikia. Alinyanyuka ili akimbie, nafsi yake iliingiwa simanzi. Shetani alimpiga kofi kisha moyo wake ulimwongoza kukitekeleza kitendo cha ajabu. “Siwezi kufa kwa upanga. Lazima nife kwa hiari. Lazima,” Carolina aliuambia moyo wakati akielekea kwenye mti wa maua aliokuwa akiupenda kupumzika wakati wa jua. Alisimama kwenye kisiki akiyatupa macho kuitazama mianga ya kurunzi iliyokuwa inamsaka. Alijua watu wale walimtafuta kwa ubaya kwani haikuwa rahisi wamtafute kwa wema. Macho yake yalimhakikishia kuwa walikuwa mbali kuweza kumpata.



    Alifanya toba kabla ya kifo chake, “We mfalme wa wafalme, siku zangu unazijua idadi yake. Kama kipepeo aliyetamani kuishi katika ndoto zake, nayakabidhi maisha yangu kwako katika mti huu wa ahadi. Nitwae utakako kwa wema, nafsi yangu haitavumilia kufa kwa upanga,” Carolina alitubu.



    Alikinyanyua kiganja kuyafuta machozi. Alianza kuukwea mti wa maua na kuambaa kwenye tawi kubwa. Alikichana tena kipande cha kanga yake alichokuwa amebakiza na kukiunga kisha kupata kamba ndefu baada ya kukiviringa. Mikono yake ilimwongoza kukifunga kipande cha kanga kwenye tawi.



    Kitanzi alikitengeneza na kukitia shingoni kama tai. Aliivuta pumzi na kuishusha wakati akihesabu kimoyomoyo, mara tatu. Alijirusha akaelea na kuligonga tawi lililokuwa karibu kwa miguu yake. Tawi lilitikisika, bado alielea kama tufe akaenda kila upande. Maumivu ya kidonda cha shingo yalimkolea na kumfanya kunguruma huku akiirusha mikono yake kutaka kukwea ili aishike kamba kujiokoa.



    Wakati Carolina anaukabidhi uhai kwenye mti aliouhusudu, Saraganda na mama yake walikuwa katika kipindi kigumu cha simanzi. Nafsi zao ziliwahukumu. Kila mmoja kwa nafasi yake alijutia uamuzi wake. Saraganda alikuwa ameupata ukweli kumhusu Carolina. Bado alionyesha kutoyaamini maneno ya mzazi wake.



    “Mama, hata kama Carolina si dada yangu wa damu, inafaa asamehewe. Inafaa apewe nafasi ya kutimiza ndoto zake kama watoto wengine. Ni kweli kasababisha aibu lakini alipaswa kusikilizwa ili kuujua ukweli. Mimi nilimwambia baba, si kwa nia mbaya. Nilitaka aketi na kumwonya dada dhidi ya tabia mbaya na si kumfukuza na kutaka kumdhuru,” Saraganda aliongea kwa unyonge.



    “Hapana mwanangu. Wewe ndiye chanzo cha haya. Usingesema ungepungukiwa nini? Tena nafsi yangu imekushiba. Unawajua watu wa kijiji hiki walivyo, kama baba yako, hawaelewi la mwalimu wala la kasisi. Wakimpata mwanangu watamuua nawe damu yake itakulilia,” aliongea mama Saraganda kwa uchungu. Macho yake yalikuwa yakibubujikwa chozi. Aliyafuta machozi kwa kanga na kunyanyuka kuuelekea mlango. Alifika na kusimama akiangaza macho yake katikati ya lile giza kuelekea kule Carolina alipita wakati akikimbia.



    “Nilimnyonyesha na kumlea kwa upendo. Mwanangu nilimpenda leo mmemtia mashakani. Mungu mlinde, mwepushe na mabaya yote. Kosa langu kumlea pasipo kumjulisha ukweli au nini? Asihukumiwe kwa uyatima wake na upofu wa tawala ya kijiji hiki,” mama Saraganda aliilaumu nafsi yake. Muda huo kwa mbali alisikia kelele zikitokea bondeni na kumfanya ajawe wasiwasi. Alijua Carolina akitiwa mikononi, adhabu yake ilikuwa kifo.



    Dua za mama Saraganda zilikuwa za kuku, kumpata kuku haikuwezekana. Msako wa kumtafuta Carolina ulifika eneo la miembe iliyolizunguka bonde lenye bustani kila upande.



    Upepo mwembamba uliojaa baridi uliendelea kumiminika pasipo kuzalisha kelele ya aina yoyote. Kila mmoja alijitahidi kumulika na kuangaza macho ili kumpata Carolina. Walijua sehemu hiyo ilikuwa ya mwisho kwa kumtafuta kwani hapakuwa na sehemu nyingine ambayo angeweza kwenda. Roy bado aliendelea kuwaza, hamu yake ilikuwa ni kumpata Carolina ili aweze kueleza ukweli.



    Wakati akiwaza alikuwa akiambaa kuelekea sehemu ya bustani yao iliyopakana na bustani ya Carolina. Aliuruka mfereji wa maji uliotokea bwawani kwao na kutua kwenye bustani ya Carolina. Mkono aliunyanyua kumulika umbali kidogo na pale. Macho yalikutana moja kwa moja na galoni jeupe lililokuwa na kitu kilichomshangaza. Kwa haraka alilisogelea. Aliyatumbua macho kutazama, aliona maji machafu yenye mchanganyiko wa damu yakiwa kama sharubati ya zambarau. Alibaki kimya kwa sekunde chache kabla hajalizungusha kurunzi kila upande. Kwa pembeni kidogo alikiona kipande cha kanga kikiwa kimelowa damu. Alijiandaa kwa makubwa!



    Hatimaye Roy aliinyanyua miguu kimyakimya kusonga mbele. Mwanga wa kurunzi ulitua kwenye mti mkubwa wa maua. Mtikisiko wa matawi ulimgutusha. Alienda mbio na kuangaza macho juu ya mti uliokuwa ukitikisika.



    “Anajiua! Uwiiiii!” Roy alitangaza. Sauti ya uoga iliyochangamana na uchungu ilipokewa na kila mmoja. Wote waliokuwa wakimsaka Carolina walipiga yowe wakati wakikimbia kuelekea alipokuwa. Roy alimpokonya Malecha sime. Alikwea mtini na kuikata kanga iliyokuwa imemshikilia Carolina. Alitaka kumwokoa!



    Baada ya kuikata kanga, mwili wa Carolina ulishuka chini kwa kasi kubwa. Alitua mikononi mwa wanamsako waliomdaka na kumlaza chini. Roy alishuka ili kujua kama alikuwa hai. Alilitega sikio kifuani kuyasikiliza mapigo ya moyo. Alikuwa bado hai! Kidonda kilikuwa kikitoa damu nyingi. Roy aliivua fulana laini na kuizungusha sehemu yenye kidonda kuizuia damu. Aliwaomba waliokuwa wamemzunguka kumpisha ili apate hewa safi ya kuvuta. Alimkandamiza kifuani mara tatu na kuanza kumpepea. Hakuwa ameyafumbua macho bali kifua kilinyanyuka juu na kushuka. Koi alikuwa akiomba kimoyomoyo Carolina atwaliwe na umauti. Kila alipomtazama Roy akihangaika kumnusuru Carolina, hasira ilimjaa.

    Ilimchukua dakika kumi Carolina hadi kuanza kuyachezesha macho yake. Roy hakufa moyo, alimnyanyua na kumkalisha vizuri. Hatimaye pumzi zilimrudia akaanza kupumua japo ilikuwa kwa shida.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Carolina alikimbia mbio za sakafuni ambazo mwishowe ilikuwa ukingoni. Wanamsako walimtia mkononi na tayari aliwasilishwa nyumbani kwa mjumbe. Ilikuwa muhimu kumfikisha kwa mjumbe akiwa mzima hata mfu, iliagizwa.

    “Mfungeni mnyororo miguuni na mikononi asitoroke,” mjumbe ilitoa amri. Koi aliuchukua mnyororo uliokuwa ikitumika kumfunga mbwa wa mjumbe. Aliuzungusha miguuni na mikononi mwa Carolina. Damu ilikuwa imetapakaa na kutanda kwenye gauni lake. Vumbi nalo liliupamba mwili ukapambika. Macho yake ya gololi yalilegea na kuwa kama ya mtu aliyelewa hashishi ya kuuchosha mwili. Alijaribu kuyafumbua macho kuwatazama watu waliokuwa wakimtesa, aliwaona kwa mbali Nafsi ilikubaliana na chochote ambacho wanakijiji walikusudia kukifanya dhidi yake.



    Roy alishikwa na fadhaa ingali nafsi yake iliumia sana. Kila alipokutanisha macho na Carolina alihisi kuhitaji msaada. Ilimlazimu kusogea hadi pale Carolina alifungwa na kuyaondoa majani yaliyokuwa yamezishika nywele. Alikuwa na nywele alizosuka zikishuka kama matuta kuanzia usoni kwenda kiogoni, ziliitwa twende kilioni. Aliutuma mkono kuzifuta damu na machozi yaliyokuwa yakimbubujika. Umati wa watu uliokuwa pale ulimkemea kwa nguvu. Roy alirudi nyuma, kiganja kilichokuwa na damu alikifuta kwa kaptula aliyokuwa ameivaa. Macho yalikuwa yakimtazama Carolina mfululizo.



    “Mjumbe, asaidiwe mtu huyu. Maumivu anayoyapata yatamtoa uhai,” Roy alitoa pendekezo wakati mjumbe na Dendego walinong’ona.



    “Asaidiwe vipi?” Mjumbe aliuliza.



    “Kidonda chake. Yanahitajika maji ya vuguvugu, ugaka na chumvi. Roy alishauri. Wakati huo alikuwa akiuelekea mshubiri uliokuwa pembeni ya nyumba ya mjumbe ambao wao waliuita ugaka, alichuma jani moja.



    “Hapana. Kwa nini alitaka kujiua?” Koi alizungumza kumpinga Roy. Wakati yakiendelea mabishano hayo, Malecha alikuwa akimtazama Carolina kwa aibu. Kila alipomtazama nafsi ilimuuma. Damu iliyokuwa ikimtoka kwenye jeraha alilolisababisha iliisuta nafsi. Aliilaani nafsi kisha alitoweka na kwenda akiepa kuyaona mateso ambayo Carolina alikuwa akiyapitia. Mjumbe aliitafakari hoja ya Roy kwa makini. Huruma ilimvaa kisha kutaka Carolina kupewa msaada.



    “Mama Jumbe! Mhudumie binti kwa maji ya chumvi na ugaka,” mjumbe alimwagiza mkewe. Wakati mama Jumbe akikukurika kuchemsha maji, mjumbe alikuwa akitafakari kanuni za kijiji chao.



    “Wazee wenzangu, utawala wa kijiji hufanya maamuzi asubuhi na kuyatekeleza usiku. Hivyo, binti akihudumiwa atafungiwa kwenye banda alimokuwa akiishi mbwa wangu aliyeliwa na fisi hadi kesho asubuhi. Kesho asubuhi tutakusanyika na kumfungua tumsikilize kabla ya hukumu.” Mjumbe alitoa maelekezo ambayo wanakijiji waliyaafiki kisha kuanza kuondoka. Roy na baba yake hawakuondoka maramoja. Walibaki kusubiri maji kisha Roy alijitoa kumhudumia Carolina kwa uangalifu. Wakati anahudumiwa, Carolina alimtazama Roy usoni na kuamini kuwa alikuwa mtu mwema.



    “Caro, usiogope, Mungu atakulinda. Nakupenda,” Roy alimnong’oneza Carolina. Baada ya kukisafisha kidonda, kiliacha kutoa damu. Roy aliamua kuichukua kata na kuteka maji mtungini, alimnywesha ingali mikono na miguu ikiwa imetiwa mnyororo.



    “Mfungueni mikono ale chakula,” mjumbe alitoa agizo. Roy iliipokea sahani ya chakula kutoka kwa mama Jumbe. Alingojea Carolina kufunguliwa mnyororo ndipo alipomnawisha mikono na kumtengea chakula. Alikishika chakula na kukitupia mdomoni kwa shida. Hali hiyo ilimpasa Roy kumlisha japo alifanya hivyo kwa wasiwasi wa kuyaogopa macho ya watu.



    Wakati Mjumbe na Dendego wakiteta, Koi alinyanyuka na kuwapa kisogo. Hakupendezwa kuona Carolina anapewa huduma nzuri kwa lengo la kumponyesha. Alimhofu Carolina akiwa na siha njema angesema kila kitu jambo ambalo lingemfanya atiwe hatiani na baraza.



    Kabla ya wanakijiji kutawanyika, waliteuliwa walinzi wawili kumlinda Carolina. Walikuwa vijana wenye umri wa kati usiovuka miaka ishirini. Walimtazama Carolina kwa huruma lakini hawakuthubutu kuivunja miiko ya kijiji chao. Ni wazi kuwa, kwa kipindi chote walichokuwa wakiishi kijijini hapo walijua kuwa Carolina alikuwa mtoto halali wa Malecha. Japo waliyasikia maneno mengi ya kuchukiza kumhusu, bado nafsi zao zilikataa kuusadiki uvumi huo.



    Macho ya Carolina muda yaligeuka chemchemi zilizotiririsha machozi yaliyomtoka na kutua chini ya ardhi yenye kiu. Roy alijitahidi kumtia moyo ili kumfanya ale kwa ajili ya kupata nguvu zilizokuwa zikimpotea. Mjumbe aliyekuwa akizungumza na Dendego aliwatazama na kujua kuwa tayari Carolina alikuwa amemaliza kuhudumiwa.



    “Mfungieni bandani usiku unazidi kukomaa,” mjumbe aliwaagiza walinzi. Walimshika na kumnyanyua. Kila mmoja aliushika mkono wakimkokota hadi kwenye banda lililokuwa pembeni kidogo na zizi la mbuzi. Waliufungua mlango na kumsukumiza ndani. Alianguka na kuketi sakafuni. Kilio alizidi kukiangua, maumivu yalimwelemea. Nafsi ya Roy ilizidi kuumia kwa kitendo alichokuwa akifanyiwa Carolina. Japo hakuwa na uwezo wa kutengua uamuzi wa wazee wake, alitamani kumnusuru.



    Mlinzi ammoja alikazana kulifunga komeo la mlango wa banda. Mwingine alikuwa akimulika na kuufanya mwanga mkali uyaumize macho ya Carolina. Carolina alijikinga kwa mikono kuukwepa mwanga usiokuwa kipimo.



    “Usiku umeingia, twende tuwapishe waulinde usiku,” Dendego alimtaka Roy kuondoka eneo hilo na kwenda nyumbani kupumzika. Roy hakujibu. Bado mashaka kuwa, pasipoyeye Carolina angepata mateso makali.



    “Kwa heri mjumbe,” Roy aliaga.



    “Mjumbe, tunaomba huyo kijana aende kwa wake zetu atuletee chakula. Njaa inauma maana usiku huu hatujapata chakula,” mlinzi mmoja alitoa ombi kwa mjumbe. Mjumbe alikaa kimya kidogo akitafakari. Akilini alifahamu kuwa, chakula pale kwake kwa jioni ile kilikuwa kimemalizika.



    “Sawa. Roy lifanyie kazi jambo hili,” mjumbe alitoa agizo kisha kuingia ndani na kuufunga mlango tayari kupumzika.

    Akiwa ameongozana na mtoto wake, Dendego huruma ilikuwa imemwingia baada ya kumtazama Carolina vile aliteseka. Fikrani aliwaza kumnusuru dhidi ya mateso aliyokuwa akiyapata.



    “Roy mwanangu, damu ya binti huyu inakulilia. Niwajuavyo wazee wa kijiji hiki, mwanamke hana lake mbele yao. Watamhukumu kwa hila,” Dendego alimweleza Roy wangali njiani.



    “Una maana gani baba?”



    “Fanya maarifa ili damu isimwagike mbele yako. Laana itakuandama hadi uzee wako.”



    “Baba, nitafanyaje wakati mambo tayari yameharibika? Yupo mikononi mwa walinzi wa kijiji na kesho wanamfikisha mbele ya baraza.”



    “Turufu uliyoipata cheza nayo kwa uangalifu. Walinzi!”



    “Ndiyo. Walinzi ni kikwazo. Sijui hata nitafanyaje?”



    “Unafahamu mwenye kiu na njaa hupumbazwa na nini?” Dendego alimtega mwanae kwa fumbo.



    “Kwa maji na chakula,” Roy alijibu. Dendego alicheka kisha kukohoa kidogo. Alifurahishwa na jibu alilolitoa Roy.



    “Sisi tuliotangulia kuliona jua tunafahamu. Mwenye njaa na kiu hupumbazwa kwa ndumba. Umeagizwa chakula, ndiyo turufu,” Dendego alimnong’oneza mwanaye kisha walitembea hadi nyumbani kwao. Roy alijua baba yake alimuunga mkono kwa kila hatua ya kumnusuru Carolina. Aliondoka akiwa na wazo hilo kichwani.



    Walipoondoka, usiku ulizidi kukomaa. Kimya kililikumbatia anga la kijiji cha Hamaniko kwa ukiwa. Koi alijaribu kulala lakini usingizi ulimruka. Kichwa kilimchemka na kuiona siku iliyokuwa usoni ikifika kwa haraka. Alijilaza kitandani ambapo alihisi kama palijaa misumari. Usingizi hakuupata na kumfanya anyanyuke kuketi. Alilala tena kisha aligeukageuka. Utulivu ulimpotea kama kuku mtetea. Macho yake mekundu yaliakisiwa na mwanga hafifu wa kibatari kilichokuwa kikitema moshi mweusi. Mara mguu juu, wakati mguu aliukunja kama siko. Ni kuweweseka tu wakati huo. Chali alijilaza na wingu zito la hoja lilimvaa.



    Hatimaye mawazo yalimvaa, “Aibu hii nitaificha wapi? Mke wangu, wanangu, wanakijiji wote, watanitazamaje? Carolina akieleza udhalimu wangu nitaaibika. Lakini hajanikubali, na sijamfanyia chochote. Je, bado ninalo kosa mbele ya baraza? Hapana. Lakini ni aibu. Mimi kumtaka mwanamwali sawa na binti yangu, nitahukumiwa. Ndiyo, nitahukumiwa. Roy anaonekana kuwa karibu na kijana mwenzake. Yawezekana yeye akasamehewa. Sasa nitafanyeje? Nikubali aibu au nichukue hatua. Nimechelewa! Carolina nikimuua, ushahidi nao utakufa. Nitasimama kumpinga na kumshinda Roy kwa nguvu. Au, Roy ndiyo adui yangu nianze naye sababu ndiye shuhuda aliyeniona kwa macho niki….! Hapana! Mtendwa siku zote huufahamu ukweli. Carolina kifo kinamhusu,” Koi aliwaza na kuwazua.



    Wima! Alinyanyuka na kuketi kitandani tena. Mkono mmoja aliutupa kidevuni akitafakari na kukitingisha kichwa. Macho yake kodokodo aliangaza kila upande. Mkono mmoja aliushusha na kuishika shuka. Taratibu aliivuta na kuuchungulia uso wa mkewe. “Ameshalala. Ndiyo, amelala hawezi kujua chochote sasa. Tena kwa kazi za kutwa amechoka sana. Hawezi kuamka,” Koi aliteta na moyo wake. Alijua mkewe alikuwa kapitiwa na uingizi mzito.



    Mguu juu, mguu kanyaga, kwa taratibu aliutua sakafuni. Meno aliyabananisha yakashikamana kama kashata. Mguu wa pili ulimfuata pacha wake akitembea. Kama duma mawindoni, ulitua kwenye sakafu. Vumbi liliuogopa unyayo, liliruka kuukwepa. Alisimama tena akamtazama mkewe usoni.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Amelala. Ee amelala,” nafsi ilimlisha ushahidi aliouamini. Jicho alilizungusha chumbani kama kinyonga. Lilitua kwenye mning’inio wa nguo zake kwenye kamba. “Koti jeusi. Nataka kuchukua hili koti,” Moyo ulichagua. Mkono ulienda mbio na kulitia koti mkononi. “Tayari naweza kwenda,” Koi alipiga hatua kuondoka. Alipiga hatua hadi kuufikia mlango uliomtoa chumbani. Alisimama na kulitega sikio lililojazwa na muungurumo wa mkewe chumbani. Hapo alijipa tena ushindi, “Hasaa, kalala fofofo….” Kushoto kisha kulia, koti alilipekua wakati mikono ikizama ndani kila mmoja na njia yake. Mikono juu aliiweka na kulitumbukiza kichwani. Aliliteremsha na kuufunga mkanda uliomkaa kiunoni sawia. Alitangaza nafsisi, “Hapa mpaka kieleweke,” Moyo ulikula kiapo cha kuupata ushahidi.



    Wakati huo taswira ya Carolina ilimjaa kichwani. Hakumwazia mema bali aliwaza kumteketeza. Kikao cha baraza kilimjaa kichwani na kuona vile alifedheheka. “Hapana! Muda huu sitauchezea,” Koi alizidi kula kiapo. Miguu yake pekupeku kama bata mzinga ilipiga hatua na kugonga mhuri sakafuni akielekea kwenye kona ya sebule yake. Mkono wa kushoto ulilizoa jambia refu lililokuwa ndani ya kilindo. Aliushika mpini na kuuvuta likachomoka kidogo kisha alilirudishia. Mkono wa kuume ulilitwaa na kulichimbia kiunoni kisha kulifunika kwa koti refu.



    Tayari vita ilikuwa ikielekea kuanza. Kiapo cha kuua kilimzunguka na kumpa mamlaka. Alibandika na kubandua miguu yake na kuushika mlango kwa kuupapasa. Aliusukuma kulitoa komeo polepole. Mlango ulikubali kufunguka, mwaaa! Upepo kutoka nje ulikipiga vikumbo kichwa chake wakati akitoka nje. Alitoka, macho yalikagua eneo lote lakini hakuona mtu. Alitokomea gizani kwenye shamba lililokuwa jirani na njia ielekeayo kwa mjumbe. Giza lilimmeza na kuiakisi rangi nyeusi ya koti lake. Alikusudia kufuta kosa kwa kiapo cha kutenda kosa jingine.



    Wakati Koi anahangaika kutaka kwenda kumdhuru Carolina, Roy alitoka bafuni kuoga. Alirudi ndani na kumkuta baba yake.

    “Baba, nipo tayari. Sasa nafanyaje?” Roy alimhoji baba yake. Dendego alikuwa kakiatamia kitanda. Aligeuka taratibu kuelekea alikokuwa kasimama mwanae.



    “Nenda kakilete chakula tufanye maarifa,” alizungumza wakati koo lake likizongwa na kohozi. Mishipa ya shingo aliikaza wakati kikohozi kikipasua kifua chake. Mkwaruzo kwenye kifua ulimsababishia maumivu makali. Alikinyanyua kichwa na kukielekeza kwenye sakafu yenye vumbi. Mdomo aliufungua kulitema kohozi twa! Taratibu alirudisha kichwa kwenye kitanda kuendelea kupumzika.



    Kushoto kulia, kushoto kulia miguu ya Roy ilipishana. Kurunzi mkononi alimulika nalo ili kuona ukurasa mpya ambapo miguu yake ingekanyaga. Koi aliyekuwa kajibanza shambani aliuona mwanga wa kurunzi na kuhofu ungemfikia. Kama nguchiro alikivamia kichaka kisha alichutama. Macho aliyakodoa kutazama sehemu mwanga ule mkali ulitokea. Taratibu ulianza kumpotea machoni, alinyanyuka na kutafakari.



    “Huyo nani? Anaenda wapi usiku huu? Inaonesha bado ni mapema sana. Pengine nirudi kwanza ningoje usiku ukomae ndipo niifanye kazi yangu kwa uhakika,” Nafsi iliushauri mwili wake. Roy hakuwa na habari nyingine wakati ule. Aliukaza mguu wake ili kukitwaa chakula alichokuwa ameagizwa. Ghafla miguu yake aliitia breki. Mwanga wa kurunzi ulitua kwenye mkono wake wa kushoto. Konyekonye! Saa yake ilimkonyeza na kumjuza kuwa ilikuwa saa tano usiku.



    Alitembea wanguwangu hadi kwenye familia walipotoka walinzi wale. Mkono wa kulia aliunyanyua akiwa kasimama mlangoni. Vidole vyake alivikunja na kuugonga mlango wa bati ukapiga kelele kwa-kwa-kwa!



    “Hodi wenyewe,” alibisha hodi. Alisogea pembeni kidogo. Lakini bado kimya kilitawala, hakuna aliyemjibu. Mguu wake aliusogeza tena hadi mlangoni. Aligonga tena safari hii kwa nguvu zaidi. “Hodi wenyewe!” Alibisha hodi. Alijivuta tena pembeni kusikiliza kama kuna mtu alisikia.



    “Karibu! Nani?” alikaribishwa. Sauti ilitokea ndani ya chumba cha nyumba ile. Ilikuwa sauti ya mwanamke ambayo Roy alitarajia kuisikia.



    “Mimi Roy. Nimeagizwa chakula na walinzi tafadhali,” Roy alijieleza wakati macho akiyaangaza kila upande. Aliyarudisha haraka hadi kwenye mlango uliokuwa ukifunguliwa.



    “Karibu. Pita ndani,” Mwanamke wa makamo alimkaribisha Roy. Alijifunga kanga kiunoni na nyingine kujitanda mabegani. Roy alimtazama na kujua ndiye aliyestahili kupata taarifa hiyo.



    “Hapa panatosha. Nifungashie chakula nikiwahishe maana watakuwa wamenisubiri kwa muda mrefu,” Roy alizungumza akielekea kuketi kwenye jiwe lililokuwa pembeni ya mlango wa nyumba ile. Mwanamke aliingia ndani. Kelele ya vyombo jikoni ilisikika masikioni kwa Roy kisha bawaba za mlango zilisikika, nywiiii! Alinyanyuka na kulipokea sufuria la chakula.



    “Asante mimi naenda,” alisema Roy wakati akindoka.



    “Sawa, asante na wewe,” mwanamke huyo aliingia ndani na kuufunga mlango. Roy alitembea harakaharaka hadi nyumbani. Mguu wake wa kulia aliutuma kuusukuma mlango ambao ulifunguka naye kuingia. Aliurudishia!



    “Mzee tayari,” alimjuza baba yake akiwa kasimama na sufuria mikononi.



    “Nakuja,” Dendego alinyanyuka kitandani kwa shida. Kitanda kilichokuwa kimemlea kililia wakati akikishuka. Aliupapasa mkongojo na kuushika akitaka kukiachia kitanda. “Yalah! A-a-a-ah! Uzee sasa umekolea,” Dendego alisema na moyo wake. Alipiga hatua mbili kisha kusimama.



    “Naomba nipatie kurunzi,” aliomba. Roy aliunyosha mkono na kumshikisha baba yake. Mzee aliinama uvunguni na kulivuta sanduku dogo lililokuwa limefunikwa na vumbi. Alilishika na kulipuliza kwa mdomo, fyuuuuuuu! Vumbi jepesi liliruka.



    Aliuagiza mkoo kulifungua na kutoa kifuko kidogo cha nailoni. Alilifunga na kulirudisha lilimokuwa awali. “Sogeza chakula hapa,” Dendego alinong’ona. Roy alimsogezea sufuria la chakula. Aliufunua mfuniko wa sufuria na kukiacha wazi. Dendego alikitoboa kifuko kwa mti mwembamba wa chelewa. Alinyunyiza ungaunga ambao ulikuwa ndani ya nailoni kisha kulifunika sufuria na kulitikisa ili kupata kuchangamana vizuri.

    “Tayari wapelekee,” Dendego alisema akiwa anakiviringa kinailoni kile kwenye karatasi ya gazeti. “Nimemaliza. Usionje chakula hicho hata punje,” Dendego alimuonya mwanaye.



    “Lakini baba, baada ya hapo itakuwaje?”



    “Wakila na kunywa, watalala usingizi mzito.”



    “Halafu nikimtorosha nitampeleka wapi? Halafu, wakigundua itakuwaje?”



    “Askari thabiti hana msamiati wa kushindwa. Kushindwa huja kama chafya. Utashinda. Ukimtoa pale msindikize hadi msitu wa Geza kisha urudi hapa haraka,” Dendego alimpa maelekezo Roy.



    “Sasa huko msituni ataishi na nani?”



    “Ukimfikisha mwambie atembee kuuvuka msitu wa Geza hadi aupate mto. Akiufikia mto itamlazimu auvuke hadi ng’ambo ya pili.”



    “Mto unaitwaje baba?”



    “Mto ule baada yam situ wa Geza ni mmoja tu, haina haja ya jina,” Dendego alijibu kwa haraka.



    “Baada ya kuuvuka mto atatembea kwenye msitu mdogo unaoitwa kabla hajakipata kijiji kinachoitwa Tuamoyo.



    Akikifikia kijiji hicho aulize kwa Bibi Chausiku au kwa Maua,” Dendego alieleza na alitia kituo. Roy alijawa na maswali mengi kichwani. Majina yalimkanganya.



    “Bibi Chausiku au Maua, ndiye nani?”



    “Huyo ni bibi yake Carolina. Alifukuzwa miaka mingi kutoka katika kijiji hiki. Nilipata taarifa kuwa yupo Tuamoyo. Huyo ndiye atampatia maelezo ya kumsaidia.” alijibu Dendego. Roy hakutaka kuuliza tena. Alikiweka chakula chini kisha kutia mkono ndani ya mkoba wa daftari. Alilitoa daftari na kuchana karatasi. Aliandika majina yote na maelekezo aliyoambiwa na baba yake ili asiweze kusahau.



    “Mzee nimekuelewa,” alijibu Roy.

    Giza liliendelea kukimeza kijiji cha Hamaniko. Mjumbe na wanamsako walikuwa tayari wameshaifunga milango ya nyumba zao na kulala fofofo. Pamoja na kulala, nafsi zao zilijaa shauku ya kutaka kuujua ukweli wa yaliyokuwa yakiendelea kijijini pale. Koi hakuwa na nia tena ya kukilalia kitanda. Fikrani aliwaza kufanya jambo lililokuwa limemkaa tangu mapema. Muda huo alikuwa sebuleni kwake. Alikuwa ameketi kwenye kigoda kuungoja usiku kukomaa. Alipokuwa ameketi, alibembea kushoto na kulia. Wakati mwingine aliegema kama tawi la mti lililovunjika baada ya upepo mkali. Alikuwa katika tafakari nzito na lepe la usungizi.



    Alijaribu kushindana na asili aliyoumbwa nayo, hatimaye usingizi uliyashinda macho yake. Alilala usingizi akiwa ameketi. Usingizi haukumstahi wala kumwogopa, ulimteka na kuzitia fikra zake kifungoni. Aliendelea kubembea kama embe mtini.



    Wakati huo, Roy aliipachika kurunzi yake karibu na usukani wa baiskeli. Alikuwa tayari kutekeleza alichokuwa amelenga kukifanya. Baba yake alimtia nguvu na moyo wa kuweza kumnusuru Carolina. Kurunzi ilishika na kunasa vizuri kisha aliiwasha ikaimulika njia na kuing’arisha. Miguu yake ilizikanyaga pedeli za baiskeli hadi kwenye njia panda iliyokuwa ikielekea msituni. Alipokifikia kichaka kidogo alitia breki kwa madaluga. Tairi la nyuma ya baiskeli lilikubali kusimama baada ya kuwa limejivuta kwa umbali na kuchimba mfereji mwembamba. Aliishuka baiskeli yake. Alilifungua sufuria la chakula wakati ambao macho pia yaliangaza kila upande kukagua kama kulikuwa na mtu wa kumtilia mashaka. Tena na tena aliyazungusha macho kwa makini, hakuona mtu. Aliipachika baiskeli yake begani. Aliunyanyua mguu wa kwanza ukakanyaga juu ya tuta. Mguu wa pili ulifuata akirukaruka hadi kufika kwenye kichaka kilichokuwa pembeni ya njia ile uchochoro. Aliisokomeza baiskeli katikati ya kichaka kilichokuwa kimestawi vizuri. Baada ya kumaliza alirukaruka tena kuyapita matuta kuelekea kwenye sufuria la chakula, alilifikia na kulitia mikononi. Alitembea kuelekea mahali ilipo nyumba ya mjumbe. Wakati huo walinzi walikuwa wanapiga miayo na kujinyoosha. Matumbo yaliwasokota kwa sababu ya njaa. Walichoka kuikagua njia ambayo Roy alitarajiwa kuipita ili kuwafikishia chakula.



    Hatimaye mwanga wa kurunzi uliwagutusha. Matumaini yaliwajaa baada ya kumwona Roy. Mate ya hamu ya chakula kilichotoa harufu nzuri ya wali yaliwajaa mdomoni. Roy alikuwa tayari amewafikia walipokuwa wameketi.



    “Mbona umechelewa sana?” Alihoji mlinzi mmoja kwa ukali. Sauti yake ilijaa hasira. Alilikwapua sufuria kutoka mikononi mwa Roy na kulifunua. Harufu nzuri ya vunana la mchele lilizipiga pua. Hamu ya kula iliongezeka. Waliliweka sufuria chini kisha walishindana kwenda kwenye mtungi wa maji uliokuwa pembeni karibu na mti mkubwa. Waliyamimina maji kwenye karai na kuiosha mikono tayari kwa chakula. Honyohonyo walikihonyoa chakula kutoka sufuriani na kukitupia mdomoni. Ikawa mkono mdomoni kisha mkono kwenye sufuria. Kila mmoja alitupia mawe pangoni mwake. Kwa kuwa tumbo hana likizo, hakukinai kukipokea chakula. Walikuwa wameipata tiba ya njaa iliyopindukia.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Chakula kitamu sana,” alisema mlinzi mmoja kwa kuhangaika. Domo lake lilikuwa limejaa chakula. Roy aliwasogezea maji ya kunywa yaliyokuwa yametiwa kwenye kibuyu. Baada ya kuwapatia na kuona jinsi walishindana kukila chakula, alisogea pembeni. Aliketi juu ya jiwe kubwa akiwatazama kwa siri wasiweze kuona alivyokuwa akiwashangaa. Nafsi yake ilikuwa ikiwaza jinsi mambo yangekuwa. Hatimaye kuwaza kukamfuata, “Wamekula. Wamekula, tayari. Lakini je, wasipolala fofofo itakuwaje? Na kama watajua hila iliyofanyika mambo yatakuwaje? Hapana. Sijui kama itawezekana,” Roy alianza kuingiwa wasiwasi. Alikiegesha kidevu chake juu ya goti wakati utawala wa hofu uliendelea kumtawala. “Wakipiga kelele itakuwaje? Najua mjumbe ataamka na nitatiwa nguvuni. Lakini, potelea mbali, liwalo na liwe,” Roy aliibishia nafsi yake akiukataa uoga. Macho yake yalihama na kuambaa sehemu ya giza. Yalisafiri hadi kwenye banda la mbwa alimokuwa amefungiwa Carolina. Macho yake aliyalazimisha kuona kilichokuwa kikiendelea ndani ya banda lile.



    “Maji, nipe maji. Nahisi kiu sana,” mlinzi aliomba maji yaliyokuwa yameshikiliwa na mwenzake. Mdomo aliupanua na kuwa kama bata aliyekuwa akihangaika kuzimeza pumba kavu zilizomkwama kooni. Alipoyapokea maji na kuyamimina mdomoni. Aliyasukuma kwa kasi kulipita koromeo na kuzama tumboni. Aliitua kata kwa kuiweka chini. Baada ya dakika chache, mikono ililiendea koromeo na kulishika. Shingo aliirusha upandeupande hatimaye alitulia kama gunia la mchele. Roy alisimama akimtazama akiwa kajawa na msangao.



    Haraka! Macho ya Roy yalitua kwa mlinzi wa pili ambaye alikuwa kaegama kwenye ukuta, naye alitulia kama mtu aliyeupiga mtama na kumsafirisha mbali kwa usingizi. Alikuwa si hai tena. Povu lilikuwa likimtoka mdomoni na kutambaa kifuani kwake. Kwa kuwa hakuwahi kuiona hali hiyo, Roy iliingiwa mchecheto. Alinyanyuka alipokuwa na kuufikia mwili wa mlinzi wa kwanza aliyekuwa na mwili mkubwa. Alimtikisa lakini hakuwa na dalili ya kuwa hai. Alimwendea mlinzi wa pili ambaye alikuwa na mwili wa wastani na kumtikisa, naye hakuwa na hali. Walinzi wote walikuwa wafu tena pasipo hata hangaiko la kuitupa mikono. Walikufa kifo cha baridi.



    “Kazi imeisha,” nafsi ya Roy ilitangaza. Moyowe uliokuwa na hofu tayari uliingiwa ujasiri mkubwa. Aliutazama mlango wa mjumbe, hakuona dalili ya kufunguliwa. Hatimaye alipiga hatua kuelekea dirishani na kulitega sikio kusikiliza kama mjumbe na mkewe walikuwa wamepitiwa na usingizi mzito. Walilala. Aliisikia miungurumo kama mshine ya kukoboa nafaka ikipishana, mara mjumbe kisha mkewe. Kweli walilala fofofo, hawakujua wala kusikia yaliyokuwa yakitendeka nje. Roy alipiga hatua hadi pale Carolina alikuwa amefungiwa. Wakati huo hakuisha kukagua kila upande wa eneo hilo. Mkono wake uliliendea komeo lililokuwa limeegeshwa na kuushikilia mlango. Alilinyonga na kuuvuta mlango taratibu. Ulifunguka.



    “Usiogope. Mimi ni Roy,” alisema kwa sauti ya kunong’ona. Mkono wake wa kuume ulimwendea Carolina, japo gizani alipapasa na kumshika. Isivyo bahati, mkono wake ulikifikia kidonda na kumtonesha. “U-u-na…” Aligugumia Carolina akitaka kutoa siahi kutokana na maumivu makali aliyoyahisi.



    “Shiiiiiiiiiii! Usipige kelele!” Alionya Roy wakati akimziba Carolina mdomo kwa kiganja chake. Aliushika mkono mmoja wa Carolina na kuuzungusha shingoni kwake. Upande upande kama kaa walitembea kwa shida. Roy aliizima tochi yake wakaenda kwa bashiri kwenye giza nene.



    “Jikaze nikuokoe,” Roy alimwambia Carolina wakati miguu yake ikimwisha nguvu.



    “Siwezi kufika mbali. Siwezi Roy. Acha waniue,” alisema Carolina kwa sauti ya chini iliyodhoofu.



    “Twende. Jikaze,” alisema Roy baada ya kubaini kuwa Carolina hakuwa na nguvu za kuweza kutembea. Japo walikuwa gizani, Roy hakuacha kukodoa akiangaza kila upande. Endapo angeona mwanga wa kurunzi popote angeongeza umakini kwa kujua kulikuwa na mtu ambaye angeweza kuwaona. Kwa kuwa hakuona mtu, aliinama na kumpachika Carolina mgongoni. Alizipiga hatua taratibu. Uzito ulimwelemea na kumfanya apumue kwa shida. Alijikaza kwa kutembea hadi alipoimaliza njia itokayo kwa mjumbe na kuingia hatua chache shambani. Alimshusha na kumlaza Carolina pembeni palipokuwa pamezungukwa na nyasi ndefu. Alilivua shati na kuanza kumpepea kwa kuwa pumzi alikuwa nazo za kuokoteza.



    “Pandisha pumzi ya kutosha kisha uishushe,” Roy alimtaka Carolina kuvuta pumzi nyingi kisha kuiachia. Kidonda kilimuuma Carolina wakati wa kutekeleza agizo hilo. Roy alitafakari sana usiku ule. Alipomtua Carolina na kumpepea alitimua mbio hadi sehemu alikokuwa ameiegesha baiskeli. Aliitwaa na kurudi nayo akiwa wanguwangu. Alimkuta Carolina akiwa ameketi kwani alikuwa amepata hewa safi na kumfanya kupumua vizuri tofauti na alipokuwa katika banda la mbwa. Alimchukua na kumpandisha kwenye baiskeli na kuianza safari kuelekea alikokuwa ameelekezwa na baba yake. Safari ya kuufuata msitu wa Geza kama alivyokuwa ameelekezwa ilikuwa si ya lelemama.



    Wakato Roy anafanikiwa kumtorosha Carolina kutoka bandani alikabiliwa na mtihani, asikamatwe! Muda huo walipotoroka, kulipita saa mbili Koi akiwa kapitiwa na usingizi. Tofauti na nia yake aligutuka kutoka usingizini akiwa kachelewa. Aliyabinya macho yake na kuyafuta kwa kiganja. Muungurumo wa mkewe aliyekuwa kalala chumbani ulisikika masikioni. Mapigo ya moyo yalimwenda mbio kwa hofu baada ya kuhisi kuwa usiku ulikuwa umekwisha. Aliuvuta mlango na kuangaza macho yake nje kwenye mbalamwezi iliyokuwa imeanza kuchomoza.



    “Yalah! Kumekucha! Lakini mbona jimbi hawawiki?” Kwa mashaka Koi alijihoji. Aliambaa baada ya kutoka mlangoni akatembea hadi upenuni aliposimama na kulikagua anga. Aliziangalia nyota ili aweze kukadiria majira ya saa wakati ule. Kwa unajimu uliokuwa umezoeleka, kwa kisi ilikuwa tayari saa nane usiku na si pambazuka kama fikra zake zilivyomtuma kuamini hapo awali. “Bado hapajakuchwa. Tena walinzi watakuwa wamelala fofofo wakati huu,” Koi alijihakikishia. Japo alikuwa peke yake, hakuishiwa maswali. “Lakini je, wakinishinda nguvu na kunitia mikononi itakuwaje? Lakini siwezi kushindwa. Heri kufa nikijaribu kuliko kuogopa nisichokijua. Nitawashinda,” Koi alijiuliza, alijijibu na wakati alijikosoa. Bado alisimama kwenye nia yake, kumuua Carolina ili ushahidi usiweze kupatikana.



    Wakati huo Koi hakutaka kungoja. Alibandika na kubandua miguu kuelekea kwa mjumbe. Jambia likiwa kiunoni, koti lilipishana na miguu iliyokuwa ikishindana kuwahi. Hatimaye alikifikia kichaka kilichokuwa karibu na nyumba ya mjumbe. Hapo alipunguza mwendo huku akikagua kila sehemu kwa mashaka. Aliuhofu mwanga wa mbalamwezi kumsaliti. Alijua walinzi wangeweza kuutumia mwanga kumwona mapema kabla hajawafikia. Aliamua kutokupita njia iliyoelekea mbele ya nyumba ya mjumbe. Alizunguka nyuma kwa mwendo wa kunyemelea. Wakati huo nuru ya mbalamwezi iliyaongoza macho hadi kwenye banda alimokuwa kafungiwa Carolina. Taratibu aliinyanyua miguu akinyata hadi kwenye ukuta. Shingo aliinyoosha kuchungulia kule walikokuwa walinzi. Mkononi alikuwa tayari na jambia lililokuwa limejaa kiu ya kuimwaga damu ya Carolina.



    “Wamelala. Tena usingizi wa pono. Haina haja kupambana nao,” Koi aliishauri nafsi yake. Alirudi nyuma kisha kuzunguka akielekea kwenye banda ambamo Carolina alifungiwa. Alichuchumaa na kutembea kwa kuchutama kama chura hadi alipolifikia banda. “Nimekuja kukuokoa. Usiogope!” Koi alinong’ona. Kimya kilimjibu. Alijivuta tena kusogea mbele hadi mlangoni. “Carolina! Carolina unanisikia?” Aliita tena na tena. Kimya! Hakuna aliyesikia akijibu kwa sauti wala mhamo wa mwili. Hofu ilianza kumtanda. Kwa fikra zake alijua Carolina alikuwa amepitiwa na usingizi. Alichomoa jambia na kutoboa kitundu. Aliinama na kuusogeza mdomo kwenye kitundu alichotoboa. “Caro! Carolina!” Aliita pasipo sauti ya kumjibu. Alikaa kimya kusikiliza mtikisiko wa mwili ndani ya banda lile, lakini hakusikia kitu.



    Hatimaye alitambaa taratibu na kuuvuta mlango wa banda akiufungua. Ulimfuata kwa haraka. Macho yalikutana na chumba kitupu. Hapakuwa na mtu. Alirudi nyuma mafichoni na kuketi akitafakari. “Ameenda wapi? Muujiza au ndo ukweli huyu ni shetani! Haiwezekani,” Koi alijihoji na kujipatia majibu mwenyewe. Mkono wake mmoja aliutuma kuokota kipande cha jiwe na kulirusha hadi mbele walipolala walinzi. Furu-furu-furu! Jiwe lilitua paa na kumpiga mlinzi. Kama kobe kwenye jumba lake, Koi alirudi kujibanza akiwa tayari kwa vita. Macho yaliganda yakitegemea kuona mtikisiko wa mwili. Kimya! Hakuna mtikisiko. Alilirudia jiwe jingine na kumponda mlinzi wa pili. Kimya! Hakuona mtikisiko wa mwili. “Walinzi gani hawa, kama walevi wa mnazi. Ngoja niwavamie inawezekana ametoroka hawajui,” Koi alijishauri. Alinyanyua miguu yake na kutembea hadi kwa walinzi na kumtikisa wa kwanza, kimya! Alimwendea wa pili, kimya! Wote hawakuwa na uhai. Hofu iliongezeka na kumfanya malaika wa ngozi yake wasimame kwa hofu.



    “Kuna nini kimetokea?” Alijihoji Koi. Macho yake makubwa kama bundi aliyaelekeza upande wa kila kona ya nyumba. Hatimaye alisimama kimya kwa sekunde chache akiwa haamini majibu ya ukaguzi alioufanya. Chini! Alipiga magoti pembeni ya mzoga wa mlinzi mmoja. Alikipeleka kiganja chake kifuani, hali ilimtia utata. Kiganja chake kililipima joto la mwili zaidi ya mara mbili. Baridi! Alikuwa amepoa kama mnofu uliootiwa kwenye jokofu. Kwa kuwa kiganja hakukiamini tena, alilisafirisha sikio lake pana kama mfuniko wa feni kuyasikiliza mapigo ya moyo. Kimya! Hapakuwa na chembe ya mdundo wa moyo. Wasiwasi uliongezeka na kuuvuruga mtazamo wake. Wazimu ulimpanda akasimama wima kama zuzu.



    “Uwiii! Uwiiii! Uwiiiii!” Koi alipiga yowe kwa nguvu. Alikitangazia kijiji kizima kilichokuwa kimetulia kuwa, kulikuwa na hali ya hatari. “Wamekufaaa! Wamekufaaaa! Wamekufaaa!” Sauti iliendelea kumtoka Koi na kuifikia kila nyumba. Mjumbe alikuwa wa kwanza kufikiwa na kelele zile. Haraka! Aliruka kama swala aliyekoswa na simba akikiacha kitanda. Aliufikia mlango na kuufungua ili kushuhudia kilichokuwa kikiendelea. Baada ya kutoka nje, akiwa kajifunga shuka lake kiunoni, mjumbe alikutana na mizoga miwili. Walinzi wa kijiji walikuwa wamelala kwa buriani. Macho yake kama taa ya treni yalitazama kila upande huku akiwa kajawa na kiwewe. Aliichunguza miili kwa makini na kujua fika kilichokuwa kimewakuta. “Wamekufa! Wamekufa. Kweli wamekufa,” Aliongea mjumbe wakati mdomo ukitikisika kwa hofu. Mbio! Aliuendea mlango wa banda na kubaini ulikuwa wazi. Carolina hakuwemo tena. “Ee! Mungu wa babu zangu. Ametoroka baada ya kuua? Au ni nani? Kweli mtoto huyu ni mzuka,” alibashiri mjumbe. Hatimaye mikono yake ilijikuta inasafiri kwenda kuufumba mdomo wake.



    Baada ya kuzisikia sauti za Koi, wanakijiji kama kundi la nyuki waliochokozwa, walimiminika hadi kwa mjumbe. Kila mtu lilimtoka yowe mdomoni, mkononi jadidi alikuwa na silaha aliyoiamini. Kila aliyekuwa akifika mbele ya nyumba ya mjumbe alisimama na kubaki kimya. Wote walipigwa na butwaa kwa walichokiona. Macho yalikuwa hayaaminiki tena bali walilazimika kuigusa miili ile ndipo waligundua kuwa umauti ulikuwa juu ya walinzi walioaminiwa na kijiji.



    Wakati huo mbalamwezi iliutapika mwanga na kuliangaza anga zima. Muda ambao wanakijiji wengi walikuwa tayari kwa mjumbe, Dendego alikuwa akichanganya miguu yake taratibu kufika kwa mjumbe. Kwa kuwa umri ulimtupa mkono, hakuweza kwenda mbio kama walivyofanya vijana wengi wa kijiji kile. Wakati akitembea, njia nzima alikuwa hana amani. Alihisi mbiu zile zilikuwa za wito mara baada ya mtoto wake kukamatwa. Alihisi kuwa alikamatwa pengine aliuawa.



    Alipofika palipokuwa na mkusanyiko, bado wanakijiji waliokusanyika walikuwa kimya. Kila mmoja alinong’ona. Minong’ono yao ghafla ilizimwa na sauti ya mjumbe.



    “Awekwe chini ya ulinzi haraka,” alitamka mjumbe kwa sauti kali na kavu. Koi aliyekuwa amesimama wima na jambia lake alibaki kuyakodoa macho asijue la kufanya. Baada ya amri ya mjumbe, vijana walimvaa na kumtia himayani. Walimkwida na kulichomoa jambia, waliliweka mbali naye.



    “Kaa chini, uko chini ya ulinzi!” Mjumbe aling’aka wakati akimsukuma. Pwata! Koi alianguka chini, katikati karibu na pale miili ya walinzi ilikuwa. Hakuwa na njia ya kuweza kukaidi wala kujitetea.



    “Ndugu zangu, mshikwa na ngozi ndiye mwizi wa nyama. Mhalifu wetu ni huyu. Koi! Ndiye yawezekana kawaua walinzi wetu. Angalia, hata binti tuliyemfungia humu hayumo. Atueleze ukweli wa jambo hili maana kikulacho ki nguoni mwako,” mjumbe alizungumza na kuufanya umati kujawa taharuki.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    Koi alitaka kuzungumza ili kujitetea lakini walimnyamazisha. Kila alilokuwa akitaka kulizungumza lilibaki kinywani mwake. Kwa usalama zaidi, wajumbe wa baraza la kijiji waliamua Koi afungwe mnyororo ule ambao alifungwa nao Carolina. Alifungwa na kusimamishwa wima kwenye mti. Mjumbe aliwasimulia wanakijiji jinsi tukio zima lilivyotokea hadi yeye alipoamka na kumkuta Koi akiwa mbele ya wafu akiwa peke yake baada ya kupiga mbiu.



    *****



    Safari ya utoro iliwachukua Roy na Carolina kuipita milima, tambarare na mabonde. Walipanda na kushuka kisha kutambaa kwenye nyika bila kukutana na mtu. Makutano ya mchanga, mashimo na vigingi vingi walivivuka katikati ya giza na mbalamwezi. Mbalamwezi iliyokuwa imetabasamu na kutanda kwenye uso wa dunia iliwawezesha kuona kila kitu kilichokuwa umbali na upeo wa macho yao.



    Kwa umbali, walikuwa wamesafiri muda mrefu kutoka kijiji cha Hamaniko. Hofu ya kukamatwa usiku ule ilitoweka bali hofu yao ilikuwa dhidi ya wanyama wakali na masahibu ya fahari za waafrika waishio usiku kwa ulozi na uganga. Kwa kuwa msafiri kafiri, hawakuchagua njia ya kupita bali waliifuata waliyokuwa wakiijua.



    Pamoja na kusafiri mwendo huo mrefu, Roy hakutaka kuzungumza maneno mengi. Alimtaka Carolina kuwa mtulivu hadi watakapofika sehemu ambayo alikusudia kumpeleka. Carolina baada ya kuona tayari wamesafiri mwendo mrefu, hofu ilianza kumvaa.



    “Roy, unanipeleka wapi?” Alihoji baada ya hofu kumzidi.



    “Nakupeleka mahali salama, huko moyo wako utatua na mashaka yote yatakuisha,” Roy alijibu. Aliendelea kuzisukuma pedeli za baiskeli kwa kasi ili angalau aweze kuwahi kufika. “Vumilia, mvumilivu hula mbivu,” aliongeza Roy.



    “Kwa nani huko?” Carolina alizidi kuhoji. Roy alibaki kimya hakujibu. “Roy, kwa nani unanipeleka?” Carolina aliendelea kuhoji baada ya kutojibiwa swali lake la awali. Akiwa katika tafakari, ghafla tairi la mbele lilipiga shimo. Baiskeli iliyumba. Ilienda kushoto kulia na hatimaye usukani ulimshinda Roy. Baiskeli iliyokuwa kasi ilikiparamia kichaka. Paa! Tairi la mbele lilitapika upepo wote na kusinyaa. Roy na Carolina waliishia chini kama mizigo ya unga. Vumbi lilitimka, lilielea juu na kuzifunika pua zao. Walibaki kimya kama waliotiwa kufuli mdomoni. Kila mmoja aliguna wakati akijikung’uta kuliondoa vumbi mwilini. Safari yao ilikuwa imepatwa mkosi kwa mara ya kwanza.



    Baada ya Roy kunyanyuka kutoka pale chini, alimfuata Carolina ambaye bado alikuwa kitako vumbini. Alimshika mkono na kuuvuta kumnyanyua.



    “Hujaumia?” Roy alimhoji Carolina akiwa tayari amesimama. Walitazamana kama bibi na bwana kwenye nembo ya taifa la Tanzania.



    “Sijaumia Roy, ila tu nahisi kukitonesha kidonda changu,” Carolina alisema akiwa kasimama wima. Roy alizipiga hatua hadi kwenye baiskeli iliyokuwa imelala chali. Aliivuta na kuisimamisha vizuri. Mnyororo uliachia na mguu mmoja wa pedeli ulikunjamana. Aliinama na kuushika mnyororo ili kuurejesha sehemu yake. Alijaribu kulizungusha tairi la nyuma, kwa faraja lilikubali. Tena miguu yake aliisimika na kukishika kiuno wakati akitafakari.



    “Ajali haina kinga,” Roy alisema akiwa kamkazia macho Carolina kupitia mbalamwezi ile.



    “Shukuru hakuna majeraha mapya,” Carolina alijibu wakati akijisogeza sehemu yenye kisiki. Alikifikia na kuketi. Roy aliiangalia sehemu ya pedeli iliyopinda hatimaye alitingisha kichwa kwa sikitiko. Aliliendea tairi na kulishika sehemu lilipokuwa limepasuka. Alibaini kuwa alihitaji marekebisho ya tija ili kuiwezesha tena baiskeli kufanya kazi kama ya awali.



    “Roy, pumzika kidogo. Safari imeshaishia hapa,” Carolina alisema kwa unyonge.



    “Hata sijui tutafanyaje,” Roy alijibu wakati akielekea kuketi pembeni kidogo na alipokuwa Carolina.

    “Tungoje pambazuko huenda tukapata msaada,” Carolina alimsihi Roy. Roy alijitupa na kujilaza kwani alikuwa amechoka sana.



    “Sawa. Kwani sasa ni saa ngapi?” Carolina alihoji. Roy aliwasha kurunzi na kuiangalia saa yake mkononi.



    “Tayari asubuhi. Saa kumi na moja na dakika arobaini,” alijibu Roy akiwa na mshangao.



    “Saa kumi na mbili kasoro? He! tumetembea usiku mzima?” alisema Carolina.



    “Ndiyo. Na tulikofika si rahisi kwa yeyote kutufikia,” alisema Roy.



    “Lakini, ni vema tuketi kichakani wasije kuwa wanatufuata kwa nyuma,” Carolina alitoa pendekezo.



    “Hilo la maana umenena,” Roy aliafiki. Alisimama kisha kuikokota baiskeli yake. Aliiweka begani wakati wakikielekea kichaka kidogo na kuketi. Waliipa kisogo njia iliyowafikisha sehemu ile.



    *****

    Usiku ule, Koi aliendelea kupata kibano. Ilimpasa kueleza ni kwa nini aliwaua walinzi wale. Mbali na hilo ilikuwa wajibu wake kutaja kule Carolina alikuwa.



    “Mimi sijui. Nawaambia sijui!” Koi alijieleza kwa kukatakata maneno. Kipigo kilimkabili mbele ya watu waliokuwa na kiu ya kujua kule alikuwa Carolina.



    “Mcharazeni mpaka aseme,” mjumbe aliagiza.



    “Sijaua!” Koi alijibu. Bakora alizozipokea zililichana koti na kuuacha mgongo wazi. Fimbo zilishindana kutua mgongoni. Milio ya fimbo iliwashtua waliokuwa karibu naye. Kila alipochwapwa, mwili wake ulichanika na kuzifanya damu kuruka na kutawanyika. Akiwa kwenye mnyororo, Koi aliyumbayumba. Aliyalazimisha macho yake kufunguka ili awatazame waliokuwa wakimtandika kama ilivyokuwa kwa Carolina, hakuweza. Jasho jekejeke lilimmiminika na kuishia kwenye nguo zake. Jelezi lilimvamia mwishowe alienda hongehonge kwa kutikisika.



    “Mpumzisheni kidogo,” Mjumbe aliwasihi vijana. Kauli ile ilifanya mijeledi ikome pakawa na utulivu. Umati wa watu waliketi kimya kungojea maamuzi ya mjumbe na baraza la kijiji kuhusu hatma ya walinzi waliouawa na mahali alipo Carolina.



    “Mjumbe, nikuume sikio,” Dendego alimtaka mjumbe. Walinyanyuka na kuelekea kando mbali na makutano usiku ule. Alimshika begani kisha kumtemea maneno.



    “Kijiji hiki kimechafuka. Tawala ya Hamaniko imeingiwa mikosi. Hatuwezi kuamua jambo wala kuitisha baraza tukiwa na wafu. Lazima wazikwe kwanza. Hiyo ndiyo lazima ya mila zetu,” Dendego alimpa ushauri mjumbe.



    “Hata mimi nililiwaza hivyo. Tutaitisha baraza baada ya mazishi ya mashujaa wetu. Mambo mengine yatafuata baada ya hapo,” mjumbe alikubaliana na ushauri.



    “Lakini, eh!... watangazie wananchi muda wa mazishi hapo kesho pamoja na muda wa kuketi kwa baraza ili wakae wakijua,” Dendego alizidi kumwaga ushauri.



    “Sawa. Tutawazika mapema asubuhi ili tufanye baraza na uamuzi tuuchukue mapema,” mjumbe alipendekeza.



    “Mizimu ya Hamaniko huwapokea mashujaa wake wakati jua likiwa wima. Jua changa ni kwa watoto na jua machweo ni kwa sisi wazee. Hawa ni jua la utosi maana ndio kwanza damu ilikuwa ikiwachemka. Saa nane inafaa,” Dendego alieleza.



    “Basi tutafanya hivyo,” mjumbe alikubali kisha walirudi kwenye halaiki. Mjumbe aliipaza sauti yake kuwajulisha sababu na maazimio yote.



    Roy na Carolina walikuwa bado wamechutama baada ya kupatwa na ajali ya baiskeli. Walikubaliana kungoja pambazuko ndipo wachukue hatua thabiti ya kuwawezesha kufika walikokusudia.



    “Roy, kwa nini umeamua kuubeba mzigo mkubwa hivi?” Carolina alihoji. Aliyaangaza macho kumtazama Roy.



    “Ni wajibu wangu. Inanipasa kufanya hivyo sababu huenda mimi ndiye chanzo cha wewe kupatwa na haya,” alijibu Roy. Macho yake yalimtazama Carolina. Tabasamu lilimtoroka Carolina ghafla akijikuta anapitiwa kwa kicheko. Alikaa kimya akitafakari kwa kina. Roy alikuwa kaibinua baiskeli na kuutoa tyubu iliyopasuka na kupafunga kwa mpira mwembamba mahali palipopasuka. Baada ya kulirudishia, aliichukua pampu na kujaza upepo.



    “Roy, nasikitika unakonipeleka sipajui. Hujaniambia kule ambako unanipeleka.”



    “Wewe unadhani nakupeleka wapi?”



    “Mzee wangu amenipa maelekezo yote. Hivyo tukifika nitakuambia na maelekezo yote nitakupatia.”



    “Napata hofu,” Carolina alisema wakati mkono wake ukiwa unakipapasa kidonda. “Hofu yangu ni hiki kidonda. Lakini nashukuru kinaonekana kutosababisha maumivu zaidi,” Alisema Carolina. Roy hakusema neno. Alimsogelea na kuutuma mkono wake kupafunua palipokuwa na jeraha.



    “Hebu nipaone,” alisema Roy. Wakati huo alimshika kichwani na mkono mwingine ulifunua jeraha. “Lilikuwa jambo baya sana. Kwa nini uliamua kujinyonga?”



    “Sitaki kukumbuka ya nyuma.”



    “Dunia ni sayari yenye vurugu nyingi, haimpasi mwanadamu kukata tamaa na kuchukua uamuzi kama uliokuwa umechukua.” Alisema Roy huku akitabasamu. Alikazana kujaza upepo kwenye tairi yake. “Lakini, pamoja na vurugu zake, wapo watu wema katikati yake.”



    “Pamoja na wewe ukiwemo,” Carolina alidakia kwa haraka.



    “Ah! Kwanini unasema hivyo?” Roy aliuliza.



    “Nakumbuka umenisaidia kwa kila hatua. Hadi sasa unaendelea kunisaidia,” alisema Carolina. Alinyamaza kidogo wakati macho yake yakiwa kwa Roy aliyekuwa akihangaika kutaka kuunyosha mguu wa pedeli uliopinda kwenye kisiki cha mti. “Sipati picha siku ile usingetokea ingekuwaje kule bustanini.”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Kila jambo huja na kisha hupita. Nalo liliisha,” alijibu Roy. Aliinyanyua baiskeli yake wima. Wakati huo nuru ya asubuhi ilikuwa imetapakaa. Usiku ulikuwa umekwisha. Muda huo walionana ana kwa ana.



    “Caro! Nitazame machoni vizuri,” Roy alimkazia macho Carolina. “Umeona nini?”



    “Macho mekundu yenye usingizi,” Carolina alijibu wakati macho yake akiyapishanisha na ya Roy.



    “Kwani unataka nione nini?” Carolina alihoji.



    “Basi kama hujaona kitu. Ninaamini ipo siku utaona ninachotaka ukione,” alisema Roy. Alianza kuikokota baiskeli kutoka pale walikuwa. “Twende tutembee mpaka kwenye lile bwawa, huko naweza kupata jiwe ili niunyoshe mkono wa pedeli,” Roy alizungumza wakati akijikinga kwa mkono kulitazama bwawa lililokuwa mbele yao. Ilikuwa baada ya kukimaliza kijiji cha Kinyunya, sehemu ya makutano ya kuelekea vijiji vyote.



    “Ulishawahi kufika huko tuendako?” Carolina aliuliza wakati naye alijikinga kuangaza macho kulitazama bwawa lile kubwa. “Inaonekana ni bwawa kubwa sana,” Caro alisema baada ya kuwa ameangalia. Roy hakulijibu swali la Carolina. Alikuwa kakazana kutembea ili kuwahi. Walitembea kwa haraka kulielekea bwawa lile. Njia iliwaongoza kisha walilifikia bwawa. Jua la jumatatu ile baada ya jumapili lilianza kupanda kwa kasi na kuwafanya ndege wa kila aina kuruka vichakani. Kulifikia bwawa ilikuwa mwendo wa wastani japo iliwatoa jasho na sugu miguuni. Hatimaye walifika kisha Roy kama matarajio yake, alipata jiwe alilolitumia kutengeneza baiskeli yake.



    Baada ya kulipa bwawa kisogo, waliteremka bonde kisha kukipanda kilima. Iliwachukua mwendo wa nusu saa kukivuka kwa taratibu. Carolina alielekea kule ambako hakuwahi kupajua. Maswali mengi yalibaki kichwani mwake akijiuliza na kuyajibu japo si kwa usahihi. Walitumia muda mrefu sana wakiwa juu ya baiskeli iliyowapandisha na kuwashusha baada ya kuwasukasuka kila upande kama maziwa kwenye kibuyu.



    “Roy, ule mbele ni msitu?” Carolina aliuliza. Hakujibiwa. “…..tena unaonekana ni msitu mnene,” aliongeza Carolina.



    “Ndiyo. Ule ni msitu,” alijibu Roy wakati akiendelea kuzipiga pedeli za baiskeli. “Bila shaka itakuwa ndiyo mwisho wa safari yangu.”



    “Msituni!” Carolina alishikwa mshangao. “Unanipeleka msituni, kwa nani?” Roy hakumjibu bali aliendelea kuzikanyaga pedeli wakiufikia msitu kwa karibu. Hatimaye walifika kwenye msitu ule mnene. Wangali bado sehemu ya kuingilia, palipokuwa na barabara inayokatiza katikati ya msitu, Roy alisimama. Alimtaka Carolina kuteremka naye hakukaidi.



    “Caro, safari ya kukutorosha imenifikisha mwisho,” Roy alimwambia Carolia akiwa kajiegesha kwenye baiskeli yake. “Maelekezo nakupatia, lakini amini utakuwa salama,” Roy alijieleza.



    “Maskini mimi!” Carolina alisema kwa hofu. “Kwenye msitu huu mnene nitafanya nini. Roy! Usiniache peke yangu. Nilijua unanipeleka kwa watu kumbe msituni?”



    “Sikiliza Caro, ninayo maelekezo.”



    “Huu msitu unaitwa Geza,” Roy aliongea akiutazama msitu kisha alirudisha macho yake kwenye karatasi. “Unatakiwa utembee kuuvuka. Ukiumaliza huu msitu, kwa mbele kidogo utaukuta mto mkubwa.”



    “Hivyo? Nifanye nini sasa?”



    “Nisikilize Caro,” Roy alisema na kumbembeleza. “Baada ya kuuvuka mto utakutana na-na-aa…!

    “Kifo?” Carolina alidakia.



    “Hapana. Utakutana na kijiji kinachoitwa Tuamoyo.”



    “Mh! Baada ya hapo?”



    “Ukikifikia kijiji cha Tuamoyo utauliza kwa Bibi Chausiku au Maua. Huyo bibi unapaswa umsimulie kisa chako chote. Na usiache kumjuza kuwa umetokea kwa Malecha?”



    “Bibi Chausiku au Maua ndiyo nani?” Alihoji Carolina. “Halafu…ah!”



    “Ukishamsimulia, mwishoni mwambie kuwa wewe ni Chausiku mtoto wa Lola uliyekuwa kwa Malecha. Hapo atakupokea na kukufahamisha mambo mengi. Maneno haya si yangu bali ni ya baba yangu.”



    “Chausiku! Mimi si Chausiku…ni Carolina, nimdanganye..au!”



    “Shika karatasi hii itakuongoza. Niliyokuambia uyafuate kama mzee wangu alivyoniambia,” Roy aliongea wakati mkono ukimpatia Carolina kipande cha karatasi. Carolina aliunyanyua mkono kukipokea. Macho alikikazia na kukiviringaviringa kwenye pembe ya Kanga na kukifunga. Macho yalikolea kuwa mekundu akimtazama Roy kwa huzuni.



    “Roy, sijui niendako. Umenileta katika nchi nisiyoitegemea wala kuwafahamu watu wake. Kule niendako sipajui. Usalama wangu pia upo mashakani. Roy…..na…” Carolina alilalama kisha machozi yalimtoroka na kutambaa mashavuni.



    “Utakuwa salama. Amini utakuwa salama,” Roy alimfariji Carolina kwa kumkumbatia kisha kumfuta machozi. “Amini, mimi nipo pamoja nawe. Nakupenda Carolina!”



    “Asante kwa wema wako. Siwezi kukulaumu, maisha yangu yangekuwa yameshakatika kitambo bila wewe. Asante!” Carolina alishukuru.



    “Usijali. Ni wajibu wangu kufanya hivyo. Nakupenda sana Carolina ingawaje…!



    “Ingawaje nini Roy?”



    “Ah! Sijui ninakokwenda kama sitahukumiwa. Hukumu yangu ni kwa ajili yako. Ugonjwa wa moyo wangu. Barua zangu kwako zimesababisha haya yote. Sikutegemea.”



    “Barua!” Carolina alihoji kwa mshangao. Kumbukumbu zake zilimrudisha kwenye ile barua iliyokuwa imeandikwa na mtu ambaye alijitambulisha kama ROC! “Eh! Wewe ndiye uliniandikia barua?” Carolina alimhoji Roy.



    “Ndiyo mimi Caro. Sikuwa na njia nyingine zaidi ya kukujulisha kuwa nakupenda. Niliamua kukutorosha hadi hapa kwa sababu nakupenda. Niendako, wanakijiji wa Hamaniko wakinihukumu sawa. Nitakufa sababu nakupenda. Japo tunaachana pasipo wewe kunijibu barua zangu, nenda jua nakupenda.”



    “Roy usiseme hivyo. Utakuwa salama. Kama ulivyoniokoa mimi, Mungu atakutetea. Amini pia nakupenda Roy. Ila tu hukusema mapema na kunijulisha. Nakupenda amini. Moyo wangu u radhi kukupokea na kukuhifadhi kama pacha wangu,” Carolina alijieleza. Alimkumbatia Roy kisha alimwachia. “Wewe ni mwanaume jasiri na mwenye huruma sana. Umenifanya nipate faraja mpya katikati ya usiku wa kutisha. Nakupenda amini. Hupaswi kusema sana, umenionyesha kwa vitendo kuwa unanipenda na si maneno matupu. Amini…”



    Carolina alianza kupiga hatua akiifuata njia iliyoukuwa ikitokomea katikati ya msitu mnene. Roy alisimama kama kisiki akimtazama. Kwa haraka mawazo yalizidi kumvaa.



    “Caro!” Roy aliita wakati akiinama kuzifyatua katambuga zake kutoka miguuni. Carolina aligeuka kumtazama. Tayari katambuga zilikuwa mkononi mwa Roy. Aliisukuma baiskeli ikaanguka chini kisha kupiga hatua chache akiwa amaeunyosha mkono. Carolina alivyoona hivyo alisimama, alimtupia macho.



    “Chukua vitakusitiri,” Roy alitamka wakati viatu vikiwa njiani kumfuata Carolina baada ya kuvirusha. Katambuga zilitua chini na kulitimua vumbi. Carolina aliinama kuzizoazoa na kuzipachika miguuni kwake. Alijaribu kutembea yangali macho yake yalikuwa yameganda usoni kwa Roy.



    “Asante Roy,” Carolina alisema angali kasimama wima kama mnazi. Roy alikuwa bubu muda huo. Alimtazama Carolina na kumjibu kwa kukitingisha kichwa mbele na nyuma. Carolina aliupunga mkono wa kuagana na kugeuka kulielekea pori. Macho ya Roy yalibaki kodo akimkodolea Carolina. Alichokuwa akikiona nyuma ya Carolina kilikuwa siri yake. Kila alipopiga hatua, mtikisiko aliouacha nyuma uliitibua furaha ya Roy. Alibaki kasimama kapigwa bumbuwazi akimsindikiza kwa macho hadi alipotokomea



    Katika kijiji cha Amani, mzee Ganda aliamka alfajiri na mapema. Moja kwa moja aliufungua mlango uliosukwa kwa miti. Alipiga hatua kuelekea kilipokuwa kijumba cha miti na kuezekwa kwa nyasi ambamo walilala vijana wake. Huko aliwaamsha na kumtaka kijana wake mmoja kujiandaa ili aianze safari ya kuelekea katika kijiji cha Hamaniko. Kama alivyodhamiria alimpatia wasia kijana awapo safarini.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Safari uiendayo ni ya msingi sana. Japo inao umuhimu kwetu na familia, safari hii inaweza kuwa na vikwazo vingi. Uwapo safarini, ukikifikia kijiji cha Hamaniko baada ya kuuvuka mto, kata majani ya mti wa muamani na yabebelee mkononi. Hata kama watakuona watu wa Hamaniko watajua wewe ni mgeni na unastahili kusaidiwa kukujua uelekeako. Majani ya muamani wakiyaona mkononi mwako watajua kuwa upo huko kwa amani na si kwa shari,” alieleza mzee Ganda.



    “Mwenyeji wangu huko Hamaniko atakuwa nani?” alihoji kijana wa mzee Ganda ili apate kufafanuliwa ukweli wa aendako.

    “Mwenyeji wako wa kwanza atakuwa mtu yule utakutana naye wa kwanza pindi utakapo kiingia kijiji cha Hamaniko. Huyo ukikutana naye, msabahi kwa utii na uoneshe kuwa u mnyenyekevu na mwenye adabu. Umenielewa?” alieleza mzee Ganda na kuhoji.



    “Ndiyo mzee, nimekuelewa,” alijibu kijana yule.

    “Mwenyeji wako wa pili atakuwa mjumbe wa tawala ya Hamaniko. Mwenyeji wa awali ukikutana naye, mwombe akufikishe kwa mjumbe kabla ya yote. Kumbuka kila tawala inao utaratibu wake. Kiongozi wa Hamaniko ndiye atakupatia msaada wa kufika unakotaka kufika. Lakini kamwe usieleze mambo ya huku kuwa yakoje na wala usithubutu kutaja kuwa Majaliwa yupo kwetu. Watu wale wanapenda visasi wanaweza kutuvamia. Ewe mwana wa ukoo, nikutumapo huko, safari yako iongoze kwenye ukoo wa Malecha. Familia yao ni wafugaji maarufu wa ng’ombe katika himaya ya Hamaniko. Ukifika kwao jitambulishe kama mwana wa Ganda, mpenda amani katika kijiji cha Amani. Na safari yako Hamaniko ni kwa ajili ya kumsabahi shangazi yako aitwaye Kalunde, aliyeolewa miaka dahari na ukoo wa Malecha akitokea Amani. Hapo watakuelewa na utafikisha salamu zangu. Pindi ukutanapo na Kalunde, jitahidi kumpa salamu zangu na umjuze kuwa, asitupe jongoo na mti wake. Siku atutembelee ili ndugu hasa vizalia wapate kufahamiana. Amani ni nyumbani kwao na asiwe na mashaka kututembelea. Nakutakia kila lililo jema. Lakini pia kumbuka, upeleleze uwepo kwa familia ya Majaliwa kisha urudipo ulete taarifa. Usikae zaidi ya juma moja. Uongozwe na hekima, mababu wakulinde uende na kurudi salama,” alieleza mzee Ganda wakati akiushika mkono wa kuume wa kijana yule na kuutemea mate kwa nuio la salama. Alimpatia fimbo ambayo upande mmoja ulikuwa na mkuki kama nyenzo yake ya kuambatana nayo.



    Kama alivyoagizwa, kijana yule aliahidi kutii maagizo yote. Aliaga kwa kupiga magoti nakuelekea kwenye mazimbo ambapo kulikuwa na kijumba kidogo cha msonge na kuabudu kabla ya kuondoka. Hatimaye alianza safari pakiwa bado hapajapambazuka. Ilimpasa kusafiri kwa mguu zaidi ya saa nane ili kuweza kukifikia kijiji cha Hamaniko.



    *****

    Pambazuko lilikinyemelea kijiji cha Hamaniko na kukifunika kwa mwanga mzuri. Upepo wa baridi la kiangazi ulimiminika taratibu na kukitanda kijiji kilichokuwa na simanzi. Koi alikuwa akiendelea kupata suluba akiwa kashikiliwa na mnyororo. Alitikisika kwa baridi yangali meno yake mdomoni yakisagana. Wanakijiji walikuwa wakiendelea kumzunguka. Hatimaye mjumbe alisimama kati yao.



    “Atafutwe! Akiwa hai au mfu, Carolina lazima apatikane,” alitoa amri. “Tawanyikeni kila mmoja na njia yake. Mashambani, kondeni hata mtini msakeni,” aliongeza mjumbe kisha aliketi.

    Kama siafu, wanamsako walitawanyika kila kona ya kijiji ili kumsaka Carolina. Akiwa hai au mfu alihitajika kupatikana. Hilo ni kwa sababu Koi hakuweza kuwapa jibu la kwamba Carolina aliuawa au alitoroka. Msako wa kumtafuta mtoro uliendelea kwa kasi. Jua nalo lilikuwa likikazana kuzitoa sharubu zake na kulitawala anga. Jua lilipanda kwa kasi bila kujali jambo lolote ambalo lilikuwa likiendelea chini ya uso wa dunia.

    Hatimaye ilikuwa saa tano za asubuhi, bado mtoro hakuweza kupatikana. Kila mwanamsako alirejea na kutoa taarifa ya kile ambacho alikiona. Baada ya wanamsako wote kurudi, mjumbe alikuwa na jambo la kuwaambia wanakijiji wenzake.

    “Ndugu zangu, naona jua limenyanyuka,” mjumbe aliongea kisha kulitazama jua. “Bila shaka mnafahamu jukumu linalofuata,” aliongeza.



    “Ndiyo mjumbe, kuchimba kaburi malaloni,” wanamsako waliitikia kwa haraka.



    “Vijana wote! Kazi hii ifanyike kwa muda mfupi,” mjumbe alitoa agizo.



    “Ndiyo Mjumbe,” waliitikia vijana wote waliokuwa pale. Walinyanyuka na kuongoza hadi sehemu ya makaburi ya kijiji ambako walizikwa wafu. Sululu mkononi na wengine majembe na sepetu waliyabeba na kushirikiana kama mchwa kuyachimba makaburi mawili. Kila mmoja alionesha ushiriki wake na utii kwa kijiji chake.



    “Mjumbe! Kazi uliyotuagiza imekamilika,” kijana mmoja alizungumza kumjulisha mjumbe ambaye alikuwa kaketi kwenye kivuli akingoja uchimbaji kukamilika. Mjumbe aliwapongeza. Aliwataka kuandaa vigoda na mikuki ambayo mashujaa wa kijiji ililazimika kuzikwa nayo.



    Wakati huo Roy alikuwa njiani kurudi. Kuupanda mlima hugharimu jasho kuliko kuushuka. Hivyo ndivyo ilikuwa safari ya kijana huyo kutoka msitu wa Gema alikokuwa amemfikisha Carolina. Njia ndefu iliyomsafirisha kwa saa sita akiwa kambeba Carolina, ilimlazimu kuipita ili kurudi Hamaniko. Wakati huo jua lilikuwa limechanua na kuliangaza anga. Roy alikuwa tayari akikinusa kijiji cha Hamaniko. Akiwa njiani hakuacha kuwaza mambo mbalimbali kuhusu hatma ya maisha yake.



    “Leo ni jumatatu. Ndiyo ni jumatatu! Shuleni nahitajika kufika. Lakini, kijijini nako kuna msiba mzito. Hata-ah! Yawezekana nikaingia hatiani ukweli ukijulikana. Potelea mbali liwalo na liwe,” Roy aliwaza wakati miguu yake iliendelea kuzisukuma pedeli. Macho yake aliyatupia kwenye saa yake iliyokuwa ikimkonyeza.

    “Tayari Saa saba inakaribia. Muda wa kwenda shuleni umeisha. Saa moja imebaki. Na kwa utaratibu wa kijiji cha Hamaniko, lazima saa nane wafu vijana huzikwa. Itanibidi kuwahi ili nisije kutafutwa. Kwa sasa watajua nipo shuleni. Eh!” Roy aliendelea kuwaza wakati baiskeli yake ikiendelea kuuteremka mlima na kutumbukia bondeni kuliko bustani zao. Safari iliyomchukua kwa saa kumi na mbili ilikuwa imemalizika.



    Baada ya kulifikia bonde, Roy alikutana na kijana mmoja aliyekuwa kaketi kwenye shina la mti mkubwa wa mwembe. Alipomtazama kwa pembeni alikuwa na kizigo cha majani ya muamani. Alikuwa akiendelea kula embe lililokuwa mkononi mwake. Kuona hivyo, Roy alifunga breki. Alielekea alipokuwa kijana yule na kumsabahi. Kijana yule baada ya kumwona Roy akimsogelea alinyanyuka kwa upole ndipo aliitikia salamu ile. Roy alijua fika kijana yule alikuwa mgeni katika kijiji cha Hamaniko na fika alihitaji msaada. Ilikuwa jadi ya kijiji cha Hamaniko kumjua kila mgeni aliyekiingia kijiji kile iwe usiku hata mchana. Yeyote aliyekuwa wa kwanza kukutana na mgeni upande wowote wa kijiji kile alihesabiwa mkosaji endapo alikutana na mgeni na kupuuza kumchukua kwenda kwa mjumbe kumtambulisha. Kila mmoja alipaswa kuhusika na ulinzi wa kijiji na usalama wake.



    “Unaitwa nani na unatokea wapi?” alihoji Roy.



    “Naitwa Ramsi. Natokea kijiji cha Amani.”



    “Ramsi! Jina lako lina maana gani eti?”



    “Jina langu maana yake ni furaha. Napenda amani na furaha.”



    “Mimi naitwa Roy, mkazi mzaliwa wa kijiji cha Hamaniko,” alijitambulisha Roy kwa kijana yule aliyekuwa kasimama mbele yake. Bila shaka unahitaji msaada, uelekeako ni wapi?”



    “Mguu wangu huu ni ndani ya Hamaniko hii. Lakini yanipasa kufika kwa mjumbe ndiko shida yangu itakuwa wazi,” alijibu Ramsi.



    “Basi karibu Hamaniko. Zingatia yale Wanahamaniko huyaishi. Kijiji chetu hakiishi hamaniko hata leo kijiji chetu kinamsiba mzito wa kuondokewa na mashujaa wake wawili,” alieleza Roy kwa mgeni. Ramsi aligutuka baada ya kusikia maneno ya Roy akieleza kuwa kijiji kilikuwa na msiba. Kwakuwa kuku mgeni hakosi kamba miguuni, aliamua kunyamaza kimya.



    “Nakuomba uniongoze hadi yalipo makazi ya mjumbe,” aliomba Ramsi.



    “Bila shaka nitakufikisha huko. Pasipo shaka pakia kwenye baiskeli nikupeleke,” Roy alimtaka mgeni kupanda kwenye baiskeli ili waianze safari kuelekea nyumbani kwa mjumbe. Akiwa anaendelea kuzinyonga pedeli za baiskeli, Roy fikrani aliwaza jinsi ya kuingia kijijini. Kwa kuwa alimpata mgeni, alifahamu fika kuwa, mjumbe atatilia mkazo uwepo wa mgeni kuliko Roy. Hata hivyo alijua fika muda huo alikuwa na sababu ya kujitetea kuwa alikuwa shuleni na wakati akiwa anarudi alikutana na mgeni njiani ndipo kumfikisha kwa mjumbe.



    Iliwachukua muda mfupi kufika kwa mjumbe kutokea bondeni. Walipofika kwa mjumbe, walimkuta mke wa mjumbe pekee akiwa jikoni. Alikuwa anaandaa chakula cha mchana. Mke wa mjumbe aliwakaribisha. Roy alimtambulisha mgeni kwa mke wa mjumbe hasa baada ya kuelezwa kuwa mjumbe alikuwa kwenye mazishi ya mashujaa wa kijiji kile. Mama yule alimpokea mgeni na kumpatia kigoda. Alimtaka aketi chini ya mti wa kivuli ambao ulikuwa nyuma ya nyumba. Kwa mbele pembeni kulikuwa na Koi ambaye alikuwa kafungwa mnyororo na walinzi wawili walikuwa wakimlinda. Ramsi hakuwa amewaona. Alipatiwa chakula na maji akanywa. Hatimaye kwa zilivyokuwa taratibu za kijiji kile, Ramsi alipaswa kwenda kwenye njia ya kuingilia kwa mjumbe kuuchomeka mkuki wake na kuyapachika majani ya muamani kama utambulisho wa uwepo wa mgeni mwenye nia njema. Alifanya hivyo haraka na kuendelea kupumzika.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Wakati huo wa jua kali Carolina aliendelea kupambana na safari kuumaliza msitu wa Gema. Jua la utosi lilikuwa limeshika tawala na kuufanya msitu mzima kupumua joto kali. Miiba iliyokuwa imesimama kila upande ilimfanya Carolina kutembea kwa hadhari. Hakuwa na nguvu tena za kumfanya atembee kwa haraka. Miguu yake iliyokuwa imechoka na kulegea ilijaa vumbi kama mfuko wa seruji. Ulimwengu ulimsaliti aliwaza na kuwazua.

    “Hamaniko nimeiacha. Baba yangu na mama yangu. Wadogo zangu. Niendako sipafahamu. Na sijui nitafika lini. Nimechoka. Mwili unanilegea, njaa imeniteka,” Carolina aliwaza wakati akiinyanyua miguu kusonga mbele. Miguu ilimchukua taratibu akielekea kwenye mti mkubwa ili apate kupumzika.



    Alipokikanyaga kivuli cha mti nguvu zilimwisha. Usingizi haukukawia, ulimvaa na kuitwaa fahamu yake. Kama gunia la nafaka alijilaza na kutulia katikati ya msitu. Aliendelea kuishi katika hali ile kwa saa mbili chini ya mti mkubwa. Usingizi! Hauna mwamba wala dhaifu, humchukua yeyote na kusahau fahari au uduni wake.



    Carolina alitopea usingizini ndani ya nchi asiyoijua. Hatimaye upepo wa adhuhuri uliovuma ulimgutusha na kumfanya akurupuke kutoka usingizini. Aliyafikicha macho na kuangaza pande zote. Ngurumo ya tumbo ilimvuruga na tumbo lilimsokota. Njaa ilikuwa imemkamata. Alitamani kula, kinywa kilikuwa na hamu ya kubugia chochote kulituliza tumbo ambalo halina likizo. Alitazama juu ya mti, macho kwa macho alikutana na matunda makubwa. “Mabichi. Halafu ni matunda gani? Sijawahi kuyaona. Lakini… ah! Nikila nitafanyaje,” Carolina alijihoji. Alinyanyuka kwa kuyumbayumba akikagua chini ya mti ule mkubwa huenda angeona matunda mabivu yaliyodondoka menyewe. “Hili hapa lililoiva,” Carolina aliliona tunda lililokuwa bivu. Aliutuma mkono kuliokota tunda lililokuwa limeoza upande. Alilinusa na kisha kubaki kimya akitafakari.



    “Mungu! Bariki chakula hiki kiufae mwili wangu,” alinena wakati mikono ikilipeleka tunda mwitu mdomoni. Mdomo aliutanua kisha aliyaruhusu meno kulilarua. Alimeza kipande kwa kipande. Alisimama kwa sekunde chache akilisikiliza tumbo lililokuwa likinguruma baada ya kulipokea tunda mwitu. Toka pale alijisogeza hadi sehemu ambapo aliona viota vingi vya ndege. Alisimama akiwa kimya. Macho aliyatuma hadi kwenye kiota kilichokuwa na makinda ya ndege. Alimwona ndege mkubwa akitua na kuufungua mdomo akiwamwagia maji kinda wake. Carolina alistaajabu sana na kumfanya azidi kutafakari.



    “Maji. Ndege huishi na kutaga karibu na maji. Katikati ya msitu huu maji yako wapi? Au mto upo karibu?” Alitafakari akiwa kasimama wima. Kisha ndege mkubwa aliruka na kutokomea zake. Dakika chache alirudi na kutua kisha kuwatemea maji kinda wake tena.



    “Hakika maji yapo karibu. Inawezekana ni ule mto nilio ambiwa,” Carolina alijiwazia kisha kuanza kuelekea upande ule ndege alikuwa akielekea na kurudi. Akiwa kaicha njia iliyomwongoza, alikatiza katikati ya msitu. Alienda kwa uoga akiyaangaza macho kila upande. Sauti za makundi ya ndege alizisikia na kumfanya kusimama kwa tafakari. Aliyapenyeza macho kwenda mbele alikouona uwazi ambao haukuwa na miti. Ndege walikuwa wakiruka na kupotelea huko. Mwilini alikuwa tayari na madonda mengi yaliyokuwa yakitokwa damu baada ya kukwaruzwa na miti yenye miiba mikali. Hakufa moyo, alijipenyeza hadi sehemu ambapo alihisi fahari ya utu wake ingerudi tena.



    “Rabi! Ni mto,” Carolina alinena kwa furaha baada ya kuufikia mto ule. Tabasamu lilimrudia akiyatazama maji yaliyokuwa yakitiririka kuelekea bondeni. Alichunguza kama kulikuwa na usalama eneo lile. Ushahidi ulioyafikia macho ulitosha kumjuza kuwa eneo lilikuwa salama. Carolina aliingia mtoni na kuyachota maji kwa viganja. Aliyatupia maji mdomoni kwa pupa. Hapo aliuhisi mwili kupoa na kuwa na ubaridi mzuri.



    Hatimaye Carolina aliketi kwenye jiwe moja kubwa akiyatazama maji yalivyokuwa yakishindana kuiparamia miamba. Maji yaliusukasuka uchafu yaliokuwa yameuokota na kusafiri nao hadi ambako yeye hakupafahamu. “Mto nimeufika. Lakini kuuvuka yaweza kuwa kazi nyingine. Safari yangu ndefu inaweza kuishia hapa. Lakini hapana, nitavuka. Ndiyo nitavuka,” Carolina aliwaza na kujipa moyo kuwa kuvuka ni lazima. Hakutaka kushindwa. Japo kwa macho aliogopa baada ya kuyaona maji yakiwa na nguvu kubwa, hakufa moyo.



    ****



    Katika kijiji cha Hamaniko mazishi yalikuwa yamekamilika. Wanamsako walikuwa wakisawazisha udongo juu ya makaburi yaliyokuwa yamepangana.



    “Ni huzuni isiyoelezeka kuwapoteza mashujaa wawili kwa mpigo,” mjumbe aliongea baada ya kumaliza mazishi. Alikuwa akipanda minyaa juu ya makaburi na kupanda mbegu za mibono kama ishara ya kuhitimisha safari ya mashujaa wale. Kijiji kile kiliamini kuwa, mbegu za mibono zikipandwa na kuota ndipo jamii nzima hufanya sherehe kufurahia mafanikio ya mashujaa hao. Ziotapo mbegu juu ya kaburi huwa na maana kuwa, mashujaa waliozikwa waliacha tumaini kwa kijiji hivyo furaha huwa juu ya kijiji kizima. Endapo mbegu zilizopandwa huacha kuota kwa siku zaidi ya kumi na nne, kijiji kizima hukumbwa na huzuni. Huamini kuwa, mbegu iliyopandwa juu ya kaburi la shujaa ikioza basi ni ishara ya kijiji kuandamwa na mikosi kama njaa kali na maafa makubwa hutokea. Imani yao ilikuwa ikienziwa.



    Kwa kuwa ilikuwa desturi ya Wanahamaniko kufanya baraza kujadili ili kutatua changamoto ambazo ilionekana kukitatiza kijiji, mjumbe aliwataka kuelekea kwake. Wahamaniko wote waliongozana kuelekea kwa mjumbe. Roy wakati huo alikuwa akikatiza kuelekea nyumbani. Alipowaona watu wengi wameongozana, alijua fika kuwa ulikuwa ni wasaa maalumu kwa ajili ya baraza kutoa maamuzi. Maandamano yalipotoweka machoni, Roy aliipanda baisketi yake kutoka pale alipokuwa kajibanza kungoja wanakijiji kupita. Moja kwa moja alienda hadi nyumbani kwao.



    Wakati Roy akifika nyumbani, kwa mjumbe mambo yalizidi kuendelea. Mara baada ya mjumbe kufika kwake akiwa kawatangulia wanakijiji, aliuona mkuki na kutambua uwepo wa ugeni asiokuwa akiujua. Haraka aliuchomoa mkuki na kuyachukua majani ya muamani na kuelekea kwenye mti ambao kila mgeni wake hukaribishwa kumngoja. Alipofika na kumkuta Ramsi, kijana yule alisimama na kumsabahi kwa adabu. Alimkaribisha na kumtaka apumzike kungoja mpaka baraza limalizike ndipo apate kumsikiliza.



    Hatimaye wakuu wa baraza wakiongozwa na mjumbe waliketi mbele ya halaiki iliyokuwa imewazunguka. Dendego naye alikuwa mmoja kati ya wazee wa baraza la kijiji hicho.

    “Hamaniko dwaaaa!” Mjumbe aliwapasha moto Wahamaniko. Nao waliitikia, “dwaaaa!” Wakati huo kila mmoja alikunja ngumi na kuunyanyua mkono wa kulia juu kwa ukakamavu. Mjumbe alijongea mbele kidogo kisha kuyaangaza macho yake. Aliwatazama vijana kwa wazee wakiwa tayari kumsikiliza.

    “Tumekamilika?” Alihoji mjumbe yangali macho yake yakimtazama kila mtu aliyekuwa pale. “Naona tuko sawasawa. Tuendelee,” Mjumbe aliipaza sauti. “Leo ni siku mhimu katika kumbukumbu za kijiji chetu. Kijiji kilichoanzishwa miaka dahari iliyopita. Kijiji kilichokumbwa na kila aina ya dhoruba nasi kusimama imara. Kijiji kinachotenda haki kwa kila mwovu!” Mjumbe aliongea kwa hisia kali. Alinyamaza kidogo. “Wembe uliomnyoa sungura fisi hauwezi kumshindwa,” aliongeza mjumbe.



    “Dwaaa! Hamaniko dwaaa!” Wanakijiji walishangilia. Walisimama na kuonesha furaha yao kwa kuzizungusha ngumi hewani.

    “Mleteni mbele ya baraza. Mshikwa na ngozi!” Mjumbe alitoa agizo. Walinzi walimfungua Koi kutoka kwenye mti. Watu walishangilia na kusimama wima walipoona Koi akiburuzwa kama mwanambuzi kwenda machinjioni. Alipofikishwa katikati ya umati ule alibwagwa chini. Uso wake uliifuata ardhi na kuigonga. Meno yaliuchana mdomo wakati damu ziliendelea kumtoka. Mchanga na vumbi viliufunika uso wake. Alikuwa akitweta, pumzi alizikokota. Hatimaye Koi alishikwa shingoni kama pakashume na kusogezwa kwenye kisiki cha mti mkubwa. Kisiki hicho kilikuwa kimekauka na kilikuwa kama gogo litumiwalo ndani ya duka la nyama. Mnyororo ulifuata na Koi alifungwa tena kama beberu angojaye magharibi ya roho kumtwaa. Mjumbe alisimama kisha kunena.



    “Hamanikoooo!”



    “Dwaaa!” Wanakijiji waliitikia.



    “Hamaniko dwaa! Tawala yetu dwaaa! Miiko kuizingatia. Kwa haki bila kupotosha. Upanga kwa upanga. Wema kwa wema. Haki kwa haki. Kilio kwa kilio. Mshale kwa mshale. Moto kwa moto. Hamaniko dwaaa!” alitamka mjumbe mfululizo. Amri mnakumbushwa. Wema uzidi maovu. Wana kuwatii wazee na wazee kuwatunza wana. Wake wawasujudu waume na waume wawatabaruku wake. Watoto kwa miungu kuzijua tamaduni. Agizo la watemi waenzi za tawala ya moto lizingatiwe. Hamaniko dwaa!” Mjumbe alizungumza na kumalizia.



    “Dwaaa! Dwalala! Dwalala!” Wahamaniko waliitikia wakiwa wamepandwa na mori.



    “Mbele ya baraza, namleta,” mjumbe alizungumza. Watu walisimama na kupiga makofi. “Koi mtuhumiwa wa kwanza,” mjumbe alisema. Wakati huo kijana mmoja alimfungua Koi mikono. Aliketi kwa kuinyosha miguu katikati ya unasi akiwa kajawa aibu.



    “Koi, unalijua kosa lako?” Mjumbe alihoji. Koi alibaki kimya akimtazama kwa ghadhabu. “Narudia tena, unalijua kosa lako?” Mjumbe alirudia. Koi alitaka kuufungua mdomo wake kuzungumza. Hasira zilimfuma akabaki kuwatazama watu kwa uchungu.



    “Moto moto moto!” Mjumbe alisema. Vijana watatu walisimama na kumgawia Koi fimbo za mgongoni harakaharaka. Alianguka na kutambaa kwenye mchanga akiugulia maumivu makali. Ghafla maji yalitua usoni kwake yaliyotiririka na kuulowesha mwili. Majivu yalikorogwa na kupakwa usoni hadi shingoni.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    “Koi, kosa lako unalijua,” mjumbe alihoji. Koi alibaki kimya akimtazama.



    “Koi tujibu,” aliongeza mjumbe.



    “Sii-si-jui!” Koi alijibu kwa shida. Mjumbe alimuuliza Koi mara nyingi lakini hakupata jibu zaidi ya kusema hajui.

    “Ahukumiwe. Huyu ndiye mshikwa na ngozi. Kilimtuma nini kuwa hapa mauaji yatokee na binti atoweke? Anajua. Lazima ahukumiwe,” Dendego alizungumza kwa unafiki angali akiujua ukweli wa jinsi Roy alivyomtorosha Carolina. Koi aliyanyanyua macho na kumtazama Dendego kumlaani.



    “Roy! Roy! Roy!” Alitamka Koi kwa sauti iliyojaa mikwaruzo. Mjumbe alitulia kimya akitafakari.



    “Roy? Kwa nini anasema Roy? Inawezekana Roy anajambo la kutueleza,” alisema mjumbe. Wakati huo alimtazama Koi kisha Dendego.



    “Mfuateni Roy!” Mjumbe alitoa agizo. Dendego aliingiwa hofu baada ya kusikia Roy akiwa anahitajika. Mwili wake uliingiwa baridi.



    “Roy atakuwa hajarudi. Shuleni hakwenda. Yataniishia leo,” Dendego aliwaza. Tayari vijana watatu walichomoka kuelekea nyumbani kwa Dendego. Koi aliunyanyua uso wake na kumtazama Dendego kwa jicho la dharau kama alikuwa akijua jambo. Mapigo ya moyo wa Dendeko yaliongeza kasi.

    Wakati ukimya ukitawala, Dendego alisimama na kutazama njia iliyotokea kwake kwa hofu. Ghafla aliwaona vijana waliokuwa wamemfuata Roy wakiwa wamemtia mikononi mwao. Roy alikuwa akijirusha kutaka kujinasua lakini hakuweza. Kwa haraka kama mzigo wa kuni alirushwa chini katikati ya unasi. Kama mlevi alitaka kuidaka ardhi wakati anayumbayumba. Hatimaye aliisalimia ardhi kwa pua yake. Vumbi lilimjaa kila sehemu ya mwili wake. Aliyatuma macho kuutazama mwili wa Koi uliokuwa umelewa kwa mateso. Hofu ilimjaa tangu unywele hadi unyayo wake akiwaza kwa hofu.



    “Kwa nini na mimi? Wameshajua kuwa nilihusika au. Siwezi kukubali hata waninyang’anye uhai wangu. Lakini. Eh! Msalaba huu Koi ataubeba. Lazima nimsingizie ingawaje sijui kwa nini kaletwa hapa,” Roy aliwaza. Dendego alivyoona mwanaye yupo katikati ya unasi, tumbo la kuendesha lilimshika na kukihisi kibofu kujawa na mkojo. Jicho lilimtoka. Alijivuta na kukiachia kiti. Haraka alienda nyuma ya nyumba ya mjumbe ambako alisimama peke yake akiwaza. “Roy usiseme. Usikubali Roy. Maisha yetu yako mashakani. Nahisi uchungu kuona akisulubiwa mbele yangu. Lakini…….nikimwacha atakosa ujasiri hatimaye atanisaliti. Lazima nisimame mbele yake nimpe nguvu,” Dendego aliushauri moyo wake. Haraka alichepuka na kurudi kuchukua nafasi yake.



    “Moto moto moto!” Mjumbe alitamka wakati macho yakiwa kwa Roy. Vijana wawili walisimama na kumwendea kumgawia maumivu.



    “Uwiii! Mamaaa!” Roy alilalama kwa uchungu. Fimbo zilimwingia na kuuchangamsha mwili wake.



    “Tuambie aliko Carolina?” Mjumbe alihoji akiwa macho kayakaza kumtazama.



    “Sijui mjumbe!” Alijibu wakati mikono yake ikipapasa na kuminyaminya sehemu ambapo fimbo zilitua na kumchana.



    “Tena, mtieni adabu,” mjumbe aliagiza. “Mpaka aseme,” mjumbe aliongeza.



    “Sijui!” Roy alilalama baada ya fimbo kuongezeka. Dendego chozi lilianza kumtoka. Alijikaza kisabuni kisha kulipangusa chozi.



    “Jana ulileta chakula saa ngapi?” Mjumbe alihoji.



    “Sikuleta mjumbe,” Roy alijibu yangali macho yake akiwa kamkazia macho baba yake kwa huzuni. Dendengo alihisi Roy alielekea kuusema ukweli.



    “Kwa nini hukuleta chakula wakati uliagizwa?” Mjumbe aliongeza swali wakati akimsogelea Roy kwa karibu. Roy alimtazama baba yake na kumwona akiwa kajawa mashaka. Jicho lilimhamisha hadi kwa Koi. Alimtazama kwa muda kisha kuuvunja ukimya.

    “Koi! Koi! Ndiyo ni Koi,” Roy aliongea kwa sauti kubwa na kumfanya kila mmoja kusikia. Koi aliposikia jina lake likitajwa aliunyanyua uso wake. Alimkazia macho Roy akisikiliza alichokuwa akitaka kusema.



    “Tuambie, Koi alifanya nini?” Mjumbe alihoji.



    “Wakati narudi kuchukua chakula, nilikutana naye. Aliniambia umemteua kuwasaidia walinzi. Hivyo alinitaka nimpe chakula awapelekee. Nilimpa kisha nilienda nyumbani kulala,” Roy alijieleza. Dendego alitabasamu kwa jawabu alilolitoa mtoto wake. Koi alijawa na ghadhabu. Aliunyanyua uso wake kumtazama Roy. Taratibu aliukunja mkono wake na kutengeneza ngumi kali. Alimtupia Roy ikampata shavuni. Alilala chali ardhini na meno kadhaa yalimng’oka. Koi hakukoma, alilikaba koromea na kutaka kulinyofoa. Wanakijiji walijaribu kumnasua Roy kutoka mikononi mwa Koi ambaye alikuwa kamviringa kama chatu.



    Dendego baada ya kuona mwanaye akiwa matatani aliuchukua mkongojo wake na kumtandika Koi kwenye fundo la mguu wake. Maumivu aliyoyapata Koi yalimfanya amwachie Roy. Koi alifungwa mnyororo mikononi na miguuni kwani alionesha kusababisha vurugu. Umati wote ulisimama na kutega sikio kwa makini.



    “Wahamaniko, ukweli siku zote haujifichi. Bila shaka Koi jambo hili amelifanya kwa makusudi kutaka kuficha aibu iliyokuwa ikimwandama,” mjumbe aliongea.



    “Toa hukumu mjumbe?” Dendego alichombeza. “Iwe fundisho kwa wengine.”



    “Hukumu inafahamika. Auaye nguvu kazi akibainika hukumu yake ni….”



    “Kusindikizwa!” Dendego alidakia ili kukazia hukumu.



    “Ndiyo Dendego. Pamoja na hilo, makazi yake yateketezwe kwa moto ili kuondoa mkosi. Ufukapo moshi huondoka mikosi yote na kuiacha himaya salama,” mjumbe aliongeza. Dendego alizidi kufarijika moyoni mwake. Mjumbe alikaa kimya akitafakari.



    “Onyo pia kwa kijana Roy!...” Mjumbe alidokeza. Dendego alisimama na kumkazia macho mjumbe. Walikutanisha macho yao angali mjumbe alikuwa imara kamtazama.



    “Dalili ya mvua ni mawingu. Roy inakupasa kuwa makini kwa kila hatua. Kwa uzembe ulioufanya italazimu uchapwe viboko kadri ya umri wako,” Mjumbe aliongea kisha kusogea kwa nyuma. Dendego alinyanyuka na kuondoka ili asiweze kuona mateso ambayo Roy angeyapata kwa bakora. Roy alishikwa na kufungwa kamba. Kila mkono ulipita upande wake na kukutana akiwa kaukumbatia mti. Alicharazwa bakora yangali maumivu yalimuingia. Alitoka pale na kuongoza nyumbani alikokwenda kuyauguza maumivu yake.



    Baada ya Roy kuadabishwa kwa fimbo, Koi alichukuliwa mzobemzobe hadi kwenye nyumba yake. Lipu! Nyumba zake zote ziliteketezwa kwa moto. Koi na mkewe walisindikizwa hadi mpakani mwa kijiji hicho na kuamriwa kukihama kijiji.



    Baada ya magharibi kuingia, vurugu za kijiji zilitulia. Mjumbe alirudi nyumbani ili kukutana na mgeni aliyekuwa kasubiri kwa muda mrefu. Ramsi alieleza shida yake na kama alivyokuwa kaagizwa, ilimpasa kuitaja familia ambayo alitakiwa kuitembelea. Mjumbe hakuwa na hiana, alimwongoza hadi ilipo familia ya Malecha. Hapo alimkabidhi kwa wenyeji wake waliompokea na kumkarimu.



    Mjumbe baada ya kuwa amemfikisha Ramsi kwa Malecha, aliondoka na kurudi kwake kwa ajili ya kupumzika. Hekaheka za siku ile zilimfanya kushinda wima akihangaika na masahibu yaliyokuwa yakikiandama kijiji cha Hamaniko.



    Kuondoka kwa mjumbe nyumbani kwa Malecha kulitoa wasaa wa Ramsi kufanya mazungumzo ya faragha na familia ya Malecha. Aliyokuwa kaelezwa yote na mzee Ganda aliwafikishia. Hakuvunja mwiko kama alivyokuwa amesisitizwa, kila jambo lilikuwa sawa. Kalunde ambaye ni mamaye na Saranganda na mke halali wa Malecha alikuwa na furaha kubwa. Ilikuwa miaka mingi asiyoweza kuihesabu kwa vidole vya mikono yake tangu aipe kisogo familia yake kipindi akiwa kigoli. Alipoolewa na punde kusikia taarifa za kifo cha baba yao, hakuwa na tumaini tena. Hakupata kuwaza kuwa nduguze walinusurika katika mauaji ya enzi zile. Kwakuwa taarifa za kifo cha babaye ziliambatana na taarifa za vifo vya wanajamii wake waliohusiana na babaye, yeye aliona vema kubaki kimya na kuyasahau majonzi yaliyokuwa yamepita. Alikusudia kulea familia yake changa na kuifanya ndilo tegemea lake.



    Kwa taarifa ya Ramsi, fika Kalunde alifungua ukurasa mpya. Alimtambulisha Ramsi kwa mumewe na nduguze ambao walikuwa ni Huruma na Saraganda. Lilivyotajwa jina la Saraganda, Ramsi alilazimika kudodosa akitaka kujua maana yake. Kalunde alimjuza kuwa, jina hilo lilikuwa la babaye ambaye aliuawa miaka mingi kipindi ambacho yeye alikuwa mdogo. Aliamua kumpatia jina hilo mtoto wake wa kiume ili kuendelea kuitunza kumbukumbu ya uwepo wa ukoo wa Ganda. Aliendelea kutanabaisha kuwa, Saraganda lilimaanisha kuwa ni uzao wa Ganda.



    Ramsi alikuwa mtu wa dodoso za chinichini na mahiri wa kuunga vipande vya habari iliyokuwa vipandevipande. Siku ya pili angali kwa wenyeji wake, aliwasikia wakifanya mazungumzo mbalimbali yaliyoihusu jamii yao. Wakati mzee Malecha akiteta na rafikize juu ya hamaniko lililokikumba kijiji chao baada ya Majaliwa kutoweka, Ramsi alisikiliza kwa makini. Hapo ndipo Ramsi ilimlazimu kuanza kupeleleza ili kuupata ukweli. Muda huo alikuwa na Kalunde, shangazi yake akijaribu kumdodosa kwa karibu.



    “Shangazi, tangu nikanyage ndani ya tawala hii, nasikia jina maarufu likitajwa, Majaliwa. Ni nani mtu huyu?” alihoji Ramsi.

    “Tafadhali ishia hapohapo. Litajwapo jina hilo hapa kijijini, mbingu na nchi hutikisika. Yakupasa kulitaja jina hilo kwa hadhari,” alisema Kalunde kwa kemeo.



    “Sababu gani inafanya iwe hivyo, shangazi?” alihoji Ramsi kwa sauti ya chini. Kalunde alitazama pande zote kutoka pale alikuwa. Hakuona mtu akiwa karibu.



    “Ni historia ndefu. Tangu binti yake na Majaliwa aliyeitwa Lola abakwe na vijana wa kijiji hiki, mambo si shwari. Alipobakwa tu bintiye, kijiji kilimlaumu na kumhukumu kulipa fahali mmoja kama haka. Majaliwa alianza kutafuta ili alipe. Kabla hajalipa, alitoweka hadi leo hakuna fununu za alipo. Wasiwasi ni kwamba alikufa ama alikimbia na kwenda nchi za mbali,” alieleza Kalunde. Ramsi alilitega sikio lake kwa makini.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    “Ndiyo! Kisha ilikuwaje, maana umesema mfululizo wa hamaniko ulifuata?” alihoji Ramsi akiwa na hamu ya kupata kila habari aliyoagizwa kuipata.



    “Baada ya Majaliwa kutoweka, kumbe bintiye alishika ujauzito baada ya kubakwa. Miezi ilikatika hadi mwaka na miezi michache bila kujifungua,” alieleza Kalunde.



    “Shangazi, haya sasa ni masimulizi ya kufikirika. Iweje mke abebe ujauzito kwa mwaka na ushee?” alihoji Ramsi.



    “Ajabu kwa mbuzi kuzaa nguruwe, kwa kijiji hiki iliwezekana. Lola aliikata miezi kumi na mitano bila kumtoa mwanaye. Basi ilipofika wakati, siku ya kumzaa mtoto yule ndipo kifo chake kilikuwa. Utadhani walibadilishana uhai, afe mama mtoto aishi,” alieleza Kalunde.



    “Shangazi, habari hii ni mpya masikioni mwangu. Ya Hamaniko sijawahi kuyasikia Amani. Huyo mtoto aliyemzaa alikuwa wa aina gani? Maana miezi kumi na mitano si muda wa kawaida,” alisema Ramsi.



    “Alikuwa binti mrembo mwenye afya yake nzuri. Usiku alipozaliwa na mamaye kutwaliwa na mauti, nami usiku ule nilijifungua huyu, Saraganda. Mme wangu alinisihi nimlee binti yule kama mwanangu. Sikukaidi. Nilimchukua na nimekaa naye hapa tangu akiwa na siku ya kwanza hatimaye kuwa mtu wa kimo mbele za watu,” alizidi kueleza Kalunde.



    “Yuko wapi binti huyo nimuone, maana ni kama siamini haya nisikiayo,” alisema Ramsi.



    “Yanini kunikata ulimi, kwanza simulizi ndo limeanza, halijafika hata nusu,” alisema Kalunde. Wakati huo alinyanyuka na kuchungulia akikagua kila upande. Hakuona mtu wa kuweza kuyasikia maongezi yale. “Kijiji hiki cha ajabu, hakiishi mauzauza tangu niolewe huku. Kila uchao na kuchwa huibuka jambo la ajabu na kustaajabisha. Tuendelee!” Kalunde alidondoa maneno. Aliketi kwenye mkeka sawia. “Sasa baada ya mtoto wa Lola ambaye ni Carolina kukua, kijiji kizima kiliingiwa wazimu. Binti kawapepeta kama ngano Wahamaniko wote. Wazee kwa barobaro, wote walivutwa na uzuri wake. Kila mmoja akaingiwa na pagaa akitaka kumjua sirini. Hapo ndipo mambo yakawa si mambo. Mume wangu hakupendezwa na hilo, aliamua kumuua kabisa,” alieleza Kalunde.



    “Yalah! Kumuua kwa sababu gani? Damu ya binti kwa mkuu wa familia ni laana kubwa kwa mujibu wa mila za kwetu Amani,” alistaajabu Ramsi.



    “Hakupendezwa na tabia zile. Basi binti alitoroka na kukimbilia tusikokujua. Hata hivyo walimtafuta na kumpata usiku uleule. Wakati wakingoja asubuhi kufika, ajabu hakuonekana. Walistaajabu kuona kibanda walichokuwa wamemfungia kikiwa wazi na walinzi waliokuwa wakimlinda wakiwa wafu tayari. Hapo ndipo ikawa nginjanginja. Hiyo jana ulipofika, mchana kulikuwa na mazishi na hukumu kwa mtuhumiwa wa utoro wa binti na muuaji wa walinzi. Sasa hatujui linalofuata tena ni lipi. Pia nakusihi, ya Hamaniko yaache Hamaniko, usishawishike kuyaingia, ni makubwa huyawezi,” alieleza Kalunde wakati Ramsi akiwa na swali jingine la kuhoji.



    “Lakini shangazi, huyo mke wa Majaliwa yeye hakupatwa na songombingo hizi?”



    “E-waaaa! Tena nilitaka kusahau. Bibi yule yaliyompata shahidi ni Mungu wake. Naye hadi sasa hatujui kule aliko kama yu hai ama ni hayati,” alieleza Kalunde.



    “Ilikuwaje labda?” alihoji Ramsi.



    “Baada ya mwanaye kufariki na kijiji kumzika, alibaki peke yake pale nyumbani. Alijishughulisha sana na kijibustani chake ili kupata mahitaji yake ya kila siku. Sasa siku wa siku ikaja ahamani. Bustani yake alivyoikuta imevurugwa na mazao kuliwa na mifugo aligomba na kwenda kushitaki kwa mjumbe.



    Hakusikilizwa na kulalama sana. Mwendo wa kumtoa kwa mjumbe hadi kwake ulileta balaa. Kwake kuna mzambarau, aliwakuta watoto mtini na kuwafukuza. Mwenzangu! Mtoto wa mmoja wa wanakijiji aliporomoka kutoka mtini na kufariki punde alipotua tu ardhini. Ilikuwa laana juu ya laana. Bibi wa watu alituhumiwa kuwa na pepo wabaya hivyo akihame kijiji. Nyumba iliwashwa moto naye walimsindikiza hadi tawala ya mbali ambako sina hakika kama alibaki hai,” alieleza Kalunde. Simulizi ile ilimjaza machozi machoni.



    “Poleni sana shangazi. Sasa familia ya Majaliwa haipo tena katika ardhi ya Hamaniko?” alihoji Ramsi.



    “Kabisa. Imefutika yote na hatujui nini kitafuata,” alijibu Kalunde. Muda huo Malecha alifika na kukuta mazungumzo yakiwa yamekwisha.



    “Nyama naona haijarudisha hata kibaba cha mahindi. Wanakijiji wote wamesusa kuinunua na tumelazimika kuizika. Wanahofu nyama kutokuwa salama baada ya kuila,” alisema Malecha baada ya kuwa ameketi kwenye mkeka.



    “Pole sana mjomba! Hao ng’ombe ni wangapi na walikufaje hadi waogopeke kuliwa? Au waliugua kimeta?” alihoji Ramsi.



    “Mpwa, ya Hamaniko tuachie Wa-hamaniko wenyewe. Ng’ombe wangu watano walikufa katika mazingira ya ajabu, kwa ghafla na kwa mkupuo. Hata siwezi kueleza. Yashaisha, hata kama nitakupua maneno yote kinywani mwangu, hayawezi kuwaamsha,” alieleza Malecha.



    “Poleni mjomba. Pamoja na fahari zote za dunia, kitu pekee cha kufanya ni kuwa wema. Naupenda sana msemo wa mzee Ganda ambaye kila siku hutuusia. Yeye husema; siku zote tenda wema, hauozi. Mavazi ya aina yoyote hata yampendeze mwanadamu namna gani, lakini vazi lake la mwisho ni sanda. Hata matembezi tufanyayo kote kwa namna yoyote, lakini mwisho wa matembezi yetu ni kaburini. Tutapanda kila aina ya usafiri wa fahari katika dunia hii, lakini gari la mwisho ni jeneza. Hata pale ambapo mwanadamu atakuwa na mizigo mingi ya kubeba, mwishowe ataubeba udongo wa milele awapo kaburini. Hivyo yatupasa kutotenda ubaya kwani hakuna anayekizidi kifo kwa kimo. Mali na kila fahari ni amali za kupita,” alieleza Ramsi.



    “Mjomba, maneno yako barafu, yamenitia baridi moyoni. Usemayo ni nasaha kubwa na nzito ulimwenguni. Laiti watu wa Hamaniko wangeyasikia haya na kuyaishi, tungekuwa kama kijiji cha Amani,” alieleza Malecha.



    “Mpwa, kila zama na manabii wake. Hamaniko yenye majonzi na damu itapita kama enzi za Firauni aliyeogopeka. Ninyi hasa wazazi wetu mnapaswa kutulea katika maadili na kuzipa kisogo hekaya za watu wa kuzimu. Hapo ulimwengu ungegeuka na kuwa sehemu salama ya kuishi,” alieleza Ramsi. Malecha alibaki kimya akitafakari.



    Kwa kuwa usiku uliingia, Ramsi alielekezwa mahali pa kwenda kulala. Aliwajuza ndugu zake kuwa, kesho yake mapema baada ya jogoo la kwanza angeondoka. Alikusudia kuianza safari kurudi Amani kwenda kumjuza mzee wake habari alizoziokota alipokuwa Hamaniko. Hawakumzuia bali walimsihi kuwasemesha kabla hajaondoka ili wampatie baraka na zawadi kwa safari yake.



    *****



    “Nimechoka! Mwili umeishinda nafsi,” Carolina alinong’ona. Alikuwa juu ya jiwe kubwa ambapo maji yaliyokuwa yakipita kwa kasi yalimpapasa. Nguo zake zililowa chepe na kuufanya mwili kujawa baridi katikati ya jua kali. Kila upande alioangaza aliuona mto uliokuwa ukiyatapika maji kwa kasi. Alikuwa akitazama sehemu ya kupata kijiti ili aweze kupima kina cha maji kabla ya kuvuka. Kwa karibu aliuona mti na kuutia mkononi.



    Alikitumbukiza kijiti kupima kina cha maji. Kina hakikuwa kirefu cha kutisha japo hakujua chini ya mto kulikuwa na tope ama jabali. Aliamili kuyaingia maji lakini alibaki kachutama juu ya jiwe lililokuwa limejaa utelezi. Katambuga alizokuwa nazo alizining’iniza shingoni baada ya kuzifunga kwa kipande cha kanga. Kwa taratibu alijivuta kama kenge na kutumbukiza mguu wake wa kushoto uliofuatiwa na mguu wa kulia. Tayari mwili wake nusu toka unyayoni ulikuwa ndani ya maji. Kasi ya maji ilikuwa kubwa. Ilimlazimu kuiwahisha mikono yake kwenda kuishika mizizi ya mti uliokuwa ng’ambo ambayo alitakiwa kwenda. Alihesabu mara tatu kisha kujivuta kuufuata mzizi ule mkubwa. Mzizi ulikubali kunepa na kumbeba.



    Carolina alikuwa mtulivu, hakupapalika akihofu maji kumzoa. Kama bembea, mzizi mkubwa wa mti ule ulimsafirisha hadi kingo ya pili ya mto. Ilimpasa kuchupa kwenye tope kabla mzizi haujabembea kurudi tena ndani ya mto. Alipochupa kwenye tope, nyayo zilinasa kama shilingi kwenye gundi. Nafsi iliingia faraja akiwa katulia akitazama sehemu ya kuweza kushika tena ili aweze kukwea kutoka. Juu yake alikuwa karibu kabisa na tawi la ule mti ambao mzizi ulimnyanyua kumvusha. Alilishika tawi kisha kijinasua. Aliukwea ukuta wa mto uliokuwa umejaa mizizi ya miti na miamba mikubwa. Kufika mwisho wa mto ilikuwa mtihani mgumu. Kila alipojivuta kama dudu washa ndipo hatari iliongezeka.



    Alipokuwa akitazama juu, alibakiza mita chache kuifikia ardhi salama baada ya kumaliza kingo ya mto. Alihisi furaha na nguvu kumnyemelea. Hamadi! Kabla hajafika mwisho alisikia sauti iliyomtia simanzi. Kacha! Jiwe alilokuwa kalikanyaga liliachia. Mguu wake mmoja ulibaki ukining’inia. Mguu wa pili ulikuwa bado umesimama imara kwenye ufa wa mwamba mkubwa. Mkono wake aliukaza kuushika mzizi mkubwa uliokuwa umejikunja kama chuma cha pua. Alipaswa kutia juhudi.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mguu wa Carolina uliokuwa hewani aluitafutia sehemu ya kukanyaga. Aliuchezesha mguu akitafuta sehemu ya kuupachika lakini alipakosa. Uzito ulizidi kudhoofisha nguvu ya mzizi aliokuwa ameushika. Ta-ta-ta! Sauti ya mzizi ilimwonya na kumtaka kuchukua hadhari. Carolina alijituliza ili asizalishe mtikisiko wa kuweza kuufanya mzizi kumkataa. Aliinamisha uso wake kutazama kule alikotoka. “Mamaa, ni mbali sana nikianguka nitakufa,” Carolina alijikanya. Aliutazama mzizi alioushika wakati akitafakari. Tayari mikono ilitikisika kwa kuwa ilikuwa imechoka. Alijishauri kuchukua uamuzi wa haraka.

    Carolina aliuzungusha mguu uliobembea na kuukutanisha na pacha wake. Hapo ufa ulikuwa umeshikilia nyayo za miguu ya miwili. Jasho jembamba lilimtoka na kuitembelea miguu iliyokuwa imemezwa na tope. Alining’inia kama kiota cha ndege au buu la kipepeo. Taratibu mkono kwa mkono alikwea na kuufanya mzizi uning’inie mapajani mwake. Alijivuta kwa ufundi.

    Hatimaye aliubana na kuukwea mzizi kama kamba na kuliendea shina la mizizi iliyokuwa imesimama kama pembe za ng’ome na kuishika wakati akikwea kwa ufundi. Aliufikia mzizi mkubwa uliokuwa umekauka, ulikuwa mkubwa na imara. Hapo alikwea na kuketi juu yake akiwa amauweka katikati ya mapaja yake. “Asante mola,” Carolina alishukuru baada ya kufika sehemu aliyokuwa akiitazama ardhi tambarare ikiambaa kuelekea sehemu aliyohisi kulikuwa na makazi ya watu.



    Baada ya kuuvuka mto, Carolina alitembea kwa shida akijikokota. Akiwa katikati ya kichaka kidogo matumaini ya kufika Tuamoyo aliyahisi. Alitafakari angali akipiga hatua kusonga mbele. Jua la machweo lilimwangaza na kufanya kivuli kirefu kilichomfuata. “Baada ya mto ni kisitu. Baada ya kisitu ni kijiji cha Tuamoyo. Asante Mungu. Bibi Maua ndiye mwenyeji wangu. Maua sijui Chausiku, basi nitaelewa huko,” Carolina aliwaza. Muda huo kile kijikaratasi hakuwa nacho. Kililowa na kusagikasagika hata maandishi yasingeweza kusomeka. Hakuweza kukumbuka majina kamili aliyokuwa kaandikiwa na Roy.



    ****************************

    Baada ya kuhisi miguu yake inaonja suluba dhidi ya mawe yaliyokuwa kwenye ardhi ya njia aliyoifuata, alikumbuka katambuga zake. Alizifungua kutoka shingoni na kuzitupia chini. Alizipachika nyayo akatembea wakati miguu ikiwa imesitirika. Upandeupande kama mlevi alijikokota. Maumivu ya kidonda cha shingo yalimsumbua baada ya hekaheka za kuuvuka mto. Kidonda kilikuwa kikivuja maji na damu mfululizo.



    Carolina alisimama na kutazama mbele kwa makini. Aliliona shamba kubwa la mihogo iliyostawi na kuwa kama kichaka cha asili. Shauku ilimwingia nafsini. Alilazimisha kupiga hatua ndefundefu akijua kuwa rafiki tumbo alipata dawa. Ilikuwa mwendo wa nukta chache kulifikia shamba la mihogo. Alipolifikia shamba, moja kwa moja aliliruka tuta la kwanza akienda hadi kwenye tuta la pili. Alipiga magoti na kuokota pande la mti mkavu. Alianza kuchimbua udongo akiufuata mpasuko mkubwa aliokuwa ameuona. Alijua kuwa, uwepo wa hogo-shamba ni mpasuko juu ya tuta. Ilikuwa mti chimba kidole fukua wakati mdomoni hamu ya kuutafuna mhogo iliongezeka. Kama nyegere aliufukua udongo kisha kuuvuta mhogo uliokuwa mkubwa na mrefu. Jiti alimaliza kazi yake, hakuwa tena na thamani kwa Carolina. Mkononi aliutia mhogo na kuuvunja katikati. Aliketi vizuri na kuupeleka mdomoni. Kama nyani mdomo aliuzungusha kuumenya akiyatoa maganda. Aliutafuna kipande baada ya kipande hadi ukapotea mikononi. Aliketi akiwa mtulivu akitafakari. Baada ya tumbo kupoa, maumivu yalianza kumjia tena kwa taratibu. Fikra tena zilimrejea.



    “Asante Mungu kwa chakula. Bilashaka Tuamoyo nimefika,” Carolina alisema utadhani alikuwa na mtu karibu yake. kutoka alipokuwa, alitazama upande ule ambao alikuwa akielekea. Kwa mbali aliziona nyumba zilizokuwa zimeezekwa kwa majani lakini zilikuwa zimesanifiwa kwa ufundi. “Nimefika Tuamoyo,” alisema Carolina wakati tabasamu likiuteka mdomo wake. Meno yake meupe na macho ya duara aliyazungusha kwa furaha. Alitulia kidogo kabla hajasimama kuanza kupiga hatua.

    “Wewe nani?” Ghafla sauti ikihoji kutokea nyuma na pale alipokuwa ameketi. Aligutuka na kusimama kisha kugeuka kutazama. Macho kwa macho alikutanisha na msichana mdogo ambaye hakuwa na nywele kichwani. Aliuwa ni mfupi, mweusi kama mpingo. Lakini sura yake ilikuwa angavu yenye kumeremeta. Aliyazungusha macho kumtazama kwa makini pasipo kuongeza neno jingine. Carolina naye alibaki kaduwaa akimshangaa. Walishangaana! Alipomtazama mtoto kwa kumshusha hadi kwenye unyayo, alikuwa pekupeku ya kuku. Mkononi alishika majani ya kisamvu. Gauni lake lilikuwa rangi mbili. Nusu ya juu kutokea kiunoni ilikuwa ni ya pinki. Sehemu hii ilijaa michirizi ya uchafu kifuani. Nusu ya chini ilikuwa nyeusi, ilikuwa imefunikwa kwa vumbi jepesi. Alionekana kujawa na uoga akitaka kukimbia. Carolina aliupanua mdomo kutabasamu wakati akijaribu kupiga hatua kumsogelea yule msichana mdogo. Mtoto alitimua mbio.

    “Mamaaaa! Mamaaaa!” mtoto alipiga kelele zilizojaa hofu. Majani ya kisamvu aliyaachia yakakipamba kichochoro cha njia yenye vumbi.



    “Nisaidie! Simama nisaidie,” Carolina aliita akiomba msaada. Mtoto alisimama mbali na kumtazama. Carolina alitembea harakaharaka kuelekea kwenye shamba lililokuwa mbele kidogo na pale alipokuwa. Mwanamke mmoja alikuwa kasimama kumtazama kwa makini.

    “Nini Tuma?” Mama yule mrefu, mwembamba mwenye mwanya juu na chini ndani ya kinywa chake alimuuliza mtoto wake. Carolina alikuwa akiendelea kutembea taratibu akiweweseka kuwafuata.



    “Mama, yule anakuja. Anadamu shingoni?” Tuma alisema wakati mkono wake akiunyosha kuelekea alikokuwa akitokea Carolina.



    “Mtu yule ni kama mlevi. Katoka wapi?’ Mama yule aliinyanyua shingo yake kutazama kwa makini. “Tena ni binti mdogo!” alisema wakati akilitupa jembe lililokuwa mkononi. Alipiga hatua kuelekea alikokuwa akitoka Carolina. Alimtazama kwa makini. Alipiga hatua na kuyamaliza matuta ya shamba lake la viazi akimfuata.



    “Msaada!” Carolina alisema. Aliketi chini zikiwa nguvu zimemwisha. Mama yule alimfuata na kumshika akimchunguza.



    “Umetokea wapi? Mbona umeumia kiasi hiki?” aliuliza mama yule. Alimtazama Carolina kwa makini wakati akiendelea kutafakari. “Asije kuwa anafuatwa kwa nyuma,” alisema mama yule baada ya kuwa ametazama kule Carolina alitokea. Muda huo Carolina alikuwa kalala na kutulia japo alikuwa akiendelea kupumua. Tuma alisogea akiwa kajawa na mshangao. Kidonda cha Carolina kilikuwa chekundu kama nyama buchani. Mdomoni mapovu yalikuwa yakimtoka.



    “Mama! Alikula mhogo shambani,” Tuma alisema baada ya kuyaona mapovu meupe yaliyokuwa yameutapakaa mdomo.



    “Mhogo! Lyongo!” Mama yule alitamka kwa hamaki. Alimbeba Carolina na kumpachika mgongoni na kwenda wanguwangu nyumbani. Alipofika alimtua chini ya mti na kumwegesha kama mzigo wa kuni. Aliingia ndani na kuchukua maziwa mabichi kwenye bakuli. Alitoka nje hadi alipokuwa Carolina. Aliutanua mdomo kwa mwiko na kuyamimina maziwa. Maziwa yalipita kwenye koromeo na kutua tumboni. Mama yule alichukua maji kwenye kikombe na kumnywesha kisha alianza kumpepea.



    “Lyongo ni mhogo sumu. Hauliwi mbichi hadi uvundikwe,” mama yule alitamka akimtazama Carolina kwa huruma.



    Wakati Carolina akipatiwa huduma, giza nalo lilikiteka kijiji cha Tuamoyo. Mama Tumaini alimchukua Carolina na kumkokota hadi ndani kwake. Aliwasha karabai na kuendelea kumhudumia. Alienda kondeni na kuchuma majani aliyokuwa akiyafahamu kisha kuyapondaponda na kumkamulia Carolina kwenye kidonda. Alifanya hivyo baada ya kumsafisha kwa maji ya uvuguvugu yaliyotiwa chumvi na mshubiri. Dawa ilimnyegea ikaingia na kumfanya ahisi maumivu makali. Aligeukageuka zingali fahamu na kumbukumbu hazikumrejea kwa haraka. Msitiri wake alimnywesha uji mwepesi na kumfunika kwa kitenge na kumruhusu kupumzika.



    Akiwa katika shughuli zake mbalimbali ndani ya nyumba yake, mama huyo alijiwa na mawazo mengi. “Msichana mdogo. Nini kimempata. Au kafanyiwa udhalimu kama ulionipata mimi?” Alijihoji. “Inawezekana. Miaka minane iliyopita nilitekwa na watu ambao hawajulikani hadi leo. Walinileta hadi msitu wa Geza na kunibaka kisha kunitelekeza,” Mama huyo picha ya mateso yaliyowahi kumkumba ilimjia. Alikaa kimya akitafakari. “Watu wale walinitesa. Waliniacha nikiwa nimezimia peke yangu msituni. Hatimaye baada ya kuzinduka ndipo nilijikuta katika kijiji cha Tuamoyo. Kinyunya sipatamani tena. Kituo cha wanyang’anyi na walanguzi. Hakika inawezekana yamempata niliyoyapitia. Ataniambia hali yake ikikaa vizuri,” Mama Tumaini alijieleza. Alisimama na kumtazama Carolina sehemu ile alikuwa amelala kisha kukitingisha kichwa chake. “Ndoto za kila msichana ni sawa na kipepeo nyikani. Hasemi wala hamsumbui kiumbe mwingine kwa ubaya. Upepo kwake humchukua na kumsukasuka kila upande kwa mbawa zake laini. Lakini, wanaommendea kumtia kinywani wapo wengi wasiohesabika. Kinyonga bwana rangi, tai, kunguru, ndege wadogo na wakubwa wote humfuata kwa nyuma ili atuapo wamtie himayani. Kipepeo na ndoto zake huishia mashakani,” Mama Tumaini alizidi kutafakari. Alipiga hatua hadi sehemu kilipo kitanda chake ambapo alimlaza bintiye Tuma.



    “Lala kipepeo mchanga, kesho yako Mungu anaijua,” alisema mama Tumaini baada ya kuwa amemtazama mwanaye na kumfunika shuka vizuri. Aliivuta shuka na kujiegesha akitafakari. Karabai aliizima pakawa na giza tititi! Carolina aliutua moyo.



    ****

    Safari ya Koi mfukuzwa na mkewe iliendelea ili kukiaga kijiji cha Hamaniko. Jua lilikuwa likizama na kupotea kwa kasi. Ndege waliruka na kukatiza kwenye anga lililokuwa limekolea kwa rangi ya chungwa bivu. Mama Tunu ambaye ni mke wa Koi alichoka na kuhitaji kupata pumziko kidogo.

    “Nimechoka mme wangu! Nahitaji kupumzika. Tumbo linanisokota kwa njaa na koo limenikauka. Tupumzike!” mama Tunu alizungumza wakati pumzi ikimpanda na kumshuka kwa shida.

    “Giza linaingia mke wangu. Jitahidi tukifikie kijiji cha Kinyunya angalau huko tutapata msaada,” Koi alimhimiza mkewe. Alimshika mkono kujaribu kumkokota.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Nimechoka mme wangu. Niache hapa kanitafutie maji na chakula,” alisema mama Tunu kisha kujibwaga chini. Alitambaa na kukifuata kichaka kidogo na kujiviringa kulala kwenye vumbi.



    “Kosa ni lipi? Hamaniko hawatutaki tena. Kengeza leo imekuwa chongo. Koi kasababisha. Iweje kosa la mmoja niadhibiwe na mimi?” aliendelea kulaumu mama Tunu.



    “Mama Tunu, twende mke wangu,” Koi alimsihi mkewe kwa kumfokea. “Usiku ushaingia,” alisema wakati akiinama kumnyanyua.



    “Hata kwa tingatinga hunitoi hapa. Chakula na maji yakija ndipo nitang’oka,” mama Tunu alisema huku akiushumburua mdomo. Koi alisimama akitafakari.



    “Kijiji cha Kinyunya kina visima vingi. Kuna bwawa kubwa kabla ya kufika huko. Kuna msitu mkubwa kabla ya huko,” alisema Koi wakati akisogea pale alipo mkewe.



    “Mama Tunu, jitahidi tutembee mpaka pale mbele kidogo, kuna bwawa na bustani. Huenda tukapata chochote cha kutafuna na maji,” alisema Koi akiwa kamkazia macho mkewe.



    “Mwanaume. Kama mimi ni ubavu wako ungeweza kusikia. Maji na chakula ndiyo nauli yangu. Kwanza utalitembezaje gari bila mafuta na dizeli ya kutosha? Siendi ng’o! Acha nife hapa utanizika na matanga utaanua,” mama Tunu aliporomoa maneno. Koi alimtazama akiwa mwenye kukata tamaa.



    “Haya mke wangu. Basi ningoje niende kukutafutia. Popote! Ndiyo popote nitafika lakini fahamu ni popote,” alisema Koi akiwa kaanza kupiga hatua kuondoka kuelekea asikokujua.



    “Ukikuta nimekufa, hakikisha mwanangu Tunu anapata habari na mwili wangu anauzika,” alisema mama Tunu wakati Koi akiwa kasimama kumsikiliza. “Mwanaume wewe laana kabisa. Zege umelikoroga mwenyewe unataka tujenge wote. Sikubali kuteseka namna hii. Wapi tunaenda? Kwa Tunu au kusiko julikana. Mateso haya yataisha lini? Tungekuwa hata na mwana angetuongoza sisi vipofu,” mama Tunu alisema.



    “Mama Tunu acha kunikumbusha yaliyopita. Tangu mwanetu tumpoteze kwa kifo cha ajabu baada ya kuporomoka mzambarauni, maisha si maisha tena. Imekuwa chozi juu ya chozi, huzuni juu ya huzuni,” alisema Koi wakati anaondoka.



    Ulipita muda kidogo Koi akiwa kaondoka. Giza lilikuwa limeambaa na kuufunika uso wa kijiji walichokuwa wametembea kwa saa zaidi ya sita kukihama. Walikuwa hawajafanikiwa kukimaliza kwa sababu walitembea kwa miguu. Umri pia uliwafanya kutembe polepole tofauti na ambavyo vijana wangeweza kufanya.



    Mama Tunu pasipo matumaini alikuwa bado kajilaza akimngoja mmewe. Tumbo lilizidi kuunguruma wakati pumzi alizivuta kwa shida. Tumboni hapakuwa na kitu. Koo nalo liliteseka kwa ukame baada ya kutembea kwa umbali mrefu bila kunywa maji. Wasiwasi na uoga ulianza kumtambaa mwilini kama mche wa mtambazi. Alinyanyuka na kujikusanya kuketi. Macho yake aliyaangaza kwa shida kulishinda giza lililokuwa limemzunguka. Kila upande aliangaza lakini uoni wake ulikuwa hafifu. Karibu hakupaona zaidi aliona kwa mbali kama kulikuwa na mienge ya moto iliyoruka kama walina asali porini.



    “Safari hii tunaelekea wapi? Usiku huu hatujakifikia kijiji chochote angalau tujisitiri. Kweli samaki mtamu hakosi mwiba,” mama Tunu alijisemea kimoyomoyo. Ghafla vishindo vya miguu alivisikia vikimjia sehemu aliyokuwa ameketi. Macho aliyakodoa kuyalazimisha yaone lakini hakufaulu.



    “Baba Tunu!” aliita kwa hofu. Kimya hakuna aliyeitikia. Vishindo vya miguu vilizidi kumsogelea kwa karibu. Alijivuta kutaka kunyanyuka. Wasiwasi ulimjaa mwili mzima. “Nani? Baba Tunu?” Kimya kilimjibu. Kwa mbali alisikia kelele za fisi waliokuwa wakicheka kwa dharau. “Mama yangu, fisi wananishambulia. Nani atanitetea!” alijisemea akiwa kajibanza kwenye kichaka.



    “Mama Tunu! Mama Tunu! Uko wapi?” Koi aliita. Alisimama kwenye kichaka tofauti na pale mkewe alikuwa. Mama Tunu alisikia na kuitikia haraka.



    “Nipo huku!” Koi aliposikia alitembea na kumfikia mkewe.



    “Nimefanikiwa ingawaje si sana. Naomba kunywa maji kisha tafuna mapera tuendelee na safari.”



    “Asante kwa kuja. Nimesikia vishindo vya wanyama nikaingiwa hofu.”



    “Watakuwa ni fisi. Nimekutana na kupishana nao wengi wakielekea bwawani.”



    “Tunaelekea wapi baada ya hapa?” mama Tunu aliuliza angali mdomo wake ukicheza kuyasaga mapera aliyopatiwa.



    “Kwa sasa tujitahidi kutembea hadi kijiji cha jirani, Kinyunya” Koi alisema na kumsikiliza mkewe.

    “Tukifika salama tutalala halafu pakipambazuka tutalazimika kwenda kwa Tunu. Hakuna jinsi,” Koi aliongeza.



    “Hata mimi nilitaka kukueleza hilo,” alisema mama Tunu. Alinyanyuka kutoka alipokuwa ameketi.

    “Twende, nimepata nguvu na kupumzika vya kutosha,” aliongeza mama Tunu. Koi na mkewe walishikana mikono na kuanza kuifuata njia iliyokuwa imejaa giza. Kila alipobandua mguu Koi ulifuata mguu wa mkewe.



    “Tukifika itakuwa vizuri sana. Nahisi kijiji cha karibu tutakipata baada ya muda mfupi,” mama Tunu alisema.



    “Unajua kijiji kilicho mbele yetu kinaitwaje?” Koi alimhoji mkewe.



    “Sijawahi kufika huku tangu niolewe nikiwa kigoli. Hadi uzee huu sijawahi kutoka Hamaniko na kusafiri umbali kama huu. Tena hata kipindi cha harusi ya Tunu sikubahatika kutoka na kutembea,” mama Tunu alijieleza.



    “Kijiji hiki mbele yetu kinaitwa Kinyunya. Kijiji hiki kipo katikati ya vijiji vyote. Kila aendaye kijiji chochote lazima hupita hapa.” Koi alisema. “Unakikumbuka?” aliongeza.



    “Ndiyo! Kinyunya maarufu kwa mabumunda na vitafunwa vya ngano. Nakumbuka tulikutana mara ya kwanza tukiwa tunapumzika baada ya safari ndefu kutokea kwetu Timbe kwenda Demani kwa mjomba. Siku hiyo nanyi mlikuwa mkitokea Timbe kuhemea msimu ule wa njaa?” Mama Tunu alikumbusha.



    “Kweli kabisa. Hapo ndipo nilikupata. Wazazi wako waliniruhusu nikutwae kama mke baada ya njaa kuzidi kijijini kwenu,” Koi alisema. “Unakumbuka msimu huo uliotishia kuwaangamiza?” Aliongeza Koi.



    “Bwana we! Usinitoneshe donda lililonyauka. Niache vipi kukumbuka! Usiku wangu wa kwanza kuupoteza usichana wangu kwa sahani ya wali. Siku hiyo ilikuwa ya machozi mengi baada ya kuiona damu na maumivu makali ambayo sitasahau.” alisema Mama Tunu. “Siwezi kusahau mateso uliyonipa. Tena kijiji hiki huwa hakinitoki ndotoni,” aliongeza mama Tunu.



    “Yaishe. Yalopita si ndwele tugange yajayo. Nazi ikiacha kole hajivuni mkwezi. Yaishe!” Koi alimsihi mkewe aliyekuwa akinung’unika njia nzima.



    “Lakini tabia hizi kwa tawala ya vijiji hivi itaisha lini? Mtoto wa kike kuwa kama samani za ndani, kugawiwa kwa pesa kiduchu hata sahani ya wali na miguu ya mbuzi?” alisema mama Tunu.



    “Njaa haina subira. Lakini umaskini ukiogopwa sana basi hayo hutokea, ukizoeleka napo hugeuka sugu,” alijibu Koi. Walikuwa wametembea gizani umbali mrefu na kukikaribia kijiji cha Kinyunya. Kwa karibu walikitazama na kuziona taa za karabai na mienge iliyomulika kila upande. Sehemu hiyo palichangamka kwani kijiji hicho ndipo sehemu ambayo watembezi toka kila kona ya tawala ya vijiji hivyo walitia kituo na kupumzika.



    Mzee Koi aliuacha mkono wa mkewe ili kila mmoja aweze kupata nafasi ya kutembea kwa uhuru. Walikuwa kwenye njia nyembamba iliyokuwa imebanwa upande mmoja na kichaka na wa pili kulikuwa na shina la mti. Walijipenyeza na kutokea upande wa pili. Kwa mbele palikuwa na kichuguu kikubwa kilichotambaa mpaka kwenye njia waliyoipita. Wangali wakitembea nyayo zao zilikanyaga sehemu ambayo hawakuiona. Koi alikivuka kichuguu vizuri. Mkewe alimfuata kwa karibu. Ghafla alihisi mwili wake kumiminiwa majimaji yaliyoanza kumwasha kama pilipili.



    “Nyoka! Pita haraka!” Koi alipiga kelele. Mama Tunu alikanganyikiwa na kukimbia hovyo.



    “Mamaa! Amenigonga!” mama Tunu alitoa siahi mbaya. Joka lilikuwa limesimama na kumtandika sawasawa. Alilishika na kuliondoa shavuni na kulipigiza chini kama ukuni. Koi alibaki kasimama wima. Mama Tunu alijikokota kumfuata mmewe. “Kwenye shavu la kushoto,” mama Tunu aliongea lingali jasho likimmiminika. Koi alipapasa sehemu iliyokuwa imegongwa na nyoka yule. Alimvuta mkewe kuondoka eneo lile. Damu ya moto ilikuwa ikitiririka.



    “Shavuni! Nifunge wapi ili sumu isisambae mwilini kwa haraka? Haiwezekani,” Koi alijishauri. Hakuweza kupata ufumbuzi wakati mkewe akiendelea kuugulia. Alipiga kelele kwa nguvu kuomba msaada. Hakutokea mtu wa kumsaidia. Joka ligongapo unyayo, kuundi kufungwa kwa kamba, kichwa apatapo ahamani madhila hayana tiba. Alimchukua mkewe mgongoni na kuanza mchakamchaka akikifuata kijiji cha Kinyunya.



    “Baba Tunu, siponi,” mama Tunu aliongea kwa kuzikokota pumzi. Jasho lilizidi kummiminika na kumlowesha mwili mzima. Koo lilimkauka na kulia kwa kiu. Koi kwa ukakamavu alijitahidi kutembea haraka. Kila hatua aliyoipiga alihisi uzito wa mkewe uliongezeka. Viungo vya mwili navyo viligeuka laini na kuelea kila upande.



    “Mama Tunu, jikaze tufike utapona,” Koi alisema kwa unyonge kisha kumtua mkewe chini na kumlaza.



    “Nakufa mme wangu. Mtunze Tunu, mtoto wa ujana wangu,” mama Tunu aliongea kwa shida. Koi alisimama na kutapatapa kila upande. Alipiga kelele kuomba msaada. Sauti yake ilisafiri hadi kuyaingia masikio ya wanakijiji wengi wa Kinyunya. Walianza kuelekea sauti ilikotoka. Wengi walifika na kumbeba ili kuwahi sehemu ambapo palikuwa na maduka ya kijiji. Walichukua mafuta ya taa na kuimwagia sehemu aliyokuwa amedokolewa. Sehemu ile hapakuwa na zahanati ya kuweza kumsaidia kwa haraka zaidi ya kumpatia huduma ya kwanza. Koi aliulizia kila pahala ambapo palikuwa na waganga wenye kutibu majeraha dhidi ya nyoka hata hakubahatika kumpata mmoja. Walimpatia maji kila wakati ili kuangalia namna mpya ya kufanya. Mama Tunu hakuwa na bahati. Alianza kupiga kelele na kuweweseka. Koi nafsi ilimuuma na chozi la huruma lilimtoka.

    “Nakufa! Na-ku-faaa!” Tu-nu!” mama Tunu aliyakokota maneno kisha mikono na shingo yake viliachana kila kimoja upande wake. Viungo vya mwili vilitulia. Alikata kauli!

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Mama Tunu! Mke wangu usiniache!” aliita Koi. Alijaribu kumtikisa, hakuweza kuamka. Mama Tunu aliiaga dunia kwa uchungu ambao hakuwahi kuutabiri. Katika kijiji alichompata Koi, ndipo Mama Tunu aliyapoteza maisha yake. Hakuwa na bahati kukivuka kijiji cha Kinyunya salama. Alikutwa na masahibu yasiyopimika. Buruani mama Tunu!



    Baada ya usiku kushuhudia kifo cha mama Tunu, pambazuko lilifuata. Mapema kabla ya jimbi la kwanza, Ramsi aliyekuwa kakitembelea kijiji cha Hamaniko alijidamka kurudi kwao. Alirudi Amani. Wakati anaondoka alipatiwa salamu na mtamba kwa ajili ya kumpelekea mzee Ganda. Wakati akiwa anamswaga ng’ombe, walipita njia moja na Saraganda aliyewahi kuhesabu namba shuleni. Vilevile muda huo Roy aliwahi kwenda shuleni japo alikuwa na hofu ya kuhojiwa na walimu kutaka kujua kule alikuwa siku ambayo alimchukua Carolina na kumtorosha.



    Walipofika shuleni, Roy hakuisha kuwaza. Alitoka darasani na mfuko wa daftari zake, aliuweka kwenye shina la mzambarau naye aliketi. Akiwa kaketi chini ya mkaratusi mkubwa, alikuwa katikati ya fikra juu ya kile alikifanya jana yake. “Carolina! Sijui kama ulifika salama. Natamani kujua lakini sina namna. Nakuona vile uliteseka kuuvuka mto huo mkubwa. Najua Mungu alikusaidia,” aliwaza wakati akili yake ilimsafirisha na kumwona Carolina akihangaika na kuuvuka mto.



    Roy alikichukua kijiti na kuanza kuchora chini. Akili ilimhamisha na kumkumbuka Carolina zaidi. Picha ya kukumbatiwa na Koi bustanini, mateso ya kufungwa mnyororo hadi jinsi alivyomtorosha ilijirudiarudia akilini. Hakuishia hapo pia alijawa na jazanda ya jinsi Carolina alivyoagana naye kule msituni. Alibaki akimtazama kwa nyuma na kumsindikiza kwa macho. Kama aliyetekenywa, tabasamu lilichanua mdomoni kwa furaha.



    Ilimchukua muda mrefu akiwa katika njozi za kumfikiria Carolina. Kama kimbunga, kumbukumbu ilimrudia. Akilini ilimjia taswira na kukumbuka jinsi walimu walivyomsulubu kwa sababu ya Carolina. “Hapana. Haiwezekani kuwa mimi ndiye nimeyafanya haya yote. Kwanini mimi? Kwa nini?” Roy alijihoji baada ya kuachiliwa na maono. “Kwa sababu nampenda! Ndiyo nampenda. Nampenda mtu ambaye sijawahi ku….!” Roy alitulia baada ya kusikia nyayo zikimfuata kutokea kwa nyuma na alipokuwa.



    “We’ shetani!” Sauti ilimfikia. Ilikuwa sauti nzito ikitokea nyuma yake. Aligeuka kutazama. Alikuwa kijana mrefu mwenye umbo la wastani. Pua yake ndefu kama ya mtusi, rangi ya ngozi yake usoni ilikuwa nyeusi iliyoteleza. Alikunja ndita na macho kuyabinya kwa hasira. Alikuwa Saraganda. “Pimbi mdokoa mahindi unawaza nini?” Saraganda alisema huku miguu yake ikiuchota mchanga na kuurusha usoni kwa Roy. “Mwenzako kaonja shubiri. Wewe hunitoshi sawa na soksi ya kichanga mguuni kwangu. Nitakushikisha adabu,” Saraganda aliongeza. Alikifungua kinywa cha mdomo wake na kutema mate mazito yaliyompata Roy usoni.



    “We vipi? Mbona unani…” Roy alisema. Kiganja chake kilienda usoni kuyafuta mate yaliyochangamana na kohozi. Kabla hajamaliza kujifuta, kibao cha moto kilitua shavuni kikifuatiwa na teke la guu la kushoto. Guu la kulia lilimkanyaga shingoni na kumlambisha mchanga. Kukurukakara! Roy alijitutumua kama jimbi mguuni mwa mchinjaji. Mikono aliituma na kuushika mguu wa Saraganda. Alijikaza kuuvuta. Paa! Saraganda alianguka na kukigongesha kichwa kwenye shina la mzambarau. Kama nyani, Roy alimrukia ili kumshikisha adabu. Taratibu alikuwa si wa kumkwida tena. Alitulia kama mzigo wa magimbi sokoni. Roy macho yalimtoka kwa hofu.



    “Saraganda! Saraganda!” Roy aliita akimtingisha Saraganda aliyekuwa katulia bila kuyapepesa macho wala kuunyanyua mkono. Damu zilikuwa kwenye kila tundu la pua yake ndefu. Mdomoni damu zilijaa na kuchuruzika. “Saraganda! Nini tena Saraganda?” Roy aliendelea kumwamsha kwa kumtingisha. Tena na tena alirudia kila baada ya muda mfupi lakini hakuamka. “Mama yangu!”



    Roy aliingiwa huruma na hofu kwa wakati mmoja. Alizitazama damu zilizochuruzika kutoka kwenye mifereji ya pua hadi kwenye mfuko wa daftari zake. Roy alinyanyuka akasimama. Mikono aliikusanya na kujishika kisogoni huku macho yakiwa kodo kamtazama Saraganda. Aliilani mikono yake na uamuzi aliouchukua. “Saraganda usiende. Nitahukumiwa Saraganda. Nisikie amka,” Roy alinong’ona wakati akijaribu kumtikisa na kumnyanyua Saraganda. “Amekufa!” Roy aliuambia moyo wake.



    Machozi yalianza kummwagika. Alimrudisha taratibu chini kisha kusimama pembeni. Jasho lilianza kumwagika na hofu iliongezeka. Alitaka kujua kama kulikuwa na mtu yeyote aliona tukio hilo. Aliangaza kila upande. “Hakuna aliyeona,” Roy alijiridhisha. Mguu mbele mguu fuata aliepa na kupotelea nyuma ya kuta za madarasa. Alichepuka hadi yalipo maliwato na kuingia ndani. “Nikimbie?” Aliiuliza nafsi yake. “Hapana!” Upande wa nafsi yake ulimkataza. Macho bado yalisafiri kupitia ukuta mfupi wa maliwato na kuona hapakuwa na mtu upande ule. “Napanda! Naepa!” Roy aliupanda ukuta na kuchupa chini nje ya uzio wa shule na kutokomea kichakani.



    Baada ya Roy kutoroka, ulipita muda ndipo kengele ya kupanga mstari ililia kwa sauti. Kama yalivyo mazoea, wanafunzi wote walimiminika hadi mstarini. Jua lilikuwa la utosi na shughuli za shule ya upili ya Hamaniko zilikuwa zikielekea kutamatika.



    “Mguu pande?” Kiranja wa zamu alitoa amri kisha wanafunzi kutii. Aliendelea, “Nyuma geuka.” Wanafunzi waligeuka kwa pamoja hadi vumbi lilitimka. “Nyuma geuka.” Kiranja aliwaamuru tena na tena. Baada ya kuwa wamegeuka kwa nyuma, wengi wao waliona mtu akiwa kajilaza chini ya mti mkubwa wa mkaratusi. Hata baada ya kuwa wamegeuka na kuitazama sehemu aliposimama kiranja, wanafunzi wengi walikuwa wakigeuka na kutazama sehemu ile na kunong’ona. “Nani yule pale chini?” Minong’ono yao haikutiliwa maanani.



    “Hamjambo wanafunzi?” Mwalimu wa zamu aliwasalimu wanafunzi baada ya kutoka ofisini.



    “Hatujambo, shikamoo mwalimu,” waliitikia yangali macho yao yalizidi kutazama sehemu ulipomti wa mkaratusi. Mwalimu aliwatazama kwa makini akifuata kule walikuwa wakitazama. Macho yake yalisafiri kwa kasi na kugongana na mti mkubwa wa mkaratusi. Alipoyashusha macho aliona mwanafunzi aliyekuwa kalala chini.



    “Nani huyo kalala pale chini ya mti?” Mwalimu wa zamu alihoji. Alipiga hatua kusogea. “Shabash! Saraganda!” alitamka wakati akiitupa fimbo yake na kumvaa akitaka kumnyanyua kutoka pale mchangani. Alimnyanyua na kujaribu kumkalisha lakini alikuwa kama uzi wa nguo, hakuweza kukalishwa. Shingo yake ililegea na kuzunguka kama feni.



    “Njoeni viranja wote,” mwalimu aliwaita. Viranja na baadhi ya wanafunzi walifika kumsaidia mwalimu. Walimbeba Saraganda hadi kwenye ofisi ya walimu na kuyafungua madirisha yaliyokuwa yakipitisha hewa vizuri. Mwalimu aliwaamuru wanafunzi kutoka ofisini. Alipiga magoti na kuyasikiliza mapigo ya moyo wa mwanafunzi wake. Kichwa alikitingisha kwa huzuni na kuipangusa mikono yake. Alitoka na kumwamuru kiranja wa zamu kuwatawanyisha wanafunzi hata bila kutoa tangazo moja. Wakati wanafunzi wanatawanyika, mwalimu aliyafuata madaftari yaliyokuwa pale chini ya mti. Alipokuwa akiyasoma majina yake yalimpatia taarifa ambayo alitaka kuihakiki.



    “Gonga kengele ya dharula haraka. Wanafunzi wote warudi hapa,” mwalimu alimwamuru mwanafunzi mmoja. Aliigonga kengele na wanafunzi walirudi mbio haraka.



    “Roy! Roy! Uko wapi?” Mwalimu alijinong’oneza nafsini bila kutamka hadharani. Muda huo aliyaangaza macho akimtafuta Roy ambaye daftari zake zilikuwa pale Saraganda alikuwa kalala. Baada ya kuhakiki kuwa Roy hakuwepo aliwaruhusu wanafunzi kutawanyika. Alirudi ofisini alimokuwa Saraganda akiendelea kupepewa na mwalimu mmoja aliyekuwa kabaki ndani akimhudumia.



    Kweli Roy hakuwa shuleni wakati ule. Alikuwa zamani kafika nyumbani na kumweleza baba yake kisa kizima. Baba yake alimtaka atoroke kwani lazima jambo lile lingemfanya ahukumiwe kwa kifo. Roy aliichukua baiskeli yake na kuifuata njia iliyokuwa ikielekea bondeni. Njia ile aliipita siku chache baada ya kumtorosha Carolina.



    Wakati Roy akitoroka, Saraganda hakuwa mzima tena. Mapigo ya moyo wake yalizima na mwili ulipoa. Walimu walimjulisha Mkuu wa shule kuhusu jambo lile. Haraka alifika naye alijiridhisha kuwa kweli Saraganda alikutwa na umauti. Kilichofuata ni uongozi wa shule kwenda kutoa taarifa kwa wazazi wa Saraganda.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Lilikuwa jambo gumu kuwafuata moja kwa moja wazazi wa Saraganda. Iliwalazimu walimu kwenda kwa mjumbe wa kijiji cha Hamaniko na kumjuza jambo hilo. Aliungana nao kutaka kuujua ukweli. Baada ya hapo walishauriana kuutwaa mwili wa Saraganda kwa machela ili kuufikisha kwa wazazi wake. Mzee Malecha na mkewe muda ule walikuwa wameketi chini ya mti wa mwembe kama mazoea yao jua liendapo adhuhuri.



    Akiwa mbele ametangulia, mjumbe aliufungua mdomo wake. Maneno yalimtoka. “Hodi wenyewe!” Malecha alinyanyua kichwa kutazama sehemu sauti ilitokea kabla ya kuitikia.



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog